Answers to supplementary Questions by Hon. Dr. Hussein Ali Mwinyi (72 total)
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pia nashukuru kwa majibu ya Waziri na amekuwa mfuatiliaji sana wakati nauliza maswali yanahusu Vikosi vya Ulinzi na Usalama. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mipaka ya jeshi inalindwa na Wanajeshi wenyewe, je, ni kwa nini kuna vikosi ambavyo vinavaa nguo za jeshi na kulinda mipaka ya jeshi na kuchafua taswira ya Jeshi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Zanzibar, kipindi cha uchaguzi kumekuwa na vikosi vingi sana na vingine havina taaluma ya kutumia silaha na wamekuwa wakiwadhuru wananchi kwa silaha za moto na waliodhurika wengine ni wazee wakongwe wa miaka 60 na kuwapatia ulemavu wa kudumu. Je, Serikali ina mikakati gani kuunda Kamati Teule kukichunguza hiki kikosi cha Mazombe ili tutambue kwa mujibu wa sheria kimesajiliwa na Serikali ipi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mipaka ya Vikosi vya Jeshi inalindwa na Wanajeshi wenyewe, hakuna kikosi tofauti kinacholinda mipaka ya Vikosi vya Jeshi. Kwa hiyo, hilo wala asipate tabu ya kudhani kwamba kuna watu wanavaa sare za kijeshi lakini sio Wanajeshi, hapana. Wanaolinda mipaka hiyo ni Wanajeshi wenyewe na hakuna tatizo kama hilo katika mipaka ya Vikosi vya Jeshi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili la hicho anachokiita kikundi au kikosi cha Mazombe, sina taarifa ya kikosi hicho na kama jambo hilo linatokea Zanzibar, basi ingekuwa vyema swali lake alielekeze kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Hicho kikosi mimi sikitambui. (Makofi)
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na matatizo mbalimbali ambayo yamesemwa na muuliza swali lakini vilevile Askari hawa hasa wastaafu nao wana matatizo yao. Kule kwangu Rombo napofanya mikutano ya uhamasishaji, simalizi kuzunguka Jimbo bila kuona mkono wa Askari mstaafu au aliyepigana Vita vya Kagera au wale waliopigana Vita vya Pili vya Dunia, wakilalamika kutopewa haki zao kikamilifu. Swali langu ni kwamba, je, Wizara ina kauli gani juu ya Askari hawa ambao bado wanaendelea kulalamikia mafao yao? (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mafao kwa wastaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania au kwa majeshi yetu kwa ujumla yapo kwa mujibu wa sheria. Tunavyofahamu sisi ni kwamba Wanajeshi wote wenye stahili za kulipwa pensheni wanalipwa pensheni. Wapo wengine ambao hawakufikisha miaka ishirini ya utumishi, wao wanalipwa kiinua mgongo kwa pamoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, inawezekana hao wanaolalamika ni wale ambao walishalipwa kiinua mgongo lakini kutokana na ugumu wa maisha sasa hivi wamekuwa wakiomba waweze kufikiriwa. Ninachoweza kumueleza Mheshimiwa Mbunge ni kwamba, ni vyema tukapata majina maalum ya hao watu, tukaangalia case zao mmoja baada ya mwingine ili tuweze kuwasaidia kwa kadri itakavyowezekana.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kuwa Mkoa wa Geita ni mkubwa uliopo pembezoni mwa mikoa inayopokea wakimbizi na kuishi kwa wasiwasi kwa sababu ya nchi za jirani zenye machafuko. Ni lini Serikali inafikiria kuleta Kambi Rasmi ya Jeshi? (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Vikosi vya Jeshi vinapangwa kwa mujibu wa mahitaji ya kiulinzi. Kwa hiyo, zile sehemu ambazo zina mipaka au zile sehemu ambazo zina mahitaji maalum ya kiulinzi ndipo vikosi huwa vinapangwa. Hata hivyo, kwa sababu muda mrefu umepita toka waangalie utaratibu wa mpango wa vikosi katika nchi yetu, nakubaliana na Mheshimiwa Musukuma kwamba pengine wakati umefika wa kutuma timu za wataalam kwenda kuangalia endapo kutakuwa kuna ulazima wa kuweka vikosi sehemu hiyo. Ikithibitika kama hivyo ndivyo, basi tutashauriana ili waweze kuanzisha vikosi huko. (Makofi)
MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafsi hii, kwanza nishukuru sana kwa kuwepo kwangu hapa leo.
Mheshimiwa Waziri hizi ajira kwa upande wa kule kwetu Zanzibar zimekuwa hali ngumu kweli upatikanaji wake na ili uipate basi ufanye kazi ya ziada kubwa sana. Je, ni kwa nini Wizara yako isikae na Wizara husika ya Zanzibar ajira hiyo ipitie sehemu ya JKU peke yake?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, kwanza nataka nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara yangu imeshakaa na Wizara inayoshughulikia vikosi vya SMZ na katika mazungumzo yetu tumewaeleza kwamba sisi tutatoa nafasi za kujiunga na JKT kupitia Wizara hiyo. Na ni hiari yao wao Wizara hiyo inayoshughulika na vikosi kuamua endapo watawachukua vijana walioko JKU ili waje kujiunga na JKT au watazigawa kama wanavyozigawa sasa kupitia Wilaya na Mikoa.
Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, ninachosema ni kwamba kukaa tumeshakaa, uamuzi bado unabaki kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Nataka nifahamishe Bunge lako Tukufu kwamba, kuna idadi maalum isiyopungua vijana 300 kila mwaka, zinapelekwa kama nafasi za kujiunga na JKT kutoka Zanzibar.
Kwa hiyo, vijana hao huwa wanapatikana kwa njia tofauti Wilayani na Mikoani na hatimaye wakishajiunga na JKT wakati wa usaili wa vyombo vya ulinzi na Usalama vyote, Jeshi la Wananchi lakini pia Magereza, Uhamiaji, Polisi na kadhalika wanachukua vijana kutoka JKT na wale ambao wana sifa zinazotakiwa wanapata ajira katika vyombo hivyo.
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Spika ahsante, Mheshimiwa Waziri katika majibu yake alizungumza kwamba watu ni lazima watoke Zanzibar waingie katika Kambi za JKT ili waweze kuajiriwa, lakini nafikiri hilo ni tatizo.
(a) Je, Waziri anajua kwamba kuna suala kubwa la rushwa katika kupata ajira?
(b) Kuna wadowezi wanaotoka Maafisa wa Kijeshi walioko Zanziabar ambao wanatumia nafasi ambazo ziko allocated kwa Wazanzibari kuwapatia watu wao kutoka Tanzania Bara nafasi zile ambazo zimetengwa kwa Zanzibar?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, kwanza kuhusu suala la rushwa wakati wa usaili wa ajira, taarifa hizo mimi binafsi sijazipokea lakini namuomba Mheshimiwa Ally Saleh kama anao ushahidi wa kutosha wa kijana yeyote aliyeombwa rushwa, walete taarifa hizo na tutazifanyia kazi kwa kuchukua hatua stahili kwa wale wote ambao wanajihusisha na vitendo hivyo. (Makofi)
Kuhusu swali la pili la nafasi za Zanzibar kuishia kupewa watu wa Bara pia naweza kusema kwamba mimi sina taarifa na utaratibu tuliouweka ni mzuri sana, kwa sababu tunapopata nafasi 300 za vijana wa Zanzibar kujiunga na JKT, tunazikabidhi kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Ni wajibu wao kuhakikisha kwamba nafasi hizo wanazigawa vile ambavyo wanapenda.
Mheshimiwa Spika, taarifa nilizonazo mimi, ni kwamba kwa utaratibu wa sasa nafasi hizo zinagawiwa kwa Wilaya na Mikoa.
Kwa hiyo, Kamati na Ulinzi za Usalama za Wilaya na Mikoa wanatakiwa wahakikishe kwamba wao ndiyo wateuzi wa vijana hao, inatokeaje mtu wa Bara anakuja anachukua nafasi zile kuwapa watu wa Bara wenzake, hilo nadhani siyo sahihi na kama ni sahihi basi udhaifu huo uko kwa wale wanakabidhiwa nafasi hizo.
MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Spika nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Spika, majeshi yetu ni vyombo vya ulinzi na usalama, na ni vyombo ambavyo wote tunastahili kuviheshimu, lakini kwa muda sasa kumekuwa na utamaduni wa kuwatumia askari kutoka Bara kuwapeleka Zanzibar, kuwaandikisha Zanzibar wakati wa uchaguzi na kuwatumia kupiga kura katika mazingira ambayo hayapo wazi.
Je, Mheshimiwa Waziri una taarifa za upelekaji wa vikosi Zanzibar kwa jukumu moja tu la kupiga kura na kisha kurejeshwa Bara?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, kwanza tutambue kwamba majeshi yetu ni ya Muungano. Kwa maana hiyo, Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania anaweza kupangiwa kufanya kazi yake sehemu yoyote ya Jamhuri ya Muungano. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini kuhusu kuandikishwa kupiga kura, Mheshimiwa Mbowe nataka uelewe kwamba utaratibu wa kupiga kura Zanzibar unafahamika na uko wazi. Huwezi kwenda leo ukaandikishwa, ukapiga kura. Ili uweze kupiga kura, ni lazima uwe ni Mzanzibari mkaazi. Hiyo ipo na ushahidi tunao. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, ambacho tunaweza kusema hapa kwa ufupi ni kwamba wanajeshi wanapopelekwa Zanzibar ni kwa ajili ya kulinda usalama wakati wa uchaguzi.
MHE. MWANTAKAJE HAJI JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Waziri nina swali moja la nyongeza.
Je, nyumba hizo zilizojengwa ziko wapi na Mkoa gani unaendelea kujengwa hizo nyumba? Ahsante.
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, nyumba hizi ziko katika Mikoa mingi ya nchi yetu, kwa upande wa Zanzibar, nyumba wameanza kujenga upande wa Pemba, bado Unguja wataingia katika awamu ya pili. Kwa hiyo, orodha ya Mikoa ni mingi siwezi kuorodhesha yote hapa, lakini nitakuwa tayari kumpatia Mheshimiwa Mbunge kwa maandishi endapo atahitaji.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kweli majibu yaliyopatikana leo, ni dhahiri kabisa hata Serikali haijui mipaka ya Kata. Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amekiri kwa kinywa kwamba wanatwaa ardhi kwa kufuata Sheria ya mwaka 1999 na kwa kuwa JWTZ hawakufuata sheria, mwanzoni waliomba hifadhi ya miezi mitatu katika Kata ya Nkende, walivyopewa wakaamua kuhodhi na Kata ya Nyamisangura na Nkende na Nyamisangura, siyo eneo la Nyandoto. Kikosi cha Jeshi kinatakiwa kukaa Kata ya Nyandoto na siyo Nyamisangura na Nkende.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa sababu hawakufuata Sheria ya mwaka 1999, kama alivyotamka mwenyewe, haoni sasa kwamba ni dhahiri wananchi hawa wanatakiwa kuhodhi maeneo yao kama mlivyoyateka mwaka 2008 mpaka sasa hivi, mwaache waendeleze shughuli zao za kiuchumi?
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, Waziri anasema kwamba wanaenda kukamilisha utathmini, ifahamike kwamba waliwazuia wananchi hawa kufanya shughuli za maendeleo kuanzia mwaka 2008, hawafanyi shughuli zozote za maendeleo. Sasa hiyo tathmini ambayo Waziri anakiri kwamba anaenda kuikamilisha mwaka huu, napenda kujua na wananchi wa Tarime wajue kwamba mtazingatia hali halisi ya mwaka 2007, ambapo Wanajeshi hao waliwakataza wananchi wasifanye shughuli zozote za maendeleo; nyumba zimebomoka, vyoo vimebomoka, mashamba yameshakuwa chakavu sasa hivi ni ardhi tu; huo utathmini ambao mnaenda kuufanya sasa hivi, unazingatia vigezo vipi? Ahsante.
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, tunakiri kwamba wananchi walizuiliwa kuendelea na shughuli za uchumi kwa sababu ya kuweka Kiteule cha Jeshi.
Napenda Mheshimiwa Mbunge aelewe kwamba amani na usalama katika eneo nalo ni muhimu kwa ajili ya shughuli za uchumi. Kwa hiyo, maelewano yalifanyika kwamba wananchi wapishe Jeshi hapo kwa ajili ya shughuli za usalama ili na wao waweze kupata fidia.
Kwa hiyo, hatua tuliyofikia ni nzuri naweza nikasema, kwa sababu sasa tunasema kwamba fedha za uthamini zimeshapatikana na zimeshatumwa kwenye Halmashauri. Ni jukumu la Halmashauri kukamilisha uthamini ili wananchi hao waweze kulipwa fidia inayostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kuhusu tathmini kuchukua viwango vya mwaka 2007 au sasa, kwa mtazamo ni kwamba viwango vya sasa vitakuwa vikubwa zaidi kuliko mwaka 2007.
Kwa hiyo, tunachosema tu ni kwamba, kwasababu uthamini huu unafanywa kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya, ni vyema Mheshimiwa Mbunge ukashirikiana na Halmashuri yako pamoja na watendaji wa Wizara yangu ili kuweza kupata tathmini stahiki bila ya mtu yeyote kuonewa. Kama kweli kuna nyumba ambazo zilikuwepo ambazo zimebomoka, tutalizingatia hilo ili kila mtu aweze kupata fidia yake anayostahili.
MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED: Mheshimiwa Spika, ahsante sana pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri lakini pia sikuridhika sana na majibu yake ambayo ameyatoa ya kubahatisha zaidi. Tunao ushahidi wa kutosha kabisa mpaka wahanga waliopigwa na kunyang‟anywa samaki wao wavuvi na JW (Jeshi la Wananchi) sasa sijui Mheshimiwa Waziri na kisingizio hapa ni license zinazotumika wanadai kwamba sizo.
Mheshimiwa Spika, sasa swali langu la kwanza katika swali la nyongeza ni aina gani ya license zinazotakiwa kutumika na wavuvi hawa?
Swali la pili, je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kufuatana na mimi tukamuonesha wale wahanga ambao walipigwa na wakati mwingine walinyang‟anywa samaki wao, matendo haya yanafanyika zaidi katika bahari ya Kigamboni na Kunduchi? Ahsante sana.
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, kwanza niseme kwamba niko tayari kufuatana na Mheshimiwa Mbunge kwenda kuwaona hao ambao inasemekana ni wahanga wa kipigo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini napenda nirudie yale niliyoyasema kwenye jibu langu la msingi kwamba kwa kuwa nchi hii inafata utawala wa sheria ni vema basi Mheshimiwa Mbunge anapopata tuhuma kama hizo akazifikisha sehemu husika.
Mheshimiwa Spika, siyo vema suala kama hili tulisikie mara ya kwanza ndani ya Bunge, sisi tupo, ofisi zetu zipo, Mheshimiwa Mbunge alipaswa kutufikishia ili tufanye uchunguzi na pale inapothibitika tuchukue hatua stahili, ningependa tuende kwa mwendo huo zaidi.
Mheshimiwa Spika, kuhusu ni aina gani za leseni niseme tu kwamba hili ni suala ambalo liko chini ya Wizara inayohusika na masuala ya uvuvi. Wanajeshi wanajukumu moja la kuhakikisha kwamba wavuvi hawatumii njia za uvuvi wa haramu basi, siyo suala la kuangalia leseni, leseni ina mamlaka zake.
Mheshimiwa Spika, hivyo, tunachoweza kusema hapa ni kwamba yanapotokea matukio kama haya toa taarifa ili tufanye uchunguzi na kuchukua hatua zinazostahili.
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza.
Kwa kuwa Wanaochaguliwa kwenda JKT kwa sifa za chuo kikuu na form six ni wachache kwa baadhi ya maeneo hasa Mkoa wa Pwani; je, Mheshimiwa Waziri yupo tayari kwamba nafasi hizi zichukuliwe na vijana wanaomaliza kidato cha nne ili kuweza kukabili ongezeko la vijana hao? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa vijana hawa wanaokwenda JKT baada kuhitimu, wengi wao wakirejea katika maeneo wanakosa ajira wakati wanakuwa na ujuzi, lakini wanashindwa kujiajiri kutokana na kutokuwa na mitaji ya kutosha; je, Wizara ipo tayari kufanya tathmini ili kuweza kuwawezesha hasa vijana ambao wameonesha vipaji katika makambi hayo? Ahsante.
