Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Margaret Simwanza Sitta (5 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili nichangie katika hoja iliyoko mezani. Pia namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai. Nawashukuru wapiga kura wa Urambo ambao wameniwezesha kuwa hapa na nawahakikishia sitawaangusha.
Vile vile nachukua nafasi hii kuishukuru familia yangu inayoongozwa na Mheshimiwa Mzee Sitta, kwa kuniwezesha kufanya kazi ninayoifanya sasa hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu muda ni mfupi na mengi ninayo ya kuongea, pengine naweza kushindwa kumalizia; kwanza kabisa, naomba nianze na kutoa maombi na shukurani. Kwanza shukurani kwa Mheshimiwa Dkt. Magufuli, amefanya kazi kubwa sana kuteua Baraza zuri, linafanya kazi sana. Nawapongeza Waheshimiwa Mawaziri wote na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa ambayo mmeonesha tayari kwamba mnaiweza. Hongereni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye maombi kwanza halafu ndiyo nieleze ninayoyataka. Mimi najikita katika zao la tumbaku tu, sina jambo lingine. Ndugu zangu, kwa Mkoa wa Tabora tumbaku ndiyo maisha, tumbaku ndio siasa. Kama sitataja tumbaku, sitawatendea haki wanyonge; wakulima walioko Urambo na Mkoa mzima wa Tabora. Mheshimiwa Waziri Mwigulu Nchemba, nakuheshimu sana na najua unaiweza hiyo kazi, ombi langu kwako, huu ni wakati muafaka ambapo masoko ya tumbaku huanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kawaida huwa masoko ya tumbaku yanaanza mwezi wa Nne. Nakuomba Mheshimiwa Waziri, katika kipindi hiki cha Bunge ukipata mwanya, uje Tabora ukutane na wakulima wa Urambo, Sikonge, Uyui, Nzega na Ulyankulu, ukutane na wakulima wote, uongee nao ujionee mwenyewe mateso wanayoyapata. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, asilimia 60 ya tumbaku inatoka Mkoa wa Tabora na kwa msingi huo, ni vizuri Mheshimiwa Waziri ukafika Tabora kwanza ukutane na wakulima wenyewe watakutafutia uwakilishi wao; pili, ukutane na Vyama vya Msingi; na tatu, utakutana na wanunuzi wenyewe. Uwasikie kila watu na vilio vyao ambavyo vinasababisha hali ya mkulima isipande hata siku moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hatuna haja ya kumbembeleza mkulima alime, yeye mwenyewe anahitaji fedha; ukimwezesha masoko ukamwezesha na pembejeo, inatosha, huna haja ya kumbembeleza. Wewe mwezeshe tu, kwa sababu masoko ndiyo kishawishi kikubwa cha mtu alime. Halafu pili, pembejeo zinazofika kwa wakati na bei nafuu. Kwa hiyo, naishauri Serikali yetu kwa kupitia Wizara ya Kilimo ishughulikie masoko kwanza, ndiyo kilio kikubwa cha walima tumbaku. Hilo ombi la kwanza, ufike wewe mwenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitashukuru pia Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa heshima kabisa, nakuomba kama ulivyokwenda Mtwara na Lindi ukaona korosho, tunakuomba na wewe Mheshimiwa Waziri Mkuu, uje Tabora uone makato wanayokatwa wakulima. Naamini kabisa, yako mengine utatoka umeagiza huko huko yapunguzwe ili kumpunguzia mkulima makato ambayo yanamfanya aendelee kuwa maskini, katika pembejeo na pia katika bei ya tumbaku yenyewe. Karibuni sana na nitashukuru Mheshimiwa Waziri atakapokuwa ana-wind up atueleze anakuja lini, angalau akituambia yuko tayari na sisi tujiandae kumpokea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, namwomba Waziri katika ku-wind up, hebu atusaidie, mpaka sasa hivi, Serikali imejitahidi imetafuta wanunuzi kutoka Japan na kadhalika. Bado hawatoshi. Tuna wanunuzi wakubwa watatu kule wamejikita, wamekuwa kitu kimoja. Wewe uliona biashara gani ambayo haina ushindani? Wote wanatoka na lugha moja; si hasara tu kwa mkulima hiyo? Wameshaelewana! (Makofi)
