Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Ali Hassan Omar (11 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia. Kwanza sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu, ambaye ametujaalia uhai na kutupa afya tukahudhuria hapa kutekeleza wajibu wetu huu ambao tumeuomba kwa
wananchi.
Pili nawashukuru wananchi wa Jimbo langu la Jang‟ombe kwa kunichagua kwa kura nyingi na kwa kumchagua Rais Dkt. Magufuli kwa kura nyingi na hatimaye leo tumepata fursa hii ya kusimama hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tatu ni kwako, kwa kunipa fursa hii ili niweze kuchangia hotuba ya Rais aliyoitoa wakati akilihutubia Bunge siku ya ufunguzi wake.
Mheshimiwa Spika, kwanza napenda nimpongeze Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kufanya baadhi ya maeneo ambayo tayari ameshayafanyia kazi baada ya kuahidi kwa kipindi kifupi sana. Hii tayari tumeona jinsi alivyokuwa na nia ya dhati ya kuifikisha Tanzania hapa ilipo. Hii imeonyesha kwamba nia yake ataipeleka Tanzania pale tunapotaka.
Maana tukichukulia hotuba tutapata ushahidi wa kutosha kwamba hivi sasa maeneo mengi yameshafanyiwa kazi na tumeyaona. Ni kweli hapa kazi tu, maneno na fitina baadaye. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa nimsifu Rais wangu, huyu ni muungwana. Kuna usemi wa Kiswahili unasema kwamba ada ya mja hunena, muungwana ni vitendo, tenda watu wataona, majisifu weka kando. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Rais baada ya kuapishwa aliahidi katika ukurasa wa 10 wa kitabu cha hotuba, kwamba atashughulikia ule mgogoro watu wanaouita wa Zanzibar. Kwa hiyo, alifanya hivyo, tumeshuhudia sote, alimwita Makamu wa Pili wa Rais, Rais wa Zanzibar,
Makamu wa Kwanza wa Rais ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha CUF, akaenda akazungumza nao na hatimaye matokeo tumeyaona kwamba Tume ya Uchaguzi imeshatangaza tarehe ya uchaguzi, nayo ni tarehe 20 Machi, 2016. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, napenda kulizungumza hili kwa sababu inawezekana kuna watu wakawa wanakosa njia za kuzungumza, wakafikiria kwamba Zanzibar kuna mzozo kiasi ambacho kwamba hakuna amani na usalama, kitu hicho siyo kweli. Ndugu zangu tufahamishane kabisa hapa, Zanzibar kuna amani na Tume ya Uchaguzi wa Zanzibar ndiyo yenye mamlaka ya kufanya uchaguzi na kutoa matangazo ya uchaguzi. Hao waliosema kwamba aliyeshinda atangazwe, atangazwe nani? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, matangazo yako mengi, kuna matangazo ya vifo yatatangazwa yote, lakini suala la kutangaza matokeo ya uchaguzi liko chini ya Tume, kifungu cha 42(1) mpaka (5), hakuna mwingine. Sasa katika suala hili la amani na mgogoro wa Zanzibar, Mheshimiwa Rais amelishughulikia vizuri sana na kwa sababu anafahamu yale mamlaka yaliyokuwepo ndani ya Zanzibar.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna watu walikuwa wakijinadi kwamba wanataka mamlaka kamili, leo wanakimbilia Marekani, wanakwenda Uingereza, wanakwenda kwa Papa, sasa hapo mamlaka hayo kamili ya ndani unayakataa mwenyewe. Wewe umetaka upate mamlaka
kamili, basi tumia Tume yako ambayo imepewa mamlaka kamili. Kwa hiyo, Tume ya Uchaguzi wa Zanzibar ina mamlaka kamili kwa mujibu wa Ibara ya 104 ya Katiba ya Tanzania na pia kwa mujibu wa Ibara ya 119 ya Katiba ya Zanzibar, hilo limeelezwa wazi na halina utata wowote.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kuhusiana na habari hiyo ya matangazo nani anagombea Urais, Mwenyezi Mungu ndiyo anaamua nani awe Rais, hatuwezi kuamua hapa.
“Qul-allahumma maalika‟lmulki tuuti-lmulka mantashaa‟u watanzi‟u-lmulka mimman tashaa‟u.” Mungu yeye ndiye anayetoa ufalme, hakukupa Mungu huwezi kuupata kokote; sema, toka mapovu, zunguka, hutoweza kupata chochote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mshairi mmoja anasema, kutapatapa haachi mfa maji baharini, ashika kila mahali aokoke maskini, kafa angali mbichi, mfa maji buriani. (Kicheko)
Sasa ndiyo maana watu wanashika kule na huku wapate hayo mambo. Watu labda hawaelewi, kwa nini Tume ya Uchaguzi ilifuta matokeo ya uchaguzi au ilifuta uchaguzi na matokeo yake hawajui. Kwanza yale ni mamlaka ya Tume, hakuna yeyote wa kuingilia Tume, ile ni Tume Huru, mambo yametangazwa wazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, natoa mfano mmoja, mnaweza mkalia nyinyi. Kura ambazo zimepigwa Zanzibar, nyingine zimepigwa za watu waliokufa. Watu wote wanaelewa kwamba ilitokea ajali ya MV. Spice, watu zaidi ya 6,000 lakini baadhi ya waliokufa mle wamepigiwa kura
zao, sasa huu ni ukiukwaji kwa mujibu wa Tume na Tume ndiyo imetoa takwimu hizo. Sasa wako watu hata vitambulisho hawana…
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Hata vitambulisho hawajachukua, lakini kura zao zimepigwa, katazameni katika taarifa ya Tume.
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Hapo hapo ndipo aliposema Rais mzozo na ndipo hapo hapo walipojadili watu na sisi tunajadili hapo hapo. Kwa hiyo, Tume ndiyo yenye mamlaka kamili, watu ambao…
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza muda wangu uulinde. Sasa wamepigishwa kura maiti, sasa hawa wanakaa wapi? Leo mnasema kama uchaguzi ule halali, hawa watu mnaweza kuturejeshea, tukawaona? Kule kwetu kuna kitu kinaitwa giningi au wamewekwa giningi? (Makofi/Vigelegele)
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Naibu Spika, hiki ndicho kilichotokea, kama hamjui, mnashabikia mnacheza ngoma si yenu, huo ndio ukweli.
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine, napenda kuipongeza Hotuba hii ya Rais na napenda Rais aendelee kutufanyia mambo mazuri. Miongoni mwa mambo mazuri katika Mfuko wa Jimbo, Rais ameahidi kwamba atautoa mapema na haraka iwezekanavyo. Kwa hiyo, tunasubiri
ili tuweze kwenda kufanya maendeleo yetu. Ombi letu katika Mfuko huu wa Jimbo uwe unawiana kwa thamani ya sasa hivi kwa sababu ulifanyiwa thamani muda wa nyuma kidogo, kwa hiyo, uende na wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo tunamsisitiza Mheshimiwa Rais, kwa sababu tunafahamu yeye ni mzee wa hapa kazi tu, ni kwamba katika mchakato huu wa Katiba Mpya, amesema amepokea kiporo, kwa kuwa ni kiporo kipashwe moto tu, halafu tuendelee,
kwa sababu mchakato wa Katiba ulikuwa umeshafikia mahali pake, tuanzie pale mahali ambapo tuliachia ili tumalize.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine katika ukusanyaji wa mapato. Tumeona jitihada zake Mheshimiwa Rais, lakini pia, tunapenda ashirikiane na taasisi au zile Professional Bodies ambazo wamo wadau wa ukusanyaji wa mapato. Mle mna Wahasibu, mna na ma-auditors wa Kampuni, ili kusifanyike udanganyifu katika ukusanyaji wa mapato na mapato yasivuje. Kwa hiyo, hii tunasisitiza sana aweze kutumia Sheria, hebu wapewe hizi Professional Bodies zipewe meno.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na yote haya, tunapenda Rais awe na mashirikiano mazuri na wafanyabiashara au Serikali iwe na mashirikiano mazuri, lakini siyo kwa ajili ya kufanya kodi isikusanywe. Kwa hiyo, wakiwa na mashirikiano hayo, Serikali itaweza kukusanya kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika suala la ulinzi na usalama; katika suala la ulinzi na usalama, nafikiri najilipalipa dakika zangu hapa! Katika suala la ulinzi na usalama hili ni jambo…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kingi, muda wako uliingiliwa hapo katikati, dakika moja ukae!
