Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Dr. Hussein Ali Mwinyi (41 total)

MHE. MATTAR ALI SALUM aliuliza:-

Kikosi cha Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) huandaa vijana kwa mafunzo mbalimbali kwa ajili ya kusubiri ajira katika vikosi vya ulinzi vya Muungano:-

(a) Je, Serikali ina mpango gani madhubuti wa kutoa ajira kwa upande wa Tanzania Zanzibar?
(b) Je, ni asilimia ngapi ya vijana wanaoajiriwa kutoka upande wa Zanzibar?

(c) Je, kwa nini utoaji wa ajira katika Wizara hii kwa upande wa Zanzibar usijielekeze katika kwenye kikosi cha Jeshi la Kujenga Uchumu (JKU)?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mattar Ali Salim Mbunge wa Shaurimoyo lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania lina utaratibu wa kuandikisha Askari wapya kupitia Makambi ya Jeshi la Kujenga Taifa. Jeshi la Kujenga Taifa hutoa nafasi katika Mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani. Kwa upande wa Tanzania Zanzibar nafasi hizo hutolewa kupitia Wizara inayoshughulikia Vikosi Maalum vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Vijana hao husailiwa kwa utaratibu uliowekwa na wanaofaulu hupelekwa katika Makambi ya Jeshi la Kujenga Taifa kufanya mafunzo sawia na vijana wa kutoka Bara.

(b) Mheshimiwa Spika, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania halina utaratibu wa kuandikisha vijana kwa kufuata asilimia, bali ni vijana wanaokuwa na sifa zinazohitajika kuandikishwa bila kujali wanatoka upande gani wa Muungano.

(c) Mheshimiwa Spika, uandikishaji askari katika Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania haujielekezi moja kwa moja kupitia Jeshi la Kujenga Uchumi kwa sababu Kambi za JKU hazina utaratibu wa kuwaweka vijana wao makambini kama inavyofanyika katika Kambi za Jeshi la Kujenga Taifa. Vijana hao huripoti asubuhi na kurejea majumbani kwao ifikapo jioni, hivyo kusababisha kwa kutokuwepo kwa muendelezo mzuri wa mafunzo na malezi ya vijana wakiwa kambini. Kwa mantiki hiyo vijana hao hawapati mafunzo yaliyokamilika ikilinganishwa na vijana wenzao wanaopata mafunzo katika Kambi za Jeshi la Kujenga Taifa.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA aliuliza:-
Kazi ya Vikosi vya Ulinzi na Usalama ni kulinda raia na mali zao pamoja na kulinda mipaka ya nchi; lakini baadhi yao wamekuwa wakienda kinyume na sheria kama vile kuwapiga na kuwasababishia wananchi ulemavu au vifo:-
a) Je, mpaka sasa ni Askari wangapi wameshachukuliwa hatua?
(b) Je, ni Askari wangapi mpaka sasa wamekutwa na hatia na kufukuzwa kazi?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maryam Salum Msabaha, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Vikosi vya Ulinzi na Usalama kazi yake ni kulinda raia pamoja na mipaka ya nchi kwa mujibu wa Sera ya Ulinzi wa Taifa. Vile vile ni kweli wapo baadhi ya Askari ambao wamekuwa wakienda kinyume cha sheria za nchi kama vile kuwapiga raia. Hata hivyo, jeshi limekuwa likichukua hatua stahiki kwa Askari ambao wamekuwa wakienda kinyume na sheria, mila na desturi za nchi na za kijeshi katika kipindi chote tangu jeshi letu lianzishwe mwaka 1964. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa swali la Mheshimiwa Mbunge halikulenga kipindi maalum, itakuwa ni vigumu kubainisha idadi ya Askari hao tangu jeshi lianzishwe. Kimsingi, jeshi limekuwa likichukua hatua stahiki za kijeshi dhidi ya wakosaji kwa mujibu wa taratibu zake na wengine kupelekwa katika Mahakama za kiraia kulingana na aina ya kosa alilolitenda mhusika. Waliopatikana na hatia walipewa adhabu stahiki kulingana na uzito wa makosa waliyotenda, ikiwa ni pamoja na vifungo vilivyoambatana na kufukuzwa utumishi jeshini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ikumbukwe kwamba Jeshi la Wananchi wa Tanzania wakati wote linasisitza nidhamu kwa Wanajeshi wake. Pale ambapo kunajitokeza utovu wa nidhamu, hatua madhubuti huchukuliwa mara moja.
MHE. MWANTAKAJE HAJI JUMA aliuliza:-
Jeshi la Wananchi la Tanzania (JWTZ) limekuwa tegemeo kwa nchi hususan katika masuala ya kiulinzi nchini:-
Je, ni lini Serikali itawapatia nyumba bora za makazi askari wa Jeshi hilo, hasa ikizingatiwa nyumba zilizopo hazitoshi?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwantakaje Haji Juma, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina nia ya kuliboresha Jeshi kwa vifaa, zana na miundombinu ikiwa ni pamoja na nyumba za makazi ya wanajeshi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafurahi kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba Serikali imechukua hatua ya kupunguza mahitaji makubwa ya nyumba kwa wanajeshi kwa kuanzisha mradi wa ujenzi wa nyumba 10,000.
Awamu ya kwanza ambayo utekelezaji wake umeshaanza, zinajengwa nyumba 6,064 katika kambi mbalimbali nchini. Katika awamu ya pili tunatarajia kujenga nyumba 3,034 kwa ajili ya askari wa ngazi ya kati na Maafisa. Pamoja na mradi huu, Serikali itaendelea kutenga bajeti kila mwaka kwa ajili ya ukarabati wa nyumba zilizopo ili kupunguza uhaba wa makazi kwa wanajeshi.
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza:-
Serikali ina mamlaka ya kutwaa ardhi na kubadilisha matumizi na kwa kufanya hivyo, Serikali inawajibika kusimamia na kuhakikisha wananchi wanaopisha matumizi mapya ya ardhi wanalipwa fidia stahiki ikiwa ni pamoja na kuwapa maeneo mbadala ili kuweza kuendeleza shughuli zao:-
Je, ni kwa nini Serikali imeshindwa kuwalipa fidia wananchi wa Kata za Nyamisangura na Nkende waliopo Halmashauri ya Mji wa Tarime ambao ardhi yao ilichukuliwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) tangu mwaka 2007?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Esther Matiko, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali huwa inatwaa ardhi kwa matumizi ya umma kwa kufuata Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999. Utaratibu huo hufuatwa kwa nchi nzima ikiwemo Nyamisangura na Nkende eneo ambalo linafahamika pia kwa jina la Nyandoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hilo lina Kiteule cha Askari wa Miguu kwa ajili ya ulinzi wa mpaka wa kati ya Musoma na Arusha. Mchakato wa kulitwaa eneo hili ulianza miaka ya nyuma na mnamo mwaka 2012 Wizara yangu ilitoa fedha kiasi kwa Halmashauri ya Mji wa Tarime ili kuwezesha kazi ya uthamini wa mali za wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya uthamini haikuweza kukamilika kwa sababu kiasi cha fedha kilichotolewa hakikutosha kumaliza kazi hiyo kutokana na ufinyu wa bajeti. Hivi sasa fedha za kukamilisha zoezi hilo zimepatikana na tayari zimeshatumwa kwa Halmasauri ya Mji wa Tarime.
Hatua inayofuata ni Halmashauri kukamilisha jedwali za uthamini na kuziwasilisha kwa Mthamini Mkuu wa Serikali kwa kupitishwa, kabla ya kuletwa Wizarani kwangu kwa ajili ya kuombewa fedha za malipo ya fidia kutoka Hazina.
MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED aliuliza:-
Kumekuwa na unyanyasaji mkubwa unaofanywa na JWTZ wa kuwanyang‟anya wavuvi samaki wao licha ya kwamba watu hao wanajitafutia kipato kupitia bahari kama Watanzania.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuondoa unyanyasaji huo unaofanywa na Jeshi la Wananchi kwa wananchi wake?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Muhammed Amour Muhammed, Mbunge wa Bumbwini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa haijawahi kupokea tuhuma yoyote inayohusu unyanyasaji unaofanywa na askari wa JWTZ kwa wavuvi nchini. Aidha, kama tuhuma hizi zina ushahidi ni bora zikafikishwa sehemu husika ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua zinazostahili.
Mheshimiwa Spika, nataka nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu kwamba, wanajeshi kama walivyo raia wote wanapaswa kuheshimu sheria za nchi na pale wanapokwenda kinyume huchukuliwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa sheria na kanuni za jeshi.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA (K.n.y. MHE. SAADA MKUYA SALUM) aliuliza:-
Vituo vingi vya afya vya kijeshi vinahudumia maafisa wa jeshi na wananchi waliopo karibu na vituo hivyo. Hata hivyo vituo hivi vinakabiliwa na upungufu wa dawa, vifaa tiba na wataalam wenye ujuzi.
(a) Je, Serikali inafahamu idadi ya vituo vyake vilivyopo Zanzibar?
(b) Je, kuna mkakati gani unafanyika kuhakikisha kuwa vituo hivyo vinapatiwa dawa, vifaa tiba na wataalam wa kuhudumia wananchi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA,WAZEE NA WATOTO (K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Saada Mkuya Salum Mbunge wa Weleza kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, kulingana na vipimo vya Umoja wa Mataifa (United Nations – UN), Zanzibar ina kituo kimoja cha afya ngazi ya tatu na vituo viwili ngazi ya pili. Aidha kimuundo kila Kikosi cha Jeshi kina kituo kidogo cha tiba.
(b) Kwa ujumla vituo vya afya vina changamoto za dawa, vifaa tiba na wataalam. Hali hiyo kwa kiasi kikubwa inachangiwa na ufinyu wa bajeti. Hata hivyo, changamoto hizo kwa sehemu kubwa zinategemewa kutatuliwa baada ya kukamilika taratibu za kuanzishwa mfuko wa Bima ya Afya kwa jeshi letu.
Aidha, changamoto ya wataalamu wa afya inategemewa kupungua baada ya wataalam wa afya walioajiriwa hivi karibuni waliopo katika mafunzo ya vitendo vikosini (exposure) na kwenye Vyuo vya Kijeshi kuhitimu mafunzo yao. Pia, upo mpango wa kuandikisha wataalamu wa afya katika ngazi ya Paramedics baada ya kupata kibali cha ajira mpya. Pia upo mpango wa kuandikisha wataalam wa afya katika ngazi Paramedics mara tu baada ya ajira mpya kuruhusiwa.
MHE. SUBIRA K. MGALU (K.n.y. MHE. MUNIRA MUSTAPHA KHATIB) aliuliza:-
Kumekuwa na ongezeko kubwa la vijana wanaomaliza kidato cha nne kutokana na ongezeko la shule za kata nchini, vijana hawa wamekuwa wakizagaa mitaani bila kujua la kufanya na matokeo yake kujiingiza kwenye vitendo hatarishi kama dawa za kulevya, uvutaji wa bangi, wizi, udokozi na kadhalika.
Je, ni kwa nini Serikali isianzishe mpango maalum wa kuwapeleka Jeshi la Kujenga Taifa vijana wanaomaliza kidato cha nne nchini ili wakimaliza mafunzo waweze kujiajiri wenyewe pamoja na kuwa wazalendo?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Munira Mustapha Khatib kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu uliopo hivi sasa, wa vijana kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa ni ule wa vijana kujitolea ambao ni wenye elimu kuanzia shule ya msingi hadi vyuo vikuu na ule wa mujibu wa sheria ambao ni kwa vijana waliomaliza kidato cha sita.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango maalum anaoushauri Mheshimiwa Mbunge wa kuwachukua vijana wote wanaomaliza kidato cha nne kwa sasa hautawezekana kutokana na uwezo mdogo wa kifedha. Hivi sasa uwezo wa JKT kuchukua vijana wa kujitolea ni ni kati ya vijana 5,000 hadi vijana 7,000 kwa mwaka kutokana na bajeti inayotolewa. Hata hivyo, ushauri huu ni mzuri na Serikali itafanya maandalizi ya kambi nyingi zaidi na kutenga bajeti kubwa zaidi kwa ajili ya uendeshaji kadri uwezo wa kifedha utakavyoruhusu.
MHE. CECILIA D. PARESSO (K.n.y. MHE. JULIUS K. LAIZER) aliuliza:-
Kwa muda mrefu kumekuwa na mgogoro wa mipaka kati ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania na Kijiji cha Lashaine Wilayani Monduli, lakini mwaka 2011 yalifikiwa makubaliano chini ya Mkuu wa Wilaya kuwa mipaka yenye mgogoro isomwe upya kwa kutumia GPS na wananchi wa kijiji cha Lashaine wamekuwa wakisubiri zoezi la kusomwa upya mipaka kwa muda mrefu.
Je, Serikali itakamilisha lini makubaliano haya kwa kutumia GPS kusoma mipaka upya ili kumaliza mgogoro huo?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Julius Laizer, Mbunge wa Monduli, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, vijiji vinavyozunguka eneo la Jeshi la Monduli vimekuwa na migogoro ya mipaka na Jeshi kwa miaka mingi. Katika kumaliza migogoro hiyo, Wizara yangu kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Monduli ilifanya vikao na makubaliano ya mipaka eneo la Jeshi na kulipima kwa kutumia vifaa vya kisasa yaani GPS mwaka 2004. Eneo la Jeshi lilipunguzwa kutoka ukubwa wa hekta 94,000 hadi hekta 86,966 ili kupisha makazi ya raia wa vijiji jirani yaliyokuwa yameingilia eneo la Jeshi kikiwemo Kijiji cha Lashaine.
Mheshimiwa Spika, tatizo la mpaka wa Jeshi upande wa Kijiji cha Lashaine ni kuzibainisha beacons zilizowekwa ili wananchi waweze kuziona kwa wazi kwa mujibu wa ramani iliyosajiliwa yaani boundary recovery.
Mheshimiwa Spika, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Laizer kuwa azma yetu ya kufufua mpaka huo bado ipo na tutafanya hivyo tutakapopata fedha za kutekeleza jukumu hilo.
MHE. HAMIDU H. BOBALI (K.n.y. MHE. VEDASTO E. NGOMBALE) aliuliza:-
Tanzania ni moja ya nchi duniani zilizoathirika kutokana na Tawala za Kikoloni na Vita vya Majimaji ni moja ya vielelezo vya athari hizo ambapo vita hivyo vilianza Wilayani Kilwa katika Kijiji cha Nandete mwaka 1905 - 1907:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha waathirika wa Vita vya Majimaji wanapata fidia kutoka kwa utawala wa kikoloni wa Kijerumani?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Vedasto Edgar Ngombale, Mbunge wa Kilwa Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, harakati za kupambana kivita dhidi ya ukoloni zilifanywa na Makabila mbalimbali hapa nchini ikiwemo Vita vya Majimaji na nyingine nyingi. Vita hivi vilifanywa na Watemi wa baadhi ya makabila wakiwemo; Mtemi Mirambo wa Tabora, Mtemi Mkwawa wa Iringa na Chifu Abushiri Bin Salim wa Uzigua, Tanga. Aidha, madhila ya ukoloni kwa wananchi ni mengi yakiwa ni pamoja na utumwa, ubaguzi wa rangi, ukandamizwaji na kuuawa kwa tamaduni zetu za asili. Pia, uporwaji wa mali zetu na ardhi bora za kilimo pamoja na mazuio ya kuendeleza vipaji vya teknolojia kama vile uundaji wa silaha. Haya ni baadhi tu ya madhila ya ukoloni. Makusudi ya vita vya watawala wetu wa jadi ilikuwa kupinga ukoloni na kutaka kujitawala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa harakati hizo za kivita za viongozi wa kijadi kwa pamoja zililenga kuwakomboa wananchi kutoka kwenye makucha ya ukoloni na kuleta uhuru kwa wananchi, siyo vyema kutoa madai ya fidia kwa jukumu hili la kizalendo lililotekelezwa na makabila mengi nchini mwetu. Badala yake madhila na athari ya Vita vya Majimaji yabaki kama sehemu muhimu ya kumbukumbu za ukombozi wa nchi yetu.
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE aliuliza:-

