Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Ally Abdulla Ally Saleh (29 total)

MHE. ALLY SALEH ALLY: Haya ahsante.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
La kwanza ni suala lile la kwamba masuala ya gesijoto na tabianchi yanasimamiwa na Mkataba wa Kimataifa unaoitwa United Nation FrameWork Convetion on Climate Change. Katika mfumo wake kunakuwa na mtu au sehemu inaitwa focal point ambapo ndipo mambo yote yanapopitia.
Ni kwa nini hakuna sauti ya Zanzibar katika hiyo focal point ya Tanzania, hakuna mwakilishi wa Zanzibar ama alternatively au kutoka Zanzibar ili kuhakikisha maslahi ya Zanzibar yanalindwa katika suala hilo? La kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kumekuwa na taarifa na hali ndiyo ilivyo kwamba Zanzibar kama visiwa vingine vidogo vingi vinaweza kukabiliwa na tatizo hili la ongezeko la gesi na mabadiliko ya tabianchi na kwa hivyo hata uwepo wake upo hatarini. Je, Serikali ina mpango gani wa kudumu na wa muda mrefu katika kuhakikisha kwamba Zanzibar inatoka katika loop kubwa zaidi ya kuilinda ili iendelee kuwepo katika uso wa dunia. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza anasema kwamba ushirikishwaji wa Zanzibar hasa katika suala zima la climate change pamoja na ongezeko la gesijoto kwamba Zanzibar inashirikishwa namna gani. Tumekuwa tukishirikiana na Zanzibar kwa karibu na ndiyo maana hili suala la mazingira limewekwa Ofisi ya Makamu wa Rais ili kuweza kufanya ushirikiano mzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, Mkutano wa Paris tunaouzungumza ulihudhuriwa na watu kumi na saba, watano walitoka Zanzibar na Ofisi ya Makamu wa Rais imekuwa ikifanya kazi bega kwa bega na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kitengo cha Mazingira, ambapo tumekuwa tukishirikana kwa kila hali.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi juzi hapa kuna suala lilitokea la kudidimia kwa ardhi, kuna sehemu kumedidimia kule Zanzibar, Ofisi yangu hapa ya Mazingira pamoja na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Kitengo cha Mazingira wameshiriki kufanya utafiti kuona tatizo hili linasababishwa na nini. Kwa hiyo, kwa ujumla tumekuwa tukishirikiana vizuri sana na Zanzibar hatua kwa hatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo limezungumzwa hapa na Mheshimiwa la kuhusu Zanzibar kama kisiwa, kama tunavyojua ni kweli kabisa kwamba, sasa hivi ni dunia nzima ipo kwenye hali ngumu ya mabadiliko ya tabia ya nchi. Joto la dunia limeongezeka kutoka kwenye standard ya kawaida na kufikia nyuzi joto zero point nane tano. Dunia nzima tunahangaika sasa hivi kuhakiksha kwamba hizi nyuzi joto haziongezeki kufikia kuzidi nyuzi joto moja point tano.
Mheshimiwa Naibu Spika, kina cha bahari kimeongezeka kwa sentimita kumi na tisa. Kwa hiyo, hili ni tishio kubwa ambalo lazima tuchukue hatua za dhati za kuhakikisha kwamba tunakabiliana na matatizo haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kwenye Mpango wa Maendeleo (framework) ambayo tumeanza nayo sasa hivi, Kitaifa tunajipanga kuhakikisha kwamba Tanzania kama Tanzania inatenga fedha za kutosha kukabiliana na suala la mabadiliko ya tabianchi. Vilevile wahisani wetu, tunaendelea kuhakikisha kwamba wanashiriki katika kuhakikisha kwamba Tanzania inapata fedha za kutosha kuhusu suala zima la mabadiliko ya tabianchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nchini Ufaransa kwenye Mkutano wa Paris, Tanzania imepata fedha dola laki tatu kwa ajili ya kukabiliana na tatizo la mabadiliko ya tabianchi. Vile vile tumepata fedha dola laki nne kwa ajili ya kuripoti mpango wa ripoti ya tatu kwa ajili ya kukabiliana na matatizo ya tabianchi. Pia tumepata fedha dola za marekani mia tatu hamsini na mbili, kwa ajili ya kuandaa tathmini ya kwanza ya kupunguza gesijoto nchini. Kwa hiyo, mikakati hii yote tunayoifanya na hatua ambazo tunazozifanya kupitia mpango wa maendeleo na bajeti yetu, zote hizi zitalenga katika kupunguza athari ya mabadiliko ya tabianchi.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niongeze machache katika kuyakamilisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya Mkutano wa Paris, kila nchi ilitakiwa kutengeneza program inaitwa intended national determined contributions, yaani kila nchi itengeneze mpango wa namna ya kutekeleza makubaliano ya Paris. Katika kutengeneza mpango ule tumeshirikana na wenzetu wa Zanzibar kwa kutambua changamoto mahususi ya kwamba Zanzibar ni kisiwa, uchumi wake unategemea utalii, utalii unategemea fukwe na fukwe zinaathiriwa sana na kupanda kwa kina cha bahari. Kwa hiyo, tumefanya hivyo na tutaendelea kufanya hivyo ili kuhakikisha kwamba Zanzibar inabaki kama ilivyo katika uzuri wake na ubora wake ili isiathiriwe na changamoto hizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu focal point tumeomba kwamba Ofisi ya Makamu wa Rais ndio iwe focal point ya Taifa letu katika utekelezaji wa mkataba ule. Ile Ofisi ya focal point itajumuisha Wazanzibar, tutahakikisha hilo linatokea kwa sababu changamoto zetu hizi ni changamoto za pamoja. (Makofi)
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu yenye takwimu na hakikisho la usalama, lakini hivi sasa vitendo vya wale wanaoitwa mazombi na masoksi vinaendelea vikifanywa fawaisha kila siku na hata juzi watu kadhaa walipigwa katika Mtaa wa Kilimani na wengine wakapigwa katika Mtaa wa Msumbiji. Pia watu hawa wamekuwa wakiranda na silaha za moto, misumeno wa kukatia miti, wamekuwa wakivamia vituo vya redio, wamekuwa wakipiga watu mitaani. Swali langu la kwanza, je, kitu gani kinazuia kukamata uhalifu huu unaofanywa fawaisha kila siku na ambao unakuza culture of impunity katika nchi yetu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Serikali haioni vijana hao wanaoitwa mazombi wanaotumia magari ya KMKM ya KVZ, volunteer, magari ya Serikali waziwazi na namba zake zinaonekana kila kitu. Je, Serikali haioni kwamba kuruhusu hali hiyo kuendelea kunaitia doa Serikali katika suala zima la haki za binadamu na utawala bora? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI: Mheshimiwa Naibu Spika, siku zote Jeshi la Polisi ama vyombo vya dola vimekuwa vikifanya kazi kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi. Haya ambayo anazungumza Mheshimiwa Ally Saleh, nadhani amezungumza maneno mazombi, sijui ana maana gani, lakini ninachotaka kusema ni kwamba kama kuna uvunjifu wa sheria katika nchi yetu, basi taarifa hizi ziwasilishwe polisi na polisi itachukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Waziri ametuambia hapa kwamba kuna sharia zinazosimamia suala hili lakini sijui kama ana taarifa kwamba watu hupigwa na kunyang’anywa mali zao na lini jambo hili litakoma ili sheria ifuate mkondo na siyo kunyang’anywa mali zao na kupigwa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Waziri amesema kwamba kuna elimu inatolewa juu ya watu hawa wa Dago ambapo kwa Wazanzibar ni jambo asili na la muda mrefu tu kutoka Bara kuja Unguja kama vile watu wanavyotoka hapa kwenda Dago Zanzibar. Je, Waziri anajua kwamba hiyo elimu anayoisema haijaenea kiasi cha kutosha ndiyo sababu ya sokomoko linalotokea katika eneo la wavuvi hawa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa kwamba watu hupigwa na kunyang’anywa mali zao hazijafika rasmi Wizarani. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba pale tutakapopata taarifa hizi tutachukua hatua stahiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nimueleze kwamba nafahamu kuna changamoto nyingi zinatokea katika Kambi za Dago hasa maeneo ya Mafia, kuna changamoto nyingi ambazo zimeripotiwa. Wizara yangu ina mkakati na mimi mwenyewe nimepanga kwamba mara nitokapo kwenye Bunge hili nitaelekea Mafia kwa sababu mbali na alichosema Mheshimiwa Mbunge tayari Wabunge wengi wa ukanda huo na hasa wanaotoka maeneo ya Mafia wameleta changamoto nyingi ambazo zipo, nitaendelea kufahamu changamoto zilizopo kule ili kuweza kuzipatia suluhu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nitumie fursa hii kupitia Bunge hili kuwasihi wananchi kwamba utaratibu wa Dago ni utaratibu mzuri lakini ni mzuri tu kama unafuatwa. Kama wavuvi wakiwa wanatoka eneo moja kwenda lingine bila kufuata taratibu ni vigumu sana Serikali kutoa msaada wowote. Kwa hiyo, ni vizuri tufuate taratibu na sheria zilizopo ili kuondoa vurugu ambazo zinatokea kwenye Dago.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la nyongeza la pili lilitaka nijibu kama kuna elimu inatolewa Zanzibar. Nimweleze Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa taarifa tulizonazo sisi ni kwamba elimu hiyo inatolewa kote na mara nyingi inatolewa kwenye halmashauri anapokwenda kuvua mvuvi siyo kule anapotoka. Kwa hiyo, tunaendelea kusisitiza kwamba kama kuna upungufu katika elimu inayotolewa, tutaendelea kuwasiliana na mamlaka husika kuhakikisha kwamba elimu hii inatolewa kwa wavuvi wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Spika ahsante, Mheshimiwa Waziri katika majibu yake alizungumza kwamba watu ni lazima watoke Zanzibar waingie katika Kambi za JKT ili waweze kuajiriwa, lakini nafikiri hilo ni tatizo.

