Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Juma Othman Hija (8 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza natoa shukrani zangu za dhati kwa Rais wa Awamu ya Tano Mheshimiwa John Magufuli kwa imani na uwezo mkubwa alionao katika kuendeleza Taifa letu. Pia napenda kuwapongeza Mawaziri wote kwa juhudi wanazoonesha katika kuendesha Wizara zao. Vile vile nachukua nafasi hii kuwashukuru wananchi wote wa Jimbo la Tumbatu kwa imani waliyonipa kwa kunichagua kuwawakilisha katika Bunge lako Tukufu. Naahidi nitaendelea kuwatumikia kwa uwezo wangu wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, napenda kutoa mchango wangu katika sehemu ifuatayo:
Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma; Katika sehemu hii imeelezwa kuwa, Serikali imetoa elimu kwa Viongozi wa Umma wapatao 3,980 katika sehemu tofauti, ikiwemo Walimu kuhusu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, mgongano wa maslahi na maadili ya Utumishi wa Umma kupitia semina, midahalo, mafunzo na vikao mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu katika sehemu hii naiomba Serikali ieleze ni Viongozi wa ngazi gani walipata mafunzo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naanza kwa kumshukuru Mungu aliyeniwezesha kuwa miongoni mwa Wabunge wa Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, nawashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Tumbatu kwa imani yao kubwa waliyonipa, kwa kunichagua kuwa Mbunge wao kwa kura nyingi sana. Natambua imani yao kwangu na nawaahidi kuwa sitawaangusha.
Tatu, natoa pongezi zangu za dhati kwa Mheshimiwa Rais wetu, Mheshimiwa John Pombe Magufuli, kwa imani na uwezo mkubwa aliouonesha katika kulitumikia Taifa letu. Namwomba Mungu ampe kila jema katika uongozi wake huu.
Nne, napenda kumpongeza Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa pamoja na Baraza lake lote la Mawaziri kwa kuonesha uwezo mkubwa wa uongozi katika sehemu zao za kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naanza kwa kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri katika maeneo yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu uwezeshaji wa wavuvi na wakuzaji viumbe kwenye maji; katika sehemu ya ruzuku za zana za uvuvi, Serikali imetenga shilingi milioni 400 ambazo zilitumika kwa ununuzi wa zana za kilimo, zikiwemo mashine za boti. Pesa hizi ni kidogo sana kwa matumizi ya nchi nzima. Ushauri wangu ni kwamba Serikali iongeze kima hiki cha fedha. Aidha, Serikali iongeze mchango wake kutoka asilima 40 angalau kufikia asilimia 50 ambazo zitawawezesha wavuvi kununua zana hizo za uvuvi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri kwenye ukurasa wa 61, imeeleza kwa ufupi sana juu ya elimu ya maradhi ya UKIMWI. Nashauri kwamba elimu hii iongezwe kwa kiwango kikubwa ili kuwapa weledi zaidi wananchi juu ya ujinga na hatimaye kuepuka kabisa maradhi haya thakili.
Mheshimiwa Naibu Spika, nahitimisha mchango kwa kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naanza kuchangia hotuba hii kwa kumshukuru Mungu kwa kuniwezesha kuwa miongoni mwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pili, napenda kuwashukuru wapigakura wangu kwa kuniamini na kunichagua kwa kura nyingi. Natambua imani yao kwangu na nawaahidi kuwatumikia kwa nguvu zangu zote. Tatu, napenda kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Magufuli kwa kuonesha imani na uwezo mkubwa wa kuendesha nchi.
Nne, napenda kumpongeza Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa pamoja na Baraza lote la Mawaziri kwa kuonesha uwezo mkubwa wa kuongoza Wizara zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuchangia hotuba hii ya Elimu, napenda kuchangia maeneo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ada za vyuo binafsi nchini. Serikali imekuwa na nia nzuri ya kuruhusu vyuo binafsi nchini, hili ni jambo zuri na la maana; masikitiko yangu katika hili ni pale inapoonekana baadhi ya vyuo kutoza ada kwa kulipa fedha za kigeni badala ya fedha ya Tanzania. Miongoni mwa vyuo hivyo ni Chuo cha Kampala (Kampala International University) kilichopo Gongo la Mboto Dar es Salaam. Namwomba Mheshimiwa Waziri kuliangalia suala hili na kuweka utaratibu maalum na kuwalazimisha walipishe wanafunzi kwa pesa za Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, usimamizi wa utekelezaji wa programu na miradi. Katika kitabu cha hotuba ya Mheshimiwa Waziri, ukurasa wa 67, 109 imeeleza namna inavyoendeleza kutekeleza Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES II). Huu ni mpango mzuri na napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa jambo hili. Napenda kumshauri Mheshimiwa Waziri, katika kutekeleza ujenzi wa majengo haya ya sekondari na hata yale ya primary ni vyema ikazingatia kujenga majengo hayo kwa kuzingatia kuwepo kwa wanafunzi wenye uhitaji maalum ili na wao waweze kutumia majengo hayo bila ya usumbufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mheshimiwa Naibu Spika, naanza kuchangia hotuba hii kwa kumshukuru Mungu kwa kunijalia kuwa miongoni mwa Wabunge wa Bunge hili lako Tukufu.
