Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. January Yusuf Makamba (9 total)

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona. Kwa kuwa kulikuwa na maelekezo Serikalini kuhusu ushirikiano wa karibu kati ya Wizara za Kisekta za SMT na zile za SMZ ambayo yalikuwa yanahimiza ushirikiano wa karibu wa kitaalamu na utafiti na pale Wizara ya Maji ilikuwa imepangwa, Waziri wa Sekta ya Maji Bara na Zanzibar tarehe 8 Juni, 2014; mkutano ule ukaahirishwa kusubiri Bunge la Katiba:-
Je, kwa sasa hivi maelewano hayo yanaendeleaje kuimarishwa? Ahsante sana.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya kazi ya Ofisi ya Makamu wa Rais ni kuratibu mahusiano kati ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mambo yasiyo ya Muungano. Mwezi wa kwanza tumetengeneza ratiba ya vile vikao ambavyo viliahirishwa na mambo ambayo yalibaki kufanyika katika kuhakikisha kwamba mahusiano hayo yanaimarishwa.
Kwa hiyo, moja ya kikao kilichopangwa kufanyika na ambacho tumeweka fedha kwenye bajeti ili kifanyike, ni pamoja na hicho unachoongelea Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda tu kuwapa faraja na taarifa wenzetu wa Zanzibar kwamba tumedhamiria kwa nguvu zote kuhakikisha kwamba Muungano wetu unaimarika katika mambo ya Muungano na yale yasiyo ya Muungano na kazi hiyo tutaifanya kwa nguvu ili kutimiza ahadi yetu kama tulivyowaahidi Watanzania. (Makofi)
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri nimuombe kumuuliza maswali madogo sana ya nyongeza.
Kwa masikitiko makubwa sana suala hili limeleta gumzo sana katika chombo cha Baraza la Wawakilishi, limeleta gumzo muda mrefu na hatimaye likatua katika chombo hiki muhimu kwa wananchi.
Mwaka 2014 Serikali mbili, Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar iliunda kamati ya wataalam na kamati hiyo ya wataalam iliongozwa na wanasheria wazito wa nchi hii akiwemo Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar…
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio swali hili nakuja nalo; imeunda Kamati iliyokuwa inaongozwa na Wanasheria Wakuu wawili kutoka Zanzibar na Bara ili kutatua changamoto zilizokuwepo katika mafuta na gesi ikiwemo ya Kisiwa hiki cha Latham na ripoti hii wakaikabidhi kwenye Serikali zote mbili. Je, ni lini Serikali imetoa ripoti ya suala hili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, Zanzibar ina mipaka yake ninachokifahamu hapa kama ni Serikali moja ni majibu yaliyojibiwa hapa; Zanzibar mipaka yake na hili eneo Zanzibar na swali lao. Tukamate wapi ambapo pana ukweli?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muda mrefu tangu mwaka 1968 ambapo suala la gesi na mafuta liliingizwa kwenye orodha ya mambo ya Muungano; baada ya hapo kwa muda mrefu kumekuwa na hoja na haja ya kuliondoa suala hilo kwenye orodha ya mambo ya Muungano; na zimefanyika jitihada mbalimbali ili kufikia azma hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuanzia mwaka 2010 ilikubalika baina ya Serikali zote mbili kwamba suala hilo liondolewe. Kamati anayoizungumza Mheshimiwa Jaku ya wataalam iliundwa ili kutafuta namna kwa sababu suala hili lipo Kikatiba na lingeweza kuondolewa Kikatiba; lakini kamati hiyo iliundwa mahususi ili kuwezesha jambo hilo lifanyike wakati mchakato wa kubadilisha Katiba unafanyika na matokeo ya kamati hiyo ilipelekea sasa kuapata mwanya ambapo Sheria ya Mafuta tuliyopitisha Bungeni mwaka jana iliruhusu Zanzibar iweze kuchimba na kutafuta mafuta na sasa kuna