Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Yussuf Salim Hussein (7 total)

MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN aliuliza:-
Kuna idadi kubwa ya vijana wa Tanzania ambao wanafanya kazi nje ya nchi zikiwemo kazi za ndani (house girls):-
(a) Je, kuna utaratibu gani unatumika kwa vijana hao kwenda kufanya kazi hizo nje ya nchi?
(b) Je, vijana wangapi wanafanya kazi hizo nje ya nchi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yussuf Salim Hussein, Mbunge wa Chambani kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ili kuratibu ajira za Watanzania wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi, Serikali imeweka utaratibu wa kutumia Wakala wa Serikali wa Huduma za Ajira Tanzania (TaESA) na kurasimisha wakala binafsi wa huduma za ajira ambao wana jukumu la kuwaunganisha watafuta kazi na waajiri wa ndani na nje ya nchi. Kabla wakala binafsi hajampeleka mfanyakazi nje ya nchi anapaswa kuwasiliana na TaESA kwa lengo la kuhakiki mikataba ya kazi na kupeleka taarifa za mfanyakazi kwa Balozi wetu katika nchi husika.
Mheshimiwa Spika, aidha, sheria haikatazi Mtanzania kujitafutia kazi na kwenda kufanya kazi nje bila kupitia utaratibu huu. Hivyo, wapo baadhi ya Watanzania wanaokwenda nje kufanya kazi kwa utaratibu wao binafsi. Napenda kuchukua nafasi hii kuwaomba wananchi wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi kufuata utaratibu mzuri uliowekwa na Serikali ambao utawawezesha kusaidiwa na Serikali hususani wakati wanapopata matatizo kupitia Balozi zetu.
Mheshimiwa Spika, jumla ya Watanzania wapatao 4,992 waliopitia utaratibu rasmi uliowekwa na Serikali kupitia TaESA wanafanya kazi nje ya nchi yetu ya Tanzania.
MHE. HAFIDH ALI TAHIR (K.n.y. MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN) aliuliza:-
Suala la raia kupigwa na kuharibiwa mali zao kwa upande wa Zanzibar limekuwa likiongezeka siku hadi siku;
Je, Serikali inatambua tatizo hili na kama inatambua inachukua hatua gani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Yussuf Salim Hussein, Mbunge wa Chambani kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kwamba kila inapofika wakati wa Uchaguzi Mkuu hasa katika kisiwa cha Pemba baadhi ya watu hujichukulia sheria mkononi kwa kuwapiga wengine na kuharibu mali zao. Aidha, Serikali itaendelea kuongeza vikosi vya ulinzi na usalama katika maeneo yote tete na kuhakikisha utii wa sheria bila shuruti unazingatiwa. Pia Serikali itaendelea kuelimisha wananchi madhara ya kujichukulia sheria mkononi dhidi ya wengine wasio na hatia.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kupitia Bunge lako Tukufu nitoe wito kwa wananchi wote kuacha mihemko na itikadi za kisiasa wakati na kabla ya uchaguzi kwani hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI (K.n.y. MHE. YUSUPH SALIM HUSSEIN) aliuliza:-
Kumekuwa na matumizi ya uvuvi haramu wa kutumia mabomu katika mwambao wa bahari ya Tanga na Pemba:-
(a) Je, Serikali inafahamu athari za mabomu yayopigwa chini ya maji?
