Primary Questions from Hon. Ussi Salum Pondeza (30 total)
MHE. USSI SALUM PONDEZA AMJAD aliuliza:-
Kituo cha Polisi Maruhubi kinakabiliwa na matatizo mbalimbali kama vile ukosefu wa askari wa kutosha; kituo hakitoi huduma saa 24, lakini pia majengo yake ni machakavu sana kiasi kwamba hayana hadhi ya kuwa Kituo cha Polisi:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka askari wa kutosha katika kituo hicho na kuhakikisha kuwa kituo kinatoa huduma zake kwa saa 24?
(b) Je, ni lini Serikali itayakarabati majengo ya kituo hicho ili yaendane na hadhi ya Kituo cha Polisi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, Mbunge wa Chumbuni, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Kituo cha Polisi cha Maruhubi ni Kituo cha Daraja “C” ambacho taratibu za utoaji huduma kwa mujibu wa miongozo ya Jeshi la Polisi kitatoa huduma kuanzia saa 12.00 asubuhi hadi saa 12.00 jioni na kuwa na askari wasiozidi 20.
(b) Mheshimiwa Spika, Serikali itakifanyia ukarabati Kituo cha Maruhubi mara tu fedha zitakapopatikana.
MHE. SALUM MWINYI REHANI (K.n.y. MHE. USSI SALUM PONDEZA AMJADI) aliuliza:-
Hapo kwanza Maafisa Uhamiaji wetu walikuwa wakipelekwa kwenye Balozi zetu kufanya kazi ya kutoa viza kwa wageni wanaotaka kuja Tanzania lakini hivi sasa Maafisa hao hawafanyi tena kazi hiyo na badala yake kazi hizo zinafanywa na Maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na hutoa viza hata kwa waombaji wasiotakiwa kupewa:-
(a) Je, kwa nini Maafisa hao wa Uhamiaji waliondolewa kwenye Balozi hizo?
(b) Je, ni sahihi kwa Maafisa wa Mambo ya Nje kufanya kazi za kutoa viza kwa wageni?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, lenye sehemu mbili kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Balozi zake mbalimbali nje ya nchi na Ofisi za Wawakilishi wa Heshima (Honorary Consuls) imeendelea kutoa huduma ya viza kwa wageni mbalimbali wanaokusudia kusafiri kuja nchini Tanzania kwa madhumuni mbalimbali. Kazi ya kutoa viza hufanywa na Maafisa wa Serikali ambao wapo Ubalozini kwa nchi zenye Uwakilishi wa Kibalozi na Wawakilishi wa Heshima (Honorary Consuls) kwa maeneo ambayo Tanzania haina uwakilishi wa Kibalozi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi za Balozi za Tanzania nje ya nchi huwa na Maafisa wa aina mbalimbali wakiwemo Maafisa Mambo ya Nje, Maafisa kutoka Idara ya Uhamiaji, Waambata Jeshi pamoja na Maafisa kutoka Idara mbalimbali za Serikali kwa kadri ya mahitaji ya Ubalozi husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, sehemu kubwa ya Maafisa katika Ofisi za Ubalozi huwa ni Maafisa wa Mambo ya Nje. Kutokana na Idara ya Uhamiaji kutokuwa na Maafisa Uhamiaji katika baadhi ya Balozi zake, kazi ya utoaji viza katika baadhi ya Balozi zisizo na Maafisa wa Uhamiaji hufanywa na Maafisa wa Mambo ya Nje. Kazi hiyo huongozwa na taratibu na misingi maalum ya kisheria kama ilivyoainishwa katika Sheria ya Uhamiaji, Sura ya 54 ya mwaka 2002.
Mheshimiwa Mwenyekiti, majukumu ya Maafisa Uhamiaji katika Balozi hizi ni kama ifuatavyo:-
(i) Utoaji wa viza kwa wageni wanaotaka kutembelea Tanzania;
(ii) Kushughulikia pasi za kusafiri za Watanzania wanaoishi katika nchi za uwakilishi;
(iii) Kutoa hati za kusafiria za dharura kwa Watanzania walipoteza pasi zao za kusafiria au ambao wameingia nchi za uwakilishi bila pasi za kusafiria;
(iv) Kutembelea magereza zenye wafungwa ambao ni raia wa Tanzania; na
(v) Kuthibitisha uraia wa wageni ambao hufika Ubalozini na kujitambulisha kuwa ni Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upangaji wa Maafisa Uhamiaji katika Balozi zetu hufanywa na Idara ya Uhamiaji. Maafisa hao hupangwa katika Balozi zetu kulingana na mahitaji ya Idara hiyo. Mathalani Idara ya Uhamiaji iliwarudisha Bwana Sylvester Ambokile aliyekuwa Afisa Uhamiaji London na kuteuliwa kuwa Kamishna Mkuu wa Uhamiaji Makao Makuu na Bwana Johari Sururu ambaye alikuwa Afisa Uhamiaji Abu Dhabi na kuteuliwa kuwa Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar. Hivyo, jukumu la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ni kuwezesha maafisa hawa kutekeleza majukumu yao pindi wanapokuwa vituoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kama ilivyokwishaelezwa si Balozi zote za Tanzania nje ya nchi zina Maafisa Uhamiaji. Hivyo, uwepo wa Maafisa Mambo ya Nje au Maafisa wengine wa Serikali katika Balozi hizo wanaotoa viza kwa wageni mbalimbali wanaokusudia kuja Tanzania hauna madhara yoyote kwa kuwa shughuli hiyo hufanywa kwa kuongozwa na utaratibu na misingi maalum ya kisheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu haina taarifa inayoonyesha kuwa kuna Maafisa Mambo ya Nje ambao wamekuwa wakitoa viza kwa waombaji wasiostahili katika Balozi zetu zilizo nje ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. USSI SALUM PONDEZA aliuliza:-
Baadhi ya watumishi wa DEPU mwaka 1999 – 2000 na Idara ya Uhamiaji hawajapandishwa vyeo mpaka sasa, licha ya kuwa na vigezo kama vya elimu na ngazi ya shahada huku wenzao wakiwa wamefikia vyeo vya Makamishna na Kamishna wasaidizi.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia watumishi kupata haki yao ya vyeo stahiki kama ilivyo kwa wenzao waliopandishwa vyeo?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, Mbunge wa Chumbuni, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, watumishi wa Idara ya Uhamiaji walioajiriwa mwaka 1999 – 2000 walikuwa na viwango tofauti vya elimu kama vile wengine wakiwemo kidato cha nne, wengine wa kidato cha sita, stashahada na wengine wakiwa na shahada. Katika watumishi wote hao hakuna aliyekuwa amefikia cheo cha Kamishna au Kamishana Msaidizi kama Mheshimiwa Mbunge alivyouliza.
Mheshimiwa Naibu Spika, watumishi hao kwa sasa wametofautiana vyeo kutokana na sababu zifuatazo:-
Moja, waliajiriwa katika vyeo tofauti kulingana na elimu zao wakati wanaajiriwa na kujiunga katika mafunzo ya awali ya uhamiaji.
La pili; baadhi yao walijiendeleza kielimu wakati wapo katika ajira ili kuinua viwango vyao vya elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuchukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria na kupelekea wengine kusimamishwa kupata vyeo kama ambavyo iko kwenye Sheria za Utumishi wa Taasisi hii.
MHE. USSI SALUM PONDEZA aliuliza:-
Mgonjwa anapotoka Zanzibar na kupelekwa kwa matibabu nje ya nchi analazimika kupata rufaa kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili licha ya kuwepo kwa Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja, Zanzibar ambayo ina madaktari wenye uwezo kama wale wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
(a) Je, kwa nini Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja haijapewa uwezo wa kutoa rufaa ya matibabu nje ya nchi?