Tanzania ni moja ya nchi duniani zilizoathirika kutokana na Tawala za Kikoloni na Vita ya Majimaji ni moja ya vielelezo vya athari hizo ambapo vita hiyo vilianzia Wilayani Kilwa katika Kijiji cha Nandete mwaka 1905-1907:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha waathirika wa Vita vya Majimaji wanapata fidia kutoka kwa utawala wa kikoloni wa Kijerumani?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Vedasto Edgar Ngombale, Mbunge wa Kilwa Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, harakati za kupambana kivita dhidi ya ukoloni zilifanywa na makabila mbalimbali hapa nchini ikiwemo Vita vya Majimaji na nyingine nyingi. Vita hivyo vilifanywa na Watemi wa baadhi ya makabila wakiwemo Mtemi Mirambo wa Tabora, Mtemi Mkwawa wa Iringa na Chifu Abushir Bin Salim wa Uzigua Tanga. Aidha, madhila ya ukoloni kwa wananchi ni mengi yakiwa ni pamoja na utumwa, ubaguzi wa rangi, ukandamizwaji, uporwaji wa mali zetu na ardhi bora za kilimo pamoja na kuuawa kwa tamaduni zetu za asili. Haya ni baadhi tu ya madhila ya ukoloni. Maksudi ya vita za watawala wetu wa jadi ilikuwa kupinga ukoloni na kutaka kujitawala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wazo la Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ihakikishe kwamba Wajerumani wanawalipa fidia waathirika ni wazo zuri. Napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara yangu itaiandikia rasmi Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ili waangalie utaratibu bora wa kufikisha kwa wahusika madai haya.
MHE. ALLY SALEH ALLY Aliuliza:-
Tanzania imekuwa ikipeleka vikosi vya kulinda amani ndani ya Afrika na sehemu nyingine duniani kadri mahitaji na hali inavyoruhusu na kutimiza dhima ya duniani.
(a) Je, mazoezi kama haya yanaimarisha jina la Tanzania kiasi gani katika jukumu hili?
(b) Kama miaka kumi iliyopita Tanzania imepeleka vikosi maeneo gani na kwa misingi gani?
(c) Changamoto gani zinakuwepo katika kukusanya vikosi hivyo kabla havijapelekwa nje ya nchi kwa kzi kama hizo?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA Alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Saleh Ally, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ni mwanachama wa Umoja wa Mataifa na inatimiza wajibu wake wa kuzisaidia nchi zenye migogoro ili kuleta amani pale inapoombwa kufanya hivyo. Ushiriki wetu umetuletea heshima kubwa duniani kwa mara zote kuonesha utayari wetu wa kutoa msaada kwa ulinzi wa amani pamoja na kazi nzuri unayofanywa na jeshi letu katika kutekeleza jukumu hili.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, katika miaka kumi iliyopita Tanzania imepeleka vikundi vya ulinzi wa amani katika maeneo yafuatayo;
(i) Lebanon, kombania mbili toka mwaka 2008;
(ii) Darfur, Sudan, kikosi kimoja toka mwaka 2009; na
(iii) DRC zaidi ya kikosi kimoja toka mwaka 2013.
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto zilizopo katika kukusanya vikundi kabla ya kupelekwa nje ya nchi kwenye majukumu ya ulinzi wa amani ni zifuatazo:-
(i) Gharama za kuvihudumia vikosi hivyo vikiwa kwenye mafunzo;
(ii) Gharama ya vifaa vya wanajeshi vitakavyotumika eneo la uwajibikaji; na
(iii) Ugumu wa kupata mafunzo ya uhalisia wa maeneo wanakokwenda kwa mfano jangwani, misituni na kadhalika.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA aliuliza:-
Kuna vijana zaidi ya 300 Mkoa wa Kaskazini Unguja ambao wanajihusisha na kazi mbalimbali za kujitolea kama vile usafi, upandaji miti, kilimo cha mboga mboga na matunda na wapo tayari kijiunga na Jeshi la Ulinzi kama wakifikiriwa:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwachukua vijana hao kujiunga na Jeshi hasa ikizingatiwa kuwa wana maadili mema na wameweza kujitolea?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Angelina Adam Malembeka, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, utaratibu wa sasa wa wananchi wa Tanzania kuajiriwa katika Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania unataka waombaji kuwa wamepitia Jeshi la Kujenga Taifa. Jeshi la Kujenga Taifa hutoa nafasi kwa kila mkoa. Vijana wanaopenda kujiunga na Jeshi hujadiliwa na kupitishwa na Kamati za Ulinzi na Usalama ngazi ya wilaya na mkoa husika. Kwa upande wa Zanzibar nafasi hizo hutolewa kupitia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na idara maalum za SMZ. Ofisi hiyo ndiyo yenye wajibu wa kupeleka mgao huo katika mikoa husika.
Mheshimiwa Spika, kuhusu vijana zaidi ya 300 wa Mkoa wa Kaskazini Unguja ambao wanajihusisha na kazi mbalimbali za kujitolea na ambao wako tayari kujiunga na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, vijana hao wanashauriwa kuomba kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa mara nafasi zitakapotangazwa. Endapo watakuwa na sifa za kuajiriwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania naamini watapewa fursa hiyo kwa kadri ya nafasi zitakavyopatikana.
MHE. KAPT. GEORGE H. MKUCHIKA aliuliza:-
Sheria ya Jeshi la Kujenga Taifa ya Mwaka 1964 (The National Service Act. 1964) imeweka ulazima wa Vijana Watanzania wanaomaliza kidato cha sita kujiunga na mafunzo ya Jeshi la kujenga Taifa kwa mujibu wa Sheria.
(a) Je, katika miaka mitatu iliyopita ni vijana wangapi waliomaliza kidato cha sita kila mwaka na kati yao wangapi walijiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa?
(b) Je, waliojiunga ni asilimia ngapi wa waliotakiwa kujiunga?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa George Huruma Mkuchika, Mbunge wa Newala Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Sheria ya Jeshi la Kujenga Taifa ya mwaka 1964 imeweka ulazima wa vijana wa Tanzania wanaomaliza kidato cha sita kujiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa mujibu wa Sheria. Hata hivyo, mwaka 1994 Serikali iliyasitisha kwa muda mafunzo hayo na kuyarejesha mwaka 2013 na yameendelea kutolewa hadi sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu za vijana waliohitimu kidato cha sita na kuhudhuria mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa mujibu wa Sheria ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2014, vijana waliomaliza kidato cha sita ni 41,968, kati yao waliojiunga na mafunzo ya Jeshi la kujenga Taifa ni 31,692, ambayo ni sawa na asilimia 75.5.
Mwaka 2015, vijana waliomaliza kidato cha sita ni 40,753, kati yao waliojiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa ni 19,990, ambao ni sawa na asilimia 48.8.
Mwaka 2016, vijana waliomaliza kidato cha sita ni 63,623, kati yao waliojiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa ni 14,747, ambao ni sawa na asilimia 23.2.
Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu zilizopo zinaonesha kupungua kwa idadi ya vijana wanaojiunga na mafunzo hayo muhimu ya Jeshi la Kujenga Taifa. Hali hii imesababishwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na kugongana kwa tarehe za kuanza mafunzo ya vijana kwa mujibu wa Sheria na kufunguliwa kwa vyuo mbalimbali hapa nchini ambapo mihula ya mafunzo huanza.
Hali hii imewafanya vijana wengi walioteuliwa kujiunga na vyuo kukosa nafasi za kujiunga na mafunzo ya JKT kwa mujibu wa Sheria. Changamoto nyingine ni uhaba wa miundombinu, rasilimali watu na fedha. Hata hivyo Serikali inaendelea na juhudi za kupata suluhu ya changamoto zilizopo.
MHE. MATTAR ALI SALUM aliuliza:-
Tatizo la makazi kwa wanajeshi wetu ni kubwa kiasi kwamba maaskari wetu kupata usumbufu na kuathiri utendaji kazi wao.
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga nyumba za makazi kwa wanajeshi wa upande wa Unguja?
(b) Je, ni nyumba ngapi Serikali imepanga kujenga Zanzibar?
(c) Je, ni lini ujenzi wa nyumba kwa upande wa Zanzibar utaanza?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mattar Ali Salum, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Serikali inao mpango wa kuboresha makazi ya wanajeshi kwa kujenga nyumba za familia idadi ya 10,000. Kwa awamu ya kwanza ujenzi wa nyumba za familia za askari idadi 6,064 umefikia hatua ya mwisho kukamilika. Aidha, katika awamu hii hakuna ujenzi unaofanyika Unguja.
(b) Mheshimiwa Spika, katika awamu ya kwanza kwa upande wa Zanzibar, nyumba zimejengwa katika Kisiwa cha Pemba. Nyumba zilizojengwa ni ghorofa 40 zenye uwezo wa kuchukua familia idadi 320. Hatua inayofuata ni kukamilisha miundombinu ya umeme na maji ili nyumba hizo zianze kutumika.
(c) Mheshimiwa Spika, mchakato wa kuanza ujenzi wa nyumba za askari awamu ya pili unaotarajiwa kukamilisha ujenzi wa nyumba 10,000 unaendelea. Mgawanyo wa nyumba hizo utazingatia hitajio katika Kambi za Jeshi kwa ujumla ikihusisha Kambi za Unguja. Ujenzi huu utaanza mara mchakato utakapokamilika.
MHE. SAADA MKUYA SALUM aliuliza:-
Vituo vya Afya vinavyomilikiwa na Jeshi la Wananchi vimekuwa vikitoa huduma za afya kwa wananchi wengi na kutokana na umadhubuti na umakini wa watendaji, wananchi wamejenga imani kubwa juu ya huduma zinazotolewa katika vituo hivyo; hata hivyo huduma hizo zimekuwa zikikabiliwa na vikwazo mbalimbali vikiwemo uhaba wa dawa, Madaktari na vitendea kazi:-