MHE. ALI HASSAN KING: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Bado dakika moja!
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Vyombo vya Ulinzi na Usalama hili suala liangaliwe, kwa sababu katika baadhi ya maeneo, watu wanavikebehi vyombo vya ulinzi na usalama. Yako maeneo ambayo vyombo vya ulinzi na usalama havifanyi kazi vizuri kwa sababu ya nature ya
maeneo yale.
Kwa hiyo, hili Mheshimiwa Rais alichukulie hatua, alisema ataboresha makazi kwa wana ulinzi wetu, watu wa ulinzi na usalama. Kwa hiyo, afanye makazi yapatikane ili waepukane na kukaa kwenye nyumba za kupanga katika maeneo ya watu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna sehemu moja siitaji, alikatwa kichwa Askari akitoka kweke kwenda kazini. Kama watakuwa wanapewa makazi, basi Askari hawataweza kufanyiwa mambo haya ambayo yako kinyume na Sheria. Ahsante. (Makofi)
Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nakushukuru kwa kunipa nafasi hii, lakini kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uhai na uzima na salama kwa leo kukutana hapa kujadiliana kuhusu bajeti ya ulinzi na usalama katika nchi yetu hii ya Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa neno moja; kule kwetu kuna ndege kwa kiarabu anaitwa bull bull, kwa Kiswahili anaitwa kasuku. Kasuku ukisema hodi, basi naye anasema vilevile hodi! Sasa kasuku yule ile hodi hajui kama maana yake ni nifungulie mlango. Kwa hiyo, imekuwa yeye ame-copy tu kwamba ndiyo amesema hodi. Nafikiri mmeshuhudia, watu wanazungumza ekari, halafu baadaye wanageuza maneno kwa sababu ni maneno ya bull bull. Anaondoka bull bull! (Kicheko/Makofi)
Mimi najikita zaidi katika kuongelea masuala ya maslahi ya wanajeshi wanapokuwa kazini na wale wanaostaafu. Nachelea kupoteza muda mwingi, nitakuwa consistency na wale waliochangia suala hili. Nitajaribu kuongelea kuhusu wastaafu wa Jeshi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mambo mawili; kuna watu waliingia kwenye mikataba huko katika majeshi tunafahamu, pengine watachukua kwa mkupuo au watakuwa wanapata pensheni. Badala yake wakaja wakataka ku-reverse, kuja kujirejesha tena upya. Kwa hiyo, hawa ilikuwa wazingatiwe jambo lao hili kwa sababu lengo ni kulinda usalama na amani ya nchi yetu na lengo ni kuwa na wanajeshi wa akiba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wote hawa walioingia kwenye mambo hayo mawili whether ya kuchukua kwa mkupuo au kupata pensheni, lengo letu kama Taifa sasa hivi ni kuwaweka kama askari wa akiba na tusiwe na wapinzani katika ulinzi na usalama.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine la kushukuru, watu wengi sana wameunga mkono hii bajeti. Hii bajeti imeungwa mkono kwa vitendo na watu wote, kwa hiyo, na mimi naiunga mkono bajeti hii na hoja hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napata mashaka kidogo; inakuaje mtu umekaa ukimwona mwanajeshi unaanza kutetemeka, una nini wewe? Una kitu gani ulichoficha? Kuna ajenda gani? Kwa nini wewe uwe unaona taabu kukutana na majeshi ya ulinzi na usalama? Kwanza anza kujiangalia kutokea hapo, una mashaka gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, niongee kitu kimoja; Jeshi la Ulinzi na Usalama kazi yake moja ni kulinda mipaka yetu nje na ndani. Mimi ni shahidi, bomu la mwanzo kulipuka baada ya uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba pale Zanzibar lililipuka mbele ya Kanisa Anglikana Mkunazini, lililipuliwa na majeshi, tulitarajia aende nani?
Mheshimiwa Naibu Spika, bomu la pili lililipuka round about ya Michenzani upande wa njia ya kutokea Bwawani. Likalipuka la kwanza pale, baada ya dakika 10 likalipuka bomu la pili; na mimi mwenyewe nilikuwa niko maeneo ya pale pale kwa sababu ni maeneo yangu ya kujidai. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, haya mabomu ikiwa tunao maadui wa ndani, kwa nini Jeshi letu la ulinzi lisifanye kazi ndani? Mabomu mengine mawili yalienda kuteguliwa katika Kambi ya JKU Zanzibar Saateni. Yametegwa na haya mabomu, tunafikiri jukumu hili ya kutegua hayo mabomu akafanye nani? Jeshi la Wananchi wa Tanzania liendelee kufanya kazi zake ndani na nje ya mipaka yetu, kwa sababu bado tunao maadui wa ndani na nje. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, halafu waliokuwa wanazungumza kwamba jeshi lilienda kuwatisha watu wasishiriki uchaguzi wa tarehe 20 Machi, wamemsahau aliyewatisha! Hivi dakika ile ile kiukweli wamesahau? Basi akili hizi zitakuwa za kuku, maana kuku ukimwinga, anaondoka. Baada ya dakika chache kuku anarudi pale pale. Itakuwa wana akili za kuku hawa, wameshahau aliyewaambia wasiingie kwenye uchaguzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi kweli Jeshi la Wananchi ndiyo limeenda kusimamia kwamba watu wasiingie kwenye uchaguzi wa marudio? Mtu anazungumza maneno hayo hapa wakati anafahamu kwamba kiongozi wake ndiye aliyesema hayo maneno. Sasa leo wanakuja kuyaleta hapa, nashangaa sana! (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo moja ambalo lilizungumzwa hapa na wengi kila mtu akikaa anasema kwamba anaunga mkono. Maneno yaliyozungumzwa na Kambi ya Upinzani, mimi namheshimu sana mzee wangu. Maneno aliyozungumza kwamba, demokrasia ya Zanzibar iliharibiwa na majeshi, nashangaa sana. Naweza nikasema, kuna mshairi mmoja anasema; “masikini roho yake, kioo kimemcheza.” (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi kweli alijipima na akajiangalia kwamba yeye aje azungumze maneno hayo hapa, amewahi kuwa kiongozi wa ngazi za juu kabisa, maskini roho yake kioo kimemcheza!
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati mwingine unapoambiwa ufanye jambo, ujaribu kutazama, wenzako wanakutoea hao! Usiwe zumbukuku ulimwengu uko huku! Ni lazima ujiangalie huko katika hali gani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niunge mkono hoja lakini kingine cha umuhimu kabisa katika kuangalia masuala haya ni hali ya uwiano katika ajira na utawala wa Jeshi la Wananchi, hili ni Jeshi la Wananchi wa Muungano wa Tanzania, ikiwemo Zanzibar na Tanzania Bara.
Kwa hiyo, hata katika utawala, leo wametajwa pale Majenerali nikasema na mimi nitasikia jina la kwetu sikulisikia, tuwe na uwiano katika masuala haya na kwenye ajira pia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo ni la msingi na kubwa zaidi, Jeshi letu litahusika na ulinzi wa mipaka katika bahari kuu. Hili liangaliwe kwa sababu ni jambo la kiuchumi na linahitaji zana za kijeshi, lakini pia kuzingatia uharamia unaofanyika katika nchi jirani ikiwemo Somalia lakini uchujaji uwe mzuri kwa sababu pia na wavuvi wetu nao huwa wanakwenda kuvua. Nilimsikia Mbunge wa Bumbwini aliuliza swali katika kipindi cha maswali na majibu kuhusiana na suala hili. Kwa hiyo, naomba masuala hayo yazingatiwe na yafanyike vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo lingine ambalo ni muhimu, nimejaribu kupima hapa na nime-synthesis hoja nyingi sana…
(NAIBU SPIKA: Kengele ya pili hiyo, Mheshimiwa muda wako umekwisha.
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi hii. Kwanza nimpongeze mzungumzaji aliyemaliza kwa shairi lake kilichochema ni chema hakibadili tabia. Tabia ya Maalim Seif ni kushindwa uchaguzi na nashangaa kwa nini mnamwachia aendelee na tabia hiyo hiyo na ataendelea kushindwa tu. Kwa hiyo, kwa kuwa hakibadili tabia siku zote atashindwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichangie katika nyumba zitakazojengwa kwa Jeshi la Polisi kwa Zanzibar. Tuweke proportion ambayo ni nzuri, lakini cha pili mawasiliano ya redio kwa Zanzibar askari wanaongoza kwa simu kule, kwa hiyo, hili nalo pia ni muhimu tulitazame. Kingine masuala ya umeme wanalipa Wakuu wa Vituo wakati mwingine, kwa hiyo na hili liangaliwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nizungumzie jambo moja, amesimama hapa kuna mtu alijiita mchungaji, lakini nikimnukuu ndugu yangu mmoja alisema sijui kanisa hilo hawa wafuasi watakuwa wakoje, mimi sisemi. Anasema kwamba, Wabunge 250 wanashindwa labda kuzijibu hoja, upinzani hauna hoja, hapa hawana hoja, hawana ajenda za kuzungumza sasa hivi wamekuwa ni virukia, kuna miti inaitwa virukia haina mizizi. Ikitajwa Lugumi wanajipaka damu za simba kama wao ndio waliomuua simba, ninyi sio, wako wenyewe waliofanya hiyo kazi, mnajipaka damu halafu mnajisingizia ninyi ndiyo mlioua simba, hamna hoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Toka wauvae ulitima kwa kulamba joka la ufisadi sasa wanadandiadandia, kwa hiyo hawana hoja ya msingi. Lakini Mheshimiwa Lwakatare kule amesema amethibitisha kwamba, wanatangwa maji kwenye kinu na hayabadiliki kwenye kinu hayawezi kupita smoothly kwa sababu ya kuyatwanga kwenu. Watu wanawashuhudia hata mngeletewa hiyo TV katika hoja zenu za kurukiarukia basi pia msingefanya kitu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa wale waliokuja na habari za matukio jamani mnasahau? Hamtajwi matokeo ya mabomu nyie? kuwamwagia watu acid, kuwaua ma-padre mbona hamtaji kama huu ni uvunjifu wa amani, mnazungumza hoja gani katika hili? Zungumzeni kitu ambacho kitaleta amani na utulivu katika nchi hii, wadau wa amani na utulivu wanajulikana na wanaochafua wanajulikana mahali popote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe unalalamika kupelekewa askari Zanzibar, unalalamika nini, wewe ndiyo mhalifu kama unalalamika, kwanini unakataa kupelekewa askari kama sio mhalifu. Sasa hili ni lazima liangaliwe, nikija kuchangia katika hoja nyingine amezungumzia Mheshimiwa Waziri katika utekelezaji wa bajeti iliyopita kwamba, wamejaribu kuzuia biashara haramu ya kuuzwa watu, hili jambo bado lipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna ndugu zetu wanapelekwa Oman, Dubai, wanapelekwa Bara Arab wanakwenda kutumikishwa bila ya hiari zao, mikataba inaondoka hapa mingine na wakifika kule wanafanyiwa mambo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuunga mkono hoja hii mimi labda hapa nizungumzie kitu kimoja, kuna wenzetu wanajaribu kulipaka matope jeshi letu la polisi, amani na utulivu wa nchi yetu ya Tanzania basi Jeshi la Polisi ndiyo mchango wake mkubwa na waharibifu wa amani hiyo na utulivu ndiyo hawa, nashangaa. Kuna msemo unasema homa mpe paka, maana yake homa mpe paka kwamba wewe kwa kuwa unaumwa ikutoke homa ile kwa kuwa paka haitomdhuru. Sasa hicho sio kitu sahihi wanachokifanya, tunapozungumzia amani na utulivu, majeshi yetu yanakwenda vizuri, kwa hiyo, tunashukuru kwa kutusaidia katika kuweka sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia hapa jambo lingine ambalo ni muhimu sana, ni usafiri kwa Jeshi la Polisi kwa Mkoa wangu wa Mjini Magharibi Unguja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai na kufika hapa katika Bunge lako hili Tukufu. Pili, nakushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii, lakini cha tatu nikupongeze sana kwa umahiri wako, ujasiri wako wa kukalia Kiti hicho. Kwa sababu hawa wenzetu wao mpaka sasa hivi kitu kinachowatoa humu ndani ni wewe siyo kwa sababu labda umewafanyia kitu kibaya ni kwa sababu umefuata kanuni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mshairi mmoja anasema, mpewa hapokonyeki, aliyepewa akapewa. Wewe ukifanya chuki bure unajisumbua. Mola ndiye atoaye, mambo yote kamiliki. Kwa yule amtakaye ambaye humbariki na yule asiyemtaka basi kupata hatodiriki. Kwa hiyo, hawa wao watasema nje lakini wewe hapo umekaa umetulia kama jina lako lilivyo. (Makofi/Vigelegele)
Mheshimiwa Naibu Spika, cheo ni jaha na jaha anayetoa ni Mungu. Jaha mpaji ni Mungu binadamu hana lake. Sasa wao kwa upande wao wanalia na hii jaha ya cheo na jaha hii ambayo mtu akipewa na Mungu, hata shetani alipopewa Nabii Adam, Mwenyezi Mungu anahadithia kwenye vitabu vya dini, anasema kwamba alivyowaambia malaika wamsujudie Adam, walisujudu isipokuwa ibilisi. Ibilisi yeye alikataa halafu akafanya kiburi. Kwa hiyo, wanachofanya hawa ni kiburi tu. Ibilisi akafukuzwa mbinguni akaambiwa toka, akatoa ahadi kwa Mungu nitakwenda huko ardhini kuwaposha waja wako. Hawapo huku, sasa wako Kahama, Mwanza, kwa ile ahadi yao kwamba watakwenda kuwapotosha Watanzania. Watanzania tunawaomba wawaelewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kumaliza uchaguzi tuliambiwa kwamba siasa zimehamia Bungeni kama wanavyozungumza watu wengine lakini sasa tazama, majimbo yale ya Wapinzani kule meupe, wote hawapo humu ndani. Hii ni sawasawa na hadithi moja ambayo niliwahi kuhadithiwa na wazee wangu kule, hadithi hiyo inazungumzia habari ya fensi ya ndoa. Katika fensi ya ndoa kuna bibi harusi huyo akipanda mumewe kitandani anatoka, akiingia mumewe chumbani katoka, kwa sababu anaogopa hajajiandaa na harusi, kwa hiyo watu wawaelewe. Kwa hiyo na hii iliyokuwa humu ni fensi ya ndoa, unapoingia watu wanaondoka, kwamba bibi harusi anamwogopa bwana harusi. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ni-conclude maneno kuhusu hawa, tusiwasemeseme sana kwa sababu kuna mshairi mmoja wa kiarabu anasema, Al junun funun alwak khalfan waheed. Wenda wazimu una matawi mengi sana na matawi ya wendawazimu hawa wenzetu wameyadandiadandia tumeyaona. Kwa hiyo, haya yote wanayokuja nayo, wameshakuja nayo mengi na hili moja katika matawi ya wendawazimu ambayo wamedandia. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, hawa wenzetu ndiyo hatuwaoni humu Bungeni lakini sisi tutajadili kwa niaba yao. Sasa nije katika kuchangia bajeti yetu hii. Matumizi ya Serikali siku zote huwa yanapangwa kwa fedha. Fedha zinazopangwa badala yake huwa tunatazama yale mambo yaliyotarajiwa kwenda kufanyika lakini mambo yanayotarajiwa kwenda kufanyika tunatarajia yatokezee kwa 100%. Inawezekana fedha zikatumwa 100% lakini kazi isifanyike kwa 100% kama ilivyokusudiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa gap hii tutaijua au itazibwa kutokana na ukaguzi unaofanywa na Mkaguzi Mkuu wa Serikali. Kwa hiyo, kuna kila umuhimu wa kuwa na taasisi hii ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali. Madhara yake kama itakuwa ukaguzi haukutosheleza ina maana kwamba mwaka unaofuata wa fedha tunaweza tukapeleka fedha tena katika miradi ileile na fedha ile isiweze kufanya kazi vizuri kwa sababu haiangaliwi, kwa hiyo, hili ni jambo muhimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha zilizotengwa katika ofisi hii ni ndogo na nasema ndogo kwa sababu gani? Fedha zilizotengwa mwaka jana katika hizo OC, sizungumzii mishahara na development, nazungumzia OC za kufanyia kazi zilikuwa ni shilingi milioni 49 lakini mpaka kufikia Machi, 2016 fedha zilizotoka ni shilingi milioni 39, lakini fedha zilizotengwa kwa ajili ya mwaka huu wa fedha ambao tunaujadili hapa ni shilingi milioni 18.5 ya Other Charges. Shilingi milioni 44 humo kuna development na P.E. Kwa hiyo, hizi fedha tuna-justify kwamba ni kidogo kwa sababu ni asilimia 37 ya fedha zilizotoka mpaka Machi. Kwa hiyo, ukija kutazama kwamba zinatarajia kufanya kazi kwa mwaka mzima tutakuja kuona upungufu wa fedha hizi ni kiasi gani. Najua Serikali itakuja na mid year review lakini katika mid year review hili nalo tulione kama ahadi ya Serikali ilivyosema. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna kitu kimoja ambacho ni kizuri. Audit inapofanyika ina stage nyingi, kuna stage ya planning. Katika stage hii ya planning auditor anapanga wapi atafanya audit ile, anapanga resources, anapanga expert’s watakaohitajika wa-audit eneo fulani lakini pia anapanga na time consuming ambayo atatumia. Sasa katika hatua hizi za mwanzo auditor anahitaji kufanya hayo mambo kama resources zitakuwa hazitoshi ina maana kwamba ingekuwa ana-audit private office siyo Ofisi ya Serikali asinge-accept hii engagement kwa sababu resources zisingemtosheleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kingine muhimu katika kufanya audit, auditor wetu ana heshima kubwa sana Kimataifa. Katika kulinda reputation yake Kimataifa ni lazima auditor wetu afanye kazi vizuri na apelekewe fedha za kutosha ili aweze kufanya kazi kwa umakini na umahiri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia bajeti ya maendeleo ni kubwa, imeongezeka kwa asilimia 100. Kwa hiyo, tunatarajia fedha za maendeleo zikakaguliwe kwani zimeongezeka kwa asilimia 100. Kitu kingine Halmashauri zetu zimeongezeka kutoka 100 na zaidi hadi kufika 181. Ina maana kwamba kuongezeka kwa Halmashauri ni indication kwamba hata fedha za audit zingeweza kuongezeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, isitoshe, tumesema kwamba Serikali imeamua kulipa madeni, lakini kabla ya kulipa madeni hayo inayakagua ili kupitisha kwamba deni gani linafaa kulipwa. Kwa hiyo, madeni haya ya Serikali yanayokaguliwa pia nayo yataongeza kazi ya auditor kwa hiyo ilipaswa fedha za auditing ziwe nyingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Serikali imeamua kufuta retention, makampuni ambayo yatafutiwa retention yatakuwa hayako radhi, hayataweza ku-submit kila kitu kikawa kiko safi. Kwa hiyo, Serikali ilipaswa iangalie suala hili ili Auditor General aweze kufanya mambo hayo ya ukaguzi. Pia taasisi kama Mahakama ya Kuzuia Ufisadi, TAKUKURU, Bunge tunategemea taarifa za CAG ili tuweze kufanya kazi. Kwa hiyo, hivi vyombo vinaweza vikakosa taarifa ya thamani katika kufanya kazi hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine nije katika deni la Taifa. Wengi wamezungumzia deni la Taifa lakini deni la Taifa ni himilivu tunakubali lakini tunasema hivi, tukope tufanye zile kazi tulizoziainisha na tumalize kazi zile tulizokopea. Kama hatukumaliza, project zikiganda katikati interest rate inalipwa ina maana kwamba tunalipa fedha zetu au tumelipa fedha zimeganda, wananchi wanalipa interest na miradi inakuwa haijakamilika. Kwa hiyo, naomba suala hili tuweze kuliangalia vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini eneo lingine ambalo naweza kuchangia ni eneo la Bodi ya Taifa ya Ukaguzi ambayo ilitajwa katika Mpango. Bodi hii ya Taifa ya Ukaguzi tukifuata nchi za wenzetu huwa wanazitumia Bodi zao za Wahasibu na Auditors ili kuweza kutoa hata mitaala ya sheria za kodi ambazo zimetoka.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na yote, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu ambae ametupa uhai na akatufanya sisi leo kuwa miongoni mwa Wabunge ambao tutachangia maslahi ya nchi hii katika mipango ya kuendesha nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha pili nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Ni nafasi adhimu ya kuweza kuchangia Mpango wa Maendeleo au Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2017/2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nizungumze kitu kimoja kidogo ambacho wasemaji wengi sana walikuwa wanakigusagusa ambalo linahusiana na masuala ya bandari.
Kwanza nakwenda huko moja kwa moja masuala ya bandari, ni kweli tumeona kwamba mzigo katika bandari umepungua lakini tunaposhauri tujaribu kuangalia katika maeneo ambayo mzigo maeneo gani yamepungua. Ukitizama katika hizi transit goods ambazo zinakwenda katika nchi jirani basi utagundua kwamba nchi ya Zambia na DRC Congo ndipo mzigo ulikopungua, lakini ukiangalia Uganda na Malawi mzigo haujapungua. Sababu zimeleezwa na wengi pengine labda VAT na pengine labda hiyo single custom territory ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa kufanya mizigo katika bandari ipungue.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika hili nilikuwa naomba Serikali ijaribu kuangalia hivyo vitu ambavyo vimetajwa hapo kwamba ni sababu na tujielekeze na tubaini kwamba hiyo kweli ni sababu; kwa sababu kuna baadhi ya mambo yalianza kabla ya hapo. Tukija katika hiyo single custom territory kwamba ilikuwa iko toka mwaka 2013 ikaanza kuwa implemented Disemba, 2014 sasa tutizame kitu gani kilichotuathiri. Na ukija kutazama katika mizigo mingine hususani ya mafuta mpaka katika nchi za Rwanda na Burundi kwa mujibu wa takwimu ambazo zimo katika kitabu cha bandari kwamba nayo pia ilipungua. Lakini ukiangalia katika nchi nyingine zimeongezeka sasa hili nilikuwa naomba tutafute sababu hasa ili tunapotibu basi tujue tunatibu kitu gani ambacho mahususi moja kwa moja kitakuwa kinatusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ninataka kulizungumzia amelizungumzia Mheshimiwa Kingu pale kwamba kuhusiana na fedha ambazo zimo katika uchumi wetu. Tunafahamu Serikali imepanga kukopa ndani, lakini moja katika changamoto ambayo Serikali yenyewe ilieleza kwamba kutoshiriki kwa sekta binafsi katika uchumi imefanya kwamba uchumi kutokukua vizuri au mambo kutokwenda sawa.
Sasa tunapoamua kukopa ndani vilevile tutasababisha hali hiyo hiyo ya kwamba fedha zitakuwa hazipatikani kwa wananchi na baadaye hawa watu binafsi hawataweza kukopa, kwa hiyo na sekta binafsi nayo itarudi katika changamoto yake ile ile ya kwamba itaanguka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naishauri Serikali iharakishe suala la kupata ile dhamana ya Kimataifa kukopa kuweza kufanya sovereign rating kwa haraka ili tuweze kupata mikopo ya nje. Lakini pia si vibaya kwakuwa soko letu la hisa la Dar es Salaam Stock Exchange linakubali kualika foreign investors ambao labda Serikali nayo ijielekeze katika kukopa kwa foreign investors ingawaje changamoto zake zinajulikana kwamba ufanisi katika soko lile pamoja na vitendea kazi siyo vizuri kwa muda huu, lakini tutakapotumia njia hiyo, kwa hiyo, tutaweza kupunguza kukopa ndani na baadaye tutajielekeza katika masuala mengine ambayo ya mikopo mizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ni muhimu sana ambalo wengi walilizungumzia, Serikali ingeweka utaratibu uliowazi kufahamu shughuli zinazofanyika. Wengi wanaozungumza hapa wanalalamikia utaratibu wa Serikali kutofikisha fedha katika masuala ya dawa, katika Halmashauri na sehemu nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa mujibu wa report ya BOT ambayo wameleeza kwamba katika mwezi wa Agost, Serikali ililipa zaidi ya shilingi bilioni 900 ili kulipia Deni la Taifa. Katika mwezi wa nyuma yake Serikali iliipa hizo report zimo katika mawasilisho ambayo yalifanywa na Gavana wa Benki Kuu tarehe 25 Agosti. Kwa hiyo, hii ndiyo imepelekea kwamba Serikali kutopata fedha za kutosha katika kuhudumia masuala mengine sasa hapa ikafikia kipindi ambacho watu wakaanza kuisema Serikali vibaya na hapa na mimi ninaomba kidogo niongee neno moja ingawa kwamba kwa wengine itakuwa siyo zuri lakini neno lenyewe ni muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu ambaye yupo hai akatafuta kurehemewa na maiti. Narudia tena, mtu ambaye yupo hai hawezi kutafuta rehema kwa aliyefariki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mtu hapa alizungumza kwamba hii Serikali imefilisika lakini akasahau Serikali hii ndiyo iliyompa yeye majengo bila kulipa akawa anafanya biashara. Sasa kama mfu ndiyo wewe unamtegemea akurehemu, sasa wewe mwenyewe ni mfu zaidi ikiwa aliyekufadhili amefilisika ina maana kwamba wewe uliyefadhiliwa umefilisika zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna msemo wa kiswahili ambao una lafudhi ya Kiarabu ambao unasema wafadhilaka wasajidaka, man-fadhilaka wasajidaka, aliyekufadhili ni bwana wako na sio pundaka; sio punda wako. Kwa hiyo, Serikali bado atabakia bwana wake huyo ambaye amefadhiliwa na Serikali hii, kwa hiyo, Serikali haijafilisika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ni muhimu nazungumza masuala ya retention ambayo pia yameshazungumzwa. Nakumbuka moja ya hoja ambayo Serikali ikaamua kufuta retention kwa taasisi zile ambazo zimefutiwa retention kwa sababu Serikali ilikuwa ikikopa pesa zake wenyewe. Zile taasisi zilikuwa zikiweka pesa benki baadaye Serikali inapopeleka dhamana zake kuuza katika masoko ya hisa, mabenki haya yananunua ambayo ni fedha za taasisi za hii Serikali, kwa hiyo ikaamua kuzitoa kuziweka huku. Sasa ufanyike utaratibu ambao uko mzuri na muafaka ili iweze kupatikana urahisi zaidi kwa fedha hizi kuingia katika mzunguko au Serikali yenyewe kama iliona taabu kukopeshwa na mabenki katika retention ambayo ziko BOT sasa je, Serikali ina mpango gani kuzitumia hizi? Labda pengine nazo zinaweza zikasaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na suala moja ambalo ni muhimu sana ni lazima tuangalie balance ya monetary policy na fiscal policy tunajua Wizara ya Fedha inashughulikia masuala ya fiscal policy, lakini Benki Kuu inashughulikia monetary policy.
Kwa hiyo, vitu hivi viwili ni lazima viwe balanced ili mambo yaweze kwenda sawa na tuweze kuepukana na mambo ambayo hayaendi vizuri. Kuna watu walisifu hapa kwamba Serikali iliyopita ya Mheshimiwa Mwinyi ilikuwa nzuri, ya Mheshimiwa Mkapa ilikuwa nzuri, ya Mheshimiwa Jakaya ilikuwa nzuri na hii pia ninaamini wataisifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mshairi mmoja anasema mpende bado yuko hai, pendo lako alipokee, ukimpenda yuko kaburini umelitupa pendo lako hewani, hayo mapenzi yenu mliyoyataja hapa mmeyatupa hewani lakini tunaamini kwamba na huyu mtampenda. (Makofi)
Sasa jambo lingine ambalo ni muhimu na kama tutalifanyia kazi itakuwa vizuri. Mheshimiwa Khatib pale alizungumza jana kitu kizuri kidogo hata kile kitu nimekipenda. Anasema kwamba alikiombea dua chama chake na akasema kwamba kuna watu wanakiombea kife, hawakiombei kife, mfano wa mtu ambaye ananyeshewa na mvua, tuseme unanyeshewa na mvua baadaye akatokezea mtu akakwambia njoo ujifiche kwenye jeneza unakufa, unajiua? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo,niongee masuala mawili ambayo muhimu. Katika…
MWENYEKITI: Ahsante.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. ALI HASSAN KING: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu definition (maelezo), recognition na money measurement kwa item ambayo imo katika Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa mwaka 2017/2018.
Mheshimiwa Naibu Spika, Definition Maelezo (Broad or Narrow definition), naishauri Serikali kuwa maelezo au definition ya item ambayo imo ndani ya mpango wa maendeleo wa Taifa iwe inahusiana na sehemu ya jambo ambalo litatekelezwa kwa kipindi hicho kuliko kueleza mradi wote ambao unatekelezwa kwa muda wa miaka mingi ijayo. Mfano, mradi wa Mchuchuma na Liganga, katika miradi hii imeelezwa kwamba itaanza na kumalizika ndani ya muda huo huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, recognition, napendekeza kuwa item ambayo itaingizwa humu kama ni mpango iwe imetimiza kigezo ambacho hatua za utekelezaji zitakuwa karibu na utekelezaji ikiwemo mikataba na muda wa dhamira ya kutekeleza ndani ya muda uliowekwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, measurement, fedha zitakazotajwa kutekeleza jambo hilo ziwe zimezingatia muda wa utekelezaji shughuli zilizoainishwa kutekelezwa na kadhalika. Kwa mfano, miradi ya Mchuchuma na Liganga imepangwa kutumia kwa jumla ya dola za Kimarekani bilioni mbili nukta tisa ambazo takribani ni shilingi trilioni sita za Kitanzania wakati katika kugharamia mpango sekta binafsi inakadiriwa kuchangia kwa shilingi trilioni saba nukta nne za Kitanzania. Miradi ya Mchuchuma na Liganga ni mfano tu lakini kwa maeneo mengi kama vile uanzishwaji wa kituo cha biashara Kurasini, ujenzi wa reli ya kati.
Mheshimiwa Naibu Spika, wingi wa fedha za maendeleo na ukuaji wa mapato ya ndani. Fedha za maendeleo kwa mwaka 2015/2016 zilikuwa trilioni nne nukta tatu, fedha za maendeleo kwa mwaka 2016/2017 zilikuwa trilioni 11.820 lakini ongezeko la makusanyo ya ndani yanakuwa kidogo. Tumeongeza fedha za maendeleo ili tuongeze uwezo wa mapato ya ndani ili tupunguze kukopa, lakini mikopo nayo inaongezeka badala ya kupungua.
Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali kuangalia kuwa fedha za maendeleo kwanza zilenge kwenye miradi itakayotoa majibu kwa haraka ili ichangie katika kukuza mapato ya ndani.
Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2016
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Naibu Spika, asante kwanza na mimi napenda nimshukuru Mwenyenzi Mungu, ambaye ametujalia uhai na uzima katika siku ya leo kuja kujadili sheria hii ambayo ya mapendekezo iko mbele yetu ya procurement, ambayo imelenga kuokoa gharama na fedha nyingi za Serikali ambazo zinakwenda katika matumizi ya umma.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kumshukuru Waziri wa Fedha na timu yake kwa kuleta muswada huu kwa wakati ili kuokoa fedha hizo, lakini pia napenda kuishukuru Kamati ya Bajeti nayo kwa kufanya uchambuzi na kupendekeza mambo tofauti ambayo yameboresha sheria hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimekusudia kuongea mambo mawili katika kuchangia muswada huu wa sheria, jambo la kwanzani matumizi ya health commodities, au manunuzi ya health commodities, vifaa tiba ambalo aliongelea kwa upana zaidi Mheshimiwa Martha Mlata, ameongelea kiundani zaidi. Sasa mimi mapendekezo yangu yanakuja hapa, kwa sababu hivi vifaa tiba kikawaida vina sifa ya kwamba vinaokoa maisha ya mwanadamu na hasa hasa katika afya za mama na mtoto ndio usiseme. Zitaokoa maisha ya watanzania kwa ujumla, kwa hiyo kuna uharaka wa kufanya jambo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pendekezo langu la kwanza, kungekuwepo na kifungu maalum ambacho kinaelezea hivi vifaa tiba. Lakini kama hilo halikuwezekana la kuwa na kifungu maalum cha kuelezea vifaa tiba, katika mapendekezo ya sheria kifungu cha 24 kimeeleza kwamba kitaongeza ibara ya 65A, ambapo hapo kutatajwa specialized goods, zimetajwa all services ambapo labda hapa inawezekana vikaingia hivi vifaa tiba.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hili neno la specialized goods or services kwamba bado halijawa maalum sana au liko general. Kwa hiyo, labda katika uchambuzi wake lingechambuliwa tukaelewa ni vifaa vya aina gani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kingine katika kifungu hicho hicho ambacho kimeelezea habari hiyo ya specializes goods cha 65A(2) ambacho kimependekezwa kimempa mamlaka Waziri kutunga kanuni, katika kanuni hizo ambazo atataja hivyo vitu kwa undani wake, basi ndani ya hizo kanuni tulikuwa tunamuomba Mheshimiwa Waziri ajaribu kuangalia hizi health commodities au vifaa tiba kwa lugha ya kikwetu, ili viweze kwenda sambamba. Kwa hiyo, vifaa tiba hivi vitakapopatikana vitaweza kutuongezea thamani ya maisha ya wanadamu katika nchi yetu. Lakini pia ili iweze kwenda sambamba na azimio la Wizara ya Afya, sasa hivi katika manunuzi tumewasikia wamejipanga kivingine, kwa hiyo iweze kuboreshwa katika hivyo vifaa tiba.
Mheshimiwa Naibu Spika, huo mchango ilikuwa ni katika masuala hayo ya vifaa tiba, ambayo pia katika sheria kuna kifungu cha 67 cha sheria mama, ambacho kiongezwe, wafanye marekebisho katika kifungu hicho ili kiweze kukaa sawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikija katika suala lingine, ambalo lilikuwa lina changamoto kubwa ya kutokuwepo kwa vigezo vya mahitaji ya sekta ya umma yaani standards, ilikuwa hakuna standards. Kwa hiyo, sheria iliyoongezwa 65B katika kifungu cha 24 cha mapendekezo ya sheria kimeeleza kwamba zitatumika hizo specialized standards.Kwa hiyo hizo standards zitakazotumika bado haijaelezwa ni za aina gani, bado iko general. Kwa hiyo itolewe ufafanuzi, itakapotolewa ufafanuzi inaweza ikaleta maana zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kingine ambacho kwa ajili ya kuboresha sheria hii pia Waziri amepewa mamlaka katika kifungu kinachofuata cha 65B(2) Mheshimiwa Waziri amepewa mamlaka tena ya kutunga regulations. Basi atakapotunga regulations kwa sababu unapoweka standards wakati mwingine kuna watu wanaweka standard kwa sababu wameshajua kwamba anaenda kununua kwa nani.
Mheshimiwa Naibu Spika,kwahiyo zinawekwa standard kama zina m-lead yule mnunuzi kwamba aelekee kwenda kununua kwa mtu gani. Kwa hiyo hii nayo itakuwa inafanyika uongo, sasa uongo huu ili uweze kuwa covered. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri katika kanuni ambayo umepewa nguvu na Kifungu hicho cha pili cha 65B basi aweze kuweka kifungu cha adhabu kwa watakaofanya makosa katika kuweka standard. Kwa sababu wengine wanaweza wakaweka standard za makusudi, za uongo ili kuweza kupotosha, kwahiyo naishauri Serikali katika suala hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine mambo niliyokusudia mawili ni haya ambayo nimeongea lakini jingine nikupongeze wewe mwenyewe kwa kusimama madhubuti katika kiti chako na kusimamia kanuni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, maana ya kanuni ni sheria na waswahili tunasema sheria ni msumeno, kwa hiyo na msumeno Al Marhumu Issa Matona alisema kwamba; hukata mbele na nyuma msumeno kazi yake. Usiutie lawama ufanyapo kazi yake. Kwa hiyo na wewe unatumia kanuni naamini unakata mbele, unakata nyuma kwa sababu unatumia kanuni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini aliendelea Al Marhumu Issa akasema kwamba, usitumie mkono kutaka kujiharibia, utakutoka mguno tayari umeshaumia, ukileta mabishano bure utakujalia. Kwa hiyo wenzetu wametumia mkono kutaka kujiharibia hizi kanuni na tayari umeshatoka mguno wameshaumia hawamo ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika kukupongeza huku, pongezi ambazo zimewafanya watu wanune wasikae humu ndani, maana yake kwamba, wameambiwa wasikae humu ndani lakini pia wamepewa sharti kwamba wasitusemeshe, wasitusalimie.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nilimsamilimia mwanaume mwenzangu akanitikisikia mabega hivi, kanijibu kwa mabega. Kwa hiyo mimisikumfahamu vizuri lakini kule kwetu kuna msemo mmoja au kuna kanuni moja kwamba mtu ambaye anaweza akamwambia bwana usimsemeshe fulani, fulani akikusalimia usimuitikie mara nyingi mume huwa anamuambia mke kwamba akikusalimie fulani usimsemeshe wala usimuitikie. Kwa hiyo na wao hiyo amri sijui wamepewa na nani maana hawatusemeshi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine la kushangaza ambayo misemo yakiswahili ipo, kama mzazi ameenda hospitali kujifungua kwa bahati mbaya mtoto akapita tunasema yule mtoto sio riziki kapita, na pia akiolewa dada yetu yeyote akipata mume lakini mume hatimizi majukumu ya nyumbani watasema kaolewa lakini mume sio riziki. Kwa hiyo na majimbo yale meupe kweli yana Wabunge lakini wale Wabunge sio riziki. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naunga mkono hoja mia kwa mia na tunamuomba Mheshimiwa Waziri achukue marekebisho ambayo tumeyapendekeza, ahsante nashukuru.
Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari za Mwaka 2016
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ili na mimi nichangie Muswada huu wa habari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ningependa nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuweka hai na leo kuja kushuhudia haya ambayo tunayaona, mengine kusema kweli kwamba ni mambo ya kushangaza kidogo, hata katika nafsi yangu nashangaa sana. Lakini siwezi kushangaa sana, unajua mtu anapokumbwa na sakaratul maut, anapokaribia kufa pale basi chochote kile kinamtoka. Atasema maneno yaliyokuwemo na yasiyokuwemo. Kwa hiyo, na hii ni sakaratul maut imewakuta watu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, alizungumzia hapa Mheshimiwa Khatib, alitaja habari nzuri kidogo. Habari ya wale waliokuwepo kule magereza Zanzibar miaka ya 90 wakati na mimi nilikuwa ni mtumishi kule. Hata hivyo, kitu kimoja tu alikosea, walikuwa rumande, kwa hiyo rumande walikuwa wakiletewa chakula kutoka nyumbani, nacheza na super league wakati huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende katika Muswada. Katika Muswada huu ambao umezungumzia masuala ya kuipa hadhi hii taaluma ya habari, imezungumzia suala la accreditation, wengine walisema humu wanashangaa kwa nini wameikuta humu accreditation au wanaona ajabu kwa nini watu wanajadiliana nayo wakati hiki kitu kilikuwepo tokea mapema. Kusema ukweli, suala la accreditation ni suala muhimu sana kwa waandishi wa habari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia hata referee basi pia naye wanafanyiwa mambo haya na wana daraja zao, leo tuje tulikatae katika uandishi wa habari. Yaani tunazungumzia habari hizi kana kwamba hatuoni nini faida yake. Kwa hiyo, hili suala la accreditation kwa waandishi wa habari ni suala muhimu na napendelea hilo suala liwepo. Cha kushangaza kwamba leo tunasema kwamba tunawatetea waandishi wa habari wakati mnawatetea huko mnakuja na nyimbo kwamba mna imani na mtu fulani, sasa mnatetea au nani aliyetetea? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja iko mbele yetu, kama tunawatetea waandishi wa habari basi hebu tujeni na kitu cha kuwatetea hao waandishi wa habari. Tukija na nyimbo hizi ambazo mnazileta humu, mnafanya kitu ambacho hakiwezekani kabisa, sio kitu kizuri kwamba hata hiyo imani yenu na hao waandishi wa habari wanaowasikiliza sijui wanawaweka daraja gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ambalo katika mjadala wetu huu, nimesoma hoja zote; nimesoma hoja ya Waziri, hoja za Kamati na hoja za upande wa Upinzani, pamoja na wengine wenzangu waliochangia, ndiyo tumesikia jinsi gani watu wanavyochangia, lakini nilichobaini kwamba kuna watu wamekuja kutia kidusi tu, kwamba ni kidusi ili bata asilike, lakini tangawizi ya kumuoshea iko, atalika bata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitazama kwenye kitabu hiki cha Kambi ya Upinzani, katika page za mwanzo kama kilipinga lakini page za mwisho, kikaja kikakubali yale ya leseni, baraza huru, hiyo ithibati. Kwa hiyo, utakuja kukuta kwamba ni kakidusi tu, lakini hiki kitu kinakubalika. Sasa hicho kidusi hapa pana tangawizi, pataoshwa na italika! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitazama humu unaweza ukaja ukakuta kwa lugha ya kilingala tunasema “poto poto” kwamba tope tupu. Huku unazungumza hivi, halafu unakuja unajikanyaga. Sasa katika hawa waandishi wa habari kama tunataka haki zao, basi moja ni hiyo accreditation kwa sababu tukitazama katika perspective ya waandishi wenyewe ambao wengi wametazama kule kwenye waandishi, hawakutazama kwa wale walaji wa habari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, suala la accreditation ni la muhimu, lakini hapa tukaja tukaleta historia, labda fulani alikuwa akifanya uandishi wa habari bila ya kuwa na taaluma, fulani alifanya uandishi wa habari bila ya kuwa na taaluma fulani. Sasa tusirudi huko, sasa hivi tunataka kwenda mbele, Taifa kama hili sasa hivi mambo mengi yamebadilika. Kuna mshairi mmoja anasema “zama zimebadilika na mambo yamegeuka” sasa zama zimebadilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, alikuwa anauliza hapa Mheshimiwa Tundu Lissu kwamba kwa nini iwe hivi katika masuala ya accreditation? Wa tilkal ayyamu nudawiluha baina nnasi, hizi ni siku ambazo mambo yanageuka, siku hazigandi, watu hawabakii vile vile, we are not static! Siku zote ulimwengu uko dynamic, mambo yako hivyo. Kwa hiyo, ni lazima tutazame jinsi ya kuweza kuwawezesha waandishi wa habari. Suala hili litawawezesha kufanya kazi zao vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni katika masuala ya habari hizi za uchochezi. Kusema ukweli ni muhimu sana kuwa na Sheria hii kwa sababu wengi wanasema daktari awe na taaluma, lakini mwandishi wa habari asiwe na taaluma. Daktari anaweza akamuathiri mtu mmoja katika chumba cha operesheni, lakini mwandishi wa habari anaweza akaathiri jamii nzima, Tanzania nzima, watu milioni 50.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hiyo accreditation ya mwandishi wa habari iwe kubwa zaidi kuliko hata ya daktari, kwa sababu daktari atamhukumu mmoja au atafanikiwa kumwathiri mmoja, lakini je, mwandishi wa habari kwa kalamu yake atawaathiri wangapi? Kuna mifano ya Rwanda 1994, kuna mifano ya Kenya 2006, kuna na mifano mingine chungu nzima ambayo inatumika. Kwa hiyo, ni lazima tutazame kwamba jinsi gani mwandishi wa habari ataweza yeye mwenyewe kupata sifa ya kuwa mwandishi wa habari na pia ile jamii ambayo anaitazama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine muhimu limezungumziwa neno la kashfa, pendekezo langu kwenye neno hili, bora lingetumika neno lingine kwa sababu kashfa ni kuweka wazi kwa maana fupi. Sasa anaweza mtu akaja akaambiwa amekashfu lakini akaweza kujitetea kutokana na asili ya neno lenyewe. Asili ya neno hili maana yake kukashfu ni kuweka wazi, inawezekana mtu kasema ukweli yaani, inawezekana ikaonekana amekashfu, akapata nafasi ya kujitetea kwa sababu hili neno asili yake ni Kiarabu, kashfa maana yake ni kufunua. Hata mtu ambaye anayepita hapa mavazi hayako vizuri inakuwa naye pia amejikashfu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hili neno kama tumekusudia kashfa ya kumsema mtu vibaya, kumwelezea mtu katika lugha mbaya ambayo itamharibia image yake, bora tungetafuta neno lingine ili hili neno la kashfa ambalo limezungumzwa humu likapata maana na katika maana hiyo ikaeleza na ikaeleweka ili kuepuka watu kuja kuweza kujitetea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la taaluma ya uandishi wa habari, huko nyuma au mpaka sasa hivi baadhi ya waandishi wa habari sio waandishi wa habari ni wanaharakati. Kwa hiyo, Sheria hii imekuja kuwafanya waandishi wa habari kuwa wanataaluma. Wengine ni wanaharakati na hata jinsi wanavyoongea, utawaona kwamba ni wanaharakati, sasa tuwatoe kwenye uanaharakati, tuwafanye wana taaluma…
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.4) wa Mwaka 2016
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai na uzima na nikushukuru wewe kutupa nafasi hii kuweza kuchangia hoja hii ambayo iko mbele yetu. Pia kuwapongeza Wabunge wapya wa Chama cha Mapinduzi ambao wamekuja katika Bunge hili, tunaahidi kushirikiana nao kwa hali na mali. Pia ninakipongeza Chama cha Mapinduzi kwa ushindi mkubwa wa kishindo kilioupata katika chaguzi za Madiwani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo na mimi nijikite katika hoja hii ya mkopo na msaada. Kusema kweli, kuna msemo wa kiarabu unasema, “maa-filbidh illa-l-barasi.” Kwenye weupe ukisugua utatia doa. Mheshimiwa Chenge alivyozungumza Mheshimiwa Chenge nafikiri watu wote hapa wameshaelewa kitu gani kinatakiwa. Kwa kuwa niliomba kuzungumza nitarejea baadhi ya maeneo ambayo nitayazungumza kama nilivyoyaelewa mimi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kitu kimoja ambacho ninapenda watu waelewe katika Bunge hili Tukufu, mwanzo nilipoona baadhi ya Wajumbe wanawasilisha ile hoja nikaona labda wanaionea huruma Zanzibar kwenye mikopo, lakini kumbe wanaona itafaidika, wanaona kumbe itafaidika sasa wakaona waeleze wazi. Kwa kushangaa baadhi ya watu wengine wakapanda yule punda wa bao, hawakujua kama wanapandishwa punda wa bao, wakaunga mkono na wao. Sasa kumbe unanyimwa maendeleo katika nchi yako, unanyimwa maendeleo katika eneo ambalo umetoka wewe kwa kukosa mkopo na msaada. Kwa hiyo, sikuelewa pale mwanzo kumbe walikuwa wako dilemma! Sasa hivi tumeshafahamu, nafikiri acha tuendelee mbele kuwajulisha Watanzania dhamana ambayo tumepewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono katika kifungu cha 12 pamoja na marekebisho ya Serikali ambayo wamekujanayo kwa sababu ya kitu kimoja. Zanzibar siyo sovereign state ambayo inaweza ikakopa yenyewe, tunakoelekea sasa hivi tunaenda kukopa mikopo ya kibiashara ni lazima kufanyike sovereign credit rating ambayo itafanyika kwa nchi na hakuna sovereign credit rating ambayo itaweza kufanyika kwa Zanzibar. Kwa hiyo, kukopa kwa Jamhuri ya Muungano ni sawa kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ni muhimu ni kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania watu hawaifahamu. Wanahisi kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kitu mbali kabisa. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Serikali ya Muungano, kama tulivyoseme, kwa hiyo, Zanzibar imo humo humo ndani yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa sheria hii kumetajwa Wizara ya Fedha na Waziri wa Fedha; kwa mujibu wa sheria hii kumetajwa Taasisi ya Benki Kuu na Gavana; kwa mujibu wa sheria hii kumetajwa Kamati ambayo itakuwa inashughulikia masuala ya Mikopo na Deni la Serikali. Sasa hivi vitu vyote ni vyombo vya Muungano, wakati wowote kiongozi wake inawezekana ikawa ni kutoka Zanzibar. Kwa hiyo, kutokana na hayo ina maana kwamba moja kwa moja Zanzibar inaweza ikafaidika na mikopo hiyo kwa kiasi kikubwa na inaweza ikafanya shughuli zake za maendeleo na kuwapatia maendeleo wananchi wa Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwanzo nilipomsikia mzungumzaji mmoja anazungumza aliposema kwamba Katiba Pendekezwa ilitaka suala hili Zanzibar iwe na uwezo wake wa kukopa, sasa leo unazungumzia Katiba Pendekezwa ambayo siyo Katiba tunayoizungumzia hapa, siyo Katiba iliyopo sasa hivi. Hii ni Serikali ya Chama cha Mapinduzi, ni Serikali inayoongozwa chini ya Serikali mbili, kwa hiyo mipango ambayo imo humu ni chini ya Serikali mbili, siyo kwa mujibu wa Katiba Pendekezwa. Katiba Pendekezwa au Katiba siku zote ni sheria mama kwa hiyo, haiwezekani azaliwe mtoto kwanza kwamba ili Sheria hii tuiweke hivyo kama ilivyo kwenye Katiba Pendekezwa halafu baadaye ndiyo aje azaliwe mama, hicho kitu ni cha ajabu sana! Hicho kitu ni cha ajabu sana na nilishangaa sana kumsikia mtu huyo anazungumza masuala hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala jingine katika masuala hayo ya kuhusiana na mikopo, kuna faida ambayo tunaweza tukaipata. Siku zote unapoenda kukopa yule anayekukopesha anaangalia default risk yako, kwa hiyo, kwa vyovyote vile kwa Zanzibar inapata faida kwa sababu default risk kwa Zanzibar ingekuwa kubwa, sasa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania default risk haiwezekani ikawa kubwa kuliko ambayo ingekuwa kwa Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije katika suala la misaada. Ingawa kuna changamoto katika suala hili misaada, lakini sote sisi tunafahamu kwamba kuna kitu kikubwa zaidi ambacho kinaweza kikakingwa kutokana na sheria hii, sote tunafahamu, kuna watu hatujui kama wameoteshwa au waliambiwa mzimuni kwamba, wewe kuna siku utakuwa Rais. Anapokosa tu anazunguka nchi zote kudai kwamba, Zanzibar inyimwe misaada, lakini kwa Tanzania hawezi! Kwa hiyo, faida hiyo ya misaada kwa Jamhuri ya Muungano ikiwepo na Zanzibar ni vizuri ili kuepukana na watu hao vitimbakwiri walioota au waliopata hicho kitu kutoka huko mzimuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, siku zote political risk kwa Zanzibar baada ya chaguzi zetu zinatokea na zinasababisha suala hili kuyumba, kwa hiyo, inapokuwepo katika sheria hii itasaidia. Kwa hiyo, mimi naunga mkono hiyo hoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania labda kuzikopesha taasisi mbalimbali. Serikali yenyewe ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania humu sote tunajua sisi ni Wabunge, pengine inakopa NMB, lakini hata humu Wabunge nao wamekopa NMB. Sasa je, wewe mtu binafsi umekopa NMB na Serikali imekopa NMB! Je, hapa kuna kasoro gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ikiwa Halmashauri, ikiwa taasisi yoyote, ikiwa kampuni yoyote, kukopa, mkopeshaji ni hiyari yake mwenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sawa.