(b) Je, kuinyima uwezo huo Hospitali ya Mnazi Mmoja ni kutoiamini hospitali hiyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, Mbunge wa Jimbo la Chumbuni, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, sio kweli kwamba Hospitali ya Mnazi Mmoja haina uwezo wa kutoa rufaa kwa wagonjwa wanaohitaji kupelekewa nje ya nchi kwa huduma za afya ambazo hazipatikani katika hospitali hiyo. Hospitali ya Mnazi Mmoja ina uwezo na ina utaratibu wake wa kutoa rufaa kwa wagonjwa wanaolazimika kupelekwa nje ya nchi kwa matibabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo Hospitali ya Mnazi Mmoja inaweza kutoa rufaa kwa wagonjwa kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili au hospitali nyingine yoyote watakayoona inafaa. Aidha, wagonjwa wengine kutoka Zanzibar huwa wanakuja Tanzania Bara kupata huduma za hospitali zilizopo bara bila kupata rufaa ya Hospitali ya Mnazi Mmoja. Wagonjwa hawa wanapohitaji kupelekwa nje ya nchi watapewa rufaa na hospitali ya mwisho inayowapa huduma kwa wakati huo. Hospitali hiyo inaweza kuwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili au nyingine yoyote ile ya ngazi ya Kitaifa. Wagonjwa hawa hawawezi kurudishwa Zanzibar kwenda kupewa rufaa.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, si kweli kuwa hospitali ya Mnazi Mmoja imenyimwa uwezo wa kutoa rufaa kwa wagonjwa wanaotakiwa kupelekwa nje ya nchi kwa uchunguzi na matibabu. Hospitali ya Mnazi Mmoja ina uwezo kamili wa kutoa rufaa kwa wagonjwa wanaotakiwa kupelekwa nje ya nchi na imejiwekea utaratibu wake wa kufanya hivyo.
MHE. FAUSTINE E. NDUGULILE (K.n.y. MHE. USSI SALUM PONDEZA AMJADI) aliuliza:-
Sheria ya kuwalinda wafanyakazi wa mahotelini na majumbani imekwama kutungwa Zanzibar na Tanzania Bara kutokana na Azimio lililofikiwa na Shirika la Kazi la Umoja wa Mataifa (ILO) kutoridhiwa na Bunge tangu Mkataba kusainiwa mwaka 2011, mkataba ambao unataka kila nchi mwanachama kuwa na Sheria ya kulinda haki za wafanyakazi hao:-
(a) Je, ni sababu zipi zinazosababisha azimio hilo kutowasilishwa Bungeni tangu Tanzania iliposaini Azimio la ILO wakati nchi nyingine zimeanza utekelezaji wake zikiwemo za Afrika Mashariki?
(b) Kwa kuwa Zanzibar haiwezi kutunga Sheria zake za kulinda haki za wafanyakazi wa mahotelini na majumbani mpaka azimio hilo lipelekwe na Ofisi yako Bungeni na kuridhiwa ndiyo kila upande utunge Sheria zake kutokana na mambo ya kazi kuwa sio ya Muungano: Je, ni lini Bunge litapokea azimio hilo la kulinda haki za wafanyakazi hao?
(c) Je, Serikali inawaeleza nini Vyama vya Wafanyakazi wa Mahotelini na Majumbani ambao walianza kufanya matayarisho ya utekelezaji wa azimio hilo, lakini wamekwama kutokana na mkataba huo kutoridhiwa na Bunge tangu kuafikiwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, Mbunge wa Chumbuni, lenye sehemu (a), (b) na (c) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa mwaka 2011, nchi wanachama wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) ikiwemo Tanzania, zilipitisha Mkataba wa Kimataifa kuhusu kazi za staha kwa wafanyakazi wa majumbani (Convention No.189 on Decent Work for Domestic Workers). Hadi sasa nchi zilizoridhia mkataba huu ni 23 kati ya nchi wanachama 189. Kwa upande wa Afrika ni nchi mbili tu zilizoridhia ambazo ni Afrika Kusini na Mauritius. Serikali inaendelea kupitia kwa makini sana maudhui ya mkataba huo ili kufanya maandalizi ya kuuridhia.
Mheshimiwa Naibu Spika, masuala ya kazi na ajira siyo ya Muungano. Tanzania ina Sheria za Kazi, hali kadhalika na Zanzibar pia wana Sheria za Kazi ambazo zinawahusu wafanyakazi wote wakiwemo wafanyakazi wa mahotelini na majumbani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa nchi yetu inazo sheria mbalimbali zinazotambua na kusimamia maslahi ya wafanyakazi nchini, wakiwemo wafanyakazi wa majumbani, wafanyakazi na vyama vyao waendelee kutambua juhudi za Serikali na kulinda na kutetea haki na maslahi ya wafanyakazi kupitia sheria, kanuni na taratibu tulizonazo. Serikali itaendelea kuelimisha jamii na wadau mbalimbali kuhusu mifumo, maudhui na taratibu za uridhiaji wa mikataba ili kufanya maandalizi stahiki kabla ya uridhiaji wa mikataba hiyo.
MHE. USSI SALUM PONDEZA aliuliza:-
Askari Polisi Zanzibar kwa muda mrefu wamekuwa wakilazimika kutumia fedha zao za mfukoni kuwahudumia chakula mahabusu wanoshikiliwa katika Vituo vya Polisi Unguja wakati jukumu hilo ni la Serikali.
(a) Je, Serikali imechukua hatua gani za kuondoa tatizo hilo tangu kulalamikiwa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora baada ya kufanya ziara ya ukaguzi na kugundua tatizo hilo?
(b) Je, ni sababu gani zimepelekea chakula kutopelekwa katika Vituo vya Polisi wakati Bunge limekuwa likiridhia matumizi ya Wizara kila mwaka zikiwemo gharama za chakula kwa mahabusu?
(c) Je, haki za binadamu zinazingatiwa vipi inapotokea askari hawana fedha za kununua chakula cha mahabusu na kulazimika kulala na njaa wakati Serikali ndiyo yenye jukumu la kuwapatia huduma ya chakula?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ussi Pondeza, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, mahabusu wanaoshikiliwa katika Vituo ya Polisi huhudumiwa na Jeshi la Polisi kwa kuwapatia mahitaji muhimu kama chakula na malazi. Serikali kupitia Jeshi la Polisi imekuwa ikitenga bajeti kwa ajili ya chakula cha mahabusu kwa kila mwaka.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, si kweli kwamba chakula huwa hakipelekwi katika mahabusu za polisi. Chakula hupelekwa kulingana na idadi ya mahabusu kama ambavyo taratibu za utoaji wa chakula zinavyoelekeza katika PGO 356.
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, kulisha mahabusu walioko katika Vituo ya Polisi ni jukumu la Serikali na si askari mmoja mmoja kutumia fedha zake za mfukoni kwa kufanya jukumu hilo. Serikali itaendelea kutimiza wajibu huo na hakuna uvunjaji wa haki za binadamu katika kuwapatia huduma za chakula mahabusu.
MHE. USSI SALUM PONDEZA AMJAD aliuliza:-
Kumekuwa na malalamiko ya matokeo ya uchunguzi yanayofanywa kwa kutumia mashine ya kutambua vinasaba (DNA) kutoka Zanzibar kutopatikana kwa wakati na kusababisha kesi mbalimbali kushindwa kusikilizwa kwa wakati muafaka zikiwemo za jinai kama ubakaji.