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nataka nieleze tu kwamba wale vijana wanaokwenda kwa mujibu wa sheria ni wengi kuliko uwezo wa Serikali wa kuwachukua kwa sasa, yaani wanaomaliza form six kabla ya kwenda kujiunga na vyuo idadi yao ni kubwa mno kiasi cha kwamba kwa uwezo wa sasa hatuwezi kuwachukua wote, ndiyo maana baadhi tu wanachukuliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, siyo sahihi kwamba wanaokwenda ni wachache.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili; na hii niseme kabla sijaingia kwenye swali la pili, kwamba Serikali inaendelea kujipanga kuongeza kambi, kuongeza majengo ndani ya makambi ili hatimaye tuweze kuchukua vijana wote wanaomaliza form six kabla ya kwenda kujiunga na vyuo waweze kupita katika Jeshi la Kujenga Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili, ni kweli kwamba kwa wale wanaokwenda kwa kujitolea ambao idadi yao ni kubwa, ni zaidi ya vijana 5,000 kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, siyo wote wanaopata nafasi ya kuajiriwa ndani ya vyombo vya ulinzi na usalama. Kwa kiwango kikubwa kama tulivyosema wakati wa bajeti yangu, takriban asilimia 71 ya vijana hao, wanapata ajira kwenye vyombo vya ulinzi na usalama, lakini asilimia iliyobaki wanalazimika kurudi nyumbani kwa sababu hakuna uwezo wa kuwaajiri wote.
Kwa hiyo, nakubalina na wazo la Mheshimiwa Mbunge kwamba ni lazima sasa tufanye utaratibu wa kuwawezesha vijana hawa ili wanaporudi waweze kujitegemea, kujiajiri wao wenyewe. Utaratibu huu umeshaanza kupangwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ili vijana hawa waweze kupatiwa mitaji na kwa kuwa wana ujuzi fulani wanaotokanao JKT waweze kujiajiri wao wenyewe.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Hivi karibuni JKT wametangaza nafasi za vijana wanaomaliza form six na wametangaza nafasi 1,500 mpaka 2,000. Nimemsikia Mheshimiwa Waziri anasema uwezo wao ni kati ya 5,000 mpaka 7,000. Nataka kufahamu, sasa ni mpango upi mwingine wa Wizara hii kuhakikisha kwamba hao zaidi ya 20,000, ambao hawajapa nafasi wanakwenda?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nieleweke kwamba kuna vijana wanaojiunga na JKT wa aina mbili. Kuna vijana tunaowaita wanajiunga kwa mujibu wa sheria, ni wale ambao wamemaliza form six kabla ya kujiunga na vyuo vikuu. Vijana hawa idadi yao tuliyoichukuwa mwaka huu ni 14,000 na sio wote ambao tunaweza kuwachukuwa kwa sababu waliohitimu form six ni wengi zaidi ya hapo, kwa hiyo, tunaendelea kujenga uwezo ili tuweze kuwachukuwa wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, wale vijana 5,000 mpaka 7,000 niliozungumzia, hao ni vijana wanaoingia kwa kujitolea, ambapo idadi yao ndiyo hiyo. Kwa hiyo, niseme tu kwamba hawa wa mujibu wa Sheria, idadi yao ni kubwa zaidi ni 14,000 na wanakaribia kuanza ndani ya wiki moja ili waweze kupata mafunzo hayo ya Jeshi la Kujenga Taifa.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ahsante naomba kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa makubalinao hayo yalifikiwa mwaka 2011 na sasa ni miaka sita, na tatizo hili limeendelea kuwepo; je, ni lini sasa kwa uhakika kabisa Serikali itaenda kumaliza huu mgogoro uliopo kati ya wananchi na eneo hilo la Jeshi?
Swali la pili, kwa kuwa migogoro hii ya mipaka ya Jeshi na maeneo ya wananchi haipo tu Monduli, iko katika maeneo mbalimbali kwa sababu mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, nafahamu kumekuwa na mgogoro huu katika maeneo mengi ambapo Jeshi ina kambi zao. Sasa ni lini kwa uhakika Serikali itatuletea taarifa hapa Bungeni kwamba ina mkakati huu wa kwenda kumaliza matatizo hayo?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba mgogoro huu ni wa siku nyingi na kwamba sasa hivi wakati umefika upatiwe ufumbuzi wa kudumu.
Mheshimiwa Spika, nilieleze Bunge lako Tukufu kwamba katika mwaka huu wa fedha, bajeti ya Wizara yangu ilitenga shilingi bilioni 12 kwa ajili ya shughuli za uthamini, upimaji na ulipaji wa fidia katika maeneo mbalimbali. Kwa hiyo, tukianza kupata fedha hizo hususan tatizo dogo kama hili la kuhuisha tu mipaka litashughulikiwa mara moja.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili la kwamba migogoro hii iko mingi na lini taarifa italetwa, nataka nikiri kwamba sehemu nyingi za nchi yetu migogoro baina ya vijiji na Kambi za Jeshi ipo na kama nilivyosema awali tatizo ni fedha za kufanya uthamini kwa yale maeneo ambayo hayajathaminiwa, fedha za kufanya upimaji kwa maeneo yanayohitaji kupimwa na fedha za kulipa fidia kwa maeneo ambayo Jeshi linatakiwa kufidia.
Mheshimiwa Spika, ikumbukwe pia kwamba kuna maeneo mengi ambayo wananchi ndiyo wameingia katika maeneo ya Jeshi. Kwa hiyo, inabidi waelekezwe, waelimishwe wasiwe wanavamia maeneo ya Jeshi. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba tutakapoanza tu kupokea hizi fedha, kazi zote hizi nilizozitaja zitaanza kufanywa ili tuondoe migogoro hii inayokabili Jeshi letu na wananchi.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, suala la Monduli linafanana na suala la Makambako.
Mheshimiwa Spika, Makambako kuna eneo linaloitwa Kipagamo ambalo miaka ya huko nyuma wananchi waliipa Jeshi kwa ajili ya matumizi ya shabaha. Maeneo hayo sasa tayari wananchi tumejenga shule na tayari kuna makazi ya watu na matumizi hayo sasa hayatumiki kama ambavyo yalivyokuwa yamekusudiwa huko nyuma kwa sababu pana shule na makazi ya watu.
Je, Serikali haioni sasa iko haja ya kuwarudishia wananchi eneo lile ili liendelee kutumika kwa shule na makazi ya watu na kwa sababu barua tulishaiandika kupitia Serikali ya Kijiji na nilimpa mwenyewe Waziri mkono kwa mkono, je, ni lini sasa Serikali itarudisha eneo hilo hilo liendelee kutumika kwa wananchi? Nakushukuru. (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, kwanza nikiri kwamba barua hiyo Mheshimiwa Mbunge alinikabidhi na nimeipokea na mimi nilichofanya ni kuipeleka Makao Makuu ya Jeshi ili wanipe maoni juu ya suala hilo. Ikumbukwe tu kwamba maeneo yaliyotolewa kwa ajili ya Jeshi yalipangiwa kazi za Jeshi, kwa hiyo inawezekana kwamba eneo hili sasa hivi halitumiki tena kwa shabaha kutokana na ukaribu wake na makazi ya watu lakini huenda linashughuli nyingine za kijeshi.
Mheshimiwa Spika, namuomba Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa hapo wavute subira tupate maoni ya Jeshi kuhusu eneo hili, ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa na ni imani yangu kwamba maoni hayo nitayapata muda siyo mrefu. (Makofi)
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kunipa nafasi ya kuuliza swali moja dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, taarifa ya utekelezaji wa ahadi za Serikali mwaka 2006 (miaka kumi iliyopita), Serikali iliahidi kuyapima, kutathmini na kutoa fidia maeneo kadhaa na ndani ya maelezo hayo maeneo yote mliyaeleza mkaainisha katika kitabu ambacho mlitupatia.
Swali linakuja, inakuwaje leo ndani ya muda wa miaka kumi Serikali haijaona umuhimu, ahadi zenu ambazo mlituambia maeneo hayo mtayapima, kutathmini na kutoa fidia na baadhi ya wameshakufa katika maeneo hayo; je, Serikali ina nia njema kulipa fidia wananchi hao? (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema awali na kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge, ni kweli kwamba tumeorodhesha maeneo yote yenye migogoro na tumeyaorodhesha maelezo ya nini kinachohitaji kufanyika. Yapo maeneo ambayo yanahitaji kwanza kufanyiwa tathmini ya fidia, yapo yanayohitaji kupimwa, yapo yanayohitaji kutolewa fidia lakini yako vilevile kama nilivyosema awali yale ambayo wananchi walivamia na hawastahili kuwa hapo. Na ukweli wa mambo ni kwamba fedha zinazohitajika ni nyingi, kila mwaka tumekuwa tukitenga katika bajeti yetu, fedha kiasi fulani ili kupunguza awamu kwa awamu mpaka tumalize. Kwa bahati mbaya sana kama mnavyofahamu Waheshimiwa Wabunge ni kwamba fidia ni gharama kubwa. Mheshimiwa Spika, maeneo mengi wananchi wamejenga na kila nyumba ina thamani yake, kwa hiyo kuweza kulimaliza hili tatizo haraka ni vigumu kwasababu ya uwezo wenyewe wa kifedha. Tunachoweza kuendelea kusema ni kwamba kila mwaka, mwaka huu wa fedha tumetenga shilingi bilioni 12, zikipatikana tutaanza sehemu moja baada ya nyingine ili kuweza kuondoa hili tatizo la muda mrefu. Mara nyingi nimekuwa nikisimama hapa nikijibu suala la migogoro ya ardhi kati ya Jeshi na Wananchi lakini ningependa kutoa wito vilevile kwa Waheshimiwa Wabunge kwamba tusaidiane.
Mheshimiwa Spika, zamani Jeshi lilikuwa lina maeneo makubwa sana. Kwa sababu ya uhaba wa ardhi, wananchi sasa hivi wamekuwa wakivamia maeneo hayo. Kwa hiyo, yale maeneo yote ya Jeshi yaliyovamiwa ambayo wananchi hawastahili kuwa hapo ni vema wakatoka katika maeneo hayo na sisi kama Serikali, wale ambao wanastahili ya kulipwa fidia tutaendelea kuwalipa kadri uwezo utakavyokuwa unaruhusu.
MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimwulize swali moja la nyongeza Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vita dhidi ya ukoloni ilikuwa imegawanyika katika maeneo mawili; kulikuwa na vita ambayo ilipiganwa na viongozi wetu wa jadi kabla ya kuingia kwa ukoloni ambapo walikuwa wana-resist ukoloni usiingie, lakini kulikuwa na Vita ya Maji Maji ambayo ni vita pekee iliyopiganwa wakati tayari Wakoloni wanatawala Tanganyika na sehemu ya nchi yetu. Kwa hiyo, Vita ya Majimaji ni tofauti na hivyo vingine alivyovitaja Mheshimiwa Waziri kwenye majibu yake ya msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile ukienda kwenye Hospitali ya Wilaya pale Kilwa, kuna orodha ndefu ya wazee wetu waliopoteza maisha tena kwa kunyongwa kutokana na Vita hivi vya Majimaji. Kwa hiyo, nataka kujua orodha ile ya wazee ambayo imewekwa pale kwenye Hospitali ya Kilwa, inatunufaishaje sisi wakazi wa Kilwa na Lindi kwa kujua tu kwamba hawa walinyongwa kwenye vita dhidi ya Ukoloni?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyo kwa vita vingine vyote, kumbukumbu huwa zinawekwa na siyo ya Majimaji tu, ukienda katika nchi yoyote iliyopigana vita, utakuta kuna makaburi ya mashujaa na kuna majina yao kama kumbukumbu za kivita. Hoja yangu katika jibu langu la msingi ni kwamba hatupaswi kama Wazalendo kuomba fidia kwa kuitetea nchi yetu. Hii siyo kwa Maji Maji tu, hata kwa Vita vya Kagera watu walipigana; watu wamepoteza maisha; tumeweka makaburi ya mashujaa kwa wale waliokwenda kukomboa Afrika nje ya nchi. Kwa hiyo, tunachosema ni kwamba tutawakumbuka kama mashujaa na tutaendelea kuwaenzi na kuweka kumbukumbu ya kivita, lakini siyo rahisi kuwalipa fidia kwa sababu walikuwa wanajitolea kwa ajili ya nchi yao; na hii imefanywa na wengi ikiwemo Vita vya Kagera. Hakuna aliyelipwa fidia, bali tunawaenzi kwa kazi nzuri waliyoifanya kuilinda nchi yetu.
MHE. TUNDU A. M. LISSU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Naomba niulize swali la nyongeza. Mwaka 2013 nilitembelea Kumbukumbu ya Vita ya Majimaji, iko Songea na ni vizuri sana kwamba angalau tumeweka kumbukumbu ya mashujaa waliopigana Majimaji; isipokuwa katika Kumbukumbu ya Mashujaa wa Majimaji kuna watu mle ambao wamepewa heshima kwenye kumbukumbu ambao hawakuwa wamezaliwa wakati Majimaji inapiganwa. Chumba kikubwa kabisa kwenye Kumbukumbu ya Maji Maji kinamhusu Laurence Mtazama Gama ambaye hakupigana Majimaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tumejenga Kumbukumbu ya Majimaji ili kumkumbuka Laurence Gama au kukumbuka waliokufa kwa sababu ya Majimaji?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, madhumuni ya kumbukumbu za mashujaa ni kuwakumbuka wale walioshiriki katika vita husika. Kwa hiyo, hii taarifa ya kwamba kuna mtu ambaye amewekwa kama kumbukumbu wakati hakushiriki, pengine imetokana na kwamba kumbukumbu hiyo inajumusiha zaidi ya mashujaa wa Majimaji. Inawezekana kuna mashujaa wengine ambao wanajumuishwa. Kwa hiyo, naomba nipate fursa hii tuliangalie vizuri suala hili ili tuweze kulitolea jibu la uhakika zaidi.
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Waziri, lakini pia kukishukuru Kiti chako kwa sababu swali hili nililileta kwa mara ya kwanza halikupata majibu muafaka ya Serikali. Kwa majibu haya kidogo napata faraja kwamba ndugu zangu wale wa Kilwa watakwenda kupata fidia kutoka Serikali ya Ujerumani chini ya usimamizi wa Serikali ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri pia Serikali katika suala hili kwamba wenzetu wa Kenya waliendesha mchakato wa kudai fidia za waathirika wa Vita ya Maumau na Serikali ya Uingereza ikatoa fidia kwa waathirika wale. Kwa hiyo, nishauri Serikali nayo ikajifunze kutoka Kenya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nina maswali mawili ya nyongeza. La kwanza, kwa kuwa historia ya Vita ya Majimaji imechanganywachanganywa na kuvurugwa; na kwa kuwa Taifa hili limedanganywa eti kwamba Kinjekitile Ngwale ndiyo kiongozi wa Vita ya Majimaji. Ukweli ni kwamba Kinjekitile Ngwale siyo kiongozi wa Vita ya Majimaji na kiongozi wa Vita ya Majimaji ni Sikwako Mbonde na majemedari wake Ngumbalio Mandai, Lindimio Machela, Ngumbe-kumbe Mwiru na wengine. Serikali iko tayari sasa kufanya utafiti wa kihistoria ili basi kuwaeleza Watanzania ukweli wa jambo hili? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa misingi hiyo ya kuchanganya historia ya Vita ya Majimaji, sherehe za kumbukumbu za Mashujaa wa Vita ya Majimaji kila mwaka zinafanywa Majimaji Songea badala ya kufanywa Nandete Kipatimu. Serikali iko tayari kuhamisha sherehe zile kutoka Majimaji Songea kwenda Nandete Kipatimu ambako ndiko chanzo cha Vita ya Majimaji?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nataka nikubaliane naye kuhusu ushauri anaoutoa kwamba Tanzania ikajifunze kutoka Kenya kwa sababu Wakenya waliweza kudai fidia ya Vita vya Maumau na waliweza kupata fidia hiyo, tunakubaliana naye na tutafanya hivyo ili tuweze kujua wenzetu wanafanyaje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili la kufanya utafiti wa kihistoria ili kupata ukweli wa vita hii na uongozi wake na kadhalika nao ni ushauri mzuri, tunaupokea tutafanya kazi hiyo. Sasa ni hapo baada ya kupata ukweli huo, ndiyo hilo swali lake la tatu litaweza kupata jibu muafaka. Kwa sababu siwezi kulijibu sasa mpaka pale historia itakapopatikana na ukweli ukajulikana ndipo tutaweza kulizungumza hilo swali lake la tatu.