sheria inatungwa katika Baraza la Wawakilishi ya kuruhusu Zanzibar ichimbe na kutafuta mafuta hata kabla Katiba haijabadilishwa rasmi na kuliondoa suala hilo kwenye orodha ya mambo ya Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo tunafahamu kwamba katika Katiba Inayopendekezwa suala hilo limezingatiwa na litaondolewa katika orodha ya mambo ya Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa ambacho napenda kusisitiza ni kwamba sisi Jamhuri yetu hii ya Muungano kama nlivyosema kwenye lile jibu la msingi ni watu wa ndugu na jamaa moja; hakuna mgogoro wowote unaohusiana na mipaka au umiliki wa eneo lolote katika Jamhuri yetu ya Muungano wa Tanzania. Na sisi pia kama ndugu tumejenga utaratibu wa kiutamaduni na kitaasisi wa kushughulikia na changamoto za Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninachopenda kutoa rai ni kwamba kwa wenzetu ambao wanapenda kutumia masuala ya Muungano kukabiliana na matatizo yao ya kisiasa, aidha, upande wa Bara au Zanzibar waache hayo mambo na watoe nafasi kwetu sisi ambao tumepewa dhamana ya kushughulikia mambo ya Muungano na Serikali iweze kufanya shughuli zake. Ahsante. (Makofi)
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ambayo sijaridhika nayo hata kidogo, naomba sasa niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa mmiliki wa shamba hili ndugu Joseph Meier alimiliki shamba hili kwa njia za ulaghai ikiwa ni pamoja na kuwapatia viatu Wenyeviti wa Vijiji wa kipindi hicho kwa tiketi ya CCM na akamilikishwa shamba hilo, je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuchukua hatua za kinidhamu kwa mmiliki huyu ambaye ni mmiliki haramu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa Serikali katika majibu yake imesema kwamba mmiliki wa hili shamba analihudumia kwa kiwango kidogo sana, kwa maana ya kwamba katika ekari 1,000 ekari zinazoendelezwa ni kama ekari 10 tu kati ya 1000; je, Serikali haioni kwa kigezo hiki tu ni muda muafaka sasa wa kumpora huyu bwana hili shamba lirejeshwe kwa wananchi wa Jimbo la Mbozi ambao hawana maeneo ya kulima?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza la nyongeza anasema kuwa huyu mwekezaji alichukua shamba hili kwa njia ya ulaghai. Sisi tunasema kwamba kama mwekezaji yeyote na ndiyo maana Msajili wa Mashirika ya Umma (TR) anapitia mikataba yote ya wawekezaji wetu ambavyo wameweza kumilikishwa mashamba na wengine ambao waliingia kwenye ubia wa mikataba mbalimbali ili kuweza kujua kama kuna tatizo lolote lile katika umiliki. Kwa hiyo, pale tunapogundua kwamba mwekezaji au mbia wetu ambaye tumeingia naye kama Serikali, kuna ubadhirifu wa aina yoyote ulifanyika, hatua zitachukuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kaguzi hizo zinaendelea kwenye Mashirika yetu ya Umma yote kuhakikisha kwamba kuna usahihi wa umiliki, lakini vilevile hakuna ulaghai wa aina yoyote na hivyo kama itabainika kwamba kuna ulaghai ulitumika katika kujipatia shamba hili hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili; kwamba huyu mwekezaji amekuwa akiendeleza shamba hili kwa kiwango kidogo sana, ambapo according to yeye Mheshimiwa Mbunge ni kama asilimia moja au mbili ya shamba alilokuwa amekabidhiwa la hekta 830, lakini ameweza kuendeleza kidogo sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyoeleza hapa kwamba kinachotakiwa sasa Mheshimiwa Mbunge ajue jukumu hili liko kwenye halmashauri yake, yupo Afisa Mteule wa Ardhi pale ambaye ana jukumu la kufanya ukaguzi kwenye shamba hilo kuona maendelezo ambayo yamefanyika na akigundua kwamba hakuna maendelezo yoyote yaliyofanyika kwenye shamba hilo, basi amwandikie notice ya siku 28 ya kufanya marekebisho na baadaye amwandikie notice ya siku siku 90 ya kujieleza kwa nini asinyang‟anywe ardhi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo kama yote haya yatafanyika, mwekezaji huyu atakuwa ameshindwa kukidhi matakwa yanayotakiwa, basi atashauriwa Waziri wa Ardhi ili aweze kulitwaa shamba hilo na Waziri wa Ardhi atamshauri Mheshimiwa Rais afute hati husika. Baada ya hapo taratibu zikikamilika, basi hati itafutwa, umiliki utafutwa na umiliki wa shamba hili utarejeshwa kwenye halmashauri ambapo halmashauri ndiyo watapanga matumizi ya namna gani shamba hili litumike baada ya kuwa limerudishwa na Serikali mikononi mwa halmashauri.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, najua moja ya changamoto kubwa inayoikabili nchi yetu ni migogoro ya ardhi na eneo ambalo inasemekana kumekuwa na migogoro ya ardhi ni pamoja na eneo la Kibada Kigamboni ambapo kuna viwanja vilipimwa na Serikali na wananchi wakapewa na Wizara husika. Sasa, nataka kujua nini status ya eneo hilo wakati Wizara imepima, imewapa wananchi lakini leo imetokea kwamba eneo ambalo amepewa mtu mmoja tayari amejitokeza mtu mwingine amesema hilo eneo ni la kwake wakati Wizara ndio wametoa hati; nini status ya eneo hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakumbuka sote hapa Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Waziri wa Ardhi akiwa hapa Bungeni alitamka kwamba migogoro yote ya ardhi ambayo Waheshimiwa Wabunge mliwasilisha humu Bungeni na migogoro mingine ambayo inahusisha taarifa mbalimbali ambazo zimeshafanyiwa uchunguzi, Mheshimiwa Waziri wa Ardhi aliunda Tume ya kupitia taarifa hizi za uchunguzi zilizofanyika, lakini na migogoro ambayo Waheshimiwa Wabunge tayari waliiwasilisha kipindi cha bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekit, nataka kuwaambia kwamba, timu hiyo ya wataalam iko kazini na Mheshimiwa Bulaya avumilie, asubiri, taarifa hiyo ya wataalam itakapokamilika tutawaletea hapa Bungeni ili kila mmoja ajue status ya kila eneo la mgogoro ambavyo limeshughulikiwa na Serikali.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Matatizo ya ardhi ambayo haijapata kuendelezwa yaliyopo katika eneo la Mbozi yanafanana kabisa na matatizo ambayo tunayo kwenye Wilaya yetu ya Karatu. Katika Kijiji cha Mang‟ola Juu kuna mwekezaji, Tembotembo ambaye amemilikishwa eka zaidi ya 3,000 lakini ameweza kuendeleza chini ya asilimia 25. Katika kijiji hichohicho pia kuna mwekezaji anaitwa Acacia naye ameendeleza eneo alilopewa kwa chini ya asilimia 10.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mashamba hayo sasa yamebadilika kuwa hifadhi na mapori bubu ya kuhifadhia wanyama wa porini ambao ni hatarishi kwa wananchi wanaolizunguka. Je, ni lini Serikali itatoa mashamba hayo na kuwarudishia wananchi hao ili waweze kuyatumia? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, masharti ya kutwaa mashamba kwa hekta zisizopungua 500 mmiliki wa shamba hilo anapewa miaka miwili tu anatakiwa awe ameliendeleza shamba hilo na asipofanya hivyo yuko halali kabisa kunyang‟anywa kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi, Namba 4 ya Mwaka 1999, kifungu cha 45 na cha 47, anayo haki ya kunyang‟anywa ardhi ile. Wale ambao ardhi yao wamekabidhiwa zaidi ya hekta 500, kama hajaiendeleza kwa asilimia 80 ndani ya miaka mitano ardhi ile inaweza kutwaliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ushauri kwa Mheshimiwa Mbunge wa Karatu, kwa sababu mamlaka haya, nani anayeanzisha kazi hii, kazi hii inaanzishwa na Afisa Mteule wa Ardhi pale halmashauri, waanzishe tu halafu watuletee, tena wafanye mapema na mimi bado nakaimu huu Uwaziri wa Ardhi ili tuweze kuyashughulikia mapema matatizo haya.