Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Yussuf Haji Khamis (5 total)

MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba kumuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa idadi ya watu ambao wanapoteza maisha kutokana na ajali za bodaboda basi hata tungekuwa vitani tungekuwa tunapigwa! Kwa hivyo, namuuliza Mheshimiwa Waziri, tuna mikakati gani ya ziada ya kutoa elimu juu ya waendesha pikipiki ili tuzipunguze ajali hizi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; barabara wanayokatisha Wabunge kuingia ndani na kutoka nje ya Bunge sio salama. Tarehe 5 juzi kagongwa Mbunge mwenzetu na kapata majeraha makubwa sana. Je, Serikali inawahakikishiaje Wabunge usalama wa eneo hilo? Ahsante.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kupata concern hiyo. Ni kweli watu karibu 7,000 ni wengi na ajali zaidi ya 31,000 ni nyingi sana. Tunalolifanya, kwanza
tumesemea iwepo elimu kwa kila mkoa na kila wilaya ambazo zinafanywa na department yetu inayoshughulika na masuala ya usafiri.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili nitoe rai hata kwa Wabunge tunapokuwa na vijana wetu, watambue kwamba vyombo hivyo pamoja na kuwa na matairi mawili lakini ni vyombo vya moto. Wazingatie masharti ya uendeshaji wake kwa sababu kwa kiwango kikubwa kwenye upande wa magari huwa kuna sababu zingine ambazo
zinasababisha ikiwepo na uchakavu wa vyombo, lakini kwa bodaboda ajali nyingi zinasababishwa na kutokuzingatia utaratibu wa uendeshaji ikiwepo kwenda mwendokasi na kuendesha vyombo hivyo kabla ya kuwa wamejifunza.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hili hapa alilosemea la pili kuhusu kuzingatia masuala ya usalama, tumeshaongea kuweza kuweka utaratibu mahsusi ambao utakuwa unadhibiti. Siku ile walikuwa wamesimamisha magari lakini
yule wa bodaboda akaja akapita moja kwa moja kama ambavyo nimesema wamekuwa na utaratibu huo wa kwenda kasi lakini tumeendelea kutoa elimu na tumesema ianzie hata ngazi za familia waweze kutambua kwamba kwenda kasi kwa vyombo hivyo vya moto pamoja na kuwa
na matairi mawili lakini vinasababisha ajali.
MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na mlolongo mrefu wa majibu ya Mheshimiwa Waziri, lakini naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mataifa mbalimbali duniani wanapozikamata meli kama hizi wanazitaifisha kwa ajili ya kujenga uchumi wa ndani ya nchi yao. Ajabu sisi meli ile tumeiacha imezama mahali (bandarini) ambapo hapana upepo, hapana wimbi wala hapana dhoruba yoyote na kupoteza thamani kubwa ya meli ile. Je, Serikali inatamka tamko gani kuhusu suala hili? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa washtakiwa wameingizwa hatiani: Je, utaratibu gani uliotumika kuwaachia huru mpaka muda huu wakawa wako nje? Ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA (K.n.y. WAZIRI WA SHERIA NA KATIBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ametolea mifano au ameelezea uzoefu wa nchi nyingine wanapokamata vyombo vya baharini au meli kama hizi. Kwanza, napenda tu kusema kwamba kwa Tanzania kufanya uamuzi ule waliouchukua imesaidia sana kukemea au ku-deter uvuvi haramu katika bahari zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia matukio ya aina hii kuanzia mwaka 2009 tangu uamuzi huu ulipochukuliwa, kwa kweli hata Wizara ya Uvuvi itakuwa ni shahidi na vyombo vyetu vinavyofanya doria katika bahari zetu, matukio ya aina hii yamepungua sana. Kwa hiyo, kwa kweli na sisi Tanzania kama nchi tumeweka mfano, tumeweka precedent ili nchi nyingine na watu wengine wenye masuala kama haya wasitumie bahari zetu kwa makosa na kuchezea rasilimali zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali la pili la Mheshimiwa Mbunge, kwamba ni utaratibu gani uliotumika katika kuwaachia huru watuhumiwa; kama nilivyoeleza, mwaka 2014 Mkurugenzi wa Mashtaka ali-enter nolle kupitia Kifungu cha 98 ambacho anayo mamlaka kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai na masuala mengine yaliyofuata hapo ilikuwa ni masuala ya diplomasia na waliweza kuachiwa huru.
MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu marefu ya Mheshimiwa Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshiwa Naibu Spika, katika majibu yake Mheshimiwa Waziri amekiri kwamba mashamba haya yamekuwa ya muda mrefu na uzalishaji wake umekuwa mdogo sana. Pia mashamba haya yanatumia hekari nyingi sana, kwa hiyo, yamechukua sehemu kubwa ya ardhi ya Tanzania. Pamoja na kukiri kwamba hakuna uhusiano baina ya Kiwanda ya General Tyre na mashamba haya. Namuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri, je, Serikali iko tayari kuleta matumizi mbadala ya mashamba haya kwa sababu hayalisaidii Taifa?(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Kiwanda cha General Tyre si kiwanda kipya ni kiwanda cha zamani sana na kilikuwa kinazalisha. Hata hivyo, marekebisho yake naambiwa yafanyiwa utafiti, ukiuliza utafiti, ukiuliza utafiti, hakimaliziki kiwanda kufanyiwa utafiti ili kuzalisha. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri haoni kwamba hatujawa tayari kuingia katika Tanzania ya viwanda kwa mwendo huu?(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kuhusu mipira au zao la mpira kuchukua ardhi kubwa na hiyo ardhi kutoweza kutumika kwa tija zaidi, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sasa mashamba ya mpira tuliyonayo hayajachukua ardhi kubwa sana. Tunachofikiria sasa kama Wizara na Serikali ni kujaribu kutafuta ardhi nyingine ili tuongeze uzalishaji wa mpira. Kwa sasa tunafikiri mpira soko lake limeimarika tena hata jirani nchini Kenya kuna soko, lakini vilevile China kuna soko kubwa. Kwa hiyo, sasa tunajaribu kuangalia namna ya kuwekeza tena kwenye mpira ili liwe tena ni zao ambao wakulima wetu wanaweza kunufaika nalo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa sasa hatufikirii ile ardhi iende kwenye matumizi mengine lakini tunachofanya ni kuendelea kuimarisha mashamba yaliyopo lakini vilevile kujaribu kuongeza ardhi nyingine ili kilimo cha mpira kiweze kupanuka. Vilevile kujaribu kuimarisha teknolojia ambayo tunatumia kwa sasa ili iweze kuendana na mahitaji ya sasa ya soko la mpira duniani.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni kuhusiana na General Tyre. Kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, Serikali inaendelea kufanya tathmini kuhusu namna bora ya kurejesha tena Kiwanda cha General Tyre kiingie katika uzalishaji. Kimsingi tulichosema ni kwamba taarifa ya awali inaonyesha kwamba tunahitaji kuboresha teknolojia iliyopo, lakini vilevile mfumo wa uendeshaji uwe ni kwa utaratibu wa kushirikiana na sekta binafsi kwa maana ya PPP ili Serikali iweze kubakia na hisa chache tu na hasa zile zinazolingana na mali au uwekezaji ambao Serikali tayari umeshaufanya, lakini huku Serikali ikijaribu kuvutia wawekezaji ili iendeshwe kwa ubia na sekta binafsi. Kwa hiyo, siyo kwamba Kiwanda cha General Tyre kimetupwa lakini ni kwamba sasa jitihada zinaendelea ili kukifufua ili kiweze kufanya kazi tena.
MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru vyanzo vya maji vinaendelea kuathirika, na kupotea siku hadi siku nchini.
Je, Serikali imeanzisha vitalu vya miti inayotunza maji ili kuipanda na kuitunza kwenye vyanzo vya maji ili vyanzo vyetu vizidi kukua na kutoathirika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na Halmashauri pamoja na taasisi zingine kukosekana kwa wataalam wanaotuelekeza aina ya miti ya kupanda na wapi. Ndiyo tukasema TFS lazima iwepo kila sehemu, kwa sasa hivi huyu wakala wa misitu ndiye anayetoa ushauri wa miti aina gani inafaa kupandwa eneo gani, eneo la vyanzo vya maji linafaa kupandwa miti ya aina gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge huduma hizi zote mtazipata sasa kila Wilaya kwa kila Ofisi ya Wakala ya Misitu ambaye anatoa maelekezo haya.
Lakini Wakala hawa watai-guide vizuri sana halmashauri kuhakikisha kwamba inavipitia vile vyanzo vyote vya maji na kuenda kupanda miti inayofaa katika kulinda vyanzo vya maji.
MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri tuliyoyazoea, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, takriban tangu kuungua kwa kitu hiki ni miaka tisa na kipindi hicho chote askari wanafanya kazi katika mazingira magumu sana kiasi wanahatarisha afya zao. Kwa kuwa Serikali imeshindwa kukamilisha kituo hiki katia muda mwafaka, je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kukifunga kituo hiki mpaka ujenzi wake ukamilike kwa usalama wa skari wetu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imetenga shilingi bilioni 2.2 kwa ajili ya kupunguza madeni ya wakandarasi. Kituo cha Mkokotoni kimetengewa shilingi milioni 200 kwa ajili ya mkandarasi aliyejenga kituo kile, nataka kujua, je, mkandarasi huyo ameshalipwa pesa zake? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi hatuna mpango wa kukifunga hiki kituo kwa sababu mipangilio ya kukiendeleza, kukikamilisha iko mbioni na ndiyo maana naomba nichukue fursa hii kumjulisha Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari tumeshafanya uhakiki na kuwasilisha Hazina ili mkandarasi aweze kulipwa na ujenzi uweze kukamilika. Kitakapo kamilika kituo hiki kitatumika. (Makofi)