MHE. RIZIKI S. MNGWALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, actually swali langu lilikuwa ni nyongeza kwa hapo kwamba katika hiyo historia kinachogombewa zaidi katika kumbukumbu ni ile orodha sahihi ya majina ya mashujaa wetu wale ili waenziwe kwa namna inavyostahiki. Kwa hiyo, nyongeza yangu ilikuwa, je, Serikali katika huo utafiti wake itatuletea pia orodha sahihi ya mashujaa hawa?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tumeshakiri kwamba tuko tayari sasa kufanya utafiti wa historia, kwa hivyo, orodha kamili itakayopatikana italetwa kama Mheshimiwa Mbunge anavyotaka.
vya Majimaji ni Mahenge ambako takribani Watanzania wakati ule Watanganyika 30,000 waliuawa kwa njaa kwa sababu wanajeshi wa Ujerumani walichoma chakula cha Watanzania ili wasiweze kuishi na kufa jambo ambalo kwa tafsiri za kivita ni sawasawa na genocide.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tayari Serikali ya Ujerumani imeomba radhi na kulipa fidia kwenye Vita ya Namaqua na Herero Namibia, Serikali sasa katika mapendekezo ambayo imeyakubali kutoka kwa Mheshimiwa Mbunge itapeleka kwa Serikali ya Ujerumani pamoja na ombi la kuomba radhi rasmi kwa mauaji ambayo wanajeshi wake waliyafanya Tanzania?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri kabisa kwamba mifano ya nchi zilizoomba fidia kwa vita vilivyotokea kipindi cha ukoloni ni mingi, hapa tumetajiwa Kenya, lakini sasa tunaambiwa Namibia. Kwa hivyo, nitawaomba wenzetu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakati wanataka kuanza rasmi taratibu hizi ili tuweze kupata hiyo fidia basi wawasiliane na nchi hizi ili kujua wameanzaje na hatimaye tuweze kupeleka hilo ombi rasmi. Wakati huohuo nataka nikubaliane na Mheshimiwa Zitto kwamba, pamoja na fidia, kama itathibitika kwamba kulikuwa kuna mambo yaliyofanyika ambayo yanaashiria genocide, basi Serikali hiyo iweze kuomba msamaha vilevile.
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Wanaokwenda kwenye maeneo hayo ambako ni kwa kulinda amani mara nyingi hukutana na kujeruhiwa au kufariki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na hapa Tanzania
tumeshuhudia wanajeshi hao wakirudi wakiwa wamefariki na wengine wakijeruhiwa. Je, Serikali, hasa kwenye watu waliofariki, ina utaratibu gani ambao unafanya familia za wanajeshi hao, wapiganaji haokuendelea na maisha baada
ya bread winner wao kufariki? Hilo la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili, Mheshimiwa
Waziri umezungumza hapa kuna matatizo wakati wa kutayarisha vikosi, lakini mimi naona hii ni fursa.
Je, Serikali haioni kwamba, kuna haja ya kujifunza na kutafuta utaalamu kutoka nchi ambazo zime-specialize katika masuala ya kulinda amani, ili iwe ni fursa ya kufungua kituo (centre) ya ku-train watu kwa ajili ya kulinda amani kwa
ajili ya eneo hili la Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika? Ahsante.
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba katika baadhi ya maeneo ya ulinzi wa amani huwa vinatokea vifo na pengine pia huwa watu wanajeruhiwa, lakini upo utaratibu madhubuti
wa kuwafidia kwa yote mawili. Nitoe tu taarifa kwamba kwa wale ambao wamepoteza maisha katika ulinzi wa amani Umoja wa Mataifa wenyewe unafidia na wanaporudishwa hapa familia zao zinapata maslahi yao yote kwa mujibu wa utumishi ambao mhusika alikuwa ameutekeleza hapa nchini.
Kwa hiyo, katika hili hakuna mgogoro, fidia huwa
zinatolewa kama utaratibu unavyotaka kwa wote
waliojeruhiwa pamoja na wale waliopoteza maisha kwa pande zote mbili, Umoja wa Mataifa na Serikali na Jeshi la Wananachi wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa kujifunza kutoka maeneo mengine juu ya ulinzi wa amani; nataka nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba, hapa Tanzania tunacho chuo cha ulinzi wa amani. Tumepata msaada kutoka kwa Serikali ya Canada, wamekijenga na mara nyingi tunatoa mafunzo, si kwa Watanzania peke yao, ikiwemo na nchi nyingine za Afrika Mashariki wanakuja hapa kujifunza mafunzo haya ya ulinzi wa amani kwa hiyo, hili halina tatizo, tunaendelea vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jibu langu la msingi, nililosema ni upungufu wa fedha za matayarisho, si suala la mafunzo, mafunzo yapo na chuo tunacho na mafunzo yanaendelea pale kama kawaida.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri nina maswali mawili ya nyongeza. Kwanza, kwa kuwa utaratibu aliousema ulishawahi kufanyika katika wilaya mbalimbali hapa nchini na baadaye tukaambiwa utaratibu huo umesitishwa, je, ni lini zoezi hilo litaanza tena ili vijana waweze kujiunga na Jeshi?
Mheshimiwa Spika, pili, ni nini kauli ya Serikali juu ya ajira ya Jeshi kwa vijana wenye maadili mema na uwezo katika Mkoa wa Kaskazini Unguja na Tanzania kwa ujumla?Ahsante.
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, utaratibu niliousema haujasitishwa, bado utaratibu huu unatumika, kila mwaka tunachukua vijana kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa kupitia katika wilaya na mikoa yao. Kwa hiyo, utaratibu huo bado unatumika. Mwaka huu tumefanya zoezi hilo mwezi Desemba na tunategemea tutakapopata fedha baada ya bajeti basi awamu inayofuata utaendelea.
Mheshimiwa Spika, kuhusu vijana anaowazungumzia Mheshimiwa Malembeka, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, ni kwamba tutakapotangaza tena kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa, nitawaomba vijana hao waombe kupata nafasi za kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa na ajira kwenda Jeshi la Wananchi zinapitia katika Jeshi la Kujenga Taifa. Si Jeshi la Wananchi peke yake, kwa sasa vyombo vyote vya ulinzi na usalama vimeamua kwa makusudi kwamba ajira zao zipitie JKT. Kwa hiyo Polisi, Magereza, Uhamiaji, Usalama wa Taifa, Jeshi lenyewe la Wananchi wa Tanzania wote wanachukua vijana waliopitia Jeshi la Kujenga Taifa, kwa hiyo nitawaomba wajiunge huko ili hatimaye waweze kupata ajira hizo.
MHE. KAPT. GEORGE H. MKUCHIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nasubiri ruhusa yako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake ambayo si mazuri sana kwa mustakabali wa maendeleo ya nchi yetu. Hata hivyo, kabla sijauliza maswali yangu mawili ya nyongeza, nataka niwapongeze Waheshimiwa Wabunge vijana wa Bunge la 10 ambao kwa hiari yao walijiunga na mafunzo ya Jeshi la kujenga Taifa, walionesha kwamba kuongoza ni kuonesha njia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali yangu ya nyongeza ni kama ifuatavyo:-
Kwa kuwa Baba wa Taifa alituandalia akafanya JKT kama ndiyo jando, mahali pa kuwafunda, kuwaandaa vizuri vijana wa Tanzania kimaadili, kiuzalendo na kiulinzi; na kwa kuwa sasa inaonekana vijana wengi hawaendi tumeporomoka kutoka asilimia 75 mpaka mwaka huu 23. Je, kwa kutokuwapeleka hawa vijana JKT, Serikali haioni kwamba inachangia kuwaunda vijana ambao hawana maadili, legelege, ambao hawana uzalendo katika nchi yao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa changamoto zilizoelezwa na Wizara nimezipitia zote ziko ndani ya uwezo wa Serikali. Je, Serikali inaweza kuliahidi Bunge hili kwamba itaunda kikosi maalum cha kupitia changamoto hizi, kuziondoa na kuhakikisha kwamba vijana wote wanakwenda Jeshi la Kujenga Taifa kwa mujibu wa Sheria na kwamba hata kama ikibidi kuomba pesa walete maombi hapa Bungeni; kwa sababu Watanzania tuna uzoefu wa kushughulikia matatizo mbalimbali kaa UPE; na kama mwaka wa jana tulivyopeleka watoto wote kutoka darasa la kwanza mpaka form four wamekwenda bila malipo? Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba vijana ambao hawapati fursa ya kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa, kwa kweli hawawezi kuwa sawa kimaadili na kiuzalendo kama wale ambao wamepitia Jeshi la Kujenga Taifa. Hata hivyo, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi ni kwamba Serikali ina nia na dhamira kubwa ya kuhakikisha kwamba vijana wote wanaomaliza kidato cha sita wanajiunga na Jeshi la Kujenga Taifa, lakini tunakabiliwa na changamoto kama nilivyoziorodhesha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli nakubaliana na Mheshimiwa Mkuchika, kwamba wakati umefika wa kuunda kikosi kazi cha kupitia changamoto zote hizi au tuseme kufanya mikutano na wadau wote kwa sababu moja ya tatizo kubwa ni mihula ya masomo. Wale wanaoanza Chuo Kikuu wanaanza mwezi Septemba jambo ambalo linasababisha tusiweze kuwachukua vijana hawa wote wengine wanakuwa wameshaanza masomo. Kwa maana hiyo ni kukaa pamoja kuangalia ni jinsi gani tunaweza tukafanya marekebisho ya mihula hii, aidha vyuo vikuu au muda ule wa kumaliza form six ili vijana wote waweze kupitia JKT angalau kwa miezi mitatua ambayo inatolewa sasa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine kubwa ni changamoto ya rasilimali fedha. Jambo hili limekuwa ni kikwazo kikubwa, tutaendelea kuomba bajeti mwaka hadi mwaka ili kuziondoa na wakati huo huo tunajipanga ili JKT liweze kujitegemea. Nadhani hiyo ndiyo njia nzuri zaidi ya kuhakikisha vijana wote wanapita huko.
MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Pamoja na majibu aliyoyatoa Mheshimiwa Waziri, takwimu zinaonesha ukweli kwamba changamoto alizozizungumza zinasababisha kupeleka vijana wachache ukilinganisha na idadi ya vijana wanaomaliza kidato cha sita. Nataka kujua, kutokana na ufinyu huo, ni vigezo gani hivi sasa wanavyovitumia katika kuteua vijana wa kwenda kwenye mafunzo haya na wale wasiokwenda watawafanyaje sasa?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hakuna vigezo maalum vinavyotumika isipokuwa tunachofanya ni random selection. Kwa maana hiyo katika kila shule wanachaguliwa vijana wachache kwa utaratibu wa random. Kwa hiyo, wale wote ambao wanachaguliwa ni wale waliopatikana kwa utaratibu huo; hakuna vigezo maalum kwa sababu wote wanastahili kuchukuliwa, lakini ni kwa sababu ya muda na rasilimali fedha ambazo nimezizungumza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni kwamba kwa wale ambao hawajapata fursa ya kwenda huko, kwa sasa hivi hakuna utaratibu wowote uliopangwa, ni matumaini yetu kwamba uwezo ukiongezeka wa kuweza kuwachukua hata wale ambao wamemaliza vyuo vikuu, basi tutafanya hivyo wakati ukifika.
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Je, Serikali haioni umuhimu wa kugeuza Kambi za JKT kuwa vyuo vya VETA ili pamoja na mafunzo ya Kijeshi, vijana pia hasa wale wa kujitolea waweze kupata mafunzo ya ufundi? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa sasa, hususani kwa wale vijana wanaoingia kwa kujitolea yana awamu mbili, kuna mafunzo ya Kijeshi ya miezi sita ya kwanza na baada ya hapo kuna mafunzo ya Stadi za Kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa Jeshi la Kujenga
Taifa linafanya utaratibu wa kupata usajili wa VETA ili waweze kutoa vyeti hivyo kwa wale wanaomaliza pale JKT. Kwa hiyo ni kwamba, Stadi za Kazi zinatolewa, zitaendelea kutolewa na usajili unatafutwa ili hatimaye vijana wanaomaliza pale siyo tu wawe wamemaliza JKT bali pia waweze kupata vyeti vya VETA. (Makofi)
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa katika majibu yake Mheshimiwa Waziri amesema kwamba changamoto kubwa ni kutokana na ratiba za wanafunzi wanaomaliza form six kwenda Chuo Kikuu muda ni mdogo na wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne mpaka kuja kuingia cha tano waliofaulu ni miezi nane. Je, anaonaje kuleta sheria hapa ili tuje tubadilishe wawe wanaenda JKT wakati wanasubiri kwenda form five?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema wakati nawasilisha bajeti yangu, kwamba wazo hili lilikuja ni wazo zuri, tulikubali kwamba tutalichukua tukalifanyie kazi kwa sababu kuna wadau wengi wakiwemo Wizara ya Elimu, tupitie nao kwa pamoja tuone uwezekano wa jambo hili. Kwa maana hiyo baada ya mazungumzo na wadau tutaweza kulitolea uamuzi.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Mimi ni muumini wa msemo unaosema kwamba mbwa mzee hafundishwi Sheria. Baadhi ya vijana hatutaweza kuwafundisha uzalendo kwa kwenda tu JKT. Enzi za mwalimu kulikuwa na program za kwata mashuleni, tulikuwa tunafundishwa kwata kwa kutumia Bunduki za mbao. Pia kulikuwa na elimu ya kujitegemea ambapo vijana walikuwa wanafundishwa uzalishaji na stadi mbalimbali ambazo zinafundishwa sasa kwenye VETA. Je, Wizara iko tayari kushirikiana na Wizara ya Elimu, kwata ikarejeshwa mashuleni, vijana wakafundishwa ukakamavu kuanzia ngazi za chini na wakati huo huo elimu ya kujitegemea ikarejeshwa mashuleni kama zamani? (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli ni wazo zuri, wanafunzi kufundishwa mapema masuala ya kijeshi pamoja na elimu ya kujitegemea ni wazo zuri. Hata hivyo, kama nilivyosema tupo katika mchakato wa kuunda kikosi ambacho kitapitia changamoto zote; na kwa sababu kitajumuisha pia watu wa Wizara ya Elimu suala hili litazingatiwa ili tuone uwezekano wake.
MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, lakini nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri ambayo ameyatoa. Nina maswali mawili madogo ya kuuliza.
Mheshimiwa Spika, zipo nyumba za zamani kabisa ambazo wanajeshi wetu wanazitumia hadi sasa na hali yake siyo nzuri kabisa.
Je, Wizara ina mikakati gani ya kuzifanyia marekebisho angalau zikaendana na hali ya sasa?
Mheshimiwa Spika, swali la pili. Katika majibu ya msingi ya Mheshimiwa Waziri, amesema hana uhakika kama atajenga nyumba Unguja kwa awamu hii.
Je, ni lini anaweza kutueleza anaweza akatuanzia nyumba za Unguja wakati Unguja bado pana matatizo makubwa ya nyumba za kijeshi? Ahsante.
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Spika, kuhusu nyumba za zamani kufanyiwa ukarabati, hilo liko katika bajeti zetu. Nataka niwaeleze tu kwamba kwa kawaida bajeti inakuwa na miradi mipya na fedha za ukarabati.
