Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Oliver Daniel Semuguruka (21 total)

MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona.
Mheshimiwa Naibu Spika, matatizo ya kiafya yanayoikabili Wilaya ya Busokelo yanafanana na Wilaya ya Karagwe, haina Hospitali ya Wilaya, inayo Hospitali Teule ya Nyakahanga inayotoa huduma za tiba kwa Wilaya mbili, Karagwe na Kyerwa. Je, ni lini Serikali itajenga Hospitali ya Wilaya ili kuboresha huduma za afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Karagwe hawana hospitali, lakini naomba niwapongeze kwamba wanafanya juhudi kubwa na ndiyo maana pale tumempeleka kijana mmoja anaitwa Dkt. Sobo, daktari mzuri sana wa upasuaji kama DMO. Ni kweli changamoto hizi, ninapata taarifa kutoka kule kila siku kwamba hakuna Hospitali ya Wilaya. Maeneo haya ni miongoni mwa maeneo tuyoyawekea kipaumbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge kwa sababu tunajua kwamba kule mnatengeneza kikosi kazi cha kuweza kuhudumia maeneo yale, naomba katika bajeti ya mwaka unaokuja sasa wekeni kipaumbele chenu ili tuhakikishe sasa Karagwe badala ya kutumia hospitali ya DDH, tutumie Hospitali zetu za Wilaya kwa kuhakikisha kwamba tunaweka nguvu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini naomba, ikiwezekana kama kuna kituo cha afya ambacho mnatumia pale kipewe nguvu ili baadaye kipandishwe kuwa hata Hospitali ya Wilaya kwa kuanzia linaweza likawa jambo jema. Lakini naomba nikwambie kwamba, Serikali itaunga mkono juhudi zote za wana-Karagwe na watu wa Mkoa wa Kagera.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lililoulizwa Na. 278, linafanana na barabara ya Mzani – Nyakahula – Mrusagamba – Mrugalama iliyopo Wilaya ya Ngara, Kagera. Pia kuna barabara ya Karagwe kupitia pori la Kimisi, Tubenako Ngara ambazo Mheshimiwa Rais aliahidi zitajengwa. Je, ni lini Serikali itakamilisha barabara hizo kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nilijibu awali, dhamira yetu ni kutekeleza ahadi zote ambazo viongozi wetu walizitoa katika nyakati mbalimbali, kuanzia awamu ya nne na awamu ya tano.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Oliva kwamba barabara hizo alizoziongelea, maadam zilitolewa ahadi, nasi tutazichukua ili tuweze kuzishughulikia kwa namna ambavyo uwezo wa kifedha utakavyokuwa unatujaalia.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa sababu kubwa ya ukosefu wa elimu kwa wakulima ni uchache wa Maafisa Ugani. Je, Serikali ina mpango gani wa kuajiri Maafisa Ugani kwa kila kijiji? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kwa kuwa wakulima wa kahawa hupeleka kahawa zao nchi jirani kufuata bei nzuri. Je, Serikali ina mpango gani kuongeza bei ya kahawa ili wananchi hawa wasipeleke nchi jirani?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama nilivyojibu katika swali la msingi kwamba tuna upungufu wa Maafisa Ugani 6,022, hii ni idadi kubwa. Vilevile kama nilivyosema katika jibu langu la msingi ni kwamba Serikali inasomesha Maafisa Ugani hawa zaidi sasa katika vyuo vyetu ili kukabiliana na huu uhaba ambao upo na vibali vya kuwaajiri vinaendelea kutolewa. Kwa hivyo, hivyo hivyo tunakwenda kukabiliana na huo upungufu na nina uhakika baada ya miaka michache ijayo kama nia ilivyo ya Serikali na Mheshimiwa Mbunge, kila kijiji kitakuwa na Maafisa Ugani wanaotakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la kahawa kuruhusiwa kuuzwa nje ya nchi, nikijibu swali lililotangulia nimesema kwamba kahawa hatutakubali iende nje kwa sababu tunavyo viwanda vya kuhudumiwa hapa hapa nchini. Hii kahawa bei yake itakuwa nzuri tukiondokana na msururu wa kodi hizo ndogo ndogo zilizopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, zao la kahawa leo tunapozungumza hapa lina kodi 26, ni kodi nyingi sana na ndiyo maana tunafanya sasa uchambuzi ndani ya Serikali ili kuona hizo kodi ambazo kwa kweli zinastahili kuondolewa, ziondolewe ili kuwapa wakulima unafuu. Kwa sababu kodi zikitozwa wanunuzi hawalipi wao, zinahamishiwa kwa muuzaji wa kahawa ambaye ni mkulima. Kwa hivyo, tukizipunguza hata kwa wanunuzi na watu wengine, mwisho wa siku atakayenufaika ni mkulima kwa sababu kodi hizo zitakuwa zimepungua na bei ya kahawa zitakuwa zimepanda.