(a) Je, kwa nini matokeo ya uchunguzi yamekuwa yakichukua muda mrefu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili wakati uchunguzi huo una umuhimu mkubwa katika kupambana na vitendo vya uhalifu?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza mashine za kutosha ili uchunguzi ufanyike kwa wakati kutokana na vitendo vya udhalilishaji wanawake na watoto kuendelea kuongezeka baina ya pande mbili za Muungano?
(c) Je, ni lini Hospitali ya Taifa Muhimbili itaweka utaratibu wa kuchunguza sampuli za Zanzibar kwa wakati kwa kutumia mashine ya kuchunguza vinasaba (DNA)?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, Mbunge wa Jimbo la Chumbuni, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, sampuli za uhalali wa watoto kwa wazazi (paternity case samples) zinafanyika kwa wepesi zaidi kuliko sampuli za makosa ya jinai (criminal case samples) kwa sababu sampuli za paternity zinachukuliwa moja kwa moja toka kwa wahusika (direct samples) na hivyo kurahisisha uchunguzi wake endapo wahusika wa uchukuaji watachukua kwa umahiri na uhifadhi utafanyika kwa namna stahili. Aidha, sampuli za uchunguzi wa makosa ya jinai (criminal case files) zinachukuliwa toka maeneo ya matukio, kwenye crime scene, hivyo, uchunguzi wake unaweza kuchukua muda zaidi kutegemeana na aina ya sampuli na eneo zilipotoka.
(b) Mheshimiwa Spika, mikakati ya Serikali katika kuongeza mashine za kutosha ili kuwezesha uchunguzi ufanyike kwa wakati kwa vielelezo vya makosa ya jinai, ikiwa ni pamoja na vitendo vya udhalilishaji wa wanawake na watoto, Serikali imedhamiria kununua mashine tatu za vipimo vya vinasaba (DNA) ili vitumike katika maabara za kanda, na hivyo kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi kwa Bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018.
(c) Mheshimiwa Spika, vipimo vya vinasaba (DNA) kwa ajili ya uhalali wa watoto kwa wazazi (paternity) na kesi za jinai (criminal case) vinafanywa na Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na sio Hospitali ya Muhimbili.
MHE. USSI SALUM PONDEZA aliuliza:-
Katiba ya Jamhuri ya Muungano inatambua uwepo wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.
(a) Je, kwa nini ripoti za Tume hiyo hazitolewi kwa muda muafaka kila mwaka kama masharti ya Katiba yanavyosema?
(b) Je, ripoti ya mwisho ya Tume hiyo ilitolewa mwaka gani na lini imewasilishwa Bungeni?
(c) Je, kwa nini harakati za Tume hiyo katika kushughulikia migogoro ya ardhi, ukaguzi wa vituo vya polisi, magereza pamoja na matukio ya uvunjaji wa haki za binadamu umezorota kinyume na miaka ya nyuma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, Mbunge wa Chumbuni, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 131(3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaelekeza Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kuwasilisha taarifa zake kwa Waziri mwenye dhamana ya masuala ya haki za binadamu ambaye hutakiwa kuwasilisha taarifa hizo nbele ya Bunge mapema iwezekanavyo. Taarifa hizo ni muhtasari wa masuala yote yaliyofanyika katika mwaka husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa huko nyuma taarifa za Tume zilikuwa zikichelewa kuwasilishwa Bungeni kwa wakati. Hata hivyo, mwezi Desemba, 2017, Tume imewasilisha taarifa zake za nyuma hadi mwaka 2014/2015 kwa Waziri mwenye dhamana ili aziwasilishe Bungeni. Taarifa ya mwaka 2015/2016 ipo katika hatua ya mwisho ya uchapaji na itakapokuwa tayari itawasilishwa kwa Waziri mwenye dhamana. Taarifa ya mwaka 2016/2017 ipo katika maandalizi na inasubiri kukamilika kwa taarifa ya ukaguzi wa hesabu za Tume.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya mwisho iliyotolewa na kuwasilishwa Bungeni ilikuwa ya kipindi cha mwaka wa fedha 2013/2014.
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo, kweli kwamba utendaji wa Tume umezorota, Tume imeendelea kufanya kazi zake kama zilivyoainishwa katika Katiba na Sheria. Aidha, Tume imekuwa ikiongeza jitihada kila mwaka kukagua vituo vya polisi, magereza, vituo vya mafunzo kwa upande wa Zanzabar, kufuatilia migogoro ya ardhi na kufuatilia utekelezaji wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora kwa ujumla. Lengo kuu la ukaguzi na ufuatiliaji huu ni kutathmini hali ya haki za binadamu na misingi ya utawala bora na kutoa mapendekezo kwa taasisi husika. Vilevile Tume imekuwa ikifuatilia utekelezaji wa haki za makundi mbalimbali ambayo ni pamoja na watoto hususani watoto walio katika mkinzano na sheria, wanawake na watu wenye ulemavu.
MHE. FAUSTINE E. NDUGULILE (K.n.y. MHE. USSI SALUM PONDEZA AMJADI) aliuliza:-
Sheria ya kuwalinda wafanyakazi wa mahotelini na majumbani imekwama kutungwa Zanzibar na Tanzania Bara kutokana na Azimio lililofikiwa na Shirika la Kazi la Umoja wa Mataifa (ILO) kutoridhiwa na Bunge tangu Mkataba kusainiwa mwaka 2011, mkataba ambao unataka kila nchi mwanachama kuwa na Sheria ya kulinda haki za wafanyakazi hao:-
(a) Je, ni sababu zipi zinazosababisha azimio hilo kutowasilishwa Bungeni tangu Tanzania iliposaini Azimio la ILO wakati nchi nyingine zimeanza utekelezaji wake zikiwemo za Afrika Mashariki?
(b) Kwa kuwa Zanzibar haiwezi kutunga Sheria zake za kulinda haki za wafanyakazi wa mahotelini na majumbani mpaka azimio hilo lipelekwe na Ofisi yako Bungeni na kuridhiwa ndiyo kila upande utunge Sheria zake kutokana na mambo ya kazi kuwa sio ya Muungano: Je, ni lini Bunge litapokea azimio hilo la kulinda haki za wafanyakazi hao?
(c) Je, Serikali inawaeleza nini Vyama vya Wafanyakazi wa Mahotelini na Majumbani ambao walianza kufanya matayarisho ya utekelezaji wa azimio hilo, lakini wamekwama kutokana na mkataba huo kutoridhiwa na Bunge tangu kuafikiwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, Mbunge wa Chumbuni, lenye sehemu (a), (b) na (c) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa mwaka 2011, nchi wanachama wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) ikiwemo Tanzania, zilipitisha Mkataba wa Kimataifa kuhusu kazi za staha kwa wafanyakazi wa majumbani (Convention No.189 on Decent Work for Domestic Workers). Hadi sasa nchi zilizoridhia mkataba huu ni 23 kati ya nchi wanachama 189. Kwa upande wa Afrika ni nchi mbili tu zilizoridhia ambazo ni Afrika Kusini na Mauritius. Serikali inaendelea kupitia kwa makini sana maudhui ya mkataba huo ili kufanya maandalizi ya kuuridhia.
Mheshimiwa Naibu Spika, masuala ya kazi na ajira siyo ya Muungano. Tanzania ina Sheria za Kazi, hali kadhalika na Zanzibar pia wana Sheria za Kazi ambazo zinawahusu wafanyakazi wote wakiwemo wafanyakazi wa mahotelini na majumbani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa nchi yetu inazo sheria mbalimbali zinazotambua na kusimamia maslahi ya wafanyakazi nchini, wakiwemo wafanyakazi wa majumbani, wafanyakazi na vyama vyao waendelee kutambua juhudi za Serikali na kulinda na kutetea haki na maslahi ya wafanyakazi kupitia sheria, kanuni na taratibu tulizonazo. Serikali itaendelea kuelimisha jamii na wadau mbalimbali kuhusu mifumo, maudhui na taratibu za uridhiaji wa mikataba ili kufanya maandalizi stahiki kabla ya uridhiaji wa mikataba hiyo.