Mheshimiwa Spika, sasa kwa mwaka huu wa fedha tuliweka fedha za ukarabati katika Bajeti ya Ngome na ni mategemeo yetu kwamba fedha zikipatikana tutakuwa tukirekebisha nyumba hizo awamu kwa awamu.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili, ni lini za Unguja zitajengwa? Kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi ni kwamba mchakato wa mazungumzo ya kupata fedha ajili ya kumalizia awamu ya pili unaendelea na utakapokamilika tu, basi bila shaka tutaanza awamu hiyo. Nataka nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba awamu hiyo itahusiaha kambi zilizokuweko upande wa Unguja.
MHE. SAADA MKUYA SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; katika mikakati ambayo imeorodheshwa ni kazi gani hasa zimefanyika katika kituo cha Afya cha Jeshi kilichopo Welezo ambacho kinahudumia wananchi wengi na hali yake ni mbaya sana. Kwa hiyo, hii mikakati imeorodheshwa lakini katika mwaka 2016/2017 ni kazi gani hasa zimefanyika katika kituo kile.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; namwomba Mheshimiwa Waziri tukiondoka Dodoma tufuatane, mguu kwa mguu twende katika Jimbo la Welezo tukatembelee kituo hiki cha afya, kipo katika hali mbaya na kinahudumia wananchi wengi na wengi wanakitegemea. Kwa hivyo, akienda akiona utajua sasa ni jinsi gani anaweza kukisaidia. (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika mikakati niliyoielezea kuna baadhi ambayo imeshaanza na kuna baadhi ambayo bado tunategemea itaanza siku za usoni. Lile la Bima ya Afya ambayo kwa kweli tunadhani ndio itakuwa mkombozi wa kuboresha huduma za afya, hilo bado halijaanza, tupo katika mchakato na ni matumaini yetu kwamba likianza fedha nyingi zitapatikana ili kuweza kuboresha vituo hivi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa yale yaliyoanza ni msaada uliotolewa na Serikali ya Marekani na Ujerumani. Tumeshafanya ukarabati na tumenunua vifaa, lakini tumeanza na ngazi za Hospitali za Rufaa za Jeshi. Kwa sababu hata kwenye Jeshi kuna vituo vya afya, hospitali na hospitali kuu. Kwa hivyo, kazi iliyofanyika kwa mfano katika Hospitali Kuu ya Lugalo, kazi zilizofanyika katika Ali Khamis Camp Pemba, kazi zilizofanyika Mwanza na kadhalika ni kubwa na tunajua kwamba kazi hii haijakamilika kwa sababu bado kuna vituo hatujavifikia ikiwemo hicho cha Welezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachoweza kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge ni kwamba tutafika, tunakwenda kwa awamu ili na chenyewe tukiboreshe wananchi pamoja na Wanajeshi waweze kupata huduma nzuri zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la kutembelea katika kituo hicho, nataka kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba nipo tayari, nitakapofanya ziara ya eneo la Unguja, basi moja ya kazi zangu itakuwa ni kufuatana naye kwenda kuangalia kituo hicho.
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, napenda kuipongeza Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kuwajengea wanajeshi kituo kizuri cha afya pale Ali Khamis Camp Jimbo la Wawi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa vitu vingi vya afya vinavyomilikiwa na Jeshi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hakuna majokofu ya kuhifadhia maiti, hata kwa Askari wenyewe pale wanapofariki kwa sababu wengine wanakaa mbali sana na maeneo ya mikoa yao. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuweka majokofu katika vituo tofauti vya Afya vya Jeshi ili Askari wenyewe wanapofariki waweze kuhifadhiwa vizuri?Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua kwamba kuna umuhimu wa kuwa na majokofu ya kuhifadhia maiti katika vituo vyetu vya Jeshi, kwa sababu vingi sasa hivi vinatoa huduma ya rufaa na bila shaka ni muhimu kuwa na majokofu hayo endapo itatokea vifo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu katika swali la msingi, ni kwamba lazima twende kwa awamu. Tunaanza kwenye vituo vikubwa na kazi hii tumeshaifanya pale Lugalo ni matarajio yetu kwamba kila fedha zitakapokuwa zinapatikana, basi huduma hii tutaiendeleza katika vituo vya chini. Kwa hiyo, nataka nimtoe hofu, jambo hili tunalijua na tutalifanyia kazi ili hatimaye vituo hivyo vipate majokofu ya kuhifadhia maiti.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, sina wasiwasi na uimara, uwezo na weledi wa Jeshi letu katika kusimamia majukumu yake na ndiyo maana nje ya mipaka yetu sasa hivi tuko salama lakini ndani ya nchi yetu hali siyo salama na mifano miwili ya juzi ya Mbunge na Meja Jenerali inadhihirisha kwamba ndani ya nchi yetu tuna matatizo.
Je, ni kwa nini sasa Jeshi la Wananchi lisishiriki kikamilifu kukomesha matumizi ya silaha na mauaji ya raia wasio na hatia ndani ya nchi yetu? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, navyoamini mimi au navyoelewa, silaha za kivita zinamilikiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania na matumizi ya silaha ndani ya nchi yetu ni matumizi ya silaha za kijeshi ambazo zinatakiwa zimilikiwe na chombo hiki.
Je, kwa nini sasa Jeshi letu halioni ni wakati muafaka kutumia IO’s wake kuhakikisha kwamba inazikamata silaha zote za kivita ambazo zinatumika kwa matumizi mabaya ya kuua raia katika nchi yetu?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kwamba kazi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania ni ulinzi wa mipaka lakini pale ambapo linahitajika au linaombwa kusaidia mamlaka nyingine iwe za kiraia au iwe Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama basi wanakuwa tayari kufanya hivyo. Tunavyozungumza ni kwamba mamlaka hizo ambazo ni Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama vikihitaji msaada wa Jeshi, mara zote Jeshi linakuwa tayari kutoa msaada huo.
Mheshimiwa Spika, kwa hali ilivyo sasa itaundwa task force itakayojumuisha Vyombo vyote vya Ulinzi na Usalama ili kuweza kulifanyia kazi tatizo hili la uvunjifu wa amani ndani ya nchi. Sina shaka kwamba kazi hiyo imeanza na nataka niwahakikishie wananchi wa Tanzania kwamba jukumu hili litafanywa vyema ili hali ya usalama ipatikane ndani ya nchi.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili la matumizi ya silaha za kivita; ni kweli kwamba silaha za kivita zinadhibitiwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania na kwamba ifanyike kazi maalum ya kuhakikisha kwamba silaha hizo zinapatikana, hiyo kazi inafanyika mara zote.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema bila shaka kwa kutumia task force hizi zilizoundwa kazi ya kuhakikisha kwamba raia au watu wengine wote ambao wanamiliki silaha za kijeshi au za kivita ambazo kikawaida au kitaratibu/ kisheria hawapaswi kuwa nazo zinapatikana na kurudishwa katika mamlaka zinazohusika. (Makofi)
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mimi ni Mheshimiwa Paresso, kwa niaba ya Mheshimiwa Magereli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa ni ukweli kwamba hakuna aliye juu ya sheria lakini wakati mwingine wanajeshi wetu baadhi wamekuwa wakijiona kwamba wao ni superior kuliko watu wengine; je, Wizara ina mkakati gani wa kuendelea kutoa elimu ili wanajeshi hao wafuate sheria na kujenga mahusiano mazuri kati ya wananchi na jeshi?
Swali la pili, pia kumekuwa na mahusiano hafifu kati ya jeshi na wananchi hasa katika yale maeneo ambao yana migogoro ya ardhi. Je, Wizara sasa ipo tayari kuhakikisha migogoro hii inaisha kwa wakati ili mahusiano haya yaendelee kuimarika?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa kutoa elimu upo. Wanajeshi mara zote wamekuwa wakikumbushwa kuishi vizuri na raia hususan wale wanaowazunguka katika makambi yao. Mara kwa mara zimekuwa zikichukuliwa hatua za kinidhamu ndani ya vikosi vyetu vya jeshi pale wanapokiuka utaratibu huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tueleze vilevile kwamba sheria za nchi hii zinataka mtu anapohisi amevunjiwa haki yake, basi ana haki ya kwenda kushtaki. Kwa kuwa wanajeshi hawako juu ya sheria, sheria hufuata mkondo wake. Kwa hiyo, hilo lizingatiwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mahusiano hafifu kwenye migogoro ya ardhi, hili napenda niliseme, kama tulivyoeleza wakati tunatoa bajeti yetu hapa, kwamba juhudi zote zinafanyika ili migogoro ya ardhi inayohusisha Kambi za Jeshi iweze kuisha. Yapo maeneo ambayo wananchi wamevamia maeneo ya jeshi, kwa hiyo, ni vizuri wananchi nao wakapewa elimu hiyo hiyo ili wasiweze kuvamia maeneo ya jeshi. Kwa yale maeneo ambayo jeshi imechukua haijalipa fidia, juhudi zinafanyika ili tuweze kulipa fidia. (Makofi)
MHE. JUMA ALI JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru. Naomba kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, mgogoro huu ni wa muda mrefu toka mwaka 1979, viongozi mbalimbali wametembelea katika eneo lile lakini hadi leo halijapatiwa ufumbuzi. Je, Mheshimiwa Waziri yupo tayari mimi na yeye pamoja na viongozi wanaolizunguka lile eneo tukae pamoja ili tuupatie ufumbuzi mgogoro huu?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba mgogoro huu ni wa muda mrefu na nataka nimfahamishe Mheshimiwa Juma kwamba mimi binafsi nimefika eneo hilo, nilifanya mazungumzo na uongozi wa kikosi pamoja na uongozi wa eneo na wananchi wa pale tulizungumza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, kinachokwamisha kutatua sasa hivi ni suala la fedha za kupima kwa sababu Jeshi lilisharidhia kufanya mabadiliko ya mipaka yake ili wananchi ambao sasa hivi wanaonekana wapo ndani ya eneo la kambi waweze kutolewa. Hata hivyo, nitakuwa tayari kuzungumza na Mheshimiwa Mbunge ili kumueleza zaidi ni hatua gani ambazo zinastahili kuchukuliwa kwa mujibu wa ziara niliyoifanya pale na fedha zikipatikana. (Makofi)
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Moja ya matatizo makubwa makubwa ambayo tumekabiliana nayo kwa wananchi wanaozunguka Kambi ya Maji Maji kikosi Namba 41 na kikosi cha JKT katika Kata ya Mchonda ni tatizo ya migogoro ya ardhi, na tatizo hili tayari tumesharipoti kwa watu wa Wizara.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kufahamu msimamo wa Serikali au Wizara juu ya fidia ambazo wameahidi kuwalipa wananchi wale ili waweze kuachia yale maeneo?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kuna Kambi nyingi ambazo zina migogoro ya ardhi. Kama ninavyosema mara kwa mara hapa migogoro hii iko ya aina nyingi, kuna migogoro ambayo Jeshi limechukua ardhi lakini wananchi bado hawajalipwa fidia, yapo maeneo ambayo wananchi wamevamia Kambi za Jeshi na na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachoweza kusema hapa ni kwamba tumeweka fedha kwenye bajeti ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ili kwa yale maeneo ambayo fidia zinahitajika tuweze kulipa ili kumaliza migogoro hii, mwaka wa bajeti haujaisha na nimategemeo yetu kwamba fedha hizo zikipatikana tutatoa fidia kwa wale ambao wanastahili kupewa fidia maana wako wengine ambao wao wamevamia kambi za Jeshi hao hawatalipwa fidia. (Makofi)
MHE. HAJI KHATIB KAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya ufafanuzi wa Mheshimiwa Waziri naomba nimuulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri amekiri katika jibu la msingi kwamba askari wa jeshi sasa hivi wanalipwa posho ya shilingi 10,000 kwa siku hela ambayo kwa maisha ya sasa ni ndogo sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini Serikali itawaongezea askari hawa posho kutoka shilingi 10,000 angalau hadi 20,000 kwa siku?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Jeshi letu la Tanzania limekuwa likipata sifa kitaifa na kimataifa kutokana na weledi na utendaji wake wa kazi, je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba Jeshi hili halitoi malalamiko kwa posho wanazolipwa, hasa ukizingatia kazi wanazozifanya? Ahsante.
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi, ni kwamba posho zinaongezwa kadri ya uwezo wa Serikali unavyoruhusu. Katika hili nimetoa mifano, kwamba tulianzia na shilingi 5,000 ikapanda mpaka shilingi 7,500 ikapanda mpaka shilingi 8,500 sasa ni shilingi 10,000; kwa hiyo, tutaendelea kuzipandisha posho hii kwa kadri uwezo wa Serikali utakavyoruhusu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na la pili kuhusu malalamiko unayoyazungumzia; nataka nikueleze Mheshimiwa Mbunge ni kwamba kwa kiwango kikubwa posho zinazotolewa sasa kwa askari na maafisa wetu zimeboreshwa kwa kiwango kikubwa. Mimi nataka nikuhakikishie kwamba wengi wanafurahia posho hizi zinazotolewa. Kama nilivyosema hakuna kinachotosha, mara zote kutakuwa kunaupungufu tu. Kwa hiyo, kwa kadri uwezo utavyoruhusu tutaendelea kuwa tunazi-review kila mwaka posho zote kuangalia uwezekano wa kuzipandisha kadri uwezo wa Serikali utakavyoruhusu.
MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na posho za ration allowance kuwa ndogo lakini pia inasemakana kuna mpango wa kuzifuta posho hizi ili askari wasipewe cash wawe wanakula ration makambini. Je, ni kweli?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, posho ya ration tutambue madhumuni yake kwanza, madhumuni ya posho ya ration ni kumlisha askari na maafisa ili waweze kutekeleza majukumu yao. Sasa wako wale ambao wako kwenye makambi, wako wale ambao wanalazimika kula ili waweze kutekeleza majukumu yao, hao kuna wazabuni katika Makambi yote wanaopewa fedha hizo ili waweze kuwalisha, lakini wale ambao majukumu yao hayapo katika Kambi wao wanapewa fedha zao taslimu ili waweze kutumia wanavyoamua wao wenyewe.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Mimi nina swali moja tu; kwa kuwa Serikali imerejesha Kambi ya JKT Mpwapwa na kwa kuwa vijana wengi wa Wilaya ya Mpwapwa wanataka kujiunga na JKT Mpwapwa, je, ni taratibu gani watumie ili waweze kujiunga na ile kambi?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba JKT ina azma ya kufungua makambi mapya katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Mpwapwa, na utaratibu utakaotumika wa kujiunga ni ule ule ambao unatumia sasa kwamba wakati ukifika JKT itatoa nafasi za vijana wa kujitolea kuomba ili kuingia katika makambi haya mapya. Kwa pale Mpwapwa haitokuwa vijana wa Mpwapwa peke yao, itakuwa kwa nchi nzima, tutazigawa nafasi kama tunavyozigawa sasa kupitia Wilayani na Mikoani na hatimaye vijana watajiunga na Kambi hiyo ya Mpwapwa itakapokuwa tayari kutoa mafunzo. Vile vile kwa siku zijazo tukiwa tayari kambi hiyo pia itatumika kwa vijana kwa mujibu wa sheria.
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, pamoja na wananchi hao ambao Mheshimiwa Waziri anakiri kwamba hawajalipwa fidia na anakiri kwamba wakati maeneo haya vikosi wanayatwaa hawajalipwa chochote bado vikosi vyetu vimeendelea kuwafukuza wananchi hawa wasifanye shughuli zozote ikiwemo kuokota korosho zao kwa wale ambao walishapanda mikorosho.
Naomba kupata kauli ya Serikali juu hatma ya watu hawa wakati wanaendelea kutengewa hii bajeti ambayo Mheshimiwa Waziri ameisema ili waweze kuendelea kufanya shughuli zao? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili Mheshimiwa Waziri naomba kupata commitment ya Serikali kwa sababu tatizo ni la muda mrefu na Tume nyingi zimeshaundwa na tayari zilishaleta majibu ya kukiri kwamba kuna tatizo.
Ni lini Serikali sasa itaenda kufanya hili zoezi ili tatizo hili liondoke na wananchi wale waweze kujua hatma yao? (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Spika, lazima tukiri kwamba tatizo kubwa limekuwa ni upungufu wa bajeti na kwa maana hiyo kupelekea wananchi wanaostahili kulipwa fidia kuchelewa. Hata hivyo, kulikuwa kuna maamuzi ya makusudi ya kuzuia wananchi kufanya shughuli za kibinadamu katika makambi haya. Sababu kubwa ya maamuzi hayo ni kwamba katika baadhi makambi haya kuna silaha na kuna milipuko ambayo inaweza kuleta athari kwa wananchi na ndiyo sababu wakakatazwa kufanya shughuli za kibinadamu.
Lakini ukiacha tatizo hilo, wapo wananchi ambao wakipewa ruhusa ya kufanya hivyo basi wanafanya maendelezo makubwa, wengine wanajenga hata nyumba ambayo inapelekea uthamini na fidia zao kuwa kubwa mno. Hizo ndiyo sababu zilizopelekea wakazuiwa kufanya shughuli zote za kibinadamu ili kwanza wasidhurike lakini pili wasiendeleze maeneo hayo kwa sababu yatapelekea fidia kuongezeka.
Mheshimiwa Spika, kuhusu commitment ya Serikali kwamba ni lini zoezi hili litakamilika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakapokuwa tumepokea fedha hizi kutoka kwenye bajeti yetu jukumu hili litafanyika mara moja ili tuondokane na tatizo hili la muda mrefu. (Makofi)
MHE. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Waziri kwa majibu mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, nchi zinazotuzunguka, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, DRC, Zambia, Malawi na Msumbiji wote wameridhia mkataba huu. Kama alivyosema Mheshimiwa Waziri kwenye jibu lake ni nchi sita tu duniani ambazo hazijaridhia na sisi Tanzania tukiwemo. Je, Serikali haioni kwamba ni aibu kubwa sana Tanzania kuwa kwenye kundi hili dogo la nchi sita ambazo zina matatizo ya ndani ambao hazikaridhia mkataba huu za kina Haiti na nyingine hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, Serikali ipo tayari kutoa ratiba (timeframe) ya kupitia kumaliza mchakato huu wa mkataba huu Serikalini na hatimaye kwenye Bunge hili kabla haujakwisha mwezi wa Juni au Septemba angalau mkataba huu uje Bungeni hapa kwa ajili ya kuridhiwa? (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, haikuonekana sababu wakati ule kwa sababu bila ya kuwa tumeridhia tuliweza kufanya shughuli zetu zote bila ya matatizo yoyote; lakini kwa sasa hivi sababu ipo. Kama nilivyosema kwenye jibu la msingi ni kutokana na matukio ya kigaidi suala hili sasa limefikia wakati muafaka turidhie ili tuondokane na kuwa katika nchi chache ambazo hazijaridhia kama nilivyosema. Ndiyo maana tumeshatayarisha waraka kwa madhumuni ya kupita katika ngazi za maamuzi ili hatimaye uletwe hapa kwa kuridhia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili la timeframe, ninachoweza kusema ni kwamba, utaratibu ni kwamba waraka ukishakamilika una hatua tatu; ya kwanza ni Cabinet Secretariat ambapo unajadiliwa na baadaye IMTC na hatimaye unapita kwenye Baraza la Mawaziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ni matumaini yangu kwamba hatua hizi tatu zitafanyika kwa haraka ili tuweze kukamilisha suala hili na mkataba huu uridhiwe. Ningependa nimwarifu Mheshimiwa Rweikiza kwamba, kwa Bunge hili tutakuwa tumechelewa, lakini huenda Septemba tukaweza kufanya shughuli hii ikakamilika.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Nakiri kwamba ni kweli Jeshi la Kujenta Taifa wametusaidia na wanaendelea kutusaidia hata katika kazi nyingine, lakini wakati shule hii inatwaaliwa ilikuwa na miundombinu mingi sana na sasa miundombinu bado haijarejeshwa yote.
Mheshimiwa Naibu Spika, Shule hii sasa haina nyumba hata moja ya Mwalimu na ukizingatia kwamba ina Kidato cha Tano na Sita ambayo ni boarding ni wasichana wanakaa peke yako. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuendelea kutupatia pesa zaidi na hasa pesa za kujenga nyumba za Walimu ambapo sasa hivi hakuna hata nyumba moja?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili wakati Serikali inatwaa eneo hili na kuipatia Jeshi limezuka suala lingine ambalo ni gumu zaidi. Wanajeshi walipokuja pale wamechukua eneo sasa la mashamba wanayolima wananchi na kufanya wananchi zaidi ya elfu tano wa Vijiji vya Kasu, Milundikwa, Kisula na Malongwe zaidi ya elfu nne kukosa mahali kabisa pa kulima. Naiomba Serikali je, iko tayari kufikiria upya na wakati mwingine ione uwezekano wa kuwagawia wananchi sehemu ya eneo ili waendelee kuendeleza maisha yao? (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi ni kwamba Wizara yangu iko tayari kuendelea kusaidiana, kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya katika kutoa vifaa vya ujenzi ili waweze kukidhi mahitaji yao ya kuifanya shule hii ipate miundombinu inayotakiwa. Bila shaka kutakuwa kuna bajeti za kawaida za kupitia Halmashauri nazo hizo wakizielekeza huko na sisi tutakuwa tayari kutoa mchango wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Serikali kutwaa eneo hili na kufanya watu wengi karibu elfu nne kukosa sehemu ya kulima nataka nimfahamishe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali haijalitwaa eneo hili bali eneo hili lilikuwa ni mali ya Serikali mali ya JKT toka mwanzoni. Kama wakati wa JKT kurudi pale imetokea kwamba eneo lililochukuliwa ni zaidi ya lile la awali hilo naweza nikalingalia, lakini ukweli ni kwamba taarifa tulizokuwa nazo ni kwamba JKT wamekwenda kuchukua eneo lao la awali walilokuwa nalo kabla ya mwaka 1994 kusitisha shughuli za JKT.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitamwomba Mheshimiwa Mbunge tukae ili tulijadili suala hili na ikiwezekana tufanye ziara pale tuone tunaweza kusaidia vipi. (Makofi)
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri sana leo ya Waziri wa Ulinzi ndugu yangu Mheshimiwa Mwinyi nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa vile idadi inayochukuliwa kwa mwaka ni ndogo sana ukilinganisha na idadi ya wanafunzi wanaomaliza shule form six na vyuo. Je, Serikali haioni umuhimu wa kupanua kiasi idadi ya wanafunzi hawa ili wapate mafunzo ambayo tunafikiri kwamba ni ya maadili na uzalendo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa vile vijana wengi wanaotoka baada ya mafunzo kutoka JKT husahau au kuacha mafunzo mazuri na maadili waliyofundishwa kule JKT. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwafuatilia vijana hawa ili wasisahau mafunzo na kuacha maadili mazuri ya wananchi?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Almas Maige kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu idadi ndogo ya vijana tunaowachukua kwa mujibu wa sheria, ni kweli kwamba wahitimu sasa hivi wanazidi 60,000, lakini uwezo wetu wa kuchukua inakadiriwa kuwa ni kama 20,000 peke yake. Kwa hiyo iko mikakati ya kuhakikisha kwamba tunaongeza idadi ya vijana wanaochukuliwa kwenda JKT kwa kuboresha miundombinu katika kambi tulizonazo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaendelea kuziboresha ili ziweze kuchukua vijana wengi zaidi na ni matumaini yetu kwamba kila mwaka tutaendelea kuongeza idadi. Hata hivyo, hivi karibuni tu tumefungua kambi mpya tano katika Mikoa ya Rukwa kule Milimbikwa na Ruwa, Mpwapwa Dodoma, Makuyuni Arusha, Itaka pamoja na Kibiti. Kwa hivyo ni mategemeo yetu kwamba, kwa kuongeza kambi hizi mpya idadi ya vijana tunaoendelea kuwachukua itaongezeka ili hatimaye wote wanaomaliza form six waweze kujiunga kwanza na JKT kabla hawajaanza vyuo vikuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili la kufuatilia vijana ili wasisahau maadili nadhani hili ni wazo zuri. Mpaka sasa hivi hakuna mkakati wa kuwarudisha tena lakini tunalipokea tutaangalia njia bora zaidi ya kulifuatilia.
MHE. SUSAN A. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Majibu ya Mheshimiwa Waziri yamekuwa ni hayo hayo kwa muda mrefu, na maswali yalikuwa ni kwa nini sasa wanafunzi wote wanaomaliza kidato cha sita wasiende JKT kwa sababu lengo la JKT kama ulivyosema mwenyewe ni suala la uzalendo na maadili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila leo wanasema wanaboresha, wanaongeza lakini sisi tunachotaka ni kwamba wote Watanzania vijana hawa tunataka wote wawe in uniform waweze kutekeleza suala zima la uzalendo na maadili ili nchi yetu maadili yasiendelee kuporomoka, sasa ni lini watahakikisha hilo linafanyika?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema jitihada zimefanyika na zimeonekana. Wakati tunarudisha tena utaratibu wa JKT baada ya kuwa tumeuacha kwa miaka mingi kuanzia mwaka 1994, idadi tuliyokuwa tunaweza kuchukua ilikuwa ndogo sana si zaidi ya vijana 5000; leo tunavyozungumza tayari tumefikia 20,000 na kambi mpya nimezitaja tunazozifungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo si maneno tu ya kurudia hii ni mkakati uliopo. Kila mwaka tunaendelea kufungua kambi mpya tunaboresha za zamani na idadi imeendelea kuongezeka. Leo tunavyozungumza kama tunachukua vijana 20,000, bila shaka ndani ya miaka michache ijayo tutaweza kukidhi mahitaji ya vijana 60,000 au 80,000 ambao watakuwa wanahitimu.
MHE. MASOUD ABDALLA SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nina swali moja dogo la nyongeza. Kuna malalamiko kadhaa kwa vijana wale ambao walioajiriwa kwenye Shirika la Uzalishaji Mali la SUMA JKT, kiwango chao cha fedha ni kidogo sana na vijana hawa wanalinda katika maeneo kadhaa na maeneo muhimu kama vile benki. Ni mara kadhaa wamekuwa wakisema kwamba mtapandisha kiwango cha posho cha vijana hawa wa SUMA JKT Guard, ni kwa nini basi Serikali imekuwa ikisuasua kwa muda mrefu hawapandishi pesa hizi na ni vijana hwa wanafanya kazi kubwa?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Masoud kuhusu vijana wanaofanya kazi kwenye Shirika la SUMA Guard. Ni kweli malalamiko hayo na sisi tumeyapata, tumezungumza na Uongozi wa SUMA Guard ili waweze kuongeza viwango ambavyo wanawapatia vijana hawa. Hivi sasa tunavyozungumza ukiacha mshahara ile basic salary, kuna posho wanazopata za usafiri, za chakula na kadhalika; lakini bado tunakiri kwamba viwango wanavyopewa havikidhi haja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaendelea kujitahidi kufanya kila linalowezekana ili maslahi kwa ujumla ya vijana hawa yaweze kuboreka. Kwa ujumla ni kwamba viwango vinavyofuatwa vinaendana na mashirika mengine ya ulinzi. Kwa hivyo ni vyema sisi kama Serikali tuone umuhimu wa kuboresha haya. Jambo hilo limechukuliwa na Uongozi wa SUMA JKT na ni mategemeo yetu kwamba wataweza kuwaboreshea viwango hivyo.
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa kuwa Serikali imeonesha nia ya kufanyia kazi wazo hili na kwa kuwa Biharamulo tuko tayari, Mheshimiwa Waziri uko tayari kwa hivi karibuni tuje mimi na Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi kwa ajili ya kuanza mazungumzo na wataalam wako wa Jeshi la Kujenga Taifa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Mheshimiwa Waziri uko tayari kututembelea ili kabla ya maongezi haya hayajaanza uone fursa zilizopo ili maongezi yawe yamesheheni ushahidi na mambo ambayo tumeyaona kwa pamoja?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kutembelea niko tayari kufanya ziara katika eneo hilo ili kutambua fursa ambazo zinaweza zikashughulikiwa ili kutoa ajira kwa vijana hao.
Kuhusu mazungumzo na wataalamu wake nina shauri nipate fursa kwanza ya kujadiliana suala hili na wataalam wa JKT ili kuona uwezekano wake na watakapokuwa wao tayari kuja basi wenzao hawa wawe tayari kwa ajili ya mazungumzo haya.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza niwapongeze vijana wote wa JKT wanaoendelea kujitolea. Kumekuwa na malalamiko ya kubaguliwa katika upande mzima wa suala la kupewa ajira kwa vijana wanaomaliza JKT hasa ajira ambazo zimetokea kwenye Jeshi la Polisi na hasa katika Operesheni ya Jakaya Kikwete.
Sasa swali langu, nini tamko la Serikali kuhusiana na tabia hii ya kibaguzi, na wapo vijana wa jimboni kwangu?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Ester Bulaya kwa kuamua kwa makusudi kujiunga na Mfunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa akiwa hapa Bungeni, pamoja na Waheshimiwa Wabunge wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la malalamiko ya ubaguzi wakati wa ajira, nataka nimfahamishe kwamba mara zote kuna kuwa kuna uhaba wa idadi ya vijana wanaoajiriwa ukilinganisha na wale walioko kwenye kambi. Kwa mfano katika kipindi kilichopita jeshi la Ulinzi liliajiri vijana 2,000 kati ya vijana 9,000 waliokuwepo kule; bila shaka wale 7,000 wataona kwamba wamepaguliwa, lakini ukweli ni kwamba nafasi zinakuwa chache wakati wao wako wengi. Ni kweli hivi karibuni Jeshi la Polisi lilitoa ajira, lakini vile vile idadi ya vijana walioajiriwa ni chache sana ukilinganisha na vijana waliokuwepo katika Kambi za JKT.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wakati mwingine vigezo vya ajira vinaweza vikafanana lakini kwa sababu ya idadi imekuwa ndogo basi kuna wengine bilashaka wataachwa ndiyo hayo yanasababisha malalamiko.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru; nina swali moja la dogo la nyongeza.
Serikali au JKT inatoa stadi za kazi ikiwemo suala zima la ushonaji; na Serikali kwa mara kadhaa kwa miaka mingi imesema ina mkakati kabambe wa kuongeza viwanda vya ushonaji nguo na hasa sare zile za jeshi, lakini imeonekana kwamba…
: ...inaonekana
kwamba kunakuwepo na kusua sua kwenye shughuli hizi, swali, je, Serikali ina mkakati gani wa ziada kuona kwamba ahadi yake ya muda mrefu ya kuongeza viwanda vya ushonaji nguo sambamba na Tangamsino mbali ya Kamesuma?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba tunao mkakati wa kuongeza idadi ya viwanda vya kuzalisha nguo katika jeshi letu na tunavozungumza tuna viwanda viwili tayari, kimoja kiko pale katika Kambi ya Mgulani na kingine kipo katika Kambi ya Ruvu. Vinafanya kazi na lengo ni kuviboresha kwanza hivi kabla hatujaanzisha vingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo ukifika pale kwenye kambi ya Mgulani utaona kwa macho yako kwamba kwa kweli juhudi kubwa zimefanyika. Sasa hivi nguo za kombati kwa mfano hatuagizi kutoka nje zina vitambaa vinanunuliwa hapa na zinashonwa hapa. Kwa hiyo, tumeanza na juhudi hiyo na hatua kubwa imepigwa na tutaendelea kuendeleza juhudi hizo. (Makofi)
MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Majibu ya Serikali hayatoshelezi, ni afadhali tu kidogo. Pamoja na majibu hayo, nina maswali mengine mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kuna kauli mitaani zinasemwa na Watanzania kwamba Tanzania inashiriki hasa hasa kwa maslahi binafsi ya kukomba mali za DRC kwa mfano. Je, Serikali ina matamshi gani kwa lengo la kuwaosha Watanzania kutokana na tuhuma hii?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Jeshi letu linapopigwa kwenye vita hasa pale DRC kuna kauli pia kwa Watanzania wanaamini kwamba Jeshi la Uganda linashiriki katika kulipiga Jeshi la Tanzania kwa kuwa wakati fulani kihistoria Waganda na Watanzania walipapurana kivita. Je, ni ipi kauli ya Serikali kuhusiana na kadhia hii? Ahsante.
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Muhammed Amour, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa bahati mbaya sana maneno kama haya yanatolewa na Watanzania ambao kwa kweli wanatakiwa wao wawe wazalendo na kuweza kupongeza juhudi za Serikali za kuwasaidia wenzetu ambao wako katika hali ambayo haina amani katika nchi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna suala la kukomba mali za DRC kwa maslahi binafsi, halipo. Tanzania haishughuliki na kuchukua chochote sehemu yoyote wanayolinda amani. Majeshi yetu yako kule kusaidia kurudisha hali ya amani, kuwalinda wananchi dhidi ya waasi ambao wanapigana katika maeneo yale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kwamba Jeshi la Uganda linashiriki katika kuwapiga Watanzania pia halina ukweli wa aina yoyote. Matukio yote yaliyotokea tuna ushahidi wa kutosha kwamba ni vikundi vya waasi. Mwanzoni walikuwa M.23 na sasa hivi kuna vikundi vingine ambavyo vinatokea katika nchi mbalimbali za jirani pale lakini hakuna ukweli kwamba Majeshi ya Uganda yanashiriki katika kuwapiga askari wa Tanzania. (Makofi)
MHE. MASOUD ABDALLAH SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, nina swali moja dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kuna vikundi vya waasi ambavyo vinapelekea kufanya hujuma kwa Vikosi vyetu vya Kulinda Amani DRC - Kongo na maeneo mengine na pale inapotokea maafa kwa hawa askari wetu kupoteza maisha huwa kuna malipo maalum kutoka Umoja wa Mataifa lakini hata Serikali yetu nayo huwa kuna kiwango cha fedha ambacho wanatoa. Je, Serikali hasa ina mkakati gani wa ziada kuleta Muswada hapa Bungeni kuongeza muda wa kulipa wajane au wagane pale ambapo wanajeshi wanapoteza maisha katika kulinda amani DRC Kongo na Sudan Kusini na maeneo mengine? (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Masoud, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Umoja wa Mataifa na Serikali ya Tanzania imekuwa ikilipa mafao yanayohusiana na ushiriki wa askari wetu katika Ulinzi wa Amani sehemu mbalimbali. Vinapotokea vifo basi kuna fedha maalum na kuna viwango maalum vilivyopangwa ambavyo hutolewa na Umoja wa Mataifa na Tanzania sisi tunatoa kwa mujibu wa Sheria ya Ulinzi na Kanuni za Majeshi zilizopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuongeza fedha kwa wajane, ni suala ambalo tunalitafakari kwa madhumuni ya kuweza kuboresha maslahi yote kwa ujumla siyo moja moja. Kwa sababu kuna maslahi mengi ambayo wanajeshi hawa wanatakiwa wayapate. Sasa hivi Sheria ya Ulinzi wa Taifa inapitiwa pamoja na Kanuni zake ili kuangalia ni viwango gani vya maslahi gani ambavyo vimepitwa na wakati ili viweze kuboreshwa kwa pamoja.
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, je, Serikali inajiridhisha vipi kwamba ile fidia ya dola 70,000 inayotolewa inawafikia walengwa hasa watoto au mke wa marehemu ambaye anakuwa amepoteza maisha anapokuwa katika vikosi vyetu vya kulinda amani nchi mbalimbali huko duniani? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ni muda mrefu sasa tunaendesha mambo yetu ya ulinzi bila kuwa na sera ya ulinzi, je, ni lini Serikali itakamilisha sera hii ili kusudi pamoja na masuala haya ya ulinzi wa amani sehemu mbalimbali duniani. Sera hiyo iweze kubainisha maeneo mbalimbali ambayo kwa namna moja au nyingine yatafanya vikosi vyetu vinavyoenda kulinda amani huko duniani viweze sio tu kunufaika kwa mujibu wa taratibu za UN, lakini pia kwa mujibu wa taratibu za nchi yetu? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Spika, fedha zinazotolewa kama fidia zinawafikia wahusika kwa sababu Tanzania tumeshakuwa na uzoefu wa jambo hili, tumeshapoteza askari wetu na kuna walioumia, fedha zilizotolewa familia zinaitwa Makao Makuu ya Jeshi na wanakabidhiwa bila ya tatizo lolote na inapobidi basi msimamizi wa mirathi ndiye ambaye anakabidhiwa akiwa pale Makao Makuu ya Jeshi. Mpaka sasa hivi kwa matukio yote yaliyotukuta hakuna tatizo la mtu kudhulumiwa na hivyo tunaamini kwamba fedha hizo huwa zinawafikia walengwa.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili ya Sera ya Ulinzi, kama tulivyowahi kusema mara kadhaa hapa Bungeni, sera hii rasimu yake ipo tayari, imeshajadiliwa na ngazi zote na kinachosubiriwa ni maoni kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kama mdau ili wakishatoa maoni yao basi hatua zilizobaki za kuikamilisha sera hii ziweze kuchukuliwa.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kupana nafasi, Mheshimiwa Waziri amesema kama askari au afisa amefariki analipwa dola 70,000. Sasa ningependa kujua dola 70,000 hizi wanalipwa warithi wake cash au kuna mgao wa Serikali unakatwa kutoka hizi kama ambavyo wanakatwa wale askari wanaoenda katika misheni zile, sijui umenielewa?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Spika, fedha hizi hazikatwi, wanapewa dola 70,000 zote lakini sio mwisho, hii ni fidia kutoka Umoja wa Mataifa lakini askari yeyote anayepoteza maisha ana fidia vilevile kutoka hapa nyumbani. Kwa hiyo, kuna fedha zinazotolewa na Wizara kwa ajili ya kulipa fidia familia ya wale ambao wamepoteza maisha wakiwa kazini.
MHE. ABDUL-AZIZ M. ABOOD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa, wananchi wa Kauzeni na Luhungo walihamia pale mwaka 1969 wakati wa Vijiji vya Ujamaa na wakapewa maeneo ambayo yalipimwa mwaka 1970 ikawekwa mipaka kati ya shirika na wananchi;
Je, kwa nini Serikali isitumie mipaka hiyo ya mwaka 1970 ili wananchi wakapata haki yao na mashamba yao yakawa katika eneo lao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, si swali lakini ningemwomba Mheshimiwa Waziri angekuja katika maeneo haya akaangalia yeye mwenyewe na kuweza kukutana na wananchi akapata ukweli ulivyo katika meneo haya. (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba upimaji wa awali umefanyika mwaka 1970 na baada ya pale kutokana na migogoro hii ya kuingiliana kati ya maeneo ya Jeshi na Wananchi, mwaka 2002 ulifanyika upimaji mpya ambao ulikuwa na lengo la kuondoa wananchi waliokuwa ndani ya mipaka ya Jeshi kwa hivyo wakaachwa nje, sasa inaonekana baada ya pale mgogoro umeendelea. Nataka nimkubalie na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba niko tayari kwenda katika eneo hilo pamoja na wataalam wangu ili tukazungumze na wananchi na kutafuta ufumbuzi wa kudumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee tu kusema kwa ufupi kwamba, matatizo ya mipaka kati ya maeneo ya Jeshi na wananchi yako sehemu nyingi sana. Naomba niwaarifu tu Waheshimiwa Wabunge kwamba nimetengeneza utaratibu maalum wa kupita katika maeneo hayo ili mimi na wataalam wangu tuthibitishe mipaka hiyo na kuhakikisha kwamba tunaondoa hii mogogoro ambayo imeendelea kwa siku nyingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu hapa kwamba kuna mgogoro ambao nimeupata kutoka kwa Mheshimiwa Mwakyembe kwenye Kata za Bondeni, Ipiyana na Kajunjumele katika Wilaya ya Kyela, nimhakikishie pia kwamba katika utaratibu nitakaopanga wa kuzunguka katika maeneo haya nitafika na pale nizungumze na wananchi ili hatimaye tuondoe matatizo yanayowakabili wananchi katika maeneo hayo. (Makofi)
MHE. MACHANO OTHMAN SAID: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwanza naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri majibu yake mazuri na ya ukweli, pamoja na majibu hayo naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, katika bajeti ya mwaka jana Mheshimiwa Waziri aliahidi kulimaliza tatizo la Kambi ya Kisakasaka ambayo iko katika Wilaya ya Magharibi B. Je, ni hatua gani zimefikiwa hadi sasa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Kambi ya Mtoni ambayo iko katika Wilaya ya Magharibi A ni ya muda mrefu na watu waliikuta kambi kabla ya kuhamia wao na kuna viashiria vya kuvamiwa na wananchi; Je, Mheshimiwa Waziri anatuambia nini kuhusu suala hili na kama kuna upimaji au tayari imeshapimwa kambi ile ya Mtoni ili kuepuka uvamizi wa wananchi katika eneo lile?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu eneo la Kisakasaka ambalo tuliahidi kwamba tutamaliza tukiweza kupata bajeti, nieleze tu kwamba mpaka sasa fedha za ulipaji wa fidia na upimaji bado hazijapatikana, ni mategemeo yetu kwamba tunaweza tukapata kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha ili tuweze kulimaliza hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Kambi ya Mtoni ni dhahiri kwamba kambi karibu zote zimepimwa lakini kuna kuhuisha mipaka, kwa hivyo tutakachofanya kama nilivyoeleza awali ni kwamba tunatengeneza utaratibu maalum sasa wa kupitia maeneo yote ili tuweze kuhakikisha kwamba mipaka yetu inahuishwa na kuwataka wananchi wale ambao hawana stahili, basi waweze kutoka katika maeneo hayo, lakini wale ambao wataonekana na stahili aidha turekebishe mipaka au wapatiwe fidia zao ili tuondokane na migogoro ambayo imeonekana kwamba haiishi kati ya Wananchi na Wanajeshi. (Makofi)
MHE. MACHANO OTHMAN SAID: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba kuuliza swali moja la nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa uzinduzi wa Ukuta wa Mererani ambao Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliuzindua, Mheshimiwa Rais aliridhika sana na kazi ambayo imefanywa na Jeshi na kuahidi kwamba vijana 2,500 wa JKT ambao walishiriki katika ujenzi huo waajiriwe na vyombo vya ulinzi vya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Je, ni hatua gani ambazo zimefikiwa kuhusu ajira za vijana wale hadi hivi sasa?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Machano Othman Said, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Mheshimiwa Rais alitoa ahadi ya kuwaajiri vijana walioshughulika katika ujenzi wa Ukuta pale Mererani. Zoezi hilo kwa kweli limeshaanza, polisi wamepokea vibali vya ajira, usaili umeanza na ni mategemeo yetu kwamba vyombo vingine vya ulinzi na usalama watakapokuwa wamepata vibali wataendelea kuwachukua vijana hawa.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, wananchi wa Kenyambi na Bugosi huko Tarime wameanza kukata tamaa baada ya huo uthamini uliofanyika tangu mwaka 2013, ni miaka mitano sasa. Bajeti iliyotengwa ya mwaka 2017/2018 ni shilingi bilioni 20, je, katika mwaka huu unaoisha fedha hizi kama zikipatikana wananchi wa Kenyambi na Bugosi huko Tarime watalipwa fidia? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa muda mrefu Serikali imekuwa na kawaida wanapochukua maeneo ya wananchi kwa matumizi ya jeshi hawalipi fidia, wanafanya hivyo kwa sababu wananchi hawana cha kufanya. Serikali ituambie, ni kwa nini tangu mwaka 2006 imekuwa ikitoa taarifa ya utekelezaji wa kupima maeneo, kuthamini na kutoa fidia lakini haifanyi hivyo? Ni kwa nini Serikali isifanye utaratibu wa kufanya matembezi ya hisani ili wananchi wapate fidia zao kwa sababu Serikali inaonekana imeshindwa? Nashukuru sana.
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Masoud Abdallah Salim, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kama nilivyojibu katika jibu langu la msingi kwamba fedha zikipatikana ndiyo kipaumbele kitatolewa kwa wananchi wa eneo hili tunalolizungumzia kwa sababu tumewapa ahadi muda mrefu, tangu mwaka 2013 uthamini umefanyika. Mheshimiwa Mbunge anayehusika, mwenye jimbo lake, mara nyingi amekuwa akiniuliza na mimi huwa nampa majibu kwamba fedha tukizipata basi kipaumbele kitatolewa kwa eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pilli, kwamba Serikali huwa hailipi fidia, kwa kweli lengo la kulipa fidia lipo, lakini kama mnavyotambua kuna changamoto za kibajeti. Ni mategemeo yetu kwamba fedha hizi zikipatikana kwa kweli tutapunguza maeneo mengi sana ambayo yanatudai, kwa sababu hizi shilingi bilioni 20 zikipatikana siyo kwamba tutaweza kufikia maeneo mengi. Ni mategemeo yetu kwamba fedha hizi zitapatikana kama ambavyo Wizara ya Fedha ilishatoa ahadi hapa. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba hakuna sababu ya kufanya matembezi ya hisani katika hili, tutakachofanya ni kuendelea kuhimiza wenzetu wa Wizara ya Fedha wakiweza kupata fungu hili basi watupatie ili na sisi tuweze kutimiza ahadi zetu.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA. Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza. Tabora hasa Manispaa imezungukwa na kambi za jeshi kwa eneo kubwa. Kutokana na hali hiyo kumekuwa na migogoro mikubwa ambayo inapelekea wananchi ambao wamekuwa wakitumia maeneo kwa muda mrefu kufikia hata kupigwa wanapokuwa wanafanya shughuli zao. Kwa mfano, kuna eneo ambalo kuna barabara inapita katika kata nne eneo la Uyui, kuna eneo la Rada, barabara hii ni ya miaka mingi na ni hiyo tu ambayo wananchi wa kata hizo nne wanaitumia, ikifika saa moja na nusu mpaka saa mbili usiku, wananchi wakipita maeneo maeneo yale wamekuwa wakipigwa na wakati mwingine hata kunyanganywa vifaa vyao vya usafiri zikiwemo baskeli. Je, Serikali ina mpango gani kuhusiana na eneo hilo ambalo wananchi wamekuwa wakitumia kama barabara?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa shughuli nyingi zimesimama katika maeneo hayo hasa za wananchi ambao walikuwa wakitumia maeneo hayo kwa kulima ambayo wamekuwa wakilima muda mrefu, lakini wengine na shughuli zao za kiutamaduni kwenye mapori ambayo wamekuwa hata hawayapi athari yoyote. Je, kutokana na hali hiyo ambayo ni ya muda mrefu Mheshimiwa Waziri yupo tayari sasa kuja Tabora ili tuweze mimi na yeye kwenda kukagua maeneo haya na kuyapatia utatuzi ambao ni mgogoro wa muda mrefu? (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, kuhusu barabara inayopita kuelekea eneo la Rada la jeshi na kwamba wananchi wanapopita hapo wanapigwa, suala hili nitalifuatilia ili niweze kupata taarifa rasmi ya nini hasa kinachoendelea. Hakuna sheria inayoruhusu wananchi kupigwa, lakini kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge nitakuwa tayari kwenda kufanya ziara katika eneo hili la Tabora Mjini ili nijionee mimi mwenyewe hali ilivyo pale na tutafute ufumbuzi, suluhu kwa ajili ya maslahi ya pande zote. Ni vema wananchi watambue kwamba, yale mapori yanayoonekana kama hayana kazi, ni maeneo ambayo wanajeshi wanafanya mazoezi, kwa hiyo yana kazi maalum. Tukifanya hii ziara, tutaweza kuambatana na viongozi wa jeshi ili tuone ni ufumbuzi gani ambao unaweza ukapatikana.
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pesa hizo zilizokwenda kununua hayo matrekta ni pesa za walipakodi wa nchi hii na ni nyingi sana na mpaka sasa hivi karibu 2.9 billion hazijarejeshwa. Mkakati mahususi a kuhakikisha kwamba, hii pesa inarudi, ni upi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni kwa nini sasa wale wote ambao walikopa haya matrekta majina yao yasiwekwe kwenye magazeti tuwajue ni akinanani hao wanaokwamisha kurudisha mikopo ya Serikali? (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ruth Mollel, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi ni kwamba, fedha zilizokuwa zimekopeshwa ni bilioni tano na kitu ambazo zimesharudishwa ni bilioni mbili, yani tuko kwenye asilimia 45 ya urejeshaji, maana yake ni jitihada kubwa zimefanyika hapo na kiwango kilichobaki kitarejeshwa kwa sababu, fedha hizi hawajakopeshwa watu nje, zimekopeshwa ndani ya Mashirika ya SUMA-JKT lenyewe kwa maana hiyo wanafanya biashara mbalimbali. Sina shaka kabisa kwamba, fedha hizi zote zitarudi na faida itapatikana kwa sababu, SUMA-JKT limejiwezesha kimtaji kuanzisha biashara nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kuhusu majina ya waliokopa matrekta kwamba, yawekwe kwenye magazeti. Jambo hili lilishafanyika, majina yaliwekwa kwenye magazeti na fedha hizi zimeendelea kukusanywa. Naomba nitoe taarifa kwamba, tokea Mheshimiwa Rais ametoa kauli ya kwamba, watu wote waliokopa warejeshe, tayari wamekusanya bilioni mbili na milioni 900.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaendelea na jitihada hizi na kama tulivyosema SUMA-JKT itaanza kuuza mali za walikopa endapo hawatarejesha baada ya kukamilika kwa zoezi la ukusanyaji wa madeni.
MHE. ALHAJI ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na jibu zuri la Mheshimiwa Waziri mhusika, kuna viongozi wa Serikali na hata humu Bungeni waliokopa SUMA katika matrekta hayo. Mheshimiwa Waziri licha ya kuwatangaza wamefikishwa kwa Spika ili tutangaziwe humu Bungeni tujue ni wapi wanaodaiwa?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Bulembo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba wako viongozi wa Serikali na baadhi ya Wabunge waliokopa matrekta haya. Juhudi tulizozifanya ni kwamba, tuliziandikia mamlaka za ajira za kila mmoja, kwa hivyo, Mheshimiwa Spika anayo orodha ya Wabunge na Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya waliohusika tumeandika barua TAMISEMI na Wizara zote kwa ujumla, kila mamlaka ya ajira imeandikiwa barua. Ni mategemeo yangu kwamba, kila mamlaka ya ajira itachukua hatua stahili ili kuweza kuzipata fedha hizi.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza:-
Mheshimiwa Spika, nianze kwa kueleza masikitiko yangu kwa jinsi ambavyo wataalam wetu wanawapotosha Mawaziri wetu. Eneo tunalolizungumzia ni sehemu ya skimu ya umwagiliaji inayogusa vijiji vitatu katika Kata ya Mwakijembe yenye ukubwa wa takribani hekta 450 na tayari Serikali imetumia zaidi ya shilingi bilioni 1.2 kuendeleza skimu hii. Kwa hiyo, siyo kweli kwamba sehemu tunayoizungumzia ilikuwa ni shamba darasa isipokuwa ni sehemu ya skimu ya umwagiliaji.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, eneo lililochukuliwa siyo hekari moja kama inavyozungumziwa bali ni takribani hekari 50, watu takribani 28 wamekumbwa na kadhia hii. Kwa sababu Waziri amepotoshwa, je, yupo tayari kuja kujionea yeye mwenyewe kule Mkinga ili wananchi hao watendewe haki?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa jambo hili nimekuwa nikilizungumza mara kwa mara hasa kwenye michango yangu ya maandishi nimekuwa nikitoa na takwimu ya uonevu huu na mara ya mwisho nilisema ni watu 14 na hii ilikuwa mwaka jana sasa imeongezeka wamekuwa watu 28 na sasa ni hekari karibu 50 zimechukuliwa. Je, Waziri yuko tayari kutoa tamko hapa la zuio kwamba kikosi kile kilichopo kule kiache tabia hii ya kuchukua ardhi ya wananchi bila ridhaa ya kijiji?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa takwimu zilizopo katika Wizara yangu na zile anazotoa Mheshimiwa Mbunge zinapishana, nadhani ni busara tukafanya kile alichoomba kifanyike nacho ni mimi kufanya ziara katika eneo hilo ili kukagua kwa pamoja kati ya upande wetu sisi kama Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa tukifuatana na wataalam wa Jeshi pamoja na watu wa Wilaya na Kijiji husika ili tuthibitishe ukubwa wa eneo lililochukuliwa na nani anayewajibika kulipa fidia. Endapo itathibitika kwamba Serikali kwa upande wetu Wizara ya Ulinzi inalazimika kulipa fidia basi tutafanya hivyo.
MHE. ALHAJ ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwinyi sitaki kukuuliza maswali kila siku lakini naomba swali hili utoe tamko. Wananchi wa Makoko katika Manispaa ya Musoma wanadai fidia mwaka wa 13, swali hili nimeshaliuliza humu, Katibu Mkuu amewapelekea barua ya kuwapa subira. Watu wamekufa, wamerithi, wameacha maeneo yao; miaka 13 Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi, naomba utoe tamko hapa Bungeni watu hawa watalipwa lini.
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Alhaj Bulembo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, suala la ulipaji wa fidia kwa maeneo yaliyotwaliwa na Jeshi lipo katika maeneo mengi. Kila mwaka wakati tunawasilisha bajeti yetu nimekuwa nikisema kwamba fedha zikitengwa tutalipa fidia. Kwa bahati mbaya fedha zinazotengwa au zinazotolewa hazikidhi kulipa watu wote kwa wakati mmoja.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka huu wa fedha tunaoumalizia tumelipa fidia eneo la Kilwa kwa ajili ya Navy Base kuwepo pale lakini bado tunatarajia Wizara ya Fedha itatupatia fedha kabla ya mwisho wa mwaka huu wa bajeti ili tuendelee kulipa fidia hizo. Tunatambua kwamba eneo la Makoko linastahili kulipwa fidia pamoja na maeneo mengine kadhaa na tutafanya hivyo kadri fedha zinapopatikana.
MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naomba nichukue fursa hii kumuuliza swali dogo Mheshimiwa Waziri wa Jeshi la Ulinzi.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa eneo la Jeshi la Kambi ya Kaboya katika Vijiji vya Mayondwe na Bugasha uhakiki ulishafanyika na kwa sababu wakati wowote Waziri anategemea kupata pesa kutoka Wizara ya Fedha, anaweza kuwahakikishia wananchi hao kwamba baada ya kulipa Kilwa sasa ni zamu ya Kaboya kabla ya mwezi Juni?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwijage, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema awali ni maeneo mengi ambayo tunastahili kulipa fidia na baadhi uhakiki umeshafanyika kama anavyosema Mheshimiwa Mbunge. Natambua kwamba eneo la Kaboya linastahili fidia na uhakiki umekamilika tunachosubiri ni fedha. Kwa maana hiyo nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba fedha zilizotengwa katika bajeti endapo zitapatikana kabla ya mwisho wa mwaka huu basi Kaboya nayo tutaijumuisha katika maeneo yatakayolipwa fidia.
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni muda mrefu sana nimekuwa nikizungumzia suala la mgogoro kati ya Wanajeshi pale Mikumi na Kitongoji cha Vikweme ambao walihamishwa kwenye Hifadhi ya Mikumi mbugani kwenda kule kwenye Vitongoji vya Vikweme tangu mwaka 1963 lakini Jeshi wamevamia eneo hilo na kuwaondoa wananchi wale kwa maumivu makali sana. Kwa kuwa suala hili nimeliongea mara nyingi, je, Waziri yupo tayari baada ya Bunge hili tuweze kuongozana ili aweze kuwasikiliza wananchi wa Jimbo la Mikumi pale Vikweme ambao wamekuwa na kilio cha muda mrefu na hasa ikizingatiwa kwamba wananchi wengi wa Mikumi tunategemea Kitongoji hiki kufanya shughuli zetu za kilimo na kujiletea maendeleo.
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Joseph Haule, Mbunge wa Mikumi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli tumewahi kuzungumzia suala hili na kama nilivyosema awali maeneo mengi yana migogoro kati ya Jeshi na wananchi kuhusiana na masuala ya ardhi. Mimi nipo tayari kufanya hiyo ziara kama anavyoshauri Mheshimiwa Mbunge ili tukaangalie ni nani hasa mwenye haki katika eneo hilo na endapo itathibitika kwamba Jeshi linalazimika kulipa fidia kama nilivyosema, tutafanya hivyo.
MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Majeshi yetu na hususan Jeshi la Wananchi ndicho chombo ambacho tunakiamini sana kwamba kina wajibu wa kulinda mipaka yetu na usalama wa raia na nchi yetu katika ujumla wake.
Mheshimiwa Spika, hivi karibuni katika mpaka wa Namanga tulishuhudia kupitia vyombo vya habari vurugu kubwa zilizofanywa upande wa Kenya ambapo magari, abiria na mizigo kutoka Tanzania yakiwemo magari yalizuiliwa na wananchi wa Kenya na kusababisha vurugu kubwa katika mpaka ule. Mheshimiwa Waziri anatupa tamko gani kama Waziri wa Ulinzi kuhusu usalama wa nchi yetu katika mpaka ule na nini kilipelekea tukio lile likafanyika likasababisha vurugu zile?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Freeman Mbowe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Jeshi la Ulinzi lina wajibu wa ulinzi wa mipaka lakini Vyombo hivi vya Ulinzi na Usalama vina majukumu tofauti. Suala la usalama wa raia ni suala la Polisi na kuna vyombo vingine vingi vya ulinzi na usalama ambavyo vina majukumu ya kulinda usalama katika maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, nachoweza kusema ni kwamba mpaka wetu kati ya Tanzania na Kenya kwa upande huo hauna tatizo lolote. Ulinzi upo pale wa kutosha na hizi vurugu zilizotokea nadhani lilikuwa ni jukumu la vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuhakikisha kwamba wanalishughulikia. Taarifa nilizonazo ni kwamba suala hili limeshughulikiwa na lilimalizwa. Kwa maana hiyo hatutarajii matukio kama haya yaendelee kutokea.
MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri lakini nina swali moja dogo la nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, upimaji wa pili wa mipaka uliofanywa mwaka 1985 uliingia mpaka katika maeneo ya wananchi ambapo wamechukua eneo kubwa la wananchi. Wananchi wamekuwa wakilalamika kuwa ile mipaka mipya imeingia ndani ya maeneo ya wananchi ambao walikuwepo pale tangu miaka 1960 tofuati na ile mipaka ya mwaka 1978. Je, Serikali ipo tayari kuwaachia maeneo yao yale ya mwanzo kwa mipaka ile ya mwaka 1978 kwa sababu mipaka ya mwaka 1985 imeingia katika makazi ya wananchi?. Je, Mheshimiwa Waziri yupo tayari kutuhakikishia jambo hili ili migogoro hii iweze kuisha?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, bahati nzuri mimi mwenyewe nimetembelea eneo hilo la Kisakasaka na nilipata maelezo ya kina juu ya mgogoro huu. Kilichopo ni kwamba wananchi wanadai eneo ambalo wao wapo ni la kwao wakati Jeshi wanadai walikuwepo muda mrefu katika eneo hilo.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema, kuna wakati CDF Mstaafu, Jenerali Mwamunyange, alikwenda pale; na katika kulimaliza tatizo hili, alitoa agizo la kurekebishwa kwa mipaka ili wananchi waliokuwa ndani ya Kambi ya Jeshi wawe nje. Kazi hiyo ilifanyika lakini bado wananchi wale hawajaridhika na utaratibu huo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kama nilivyosema awali, tunaunda Kamati au Tume ndogo itakayopitia matatizo ya migogoro ya ardhi katika Zanzibar nzima, kwa sababu siyo hapa tu, kuna maeneo mengi yana migogoro; ili tuweze kupata ufumbuzi wa kudumu. Kwa wale wanaostahili fidia, watalipwa fidia na wale ambao hawana haki, basi watalazimika kuyaachia maeneo hayo ili Jeshi liweze kufanya shughuli zake.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Migogoro ya ardhi kati ya Jeshi na wananchi, kama alivyosema ipo nchi nzima, lakini nimekuwa nikizungumzia utatuzi wa mgogoro kati ya Jeshi la Wananchi na Mtaa wa Bugosi na Kenyambi kule Tarime ambao umedumu kwa muda mrefu sana na Mheshimiwa Waziri anaelewa; ni lini sasa Serikali itaona kwamba imeshindwa kupata fedha za fidia kuwalipa hawa wananchi, ukizingatia Jeshi la Wananchi limetoka kwenye Kambi yao, limekuja kwenye makazi ya wananchi?
Mheshimiwa Spika, kama hakuna fedha, tunaomba warudishe hii ardhi kwa wananchi ili waendelee na shughuli zao za maendeleo. Ni lini Serikali itawarudishia ardhi wananchi hawa wa Tarime?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, ni kweli kuna tatizo la mgogoro wa ardhi katika eneo hili la Tarime la muda mrefu, ninayo taarifa hii, tumeshazungumza mara kadhaa na Mheshimiwa Mbunge. Wataalam wameshauri na tathmini ya fidia imefanyika, kinachosubiriwa ni fedha ili ziweze kulipwa.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema, katika mwaka huu wa fedha, bajeti yetu ilikuwa ni shilingi bilioni 20 katika kulipa fidia na upimaji wa ardhi katika maeneo mbalimbali. Bahati mbaya sana tumepokea kama shilingi bilioni tatu ambazo tumeshazilipa kule Kilwa, lakini mwaka wa fedha haujaisha, tuna matumaini kwamba fedha zitapatikana na zikipatikana tutaendelea kulipa katika maeneo haya ambayo uhakiki umeshafanyika.
Mheshimiwa Spika, namwomba Mheshimiwa Esther avute subira, ajue kwamba Jeshi nalo lina umuhimu wa kuwepo maeneo haya. Katika ulinzi wa nchi lazima tuone umuhimu wa taasisi hii ya Jeshi kuwepo. Siyo vizuri au siyo rahisi tu kusema kwamba kila ambapo tunashindwa kulipa fidia kwa wakati, basi Jeshi liondoke wananchi warudishiwe ardhi; ulinzi utafanywa na nani? Kwa hiyo, naomba subira iendelee na bila shaka tutalimaliza tatizo hili kwa haraka iwezekanavyo.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza imeelezwa kwamba TFDA ndiyo Mamlaka ambayo inashughulikia chakula na dawa, lakini kwa hali ya uhalisia TFDA yenyewe capacity yake ni ndogo sana ya kuweza kupima vinasaba vyote Tanzania nzima kwa sababu Ofisi yao Kuu iko pale Dar es Salaam na wana vifaa vichache sana.