(a) Je, Waziri anajua kwamba kuna suala kubwa la rushwa katika kupata ajira?

(b) Kuna wadowezi wanaotoka Maafisa wa Kijeshi walioko Zanziabar ambao wanatumia nafasi ambazo ziko allocated kwa Wazanzibari kuwapatia watu wao kutoka Tanzania Bara nafasi zile ambazo zimetengwa kwa Zanzibar?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, kwanza kuhusu suala la rushwa wakati wa usaili wa ajira, taarifa hizo mimi binafsi sijazipokea lakini namuomba Mheshimiwa Ally Saleh kama anao ushahidi wa kutosha wa kijana yeyote aliyeombwa rushwa, walete taarifa hizo na tutazifanyia kazi kwa kuchukua hatua stahili kwa wale wote ambao wanajihusisha na vitendo hivyo. (Makofi)

Kuhusu swali la pili la nafasi za Zanzibar kuishia kupewa watu wa Bara pia naweza kusema kwamba mimi sina taarifa na utaratibu tuliouweka ni mzuri sana, kwa sababu tunapopata nafasi 300 za vijana wa Zanzibar kujiunga na JKT, tunazikabidhi kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Ni wajibu wao kuhakikisha kwamba nafasi hizo wanazigawa vile ambavyo wanapenda.

Mheshimiwa Spika, taarifa nilizonazo mimi, ni kwamba kwa utaratibu wa sasa nafasi hizo zinagawiwa kwa Wilaya na Mikoa.

Kwa hiyo, Kamati na Ulinzi za Usalama za Wilaya na Mikoa wanatakiwa wahakikishe kwamba wao ndiyo wateuzi wa vijana hao, inatokeaje mtu wa Bara anakuja anachukua nafasi zile kuwapa watu wa Bara wenzake, hilo nadhani siyo sahihi na kama ni sahihi basi udhaifu huo uko kwa wale wanakabidhiwa nafasi hizo.
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT)
24
Kwa kuwa, katika jibu lake la msingi Mheshimiwa Waziri amesema sababu moja kubwa ya uwekezaji au kuvutia uwekezaji ni kukua kwa biashara, na kwa kuwa Mikoa ya Kusini, Ruvuma, Lindi, Mtwara ina karibu Watanzania milioni 5, na kwa sababu kwa Mikoa hii haijapata huduma ya uhakika ya usafiri wa meli kwa zaidi ya miaka 10 hivi sasa.
Je, Serikali haioni kuna haja sasa ya kuipa kipaumbele cha juu kabisa Mikoa hii kushawishi wawekezaji kuwekeza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumhakikishia tumelisikia hilo tukalifanyie kazi, tutakuja na majibu pale Serikali itakapoona njia ya muafaka kulifanyia kuhusu wasafiri hao wa maeneo ya Kusini.
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa kweli hii ni standard answer, hata tungefumba macho tu tungejua kwamba jawabu lingekuwa hili. Ni kawaida swali hili limeulizwa hii mara ya tano tangu mimi kuingia Bungeni na Serikali yenye macho, masikio, yenye pumzi, inasema haijui chochote kinachotokea kule Zanzibar. Hili ni jambo la aibu kwa Serikali.
Mheshimiwa Spika, sasa je, kwa sababu hapa mimi mwenyewe nimeleta ripoti za haki za binadamu na nikawapa baadhi ya Mawaziri hapa kuonesha matendo yanayoonekana Zanzibar. Je, Bunge hili kwanza halioni wakati sasa umefika wa kuunda Tume ya Kibunge kuchunguza mambo yanayotokea Zanzibar? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa sababu wananchi wa Zanzibar sasa hawana imani na vituo vya polisi ambako wamekuwa wakiripoti. Je, Mheshimiwa Waziri uko tayari kutoa commitment humu ndani Bungeni leo kwamba tukutane Uwanja wa Amani tarehe ambayo yeye anataka, tumletee wananchi ambao wameonewa, wamenyanyaswa, wamepigwa, wamedhalilishwa, tumuoneshe kwamba watu wapo na ushahidi wa hili Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani akiri, mara ngapi nimemwandikia na hata siku moja hajaja Unguja wala Pemba tukafanya naye kazi kuhusu suala hili? Ahsante.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ni kweli Mheshimiwa Mbunge ameshatoa hoja hizo na ameandika, lakini sehemu moja tu anasema Waziri wa Mambo ya Ndani hajaja Unguja ama Pemba. Mimi nimeshafika Unguja na Pemba na…
Mheshimiwa Spika, taratibu za utendaji wa kazi zinafanyika kwa kutumia vikao na baadhi ya Wabunge nilikutana nao, tena Wabunge wa Majimbo mpaka Pemba na Mheshimiwa Khatib ni Mbunge mmojawapo na nilionana naye.
Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba utaratibu wa upokeaji wa malalamiko upo kwa njia zilizo rasmi na hakuna utaratibu wa kuweka parade uwanjani kupokea malalamiko. Kwa sababu vitendo vya aina hiyo ikiwa vimetokea tunapokea malalamiko na kuna taasisi nyingine ambazo zinatakiwa ku-verify kwamba vile vilifanyika.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa sababu Mheshimiwa Mbunge ndiyo tunaanza tu Bunge leo, waelekeze watu wako na mimi nitawaelekeza watu wangu wafike na wafikishe hayo malalamiko, halafu verification zifanyike kujua ukweli wa hicho kinachofanyika.
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Zama hizi si rahisi kukataa kuja kwa wawekezaji kuwekeza katika shule za kigeni na vyuo vikuu mfano ni Shule za Sekondari kama Feza na nyinginezo. Serikali haioni kuna haja kwa utata huu unaotokezea, kwa mfano Chuo cha KIU, Chuo Kikuu cha Zanzibar kiliwahi kutoza kwa dola na Serikali inasema haijui kuwa na sera ya vyuo au shule zinazokuja hapa ili waelewe nini wafanye na nini wasifanye ikiwa ni pamoja na kutolazimishwa na nchi za kigeni kufunga shule kwa sababu ya maslahi yao? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi vyuo vyote vimeshaelekezwa na vimejua nini wajibu wao kufuatana na kanuni na taratibu na sheria hizi. Labda jambo ambalo naweza nikalichukua ni kuendelea kuvikumbusha vyuo kama ambavyo tumekuwa tukifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutumia nafasi hii niombe tu kuvisisitiza vyuo pamoja na kwamba wanao uhuru huo wa kuweza kutumia fedha za kigeni lakini suala liwe ni kwamba mwananchi wa Tanzania sarafu yake ni Shilingi ya Kitanzania. Kwa hiyo, hiyo ipewe kipaumbele badala ya kutoa kipaumbele kwa fedha za kigeni.
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa hiki ni kituo cha pamoja au cha ubia kama ambavyo ingepaswa kuonekana wazi wazi katika taasisi mbalimbali za Muungano. Swali langu linakuja, je, Naibu Waziri anaweza kutuambia pamoja na kueleza kwamba nafasi za ushindani kuna Wazanzibari wangapi walioajiriwa katika taasisi hiyo? (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba vituo hivi ni pamoja na kufanya biashara na biashara huwa na faida na hasara. Je, Zanzibar imewahi kupata mgao wake wa faida japo nyama ya sungura ya 4.5%?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kwamba kuna Wazanzibari wangapi wameajiriwa katika kituo hicho nimekwisha sema kwamba kwa uelewa wangu mpaka sasa hivi sijaona kama kuna Mzanzibari ambaye ameajiriwa maana yake nimesema kwamba ajira zinatolewa na watu wanatakiwa kuchangamkia fursa hizo na kama wana uwezo na capacity na wanaofanyiwa interview wakishinda basi wataajiriwa. Lakini pia tunawahamasisha zinapotokea fursa na nafasi zinapotangazwa basi watu kutoka Zanzibar waombe nafasi hizo. Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusu suala la pili ambalo Mheshimiwa Mbunge ameliuliza kwamba kituo kinafanya biashara, je, Zanzibar imepata gawio kiasi gani katika miaka yote hiyo. Kama anavyofahamu kwamba kama hii ni taasisi ya Muungano tunajua kwamba gawio huwa linakwenda katika Mfuko Mkuu wa Serikali kwa hiyo, kutokana na huo Mfuko Mkuu wa Serikali kwa ujumla wake wanapata lile gawio kutokana na Sheria inavyotutaka. Ahsante.

