Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Doto Mashaka Biteko (3 total)

MHE. SUSANNE P. MASELE aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatekeleza kauli ya Mheshimiwa Rais kuhusu kuwapatia wachimbaji wadogo wadogo kipaumbele cha leseni na vibali vya kuchimba madini kwa kuonesha mfano kwa wachimbaji wadogo wa machimbo ya Dhahabu ya Ishokelahela, Misungwi?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijajibu swali la Mheshimiwa Susanne Masele naomba nichukue nafasi hii nimshukuru sana Mungu kwa kunipa kibali cha kusimama hapa, lakini vile vile nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa Imani kubwa aliyonipatia na akaona naweza kumsaidia kwenye Sekta hii ya Madini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo naomba sasa nijibu swali la Mheshimiwa Susanne Peter Masele Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, wachimbaji wa Madini wadogo wa Ishokelahela Wilayani Misungwi walivamia na kuanza shughuli za uchimbaji wa madini ya dhahabu katika eneo la Leseni kubwa ya utafutaji wa madini inayomilikiwa na Kampuni ya Carlton KitongoTanzania Limited yenye ukubwa wa kilomita za mraba 12.4 tokea mwezi Julai, 2017. Kabla ya hapa wachimbaji hao walikuwepo lakini kwa kiasi kidogo. Mpaka kufikia sasa leseni hiyo imevamiwa na wachimbaji wadogo zaidi ya 1000 ambao wanachimba madini hayo ya dhahabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leseni ya Carlton KitongoTanzania Limited ilitolewa tarehe 5 Agosti, 2014 na itamaliza muda wake wa awali tarehe 4 Agosti 2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkuu wa Wilaya ya Misungwi kwa kushirikiana na kampuni ya Carlton Kitongo Tanzania Limited ambaye ni mmiliki wa leseni hiyo waliamua kutenga eneo kwa ajili ya kuwaachia wachimbaji wadogo ambalo likuwa linamilikiwa na kampuni hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, makubaliano hayo yalihitimishwa rasmi mwezi Desemba mwaka 2017 kati ya mmiliki wa leseni na vikundi ambayo viliungana kuunda kikundi kimoja kwa jina la Basimbi and Buhunda Mining Group. Nakala ya makubaliano hayo ipo Ofisi ya Madini Mwanza na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Misungwi. Vikundi hivyo vilipatikana baada ya Wizara kupitia Ofisi yetu ya Madini Mkoani Mwanza kutoa elimu ya umuhimu ya kujiunga katika vikundi na kuendesha shughuli za uchimbaji madini ili ziweze kuwa na tija zinazozingatia matakwa ya Sheria ya Madini na Kanuni zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza kauli ya Mheshimiwa Rais kuhusu kuwapatia wachimbaji wadogo kipaumbele cha leseni na vibali vya kuchimba madini, leseni za wachimbaji madini katika eneo hilo zitatolewa kwa vikundi hivyo mara tu baada ya taratibu za kisheria za kushughulikia maombi hayo kukamilika.
MHE. ANNA J. GIDARYA aliuliza:-
Mgodi a Tanzanite ulioko Mererani, Wilaya ya Semanjiro ni mgodi wenye idadi kubwa ya vijana wanaofanya kazi katika mgodi huo na kumekuwa na historia ya matukio ya maafa kila mwaka ya vifo vya watu wengi.
(a) Je, Serikali imefanya utafiti gani ili kubaini chanzo cha maafa hayo yanayolikumba Taifa kila mwaka na kusababisha kupoteza nguvu kazi ya Taifa letu?
(b) Je, Serikali haioni umuhimu wa kuanzisha utaratibu maalum kwa wamiliki wa vitalu vya Tanzanite kuwalipa kifuta jasho wahanga wote wanaopatwa na maafa wanapokuwa kazini?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Anna Joram Gidarya, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, mapitio ya taarifa za ajali yanaonesha kuwa ajali nyingi husababishwa na wachimbaji wadogo kutokuzingatia tahadhari ya usalama wanapotekeleza majukumu yao ya uchimbaji madini. Hivyo, Serikali imekuwa ikifanya juhudi za ukaguzi wa maeneo ya uchimbaji na kuwaelimisha wachimbaji kuchukua tahadhari za usalama wakati wa kufanya kazi pamoja na kuwahamasisha kuunda timu za wakaguzi katika maeneo yao kutoka miongoni mwa wachimbaji ambao hupewa elimu ya ukaguzi na wataalam wetu wa Wizara ya Madini. Hivyo, nawasihi wachimbaji wa madini kutambua umuhimu wa kuzingatia taratibu na usalama wa kazi kwa uchimbaji ili kulinda afya na uhai wao.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Serikali imeanzisha Mfuko wa Fidia ya Wafanyakazi kupitia Sheria Namba 20 ya mwaka 2008 ya Fidia ya Wafanyakazi. Wizara itahamasisha wamiliki wa leseni na wachimbaji kujiunga na mfuko huu ili kupata kifuta jasho wanapopatwa na maafa wanapokuwa kazini.
MHE. IGNAS A. MALOCHA aliuliza:-
Katika ukanda wa Bonde la Ziwa Rukwa katika Jimbo la Kwela, kwenye ukingo wa Milima ya Lyamba Iyamfipa inayoambaa katika Kata za Mfinga, Mwadui, Kalumbaleza, Nankanga, Kapeta hadi Kaoze, baadhi ya wananchi wamekuwa wakiokota madini mbalimbali bila kutambua ni madini ya aina gani.
(a) Je, Serikali imeshafanya utafiti wowote katika maeneo hayo?
(b) Kama jibu ni hapana, je, ni lini utafiti utafanyika ili kujua eneo hilo lina madini gani?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTTO M. BITEKO) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ignas Aloyce Malocha, Mbunge wa Kwela kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia miaka ya 1950 Serikali imekuwa ikifanya utafiti mbalimbali wa awali wa madini kwenye maeneo ya Ukanda wa Bonde wa Ziwa Rukwa yakiwemo maeneo ya Jimbo la Kwela kwenye mwambao wa milima ya Lyamba Iyamfipa. Utafiti wa awali ulibaini uwepo wa madini mbalimbali yakiwemo madini ya vito kama vile Garnet, Kyanite, Zircon na Sapphire na mengineyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa za uwepo wa madini katika Ukanda wa Bonde wa Ziwa Rukwa zinapatikana kwenye ofisi zetu za Wakala wa Jiolojia Tanzania. Hata hivyo nachukua nafasi hii kuwashauri sana ndugu zetu wote wakiwemo wa Jimbo la Kwela kutumia Ofisi zetu za Madini za Kanda ya Magharibi iliyoko Mpanda na taarifa zilizopo kwenye ofisi ya Wakala wa Jiolojia iliyoko Dodoma, ambapo wako wataalam watawasaidia kuyachambua madini hayo pamoja na kuwashauri namna ya kufaidika na rasilimali hiyo ya madini.