(b) Je, Serikali imechukua hatua gani kukomesha aina hiyo ya uvuvi.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yussuf Salim Hussein, Mbunge wa Chambani, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inafahamu athari za mabomu yanayotumiwa baharini kwa nia ya kuua samaki na viumbe wengine. Matumizi ya mabomu kwa nia ya kuvua samaki yana athari kubwa kwa samaki na mazingira ya baharini kwa kuwa huua samaki na viumbe wengine, uharibu matumbwawe ambayo ni mazalia na makulia ya samaki, uharibifu wa mazingira na ikolojia ya bahari ikiwemo mfumo wa maisha ya samaki. Pia, ni tishio kwa maisha ya binadamu na usalama wa nchi kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, athari nyingine ni pamoja na kupungua kwa rasilimali za uvuvi, kupoteza kipato, kuongezeka kwa mmomonyoko wa fukwe za bahari; huathiri afya za walaji na shughuli za utalii katika Hifadhi za Bahari na maeneo tengefu. Uharibifu huu unapofanyika unachukua miongo mingi zaidi ya miaka 100 kurudi kwenye hali yake ya awali kutegemea aina ya matumbawe na mazingira yaliyoharibika.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nilitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba mabomu siyo zana ya uvuvi bali ni silaha ya kivita na maangamizi. Aidha, jukumu la kudhibiti uvuvi wa kutumia mabomu, Halmashauri ndizo zenye maeneo ya uvuvi kisheria, Sheria ya Uvuvi namba 22 ya mwaka 2003 na kanuni zake za mwaka 2009 zimekasimu mamlaka ya udhibiti na usimamizi wa rasilimali za uvuvi katika Halmashauri zote nchini. Wizara ina jukumu la kuandaa na kusimamia utekelezaji wa sera, sheria na kanuni zinazotumika katika uhifadhi, udhibiti na usimamizi wa rasilimali za uvuvi nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuongeza nguvu ya kudhibiti uvuvi haramu Serikali ilianzisha mfumo wa kushirikisha jamii katika vikundi vya usimamizi shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (Beach Management Unit) kwa lengo la kuwaelimisha wananchi juu ya athari ya matumizi ya mabomu na uvuvi haramu kwa ujumla na faida za kuwa na uvuvi endelevu kwa manufaa yao na Taifa kwa ujumla ili waweze kusimamia rasilimali hiyo kwani wavuvi haramu hutoka miongoni mwao. Hata hivyo, juhudi hizo hazijaweza kukomesha matumizi ya mabomu katika uvuvi baharini kwa kuwa vyanzo vya mabomu ni kwenye migodi ya madini, ujenzi wa barabara na mengine hutengenezwa kienyeji na wavuvi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua ukubwa wa tatizo hili Serikali imeunda kikosi kazi kwa lengo la kushughulikia uharibifu wa kimazingira ikiwemo kudhibiti uvuvi haramu na mabomu kinachoundwa na wajumbe kutoka Ofisi ya Rais; Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka; Wizara ya Mambo ya Ndani; Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa; Nishati na Madini; Maliasili na Utalii; Kilimo, Mifugo na Uvuvi; na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na kinakaratibiwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP).
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuziagiza Halmashauri za Ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi kushirikiana na jamii kusimamia kikamilifu udhibiti wa uvuvi wa mabomu, ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua za kisheria wale wanaojihusisha na uvuvi na mabomu.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN aliuliza:-
Karibu theluthi moja ya ardhi ya Tanzania ni misitu na kuna uhaba mkubwa wa watalaam wa misitu nchini.
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kukiboresha Chuo cha Misitu cha Olmotonyi?
(b)Je, kila mtalaam wa misitu aliyepo leo anasimamia hekta ngapi za eneo?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yussuf Salim Hussein, Mbunge wa Chambani, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba kuna upungufu wa watalaam wa misitu nchini. Kwa sasa kila mtalaam wa misitu aliyepo anasimamia jumla ya hekta 25,000 za misitu. Kimsingi uwiano huu ni mara tano zaidi ya uwiano unaokubalika Kimataifa wa mtaalam mmoja kwa hekta 5, 000. Kwa kutambua hali hii, Wizara yangu imeanza kutatua tatizo hili kwa kuboresha miundombinu ya Chuo cha Misitu Olmotonyi.
Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na Serikali ya Norway inatekeleza mradi wa kuwezesha jamii kupitia mafunzo ya shughuli za usimamizi shirikishi wa mistu na mabadiliko ya tabianchi. Mradi huu unalenga kukijengea chuo uwezo kwa kukarabati nyumba za watumishi saba, kuimarisha maktaba ya chuo kwa kuweka samani, vitabu vya kiada na vitabu 137 vya mada 22 tofauti, vifaa 62 vya kufundishia, kompyuta 15 na kutoa mafunzo ya kompyuta kwa wakutubi watano; ukarabati wa mtandao wa mawasiliano na kuunganisha chuo na Mkongo wa Taifa.
Mheshimiwa Spika, pia mradi unaendelea na ujenzi wa bweni moja lenye uwezo wa kuchukua wanachuo 100 na ukumbi wa mihadhara wenye uwezo wa kuchukua wanachuo 200 kwa wakati mmoja. Vilevile mradi umewajengea uwezo wa kutumia mbinu bora za kufundisha wahadhiri 16 wa chuo hicho. Mradi unatoa mafunzo kwa jamii ya vijijini kuhusu kuhifadhi misitu na shughuli mbadala za kiuchumi.
Mheshimiwa Spika, kupitia mradi huu, Serikali inatoa ufadhili kwa wananfunzi wa ngazi za cheti na ngazi za diploma ili waweze kukamilisha mafunzo yao katika chuo chetu.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miaka mitatu, kuanzia mwaka 2013/2014 mpaka 2015/2016, Wizara kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania imegharamia ukarabati wa nyumba tisa za watumishi, kumbi za chakula na mikutano; na ununuzi wa kompyuta mbili na basi aina ya Tata kwa ajili ya usafiri wa wanafunzi wanapokwenda kupata mafunzo nje ya chuo.
Mheshimiwa Spika, kutokana na hatua hizi, chuo kumeongeza uwezo wake wa kupokea wanafunzi wengi zaidi na kuwajengea uwezo wawe wataalamu mahiri katika ngazi ya masomo yao.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN aliuliza:-
Kumekuwa na ongezeko kubwa sana la uwekezaji katika sekta ya utalii nchini:-
Je, Serikali imejipanga vipi ili kukabiliana na ongezeko hilo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yussuf Salim Hussein, Mbunge wa Chambani, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba kumekuwa na ongezeko la uwekezaji katika miundombinu na mahitaji mengine yanayochangia ukuaji wa sekta ya utalii nchini; ikiwa ni pamoja na ujenzi wa hoteli za aina na madaraja mbalimbali, uimarishaji wa vyombo vya usafiri kuelekea ndani ya hifadhi na maeneo mengine yeye vivutio na uboreshaji wa vifaa mbalimbali vinavyotumika kuhudumia watalii; mambo ambayo kwa kiwango kikubwa hutekelezwa na sekta binafsi.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Serikali, pamoja na mambo mengine, ujenzi wa barabara na viwanja vya ndege uliokamilika na unaoendelea, ununuzi wa ndege mbili uliokamilika na zingine nne zinazotarajiwa kuja nchini katika siku za karibuni, zote ni jitihada zinazochangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa sekta ya utalii nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mafanikio haya yamewezesha kuongezeka kwa idadi ya watalii ambapo mwaka 2016 idadi hiyo iliongezeka kutoka jumla ya watalii 1,137,182 wa mwaka 2015 hadi jumla ya watalii 1,284,279 kwa mwaka 2016. Hii ikiwa sawa na ongezeko la asilimia 12.9 na ongezeko linaloendelea kuonekana katika hifadhi moja kwa moja ikiwa ni pamoja na eneo la Hifadhi la Ngorongoro na Hifadhi za Taifa zinazosimamiwa na TANAPA.
Mheshimiwa Spika, ili kufanya ongezeko hilo liwe na tija na endelevu Wizara yangu imejikita katika kusimamia ubora wa huduma na utoaji huduma, kutangaza zaidi vivutio hususan vivutio vipya na kusambaza shughuli za utalii nchi nzima hususan Ukanda wa Kusini (The Southern Circuit) ili kutimiza azma ya Serikali kwa mujibu wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa Mwaka 2016/2017 – 2020/ 2021 unaoainisha utanuaji wa uwigo wa mazao ya utalii (diversification of tourism products) kama mojawapo ya hatua muhimu za kuchukua (key interventions) katika kukuza utalii nchini.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu inatoa wito wa sekta binafsi kuongeza mbinu, bidii na mitaji kuunga mkono jitihada za Serikali katika kukuza utalii na uchumi wa Taifa kwa ujumla.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN aliuliza:-
Je, ule mpango wa Serikali wa kuzalisha vifaranga na kuwapa wafugaji umefikia wapi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yussuf Salim Hussein, Mbunge wa Chambani kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa Serikali wa kuzalisha na kusambaza vifaranga kwa wafugaji wa samaki unaendelea kutekelezwa kupitia bajeti ya kila mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imeendelea na mkakati wake wa kuimarisha miundombinu ya uzalishaji wa vifaranga bora vya samaki katika vituo vyake vya Kingolwira (Morogoro), Mwamapuli (Tabora) na Ruhila (Ruvuma) ambapo kwa kipindi cha mwaka 2009/2010 mpaka mwaka 2017/2018 jumla ya vifaranga milioni 21 vilizalishwa na kusambazwa kwa wafugaji kwa bei ya ruzuku ya shilingi 50 kwa kifaranga aina ya sato na shilingi 100 kwa kifaranga aina ya kambale.
Mheshimiwa Mwenekiti, aidha, bei ya vifaranga kwenye mashamba ya watu na taasisi binafsi ni kati ya shilingi 150 hadi shilingi 300 kwa kifaranga kimoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2018/2019 Wizara imekamilisha ujenzi wa hatchery ya kisasa ya kituo cha Kingolwira (Morogoro) yenye vitotoleshi 20 vyenye uwezo wa kuzalisha vifaranga takribani milioni 15 kwa mwaka.
Aidha, ni mkakati wa Wizara kujenga hatchery kama hiyo na kufunga vitotoleshi kama hivyo kwenye vituo vya Mwamapuli (Tabora) na Ruhila (Ruvuma) kwa lengo la kuzalisha takribani vifaranga milioni 45 kwa mwaka kutoka sekta ya umma ifikapo mwaka 2021.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika kudhibiti ubora wa vifaranga wa samaki wa kufugwa Wizara imeendelea na mkakati wake wa kuimarisha vituo vyake kwa lengo la kuhifadhi samaki wazazi bora (broodstock) watakao sambaza kwenye hatchery za sekta binafsi zinazotambuliwa na Wizara ili kuongeza uzalishaji wa vifaranga kwa mwaka kutoka vifaranga 14,120,000 (2016/2017) hadi vifaranga 60,000,000 ifikapo mwaka 2022.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imeendelea kuhamasisha Halmashauri na sekta binafsi kuanzisha vituo vya kuzalisha vifaranga bora vya samaki ambapo vituo 23 vimeanzishwa na kuzalisha takribani vifaranga milioni 20 kwa mwaka na kusambazwa kwa wafugaji. Aidha, ni lengo la Wizara kushirikiana na mamlaka za Serikali za Mitaa na sekta binafsi kutekeleza mikakati wa kuongeza uzalishaji wa samaki wa kufuga kutoka tani 10,000 tulizonazo sasa hadi tani 50,000 ifikapo mwaka 2020/2021(Makofi).
MHE. ALLY SALEH ALLY (K.n.y. MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN) aliuliza:-
Je, Chuo cha Utalii kimetoa wahitimu wangapi wa fani za hoteli za kitalii kwa mwaka 2016/2017?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa maliasili na utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yussuf Salim Hussein, Mbunge wa Chambani, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Chuo cha Taifa cha Utalii ni Wakala uliopo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii wenye dhamana ya kutoa mafunzo ya ukarimu na utalii nchini. Aidha, chuo kinatoa ushauri wa kitaalam na kufanya utafiti katika fani ya ukarimu na utalii. Chuo cha Taifa cha Utalii kina ithibati kutoka Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) ili kutoa mafunzo ya ukarimu, usafiri na utalii kwa ngazi za stashahada na astashahada.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa masomo 2016/2017 kupitia kampasi zake tatu za Bustani, Temeke Dar es Salaam na Sakina Arusha, kilitoa mafunzo ya ukarimu, usafiri na utalii kwa wahitimu 329 kama ifuatavyo:-
(a) Stashahada ya Usafiri na Utalii (Ordinary Diploma ni Travel and Tourism) wahitimu 43;
(b) Stashahada ya Ukarimu (Ordinary Diploma in Hospitality Operations) wahitimu 15;
(c) Astashahada ya Ukarimu (Technician Certificate in Hospitality Operations) wahitimu 78;
(d) Mafunzo ya Muda Mfupi (Short Courses in Food Production and Pastry and Bakery) wahitimu 78; na
(e) Mafunzo ya Uhitaji Maalum (Tailor Made Courses in Hospitality and Tourism) wahitimu 79.
Mheshimiwa Naibu Spika, mafunzo hayo yamekuwa yakitolewa kwa kutumia mitaala inayofuata Mfumo wa Kujenga Ujuzi na Maarifa (Competence Based Education and Training) inayosimamiwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE).