Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Khalifa Mohammed Issa (10 total)

MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA aliuliza:-
Dawa za kulevya nchini zimekuwa na athari kubwa sana kwa wananchi wetu hususan kundi la vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa:-
(a) Je, Serikali haioni kuwa kwa kutumia vyombo vyake inaweza kubaini watumiaji, wauzaji mpaka vigogo wanaoingiza na kusambaza dawa nchini?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa dhati wa kuwaweka waathirika wa dawa za kulevya katika makambi maalum ya kuwatibu na hatimaye kurudi katika hali yao ya kawaida?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU - MHE. DKT. ABDALLAH S. POSSI) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khalifa Mohamed Issa, Mbunge wa Mtambwe lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali siku zote hutumia vyombo vyake kuwabaini, kuwakamata na kuwachukulia hatua za kisheria wafanyabiashara wadogo na wakubwa wa dawa za kulevya nchini kwa kushirikiana na wananchi wakiwemo watumiaji wa dawa za kulevya. Juhudi hizi zimefanikisha kuwakamata wauzaji wadogo na wakubwa na kuwafikisha kwenye vyombo vya kisheria. Baadhi ya watuhumiwa wakubwa wa biashara hiyo waliokamatwa ni Ali Khatibu Haji (maarufu kwa jina la Shkuba), Mohammed Mwarami (maarufu kwa jina la Chonji na Mwanaidi Mfundo maarufu kwa jina la Mama Leila).
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na Asasi za Kiraia inaendelea na progamu maalum ya kutoa huduma za upataji nafuu katika maeneo mbalimbali nchini. Aidha, Serikali imetoa mwongozo wa uendeshaji wa huduma hizo na inaendelea na ujenzi wa kituo kikubwa cha huduma za matibabu na utengemano katika eneo la Itega, Mjini Dodoma na inaratibu ujenzi wa kituo kama hicho Mjini Tanga.
MHE KHALIFA MOHAMMED ISSA aliuliza:-
Imekuwa ni kawaida kwa ndege ndogo zenye uwezo wa kubeba abiria kumi hadi kumi na sita kuendeshwa na rubani mmoja bila ya kuwa na msaidizi na rubani kama binadamu anaweza kukumbwa na hitilafu yoyote kiafya na kushindwa kumudu kuongoza ndege:-
(a) Je, Serikali haioni kuwa kuruhusu ndege kuongozwa na rubani mmoja ni sawa na kuyaweka rehani maisha ya abiria?
(b) Je, sheria za nchi yetu na zile za Kimataifa zinasemaje juu ya ndege ya abiria kurushwa na rubani mmoja?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa khalifa Mohamed Issa, Mbunge wa Mtambwe, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, taratibu zinazoongoza fani ya kuendesha ndege hapa nchini huongozwa na miongozo inayokubalika Kimataifa na ambayo imeridhiwa hapa nchini na Bunge. Katika taratibu hizo kuna matakwa ya kisheria na kiufundi ambayo yakifuatwa yanawezesha kuwa na uwezekano mdogo sana wa marubani kukumbwa na athari ya kiafya na kushindwa kumudu kuendesha ndege.
