Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Jaffar Sanya Jussa (2 total)

MHE. USSI SALUM PONDEZA (K.n.y. MHE. JAFFAR SANYA JUSSA) aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itavipatia Vituo vya Polisi vya Paje na Jambiani samani za ofisi pamoja na magari kwa ajili ya patrol?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jaffar Jussa, Mbunge wa Paje, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuna uhaba wa magari pamoja na samani katika Vituo vya Polisi vya Paje na Jambiani, kama ilivyo kwenye maeneo mengine hapa nchini. Kwa sasa Vituo vya Polisi cha Paje na Jambiani vinapata huduma za doria kutoka kwa OCD wa Makunduchi, hali inayosababisha kuwa na changamoto katika utekelezaji wa majukumu ya kiusalama.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Polisi lipo katika mchakato wa kupokea magari mapya yaliyonunuliwa na Serikali ambayo yatagawawiwa kwa kuzingatia kiwango cha uhalifu, idadi ya watu na ukubwa wa eneo katika kamandi husika. Aidha, Jeshi la Polisi litaendelea kutumia bajeti inayotengwa kutimiza azma ya Serikali ya kuhakikisha kuwa linakuwa na vitendea kazi vya kutosha, ikiwa ni pamoja na magari na samani katika vituo vya Polisi kote nchini.
MHE. JAFAR SANYA JUSSA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itavipatia Vituo vya Polisi vya Paje na Jambiani samani za Ofisi pamoja na magari kwa ajili ya doria?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, sasa naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jaffar Sanya Jussa, Mbunge wa Paje, kutoka Mkoa wa Kusini Unguja, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua changamoto ya ukosefu wa samani katika Vituo mbalimbali vya Polisi nchini, ikiwa ni pamoja na Vituo vya Paje na Jambiani kutoka Mkoa wa Kusini Unguja na hii ni kutokana na ufinyu wa bajeti. Aidha, Serikali imekuwa ikishirikiana na wadau werevu wa ulinzi na usalama ili kuhakikisha Vituo vya Polisi vinapata samani za kisasa ili kuongeza ufanisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kituo cha Paje wadau werevu wamechangia meza sita, viti kumi na nne na makabati manne. Pia katika Kituo cha Jambiani Mkoa wa Kusini Unguja wamechangia meza tatu, viti sita na mabenchi mawili na wameahidi kuchangia ama kuendelea kufanya hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali inatambua pia umuhimu wa vyombo vya usafiri katika kutekeleza majukumu ya Jeshi la Polisi. Jeshi la Polisi linatarajia kupata magari kwa ajili ya kutendea kazi na pindi yatakapofika yatatengwa kwenye maeneo yenye uhitaji wa magari na Vituo vya Paje na Jambiani vitazingatiwa zaidi. Nashukuru.