MHE. MACHANO OTHMAN SAID (K.n.y. MHE. USSI SALUM PONDEZA) aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itachukua hatua dhidi ya wauzaji wakubwa wa dawa za kulevya wanaoingiza na kuuza badala ya kuakamata waathirika ambao wanahitaji misaada na ushauri nasaha wa kuachana na matumizi ya dawa hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. ANTONY P. MAVUNDE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, Mbunge wa Chumbuni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imejipanga na inaendelea kukabiliana na wafanyabiashara wakubwa na wadogo wa dawa za kulevya ambao wote wanasababisha madhara kwa jamii kwa kufanya biashara hiyo. Hadi kufikia Februari, 2018 jumla ya wanyabiashara 3,486 wa dawa za kulevya walikamatwa na kufikishwa mahakamani. Kati ya hao zaidi ya asilimia 30 ni wafanyabiashara wakubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wamekimbia nchini kutokana na ukali wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Namba Tano ya mwaka 2015 na marekebisho yake ya mwaka 2017 pamoja na udhibiti unaofanywa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola. Aidha, Serikali imeendelea kudhibiti matumizi ya dawa za kulevya kwa kutoa elimu ya madhara ya dawa za kulevya kwa watumiaji na jamii kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa wale walioathirika kwa kutumia dawa za kulevya, wanapopatikana Serikalini imekuwa ikijikita zaidi kutoa ushauri nasaha, tiba na kuwahamasisha kupata tiba hiyo kwani hutolewa bure. Hadi kufikia mwezi Februari, 2018 zaidi ya warahibu 5,560 wamendelea kupata tiba katika vituo vya Serikali, mpango wa Serikali ni kusambaza huduma hii nchi nzima ili kuwafikia waathirika wengi wenye uhitaji.
MHE. USSI SALUM PONDEZA aliuliza:-
a) Je, katika kipindi cha mwaka 2016/2017, ni vijana/ wanafunzi wangapi walikosa vigezo vya kupata mkopo wa elimu ya juu?
b) Je, Serikali inatumia utaratibu gani kuwatambua wanafunzi wanaotoka katika familia maskini katika utaratibu wa utoaji wa mikopo ya elimu ya juu?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI (K.n.y. WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA
TEKNOLOJIA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, Mbunge wa Chumbuni lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa masomo 2017/2018, jumla ya wanafunzi 46,131 waliomba mikopo. Maombi ya mkopo ya wanafunzi hawa yalichambuliwa ili kupima uhitaji wao kwa kuzingatia Sheria ya Bodi ya Mikopo Sura ya 178 na mwongozo wa utaoji wa mikopo kwa mwaka 2017/2018.
Baada ya uchambuzi wa maombi hayo kukamilika, Serikali kupitia Bodi ya Mikopo iliwapangia mikopo wanafunzi 33,920 wa mwaka wa kwanza ambao maombi yao yalikidhi vigezo na sifa zilizoainishwa katika sheria na mwongozo uliotolewa 2017/2018. Waombaji wengine 12,211 hawakupangiwa mkopo kwa sababu hawakukidhi vigezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu na sifa za utoaji mikopo ya elimu ya juu unaongozwa na sheria iliyoanzishwa na Bodi nya Mikopo ya Elimu ya Juu, Sura namba 178. Kwa mujibu wa sheria hii mikopo ya elimu ya juu inapaswa kutolewa kwa Watanzania wahitaji na wenye sifa yaani need and eligible.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kifungu namba 17 cha sheria ya Bodi ya Mikopo kimetaja sifa kuu kuwa ni Utanzania, aliyedahiliwa katika Taasisi ya Elimu ya Juu inayotambulika na Serikali, asiwe na vyanzo vingine vinavyogharamia masomo yake na kwa wanafunzi wanaoendelea na masomo wawe wamefaulu mitihani yao kuwawezesha kuendelea na mwaka unaofuata
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, sheria inaipa mamlaka Serikali kupitia Bodi ya Mikopo kuandaa utaratibu na mwongozo wa utoaji mikopo kwa wahitaji wenye sifa. Katika mwaka wa masomo 2017/2018, Serikali kupitia Bodi ya Mikopo iliandaa mwongozo unaopatikana katika tovuti ya Bodi ya Mikopo (www.heslb.go.tz).
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwongozo pia ulitoa kipaumbele kwa makundi maalum kama yatima, wenye ulemavu, au wenye wazazi wenye ulemavu na wale ambao masomo yao ya sekondari ya stashahada yalifadhiliwa na wafadhili mbalimbali.
MHE. MACHANO OTHMAN SAID (K.n.y. MHE. USSI SALUM PONDEZA AMJADI) aliuliza:-
Vijana wa Kitanzania wanakabiliwa na tatizo sugu la ukosefu wa ajira na hivyo nguvu kazi kupotea badala ya kutumika kwa uzalishaji:-
(a) Je, Jeshi la Kujenga Taifa lina mpango gani wa kutumia nguvu kazi ya vijana kwa kuanzisha miradi ya kilimo cha kisasa ili kuondoa tatizo la ajira?
(b) Je, ni vijana wangapi wamenufaika na ajira kwa kila mwaka kupitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT)?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, Mbunge wa Chumbuni, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mafunzo ya kijeshi ambayo vijana huyapata kwa muda wa miezi sita, vijana hao pia hujifunza shughuli mbalimbali za uzalishaji mali katika kambi wanazopangiwa baada ya mafunzo ya kijeshi. Shughuli hizo hufanyika ndani ya mwaka mmoja na nusu kati ya miaka miwili ambayo wanajitolea wanapokuwa JKT. Baada ya kumaliza muda huo, tunaamini kwamba vijana wanakuwa wamepata ujuzi ambapo wanaweza kujiajiri au hata kuajiriwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Kujenga Taifa lina mashamba makubwa ya kilimo yanayotumia pembejeo na zana za kisasa za kilimo kama vile mbegu bora, matrekta, mashine za kupandia na mashine za kuvunia (harvesters) hutumika. Mashamba hayo hulimwa kama mashamba darasa kwa ajili ya kuwafundishia vijana walioko JKT. JKT hulima mashamba hayo, si kwa lengo la kuajiri vijana, bali kuwapatia ujuzi ambao watautumia baada ya kumaliza muda wa mafunzo ya JKT. Baada ya kumaliza mafunzo wanaweza kuanzisha miradi ya kilimo cha kisasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mafunzo hayo, vijana hupewa mafunzo ya ujasiriamali ikiwa ni pamoja na mafunzo ya ufugaji wa nyama, samaki na nyuki, kupanda na kuvuna miti ya mbao, kuongeza thamani ya mazao ya nafaka na mbegu za mafuta ambayo Wizara ina imani kwamba yatawawezesha vijana hawa kujitegemea kwa kutumia stadi za ufundi, kilimo, mifugo na uvuvi walivyojifunza wakiwa JKT.
Mheshimiwa Mwenyekiti, idadi ya vijana walioajiriwa na vyombo vya ulinzi na usalama kuanzia mwaka 2003 hadi 2017 jumla yao ni 42,593. Aidha, idadi ya vijana 3,576 wameajiriwa na SUMAJKT Guard Ltd.
MHE. USSI SALUM PONDEZA aliuliza:-
(a) Je, ni viwanda vingapi vimeanzishwa tangu Serikali ya Awamu ya Tano ianze utekelezaji wa mpango wa kuimarisha uchumi wa kati wa viwanda?
