Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. January Yusuf Makamba (16 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa fursa hii. Naanza moja kwa moja kwa kutoa pongezi kwa hotuba nzuri aliyoitoa Rais wetu mpendwa, hotuba ambayo imetoa dira na mwelekeo wa Tanzania mpya. Kwa kauli ya hotuba ile na vitendo vilivyofuatia baada yake, tunaanza kuiona kabisa safari ya kupata Taifa jipya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, safari hii haitakuwa nyepesi, itakuwa ngumu, tutajaribiwa njiani, tutakejeliwa, tutakebehiwa, tutatiwa mashaka kuhusu mwenendo wetu, kuhusu mwelekeo wetu, lakini napenda kuwasihi Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote kwamba tumuunge mkono Mheshimiwa Rais. Unapotaka kutengeneza keki ya mayai au chapati za mayai ni lazima upasue mayai. (Makofi)
Mheshimwa Naibu Spika, zamani kulikuwa na dawa zimeandikwa shake well before use, lazima utikise ndipo unywe dawa, ndipo ifanye kazi. Kwa hiyo, mitikisiko hii inayotokea ni sehemu ya kujenga Taifa jipya na wala watu wasipate mashaka wala wasiwasi kwamba nchi yetu inaelekea katika mwelekeo ambao sio wenyewe. Tulifika mahali tulihitaji Rais wa aina hii na tumempata na tumuunge mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nizungumze kuhusu Zanzibar. Uchaguzi ni mchakato wa kikatiba na ni mchakato wa kisheria. Wakati tulipoamua kuingia kwenye Mfumo wa Vyama Vingi, tulibadilisha Katiba yetu, tukatengeneza taasisi zitakazotusaidia kuendesha uchaguzi wa ushindani na sheria ambazo zitatusaidia kuendesha siasa ya ushindani.
Kwa upande wa Zanzibar, Katiba ya Zanzibar Ibara ya 119 iliweka Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ambayo ilipewa majukumu na mamlaka ya namna ya kufanya na ikapewa uhuru mkubwa. Vilevile ikatungwa Sheria Na. 11 ya mwaka 1984 na ikabadilishwa mara kadhaa ili kukidhi mahitaji ya siasa ya ushindani.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar Kifungu cha 5(a) kinasema kwamba; “Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ina jukumu la usimamizi wa jumla wa mwenendo wa uchaguzi.” Maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba Tume imepewa nguvu na Mamlaka ya Kikatiba na Kisheria kufuta matokeo ya uchaguzi pale inapojiridhisha kwamba sababu na kasoro zilizojitokeza kwenye uchaguzi haziwezi kutoa matokeo yanayoakisi utashi wa watu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mamlaka ya Tume kuhusu kufuta uchaguzi wa Zanzibar hayana mashaka yoyote; hayana mashaka ndani ya Katiba, wala ndani ya sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Tume ilitoa sababu nane za kufuta matokeo. Sababu mojawapo ikiwa ni malalamiko ya vyama vya siasa; ikiwa ni mgombea mmoja kujitangaza kwamba ameshinda ambapo ni kinyume kabisa na sheria, jambo ambalo lingeweza kupelekea machafuko na mtafaruku. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Tume ilikaa katika Mkutano wake wa tarehe 28 Oktoba, 2015 na kupitisha uamuzi wa kufuta matokeo yale.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Katiba ya Zanzibar upo utaratibu wa Tume kufanya maamuzi. Ibara ya 119(10), kwamba Tume itakapokaa maamuzi yake ni halali anapokuwepo Mwenyekiti au Makamu na wajumbe wengine wanne. Vilevile Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar inatamka kwamba kanuni, maelezo na matangazo yote ambayo Tume ina mamlaka ya kutunga au kutoa, yatahesabika kwamba yametungwa kisheria kama yamewekwa sahihi na Mwenyekiti wa Tume au Mkurugenzi wa Uchaguzi. (Makofi)
Tangazo lililotolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi wa Zanzibar kufuta matokeo kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar ni tangazo halali kisheria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile baada ya hapo tangazo lile, kama invyohitajika kwenye Katiba, liliwekwa kwenye Gazeti la Serikali kama hati ya kisheria namba 130 kwenye GN Namba 6587 ya tarehe 6 Novemba, 2015. Kwa hiyo, mjadala wa mamlaka ya Tume ya Uchaguzi kuhusu kufuta matokeo yale haupaswi kuwepo kwa sababu mamlaka yale inayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tarehe 21 Januari , 2016 Tume iliamua na kutangaza tarehe ya kurudiwa kwa uchaguzi. Kama Katiba inavyoelekeza katika Ibara ya 119 (10) kwamba maamuzi ya Tume ili yafanyike, ni lazima akidi itimie na lazima wengi wakubaliane na uamuzi ule.
Katika kikao cha Tume cha tarehe 21 mwezi wa Kwanza cha kuamua kutangaza kurudiwa kwa uchaguzi, akidi ilitimia na wengi walikubaliana na uamuzi ule. Kwa hiyo, uamuzi ule ni halali kisheria na Kikatiba. Katiba ya Zanzibar inasema kwamba hakuna mwenye mamlaka, hata Mahakama ya kuhoji au kuchunguza maamuzi yanayotolewa na Tume kuhusu uchaguzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wote tunajua kwamba uamuzi ule ulikuwa halali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu lazima iendelee kuwa nchi ya amani, ni lazima iendelee kuwa nchi ya utulivu na msingi wa amani na utulivu ni kuheshimu Katiba na sheria ambazo tumezitunga sisi wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine linalozungumzwa ni kwamba kama matokeo ya uchaguzi ulioendeshwa na Tume Zanzibar yamekubalika na kwamba kama tuna Wabunge kutoka Zanzibar humu, iweje basi uchaguzi wa Zanzibar uharibike na matokeo yafutwe? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, chaguzi zile ni mbili tofauti, zimefanyika kwa Katiba mbili tofauti, Tume mbili tofauti, sheria mbili tofauti, madaftari mawili tofauti, utaratibu wa kuhesabu kura tofauti, wasimamizi tofauti, hata wino kuna wino wa NEC na wino wa ZEC. Kwa hiyo, haishangazi wala haistaajabishi kwamba uchaguzi mmoja ukaharibika mwingine ukawa halali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kinachounganisha chaguzi hizi mbili ni kitu kimoja tu ni kwamba zilifanyika siku moja, lakini chaguzi hizi ni tofauti. Hoja kwamba kama uchaguzi huu ulikwenda sawa na mwingine siyo sawa, haina mashiko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuwasihi wenzetu ambao wameamua kutafuta suluhu hii kwa nje ya Katiba na nje ya sheria, wanakosea na kwamba hakuna miongoni mwetu ambaye ana uwezo wala mamlaka ya kuiamrisha Tume ifanye kingine nje ya Katiba na nje ya sheria. Viongozi wa nchi yetu akiwemo Rais wetu, wamefanya jitihada kubwa na za kutosha kuhakikisha kwamba nchi yetu inaendele kuwa ya amani na kwamba maamuzi haya ya Tume ambayo hatuna mamlaka nayo, hayapelekei katika vurugu na mtafaruku. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wajibu wa kulinda amani na umoja wa nchi yetu ni wajibu wa viongozi wa kisiasa. Maamuzi ambayo viongozi wa kisiasa wa Zanzibar watayachukua, kama yatakuwa ni maamuzi ya kusababisha vurugu na fujo na mtafaruku, basi damu ya Watanzania itakuwa mikononi mwao.
Sisi kwa upande wa Chama cha Mapinduzi na kwa upande wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wajibu wetu ni kuhakikisha kwamba nchi yetu ianendelea kuwa ya amani, utulivu na usalama. Tunao wajibu wa kuheshimu maamuzi ya Tume na hicho ndicho tutakachofanya. Hatuna mamlaka ya kuiamrisha Tume ifanye vinginevyo kinyume na utaratibu wake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niliona niseme hayo. Yapo mengine yamezungumzwa yakiwemo masuala ya bomoa bomoa, tutayazungumza wakati wa michango ya kuchagia kwenye Mpango. Nashukuru sana kwa nafasi hii. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshmiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Napenda kumpongeza sana Dkt. Mpango, Naibu wake na Makatibu Wakuu na timu nzima ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa kazi nzuri ya kuandaa Mpango na kuuwasilisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tumefarijika na kama Serikali tumeweka hifadhi ya mazingira kama vipaumbele muhimu katika mipango ya maendeleo ya nchi. Wakati wa bajeti Serikali italeta mipango ya kina ya kueleza tafsiri yake hasa ni nini na nini kitafanyika katika kuhakikisha kwamba hifadhi ya mazingira inazingatiwa katika mipango ya maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kwamba nimefadhaika kidogo kwa michango iliyotoka hapa Bungeni kwa Wabunge walio wengi. Sisi Wabunge bila kujali Majimbo yetu, shida za watu wetu zinafanana bila kujali Jimbo ni la Upinzani au ni la CCM. Unapoikejeli Serikali, unapomkejeli Rais, unapowakejeli Mawaziri, angalau acha fursa ya uwezekano wa kuomba ushirikiano, kufanya kazi na Serikali hiyo hiyo, Rais na Mawaziri hao hao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi ndiyo wenye Serikali, ndiyo tunapanga bajeti, ndiyo tunatekeleza maendeleo. Acha fursa ya ubinadamu wa kuweza kufanya kazi kwa pamoja. Mimi naelewa kwamba Upinzani kazi yao kulaumu, lakini ipo fursa ya kutoa Mpango mbadala. Hivi ninyi kwa kazi anayoifanya Mheshimiwa Magufuli leo, kipi mngefanya tofauti? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Bunge lililopita walikuwa wanatulaumu kuna uzembe, kuna ubadhirifu, kuna ufisadi; Mheshimiwa Magufuli anatibu uzembe, ubadhirifu, ufisadi bado mnatulaumu. What would you have done differently, leo kama mngekuwa na Serikali? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na tishio hapa, watu wanazungumza amani itavurugika. Maarifa yaliyounda nchi yetu, maarifa yaliyounda Muungano wetu, maarifa yaliyolinda amani yetu mpaka leo ni makubwa kuliko ukomo wa kufikiri wa baadhi ya watu hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Muungano wetu utadumu, amani yetu itadumu, nchi yetu itakuwa moja, hizi kauli za kutisha kwamba nchi italipuka, kutakuwa na mvurugano, tusiwatishe wananchi dola ipo na busara ya viongozi ambao walishiriki kwenye kuiunda nchi hii ipo. Wapo ndani ya Chama cha Mapinduzi, wapo ndani ya Serikali, nchi yetu itaendelea kuwa ya amani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ufumbuzi wa suala la Zanzibar, naelewa haja ya kuonesha hisia ndani ya Bunge hili, lakini ufumbuzi haupo ndani ya Bunge hili. Ufumbuzi wa suala la Zanzibar haupo kwenye Ofisi za Mabalozi wa kigeni, ufumbuzi wa suala la Zanzibar haupo barabarani na mitaani. Ufumbuzi upo ndani ya Katiba na ndani ya Sheria za Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme tu kwamba tupo kama Serikali, tupo imara, tutafanya kazi yetu bila uoga, bila wasiwasi na Mheshimiwa Rais anafanya kazi nzuri, anaungwa mkono na Watanzania wote na wenzetu msione aibu kumuunga mkono. Siyo dhambi kama mtu anafanya kazi nzuri, kama Serikali inafanya kazi nzuri, kama Mawaziri wanafanya kazi nzuri, siyo dhambi kuwaunga mkono kwa sababu nchi yetu ni moja, kazi yetu ya kuleta maendeleo ni moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa na nianze kwa kutoa pongezi kubwa kwa Wizara ya Fedha na Mipango kwa kuandaa Mpango madhubuti waliouwasilisha hapa Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka jana tulienda kwenye uchaguzi na kila chama kilitoa ahadi kwa Watanzania. Watanzania wakakiamini Chama cha Mapinduzi na wakaamini kwamba ahadi za CCM ndizo zinazotekelezeka, jukumu la kwanza kabisa la chama kinachoshinda uchaguzi ni kuunda Serikali. Kwa hiyo, Serikali imeundwa, Serikali imara na Serikali madhubuti. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jukumu la kwanza la Serikali iliyoundwa baada ya uchaguzi ni kutengeneza mpango unaotafsiri Ilani na ahadi za chama kilichoshinda. Hilo ndilo tunalolifanya sasa. Jukumu la pili la Serikali iliyoshinda ni kutengeneza bajeti za kila mwaka za kutekeleza mpango ambao tumesema unatafsiri ilani na ahadi za chama, hilo ndilo linalokuja katika kikao hiki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mantiki ya kawaida inasema kwamba kama wenzenu wameshinda, wameunda Serikali, wametengeneza mpango ambao unatafsiri yale yaliyowafanya washinde, wenzenu mnapaswa kuwapa nafasi watekeleze mipango yao na bajeti yao. Wanaposhindwa baada ya miaka mitano au katikati tunapofanya tathmini ndipo tunapokuja na kusema ninyi mmeshindwa. Hatuwezi wakati tunatengeneza mpango wetu ambao unatafsiri yale tuliyowaahidi Watanzania tunasimama tunasema ninyi kile, ninyi kile, ninyi hiki. Tupeni nafasi, ni Serikali mpya, tutekeleze ya kwetu katika mwaka wa kwanza kabisa wa Serikali hii ndipo tuje tuzungumze yale ambayo...
Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, kwa staili na kasi ya Serikali hii ya Awamu ya Tano hakuna hata chembe ya shaka kabisa kwamba yale tuliyoyaahidi, tuliyoyaandika katika Mpango wetu huu na katika bajeti tutakayoileta yatatekelezwa kwa ukamilifu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukitazama sura, kauli, umakini wa Rais wetu na Wajumbe wa Baraza lake la Mawaziri na Wabunge wa upande wa CCM kwa ujumla, hakuna shaka yoyote kwamba tumedhamiria kutengeneza nchi mpya. Tumedhamiria kutengeneza Taifa jipya, Taifa lenye haki, Taifa lenye usawa na Taifa lenye heshima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, huko nyuma katika miaka mingi tulijaribu kutengeneza Taifa la namna hiyo…
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Naibu Spika Taarifa!..
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa heshimia na taadhima napenda kuikataa taarifa hiyo na napenda kuikataa bila kueleza sababu, sababu za kuikataa ni dhahiri kabisa. Isingependeza kupoteza muda kueleza sababu za kuikataa kwa sababu zinaeleweka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika naomba niendelee …
NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, naomba basi tusikilizane!