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Tatizo la ardhi kwenye Wilaya ya Mbozi linafanana sana na tatizo lililopo kwenye Mji wetu wa Tunduma. Katika Mji wa Tunduma katika Kata ya Mpemba kuna ardhi karibu ekari 500 ambazo zinamilikiwa na Shirika la Nyumba la Taifa na mpaka sasa hivi eneo lile halijaendelezwa zaidi ya miaka minane. Je, Serikali inasema nini ili kuikabidhi halmashauri, ambayo haina hata eneo la kujenga makao makuu ili iweze kutumia ardhi ile?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na swali hili ambalo limekuwa kila Mheshimiwa Mbunge akiliulizia, naomba tu nitoe wito kwa Wakurugenzi wa Halmashauri pamoja na Maafisa wetu Wateule wa Ardhi popote nchini, katika maeneo na katika malalamiko ya namna hii, Sheria ya Ardhi Namba 4 ya Mwaka 1999 imewapa nguvu. Kwa hiyo, walianzishe jambo hili watuletee na sisi kama Serikali hatutawaangusha.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali yenye mikakati mizuri. Naomba nitumie muda wangu kuuliza swali moja tu la nyongeza. Mamlaka ya Maji ya Mji wa Mwanuzi Wilayani Meatu inasuasua kwa kuwa chanzo chake cha bwawa kimejaa matope na kuathirika na mabadiliko ya tabianchi sambamba na chanzo cha New Sola Zanzui kilichopo Wilaya ya Maswa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira imefanikiwa kupata sh. 230,000,000,000 ikiwa ni mkakati wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwa kutoa maji Ziwa Victoria na kuyaleta Mkoa wa Simiyu na usanifu bado unaendelea. Je, Serikali haioni haja katika usanifu huo ikajumuisha kupeleka bomba kuu katika Makao Makuu yote ya Mkoa wa Simiyu ikiwemo Wilaya ya Meatu na Maswa kwa awamu ya kwanza kwa sababu Wilaya hizi zimeathirika kiasi kikubwa na ukame na ziko katika phase two na fedha ya phase two haijapatikana?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kumshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia na kuuliza swali na kwa umakini anaouonesha katika kufuatilia shida za maji za wananchi wa Mkoa wa Simiyu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nimpe habari njema kwamba baada ya kupatikana sh. 250,000,000,000 siyo 230,000,000,000 za awamu ya kwanza sasa tunaanza utaratibu wa kupata fedha nyingine zaidi za awamu ya pili ambazo zitapeleka maji sasa katika maeneo yote aliyoyataja pamoja na mkoa mzima na mikoa mingine ambayo inakabiliwa na ukame mkubwa unaotokana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Kwa hiyo, Serikali inatamka rasmi kwamba, inatambua changamoto ya maji na ina mipango ya kuyapeleka kwa wananchi wote wanaokabiliwa na ukame katika eneo hilo kwa kupitia mradi huu. (Makofi)
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na jibu zuri la kuridhisha la Serikali nina swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na Mto Lukuga kupoteza maji katika Ziwa Tanganyika, je, Serikali iko tayari kuwahamasisha wananchi wanaokata miti katika milima yote inayozunguka Ziwa Tanganyika, ili wakati wa masika maporomoko yote yanayoleta tope, mchanga, kupunguza kina cha maji ya Ziwa Tanganyika, kuacha shughuli hizo?
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, je, Serikali iko tayari kuwaelimisha wananchi waache kukata miti hovyo na kuwachukulia hatua wote wanaofanya kandokando ya Ziwa Tanganyika kufanya shughuli ambazo Serikali hairidhishwi, kama kujenga karibu na ziwa na kuharibu vyanzo vya maji vinavyoporomosha maji katika Ziwa Tanganyika?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niseme kwamba, nilipata fursa ya kwenda Kinshasa kwa ajili kukutana na Mawaziri wenzangu wa Mazingira kuhusu suala la kupungua kwa kina cha maji cha Ziwa Tanganyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikutana na Waziri wa Burundi, Zambia na Congo; na mpaka sasa hivi, nimpe tu taarifa njema Mheshimiwa Keissy, kwamba tumefika mahali pazuri kati ya Serikali hizi na Benki ya Dunia kuhusu upatikanaji wa zile fedha za kujenga banio ili kuzuia maji kutoka kwa kasi kwenye Ziwa Tanganyika kwa upande wa Congo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu hili suala la pili, ni kweli changamoto ipo kubwa. Nilipata bahati ya kutembea mikoa yote iliyo katika Mwambao wa Ziwa Tanganyika na kuna tatizo kubwa sana la shughuli za kibinadamu zinazosababisha ziwa kujaa tope na hata Bandari ya Kigoma pamoja na Kasanga na miji yote iliyoko kando ya mwambao kupata changamoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumetoa maelekezo kwa Wakuu wa Wilaya na viongozi wa halmashauri katika maeneo yote kuhakikisha kwamba, Sheria ya Mazingira inazingatiwa na shughuli za kibinadamu katika mita 60 kutoka kwenye mwambao wa Ziwa zinasitishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu changamoto iliyopo kwa sababu watu wengi wanategemea uvuvi na shughuli nyingine na maji yaliyopo pale kufanya hiyo. Kwa hiyo, tunategemea ushirikiano wa Mheshimiwa Mbunge ambaye yeye ni mwanamazingira mzuri sana, Mheshimiwa Keissy, pamoja na viongozi wote tuweze kufanikiwa katika hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, wito wangu ni kwamba, Wakuu wa Mikoa ya mwambao wa Ziwa Tanganyika wanaweza kufanya mkutano na forum pamoja na Wabunge, ili kujadili ustawi wa Ziwa Tanganyika kwa ujumla na sisi Ofisi ya Makamu wa Rais tutakuwa tayari kuunga mkono huo mkutano (forum) wa wadau wote wa Ziwa Tanganyika, ili kuangalia suala hilo na masuala mengine yanayohusiana na ustawi wa ziwa hilo.
MHE. RUKIA AHMED KASSIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, aliyekuwa Waziri katika Wizara ambayo ilikuwa ikishughulikia mambo ya Muungano, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ambaye sasa hivi ni Makamu wa Rais, aliwahi kutuambia kwamba kuna kikao ambacho kilikaa kati ya pande hizi mbili, Wajumbe kutoka Zanzibar na Wajumbe kutoka Tanzania Bara waliokuwa wakizungumzia kuhusu kero ambazo zinahusu mambo ya Muungano. Je, Mheshimiwa Waziri anaweza kutuambia ni Wajumbe gani hao ambao walikuwa wakikutana kuzungumzia kero hizi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, huko nyuma kumekuwa na taratibu mbalimbali za kushughulikia changamoto za Muungano hatuziiti kero ni changamoto za Muungano. Mwaka 2006 ukaanzishwa utaratibu mpya wa kikao cha Kamati ya Pamoja kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti,Kikao kile cha Kamati ya pamoja kilikuwa kinaongozwa na Makamu wa Rais pamoja na Watendaji Wakuu wa Serikali za pande mbili. Maana ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi wa Zanzibar au Waziri Kiongozi kabla ya mabadiliko ya Katiba ya 2010.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kikao kile kinajumuisha Mawaziri wote ni Mabaraza ya Mawaziri ya pande zote mbili za Muungano wetu. Kwa taarifa tu kikao cha mwisho kilikutana tarehe 13 Januari, 2017 kule Zanzibar ambapo kilijumuisha Mawaziri wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mawaziri wote wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kikao hicho kinatanguliwa na kikao cha Makatibu Wakuu wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makatibu Wakuu wote wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Kabla ya hapo kinatanguliwa na kikao cha wataalam wa masuala husika yatakayozungumzwa katika kikao hicho kwa pande zote mbili za Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, kikao hiki na utaratibu huu ni mkubwa, ni mzuri na umetusaidia sana kupunguza changamoto za Muungano. (Makofi)