Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Ali Hassan Omar King (9 total)

MHE. ALI HASSAN OMARY KING aliuliza:-
Tatizo la Mazingira ni tatizo mtambuka na tumeona jinsi Serikali ilivyojipanga kutatua tatizo hili kwenye maeneo tafauti:-
Je, Serikali imejipanga vipi kutatua tatizo la mazingira linalojitokeza la kudidimia kwa ardhi kwenye makazi ya watu?
NAIBU WAZIRI WA MUUNGANO NA MAZINGIRA (MHE. LUHAGA J. MPINA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ali Hassan King, Mbunge wa Jang’ombe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa kumejitokeza tatizo la kudidimia kwa ardhi na nyumba za makazi ya watu kwa vipindi na maeneo tofauti katika maeneo ya Zanzibar hususani 1998 na 2015. Kufuatia matukio haya, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) iliunda timu ya wataalam kutoka sekta mbalimbali ili kufanya utafiti wa kina na kubaini chanzo cha tatizo hili chini ya utaratibu wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, kupitia Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utafiti huo ulibaini sababu kubwa ya kudidimia kwa ardhi ni udhaifu wa ardhi hususani katika eneo la Jang’ombe ambalo liliwahi kuchimbwa udongo na mchanga kwa ajili ya kujengea nyumba za Mji Mkongwe katika kipindi cha zaidi ya karne tatu zilizopita. Uchimbaji huo uliacha mashimo makubwa yaliyofunikwa na udongo kidogo kidogo kwa miaka mingi na hatimaye maeneo hayo kujengwa nyumba za makazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali hiyo pia ilichangiwa na kujaa maji katika maeneo hayo kutokana na kiwango kikubwa cha mvua zilizonyesha katika miaka ya matukio yaani 1998 na 2015. Aidha, sababu nyingine zinazoweza kusababisha kudidimia kwa ardhi ni pamoja na udhaifu wa miamba ya chini ya ardhi kuhimili uzito wa majengo, maeneo husika kuwa na asili ya unyevu mkubwa (wetlands) pamoja na sababu zitokanazo na athari za mabadilliko ya tabianchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuzuia madhara yanayotokana na kudidimia kwa ardhi, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaendelea kuchukua hatua zifuatazo:-
(i) Kuyafanyia uchunguzi wa kina maeneo yote yenye matatizo ya kudidimia kwa ardhi na kuorodhesha nyumba zilizomo katika maeneo hayo na wahusika watapatiwa maeneo mengine kwa ajili ya kujenga nyumba za makazi ya kudumu. Hivi sasa upimaji wa viwanja 500 katika eneo la Tunguu unafanyika ili wananchi watakaohamishwa katika maeneo yanayodidimia wapatiwe viwanja. (Makofi)
(ii) Kuandaa utaratibu wa kudhibiti ujenzi holela katika maeneo ya miji na vijiji na kuboresha barabara na njia za maji ya mvua ili kuzuia madhara ya mafuriko na kudidimia kwa ardhi; na
(iii) Kuelimisha wananchi kupitia vyombo vya habari na matangazo kuhusu madhara ya mvua kubwa ikiwemo kudidimia kwa ardhi na mafuriko ili kuchukua tahadhari na kuepusha maafa.
MHE. ALI HASSAN OMAR KING aliuliza:-
Serikali ina mpango gani wa kutatua tatizo la makazi kwa askari wa Jeshi la Polisi na Mheshimiwa Rais aligusia azma hiyo alipokuwa akilihutubia Bunge hili la Kumi na Moja kwenye kikao cha ufunguzi.
Je, Serikali imepanga kujenga mikoa mingapi majengo hayo ikiwemo Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ali Hassan King, Mbunge wa Jang‟ombe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza kuchukua hatua za makusudi kukabiliana na uhaba wa nyumba za Jeshi la Polisi. Kwa kutumia mifuko ya Hifadhi ya Jamii, chini ya mpango wa mikopo wenye riba nafuu Serikali imeshajenga nyumba 360 katika Mikoa ya Dar es Salaam, Unguja na Pemba.
Mheshimiwa Spika, Serikali pia inakusudia kujenga nyumba nyingine 4,136 katika mikoa 17 ya Tanzania Bara na Zanzibar. Aidha, Serikali itaendelea kutatua changamoto za uhaba wa nyumba za askari kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo mikopo yenye riba nafuu, Miradi Shirikishi (PPP) na kwa kutumia fedha za bajeti ya Serikali kadri hali ya uchumi itakavyokuwa ikiimarika.
Mheshimiwa Spika, mkakati huu utakwenda sambamba na Mipango ya Maendeleo ya Serikali ukilenga kufikia idadi ya nyumba za makazi kwa askari wote waliopo sasa na watakaotarajiriwa kuajiriwa baadaye.
MHE. ALI HASSAN OMAR KING aliuliza:-

Je, kwa nini uvuvi wa kuzamia kwa kutumia chupa umezuiliwa?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ali Hassan King, Mbunge wa Jang’ombe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, shughuli za uvuvi nchini zinasimamiwa kwa mujibu wa Sheria Na.22 ya Mwaka 2003 na Kanuni zake za mwaka 2009 na Miongozo mbalimbali ambayo hutolewa kwa ajili ya kusimamia na kuhakikisha kuna matumizi endelevu ya rasilimali za uvuvi. Kwa mujibu wa Kanuni ya Uvuvi ya Mwaka 2009, kifungu cha 66(I – Q), vifaa vya kupumulia chini ya maji au scuba au mitungi ya gesi haviruhusiwi kutumika kwa ajili ya kuvua samaki au viumbe wengine wa baharini. Aidha, kwa mujibu wa kifungu cha 66(2), vifaa vya kupumulia chini ya maji au mitungi ya gesi vinaweza kutumika tu kwa ajili ya uvuvi wa burudani (sport fishing), uvuvi wa samaki wa mapambo, mafunzo na utafiti na ni kwa kibali maalum.

Mheshimiwa Spika, wavuvi haramu wanaotumia milipuko hutumia mitungi ya gesi kuzamia kwa ajili ya kukusanyia samaki waliowaua kutokana na milipuko hiyo. Athari za milipuko ni pamoja na kuharibu matumbawe, (coral reefs) na mazingira ya baharini kwenye maji ambayo ni mazalia na makulia ya samaki pamoja na viumbe wengine na hivyo kuharibu mfumo wa ikolojia ambao unatishia kutoweka kwa kizazi cha samaki. Kuua samaki bila ya kuchagua wakiwemo samaki wachanga na mayai yake na hivyo kuhatarisha uendelevu wa rasilimali za uvuvi nchini.

Pia milipuko husababisha wavuvi kupata ulemavu na hata kifo, hivyo kutokana na sababu hizi Serikali iliamua kupiga marufuku uvuvi wa kutumia chupa au mitungi ya gesi.
MHE. ALI HASSAN OMAR KING Aliuliza: -

Je, Serikali imefikia hatua gani katika kufuatilia fedha za wananchi zilizopo katika Benki ambazo zimezuiliwa kuendesha shughuli zao hapa nchini?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu tangu niteuliwe kuwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kuchukua nafasi hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema kwa kuijaalia nchi yetu amani na utulivu na kutujaalia sisi sote uzima na afya njema.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nichukue nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Rais wangu, Dkt John Pombe Joseph Magufuli kwa kuniamini na kuniteua katika nafasi hii. Aidha, nitoe shukrani kwa familia yangu kwa kuendelea kunitia moyo hivyo kunipa nguvu na kuendelea kutekeleza majukumu yangu kiufanisi. Vilevile niwashukuru viongozi wangu wa CCM pamoja na UWT kuanzia ngazi ya Mkoa hadi Taifa kwa kuniamini na kunipa nafasi hii kuwa mwakilishi wao hapa Bungeni. Ahsanteni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo mafupi, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ali Hassan King, Mbunge wa Jang’ombe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2017 na 2018, Benki Kuu ya Tanzania ilizifutia leseni ya kufanya biashara ya kibenki benki saba kwa mujibu wa vifungu vya 11(3)(i), 41(a), 58(2)(a), na 61(1) vya Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006. Benki zilizofutiwa leseni ya kufanya biashara nchini ni pamoja na: FBME Bank Limited; Mbinga Community Bank Plc, Njombe Community Bank Limited, Kagera Farmers’ Cooperative Bank Limited, Meru Community Bank Limited; Efatha Bank Limited; na Covenant Bank for Women (T) Limited.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuzifutia leseni benki hizo Benki Kuu ya Tanzania iliteuwa Bodi ya Dhima ya Amana (Deposit Insurance Board) kuwa Mfilisi. Katika kutimiza wajibu wake wa msingi Bodi ya Bima ya Amana ilianza zoezi la kulipa fidia ya bima ya amana ya Sh.1,500,000 kwa waliostahili kulipwa bima ya amana na zoezi hili bado linaendelea kwa wateja ambao hawajajitokeza kuchukua fidia. Sanjari ya zoezi hili DIB inaendelea na zoezi la ufilisi wa benki hizo tajwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Desemba 2020, Sh.9,440,305,975.88 zimeshalipwa kwa wateja ambao wenye amana katika Benki sita za Wananchi (Community Banks) kama zilivyotajwa hapo juu ukiiondoa Benki ya FBME. Malipo hayo ni sawa na asilimia 77.27 ya kiasi cha Sh.6,393,690,743.89 zilizotengwa kwa ajili ya kulipa fidia. Aidha, jumla ya wateja waliolipwa ni 21,675 kati ya wateja 57,076 ikiwa ni asilimia 37.98 ya wateja waliokuwa na amana zilizostahili fidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Benki ya FBME, hadi mwishoni mwa mwezi Desemba 2020, jumla ya Sh.2,428,779,092.11 zimelipwa kwa wateja wenye amana ambazo ni sawa na asilimia 52.13 ya kiasi cha Sh.4,659,011,005.76 zilichotengwa. Aidha, jumla ya wateja waliolipwa ni 3,443 kati ya wateja 6,628 ambao ni sawa na asilimia 51.95 ya wateja waliokuwa na amana zinazostahili fidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, wateja waliokuwa na amana inayozidi Sh.1,500,000/= watalipwa kiasi kilichobakia chini ya zoezi la ufilisi ambalo kwa mujibu wa sheria na taratibu za ufilisi kitakacholipwa kitategemea fedha zitakazopatikana kutokana na kuuza mali za benki husika. Zoezi hilo la kukusanya madeni na mali za benki hilo linaendelea ili kupata fedha za kuwalipa wateja wenye amana zenye thamani zaidi ya Sh.1,500,000/=. Ahsante.
MHE. ALI HASSAN OMAR KING aliuliza:-

Je, wizi unapotokea kwenye akaunti ya benki ya mteja uliofanywa na mtumishi wa benki ni nani mwenye wajibu wa kumlipa mteja?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ali Hassan Omar King, Mbunge wa Jang’ombe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, wizi unapotokea kwenye akaunti ya benki ya mteja, uchunguzi wa kina hufanywa na vyombo husika katika masuala ya upelelezi ikiwa ni pamoja na Jeshi la Polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa kadri hali na mazingira ya tukio yatakavyokuwa yametokea.

Mheshimiwa Naibu Spika, endapo ikibainika kuwa wizi huo umefanywa na mtumishi wa benki, hatua stahiki huchukuliwa kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo ikiwa ni pamoja na mteja kulipwa kiasi cha fedha alichoibiwa na mhalifu kuchukuliwa hatua za kinidhamu pamoja na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria. Pia, Benki Kuu hutoa adhabu kwa benki husika pale inapobainika kwamba utaratibu uliowekwa na benki husika ulikuwa na kasoro zilizochangia kuibiwa kwa fedha za mteja.
MHE. ALI HASSAN OMAR KING aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatatua mgogoro wa bei ya umeme unaotumika na Watanzania waishio Zanzibar ili kuweka usawa kwa Watanzania wote?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa wa Nishati naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ali Hassan Omar King, Mbunge wa Jang’ombe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimeendelea kushughulikia suala la bei ya kuuza na kununua umeme baina ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) ili kuupatia ufumbuzi mgogoro huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha mwaka 2020/2021 Timu ya Wataalamu wa Taasisi husika zilikutana katika vikao mbalimbali na kufanya uchambuzi wa kina wa vigezo vilivyohusika katika kupanga bei hiyo ya kuuzia umeme kwa wateja wakubwa wa kununua umeme ikiwemo ZECO. Kutokana na uchambuzi huo, inapendekezwa kuwa vigezo hivyo vipitiwe upya ili kuleta unafuu kwa wateja wa aina hiyo ikiwemo ZECO.

Mheshimiwa Naibu Spika, mapendekezo hayo yaliwasilishwa katika Kamati ya Wizara zinazoshughulikia masuala ya Muungano ili kufanyia kazi mapendekezo hayo na kupata ufumbuzi wa kudumu wa suala hili.
MHE. ALI HASSAN OMAR KING aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kufungua Ofisi Ndogo ya Hazina Zanzibar kama ilivyo kwa taasisi nyingine za Muungano ili kurahisisha huduma kwa wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wanaoishi Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ali Hassan Omar King, Mbunge wa Jang’ombe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, huduma za malipo ya mafao ya wastaafu wanaolipwa na Wizara ya Fedha na Mipango hufanyika kupitia Ofisi za Hazina Makao Makuu, Dodoma. Aidha, Ofisi za Hazina Ndogo zilizopo katika Mikoa ya Tanzania Bara hutumika kwa ajili ya kukusanya hoja za wastaafu na kuziwasilisha Hazina Makao Makuu, Dodoma.

Mheshimiwa Spika, kwa wastaafu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanaoishi Zanzibar, Wizara ya Fedha na Mipango ya Serikali ya Muungano wa Tanzania mara zote imekuwa ikifanya kazi kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa ajili ya kupokea hoja za madai ya wastaafu hao na kuziwasilisha Hazina Makao Makuu, Dodoma kwa ajili ya taratibu za malipo.

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Fedha na Mipango ya Serikali ya Muungano wa Tanzania itaimarisha ushirikiano na Wizara ya Fedha na Mipango ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuwahudumia wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wanaoishi Zanzibar kama ambavyo hushirikiana na Ofisi za Hazina Ndogo zilizopo Tanzania Bara.
MHE. ZAYTUN S. SWAI K.n.y. MHE. ALI HASSAN OMAR KING aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itawatambua watoto wenye ulemavu ambao wanaishi kwenye mazingira magumu ili kuwasaidia kwa matibabu na kimaisha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ali Hassan King, Mbunge wa Jang’ombe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuwatambua na kuwapatia huduma stahiki watu wenye ulemavu ikiwa ni pamoja na waishio katika mazingira hatarishi zaidi kwa kuzingatia aina ya ulemavu walionao na hitaji la msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utambuzi huo umekuwa ukifanyika kwa kuzingatia Sera ya Taifa ya Maendeleo na Huduma kwa Watu wenye Ulemavu ya mwaka 2004. Kwa kuzingatia sera hiyo, Serikali imeanzisha Rejesta ya Utambuzi wa Watoto Waishio katika Mazingira Hatarishi zaidi. Serikali imeweka pia mfumo wa ulinzi na usalama wa watoto. Aidha, Serikali imekamilisha Mwongozo wa Utambuzi wa Mapema wa Afua na Stahiki za Watoto wenye Ulemavu wa mwaka 2021 unaoainisha namna sahihi ya kumtambua mtoto mwenye ulemavu na afua anazostahili kupatiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto wenye ulemavu waishio katika mazingira hatarishi zaidi hupatiwa huduma kupitia afua mbalimbali ikiwemo kupatiwa elimu kupitia shule zenye vitengo maalum na jumuishi; kuwapeleka katika hospitali kwa ajili ya kupatiwa afua za matibabu, kupatiwa stadi za maisha kwa lengo la kuwajengea uwezo ili waweze kujitegemea na kujilinda; kupatiwa uchangamshi wa awali na huduma za utengamao; kuwarejesha katika familia zao na kuwaweka katika familia za kuaminika (fit family); utoaji wa vifaa saidizi; kuwaunganisha na vyuo maalum vya watu wenye ulemavu kwa ajili ya kupatiwa ujuzi na huduma za marekebisho na kwa wale ambao hawana walezi au wazazi hupelekwa kwenye makao ya watoto kwa ajili ya huduma mbalimbali.
MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN K.n.y. MHE. ALI HASSAN OMAR KING aliuliza: -

Je, TRA itasitisha lini kukusanya na kuzirudisha fedha za VAT ilizokusanya kutoka kwenye miamala ya mtandaoni iliyofanywa Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ali Hassan Omar King, Mbunge wa Jimbo la Jang’ombe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria za Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa pande zote mbili za Muungano zimeweka msingi wa kutoza na kukusanya VAT pale ambapo huduma inapotolewa. Kwa muktadha huo, huduma ikitolewa Tanzania Bara, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inatoza VAT ya asilimia 18 kwa mujibu wa Sheria ya VAT inayotumika Tanzania Bara na huduma ikitolewa Zanzibar, Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) inatoza VAT ya asilimia 15 kwa mujibu wa Sheria ya VAT inayotumika Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kutambua sehemu ambapo huduma imetumika, Serikali za pande zote mbili za Muungano ziliunda mfumo wa kielektroniki ujulikanao kama Electronic Revenue Collection System (e-RCS) wenye uwezo wa kutambua miamala yote inavyofanyika na hivyo kusaidia kutunza takwimu sahihi za mauzo yanayotokana na miamala ya mitandao inayofanywa na watumiaji wa kila upande. Mfumo huu unasimamiwa na kamati ya wataalam wa kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB).

Mheshimiwa Mwenyekiti, mifumo ya kampuni zote za simu hapa nchini imeunganishwa na mfumo wa Serikali wa e-RCS na taarifa za miamala ya mitandao hutolewa kila mwezi ikiainisha bayana huduma zilizotumika Tanzania Bara na zile zilizotumika Zanzibar. Ahsante.