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa zana ya D by D inaonekana bado haieleweki hata kwa sisi Wabunge; je, Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ikiwemo sisi Wabunge na Madiwani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli hii dhana imekuwa ni dhana ngeni, japo imeanza muda mrefu; lakini hata ukifanya rejea, wakati mijadala yetu katika bajeti mbalimbali za sekta unaona kwamba hata Waheshimiwa Wabunge, ile concept nzima ya D by D bado haijakaa vizuri. Leo hii tulivyokuwa tukijadili katika Wizara ya Elimu, tulivyokuwa tukijadili katika Wizara ya Afya, ukiangalia michango ya Wajumbe wengi sana dhana ya D by D haijakaa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ndiyo maana hata katika kikao chetu tulivyokuwa tukifanya na Wizara ya Afya, Wataalam na sisi Viongozi Wakuu tulivyokuwa tukibadilishana mawazo tukasema ni vyema sasa dhana hii kwanza ikiwezekana iingie hata kwa watu walioajiriwa wa Serikali, wajue falsafa halisi ya dhana ya D by D. Maana yake katika Mpango huu imetupa changamoto pana.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tutaangalia jinsi gani tutafanya ili mradi hata Wabunge na Waheshimiwa Madiwani wote kwa pamoja na Watumishi wote wa Serikali wajue nini concept ya D by D? Nini maana ya dhana ya kurudisha madaraka kwa wananchi?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hoja yake ni ya msingi, nadhani tutaifanyia kazi kama Ofisi ya Rais, TAMISEMI.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba uelewa siyo mzuri sana kwenye dhana hii ya ugatuaji wa madaraka, nami napendekeza tu kwa sababu dhana hii ina maudhui makubwa sana katika msingi wa utawala wa nchi yetu. Inapokuwa haieleweki, inasababisha hata mijadala wakati mwingine kutoka nje ya context na pengine siyo kawaida kuonekana pengine mjadala huo anayetoa kwenye context ni mtu ambaye ana nafasi kubwa na kwamba jambo hili lipo kikatiba sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa napendekeza na pengine naomba kwa kupitia swali hili tuone utaratibu kwa sisi Serikali na Bunge; namna ya kufanya kwanza semina hata kwa Wabunge wote kabisa kwenye jambo hili. Mfanye semina na ikibidi kile Chuo chetu cha Uongozi ndiyo kije kituwezeshe katika jambo hili na kama tuna Wataalam ndani ya Serikali tunaweza tukatoa Watalaam, lakini kama kuna wataalam ndani ya Bunge, tutoe. Kwa sababu jambo hili kwa mimi ambaye ni mwanataaluma wa eneo hilo, napata nalo shida sana. Kusema ukweli context imepotea kabisa kwa sababu watu wanatafuta hata kwa upungufu fulani wanafikiri solution ni ku-centralize tena badala ya ku-decentralize. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nadhani tuone namna bora ya kuweza kufanya semina kubwa nzuri ya watu kupata uelewa juu ya jambo hili.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona. Tatizo la barabara ya Kidatu na Ifakara linafanana na barabara ya junction ya kuelekea Rusumo almaarufu kama zero-zero kupitia barabara ya Nyakahula - Rusahunga mpaka Nyakanazi. Hiyo barabara imekuwa ikifanyiwa ukarabati mara kwa mara lakini bado inaharibika kwa muda mfupi sana. Je, Serikali ina mpango gani wa kufanya matengenezo makubwa katika barabara hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hiyo anayoongelea hivi sasa tunavyoongea ina mkandarasi anayefanya matengenezo. Ni kweli hoja anayoongelea kwamba, kunakuwa na matengenezo ya mara kwa mara na hii inatokana na matumizi makubwa sana ya malori makubwa yanayopita katika barabara hiyo na naamini matengenezo ya sasa yamezingatia ukubwa wa matumizi ya barabara hiyo na hivyo matengenezo yake sasa yatakuwa ya muda mrefu tofauti na huko nyuma.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Jeshi la Polisi lina uhaba wa vitendea kazi vya kisasa kuweza kudhibiti matukio ya uhalifu; je, Serikali ina mpango gani kutoa vifaa vya kisasa zaidi kwa askari wetu waliopo katika maeneo ya mipakani?
Swali langu la pili; ili askari aweze kufanya kazi zake na kudhibiti matukio ya uhalifu kwa ufanisi ni muhimu akawa na mazingira rafiki kuanzia nyumbani.
Je, ni lini Serikali itatekeleza kwa vitendo ahadi ya kujenga makazi ya hadhi ya askari wa Jeshi la Polisi katika Wilaya zote za Mkoa wa Kagera?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kuwa na concern ya hali ya usalama katika mpaka wa Kagera, lakini naomba tu nimthibitishie kwamba, si Jeshi la Polisi ama Serikali kupitia Jeshi la Polisi kwa kutambua umuhimu na unyeti wa maeneo ya nchi yetu yaliyoko mipakani ikiwemo Kagera huwa kwa kawaida inatoa kipaumbele katika ugawaji wa vifaa katika maeneo hayo hususan vitendea kazi ikiwemo silaha, magari na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mzuri ni kwamba, kwa Mkoa wa Kagera pekee tunahakikisha kwamba tunawapatia Askari wetu walioko mipakani silaha za kutosha lakini silaha nzito ili kuweza kukabiliana na wimbi la wahamiaji haramu ambao mara nyingi wamekuwa wakisababisha ukosefu wa amani katika mikoa yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia hakuna hata Kituo kimoja cha Polisi katika mipaka ya nchi yetu ambacho hakina gari mpaka sasa hivi tunavyozungumza. Kwa hiyo, ni kuonesha kwamba tunatoa nguvu kubwa sana na kipaumbele katika maeneo ambayo yapo mpakani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la pili ni kweli kuna matatizo ya makazi, sio tu Kagera lakini katika mikoa mbalimbali nchi nzima na ndiyo maana tumekuwa tukizungumza hapa kuna mipango ya Serikali ya ujenzi nyumba 4,136 ambayo mpaka sasa hivi tunasubiri approval kutoka Hazina ili mradi ule uanze kutekelezeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Kagera, kuna ujenzi wa nyumba 12 ambazo tunaendelea nazo hatua kwa hatua kadri ya pesa zitakazopatikana tumalize katika eneo la Buyekera ambalo litasaidia kupunguza makali ya matatizo ya makazi kwa askari wetu.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana
kwa kuniona. Matatizo yaliyopo ya usikivu wa simu Jimbo la Nanyumbu ni sawa
na yaliyopo Wilaya ya Ngara katika Kata ya Mganza, Nyakisasa, Keza, Kabanga
na Rusumo, ambayo yanaingiliana na nchi jirani za Rwanda na Burundi. Je,
Serikali ina mpango gani wa kuboresha usikivu wa simu katika Kata hizi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa
Naibu Spika, nimemsikia na vilevile nilimsikia Mbunge wa Jimbo ameeleza kwa
muda mrefu sana matatizo ya Jimbo hilo. Namwona pale nimhakikishie na
nimhakikishie Mheshimiwa Semuguruka kwamba, upacha wao ni lazima uzae matunda katika miaka hii mitano na tutafuatilia maeneo hayo ili hatimaye
mawasiliano yapatikane ya uhakika.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa sasa MSD ina Bohari Kikanda. Je, Serikali ina mpango gani wa kufungua Bohari ya MSD kila Mkoa ili kurahisisha usambazaji wa madawa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; Serikali imejiandaaje kudhibiti upotevu, wizi wa dawa kwa watumishi wasio waaminifu katika zahanati na vituo vya afya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Swali la kwanza kuhusu Serikali kujenga bohari za dawa kila mkoa; kwamba tuna mpango gani; kwa sasa hatujawa na mpango wa kufanya hivyo kwa sababu tunaamini utaratibu wa kuwa na bohari kwenye kila kanda bado haujakwama. Ni kwamba tunahitaji kufanya maboresho kidogo tu ili tuweze kuongeza tija na ufanisi kwenye kuhakikisha vituo vya umma vinapata dawa kadri ambavyo vinahitaji na kwa haraka kadri ambavyo inawezekana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mfumo wetu wa sasa hivi wa Supply Chain Management, tunaamini bado haujakwama na ndiyo maana tumeendelea kuuboresha. Tulikuwa na changamoto kidogo za kifedha, ambazo kama ambavyo sisi Wabunge ni mashahidi na naomba nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa azma yake thabiti ya kuongeza