(b) Je ni viwanda vingapi vilibinafsishwa na kushindwa kuendelezwa ambavyo vimerejeshwa Serikalini tangu kuanza utekelezaji wa mpango wa kuimarisha uchumi wa kati wa viwanda?
(c) Je sekta ya viwanda inachangia kiasi gani pato la Taifa?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali na Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, Mbunge wa Chumbageni, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na juhudi za kujenga uchumi wa viwanda zinazofanywa na Serikali ya Awamu Tano, tangu iingie madarakani hadi kufikia Disemba, 2018 jumla ya viwanda 3,504 vimeanzishwa nchini. Viwanda hivyo vinajumuisha viwanda vidogo sana 2,500; viwanda vidogo 943; viwanda vya kati 51; na viwanda vikubwa 10.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu kwa kushirikiana na Ofisi ya Msajili wa Hazina imekuwa ikifanya tathmini ya viwanda 156 vilivyobinafsishwa na kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukulia kwa viwanda 68 ambavyo havijaendelezwa. Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ilijiridhisha na mapendekezo yaliyotolewa na kuiwezesha Ofisi ya Msajili wa Hazina kuchukua hatua. Kutokana na kuchukua hatua hiyo tayari viwanda 14 vimesharejeshwa Serikalini na juhudi za kuvitafutia wawekezaji wengine walio tayari kuviendeleza zinaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa hali ya uchumi ya mwaka 2017, mchango wa sekta ya viwanda katika pato la Taifa ni asilimia 5.5, ikilingalishwa na asilimia 4.9 ya mwaka 2016, sawa na ongezeko la asilimia 0.6.
MHE. USSI SALUM PONDEZA aliuliza:-
Wananchi wa Kisakasaka, Mkoani Mjini Magharibi Unguja wamekuwa na mgogoro wa ardhi wa muda mrefu na Kambi ya Jeshi la Wananchi na hivyo kuathiri shughuli zao za kiuchumi:-
(a) Je, Serikali imechukua hatua gani kumaliza mgogoro huo?
(b) Je, ni sababu gani zimesababisha mgogoro huo kudumu zaidi ya miaka 40?
(c) Je, ni lini Taasisi husika za Serikali zitakaa pamoja na kumaliza mgogoro huo?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, Mbunge wa Chumbuni lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Kambi ya Kisakasaka yenye ukubwa wa hekari 490 ilianzishwa mwaka 1978 lengo likiwa ni kulinda anga na Manispaa ya Mji wa Zanzibar na vituo muhimu. Eneo hilo liliwahi kupimwa mwaka 1985 lakini halikuwahi kupatiwa hatimiliki kwa sababu Sheria mpya ya Ardhi ya Zanzibar Na. 12 ya mwaka 1992 haikutambua upimaji uliofanywa kabla ya hapo. Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa inatambua uwepo wa mgogoro husika na imekuwa ikichukua hatua kadhaa kuumaliza kama ifuatavyo:-
(i) Mwaka 2013 fedha kiasi cha Sh.4,150,000/= kililipwa kwa Idara ya Upimaji na Ramani ya Zanzibar ili kufanya kazi ya upimaji na kuandaa hatimiliki. Kazi hii haijafanyika kwa sababu wananchi hawakuridhika na upimaji huo.
(ii) Katika muendelezo wa kumaliza mgogoro huo, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi alitembelea aneo hilo na kuridhia mipaka irekebishwe kwa kuzingatia maslahi mapana ya Jeshi na mahitaji ya ardhi kwa wananchi.
(b) Mheshimiwa Spika, baadhi ya sababu zilizopelekea mgogoro kudumu kwa muda mrefu ni kukosekana kwa fedha za kugharamia kazi za upimaji, uthamini na ulipaji fidia katika maeneo yaliyotwaliwa na Jeshi.
(c) Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imekubali kuunda Kikosi Kazi kitakachopitia maeneo yote yenye migogoro kwa Zanzibar ambacho kitatoa mapendekezo ya kudumu ya kumaliza migogoro hiyo.
MHE. USSI SALUM PONDEZA aliuliza:-
Viongozi wa Kitaifa wanaofanya ziara Tanzania walikuwa wakifika Zanzibar na kuonana na Rais wa Zanzibar:-
(a) Je, kwa nini katika siku za karibuni viongozi hao wamekuwa wakiishia Tanzania Bara?
(b) Je, ni viongozi wangapi wa Kimataifa ikiwemo Marais ambao wamefanya ziara Tanzania katika kipindi cha 2016/2017 na nchi wanazotoka?
(c) Je, kati ya viongozi hao wangapi wamefika Zanzibar na wangapi hawakufika na kwa sababu gani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza Mbunge wa Chumbuni len ye kipengele (a), (b) na (c) kama ifuatavyo;
Mheshimiwa Spika, kwa kawaida viongozi wa Kitaifa wanapokuja nchini wanakuwa na ratiba ya maeneo ambayo wameyaainisha kuyatembelea kulingana na muda waliopanga kuwepo nchini. Pamoja na hilo Wizara imekuwa ikiwashauri viongozi hao kuzuru maeneo m balimbali ya nchi hususan Zanzibar ili pamoja na mambo mengine kukutana na kufanya mazungumzo rasmi na viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo Zanzibar.
Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2015 hadi Aprili, 2019 jumla ya viongozi 21 wa Kimataifa walitembelea Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Viongozi hawa walitoka katika nchi za Afrika Kusini, Burundi, Chad, Cuba, Ethopia, India, Jamhuri ya Democrasia Congo, Jamhuri ya Korea, Msumbuji, Morocco, Mauritius, Misri, Malawi, Rwanda, Uturuki, Uganda, Vietnam, Sudan Kusini, Sri Lanka, Switzerland, Zambia na Zimbabwe.
Mheshimiwa Spika, kati ya viongozi hao wa Kimataifa waliotembelea Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tisa walifika Zanzibar na 12 kati yao hawakufika Zanzibar. Sababu zinazopelekea kutofika kwao ni kutokana na aina ya ziara, ratiba ya ziara husika na ufinyu wa muda katika ziara. Sababu nyingine ni vipaumbele na malengo ya ziara za viongozi hao pamoja na utashi wa kiongozi husika. Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeendelea kushauri viongozi wa Kitaifa kutoka nchi za kigeni wanaozuru nchini kutembelea Zanzibar katika ratiba zao. Aidha, Wizara kupitia Idara ya Mambo ya Nje Zanzibar imekuwa ikifanya maandalizi stahiki ya kiitifaki ili kurahisisha viongozi hao kutembelea Zanzibar.
MHE. JAKU HASHIM AYUOB (K.n.y. MHE. USSI SALUM PONDEZA) aliuliza:-
Kumekuwa na malalamiko ya bidhaa zinazozalishwa Zanzibar kupata vikwazo kuingia katika Soko la Tanzania Bara:-
(a) Je, Serikali imechukua hatua gani kuondoa tatizo hilo katika kulinda misingi ya Muungano hasa baada ya maziwa na sukari kuwekewa vikwazo zaidi?
