Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Abbas Ali Mwinyi (2 total)

MHE. KAPT. ABBAS ALI MWINYI aliuliza:-
Ndege za Serikali aina ya Fokker 50 iliyoletwa nchini mwaka 1992 na Fokker 28 iliyoletwa nchini mwaka 1978 ni chakavu na teknolojia zake zimepitwa na wakati. Aidha, Kampuni iliyotengeneza aina hizo za ndege imeshafungwa hivyo upatikanaji wa vipuri vya ndege hizo kuwa mgumu na gharama kuwa kubwa.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuzibadilisha ndege hizo na kuleta mpya?
Je, ni lini Serikali itarekebisha hali ya hanger la kuegeshea ndege za Serikali?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimwa Kepteni Abbas Ali Mwinyi, Mbunge wa Fuoni lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli ndege aina ya Fokker 28 na Fokker 50 zina umri mkubwa. Hata hivyo kiutaalamu usalama wa ndege huwa haupimwi kwa miaka iliyonayo bali hupimwa kwa masaa iliyoruka. Hivyo, kwa hali ya kawaida muda wa masaa ya ndege kuwa chakavu (beyond economic benefit) ni masaa 90,000 na kati ya ndege hizi mbili hakuna hata ndege moja yenye masaa zaidi ya 15,000. Aidha, ndege hizo zimekuwa zikifanyiwa matengenezo kwa kuzingatia ratiba.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa ndege ya Fokker 50 ipo kwenye ubora wa kutumika na inaendelea kuhudumia viongozi wetu. Ndege ambayo haitumiki ni Fokker 28 kwa sababu ina matatizo ya breki na engine ya kulia. Serikali imewasiliana na mtengenezaji ili kuweza kutatua matatizo hayo. Ndege hizi mbili bado zina teknolojia ya kisasa na zimekuwa zikipelekwa kwenye matengenezo ya lazima kwa mujibu wa matakwa ya Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO) na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA). Kimsingi vipuli vya ndege hizo bado vinapatikana.
Mheshimiwa Spika, Kampuni ya kutengeneza ndege hizi haijafungwa bali wamesimamisha utengenezaji wa ndege mpya na wanaendelea kutoa huduma ya matengenezo (maintenance support) kwa zile ndege ambazo zimekwishawahi kutengenezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili, Serikali inatambua changamoto za karakana ya kutengeneza ndege za (TGFA) kutokana na uchakavu. Tayari nimeshawaagiza Wakala wa ndege za Serikali TGFA kufanya tathimini ya gharama halisi zitazotumika kwa ajili ya kukarabati Karakana hiyo. Gharama halisi zitakapopatikana, Serikali itafanyia kazi marekebosho ya hanger hilo. Ahsante. (Makofi)
MHE. JUMA OTHMAN HIJA (K.n.y. MHE. CAPT. ABBAS ALI MWINYI) aliuliza:-
(a) Je, Mfuko wa Bima ya Afya una wanachama wangapi na ni asilimia ngapi ya Watanzania wamejiunga na bima hiyo?
(b) Je, kwa nini baadhi ya hospitali, hasa za binafsi, hazikubali malipo kwa kutumia kadi hizo za Bima ya Afya?
(c) Je, Mfuko wa Bima ya Afya umefikia malengo ya kuanzishwa kwake?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kepteni Abbas Ali Hassan Mwinyi, Mbunge wa Fuoni, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ulianzishwa mwaka 2001 kwa Sheria Sura ya 395. Hadi kufikia Juni, 2018 Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ulikuwa una wanachama wachangiaji 858,137 ambao wanaufanya mfuko kuhudumia jumla ya wanufaika 3,918,999 sawa na 7% ya Watanzania wote. Katika kipindi hicho hicho Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ulikuwa na jumla ya wanufaika 13,398,936 sawa na 25% ya Watanzania wote hivyo, kufanya wananchi wanaonufaika na Mpango wa Bima ya Afya nchini chini ya NHIF na CHF kufikia 17,317,935 sawa na 32% ya Watanzania wote, lengo la mfuko ni kufikia 50% ya Watanzania wote ifikapo mwaka 2020.
(b( Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya hospitali zinakataa kadi za NHIF kutokana na sababu mbalimbali, zikiwemo hospitali kutosajiliwa na mfuko, kufutiwa usajili na kufanya vitendo vya udanganyifu na kukataa bei za huduma za NHIF.
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya unahudumia watumishi wote wa umma, kama ilivyokusudiwa wakati wa kuanzishwa kwakwe pamoja na kuchangia kwa kiasi kikubwa kwa rasilimali fedha katika sekta ya afya, mfano, zaidi ya 80% mpaka 90% ya mapato ya vituo vya kutolea huduma za afya zinategemea fedha za NHIF.
Hata hivyo, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya unaendelea kutekeleza mkakati wake wa kuongeza wigo wa wanachama kwa kuandikisha makundi mbalimbali katika sekta rasmi na isiyo rasmi, ikiwemo wajasiriamali wadogo wadogo na watoto chini ya miaka 18 chini ya Mpango wa Toto Afya Card na makundi ya wakulima kupitia Mpango wa Ushirika Afya ambao mpango huu ulizinduliwa rasmi na Mheshimiwa Waziri Mkuu katika Halmashauri ya Wilaya ya Kahama, Shinyanga, hivi karibuni.