Je, Serikali imeweka mkakati gani madhubuti wa kuhakikisha kuwa vifaa tiba, dawa na Madaktari vinapatikana ili kutoa huduma bora?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Saada Mkuya Salum, Mbunge wa Welezo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa linaendelea na hatua ya kuboresha huduma za tiba Jeshini, kama ifuatavyo:-
(a) Kuendeleza kuwashawishi wataalam wa tiba wenye sifa kujiunga na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kulingana na nafasi za ajira zinazopatikana.
(b) JWTZ limeendelea na utaratibu wa kuwaendeleza Maafisa, Askari na Watumishi wa Umma kupata elimu katika ngazi mbalimbali zikiwemo Stashahada, Shahada na Shahada ya Uzamili kupitia vyuo vyetu vya kijeshi mfano “Military College of Medical Services” pamoja na vyuo vya kiraia nje ya Jeshi. Aidha, Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kuwadhamini wataalam wa tiba wanaosomea Shahada ya Uzamili na Uzamivu.
(c) Serikali kupitia Wizara ya Afya imekuwa ikiendelea kutoa ruzuku na kuongeza upatikanaji wa madawa na vifaa tiba.
(d) Kupitia wafadhili mbalimbali mfano Serikali ya Marekani na Serikali ya Jamhuri ya Ujerumani, huduma za tiba zimeendelea kuboreshwa hasa kwa kuongeza miundombinu na vifaa tiba.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu niliyotoa katika sehemu (a) mpaka (d), Wizara yangu iko katika mchakato wa kuanzisha Mfuko wa Bima ya Afya kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania. Ni imani yetu kuwa Mfuko huo utakapoanzishwa utaweza kuongeza rasilimali fedha katika utoaji huduma za afya Jeshini. Fedha hizo za ziada zitatumika katika kuboresha miundombinu na upatikanaji wa dawa na vifaatiba hivyo kuboresha huduma za afya kwa Wanajeshi na wananchi wanaotumia vituo vya afya vya Jeshi kupata tiba. (Makofi)
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN (K.n.y. MHE. TWAHIR AWESU MOHAMMED) aliuliza:-
Tanzania ni nchi yenye amani kubwa katika nchi za Maziwa Makuu.
• Je, Serikali imejipanga vipi kuimarisha amani katika nchi yetu?
• Je, mipaka yetu na nchi zenye mizozo na wakimbizi imeimarishwa kiasi gani kiulinzi?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA aliuliza:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Twahir Awesu Mohammed, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, kimsingi suala la kuimarisha usalama na amani ya nchi yetu ni jukumu la kila Mtanzania. Hata hivyo, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania ambalo ndilo lenye jukumu la kulinda mipaka yetu ya Kimataifa na kuimarisha amani nchini limekuwa likishirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama pamoja na wadau wengine kuhakikisha kuwa hakuna adui wa ndani au wa nje anayeweza kuhatarisha au kuvuruga amani ya nchi yetu.
(b) Mheshimiwa Spika, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania limejipanga kikamilifu katika kuhakikisha kuwa mipaka ya nchi yetu inalindwa muda wote dhidi ya adui yeyote atakayejitokeza kuivamia.
Aidha, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama limeimarisha ulinzi katika maeneo ya mipaka yenye wakimbizi kwa kuweka viteule na vifaa vya kutosha. Hatua hii imesaidia kuzuia na kukabiliana na vitendo vyote vya kihalifu vinavyoweza kusababishwa na wakimbizi katika mipaka na katika makambi waliyopangiwa.
MHE. CECILIA D. PARESSO (K.n.y. MHE. LUCY S. MAGERELI) aliuliza:-
Askari wa JWTZ wamekuwa wakijichukulia sheria mkononi kwa kutesa raia na saa nyingine Jeshi la Polisi. Matukio haya yamekuwa yakifanyika maeneo ya starehe, kwenye foleni za magari, mitaani na katika magari ya usafiri wa umma. Hivi karibuni Mkoani Tanga, kijana mmoja kondakta wa daladala alimzuia mtoto wa mwanajeshi kupanda daladala yake bila nauli, alikamatwa na kuteswa na wanajeshi ndani ya Kambi, kitu kilichopelekea kifo chake.
(a) Je, sheria ipi inawapa wanajeshi haki ya kutesa raia?
(b) Je, Serikali inachukua hatua gani kukomesha hali hii?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Lucy Simon Magereli, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hakuna sheria yoyote inayowapa haki wanajeshi kutesa raia au kuvunja sheria.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, matukio ya wanajeshi kushambulia raia au raia kushambulia wanajeshi mara nyingi yamekuwa yakijitokeza katika mazingira yanayohusisha kutofautiana kauli, ulevi, wivu wa kimapenzi na hata ujambazi. Hivyo katika kushughulikia hali hii, mara nyingi kesi hufunguliwa kwenye mahakama za kiraia na hukumu kutolewa kwa mujibu wa sheria zilizopo hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa hakuna mtu aliye juu ya sheria inashauriwa wanaokubwa na kadhia hii wapeleke mashtaka kwa mujibu wa taratibu zilizopo ili sheria ifuate mkondo wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taratibu zilizopo za Jeshi letu la Ulinzi, afisa au askari anapopatijkana na hatia katika mahakama za kiraia na kuhukumiwa adhabu ya vifungo au nyinginezo, pia hupoteza sifa za kuendelea kulitumikia Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania. Aidha, maafisa na askari mara kwa mara wamekuwa wakiaswa kuishi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo.
MHE. JUMA ALI JUMA aliuliza:-
Kuna mgogoro wa ardhi kati ya Jeshi na wananchi wa Kisakasaka hali inayoleta wasiwasi kwa wananchi.
(a) Je, ni lini Serikali itaupatia ufumbuzi mgogoro huo?
(b) Je, kwa nini Serikali isiwaruhusu wananchi hao kuendelea na shughuli za kilimo na mifugo wakati wakisubiri ufumbuzi wa tatizo hilo?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Juma Ali Juma, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, inatambua uwepo wa mgogoro wa ardhi kati ya Jeshi na Wananchi katika eneo la Kisakasaka. Katika kupata ufumbuzi wa kudumu wa mgogoro huu, Makao Makuu ya Jeshi iliridhia kurekebisha mpaka wa Kambi ya Kisakasaka ili kuwaachia wananchi eneo lenye mgogoro na hivyo kuleta suluhisho la kudumu kwenye mgogoro huo. Zoezi hilo halijafanyika kutokana na ufinyu wa bajeti, hata hivyo katika mwaka huu wa fedha wa 2017/2018 tunategemea kutekeleza zoezi hili.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa napenda kuwasihi wananchi wawe wastahimilivu wakati Serikali inachukua hatua stahiki ili kuzuia madhara yoyote yanayoweza kutokea kwa wananchi endapo wataendelea na shughuli za kilimo na mifugo katika eneo hilo.
MHE. HAJI KHATIB KAI aliuliza:-
Serikali imeandaa utaratibu wa kuliwezesha Jeshi la Wananchi wa Tanzania kufanya shughuli zake kwa kuwapatia posho mbalimbali ikiwemo ration allowance.
Je, ni lini Serikali itaongeza posho hiyo iendane na maisha yalivyo sasa?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Haji Khatib Kai, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali inao utaratibu wa kuliwezesha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kufanya shughuli zake kwa kuwapatia maafisa na askari posho za aina mbalimbali ikiwemo ration allowance. Serikali imekuwa ikiboresha maslahi na stahiki mbalimbali kwa maafisa na askari kwa kuzingatia hali ya maisha ya wakati husika na uwezo wa Serikali kifedha kumudu kulipa stahiki hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ration allowance inalipwa kwa maafisa na askari wote. Serikali ilipandisha kiwango cha posho ya chakula (ration allowance) kwa nyakati tofauti. Kwa mfano, mwaka 2011 ration allowance ilikuwa shilingi 7,500, mwaka 2014 ration allowance ilipanda kufikia shilingi 8,500 na mwaka 2015 ilipandishwa kufikia shilingi 10,000, kiasi ambacho kinaendelea kutolewa hadi hivi sasa. Kwa hivyo, Serikali itaendelea kuboresha posho ya chakula na posho nyinginezo kadri uwezo wa Serikali utakavyoruhusu.
MHE. HASSAN E. MASALA aliuliza:-
Je, ni nini kauli ya Serikali katika kushughulikia tatizo la migogoro ya mipaka katika Kambi za JKT Nachingwea na Kikosi Namba 41 Majimaji na vijiji vinavyozunguka Kambi hizo?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Elias Masala, Mbunge wa Nachingwea, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu inatambua kuwepo kwa migogoro katika maeneo mbalimbali kati ya Kambi za Jeshi na vijiji jirani au maeneo yaliyotwaliwa na Jeshi kwa maslahi mapana ya nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya 41 KJ (Majimaji) ilipimwa mwaka 2005, wananchi waliokuwepo wakati wa upimaji idadi yao walikuwa 61. Katika Kambi ya 843 KJ ya JKT iliyopo Nachingwea mwaka 2009 Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea ilichukua jukumu la kuainisha mipaka kati ya Kambi hiyo na Kijiji cha Mkukwe. Wananchi waliokuwa ndani ya Kambi wakati wa kubaini mipaka hiyo walikuwa ni kaya tisa.
Mheshimiwa Spika, mwaka huu wa fedha 2018/2019 Wizara yangu imetenga bajeti kwa ajili ya uthamini na kulipa fidia kwa wananchi wanaostahili. Baada ya uthamini, wananchi wenye stahiki ya malipo watalipwa fidia zao kwa mujibu wa sheria na kanuni za fidia za ardhi zilizopo.
MHE. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza:-
Tanzania haijaidhinisha na kujiunga rasmi na mkataba wa kupambana na silaha za sumu (Biological Weapons Convention):-
(i) Je, kwa nini Tanzania haijajiunga na mkataba huo?
