Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Salim Hassan Turky (2 total)

MHE. SALIM HASSAN ABDULLAH TURKY: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kuniona pamoja na majibu mazuri sana ya Waziri. Lakini katika majibu haya kuna swali la msingi ambalo Waziri naona kalikimbia, nalo ni kwamba Zanzibar kuna kiwanda cha sukari kinazalisha na kinauza sukari ile kwa shilingi 65,000 na hawaagizi sukari kutoka nje wao wamewekeza wanazalisha sukari wanauza shilingi 65,000 kwa wananchi wa Zanzibar.
Mheshimiwa Spika, swali la msingi ni kwamba viwanda vyetu vya Bara kwa nini hawawezi kutushushia bei saa hizi na ushahidi kamili ni huu ambao natoa na Bunge hili lisikie sasa hivi. Ni kwamba sukari sasa hivi katika soko la dunia linauzwa kwa bei ya dola 390, ukilipa kodi ya asilimia 25 na VAT asilimia 18 sukari hiyo inasimama kwa bei shilingi 65,000, leo Watanzania tunalanguliwa kwa kuuziwa sukari hiyo shilingi 110,000 kwa misingi gani? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, na hapa hapa tuliomba cost of production ndani ya Bunge hili wakati Naibu Waziri akiwa Malima toka mwaka ule mpaka leo cost of production ya viwanda hivi hatujaletewa ndani ya Bunge hili jamani. (Makofi)
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Spika, nimejitahidi kulieleza suala hili ila muda wenyewe hautoshi. Ni kwamba gharama za uzalishaji kwa viwanda vya Bara ziko juu kuliko Zanzibar, naomba nimepewa muda, muache niwaeleze.
MHE. SALIM HASSAN ABDULLAH TURKY: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Ukiangalia juhudi za Serikali ya kukuza uchumi huu, sasa hivi jinsi hizi benki zinavyokwenda tunaanza kupata mshituko kidogo. FBME imezama, M Bank nayo imezama, M Bank kama ninafahamu ni benki ya Tanzania hatuwahitaji Ma-Cyprus kuja kutujibu, lakini bado zile dhamana ambazo ni za Serikali, naomba sana kwamba Serikali itoe tamko rasmi kwa sababu wateja ni wengi ambao wanahangaika na Serikali iko hapahapa na hii benki iko hapahapa, na sasa hivi imechukuliwa na benki nyingine ya Serikali yetu.

Kwa hiyo, tunaomba sana tujulishwe hii hatma ya kudai fedha za M Bank, tunazipata vipi kwa uharaka wake? Ili watu waamini kuweka fedha benki maana sasa hivi sasa watu kuweka fedha benki tunaanza kuogopa, tunaona hizooo, zinazama.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kuna usalama mkubwa sana ndani ya Taifa letu, kwenye taasisi zetu za kifedha kwa sababu Benki Kuuu ya Tanzania iko macho na iko makini kusimamia sheria ya kuazisha benki hizi na taasisi za kifedha.

Mheshimiwa Spika, na niliombe sana Bunge lako Tukufu, tunapokuja na sheria ya kusimamaia hizi taasisi za kifedha, muwe mnatuunga mkono, ni kwa sababu tunaona wengi wa wateja wetu wanapoteza fedha kwa kuingia katika mifumo ambayo siyo sahihi na nilishukuru Bunge lako Tukufu kwa kuturuhusu kwenye Bunge letu la mwezi wa 11 kupitisha sheria ya huduma ndogo za fedha na sasa tunawafikia wote kule walipo ili kuhakikisha wateja wetu wote wanakuwa salama.

Mheshimiwa Spika, na niseme, hili la M Bank, kama alivyosema muuliza swali, M Bank imechukuliwa na benki nyingine. Kwa maana hiyo, M Bank siyo kwanza wataja wake wanatakiwa kusubiri mchakato kwa sheria ya ufilisi, hapana. Benki iliyoichukua M Bank, ina jukumu na dhamana kubwa ya kuhakikisha wateja wote wanalipwa na wanalipwa amana zao zote pale wanapozihitaji.

Mheshimiwa Spika, lakini niwaambie watanzania kwamba, kuweka fedha zao kwenye benki zetu ni salama na benki ambayo M Bank imeunganishwa inafanya vizuri na niwaombe waendelee kuacha amana zao huko kwa sababu faida ni kubwa ya kuacha fedha zao kwenyeakaunti zao.