Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Abbas Ali Mwinyi (3 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. KAPT. ABBAS ALI MWINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ununuzi wa ndege mpya kutoka Bombardier umefikia hatua gani? Ni lini hasa ndege hizo zitawasili tayari kwa kutumika (time frame)? Ndege ngapi zinategemea kununuliwa kwa hatua hii ya awali?
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Tanzania Airport Authority (TAA) mamlaka yake yanagusa pande zote mbili za Muungano (Unguja na Pemba)?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa takribani miaka sita sasa cheo cha Ukurugenzi Mkuu wa Shirika la ATCL kimekuwa kikikaimiwa (acting), lini hasa utakuwa mwisho wa kukaimu? Je, unatambua kuwa ndege pekee inayomilikiwa na ATCL, Dash 8-300 imeacha kuruka toka tarehe 11/5/2016 na hakuna taarifa, kipi hasa kimesababisha hali hiyo? Naomba maelezo kuhusiana na hilo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa
MHE. CAPT. ABBAS ALI MWINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia katika Wizara hii muhimu kwa Taifa letu ambayo imeendelea kudumisha amani na utulivu kwa Taifa letu pamoja na kulinda Muungano dhidi ya maadui wa ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na ufinyu wa bajeti kumekuwa na upungufu mkubwa wa makazi ya wanajeshi wetu na wale waliobahatika kupata makazi, hayapo katika hali ya kuridhisha. Upungufu huo wa makazi unapelekea baadhi ya wanajeshi kuishi nje ya Kambi za Jeshi, jambo ambalo ni hatari kwa askari wetu. Suala la askari kuchanganyika na raia kunawashushia hadhi yao kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na changamoto kubwa ya ajira kwa vijana wanaomaliza JKT Bara na Visiwani. Nashauri Wizara ya Ulinzi zishirikiane na Wizara nyingine kutoa vipaumbele vya ajira kwa vijana wanaomaliza JKT. Hii itasaidia kwa kiwango kikubwa kurudisha nidhamu ya utumishi wa umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri, atakapokuja kuhitimisha (kufanya majumuisho) ananiambie nafasi za ajira zinazopelekwa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ziko kwa uwiano gani ukilinganisha na Tanzania Bara?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na uwiano mdogo kati ya wanawake na wanaume kwa maafisa wa ngazi za juu wa uongozi wa JWTZ. Naomba kujua kutoka kwa Mheshimiwa Waziri, anapokuja kuhitimisha, ni kwa nini hali hii inajitokeza?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, hali ya ulinzi na usalama wa mipaka ya nchi yetu ni shwari kwa mujibu wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri. Napenda kujua mgogoro wa mpaka wa Malawi na Tanzania kupitia Ziwa Nyasa ambao umechukua muda mrefu, ambao unaweza kuleta athari za uwekezaji katika nchi yetu, na hivyo kupelekea hasa Ukanda wa Nyasa kudorora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. CAPT. ABBAS ALI MWINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka wa jana 2016 tulipata taarifa kuwa kuna fedha zilizopelekwa kwenda Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutoka Serikali ya Muungano (Fedha hizo zinatoka Serikali ya India) kwa lengo la kufanya utatuzi wa kero za maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli kero hiyo inazidi kuwa kubwa na kutishia vibarua vyetu kama Wabunge. Je, fedha hizo kweli zilipelekwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Muungano ilipata mrejesho wowote juu ya suala hili? Serikali ya Muungano ina nini cha kusema kuhusiana na kadhia hii?

Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa kuwa Serikali ya India ina makusudio ya kuikopesha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dola za Kimarekani 500 milioni na hatimaye Zanzibar kufaidika na fedha hizo, Zanzibar mgao wake ni kiasi gani kati ya hizo? Je, nini kinachokwamisha mkopo tajwa usitolewe mpaka sasa na hasa ukitilia maanani kuwa Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi inatuelekeza utatuzi wa kero hiyo?