upatikanaji wa dawa kwa kutuongezea bajeti kwenye eneo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, changamoto ya kifedha tuliyokuwanayo ambayo ilikuwa inashusha tija na ufanisi, sasa inaelekea kuondoka na mfumo wa upatikanaji wa dawa umeimarika sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuhusu udhibiti, naomba nitumie Bunge lako Tukufu kuwaomba Waheshimiwa Wabunge wote, Madiwani wote na Viongozi wote kuanzia Viongozi wa Mikoa na Wilaya washiriki kikamilifu katika kusimamia udhibiti wa mfumo wa upatikanaji wa dawa kwenye vituo vyetu kwa sababu, jambo hili haliwezi kuwa ni la sisi tu tuliopo Fungu 52, kwa maana ya Wizara ya Afya pekee. Kwa sababu, mfumo wetu wa udhibiti upo, kwamba kwenye kila zahanati, kila Kituo cha Afya na kwenye kila hospitali, kuna Kamati ya Udhibiti wa Dawa, Vifaa, Vifaa Tiba na Vitendanishi ambapo ndani yake kuna viongozi wa kuchaguliwa na kuna watendaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo ni kwamba, mfumo huu hausimamiwi ipasavyo. Kama ungefanya kazi ipasavyo, kwa hakika, tungeweza kudhibiti wizi na ubadhirifu wa madawa ambao umekuwa ukitokea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu, kama kuna mtu ana taarifa yoyote ile ya mahali ambapo kuna wizi ama upotevu wa dawa ambao umejitokeza, atupe taarifa na sisi tutachukua hatua haraka.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona niulize swali ndogo la nyongeza. Matatizo ya usikivu wa simu yaliyopo Mpanda vijijini ni sawa na yaliyopo Wilaya ya Ngara kata Muganza, Nyakisasa Keza, Kabanga na Rusumo. Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha usikivu wa simu katika kata hizo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema Serikali ina nia ya dhati kabisa yakufikisha mawasiliano kila sehemu na hasa, eneo hili analoliongelea ni maeneo ya mpakani na maeneo ya mpakani tuna utaratibu maalum wa kuhakikisha kwamba mawasiliano yanafika haraka katika maeneo hayo. Kwa hiyo Serikali itahakikisha inafikisha mawasiliano mara fedha zitakapozipata.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona. Tatizo la maji lililoko Mkoa wa Pwani linafanana kabisa na tatizo la maji lililopo Jimbo la Ngara ambapo tunapata maji kwa wiki mara moja au mara mbili. Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua tatizo hili la maji katika Wilaya ya Ngara?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, tayari Wizara yangu inatafuta mkandarasi mshauri ambaye ataanza kufanya design ya kutumia maji ya Mto Rubuvu kupeleka Ngara kwa sababu yale maji ni mengi kwa hiyo yatasambaa maeneo mengi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nikwambie tu kwamba Serikali, Wizara yangu haijalala tayari inaangalia maeneo yote na kutumia vyanzo vilivyopo kuhakikisha kwamba, wananchi wanapata maji safi na salama.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona niulize swali dogo la nyongeza. Matatizo yaliyopo Iramba Mashariki yanafanana kabisa na matatizo yaliyopo Wilaya ya Ngara. Vijiji vingi vya Wilaya ya Ngara, hasa Tarafa ya Lulenge, havina umeme. Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka umeme katika vijiji hivyo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami niungane nawe kuwapongeza Wabunge Viti Maalum na Wabunge wote ambao kwa kweli Bunge zima hili leo ni ushuhuda kwamba, limekuwa likifuatilia miradi ya nishati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Oliver kwa swali lake zuri ameuliza kwamba, Vijiji vya Wilaya ya Ngara ni lini vitapatiwa nishati ya umeme. Nataka nimjibu kwamba, kama ambavyo tumekuwa tukitoa taarifa ndani ya Bunge lako na si taarifa tu kwamba labda ni porojo ni kweli, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli inatekeleza huu mradi kabambe wa kupeleka umeme katika vijiji vilivyosalia 7,873.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe pia ni shahidi. Jana wakati tunahitimisha taarifa ya Kamati yetu ya Nishati na Madini, Mheshimiwa Waziri wangu wa Nishati alitoa taarifa kuwashwa kwa umeme katika vijiji 24 katika utaratibu huu wa REA awamu ya tatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Wilaya ya Ngara Mkandarasi yupo anafanya kazi. Ameanza zile kazi za awali za upembuzi na kadhalika lakini kwa sasa Wakandarasi wote nchi nzima wana-mobilise vifaa na wengine wako site wanaendelea na kazi mbalimbali. Nataka nilitibitishie Bunge, ile awamu ya kwanza ambavyo ni vijiji 3,559 tumesema mpaka Juni, 2019 viwe vimekamilika halafu tunaanza safari nyingine ya kumalizia vijiji vingine. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina masawali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mgodi wa Kabanga Nickel una mda mrefu sana, kama nilivyouliza kwenye swali langu la msingi, tangu mwaka 1970 na wachimbaji walianza tangu mwaka 1973. Wananchi wa Ngara tulikuwa tukiona ndege za wazungu zikija na kuondoka wakidai kwamba wanapeleka sample na hawarudi tena, isije ikawa kama makinikia. Je, huu mgodi wa Kabanga Nickel utaanza lini rasmi ili wananchi wa Ngara na Serikali kwa ujumla tuweze kunufaika? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; Sheria na mauziano ya Makampuni inataka mnunuzi na muuzaji kulipa kodi ya Serikali. Mgodi wa Kabanga Nickel umekwisha kubadilisha wamiliki zaidi ya wanne. Je, Serikali Kuu na Halmashauri Kuu ya Wilaya ya Ngara imenufaika vipi na huo umiliki wa kubadilisha wamiliki kila mara?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimpongeze sana Mheshimiwa Semguruka kwa jinsi anavyofuatilia maslahi ya wananchi wa Mkoa wa Kagera pamoja na wananchi wa Ngara kwa ujumla wake. Nampongeza pia anavyoshirikiana na Waheshimiwa Wabunge wengine majirani wa Biharamulo, Ngara na wengine, hongera sana Mheshimiwa Semuguruka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na swali la kwanza. Ni kweli kabisa huu mradi umeanza tangu mwaka 2009, kwa kweli si miaka ya 1970 iliyopita. Hata hivyo niseme tu kwamba kazi inayofanyika sasa hivi ni kukamilisha upembuzi yakinifu, na natarajia kufungua mgodi mara tu baada ya bei ya nickel kuimarika. Hata hivyo tumempa muda wa mwaka asipofanya hivyo eneo hilo tutalichukua tutawamilikisha wawekezaji wengine wenye nia na uwezo wa kufanya kazi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, manufaa yatakayopatikana mgodi huo ukifunguliwa ni pamoja na kutoa ajira kwa wananchi wengi wa Bugarama na Kanyenyi, kadhalika watalipa mafao ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusiana na uhamishaji, Sheria za Kodi zinamtaka mmiliki yeyote akihamisha au kuuza hisa au leseni yake anatakiwa kulipa capital gain ya asilimia 10 na kwa upande wa Sheria ya Madini kifungu cha 9(1) cha mwaka 2010 kinataka mmiliki akianza kuhamisha analipa dola 3,000. Kwa hiyo, atakapofika hatua hiyo Mheshimiwa Semuguruka haya mafao ya Serikali yataingia. (Makofi)
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Nina swali dogo la nyongeza. Kwa nini Serikali isiwezeshe lishe kwa kaya duni ambazo zinatumia dawa za kupunguza makali ya UKIMWI?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hatuna mpango wa kuwezesha chakula kwenye kaya duni au kaya yoyote ile. Tunaamini wagonjwa na watu wengine wanapaswa kuhudumiwa na familia zao. Hata hivyo, tunatoa dawa ama kemikali ambazo zina nutritive effect, zina effect ya kuongeza lishe kwenye miili ya wagonjwa wanaotumia dawa hizi. Kwa hiyo, tunawapo multivitamins na dawa nyingine inatosheleza kwa kweli kuhimili mikikimikiki ya ART.