(ii) Je, Serikali inafahamu madhara ya kutoidhinisha rasmi mkataba huo?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ilisaini Mkataba wa Kupambana na Silaha za Baiolojia na Sumu tarehe 1 Agosti, 1972, lakini mpaka sasa haijaridhia mkataba huo. Kutoridhiwa kwa mkataba huo kulitokana na kutoonekana athari zake za moja kwa moja kwa wakati huo ambapo matumizi salama ya mkataba ikiwemo utafiti wa magojwa ya binadamu, wanyama na mimea yameendelea kufanyika nje ya mkataba huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto zinatokana na matishio mbalimbali ikiwemo ugaidi, zimesababisha hitajio la kuridhiwa kwa mkataba huo na kutekelezwa kwa vitendo baada ya kutungiwa sheria. Kutokana na umuhimu wa suala hili, Rasimu ya Waraka wa Mapendekezo ya kuridhia mkataba huo imeandaliwa na baada ya kupitia ngazi mbalimbali za maamuzi, azimio litaandaliwa kwa kuwasilishwa katika Bunge lako Tukufu kwa ajili ya kuridhiwa.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inafahamu madhara yaliyopo hivi sasa ya kutoridhiwa kwa mkataba huo. Baadhi ya madhara hayo ni kama ifuatavyo:-
Kwanza, Tanzania kuwa katika kundi dogo la nchi ambazo hazijaridhia mkataba huo kama vile Haiti, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Misri, Somalia na Syria. Tanzania kuwepo katika kundi hili hakutoi taswira nzuri kwa Jumuiya ya Kimataifa kwani kati ya nchi hizo nyingi zina migogoro ya muda mrefu ya ndani.
Pili, kunanyima fursa kwa wataalam wetu kupata mafunzo mbalimbali yanayotolewa katika kujenga uwezo na kukabiliana na athari za mashambulizi ya silaha sumu na kibaiolojia.
Tatu, kunanyima fursa kwa wataalam na viongozi wa Kitanzania kushiriki kwenye uongozi wa taasisi mbalimbali za kimataifa zinasimamia sheria za silaha za kibaiolojia na sumu.
Nne, kunakosesha Serikali kutoa haki za msingi kupitia mahakama kwa makosa mbalimbali yanayoweza kufanywa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA aliuliza:-
Wananchi wa Kata ya Nkandasi wamejitahidi kujenga Shule ya Sekondari ya Kata ya Milundikwa hadi kufikia Kidato cha Sita, lakini Serikali kupitia Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imeamua shule hiyo kuhamishwa mara moja kuanzia tarehe 1 Januari, 2017 ili kuliachia Jeshi:-
(a) Je, Serikali inatoa mchango gani katika uhamishaji na ujenzi mpya wa shule hiyo?
(b) Je, Serikali iko tayari kufanya tathmini ya miundombinu yote ya shule na majengo yaliyojengwa na wananchi na thamani hiyo kuitoa katika fedha taslimu kwa ujenzi mpya wa shule?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Desderius John Mipata, Mbuge wa Nkasi Kusini, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la Milundikwa lilikuwa ni Kambi ya JKT iliyokuwa ikiendesha shughuli za malezi ya vijana na uzalishaji mali kabla ya Serikali kusitisha mpango wa kuchukua vijana mwaka 1994. Wakati JKT linasitisha shughuli zake katika Kambi hiyo liliacha majengo ya ofisi na nyumba za makazi, baadaye Halmashauri ya Wilaya ilianzisha shule ya Sekondari ya Milundikwa na kuongeza miundombinu michache katika shule hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hatua ya kuliongezea Jeshi la Kujenga Taifa uwezo wa kuchukua vijana wengi zaidi mwezi Novemba mwaka 2016 Serikali ilitoa maelekezo kwa JKT kufufua makambi yaliyokuwa yameachwa mwaka 1994 likiwemo la Milundikwa. Kufuatia maagizo hayo ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Nkasi na Halmashauri ya Wilaya hiyo waliratibu na kusimamia utaratibu wa kuhamisha Walimu na wanafunzi waliyokuwa katika shule Milundikwa kwenda katika shule jirani. Baadhi ya wanafunzi walihamishiwa katika shule ya Sekondari ya Kasu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuchangia maendeleo ya wanafunzi waliokuwa wakisoma katika Shule ya Sekondari ya Milundikwa mnamo tarehe 9 Februari, 2017 Wizara ya Ulinzi na JKT kupitia Makao Makuu ya JKT ilitoa mabati idadi 2,014 ili kuhakikisha kuwa vyumba vya madarasa vilivyokuwa vinaendelea kujengwa vinakamilika na kuanza kutumika. Wizara yangu itakuwa tayari kuendelea kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya katika kutoa vifaa vya ujenzi kadri uwezo utakavyoruhusu.
MHE. ALMAS A. MAIGE aliuliza:-
Hivi karibuni Serikali kupitia JKT imeanzisha tena mafunzo ya vijana wa kujitolea na wale wa mujibu wa sheria waliomaliza kidato cha sita au kutoka vyuo hapa nchini.
• Je, ni kweli kuwa JKT wanachukua wanafunzi kwa mujibu wa sheria kutoka katika shule na vyuo vya Serikali tu?
• Je, Serikali haioni kuwa vijana kutoka shule na vyuo binafsi wanahitaji pia mafunzo muhimu ya uzalendo na kujiendeleza kiuchumi?
• Je, ni vijana wangapi kwa mujibu wa sheria kwa mwaka 2017/2018 wamechukuliwa na JKT katika shule na vyuo binafsi nchini?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Almas Athuman Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
a) Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wa mujibu wa sheria huchukuliwa moja moja kutoka shule za Serikali na binafsi bila kuhusisha vyuo. Vijana kutoka vyuo vya Serikali na binafsi hujiunga na mafunzo ya JKT kwa utaratibu wa kujitolea ambapo utaratibu wa kuwapata hupitia katika usaili unaofanyika ngazi za Wilaya na Mikoa ambapo unahusisha pia vijana wengine wenye sifa bila kujali shule aliyotoka.
b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaona umuhimu wa kuchukua vijana kutoka shule na vyuo binafsi kwa ajili ya mafunzo katika Jeshi la Kujenga Taifa, ndiyo maana uteuzi wa vijana unahusisha shule zote za Serikali na binafsi. Vijana ambao ni wahitimu wa vyuo vya Serikali au binafsi huingia JKT kwa utaratibu wa kujitolea kama nilivyosema awali.
c) Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana waliojiunga na JKT kutoka shule binafsi idadi yao ni 7,076 ambapo kati yao wavulana ni 5,432 na wasichana ni 1,644. Idadi hiyo ni kati ya vijana 20,000 walioitwa kujiunga na mafunzo kwa mujibu wa sheria kwa mwaka 2017/2018.
MHE. OSCAR R. MUKASA aliuliza:-
Je, ni lini Jeshi la Kujenga Taifa litakuja na mkakati wa kuwa na miradi itakayounganishwa na jitihada za vijana wasiokuwa na ajira Wilayani Biharamulo na kwingineko kwa namna isiyohitaji uwekezaji mkubwa wa kujenga Kambi za Kijeshi?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Oscar Mukasa, Mbunge wa Biharamulo Magharibi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua hitaji kubwa la kuanzishwa Kambi za JKT kwenye Mikoa na Wilaya ambazo hazina Kambi za JKT ikiwemo Biharamulo. Jeshi la Kujenga Taifa limeeleka nguvu kwenye vikosi vilivyoanzishwa awali na baadaye kusitisha shughuli za kuchukua vijana mwaka 1994. Aidha, JKT inaanzisha kambi mpya katika maeneo mbalimbali kwa awamu kwa kadri bajeti yake itakavyoruhusu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa Jeshi la Kujenga Taifa limejikita katika kutoa mafunzo ya stadi za kazi kwa vijana waliojiunga na JKT kwa kujitolea. Lengo ni kuwa endapo vijana hawa watakosa ajira katika vyombo vya Ulinzi na Usalama waweze kujiajiriwa na taasisi nyingine za Serikali, sekta binafsi au wajiajiri wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa vijana wanaopata fursa hii ya kujiunga na JKT kwa kujitolea ni wachache kulingana na mahitaji; wazo la Mheshimiwa la kulitaka Jeshi la Kujenga Taifa kuanzisha miradi iliyohitaji uwekezaji mkubwa na kuwashirikisha vijana wasio na ajira katika maeneo mbalimbali yasiyokuwa na kambi za JKT ikiwemo Biharamulo ni wazo zuri ambalo tunalipokea na tunaahidi kulifanyia kazi ili kuona uwezekano wa kulitekeleza.
MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED aliuliza:-
Kwa kipindi cha kirefu sasa nchi yetu imekuwa ikipeleka Askari wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) nje ya nchi ambako kuna vita vya wenyewe kwa wenyewe na kusababisha misiba mikubwa sana kwa Askari wetu:- Je, Serikali inasema nini kuhusiana na kadhia hiyo?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Muhammed Amour Muhammed, Mbunge wa Bumbwini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania kama Mwanachama wa Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, Jumuiya za Kikanda kama East Africa Community na SADC na Jumuiya ya Nchi za Maziwa Makuu inao wajibu wa kushiriki katika Ulinzi wa Amani katika nchi mbalimbali. Madhumuni ya kupeleka askari wetu huko ni kwenda kulinda amani na sio kushiriki kwenye mapigano. Kwa bahati mbaya sana, yapo matukio ya kushambuliwa kwa askari wetu yaliyofanywa na vikundi vya waasi yaliyopelekea kupoteza maisha ya baadhi ya askari wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Wananchi wa Tanzania limechukua hatua ya kutoa mafunzo ya kutosha kwa vikosi vyetu vinavyopewa jukumu hili, pamoja na kuwaongezea vifaa vya kisasa ili waweze kujilinda dhidi ya mashambulio ya vikundi vya waasi. Hivyo, mtazamo wa Serikali ni kuendelea kushiriki katika shughuli za Ulinzi wa Amani katika nchi mbalimbali ili kutimiza wajibu wetu Kimataifa na huku tukichukua kila tahadhari kuepusha maafa yaliyowahi kutokea.
MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza:-