MWENYEKITI: Uliza swali.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu, je, ni lini Serikali itaiongezea vifaa TFDA iweze kufanya kazi yake sawasawa nchi nzima?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuna dawa pia ambazo inasemekana na wataalam wa afya, kwamba zinapelekea kuharibu miili ya binadamu na hasa zile dawa za kufanya rangi ya watu weusi iweze kuwa nyeupe, je, Serikali imechukua hatua gani mpaka hivi sasa ili kuwafanya Watanzania wengi wanaotumia dawa hizi wasiweze kupata madhara?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA (K.n.y. WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maftaha kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nataka nimhakikishie kwamba uwezo wa TFDA sio mdogo kama anavyodhani, Taasisi hii ni kubwa, ina Maabara ya kisasa sana pale Dar es Salaam lakini pia imeanza kujenga uwezo Kikanda na sio kwamba wanafanya kazi Dar es Salaam peke yake, wako katika Kanda mbalimbali katika nchi yetu, na wana maabara inayotembea, (mobile lab) kwa maana hiyo nadhani uwezo wao ni mzuri na wataendelea kuuboresha ili kuweza kufika nchi nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili la dawa ambazo zinasababisha au tunaziita hizi dawa za kujichubua, ili watu wabadilike rangi zao, hili napenda nimwarifu Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu, kwamba TFDA imekuwa ikichukua hatua mara nyingi sana. Dawa nyingi sana zimeshaondolewa kwenye soko zenye madhara haya na hizi mara nyingi ni dawa ambazo zina maada inayoitwa steroid ambazo kwa kweli zinaharibu ngozi na zinaweza kusababisha madhara makubwa, zimekuwa zikiondolewa na wahusika wamekuwa wakipigwa faini na kwa maana hiyo sasa hivi kuna udhibiti mzuri sana wa dawa zinazosababisha madhara haya.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kumekuwa na wimbi kubwa la ongezeko la matumizi ya dawa za nguvu za kiume, enzi zenu nakumbuka kulikuwa na mkuyati, lakini sasa hivi, kuna super moringe, mundende, super gafina, gasosi mix, super shafti, sado power, amsha mzuka, Kongo dust na hii Kongo dust imeonesha kuwa mafanikio makubwa. Je, Serikali imeshafanya utafiti nini kinasababisha tatizo hili la watu kutokuwa na nguvu za kiume kupelekea kutumia sana hizi dawa?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA (K.n.y. WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mlinga kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu zinazopelekea kupungua kwa nguvu za kiume ni nyingi, ikiwemo magonjwa mbalimbali kama vile kisukari, msongo wa mawazo na kadhalika, kwa hiyo kuna sababu nyingi zinazopelekea matatizo haya na ndio maana watu wengi wamekuwa wakitafuta ufumbuzi wa tatizo hilo. Ninachoweza kusema hapa ni kwamba ziko dawa zenye maada ambazo sio za kikemikali, ambazo ni bora zaidi zitumike kuliko kemikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili kama nilivyosema awali TFDA wanao uwezo wa kubaini ni dawa gani ambazo zinasababisha madhara na zile ambazo zinasababisha hakuna budi kutolewa taarifa mapema ili ziweze kuondolewa kwenye soko, lakini tunatambua kwamba sasa hivi kuna dawa zilizopitishwa na Mamlaka za Udhibiti ambazo zinauzwa kihalali kabisa za kuweza kuongeza nguvu za kiume na ambazo hazijaripotiwa kuwa kuna matatizo kama ya athari zinazopelekea kutokana na matumizi ya dawa hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wetu ni kwamba wanaotaka kutumia dawa hizi waendelee kutumia zile ambazo zimethibitishwa kitaalam na wasitumie zile ambazo hazina uthibitisho ili wasiweze kupata madhara.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na wimbi kubwa la wanaume na vijana kutumia dawa za kuongeza nguvu za kiume, sasa hivi kuna baadhi wanatumia dawa za kukuza maumbile ya kiume, nataka kujua nini madhara yake na ni kwa nini wanafanya hivi?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA (K.n.y. WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Susan Lyimo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na taarifa nyingi za dawa zinazoweza kukuza maumbile na wito wangu ni kwamba, watu waendelee kuhakikisha kwamba hawatumii dawa yoyote ambayo haijasajiliwa, haijathibitishwa kitaalamu kwa sababu inaweza ikasababisha madhara na wale ambao wanatoa taarifa hizi bila ya uthibitisho kwa kweli wanafanya kosa na wanatakiwa wachukuliwe hatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taarifa nilizokuwa nazo ni kwamba hakuna dawa yoyote ambayo kitaalam imethibitishwa na imepewa kibali kwa ajili ya matumizi kama hayo. Kwa hivyo nawaomba Watanzania wawe makini wanapotaka kununua dawa kama hizi kwa sababu zinaweza zikawa zina madhara. Tungependa wananchi watoe taarifa endapo wamewahi kutumia na wamepata madhara yoyote ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, fedha ambayo Mheshimiwa Waziri ameitaja ya malipo ya shilingi bilioni 3 ni ile ambayo inaenda kulipwa kule Kilwa Masoko, Rasi Mshindo na Navy Command. Kuna maeneo yaliyotwaliwa na Jeshi baadhi ya wananchi wameshafariki dunia na Serikali inaendelea kutekeleza miradi mikubwa kwa fedha za ndani ikionyesha kwamba wananchi hawa tayari wamedhulumiwa na hawana chao.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali utuambie ni kwa nini basi mmechukua muda mrefu hamtaki kuwalipa wananchi hawa ili hali mnaenda kutekeleza miradi mikubwa ndani ya nchi kwa fedha za ndani? Lini fedha za wananchi hawa zitapatikana?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, taarifa ya utekelezaji wa ahadi za Serikali mwaka 2006 ilieleza wazi kuna maeneo kadhaa ya Jeshi yaliyoorodheshwa ambapo wananchi wanadai fidia na Serikali ikaahidi kwamba itaendelea kulipa. Ukiangalia bajeti iliyopita shilingi bilioni 27 fedha hazikutolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri atuambie bajeti yake ya kesho anawaambia nini wananchi hawa wanaolalamika kwa muda mrefu, wamekata tama na wengine wameshafariki na lakini hawana mategemeo ya kulipwa fedha zao? Naomba Waziri atuambie waziwazi wananchi hawa ambao wamekata tamaa, wanyonge hawa na ninyi ndiyo watetezi wa wanyonge watapata lini? Naomba majibu ya kweli.
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Masoud Abdalah Salim, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba shilingi bilioni 3 zilizotolewa ni kwa ajili ya Rasi Mshindo kule Kilwa. Nimpe tu taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba kati ya fedha tulizoidhinishiwa bajeti iliyopita shilingi bilioni 20.9 ukiacha shilingi bilioni tatu ambazo zimeshalipwa shilingi bilioni 16 zimeshatengwa na kazi inayofanyika sasa hivi ni uhakiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ukichukua zile shilingi bilioni tatu na shilingi bilioni 16 utaona shilingi bilioni 19 zitatolewa katika bajeti hii ambayo tunamalizia. Kwa hiyo, hatuna shaka kwamba baada ya uhakiki maeneo mengi haya yatalipwa.
Kuhusu bajeti ijayo, namwomba Mheshimiwa Mbunge avute subira. Ukweli ni kwamba kama tutafanikisha kulipa shilingi bilioni 19 kati ya shilingi bilioni 20 zilizotengwa katika bajeti tunayomalizia basi bila shaka kwa sehemu kubwa tutakuwa tumetimiza ahadi zetu.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza, shirika limekuwa likipata tenda kutoka ndani ya Serikali na limekuwa likifanya kazi hizi kwa weledi mkubwa sana. Je, Serikali ina mikakati gani kuhakikisha shirika linalipwa kwa wakati ili hata zile changamoto ndogondogo wanapopata zile hela kwa wakati wapate kuzitatua wenyewe?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; miundombinu ya haya mashirika, hiki Kikosi cha Mizinga kwenye makambi mengi ni chakavu na si rafiki sana na ni siku nyingi. Sasa Serikali ina mikakati gani ya kutenga fedha na kuangalia hiki kitengo kwa sababu hiki kitengo ni kwa kazi maalum na kinafanya kazi kwa ujasiri na kwa weledi mkubwa. Je, Serikali na Wizara ya Fedha ina mkakati gani kuhakikisha kwamba kile kinachotengwa kwa ajili ya kitengo hiki kinapelekwa ili kutoa hizi changamoto ambazo zipo katika Kikosi hiki cha Mizinga katika hili Shirika la Mzinga? Ahsante.
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maryam Msabaha kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu malipo kwa kazi ambazo shirika linafanya za Serikali naweza nikamueleza Mheshimiwa Mbunge kwamba malipo hayo yanafanyika. Hivi karibuni Shirika la Ujenzi la Mzinga limepata kazi kadhaa ikiwemo ujenzi wa ofisi za Serikali hapa Dodoma, lakini katika baadhi ya halmashauri pia wamekuwa wakipata kazi. Kwa taarifa nilizokuwa nazo ni kwamba malipo yanafanyika na fedha hizo zinawasaidia kuboresha mambo madogomadogo katika shirika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu miundombinu ya shirika lenyewe; ni kweli kwamba kwa kiwango kikubwa miundombinu pale katika Shirika la Mzinga imechakaa, ni ya muda mrefu na ndiyo maana kama nilivyosema katika jibu langu la msingi ni kwamba sasa wametengeneza mpango mkakati ambao kwa kiwango kikubwa ukipata fedha utaweza kushughulikia yote haya ikiwemo kuboresha miundombinu, lakini kuleta wataalam waliobobea katika fani hizo na kuwa na mtaji wa kuweza kuendeleza shirika hili. Ni matumaini yetu kwamba mpango mkakati huo utapitishwa na Serikali ili shirika liweze kupata fedha na kuweza kuboresha miundombinu yake.
MHE. KANALI (MSTAAFU) MASOUD ALI KHAMIS: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri ambayo yamefafanua na itawasaidia wale ambao walikuwa na utata kuhusu jambo hili, lakini pia nina swali moja la nyongeza;
Mheshimiwa Spika, nyumba nyingi za Jeshi wanazoishi Wanajeshi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania kupata athari na kuharibika wakati mwingine hufika wakati hawa wakashindwa hata kuishi Askari. Je, Serikali haioni sasa umefika muda wa kuwapa uwezo wanaoishi katika nyumba hizi kuzifanyia matengenezo kwa kupitia kitengo cha ujenzi ndani ya Jeshi, kuzifanyia tadhimini na baadaye kumruhusu anayeishi kufanya matengenezo na kumrudishia hela zake.(Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, wazo hilo ni nzuri, kwamba kitengo cha ujenzi cha Jeshi kifanye tathmini na kuwaruhusu wanaoishi wazitengeneze na kisha kulipwa lakini utekelezaji wake una shida kidogo kwa sababu ya uwezo wa kulipa fedha hizo, ndiyo maana sasa hivi kupitia bajeti ya maintenance ya Ngome tunafanya ukarabati mdogo mdogo kwa maofisi na makazi ya Wanajeshi katika kambi mbalimbli lakini kasi yake ni ndogo kutokana na uwezo uliopo. Kwa hiyo, wazo hili linapokelewa na pale uwezo utakapo ruhusu basi litafanyiwa kazi. (Makofi)
MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Waziri anakiri katika masuala yake kwamba elimu ilitolewa baada ya vita vya Kagera, lakini waathirika wakubwa katika kadhia hii ya mabomu ni watoto wadogo hasa wanafunzi wa shule za msingi. Inaonekana kabisa kwamba elimu hawajapatiwa ya kutosha au hata kama inapelekwa haiwafikii. Sasa swali langu lipo hapa; je, Serikali iko tayari kuingiza kipindi maalum katika masomo yao wanafunzi wa shule za msingi ili wapatiwe elimu ya kujikinga na mabomu na athari zake? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, umiliki na udhibiti wa silaha za mabomu pamoja na silaha nyingine ni jukumu la vyombo vya ulinzi na usalama. Kwa hiyo, kutapakaa hovyo kwa mabomu kumepelekea wanafunzi wa Shule ya Kihanga, Ngara, Kagera kupoteza maisha na wengine wengi wao kujeruhiwa. Je, Serikali iko tayari kuwalipa fidia wale waliopata janga hili? Ahsante.
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la kwanza kwamba Serikali iwe tayari kuingiza somo maalum katika mitaala ya shule za misingi, hili ni wazo zuri na linazungumzika na sisi tutaendelea kuzungumza na wenzetu wa Wizara zinazohusika na elimu ili kuweza kuona uwezekano wake. Wakati hayo yanaendelea, elimu imekuwa ikitolewa katika maeneo hususan yale maeneo ambayo yanaonekana yana matatizo na lengo ni kuwapa elimu wahusika na wao waweze kupeleka katika shule zinazopatikana katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili la kwamba inapotokea kwamba mtu amepata tatizo linalohusiana na mabomu au silaha nyingine mbalimbali basi walipwe fidia, niseme tu kwamba kwa kiwango kikubwa ili kuweza kuondoa tatizo hili, ni muhimu kuhakikisha kwamba elimu inatolewa. Kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi kwamba wahandisi wetu wa medani mara zote wamekuwa tayari kwenda katika maeneo yenye mashaka, yenye matatizo ili kuweza kuondoa mabomu haya ili kuepuka athari badala ya kujikita katika suala la kusubiri watu wapate matatizo halafu fidia zitolewe. Hata hivyo, ikithibitika kwamba aliyepata madhara haya yametokana na mabomu ya kutupwa kwa mkono ambayo hayakuweza kuondolewa kwa wakati, basi kwa kawaida fidia huwa zinatolewa.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja dogo Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inapotokea athari ya vifo au majeruhi kwa wananchi waliopata milipuko ya mabomu au kuokota mabomu, Serikali mara nyingi huwa wanatoa fidia kama kule Mbagala na Gongo la Mboto. Mheshimiwa Waziri utakumbuka kwamba kule Tunguu kuna watoto waliokota mabomu na walifariki wawili na wananchi wengine walipata majeruhi. Narudia hili kwa Mheshimiwa kwamba wale watu wataweza kupewa fidia. Ni kwa nini basi hadi leo wale watoto wawili au na majeruhi kule Tunguu ambao walipata athari hii hawajapata fidia? Na ni lini watapata fidia yao?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepokea tatizo hili lililotokea Tunguu, nitamuomba Mheshimiwa Mbunge anipe uhakika wa suala lenyewe kwa maandishi ili liweze kufanyiwa kazi. (Makofi)
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake japo hayajaniridhisha kwa sababu swali langu la msingi nilihitaji kujua ni vijana wangapi kutoka Wilaya ya Kaskazini A na Wilaya ya Kaskazini B ndani ya Mkoa wa Kaskazini Unguja ambao wamepata ajira katika jeshi kwa miaka mitatu, lakini amenipa jibu la jumla la Zanzibar yote.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nilitaka kujua ni lini vijana wa Mkoa wa Kaskazini Unguja watapata ajira katika jeshi ili kuondoa malalamiko yaliyopo hivi sasa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili kwa kuwa manug’uniko ni mengi yanayotokana na vijana kujitolea kwa muda mrefu lakini hawapati ajira. Ni mkakati gani ambao Serikali umeupanga ili kuhakikisha vijana hawa wanapata ajira hiyo kwa kuzingatia pia jinsia maana hapa katika orodha yake inaonyesha wanaume 720 wanawake 280?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Malembeka kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali la kwanza anasema sikumpa takwimu za ni vijana wangapi kutoka Wilaya ya Kaskazini A na B waliojiunga na JKT. Katika jibu langu la msingi nilitoa takwimu za jumla za vijana wanaochukuliwa kutoka Zanzibar na nikaeleza kwamba jukumu la kupanga idadi kwa Wilaya za Zanzibar linafanywa na SMZ. Kwa hivyo takwimu sina na Mheshimiwa akizihitaji itabidi azipate kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa sababu wao ndiyo wanapanga kwa mujibu wanavyoamua, sisi tunakabidhi kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wao wanagawa wanavyopenda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, katika hilo hilo la kwanza alikuwa anauliza lini vijana watapata ajira ili kuondoa malalamiko. Nataka ieleweke kwamba kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa lazima vijana waelewe kwamba siyo ajira, kujiunga na JKT ni kwenda kupata mafunzo ya kijeshi pamoja na study za kazi. Wachache watapata ajira katika vyombo vya Ulinzi na Usalama, walio wengi watabidi wajiajiri wenyewe au waajiriwe na sekta binafsi. Hili ni muhimu lieleweke, wasielewe kwamba kujiunga na JKT ndiyo ajira. Tunachukua vijana wengi na nilitoa takwimu hapa wakati wa bajeti yangu kwamba tunachukua takribani vijana 20,000 kwa mwaka. Vyombo vya ulinzi na usalama havina uwezo wa ku-observe kuchukua wote hao katika ajira, watapata wachache na walio wengi watakuwa wamepata study za kazi ili waweze kujiajiri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ni mkakati gani wa kupatia ajira na kwa kuzingatia jinsia, hawa tuliowataja ni vijana wanaojiunga na JKT na siyo ajira. Kwa maana hiyo kule wanapofanya usaili kuna vigezo ambavyo vinafuatwa, mara nyingi wasichana hawajitokezi kwa wingi lakini wanaojitokeza wengine wanakosa sifa zinazotakiwa na ndiyo maana unaona kuna tofauti ya idadi hapa. Kwa hiyo, mkakati uliopo ni kuwasaidia vijana hawa, wale wanaokosa ajira katika vyombo vya ulinzi na usalama kuweza kuwapa study za kazi ili waweze kuajiriwa na sekta nyingine pamoja na kujiajiri wao wenyewe.