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona niulize swali dogo la nyongeza. Tatizo la maji lililoko Kibamba linafanana kabisa na tatizo la maji lililoko Wilaya ya Ngara hasa Kata ya Mbuba, ambayo ina shule za sekondari mbili wanafunzi wanatembea kilomita mbili kwenda kufuata maji mabondeni na husababisha wanafunzi kukatisha masomo yao kwa kupata mimba na ukizingatia tamko la jana la Mheshimiwa Rais. Je, Serikali ina mpanga gani wa kumaliza tatizo hili, hasa katika Kata hii ili kunusuru ndoto za wadogo zetu, au watoto wetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba katika hizo shule mbili kiko kisima pale Ngara Mjini ambacho pampu yake ilikuwa imeharibika, tayari Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo hilo amefanya juhudi, mashine imepatikana. Wizara ya Maji na umwagiliaji tunampelekea fedha ili akaongeze mashine nyingine na kumpa fedha kwa ajili ya kutandika mabomba kutoka kwenye hicho chanzo ili shule zote mbili hizo ziweze kupata maji, tuondoe usumbufu wa watu kutembea mwendo mrefu na kupata hayo madhara ambayo unayazungumza.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona niulize swali dogo la nyongeza. Swali lililoulizwa namba 167 linafanana kabisa na Wilaya ya Ngara. Wilaya ya Ngara haina jengo la Mahakama, inatumia jengo la DC.
Je, ni lini Serikali itajenga Mahakama ya Wilaya Ngara? (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Ngara imepangiwa kujengewa Mahakama ya Wilaya katika mwaka wa 2019/2020 na pia Mahakama ya Mwanzo Lulenge mwaka 2019/2020. (Makofi)
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri; ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulingana na taarifa za viwanda tunazozisoma na kuzisikiliza kila siku, kwa jibu ni kuwa Kagera bado tuko nyuma katika viwanda. Sasa nini mpango wa Wizara yako kushirikiana na mimi pamoja na wananchi wa Mkoa wa Kagera kuhamasisha ujenzi wa viwanda?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, Serikali ina mpango gani wa kuwawezesha wananchi wa Kagera wajasiriamali wadogo wadogo ili waweze kupata mikopo ya riba nafuu ili waweze kufungua viwanda?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, jitihada za uhamasishaji zinaendelea, shughuli zinazofanywa na Wizara ya Mifugo za kuondoa uvuvi haramu zinalenga kuona kwamba katika ziwa letu tunapata samaki wa kutosha ili viwanda vya samaki viweze kujengwa. Lakini yako makampuni ambayo tumeshawasiliana nayo, kiwanda cha kutengeneza maziwa kitajengwa Kagera. Pia kampuni moja kutoka Uganda ya Uvan inataka kujenga kiwanda cha vanilla. Suala la uhamasishaji ni endelevu.
Nipende kukuahidi wewe na Wabunge wenzangu na wananchi katika Mikoa ambayo nataka kufanya kazi nayo ya uhamasishaji ni pamoja na Kagera, Kigoma, Mara, Katavi na Ruvuma. Katika miezi minne ijayo tutafanya kampeni kubwa…
…ya mazao ya shamba ambayo tunataka kuyaimiza yaweze kuzalisha bidhaa za viwandani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuwawezesha wananchi akina mama na akina dada kifedha…

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba tunao mfuko wa NADef. Jambo la muhimu si pesa, jambo la muhimu ni kwenda kupata idea na kupata mawazo SIDO. Mkishapata mawazo kupitia SIDO mtanufaika na mfuko wa NADef lakini iko mifuko mingine ambayo iko chini ya Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Nitakapozindua kitabu cha mwongozo wa kujenga viwanda kwa local government katika bajeti yangu siku ya Alhamisi kitabu hicho kitagawiwa mtaweza kujua pesa zinapatikana wapi.( Makofi)
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniona niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Ujenzi wa Kituo cha Polisi Keza, Wilaya ya Ngara, kilichojengwa kwa nguvu za wananchi, kitakamilika lini maana kina zaidi ya miaka saba kimeezekwa bado finishing. Je, ni lini Serikali itamalizia ujenzi huo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Kituo cha Keza nacho ni miongoni mwa vituo ambavyo havijakamilika. Bahati njema ni kwamba mwaka huu wa fedha katika Mkoa wa Kagera tumetenga takribani bilioni 1.56 kwa ajili ya kumaliza miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo haijakamilika, ikiwemo nyumba pamoja na vituo vya Polisi. Hiyo inaonesha azma ya Serikali ya kuweza kukabiliana na changamoto ya kumaliza vituo hivi ambavyo havijakamilika pamoja na nyumba za Askari nchi nzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba dhamira ya Serikali ipo na pale ambapo hali ya kifedha itakaa vizuri basi tutakamilisha kituo hicho pamoja na vituo vingine ambavyo kama alivyosema mwanzo kwamba viko sehemu mbalimbali katika nchi yetu. (Makofi)

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri na niwapongeze sana Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia hoja hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo Mheshimiwa Oliver Semuguruka amesema, ni kweli tuna vituo vingi ambavyo vimeshafikia hatua hiyo, niwapongeze sana Waheshimiwa Wabunge kwa sababu wamechangia kwa kiwango kikubwa sana. Kwa sababu ni wengi tu siwezi kuwataja wote, lakini natambua Mheshimiwa Maige, Mheshimiwa Ritta Kabati, Mheshimiwa Oran Njeza na wengine wengi ambao mmechangia ujenzi wa vituo hivi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kituo kilichoulizwa, Mheshimiwa Ulega hapa ndiye aliyekianzisha, niwaombe Waheshimiwa Wabunge kwa sababu wameongelea sana masuala haya ya vituo ambavyo vimeshafikia hatua ya kukamilishwa pamoja na nyumba za vijana wetu ambazo zimejengwa kwa nguvu za wananchi, kwa sababu bado tuko hapa na bajeti tumeshapitisha, niwaombe Waheshimiwa Wabunge wanipenyezee maeneo ambayo yana vituo hivyo ili tunavyomaliza Bunge twende tukae ngazi ya Wizara tuweze kuweka vipaumbele ili tusiharibu nguvu kazi za wananchi ambazo zimeshafanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Joseph Selasini ameliongelea sana jambo hili, leteni hivyo vituo ili tutakapokwenda kukaa kwenye ofisi tuweze kuona kile tulichonacho na kuweza kumalizia vile ambavyo vimeshafikia hatua za kumaliziwa. (Makofi)
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Swali namba 19 lililoulizwa linafanana kabisa na changamoto iliyopo Jimbo la Ngara. Hivi juzi tulishuhudia gari zikiungua border ya Rusumo na ikapelekea kifo cha dereva, hakukuwa na gari la zimamoto. Je, ni lini Serikali itatuletea gari la zimamoto Wilaya ya Ngara?
NAIBU WAZIRI MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Oliver kutokana na kuumwa kwake na maendeleo ya vyombo ama taasisi zetu zilizopo Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa Mkoa wa Kagera ikiwemo Jeshi la Zimamoto. Kuhusiana na Wilaya ya Ngara, ukiachilia mbali mikakati ambayo nimeizungumzia nikijibu swali la msingi la Mheshimiwa Aisharose Matembe ambalo linagusa Wilaya zote nchini, mikakati ni ile ile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tuna pia tuna mipango mingine mbalimbali ambayo tunaendelea nayo, ambayo tunaamini kabisa ikikaa sawa basi changamoto hii ya upungufu wa magari ya zimamoto itapungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mpango wa kuweza kupata mkopo kupitia nchi za Belgium na Australia ambayo itatuwezesha kupata vitendea kazi ikiwa ni pamoja na magari mapya kabisa. Michakato ya kupata mikopo hiyo nayo inakwenda vizuri na iko katika hatua nzuri pale ambapo itakapokuwa imekamilika naamini kabisa tukichanganya na mikakati niliyozungumza katika swali la msingi basi matatizo ya magari ya zimamoto na vitendea kazi nchini ikiwemo Ngara yatakuwa yamepungua kwa kiasi kikubwa. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Tatizo lililopo Mtwara linafanana kabisa na tatizo lililopo Mkoa wa Kagera. Umeme ukatika mara kwa mara hasa Bukoba Mjini, Bukoba Vijijini, Muleba, Missenyi na Karagwe. Je, ni lini tatizo hili la kukatika umeme litakwisha?