Je, ni lini Serikali italeta mabadiliko katika sheria inayosimamia malipo ya fidia kwa askari anayejeruhiwa au kupoteza maisha akiwa anatekeleza majukumu ya kulinda usalama ndani au nje ya nchi kwenye vyombo vya UN au SADC Mission ili kuendana na mabadiliko ya kupanda kwa gharama za maisha?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, malipo ya fidia kwa askari aliyejeruhiwa au kufariki akiwa anatekeleza majukumu ya ulinzi wa amani katika Umoja wa Mataifa hupangwa na kusimamiwa na Umoja wa Mataifa. Kwa kawaida, Umoja wa Mataifa hukaa vikao vya maamuzi na kutoa waraka ambao kwa ujumla hutekelezwa na nchi zote zilizopeleka majeshi katika Misheni za Umoja wa Mataifa unaofafanua stahiki mbalimbali za malipo kwa wanajeshi wanaoumia au kufariki wakati wa kutekeleza majukumu ya ulinzi wa amani. Waraka huo huzijulisha nchi wanachama zinazochangia vikosi, Maafisa wanadhimu na waangalizi wa amani stahiki ya malipo. Hivyo, siyo jukumu la nchi husika kuamua ilipwe fedha kiasi gani.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Misheni za SADC, hadi sasa hakuna Misheni inayomilikiwa na SADC pekee, bali iliyopo inaitwa Force International Brigade ambayo imeunganishwa na Misheni ya Umoja wa Mataifa nchini DRC ambayo taratibu za kulipa askari aliyeumia au kufariki bado inasimamiwa na Umoja wa Mataifa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa afisa au askari aliyeumia, utaratibu huo hufanyika kwa kuwasilisha nyaraka muhimu ambazo hutoa mwelekeo wa kiwango alichoumia ili alipwe kulingana na stahili.
Mheshimiwa Spika, kwa afisa au askari aliyefariki, Umoja wa Mataifa kwa sasa inalipa fidia ya dola za Kimarekani 70,000 kwa askari wa nchi yoyote aliyefariki akiwa anatekeleza majukumu ya ulinzi wa amani katika Misheni za Umoja wa Mataifa.
MHE. ABDUL-AZIZ M. ABOOD aliuliza:-
Kuna mgogoro wa ardhi kati ya Jeshi la Wananchi kwenye mipaka katika Kata ya Kauzeni na Luhongo ambapo wananchi wanashindwa kufanya shughuli zao za maendeleo hasa kilimo, Jeshi linaweka mipaka na kuingiza ndani ya mashamba ya wananchi wakati miaka yote maeneo hayo yalikuwa nje ya mipaka ya Jeshi:-
• Je, ni lini Serikali itawarudishia wananchi maeneo yao ya kilimo?
• Je, kwa nini Serikali isichukue hatua kwa kuruhusu wananchi wamiliki maeneo hayo ambayo ni ya asili na Jeshi limewakuta wananchi katika eneo hilo?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abdul-Aziz Mohamed Abood, Mbunge wa Morogoro Mjini, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ufumbuzi wa mgogoro wa mipaka ulishafanyika kwa kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro. Hivyo, kimsingi Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania halina mgogoro na wananchi kwenye mipaka ya Kata za Kauzeni na Luhongo hasa baada ya upimaji mpya wa mwaka 2002 ambapo uliacha nje maeneo ya vijiji. Manung’uniko yaliyopo yanatokana na uamuzi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kusitisha utaratibu wa kuwaruhusu kwa muda baadhi ya wananchi kulima mashamba ndani ya mipaka yake kwa sababu za kiulinzi na kiusalama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo yanayomilikiwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania yapo kwa ajili ya ulinzi wa nchi na sehemu hizo zipo kimkakati kwa ajili ya usalama wa nchi. Serikali imetumia rasilimali nyingi za wananchi wa Tanzania kujenga miundombinu iliyopo kwenye eneo hilo. Hivyo, haitokuwa vema kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kuondoka katika maeneo yaliyochaguliwa kistratejia kwa ajili ya ulinzi. Ni vema wananchi waelimishwe juu ya jambo hili na nimwombe Mheshimiwa Mbunge ashirikiane na wadau mbalimbali katika Halmashauri ya Mkoa kutoa elimu kwa wananchi. (Makofi)
MHE. MACHANO OTHMAN SAID (K.n.y. MHE. SALUM MWINYI REHANI) aliuliza:-
Kambi za Jeshi za Ubago na Dunga zinawanyanyasa wananchi wa Shehia ya Kidimi kwa kuwataka waondoke katika maeneo hayo ambayo ni ya iliyokuwa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Ushirika kwa zaidi ya miaka 40 wameanza kupima na kuweka bikoni:-
Je, Serikali inatoa tamko gani juu ya hali hiyo na hatma ya wananchi wanaoishi kwenye maeneo hayo?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Salum Mwinyi Rehani, Mbunge wa Uzini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya Ubago na Dunga yalipimwa mwaka 1985, kwa unyeti wake Uongozi wa Mkoa na Wilaya husika zilishirikishwa. Aidha, taratibu zote za utwaaji ardhi kwa matumizi ya umma zilitumika na kuruhusu maeneo haya kupimwa yaani Ubago na Dunga. Maeneo yote mawili tayari yamejengwa miundombinu ya Kijeshi ambayo siyo rafiki kwa matumizi mengine ya kiraia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Ardhi Na. 12 ya mwaka 1992 ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, ilipoanza kutumika, ramani za upimaji wote uliofanyika kabla ya 1992 zilitakiwa kupitiwa upya. Hivyo, ramani za upimaji wa maeneo ya Ubago na Dunga zilikwama kupata Hatimiliki kutokana na sheria hiyo. Hali hii ilitoa mwanya kwa wananchi kuingilia sehemu ya maeneo ya Kambi kwa shughuli za kiraia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 19 Mei, 2018 kulifanyika kikao na ukaguzi wa pamoja kati ya Wizara yangu na Waheshimiwa Mawaziri wa SMZ pamoja na Mkurugenzi wa Mipango Miji na Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani wa Zanzibar kwa lengo la kupata ufumbuzi wa kudumu wa wananchi walioko katika maeneo haya. Ukweli ni kwamba eneo hili linatumiwa na JWTZ kihalali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, timu ya watalaam kutoka Idara ya Ardhi ya SMZ ikishirikiana na Uongozi wa Mkoa na Wilaya husika wanaendelea na zoezi la kufanya tathmini ya uvamizi wa maeneo haya ili hatimaye kusaidia kufikia uamuzi kuhusu hatma ya wananchi ndani ya maeneo haya nyeti ya JWTZ.
MHE. MACHANO OTHMAN SAID (K.n.y. MHE. USSI SALUM PONDEZA AMJADI) aliuliza:-
Vijana wa Kitanzania wanakabiliwa na tatizo sugu la ukosefu wa ajira na hivyo nguvu kazi kupotea badala ya kutumika kwa uzalishaji:-
(a) Je, Jeshi la Kujenga Taifa lina mpango gani wa kutumia nguvu kazi ya vijana kwa kuanzisha miradi ya kilimo cha kisasa ili kuondoa tatizo la ajira?
(b) Je, ni vijana wangapi wamenufaika na ajira kwa kila mwaka kupitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT)?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, Mbunge wa Chumbuni, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mafunzo ya kijeshi ambayo vijana huyapata kwa muda wa miezi sita, vijana hao pia hujifunza shughuli mbalimbali za uzalishaji mali katika kambi wanazopangiwa baada ya mafunzo ya kijeshi. Shughuli hizo hufanyika ndani ya mwaka mmoja na nusu kati ya miaka miwili ambayo wanajitolea wanapokuwa JKT. Baada ya kumaliza muda huo, tunaamini kwamba vijana wanakuwa wamepata ujuzi ambapo wanaweza kujiajiri au hata kuajiriwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Kujenga Taifa lina mashamba makubwa ya kilimo yanayotumia pembejeo na zana za kisasa za kilimo kama vile mbegu bora, matrekta, mashine za kupandia na mashine za kuvunia (harvesters) hutumika. Mashamba hayo hulimwa kama mashamba darasa kwa ajili ya kuwafundishia vijana walioko JKT. JKT hulima mashamba hayo, si kwa lengo la kuajiri vijana, bali kuwapatia ujuzi ambao watautumia baada ya kumaliza muda wa mafunzo ya JKT. Baada ya kumaliza mafunzo wanaweza kuanzisha miradi ya kilimo cha kisasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mafunzo hayo, vijana hupewa mafunzo ya ujasiriamali ikiwa ni pamoja na mafunzo ya ufugaji wa nyama, samaki na nyuki, kupanda na kuvuna miti ya mbao, kuongeza thamani ya mazao ya nafaka na mbegu za mafuta ambayo Wizara ina imani kwamba yatawawezesha vijana hawa kujitegemea kwa kutumia stadi za ufundi, kilimo, mifugo na uvuvi walivyojifunza wakiwa JKT.
Mheshimiwa Mwenyekiti, idadi ya vijana walioajiriwa na vyombo vya ulinzi na usalama kuanzia mwaka 2003 hadi 2017 jumla yao ni 42,593. Aidha, idadi ya vijana 3,576 wameajiriwa na SUMAJKT Guard Ltd.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM (K.n.y. MHE. ESTHER M. MATIKO) aliuliza:-
Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limejitwalia maeneo ya wananchi wa Kenyambi na Bugosi kinyume kabisa na sheria baada ya kukaribishwa kwa hifadhi ya muda kufuatia kukatika kwa mawasiliano kati ya kambi yao iliyopo Kata ya Nyandoto na Tarime Mjini:-
a) Je, ni kwa nini Serikali imeshindwa kuwalipa fidia wananchi hao waliochukuliwa ardhi yao na JWTZ tangu mwaka 2007?
b) Je, ni kwa nini JWTZ wasirudi kwenye kambi yao iliyopo Kata ya Nyandoto yenye eneo kubwa kuliko kuchukua maeneo yaliyo katikati ya makazi?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko, Mbunge wa Tarime Mjini, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa inatambua umuhimu wa kulipa fidia ya ardhi iliyotwaliwa. Uthamini kwa ajili ya fidia kwa wananchi umefanyika tangu mwaka 2013. Ufinyu wa bajeti ya Serikali ndiyo umechelewesha kufanyika kwa malipo ya fidia hiyo. Katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali kupitia Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ilitenga shilingi bilioni 20.03 kwa ajili ya ulipaji wa fidia na masuala mengine yanayoendana na upimaji wa maeneo. Naamini fedha hizo zikipatikana, ulipaji wa fidia ya ardhi utafanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la Nyandoto lipo chini ya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime. Mwaka 1992 Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania lilikabidhi eneo hilo kwa Halmashauri ya Wilaya ambayo imelipangia matumizi mengine.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA aliuliza:-