Mheshimiwa Mwenyekiti, marubani hupimwa afya zao na Madaktari Bingwa kila muda maalum kulingana na umri kama ilivyoainishwa katika Kanuni ya 140 mpaka 177 ya The Civil Aviation Personnel Licensing Regulations, 2012. Hivyo basi, Serikali inaruhusu ndege kuendeshwa na rubani mmoja kwa kuzingatia taratibu hizo. Aidha, Kanuni ya 32(5) inasema kwamba ndege iliyoandikishwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuruka kwa shughuli za kibiashara yenye uzito unaozidi kilo 5,700 itakuwa na marubani wasiopungua wawili.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, shughuli za usalama wa anga nchini zinaongozwa na Sheria Namba 80 (Civil Aviation Act) na Kanuni zilizotengenezwa chini yake. Aidha, urushaji wa ndege yenye abiria tisa au zaidi unaongozwa na Kanuni ziitwazo The Civil Aviation Operation of Aircrafts Regulations, 2012 ambapo ndege inayotimiza vigezo vilivyowekwa kwenye vifungu Namba (2), (3) na (4) vya Kanuni ya 32 kuwa na uzito wa chini ya kilogramu 5,700 inaruhusiwa kuendeshwa na rubani mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika viwango vinavyotolewa na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO) kwenye kiambatisho Namba 19 chini ya Mkataba wa Kimataifa wa Usafiri wa Anga wa Chicago, hakuna kiwango chochote kinachobainisha wazi kuwa ndege yenye uwezo wa kubeba abiria 10 au zaidi ni sharti iendeshwe na marubani wawili. Pia, hakuna hata mapendekezo ya kiutekelezaji (recommended practice) kwenye suala hilo. Aidha, kiambatisho cha sita chenye sehemu tatu kinachohusisha uendeshaji wa ndege (operations of aircrafts) ambacho ndicho kinachozungumzia idadi ya marubani katika uendeshaji wa ndege hakuna katazo hilo.
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA aliuliza:-
Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) upo katika Awamu ya Tatu ya utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ili ziweze kumudu mahitaji ya chakula, elimu, afya na lishe bora kwa watoto:-
(a) Je, Serikali haioni ipo haja ya kuongeza viwango vya ulipaji kwa kaya maskini hasa ukizingatia upandaji wa bei za mahitaji ya kila siku na kuporomoka kwa thamani ya sarafu yetu?
(b) Je, ni vigezo gani vya uhakika vinatumika ili kupata kaya maskini?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Khalifa Mohamed Issa, Mbunge wa Jimbo la Mtambwe, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ni wa miaka kumi na utatekelezwa kwa vipindi viwili vya miaka mitano mitano kuanzia mwaka 2013 – 2023. Madhumuni ya Mpango huu ni kuwezesha kaya maskini kuongeza kipato na fursa na kuinua kiwango cha matumizi yao.
Mheshimiwa Spika, kiwango kinachotolewa kwa walengwa ni ruzuku ambayo ni kichocheo cha kuifanya kaya iweze kujikimu hasa katika kupata mahitaji muhimu huku ikiendelea kujiimarisha kiuchumi kwa kuweka akiba na kutekeleza miradi ya ujasiriamali ili iweze kusimama yenyewe na kujitegemea baada ya kutoka kwenye umaskini uliokithiri.
Mheshimiwa Spika, ruzuku inayotolewa kwa walengwa imeongezwa baada ya kufanyiwa mapitio kwa kuangalia hali halisi. Hata hivyo, ieleweke kwamba viwango vinavyotolewa vilipangwa hivyo ili kaya maskini iendelee kujishughulisha na kazi nyingine za kuongeza kipato na
isitegemee ruzuku peke yake. Kwa uzoefu uliopatikana, umeonesha kwamba kwa kiwango hicho walengwa wameweza kuboresha maisha yao kwa kufanya shughuli mbalimbali ikiwemo kilimo, ufugaji, ujasiriamali na ujenzi wa nyumba bora, hivyo viwango hivyo vya ruzuku sio kidogo kama wengi wetu tunavyodhani.

(b) Mheshimiwa Spika, vigezo vya kupata kaya maskini huainishwa na jamii katika mkutano wa hadhara unaoendeshwa na wawezeshaji kutoka Halmashauri za Wilaya na kusimamiwa na viongozi wa vijiji/mitaa/shehia. Jamii huweka vigezo vya kaya maskini sana katika maeneo
yao. Hata hivyo, vigezo vikuu katika maeneo mengi ni kaya kukosa/kushindwa kugharamia mlo mmoja kwa siku, kaya kuwa na watoto ambao hawapati huduma za msingi kama elimu na afya kutokana na kuishi katika hali duni, wazee, wagonjwa wa muda mrefu na watoto yatima wanaoishi katika mazingira magumu na pia kukosa makazi ya kudumu au nyumba na mavazi muhimu.
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA aliuliza:-
Wananchi wengi wajasiriamali huwa hawapati mikopo katika taasisi za fedha kwa sababu hawana uzoefu na ujuzi wa kutayarisha andiko la uchanganuzi wa miradi ya kibiashara, pia hawana mali ya kuwawezesha kuweka dhamana.
Je, ni lini Serikali itaweka mpango madhubuti unaotekelezeka ili wananchi hao waweze kukopesheka?
Je, Serikali haioni muda umefika sasa kuzitaka taasisi za fedha kupunguza masharti ya ukopeshaji ili wajasiriamali waweze kupanua miradi yao na kuwapatia ajira watu wengine?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khalifa Mohamed Issa, Mbunge wa Mtambwe, lenye sehemu (a) na kama ifuatavyo:-
• Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inawawezesha wananchi ili waweze kukopesheka kupitia Sera ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ya mwaka 2004 na Sheria ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Na. 6 ya mwaka 2004. Sera ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi imeiainisha nia ya Serikali ya kuweka mazingira mazuri ya upatikanaji wa mitaji kwa kuboresha vyanzo vya akiba na kuchukua hatua za kuondoa vikwazo mbalimbali ili kuwezesha mabenki kukopesha kikamilifu amana zilizopo na kwa gharama nafuu kupitia vikundi vidogo vidogo na pia SACCOS na VICOBA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na sera hii, mipango, miradi na mifuko kadhaa imeanzishwa na Serikali ili kuwezesha wananchi kukopa kwa urahisi. Aidha, Serikali inaendelea kusimamia mipango na mifuko ya uwezeshaji nchini na wananchi wengi wanaendelea kunufaika na mikopo inayotolewa ambayo ina masharti nafuu.
• Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wetu wa mabenki na taasisi za fedha kwa sasa unaendeshwa kwa utaratibu wa ushindani, hivyo viwango vya riba pamoja na masharti mengine huwekwa na taasisi husika ili kuhakikisha marejesho. Jukumu la Serikali ni kuweka mazingira mazuri kwa vyombo hivyo kuweza kutoa huduma kwa wananchi.
Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania kulingana na mazingira inaendelea kuangalia viwango vya riba kwa mabenki na taasisi za fedha ili ziweze kumudu kupata fedha kwa ajili ya kukopesha wajasiriamali kwa riba ndogo. Mfano, ni hatua ambayo imechukuliwa na Benki Kuu hivi karibuni ya kupunguza kiwango cha riba kwa mikopo yake kutoka 16% mpaka 12%.
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA aliuliza:-
Kwa takwimu zilizopo inakisiwa kuwa watu wote wanaoishi na Virusi vya UKIMWI Tanzania ni zaidi ya milioni moja na laki tano na inaaminika kuwa na wanawake ndio waathirika wakubwa zaidi ikilinganishwa na wanaume.
Je, ni sababu gani za kataalam ambazo zimesababisha W anawake kuwa ni waathirika zaidi kuliko Wanaume?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Khalifa Mohamed Issa Mbunge wa Mtambwe kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, sababu za kitaam zinazosababisha wanawake kuathirika zaidi na maambuzi ya VVU na UKIMWI zipo kama nne na naomba nizitoe kama yafuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, sababu ya kwanza ni ya kimaumbile na kibaiolojia. Mwanamke yuko katika hatari zaidi ya kuambukizwa VVU ukilinganishwa na wananume kwa kuwa maumbile ya mwanamke ni rahisi kupata michubuko wakati wa tendo la ndoa na hivyo kurahisisha virusi vya UKIMWI kupenya. Aidha, maumbile ya mwanamke hupokea mbegu za kiume kutoka kwa wanaume wakati wa tendo la ndoa. Iwapo mwanamke atafanya mapenzi na mwanaume mwenye VVU, mwanamke huyo anaweza kuambukizwa virusi vya UKIMWI.
Mheshimiwa Naibu Spika, sababu ya pili kwamba kuna tabia na mazingira hatarishi ambayo husababisha hatari zaidi kwa wanawake kuambukiwa VVU, ikiwa ni pamoja na kufanya biashara ya ngono na kuanza mapenzi katika umri mdogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sababu ya tatu ni mfumo dume uliokuwepo katika jamii yetu unaowapa fursa wanaume ya kuamua kufanya ngono na wanawake wengi, kutotumia kondomu, kuoa wasichana wenye umri mdogo na na hata kufanya ukatili wa kijinsia. Mfumo huu unasababisha baadhi ya wanawake kuambukizwa VVU na hata kushindwa kueleza hali zao za maambukizi kwa wenza wao kwa kuhofia kuachika, kutengwa au kufukuzwa kutoka kwenye familia. Kwa kawaida mfumo dume huambatana na wanyanyapaa na ubaguzi ambao pia ni kikwazo kikubwa kwa wanawake kuwa wazi kuhusu hali zao za maambukizi ya VVU na hasa na hasa kutengwa na familia yao au jamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, na sababu ya mwisho ni kwamba wanawake wengi hujitokeza kupima kuliko wananume. Nitoe rai kwa wanaume kujitokeza kupima, tusitumie wenza wetu kama kipimo cha maambukizi yetu sisi.
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali italeta Bungeni Muswada wa Mabadiliko ya Sheria ya Mkopo wa Elimu ya Juu ili kuwapunguzia mzigo mkubwa wa malipo wanufaika wa mkopo huo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Khalifa Mohamed Issa, Mbunge Mtambwe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikifanya mapitio katika tozo na makato yanayohusu mikopo ya elimu ya juu ili kuwapunguzia mzigo wa tozo na makato wanufaika wa mikopo hiyo.