Mheshimiwa Waziri, utakapokuwa una-wind up tunaomba utueleze, mpaka sasa hivi Serikali imefikia hatua gani ya kutafuta wanunuzi wengine wa tumbaku ili zao liwe na ushindani na mkulima naye apate anachostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu ambalo naomba ujibu wakati unapo-wind up, ni jinsi gani ambavyo Serikali inalifikiria suala la kuwa na Kiwanda cha Tumbaku Tabora? Mkoa wa Tabora unaotoa asilimia 60 ya tumbaku, halafu cha ajabu, inabebwa na magari yanaharibu barabara yanapeleka Morogoro. Sisi tunataka kiwanda kijengwe pale pale. Siyo hivyo tu, ubaya wake ni kwamba, wanunuzi wajanja sana, wanaipima tumbaku ikiwa Urambo au Tabora kwa ujumla; ikifika Morogoro wanapima tena. Kwa hiyo, ile bei anayopewa mkulima ni ile ambayo wamepima Morogoro. Ni haki hii? Gari ikiharibika njiani, ikikaa wiki nzima! Kwa hiyo, Serikali inasemaje kuhusu kujenga Kiwanda cha Tumbaku Mkoa wa Tabora? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia cha ajabu jamani ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, mliona zao gani lina grade 72? Tumbaku eti ina grade 72! Miaka ya nyuma ilikuwa grade saba; sasa hivi wamenyumbuisha mpaka zimekuwa sasa eti grade 72. Wewe uliona wapi? Shina la tumbaku ni majani 12 mpaka 16; eti majani 12 - 16 yana grade 72, si uonevu tu huo! Kwa hiyo, Mheshimiwa utuambie mtapunguzaje grade za tumbaku utakapokuwa una-wind up. Huu ni uonevu wa hali ya juu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia hivi sasa ninavyoongea, Urambo na naamini Wabunge wenzangu, kwenu masoko ya tumbaku hayajaanza. Kwa kawaida Masoko ya tumbaku yanaanza mwezi wa Nne na kuitendea haki mara nyingi, iishe mwezi wa Nane na ikizidi kabisa mwezi wa Tisa mwisho. Mwaka 2015 wameendelea mpaka mwezi wa Kumi na Moja. Unajua tatizo lake ni nini? Inavyozidi kukawia na thamani inazidi kushuka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nashangaa! Naomba Mheshimiwa Waziri utakapokuwa una-wind up utuambie, kwa nini bodi mpaka sasa hivi hawajaenda kuhimiza uanzaji wa masoko ya tumbaku na kwamba mtaiwezeshaje Bodi ya Tumbaku ili ifanye kazi kikamilifu ili kweli masoko ya tumbaku yaanze kwa wakati na yaende kwa haraka? Sasa hivi masoko ya tumbaku yanaweza kufanyika hata mara moja tu kwa mwezi, ambapo miaka ambayo ilikuwa inafanya vizuri, ilikuwa na masoko hata mara tatu au mara nne kwa mwezi, jambo ambalo lilikuwa linawasaidia sana wakulima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hayo ndiyo ambayo naomba mtakapokuwa mna-wind up mtuelezee mikakati yenu kama Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nadhani nimezungumzia kuhusu makato mbalimbali ambayo mtatueleza kwamba makato haya, mtayapunguza kwa kiasi gani. Nilikuwa naangalia makato ya mkulima, jamani ndugu zangu, kama kuna mtu anayeyonywa hapa duniani, ni mkulima wa tumbaku. Eti kuna Kodi ya Kupakua, Kodi ya Usafirishaji, Kodi ya Damage, yaani kuharibika; eti Kodi ya Insurance! Ninyi mliona wapi mkulima na mambo ya insurance. Halafu sasa akishauza, anakatwa; Halmashauri inachukua, Union inachukua, Vyama vya Msingi vinachukua; yeye mkulima abaki na nini? Kwa hiyo, nafikiria haya ndiyo makato ambayo tunategemea mtatusaidia kuona ni jinsi gani ambavyo mnayapunguza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu zangu kama nilivyosema, tukija kwa upande wa kilimo cha tumbaku, nimeomba kwamba wakati wa ku-wind up Mheshimiwa Waziri azungumzie jinsi gani atakavyoiwezesha Bodi ya Tumbaku.
Bodi ya Tumbaku ndugu zangu ndiyo ambayo inaajiri classifiers, wale wanaopanga madaraja (grade) za tumbaku. Sasa utakuja kukuta kwamba wengi wamestaafu, Serikali haijaajiri mpaka sasa hivi. Kwa Wilaya zetu za Mkoa wa Tabora, Wilaya moja haipaswi kuwa na chini ya classifiers watano. Eti sasa hivi katika Wilaya zetu zote zilizoko Mkoa wa Tabora, zile zinazolima tumbaku wako classifiers watatu. Mmoja aende Kaliua, mwingine aende Ulyankulu na mwingine Sikonge. Wataweza wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, unakuta classifier mmoja anapanga mabelo 1,500 kwa siku, saa 3.00 mpaka saa 11.00, si wizi tu huo! Yeye ana akili gani ya kupanga belo 1,500 kwa siku? Kwa hiyo, badala yake bei wanabambikiziwa tu. Halafu walivyofanya ni kwamba, mpaka uipate hiyo hela; tumbaku inatakiwa kama ikiwa nzuri ilipwe Dola tatu angalau kwa kilo, lakini walivyozipanga sasa.
MHE. MARGARET S. SITTA: Sijui hiyo kengele ndiyo ya kwanza au ya mwisho!
NAIBU SPIKA: Ya mwisho Mheshimiwa!
MHE. MARGARET S. SITTA: Ooh! karibuni sana Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, mjionee wenyewe tunavyonyanyaswa huko.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampa hongera sana kwa kazi nzuri Mheshimiwa Waziri na Wizara kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, asilimia 60 ya tumbaku Tanzania inalimwa Urambo Mkoa wa Tabora. Je, Serikali hii haioni kuna umuhimu wa kiwanda cha Tumbaku? Kwa sasa tumbaku inasafirishwa kwa magari kwenda Morogoro jambo ambalo limepunguza kiwango au daraja la tumbaku, wakati huo huo barabara zinaharibika. Aidha, kuwakosesha ajira vijana wa Urambo na Tabora kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haoini umuhimu wa kuokoa matunda ya Tanzania kwa kushawishi wawekezaji?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru kwa kunipa dakika tano niseme niliyokuwa nimepanga kusema. La kwanza, namuunga mkono Mwalimu Bilago kwamba hili suala la watoto wa kike wanaopata mimba wanaachwa bila kushughulikiwa amelichokoza leo kwa Waziri anayehusika na usawa wa jinsia, namwomba na nawaomba Waheshimiwa Wabunge tulirudishe wakati Wizara ya Elimu itakapokuja kuleta bajeti yake hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nawaunga mkono Waheshimiwa Wabunge wote waliosema kwamba vifaa vinavyowasaidia akina mama na wasichana kujihifadhi vipunguziwe kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwa upande wa Urambo. Kama walivyosema vifo vya akinamama tunaweza kuvipunguza pale ambapo tu kutakuwa na mkakati maalum, nami naamini Waheshimiwa Mawaziri waliochaguliwa wana uwezo, mwakani watakuja na mikakati mizuri zaidi, hongereni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue mfano kwa upande wa watumishi, tazama Urambo ilivyo, tuna zahanati 20, ni zahanati tano tu ambazo zina Matabibu. Sasa unategemea nini anapopelekwa mwanamke mwenye mimba ambaye ameshindwa kujifungua kwenye zahanati 15 ambazo hazina Matabibu? Pia kama walivyosema wenzangu, kuna mradi wa ADB, umetuacha sisi Urambo na Zahanati ya Wilaya; nusu imejengwa, pia theatre kwenye upande wa Kituo cha Afya, Usoke imeachwa nusu kwa upande wa Usoke na Isongwa; kliniki zilizokuwa zinajengwa, zimeachwa nusu halafu Serikali inatuambia sisi wenyewe tumalize, haiwezekani! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sisi wote Wabunge ambao tumeguswa na huu mradi wa ADB tufanye mpango wa kuona Serikali itajibu nini kuhusu kutuachia jukumu la kumaliza majengo ambayo yapo nusu. Pia chukua kwa mfano, wenzangu wamezungumzia juu ya OC zilivyopunguzwa, mwaka 2015 Urambo ilipewa shilingi milioni 185, mwaka huu imepewa OC milioni 60. Jamani itafanya kitu gani? Kulisha wagonjwa na kila kitu! Kwa hiyo, tunaiomba Serikali iangalie jinsi ambavyo inakata mambo mengine ambayo yataathiri sana afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia On call Allowance kwa mfano Urambo tangu Januari mpaka leo hawajapata On call Allowance, mnategemea wafanyakazi watafanya kazi kwa moyo kweli! Kwa hiyo, tunaomba On call Allowance zipelekwe ili wenzetu waweze kufanya kazi kwa moyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wafanyakazi wapya wanaopelekwa kwenye wilaya hizi hawapelekewi fedha za kujikimu kabla hawajafika. Kwa hiyo, hilo nalo tunaomba litendeke. Pia Wilaya ya Urambo haina gari la chanjo. Tunaomba gari la chanjo, Mheshimiwa Waziri atakapojibu atuambie lini angalau watu wa Urambo tutapata gari la chanjo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naunga mkono wenzangu waliosema mfumo wa watumishi katika Wizara ya Afya uangaliwe upya. Kwa mfano, sisi tumepata kibali cha kuajiri, lakini tuliomba kibali wakasema mtaajiri, lakini eti tunaambiwa tusubiri mpaka Wizara itangaze. Itatangaza lini? Tunaomba Serikali ituambie ni lini Serikali itatangaza ajira? Kwa sababu kama nilivyowaambia ni kwamba, tuna Matabibu watano tu katika zahanati 20, lakini wametuacha tusubiri mpaka Wizara itakapotangaza. Kwa hiyo, naunga mkono wenzangu waliosema kwamba mfumo wa kuhudumia watumishi ndani ya Wizara au Sekta hii ya Afya uangaliwe upya, inawezekana pengine tukahitaji mfumo mzima ubadilishwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu sasa kutokana na maingiliano ya majukumu inakuwa ni vigumu sana kuajiri kwa wakati, mambo ambayo yangeweza kufanyika ndani ya TAMISEMI, unaambiwa yasubiri huko juu. Kwa hiyo, nami naunga mkono kwamba mfumo mzima uangaliwe wa jinsi ya kuhudumia watumishi ndani ya Halmashauri zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naangalia hivi vifo vya akinamama, ndugu zangu, ni vita! Kila siku wanawake 42 wanakufa! Kungekuwa labda na uwezekano wa hawa akinamama 42 kila siku wakazikwa pamoja, nadhani lingekuwa shamba la ajabu kabisa kwa sababu kama kila siku ni 42 kwa mwezi ni elfu moja mia tano na ngapi huko! Kwa hiyo, ingekuwa hata pengine tunakwenda kuzuru sisi, kuwasalimu wenzetu ambao wamefariki wakifanya wajibu wao waliopewa na Mwenyezi Mungu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri wa Afya aje na mkakati mzuri zaidiā€¦
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie hotuba ya Bajeti iliyotolewa na Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naipongeza Serikali yote kwa jinsi ambavyo imeleta mpango na bajeti ya kuthubutu, tusiogope kuthubutu, changamoto zitakazojitokeza huko mbele ya safari tutazitatua, lakini naipongeza sana Serikali pamoja na Waziri kwa uwasilisho mzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naishukuru sana Serikali kwa kuamua kujenga reli kwa standard gauge, kwetu sisi tunaotoka Tabora, Kigoma na Mwanza ni ukombozi mkubwa. Natunaomba mpango uanze mara moja mwaka huu wa fedha ili tusaidie kupunguza bei kutokana na usafiri wa reli utakaopunguza bei ya bidhaa zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napongeza Serikali kwa kuja na mpango wa maji, ombi langu mimi ni kwamba ili akina mama watokane na ubebaji wa maji kwenye vichwa, badala ya shilingi 50 kama walivyopendekeza Kamati ya Bajeti tuongeze zifike shilingi 100 ili akina mama vijijini wapate maji wajikomboe na wafanye kazi zingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika mimi ningeanza na upandewa mtu ni afya. Bila afya hakuna chochote kinachowezekana. Ningejikita zaidi kwa upande wa mama na mtoto. Ndugu zangu tuwapongeze wakinamama na nafasi ingeniruhusu ningewaomba akina mama na akina baba wote tusimame tuwape heshima akina mama wanaofariki kwa njia ya uzazi, wanafanya kazi kubwa na wanafariki katika kutimiza wajibu wao.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona zimetengwa asilimia tisa ya bajeti nzima kwa ajili ya afya. Naiomba Serikali ifikishe asilimia 15 kama walivyokubaliana katika Azimio la Abuja. Lakini pia mimi ningependa katika kujumuisha tupate majibu mpango wa MMAM uliishia wapi? Kwa sababu mpango wa MMAM ulikuwa na lengo la kuongeza zahanati ili wakinamama wafike haraka kwenye zahanati ili wasipoteze maisha yao. Tunataka tathmini ya mpango wa MMAM. Zahanati nyingi hazijajengwa, lakini pia zina upungufu mkubwa wa watumishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwapeni mfano wa Urambo tuna zahanati 20 ni zahanati tano tu zenye Maafisa Tatibu. Ni haki mama mjamzito mwenye complication kweli akapewe prescription ya dawa na muuguzi?