(b) Je, Zanzibar inaweza vipi kutumia Soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki wakati soko la ndani bado bidhaa zinazozalishwa zinawekewa vikwazo?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ussi Pondeza Mbunge wa Chumbuni, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka utaratibu mahsusi wa kushughulikia changamoto zisizo za Muungano zikiwemo za kibiashara ili kuimarisha Muungano wetu. Utaratibu huo huendeshwa kwa kutumia vikao vya ushirikiano wa kisekta ambapo Ofisi ya Makamu wa Rais imetoa mwongozo kwa sekta za pande mbili za Muungano kujadili changamoto kupitia vikao kuanzia ngazi ya Wataalam, Makatibu Wakuu na Mawaziri na kushauri mamlaka za maamuzi. Utaratibu huo unazingatia pia kutekeleza matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 katika kuimarisha Muungano wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, chini ya utaratibu huo, Sekta ya Viwanda na Biashara kwa nyakati tofauti imekuwa ikipokea, kujadili na kutafutia ufumbuzi changamoto za biashara zilizoibuliwa kutoka pande zote mbili za Muungano. Baadhi ya bidhaa zilizowahi kushughulikiwa chini ya utaratibu huo ni pamoja na kuku, sukari, maziwa na bidhaa nyinginezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia utaratibu huo, mwaka 2019 Wizara ya Viwanda na Biashara (SMT) na Wizara ya Biashara na Viwanda (SMZ) kwa pamoja zilipewa maagizo ya kushughulikia malalamiko kuhusu suala la sukari kutoka Zanzibar kuingia Tanzania Bara. Wizara hizo ziliunda Timu ya Pamoja ya Wataalam ambao walichambua suala hilo na kuwasilisha taarifa yake kwa Viongozi wa Wizara hizo mwezi Septemba, 2019 kwa hatua zinazofuata. Hivi sasa suala hilo linafanyiwa kazi kupitia ngazi zilizobainishwa ili hatimaye maamuzi yaweze kufanyika. Hivyo, namuomba Mheshimiwa Mbunge aendelee kuwa na subira katika suala hilo na yale yanayofanana nalo yanayoendelea kushughulikiwa ili kupata suluhu ya kudumu, yenye tija na maslahi mapana kwa pande zote mbili za Muungano.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa jitihada anazofanya kufuatilia kwa karibu na kushauri namna ya kuboresha na kuimarisha masuala yanayohusu biashara kati ya pande hizi mbili za Muungano.
MHE. USSI SALUM PONDEZA AMJADI aliuliza:-
Vituo vingi vidogo vya Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja vimefungwa na kuwapa wakati mgumu wananchi wanapohitaji huduma ya polisi wakati vilikuwa vinasaidia kupambana na uhalifu kwa wakati muafaka:-
(a) Je, ni kwa sababu gani vituo hivyo vimefungwa na wananchi kulazimika kupata huduma katika vituo vikubwa kinyume na malengo ya kuanzishwa kwake?
(b) Je, ni kwa nini vituo vya Kilimani, Mkunazini, Mlandege pamoja na vituo vingine vimefungwa na wananchi kulazimika kufuata huduma umbali mrefu?
(c) Je, hatua ya kufunga vituo hivyo inasaidia vipi katika kupambana na uhalilfu hasa katika maeneo ya katikati ya mji wa Zanzibar na Serikali ina mpango gani na majengo yake?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, Mbunge wa Chumbuni, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Vituo vya Polisi vimegawanyika katika madaraja matatu, ambayo ni Daraja A, B na C. Utendaji kazi wa vituo hivi unazingatia Kanuni za Kudumu za Jeshi la Polisi (POG). Mathalani, kwa mujibu wa PGO 287(2), vituo Daraja A na B vinatakiwa kufunguliwa na kufanya kazi saa 24 na vituo Daraja C vinatakiwa kufunguliwa na kufanya kazi saa 12 tu kuanzia saa 12.00 asubuhi hadi 12.00 jioni.
(b) Mheshimiwa Spika, vituo ambavyo havitumiki kwa sasa ikiwemo vituo vidogo vya Mwembeladu, Shaurimoyo na Forodhani inatokana na sababu mbalimbali ikiwemo uchakavu, vipaumbele kwenye mgawanyo wa rasilimali watu na kadhalika. Aidha, kwa sasa maeneo hayo ambayo yalikuwa yanahudumiwa na vituo hivyo yanahudumiwa na vituo vikuu ya polisi vilivyo karibu.
(c) Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Jeshi la Polisi inapambana na vitendo vya uhalifu maeneo ya katikati ya Mji wa Zanzibar kwa kuimarisha ulinzi, misako na doria.
MHE. USSI SALUM PONDEZA Aliuliza:-
(a) Je, Serikali haioni kuwa umefika wakati wa wanafunzi wote kunufaika kwa 100% bila kujali shule walizosoma?
(b) Je, Serikali inawasaidiaje wazazi waliostaafu ambao wameshindwa kuchangia gharama za elimu ya juu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA Alijibu: -
Mheshimwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, Mbunge wa Jimbo la Chumbuni lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo: -
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, mikopo inayotolewa na Serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu inaongozwa na Sheria ya Bodi ya Mikopo (SURA 178) ambayo inaelekeza kuwa walengwa wa mikopo hiyo ni wahitaji (needy).
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa uhitaji wa mwanafunzi hupimwa kwa kuchambua taarifa zilizowasilishwa wakati wa maombi ya mkopo, zikiwemo gharama za masomo ya sekondari au stashahada. Uchambuzi huu hutumia king’amua uwezo (means testing tool) ambacho hubaini kiwango cha uhitaji cha mwombaji mmoja mmoja ukilinganisha na wengine.
Aidha, uhitaji wa mnufaika unatumika kuamua kiasi anachopangiwa kulingana na gharama ya shahada aliyodahiliwa. Baada ya uchambuzi linganishi, waombaji hupangiwa mikopo kulingana na uhitaji wao. Katika mwongozo, vigezo na sifa za kunufaika na mikopo ya elimu ya juu, hakuna kigezo mahususi cha shule aliyosoma mwombaji na mnufaika.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu waombaji wa mikopo ambao wazazi wao wamestaafu katika utumishi, Serikali inaamini utaratibu wa sasa wa kutambua na kuwapangia mikopo wahitaji wanaotoka katika familia zisizo na uwezo wa kumudu gharama za elimu ya juu kwa watoto wao unajitosheleza. Hata hivyo, Serikali ipo tayari kuendelea kupokea maoni ya namna ya kuboresha zaidi utaratibu huu.
MHE. USSI SALUM PONDEZA aliuliza: -
(a) Je, kwanini Serikali isihamishe Kambi za Jeshi la Wananchi (JWTZ) Zanzibar ambazo zipo katikati ya makazi ya watu kutokana na kasi ya maendeleo ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza? na
(b) Je, Serikali inachukua hatua gani za kumaliza mgogoro wa muda mrefu wa mpaka kati ya wakulima na JWTZ kambi ya Kisakasaka?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda nitoe shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu. Kwa kuniteua kuwa Mbunge na hatimaye kuniteua kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Lakini pia na kwako kwa ushirikiano ambao nimekuwa nikiupata tangu niteuliwe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya hapo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, Mbunge wa Chumbuni kama ifuatavyo: -
(a) Mheshimiwa Spika, Makambi na Vikosi vya Ulinzi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania yameundwa kwa Mamlaka ya Sheria ya Ulinzi wa Taifa Na. 24 ya Mwaka 1966, ambayo imefanyiwa marekebisho na Sheria Na. 192 ya Mwaka 2002. Makambi haya na Vikosi yamejengwa kimkakati kukabiliana na tishio lolote dhidi ya Nchi yetu. Maeneo haya ni muhimu sana kwa ulinzi na usalama.
(b) Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua uwepo wa migogoro baina ya Jeshi na wananchi wa Vijiji vya Sheha za Kisakasaka, Mwangani, Kombani, Fuoni na Kondemaji. Kwa nyakati tofauti serikali imefanya jitihada za kutatua mgogoro huu. Hivi sasa Wizara yangu inatekeleza Mkakati maalum wa miaka mitatu wa kupunguza au kumaliza kabisa migogoro ya ardhi baina ya Jeshi na wananchi.