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia maelekezo ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuanzia tarehe 01 Julai, 2021 Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, itafuta Tozo ya Asilimia Sita (6%) ya kulinda thamani ya fedha inayotozwa kwa wanufaika wa mikopo hiyo. Vilevile, Bodi ya Mikopo itatekeleza maelekezo yangu ya kuondoa tozo ya asilimia kumi (10%) ya wanufaika wanaochelewa kurejesha mkopo baada ya muda wa miezi 24 kupita baada ya kuhitimu.

Mheshimiwa Spika, kutokana na kupunguzwa kwa mzigo wa makato na tozo, nitoe wito kwa wanufaika wote wa mikopo ya elimu ya juu ambao hawajajitokeza, kuanza kurejesha mikopo hiyo ili fedha hizo ziwasomeshe Watanzania wengine wahitaji.
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha uwepo wa marubani wawili kwenye ndege ndogo za abiria?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Khalifa Mohamed Issa, Mbunge wa Mtambwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ndege zote kwa mujibu wa vyeti vya utengenezaji (type certificate) huwa zina taarifa inayoelekeza mambo muhimu ya kifundi na usalama yahusuyo operesheni za ndege hizo. Pamoja na hizo nyaraka mbili, pia kuna kitabu cha maelekezo ya matumizi. Ndege zote zenye uzito wa kilogramu 5,700 kwenda chini ni ndege za rubani mmoja kwa mujibu wa nyaraka za mtengenezaji.

Mheshimiwa Spika, aidha, kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga na Sheria ya Kimataifa ya Usafiri wa Anga, haizuii ndege hizo kuendeshwa na rubani mmoja na ni salama kufanya hivyo. Hata hivyo, nchi yetu imeweka sheria ya kuwa na marubani wawili kwa ndege yoyote ya abiria yenye uzito unaozidi kilogram 5,700 hata kama mtengenezaji wake anaruhusu rubani mmoja mmoja, katika kujiwekea wigo mpana wa kuweka usalama wa anga.