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Serikali katika mwaka huu wa fedha iangalie; na ndiyo maana nasema iongezewe bajeti ili kuwe na wafanyakazi wengi wa kutosha wa hospitali na zahanati. Urambo ina uhaba wa wafanyakazi 150, na nimeshatoa mfano kwamba zahanati tano tu ndizo zina Maafisa Tabibu ambao siyo haki hata kidogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kulikuwa na mradi huu wa ADB. Mimi naiomba Serikali iangalie jinsi gani ya kukamilisha zile theaters zilizokuwepo, najua hii bajeti katikati huko italeta tu mabadiliko ya kuomba nyongeza ya fedha, kwa sababu Serikali hii inathubutu. Tuna theater Urambo na sisi tulikuwa tunafikiri kwamba njia mojawapo ya kupunguza vifo vya kina mama na watoto ni kuwa na theater katika vituo vya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini cha ajabu ni kwamba Urambo nzima yenye kata 18 tuna kituo cha afya kimoja tu halafu hakina theater ni haki hii? Halafu theater iliyokuwa inajengwa imeishia kwenye linter kwa mpango wa ADB.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Urambo jamani tunahudumia mpaka Uvinza na ile miji ya karibu ya Mkoa wa Kigoma kutokana na umbali, lakini cha ajabu theater iliyokuwa inajengwa Urambo imeishia kwenye linter. Ndugu zangu nipeni pole mimi Mbunge wa huko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kwa kuthamini afya ya mama na mtoto mpango wa ADB ulikuwa unajenga clinic ya mama na mtoto, jamani imeachwa imechimbwa msingi mpaka leo. Lakini pia kulikuwa na kliniki ya mama na mtoto katika sehemu ya Isongwa imeachwa katika hatua ya msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, na ninasikitika, nina barua hapa kutoka Wizarani inayotutaka sisi wenyewe tumalize, Halmashauri inaweza kupata shilingi milioni 500 za kumaliza theatres? Na hayo ni majengo tu hayahusiani na vifaa. Nina barua hapa ya kusikitisha sana ya kutuambia sisi kama Halmashauri tumalize miradi ya ADB, kwa nini walileta mradi ya ADB kama walikuwa wanajua sisi tuna uwezo? Mimi ningeomba suala hili la theatres zilizoachwa bila kumalizwa zote pamoja na majengo ya kliniki yamaliziwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia sisi Kanda ya Magharibi hatuna Hospitali ya Rufaa, je, Serikali inafikiriaje kuhusu Kanda ya Magharibi nayo kupata Hospitali ya Rufaa?
