Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Dr. Hussein Ali Mwinyi (3 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi kuchangia hoja iliyo mbele yetu jioni ya leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utajikita katika kujibu hoja zilizotolewa na Msemaji wa Kambi ya Upinzani juu ya role iliyochukuliwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kipindi cha uchaguzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Msemaji wa Kambi ya Upinzani alianza kwa kusema kwamba Zanzibar imetekwa na Jeshi la Tanganyika tangu kipindi cha uchaguzi wa kwanza hadi wa pili na majeshi yako Zanzibar in full combat kana kwamba nchi iko katika vita. Naomba nimueleze Mheshimiwa Msemaji wa Kambi ya Upinzani kwamba hakuna Jeshi la Tanganyika. Nitawaomba Waheshimiwa Wabunge kwa kufuata Katiba ya nchi, jeshi ni moja na ni Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa maana ya kujibu swali la kuwa kwenye combat, naomba nimuelimishe Mheshimiwa kama ifuatavyo. Kazi kubwa tatu za Jeshi ni ulinzi wa mipaka, ulinzi wa amani na kutoa msaada kwa mamlaka za kiraia au vyombo vingine vya ulinzi na usalama wanapohitajika kufanya hivyo. Hili suala ni la Kimataifa wakati wa uchaguzi majeshi yote yanakuwa standby. Ndiyo maana jeshi linakuwa kwenye combat kwa sababu ni kipindi cha standby, cha tahadhari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawaishii kuwa standby tu hata major installations katika nchi zinalindwa na jeshi wakati wa uchaguzi. Bandari, viwanja vya ndege, redio na televisheni na sehemu ambazo ni za uzalishaji mkubwa wa umeme na kadhalika, wakati huo vinalindwa na jeshi kwa sababu ya kuweka tahadhari. Kwa hiyo, hiyo ndiyo sababu kwa nini walikuwa kwenye combat na hii ni ya Kimataifa unaweza uka-check nchi yoyote wakati wa uchaguzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili alilolizungumzia Mheshimiwa alisema Jeshi la Tanganyika linatumika kuulazimsha Muungano. Kama nilivyosema awali kwanza hakuna Jeshi la Tanganyika. (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Hata hivyo, niseme kwamba Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania ni kielelezo cha Muungano wenyewe. Toka tulipoungana mwaka 1964, jeshi limekuwa ni moja, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania pande zote mbili. Kwa hiyo, hakuna suala la kulazimisha utawala, ni suala la kwamba jeshi liko Zanzibar kwa madhumuni ya kulinda mipaka ya nchi yetu kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa alisema katika uchaguzi wa marudio, Serikali ya Muungano ilipeleka majeshi na silaha Zanzibar ili kuhakikisha kuwa malengo yao ya kuendelea kuitawala Zanzibar kimabavu yanaendelea.
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Niwaeleze Waheshimiwa kwamba Jeshi toka mwaka1964 lina vikosi vyake Zanzibar. Vikosi hivyo kwa taarifa yenu si kwamba havina silaha siku zote silaha zipo. Tuna haja gani ya kupeleka wanajeshi, tuna haja gani ya kupeleka silaha wakati wa uchaguzi wakati miaka yote viko kule. Tunachosema jeshi liko kule kwa madhumuni ya kulinda mipaka yetu na kuleta amani si vinginevyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, anasema JWTZ limepata heshima kubwa katika medani za Kimataifa kwa nidhamu na uhodari wake wa kulinda amani katika nchi nyingine lakini Serikali ya Jamhuri ya Muungano imekuwa ikilitumia jeshi hili vibaya kwa kulipeleka Zanzibar kwenda kusaidia kufanya ghilba…
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Ya uchaguzi na hivyo kujikuta kwamba linashiriki katika uvunjifu wa amani badala ya kuleta amani. Mimi ninachosema ni kwamba, kwanza namushukuru kwa kuelewa kwamba jeshi letu lina sifa ya Kimataifa ya ulinzi wa amani. Nchi zote duniani zinalisifia jeshi letu kwa sababu ya weledi na nidhamu. Narudia kusema liko pale Zanzibar kwa madhumuni ya kulinda amani, kulinda mipaka yetu na sovereignty ya nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa aliendelea kusema kwamba Jeshi la Wananchi wakati wa uchaguzi lilikuwa likifanya uandikishaji wa wapiga kura katika makambi yao nje na utaratibu wa uandikishaji wa wapiga kura. Mimi nasema Mheshimiwa tumwogope Mungu.
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, haijawahi kutokea na wala haitatokea watu kuandikishwa katika makambi ya jeshi.
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Si kweli na kama unao ushahidi nitapenda niuone na hilo naweza nikakuhakikishia, jambo hili halipo kabisa. (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, aliendelea kusema kwamba Serikali ilieleze Bunge ni kwa nini inatumia vibaya Jeshi la Wananchi wa Tanzania katika masuala ya kisiasa.
Mimi ndiyo nasema sasa kwamba nyie ndiyo mnaliingiza jeshi katika masuala ya siasa. Jeshi halijawahi kutumika kisiasa hata siku moja na mara zote nasema ni vyema Waheshimiwa Wabunge tukazungumza siasa zetu bila kuliingiza jeshi. Kwa sababu Jeshi la Wananchi wa Tanzania linafanya kazi nzuri ya kulinda amani na nakuambieni kukosa kuwa na Jeshi la Tanzania katika uchaguzi huu pale Zanzibar pasingekalika.
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Si kweli na kama unao ushahidi nitapenda niuone na hilo naweza nikakuhakikishia, jambo hili halipo kabisa. (Makofi)
(Hapa baadhi ya Wabunge walikuwa wakiongea bila mpangilio)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, aliendelea kusema kwamba Serikali ilieleze Bunge ni kwa nini inatumia vibaya Jeshi la Wananchi wa Tanzania katika masuala ya kisiasa.