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, naomba kuongezea na hasa kile kipengele cha pili kuhusu gawio. AICC haijawahi kupata gawio na hivi sasa Joint Finance Commission na Ofisi ya Msajili wa Hazina wameunda kikosi kazi ambacho kitachambua na kukisaidia kile kituo ili kiweze kupata faida na kuleta gawio Serikalini kuanzia mwaka ujao wa fedha.
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Wanaokwenda kwenye maeneo hayo ambako ni kwa kulinda amani mara nyingi hukutana na kujeruhiwa au kufariki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na hapa Tanzania
tumeshuhudia wanajeshi hao wakirudi wakiwa wamefariki na wengine wakijeruhiwa. Je, Serikali, hasa kwenye watu waliofariki, ina utaratibu gani ambao unafanya familia za wanajeshi hao, wapiganaji haokuendelea na maisha baada
ya bread winner wao kufariki? Hilo la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili, Mheshimiwa
Waziri umezungumza hapa kuna matatizo wakati wa kutayarisha vikosi, lakini mimi naona hii ni fursa.
Je, Serikali haioni kwamba, kuna haja ya kujifunza na kutafuta utaalamu kutoka nchi ambazo zime-specialize katika masuala ya kulinda amani, ili iwe ni fursa ya kufungua kituo (centre) ya ku-train watu kwa ajili ya kulinda amani kwa
ajili ya eneo hili la Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika? Ahsante.
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba katika baadhi ya maeneo ya ulinzi wa amani huwa vinatokea vifo na pengine pia huwa watu wanajeruhiwa, lakini upo utaratibu madhubuti
wa kuwafidia kwa yote mawili. Nitoe tu taarifa kwamba kwa wale ambao wamepoteza maisha katika ulinzi wa amani Umoja wa Mataifa wenyewe unafidia na wanaporudishwa hapa familia zao zinapata maslahi yao yote kwa mujibu wa utumishi ambao mhusika alikuwa ameutekeleza hapa nchini.
Kwa hiyo, katika hili hakuna mgogoro, fidia huwa
zinatolewa kama utaratibu unavyotaka kwa wote
waliojeruhiwa pamoja na wale waliopoteza maisha kwa pande zote mbili, Umoja wa Mataifa na Serikali na Jeshi la Wananachi wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa kujifunza kutoka maeneo mengine juu ya ulinzi wa amani; nataka nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba, hapa Tanzania tunacho chuo cha ulinzi wa amani. Tumepata msaada kutoka kwa Serikali ya Canada, wamekijenga na mara nyingi tunatoa mafunzo, si kwa Watanzania peke yao, ikiwemo na nchi nyingine za Afrika Mashariki wanakuja hapa kujifunza mafunzo haya ya ulinzi wa amani kwa hiyo, hili halina tatizo, tunaendelea vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jibu langu la msingi, nililosema ni upungufu wa fedha za matayarisho, si suala la mafunzo, mafunzo yapo na chuo tunacho na mafunzo yanaendelea pale kama kawaida.
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na ahsante kwa mwalimu wangu. Napenda kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mwalimu wangu utakuwa unajua kwamba katika siku za karibuni kumekuwa na vitendo vingi vya utesaji na vimekuwa vikitajwa hadharani, lakini Mahakama zitapewa nguvu zaidi kama Tanzania itaridhia mikataba ya Kimataifa. Kuna mkataba mmoja muhimu wa Convention Against Torture mpaka leo Serikali inasuasua kujiunga.
Je, ni lini Serikali itaridhia mkataba huo muhimu ili Mahakama zipate nguvu zaidi kushughulikia masuala haya? Pamoja na kwamba suala hilo limetajwa katika Katiba, lakini mkataba huo ni muhimu.
Swali la pili, hadi sasa mfumo uliopo hauruhusu Ripoti ya Haki za Binadamu kujadiliwa katika Bunge, inawasilishwa lakini haijadiliwi na kwa maana hiyo, Waheshimiwa Wabunge hawana uelewa wa pamoja au uelewa mkubwa wa kujua kiasi gani madhara ya haki za binadamu na namna zinavyokiukwa kwa kulinganisha hata ripoti ya karibuni ya Amnesty International inayoonesha kwamba ukiukwaji wa haki za binadamu Tanzania ni mkubwa sana.
Je, kwa weledi wako, ushawishi wako, karama ulizopewa na Mwenyezi Mungu, ni vipi utaweza kuishawishi Serikali ili ripoti hiyo iweze kujadiliwa ili Waheshimiwa Wabunge wajue yapi yanatokezea katika nchi yao?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, kama alivyoeleza, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yenyewe inakataza vitendo vyovyote vya kumtesa, kumtweza na kumdhalilisha mtu. Tafsiri ya Ibara hiyo ya Katiba imewekwa wazi na Mahakama na Rufaa katika kesi ya Mbushuu Mnyaroje dhidi ya Serikali ambapo Mahakama ya Rufaa ilieleza wazi kabisa kwamba vitendo vyovyote vinavyomtesa mtu, kumtweza na kumdhalilisha, havikubaliki na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mahakama ya Rufaa ilikwenda mbele zaidi, ilitumia mikataba ya Kimataifa ile ambayo Tanzania imeridhia na ile ambayo haikuridhia kama msaada kwao wa kutafsiri maana ya neno au maneno utesaji, udhalilishaji na utwezaji. Kwa hali hiyo basi, maoni hayo kwamba mkataba huu dhidi ya utesaji ambao tayari misingi yake imo ndani ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ambayo tayari Mahakama ya Rufaa ambayo ndiyo Mahakama ya mwisho ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeyakubali, yatafikiriwa ili kwa wakati muafaka jambo hilo lifanyike. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Ripoti ya CHRAGG kuletwa Bungeni, maoni hayo nimeyapokea na labda kwa upya wangu nitauliza ni jinsi gani yanafikishwa, maana hata kikao kimoja cha Baraza la Mawaziri sijakaa ili nijue utaratibu wa kuyafikisha, kujadiliwa ili nikiongozwa njia ya kuku mgeni kamba kuwa imefunguka, basi nitajua jinsi ya kwenda nalo.
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kwamba katika hali halisi inavyoonesha kwamba Tanzania haijawahi kuwakilishwa nje ya michezo ya kuogelea, mpira wa miguu, riadha, ngumi katika ile michezo ambayo huwa inataka qualifications, lakini moja ya tatizo kubwa ni choice ya michezo yenyewe na pili ni ufadhili wa michezo yenyewe. Mimi siamini kwamba Serikali ndiyo isimamie kufadhili michezo kwa sababu ina-priority nyingi.
Je, Waziri haoni kwamba wakati umefika sasa kuja na mwongozo au sera ya namna ya corporate Tanzania kuchangia katika michezo? Kwa mfano Uingereza British lottery ndiyo inayodhamini Olympic system nzima ya Uingereza. (Makofi)
Swali la pili, ipo michezo ambayo kwa gharama zake
na kwa uenezi wake ni rahisi sana kuenea, mchezo chess investment kubwa wanayotaka ni chess board ambayo in-cost labda dola sita au dola saba, baada ya hapo ni kuwa-train tu watoto au vijana.