Kwa muda mrefu kumekuwa na migogoro ya mipaka baina ya wananchi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika maeneo ya Mkonkole Kata ya Tambuka Reli, Usule Kata ya Mbungani na Kata ya Cheyo Tabora Mjini:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa haraka wa kutatua mgogoro huo ambao ni wa muda mrefu?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Emanuel Adamson Mwakasaka, Mbunge wa Tabora Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika Mji wa Tabora, JWTZ lina Kambi kwenye maeneo ya Airport, Cheyo, Bomani, Mirambo, Usule na Kalunde. Maeneo yote hayo yalipimwa na ramani zake kusajiliwa. Wakati wa upimaji maeneo mawili walikutwa watu wachache. Eneo la Airport alikutwa mwananchi mmoja aliyekuwa anaishi hapo. Mwananchi huyo alishafanyiwa uthamini na ameshalipwa fidia yake. Katika eneo la Usale zilikutwa familia tatu. Wizara ya Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa limefanya mawasiliano na familia hizi kwa ajili ya kufanyiwa uthamini na hatua ya kulipwa fidia kwa kuzingatia upatikanaji wa fedha za maendeleo kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019.

Mheshimiwa Spika, katika juhudi za kuendeleza makazi katika Mji wa Tabora, Halmashauri ya Manispaa ya Tabora ilianza kupima viwanda ndani ya eneo la Kambi ya Mirambo ambalo tayari lilikuwa limepimwa. JWTZ ilichukua hatua ya kulifikisha suala hilo katika Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Tabora ambayo ilisimamisha zoezi hilo. Wakati zoezi linasimamishwa, tayari wananchi wengine wameshagawiwa viwanja. Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa inaendelea kuwasiliana na Halmashauri ya Manispaa ya Tabora ili kuwaondoa wananchi hao ambao walipimiwa viwanja ndani ya eneo hilo likiwemo eneo la Tambuka Reli. Uondoshaji wa wananchi hawa utawezesha eneo hilo kuwa huu kwa matumizi ya kijeshi pekee.
MHE. RUTH H. MOLLEL (K.n.y. MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA) aliuliza:-

SUMA-JKT Idara ya Zana za Kilimo ilikopesha 5,355,153,000/= kwa idara mbalimbali ndani ya SUMA-JKT. Taarifa za CAG zimeonesha kuwa hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2016 ni kiasi cha Sh.534,785,000/= ambayo ni kiasi chini ya asilimia 10 ndio kilirejeshwa:-

(a) Je, ni kiasi gani hadi sasa kimerejeshwa kwenye Idara hiyo ya Zana za Kilimo?

(b) Je, Serikali itakubaliana na mimi kwamba, uzembe huu wa kutohakikisha mikopo ya fedha za Serikali inarudishwa kwa wakati ili wakulima wengine nao waweze kukopeshwa kumechangia kukwamisha juhudi za kupunguza umaskini nchini?

(c) Je, Serikali inachukua hatua gani kuwawajibisha waliohusika na utoaji huo wa mikopo bila kuhakikisha inarudishwa kwa wakati?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Naghenjwa Livingstone Kaboyoka, Mbunge wa Same Mashariki, lenye Sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa mradi wa zana za kilimo wa SUMA-JKT ulikopesha miradi mingine ndani ya SUMA-JKT jumla ya shilingi 5,355,153,000/= kama ilivyoelezwa katika Taarifa ya CAG ya mwaka 2015/2016 na kwamba mpaka kufikia tarehe 30 Juni, 2016, kiasi cha shilingi 534,785,000/= ndicho kilikuwa kimerejeshwa. Hadi kufikia tarehe 31 Januari, 2019, jumla ya shilingi 2,389,082,000/= zimerejeshwa katika mradi wa zana za kilimo ambayo ni sawa na asilimia 45 ya fedha zote zilizokopeshwa. Hivyo, mpaka sasa fedha ambazo bado hazijarejeshwa ni shilingi 2,966,071,000/=.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo kubwa la kukopesha fedha hizo lilikuwa ni kuiwezesha kimtaji miradi ndani ya SUMA-JKT pamoja na miradi mingine mipya baada ya kujiridhisha kuwa ina tija. Hivyo, lengo hili halikwamishi juhudi za kupunguza umasikini nchini, basi linaongeza mapato katika miradi ya shirika kwa ujumla.

(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la SUMA-JKT limeendelea kuhakikisha fedha zilizobaki zinarejeshwa katika mradi wa zana za kilimo kwa kuchukua hatua zifuatazo:-

(i) Kuhakikisha uwepo wa mikataba kati ya mradi wa zana za kilimo na mkopaji, pia mikataba iliyokuwa na upungufu imerekebishwa;

(ii) Kuhakikisha miradi iliyokopeshwa inazalisha kwa faida ambapo sehemu ya fedha hiyo huwasilishwa moja kwa moja katika mradi wa zana za kilimo; na

(iii) Kuweka baadhi ya miradi iliyokopeshwa chini ya usimamizi wa moja kwa moja wa mradi wa zana za kilimo.
MHE. DUSTAN L. KITANDULA aliuliza:-

Katika kuimarisha ulinzi wa mipaka yetu na nchi jirani ya Kenya, Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) limechukua mashamba ya baadhi ya wananchi wa Kata ya Mwakijembe:-

Je, ni lini wananchi hao watapewa fidia kwa ajili ya ardhi/mashamba yao yaliyochukuliwa na Jeshi?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dunstan Luka Kitandula, Mbunge wa Mkinga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania limeanzisha Kituo cha Ulinzi katika eneo la Kata ya Mwakijembe, Wilaya ya Mkinga lenye hekari moja mwaka 2017. Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga iliona umuhimu wa kutenga eneo hilo kwa matumizi ya Jeshi ili kuimarisha ulinzi kwenye maeneo ya mpakani. Eneo hilo awali lilikuwa ni shamba darasa la mradi wa umwagiliaji uliokuwa unaendeshwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa eneo hili lilikuwa linasimamiwa na uongozi wa Wilaya kabla ya Jeshi kuingia hapo, ni busara suala la fidia kama lipo likawasilishwa kwenye uongozi wa Wilaya ya Mkinga.
MHE. USSI SALUM PONDEZA aliuliza:-

Wananchi wa Kisakasaka, Mkoani Mjini Magharibi Unguja wamekuwa na mgogoro wa ardhi wa muda mrefu na Kambi ya Jeshi la Wananchi na hivyo kuathiri shughuli zao za kiuchumi:-

(a) Je, Serikali imechukua hatua gani kumaliza mgogoro huo?

(b) Je, ni sababu gani zimesababisha mgogoro huo kudumu zaidi ya miaka 40?

(c) Je, ni lini Taasisi husika za Serikali zitakaa pamoja na kumaliza mgogoro huo?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, Mbunge wa Chumbuni lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, Kambi ya Kisakasaka yenye ukubwa wa hekari 490 ilianzishwa mwaka 1978 lengo likiwa ni kulinda anga na Manispaa ya Mji wa Zanzibar na vituo muhimu. Eneo hilo liliwahi kupimwa mwaka 1985 lakini halikuwahi kupatiwa hatimiliki kwa sababu Sheria mpya ya Ardhi ya Zanzibar Na. 12 ya mwaka 1992 haikutambua upimaji uliofanywa kabla ya hapo. Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa inatambua uwepo wa mgogoro husika na imekuwa ikichukua hatua kadhaa kuumaliza kama ifuatavyo:-

(i) Mwaka 2013 fedha kiasi cha Sh.4,150,000/= kililipwa kwa Idara ya Upimaji na Ramani ya Zanzibar ili kufanya kazi ya upimaji na kuandaa hatimiliki. Kazi hii haijafanyika kwa sababu wananchi hawakuridhika na upimaji huo.

(ii) Katika muendelezo wa kumaliza mgogoro huo, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi alitembelea aneo hilo na kuridhia mipaka irekebishwe kwa kuzingatia maslahi mapana ya Jeshi na mahitaji ya ardhi kwa wananchi.

(b) Mheshimiwa Spika, baadhi ya sababu zilizopelekea mgogoro kudumu kwa muda mrefu ni kukosekana kwa fedha za kugharamia kazi za upimaji, uthamini na ulipaji fidia katika maeneo yaliyotwaliwa na Jeshi.

(c) Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imekubali kuunda Kikosi Kazi kitakachopitia maeneo yote yenye migogoro kwa Zanzibar ambacho kitatoa mapendekezo ya kudumu ya kumaliza migogoro hiyo.
MHE. JANET Z. MBENE aliuliza:-

Serikali ilinunua mashine ya kujengea kutoka Marekani kwa fedha nyingi sana kwa lengo la kuitumia kujenga nyumba nyingi za watumishi, ofisi na taasisi na kadhalika kwa haraka zaidi, mashine hiyo kwa muundo wake ina uwezo wa kujenga nyumba kwa bei nafuu zaidi na hivi sasa kuna upungufu mkubwa wa nyumba za walimu, madarasa, maabara, mabweni, nyumba za wauguzi, madaktari na vituo vya afya:-

(a) Je, ni nyumba ngapi na kwa gharama gani zilizojengwa na Jeshi la Ulinzi na Kujenga Taifa kwa kutumia mashine hiyo na kama zimejengwa kwa ujenzi wa kawaida zingetumia kiasi gani?

(b) Je, ni kwa nini mashine hiyo haitumiki kujenga nyumba zinazohitajika wakati kuna upungufu mkubwa sana wa nyumba za Serikali?

(c) Je, Serikali iko tayari kufanya tathimini na kutuletea Bungeni mpango mzima wa kuanza kutumia mashine hiyo kujenga nyumba zinazohitajika?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI (K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Janet Zebedayo Mbene, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, nyumba nne zilijengwa wakati wa mafunzo kwa gharama ya shilingi 1,325,000,000 na majengo matano yalijengwa baada ya mafunzo kwa gharama ya shilingi 9,216,653,699.50. Gharama za majengo yote jumla yake ilikuwa ni shilingi 10,541,653,699.50. Majengo haya ni pamoja na ukumbi (multipurpose hall) na nyumba za kuishi katika Kambi ya Twalipo Dar es Salaam; Banda la Jeshi la Wananchi wa Tanzania la Maonesho Sabasaba; na Ofisi ya muda ya Kitengo cha Uwekezaji TIC. Nyingine ni Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Kihangaiko; Kiteule cha Kijeshi Tarime; Karakana ya Wakala wa Vipimo na Mizani Misugusugu Kibaha; ghala la kuhifadhia nafaka la SUMA JKT kule Chita; na kumbi za burudani za SUMA JKT Mwenge Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, majengo haya kama yangejengwa kwa ujenzi wa kawaida gharama zingefikia shilingi 11,981,649,808.70. Mbali na teknolojia hii kuwa ya nafuu katika gharama za ujenzi uliofikia asilimia 15%, unafuu mkubwa upo katika ujenzi unaokadiriwa kuwa na asilimia 70%.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwango kikubwa mashine hizi hazitumiki ipasavyo kutokana na ukosefu wa fedha za maendeleo kwa ajili ya ujenzi wa substructure yaani ujenzi toka chini hadi usawa wa msingi. Malighafi inayotumka ni steel coil ambayo kwa matumizi ya Kijeshi kama fedha za maendeleo zingepatikana ingeweza kukidhi mahitaji.

(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, mitambo ya UBM (Ultimate Building Machine) ilinunuliwa na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa ajili ya kutekeleza shughuli za ujenzi ndani za Wizara. Hata hivyo, Wizara ya Ujenzi na Jeshi la Kujenga Taifa liko tayari kushirikiana pamoja na taasisi nyingine za Serikali katika ujenzi wa majengo hayo. Aidha, Wizara iko tayari kuandaa mpango kabambe kwa kutumia teknolojia hiyo ili kuwezesha ujenzi wa majengo mbalimbali ya Serikali. Ahsante.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM aliuliza:-

Kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu ya wananchi ambao maeneo yao yametwaliwa na Jeshi la Wananchi (JWTZ) pasipo kulipwa fidia:-

Je, Serikali ina mpango gani wa haraka kulipa fidia kwa wannachi hao?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Masoud Abdalah Salim, Mbunge wa Ntambile, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika ni kweli yapo maeneo mbalimbali yaliyotwaliwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kwa ajili ya utekelezaji wa jukumu la ulinzi wa nchi na mipaka yake. Baadhi ya maeneo hayo yamelipwa fidia na mengine mchakato wa kulipa fidia kwa wamiliki unaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa Serikali uliopo ni kuendelea na utaratibu wa kulipa fidia stahiki kwa wananchi kadri hali ya fedha itakavyoruhusu na kwa mujibu wa Sheria ya Utwaaji Ardhi kwa ajili ya matumizi ya umma. Kwa mwaka wa fedha 2018/2019, Wizara ilitenga shilingi bilioni 20.9 kwa ajili ya kulipa fidia maeneo yaliyotwaliwa na jeshi. Baada ya uhakiki wa malipo ya fidia tayari kiasi cha shilingi bilioni 3 kimelipwa kama fidia. Aidha, uhakiki wa madai ya fidia unaendelea katika maeneo mengine na mara uhakiki utakapokamilika Serikali kupitia Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa italipa fidia hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba wananchi wawe na subira wakati Serikali inakamilisha uhakiki ili kuwalipa stahiki zao.
MHE. HASSAN E. MASALA aliuliza:-

Kambi za Jeshi 41KJ, 452 Medium ni miongoni mwa kambi kongwe na zenye mchango mkubwa katika Ulinzi wa Taifa letu. Kutokana na ukongwe huo, kambi hizo zimechakaa miundombinu yake mfano shule na zahanati zilizopo kwenye kambi hizo:-

(a) Je, nini mpango wa Serikali juu ya kuboresha miundombinu ya Zahanati zilizopo kwenye kambi hizi?