Mimi ndiyo nasema sasa kwamba nyie ndiyo mnaliingiza jeshi katika masuala ya siasa. Jeshi halijawahi kutumika kisiasa hata siku moja na mara zote nasema ni vyema Waheshimiwa Wabunge tukazungumza siasa zetu bila kuliingiza jeshi. Kwa sababu Jeshi la Wananchi wa Tanzania linafanya kazi nzuri ya kulinda amani na nakuambieni kukosa kuwa na Jeshi la Tanzania katika uchaguzi huu pale Zanzibar pasingekalika.
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja.
Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuhitimisha hoja yangu jioni ya leo. Niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia katika hoja hii, wale waliochangia kwa kuzungumza ambao idadi yao ilikuwa ni 24 na wale waliochangia kwa maandishi ambao idadi yao ilikuwa ni 31. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Halima Mdee alinitahadharisha kwamba nisije nikasema muda wa kueleza umekwisha. Ukweli ni kwamba kwa idadi hii si rahisi kumgusa kila mmoja wenu. Nataka niwahakikishie kama kawaida yetu, baada ya kukamilisha kazi hii tutaleta majibu yote kwa maandishi kwa kila mchangiaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nianze kwa kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote. Leo asubuhi wakati tumeanza shughuli za bajeti hii ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa nilipata moyo sana kuona kwamba Wabunge wote wa pande zote mbili wakiwa wanaliunga mkono jeshi letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakubali kabisa kwamba, baada ya uchaguzi siasa huwa zinahamia Bungeni. Pia ni sahihi kabisa kila mmoja kupiga siasa humu ndani ya Bunge lakini naendelea kuwasihi Waheshimiwa Wabunge tujitahidi sana kutoliingiza jeshi katika siasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo kwa bahati mbaya sana, nadhani ni kwa sababu ya kuzidiwa tu na hisia zetu za kisiasa zimetoka kauli humu ambazo kwa kweli zisingepaswa kutoka lakini bado tunayo nafasi ya kujirekebisha. Naamini Waheshimiwa Wabunge wa Kambi ya Upinzani na wa Chama Tawala sote tunatambua mchango mkubwa wa jeshi katika nchi yetu na sote tunaliunga mkono na ndiyo maana asubuhi mlimshangilia sana Mkuu wa Majeshi kwa kutambua mchango wa jeshi katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kueleza maelezo hayo ya utangulizi, sasa naomba niingie katika hoja za Waheshimiwa Wabunge. Nitaanza na hoja za Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama. Kwanza walisema kwamba Serikali itoe fedha za maendeleo zitakazotengwa katika mwaka huu wa fedha kwa ukamilifu na kwa wakati na pia Serikali ilipe madeni yote yaliyohakikiwa na Hazina. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sote ambao ni Wabunge tunafahamu kwamba tunapanga bajeti lakini mwisho wa siku inategemea sana na makusanyo ya Serikali. Ni mategemeo ya kila mmoja wetu kwamba Serikali ikikusanya vyema kama ambavyo mwelekeo unaonesha, bila shaka fedha hizi zitapatikana na tutaweza kutekeleza yale ambayo tumeyapanga katika mwaka huu wa fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia imetakiwa tushiriki kubuni mbinu za kuzalisha mazao ya kiraia ili kuongeza mapato. Napenda kutoa taarifa kwamba mashirika yetu yote, Suma JKT, Mzinga na Nyumbu, yanafanya juhudi mbalimbali ya kuzalisha mali ili waweze kupata kipato cha ziada. Kwa mfano, shirika la Mzinga wanazalisha risasi za kiraia pamoja na milipuko kwa ajili ya migodi. Nyumbu wanazalisha power tillers na mashine za matofali. Suma JKT wanasindika mazao ya nafaka na uunganishaji wa matrekta. Aidha, mashirika haya yanaendeleza ubunifu mbalimbali ili kuweza kuongeza kipato chao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi ya wanajeshi zilengwe kwa askari wa vyeo vya chini. Hapa tunasema katika mradi huu unaoendelea sasa ambapo nyumba 6,064 idadi yote imeelekezwa kwa askari wa vyeo vya chini. Hivyo ushauri huu unaenda sambamba na mpango wetu. Ni awamu ya pili ambayo tunalenga kuwapatia nyumba maafisa na wale askari wa vyeo vya juu.