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye kilimo. Mimi naipongeza hii Serikali kwa kushughulikia sana suala la viwanda ili kuinua hali ya wananchi. Tunaomba badala ya tumbaku kutoka Tabora kupelekwa Morogoro tuwe na kiwanda, na sisi tuna hitaji viwanda kwa sababu vitatupa pia ajira kwa watu wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye ukurasa wa 45 nimesoma, Serikali imeandika hapa kwamba inafahamu vizuri sana changamoto za wakulima. Nimeona hapa nikafarijika nikasema ahaa kumbe Serikali inajua. Ukurasa wa 35 inasema kwamba hata hivyo bado sekta hii ya kilimo inakabiliwa na changamoto kadhaa zikiwemo za kodi na tozo za mazao zisizo na tija. Tumbaku ina kodi zaidi ya 12, halafu wanasema tena uhaba wa pembejeo ambazo pia zina kodi nyingi, vifaa duni, masoko na uhaba wa Maafisa Ugani, kumbe Serikali inajua? Je, Serikali inachukua hatua gani katika kutimiza haya kutatua changamoto hizo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la zao la tumbaku, tumbaku ni jani, mwezi wa pili tu jani linaiva, jani likishaiva masoko yanatakiwa yaanze mara moja mwezi wa tatu, lakini utaona cha ajabu masoko yanasuasua hadi leo hii. Bodi ya Tumbaku haina fedha nimeongea nao hawana fedha, wakulima watafanyaje?
Mheshimiwa Naibu Spika, tumbaku ndugu zangu inavyokaa inapoteza ubora na inapoteza uzito. Inapofika Morogoro imepoteza uzito, je, ni haki hii?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nawashukuru, Naibu Waziri wa Kilimo amesema na mimi naomba nirudie sijui kama itakuwa ni vibaya, kwamba anakuja Tabora, pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu waone shida zinazowakabili wakulima wa tumbaku waongee nao, vyama vya msingi vinakufa watafanyaje? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, makato kwenye pembejeo ni mengi, makato kwenye zao lenyewe mengi, kuna uhaba wa wanunuzi. Naomba mtuambie; kwa kuwa mnatambua; kwenye ukurasa wa 35; Serikali inachukua hatua gani ya kupata masoko zaidi ili kuwe na ushindani wa masoko? Haya makampuni matatu hayatoshi, yana ukiritimba, tunataka masoko mengine kutoka nje, nchi za Japan pamoja na China, Serikali inasema nini kuhusu hili?
Lakini pia wenzetu, kwa mfano wa Uganda wajanja wale wame-market kahawa yao wameiuza ndiyo maana unaona watu wa Kagera wanapeleka kahawa kuuzia Uganda. Kwa nini na sisi tusishirikishe Wizara ya Mambo ya Nje ili tumbaku yetu iuzwe? Kwa sababu ladha na harufu iliyo kwenye tumbaku tunayolima sisi watu wa Tabora ndiyo inayofunika duniani kote waulizeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa nini na sisi tusiitangaze kwa kutumia pia Wizara ya Mambo ya Nje, Mabalozi, nchi majirani ili tumbaku yetu na sisi ivutie tupate wanunuzi wengi zaidi. Mimi ninachoshukuru ni kwamba Mheshimiwa atakuja ajionee mwenyewe. Lakini naomba sana Bodi ya Tumbaku iwezeshwe ili iweze kufanya kazi, na pia nimesema kiwanda cha tumbaku kijengwe Mjini Tabora.
Mheshimiwa Naibu Spika, itakuwa kwa kweli siyo haki kama nikimaliza bila kusemea mtoto wa kike. Nimeona mipango mingi ya Wizara ya Elimu, mimi naomba kujua elimu bure inayotolewa itamsaidiaje mtoto wa kike hapa katikati pasiwe na tatizo lolote la kumfanya atoke nje ya darasa ili amalize kuanzia kidato cha kwanza hadi mwisho? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba Wizara itakapokuja kumalizia ituambie kutokana na wingi wa taasisi za elimu zilizo nchini ni lini Mamlaka ya Ukaguzi itaundwa ili ukaguzi kweli ufanyike kikamilifu?
Mheshimiwa Naibu Spika, ni mengi ambayo ningeongea lakini bado nawakumbuka walimu wangu, tunaomba chombo kile kinachoundwa kwa ajili ya walimu kifanye kazi ipasavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hiyo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika,
nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. La kwanza kabisa,
kwa niaba ya familia yetu ya marehemu mzee Sitta,
nachukua nafasi hii kuishukuru Serikali inayoongozwa na
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Serikali nzima,
uongozi wa Bunge unaoongozwa na Mheshimiwa Spika,
Waheshimiwa Wabunge, viongozi wa vyama kisiasa,
viongozi wa dini, wananchi wote Tanzania kwa jinsi ambavyo
walitufariji sana sisi familia ya marehemu Mzee Samuel Sitta;
tunawashukuru sana, tunaomba ushirikiano mliotupa sisi
uendelee. (Makofi)
Mungu ibariki Tanzania, lakini pia tunamwomba
Mungu aiweke roho ya marehemu Samuel Sitta mahali pema
peponi, Amina.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nichukue nafasi hii
kumpa pole Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge
kwa kifo cha mwenzetu, Mheshimiwa Dkt. Macha,
tumwombe Mwenyezi Mungu aiweke roho ya marehemu Dkt.
Elly Macha mahali pema peponi, Amina.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitazungumzia katika sekta
tatu. Kwanza kabisa naomba nianze na Sekta ya Kilimo. Kwa
niaba ya wananchi wa Jimbo la Urambo, nasema wazi
kwamba huwezi kuzungumzia hali ya kiuchumi na maendeleo
ya kiuchumi ya wananchi wa Urambo bila kuzungumzia suala
la tumbaku. Nawapongeza Waheshimiwa Wabunge wote
mnapoongea mkizungumzia suala hili kwa sababu ni muhimu
sana katika maendeleo ya wananchi wa Urambo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa
Waziri Mkuu kwa niaba ya wananchi wa Urambo kwa jinsi
alivyochukua hatua mbalimbali katika kunusuru zao la
tumbaku, nakushukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Pamoja na hatua mbalimbali ambazo Mheshimiwa Waziri
Mkuu amezichukua bado kuna maswali ambayo ningeiomba
Serikali ichukue hatua za haraka kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, kwa kuwa Bodi
ya Tumbaku imevunjwa, je ni lini Serikali itaunda bodi mpya
kwa sababu sasa hivi mwezi wa Nne ndiyo masoko ya
tumbaku yanatakiwa yaanze? Pia, pamoja na kuunda bodi
mpya, Serikali imejipanga vipi kuiimarisha Bodi mpya ya
Tumbaku ili iweze kufanya kazi zake kwa ufanisi zaidi hususan
upatikanaji wa classifiers, wale ambao wanapanga tumbaku
katika grades zinazotakiwa wakati wa kuuza tumbaku na
msimu ndiyo huu mwezi wa Nne?
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile ningependa Serikali
itueleze, wakulima wana tozo nyingi, sasa hizi tozo Serikali
imejipangaje kuziondoa ili mkulima naye anufaike na zao
lake analolihangaikia mwaka mzima?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini wakati huo huo amri
ilitolewa na Serikali ya kuvunja uongozi wa AMCOS mbili za
Utenge na Nsenda, lakini msimu wa tumbaku umefika, lini
Serikali itaondoa amri hiyo ili kuwe na uongozi katika AMCOS
hizo waweze kushughulikia uuzaji wa tumbaku haraka
iwezekanavyo kwa sababu kama nilivyosema mwezi wa Nne
ndiyo wanaanza?
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la tumbaku,
tunaiomba sana Serikali itilie mkazo hasa upatikanaji wa
mbolea. Tunapoanza na mbolea kuchelewa kutakuwa na
matatizo makubwa. Je, wakati huu ambapo Bodi ya
Tumbaku imevunjwa nani atakayeshughulikia suala la
upatikanaji wa mbolea haraka iwezekanavyo?
Mheshimiwa Naibu Spika, nirudi kwenye upande wa
changamoto nyingine tuliyonayo, upande wa suala la maji.
Sasa hivi sisi Urambo hatuna maji na kuna mpango ambao
Serikali imeuandaa wa kupata maji kutoka Malagarasi, lakini
utachukua muda mrefu, je, Serikali imejipangaje kipindi hiki
ambacho mradi wa Malagarasi unaendelea, hawawezi
kutuchimbia visima, hawawezi kutuchimbia mabwawa ili
tutumie wakati tukisubiri mradi huu wa maji wa muda mrefu
kutoka Mto Malagarasi? Kwa hiyo, tunaiomba Serikali ifanye
hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu ni suala la afya.