Je, Serikali inaweza kushaurika kwamba huu ni mmoja kati ya mchezo ambao unaweza kuwa kipaumbele katika Taifa, kwa sababu hauna gharama na kwa sababu unaweza ukaenea katika hali ya haraka katika nchi?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Ally Saleh Ally kwa jinsi alivyo mdau mkubwa katika maendeleo ya michezo na amekuwa akichangia sana sana masuala ya michezo katika Bunge hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lake la kwamba kuna michezo ambayo haijawahi kuwakilishwa Kimataifa, nitoe mfano tu kwamba kwa mchezo wa kuogelea nchi yetu imeshawahi kuwakilishwa, kuna vijana ambao walishawahi kwenda Canada na wakaiwakilisha nchi yetu, tuliwapa bendera na mmoja alishika namba nne, lakini pia hata riadha, walishawahi kuwakilisha nchi yetu kimataifa na mmojawapo ni Simbu na anamfahamu. Ndugu Simbu ameshawahi kutuwakilisha Kimataifa na Serikali huwa inatenga bajeti kwa ajili ya hawa, lakini hatua za awali huwa zinafanywa na Tanzania Olympic Committee ambapo inawaandaa wale wachezaji na fedha zinatoka Olympic Kimataifa na wanapofuzu sasa kushiriki mashindano yale Kimataifa ndipo Serikali inapowawezesha. Mwaka 2016/2017 Serikali ilitenga fedha na wanariadha wetu waliweza kuiwakilisha Tanzania katika michezo ya Olympic.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mwongozo wa ushiriki wa sekta binafsi tunakubaliana na hilo lakini tunakwenda hasa na sera kwa sababu, sera yetu inatutaka kusimamia michezo sio tu kwa kuegemea kutambulika Kimataifa, tunasimamia michezo kwa madhumini mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kuimarisha afya, afya ya Watanzania kwa ujumla, pia kudumisha amani, umoja, mshikamano na upendo, vilevile kuhakikisha kwamba tunatambulika kimataifa kama anavyosema na kumjenga Mtanzania kuwa jasiri, kukabiliana na matatizo mbalimbali. Kwa hiyo, yako masuala ya msingi ambayo yanatupelekea Serikali kusimamia michezo.
Kwa upande wa mchezo anaoupendekeza wa chess katika swali lake la pili, tunapenda sana kutoa wito kwa wananchi wote kwa wananchi wote kwamba pale ambapo kuna michezo wanayoiona ni mipya na inafaa kuingizwa katika sekta ya michezo na hasa katika shule za msingi na sekondari, ili wanafunzi wetu waweze kujifunza, tunahimiza kwamba wananchi kama hao, Walimu ambao wanaweza kufundisha michezo hiyo wajitokeze ili waweze kufundisha kwa sababu, Azimio la Michezo la Umoja wa Mataifa la mwaka 1978 linahimiza wananchi wafanye ile michezo wanayoiweza, michezo wanayoipenda, michezo ambayo wana amani nayo. Ahsante. (Makofi)
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Spika, ahsante. Majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri ni mazuri kabisa na juzi tu nilibahatika kupata mafunzo na Wajumbe wa Kamati ya Katiba na Sheria kuhusu Mfuko huu. Ni Mfuko mujarabu kabisa kwa watu wengi, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Kwanza Naibu Waziri anaonaje akieneza elimu ya Mfuko huu ambao mafao yake yametandawaa na yanaweza kuwafaa watu wengi sana? Anaonaje kukuza elimu ili wafanyakazi au waajiri wengi waweze kujiunga?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Serikali haioni sasa ni wakati wa hata Wabunge kuingizwa katika Mfuko huu kwa sababu ya manufaa yake ambayo hayawi-covered na Bunge lenyewe au na Mifuko mingine ya kijamii? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA):
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza kuhusu elimu, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi umeendelea kutoa elimu katika ngazi za Mikoa na mpaka Taifa na kuhusisha taasisi mbalimbali na lengo lake ni kuendelea kuwajengea umma wa Watanzania uelewa juu ya Mfuko huu na vilevile mafao yanayotolewa na Mfuko huu.
Mheshimiwa Spika, kwa taarifa tu ni kwamba Mfuko huu unakuja kutibu lile tatizo la miaka mingi ya malipo ya fidia kwa wafanyakazi ambapo kwa mujibu wa Sheria ya mwaka 1949 malipo ya mfanyakazi aliyekuwa akiumia kazini ilikuwa ni takribani kiasi cha Sh.108,000 lakini sasa sheria hii imekuja kutibu changamoto hiyo na tumeendelea kutoa elimu kuhusiana na Mfuko huu.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea kutoa elimu zaidi ili wananchi na hasa wafanyakazi na waajiri wote wauelewe vema na waweze kuitii sheria hii.
Mheshimiwa Spika, swali la pili la nyongeza ameuliza kuhusu Wabunge kuingizwa katika utaratibu huu. Kwa mujibu wa Mwongozo wa Mfuko huu, una-cover both private sector and public sector. Tumepokea maoni ya Mheshimiwa Mbunge ambayo yanahitaji majadiliano, lakini kwa sasa niseme pindi pale jambo hili litakapofanyiwa kazi tutaona namna ya kushirikisha taasisi hizi mbili na kuona uwezekano wake.
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kumuuliza Mheshimiwa Waziri, je, anaweza kutueleza hapa kwamba kuna chuo chochote kile ambacho kinaendesha kozi ya ubobezi ya diplomasia ya kiuchumi hivi sasa? Kama hakipo, je, Serikali ipo tayari kutumia nafasi yake kushawishi specifically kuendesha kozi hizo bobezi katika kiwango cha Masters na Ph.D ili tupate hao watalaam wanaotakiwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, vyuo vya ubobezi wa diplomasia viko vingi, lakini kama nilivyosema kwenye majibu ambayo niliongezea katika maswali ambayo ameuliza Mheshimiwa Ngwali, nimesema kwamba katika bajeti ya Wizara, katika vitengo vyetu tumepanga bajeti ya kuhakikisha kwamba hao watumishi wanapata mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu na mafunzo haya wanayapata kutoka kwenye Chuo cha Diplomasia, vilevile wanapata nje ya nchi ambako kuna mafunzo ambayo ni ya ubobezi pia.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Ally Saleh kwamba jambo hili Wizara inalitambua.
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Bunge hili limenipa heshima ya kuwa mwakilishi katika Bunge hili la SADC, lakini mpaka hivi sasa sifikiri kama SADC inaeleweka sana kwenye umma wa Watanzania. Ili kuongeza uhalali wake.
Je, Waziri haoni sasa kuna haja ya kuijulisha SADC kwa umma zaidi kuliko ilivyo hivi sasa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lingine ni kwamba kwa kuwa fursa zilizopo ni nyingi mno na jana tulijadili sana suala la economic diplomacy ambayo siku zote ni two way na inataka uwe very aggressive katika kuikabili; fursa zilizopo ni nyingi sana.
Je, Serikali haioni kwamba sasa wakati umefika mkakati wa Watanzania kunasa fursa zilizoko SADC uwe wazi ili Watanzania wengi waweze kuzinasa fursa hizo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na Mheshimiwa Ally Saleh kwamba wakati umefika wa kunadi fursa zilizoko katika Jumuiya hii ya SADC. Na sisi kama Wizara, kama mnavyojua kwamba tumeweka mkakati wa kutangaza na kutoa vipindi tofauti tofauti katika redio, tv, brochures, lakini pia tutaweka mkakati wa makusudi kwenda sehemu mbali zaidi kwa kuwaita wafanyabiashara na watu wa kawaida ili waweze kujua fursa zilizoko katika SADC.
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Jana tu nilimpongeza Waziri Mkuu kwenye twitter kwa tamko lake ambalo limesema kila Wizara na Idara itoe taarifa kila mwaka imetenga kiasi gani kwenye kuimarisha huduma kwa watu wanaoishi na ulemavu. Nafikiri hili ni tamko zuri sana na linafaa kupongezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali imejipangaje, utaratibu huu tutaanza kuuona katika mwaka huu wa fedha? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu huu kama Serikali tumeu-plan kwamba uanze kuonekana katika bajeti ya mwaka huu wa fedha. (Makofi)
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nakubaliana na Waziri kwamba suala la kwanza ni ukaguzi, lakini kwa kweli suala la ujuzi na utaalam ndio muhimu sana katika uokozi.
