Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Ali Hassan Omar King (12 total)

MHE. ALI HASSAN OMARY KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Kwanza, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri ambayo hata na mimi sasa nimeelewa nini tatizo na chanzo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa zimewekwa hatua za kuchukuliwa kama ambazo tumeziona pale, namuomba Waziri ambaye anahusika na masuala haya ya mazingira na utafiti, japo siku moja twende tukaone ile hali tuweze kuangalia nini kifanyike ili tuweze kupata ufumbuzi zaidi ya hapa ambapo tumeona. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MUUNGANO NA MAZINGIRA (MHE. LUHAGA J. MPINA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Ali Hassan King kwa jinsi alivyo na mapenzi mema hasa katika suala zima la mabadiliko ya tabia nchi. Ninachopenda kumhakikishia tu hapa kwamba niko tayari na tutafuatana na Mheshimiwa Mbunge tutatembelea maeneo haya yote ambayo yamedidimia na tutaungana na wataalam wengine kutoka Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais. Nataka nimwambie tu kwamba bila kupoteza muda siku ya Jumanne na Jumatano nitakuwa Zanzibar kwa ajili ya kazi hii na tutafuatana naye.
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Kwanza napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri na Wizara hii ya Mambo ya Ndani kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuimarisha ulinzi na usalama katika nchi yetu.
Mheshimiwa Waziri atakubaliana na mimi kwamba katika majengo hayo ambayo yamejengwa 360 kwa misimu hiyo iliyopita ni jengo moja ninalolikumbuka mimi ambalo lipo pale Mkoa wa Mjini - Ziwani Polisi kwenye Jimbo langu. Pia Serikali imejenga jengo lingine kwa upande wa Zanzibar kule Pemba, haya majengo ukitazama ki-percentage ni madogo zaidi. Lakini mimi sina uhakika na taarifa hizi za 360; sasa namuuliza Mheshimiwa Waziri katika 360 ni majengo mangapi yalijengwa kule Zanzibar na katika haya 4,130 mangapi yanatarajia yatajengwa kule Zanzibar? Hilo swali la kwanza.
Mheshimiwa Spika, swali la pili Seriklai iliji-commit katika mwaka 2011, Juni kwamba kwa kupitia bajeti wa mwaka ule ingelifanya ukarabati majengo ya Ziwani Polisi, lakini pia wangelijenga na uzio na mpaka hivi sasa ninavyozungumza kwamba askari wanajitegemea wenyewe kufanya ukarabati katika nyumba ambazo wanaishi.
Je, Waziri atanihakikishia ni lini Serikali itakuja kufanya ukarabati wa majengo yale ya Ziwani Polisi pamoja na kujenga uzio? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge wa Jang‟ombe kwa ushirikiano wake mzuri sana ambao anatupa kwani ameshiriki katika ujenzi wa Kituo cha Afya pale Ziwani pamoja na uchimbaji wa kisima cha maji. Tunampongeza sana na tunamuahidi ushirikiano zaidi.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na maswali yake mawili, ni kwamba mradi wa nyumba 4,136 ambazo tunatarajia tujenge ni nyumba 200 ambazo zinatarajiwa kujengwa Unguja na nyumba 150 zinatarajia kujengwa Pemba, kwa hiyo ukifanya jumla ya idadi ya nyumba zote 350. Pia ameuliza kuhusiana na zile nyumba ambazo zilijengwa kupitia mradi wa NSSF. Ni kwamba nyumba zilizojengwa ni kweli maghorofa yale yalikuwa ni mawili kwa maana ya Unguja na Pemba lakini yana uwezo wa kukaa familia 12 kila moja kwa hiyo kufanya jumla ya familia 24.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la ukarabati wa nyumba za Ziwani ni kweli nyumba zile ni chakavu lakini kama ambavyo tunazungumza siku zote kwamba, nyumba hizi za Polisi nyingi ni chakavu. Ndiyo maana tuna mchakato wa kuweza kurekebisha nyumba hizi pamoja na kujenga mpya. Kwa hiyo, niseme tu kwamba tunafahamu gharama za ujenzi wa nyumba hizo, ukarabati huo ambao unakadiriwa kufika takribani shilingi milioni 400; kwa hiyo tutajitahidi kwamba pale fedha itakapopatikana tuweze kuanza hiyo kazi haraka itakapowezekana.
Mheshimiwa Spika, tunafahamu umuhimu wa nyumba za Ziwani, ikiwa ni Makao Makuu ya Jeshi la Polisi na chimbuko la historia hata Mapinduzi ya Zanzibar yalianzia pale.
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Jibu la msingi la Mheshimiwa Waziri amesema kwamba kodi hizo zinalipwa kwa kigezo cha usajili. Ukweli ni kwamba kampuni zote zinasajiliwa kutokana na headquarter alipo regulators. Kwa hiyo, mabenki mengi na makampuni ya simu yako Bara na regulators wake wako Bara, usajili wake unafanyika Bara wanalipia Zanzibar. Lakini ukweli upo kwamba mkaa na maiti haachi kulialia na mtegemea nundu haachi kununa, je, Serikali iko tayari kutumia kigezo cha operations za hizi kampuni kodi ikawa-charged kule ambapo zina-operate?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, kodi ambayo tunaiita corporate tax inalipwa kule ambako kampuni imesajiliwa. Hilo alilolisema Mheshimiwa Ali King ni
sahihi lakini pia naomba ndugu zangu tuweze kuangalia uhalisia ulivyo. Kwa mfano makampuni makubwa kama Kampuni ya Bakhresa, Kampuni ya Zanzibar Insurance, Kampuni ya Zantel zimesajiliwa Zanzibar na kodi ya mapato inalipwa kule Zanzibar.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hicho anachokisema naomba nimwambie Mheshimiwa Ally King kwamba hata hizi ambazo zinakusanywa kule Zanzibar, zinakusanywa huku Bara kwa pamoja zinaingia katika mfuko mkuu wa Serikali na kwa pamoja fedha hizi zinapoingia kwenye mfuko mkuu wa Serikali tunaweza pia kuhudumia
Serikali zote za pande mbili ya Bara na Zanzibar.
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwanza nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri kwamba uhai wa Taifa ni kodi. Lakini kuna kodi inakuwa-charged mara mbili ya VAT kwa bidhaa hizo za vifaa vya ujenzi ambavyo vinakwenda Zanzibar kwa wale ambao non registered for VAT. Je, Serikali ina maelezo gani juu ya kutatua kero hii ya double VAT?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza si sahihi kusema kodi inalipwa mara mbili kwa kutoka Tanzania Bara kwenda Tanzania Zanzibar si sahihi. Kodi ya VAT ni kodi ya mlaji inayolipwa na malaji wa mwisho na kodi hii inakuwa-charged mara moja tu, kodi ambayo najua ina changamoto ya kusema kwamba ina sura ya kulipwa mara mbili lakini kiuhalisia hailipwi mara mbili ni kodi ya import duty ambayo kwa wenzetu Wazanzibari wanapoingiza bidhaa kule Zanzibar mfumo wanaotumia haulingani na mfumo wa Tanzania Bara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo na ile pia hatuwezi kusema ni double taxation ile ni kuhakikisha kwamba kunakuwa na usawa katika soko wa bidhaa zinazoingizwa kutoka nje ya nchi.
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi. Waswahili wanasema usipoziba ufa utajenga ukuta na usipotibu utazika, swali langu dogo tu, namuuliza Mheshimiwa Waziri. Ni lini Serikali itakusanya mchango wa maafa kwa jengo bovu la Ziwani Polisi la Kilimanjaro pindi maafa hayo au jengo litakapoanguka. Ahsante.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili limeletwa mara kadhaa. Niseme tu, kwa sababu tuna siku chache kabla hatujakwenda kwenye bajeti yetu tutapa fursa tuongee na Mheshimiwa Mbunge ili tukubaliane kuhusu ni lini kwa sababu swali lake ametaka tumtajie ni lini tutachukua hatua hiyo aliyoisema yeye.
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nimesikia jawabu la Serikali, lakini yeye amejibu mabomu hakujibu gesi. Gesi katika kuzamia haina madhara yoyote kwa sababu kwenye kina kirefu cha maji wenyewe tunaita bahari lujii inawezekana ikawa watu wanatumia nyavu kwa hiyo nyavu imekwama kule chini, kwa sababu ni kina kirefu anaweza akatumia gesi kuzamia kwenda kule. Halafu kingine, hayo mazingira ambayo anayasema Mheshimiwa Waziri kwamba yanaweza yakaharibiwa kwa mabomu kwa baharini wakati mwingine maji yanakupwa yanaweza yakafikika hata kwa miguu lakini haja ya gesi inakuwepo pale maji yanapojaa.

Mheshimiwa Spika, naomba Waziri azidi kuniambia chupa inaharibu kitu gani alichotaja hapa ni mabomu, chupa inaharibu kitu gani, mabomu yanaweza yakategwa hata bila ya chupa. Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ally Hassan King, Mbunge wa Jang’ombe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika jibu langu la msingi nimeeleza kwamba ugomvi wetu siyo chupa, ugomvi ni matumizi yanayotokana na ile mitungi ya gesi. Kwa maana tunafahamu kuna mahali katika bahari umbali kwa maana ya kina kilomita 40, mvuvi ni lazima awe na namna ya kuweza kumfikisha kule na kufanya shughuli yake, lakini kwa utafiti wetu hapo nyuma ilionekana wazi kwamba waliokuwa wakienda kufanya uzamiaji, ukiacha wale waliofanya uzamiaji kwa ajili ya sport fishing na utafiti, wengine wote walikuwa ni wale wanaoambatana na shughuli za uvuvi haramu na ndiyo maana Serikali ikasema kwa sababu hiyo basi tutazuia zoezi hili isipokuwa kwa kibali maalum cha wale wanaofanya utafiti na wale wanaofanya sport fishing.

Naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba kwa sasa Serikali tupo katika kuboresha sheria zetu na kuboresha kanuni zetu, tumekisikia kilio hiki cha wavuvi wazamiaji na sisi tunakifanyia kazi, endapo sheria hizi zitapitishwa na kanuni hizi mpya tuna imani kwamba inawezekana katika jambo ambalo litakuwa limekwenda kuboreshwa mojawapo ni jambo hili. (Makofi)
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha kwa majibu yake mazuri na amenipa mwongozo na yametoa matumaini, lakini nina maswali mawili mdogo ya nyongeza: -

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa ni wengi walioweka amana zao pale walitumia viinua mgongo vyao kuweka amana katika Benki ya FBME, hasa kule kwetu Zanzibar nilikotoka. Amesema wamelipwa wateja nusu na waliobakia bado hawajalipwa na watakaolipwa watalipwa kutokana na fedha ambazo watapata amount ambayo haitazidi 1,500,000/=; na kwa kuwa hii benki ni ya nje; na kwa mujibu wa Sheria ya Benki na Financial Institutions, BOT ndio wenye dhamana ya kukaribisha mabenki ndani, swali langu;’ je, ni lini watalipwa fedha zao zote kwa sababu, benki hii haijafilisika FBME?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni lini Benki Kuu ya Tanzania itaacha kuingiza benki hovyo hovyo kama hizi za kutoka nje zikaleta madhara katika nchi yetu? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Hassan King kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza alilouliza Mheshimiwa King amesema kwamba, lini wateja hao ambao wana amana zao katika benki ya FBME watapatiwa fedha zao. Kama nilivyoeleza katika jibu la msingi, wateja waliokuwa na amana zaidi ya shilingi 1,500,000 watalipwa kiasi kitakachobaki chini ya zoezi la ufilisi wa benki ambapo kwa mujibu wa sheria na taratibu kiasi kitakacholipwa kitategemea fedha zitakazopatikana kutokana na kuuza mali za benki husika. Suala hili liko chini ya mujibu wa sheria, kwa hivyo sheria zitakapomalizika Mheshimiwa King basi, wateja wote wenye amana katika benki hiyo watalipwa pesa zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; anaulizia lini benki zitatoa ukomo wa kuchukua benki ambazo hazina faida katika nchi yetu. Mheshimiwa King jibu lako la pili naomba nilichukue ili nikalifanyie kazi na nitakujibu kwa barua ili uelewe maelezo zaidi katika Serikali yetu, uweze kupata ufafanuzi zaidi wa kupata jibu lako sahihi. Ahsante. (Makofi)

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyoyatoa. Nataka tu niongezee kakipengele kadogo kale ambako kanaongelea lini hawa watu watapata fedha. Kwa benki hii ambayo Mheshimiwa Mbunge ameuliza utaratibu huu ambao ameuelezea Mheshimiwa Naibu Waziri umekuwa mrefu kwa sababu benki hii ilikuwa ina-operate katika nchi mbili. Kwa maana hiyo, ule utaratibu wa mufilisi kuweza kukusanya madeni na kukusanya na mali zote ili azibadilishe ziwe fedha ili aweze kuwalipa wale wateja ambao amana zao zilikuwa zinazidi kile kiwango cha awali ambacho wanapewa pale benki inapokuwa kwenye mufilisi, kikamilike. Kwa hiyo, hicho kikishakamilika hapo ndipo ambapo mufilisi ataweza kufanya hiyo kazi ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri ameisema na hawa wateja waweze kupata hizo fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili la pili ambalo Mheshimiwa muuliza swali ndugu yangu King amesema ni lini Benki Kuu itaacha kuruhusu mabenki yaingine hovyo hovyo. Nimhakikishie kwamba, mabenki hayaingii hovyo hovyo na Serikali inafanya due diligence kwa kila benki inapotaka kufanya kazi hapa nchini na ndio maana Benki Kuu iliingilia kati ilipoona baadhi ya mabenki hawaendi sawasawa na vile ambavyo yanatakiwa yafanye kwa mujibu wa sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe rai tu kwa wananchi wetu kwa sababu, huwa kuna report zinazotolewa kila miezi mitatu na kunakuwepo na mkutano mkuu wa wadau wa benki na sisi tuwe tunafuatilia ili tuweze kuona mienendo ya benki. Tusisubirie tu Benki Kuu ambaye ni msimamizi aweze kufanya jukumu hilo ambalo linawahusu pia, wadau wadau wa benki ambao wanatakiwa watoe muongozo kwa benki yao. (Makofi)
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa jawabu hili zuri naipongeza sana Serikali kwa kuwa na utaratibu mzuri wa kuwajali wananchi wake dhidi ya vitendo hivi vya uhalifu vinavyotokeza katika mabenki ambavyo hufanywa na watumishi ambao sio waaminifu. Nimepata tamaa sasa na mimi. Swali la kwanza; je, ni lini Serikali itawalipa wateja 103 wa Tawi la NBC la Zanzibar Forodhani ambao fedha zao kiasi cha milioni 400 ziliibwa na watumishi wa benki hii ya NBC Forodhani kule Zanzibar pamoja na kuichukulia hatua au adhabu hiyo benki ya NBC kwa kutowalipa wateja hao?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; ili kuhakikisha kwamba hawa wazee wanalipwa fedha zao hizi za kiinua mgongo ambao wengine tayari wameshafariki; je, Serikali iko tayari kufuatilia kwa haraka pamoja na mimi kuhakikisha kwamba haya waliyosema yanatokea?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ali Hassan King kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimejibu katika swali la msingi nilieleza kwamba, kwanza nieleze kwa mujibu wa Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya Mwaka 2006 inaeleza kwamba moja ya majukumu ya Benki Kuu ni kusimamia ufanisi na usalama wa wateja, kusimamia na benki nyingine ili kuhakikisha usalama na ufanisi wa amana za wateja katika benki. Hiyo ndiyo dhamana yake kubwa. Kwa hiyo ikiwa tukio hili ambalo limejitokeza katika Benki ya National Bank of Commerce (NBC) ya uhalifu ambao umetokezea sasa haijaelezewa na muuliza swali kwamba uhalifu huu umesababishwa na nani. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge muuliza swali kwamba nitakapotoka hapa nitafuatilia suala hili tujue kwamba je, wizi huu ulivyofanyika, uchunguzi umeshafanyika kama ambavyo nimejibu katika swali la msingi? Kama uchunguzi huu umefanyika ni nani ambaye amesababisha uhalifu huu? Kama suala hili limesababishwa na wafanyakazi watumishi wa benki, basi hatua zitachukuliwa. Kama suala hili limesababishwa na mifumo ya Benki, basi Benki Kuu ya Tanzania itachukua dhamana ya kuhakikisha kwamba fedha zile zinarudishwa na benki ile na zitachukuliwa hatua benki husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niseme kwa sababu suala lake sio suala ambalo ni mahsusi, nahitaji kufahamu kwa undani hasa kujua hasa wizi huu uliojitokeza chanzo chake ni nini na kama uchunguzi umefanyika, umefikia katika hatua gani ili tuweze kutoa maelekezo ya jinsi gani hatua zitachukuliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kwamba tutakuwa tayari kufuatilia, ndiyo maana nikaeleza kwamba kwa sababu jambo hili ni jambo ambalo yeye Mheshimiwa Mbunge analifahamu zaidi tutakuwa tayari mimi na yeye tushirikiane tufuatilie ili tufahamu kabisa kwamba jambo hili limefika katika hatua gani na tuweze kuchukua hatua pale ambapo tumefikia.
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Spika, ahsante; humu mna jibu hakuna jawabu, kwa sababu nilichoomba kwamba ni lini Serikali itafungua Ofisi ya Hazina Ndogo lakini jibu lililokuwemo humu wamesema watafanya mashirikiano na Wizara ya Fedha ya Zanzibar kitu ambacho hakiwezekani kwamba taarifa za Serikali ya Jamhuri ya Muungano zikawepo katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Hawa wazee taarifa zao zipo Wizara ya Fedha ya Muungano, wanapokuwa na matatizo wanakwenda Dar es Salaam na wanachukua muda mwingi hadi wengine wanasamehe mafao yao. (Makofi)

Sasa nataka jawabu Serikali ina mpango gani wa kuwa na ofisi kama ilivyokuwa ofisi nyingine? Mpango wa kuwa na ofisi, hilo lingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, je, hawa wazee wanaokuja mpaka wakakata tamaa wakarudi wakasamehe mafao yao Serikali itachukua hatua gani?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ali Omar Hassan King, Mbunge wa Jang’ombe kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza hatujapokea malalamiko ambayo yanaonesha kuna usumbufu wa malipo ya wastaafu kupitia utaratibu ambao tunao sasa hivi wa kushirikiana kati ya Wizara za Fedha za pande mbili za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hivyo, nimuombe Mheshimiwa Mbunge kama ana malalamiko mahususi ambayo pengine hayajatufikia sisi, basi ayawasilishe tutayashughulikia haraka iwezekanavyo.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na lini tutajenga ofisi, masuala ya ujenzi wa ofisi ni masuala ambayo yanahitaji bajeti na uwezo wa kifedha na maandalizi. Kwa hiyo, kutoa kauli hasa ni lini kwa sasa hivi inaweza ikawa sio rahisi sana hata hivyo Mheshimiwa Mbunge nimhakikishie kwamba kwa sababu ofisi hizi ndogo zilizopo mikoani kwa upande wa Tanzania Bara ambazo zimejengwa huwa zinafanya kazi kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ya Umma na Kanuni zake ambayo pamoja na mambo mengine, zinahudumia Ofisi za Makatibu Tawala wa Mikoa pamoja na Idara za Serikali ya Muungano ambazo kwa upande wa Zanzibar Ofisi za Tawala za Miko ana hizi Idara za Serikali shughuli zake zinafanywa na Wizara ya Fedha ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Kwa hiyo, shughuli zile hazijakwama kwa upande wa Zanzibar kwa sababu zinasimamiwa na Wizara ya Fedha ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ambayo sio masuala ya Muungano.

Mheshimiwa Spika, zipo taasisi ambazo tayari zimeshajengwa majengo huko kama BOT na TRA zina Ofisi Zanzibar, kwa hiyo, masuala mengine ya ujenzi wa miundombinu ni masuala ambayo hayaendi kwa wakati mmoja, yanakwenda hatua kwa hatua.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba concern yake Serikali tunaitambua na pale ambapo hali itaruhusu basi tutakamilisha utaratibu huu ambao amependekeza.
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Spika ahsante, kwa kuwa ni swali la msingi liliulizia bei ya umeme, nami niulize ni lini TANESCO itatausha bei ya umeme inayouza ZECO?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ali King kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, TANESCO kwa maana ya Shirika la Umeme Tanzania imekuwa na mkataba na Shirika la ZECO kwa maana ya Shirika la Umeme la Zanzibar kwenye kuuziana umeme. Tumekuwa na bei ambazo zinatofautiana; na tumekuwa tuna majadiliano kwa muda mrefu katika eneo hili na jambo hili likapelekwa mpaka kwenye kamati zetu zinazoshughulikia maswali ya na Muungano.

Mheshimiwa Spika, issue kubwa ilikiwa ni habari ya bei. TANESCO walikuwa wanaona wakiuza umeme kwa shilingi 130/= ambayo wenzetu wa ZECO wanaihitaji hawataweza kwa sababu itakuwa ni hasara. ZECO wanasema sisi tukiwauzia kwa shilingi 156/= ambayo tunaona ni gharama za chini za kuzalisha, hatutaweza kufanikiwa kwa sababu ZECO wanasema hiyo kwao ni gharama kubwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kumekuwa na mazungumzo yanayoendelea na suala hilo limepelekwa katika Kamati ile inayoshughulikia masuala ya Muungano na tunasubiria maelekezo ya Serikali ili kuona namna gani tunaweza kusaidia mashirika haya mawili yaweze kuendelea kushirikiana na kukamilisha upelekaji wa umeme kwa gharama nafuu kwa wenzetu wa Zanzibar. (Makofi)
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, hii habari ya vituo hayo yote tisa lakini kumi kuna Kituo Chukwani kimejengwa kwa nguvu za wananchi na kisha pauliwa tayari. Sasa ni ipi commitment ya Serikali ili kuja kumaliza kituo kile ambacho kinahitaji milioni 30 tu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ali Hassan King, Mbunge na Mtumishi wa wananchi wa Jimbo la Jang’ombe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kiukweli ni kwamba kituo hiki tunakifahamu na binafsi nimeshakwenda kufanya ziara kwenye kituo hiki na hiyo amount ya fedha iliyotajwa tunaifahamu, kikubwa tulimwambia Mheshimiwa Mbunge ambaye alitupeleka katika eneo lile, ilikuwa ni Mheshimiwa Shaha. Mheshimiwa Ahmada Shaha tulikwenda kuona, kikubwa tulichomwambia kwamba sasa tunakwenda kutafuta fedha kwa sababu kama unavyojua siyo jambo la kusema kwamba tunachukua tu kesho tunakwenda kujenga. Ni jambo ambalo linahitaji taratibu za upatikanaji wa fedha kwa hiyo kikubwa nimwambie tu kwamba kituo hicho tunakifahamu na sasa tunakwenda kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwanza nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri maana yamekuwa safi tofauti na penalty ya Simba ya jana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua kwamba hawa watoto wenye walemavu mara nyingi huwa wanarandishwa randishwa mitaani na unaweza ukaja ukamkuta mtoto anarandishwa mtaani na watoto wenziwe maana yake mpaka hawa wengine wanakosa zile haki za watoto.

Sasa ndiyo maana nikauliza ni lini kwa sababu tunaona bado wako mtaani wanarandishwa ni lini hasa hatua stahiki za ukweli ukweli zitachukuliwa ili kupunguza lini wimbi? Hilo la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali la pili wazee wengi huwa wanashindwa hizo huduma tunazoambiwa wanapewa wanashindwa kuwapelekwa watoto hawa kwenda kupata huduma, wengine wanahitaji kwenda kupelekwa kwenye mashine kufanyishwa mazoezi, lakini wengine wanahitaji mambo tofauti tofauti, lakini ingawa limejibiwa hapa lakini tunaona kwamba ni bado hicho kitu kinaendelea.

Kwa hiyo niiulize Serikali ni lini hili jambo la watoto kupatiwa hizi huduma ambazo wanahitaji wakati mwingine zinatolewa kwa pesa watapata bure ili wale wazee nao waweze kupata faraja? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ali King, la kwanza akiuliza kwamba hawa watoto wamekuwa wakirandishwa randishwa mitaani kwa maana ya kuzururishwa.

Ni lini hatua stahiki zitachukuliwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari Serikali wamekwisha kuanza kuchukua hatua hasa pale matendo kama hayo yanapofanyika mitaani na kwa kuzingatia mwongozo huo ambao umetolewa ambao ni Mwongozo wa Taifa Utambuzi wa Mapema Afua Stahiki za Watoto wa Watu Wenye Ulemavu. Lakini pia kwa mujibu wa sheria tulizonazo na moja ya sheria ni hizo za utekelezaji wa sheria za watoto ambapo watoto wana haki na stahili zao zimeainishwa kwa mujibu wa sheria.

Kwa hiyo, pale inapobainika kwamba kuna changamoto kama hizo kwenye mitaa yetu hatua zimekuwa zikichukuliwa kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani kwa sababu zimeainishwa kwa mujibu wa sheria ya mwaka 2019. Kwa hiyo, hatua tayari tumekwisha kuanza kuchukua.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri inatosha ameshakuelewa.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kuhusu huduma; tayari Serikali imekwisha kutambua watoto zaidi ya 76,247 na ilibaini watoto wenye changamoto hizo ni 42,373 na hivyo tayari umekwisha kuingia kwenye mpango kupitia rejista ambayo iko ya utambuzi chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Makundi Maalum, lakini sambamba na hilo pia Ofisi ya Rais, TAMISEMI inaendelea na shughuli hiyo ya usimamizi na uratibu wa masuala ya ulinzi na usalama wa Watoto, ahsante.