Mheshimiwa Spika, aidha, Mamlaka ya Usafiri wa Anga imeweka utaratibu wa kuhakiki afya za marubani mara kwa mara kwa mujibu wa sheria. Uhakiki wa kati na mkubwa hufanyika kila baada ya miezi sita kwa marubani wenye umri unaozidi miaka 40 na kila baada ya miezi 12 kwa marubani wenye umri wa chini ya miaka 40. Uhakiki wa mara kwa mara na wa kushtukiza pia hufanyika. Aidha, rubani yeyote anayekutwa na changamoto za kiafya huwekewa sharti la kutoruka peke yake au kuzuiwa kuruka kabisa. Ahsante.
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA aliuliza: -

Je, ni kwa kiwango gani Mbunge anashirikishwa katika miradi inayoibuliwa na wananchi katika Jimbo lake kupitia TASAF?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Khalifa Mohamed Issa, Mbunge wa Mtambwe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, uibuaji wa miradi ya jamii inayochangiwa na TASAF hufanyika kwenye mikutano ya jamii ambayo huendeshwa na wataalam chini ya usimamizi wa viongozi wa maeneo hayo. Mbunge au Mwakilishi wa eneo husika kama anakuwepo wakati zoezi la kuibua miradi likifanyika hazuiwi kushiriki kwa kuwa hakuna mwongozo unaomtaka Mbunge asiwepo wakati wa zoezi la kuibua miradi.

Mheshimiwa Spika, wananchi huibua miradi ambayo inatatua kero walizonazo katika jamii kutokana na kukosekana kwa huduma stahiki. Ikiwa wananchi wote kwenye mkutano wameridhia mradi fulani kutekelezwa, basi moja kwa moja huo unakuwa ni chaguo lao. Lakini kama kuna miradi miwili au mitatu iliyopendekezwa, jamii hupiga kura na mradi utakaopata kura nyingi ndio unapewa kipaumbele cha kuanza kutekelezwa. Jamii ikishaamua mradi wa kutekeleza, timu ya Wataalam hufanya bajeti ya mradi huo na kurudi tena kwa wananchi kukubaliana kuhusu mchango wa jamii kabla bajeti hiyo haijawasilishwa TASAF kwa hatua nyingine.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kupambana na magonjwa yasiyoambukiza?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa Serikali katika kupambana na magonjwa yasiyoambukiza ni kutoa elimu kinga, kusomesha Madaktari Bobezi kwenye eneo hili pamoja na ununuzi wa dawa na vifaa tiba vya teknolojia ya juu katika utambuzi na tiba ya magonjwa yasiyoambukiza.
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA aliuliza: -

Je, ni kero zipi za Muungano zilizoibuliwa na kutatuliwa toka kuasisiwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khalifa Mohamed Issa Mbunge wa Mtambwe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali za pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimejadili na kuzipatia ufumbuzi jumla ya changamoto 22, ambapo baadhi ya

changamoto hizo ni gharama za kushusha mizigo Bandari ya Dar es Salaam kwa mizigo inayotoka Zanzibar, utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia, utaratibu wa vikao vya kamati za pamoja za SJMT na SMZ vya kushughulikia masuala ya Muungano. Aidha, changamoto zote zilizopatiwa ufumbuzi zimefafanuliwa kwa kina na zinapatikana kupitia tovuti yetu ya Ofisi ya Makamu wa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja zilizobakia kutatuliwa ni nne, ambazo ni Mapendekezo ya Tume ya Pamoja ya Fedha, Usajili wa Vyombo vya Moto, Uingizaji wa Sukari katika Soko la Tanzania Bara, na Mgawanyo wa Mapato Yatokanayo na Hisa za SMZ zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki na Faida ya Benki Kuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.