Mheshimiwa Naibu Spika, jeshi kumiliki maeneo ya ardhi kisheria. Suala hili tunalitambua ilikuwa ni kasoro kubwa. Siku za nyuma taasisi za Serikali zilikuwa zinapewa government allocation peke yake lakini kila siku zikienda na uhaba wa ardhi imekuwa kuna uvamizi katika maeneo haya na ndiyo maana sasa tumeona umuhimu wa kupima maeneo yote ya jeshi na kuyapatia hati ili waweze kumiliki kisheria. Wakati tunafanya hayo, tutaendelea kuhakikisha kwamba maeneo ya jeshi yanatunzwa hivyo kuweza kupunguza uvamizi unaotokea katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, upimaji na ulipaji fidia kwa maeneo ya jeshi ufanyike. Kama ilivyoelezwa kwenye hotuba yangu, ibara ya 60 na 61 katika ukurasa wa 43 na 44 na kufafanuliwa katika hoja Namba tatu ya ukurasa wa 57, Wizara itaendelea kushirikiana na mamlaka husika ili kukamilisha upimaji na ulipaji fidia kwa maeneo ya jeshi. Natambua Waheshimiwa Wabunge wengi wamechangia katika maeneo haya ya kutaka uthamini, upimaji na ulipaji wa fidia. Katika bajeti ya mwaka huu kama mtakavyoona katika fedha za maendeleo, tumeweka shilingi bilioni 27.7 lengo ni kuanza kupunguza yale maeneo ambayo yanahitaji kulipiwa fidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, jeshi kutambua na kulinda mipaka yake. Jambo hili sasa linafanyika kwa nguvu zote, tunaweka mabango na tunapanda miti katika maeneo yetu ya mipaka ili wananchi waelewe fika wapi maeneo ya jeshi yanaanzia na wapi yanaishia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kurasimisha makabidhiano ya maeneo yanayotolewa na mamlaka za kiraia kwa jeshi na kuweka uzio maeneo yote ya jeshi. Ushauri umezingatiwa, tutashirikiana na mamlaka za mikoa kuhakikisha kumbukumbu za makabidhiano ya ardhi waliyoitoa kwa jeshi zinawekwa vizuri. Uwezekano wa kuweka uzio maeneo yote ya jeshi ni mdogo kwani maeneo hayo ni makubwa sana mfano eneo la Monduli, Tondoroni na Msata. Tunachoweza kufanya ni kuweka ukanda wa tahadhari yaani buffer zone na mabango ya tahadhari ya maeneo yote ya jeshi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la uboreshaji wa pensheni za wanajeshi wastaafu hasa kwa ngazi ya kuanzia Private hadi Brigedia Jenerali kwamba limefikia wapi. Serikali imetambua umuhimu wa kuboresha pensheni kwa wastaafu ikiwemo wanajeshi. Hivyo suala hili linaendelea kufanyiwa kazi kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Wizara ya Fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kutenga bajeti ya kutosha kuwezesha JKT kuchukua vijana wote wanaomaliza kidato cha sita kwa ajili ya mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria. Ushauri huu umepokelewa na ndiyo azma yetu. Hata hivyo, kama tulivyojibu, Wizara itaendelea kuwasiliana na Hazina ili kutoa fedha za kutosha kuliwezesha JKT kuchukua vijana wote wanaomaliza kidato cha sita kujiunga na mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria kwa wakati mmoja kadiri hali ya fedha itakavyoruhusu.
Mheshimiwa Naibu Spika, fidia kwa vijana wa JKT wanaoumia wakiwa mafunzoni. Wizara imepokea ushauri wa Kamati na itaufanyia kazi sanjari na kuboresha Sheria ya Ulinzi wa Taifa na sheria iliyoanzisha JKT.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maeneo hayo ambayo yalitolewa na Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama, naomba sasa niingie kwenye hoja ya Kambi ya Upinzani. Kwanza kulikuwa na hoja ya upendeleo katika ajira za jeshi. Labda nielezee kidogo utaratibu unaotumika katika ajira ili tuondokane na wasiwasi kwamba kuna upendeleo. Kwanza niseme tu kwamba ajira jeshini kwa sasa wanachukuliwa vijana ambao wako katika makambi ya JKT peke yake, jeshi halichukui tena uraiani. Kwa maana hiyo ni kwamba wale vijana wanaokwenda JKT wakati wa ajira wanafanyiwa usaili vijana hao, kwa hivyo sioni upendeleo unatokea wapi. Sasa hawa wa JKT wanapatikanaje? Kila mwaka tunatoa nafasi kupitia mikoa hadi wilaya, ili wilaya zenyewe zichuje vijana katika maeneo yao na kuwapeleka JKT. Kwa hiyo, hii hoja ya kwamba kuna upendeleo, kwa kweli sioni upendeleo huo utatokea wapi wakati hatuchukui uraiani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ilikuwa Wizara inalishughulikiaje suala la migogoro ndani ya vyama vya wanajeshi wastaafu. Jibu ni kwamba Wizara kupitia Makao Makuu ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, imevishawishi vyama vyote vya wanajeshi wastaafu kuunda chama kimoja tu cha Kitaifa ambacho kitaendeshwa kwa mujibu wa sheria na taratibu za kijeshi. Hivi sasa kuna vyama kama alivyovitaja lakini viko chini ya kanuni za mashirika yasiyokuwa ya kiserikali (NGO‟s). Kwa hivyo, inatupa shida kama Serikali kufanya nao kazi na kuwasaidia kama inavyotakiwa lakini wakiwa chama kimoja ambao watafuata taratibu za kijeshi, bila shaka itakuwa rahisi kwetu kuwapa msaada utakaostahili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la uteuzi wa wanajeshi kwenye nafasi za kisiasa kama ilivyokwishasemwa na walionitangulia AG na wengine, ndugu zangu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inampa mamlaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kumchagua mtu yeyote kwa nafasi yoyote. Kwa hivyo, haijavunjwa Katiba hapa na kwa utaratibu wa sasa wanajeshi wote hawaruhusiwi kujihusisha na vyama vya siasa. Hata hivyo, Mheshimiwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu anayo mamlaka ya kumpangia kazi mwanajeshi yeyote kadiri anavyoona inafaa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili napenda nikuambieni kwamba yapo maeneo ya nchi yetu ambayo yako katika mipaka yana changamoto nyingi za kiulinzi na usalama ndiyo maana ikaonekana ni busara kupeleka Wanajeshi. Kuna Wilaya kule kuna wakimbizi ambapo hali ya ulinzi na usalama imeharibika kwa sababu ya silaha zinazoingizwa, kwa sababu ya watu wanaoingia kwa mawimbi makubwa ya wakimbizi na kadhalika. Wakipelekwa wanajeshi kule experience imeonesha kwamba kazi ya ulinzi na usalama inafanyika vyema zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Serikali iwaagize Wakuu wa Vikosi vyote vya JKT kutengeneza programu ya uzalishaji mali katika kilimo, uvuvi na mifugo. Kama ilivyoelezwa katika ibara ya 53 ya hotuba yangu, ushauri huu umepokelewa na taarifa za uzalishaji mali na mapato itaendelea kutolewa katika Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama. Ukweli ni kwamba programu za uzalishaji mali katika vikosi vyote vya JKT zipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itoe fedha zote zitakazotengwa katika bajeti ya Wizara ya Ulinzi. Hili ni kama nilivyosema awali, itategemea sana na mapato ya Serikali lakini ni mategemeo yetu kwamba kwa sasa kwa sababu ukusanyaji ni mzuri, hatuna shaka kwamba fedha zilizotengwa zitaweza kupatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niingie katika kile kisehemu ambacho kilikuwa kinazua mgogoro, nacho ni jeshi kuingilia kazi za polisi Zanzibar. Ndugu zangu nataka niseme, wakati nachangia hotuba ya Ofisi ya Makamu wa Rais nilitoa maelezo ya kina na nilidhani tumeelewana ni kwa nini jeshi wakati wa uchaguzi linakuwa standby. Narudia kusema kwamba wakati wa uchaguzi au nianze kwa kuelezea majukumu ya jeshi, majukumu ya jeshi makuu ni matatu. Kwanza ni ulinzi wa mipaka yetu; pili ni ulinzi wa amani; na tatu ni kutoa msaada kwa mamlaka za kiraia na vyombo vingine vya ulinzi na usalama wanapohitajika kufanya hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wakati wa uchaguzi Zanzibar, jeshi liliona ni muhimu kukamata major installations kwa ajili ya usalama. Maeneo ya airport, bandari, redio na maeneo mengine kama hayo vililindwa na jeshi kwa ajili ya kuhakikisha usalama wa ziada lakini hakukuwa na nia ya kumtisha yoyote, nia ilikuwa ni kuleta usalama. Kama walivyosema wengi hapa, naomba nirudie kauli ile kwamba, walinzi ni walinzi anayeogopa mlinzi ni mhalifu. Hakuna sababu kwa nini uwaogope walinzi kama huna nia mbaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunachosema ni kwamba, wanajeshi walikuwa on standby endapo itatokea vurugu na mamlaka ya vyombo vingine vya ulinzi na usalama watahitaji msaada wao wawe tayari kutoa msaada. Hata hivyo, ukweli unabaki pale pale kwamba wakati wa uchaguzi, ninyi ni mashahidi, mimi pia nilikuwa Zanzibar nimepiga kura, sehemu zote zilikuwa zinalindwa na polisi, jeshi walikuwa kwenye barracks zao isipokuwa hizo major installations nilizoelezea hapa, basi! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna hoja kwamba ni faida gani tunapata kwa JWTZ kushiriki katika operesheni za amani. Kwanza nishukuru kwa wote waliochangia na kusema kwamba kazi inayofanywa na jeshi kwenye ulinzi wa amani ni nzuri, tumepata sifa nyingi na tunawaunga mkono wanajeshi wetu waendelee kutuwakilisha vyema sehemu hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, faida tunazozipata kwanza tunapata uzoefu wa Kimataifa na mbinu mpya. Pili, wanajeshi binafsi wanafaidika kwani hupata kipato kwa kushiriki ulinzi wa amani. Tatu, ulinzi wa amani umeliletea sifa jeshi letu Kimataifa. Katika takwimu za ubora zilizotolewa hivi karibuni jeshi letu Kimataifa lipo katika nafasi ya 27 ndiyo sababu sisi tunapata nafasi nyingi za kwenda kulinda amani katika nchi mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee na hoja nyingine kama ifuatavyo:-
Ushauri wa kutumia vyombo katika shughuli za maendeleo na uzalishaji. Hili alilitoa Mheshimiwa Shamsi Nahodha nadhani nimeshalisema kwamba taasisi zetu zote zinafanya kazi hii ya kuzalisha mali na kufanya tafiti ili ziweze kupata kipato cha ziada.
Vijana wanaomaliza JKT wasiachwe bila ajira. Kama nilivyosema na alivyosema Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, tuna mambo mawili, si rahisi kuwaajiri vijana wote ambao wanaingia JKT, lakini ni lazima tujipongeze kwa sababu tumefanya kazi nzuri. Takwimu zinatuonesha kuanzia mwaka 2001 - 2015, kati ya vijana wote waliochukuliwa katika makambi ya JKT walioajiriwa ni asilimia 72.9, hawa wameingia katika vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama.
Mheshimiwa Naibu Spika,Waliobaki ambao ni wachache kama asilimia 30 sasa ndiyo tumekuja na mpango huu wa uwezeshaji, wanapewa mafunzo kule na wakitoka watapewa mitaji ili waweze kujiajiri wao wenyewe. Kusema kuwaajiri asilimia 100 haiwezekani, ingekuwa vyema na ningependa iwe hivyo lakini kwa bahati mbaya bado uwezo wetu haujafikia hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na ushauri wa kuwa na database ya vijana wa JKT. Database hiyo ipo kwa wale wanaoajiriwa na wale wanaorudi nyumbani kwa sababu nao ni jeshi la akiba.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ilikuwa ni kuimarisha vyuo vya ufundi stadi JKT ili vijana wapate stadi za kazi. Ushauri umepokelewa, Wizara inaendelea kuchukua hatua za kuimarisha vyuo vya ufundi stadi JKT kwa kuviwezesha kivifaa na wataalam kadiri bajeti inavyoruhusu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mgogoro wa ardhi Tondoroni, Makuburi na Ihumwa. Tondoroni mgogoro umekwisha kupitia Mahakama kesi namba 48 ya mwaka 2005 ambapo Serikali ilishinda. Hata hivyo, wahusika halali walikwishalipwa fidia kupitia Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mgogoro wa Makuburi Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni imeandaa mchoro wa mipango miji kwa kuzingatia marekebisho ya mpaka mpya wa kambi ambapo eneo la jeshi litazungukwa na viwanja vilivyopimwa. Tulichofanya pamoja na kwamba wananchi walivamia eneo la jeshi tumeweka mipaka mipya wao tukawatoa nje ya ile mipaka kuweza kuwa-accommodate ili wasilazimike kuondoka au kulipwa fidia. Kwa maana hiyo, tatizo hapa naliona limekaa vizuri lakini manispaa nayo imechukua jukumu la kuwapimia wananchi wale ili wawe na hati na isiwe tena ni eneo ambalo halijapimwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la Kambi ya Ihumwa halina mgogoro. Tatizo lililopo ni la eneo dogo la nyongeza ambapo taratibu za kulipima na kulifanyia uthamini bado hazijakamilika. Kama nilivyosema tukipata fedha tutakamilisha taratibu hizo ili tuweze kulimiliki kihalali.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Zungu alitaka pensheni za vyombo vya ulinzi na usalama ziwe na taratibu zake maalum badala ya taratibu hizi za kawaida za utumishi wa umma. Hili ni wazo zuri, tunalipokea na ushauri huu utazingatiwa na tutawasiliana na wenzetu wa Hazina na Ofisi ya Rais, Utumishi ili tuangalie ni jinsi gani tunaweza kufanya lakini sote tunakubaliana na ninyi kwamba kuna baadhi ya wenzetu ambao walistaafu zamani pensheni zao haziridhishi, ni ndogo sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu misheni zetu tunapokwenda nje ya nchi, walitaka kujua fedha za misheni, hili nadhani nimeshalijibu na nitoe tu ufafanuzi wa ziada kwamba ziko fedha ambazo zinapatikana ukiacha zile ambazo wanalipwa wanajeshi wenyewe, sisi tunawalipa asilimia 80 ya zile zinazolipwa kutoka kule UN lakini jeshi pia linapata fedha kwa ajili ya kuwa na zana zake kule na pili matengenezo na tatu kuweza kupeleka zana mpya. Kwa hiyo, malipo ya fidia ya UN yanatolewa na fedha hizo zinalipia posho kwa wanajeshi, kugharamia ukarabati wa zana, kununua vifaa na zana mpya, kuandaa vikosi vipya kwenda kubadili vile vinavyorejea na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna hoja ya kutaka kujua tofauti ya Chapter Six na Chapter Seven katika malipo. Malipo ya fidia ya UN hayatofautishi kama ni operation ya Chapter Six au ya Chapter Seven, yote yanafanana na ni sawa, ni chapters zinazotofautisha utendaji katika eneo la ulinzi na amani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu wanajeshi wetu waliopoteza maisha au kuumia kwenye operations hizo wote walishalipwa kikamilifu kwa mujibu wa taratibu za UN na za JWTZ. Kwa sasa hakuna familia yoyote inayolidai jeshi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine lililochangiwa lilikuwa ni suala la Duty Free Shops kama alivyochangia Mheshimiwa Maryam Msabaha kwamba bidhaa zinazouzwa kule hazina nafuu na zile zinazouzwa mitaani. Tumepata malalamiko haya na nataka nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo hili tunalifanyia kazi kwa nguvu kabisa. Lengo letu ni kwamba mashirika yetu ya jeshi ndiyo yaendeshe maduka haya ikiwemo Mzinga ambao wameshaanza katika baadhi ya vikosi, tunataka Suma JKT waingie ili hatimaye maduka yote ya jeshi yaendeshwe na jeshi lenyewe na kwa kufanya hivyo tutaondokana na tatizo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, huduma za mabwalo kweli tunalo tatizo na kazi ya ukarabati wa mabwalo linatekelezwa kwa kadiri bajeti zinapopatikana. Ni kweli kwamba mabwalo mengi kwa sasa hali yake sio nzuri kutokana na uhaba wa bajeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri kuhusu bajeti, madeni na maeneo ya jeshi, nadhani hili tumeshalitolea ufafanuzi. Tumesema kwamba bajeti ikiruhusu tutahakikisha tunaondoa matatizo yote haya yanayoonekana.