Je, Serikali imejiandaa vipi katika suala hili la kutayarisha umma na wataalam wa kuweza kufanya uokozi kuliko kungojea kutibu badala ya kuzuia?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tumeongelea umuhimu wa shughuli za SUMATRA na hapa tuliongelea masuala ya ukaguzi, lakini unafahamu kwamba SUMATRA wana kituo kikubwa Dar es Salaam ambacho kinashughulika na masuala ya uokozi katika bahari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo hiki vilevile kina vituo vidogo Mwanza na wanawasiliana na vituo vingine vya sehemu mbalimbali katika Bahari ya Hindi ili kuhakikisha kwamba kama kunatokea tatizo lolote vyombo hivi ambavyo vinashirikiana hata na wenzetu wa Marine Service kuhakikisha kwamba usalama wa baharini unakamilika. Mheshimiwa Ally Saleh unafahamu kuna tower kubwa sana kwenye Bandari ya Dar es Salaam kazi yake kubwa ni kuhakikisha kwamba ina-coordinate shughuli zote za uokozi na wataalam tunao.
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Spika, pamoja na sifa nyingi Mheshimiwa Waziri alizozimimina kwa bondia Hassani Mwakinyo, kama ulivyosema ni kwamba hajulikani, hata nchi ilikuwa haijui kama anapigana mpaka jana usiku baada ya kutoka matokeo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia katika Kombe la Dunia mchezaji mwingine kutoka Tanga alijitokeza akichezea timu ya Denmark tukabaki tunauma vidole tu, hatukujua kwamba mchezaji yule yupo na anaweza kuisaidia Tanzania.
Mheshimiwa Spika, je, Mheshimiwa Waziri haoni sasa kuna haja ya kuwa na kanzi data endelevu ili kufuatilia vipaji vya watoto wetu wanaozaliwa nje, kuwashawishi kuja kuchezea Tanzania katika timu mbalimbali? kanzi data endelevu? (Makofi)
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, naomba tu nimtaarifu Mheshimiwa Ally Saleh kwamba mwanamasumbwi Mwakinyo katika tasnia ya michezo tulikuwa tunamfahamu kabla ya ushindi wake mkubwa, alikuwa Bingwa wa WBA Bara la Afrika sasa huyu mtu Bingwa wa Afrika, usipomjua sasa na wewe lakini tulikuwa tunamtambua.
Mheshimiwa Spika, lingine nimeeleza kwamba katika Wanamasumbwi 1,854 wa Welterweight katika dunia alikuwa wa 174, hapo pia siyo padogo ni pakubwa. Kwa hiyo, tumpongeze tu huyu kijana na tunachukua hatua kweli sasa hivi kuhakikisha kwamba vijana wetu wengi wanaofanya vizuri katika michezo duniani tunawatambua na tunaendeleza vipaji vyao.
Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie tu Mheshimiwa Ally Saleh kwamba hatua hizo tumeshachukua na utaona baada ya muda siyo mrefu kwamba tunawakusanya wote kuweza kuchangia maendeleo ya michezo hapa nchini.
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mchezo wa chess unachezwa na karibu watu milioni 800 duniani kote, lakini pia katika hali ya ushindani wa hali ya juu unachezwa na karibu watu milioni 20. Pia kuna chess olympia yaani olympic ya chess peke yake. Kwa jibu hili la Serikali, sioni nia yao kama wanataka mchezo huu ukue ufikie katika huo ukubwa (magnitude) ambayo nimeielezea kwa sababu wanasema kwamba ukuzwe na wadau.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali iko tayari; kwa sababu mchezo huu hauna gharama kubwa katika kuuwekeza, ipo tayari kuwashawishi Cooperate Tanzania iuchukue mchezo huu, iukuze na uweze kuchezwa katika upana mkubwa angalau tuwakute wenzetu Kenya, Uganda na Zambia majirani zetu ambao wapo mbele?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amekiri kwamba mchezo huu unakuza akili na ufikiri, lakini mchezo huu maumbile yake unafundisha namna ya kujihami na namna ya mbinu za kijeshi. Je, Serikali iko tayari kutumia nafasi yake kuona kwamba mchezo huu unachezwa katika hali ya kukuza vyombo vya ulinzi? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba tu nisisitize kama nilivyosema kwenye swali langu la msingi kwamba kwa kweli hakuna mchezo wowote hapa nchini uliokuzwa na Serikali bila wadau, haitawezekana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Ally Saleh ajitahidi kwa nafasi yake ya Ubunge kuhimiza wadau mbalimbali waweze kuubeba huu mchezo kama michezo mingine inavyofanyika na Serikali tupo tayari kutengeneza miundombinu sahihi na mazingira ya kuweza kuhakikisha kwamba mchezo huu unakua kwa kasi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mchezo wa chess ni kweli kabisa nakubaliana naye kwamba ni mchezo ambao unahitaji akili, kama vilevile ambavyo mchezo wetu wa utamaduni wa bao unavyohitaji akili katika kuucheza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi nimefurahi sana wadau wa bao wameamua sasa huu mchezo uende Kitaifa. Nampongeza sana mwanabao mashughuli hapa nchini Mandei Likwepa na wenzake waendelee na sisi tutawasaidia kuweza kuuhamasisha huu mchezo ambao ndiyo chess ya Kiafrika. Nina uhakika tukiuongezea vilevile manjonjo mbalimbali unaweza kuwa pengine bora kupita hata huo wa chess kwa sababu hatujaufanyika kazi vya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimalizie tu kwa kusema kwamba tunakubali mchezo wa chess ni muhimu, ni mkubwa na unahitaji akili hata kwa majeshi ungefaa sana, lakini hata kwa wanafunzi wetu kutoka shule ya msingi mpaka Vyuo Vikuu unafaa sana, lakini naomba wadau wawe mstari wa mbele badala ya kuisubiri Serikali ndiyo itangulie mbele katika mchezo huu.
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Swali la kwanza, Tanzania tunalenga kujiondoa kwa watalii 1,300,000 kwa mwaka na pia kujiondoa kwenye mchango wa utalii katika pato la Taifa kwa asilimia 17.5 na pia kufikia ajira milioni mbili zinazotokana moja kwa moja na utalii. Je, Serikali haioni kiwango cha diploma na certificate ni kidogo kwa sasa na kwamba tuende kwenye degree? Ni lini Serikali inajipanga kuongeza hadhi chuo hicho kiwe na uwezo wa kutoa degree?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, injini ya kutawala sekta ya utalii ni elimu na ujuzi katika eneo la menejimenti. Je, ni lini Serikali inapanga kuwezesha Chuo hicho cha Utalii kutoa course ya juu ya menejimenti ili kuondoa wageni kutawala sekta hii katika eneo la menejimenti? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Ally Saleh, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba mpaka sasa hivi tumekuwa tukitoa stashahada na astashahada lakini hivi sasa Serikali ina mpango wa kuanzisha degree katika maeneo hayo kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Columbia kutoka Canada. Baada ya kukamilika mitaala na ikishapitishwa, basi tutaanza kutoa hizo degree ambazo zitawaandaaa vijana wetu katika hizo fani ambazo Mheshimiwa Mbunge ameuliza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kuhusu masuala ya mafunzo ya menejimenti, ni kweli kabisa tumekuwa na changamoto kubwa katika mafunzo na course zinazotolewa kwa ajili ya menejimenti kuwaandaa vijana kuweza kushika nyadhifa mbalimbali katika hoteli zetu na katika maeneo mbalimbali. Hivi sasa Wizara kuanzia mwaka wa fedha 2018/ 2019 tunategemea kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa watu mbalimbali, ambayo yatahusu watu zaidi ya 800 katika maeneo ya menejimenti ili kuwaandaa na kuweza kushika nyadhifa mbalimbali na nafasi katika utumishi katika maeneo ya utalii.
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Tatizo la ubakaji watoto linaoneka ni kubwa sana Mkoani Mara. Kamati ya Katiba na Sheria juzi ilikwenda Mara na tukapata taarifa za kutisha kutoka kwa Mkuu wa Mkoa Mheshimiwa Malima. Kuna Mwalimu kwa mfano amewafanya wake zake watoto 10 wa darasa la kwanza.

MBUNGE FULANI: Darasa la kwanza?

MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Spika, nitarudia, amewafanya wake zake watoto 10 wa darasa la kwanza.

MBUNGE FULANI: Aaaah.

MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Spika, kuna taarifa nyingi za kutisha juu za ubakaji kwa rika zote, kwa watu wazima na kwa watoto. Je, Serikali ama kupitia Wizara ya Afya au Bunge haioni haja sasa ya kuunda Tume au ya kutafuta utaratibu wa kwenda kulitazama tatizo hili ambalo ni kubwa inafika watu wanauliwa? Risasi zinatumika halafu watu wanakimbia upande wa pili wa Kenya inakuwa vigumu kulishughulikia. Mkuu wa Mkoa Adam Malima alikuwa na pain kubwa alipokuwa akituelezea juu ya suala hili. Naomba Serikali ifikirie jambo hili, ahsante.
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, pamoja na shinikizo kubwa kutoka nchi za Magharibi, shinikizo la ndoa za jinsia moja, shinikizo la kuuona ushoga kama haki za binadamu, bado nchi 38 kati ya nchi 54 za Afrika zinapinga masuala hayo na Tanzania ni mojawapo. Si hivyo tu, sisi tume-criminalize yaani vitendo hivyo ni makosa ya jinai na watu wanafungwa. Kwa hiyo, bado sisi ni moja ya nchi ambazo tumekaa vizuri katika kulinda jamii yetu.

Mheshimiwa Spika, tatizo kubwa ni kwamba jamii inaficha haya matatizo. Kwa mfano, matatizo ya watoto kulawitiwa au kubakwa kwa sehemu kubwa yanafanywa na ndugu katika jamii. Tukianza upelelezi familia zinawalinda hawa watu hawatoi ushahidi, ni tatizo kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, katika sheria kama hakuna ushahidi huwezi ukamfunga mtu na kosa hili ni kubwa, adhabu ni kali sana.

Mheshimiwa Spika, naomba nitoe wito kwa Tanzania tatizo ni kubwa sasa, tunaomba ushirikiano kwa vyombo vya dola ili tuweze kuwapata hawa wahalifu wanaojaribu kuchafua generation ya kesho, kesho kutwa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Spika, ahsante. Katika siku chache ambazo nimeridhika la jibu la Serikali, this is a very good answer from the Government. Kuna takwimu za kutosha, kuna maelezo ya kutosha. Hivi ndivyo ambavyo ningetarajia majibu ya Mawaziri wengine yawe kama haya. Nina maswali mawili ya ziada. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, chuo chetu ni cha miaka mingi hivi sasa na kama uzoefu, basi upo wa kutosha: Je, Mheshimiwa Waziri katika muongo ujao, miaka kumi ijayo, anakionaje chuo chetu? Kitakuwa kimefikia hadhi na kiwango gani?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kada ya wana- diplomasia ni muhimu sana, kuna ambao tunaamini kwamba chuo hiki kinapaswa kuwa ndiyo alama ya Tanzania maana Career Diplomacy na hata Political Diplomacy wote wanapita hapa ili kwenda ku-shape sera na mitizamo na namna ya kuilinda na kuitetea Tanzania.

Je, kwa kiasi gani chuo hiki kinaweza kutumika kuwa ni think tank ya kujenga sera na mikakati ya kidiplomasia ili kwenda kuitetea nje kwenye ushindani na ukinzani wa Kidiplomasia?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Awali ya yote, nichukue fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Ally Saleh kwa pongezi alizozitoa kwa jibu ambalo tumelitoa. Pili, nichukue fursa hii kujibu maswali yake mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza aliuliza: Je, tunakionaje chuo kwa miaka kumi ijayo? Naomba tumweleze Mheshimiwa Ally Saleh, Mbunge wa Malindi pamoja na Watanzania wote kwamba Chuo chetu cha Diplomasia ni chuo ambacho kinaheshimika sana Barani Afrika. Umeona idadi ya nchi ambazo zimeleta wanafunzi hapa na zinaendelea kuleta wanafunzi hapa, hiyo ni ishara tosha kwamba heshima ya chuo hiki ni kubwa.

Mheshimiwa Spika, Mpango wa Wizara ni kukifanya Chuo hiki sasa kivuke mipaka kwenda nje ya mipaka. Tuna makubaliano ya awali na ndugu zetu wa Argentina waweze kukitumia chuo hiki kupata elimu ya Diplomasia. Hiyo ni ishara kwamba tunavyokwenda miaka kumi ijayo, yajayo yanafurahisha zaidi.

Mheshimiwa Spika, swali la pili aliuliza; je, Chuo kinaweza kuwa kama think tank? Hivi sasa kada ya Diplomasia inakuwa vizuri, tumepata wataalam wengi na sisi kama Serikali tunaendelea kuimarisha hiki chuo kwa kuweza kusomesha waatalam wengi zaidi na kuleta wengine kutoja nje kwa kupitia nyanja za ushirikiano ili kukifanya chuo hiki kiendelee kuheshimika na kitoe waatalam wengi watakaosaidia Tanzania katika Diplomasia.
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana kabisa na hoja ya Mheshimiwa Bagwanji kwamba wakati wa uchaguzi kunakuwa na fujo nyingi Zanzibar. Ni kweli vilevile kwamba wakati huo kunakuwa kama uwanja wa vita Zanzibar; vifaru, magari ya deraya na vitendo vya kiharamia vingi vinafanywa na vikosi vya SMZ. Je, ni lini Serikali ya Muungano itaacha kutaka interest za matokeo ya Zanzibar kwa kuingilia kwa njia mbalimbali na badala yake waaachie mfumo wa demokrasia ufanye kazi na mshindi apewe ushindi wake?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Ally Saleh, Mbunge Malindi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza si sahihi kwamba Serikali imekuwa ikiingilia chaguzi. Hata hivyo, kuhusiana na hoja yake ya ulinzi kuimarika nyakati za uchaguzi Zanzibar hii inatokana na vitendo vya kiharamia ambavyo vimekuwa vikifanywa mara nyingi na hasa na vyama na upinzani. Tumeshuhudia katika uchaguzi mbalimbali hususani Chama Kikuu cha Upinzani Zanzibar wamekuwa wanaongoza katika ukiukwaji wa taratibu za sheria za uchaguzi.

WABUNGE FULANI: Aaaaa.

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumza hivyo kwa uthibitisho nikiwa nasimamia Jeshi la Polisi, nakijua nachokizungumza kwamba nathibisha kwamba Chama Kikuu cha Upinzani Zanzibar kimekuwa kikikiuka taratibu za uchaguzi na kufanya vitendo ambavyo ni kinyume na sheria. Kwa hiyo, Jeshi la Polisi ama vyombo vya dola vitakuwa imara zaidi kudhibiti uvunjifu wa sheria ambao unafanywa na vyama hivyo katika chaguzi mbalimbali.
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kwa bahati ni siku ya watoto, yamekuja maswali mawili mfululizo na yakilenga juu ya suala la kudumaa, suala la makovu ya kuona mambo mabaya na ukuaji kiakili; lakini haya yote kama alivyosema Mheshimiwa Selasini yanaweza kwenda katika kitu kinaitwa All Childhood Development.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina fursa ya kukopa kwa mkopo nafuu kutoka World Bank dola milioni 200 kwa miaka mitatu sasa; na Serikali haijafanya hivyo ili iweze kutekeleza hiyo program ya All Childhood Development. Je, Serikali ni lini itawasiliana, ita-finalize na World Bank ili mkopo huo uweze kupatikana na uweze kutumika kwa ajili ya All Childhood Development tupate watu wenye akili zaidi katika Taifa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali tunafanya kazi kwa karibu sana na World Bank na katika programu mbalimbali za maendeleo ya awali ya watoto, moja ya maeneo ambayo tumejikita katika hizi huduma za afya, ama huduma za msingi katika hizi siku 1,000 za mwanzo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa kuwa hili analoniambia Mheshimiwa Mbunge kwangu linaonekana kwamba ni jipya, basi namwomba anipe maelezo zaidi katika suala hili ili tuweze kufuatalia, lakini World Bank tunafanya kazi nao kwa karibu sana na tunashirikiana sana katika masuala ya ustawi na maendeleo ya watoto.
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante pamoja na majibu yaliyotolewa na Mheshimiwa Jenista na Mheshimiwa Naibu Waziri suala la Local content ni muhimu sana katika nchi yoyote ili uchumi ubakie ndani na sio utoke nje. Lakini inahitaji maandalizi kama alivyosema. Sasa hivi sasa tuna sectoral individual locally content policies. Je, Serikali iko tayari sasa kuja na sera kubwa na mabadiliko ya sheria juu ya local content na pia sheria hiyo iwemo na vifungu ambavyo vinaweza kuwawzesha wananchi kifedha ili wafaidi localy content?
MHE. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa swali la nyongeza lililoulizwa na Mheshimiwa Ally Saleh na Mheshimiwa Ally Saleh anafahamu kwenye Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria tumekuwa tukitoa taarifa hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshaanza hiyo kazi nzuri baadhi ya sheria ambazo zimekwisha kutungwa kwa mfano Sheria ya Mafuta na Gesi, hizo zote zimeshawekewa misingi ya kisera ya local content na imeshaanza kufanya kazi kwenye kanuni na sheria hizo. Lakini naomba nimhakikishie ili kufanya maandalizi hayo muhimu Ofisi ya Waziri Mkuu imeshatoa mwongozo wa local content katika miradi yote ya kimkakati ambayo inaendelea kwa sasa ndani ya Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo hii miradi yote ujenzi wa reli na miradi mingine yote mikubwa ya kimkakati sasa hivi mwongozo wa local content umekuwa ukitumika na sisi kama Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi tunasimamia kwa karibu sana kuhakikisha wazawa wanafaidika na miradi hii mikubwa ya kimkakati ndani ya Taifa letu.
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kabla ya swali la nyongeza kwanza nilitaka kusema kitu juu ya mfumo wetu huu wa Bunge Mtandao, pengine hili linafaa kurekebishwa.

Mheshimiwa Spika, muuliza swali yupo nje ya Bunge na swali limekuja hakuna access aliyopewa muuliza swali kuweza kulipata swali in advance. Kwa hiyo, nimesikiliza swali moja kwa moja bila ya kuwa na taarifa kwa sababu mwenye swali hakuwa na njia ya ku-access.

SPIKA: Mheshimiwa Ally Saleh, hilo lilikuwa tulifanye kwa utaratibu mwingine ni kwamba tu mfumo mtandao unakupiga chenga, lakini hayo mambo yako covered kabisa. Kwamba mwenye swali Mbunge yeyote kama hayuko Bungeni analitaarifu Bunge na anataarifu ni nani amuulizie swali lake na huyo anayemuulizia swali lake anatumiwa majibu yote na kila kitu anatumiwa; kwa hiyo, hayo yote yako covered, mfumo mtandao yaani uko kisawasawa, uliza swali lako Mheshimiwa Ally Saleh. (Makofi)

MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, lakini mwenye swali ndio kaniambia kwamba hakuna taarifa yoyote aliyoitoa. Ahsante.

SPIKA: Mheshimiwa Ally Saleh, Spika akishakujulisha unamuamini Spika au unamuamini mwenye swali ambaye wala Bungeni hayupo? (Kicheko)

MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Spika, nashukuru; dhana ya swali hili ni kwenye haki jamii na kwamba, issue kubwa ni kupunguza idadi ya msongamano. Mheshimiwa Waziri hapa amesema kwamba kuna tatizo la idadi ya Majaji au Mahakimu, sasa je, anafikiri katika muda gani Wizara inajipa muda gani kuhakikisha kwamba hali itakuwa inatosha kiwango cha Mahakimu, Majaji na kulingana na kasi ya matendo ya jinai?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, amezungumza habari ya moja katika tatizo ni suala la ushahidi. Je, Mheshimiwa Waziri hafikiri kwamba kuna haja sasa ya kukazia kwenye suala la kukusanya ushahidi kujaribu kutumia mbinu mpya na za kisasa zaidi ili ushahidi ukamilike na ufikishwe Mahakamani kwa wakati, ili raia waweze kupata haki?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, katika Awamu hii ya Tano tumejitahidi sana, Serikali sio tu katika kuteuwa Majaji na Mahakimu, lakini pia katika kufungua Mahakama mpya kwenye Wilaya mbalimbali. Kwa kufuata utaratibu huu inaonekena kwamba katika kipindi cha maendeleo cha miaka mitano hii mafanikio ukilinganisha kipindi cha nyuma imekuwa ni asilimia 33.5.

Mheshimiwa Spika, kwa kutazama mwelekeo huu ninadhani tutaweza kufikia hatua nzuri tukimaliza mpango huu wa maendeleo ambao tunaona unamalizika mwaka huu na tukifuata utaratibu tuliokuwa katika mpango uliopita tunaweza kufikia zaidi ya asilimia 50 kwa kuweza kukamilisha mwelekeo wa ujenzi na uteuzi katika miaka mitano ijayo.