Mheshimiwa Spika, kulingana na Mpango huu, Wizara imepanga kufanya upimaji na uthamini katika maeneo haya niliyoyataja katika robo ya pili ya Mwaka wa Fedha 2021/ 2022 ambayo ni robo hii. Wizara inawaomba wananchi kuendelea kuwa na subira wakati Wizara ikiendelelea na utekelezaji wa Mkakati huu wa upimaji na uthamini wa maeneo yote ya Jeshi.
(c) Mheshimiwa Spika, naomba pia nitoe rai kwa wananchi wanaoishi jirani na maeneo ya Jeshi, kuacha kuvamia maeneo hayo kwani ni hatari kwa usalama wao, na ni vigumu kwa Jeshi kuhamisha makambi kwa kuwa makambi hayo yamejengwa kimkakati. Nawasilisha. (Makofi)
MHE. USSI SALUM PONDEZA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itafanya ziara kwenye Vituo vya Polisi vya zamani na nyumba za kuishi Askari Unguja na Pemba ili kushuhudia uchakavu uliopo na ni kiasi gani kimetengwa kwa ajili ya matengenezo ya Vituo vya Polisi nchini kwa Mwaka 2021/2022?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, Mbunge wa Chumbuni, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali ilishatembelea na kuona uchakavu wa vituo vya polisi na nyumba za makazi ya askari huko Zanzibar na maeneo mengine ya Tanzania Bara. Zoezi la kufanya tathmini ya uchakavu kujua gharama zinazohitajika ili kufanya ukarabati zinaendelea nchi nzima. Zoezi hili litakapokamilika, Serikali itatenga fedha kwa ajili ya ukarabati kulingana na upatikanaji wa fedha kwa mwaka ujao (2022/2023) kama ilivyofanyika mwaka huu.
Mheshimiwa Spika, katika Bajeti ya Serikali ya mwaka 2021/2022, Serikali imetenga fedha kiasi cha shilingi 2,000,000,000 kwa ajili ya ukarabati wa Vituo vya Polisi na ujenzi wa nyumba za askari. Ahsante sana.
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI K.n.y. MHE. USSI SALUM PONDEZA aliuliza: -
Je, ni kwa nini kusiwe na Mahakama ya Rufaa Tanzania Kanda ya Zanzibar badala ya kesi kusikilizwa kwa mwaka mara moja?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, Mbunge wa Chumbuni, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Mahakama ya Rufaa Kanda ya Zanzibar ipo kwa sasa na inaendesha shughuli zake kupitia Masijala ndogo iliyopo Jengo la Mahakama Kuu ya Zanzibar. Hata hivyo, Serikali inaona umuhimu wa kuwa na jengo la Mahakama ya Rufani Zanzibar na inaendelea kulifanyia kazi.
MHE. USSI SALUM PONDEZA aliuliza: -
(a) Je, ni kwa nini Serikali isiongeze uzalishaji wa mafuta ya alizeti nchini kwa ajili ya Soko la Zanzibar na Bara kuliko kuagiza kutoka nje ya nchi?
(b) Je, hali ya uzalishaji wa mafuta ya alizeti ikoje kwa mwaka na ni mikoa gani inayozalisha zaidi Tanzania Bara?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, Mbunge wa Chumbuni lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza mkakati wa kuongeza uzalishaji wa mazao ya mafuta nchini kwa lengo la kupunguza uagizaji wa mafuta ya kula na kuongeza uzalishaji kutoka wastani wa tani 700,000 hadi tani 1,500,000 ifikapo mwaka 2025. Utekelezaji wa mpango huo unajumuisha ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji kwenye mashamba ya mbegu ya Wakala wa Mbegu za Kilimo ambapo kwa mwaka 2022/2023 jumla ya shilingi bilioni 43.03 zitatumika kwa lengo hilo.
Mheshimiwa Spika, mahitaji ya mafuta ya kula nchini ni tani 650,000 kwa mwaka. Tathmini ya mwaka 2020/2021 inaonesha kuwa uzalishaji wa ndani wa mafuta ya alizeti ni asilimia 75 ya kiasi cha wastani wa tani 300,000 za mafuta ya kula yanayozalishwa nchini kwa mwaka. Mikoa inayozalisha alizeti kwa wingi ni Singida, Dodoma, Manyara, Shinyanga, Iringa, Tabora, Morogoro, Ruvuma, Mbeya, Arusha, Lindi, Mtwara, Rukwa na Mara.
MHE. USSI SALUM PONDEZA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itajenga majengo ya Wizara ya Elimu Zanzibar ili kutoa huduma kwa wakati na kupunguza gharama za kukodi Ofisi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, Mbunge Chumbuni, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Zanzibar kuna Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, yenye majengo yake, ambayo ina Idara ya Elimu ya Juu inayoongozwa na Mkurugenzi kwa lengo la kuhakikisha kuwa wanafunzi wa elimu ya juu wanapata huduma. Vilevile, zipo Taasisi za Elimu ya Juu zinazotoa huduma kwa wanafunzi kama vile; Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Taasisi ya Sayansi na Teknolojia Karume, Taasisi ya Sayansi ya Bahari (IMS) na Tume ya Taifa Sayansi na Teknolojia (COSTECH).
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kujenga ofisi katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kusogeza huduma za elimu karibu na wananchi kulingana na upatikanaji wa fedha. Aidha, ni nia ya Serikali kuhakikisha kuwa kila Taasisi ya Umma inakuwa na majengo yake kwa lengo la kupunguza gharama za kukodi ofisi. Nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. ABDUL-HAFAR IDRISSA JUMA K.n.y. MHE. USSI SALUM PONDEZA aliuliza: -
Je, ni nchi ngapi zimeshafungua Ofisi zao za Ubalozi Jijini Dodoma baada ya zoezi la kuhamisha Makao Makuu ya Serikali Dodoma?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Pondeza Mbunge wa Chumbuni, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, hadi sasa nchi tatu zimeshafungua Ofisi Ndogo za Ubalozi Jijini Dodoma. Nchi hizo ni Uingereza, Ujerumani na China. Hata hivyo, Wizara inaendelea kuzishawishi nchi nyingine kufungua Ofisi zao hapa Jijini Dodoma.
Mheshimiwa Spika, katika hatua nyingine baadhi ya Mashirika ya huduma za jamii na maendeleo ya Umoja wa Mataifa yameshafungua Ofisi zake Jijini Dodoma. Mashirika hayo ni pamoja na UNDP, UNICEF, UN Women, WFP, WHO, UNFPA, FAO, IFAD, IOM, UNAID, UNCDF na UNIDO.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. RASHID A. SHANGAZI K.n.y. MHE. USSI SALUM PONDEZA aliuliza: -
Je, lini hatua iliyobakia katika mchakato wa kupata Katiba Mpya itakamilishwa?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, naomba kujibu sasa swali la Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, Mbunge wa Chumbuni, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutambua umuhimu wa mchakato wa kupata katiba mpya aliunda kikosi kazi kilichoongozwa na Profesa Mukandara ambacho pamoja na masuala mengine, ilikuwa ni kuhuisha mchakato wa Katiba mpya. Katika hilo, kikosi kazi hicho kimetoa mapendekezo ya hatua sita za kufuatwa katika kukamilisha mchakato wa kupata Katiba Mpya. Hatua hizo ni hizi zifuatazo: -
(i) Kuwepo kwa mjadala wa Kitaifa wa kupata muafaka wa masuala ya msingi;
(ii) Kuhuisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba;
(iii) Kuundwa kwa Jopo la Wataalam wa kuandaa Rasimu ya Katiba;
(iv) Rasimu ya Katiba kupitishwa na Bunge;
(v) Kutoa elimu ya uraia; na
(vi) Rasimu ya Katiba kupigiwa kura na wananchi.