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa aina ya taarifa iliyotolewa haistahili hata kuielezea kwa nini naikataa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee kwa kueleza kuhusu mazingira. Nashukuru sana kwamba katika Bunge hili kuna Wabunge wengi wanamazingira na naomba sana tutakapoleta bajeti yetu ya Ofisi ya Makamu wa Rais tutatoa dira mpya na mwelekeo mpya wa namna ya kulinda na kuhifadhi mazingira ya nchi yetu, tunaomba mtuunge mkono. Tutaeleza namna tunavyotaka kujenga uwezo wa kitaasisi wa Serikali na uwezo wa kifedha wa Serikali katika kugharamia shughuli za ulinzi wa mazingira. (Makofi)
Mwisho ni kuhusu Muungano, kuhusu Uchaguzi wa Zanzibar. Vitabu vinavyotuongoza kuhusu suala la Zanzibar kwa maana ya Katiba ya Zanzibar na Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar vinatuelekeza kwamba jambo hili limekwisha. Suala hili limekwisha, treni imeshaondoka kwenye kituo, wenzetu hawakushiriki, wamefanya uamuzi wa kimkakati ambao umewaondoa katika ushiriki wa siasa na maendeleo ya Zanzibar. Ni uamuzi wao, ni uamuzi ambao wataendelea kuujutia.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama CCM tunaamini kwamba ujenzi wa Taifa letu kwa ujumla ni jukumu letu sote na tunawakaribisha wenzetu hata kama wako nje ya Serikali kuendelea kushirikiana na sisi kuijenga Zanzibar na kuijenga Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kushukuru sana wote waliochangia hoja hii, wamefika wachangiaji 43 waliochangia kwa maandishi na kwa kuzungumza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru sana kwa waliotuunga mkono, tunashukuru waliotuongezea mawazo na vilevile tunawashukuru waliotukosoa. Tutajibu baadhi ya hoja hapa kwa sababu muda ni mdogo na nyingine tutazijibu kwa maandishi na kuwakabidhi Waheshimiwa Wabunge kabla ya mwisho wa Mkutano huu wa Bunge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo kubwa ambalo limezungumzwa kwa hisia kubwa na Wabunge wa pande zote linahusu uchaguzi wa Zanzibar na ndilo nitakaloanza nalo na nitaanza kwa kunukuu Katiba ya Zanzibar ambayo inatambulika na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 72(1) inasema; “Mahakama Kuu ya Zanzibar ndiyo pekee yenye mamlaka na uwezo wa kusikiliza na kuamua mashauri yote yanayohusiana na uchaguzi wa Zanzibar.” (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hayo ndiyo majibu yetu kuhusu uchaguzi wa Zanzibar, sitazungumza lolote hapa kwa sababu hapa siyo mahali pake, mahali pake pameelezwa kwenye Katiba ya Zanzibar. Vilio vyovyote vinavyohusu uchaguzi wa Zanzibar vikiletwa hapa Bungeni kwa kweli hapana msaada wowote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja iliyoko mbele yetu ni ya Muungano na Mazingira. Nianze tu kwa kusema kwamba mimi sikuzaliwa wakati wa Tanganyika, nimezaliwa wakati wa Tanzania kama ilivyo asilimia 92 ya Watanzania, sijui nchi yoyote zaidi ya Tanzania. Asilimia 92 ya Watanzania hawajui nchi yoyote zaidi ya Tanzania. Leo Tanzania hii uhalali wake ukihojiwa naumia binafsi.
Nadhani kwa viongozi ambao tumepewa dhamana na tuko kwenye Bunge ambalo juu lina nembo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni muhimu kabla hatujatoa maoni na kuzungumza kuhusu jambo kubwa kama hili tukajua shabaha yake, malengo yake, madhumuni yake na chimbuko la Muungano wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakumbuka kwamba kwenye miaka ya 1960 kulikuwa na hisia kubwa sana Barani Afrika za ukombozi, tulikuwa tunatafuta uhuru, tulikuwa tunataka kujikomboa na moja ya nyenzo kubwa za kujikomboa zilikuwa ni umoja wa watu wa Afrika. Hisia hizo za ukombozi zilihamasisha tuungane. Sisi bahati yetu Watanganyika na Wazanzibari Muungano wetu ulikuwa ni kurasimisha udugu ambao tayari upo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waasisi wa Muungano walikuwa na maarifa makubwa, walitafakari, walifikiria sana aina ya Muungano unaoendana na mazingira ya nchi yetu, aina ya Muungano unaoendana na ukubwa wa pande zote mbili, idadi ya pande zote mbili, tamaduni zetu na muingiliano ambao ulikuwa tayari umeshajitokeza kabla ya Muungano. Wale wazee walifikiria yote tunayoyazungumza sasa, Serikali hizi, zile na zile. Walipoamua, ndiyo maana Muungano huu umedumu, hawakuamua kwa pupa, hawakuamua kwa papara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kama mwanafunzi wa umoja wa mwafrika, kama mwanafunzi wa historia ya Afrika, nimechukua muda mrefu kujifunza. Mmoja wa mwalimu wangu ambaye nimejifunza kwake yuko hapa, Balozi Job Lusinde. Nimetumia saa nyingi kuwa naye na moja ya swali nililomuuliza ni kwamba hebu niambie ilikuwaje, mliamuaje, chimbuko lake lilikuwa nini, nani alianzisha wazo! Nawasishi viongozi wenzangu Wabunge kwamba kama tunataka kuupa jina baya Muungano angalau tujue basi chimbuko lake. Naamini kwamba tukijua chimbuko lake, shabaha yake, malengo yake, kidogo tutapunguza ukali wa lugha tunayoitumia katika kuupa jina baya Muungano wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Muungano wetu ulikuwa ni sehemu ndogo ya mradi mkubwa wa ukombozi wa mwafrika. Baadhi wanadhani kwamba umoja wetu sisi hauhitajiki sasa hivi, lakini leo unahitajika zaidi kuliko ilivyokuwa mwaka 1964. Kuna nchi nyingine zimeungana miaka 200 iliyopita, Marekani kwa mfano, zile federal government wana miaka zaidi ya 200 na hawajamaliza changamoto za muungano wao lakini hawazungumzii kuuvunja kwa sababu ya changamoto zilizopo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliaswa na waasisi wa nchi yetu kwamba sisi ambao tunatafuta kuwa nchi zinazoendelea tunahitaji umoja zaidi kuliko wengine. Inawezekana baadhi yetu hatuoni mantiki, hatuoni busara waliyoiona waasisi wa Muungano wetu, hiyo ni sawa kabisa kwa sababu watu tunatofautiana. Wito wangu tu ni kwamba hebu tu-moderate lugha zetu kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma na nimesikiliza taarifa ya Kambi ya Upinzani kuhusu Muungano na mambo mengineyo na nimesikitishwa sana na baadhi ya lugha zilizotumika mle. Baadhi ya mambo yamejibiwa na Waziri Mheshimiwa Dkt. Mwinyi lakini kutumia maneno kwenye taarifa ile ya ukoloni na unyonyaji unaofanywa na Tanganyika dhidi ya Zanzibar, ni lugha ya kutugawa Watanzania. Inawezekana kuna mambo yanayoleta manung‟uniko kwenye Muungano, ni kweli inawezekana, lakini kwenda kwenye kiwango hiki cha kutumia maneno haya ya ukoloni na unyonyaji unaofanywa na Tanganyika dhidi ya Zanzibar ni lugha ambayo unapolaumiwa kwamba hupendi muungano huwezi kukataa kwa sababu umetumia lugha hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Jeshi la Tanganyika ameshajibu Mheshimiwa Mwinyi. Niendelee tu kwa kusema kwamba, ndugu yangu wa Konde pale rafiki yangu sana Mheshimiwa Khatib, anasema kwamba Muungano huu haufai kwa sababu tuko maskini, tuliungana ili tuwe matajiri. Mimi nataka kumuambia kwamba kwa sababu tuko maskini ndiyo tunauhitaji zaidi Muungano wetu huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napata shida kuelewa kitu kimoja kwamba Muungano haufai lakini Ubunge wa Bunge la Muungano unafaa. Mimi mantiki siioni labda ni ile ya kusema nyama ya nguruwe haramu, mchuzi wake halali. Inabidi tuamue kitu kimoja, kama hatuamini katika Muungano hatuwezi kuamini katika taasisi za Muungano ikiwemo Bunge la Muungano na hatuwezi kuwa sehemu ya taasisi za nchi ambayo hatuikubali na hatuiamini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja imetolewa kwenye Taarifa ya Upinzani kwamba ni CUF na napenda kunukuu hivyo hivyo, ni CUF na kiongozi wake Maalim Seif ndiyo pekee wanaolinda Muungano hadi kufikia ulipofikia, ukurasa wa 13, haya ni matusi kwa viongozi wote waliowahi kuongoza nchi hii. Kwa sababu wamefanya kazi kubwa ya kuulinda muungano, kuimarisha na kuujenga. CUF imeanza kuingia kwenye harakati mwaka 1992 wakati Muungano upo na unaendelea. Unaposema kwamba ni yeye peke yake tu ndiyo anafanya Muungano uwepo na udumu maana yake Mwalimu Nyerere, Karume, Mwinyi, Mkapa, Salmin Amour, Karume wa pili wote hawakuwa na maana yoyote isipokuwa kiongozi mmoja kule Zanzibar. Ndiyo maana nasema hebu tuya-moderate kidogo haya maneno ili angalau tutoke tukiwa tunaonekana tuna busara katika Bunge hili. (Makofi)
Mheshimiwa mwenyekiti, baadhi ya mambo tutayajibu kwa maandishi kwa sababu hatuwezi kuyajibu yote hapa, niende kwenye michango ya baadhi ya Wabunge.
Mchango wa Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha kuhusu mapendekezo ya mgawanyo wa mapato jambo ambalo ni la msingi sana na jambo ambalo ndilo litapelekea kwenye ile dhana ya msingi ya kwamba kila upande uchangie na upate kulingana na mchango wake na ukubwa wake. Mheshimiwa Vuai amesema kwamba katika miaka kumi ya yeye kuwa Waziri Kiongozi na miaka mitatu ya kuwa Waziri kwenye Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hawakufanikiwa kulimaliza suala hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimueleze ndugu yangu kwamba Serikali hii imeingia madarakani miezi sita iliyopita, sisi hatutatumia miaka kumi kama aliyoitumia yeye katika Serikali iliyopita. Naomba niseme tu kwamba atupe nafasi na tumeanza, barua yangu ya kwanza kabisa kama Waziri katika Serikali hii na ilichelewa kwa sababu Waziri wa Fedha alichelewa kuteuliwa, ilikwenda kwa Waziri wa Fedha kuhusu kushirikiana kuandaa Waraka wa Baraza la Mawaziri wa kupitisha mapendekezo ya Tume ya Pamoja kuhusu mgawanyo wa mapato. Wizara ya Fedha imelifanyia kazi jambo hilo, Waraka upo tayari na wakati wowote utapelekwa kwenye Baraza la Mawaziri na kufanyiwa maamuzi ikiwemo uanzishwaji wa Akaunti ya Pamoja. Jambo hili litahusu pia mgawanyo wa zile asilimia 4.5 na kadhalika litafanyiwa kazi mara mapendekezo haya yatakapopitishwa kwa hiyo kazi inafanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Menyekiti, lakini kabla ya hapo kuna arrangement za muda ambazo zinaendelea ikiwemo hiyo 4.5 kwa GBS na gawio la BOT. Pia VAT inayokusanywa Zanzibar kwa wafanyakazi wa Bara wanaofanya kazi Zanzibar inabaki Zanzibar na PAYE kwa maana hiyo na VAT inayokusanywa na TRA kwa upande wa Zanzibar inabaki Zanzibar na PAYE kwa wafanyakazi wa Bara wanaofanya kazi Zanzibar inabaki Zanzibar vilevile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Fakharia amezungumzia kuhusu Sekretarieti ya Ajira. Waziri wa Utumishi alitoa taarifa hapa kwamba tutafungua ofisi Zanzibar katika mwaka wa fedha unaokuja. Kwa hiyo, ofisi hiyo itafunguliwa na mimi niliwaunganisha Waziri wa Utumishi, dada yangu Mheshimiwa Angellah Kairuki na Waziri wa Utumishi, Mwalimu Haroun kule Zanzibar na Mheshimiwa Kairuki amepanga tarehe ya kwenda kutazama jengo na mahali ambapo ofisi itakuwepo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wiki nne zilizopita niliandika barua kwa Mawaziri kama saba hivi ambao wanasimamia taasisi za Muungano na kuwaomba kwamba watuletee mgawanyo wa ajira kati ya watumishi wa Zanzibar na watumishi wa Tanzania Bara kwenye taasisi za Muungano. Makubaliano yaliyokuwepo ni ya asilimia 79 kwa 21, makubaliano ya muda na Waheshimiwa Mawaziri hawa wameanza kunitumia. Nimeona kwa mfano Wizara ya Mambo ya Nje ambayo ndiyo inalalamikiwa sana kwa mwaka 2014/2015, katika nafasi 27 zilizotoka nafasi saba asilimia 26 zilikuwa Zanzibar na nafasi 20 asilimia 74 zilikuwa upande wa Tanzania Bara. Kwa hiyo, tumeanza na tutaendelea kwa sababu tunayo dhamira ya kuimarisha Muungano wetu, hatutachoka wala hatutachukizwa na maneneo ya kuudhi yanayozungumzwa dhidi ya muungano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kaka yangu Mheshimiwa Daniel Nsanzugwanko amezungumza na napenda nikiri kwamba tulipitiwa. Tulipitiwa kwa msingi kwamba sisi tulichukua human activities zote zinazoathiri mazingira ikiwemo wingi wa watu katika eneo dogo kwa wakati mmoja. Nakubali kwamba tungetaja wakimbizi kama ni changamoto mahsusi ya mazingira. Bahati nzuri maeneo aliyoyataja mimi nimefanya kazi miaka 20 iliyopita, nilikuwa Meneja wa Kambi ya Wakimbizi kule Mtabila, nafahamu Mtabila, Muyovosi, Lugufu, Nyarugusu, Kanembwa na kwingineko, kwa hiyo, Heru Juu, Heru Shingo na Mabanda kote ni kwetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nithibitishe kwamba kweli uharibu wa mazingira ni mkubwa sana unaotokana na uingiaji wa wakimbizi. Kwa hiyo, sisi kama Wizara tutawasiliana na Mashirika ya Kimataifa yanayohudumia wakimbizi kwamba kazi yao isiwe ni kulisha wakimbizi tu bali kutoa mchango kwenye kurudisha mazingira ya eneo lile kwenye hali nzuri. Mimi naahidi kutembelea mwenyewe kujionea mambo yalivyo huku. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, badhi ya Wabunge wamezungumzia masuala ya NEMC. Kwenye hotuba yetu tumezungumza jinsi ambavyo tutabadilisha na kupitia mfumo mzima wa kupitia vyeti vya tathmini ya athari kwa mazingira ili visiwe vinatumika kuchelewesha miradi ya uwekezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya Wabunge wamesema kwamba ofisi yetu ina bajeti ndogo na ina uwezo mdogo wa kitaasisi wa kudhibiti changamoto kubwa za mazingira. Mkitazama kwenye hotuba yetu ya bajeti katika maelezo ya Mfuko wa Mazingira, moja ya maelezo ya kazi ni kujenga uwezo wa kitaasisi wa Serikali ikiwemo NEMC kukabiliana na athari za mazingira. Kwa hiyo, Mfuko ule utakapoanza ofisi yetu itakuwa na uwezo mkubwa wa kifedha na rasilimali watu wa kuweza kudhibiti mazingira ikiwemo kuajiri Maafisa Wakaguzi wa Mazingira nchi nzima ili kila Halmashauri iwe na watumishi na hizi kamati kwenye kila kata na kijiji ili ziweze kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma Taarifa ya Kambi Rasmi ya Upinzani ya dada yangu Mheshimiwa Pauline na napenda kumshuru sana kwamba kwa dhana na falsafa tunakubaliana bila shaka yoyote. Tunakubaliana kwamba mazingira ni jambo kubwa na pana na kule tunapoenda kwenye uchumi wa viwanda lazima tuzingatie hifadhi ya mazingira. Hilo tunakubaliana na tunashukuru kwa sehemu kubwa ushauri mlioutoa tutauzingatia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie mambo machache tu kwenye taarifa ile ambayo yanahitaji kurekebishwa. Kwenye ukurasa wa 19 ripoti imesema kwamba kwenye mradi wa DART tathmini ya mazingira haikufanyika. Nilitaka tu nisahihishe kwamba tathmini ilifanyika na cheti Na. EC/EIS/146 cha tarehe 30/6/2009 kilitolewa na masharti yalitolewa kwa waendesha mradi ule wa mambo ya kuzingatia katika hifadhi ya mazingira kwenye mkondo ule. Kwa hiyo, nilitaka niseme hilo la uelewa kwamba kwenye mradi ule tathmini ilifanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ripoti ya Mheshimiwa Pauline ilizungumzia kuhusu ripoti ya CAG ambayo ilitambua udhaifu kwenye utayari wa NEMC kwenye tasnia hii ya gesi na mafuta. Tumepokea sisi taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu na tutafanyia kazi mapendekezo yale. Mapendekezo yale utekelezaji wake unahitaji uwezo mkubwa na hakuna shaka yoyote kwamba tunaujenga. Niseme tu kwamba Sheria ya Gesi na Mafuta ambayo ndiyo ingetupa nguvu na uhalali sisi wana mazingira kuhusu ufuatiliaji imepitishwa mwaka jana tu na bahati nzuri sheria ile inatambua Sheria ya Mazingira na inatoa nafasi kwa NEMC kufanya kazi hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia taarifa ya Kambi Rasmi ya Upinzani imezungumzia miradi yenye shaka, miradi ambayo anasema inanukanuka ufisadi kidogo.
Mimi niseme tu kwamba tumepokea angalizo na mtu yeyote ambaye ananyoosha kidole kwamba mahali fulani inawezekana pana harufu anakusaidia. Sisi tunachukua taarifa hizo kama msaada kwa sababu Serikali hii imeamua kupambana na maovu ikiwemo rushwa na ufisadi. Kwa hiyo, haiwezekani nikasimama hapa nikakulaumu kwamba kwa nini umesema, nasimama hapa kukushukuru kwamba ni jambo ambalo tutalifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ila niseme tu kwamba miradi ile ina fedha za ndani kwa maana ya fedha zetu na za wafadhili, fedha za ndani zinaitwa counterpart fund. Kwa hiyo, siyo ajabu ukitazama makaratasi yetu ukakuta mradi wa ukuta, ukatazama karatasi la mfadhili ukakuta mradi wa ukuta kwa sababu fedha hizi zinakaa pamoja. Vilevile miradi hii inakaguliwa na CAG na katika miaka miwili iliyopita imepata hati safi lakini angalizo tumelipokea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu jana wakati nakutana na wataalam Wizarani nilielekeza kwamba wasiondoke kesho ili tupitie miradi yote. Kwa sababu kuna miradi mingi vya mazingira ambayo wakati mwingine hatuna taarifa za kina ili tuijue kila mradi ni upi, gharama zake ni zipi, umefikia wapi, unanufaisha watu wangapi, uliamuliwaje upelekwe huko ulikopelekwa na tunaweza kufanya maamuzi ya kuhakikisha kwamba miradi hii inawanufaisha watu wengi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepokea mchango wa Mheshimiwa Rehani Mwinyi anazungumzia kuhusu Mfuko wa Mazingira kwamba ndiyo mkombozi wa mazingira yetu na mimi nakubaliana naye asilimia 100. Katika mwaka huu wa fedha tunafanya mazungumzo ndani ya Serikali kuhusu vyanzo mbalimbali vya Mfuko huu na tunategemea support ya Bunge tutakapokuwa tumemaliza Serikalini. Mfuko huu kama tulivyosema kwenye hotuba yetu tunataka kwa kuanzia uwe na shilingi bilioni 100 lakini fedha hizi hazitoshi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama ya kuhifadhi mazingira na kukabiliana na athari za mazingira na kurudisha mazingira katika hali yake ya kawaida kwa mwaka ni karibu shilingi bilioni 350. Ili turudi katika hali ambayo tunataka tuwe lazima fedha hizi zipatikane kwa miaka 17 mfululizo lakini sisi tunaomba shilingi bilioni 100. Nina imani kwamba ndani ya Serikali tutakubaliana kuhusu maeneo gani tunaweza kupata vyanzo hivyo ili Mfuko huu uanze ili tuwe na uwezo wa kuja katika maeneo yote kama aliyosema dada yangu Mheshimiwa Maufi kule Rukwa na kusaidia kurekebisha mazingira yaliyoharibika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatupaswi kutegemea wahisani kwa kuhifadhi mazingira ya nchi yetu kwa sababu huo ndiyo umekuwa mwelekeo mkubwa. Kuna dhana kwamba kwenye mazingira kuna hela nyingi za misaada lakini nchi hii ni ya kwetu, itarithiwa na watoto na wajukuu wetu, wahisani hapa siyo kwao. Kwa hiyo, sisi tuna wajibu mkubwa zaidi wa kuchanga ili kuhifadhi nchi yetu iendelee kuwepo siku nyingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie tena kwa kushukuru kwa kupata fursa hii, nawashukuru Wabunge wote waliochangia, nashukuru kwamba mmetusaidia na naomba muendelee kutuunga mkono.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru wageni wetu walikokuja hapa siku ya leo ambao nimewataja, wale vijana wa mwaka 1964 waliochanganya udongo, Mzee Job Lusinde, wamekaa mpaka jioni hii na nina hakika matumbo yalikuwa yanawazunguka wakati Muungano ambao waliushuhudia unaundwa ulikuwa unadhalilishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwaambie kwamba Serikali yao ipo imara katika kuulinda na kuhakikisha unaimarika ili kazi waliyoifanya iwe na matunda na iendelee kuwa sehemu ya urithi wa nchi yetu. (Makofi/Vigelegele)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba kutoa hoja.
Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa fursa ya kuzungumza na napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri aliyoitoa na kwa mipango mizuri ya Wizara.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika taasisi ambapo uongozi unafundishwa vizuri kwa nadharia na vitendo ni pamoja na jeshini na hii ni kote duniani, iwe West Point, Sandhurst au Monduli. Tangu nchi yetu ipate uhuru, viongozi wa Taifa hili tangu Baba wa Taifa mpaka Rais Magufuli wameenda jeshini kuchota katika kisima cha hazina ya uongozi iliyopo jeshini ili kusaidia kuongoza nchi yetu. Askari wetu wote walioombwa au walioteuliwa kutumikia nafasi za uongozi katika nchi na katika siasa kutoka jeshini wamefanya kazi nzuri na kubwa na mifano iko mingi, Jenerali Kimario, Jenerali Sarakikya, Jenerali Luhanga na wengineo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi kwa sababu katika hotuba ya Kambi ya Upinzani, ukurasa wa 12 kuna hoja imetolewa pale, kwamba ili kulinda na kusimamia maadili ya kazi ya jeshi, Wanajeshi wasihusishwe kabisa na kazi za siasa iwe wapo kazini au wamestaafu. Wanaendelea kusema kwamba kwa kuwateua kushika nafasi za siasa wanapostaafu, kunaweza kuwafanya wale wengine waliopo kazini kutozingatia maadili yao ya kazi na kuanza kujipendekeza kwa watawala. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika ngazi kumi za uafisa jeshini, ngazi saba Rais ndiye anayepandisha vyeo. Kwa hiyo, kama kuna hoja ya kujipendekeza kwa Askari wetu, isingekuwa kwenye ngazi za siasa hata kule kule waliko jeshini kama tunaamini kwamba kwa weledi wao na mafunzo yao wametengenezwa na wamefundishwa katika hulka za kujipendekeza ingekuwa tunaiona kuanzia sasa kwa sababu bado Rais anapandisha vyeo jeshini. Kwa hiyo, nadhani kwamba ni kuwadhalilisha Askari na Maafisa wetu kwa kusema kwamba wanajipendekeza kwa watawala ili wapate nafasi.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi letu limewekwa chini ya mamlaka ya kiraia na sisi viongozi wa kiraia tunapigiwa saluti wakati mwingine na Askari. Leo wakati tunapitisha bajeti hii, wamekuwepo Askari na Maafisa wengi na wameshuhudia jinsi tunavyoendesha mambo yetu, nadhani baada ya kupitishwa bajeti hii na naamini itapita, tutakapokuwa tunarudi nyumbani kwetu tutafakari kama waliyoyaona tunayafanya Askari wetu leo hapa kama kweli watatupigia saluti huku ndani ya mioyo yao wakiwa hawaamini kama tunazistahili kama watakuwa wanakosea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu wa Spika, naomba nimalizie kwa kuwashukuru Askari wetu wote, Maafisa na wale wanaowaongoza kwa kuendelea kuifanyia kazi nzuri nchi yetu. Napenda kuwashukuru binafsi kwa kutuongoza na kufanya kazi vizuri. Napenda makusudi kabisa niwataje kwa sababu huwa hawatajwi hasa viongozi wale, Mkuu wa Majeshi yetu Jenerali Mwamunyange, ahsante sana. Mnadhimu Mkuu Lieutenant General Mabeyo, ahsante sana. Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu, Meja Jenerali Mwakibolwa ahsante sana. Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Wanamaji, Rogastian Laswai, ahsante sana. Mkuu wa JKT, Brigedia Jenerali Isamuhyo, ahsante sana. Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Anga, Brigedia Jenerali Ingram, ahsante sana. Mnastahili shukrani zetu sana kwa kazi nzuri mnayoifanya, kwa sacrifice mnayoichukua kulinda mipaka ya nchi yetu, kulinda amani ya nchi yetu na wakati mwingine maneno ambayo yanasemwa humu ndani ya kuwadhalilisha hamuyastahili na Watanzania wote wako nyuma yenu, ahsanteni sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 – Wizara ya Fedha na Mipango
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa fursa ya kuchangia. Kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara; kwa kazi nzuri waliyoifanya katika kuandaa bajeti hii. Nawapongeza sana Wabunge wa CCM kwa kutimiza wajibu wao waliotumwa na wananchi wao kwa kutimiza sababu yao ya kuchaguliwa kwa kuingia Bungeni kufanya kazi waliyotumwa na wananchi na kueleza shida za wananchi wao mbele ya Serikali, nawapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yako mambo kadhaa ambayo ningependa kuyazungumzia, la kwanza ni suala la VAT kwa Zanzibar na Bara. Kuna upotoshaji mkubwa sana kwamba hatua iliyochukuliwa na Serikali, hatua nzuri kabisa ya kuhakikisha kwamba bidhaa zinazozalishwa Tanzania Bara kwenda Zanzibar VAT inakusanywa Zanzibar; na bidhaa zinazozalishwa Zanzibar na kuletwa Tanzania Bara VAT inakusanywa Tanzania Bara. Kuna upotoshwaji mkubwa sana unaofanywa na wenzetu kule Zanzibar kwamba hatua hiyo inaiumiza Zanzibar, si kweli, ni kunyume chake. Hatua hii inainufaisha Zanzibar, hatua hii itawaumiza wale wadanganyifu wachache, waliokuwa wanatumia utaratibu huu kujipatia kipato ambacho sio halali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, ambalo ningependa kulizungumzia ni ahadi ya Chama cha Mapinduzi kwenye Ilani yetu kwamba kila kijiji kitapatiwa shilingi milioni 50 kwa ajili ya uwezeshaji, ukopeshaji wa wajasiliamali. Ahadi hii ya CCM ni hatua kubwa ya kimapinduzi ya kumuondoa Mtanzania katika lindi la umaskini. Mzunguko wa shilingi milioni 50 katika kijiji ni pesa nyingi sana zitakazoleta chachu ya maendeleo pale kijijini. Serikali katika mwaka huu wa fedha kama ambavyo mmeona, imetenga shilingi bilioni 59 kama kianzio, lakini zaidi ya hapo Serikali imeunda jopo la wataalam ambalo linatengeneza utaratibu madhubuti kabisa. Utaratibu utakaozingatia uzoefu wetu huko nyuma wa mifuko mbalimbali na mafanikio ya mifuko hiyo ili tuwe na utaratibu mzuri utakaohakikisha fedha hizi zinatumika kama zilivyopangwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hili ni jambo kubwa linabidi lifanyike kwa umakini na umahiri mkubwa ili tusipoteze fursa hii adhimu katika kuwaokoa watu wetu. kwa hiyo utaratibu mzuri unaotengenezwa na Serikali utaletwa hapa Bungeni ili kabla ya kutumika na ninyi Waheshimiwa Wabunge muwe na mchango wenu katika aina ya utaratibu ambao Serikali itautumia na ikiwezekana kabisa aidha ni kwa kuleta Sheria mpya au kufanya mabadiliko ya Sheria katika Sheria ya Uwezeshaji sasa hivi. Ili fedha hizi ziwe katika msingi wa kisheria na ziweze kutumika vizuri kuliko mifuko mingine yote huko nyuma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukweli kwamba zimetengwa shilingi bilioni 59, haina maana kwamba tutashindwa ndani ya miaka mitano kufanya vijiji vyote; tumeweka hizi ili tuanze na tujifunze na kadri tutakavyokuwa na utaratibu mzuri, kasi ya kupanga fedha nyingi zaidi ili tutimize ahadi hii kwa miaka mitano inakuwepo. Kwa hiyo napenda kuwahakikishiwa Waheshimiwa Wabunge na watanzania, kwamba hii ni ahadi ya CCM, hii ni ahadi ya Rais na itatimia bila shaka yoyote.
Naomba niseme kidogo jambo moja muhimu. Sisi Chama cha Mapinduzi tulipomteua Dkt. John Pombe Magufuli kuwa mgombea wetu, tulitoa statement duniani kwamba tunahitaji aina mpya ya nchi kutokana na aina ya kiongozi huyo. Kwetu sisi kumteua yeye tulitoa kauli duniani kwamba tunataka mabadiliko ya kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mabadiliko ya kweli hayawezi kuletwa kwa hatua ndogo ndogo, mabadiliko ya kweli yanaletwa hatua kubwa na yanaletwa na uthubutu na uthubutu huo umeanza kujidhihirisha katika bajeti ya mwaka huu, tumethubutu kwamba tunaweza kukusanya shilingi trilioni 29.5; tumethubutu kwamba tunaweza kutenga asilimia 40 kati ya hizo kwa maendeleo. Unapothubutu jambo kubwa kuna watu watatia shaka, sisi wana CCM Serikali hii ni ya kwetu, Bunge hili ndio wengi, ilani ni ya kwetu, tusitetereke katika uthubutu wetu wa kukusanya shilingi bilioni 59 tumsaidie Rais tuisaidie nchi yetu kufikia malengo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, imezungumzwa suala la hatua za kikodi hapo mbalimbali imetokea malalamiko kwamba kodi ni kubwa, kodi ni nyingi zitadhohofisha uwekezaji. Jambo hilo si la kweli kwa sababu utafiti unaonyesha mimi hapa ninayo ripoti inaitwa Tax incentive in a global perspective inasema kwamba; survey analysis shows that host country taxation and international investment incentives generally play only a limited role in determining the international pattern of FDI. Factors like market characteristics, relative production costs and resource availability explain most of the cross-country variation in FDI inflows. Transparency, simplicity, stability and certainty in the application of the tax law and in tax administration are often ranked by investors ahead of special tax incentives.
Suala siyo kiwango cha kodi, suala ni mfumo wa kodi. Kwa hiyo, miaka yote tumeaminishwa kwamba ukiweka kodi ndogo wanakuja, ukiweka kodi kubwa hawaji, dhana hiyo si ya kweli. Ukitengeneza mambo mengine vizuri zaidi ndiyo wanakuja ikiwemo uhakika wa mfumo wa kodi. Kwa hiyo, tusiwatishe wananchi na tusitishane hapa kwamba kiwango cha kodi tulichoweka kitafukuza wawekezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ngoja nimalize kwa kusema kwamba Rais Magufuli tumempa usukani wa kuiongoza nchi yetu, lakini nchi hii ni yetu sote na sisi tunawajibu wa kumsaidia ili tufanikiwe. Rais Magufuli akifanikiwa, nchi yetu imefanikiwa sisi tusiwe kama watazamaji kwamba ngoja tumuone atafanyaje, sisi tuko naye kwenye basi hili tumsaidie. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hatua tunazochukua nchi yetu ni sawasawa na gari nzuri aina ya benzi iliyoingia kwenye matope tunataka kuirudisha kwenye lami, hatua ya kuirudisha kwenye lami itakuwa na misukosuko, kuna wengine wataamua kushuka lakini tuendelee kuwa ndani ya gari hilo mpaka likae kwenye lami lifike safari. Maendeleo yanahitaji sacrifice, katika bajeti hii Wabunge sisi tume-sacrifice, tume-sacrifice kwa kukubali kukatwa kodi, kila mtu lazima a-sacrifice, wafanyabiashara, waendesha bodaboda, kila mmoja lazima a-sacrifice ili nchi yetu iende mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalize kwa kusema mwaka 1961 wakati Rais Kennedy wa Marekani anaapishwa aliwaambia wa Marekani kwamba ask not what your country can do for you, but what you can do for your country. Ni wakati sasa kwa Watanzania wote kutokaa siku zote na kujiuliza nchi hii itanifanyia nini bali sisi tutaifanyia nini nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa fursa ya kuchangia hoja ya Waziri.
Kwanza, nianze kwa kutoa pongezi kubwa sana kwa hotuba nzuri na mipango mizuri iliyotolewa katika hotuba ya leo. Vilevile napenda kumpongeza Mheshimiwa Nape Nnauye, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara kwa kazi nzuri sana wanayoifanya katika majukumu waliyokabidhiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nikubaliane na sehemu ya mchango iliyotolewa asubuhi hii na Mheshimiwa Zitto Kabwe, kwamba kijana akipewa majukumu na akafanya vizuri basi ni fahari kwa vijana, kauli hiyo ni sahihi kabisa. Pia naamini kwamba kijana akipewa majukumu anastahili kutiwa moyo, kuungwa mkono hasa na vijana wenzake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya mchango ulivyotoka asubuhi, ni kana kwamba Mheshimiwa Nape kazi hii amepewa miaka minne iliyopita na imeshamshinda na hana ubunifu. Aina ya mchango ule unakatisha tamaa, haumpi moyo Mheshimiwa Nape kama inavyostahili. Majukumu haya Mheshimiwa Nape amekabidhiwa takribani siku 160 zilizopita, kwa hiyo, bado kuna muda mrefu wa kufanya kazi na kuonesha ubunifu, na mimi sina shaka yoyote kabisa na uwezo wake wa kufanya kazi hii vizuri. Sikubaliani kabisa na dhana kwamba katika nchi hii mtu anayechukiwa zaidi ni Mheshimiwa Nape Nnauye. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana nilipata bahati, Mheshimiwa Nape aliniomba nimsindikize kwenye Chuo Kikuu cha Dodoma ambapo kulikuwa na shughuli ya vijana; walikuwa wengi takribani 8,000 mpaka 10,000. Alipotambulishwa, nilliyoyaona hayaendani na kauli zinazosema kwamba hapendwi hapa Watanzania. Ushuhuda wa mambo hayo siyo maneno yangu tu, hata record ya shughuli hiyo ipo wazi na ilioneshwa. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesimama kuchangia hotuba hii, lakini hasa hasa kuzungumzia hotuba ya Msemaji wa Kambi ya Upinzani hasa ukurasa wa 11. Niseme tu kwamba binafsi huwa naheshimu karibu kila mtu hapa Bungeni na sijawahi kuinua mdomo wangu au kauli yangu pale mtu anapotoa mchango wake. Kwa hiyo, nategemea heshima hiyo iwe accorded kwa Waheshimiwa Wabunge wote, kwamba kila mtu anapopewa nafasi ya kuzungumza, basi angalau kwa Kiingereza wanasema; “decorum.” Kwamba angalau kuwepo na decorum ya kumheshimu mwenzako amalize anachosema na fursa inapopatikana, kama hukubaliani naye, basi unaweza kusema hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ukurasa wa 11 wa hotuba, imejengwa dhana hapa kwamba Chama cha Mapinduzi na Serikali ya Chama cha Mapinduzi na Mheshimiwa Rais anabagua wasanii. Katika vitu ambavyo viko mbali na ukweli, hiki ni namba moja. Linalozungumziwa hapa ni kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alialika baadhi ya wasanii na kuwabagua wengine. Kwa hiyo, wenzetu wanasema hicho ni kitendo cha Serikali, cha Rais kuwabagua wasanii ili awatumie kwa ajili ya maslahi ya kisiasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipata bahati ya kuandaa hiyo shughuli inayozungumzwa na kushiriki kuiendesha. Katika shughuli ile Mheshimiwa Rais alitoa maelekezo kwangu na kwa wenzangu kwamba angependa kutoa shukrani kwa makundi mbalimbali yaliyoshiriki kwenye kampeni ya CCM wakiwemo wasanii walioshiriki katika kampeni ya CCM.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa uchaguzi kulikuwa na wasanii ambao walituunga mkono CCM na kuna wasanii ambao hawakutuunga mkono. Katika shughuli ile walialikwa wasanii, madereva, makundi mbalimbali; vijana wa IT pia walishiriki. Ilikuwa ni shughuli ya Mheshimiwa Rais kutoa shukrani kwa watu walioshiriki katika kampeni yake na kampeni ya CCM. Shughuli ile ya kushukuru watu imeendelea, haikuishia kwa makundi yale ambayo yalialikwa mwezi wa pili ambapo mimi nilishiriki, lakini pia viongozi wa CCM na viongozi wengine na kazi hiyo inaendelea.
Katika shughuli ile, masuala ya maslahi ya wasanii yalizungumzwa kwa mapana yake. Mheshimiwa Rais alielekeza hatua kadhaa za msingi za kuchukua na Mheshimiwa Waziri amezizungumza baadhi ya hatua hizo leo za kusaidia wasanii kujikwamua na changamoto zilizopo. Bahati nzuri sasa katika hatua zilizochukuliwa, katika utekelezaji wake zitawanufaisha wasanii wote waliotuunga mkono na ambao hawakutuunga mkono, walioshiriki shughuli ile na ambao hawakushiriki shughuli ile kwa sababu hatua zile hazibagui mtu, hazibagui wasanii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilitaka nichangie, niweke record sahihi kwamba Mheshimiwa Rais wetu ni Rais wa watu wote na ni Rais wa wasanii wote. Serikali ya CCM ni Serikali ya watu wote, ni Serikali inayowaongoza na kuwaletea maendeleo hata wale ambao hawakutuunga mkono; kwa sababu sisi ndio tumekabidhiwa dhamana ya uongozi wa nchi na dhamana ya kuleta maendeleo ya nchi hii, na kazi hiyo tunaifanya na tutaifanya vizuri; na matokeo ya kazi hiyo yataonekana mwaka 2020 pale ambapo tutaongezeka na tutarudi kwa kishindo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalize tena kukushukuru kwa fursa hii na kwa kumpongeza sana na kumtia moyo ndugu yangu, Mheshimiwa Waziri Nape na timu yake. Sisi tunaokujua vizuri, waswahili wanasema haja ya mja kunena, muungwana ni vitendo. Si haki kuhukumiwa kwa neno moja kukosekana kwenye hotuba wakati kazi unaifanya ya kusukuma soka la nchi hii na sisi wote tunakujua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa fursa ya kuchangia katika hoja hii.
Kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri pamoja na timu yao nzima, kwa kazi nzuri wanayoifanya na kwa hotuba nzuri waliyoitoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kusema kwamba nafarijika sana kwamba kama Taifa, sasa tumefika tuna mjadala kuhusu matumizi ya rasilimali ya asili, ikiwemo ardhi kwa maendeleo yetu. Nafarijika kwamba sasa tuna mjadala kuhusu uhusiano kati ya mazingira na maendeleo, naamini kwamba mjadala huu unaweza kufanywa kwa busara, kwa hekima, bila jazba, wala vitisho ili tuweze kupata muafaka katika jambo hili muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, toka awali ni kwamba Serikali ya Awamu ya Tano ni Serikali ya wakulima, Serikali ya wavuvi, Serikali ya wafugaji, Serikali ya watu wanaofanya shughuli zote katika nchi hii. Asiondoke mtu na dhana hapa, kwamba Serikali ya Awamu ya Tano au Waziri katika Serikali ya Awamu ya Tano anapendelea kundi moja au lingine katika Taifa letu. Hilo siyo kweli na halipo tumechaguliwa na watu wote, tumechaguliwa na kura za Watanzania wote.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1961, kwenye Mkutano uliofanyika Arusha mwezi Septemba, Rais wa Tanganyika wakati ule Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alitoa hotuba ambayo ndiyo iliweka msingi wa uhifadhi ambao tunaendelea nao leo, Mwalimu Nyerere alisema, inaitwa Arusha Manifesto, kipande kimoja kizuri sana ambacho kwa kifupi kilisema, kwamba sisi kama Taifa tumepewa dhamana ya kuhifadhi wanyama pamoja na maeneo ambayo wanyama wanaishi na tumepewa dhamana hiyo kwa ajili ya enjoyment ya hivyo vitu, lakini pia kwa sababu ya uhai na maisha yetu yanayokuja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uhifadhi wa misitu na uhifadhi wa wanyamapori, siyo kwa ajili ya misitu, siyo kwa ajili ya wanyamapori peke yake. Hifadhi ya misitu na hifadhi ya wanyamapori una uhusiano wa moja kwa moja na upatikanaji wa mvua na upatikanaji wa mvua, una uhusiano wa moja kwa moja na maendeleo ya kilimo, upatikanaji wa mvua una uhusiano na upatikanaji wa malisho. Kwa hiyo, hifadhi ya misitu ina uhusiano na ustawi wa ufugaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, misitu inatoa huduma za kiikolojia ambazo zinafanya nchi yetu ipumue. Sasa hapa kumekuwa na mjadala, kana kwamba uhifadhi na ufugaji ni kama lila na fila hazifungamani. Uhifadhi na ufugaji siyo dichotomous, tunaweza kufanya vyote kwa wakati mmoja na tukafanya vizuri kabisa. Kuna dhana inajengwa kwamba hapa kuna ukinzani kati ya ufugaji na utalii. Msingi premise ya huo mjadala siyo sahihi. Kama Taifa tuna uwezo wa kufuga na kunufaika na ufugaji na tuna uwezo wa kuhifadhi na kunufaika na manufaa ya uhifadhi. Isijengwe dhana kwamba hizi ni shughuli zinazokinzana kwa hiyo lazima tuchague moja siyo kweli, kwa miaka yote tumekuwa tunafanya mambo yote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilio sahihi cha wafugaji ni kwamba, kila mfugaji apatiwe eneo na amilikishwe eneo la kufuga, kilio sahihi cha wakulima ni kwamba kila mkulima apatiwe eneo na amilikishwe na hii ndiyo ahadi yetu Chama cha Mapinduzi, kwamba kila mfugaji na kila mkulima atamilikishwa eneo lake ili wafanye shughuli zao kwa tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, chanzo cha migogoro inayozungumzwa siyo shughuli watu wanazofanya. Chanzo cha migogoro inayozungumzwa ni kwamba maeneo haya hayakupimwa na ndiyo maana Waziri Mheshimiwa Lukuvi alikuja katika hotuba yake na mpango mkubwa wa matumizi ya ardhi pamoja na upimaji wa ardhi ambao utapelekea kupunguza migogoro hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu cha msingi sisi kama Taifa ni kwamba shughuli zile ambazo tunaamini zinaharibu mazingira ni lazima zifanyike kwa tija. Inawezekana kabisa kwamba kwenye kilimo, katika heka moja kama tutaweza kupata tani nyingi zaidi za mahindi, basi haihitajiki ardhi kubwa zaidi ili kuweza kupata manufaa. Vilevile katika ufugaji inawezekana kabisa kwamba ukafuga katika eneo na hautalazimika kutafuta eneo lingine lakini ukanufaika na manufaa ya ufugaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili ufugaji udumu kwa miaka 100 ijayo, lazima tuhakikishe kwamba tunalinda kile tunaita natural capital. Katika dunia hii nchi zinatofautiana na utajiri wa rasilimali asili. Tanzania tunayo, inawezekana hatuna mtaji mkubwa wa kifedha, lakini tunao utajiri mkubwa wa natural capital, tunaweza tukaamua hapa Bungeni kwamba basi tufuge vizuri kwa miaka 20 ijayo, lakini baada ya hapo hakuna ufugaji tena, hakuna kilimo tena na hakuna mazingira tena. Kwa hiyo, katika mambo ambayo Serikali inayapanga kuyafanya, ni kuhakikisha kwamba shughuli hizi watu wetu wanazofanya zinadumu katika miaka mingi ijayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu mfumo wake wa kiikolojia una mito na mabonde mengi ambayo ndiyo yanafanya maisha yetu yawezekane, tunayo mito mikubwa Mto Pangani, Mto Ruvu, Mto Ruaha na mingineyo. Sehemu kubwa ya vyanzo vya mito hii ni kwenye maeneo yaliyohifadhiwa. Tukitaka Taifa letu life, mito hii itoweke, mabonde haya ambayo yana-sustain uhai wetu yatoweke, basi tusijali hifadhi ya misitu na hifadhi ya maeneo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hoja kwamba watu wameongezeka, mifugo imeongezeka, kwa hiyo basi tugawe. Ukweli ni kwamba kwa sababu hiyo kwamba watu wameongezeka ndiyo uhifadhi unahitajika zaidi. Katika nchi ndogo kisiwa Uingereza wamehifadhi asilimia 25 pamoja na kuwa na tatizo kubwa la ardhi katika ile nchi, asilimia 25 imehifadhiwa na bado maisha yanaendelea nasi kadri tunavyoendelea kama Taifa, shughuli zetu zitakuwa za tija zaidi na zitaondoka katika matumizi ya ardhi zaidi, na tutaweza ku-sustain maisha yetu bila shaka yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme hapa bila shaka yoyote, kwamba binadamu ndio tunasemekana kwamba ni wanyama wenye akili kuliko wanyama wote. Tukishindwa kuhifadhi rasilimali asili, zinazowezesha maisha yetu leo, tukishindwa kuhifadhi rasilimali asili kwa watoto wetu na wajukuu wa wajukuu wetu, basi heshima yetu binadamu kama mnyama mwenye akili kuliko wote itabidi itiliwe shaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba kuunga mkono hoja kwa kusema kwamba Serikali ya Awamu ya Tano inawajali wakulima na wafugaji katika usawa wao. Serikali ya Awamu ya Tano haipo hapa kusema shughuli hii ni bora kuliko shughuli ile nyingine, ili mradi shughuli inaendesha maisha ya watu wetu kwetu ni shughuli muhimu na tutahakikisha kwamba wanayoifanya wananufaika. Wakati huo tunahifadhi nchi yetu kwa sababu sisi tumekabidhiwa tunapita, kuna wajukuu wetu na wajukuu wa wajukuu zetu watakuja kupita, na watakuja kutushangaa, kwamba urithi tuliopewa sisi tulioachiwa na waliotuachia nchi hii, tumeuharibu kana kwamba ndiyo watu wa mwisho kuishi katika nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima kubwa nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuzungumza. Napenda nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu - Balozi Mlima, watendaji wakuu, watumishi na maafisa wote wa Wizara ya Mambo ya Nje kwa kazi nzuri wanayoifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kazi yangu ya kwanza baada ya shule nilikuwa Afisa wa Mambo ya Nje, daraja la II, chumba changu kilikuwa 132. Katika Wizara hapa nchini kwetu au taasisi zenye kiwango cha juu cha uweledi wa utendaji ni pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje. Tunayo fahari kubwa ya kusema kwamba utamaduni huo wa uweledi na professionalism umeendelea na umezidi kuimarika chini ya Waziri mpya na Serikali mpya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika vitu wanavyohitaji wenzetu wa Wizara ya Mambo ya Nje kutoka katika Bunge hili ni support, ni kuungwa mkono kwa sababu wanatuwakilisha nje ya nchi wanabeba bendera yetu. Foreign policy (Sera ya Mambo ya Nje) ni extension ya domestic policy, ni extension ya mambo tunayotaka kuyafanya, ni kiwezeshi cha malengo ya maendeleo ya Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu Serikali hii iingie madarakani sasa hazijafika siku 180. Kwa hiyo, hukumu iliyotolewa leo dhidi ya Serikali hii hasa kwenye hotuba ya Upinzani kwamba hatukufanya vizuri kwenye Sera ya Mambo ya Nje ni hukumu ambayo siyo ya haki kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yamezungumzwa mambo mengi yakiwemo masuala ya uteuzi wa Mabalozi. Kwanza nadhani Waziri pia atalieleza, procedure ya uteuzi wa Mabalozi inabidi uielewe kabla hujatoa hukumu ya aina ya Mabalozi wanaoteuliwa. Vilevile Rais Magufuli ameteua Mabalozi watatu tu tangu aingie madarakani. Amemteua Dkt. Asha Rose Migiro, Dkt. Dau na Chikawe na taratibu za uteuzi zinaeleweka na huwezi kuniambia katika hawa walioteuliwa hakuna mwenye sifa ya kushika nafasi ya Ubalozi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kusema kwamba kuna baadhi ya mambo ambayo tunaruhusiwa kuyafanyia siasa lakini suala la hadhi na heshima ya watu Rais anaowatuma kutuwakilisha nje ya nchi siyo ya kufanyia siasa. Hawa watu tunapowatuma kule nje wanabeba bendera yetu sisi, Bunge hili halipaswi kutumika kuwadhalilisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, msingi mkuu wa Sera ya Mambo ya Nje ni kulinda, kutetea na kusukuma maslahi ya Taifa katika mawanda ya kimataifa. Unapoihukumu Serikali hii katika mambo ya Sera ya Nje lazima useme ni wapi, ni lini na ni kwenye jambo gani tumeshindwa kutetea maslahi ya nchi yetu. Huwezi kuihukumu Serikali hii kwenye Sera ya Mambo ya Nje ukashindwa kusema ni kwenye jambo gani, ni lini na ni wapi tumeshindwa kulinda na kutetea maslahi ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, imani yangu ni kwamba wenzetu hawakusema hayo mambo kwa sababu hakuna, tumeweza na tumefanikiwa. Kwa sababu ingekuwepo mahali ambao tume-fail tungeona kwenye hotuba yao. Tangu Serikali hii iingie madarakani katika mikutano yote na katika forum zote ambazo maslahi ya Tanzania yalihusika tuliwakilishwa na tuliwakilishwa kwa mafanikio makubwa iwe ni Paris, New York na kwingine kokote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera ya Mambo ya Nje haiendeshwi kwenye vacuum bali inaendeshwa katika context ya sifa ya nchi, katika context ya sifa ya Rais na katika historia ya nchi. Sifa ya Tanzania duniani ni nzuri na sifa ya Rais wetu duniani ni nzuri na sifa ya Tanzania leo ni nzuri zaidi kutokana na kazi nzuri anayoifanya Rais hapa ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Rais ameamua kuweka mambo sawa hapa ndani, kazi nzuri anayoifanya ndani inazidi kufungua fursa na milango kwa nchi yetu nje na kwa Watanzania waishio nje. Moja ya nyenzo kubwa ya diplomasia ni reputation na sifa ya kiongozi. Sifa ya Rais wetu imeiongezea sifa nchi yetu, imewezesha kazi ya nje ya nchi ambayo wenzetu hawakuifanya vizuri. Kwa hiyo, unaposema Rais hasafiri wakati huo huo kazi anayoifanya inawezesha Sera yetu ya Mambo ya Nje iende vizuri kunakuwa hakuna mantiki hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba moja ya matunda ya kazi nzuri ya Wizara ya Mambo ya Nje ni kwamba sasa hivi sisi tuko kwenye viwanda, ndiyo msingi mkuu wa mpango wetu wa maendeleo ya miaka mitano. Nchi ya China imechagua nchi nne Afrika ambapo itahamishia sehemu ya viwanda vyake. Nchi hizo ni Ethiopia, Kenya, South Africa na Tanzania. Hilo halikutokea kwa ajali, halikutokea kwa kurusha karata, limetokea kutokana na jitihada nzuri za wenzetu wa Wizara ya Mambo ya Nje na limetokana na kazi nzuri anayoifanya Rais wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya urithi tunaoachiwa na viongozi waliotutangulia ni sifa ya nchi. Moja ya wajibu wetu viongozi wa siasa bila kujali vyama ni kuulinda urithi. Tunao wajibu Wapinzani na sisi kwenye Serikali na Chama Tawala kulinda urithi tulioachiwa na waliotangulia kwenye nchi hii.
Unapoitukana nchi yako ndani ya Bunge unajitukana wewe nje kwa watu tunaowawakilisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mchezo mmoja wa Shakespeare unaitwa Macbeth na nataka nizungumze kwenye quote moja kwenye act five inasema:-
“Life is but a walking shadow, a poor player,
That struts and frets his hour upon the stage,
And then is heard no more.
It is a tale told by an idiot, full of sound and fury,
Signifying nothing”. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba ya Kambi ya Upinzani Bungeni is full of sound and fury amounting to nothing. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalize kwa kuzungumzia suala alilolizungumzia Mheshimiwa Jaku na Mheshimiwa Keissy Mohamed. Nchi yetu sisi ni ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar. Baadhi ya kauli tunazozitoa humu ndani lazima ziheshimu Muungano wetu. Mheshimiwa Keissy Mohamed ni Mbunge wa CCM lakini lugha aliyoitumia sisi kama Serikali hatuikubali na Mheshimiwa Jaku vilevile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inafanya mambo makubwa matatu katika concern walizoleta. Kwanza, Ofisi ya Rais, Utumishi imetoa Waraka wa kuwezesha taasisi za Muungano zitengeneze utaratibu wa mgawanyo wa watumishi wa umma kutokana na quota iliyokubalika ya asilimia 79 na 21. Nimewaandikia Mawaziri wenye taasisi za Muungano kuhakikisha kwamba tunatimiza agizo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, Tume ya Pamoja ya Fedha ilitengeneza mapendekezo kuhusu mgawanyo wa mapato na vyanzo vya mapato ya kuchangia shughuli za Muungano. Tumetengeneza Waraka wa Baraza la Mawaziri kwa ajili ya mgawanyo mpya kupitiwa ili tuweze kupata mgawanyo unaoakisi ukubwa wa uchumi na idadi ya watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, sasa hivi Zanzibar kwa makubaliano inaweza kutafuta misaada yake yenyewe nje ya Tanzania. Hayo ni mafanikio makubwa yaliyotokana na Serikali yetu katika kuimarisha Muungano wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri na timu yake na naunga mkono hoja hii.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa fursa ya kuchangia. Kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara; kwa kazi nzuri waliyoifanya katika kuandaa bajeti hii. Nawapongeza sana Wabunge wa CCM kwa kutimiza wajibu wao waliotumwa na wananchi wao kwa kutimiza sababu yao ya kuchaguliwa kwa kuingia Bungeni kufanya kazi waliyotumwa na wananchi na kueleza shida za wananchi wao mbele ya Serikali, nawapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yako mambo kadhaa ambayo ningependa kuyazungumzia, la kwanza ni suala la VAT kwa Zanzibar na Bara. Kuna upotoshaji mkubwa sana kwamba hatua iliyochukuliwa na Serikali, hatua nzuri kabisa ya kuhakikisha kwamba bidhaa zinazozalishwa Tanzania Bara kwenda Zanzibar VAT inakusanywa Zanzibar; na bidhaa zinazozalishwa Zanzibar na kuletwa Tanzania Bara VAT inakusanywa Tanzania Bara. Kuna upotoshwaji mkubwa sana unaofanywa na wenzetu kule Zanzibar kwamba hatua hiyo inaiumiza Zanzibar, si kweli, ni kunyume chake. Hatua hii inainufaisha Zanzibar, hatua hii itawaumiza wale wadanganyifu wachache, waliokuwa wanatumia utaratibu huu kujipatia kipato ambacho sio halali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, ambalo ningependa kulizungumzia ni ahadi ya Chama cha Mapinduzi kwenye Ilani yetu kwamba kila kijiji kitapatiwa shilingi milioni 50 kwa ajili ya uwezeshaji, ukopeshaji wa wajasiliamali. Ahadi hii ya CCM ni hatua kubwa ya kimapinduzi ya kumuondoa Mtanzania katika lindi la umaskini. Mzunguko wa shilingi milioni 50 katika kijiji ni pesa nyingi sana zitakazoleta chachu ya maendeleo pale kijijini. Serikali katika mwaka huu wa fedha kama ambavyo mmeona, imetenga shilingi bilioni 59 kama kianzio, lakini zaidi ya hapo Serikali imeunda jopo la wataalam ambalo linatengeneza utaratibu madhubuti kabisa. Utaratibu utakaozingatia uzoefu wetu huko nyuma wa mifuko mbalimbali na mafanikio ya mifuko hiyo ili tuwe na utaratibu mzuri utakaohakikisha fedha hizi zinatumika kama zilivyopangwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hili ni jambo kubwa linabidi lifanyike kwa umakini na umahiri mkubwa ili tusipoteze fursa hii adhimu katika kuwaokoa watu wetu. kwa hiyo utaratibu mzuri unaotengenezwa na Serikali utaletwa hapa Bungeni ili kabla ya kutumika na ninyi Waheshimiwa Wabunge muwe na mchango wenu katika aina ya utaratibu ambao Serikali itautumia na ikiwezekana kabisa aidha ni kwa kuleta Sheria mpya au kufanya mabadiliko ya Sheria katika Sheria ya Uwezeshaji sasa hivi. Ili fedha hizi ziwe katika msingi wa kisheria na ziweze kutumika vizuri kuliko mifuko mingine yote huko nyuma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukweli kwamba zimetengwa shilingi bilioni 59, haina maana kwamba tutashindwa ndani ya miaka mitano kufanya vijiji vyote; tumeweka hizi ili tuanze na tujifunze na kadri tutakavyokuwa na utaratibu mzuri, kasi ya kupanga fedha nyingi zaidi ili tutimize ahadi hii kwa miaka mitano inakuwepo. Kwa hiyo napenda kuwahakikishiwa Waheshimiwa Wabunge na watanzania, kwamba hii ni ahadi ya CCM, hii ni ahadi ya Rais na itatimia bila shaka yoyote.
Naomba niseme kidogo jambo moja muhimu. Sisi Chama cha Mapinduzi tulipomteua Dkt. John Pombe Magufuli kuwa mgombea wetu, tulitoa statement duniani kwamba tunahitaji aina mpya ya nchi kutokana na aina ya kiongozi huyo. Kwetu sisi kumteua yeye tulitoa kauli duniani kwamba tunataka mabadiliko ya kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mabadiliko ya kweli hayawezi kuletwa kwa hatua ndogo ndogo, mabadiliko ya kweli yanaletwa hatua kubwa na yanaletwa na uthubutu na uthubutu huo umeanza kujidhihirisha katika bajeti ya mwaka huu, tumethubutu kwamba tunaweza kukusanya shilingi trilioni 29.5; tumethubutu kwamba tunaweza kutenga asilimia 40 kati ya hizo kwa maendeleo. Unapothubutu jambo kubwa kuna watu watatia shaka, sisi wana CCM Serikali hii ni ya kwetu, Bunge hili ndio wengi, ilani ni ya kwetu, tusitetereke katika uthubutu wetu wa kukusanya shilingi bilioni 59 tumsaidie Rais tuisaidie nchi yetu kufikia malengo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, imezungumzwa suala la hatua za kikodi hapo mbalimbali imetokea malalamiko kwamba kodi ni kubwa, kodi ni nyingi zitadhohofisha uwekezaji. Jambo hilo si la kweli kwa sababu utafiti unaonyesha mimi hapa ninayo ripoti inaitwa Tax incentive in a global perspective inasema kwamba; survey analysis shows that host country taxation and international investment incentives generally play only a limited role in determining the international pattern of FDI. Factors like market characteristics, relative production costs and resource availability explain most of the cross-country variation in FDI inflows. Transparency, simplicity, stability and certainty in the application of the tax law and in tax administration are often ranked by investors ahead of special tax incentives.
Suala siyo kiwango cha kodi, suala ni mfumo wa kodi. Kwa hiyo, miaka yote tumeaminishwa kwamba ukiweka kodi ndogo wanakuja, ukiweka kodi kubwa hawaji, dhana hiyo si ya kweli. Ukitengeneza mambo mengine vizuri zaidi ndiyo wanakuja ikiwemo uhakika wa mfumo wa kodi. Kwa hiyo, tusiwatishe wananchi na tusitishane hapa kwamba kiwango cha kodi tulichoweka kitafukuza wawekezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ngoja nimalize kwa kusema kwamba Rais Magufuli tumempa usukani wa kuiongoza nchi yetu, lakini nchi hii ni yetu sote na sisi tunawajibu wa kumsaidia ili tufanikiwe. Rais Magufuli akifanikiwa, nchi yetu imefanikiwa sisi tusiwe kama watazamaji kwamba ngoja tumuone atafanyaje, sisi tuko naye kwenye basi hili tumsaidie. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hatua tunazochukua nchi yetu ni sawasawa na gari nzuri aina ya benzi iliyoingia kwenye matope tunataka kuirudisha kwenye lami, hatua ya kuirudisha kwenye lami itakuwa na misukosuko, kuna wengine wataamua kushuka lakini tuendelee kuwa ndani ya gari hilo mpaka likae kwenye lami lifike safari. Maendeleo yanahitaji sacrifice, katika bajeti hii Wabunge sisi tume-sacrifice, tume-sacrifice kwa kukubali kukatwa kodi, kila mtu lazima a-sacrifice, wafanyabiashara, waendesha bodaboda, kila mmoja lazima a-sacrifice ili nchi yetu iende mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalize kwa kusema mwaka 1961 wakati Rais Kennedy wa Marekani anaapishwa aliwaambia wa Marekani kwamba ask not what your country can do for you, but what you can do for your country. Ni wakati sasa kwa Watanzania wote kutokaa siku zote na kujiuliza nchi hii itanifanyia nini bali sisi tutaifanyia nini nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa fursa ya kutoa mchango. Kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Hawa Ghasia pamoja na Kamati yake kwa kazi nzuri waliyoifanya naunga mkono hoja waliyoitoa na mapendekezo waliyoyapendekeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wote tunafahamu kwamba Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliongoza nchi yetu hii kwa miaka 24 na tangu ametutoka ni miaka 17 na siku zote bado amebaki kuwa rejea ya masuala mbalimbali ya uongozi wa Taifa letu na kwa kweli amekuwa kama sehemu ya uongozi wa nchi kwa maana ya reference hata akiwa kaburini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini imekuwa hivyo? Je, ni kwa sababu ameifikisha nchi yetu kule kwenye ndoto kabisa ya maendeleo makubwa ya kiuchumi, hapana. Ni kwa sababu dhamira yake ya kutufikisha huko ilikuwa wazi na ilieleweka pamoja na kwamba hatukufika kule tulikokuwa tunatarajia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais Dkt. Magufuli sasa hivi ana miezi 15 tu ya uongozi wake. Dhamira ya kutupeleka kwenye nchi ya neema hamna mtu yeyote anayeweza kubisha katika Bunge hili kwamba ipo. Dhamira iko wazi, ni nzuri na inaeleweka.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais wetu sasa hivi na Serikali ya Awamu ya Tano ina miezi 15 tu madarakani kati ya miezi 120 ambayo tunatarajia Rais aiongoze nchi yetu. Leo tunachojadili ni robo tu ya bajeti ya kwanza kamili ya Serikali ya Awamu ya Tano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo, hamna ubishi kabisa kwamba kuna improvement kwenye kila eneo la utendaji wa Serikali na unapojenga misingi, unapoimarisha misingi ili mbele iwe rahisi kabisa kutengeneza mambo yawe rahisi nafahamu kuna watu watapata shaka watakuwa na uwoga, watapinga. Naamini kwamba nchi hii ni yetu sote na wakati mwingine unasikitika kwamba inapotolewa habari mbaya hapa Bungeni au habari ya kusikitisha, kwa mfano tunaposema Benki fulani imepata hasara nashangaa kuna watu wanapiga makofi kana kwamba hiyo ni habari ya kufurahisha. Nchi hii ni nchi yetu sote, habari ya kusikitisha ni yetu sote. Wawe Wapinzani, wawe watu wa CCM.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tusifike mahali tukaamini kwamba mambo yanapotokea na kunapotokea setbacks basi kuna watu wanapaswa kufurahia. Nchi hii ni yetu sote, watu tunaowaongoza ni wetu sote, hivyo, naamini kabisa kwamba mtu yeyote mwenye akili timamu hawezi akasimama leo akasema nchi yetu imerudi nyuma badala ya kwenda mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna ndugu amesimama amezungumza kuhusu Zanzibar kwamba kuwe na mazungumzo, tukae, kaka yangu Mheshimiwa Mtulia. Sasa uchaguzi Zanzibar ulikwishafanyika, Serikali ilishapatikana, Serikali halali, imechaguliwa kwa kura halali na ni muhimu kutambua kwamba Serikali ile ni ya Umoja wa Kitaifa kwa sababu kuna vyama vinne ndani ya Serikali ile na Serikali ile iko tayari kuzungumza…
MWENYEKITI: Malizia, malizia.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba unilinde muda wangu umeliwa.
Wenzetu watusaidie kwamba tuzungumze na nani kwa sababu CUF ziko mbili, tuzungumze na ipi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuzungumze na ile iliyochukua ruzuku au ile nyingine?
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa na mimi kuchangia hoja hii ya Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuipongeza Kamati na Mwenyekiti na Kamati nzima kwa kweli kwa ripoti nzuri waliyoiandika, kwa mapendekezo mazuri, lakini pia kwa ujumla kwa kazi nzuri wanayoifanya kuisadia Serikali wakati wote ambapo tumekuwa tunafanya nao. Kamati hii imesheheni wanamazingira, wanafahamu changamoto zilizopo na wamekuwa wanatusaidia vizuri sana katika kufanya kazi zetu. Nawapongeza na nawashukuru sana. (Makofi)
Waheshimiwa Wabunge, kwanza tumepokea mapendekezo ya Kamati, ni mazuri na mimi nayaunga mkono, lakini pia tumesikia michango ya Wabunge kuhusu masuala ya mazingira. Wabunge wote waliochangia kuhusu eneo hili wamesema hali ya mazingira nchini ni mbaya na mimi nataka niseme kwamba hali ya mazingira nchini ni mbaya sana, si tu ni mbaya, ni mbaya sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maji katika nchi yetu ni rasilimali kubwa, ukitazama mito, vijito, mabwawa, chemichemi, kila mwaka unaopita tunapata changamoto ya upatikanaji wa maji, kwenye ardhi rutuba inapungua, matumizi yasiyozingatia kanuni za masingira, misitu inateketea, mvua hazitabiriki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mwaka hapa tunakutana kupanga maendeleo na kupanga maendeleo na kupanga fedha za maendeleo. Ile shughuli za kupanga maendeleo na kupanga fedha za maendeleo itakuwa haina maana kabisa kama hatutazingatia umuhimu wa kuhifadhi mazingira kwenye sekta zote. Ukitaja kilimo, hakiwezekani kuwa na manufaa kama hakizingatii mazingira. Afya, elimu, maji, utalii, hakuna sekta isiyoguswa na mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maendeleo ya nchi yetu yana mahusiano moja kwa moja na hifadhi ya mazingira lakini pia hata uwezeshwaji wa wanawake (women empowerment) na yenyewe moja kwa moja ina uhusinano wa hifadhi ya mazingira. Tunapozungumza ukosekanaji wa maji unaotokana na changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi wanaoathirika zaidi ni akina mama. Tunapozungumza suala la nishati ya kupikia, wanaotumia muda mrefu kwenda kutafuta kuni na hata wakati mwingine kuingia katika mazingira hatarishi huko porini ni akina mama na ndiyo maana sikushangaa kwamba Wabunge waliochangia kwa sehemu kubwa kwenye mazingira ni akina mama, Mheshimiwa Leah Komanya, Mheshimiwa dada yangu mpendwa sana Hawa Bananga, Dkt. Christine Ishengoma, Mama Mwanne Mchemba kwa sababu ni jambo linalowagusa akina mama sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme kwamba tumepokea mapendekezo na tumeyakubali na tunapenda Bunge litusaidie kwa sababu Bunge ndilo linalogawa fedha, Bunge ndilo linaloamua fedha kiasi gani ziende katika maeneo gani. Waheshimiwa Wabunge, mkiamua ninyi kwamba Mfuko wa Mazingira katika mwaka ujao wa fedha uwe na shilingi bilioni 200 badala ya sifuri mnaweza kufanya hivyo. Sisi tulipanga katika bajeti iliyopita, tulijadiliana ndani ya Serikali lakini na hapa Bungeni kuhusu uwezekano wa mfuko wetu kupata vyanzo vya moja kwa moja kwenye tozo mbalimbali ili uweze kuwa na fedha nyingi zaidi ili mimi kama Waziri mwenye dhamana ya Mazingira nikipita kwenye majimbo nikiona unahitaji miche 10,000 niwe na uwezo wa kukupatia miche 10,000. Nikiona unahitaji kwa kupitia Mfuko wa Mazingira, vyanzo vya maji vitunzwe kwenye jimbo tuweze kufanya hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo napenda nirudishe changamoto hii kwa Waheshimiwa Wabunge kwamba tunaelekea kwenye bajeti na kama kweli tunaamini mazingira ni muhimu basi pale tuoneshe kwa vitendo kwamba Mfuko wa Mazingira upate vyanzo vyake vya moja kwa moja kama ambavyo mfuko wa barabara unapata vyanzo moja kwa moja, kama ambavyo Mfuko wa Nishati unapata vyanzo moja kwa moja na mifuko mingineyo, mtakuwa mmetusaidia na mtakuwa mmeisaidia nchi yetu sana. Kwa hiyo ndugu zangu bila fedha hifadhi ya mazingira ni jukumu la moja kwa moja la msingi la Serikali. Sekta binafsi inaweza kushiriki kwenye hifadhi ya mazingira lakini hatuwezi kubinafsisha hifadhi ya mazingira. Lazima sisi kama Bunge tupange fedha ili zitumike huko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wengi wamezungumzia kuhusu tatizo la mkaa. Tumeamua sisi kama Serikali kwa kushirikiana na wenzetu wa Wizara ya Maliasili na Utalii kukabiliana na changamoto hii. Sasa hivi tutaleta mapendekezo; tozo kwenye kila gunia la mkaa ni shilingi 16,000 za TFS; labda Halmashauri inaweza na yenyewe inaweza ikacharge shilingi 2,000. Tunataka tuongeze kodi kwenye mkaa ili tuweze kupata fedha nyingi zaidi na tutapenda fedha hizo ziingie kwenye mfuko wa mazingira. Tungependa Wabunge mtusaidie tuamue na Waziri wa Fedha yuko na mazungumzo yanaendelea Serikalini; kwamba zile teknolojia ambazo zinasaidia uhifadhi wa mazingira basi zisamehewe kodi ili gesi iwe bei rahisi, majiko ya gesi yawe bei rahisi ili wananchi wa kawaida waweze kuyamudu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mradi wa maji Simiyu, Mheshimiwa Naibu Waziri amezungumza vizuri ila nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba moja ya nyenzo ambazo tumeamua kuzichukua kama Ofisi ya Makamu wa Rais ni kutumia hii mifuko mikubwa ya kifedha ya kimataifa kupata fedha kwa ajili ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi lakini fedha hizo kuziingiza kwenye miradi ya maendeleo. Kwa mfano, kwa uhakika kabisa Mkoa wa Simiyu utapata shilingi bilioni 200 kwa ajili ya upatikanaji wa maji kutokana na Mfuko wa Mazingira wa Dunia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka kwenye maeneo yote yenye ukame kama Serikali tujenge hoja kwamba ukame ule unatokana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Kwa hiyo, fedha inazosaidiwa Tanzania kwenye kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi tuzipeleke kwenye maeneo kama hifadhi ya maji, kilimo cha umwagiliaji na kadhalika. Tukifanikiwa katika mwezi huu wa tatu unaokuja kupata fedha hizo shilingi bilioni 200 itafungua mlango wa kupata dola milioni 800 kwa ajili ya maji katika nchi yetu. Huu ni mradi ambao tunaufatilia kama Ofisi ya Makamu wa Rais na tutafanikiwa, tutakapofanikiwa basi wetu tutakuwa tumewapunguzia kero.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ukataji wa miti na kilimo cha kuhamahama, nimesikia nilipata nafasi ya kufanya ziara ya mikoa kumi katika nchi yetu na baada ya Bunge hili tutazunguka katika mikoa yote siyo tu kukagua hali ya uharibifu wa mazingira bali kuchukua hatua wakati ule ule tutakapoona kuna uharibifu wa mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kule kwenye tumbaku Tabora, tumeamua sasa kupiga marufuku matumizi ya yale mabani ya zamani ya kienyeji ambayo yanatumia magogo mengi na kupelekea ukataji wa miti na misitu ya nchi yetu. Ningependa Bunge lako liwe ni Bunge la wanamazingira. Naomba tusaidiane sana, Waheshimiwa Wabunge mkiishika ajenda ya mazingira tutatoka, pamoja na kwamba inawezekana athari za uharibifu wa mazingira zisionekane papo kwa papo lakini madhara yake huko mbele yatakuwa maisha magumu sana kwa Watanzania. Kwa hiyo, tuna uwezo wa kuweka historia kama Bunge la kwanza lililoweka fedha nyingi zaidi kwenye hifadhi ya mazingira na kuyaokoa mazingira ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakuja hapa kila mwaka tunaomba fedha nyingi kwenye bajeti ya maji, lakini unaweza kuomba fedha na kujenga miundombinu ya maji kama hatukupanga fedha za kuhifadhi vyanzo vya maji tutakuwa tumepoteza fedha kwenye kujenga mabomba ya maji wakati kule maji yanakotoka hatujayahifadhi.
Kwa hiyo, katika shughuli zote ambazo tunazipanga katika Bunge hili mazingira ndiyo msingi wake na Serikali tunaishukuru sana Kamati kwamba jambo hili imeliona na inalishughulikia, tunategemea sasa spirit hii ya Kamati basi Bunge zima na yenyewe italichukua ili itakapofika wakati wa bajeti basi wote tuzungumze kwa kauli na sauti moja ili tuweze kuisaidia nchi yetu.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nashukuru sana kwa fursa hii, naishukuru tena Kamati na ninawashukuru wote mliochangia kwenye hoja hii.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nianze kwa kuzipongeza Kamati zote mbili kwa kazi nzuri walizofanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niongezee kwenye maelezo ya Naibu Waziri wa Afya kuhusu suala la viroba na vifungashio vya plastiki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili liko chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais na kanuni tuliandika kwa sababu linapigwa marufuku kwa kanuni za chini ya Sheria ya Mazingira. Suala hili ni mtambuka, lina upande wa kodi, kwa maana ya Wizara ya Fedha, lina upande wa viwanda, Wizara ya Viwanda na Biashara, lina upande wa Wizara ya Afya kwa maana ya TFDA na Udhibiti wa Vyakula na Vinywaji, lakini pia upande wa mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunachofanya sasa ni Wizara zote kuandika karatasi ya pamoja ambayo itawezesha hatua tutakazochukua ziweze kutekelezwa kwa msukumo na mtazamo wa pamoja na kutapatikana balance kati ya haja ya kuhakikisha kwamba mapato yanaendelea kupatikana kwa nchi, lakini tunalinda afya za watu wetu na mazingira ya watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, suala hili linataka tafakuri ya kina ya pamoja ndani ya Serikali na ndiyo kinachofanyika na taarifa rasmi ya mwisho ya maamuzi hayo italetwa ndani ya Bunge hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru kwa kunipa nafasi.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii na nakupongeza kwa namna ambavyo umetuongoza tangu asubuhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kutoa shukrani kwa wote waliochangia katika hoja yetu, kwanza kwa Kamati zote mbili, lakini pia kwa wasemaji wote wawili wa Kambi ya Upinzani kwenye masuala ya Muungano na Mazingira. Tumepokea maoni ya Waheshimiwa Wabunge wote, kwa heshima na taadhima na moyo mkunjufu na ushauri mlioutoa tutaushughulikia. Wamechangia Wabunge 57 na kwa kweli kwa hoja ya siku moja kwa Wabunge 57 ni wengi, inaonyesha ni jinsi gani ambavyo kuna hamasa kubwa katika mambo haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna baadhi ya mambo ambayo tutayatolea majibu sasa na kuna mengine tutayatolea majibu kwa maandishi na kuwapelekea Waheshimiwa Wabunge kwa sababu muda tulionao hapa hautatutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimefurahi na kufarijika kwamba yanapokuja masuala ya mazingira Waheshimiwa Wabunge wote wa upande huu na upande ule tunaungana. Kwa hiyo, napata faraja kwamba katika vitu vinavyoliungasha Bunge ni hifadhi ya mazingira. Hiyo inafanya kazi yangu iwe rahisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninao marafiki wengi kwa upande ule kwa sababu ya masuala ya mazingira. Wapo watu ambao wanaonekana ni wakorofi kwa upande mmoja, lakini ukiingia ndani ya nyoyo zao ni wanamazingira wazuri sana hata Mheshimiwa Halima Mdee ni mwanamazingira mzuri sana, kwa hiyo, nawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, imani yangu ni kwamba kwa kadri siku zinavyoenda kila Mbunge atakuwa mwanamazingira na hili linatupa faraja kubwa sana. Hii inatokana na hali halisi ambayo Waheshimiwa Wabunge wanaiona katika majimbo yao na huko wanakoishi kuhusu uharibifu wa mazingira. Imani yangu ni kwamba hamasa hii itapelekea uwekezaji mkubwa katika hifadhi ya mazingira nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende haraka haraka kwenye hoja zilizotolewa. Kwanza, ni Mfuko wa Mazingira. Watu wengi wamezungumza kuhusu hili na nimesikitika kidogo dada yangu Mheshimiwa Dkt. Immaculate Sware ametulaumu kwamba miaka yote mfuko upo haujaanza, nilidhani kwamba angesema hongereni angalau kwa kuanza mwaka huu na ningependa utupe moyo na utuunge mkono kwa sababu ndio tumeanza na tunahitaji support yako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wengi wameongelea namna ya kuupatia mfuko fedha. Sheria iliyoanzisha mfuko huu iko wazi kabisa vyanzo vimeainishwa humu. Katika nchi yetu zipo shughuli za kiuchumi na kiuzalishaji mali ambazo zinapelekea uharibifu wa mazingira. Kwa mfano, biashara ya mkaa ambapo Serikali inapata mapato, lakini biashara ile inaharibu mazingira; biashara ya magogo, Serikali inapata mapato lakini biashara ile inaharibu mazingira; uingizaji wa magari chakavu, Serikali ina-charge zaidi kwa shughuli hiyo lakini fedha hii haiji kwenye mazingira na uchimbaji wa madini vilevile kwenye leseni kuna fees zinatolewa. Kwa hiyo, sisi tunaongea na wenzetu wa Wizara ya Fedha kuona ni namna gani katika hizi shughuli ambazo zinaharibu mazingira lakini Serikali inapata tozo basi sehemu ya tozo ije kwenye Mfuko wa Mazingira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia Sheria ya Mazingira katika kifungu cha 213 kinaelezea sources of funds kwa mazingira na kinasema; “(a) such sums of money as may be appropriated by Parliament.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu hizi kinawapa nguvu Waheshimiwa Wabunge kuujaza mfuko huu pesa. Kwa hiyo, hatuna sababu ya kulalamika kuhusu fedha kidogo kwenye hifadhi ya mazingira wakati sisi wenyewe Wabunge tuna uwezo wa kuwa-appropriate pesa kwa ajili hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, imezungumzwa hapa kuhusu suala la Baraza la Rufani. Na mimi nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge aliyesema kwamba Waziri siyo kazi yako kupiga faini, ile ni kazi ya Mkaguzi wa Mazingira na imeandikwa kwenye sheria. Nakubaliana kabisa na yaliyoelezwa kwamba wewe ni mamlaka ya rufaa kwa anayepigwa faini na hata mimi nikifanya kitendo kile naweza kukatiwa rufaa kwenye Baraza la Rufaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini moja ya changamoto ya kutokuwepo kwa Baraza ni mfuko huu kutokuwa na pesa kwa sababu ukienda kwenye sheria kifungu cha 205 vyanzo vya fedha za Baraza la Rufani kinasema ni Mfuko wa Mazingira. Kwa hiyo, kama Mfuko wa Mazingira hauna fedha Baraza la Rufani halipo. Kwa hiyo, utaona kuna muunganiko wa ujenzi wa kitaasisi wa hifadhi na usimamizi wa mazingira. Kwa hiyo, tukilimaliza suala la Mfuko wa Mazingira tutakuwa tumemaliza suala la Baraza la Rufani vilevile. Nadhani Mheshimiwa Gekul ndiye aliyezungumzia jambo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla kuhusu fedha kidogo kwenye hifadhi ya mazingira ukweli upo wazi, wote mnaona. Jawabu ni moja kupanga fedha zaidi na pili kuujaza mfuko. Hata hivyo, kuna jambo lingine tumelifanya na nimesema kwenye hotuba kwamba mwaka huu sasa tumefanikiwa kila Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Sekretarieti ya Mkoa na Wizara itakuwa na kifungu kwenye bajeti kinaitwa kifungu cha hifadhi ya mazingira kwa sasa hakuna. Wenzetu watakapokuwa na vifungu hivyo wataamka na kupanga shughuli za hifadhi za mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tunahangaika kutafuta ufadhili kwenye hifadhi ya mazingira kutoka kwa wenzetu sehemu mbalimbali. Tumeeleza asubuhi kwamba kwa jitihada za ofisi yetu tumeweza kufanikisha upatikanaji wa shilingi bilioni 230 kwa ajili na mradi wa maji. Tunaendelea na nataka niwahakikishie kama Mungu akipenda na kama tutaendelea kuwepo kwenye nafasi hizi nikisimama tena hapa mwakani, nitakuja na habari nzuri zaidi kuhusu upatikanaji wa fedha nyingi zaidi kutokana na ufadhili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu viroba Mwanasheria Mkuu ameliongelea sina haja ya kurudia sana lakini napenda kukumbusha tu kwamba Serikali ilitoa taarifa ya kwanza kabisa ya dhamira yake ya kupiga marufuku viroba na mifuko ya plastiki Bungeni hapa kwenye bajeti ya mwaka jana mwezi Mei na mpaka shughuli ile imesimamishwa ilikuwa Machi 1 ni miezi kumi. (Makofi)
Kwa hiyo, sikubaliani kabisa na hoja kwamba hakukuwa na taarifa ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilichokuwepo ni kwamba wenzetu kwa kuzoea ile habari kwamba Serikali ikisema haitendi kuna watu kabisa waliingiza mitambo wakatengeneza stock mpya. Ukienda kwenye Hansard hapa Bungeni utaona hilo, lakini tarehe 16 Agosti, pia tukatoa taarifa kwa umma kwamba tutapiga marufuku viroba tarehe 01 Januari 2017, lakini unakutana na mtu anakuambia mimi nimeingiza mzigo juzi. Sasa kama unaagiza mzigo wakati ukiwa na taarifa kwamba Serikali ina dhamira gani kuhusu biashara hiyo yanayokukuta ni kwamba umeamua wewe mweyewe yakukute. Licha ya hivyo, Serikali itaendelea kufanya mazungumzo na wafanyabiashara hawa ili kuangalia utaratibu nzuri wa namna ya kumaliza kabisa shughuli hii. Wote tunakubaliana kuna manufaa makubwa zaidi kwenye kupiga marufuku shughuli hii kuliko kuacha iendelee, hilo halina ubishi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu upandaji miti, Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumza kuhusu utaratibu wa upandaji miti hapa nchini. Tunafahamu kwamba tangu uhuru nchi yetu imefanya jitihada mbalimbali za kupanda miti, lakini hatukupa mafanikio ya kuridhisha. Mkakati mpya tulioutengeneza umezingatia sababu za kufeli kwa mipango ya siku za nyuma, umeshirikisha sekta binafsi na mamlaka zote, tumeandika kila kata hapa nchini inastawi mti gani na unapaswa kupandwa wakati gani. Mkakati huo tutautoa kwa ajili ya kuelimisha Wabunge na wananchi jinsi ya kuutekeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hapa nchini idadi ya miti yote iliyopo asilimia kumi tu ndiyo ya kupanda asilimia 90 ndio miti ya asili inayoota yenyewe. Kwa hiyo, namna nzuri ya kuwa na miti hapa nchini ni kuhifadhi ile ambayo tunayo tayari, ile miti ya asili. Kwa sehemu kubwa nchi yetu ina miti ya miyombo ambayo inaamka kwa haraka zaidi pale inapoachwa ikue. Kwa hiyo, kikubwa zaidi ni kuacha kupanda miti na kupanda miti vilevile lakini matumaini makubwa yapo kwenye kuhifadhi miti na misitu tuliyo nayo. Ipo miradi mingi zaidi na taratibu nyingi tutazitumia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, dada yangu Mheshimiwa Pauline amesema asubuhi kwamba kuna harufu ya kifisadi kwenye baadhi ya miradi, lakini hakutusaidia kwamba ni katika eneo gani hasa kwa sababu ufisadi upo wa namna nyingi. Je, ni kwenye procurement au malipo? Namwomba hata kwa kuninong’oneza anieleze ili nilishughulikie jambo hili kwa sababu ni jambo hatutaki liwepo kwenye ofisi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwakikishie kwamba miradi hii kwa masharti ya ufadhili wake kila mwaka inakaguliwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali. Kumefanyika ukaguzi 2013/2014, 2014/2015 na ripoti ya 2016 inakuja na wamejiridhisha kabisa kwamba miradi ile iko safi kabisa na inatekelezwa kwa kiwango kilichotarajiwa. Kwa hiyo, sisi tunaamini kabisa kwamba hakuna tatizo lolote lakini kama dada yangu Mheshimiwa Pauline una taarifa naomba unijulishe ili nianze kufuatilia hapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumzia kuhusu matumizi ya mkaa. Matumizi ya mkaa ni changamoto kubwa na ni sababu kubwa inayopelekea uharibifu wa mazingira nchini mwetu. Sisi kama Ofisi ya Makamu wa Rais tumeamua kuchukua leadership kwenye jambo hili kwa sababu ndugu yangu na mzee wangu Mheshimiwa Profesa Maghembe mkaa kwake ni chanzo cha mapato, wakati mimi kwangu mkaa ni uharibifu wa mazingira. Mimi nina interest kubwa zaidi nchi yetu ika- transition kutoka kwenye matumizi ya mkaa kwa sababu kwa kadri siku zinavyoenda nishati za kupikia mbadala zinaendelea kuwa nafuu na zinaweza kushindana kwenye soko la mkaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tulifanya kongamano kubwa ambalo tuliliongoza na wadau wote wa utengezaji wa mkaa. Tumeamua kuanzisha shindano kubwa kabisa la kitaifa na wale majasiriamali wote wanaoweza kutengeneza nishati mbadala waje watuonyeshe tutawapa zawadi. Zawadi ya kwanza kabisa itakuwa zaidi ya shilingi milioni 400 na tutawawezesha kupanua biashara yao hiyo, viwanda vya mkaa vitaanzishwa ili taratibu tuondoe mkaa kwenye soko siyo kwa kuupiga marufuku bali kwa kuufanya ushindwe kwa bei na nishati nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu kwamba kuna Wakuu wa Wilaya na baadhi ya maeneo wamepiga marufuku usafirishaji wa mkaa kutoka kwenye maeneo yao ni hatua njema. Hata hivyo, lazima twende nayo taratibu kwa sababu mji kama Dar es Salaam ambapo asilimia 60 ya mkaa unatumika Dar es Salaam na pale hakuna sehemu unaweza kuzalisha mkaa, kwa hiyo, lazima tuwezeshe watu kupata nishati inayolingana na bei ya mkaa ndipo tuweze kupinga marufuku kabisa matumizi ya mkaa. Huko ndiko tunakoelekea, hii road map ambayo tunakuja nayo itaeleza miaka mingapi na kwa utaratibu gani tutaondoa matumizi ya mkaa hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niseme tu pia katika mkaa unaozalishwa nchini kwa sehemu kubwa mkaa huo unakwenda kuchoma nyama Uarabuni. Ukienda kwenye bandari zile za Bagamoyo, Mbweni majahazi na majahazi yamejaa mkaa unaenda Unguja. Unguja haiwezi kutumia mkaa wote ule unaoenda kule, ukifika Unguja unapanda tena unaenda Mombasa - Shimoni. Ukifika kule unawekwa kwenye magunia mazuri made in Kenya unaenda kuchoma nyama Uarabuni. Nataka niombe ruhusa ya Mheshimiwa Rais niende Kenya nikazungumze na wenzetu ili tuweze kuona namna gani tunaweza kushirikiana pamoja na Wizara Maliasili kupiga kabisa marufuku suala hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wengi wameongelea kuhusu namna tunavyoweza kuzibalisha taka ngumu ziwe rasilimali. Sisi kwenye ofisi yetu hazipiti wiki mbili tunapokea mwekezaji, mapendekezo, proposal ya mtu anayetaka kuzalisha umeme kwa kutumia taka. Bahati mbaya sana hawa watu wanaoleta hii miradi wanazunguka sana hawajui pa kuanzia. Wengine wanaanzia TANESCO, wengine Wizara ya Nishati, wengine TAMISEMI, wengine wanakuja kwetu na wengine wanakwenda EWURA. Kwa hiyo, matokeo yake ni kwamba hapa nchini mpaka sasa hakuna mradi uliofanikiwa kwa sababu hakuna mwongozo
na utaratibu wa kushughulikia miradi hii wakati taka zipo nyingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Mheshimiwa Makamu wa Rais mwezi Mei ataitisha kikao ambacho kitakuwa ni kati ya sisi Wizara ya Nishati, TAMISEMI Halmashauri za Majjiji zote EWURA na TANESCO na kikao hicho ndicho kitaamua kuhusu mwongozo wa kukaribisha uwekezaji wa sekta binafsi kwenye shughuli ya kuchakata kata. Kwa wale Waheshimiwa Wabunge ambao wamekuwa na hoja hizi, naomba wawe na subira Serikali itatoa mwongozo kutoka kwenye Ofisi ya Makamu wa Rais kuhusu namna gani tunaweza kurahisisha na kuharakisha uwekezaji wa sekta binafsi katika kuchakata taka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mazingira ya bahari na pwani, Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumza kuhusu mambo mawili. Kwanza, uvuvi haramu lakini pili watu wanaokaa pwani wanajua jinsi fukwe zinazovyoliwa kutokana na mabadiliko ya tabianchi. Sisi ofisi yetu inao mkakati, Mheshimiwa Ghasia na Waheshimiwa wengine wameongea, mtakumbuka miezi mitatu iliyopita ofisi yetu sisi na mimi niliongoza nilikuwa Mwenyekiti wa kikao cha Mawaziri kama sita hivi tena wazito, Mheshimiwa Mwinyi, Mheshimiwa Mwingulu, Wizara ya TAMISEMI na Maliasili ambapo tulikaa na kutengeneza mkakati wa pamoja wa kukabiliana na uvuvi haramu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika wiki chache zijazo mtaona operesheni kubwa ya Kiserikali, tusingependa kuizungumza kwa sababu tunakabiliana na watu wanaofanya kazi shughuli haramu ambayo itamaliza kabisa tatizo hili la uvuvi haramu. Vilevile tutaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kugharamia miradi ya mabadiliko ya tabia nchi katika maeneo ya kanda za Pwani kwa kujenga kuta kama tunavyojenga pale Ocean Road, Pangani, Kigamboni na Zanzibar lakini kupanda mikoko kama tunavyofanya kule Rufiji. Kwa hiyo, tunaendelea kutafuta fedha nyingi kwa ajili hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mchango wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa Zanzibar, Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha na Mheshimiwa Ali Hassan Omar King wameongelea, hii ndiyo dhamira yetu. Ule mradi aliouongelea Mheshimiwa Shamsi nimechukua mawazo yale na tutaupanua na kuukuza. Shida kubwa ya wavuvi wadogo ni kuweza kufika mbali. Kwa hiyo, ili uwasaidie, usiwasadie kwa namna ambayo wataendelea kufika pale pale karibu. Kwa hilo, tumelichukua na tutalifanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tunaamini kwamba mchango wa Tanzania Bara kwa maendeleo ya Zanzibar siyo wa Serikali peke yake bali hata mfumo wa uchumi unaowezesha biashara kubwa zaidi na rahisi zaidi kwa pande zote mbili ili Zanzibar uchumi wake uhamasike zaidi kutokana na kuwa karibu na sehemu yenye uchumi mkubwa zaidi. Kwa hiyo, tutaendelea kushirikisha wenzetu wataalam wa biashara na uwekezaji ili tuweze kukamilisha hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Muungano is a fact of life yaani lazima tukubaliane wote hapa na hata kama hukubali na kama viongozi lazima tuwe honest kwamba hatuna namna nyingine zaidi ya Muungano. Mwingiliano ni mkubwa, ni wa muda mrefu na gharama ya kuuondoa ni kubwa zaidi kuliko juhudi tunazoweza kuzitumia kuzirekebisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nadhani uwekezaji kwenye kuimarisha Muungano ni muhimu zaidi kuliko tafakuri ya namna tunavyoweza kuachana. Kwa hiyo, napenda juhudi za wanasiasa wa pande zote mbili ziwe katika kuuimarisha Muungano huu. Mnanifahamu mimi ni mtu ambaye sina tatizo na mawazo ya aina yoyote na hakuna hoja inaweza kutufarakanisha au kututenganisha kwenye Muungano. Kwa hiyo, siasa nzuri zaidi ndugu zangu siyo siasa ya kuubeza Muungano ni ya kujenga, siasa nzuri zaidi siyo ya kuupa jina baya ili uhalalishe kuumong’onyoa. Siasa nzuri ni kuupa hadhi yake unaostahili ili tuweze kuwekeza katika juhudi za kuuimarisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Ally Saleh amesema kwamba utaratibu wa kutatua kero haufai, lakini nitaka nimwambie tu kwamba utaratibu huu wa tangu mwaka 2006 ndiyo umetupunguzia kero kutoka 15 mpaka tatu sasa hivi. Kwa hiyo, ndugu yangu kama kuna mawazo ya utaratibu bora zaidi sisi tuko wazi kabisa na mimi nipo tayari kupokea mawazo kuhusu utaratibu bora wa kushughulikia kero za Muungano kwa sababu nchi hii ni yetu sote na mawazo bora zaidi ya kuimarisha Muungano ofisi yetu inayapokea. Kwa hiyo, tupendekeze tu kama yapo mawazo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wamezungumza kuhusu kukauka kwa mito, vyanzo vya maji na maziwa, ni kweli. Katika ziara zangu nchini nafanya makusudi kutembelea vyanzo vya maji, maziwa na mito. Nimetembelea Ziwa Tanganyika, Ziwa Jipe, Chala, Natron, Manyara, Eyasi na nimejionea mwenyewe jinsi gani tunavyoelekea kwenye kuangamia.
Waheshimiwa Wabunge, ninaposema kuelekea kuangamia ninamaanisha hivi, ukienda kule Jipe utaona zile jamii za pale hata aina ya samaki wanazovua ni visamaki vidogo, mtu akitaka kwenda kuvua ni lazima apite kwenye magugu yaliyojaa kwenye ziwa. Lile ziwa nusu liko upande wa Tanzania na nusu liko upande wa Kenya. Ukipiga picha ziwa lile utaona upande wa Tanzania ndiyo kumejaa magugu, upande wa Kenya kuna hoteli pembeni ya ziwa watu wanaogelea, hii ni aibu kubwa kwa nchi yetu na hii tunafanya wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sisi kama Ofisi ya Makamu wa Rais tumeamua kwamba tutaanzisha mradi mkubwa kabisa wa kitaifa wa kutunza maziwa madogo madogo katika nchi yetu. Nimewaambia kabisa wataalam wa Wizara nitawapa likizo ya wiki tatu wakakae mahali waandike mradi wa maziwa madogo nane hapa nchini na namna tunavyoweza kuyahifadhi. Kwa hiyo, tutawaletea taarifa hiyo tutakapokuwa tumekamilisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwaambie hali ya uharibifu wa vyanzo vya maji ni kubwa sana tutapoteza mito katika nchi hii. Waheshimiwa Wabunge, naomba niseme, watoto na wajukuu zetu watakuja kutushangaa sisi tulikuwa ni watu wa namna gani ambao tulikuwepo na kushuhudia na kuwezesha upoteaji wa kitu kama mto, unawezeshaje mpaka mto upotee? Kwa hiyo, ngoja niishie hapo nisije nikasema maneno mabaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu NEMC, Waheshimiwa Wabunge wamesema kwamba kuna haja kubwa ya kujenga uwezo wa NEMC na hilo tunalifanya. Ni taasisi ambayo imepewa mamlaka makubwa lakini uwezo wake wa kitaasisi na fedha hauendani na majukumu iliyopewa na sheria. Kwa moja ya kazi yetu sisi ni kujenga uwezo wa taasisi hii ili iendane na hadhi na heshima ya taasisi yenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye nchi nyingine Mkurugenzi Mkuu wa NEMC analindwa kutokana na kazi kubwa anayoifanya. Nchi hii Mkurugenzi Mkuu wa NEMC anaweza akapita kantini hata hujui ni nani wakati ni taasisi kubwa yenye mamlaka makubwa kabisa inayoweza kuzuia hata ndege zisiruke kwa sheria hii. Mkurugenzi Mkuu wa NEMC anaweza akasema Emirates isiondoke mpaka nijihakikishie kwamba haivujishi mafuta, ndiyo nguvu ya kisheria ya taasisi zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo sisi moja ya majukumu yetu tangu tulipoingia Wizarani ni kujenga uwezo wa kitaasisi, ndiyo maana tumefufua Mfuko na Baraza la Rufaa. Watu wa NEMC mkiongea nao watawambia, NEMC tuliyoikuta na NEMC ya sasa kama alivyosema Naibu Waziri ambayo ilikuwa inakusanya shilingi bilioni 5 sasa hivi 12 ni tofauti. Kazi hiyo itaendelea na katika siku chache zijazo mtasikia kazi tutakayoifanya NEMC ya kubadilisha mambo pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mzee wangu Mheshimiwa Nsanzugwanko ananiangalia sana nataka niseme jambo lake, mwaka jana wakati tunawasilisha bajeti hapa, Mheshimiwa Nsanzugwanko na Mheshimiwa Bilago walisimama na kushika mshahara kwa kusema kwamba hatujazungumza lolote kuhusu uharibifu wa mazingira unaofanywa na wakimbizi. Nataka niwaambie kwamba baada ya lile jambo mimi nikafanya safari kwenda kwenye kambi za wakimbizi, bahati mbaya sikusema kwenye hotuba na nikatembelea Nyarugusu, Makere, Mtabila na vijiji vyote vinavyozunguka kambi za wakimbizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikawaita wakuu wote wa UNHCR kule Kigoma na nikawapa maelekezo yafuatayo siyo kwa mdogo ni kwa barua. Kwanza, makambi yote ya wakimbizi Tanzania yafanyiwe EIA. Sheria yetu inasema, maeneo ya makazi makubwa lazima yawe na environmental impact assessment lakini nilistajabishwa kwamba makambi yale yalikuwa hayana environmental impact assessment. Kwa hiyo, kwanza tukawapiga faini kwamba hawakuwa na EIA lakini pia tukawalazimisha wafanya EIA ambayo itatoa masharti ya matumizi ya eneo lile ikiwemo hifadhi ya mazingira, hilo ni agizo la kwanza nililowapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, agizo la pili nililowapa, ni kwamba walikuwa na pilot project ya kuwapa majiko ya gasi wakimbizi. Tukasema kwanza isiwe pilot iwe ni mradi, lakini usiishie kwa wakimbizi bali uishie pia kwa jamii inayozunguka kambi hizo ili wasikate kuni. Agizo la tatu nililowapa ni kwamba wachangie kwenye miradi ya maendeleo katika vijiji vinavyozunguka makambi ya wakimbizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua alininong’oneza kwamba atashika tena mshahara lakini naamini taarifa hii itamridhisha na ataachia mshahara wangu kwa sababu kazi tumefanya na tunafuatilia. Ulinituma na nimeenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia ulisema kwamba Kasulu kuna tatizo la vyanzo vya maji na tumepeleka timu na tutaandika mradi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge, naomba nimalize kwa kusema kwamba kazi tuliyopewa na Taifa ya kusimamia uimara wa Muungano tunaifanya vizuri, naamini kabisa kwamba katika kipindi cha mwaka mzima uliopita, hamjasikia kelele, malalamiko kuhusu Muungano kama mlivyokuwa mmezoea kusikia siku za nyuma. Hili jambo halijatokea kwa ajali kwamba watu wamelala ni kwamba kuna kazi imefanyika ya kuhakikisha kwamba tunapunguza kero na malalamiko. Muungano na jina baya la Muungano halipo tena kwenye vichwa vya habari. Hii siyo kwa sababu akina Mheshimiwa Ally Saleh wanachapana bakora kule hapana, hii ni kwa sababu tumefanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia wote mnafahamu kwamba hifadhi ya mazingira kama alivyosema Naibu Waziri na Mwenyekiti imeongezeka na tutaendelea kufanya kazi kubwa, naomba muendelee kutuamini na kutuwezesha. Kama mnavyojua sisi ni rafiki wa watu wote na kwa maneno hayo, nategemea hatutapata shida sana kwenye kupitisha bajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru wote waliochangia na naomba kutoa hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. JANUARY Y. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza Viongozi Makatibu Wakuu wa Wizara na Watendaji wa Taasisi zilizo chini ya Wizara, ikiwemo TANROADs kwa kazi nzuri mnayoifanya. Kazi inaonekana na jitihada pia zinaonekana. Kwa miaka zaidi ya 20 sasa wananchi wa Kongowe na Bumbuli wamekuwa wanangoja barabara ya kwanza ya lami katika eneo hilo. Wamekuwa wanaipigia kura CCM kwa matumaini hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, ahadi ya barabara ya kutoka Soni – Bumbuli – Kwashemshi – Korogwe kujengwa kwa kiwango cha lami bado imebaki ahadi ya kwenye Ilani na kwenye Kauli za Viongozi. Wananchi hawa sasa wanakata tamaa. Mwaka jana kwenye vitabu vya bajeti barabara hii ilionesha sifuri, yaani haikupangiwa fedha. Jambo hili lilitusikitisha. Mwaka huu tumeona fedha kidogo sana kwa ajili ya kumalizia design kwa kipande cha mwisho. Naomba na kupendekeza kwamba, kwa kuwa kipande cha Soni – Bumbuli tayari design imefanyika, fedha zipangwe kuanza angalau kilomita 10 za lami mwaka ujao wa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara za kupandishwa madaraja kuwa za TANROADs; vilevile tulipendekeza barabara mbili na kuzipitisha katika michakato yote husika kwa ajili ya kupandishwa madaraja. Barabara hizo ni: Kwanza, barabara ya Soni - Baga – Ngwashi – Milingano – Mashawa na pili ni Soni – Mponda – Tawota – Keronge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hizi zinaunganisha Wilaya na Majimbo matatu. Tunasubiri majibu ya Wizara kwa maombi haya.
Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari za Mwaka 2016
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa fursa ya kuchangia hoja hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tuanze na kitu gani ambacho hakipo kwenye mjadala. Jambo ambalo halipo kwenye mjadala leo ni umuhimu wa vyombo vya habari na umuhimu wa waandishi wa habari. Kwa sababu nimeona naona jana tumetumia muda mrefu sana kuzungumza kuhusu umuhimu wa vyombo vya habari na umuhimu wa waandishi wa habari, sote tunakubaliana katika hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wengine wameenda mbali kwa kulinganisha waandishi wa habari sawa na taaluma nyingine, Madaktari, Wahandisi, nami nakubaliana na hilo, kwamba kwa hapa tulipofikia kwa umuhimu wa taaluma ya uandishi wa habari, kwa umuhimu wa tasnia ya habari katika ujenzi wa demokrasia, umuhimu wake ni sawa na taaluma zile nyingine ambazo tunazitaja kwamba, ni muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tukishakubaliana hivyo kwamba, uandishi wa habari ni taaluma muhimu kwa vyovyote lazima tukubaliane kwamba, lazima kuwe na udhibiti wa Serikali katika taaluma hii na tasnia hii muhimu kwa sababu, huwezi kusema kwamba, uandishi wa habari ni muhimu sana sawa na uhandisi lakini ukaishia hapohapo. Kwa maana hiyo basi, tasnia hii, taaluma hii iendeshwe shaghalabaghala bila udhibiti mahususi, bila kuwepo na mamlaka na sheria inayoweka viwango. Kwa hiyo, sheria hii imeenda kutekeleza hisia zetu, kwetu sisi, tasnia ya habari ni muhimu kwa nchi yetu, ndiyo maana tumeweka udhibiti, tumeweka viwango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda turudi kwenye dhana ya udhibiti kwa ujumla. Hapa kihistoria katika nchi yetu kuna baadhi ya huduma na biashara ambazo zimekuwa zinadhibitiwa na msingi wa udhibiti huo ni maslahi mapana ya jamii kutokana na shughuli zile. Kwa mfano, tunadhibiti huduma ya mawasiliano, tunadhibiti dawa, tunadhibiti shughuli nyingine muhimu; sasa msingi wa udhibiti wa tasnia hii ni kwamba, ipo njia panda kati ya huduma kwa demokrasia kwa upande mmoja, lakini vilevile biashara kwa upande mwingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uandishi wa habari na tasnia ya habari inatoa huduma kwa demokrasia ya nchi yetu, lakini wakati huohuo ni biashara vilevile. Kwa hiyo, hii dhana ya kuachia self regulation wakati kuna hatari kubwa kwamba, ile self regulation inaweza ikatumika vibaya na maslahi ya kibiashara yakachukua nafasi kubwa zaidi katika udhibiti kuliko huduma kwa demokrasia. Ndiyo maana tumeamua kwamba, Serikali angalau kwa sasa ndiyo ambayo ipewe nafasi ya kuweka viwango, kwa hiyo hii ni muhimu kufahamu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nchi ambazo zimeendelea katika tasnia ya habari zilishajaribiwa namna zote, kule Marekani, Uingereza kwa mfano, kulikuwa na kitu kinaitwa Press Complaints Commission ambayo ilikuwa ni chombo cha self regulation katika tasnia ya vyombo vya habari, tasnia ya magazeti, lakini tunafahamu miaka karibu 16 iliyopita kile kitu kilivunjwa. Kilivunjwa kwa sababu, kilishindwa kuweka balance sahihi kati ya maslahi ya kibiashara ya wenye vyombo vya habari na maslahi mapana ya umma na kikaanzishwa chombo kingine mahususi kabisa madhubuti ambacho kiko chini ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti,vile vile katika nchi ya Norway ambayo wote tunaisifia kwamba ni nchi ambayo imeendelea kidemokrasia, inajali haki za binadamu, kwenye Wizara ya utamaduni na mambo ya kanisa (Ministry of Culture and Church Affairs) kuna kitu kinaitwa (Norwegians Media Authority), chombo cha Serikali, ambacho kinatoa leseni, kinadhibiti ubora, kinasema nani anunue chombo kipi na kwa kiasi gani; yote ni kwa ajili ya kuhakikisha kwamba jambo hili linaendeshwa kwa namna nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefurahi kwamba Mheshimiwa Lissu, hapa ametoa historia kwamba wakati wa chama kimoja, wakati vyombo vyote vya habari vinamilikiwa na Serikali, wakati hakuna magazeti mengine ya binafsi kulikuwa tayari na accreditation ya waandishi wa habari. Sasa anachotuambia ni nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, anachotuambia ni kwamba; ithibati haina uhusiano na kuminya demokrasia au kuminya sauti. Kama wakati wa chama kimoja ambapo hakukuwa na ushindani wala upinzani bado Serikali iliamua kuwe na viwango katika tasnia hii, dhana ni ile ile, kwamba kinachotakiwa hapa ni kuwa na viwango sahihi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, unaposema kwamba sasa hivi Serikali inalileta jambo hili kwa sababu inataka iminye waandishi, au iminye tasnia ya uandishi inaenda kinyume na historia ambayo ameitoa mwenyewe kwamba hata huko nyuma jambo hili lilikuwa linafanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ningekuwa mwandishi wa habari, katika kutazama sheria hii ningejiuliza mambo mawili. Kwanza liability yangu katika shughuli yangu iko wapi, pili, je, sheria iliyowekwa inaruhusu au hairuhusu kwa kiasi gani watu kuivamia tasnia hii na kuiondoa thamani? Sasa uzuri wa sheria hii ni kwamba inatenganisha liability kwa kila kundi. Mwandishi liability yake iko peke yake na makosa ya mmiliki au mchapishaji hayawezi kuchukuliwa na mwandishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia sheria nyingi za namna hii, huu ni ubunifu mkubwa kwenye sheria yetu kwa sababu unamlinda mahsusi mwandishi wa habari asiingie kwenye liability, asiingie kwenye matatizo kwa sababu ya makosa ya mtu mwingine. Ingekuwa mimi hili jambo lingekuwa la kusherekea na kufurahia na la kupongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili, nadhani wenzetu, rafiki zetu ambao tunafanya nao kazi sisi kama Serikali, kama Chama Tawala, waandishi wa habari, ningependa na kufurahia utaratibu ambao unakinga hii taaluma isivamiwe na watu ambao wanaiondolea sifa. Sheria hii ndicho chombo kinachoweza kwa sababu sifa na heshima ya uandishi wa habari inaondolewa na watu wachache sana ambao hakuna sheria wala taratibu za kuwazuia wasiingilie. Kwa hiyo, ningekuwa mimi, ningefurahia exclusivity katika hii shughuli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia, best practices za jambo hili duniani kote, mwaka juzi Kenya walipitisha sheria wakaweka na dhamana kabisa (bond), kwamba ukitaka kuanzisha chombo cha habari unaweka fedha nyingi chini, ili pale utakapokutwa na makosa ikitoka judgment ile fedha inachukuliwa. Hapa sisi hatukuamua kufanya hivyo kwa sababu tuliona kwamba ni vyema watu wote wanaotaka kuingia kwenye biashara hii wapate fursa ya kuingia kwenye biashara hii bila kuwa na vikwazo, bila kuwa na upinzani wowote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nadhani na naamini kwamba umefika wakati sasa kwenye baadhi ya mambo tukubaliane kama Taifa, kwamba lazima shughuli hii ambayo inaathiri sana maisha ya watu, uendeshaji wa demokrasia yetu lazima iendeshwe kwa utaratibu murua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huko nyuma yalifanyika makosa ambapo haki za watu na nimshukuru ndugu yangu Mheshimiwa Zitto amesema yeye amekuwa mhanga mkubwa sana wa kuandikwa na kutukanwa na yeye anadhani ni sawa na ni sahihi, lakini kwa watu wengine ambao si wanasiasa, ambao hawako kwenye shughuli yetu sisi ambao tumezoea kusemwa na kutukanwa, uvumilivu wetu na nafasi yetu ya kuvumilia matusi tusiihamishie kwa watu wengine ambao hawana hatia wala hawana makosa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kumalizia nampongeza sana Waziri, kwamba ametengeneza historia kwa kutuletea sheria nzuri. Naamini kabisa tasnia hii ni muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu. Sisi tunapenda na tunategemea waandishi wa habari na uandishi wa habari kwa maendeleo na demokrasia ya nchi yetu, hakuna namna ambayo Serikali hii inaweza kuminya uhuru wa habari. Kama kuna kitu ambacho Serikali hii inataka ni kupata msaada wa waandishi wa habari katika kupambana na rushwa na ufisadi na maovu yote katika jamii kwa sababu wao wana nafasi kubwa ya kuweza kuisaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hii itawezesha waandishi wa habari waisaidie Serikali, wamsaidie Mheshimiwa Raisi wetu na chama chetu katika kuijenga jamii yetu upya na kujenga jamii nzuri. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, hongera sana na naamini kwamba tutaipitisha sheria hii na huko mbele kama kutakuwa na marekebisho tutayafanya yanapostahili, lakini kwa sasa kwa ilivyoandikwa ni nzuri na inastahili kupitishwa .
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.