Ningeiomba Wizara ya Afya kwanza kwa kuanzia hebu ibane
halmashauri kwa kushirikiana na viongozi wa halmashauri
(TAMISEMI); kwamba ni jinsi gani halmashauri zimepanga
fedha hususan kwa ajili ya kuokoa maisha ya mama na
mtoto? Kila siku wakati wa kujifungua hapa Tanzania
tunapoteza akinamama 30. Je, Serikali kwa kupitia Wizara
ya Afya imejipangaje ili kuhakikisha kwamba fedha mahususi
zinapangwa kwa ajili ya kuokoa vifo vya akinamama na
watoto?
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati huohuo nichukue
nafasi hii kuishukuru sana Serikali kwa kuchagua Jimbo la
Urambo au Wilaya ya Urambo kuwa miongoni mwa wilaya
ambazo zitapata fedha moja kwa moja kupelekwa kwenye
vituo vya afya, zahanati na hospitali.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, nauliza moja
tu; je, Serikali imejipangaje kuhakikisha kwamba zahanati
zetu zinakuwa na watumishi waliotosha? Kwa mfano, sisi tuna
zahanati 21, hamuwezi kuamini katika zahanati 21, 15 hazina
maafisa tabibu, sasa wagonjwa wanaandikiwa matibabu
na nani? Wakati huo huo upungufu ni asilimia 77, yaani ufanisi
wa utumishi ni aslimia 33 tu. Sasa fedha zikipelekwa moja
kwa moja kwenye zahanati na vituo vya afya nani
anashughulikia fedha hizi?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, natoa ushauri
kwamba haraka iwezekanavyo tusaidiwe sisi wa Jimbo la
Urambo kupewa wafanyakazi wa kutosha haraka sana ili
waweze kutekeleza hili zoezi la kupeleka fedha moja kwa
moja kwenye zahanati. Wewe fikiria mahali ambapo kuna
watumishi wawili nani anamwangalia mwenzake? Nani
anatimiza wajibu wa kuhudumia wagonjwa? Nani anatunza
fedha? Kwa hiyo la kwanza ni upatikanaji wa watumishi
haraka iwezekanavyo lakini pili, tunaiomba Serikali iajiri
wahasibu ili hizi fedha zitakazokuwa zinapelekwa kwenye
zahanati ziweze kutunzwa kadri iwezekanavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema,
kutokana na uhaba mkubwa watumishi kwa asilimia 77
katika Jimbo langu, naamini na wenzangu wako kwenye
matatizo ya hivyo hivyo. Mimi kama Mbunge wa Jimbo la
Urambo naomba Wizara husika ituanzishie Chuo pale pale
kama ilivyo Nzega na kadhalika ambacho kitafundisha
Watumishi wa kada ya kati ili na sisi tupate watumishi haraka
iwezekanavyo kutokana na uhaba tuliokuwa nao.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Kanda ya Magharibi,
ukichulia hasa Mkoa wa Kigoma na Tabora, hatuna Hospitali
ya Kanda. Tunachukua nafasi hii kuiomba Serikali na sisi Mkoa
wa Kigoma na Tabora tujengewe Hospitali ya Kanda kwa
sababu inatubidi kuja Dar es Salaam au kwenda Mwanza
wakati wenzetu wanazo karibu kadri iwezekanavyo. Kwa
hiyo, tunaomba Serikali ifanye hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nilikuwa nafikiria
kwamba hili suala la upatikanaji wa Watumishi wa Afya,
Serikali ilitilie maanani ndugu zangu. Kwa hali ilivyo, kama
Serikali haitachukua mkakati maalum, tutapata shida sana
kuhusu watumishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri suala la upungufu
wa Watumishi wa Afya liangaliwe ipasavyo na nitashukuru
sana. Kama viongozi wetu, Mawaziri mtakuja kwetu kule
kama alivyofanya Mheshimiwa Waziri Mkuu kuja Tabora
kuangalia suala la Tumbaku na Mawaziri husika naomba mje
mwangalie uhaba wa watumishi tulionao kwenye Mkoa wetu
wa Tabora kwa ujumla lakini pia Wizara Afya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nashukuru kwa
kupata nafasi, lakini naomba sana, katika kujumuisha hapa,
tupate majibu, lini tumbaku itapata uongozi wa haraka
iwezekanavyo? Ile Bodi ya Tumbaku ipate uwezo wa kuajiri
wafanyakazi wa kutosha ili masoko sasa yanayoanza mwezi
huu yaende kama yalivyopangwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa
kunipa nafasi.