Mheshimiwa Spika, baada mapendekezo ya kikosi kazi, tarehe 6 Mei, 2023, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassani, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alimuagiza Msajili wa Vyama vya Siasa kuitisha Kikao Maalum cha Baraza la Vyama vya Siasa wakiwemo wadau mbalimbali kujadili mapendekezo ya kikosi kazi na kupendekeza taratibu za kuzingatia katika kuanzisha mchakato wa kupata Katiba mpya. Ahsante.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID K.n.y. MHE. USSI SALUM PONDEZA aliuliza:-
Je, ni tafiti ngapi za mafuta zimefanyika nchini na yapi matokeo ya tafiti hizo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Nishati napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, Mbunge wa Chumbuni, Kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania kwa kushirikiana na Kampuni za Kimataifa za Nishati imeendelea na tafiti za mafuta na gesi nchini kwa maeneo ya baharini na nchi kavu ambapo hadi kufikia mwezi Januari, 2024, jumla ya tafiti 84 zimefanyika.
Mheshimiwa Spika, kupitia tafiti ambazo zimeshafanyika, tumeweza kugundua uwepo wa gesi asilia tu. Hata hivyo, TPDC inaendelea na utafutaji wa mafuta katika maeneo ambayo yana viashiria vya uwepo wa mafuta. Maeneo hayo yanajumuisha bonde la Eyasi Wembere, Ziwa Tanganyika na bonde la Kilosa-Kilombero, ahsante.
MHE. USSI SALUM PONDEZA aliuliza:-
Je, sababu gani zilisababisha maduka ya kubadilisha fedha kuondolewa katika biashara na wananchi wengi kupoteza ajira zao?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, Mbunge wa Chumbuni, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mwaka 2016, Benki Kuu ya Tanzania ilifanya ukaguzi wa maduka ya kubadilisha fedha za kigeni na kugundua miamala mbalimbali kwa baadhi ya maduka kinyume na matakwa ya sheria na kanuni za usimamizi wa maduka ya fedha za kigeni na udhibiti wa utakatishaji wa fedha haramu. Kufuatia hali hiyo, mwaka 2018 na 2019, Benki Kuu kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za Serikali ilifanya operation ya ukaguzi maalum kwenye maduka yote ya kubadilisha fedha za kigeni nchini na kubaini makosa mbalimbali ikiwemo:-
(i) Kutofanya utambuzi wa wateja kabla ya kutoa huduma kinyume na kifungu cha 15(1) cha Sheria ya Udhibiti wa Utakatishaji Fedha Haramu, Sura 423 na kanuni ya 17 ya Kanuni za Udhibiti wa Utakatishaji Fedha Haramu;
(ii) Kugawa miamala ya wateja kwa lengo la kukwepa kutunza kumbukumbu muhimu zinazoonyesha uhalali wa miamala kinyume na Kanuni ya 23(4) ya Kanuni za Biashara ya Kubadilisha Fedha za Kigeni, 2015;
(iii) Kutokutoa stakabadhi za miamala kinyume na Kanuni ya 23(1) ya Kanuni za Biashara ya Kubadilisha Fedha za Kigeni, 2015;
(iv) Kutokuwasilisha taarifa sahihi za miamala Benki Kuu na hivyo kuathiri upatikanaji wa takwimu muhimu kwa ajili ya shughuli za kiuchumi; na
(v) Baadhi ya maduka yalikuwa yanajihusisha na uhamishaji wa fedha nje ya nchi bila kuwa na kibali au leseni kutoka Benki Kuu.
Mheshimiwa Spika, baada ya operesheni hiyo, Benki Kuu ya Tanzania ilibatilisha leseni za maduka ya kubadilisha fedha za kigeni yaliyokutwa na makosa. Maamuzi hayo yalifanyika kwa mujibu wa Kanuni ya 36(1)(b) na 2(d) ya Kanuni za Biashara ya Kubadilisha Fedha za Kigeni, 2015 iliyorejewa mwaka 2019, ahsante.
MHE. RAMADHANI SULEIMAN RAMADHANI K.n.y. MHE. USSI SALUM PONDEZA aliuliza:-
Je, lini Serikali itaamua kuwekeza kwa nguvu katika Viwanja, Walimu na Mawakala wa michezo inayoonekana kuleta tija kwa Taifa?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, Mbunge wa Chumbuni, ambalo limeulizwa kwa niaba yake na Mheshimiwa Ramadhan Suleiman Ramadhan, Mbunge wa Chakechake, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza ujenzi wa viwanja vya mpira wa miguu vya Arusha, Dodoma, Fumba-Zanzibar, Ilemela Jijini Mwanza pamoja na Akademia na Hosteli katika Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya. Vilevile, Serikali inaendelea na ukarabati wa Viwanja vya Benjamin Mkapa na Uhuru – Dar es Salaam, Amani na Gombani vya Zanzibar kwa ajili ya maandalizi ya CHAN 2023 na AFCON 2024. Aidha, Serikali inaendelea na mpango wa ukarabati wa miundombinu ya shule 56 za michezo pamoja na viwanja vitano vya mpira wa miguu vya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha kuwa kuna walimu wa kutosha wa michezo, Serikali imekuwa ikiongeza udahili katika vyuo vinavyotoa mafunzo ya walimu wa michezo, hususan Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Hadi kufikia mwaka 2023/2024 jumla ya wanafunzi 812 wamehitimu katika Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Baraza la Michezo la Taifa imeendelea kusajili Mawakala wa Michezo mbalimbali, ambapo jumla ya mawakala 233 walisajiliwa kuanzia mwaka 2018 hadi mwezi Desemba, 2023, ahsante.
MHE. FESTO R. SANGA K.n.y. MHE. USSI SALUM PONDEZA aliuliza:-
Je, Serikali inachukua hatua gani kwa wananchi wanaochukua mafuta baada ya magari ya kubeba mafuta kupata ajali?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Adhabu, Sura ya 16, kama ilivyofanyiwa marejeo Mwaka 2022, Kifungu cha 258 na 265, ni kosa Kisheria kuchukua mali ya mtu mwingine bila idhini ya mwenye mali ama kuwa na dai la haki. Hivyo, kitendo cha kuchukua mafuta baada ya magari ya kubeba mafuta kupata ajali, bila kuruhusiwa na mwenye mali, ni kutenda kosa la wizi. Serikali kupitia Jeshi la Polisi imeendelea kuwachukulia hatua za Kisheria wahalifu wote waliokamatwa kwa kosa hilo na kuwafikisha Mahakamani. Ahsante sana.
MHE. USSI SALUM PONDEZA aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu ya uzalendo kwa wananchi wakati Taifa lipo katika mageuzi makubwa ya uchumi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, Serikali imekuwa ikitoa elimu ya uzalendo kwa wananchi kupitia majukwaa mbalimbali kama vile vyombo vya habari na matamasha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Serikali kwa kutambua umuhimu wa kutoa elimu ya uzalendo kwa kizazi cha sasa na baadaye, ilifanya maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 pamoja na Mitaala ya Elimu ya Awali, Msingi, Sekondari na Vyuo vya Ualimu wa mwaka 2023 ambapo katika maboresho hayo elimu ya uzalendo imetiliwa mkazo na itakuwa ikifundishwa katika Somo la Historia ya Tanzania na Maadili kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha sita. Somo hili litabeba maudhui yanayolenga kumjenga Mtanzania kuwa mzalendo na mwajibikaji anayefahamu historia, desturi, mila na maadili ya nchi yake.