Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Doto Mashaka Biteko (8 total)

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. DOTO M. BITEKO – MWENYEKITI WA KAMATI YA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa
Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii nikushukuru sana wewe kwa kunipa fursa hii, lakini
vilevile niwashukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini pamoja na Waziri wa
Nishati na Madini na Wabunge wote waliochangia hoja hii. Kwa kweli michango yao imekuwa
mizuri na imeboresha sana taarifa yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, wachangiaji kwenye hoja yetu walikuwa 32, hawa wote 32
wamechangia kwa kusema, lakini Waheshimiwa Wabunge tisa wamechangia kwa kuandika.
Katika kujumuisha hoja yetu nitaelezea tu mambo machache ambayo yamejitokeza kwenye
michango ya Waheshimiwa Wabunge na wachangiaji wengine kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo kubwa ambalo Waheshimiwa Wabunge wengi
wamelichangia ni suala la umeme, na suala la umeme hili wamelijadili katika maeneo yote
mawili – upande wa TANESCO na upande wa REA, hoja hii imechangiwa na Wabunge 27. Kwa
upande wa TANESCO, Waheshimiwa Wabunge wengi wameeleza masikitiko yao, wameeleza
msisitizo wao, wametoa maoni yao juu ya madeni ya TANESCO na kuomba kuwepo kwa
namna ambayo TANESCO itaweza kutoka kwenye mkinzano huu wa madeni makubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwenye upande wa REA, Waheshimiwa Wabunge wengi
wamezungumzia juu ya usimamizi wa miradi ya REA, wamezungumzia vilevile upelekaji wa
fedha za miradi ya REA na na wakandarasi kuwashirikisha viongozi wakati wakandarasi hao
wanapokwenda site na kuongeza ule wigo (scope) kwenye maeneo ambako miradi hii
inakwenda. Mambo haya yote kwenye taarifa yetu tuliyaeleza na Waheshimiwa Wabunge
nawashukuru sana kwa michango yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa madini jumla ya Wabunge 19 wamechangia
hoja hii, na mambo yaliyojitokeza kwenye michango yao ni pamoja na suala la wachimbaji
wadogo wadogo. Kwanza wachimbaji wadogo wadogo kupatiwa maeneo ya kuchimba, lakini
vilevile wachimbaji hawa wadogo wadogo kupatiwa ruzuku ili iweze kuwasaidia kuchimba
kisasa. Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumzia vilevile hili jambo la wachimbaji
wadogo wadogo kuvamia leseni za wachimbaji, jambo hili kwenye Kamati pia na Serikali ilitupa
ufafanuzi wa kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia wamezungumzia suala la Tanzanite. Tanzanite
kupatikana Tanzania na Tanzania isiwe ya kwanza kwenye muuzaji wa Tanzanite linawakera
Waheshimiwa Wabunge wengi kama ambavyo linawakera Watanzania wengi. Lakini naomba
tu nitoe taarifa, Serikali jambo hili imelichukua kwa uzito wake na kwenye kamati tulipewa
taarifa kwamba Serikali imepeleka ukaguzi maalum (special audit) na nilidhani tusizungumze
sana hili kwa sababu baada ya taarifa ile kuja tutakuwa na mahali pa kuanzia kuishauri Serikali
vizuri. Kwa hiyo, nadhani hili tuiachie Serikali kwa sababu imeshalichukua kwa uzito wa aina
yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumzia STAMICO,
Wabunge sita wamechangia juu ya STAMICO na wameelezea juu ya kuhodhi maeneo mengi
ya STAMICO. Hili ni kweli, lakini hata kwenye kamati wajumbe walilizungumza kwa uchungu sana
kwa sababu STAMICO ana maeneo mengi ambayo ameyashikilia lakini hachimbi, ameingia
ubia na wawekezaji, wale wawekezaji kwa miaka karibu 12 hakuna wanachofanya. Tunaitaka
na kuiomba Serikali kwamba sasa ifike mahali hawa wabia walioingia JV na STAMICO waanze
kufanya kazi, vinginevyo itakuwa ni kupoteza muda.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wanaovamia yale maeneo ambayo yako dormant
utakosa sababu ya kuwaondoa kwa sababu wewe hilo eneo umelishika. Kwa mfano
Mheshimiwa Bukwimba amezungumzia suala la Bacllif. Pale kuna leseni 12 ambazo STAMICO
wameingia mkataba pamoja na TANZAM 2000; lakini toka wameingia makubaliano hayo
hakuna kinachoendelea. Kwa hiyo, wananchi wale wanaweza kuvamia kwa sababu hawaoni
jambo lolote linaloendelea, na Serikali imechukua hatua juu ya jambo hili, inaielekeza STAMICO Mheshimiwa Naibu Spika, na niwaombe Waheshimiwa Wabunge waliopendekeza
kuifuta STAMICO, mimi nadhani tui-capacitate STAMICO. Itakuwa ni jambo la aibu sana sisi
wenyewe, Serikali, Watanzania tunaanzisha shirika letu wenyewe tunaliua halafu tunaanzisha
lingine, kwani Watanzania tutawatoa wapi? Si ni hawahawa tutakaowapata kuunda shirika
lingine? Mimi nilikuwa naomba tuipe nguvu, tuisimamie vizuri STAMICO iweze ku-deliver kwa
wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kinachopungua pale STAMICO ni mambo mawili; jambo la
kwanza ni upelekwaji wa fedha lakini jambo la pili ni usimamizi ulio madhubuti. Mimi naomba
nichukue nafasi hii kuwapongeza sana Wizara, kila mara wanapitishapitisha mikono yao pale
STAMICO. Ninaamini baada ya muda fulani pengine tunaweza tukaona matokeo yanabadilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, upo mgodo wa Serikali ambao ni wa Stamigold. Mgodi huu
unasimamiwa vizuri sana na Watanzania, kuanzia mfagizi, mlinzi mpaka MD wa mgodi ule ni
Mtanzania, mswahili mwenzetu. Nao wana changamoto ambazo wamezieleza. Changamoto
ya kwanza wanayoizungumzia hawana MDA, ile Mining Development Agreement,
tumewaomba Serikali wahakikishe wanafanya kazi ya kuwapatia hiyo MDA.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile mitambo waliyonayo yote ni ya kukodi hawana
mtambo hata mmoja wa kwao, jambo ambalo linasababisha gharama ya uendeshaji wa
mgodi ule kuwa kubwa sana, zaidi ya asilimia 31.7 ya gharama za uendeshaji zote zinakwenda
kwenye ukodishaji wa mitambo. Tumeiomba Serikali na katika hili nitumie nafasi hii kuiomba
Wazara ya Fedha kama migodi mikubwa ya kigeni tunaipa exemption ya mafuta, kwa nini
mgodi wetu wenyewe wa Stamigold ambao kwa asilimia mia moja ni wa Serikali, na wenyewe
tusiupe exemption ili na wao wapunguze gharama za uendeshaji, tuapte faida haraka?