Mheshimiwa Spika, katika suala la upelelezi na mashahidi, mfumo mzima wa Mahakama sasa hivi ni kufanya kazi kwa karibu na mtambuka na vyombo vyote vinavyofanya kazi pamoja na haki, hasa Wizara ya Mambo ya Ndani, lakini pia tumeanzisha utaratibu wa electronic ambapo tunaweza kusajili, tunaweza kupata ushahidi kwa kutumia electronic katika mikoa mitatu sasa hivi na nia yetu ni kuhakikisha kwamba mfumo huu wa electronic unaenezwa kwenye mikoa mingine. Na kwa kweli, umesaidia sana katika kuharakisha mfumo mzima wa kutoa haki ikiwa ni pamoja na kutoa ushahidi. Ahsante.
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa kitu chema kinaanza nyumbani basi napenda kumuuliza Mheshimiwa Waziri kwa nini lugha ya alama haianzii hapa Bungeni pale juu tukawa na mkalimani maana hii haioneshi kwamba kweli tunataka mabadiliko kwa sababu Bunge lilitakiwa liwe mfano? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU (MHE. STELLA IKUPA ALEX): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ally Saleh, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ndani ya Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wapo wakalimani wa lugha ya alama wawili. Hata sasa hivi tunavyozungumza haya yanayoendelea hapa yanatafsiriwa kwa lugha ya alama. Ahsante.
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, base ya swali langu ni kwamba na-target Jumuiya, Nchi Wanachama na wananchi wanafaidikaje na hali hiyo. Sasa uchaguzi wa Serikali za Mitaa ndio chanzo cha awali kabisa cha kupima utawala bora kwa upande wa haki ya kuchagua na kuchaguliwa, haki ya maoni na kujieleza kwa hapa njia ya kufanya kampeni, lakini pia ni kigezo cha kupata Serikali Shirikishi kadri inavyowezekana.

Je, kwa hali hii ya wagombeaji kutoka upande wa upinzani kukatwa kwa zaidi ya asilimia 90. Je, Tanzania haioni kwamba inakiuka matakwa hayo ya Afrika Mashariki?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kwa matukio tunayoyaona hapa nchini madai ya haki za binadamu ambayo hata Human Right International Watch juzi imetutaja lakini pia kwamba ku-shrink kwa public space pia kuwanyima wananchi fursa ya kuona Bunge live, kuwaweka mashehe wa kiislamu kwa miaka saba ndani bila kuwafungulia shauri na pia kutokuwa na Tume Huru…

MWENYEKITI: Sasa Mheshimiwa Ally Saleh, swali unaongeza, unaongeza uliza mawili tu moja tayari, la pili malizia.

MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Je, Serikali ya Tanzania haioni kwamba haikidhi vigezo vya kuwa na utawala bora na haki za binadamu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza anasema je, Tanzania haikiuki viwango kwa mujibu wa Afrika Mashariki. Tanzania ni nchi ambayo inafuata misingi ya utawala bora, misingi ya haki ya binadamu kama ambavyo imeainishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na nyaraka nyingine za Kimataifa. Endapo kunatokea malalamiko yoyote tumesema bayana kupitia Afrika Mashariki, yeyote ambaye amekwazwa na lolote anaweza akaenda kulalamika kupitia Bunge la Afrika Mashariki pia kupitia Mahakama ya Afrika Mashariki na Serikali ya Tanzania ndio imeamua kuwa mwanachama ili kuwapa fursa wananchi wake kutoa malalamiko kwenye vyombo hivyo. Hicho ni kitendo cha wazi kabisa kwamba Serikali hii inaweza na inajali haki za binadamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, amesema pia kuna malalamiko kuna Human Right International Watch; malalamiko yanatoka mengi sana, ni vizuri yachunguzwe, yanatoka wapi, yanaletwa na nani na kwa nia ipi na yakifika yashughulikiwe kwa mujibu wa muundo ambao unao. Hata hivyo, nimhakikishie Mheshimiwa Ally Saleh (Alberto), Mbunge wa Malindi kwamba Tanzania ni nchi ambayo inaheshimu sana haki za binadamu, demokrasia na utawala bora. (Makofi)
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Spika, ahsante. Mheshimiwa Naibu Waziri amezungumzia habari ya huduma stahiki na sasa hivi mobility ni huduma stahiki kwa watu wenye ulemavu. Swali langu linakuja kwamba, je, haoni ni wazo nzuri sasa kwamba Serikali itoe agizo kwamba katika parking lots katika public spaces kunakuwa na uhakika wa nafasi ya kuwekwa maalum kwa watu wenye ulemavu ambao aidha wanaendeshwa au wanaendesha wenyewe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza Mheshimiwa Ally Saleh kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, huu ni ushauri mzuri ambao tunaupokea, lakini pia kama serikali tayari tumekwishaanza kufanya hivyo, hata tukienda kwenye airport mpya ambayo tumeijenga pale Dar es Salaam tumeona kabisa kuna parking maalum kwa ajili ya watu wenye ulemavu. Pia hata kama ukienda maeneo mengine hili limekuwa likifanyika, lakini tunapokea kama ushauri ili tuendelee kuhamasisha maeneo mengine kuwa na parking maalum kwa ajili ya watu wenye ulemavu. Vile vile kwa Watanzania wote ambao wananisikia waweze kulitekeleza hili kuhakikisha kwamba parking za watu wenye ulemavu zinakuwepo. Kwa kweli inakuwa ni usumbufu mtu mwenye mwenye ulemavu akifika akikuta magari yamejaa anaanzia kuhangaika na hasa akiwa anaendesha yeye mwenyewe. Ahsante.
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kuniruhusu kuuliza maswali mawili ya nyongeza, la kwanza ni kwamba kwa miaka miwili sasa, kumekuwa na matokeo ya kutisha ambayo kwa kweli, si asili ya Kitanzania, yakitokea kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu ni pamoja na kutekwa, kupigwa, kuteswa, kubamiza upinzani na mambo kama hayo, Je, Serikali kwa nini haijitokezi ikasimama ikahesabiwa ili tuone kama kweli haki zinalindwa Kikatiba na Kisheria? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Kwa muda sasa takribani, pengine miaka miwili, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora, haina Uongozi, na kwa hivyo pengine kuna ombwe la kutazama matukio mbalimbali ya haki za binadamu. Najua hivi sasa kuna mchakato wa kutafuta hao watu wa kujaza nafasi za Tume ya Haki za Binadamu, lakini Je, kwa nini Serikali inaachia hali kudorora mpaka Tume muhimu kama hii ikakosa uongozi kwa zaidi ya miaka miwili? (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, matukio ambayo umeyataja, na ambayo yametokea, yanajulikana Serikalini na Vyombo husika na hasa Jeshi la Polisi na Vyombo vingine vya Usalama vimekuwa vikifuatilia matukio hayo. Mara nyingi tunapata taarifa na majibu yanaridhisha, lakini kazi upelelezi na kazi ya kufatilia vituko kama hivyo na vitendo kama kama hivyo, inaweza ikachukua muda na Serikali imekubali kuchukua majukumu hayo na maswali haya yanaulizwa na wananchi kama unavyouliza, yanaulizwa pia Kimataifa na tuko tayari kutoa taarifa sahihi hapo vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama vitakapokamilisha uchunguzi wa namna hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni kuhusu uongozi wa Tume ya Haki za Binadamu, Tume ile ina Bodi tayari, ina watendaji tayari mchakato wa kumtafuta Mwenyekiti, au Mtendaji Mkuu, imekamilika na kilichobakia sasa ni kufikisha jina hilo baada ya upekuzi kukamilishwa na Vyombo vya Usalama na kuipeleka kwa Mamlaka ya uteuzi na hiyo inaweza kutokea wakati wowote, lakini kazi imekwisha kamilika na inaweza kutokea wakati wowote. (Makofi)