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali moja lilikuja kuhusu wastaafu kulipwa kila mwezi. Tunachosema ni kwamba wala hatuna tatizo na wastaafu kulipwa kila mwezi kwa sababu hapo awali wastaafu walikuwa wanalipwa kila mwezi, ni wastaafu wao wenyewe waliomba kwamba sasa walipwe kwa miezi sita, walidai kwamba ile pensheni ya kila mwezi ni ndogo na wanakuwa wameshakopa, kwa hiyo, angalau wapewe ya miezi sita, wakapewa ya miezi sita. Baadaye wakabadilisha wakasema hiyo inakuwa muda mrefu sana, wakaletewa ya miezi mitatu. Kwa hiyo, kama sasa hivi wako tayari kurudi mwezi mmoja wala sioni tatizo lolote, haya ni matakwa ya wastaafu wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu uanzishwaji wa bima ya afya kwa wanajeshi hili tunalipokea na tunaona umuhimu wake. Bima ya afya kwa wanajeshi ni muhimu kwa sababu sasa hivi tunapata shida sana, bajeti ya kutoa huduma za afya jeshini haitoshelezi na kwa maana hiyo tunao mpango wa kuanzisha bima kwa ajili ya wanajeshi wote, wawe kazini au wastaafu ili hatimaye tuondoe matatizo yao ya kupata huduma zinazostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mambo yaliyochangiwa kama nilivyosema ni mengi, naomba sasa niingie kwenye hoja za Mheshimiwa Sophia Mwakagenda. Anasema Amiri Jeshi Mkuu kuvaa sare za jeshi yeye anaona hili sio sawasawa. Kwanza nieleze kwamba Uamiri Jeshi Mkuu siyo cheo bali ni wadhifa. Kwa mujibu wa taratibu za kijeshi, Amiri Jeshi Mkuu anapoamua kuvaa sare ya jeshi katika shughuli yoyote ile ya kijeshi kama vile kufika katika eneo la mazoezi ya kijeshi, anaruhusiwa kwa mujibu wa taratibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hili wala halijaanza hapa kwetu wala halijaanza katika awamu hii, Baba wa Taifa alivaa sare za jeshi, hapo nchini Kenya juzi juzi tu tumeona Rais Kenyatta kavaa sare za jeshi. Sioni kwa nini hii inakuwa hoja kubwa kwa sababu yeye ndiye Amiri Jeshi Mkuu. Anapoamua kuvaa afanane na wanajeshi wakati anaenda kwenye mazoezi yao wala hakuna tatizo hata kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu wanajeshi wastaafu kuvaa sare za jeshi, maelezo ni kwamba mwanajeshi mstaafu anaweza kuvaa sare za jeshi katika shughuli yoyote lakini awe amepata kibali cha Mkuu wa Majeshi. Mkuu wa Majeshi huwa anatoa vibali hivyo kwa shughuli maalum ikiwemo ile ya kuapishwa Wakuu wa Mikoa alitoa kibali wavae kwa sababu wala hakuna tatizo, wale ni wanajeshi kwa sasa baada ya kustaafu ni jeshi la akiba, watakapohitajika wakati wowote wanaitwa ili waweze kufanya kazi za jeshi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Kai alikuwa na hoja ya kukosekana kwa fedha za maendeleo kwa Ngome. Hili nimeshalizungumza toka awali, tunaelewa changamoto za bajeti na hii ni kwa Serikali nzima na wala siyo Wizara ya Ulinzi peke yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja pia kukosekana kwa fedha za kulipia fidia maeneo ya ardhi. Kama nilivyosema mwaka huu tumetenga shilingi bilioni 27.7, ni mategemeo yetu kwa kiwango kikubwa tutaweza kupunguza tatizo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, uchaguzi wa marudio Zanzibar. Jeshi kupelekwa Zanzibar Waziri atafute maneno mengine lakini siyo kwamba hawakupelekwa. Ndugu zangu naomba nirudie, nilisema hivi, watu wakisikia kwamba tunasema jeshi lilipelekwa Zanzibar wakati wa uchaguzi kila mtu atadhani jeshi halipo Zanzibar. Zanzibar kuna brigade siyo platoon wala siyo kombania kuna brigade. Brigade ya askari wa infantry iko Zanzibar na isitoshe kuna vitengo vya wanamaji, kuna vitengo vya airforce. Sasa tunapokuwa tunabishana kwamba jeshi lilipelekwa au halikupelekwa, naona haina msingi sana kwa sababu tayari jeshi lipo Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jeshi liko Zanzibar kwa dhumuni moja tu, nalo ni kulinda mipaka ya nchi yetu ya ujumla ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ndiyo kazi yake ya msingi kulinda mipaka yetu. Kwa hiyo, haiwezekani wasiwepo wakati mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iko mpaka kule Zanzibar. Kwa hiyo, nadhani kama walipelekwa au hawakupelekwa isiwe hoja, hoja ni kwamba jeshi liko pale kwa kazi moja ya kulinda mipaka yetu na wakati wa uchaguzi kama ilivyo international standard kwa nchi zote wanajeshi wanakuwa standby ili kukitokea machafuko waweze kusaidia, basi! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jeshi limetumika kuwatisha watu waliotulia. Mimi nasema jeshi limekuweko pale kusaidia watu watulie kwa sababu matukio yalikuwepo na wala hatuwezi kukataa. Mabomu yalirushwa wala sisemi mimi vyombo vya habari vimesema karibia na uchaguzi na wakati wa uchaguzi si kulikuwa na mabomu ya mkono yanarushwa, si yalitokea? Sasa kweli jeshi lisingekuwepo ile hali ya usalama na amani ingekuwepo mpaka leo? Sisi tunasema jeshi liko pale kwa kazi moja ya kulinda amani si kwa kazi ya kumtisha mtu yeyote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja kwamba wanajeshi wa ngazi ya chini wanalipwa ration allowance tofauti na wa ngazi ya juu, si kweli. Jeshini ration allowance ni moja tu, anayopata private na anayopata general ni hiyo hiyo. Kama umepata taarifa kwa mtu yeyote si kweli, hapa nakataa kabisa, ration allowance ni hiyo hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Fakharia anasema nafasi za ajira za Zanzibar, kwa nini vijana wasichukuliwe kutoka JKU badala ya kupitia mikoani na wilayani. Jibu ni rahisi, sisi huwa tunapeleka nafasi za Zanzibar kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Tunawaachia uhuru wa kuamua wanazigawa kwa taratibu gani. Wakiamua kupeleka mkoani na wilayani ni juu yao, wakiamua kupeleka JKU ni juu yao. Kwa hiyo, kama tunaona JKU ni utaratibu mzuri zaidi kwa pamoja sisi Wabunge wa Zanzibar tuishauri SMZ ichukue vijana hao kupitia JKU. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nyumba za makazi zijengwe na Unguja pia, hii iko katika mpango wetu wa Awamu wa II. Awamu ya I kwa Zanzibar ilianza Pemba na Awamu ya II tutapeleka Unguja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wanajeshi wastaafu kulazimika kwenda Bara kushughulikia mafao yao. Hili nalikubali kwamba ni usumbufu, hawa watu hawana fedha, wanatakiwa wasafiri mpaka makao makuu, tutatengeneza utaratibu ili brigade pale ishughulike na mafao haya kwa kuwasaidia kuchukua maelezo yao wao wayapeleke makao makuu ili waweze kupata huduma kwa urahisi bila kusafiri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu maswali ya Khadija Hassan Aboud ambapo yeye alishauri vijana wa JKT waajiriwe jeshini. Napenda kumtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba ndivyo tunavyofanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, aliendelea kushauri JKT iwe na aina mbili za mafunzo wale wa ujasiriamali na wale wa kuingia jeshini, tunadhani kwa sasa huo hautakuwa utaratibu mzuri sana kwa sababu uwezo wa kufanya hivyo hatuna. Hata hivyo, ikumbukwe kwamba lengo la JKT si kutoa ajira ni kuwafunza vijana wetu wa Kitanzania uzalendo, utaifa na kuhakikisha kwamba wakiwa pale basi wanapata mafunzo ya kijeshi lakini pia ujasiriamali kwa maana ya stadi za kazi ili waweze kujiajiri. Kwa hiyo, hili tutalitazama kwa wakati ujao.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba niingie katika hoja za Mheshimiwa Kubenea ambazo kwa kweli zimenisikitisha sana kwa sababu hazina punje ya ukweli ndani yake. Nasikitika kusema kwamba Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano anaweza akachukua maneno ya mitaani akaingia nayo ndani ya Bunge akayasema bila ya kuwa na ushahidi, hii ni hatari tena ni hatari kubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimwarifu Mheshimiwa Kubenea, sijui kama yupo humu ndani…
(Hapa baadhi ya Waheshimiwa Wabunge walikuwa wakiongea bila mpangilio)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, tuhuma anayoitoa kwamba jeshi limeingia mkataba na kampuni inayoitwa Hainan Construction ambapo jeshi litatoa eneo kubwa la ardhi kwa kampuni hiyo ili ijenge nyumba na kwamba kampuni hiyo itatumia kwa miaka 40 hazina punje ya ukweli ndani yake. Si kweli na naku-challenge ukiweza kuniletea uthibitisho huo mimi nitajiuzulu kwa sababu maneno unayoyasema ni ya mitaani. Nasikitika sana Mheshimiwa Mbunge kuleta maneno yasiyokuwa na uthibitisho kwa sababu maneno hayo ni ya uwongo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili alilolisema ambalo limenihuzunisha zaidi, anasema kampuni hiyo hiyo itaingia mkataba pia wa kumjengea nyumba Dkt. Hussein Mwinyi, huu siyo mgongano wa kimaslahi? Naliomba Bunge lako litumie utaratibu wa kikanuni, Mheshimiwa Kubenea akishindwa kuthibitisha maneno haya achukuliwe hatua stahiki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni kwa sababu tusije ndani ya Bunge tukaharibu majina ya watu, tukawadhalilisha kwa sababu tu ya kuwa na uhuru wa kuzungumza ndani ya Bunge na immunity tunayopewa. Nasema uhuru tunao, immunity tunayo lakini kudhalilisha watu kwa maneno ambayo hayana ushahidi kukomeshwe. Huu ni uwongo mtupu, hakuna jambo kama hili. Kwanza hiyo kampuni hata kuwajua siwajui. Pili, haiwezekani maneno haya akayaleta kama hakuna mkataba wa ushahidi kama anao alete tuuone, hakuna hiki kitu, ni uwongo mtupu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Kubenea aliendelea kusema kuwa kuna tuhuma za udhalilishaji kwa wanajeshi wetu waliokwenda kulinda amani Kongo, je, ni hatua zipi zimeshachukuliwa hadi hivi sasa? Nataka nimweleze Mheshimiwa Kubenea kwamba, tuhuma zinapotolewa ni wajibu wa mamlaka zinazohusika kuchunguza, huwezi kuvamia tuhuma ukachukua uamuzi. Jeshi liliunda Bodi ya Uchunguzi, wamekwenda Kongo kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa ufanyike uchunguzi wa kina ili watakapokuja kutoa taarifa za uchunguzi na ikithibitika kwamba kuna unyanyasaji wa kijinsia ulifanyika au walifanya askari wetu hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi ya waliofanya vitendo hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jeshi hili linaendeshwa kwa mujibu wa sheria na kanuni za jeshi, kwa hivyo, hakuna mtu anayeruhusiwa kufanya jambo lolote kinyume na utaratibu akaachiwa lakini tunachosema uchunguzi ni lazima ufanyike. Udhalilishaji uliosemwa na Umoja wa Mataifa ni pamoja na ubakaji, baadhi ya watu wamedai katika ubakaji huo wamepata watoto, unafanyaje uamuzi wa kwamba huyu amekosa bila kufanya DNA test ya kugundua kama hao watoto kweli ni wa huyo anayeambiwa ni baba yao? Kwa hiyo ni kwamba uchunguzi unaendelea na ni mategemeo yetu kwamba utakapokamilia na ukithibitika hatua stahiki zitachukuliwa. Hii ni kawaida kabisa wala Mheshimiwa asipate tatizo lolote hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hoja nyingine nyingi ambazo zimetolewa, lakini nadhani kwa ujumla wake nimezi-summarize kwa pamoja ili tuweze kupata maelezo ya ujumla lakini nitakuwa tayari kutoa maelezo ya ziada nitakapohitajika. Kama nilivyosema awali wakati wa vifungu pia nitakuwa tayari kutoa maelezo kwa kadiri yatakavyohitajika.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nami naomba nianze kuchangia hoja hii kwa kuishukuru Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kwa ushirikiano mkubwa wanaonipa mimi pamoja na watendaji wangu. Nataka niwahakikishie kwamba tutaendelea kushirikiana nao. Aidha, nawapongeza kwa kazi nzuri wanayoifanya. Tumekuwa tukifanya kazi pamoja nao tukitembelea maeneo mbalimbali na tunawashukuru sana kwa usimamizi wao na ushauri wao kwa Wizara yangu. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hoja kadhaa ambazo zimetolewa na napenda nianze na zile za Kamati kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la beacons kutokuwepo katika mipaka yetu. Ni kweli hili ni tatizo la muda mrefu lakini napenda niseme kwamba hatua zimeanza kuchukuliwa. Tumechukua hatua za aina mbili. Kwanza ni mazungumzo kati ya Wizara zinazohusika kwa upande wetu wa Tanzania pamoja na ule upande wa majirani zetu. Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi hii imekamilika kwa mpaka wa Tanzania na Kenya na beacons zimeanza kurudishiwa na mazungumzo yapo katika hatua nzuri kwa upande wa Tanzania na Uganda. Ni mategemeo yetu kwamba baada ya kukamilika kwa mazungumzo hayo, basi tutarusha zile beacons na kuweka buffer zone ili wananchi wasiingilie ile mipaka kisheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati pia imeeleza juu ya suala la marekebisho ya Sheria ya JKT ili iweze kutoa fidia kwa vijana wanaoumia wakiwa kwenye mafunzo. Hili tunalikubali, ni ushauri mzuri sana na ni kweli kwamba wapo vijana wanaopata matatizo ya kiafya na wengine wanaoumia kupitia yale mazoezi yanayofanyika kule. Kwa hiyo, ni jambo ambalo na sisi tunalipokea na tutafanya utaratibu wa kufanya marekebisho ili waweze kupata fidia iwapo watakuwa wameumia wakiwa katika mafunzo. Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja ya idadi ya vijana wa JKT waliochukuliwa mwaka huu. Napenda nitoe taarifa kwamba vijana waliochukuliwa kwenda JKT ni wa aina mbili; wale wa mujibu wa sheria ambao mwaka huu idadi yao ni 14,748 na wale wanaojitolea wamechukuliwa 9,848. Kwa hivyo, hao ndiyo ambao wamepata nafasi safari hii. Tunatambua kwamba idadi hii ni ndogo na inabidi tuwachukue wengi zaidi hususani wale wa mujibu wa sheria na tutaendelea kujenga miundombinu katika makambi yetu ili tuweze kuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kuweza kuwachukua walio wengi zaidi. Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hoja hizo za Kamati sasa niingie kwenye hoja za Waheshimiwa Wabunge mmoja mmoja na nianze na ile ya Mheshimiwa Rweikiza ambaye ametaka kujua ni kwa nini hatujasaini na ku-ratify ule Mkataba wa Biological Weapon Convention. Nataka nimpe taarifa Mheshimiwa Rweikiza kwamba kuna mikataba ya aina hii miwili; wa kwanza ni ule Chemical Weapons Convention na wa pili ni Biological Weapons Convention. Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, Chemical Weapons Convention tulishasaini na tumeshauridhia, kwa hiyo, pale tumemaliza. Kwa upande wa Biological Weapons Convention kusaini tulishasaini kilichobaki ni kuridhia na ku-domesticate kwa maana ya kwamba kuingiza katika sheria za nchi ili uweze kutumika katika sheria za nchi. Kazi hiyo inaendelea na iko katika hatua ya Cabinet Secretariat ili hatimaye iweze kufika Bungeni. Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mattar alitoa mapendekezo kwamba asilimia ya vijana wanaochukuliwa kuingia JKT kutoka Zanzibar basi angalau ipatikane asilimia kumi ya wale wa jumla wanaochukuliwa. Tunaweza kusema kwamba kwa sasa hivi au kwa mwaka huu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilipewa nafasi 300 na tunaona umuhimu wa kuongeza nafasi hizo. Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimuahidi kwamba mwaka hadi mwaka tutaendelea kuwa tunaongeza idadi hii japo siyo kwa kufikia asilimia kumi ili tuweze kupata vijana wengi zaidi kutoka upande wa pili wa Jamhuri yetu, lakini wakati huo huo lazima tujenge miundombinu zaidi ili tuweze kupata idadi kubwa zaidi ya vijana wanaoingia katika Jeshi la Kujenga Taifa. Mheshimiwa Mwenyekiti, naye vilevile alishauri kwamba badala ya utaratibu unaotumika sasa ule wa kupitia Wilayani na Mikoani alishauri kwamba pengine vijana wachukuliwe kutoka JKU. Ambacho naweza kumwambia Mheshimiwa Mbunge kuhusu hili ni kwamba uamuzi wa jambo hili upo juu ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi yetu sisi au mimi kama Waziri wa Ulinzi huwa napeleka nafasi zile kwa Makamu wa Pili wa Rais na tunawaachia jukumu la kuamua wao wanataka kutumia utaratibu gani. Mpaka sasa wamekuwa wakizigawa Wilayani na Mikoani. Kwa hivyo, naweza kumshauri Mheshimiwa Mbunge kwamba ni vyema akazungumza na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuangalia utaratibu kama huo wa JKU utakuwa ni bora zaidi. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hoja ya Mheshimiwa Zitto Kabwe ya kuhusu Kanali Kashmir kwamba hajastaafishwa rasmi. Kwanza nataka nimpe taarifa ya kwamba Kanali Kashmir ni kweli alikuwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania na cheo chake kilikuwa ni Chief of Logistics and Engineering (CLE) na sio Chief of Staff. Chief of Staff wakati wake yeye cheo hicho hakikuwepo ni baada ya yeye kutoka mwaka 1974 ndipo kilipoanzishwa cheo cha Chief of Staff. Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachosema ni kwamba kuhusu maslahi ya kustaafu ni suala la kisheria. Kama ni kweli kuna uthibitisho kwamba Kanali Kashmir hajalipwa jambo hili litaangaliwa kisheria aweze kupata mafao yake. Hata hivyo, taarifa nilizokuwa nazo ni kwamba wakati anatoka Jeshini kwenda SUDECO fedha za Jeshi alikuwa ameshapata na baada ya kustaafu kule SUDECO alitakiwa alipwe upande ule ule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo mengine nitayaleta kwa maandishi. Naunga mkono hoja na ahsante sana.