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Oliver naye ameuliza ni lini Mkoa wa Kagera suala la kukatika kwa umeme litapungua kama siyo kumalizika kabisa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba ni kweli tunatambua Mkoa wa Kagera ambao kwanza wanapata umeme kutokea Uganda, tunanunua kama megawati 10 kutoka Uganda ambazo tunazisambaza katika maeneo yale, lakini Serikali pia kwa kuliona hilo, ndiyo maana sasa imejitahidi kuunganisha Wilaya za Ngara na Biharamulo kwenye Gridi ya Taifa. Mkakati huo unaendelea na pia tuna mpango wa kujenga transmission line ili umeme ambao utazalishwa katika maeneo ya Rusumo ambao tumeingiza megawati 80 tuweze kusambaza katika maeneo ya Mkoa wa Kagera na kuweza kutatua tatizo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namshukuru Mheshimiwa Mbunge na ninampongeza kwa ufuatiaji wake na Wabunge wote wa Viti Maalum ambao wanafuatilia sekta ya nishati, nawashukuru sana.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia kuchelewa kwa kesi hizi ni vidhibiti kutopelekwa maabara kwa Mkemia Mkuu haraka ili kuthibitisha. Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua changamoto hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa marekebisho ya sheria yaliyofanyika mwaka 2017, hivi sasa Sheria ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya Kifungu cha 4(n) ambacho kimeongezewa baada ya marekebisho kimeweka utaratibu wa kwamba hivi sasa kwa kuzingatia kwamba kuna mashauri mengi ambayo yanasimama kwa kusubiri vidhibiti kutoka katika Ofisi ya Mkemia Mkuu, sasa kupitia sheria hii imeanzishwa laboratory katika Ofisi ya Kamishna Jenerali ili kuhakikisha kwamba mamlaka pia nayo iwe na wajibu huo wa kuchunguza na kutoa taarifa ili kujaribu kusaidia expedite kesi hizi zisichukue muda mrefu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimwondolee hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ilichukua hatua kwa marekebisho hayo ya sheria na hivi sasa ukiacha Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Jeshi la Polisi lakini... kazi hiyo pia.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Changamoto iliyopo Njombe inafanana kabisa na changamoto iliyopo uwanja wa ndege wa Bukoba kwamba ni mfupi na kupelekea ndege kutua kwa shida au kuruka kwa shida mfano kama Bombadier. Je, ni lini Serikali itaongeza urefu wa uwanja huo?
NAIBU WAZIRI, UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS JOHN KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, nianzie uwanja wa ndege wa Bukoba, yako maboresho muhimu yamefanyika na huduma inaendelea vizuri na ndege zinashuka vizuri na miruko imeongezeka. Pia ule mpango wa kuuboresha uwanja huu tunaendelea na hatua ya kutathmini maeneo ambayo tutahamisha wananchi, Mheshimiwa Mbunge anafahamu ili sasa ule urefu wa sehemu ya kurukia na kutoa ndege iweze kuongezeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi kwamba zile hatua za kufanya maboresho ya viwanja mbalimbali nchini ziko kwenye mpango na Waheshimiwa Wabunge wanafahamu, mara kadhaa tumezungumza namna ya viwanja, hata leo nimerejea kuzungumza viwanja vingi ambavyo tunaendelea kujenga.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tutaendelea kuimarisha ili kuhakikisha kwamba tuna viwanja wa ndege ambavyo vitamudu kutoa huduma katika maeneo ya Mikoa yote. Tutaendelea kutoa maeneo mengine ambayo ni maalumu kama ilivyoonekana kwamba uwanja wa ndege wa Mafia, kama nilivyozungumza jana, tunaupeleka katika hatua uwe na hadhi ya kimkoa ili huduma ziongezeke.

Mheshimiwa Naibu Spika, viko viwanja vingine ambavyo tunaendelea kuvipanua. Kwa mfano, tunaendela kupanua uwanja wa ndege wa Kigoma, Tabora, Shinyanga na Bariadi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niwaambie tu Waheshimiwa Wabunge waamini tumejipanga kuhakikisha kwamba pamoja na Serikali kuendelea kuliboresha shirika letu kwa kununua ndege, italeta maana pale ambapo Serikali inanunua ndege na ndege zinaenda kuwahudumia Watanzania kwa ujumla. (Makofi)