Tunatoa fursa hii kwa wageni, migodi ya ndani tunaibinya, nilikuwa naomba jambo hili
lichukuliwe kwa uzito wake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wamezungumza juu ya mafuta, ujenzi wa farm tank na hili
tumelipata kutoka kwa wadau wote tuliokutana nao, wameeleza umuhimu wa kuwa na
Central Storage System ya mafuta baada ya kuwa yamepakuliwa kabla ya kusafirishwa
kwenda kwa watumiaji wengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, nirudie tena, niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa
michango yao na kwa kweli niseme toka nimekaa kusikiliza mchangiaji wa kwanza mpaka wa
mwisho mimi binafsi nimejifunza vitu vingi. Wameona mambo haya kwa macho ya tofauti
pengine na kamati tulivyoona. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, ninaomba sasa Bunge lako likubali
kuipokea taarifa hii na kuwa Maazimio ya Bunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. DOTO M. BITEKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nami nichukue nafasi hii nikushukuru sana kwa kunipa nafasi hii na kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kusimama hapa, nichukue nafasi hii kuwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Bukombe kwa kunichagua na kunituma niwe mwakilishi wao katika nyumba hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza sana aliyewasilisha Mapendekezo ya Mpango ambao tunaujadili hivi sasa. Mapendekezo ya Mpango huu tumeletewa ili tuweze kuyaboresha, nami naomba niboreshe katika maeneo kadhaa kwa sababu ya muda, ili tuweze kuboresha zaidi Mpango huu kwa masilahi ya watu wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, naomba sana, tunapokuwa tunaangalia namna ya kukuza uchumi wa nchi, ni lazima tuangalie zaidi upatikanaji wa ajira kwa vijana. Nchi hii ina vijana wengi sana, asilimia zaidi ya 40 ni vijana ambao wanaweza kuajiriwa au ni nguvu kazi ya nchi hii. Hawa wasipowekwa maalum kwenye Mpango, namna gani watapatiwa ajira na tukafanya projection ni wangapi watapata ajira kwa Mpango huu, tutakuwa tunachelewesha kukua kwa uchumi wa nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namna pekee ya kuweza kuwapatia vijana hawa, mathalan wa Bukombe ili uweze kuwapatia ajira, ni lazima uwatengee maeneo ya kuchimba dhahabu. Bukombe ndilo eneo pekee katika Mkoa wa Geita ambapo maeneo mengi yana dhahabu nyingi, lakini vijana wa Bukombe hawajapatiwa maeneo ya kuchimba dhahabu. Vijana hawa hawawezi kuielewa Serikali kama hawajapatiwa maeneo ya kuweza kufaidi rasilimali za nchi ambazo Mungu amewapatia na wamezaliwa wamezikuta hapo. Wakati umefika Mheshimiwa Waziri tuje na Mpango wa kuangalia namna gani vijana wanapatiwa maeneo ya kuchimba dhahabu katika Mpango wetu huu tulionao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la umeme. Watu wengi hapa wamezungumza, wamepongeza uwepo wa umeme wa REA. Sisi tuna REA I na REA II, mpaka sasa, lakini Wilaya ya Bukombe haijawahi kupata hata awamu moja ya umeme wa REA.
Nakuomba sana Mheshimiwa Profesa Muhongo na Naibu Waziri wako, nafahamu ninyi ni watu wasikivu, mtusaidie Bukombe na sisi tupate umeme wa REA. Haina maana nimesimama hapa kama Mbunge, wenzangu wanashangilia umeme na wewe Mheshimiwa Profesa Muhongo ulisema, sitaenda REA III mpaka viporo vya REA I na REA II viishe, wakati mimi hata REA I na REA II sijawahi kuiona! Mheshimiwa Profesa Muhongo nakusihi sana, Bukombe uitazame kwa jicho la huruma. Tunahitaji umeme kwa ajili ya maendeleo ya watu wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Uyovu kuna Kituo cha Afya, kinafanya huduma kubwa ya kuhudumia watu, kinahudumia Wilaya ya Bukombe, kinahudumia Wilaya ya Chato, kinahudumia Wilaya ya Biharamulo, lakini hakuna umeme pale. Madaktari wangu pale wanafanya operation kwa tochi. Jana nimepigiwa simu, wanazalisha mama mmoja wanatumia tochi. Mheshimiwa Waziri, nakuomba sana utusaidie umeme kwa ajili ya watu wa Bukombe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, naomba niipongeze sana Serikali kwa kuja na Mpango wa elimu bure kwa Watanzania. Mpango huu kwa maoni yangu naona kama ukichelewa. Kuanzia sasa watoto kuanzia darasa la kwanza mpaka la kumi na mbili watapata elimu bure. Ninafahamu wako watu wengine ambao wanaweza wakapuuza Mpango huu kwa kuona kwamba ni siasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwahakikisheni, tulipoanza na Mpango wa kujenga Shule za Kata, watu walitokea hapa wakapuuza namna ile ile, lakini leo ninavyosimama hapa na kuongea mbele yako, Shule za Kata ndiyo zimetusaidia kupata Wataamu wengi wa nchi hii. Nitakupa mfano kwenye Wilaya yetu ya Bukombe, Shule ya pili kwa kufanya vizuri Kidato cha Sita ni Shule ya Kata ya Lunzewe Sekondari, ambayo watu wakati tunaanza walianza kupuuza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali, tusukume na namwomba sana Mheshimiwa Simbachawene, endelea kutuelimisha Watanzania. Tunavyoanza siyo rahisi! Siyo rahisi tunavyoanza tukaenda na mafanikio ya moja kwa moja. Tutapata setbacks hapa na hapa, lakini kadri tunavyoendelea ndivyo tutakavyokuwa tuna-improve ili twende mbele zaidi kwa maslahi ya Watanzania.
Mheshimwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Mawaziri, naomba sana, sasa tumeshafanya vya kutosha; tumejenga madarasa, sijawahi kuona Mpango wa kuwasaidia Walimu, kuwa-motivate Walimu kufanya kazi vizuri. Walimu wa Tanzania wanafanya kazi katika mazingira magumu. Walimu wa Tanzania bado wanalipwa kwa viwango ambavyo havikidhi maisha yao kwa siku 30. Walimu wa Tanzania bado wana waajiri wengi na wanawajibika kwa watu wengi wakati wao ni watu wale wale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeomba na tumelia kwa muda mrefu Walimu wapatiwe Tume ya Utumishi wa Walimu. Wamepatiwa, sasa ninaomba Serikali iharakishe mfumo wa kurekebisha Kanuni hizo zinazotengenezwa ili Tume ya Utumishi wa Walimu ianze kufanya kazi tuwahudumie Walimu wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Mfumo wa Elimu ndugu zangu umegawanyika katika sehemu tatu, sehemu ya kwanza ni Mtaala, sehemu ya pili ni udhibiti wa ubora na sehemu ya tatu ni Examiner au Mtahini yule anayeangalia matokeo ya kile walichojifunza Wanafunzi. Upande wa mtaala ambako Mwalimu ndiko yupo, hakuna nguvu kubwa iliyowekwa kwa muda mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaangalia madarasa, ndiyo! Tunaangalia madawati, amina! Tunaangalia chaki, sawa! Lakini lazima tumwangalie Mwalimu ambaye ndiye mhusika Mkuu na msimamizi mkuu wa Mtaala wa Elimu katika nchi hii. Walimu hawa wanapokuwa wanalalamika na kulia, msitarajie tutapata matokeo ya uhakika. Tunaweza tukawalazimisha wakae darasani, watafanya kazi lakini nataka niwaambieni, motivation ya Walimu wa nchi hii bado iko chini. Iko kazi tunapaswa kufanya, tuje na Mpango Waziri wa Fedha, mpango maalum wa kutengeneza frame work ya motivation ya Walimu. Nchi nyingine zimeshafanya jambo hilo na zimefanikiwa sana. Naomba sana Mheshimiwa Waziri, jambo hili tuliangalie kwa jicho la pili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi pale Bukombe kuna zao maarufu sana. Asali bora nchi hii inatoka Bukombe. Asali inayovunwa Bukombe na watu wamejiunga kwenye vikundi, wanafanya kazi kama yatima. Wako kwenye Vikundi watu 6,000, wanavuna asali zaidi ya lita milioni moja kwa mwaka, lakini hakuna hata Kiwanda kimoja cha kusindika asali. Nakuomba Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara na tulishazungumza, tuangalie namna ya kupata Kiwanda cha Kusindika Asali ya watu wa Bukombe ili asali yao ipate bei kubwa, ipate soko la uhakika, tubadilishe maisha yao kwa kuwapatia fursa ya kuendeleza maisha yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba, vile vile Wilaya ya Bukombe tuna mifugo mingi, lakini mifugo hiyo haichangii kwenye pato la Taifa. Nchi hii ina mifugo milioni 25, lakini ukiangalia takwimu kwa hali ya uchumi, kwa taarifa ya hali ya uchumi ya Juni, 2015, utaona nchi hii pamoja na kuwa na mifugo milioni 25, tumeuza nje ya nchi mifugo 2,139 na tumepata Shilingi bilioni 34 peke yake. Tuna mbuzi milioni 15, lakini tumeuza mbuzi 264; tumepata Shilingi bilioni 1.7.
Nakuomba Mheshimiwa Waziri wa Mifugo, utakapokuja kujumuisha, uje na Mpango wa kutusaidia wafugaji hasa wa Kanda ya Ziwa, wafugaji wa Tanzania, tupate malisho, tumechoka kukimbizana na Wahifadhi wa Wanyamapori, ma-game kupigana kila siku na kuanza kuhangaishana kutozana vifedha vidogo vidogo hivi, wakati tuna uwezo wa kuchangia kwenye Pato la Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, nimekuwa na Naibu Waziri, Mheshimiwa Engineer Ramo, mtu msikivu sana. Alikuja Jimboni kwangu, akazungumza na wafugaji pamoja na Waziri wa Mifugo, walituambia mambo mengi ya kufanya, lakini cha ajabu, baada ya kauli zao kutoka, siku mbili, tatu, kauli ile ikabadilika kabisa. Wale wafugaji sasa hivi huko ninavyoongea wanatimuliwa kama wakimbizi kwenye nchi yao. Naomba Serikali tuangalie namna ya kuwasaidia watu hawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba tatizo la maji, Wilaya ya Bukombe bado tuko nyuma sana. Watu wanaweza kusema kwenye makaratasi asilimia 30 ya watu wanapata maji, hapana. Wanaopata maji Bukombe ni chini ya asilimia 30 na actually ni chini ya asilimia kumi. Miradi iliyopo mingi imeshasimama. Mradi wa Msasa haufanyi kazi, Mradi wa Kilimahewa haufanyi kazi ipasavyo, pale Ruhuyobu tuna miradi miwili; mradi mmoja peke yake ndiyo unaofanya kazi, mradi mwingine umesimama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi hii ni kazi ambayo tunahitaji tuione. Nami namwomba Mheshimiwa Waziri wa Maji, unapokuwa na kale kampango ka kupeleka maji Tabora, Nzega, Bukombe pale ni karibu, ukipitia Mbogwe, tunapata maji ya Ziwa Victoria, biashara hii inaisha. Nitakapokuwa nikisimama hapa, Mheshimiwa Waziri wa Maji, nitakuwa nazungumza mambo mengine, siyo maji. Saa imefika, naomba mtusaidie wananchi wa Bukombe tuweze kupata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, najua muda wangu umekwisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. DOTO M. BITEKO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na pongezi nyingi kwa Mheshimiwa Waziri Mwigulu kwa kazi yake nzuri ya kutusaidia sana kutatua changamoto mbalimbali Jimboni kwangu, nina mchango ufuatao kwa Wizara:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo cha zao la pamba kimekuwa kikisuasua sana kutokana na uwepo wa changamoto nyingi kwenye zao hili. Ubora wa mbegu ya pamba unakatisha tamaa. Tunaiomba Serikali sasa iweke kipaumbele kwenye uzalishaji wa mbegu bora za pamba.
Mheshimiwa Naibu Spika, msimu uliopita Wilaya ya Bukombe ilikuwa na mnunuzi mmoja tu wa pamba, jambo lililofanya bei ya pamba kukomea sh. 800/= kwa kilo. Naiomba Serikali itoe maelekezo ili uwepo wa soko huria wauone pia Wanabukombe.
Mheshimiwa Naibu Spika, wapo wakulima ambao waliingia kilimo cha mkataba, lakini kutokana na hali ya hewa, kuna mazao yaliharibiwa na hivyo kuwafanya wakulima hawa wawe na deni ambalo itakuwa vigumu kulilipa. Naiomba Serikali iweke utaratibu wa kutoa fidia kwa wananchi ambao mazao yao yameharibiwa na mvua.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Geita ni miongoni mwa mikoa mipya, lakini Ofisi ya Kilimo Mkoa, haina gari. Naiomba Serikali itupatie gari la Idara ya Kilimo Mkoa wa Geita.
Mheshimiwa Naibu Spika, usambazaji na utoaji wa pembejeo uzingatie majira halisi ya kilimo. Kumekuwa na mazoea ya kuleta pembejeo nje ya muda wa msimu wa kilimo. Nashauri Wakala wa Mbegu uimarishwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, ufugaji wa samaki ni jambo linalopaswa kupewa kipaumbele sana. Serikali sasa ianze kutoa ruzuku kwa ufugaji wa samaki. Aidha, Serikali pia ianzishe utoaji wa elimu ya ufugaji samaki.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sekta ya Mifugo ina changamoto nyingi. Mifugo haina maeneo ya malisho, Wilaya ya Bukombe haina maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya mifugo. Naomba Wizara ishirikiane na Wizara nyingine kutenga maeneo ya wafugaji. Huduma za ki-veterinary sasa zifufuliwe ili mifugo mingi iweze kupata huduma ipasavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. DOTO M. BITEKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Naomba na mimi nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi hii ya kuzungumza mbele ya Bunge lako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nianze moja kwa moja, nina miradi ya barabara ambayo iko kwenye Wilaya yetu ya Bukombe ambayo namuomba Mheshimiwa Waziri aiangalie kwa jicho la pili kwa sababu Wilaya ya Bukombe kwa ramani yake jinsi ilivyo, upande wa Kusini imepakana na hifadhi kwa hiyo hakuna namna ya kupita. Namna pekee ya kufungua Wilaya ya Bukombe ni kufungua barabara za upande wa Kaskazini. Kwa hiyo, ninakuomba sana Mheshimiwa Waziri utuangalie Wilaya ya Bukombe utuunganishe na Wilaya nyingine za Mkoa wa Geita na mikoa ya jirani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, iko barabara inayotokea Ushirombo inapita Katome, inapita Nyang‟orongo, inapita Nanda, inapita Bwelwa, inapita Iboya, inapita Bwendamwizo, inapita Ivumwa, inapita Wigo, inatokea Nyaruyeye Wilaya ya Geita, inakwenda Nyarugusu inatokea Buyagu hadi Geita Mjini. Barabara hii ni muhimu sana kwa sababu inawasaidia wananchi wa Wilaya ya Bukombe kusafirisha mazao yao kuyapeleka Geita. Barabara hii ni muhimu sana kwa sababu inawaunganisha wananchi wa Wilaya ya Bukombe pamoja na wananchi wa Wilaya ya Nyang‟hwale kwenda mkoani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba pia, Mheshimiwa Waziri aingalie barabara ambayo inatuunganisha Bukombe pamoja na Wilaya ya Chato. Barabara hii ni muhimu sana kwa uchumi wa wananchi wa Geita, kwa wananchi wa Chato, pamoja na wananchi wa Bukombe. Barabara yenyewe ni hii inayopita Bulega, inatokea Kavoyoyo, inaenda Shisabi, inaenda Mwabasabi, inaenda Matabe, inatokea Bwanga kwa Dkt. Kalemani, tunaunganishwa na Daraja moja la Nyikonga. Mheshimiwa Waziri tunakuomba sana hii barabara ni muhimu sana, uiweke na yenyewe iweze kutusaidia kwenye kukuza uchumi wa watu wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Lunzewe Bwanga, leo ni miaka miwili imesimama haijengwi. Ni barabara ambayo inajengwa kwa kiwango cha lami, kwa muda wote huu haijafanyiwa kazi, lakini mbali na hivyo wananchi wa Lunzewe pale hawajalipwa fidia kwa miaka yote hiyo. Hawawezi kuendeleza nyumba zao, hawawezi kufanya chochote kwa sababu wanasubiri fidia kutoka TANROADS. Ninakuomba sana Mheshimiwa Waziri utusaidie barabara hii ijengwe, lakini vilevile wananchi wale waweze kupata fidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba vilevile, Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni aliwaahidi wananchi wa Bukombe; na hii ni sauti ya wananchi wa Bukombe inakulilia Mheshimiwa Waziri, kilometa tano za lami kwenye Mji wa Ushirombo tunaziomba. Sijaona mkakati wa aina yoyote wa kutekeleza ahadi hii, ninakuomba sana, wananchi wanaamini kwamba ahadi hii itatekelezwa na tuanze sasa hivi. Kilometa tano tu na sisi pale tupate lami Mheshimiwa Waziri, ili siku ukija na suti yako usitoke na vumbi, uje uko smart, utoke ukiwa smart kwa sababu utakuwa umetuleta barabara ya lami. Ninakuomba sana uzingatie hilo Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, uwanja wa ndege wa Geita. Mkoa wa Geita ndio mkoa unaotoa dhahabu na madini, Wizara ya Nishati na Madini mapato yake makubwa yanatokea Geita, lakini jambo la kusikitisha ni kwamba pamoja na upya wake hatuna uwanja wa ndege. Uwanja wa ndege tuanaotumia ni ule wa Geita Gold Mine. Ninakuomba sana Mheshimiwa Waziri, umeonesha hapa kuwa ziko fedha ambazo zimepangwa kwa ajili ya uwanja wa Geita, tunaomba fedha hizo zitolewe, uwanja wa Geita ujengwe kwa haraka ili wananchi wetu waweze kupata maendeleo na usafiri wa anga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ninaomba vilevile nimuombe sana Mheshimiwa Waziri, ile barabara inayotoka Katoro kuja Ushirombo, inapita Nyang‟hwale, barabara hii ni barabara kubwa inapitisha magari makubwa. Barabara hii tunaomba na yenyewe uiwekee lami kwa sababu, hii barabara ukiiwekea lami, utapunguza mizigo kwenye barabara ya Bwanga ambayo kwa vyovyote vile haiwezi kuhimili mizigo ya magari mengi yanayopita pale.
Mimi ninafahamu kwa Serikali hii ya Awamu ya Tano mambo haya yanawezekana. Ninakutia moyo Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, ninakutia moyo nikiamini kwamba maneno haya niliyoyaomba na sauti ya Wanabukombe utaizingatia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, Mungu akubariki sana. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. DOTO M. BITEKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii na mimi nichangie Wizara hii. Kabla sijafanya hivyo nimshukuru sana Mungu kwa kunipa nafasi hii ya kuweza kusimama tena hapa na kuchangia Wizara hii muhimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama walivyoanza walionitangulia naomba nianze kwa kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri na timu yake ya Maliasili na Utalii kwanza kwa kutuletea hotuba hii nzuri, detailed na imegusa kila sekta kwenye Wizara yake. Naomba vilevile niwapongeze sana Wajumbe wa Kamati inayosimamia Wizara hii nao kwa hotuba yao nzuri ambayo imetoa maoni na ushauri ambayo kwa kweli yanatusaidia sisi tunaochangia kuweza kujua maeneo gani yatafanyiwa kazi na Kamati iliona. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa muda mrefu tumemwona Mheshimiwa Waziri anavyohangaika na kupambana na ujangili nchini. Waziri na Wizara imeonyesha nguvu yake yote kwenye jambo hili. Nataka niwatie moyo kupitia mchango wangu huu kwamba kazi wanayoifanya ni kwa faida ya nchi, waendelee mbele na wasivunjike moyo. Tumeona wale majangili wote waliotungua ndege wamekwishakamatwa. Juzi niliona video moja kwenye mitandao ya kijamii maaskari wetu wamekamata majangili haya yaliyokuwa yanafanya kazi ya kuua wanyama wetu. Naomba niwatie moyo na kuwaombea kwa Mungu waendelee bila shaka wanyama hawa ni kwa faida ya nchi yetu na vizazi vyetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Bukombe asilimia 40 ya ardhi ya Bukombe ambayo ni kilometa za mraba 8,055.59 ni hifadhi. Wananchi wanaoishi Bukombe wana maingiliano ya karibu na hifadhi ya Kigosi Moyowosi lakini mahusiano ya Kigosi Moyowosi hayajawahi kuwapatia faida na hapa nataka niseme kwa uchungu kidogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi walio wengi wa Wilaya ya Bukombe wana majonzi makubwa na hifadhi hii. Nimesimama hapa kumwomba Mheshimiwa Waziri atakaposimama na kuhitimisha aje na majibu ambayo yatawapa tumaini watu wa Bukombe juu ya mahusiano mabaya ya Wahifadhi na wananchi wa Wilaya ya Bukombe. Nenda Ngara, nenda Biharamulo, njoo Bukombe, pita Mbogwe, nenda Kahama, nenda Ushetu kwa jirani yangu Kwandikwa kila Mbunge aliyemo humu ambaye anawakilisha maeneo haya hana habari njema ya kuelezea juu ya mahusiano ya Maliasili pamoja na wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, yako manyanyaso makubwa ambayo yamefanyika ukiambiwa hapa unaweza ukatokwa na machozi. Leo nataka niyazungumze haya na niseme hadharani ikiwa sitapata majibu, watu wa Bukombe watanishangaa kuunga mkono bajeti hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano, Kitongoji cha Idoselo kilichoko kwenye Kijiji cha Nampalahala, watu wa Maliasili wameingia hapo, wamechoma moto nyumba za wananchi 40, kijiji ambacho kina GN ya Serikali kwa maana hiyo kimetambuliwa na Serikali! Katika kijiji hicho tumefanya uandikishaji wa BVR, kampeni tumepiga kule, walishachagua Mwenyekiti wa Kijiji, kilishasajiliwa, kina GN ya Serikali, watu wametoka nyumbani wamekula chai wameshiba vizuri, wana magari na mafuta ya Serikali, wana kiberiti na bunduki, wanaenda kuchoma nyumba za wanachi ambao hawana uwezo wa kujitetea, wamepiga na wameharibu mazao ya watu, watu hao wapo wanaendelea kutamba na kusema kwamba mtatufanya nini. Jambo hili lisipopata majibu leo namwambia Mheshimiwa Waziri hapa hapa nakufa na yeye. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani wananchi wale ambao wamelima mashamba yao, mazao yao yamekua yamefikia mahali fulani wanatumaini kwamba baada ya miezi fulani tunakwenda kuvuna tulishe familia zetu, tusomeshe watoto wetu, ananyanyuka mtu mmoja tu au wawili kwa sababu wana nembo ya Serikali kwa maana ya Maliasili wanakwenda kuchoma nyumba zao na baadaye wanatamba kwenye vyombo vya habari tumechoma vibanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nikuhakikishie ikiwa wao wana maghorofa, hivyo vibanda vya wananchi wao ni maghorofa yao. Ikiwa wao wanakula vizuri hayo waliyosema ni vi-plot wao ndiyo mashamba yao ambayo yanalisha familia zao. Lazima nipate majibu kwenye Bunge hili, lazima wananchi wa Bukombe wafutwe machozi kwa jambo la ukaidi, kwa jambo hili kubwa lililofanyika Wilaya ya Bukombe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Bukombe pamoja na mambo haya, kuna manyanyaso makubwa yamefanyika. Wako wananchi wamevunjwa miguu, wako wananchi wamevunjwa mikono, wako wananchi wamefanywa kuwa walemavu wa kudumu, walikuwa wanalima kwa ajili ya familia zao, leo watu hawa hawawezi kufanya hivyo kwa sababu wamekuwa walemavu, aliyefanya ni nani? Baadhi ya Askari wasio waaminifu wa Maliasili wamewaumiza watu hawa. Nataka majibu wananchi hawa mnawafanyia nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara hii imepiga risasi ng‟ombe za wananchi, nataka majibu ni kwa nini. Ng‟ombe waliopigwa risasi ni wa Ndugu Masanja Njalikila, ng‟ombe sitini (60); Ndugu Hamisi Ngimbagu, ng‟ombe wanane (8); Ndugu Manzagata Mang‟omb,e ng‟ombe mmoja (1); Ndugu Fikiri Masesa, ng‟ombe wawili (2); Ndugu Sikujua Majaliwa, ng‟ombe kumi na nane (18); Ndugu Blashi Ng‟wanadotto, ng‟ombe arobaini na tatu (43); Ndugu Juma Masong‟we, ng‟ombe kumi na mbili (12); Ndugu Mussa Seni, ng‟ombe wawili (2); Ndugu Serikali Andrea, ng‟ombe wawili (2); Ndugu Juma Langa, ng‟ombe kumi na nane (18) na Ndugu John Mashamba, ng‟ombe wawili (2); jumla ng‟ombe 215. Ndugu Jofrey Omboko punda wake wane (4) wamepigwa risasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa leo nataka majibu hatma ya watu hawa inapatikanaje. Kama inabidi nisimame kwenye Bunge hili nilie machozi kwa ajili ya wana Bukombe nitafanya hivyo, lakini watu wangu wapate majibu. Haiwezekani niwepo Mbunge hapa nimekaa kwenye kiti hiki cha kuzunguka, wananchi wangu wana mateso na nijione Mbunge mwenye furaha, hilo sitafanya. Naomba nipatiwe majibu, vinginevyo sitaunga mkono hoja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo lingine limetokea na hili ni la kisheria na naunga mkono usimamiaji na utii wa sheria. Iko tabia ya watu kupewa adhabu ya kutaifishwa mifugo yao. Leo ninavyosimama hapa jumla ya ng‟ombe 603 za wananchi wa Bukombe wametaifishwa, wamechukuliwa kuanzia siku ile ni mali ya Serikali. Nataka niseme kwenye kundi la wale waliopelekwa Mahakamani wenye ng‟ombe walikuwa watano (5), watatu (3) walikubali kutoa fedha, wakapelekwa Mahakamani wakadanganywa kwamba wakiwa huko wataachiwa Mahakamani.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme fedha zao wamekula na ng‟ombe zao zimetaifishwa lakini wako wawili (2) waliokataa kutoa fedha kujumuishwa tu kwenye mashtaka yale wakati wanadai ng‟ombe wao Maliasili wamekataa kuwaweka. Wamekwenda kuhukumiwa wale ng‟ombe kama ng‟ombe wasiokuwa na mwenyewe. Watu hawa wamekwenda Polisi, wameripoti Maliasili wakawaambia tunaomba mtufanyie jambo moja mtuingize kwenye mashtaka na sisi tushtakiwe wamekataa kuwapeleka wanasema hawa ng‟ombe hawana mwenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, unyanyasaji huu una-turnish image ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Unyanyasaji huu hauwezi kumfanya Mbunge wa Bukombe afurahie Wizara ya Maliasili na utalii. By the way kwenye Sheria zao za Maliasili na Utalii sisi tunaopakana na hifadhi tunapaswa kupata asilimia 25% ya mapato yale. Toka nimekuwa Bukombe pale sijawahi kuona hata shilingi moja inapelekwa Bukombe. Naomba na hiyo hela Mheshimiwa Waziri na yenyewe aniambie naipataje kwenye Halmashauri yetu?
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi hii na naomba niseme ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. DOTO M. BITEKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi nyingi sana kwa Wizara kwa hotuba nzuri sana. Pamoja na mambo mengine, naiomba Wizara iangalie na isaidie wananchi wa Bukombe kwa mambo kadhaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo kubwa la Wilaya ya Bukombe ni la hifadhi ya Kigosi Muyowosi. Nashauri Wizara iwe na mpango wa kuwashirikisha wananchi katika uhifadhi na kuweka mahusiano mazuri kati ya wananchi na wahifadhi
Kwa kuwa eneo kubwa la Wilaya ya Bukombe ni hifadhi, naiomba Wizara na kuishauri iweke Ofisi ya Maliasili Wilayani Bukombe. Kwa sasa wananchi wanafuata huduma Wilayani Kahama ambako ni mbali kwa kilometa 96. Nawatakia kazi njema Waheshimiwa Waziri na Naibu Waziri
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. DOTO M. BITEKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii, na mimi nichangie Bajeti Kuu ya Serikali. Kabla ya kufanya hivyo, naomba tena nimshukuru Mungu kwa nafasi hii, ambaye amenipa uhai niweze kusimama tena mbele yako ili niweze kusema machache.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikupongeze sana wewe binafsi kwa namna unavyoliendesha Bunge letu. Wewe umekuwa kamanda wa makamanda; tumeona hapa makamanda wanakukimbia kila ukitokea; na hiki ni kiashiria kwamba wewe hutishiki, uko imara. Na mimi nakuhakikishia tu kwamba sisi Wabunge wenye nia njema tuko pamoja na wewe. Endelea kutuongoza kwa kufuata kanuni zetu na taratibu tulizojiwekea, bila shaka na Mungu atakubariki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa bajeti aliyoiwasilisha. Bajeti hii bila shaka inatutatulia changamoto nyingi, lakini yako mambo ambayo nadhani yanahitaji kuboreshwa kidogo; na kwa maoni yangu ndiyo haya yaliyonifanya nisimame. Nianze na sekta ya elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sekta ya elimu imetengewa jumla ya bajeti ya shilingi trilioni 4.8 na unafahamu kwamba kwenye Azimio la Dakar tulikubaliana kwamba kila nchi itenge 6% ya GDP yake ipelekwe kwenye elimu. Ukiangalia hapa, pesa ambazo tunapeleka kwenye elimu shilingi trilioni 4.8, fedha nyingi kati ya hizo tumesema, zinazokwenda kwenye maendeleo ni shilingi bilioni 897.7 na shilingi bilioni 427.6 zinakwenda kwenye matumizi mengineyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha hizi za maendeleo zilizotengwa; 50% yake inakwenda kwenye mikopo ya wanafunzi. Kwa maoni yangu naona inaondoa dhana ya maendeleo, inaingia kwenye dhana ya matumizi mengineyo. Na mimi ninadhani, hizi fedha ambazo zimepekwa kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi, zilipaswa zitoke kwenye kifungu cha maendeleo zije kwenye kifungu cha matumizi kwa sababu zenyewe zinakwenda kutumika kwa ajili ya kuwapatia mikopo wanafunzi. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri aje atueleze kwa nini fedha hizi zinapelekwa kwenye maendeleo badala ya matumizi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumezungumza miaka mingi, na mimi kabla sijawa Mbunge nilikuwa nafutailia Bunge hili. Kwa muda mrefu tumekuwa tukihangaika na kuifanya Idara ya Ukaguzi kuwa Wakala wa Ukaguzi wa Elimu Tanzania. Elimu ya Tanzania hii dawa yale iko kwenye ukaguzi; elimu ya Tanzania ili iwe bora lazima kuwe na mtu ambaye anaiangalia kila siku. Idara ya Ukaguzi ambayo iko chini ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, leo Sayansi na Teknolojia; fedha inayopewa ni kidogo sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nenda kila kona ukaangalie, Idara ya Ukaguzi wana hali mbaya ya kifedha. Magari yao hata matairi hayana; magari yao hata mafuta hayana; uwezo wa kukagua kwa maana ya capacity ya wafanyakazi ni kidogo. Leo kwenye bajeti hii ukaguzi wametengewa 20% peke yake; fedha hizi ni kidogo sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa tunadhani kwamba tunapiga hatua, tunakwenda mbele kwa kuifanya Idara hii kuwa Wakala Maalum wa Ukaguzi wa Elimu nchini ili quality assurance tunayoizungumza kila mara iweze kuwa na uhakika zaidi, lakini leo ninaona tunarudi nyuma badala ya kwenda mbele. Naomba sana Idara hii iangaliwe, wafanyakazi wake, miundombinu pamoja na vitendea kazi, wapatiwe ili tuweze kukagua elimu ya nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka nilizungumzie ni kilimo. Kilimo kimetengewa shilingi trilioni 1.6 na kimebeba 4.9% ya Bajeti yote ya Serikali ukiondoa madeni. Mwaka wa 2014 walikopesha matrekta 118; mwaka 2015 wamekopesha matrekta 74 peke yake na mwaka huu tunarudi nyuma tena. Tulikuwa tunaamini kwamba kilimo ndiyo sekta ambayo inaajiri Watanzania wengi zaidi, tulipaswa kuweka nguvu zaidi pale kuliko kuiangalia kwa namna ambayo tunaiangalia hivi sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nikwambie mwaka huu wa kilimo na msimu huu wakulima wa pamba hawana habari njema wanayoielezea. Mbegu waliyopewa haijaota. Nenda Bukombe pale, wakulima wanalalamika mbegu waliyopewa 73% tu ndiyo iliyoota, haikuota. Wamepewa dawa za kuua wadudu, hazikuua wadudu, lakini wakulima hawa hawana namna ya kufidiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Bunge hili tuiombe Serikali, wakulima ambao walipelekewa dawa ambazo hazikuua wadudu, wakulima ambao walipelekewa mbegu ambazo hazikuota, Serikali ije na commitment ya kuwafidia watu hawa kwa sababu, wametumia nguvu kubwa kuwekeza pale; na kilimo hiki ni mara moja baada ya mwaka mmoja. Tusipowapa kifuta machozi watu hawa, nataka nikuhakikishie mwaka mzima watu hawa watakuwa maskini kwa sababu kile wanachokitarajia hawatakipata. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nizungumzie vilevile kwenye eneo la wachimbaji wadogo wadogo. Wilaya yetu ya Bukombe na Mkoa wa Geita, kama unavyofahamu, ni Mkoa ambao una dhahabu nyingi. Uchumi wa Geita unategemea dhahabu na ndiyo maana hata Mheshimiwa Serukamba alivyosema katika mikoa maskini, indicators au vigezo walivyovitumia kuifanya Geita kuwa mkoa wa pili kwa umaskini Tanzania hata mimi ilikuwa inanisumbua.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakuomba sana na Mheshimiwa Waziri wa Fedha, fedha za ruzuku kwa ajili ya wachimbaji wadogo wadogo tuzipeleke. Shilingi milioni 900 hizi tulizozitenga zisiishie kwenye makaratasi, ziende kwenye reality, tuwapalekee wachimbaji wetu wadogo wadogo waweze kuchimba kisasa ili waweze kujikwamua kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Geita vijana wengi uchumi wao na hasa wa Bukombe, wanategemea uchimbaji wa dhahabu. Ukienda huko kila mmoja anakuuliza ni lini mnatuletea maeneo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimemsikia Mheshimiwa Naibu Waziri anasema kuanzia mwezi wa saba. Ninaomba mwezi wa Saba iwe kweli, wachimbaji wadogo wadogo waanze kuchimba. Tusianze tena kuambiwa bado tuko kwenye michakato. Jamani wamesubiri michakato muda mrefu, sasa hivi wanahitaji kuona matokeo ya kuchimba na wanapatiwa eneo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie kidogo ufugaji wa nyuki. Ufugaji wa nyuki ni eneo ambalo kwa Wilaya ya Bukombe limeajiri Watanzania wengi sana. Wako watu zaidi ya 6,000 wameajiriwa kwenye sekta ya ufugaji wa nyuki, lakini watu hao hawana mtu wa kuwasaidia, wanafanya kwa mizinga ya kienyeji. Nimeangalia takwimu kwenye Hali ya Uchumi wa nchi, kuanzia mwaka 2010 sekta ya ufugaji wa nyuki inashuka. Mwaka 2010 tani 428 tu; mwaka 2011 tukashuka, tukavuna tani 343; mwaka 2012 tukashuka, tukavuna tani 103; mwaka 2013 tukashuka, tukavuna tani 83.
Mheshimiwa Naibu Spika, wafuga nyuki hawa wakipewa fedha kidogo tu kwa ajili ya kuwa na mizinga ya kisasa, kwa ajili ya kufuga nyuki kwa namna ya kisasa, nataka nikuhakikishie, inatoa ajira kubwa sana kwa Watanzania na hasa wananchi wa Bukombe.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda Uyovu, ukienda Namonge, kule kote wananchi wa kule wanategemea ufugaji wa nyuki ili waweze kupata mapato yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakuomba sana, mazingira haya wezeshi tuyafanye kote. Nchi yetu, amezungumza Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwenye bajeti yake kwamba kazi tuliyonayo sasa hivi ni kutengeneza mazingira wezeshi ya wawekezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nasoma kwenye taarifa moja ya urahisi wa kufanya biashara duniani; nchi yetu ni ya 139 kwa urasimu. Ukitaka kufungua biashara Tanzania, unahitaji siku siyo chini ya 19 ili uweze kufungua biashara. Mazingira haya ambayo siyo wezeshi hayawezi kuwavutia wawekezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeangalia vilevile kwenye compliance, hivi tunawalindaje wawekezaji kama nchi? Nchi yetu ni nchi ya 64. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu tuna kazi kubwa ya kufanya, namwomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha arekebishe haya, tuweze kuwasaidia Watanzania…

NAIBU SPIKA: Ahsante.
Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo
MHE. DOTO M. BITEKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana kwa nafasi hii lakini vilevile niwashukuru sana Wajumbe wa Kamati ya LAAC pamoja na PAC kwa taarifa yao nzuri ambao kwa kweli wamefanya kwa niaba yetu sisi Bunge zima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati ya LAAC imekuja na mapendekezo tisa kwa mujibu wa tarifa hii. Mimi naomba nitangulie kusema nayaunga mkono mapendekezo yote hayo ambayo imeyatoa. Kwa kweli ukisoma taarifa hii utaona Kamati hii imechukua muda mwingi sana kufanya kazi. Sisi kama Wabunge kwa sababu kazi hii wamefanya Wabunge wenzetu tunawajibika kuwapongeza sana Wajumbe na uongozi wote wa Kamati hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza lililozungumzwa kwenye Kamati hii na mimi nataka nichangie kidogo kwenye maeneo hayo ni upelekaji wa fedha kwenye Halmashauri zetu. Kila Mbunge aliyesimama hapa amezungumza kwa namna tofauti tofauti namna ambavyo kutokupelekwa kwa fedha za maendeleo kwenye Halmashauri kunavyoathiri miradi ya maendeleo kwenye Halmashauri zetu. Wewe unafahamu na Bunge linafahamu shughuli nyingi tunazofanya sisi Wabunge zinatekelezwa kwenye ngazi ya Halmashauri, kama Halmashauri hizi hazipatiwi pesa bila shaka mwisho wa siku hatutakuwa na jambo la maana la kujivunia kwamba tumefanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, kwenye Wilaya yetu ya Bukombe tumepeleka maombi mbalimbali ya fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Barabara nyingi zilizopo kule kwa muda mrefu hazipitiki kwa sababu maeneo mengi ya Wilaya yetu ya Bukombe yapo kwenye milima, barabara zile zimekatika, hazipitiki. Barabara kama za Maghorofani, Mchangani, Imalanguzu, Nifa, Rulembela na Kelezia hizi zote hazipitiki kwa sababu hazijawahi kufanyiwa matengenezo mwaka uliopita na mwaka huu vilevile hatujawahi kupata fedha. Kwa hiyo, naunga mkono mapendekezo ya Kamati ya kwamba sasa Serikali iharakishe kuzipeleka pesa kwenye Halmashauri ili tuweze kupata maendeleo haya na ukarabati wa miradi hii uweze kukamilika.
kufurahi. Wilaya ya Bukombe na Wilaya nyingine kwenye Mkoa wa Geita na hili nimeliuliza humu Bungeni, nimekwenda TAMISEMI nimewauliza fedha za walimu waliosimamia mtihani wa kidato cha nne mwaka jana ziko wapi? Wengine wakaniambia uende kwa watu wa Wizara ya Elimu, wengine wanasema hapana nenda TAMISEMI, shilingi milioni 35 walimu wa Bukombe kila tukikutana ndiyo jambo wanaloniuliza. Kila tukionana wananiambia Mheshimiwa pamoja na maneno mazuri uliyonayo kahela ketu kako wapi? Naomba hapa kahela haka kapatikane, watu hawa wapewe chao, watu hawa wajijue na kahela kao haka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumesimamisha kupandisha vyeo vya walimu kwa sababu tulikuwa tunashughulikia watumishi hewa, tumesimamisha mishahara iliyokuwa imepandishwa ikarudi ili tumalize jambo la watumishi hewa, hata haka ka kusimamia mitihani na kenyewe kanasimama, hapana! Naomba sana walimu hawa walipwe fedha zao ili waweze kufanya kazi yao kwa juhudi wakiwa wanajua kwamba Serikali inawapenda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ajira ya mwaka jana iliandikwa barua TAMISEMI kwenda kwenye Halmashauri zote walimu wapya walioajiriwa fedha zao zile Halmashauri zichukue kwenye akaunti yoyote pesa zilipe nauli. Wilaya ya Bukombe shilingi milioni 58 zilichukuliwa ni fedha za wakandarasi zikalipa nauli walimu wapya waliokuwa wameajiriwa, zikalipa subsistence allowance kwa ajili ya walimu wale wapya, fedha hizo hazijalipwa, wakandarasi wanatafuta hela, Halmashauri inahaha ipate wapi pesa ya kuweza kuwalipa wakandarasi hawa. Halmashauri hii ikishtakiwa na ambavyo hatuna fedha imani yangu ni kwamba hatuwezi kutoboa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba TAMISEMI kwa barua ile mliyoandika ya kwamba wachukue fedha kwenye akaunti yoyote mtarudisha, rudisheni hizi fedha sasa hivi Halmashauri kule hali ni mbaya. DT hata kukaa kwenye kiti anaona shida, Mkurugenzi kukaa kwenye kiti anaona shida kwa sababu wakandarasi hajui watakuja kwa wakati gani. Naomba Wizara ya TAMISEMI tuhakikishe kwamba madai haya tunayashughulikia haraka iwezekanavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lipo lililosemwa hapa na watu kwenye Waraka tmezungumzia asilimia kumi ya vijana na akina mama, naomba hili jambo tuanze…
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.