(b) Je, nini mpango wa Serikali wa kuboresha miundombinu ya shule hiyo iliyopo kwenye kambi hizo?

(c) Je, nini mpango wa Serikali juu ya kuboresha miundombinu ya Medium Workshop hiyo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Elias Masala, Mbunge wa Nachingwea, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kambi ya Jeshi 41KJ na 451KJ ni miongoni mwa kambi kongwe na zenye mchango mkubwa katika ulizi wa Taifa letu. Kutokana na ukongwe wa kambi hizo, umepelekea kuchakaa kwa miundombinu ya zahanati, shule na medium workshops zilizopo huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uboreshwaji wa miundombinu ya hospitali kuu ya kanda iliyopo chini ya kambi ya Jeshi la 41 KJ, umekamilika likiwemo jengo kuu la hospitali, wodi za wagonjwa, chumba cha kuhifadhia maiti pamoja na vitanda vya malazi na kujifungulia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto iliyopo ni upungufu wa wataalam pamoja na madawa, ambapo kwa hatua za awali Jeshi la Wananchi wa Tanzania tayari limeshawaandikisha madaktari 300 ambao wamepelekwa Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli na wanatarajiwa kutawanywa katika hospitali na vituo vya afya mbalimbali nchini, ikiwemo hospitali kuu ya kanda iliyopo 41KJ. Changamoto ya upungufu wa madawa itashughulikiwa kadri ya fedha zinatakavyopatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, 451KJ, ina kituo kidogo cha afya ambacho hutoa huduma ya kwanza kwa Maafisa, Askari, pamoja na raia waliopo jirani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shule inayozungumziwa hapa ni Shule ya Msingi ya Maji Maji iliyopo katika Kambi ya Jeshi 41KJ. Kwa nyakati tofauti Serikali imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu mbalimbali ya shule za msingi zikiwemo shule zilizopo katika maeneo ya Jeshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inaendelea kufanya mawasiliano na Wizara yenye dhamana ya kusimamia Shule za Msingi (TAMISEMI) ili ione uwezekano wa kutenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya Shule ya Msingi Maji Maji iliyopo katika Kambi ya Jeshi 41KJ Wilayani Nachingwea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha za bajeti zimekuwa hazitosherezi katika kufufua karakara hiyo, hivyo Jeshi la Wananchi Tanzania limeweka mikakati ya kufufua miundombinu ya karakana ili iweze kujiendesha kibiashara kwa ajili ya kulihudumia Jeshi na Wananchi kwa ujumla. Aidha, mchakato wa kuipeleka karakana hiyo katika ngazi ya VETA unaendelea chini ya Makao Makuu ya Jeshi.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA aliuliza:-

Shirika la Mzinga limekuwa likifanya kazi zake kwa weledi na uaminifu mkubwa lakini lina changamoto za vifaa kama vile mashine za ramani:-

Je, kwa mwaka 2019/2020 Serikali ilitenga kiasi gani cha fedha kwa ajili ya Shirika hilo?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maryam Salum Msabaha, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka wa Fedha 2019/2020, Shirika la Mzinga limetengewa jumla ya shilingi 2,000,000,000.00 kwa ajili ya kutekeleza Miradi ya Maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha shirika linatekeleza majukumu yake kwa ufanisi, shirika limeanza kutekeleza Mpango Mkakati wa Miaka Mitano (2017/2018 – 2021/2022) ambao unakusudia kupanua wigo wa uzalishaji wa mazao ya kijeshi. Aidha, shirika limepanga kuanzisha kiwanda cha kutengeneza baruti kwa ajili ya matumizi yasiyo ya kivita (civil explosives) na kupanua mradi wa kutengeneza mashine ndogo ndogo zitakazowezesha wajasiriamali kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na misitu.
MHE. KANALI (MST.) MASOUD ALI KHAMIS aliuliza:-

Serikali imekuwa ikijitahidi kujenga nyumba kwa ajili ya wapiganaji wake ili waishi kambini kama taratibu za Jeshi zinavyoelekeza:-

(a) Je, kwa nini sasa nyumba nyingi katika Kambi za Jeshi wanapewa wafanyakazi ‘Raia Jeshini’ kwa ajili ya kuishi?

(b) Je, wafanyakazi raia wana haki ya kupewa nyumba za kuishi za Askari?

(c) Je, kwa nini Askari wanaruhusiwa kuzihama nyumba zilizojengwa kwa ajili yao na kuhamia katika nyumba binafsi?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENA TAIFA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kanal (Mstaafu) Masoud Ali Khamis Mbunge wa Mfenesini, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, raia wanaofanya kazi Jeshini hupewa nyumba za kuishi kwa mujibu wa Kanuni za Majeshi ya Ulinzi ya Wananchi wa Tanzania. Aidha, ugawaji wa nyumba hizo unategemea na uwezo uliopo.

(b) Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni za Majeshi ya Ulinzi ya Wananchi wa Tanzania Juzuu ya kwanza (Utawala), Ibara ya 21.30 Makazi ya waliooa kutumia Raia, Kifungu Kidogo cha Kwanza (1) kinasema, bila kuathiri maagizo yoyote yaliyotolewa na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, wakati makazi yanayofaa ya kiraia hayapatikani, Kamanda wa Kituo, Kikosi au sehemu nyingine anaweza kumgawia makazi ya waliooa raia ambaye ni Mtumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye anajaza nafasi katika Muundo wa Jeshi na ambaye si kibarua.

Hali kadhalika, Juzuu ya Kwanza (Utawala) Ibara Ndogo ya Pili inaeleza kuwa, kwa idhini ya Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Kamanda Kituo Kikosi au sehemu nyingine anaweza kumgawia makazi ya waliooa raia, mbali na yule aliyetajwa katika sehemu ya kwanza ya aya hii, wakati kazi zake ni zile ambazo zinachangia ufanisi au maslahi ya kituo, kikosi au sehemu nyingine, endapo makazi yanayofaa ya kiraia hayapatikani anaweza kupewa nyumba kuwa makazi.

(c) Mheshimiwa Spika, Maafisa au Askari wanaruhusiwa kutoka kambini au vikosini na kuhamia katika nyumba zao binafsi. Aidha, hulazimika kubaki kambini au vikosini kutokana na sababu maalum za kimajukumu.
MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS Aliuliza:-

Kumekuwa na matukio ya watoto kuokota mabomu wakidhani ni vyuma chakavu na kisha kuwalipukia na kusababisha madhara makubwa ikiwemo vifo. Hivi karibuni watoto watano wamepoteza maisha na zaidi ya watoto 40 kujeruhiwa katika Shule ya Msingi Kihanga iliyopo Ngara Mkoani Kagera.

Je, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti na kukomesha tatizo hili?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA Alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Yussuf Haji Khamis, Mbunge wa Nungwi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo mengi duniani yanakabiliwa na changamoto ya kutapakaa kwa kwa silaha ndogo ndogo yakiwemo mabomu ya kutupwa kwa mkono. Pamoja na Tanzania kuwa ni nchi yenye amani, baadhi ya nchi zinazotuzunguka zimejikuta zikitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe. Hali hiyo imesababisha baadhi ya wakimbizi kukimbia na silaha yakiwemo mabomu ya kutupwa kwa mkono na kuyatekeleza baada ya kujiona wapo salama au kuwauzia wahalifu jambo ambalo limechangia kuwepo kwa mabomu hayo katika baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Kagera.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya vita vya Kagera, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania lilitoa elimu kwa wananchi kutookota vitu vinavyong’ara, vifaa vya chuma na pindi wanapoona vitu hivyo watoe taarifa Vituo vya Polisi au kwenye Kambi za Jeshi iliyo karibu. Kwa maeneo yaliyotiliwa mashaka wananchi walipewa tahadhari ya kutolima, kutopita au kulisha mifugo. Aidha, Jeshi la Wananchi lilipeleka Wahandisi wa Medani kukagua maeneo hayo na kujiridhisha kama yapo salama kwa wananchi kuendelea na shughuli zao za kawaida. Hivyo, inashauriwa wananchi katika mkoa huo na mingine kuendelea kuchukua tahadhari wanapoona vitu vyenye asili ya chuma.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA aliuliza:-

(a) Je, ni vijana wangapi kutoka Wilaya ya Kaskazini A na Wilaya ya Kaskazini B wamepata nafasi ya kujiunga na Jeshi kuanzia mwaka 2015?

(b) Je, mgawanyo wa idadi ya vijana wanaojiunga na Jeshi kwa kila wilaya nchini upoje?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Angelina Adam Malembeka Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita yaani kuanzia mwaka 2015 hadi 2018 vijana walijiunga na JKT kutoka Zanzibar kwa kujitolea ni kama ifuatavyo:-

(i) Mwaka 2015/2016 vijana 300;
(ii) Mwaka 2016/2017 vijana 300;
(iii) Mwaka 2017/2018 vijana 400 kwa hivyo jumla katika miaka hiyo mitatu ni vijana 1000.

Jukumu la kugawa nafasi hizo kwa wilaya liko chini ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Kwa mwaka 2019/20 Zanzibar imetengewa nafasi 500.

(b) Mheshimiwa Naibu Spika, mgawanyo wa idadi ya vijana wanaojiunga na JKT kwa kujitolea kwa kila mkoa huzingatia uwiano wa idadi ya watu kulingana na takwimu za sensa ya Taifa ya watu na makazi, elimu, jinsia na sifa nyingine zinazokuwa zimeainishwa na mkuu wa JKT. Zoezi hili ikiwa ni pamoja na mgawanyo wa vijana hadi ngazi ya wilaya huratibiwa na wakuu wa mikoa husika baada ya Makao Makuu ya JKT kuainisha idadi ya vijana kwa kila mkoa.