Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Doto Mashaka Biteko (7 total)

MHE. SUSANNE P. MASELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, baada ya taratibu kukamilika, je, Serikali itachukua muda gani kuwapatia leseni wachimbaji hao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, yamejitokeza madai kuwa zuio la mchanga pale bandarini makinikia halikuwagusa wachimbaji wakubwa tu hata wadogo pia.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba wachimbaji hao wadogo wanasafisha mchanga wao hapa nchini ili kuendeleza uwekezaji na kutengeneza ajira zaidi kwa wachimbaji hawa wadogo? (Makofi). Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itachukua muda gani, naomba nimjibu Mheshimiwa Mbunge kwamba, taratibu za kuunda Tume ambayo ndiyo imepewa mamlaka ya leseni ya uchimbaji madini, iko katika hatua za mwisho za kuundwa. Mara itakapokamilika kazi hiyo itaanza mara moja, kwa hiyo, haitachukua muda mrefu sana baada ya Tume hiyo kuwa imeshakamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili la zuio la mchanga, naomba nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na Watanzania, kwamba Sheria ya Madini haijazuia usafirishaji wa michanga nje ya nchi isipokuwa zipo taratibu na sheria ambazo yule mtu anayetaka kusafirisha mchanga kama madini lazima azifuate kwa mujibu wa sheria. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie kwamba tumezuia yale makontena kwa sababu yalikuwa na mgogoro ambao Serikali tuliona kuna haja ya kujiridhisha kabla ya kuruhusu.
Mheshimiwa Mwenyekti, kama kuna wananchi ambao wana madini ya mchanga ambao wanataka kuyasafirisha kwenda nje ya nchi kama wengine ambavyo wanapata vibali na wao wafuate taratibu watapewa vibali. (Makofi)
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Serikali iliahidi kutenga maeneo ya Ibindi, Dirifu, Society na Kapanda kwa wachimbaji wadogo wa huko Mpanda, je, ni lini wachimbaji hawa watapatiwa leseni?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Kapufi kwa ufuatiliaji wake kwenye jambo hili. Kwa muda mfupi ambao nimeingia ofisini amekuwa mara nyingi akiniambia jambo hili juu ya wachimbaji wake wadogo wadogo. Naomba nitumie fursa hii kuwaambia Watanzania wote wakiwepo na wananchi wa Kibindi kwamba wale wote ambao wamejiunga kwenye vikundi wakaomba maeneo mbalimbali kwa ajili ya uchimbaji madini Wizara ya Madini iko tayari kuwasaidia mara tu, Tume ya Madini itakapoanza kazi baada ya kuwa imekwishakuundwa.
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nami nimpongeze Mheshimiwa Dotto kwa kuchaguliwa kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Madini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo naomba niombe kuuliza au kupata kauli ya Serikali juu ya lini Serikali itaruhusu mwekezaji wetu Gulf Concrete awalipe fidia wananchi wapatao 80 wanaoishi katika maeneo mbalimbali ya Kata ya Lugoba ili waweze kuendeleza eneo lile na wao waweze kuondoka na kulinda afya zao?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTTO M. BITEKO): Mheshimiwa Mwenyekiti, mwekezaji wa Gulf Concrete and Cement Product ambaye yuko Chalinze kwenye Kijjiji cha Nguza amekuwa akichimba kwa muda mrefu kwenye eneo hilo; na kwa kweli anachimba kwenye eneo hilo ametengeneza ajira zaidi ya 170 kwa watu wa Chalinze ambako Mheshimiwa Mbunge anafuatilia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumetoa mgogoro mdogo ambao sisi kama Wizara ya Madini tunaushughulikia. Mwekezaji huyu amechimba na akaingia kwenye eneo la mwekezaji mwingine ambaye ana leseni anaitwa Global Mining; ameingia kwenye eneo ambalo lina ukubwa kama hekta 1.5.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulichofanya kwa sasa, tunataka tuumalize kwanza mgogoro huu ambao yeye Gulf Concrete ameingia kwenye eneo la mtu mwingine. Tukishamaliza twende kwenye hatua ya pili sasa ya kumsaidia Mwekezaji huyo ambaye kwa kweli ana tija kwa watu wa Chalinze na watu wa Mkoa wa Pwani aweze kulipa fidia ili aendeleze mradi wake.
MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, pamoja na majibu ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na utaratibu wa Serikali pindi tu mawe yanapotoka kulazimisha wamiliki kupitisha mawe hayo kwenye chumba maalum (strong room) kabla ya kuuzwa mnadani, jambo ambalo limesababisha usumbufu mkubwa kwa wamiliki wa vitalu kutokuwalipa wafanyakazi hao kwa wakati.
Je, ni nini sasa kauli ya Serikali ili kuondoa usumbufu huu kwa wamiliki wa mgodi huu wa Tanzanite?
Swali la pili pamoja na wamiliki wa migodi wa Tanzanite kuwa na vibali halali kumekuwa na utaratibu wa Serikali kuuza mawe hayo kwenye mnada kwa bei ya kutupa; je, Serikali haioni kama wamiliki hawa wa migodi wanapata hasara kubwa pamoja na kuwa wanalipa kodi ya Serikali?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO): Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nataka nieleze tu kwamba tunawalazimisha watu kupitisha mawe kwenye strong room kabla ya kuuzwa, lengo letu ni moja tu kutaka kujua uhakika wa kiasi gani cha mawe yamezalishwa ili Serikali iweze kupata kodi zake na tozo zake mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, hili hatuwezi kurudi nyuma madini haya ya Tanzanite yamekuwa yametoroshwa na nchi hii imepata aibu kubwa. Asilimia 20 tu ya madini yote ya Tanzanite yanayochimbwa ndiyo tunaweza kuyaona yameingia kwenye mfumo wa Serikali. Kwa hiyo, tumeweka nguvu kubwa ya udhibiti na usimamizi na hili Mheshimiwa Anna ninamwomba aunge mkono juhudi za Serikali kwenye jambo hili tusirudi nyuma.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili utaratibu wa kuuza mawe haya kwenye mnada ni utaratibu ule ule na umekuwepo kwa muda mrefu, bei iliyopo pale sio bei ya kutupwa ni bei ya ushindani wale wanaotaka kununua wote wanakwenda kwenye eneo la mnada wanatoa bei zao yule anayeshinda anapewa kwa bei nzuri. Hili tunataka kulifanya kwa uzuri zaidi na litakuwa katika Mkoa wa Manyara ili lisimamiwe vizuri zaidi Serikali iweze kupata kodi zake. Ahsante. (Makofi)
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibuni tulifanya mabadiliko ya Sheria ya Madini na katika kudhibiti na kusimamia CSR tulielekeza Halmashauri husika kushirikishwa katika mipango. Inaonyesha kwamba huko nyuma taarifa ambazo zipo kwenye Halmashauri zetu ni miradi hii ilikuwa inakuwa inflated na mingi ilikomea njiani.
Ni nini maelekezo ya Serikali kwa sababu migodi itaendelea kusimamia yenyewe na kutangaza kazi yenyewe katika sheria ijayo?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze tu kwa kueleza kwamba Mheshimiwa Kanyasu kwa muda mrefu amekuwa mtu ambaye ana kilio kikubwa juu ya matumizi ya hizi fedha za CSR zinazotolewa na migodi hapa nchini, wananchi wa Geita wanajua hilo na amekuwa akilisema hata hapa Bungeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli sheria mpya ya madini, marekebisho mapya kwenye Sheria yetu ya Madini ya mwaka 2010 imetoa utaratibu maalum kwa watu wote wenye migodi kutengeneza plan ya matumizi ya CSR na kuipeleka kwenye Serikali ya Halmashauri ili iweze kupata approval.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna changamoto imejitokeza kwenye migodi mingi ambapo ni kweli kabisa kama alivyosema Mheshimiwa Kanyasu inflation ya bei ya vitu imekuwa kubwa mno na miradi mingi imekuwa miradi ambayo haifiki mwisho. Sasa kama Wizara tunaandaa utaratibu wa kukagua CSR ambazo zimekwishakutolewa ili tuone kama kweli fedha hizi zilizotolewa ziliwafikia wananchi na halikuwa jambo la kutegeshea tu. Ahsante. (Makofi)
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali ndogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, wachimbaji wadogo wadogo wamekuwa wakipata maafa makubwa sana kwenye migodi na ukaguzi mnasema unafanyika, ningependa kujua huu ukaguzi unafanyika kwa mfano kila mara baada ya miezi mingapi ili tujue kwamba kweli hawa watu wanasimamiwa ili kusudi kuepusha hizi ajali zinazotokea mara kwa mara.
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO): Mheshimiwa Naibu Spika, ukaguzi kwenye migodi ni utaratibu maalum wa Wizara yetu ya Madini kukagua mara kwa mara na hatuna muda maalum, wakati wowote kwenye migodi tunakwenda tunakagua kujiridhisha kama kuna compliance ya kufuata sheria yetu ya madini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye migodi yote ziko Kamati ndogo ndogo za ndani kwenye hiyo migodi ambazo zinafanya kazi ya ukaguzi. Niwaombe wamiliki wote wa leseni kuzitumia Kamati hizi za ukaguzi ili tuweze kupunguza maafa.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la msingi nimueleze tu Mheshimiwa Mbunge kwamba wachimbaji wadogo wenyewe waangalie usalama mahali pa kazi, kwa sababu mtu wa kwanza wa kuangalia usalama wake ni yeye mwenyewe mchimbaji kabla ya Serikali kuja. Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. (Makofi)
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kushika nafasi hiyo mpya na kwa kweli ameanza kuifanya vizuri Mwenyezi Mungu aendelee kumuongoza aendelee kuifanya vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza sisi sote tunafahamu wazi kwamba maeneo yaliyo na madini yanatoa fursa kwa vijana wengi kujiajiri kwa machimbo madogo madogo kwa kujipatia kipato na vilevile Serikali kukusanya kodi. Tunafahamu kwamba Serikali ilishafanya utafiti katika maeneo mengi, lakini utafiti huo uko ndani ya vitabu mpaka uende maktaba jambo ambalo sio rahisi wananchi wa kawaida vijijini kutambua wapi kuna madini.
Mheshimiwa Naibu Spika, je, kwa nini Serikali isiainishe maeneo yote yenye madini kwa uwazi ili wananchi waweze kuyatambua na kufanya kazi ya uchimbaji mdogo mdogo?
La pili umesema kwamba wananchi wanaweza kutumia ofisi za kanda za Magharibi zilizopo Mpanda na Dodoma, jambo ambalo ni vigumu kwa wananchi wa kawaida hasa wa vijijini kuzitumia ofisi hizo kutokana na umbali uliopo. Kwa nini Serikali isiweke branch katika mikoa yote ili kurahisisha wananchi kuzishilikia ofisi hizo?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTTO M. BITEKO):
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ijulikane tu kwamba matumizi ya ofisi zetu za Wakala wa Jiolojia ni matumizi ambayo yanawahusu Watanzania wote. Ni bahati mbaya tu kwamba wageni wanaotoka nje kuja kutafuta madini hapa nchini wao wanazitumia zaidi ofisi hizi kuliko sisi Watanzania.
Naomba nitoe wito sasa kwa Watanzania wote tuzitumie Ofisi zetu hizi za Wakala wa Jiolojia ili ziweze kutusaidia katika sekta hii ya madini.
Lakini la pili kwa nini Serikali sasa isiweke branch kwa kila Wilaya na kila maeneo. Naomba nimuombe Mheshimiwa Malocha, na kwasababu amekuwa mdau mkubwa sana wa kufuatilia jambo hili kwaajili ya wananchi wake; sisi ni watumishi wa wananchi, sisi hatukai ofisisni Mheshimiwa Malocha ukiwahitaji wataalamu wetu wa Jiolojia kuja kwenye eneo lako wakati wowote watakuja, na hata kama utamuhitaji Waziri mwenyewe atakuja kwasababu sisi ni watumishi wa wananchi.