Pili, nachukua fursa hii kwa kuwapongeza wananchi wangu wa Jimbo la Tumbatu kwa kunichagua kwa kura nyingi kuwa Mbunge wa Bunge hili. Natambua imani kubwa waliyonayo kwangu na naahidi sitawaangusha.
Tatu, napenda kumpongea kwa dhati Mheshimiwa Rais, Dkt. Magufuli kwa kuonesha imani na uwezo mkubwa wa kuongoza nchi yetu. Aidha, napenda kumpongeza Waziri Mkuu Mheshimiwa Majaliwa pamoja na Baraza lake la Mawaziri kwa uimara wao katika kuongoza Wizara zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri, napenda kuchangia katika maeneo yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, tozo la KUA katika Kisiwa cha Zanzibar. Kwanza napenda kutoa masikitiko yangu makubwa kuona kwamba katika hotuba yote ya Mheshimiwa Waziri Zanzibar haikutajwa hata kidogo pamoja na kwamba ni miongoni mwa wateja wakubwa wa TANESCO.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, namwomba Waziri anieleweshe, kwa nini Zanzibar inatozwa bei kubwa ukilinganisha na wateja wengine? Kwa mfano, KUA moja inatozwa sh. 16,550/= kwa Zanzibar lakini kwa wateja wengine KUA moja (KUA) inatozwa sh. 13,200/=.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuipongeza Serikali kwa juhudi inayochukuwa katika kuwapelekea wananchi huduma hii katika vijiji vyao. Katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri haikuzungumza vijini na maeneo yaliyosambaziwa umeme. Naomba Mheshimiwa Waziri aoneshe maeneo hayo (locations) na kiwango cha usambazaji (Kms) uliofanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia hali ya ujenzi wa line hizo haioneshi kama zimejengwa kwa wataalam wa mambo ya umeme. Inaonekana kuwa hakuna design yoyote iliyofanyika kabla ya kujengwa line hizo. Ni vyema, Makandarasi kwa usimamizi wa TANESCO wakalazimishwa kuwa na design pamoja na profiles ya kazi hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kawaida lifetime ya nguzo za umeme huwa ni zaidi ya miaka 20 lakini nguzo ambazo zinatumika katika kazi hii hasa za REA hazioneshi umadhubuti halisi kwa kazi hii. Hivyo nakuomba Mheshimiwa Waziri anieleze lifetime ya nguzo hizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naanza kuchangia hotuba hii kwa kumshukuru Mungu aliyeniwezesha kuwa miongoni mwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nachukua fursa hii kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Tumbatu, kwa kunichagua kwa kura nyingi kuwa Mbunge wao, natambua imani kubwa waliyonayo kwangu na naahidi kuwatumikia kwa nguvu zangu zote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, napenda kumpongeza Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Magufuli kwa kuonesha imani na uwezo mkubwa wa kuiongoza nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, napenda kumpongeza Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa pamoja na Baraza lote la Mawaziri kwa kuonesha umahiri wa kuongoza katika Wizara zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuchangia hotuba hii napenda kuchangia katika maeneo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu udhibiti wa migogoro ya ardhi nchini yanaongezeka siku hadi siku. Hii inasababishwa pamoja na mambo mengine, uhaba wa ardhi inayosababishwa na ongezeko la watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la ongezeko la watu namshauri Mheshimiwa Waziri achukue hatua ya kushirikiana na Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani kuangalia kwa makini uingiaji wa wakimbizi ambao nao pia wanasababisha ongezeko la watu nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, teknolojia ya habari katika kitabu cha hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 27 (36) amezungumzia juu ya teknolojia hii, ni teknolojia inayohitaji ujuzi mkubwa. Ushauri wangu ni kwamba kazi hii pamoja na kupewa makandarasi, Wizara ichukue juhudi za makusudi kuwaelimisha wafanyakazi wazalendo ili kwa baadae kuepuka na hasara za kuwapa kazi makandarasi badala yake kazi hizo zifanywe na wafanyakazi wa Wizara hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mipaka ya Kimataifa, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 34 (46) Waziri ameelekeza namna ya juhudi inayochukua juu suala hili la mipaka ya Kimataifa. Mheshimiwa Waziri ameeleza kukwama kwa upimaji wa mipaka kati ya Tanzania na Burundi. Namuomba Mheshimiwa Waziri anieleze ni kiasi gani kazi hiyo imeathiri zoezi hili kutokana na hali aliyoieleza kuwa ni ya kisiasa.
Mheshimwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naanza kutoa mchango wangu kwa kumshukuru Mungu kwa kuniwezesha kuwa Mbunge wa Bunge hili. Pili nawashukuru wapiga kura wangu kwa kunichagua kwa kura nyingi kuwa Mbunge wao, natambua imani kubwa waliyonayo kwangu na nawaahidi nitawatumikia kwa nguvu zangu zote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Rais wetu Mheshimiwa John Pombe Magufuli kwa kuonesha imani na uwezo mkubwa wa kuendesha nchi yetu, Mungu ampe umri na afya njema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nne napenda kumpongeza Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa pamoja na Baraza lake la Mawaziri kwa kuonesha uwezo mkubwa wa kuongoza Wizara zao. Katika kuchangia hotuba ya Waziri napenda kuchangia katika maeneo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu sekta ndogo ya ufugaji, kumekuwa na migogoro isiyomalizika kati ya sekta ya ufugaji na wakulima. Hili ni tatizo ambalo Wizara hii inapaswa kulishughulikia kwa namna ya pekee. Naomba Wizara ianzishe idara maalum ndani ya Wizara hii ya kushughulikia migogoro hii ili kuondosha kabisa tatizo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu sekta ndogo ya utalii, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 15 imeeleza hali ya sekta hii inavyochangia upatikanaji wa fedha. Takwimu zinaonesha kwenye ukurasa huu ni ndogo, hazilingani na namna uingiaji wa watalii katika nchi yetu. Watalii wanaoingia ni wengi sana hivyo nashauri Wizara ichukue mikakati zaidi ya kuziba mianya ya upotevu wa fedha za watalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mamlaka ya usimamizi wa wanyama pori. Nachukua fursa hii kuipongeza Wizara kwa kuanzisha mamlaka hii ni jambo zuri katika kusimamia na kuwalinda wanyama pori wetu. Nashauri Wizara iharakishe kupeleka mamlaka hii katika Wilaya zote za nchi ili huduma hii ipatikane nchi nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naanza kuchangia hotuba hii kwa kumshukuru Mungu kwa kunijalia kuwa miongoni mwa Wabunge wa Bunge hili. Pili nachukua fursa hii kumpongeza Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuonesha imani na uwezo mkubwa wa kuongoza nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, nawapongeza wapiga kura wangu kwa kunichagua kwa kura nyingi kuwa Mbunge wao. Natambua imani yao kubwa waliyonayo kwangu na nawaahidi sitowaangusha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuchangia hotuba hii napenda kuchangia katika maeneo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, sifa na muda wa wafanyakazi wa Ubalozini. Napenda kuipongeza Wizara na Serikali kwa jumla kwa utaratibu mzuri wa kuwapangia na kuwateua wafanyakazi wa Balozi zetu. Napenda kumuuliza Mheshimiwa Waziri ni sifa gani wanazotumia katika kuwateua wafanyakazi wetu pamoja na Mabalozi katika nchi za nje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo cha Diplomasia. Nachukua nafasi hii kuipongeza Wizara kwa kukiendeleza chuo hiki muhimu katika kuzalisha na kutayarisha wataalam wetu. Chuo hiki kama vilivyo vyuo vingine kinahitaji mahitaji kama vile mikopo na kadhalika. Napenda kumuuliza Mheshimiwa Waziri kuna mpango gani wa mikopo kwa wanafunzi wanaosoma katika chuo hiki?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jumuiya ya Afrika ya Mashariki. Jumuiya hii ni ya muda mrefu na ina uzoefu mkubwa. Napenda kueleza wasiwasi wangu juu ya ongezeko la nchi wanachama wa jumuiya hii. Nchi hizi zilizo nje ya Afrika Mashariki zina matatizo makubwa katika nchi zao na ndiyo wanaotuongezea watu katika mipaka yetu. Aidha, zimetuongezea uhalifu na ujangili na matatizo mengine. Hivyo, namwomba Mheshimiwa Waziri aliangalie suala hili na wasite kuongeza wanachama walioko nje ya Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nachukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na Watendaji wake kwa kazi nzuri waliyoifanya katika kutengeneza Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2017/2018.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchangia Mpango huu kwenye maeneo yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina azma nzuri katika kuelekea katika uchumi wa viwanda. Hili ni jambo jema sana litakaloivusha nchi yetu katika kuelekea kwenye uchumi mzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika miaka ya 1970 tuliweka viwanda vingi sana ambavyo kwa sasa vimepoteza uwezo wake na vingine vimekufa kabisa. Hivyo, kwanza naishauri Serikali iangalie sababu za kuanguka kwa viwanda hivyo. Sababu hizo ndizo zitakazotuongoza kuelekea kwenye azma hii baada ya kuzifufua.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, ni vyema Serikali ianze kujiandaa kwa kutayarisha rasilimali ambazo zitaweza kukabiliana na suala hili. Miongoni mwa rasilimali hizi ni rasilimali watu (HR). Serikali ianze kuwasomesha watu wetu badala ya kuja kutegemea wataalam kutoka nje ya nchi kama ilivyo katika sekta nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante.