MHE. ALI VUAI KHAMIS: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Serikali naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa maeneo hayo yaliyotajwa ni maeneo ya utalii na kumekuwa na matukio ya uhalifu; je, Serikali ina mpango gani wa kuimarisha ulinzi wa dharura ili kuwe na amani?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa ujenzi wa nyumba na kituo cha polisi ni jukumu la Wizara; je, Serikali haioni haja ya kwenda kukaa na Serikali ya Mkoa, halmashauri na jimbo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kuhusu umuhimu wa kuimarisha usalama kwenye eneo hili lenye watalii wengi, nitumie nafasi hii kumwekeleza IGP na hususani Kamishina wa Polisi Zanzibar kuimarisha huduma za doria ya magari ya askari wanaokwenda kwa miguu au pikipiki ili kuhakikisha wananchi na watalii wanaotembelea eneo hilo wanakuwa salama.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili la kuimarisha ujenzi wa nyumba kupitia mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa (Halmashauri), hicho ndicho kipaumbele cha Wizara kwamba katika vituo vinavyojengwa hasa vile vidogo vya Daraja C ni jukumu la mamlaka zetu za Serikali za Mitaa ambazo ni moja ya kazi za msingi ya Serikali za Mitaa. Wizara imekuwa ikisaidiana na halmashauri hizi kukamilisha majengo hayo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tuendelee kushirikiana kuzihamasihsa halmashauri hizi ili watimize huo wajibu wao nasi tutimize wajibu wa kujenga vituo vikubwa na ku–support vituo vidogo wanapokuwa wamefikia kiwango cha umaliziaji, ahsante. (Makofi)