Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Juma Othman Hija (16 total)

MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri napenda kumuuliza swali moja la nyongeza:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza katika majibu yake ya msingi anasema kwamba, Serikali imepata kiwanja! Sijui maana yake ni nini kwa sababu hicho kiwanja ni chetu watu wa Jimbo, siyo Serikali! Pamoja na hayo mpaka sasa hivi hatuoni dalili za uharaka wa ujenzi wa suala hili. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri anatuambia ni lini angalau wataanza kuweka msingi katika suala hilo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tuna dhamira ya dhati ya kujenga hiki kituo, lakini kama ambavyo nimezungumza mwanzo kwamba, tuna changamoto nyingi sana za mahitaji ya vituo mbalimbali. Kwa hiyo, ningechukua fursa hii kutoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge, akiwemo Mheshimiwa Mbunge wa Tumbatu, kuangalia uwezekano wa kuharakisha jitihada hizi kwa kuanza kushirikisha wananchi na hata ikibidi kutumia Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo ili baadaye Serikali iweze kuongeza nguvu zake.
MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mwenyekiti ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba kuuliza swali moja fupi la nyongeza. Malalamiko haya ni ya muda mrefu sana na kila siku yanazidi kwa wananchi. Je, Wizara imewahi angalau kuwaonya wamiliki wangapi angalau kwa barua mpaka kufikia mwaka uliopita?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yetu imeshawahi kuwaonya wamiliki IMTU na mwenzao KIU kwa kukiuka masharti hayo na hivyo tunazidi kusisitiza wamiliki wote wachukue fedha ambayo ni ada kwa kutumia fedha za Kitanza ni ana pale inapobidi iwe tu kwa wananfunzi ambao wanatoka nchi za nje
MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina swali moja la nyongeza.
Katika majibu yake ya msingi anasema kwamba Serikali inakamilisha mipango ya kupata fedha ya kujenga kituo hiki. Je, anaweza kutuambia kwa kiasi gani mipango hii imefikia? Under what percentage imefikia? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO NA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimejibu katika swali langu la msingi ni kwamba wakati Serikali inajipanga kuweza kuanza mchakato wa ujenzi wa Kituo cha Polisi Tumbatu, tayari kuna jitihada mbalimbali ambazo zimeshachukuliwa kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo yale. Ukiachia mbali jitihada ambazo nimezijibu katika swali la msingi za kuhakikisha kwamba tunaendeleza kupeleka askari wa doria mara kwa mara, lakini pia sasa hivi karibu na eneo la Tumbatu kwenye eneo la Mkokotoni kuna ujenzi wa Kituo cha Polisi Mkokotoni ambapo kiko katika hatua za mwisho kukamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka huu tumetenga fedha takribani shilingi milioni 200 kwa ajili ya kulimpa mkandarasi ili aweze kuendelea na kukamilisha kituo hicho ambacho kipo katika hatua ya mwisho. Tunaamini kabisa kwamba Kituo cha Mkokotoni kikimalizika, kitasaidia sana kuweza kusogeza karibu na Tumbatu huduma za polisi wakati ambapo jitiahada za ujenzi wa Kituo cha Tumbatu zikiwa zinaendelea.
MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri napenda kumuuliza swali moja la nyongeza.
Kwa upande wa Tanzania Bara maeneo yatakayohusika ameyataja, je, kwa upande wa Tanzania Zanzibar ni maeneo gani yatakayohusika na mradi huu?(Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa kama unavyofahamu fedha zile zimetolewa dola milioni 31 kwa ajili ya Zanzibar, lakini atakayeamua kwa upande wa Zanzibar fedha zile zinaenda kipande gani cha nchi ya Zanzibar ni Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Kwa hiyo, tumeshawasiliana nao wamesema wanafanya majadiliano na Serikali kwa ngazi za juu ili kuweza kuamua kwamba fedha hizi zitakwenda kuhudumia sehemu gani ya Zanzibara. (Makofi)
MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, wasiwasi wangu katika swali langu la msingi ni viwango vya miundombinu hii hasa nguzo. Wamesema kwamba TANESCO wana zoezi la kukagua nguzo kabla ya matumizi. Swali langu liko hapa: wanachukua hatua gani wanapogundua kwamba nguzo hizi ziko chini ya viwango? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Juma Othman Hija, kwa swali lake la nyongeza. Kama ambavyo jibu langu la msingi limesema, Shirika la TANESCO hufanya ukaguzi kwanza wa vifaa hivi kabla havijatumika kwenye miradi hii. Kwa hiyo, endapo inagundulika nguzo hizi hazina ubora, nguzo hukataliwa na wanaotekeleza miradi miradi hiyo huelekezwa kutimiza vigezo na hasa vile viwanda ambavyo vinatengeneza hizi nguzo. Ahsante sana.
MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Tafsiri hii ni nzuri sana, lakini ni ya kitaalam zaidi. Je, sasa Serikali ina mpango gani kuwaelimisha wananchi juu ya tafsiri hii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza nimhakikishie tu Mheshimiwa Hija kwamba toka maambukizi ya virusi vya UKIMWI yalipotokea miaka ya mwanzo ya 1980 Serikali pamoja na wadau mbalimbali tumekuwa tukishirikiana kuelimisha wananchi juu ya virusi vya UKIMWI, UKIMWI, magonjwa nyemelezi, lakini pia madhara yanayotokana na UKIMWI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi hiyo imeendelea na imefanyika kwa ufanisi mkubwa na kwa mafanikio makubwa sana. Ndiyo maana leo hii ninavyozungumza hapa, kiwango cha maambukizi ya UKIMWI kimepungua sana mpaka kufikia sasa hivi tuna kiwango kama cha asilimia 4.6 tu (prevalence rate).
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa msingi huo tuna mafanikio makubwa sana kwenye eneo hili kuliko anavyofikiria. Vile vile tutaendelea kutumia mbinu ambazo tumekuwa tukitumia, lakini pia ubunifu wa taasisi mbalimbali tunazoshirikiana nazo kuweza kuzidisha uelewa wa wananchi juu ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI na UKIMWI wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda tu kwa ufupi nitoe elimu tu kidogo hapa kwamba virusi vya UKIMWI, yaani VVU ama HIV ama kitaalam Human Immunal Deficiency Virus, ni kirusi ambacho kipo katika familia ya retroviridae na viko virusi vingi vinavyosababisha magonjwa mbalimbali yanayosababishwa na virusi hiki nacho kimo katika kundi hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi kinayofanya ni kuingia kwenye chembe chembe ya mwanadamu ya aina ya white blood cell ambayo inahusika na kinga mwilini na kitakaa mle kwa miaka kati ya hiyo mitano mpaka 10 hadi 12 bila kujulikana na baada ya hapo sasa kama mtu alipima atajulikana, lakini kama hakupima, haitajulikana kwamba ana maambukizi. Kuanzia hapo zile cells za kinga zitapungua mwilini na mtu sasa ataanza kuonesha dalili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale mtu anapoanza kuonesha dalili kwamba amepungua kinga mwilini, ndiyo tunasema amepata UKIMWI. Hiyo ndiyo tofauti. Isipokuwa unaweza ukaishi na hicho kirusi kwa muda huo niliousema bila kuonesha dalili; na kwa maana hiyo, utakuwa na kirusi tu, lakini hauna UKIMWI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa UKIMWI maana yake ni ugonjwa unaokuja baada ya kuwa umeambukizwa virusi vya UKIMWI labda miaka mitano ama kumi huko nyuma, kinga ikashuka, sasa ndiyo unaanza kupata UKIMWI na kwa sababu kinga imeshuka, magonjwa ambayo kwa kawaida hayatokei kwenye watu wenye afya, yanaanza kutokea kwako kama magonjwa mbalimbali ya cancer mbalimbali, kama Kaposi’s sarcoma, magonjwa ya kukohoa kama Kifua Kikuu, magonjwa ya kifua kisichopona mara kwa mara; magonjwa ya ngozi kama herpes zoster na vitu vingine. Kwa hiyo, hapo tunasema sasa una UKIMWI.
MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwanza na mimi nipongeze Wizara kwa speed nzuri wanayochukua ya kusambaza umeme vijijini. Hata hivyo nina suala moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maeneo ambayo Mheshimiwa Wazairi ametueleza pia kuna taasisi za Serikali ambazo Mheshimiwa Waziri hakuzitaja. Je, nini mikakati ya kuziunganishia taasisi za Serikali, umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa. Kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Hija kwa pongezi zake kwenye swali lake; la nyongeza ameuliza mkakati wa Serikali wakusambazia umeme taasisi za Kiserikali. Kama nilivyosema kwenye jibu langu la mzingi katika utekelezaji wa REA I na II kulikuwa na mapungufu ya kuruka baadhi ya maeneo na hususani Taasisi za Kiserikali utekelezaji wa REA III kama Serikali tumetoa maelekezo kwamba taasisi zote za Serikali zipatiwe kipaumbele na napenda kuwashukuru wakandarasi wote wamekuwa wakitekeleza maelekezo haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo napenda nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwa sasa kwa makandarasi wameendelea kuunganisha maeneo ya Kiserikali iwe ya zahanati, miradi ya maji, vituo vya afya na hospitali. Nakushukuru.
MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, lakini nina swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu zinaonesha kwamba, bado asilimia ni ndogo sana ya watumizi wa mfuko huu. Je, Serikali ina mikakati gani ya kuwaelimisha Wananchi, ili aweze kujiunga na mfuko huu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tunatambua kwamba bado idadi kubwa sana ya Watanzania hawajafikiwa na huduma ya bima ya afya, lakini tunatambua vilevile gharama za matibabu zinazidi kuongezeka. Kwa hiyo, sisi kama Serikali tunaendelea kupanua wigo wa vifurushi vyetu ili kuhakikisha kwamba tunaweza kuwafikia Watanzania wengi zaidi, lakini sambamba na hilo tunaendelea kuboresha vifurushi, lakini tunaboresha vilevile utaratibu wa wananchi kuweza kuchangia na moja ya mkakati tunaoufikiria ndani ya Serikali ni utaratibu wa jipimie, ambapo mwananchi atakuwa anachangia kadiri kipato chake kinavyoruhusu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mkakati wa muda mrefu ambao tunaendelea kuufanyia kazi, dunia ya sasa imeelekea katika Mpango wa Bima ya Afya kwa wananchi wote na sisi kama Tanzania tumeridhia azimio hilo la kidunia na sasa hivi tuko katika mchakato wa kuandaa muswada wa sheria ambao utafanya bima ya afya kuwa ni kwa lazima kwa Watanzania wote.
MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Namshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake marefu lakini ambayo hayakujibu swali langu la msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la msingi ni kwamba nilikuwa naulizia matayarisho ya rasilimali watu ambao watakuja kuendesha viwanda vyetu. Mheshimiwa Waziri amenijibu mambo ya mikopo, elimu na kadhalika. Nilichokuwa naulizia hapa ni kwamba sisi sasa hivi tuna siasa ya kuendesha viwanda. Je, tuna matayarisho gani ya kuja kuendesha hivi? Tuna matayarisho kwamba kwa mfano, mtu anaweza akawekeza viwanda lakini baadaye viwanda vile vikaja vikaendeshwa na watu kutoka nje ya nchi. Je, sisi Watanzania tuna matayarishoi tgani ya kuja kuendesha viwanda hivi? Hilo ndiyo swali langu lilikuwa la msingi lakini siyo suala hili ambalo Mheshimiwa Waziri amenijibu.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake ya msingi aliyoanza nayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2014/2015 Serikali ilifanya tafiti kubwa mbili muhimu sana kwneye nchi yetu. Utafiti wa kwanza ni kujua aina ya nguvukazi tuliyonayo na utafiti wa pili ni aina ya ujuzi uliopo katika nguvukazi tuliyonayo wa kuweza kukidhi uchumi kwenye sekta za vipaumbele ambavyo vimewekwa kwenye mpango wa maendeleo, na hasa kwenda kwenye uchumi huo wa viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, baada ya tafiti mbili hizo kubwa kufanyika mpaka sasa ndani ya nchi yetu tunajua mahitaji ya ujuzi katika uchumi wa viwanda yanapungukiwa kwenye maeneo yapi. Ndiyo maana Ofisi ya Waziri Mkuu baada ya kugundua hayo mahitaji ya ujuzi unaohitajika kwenye viwanda na Waheshimiwa Wabunge kila mwaka mmekuwa mkitutengea bajeti ya shilingi bilioni 15; sasa bilioni 15 hizo ndizo zinazotumika kwenye programu tano alizozisema Mheshimiwa Naibu Waziri na nyingine za kujenga ujuzi kwa mahitaji ya viwanda vilivyoko katika nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwahakikishie Wabunge jambo hilo tunalielewa na tunalifanyiakazi vizuri sana.
MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri na ya kutosheleza kabisa, lakini nina swali moja dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni Serikali imekuwa na zoezi la kuyafungia maduka ya Bureau De Change nchi nzima. Je, zoezi hili ni miongoni mwa mikakati ya kuimarisha fedha yetu au ni kwa madhumuni gani?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali moja la Mheshimiwa Juma Othman Hija, Mbunge wa Tumbatu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyouliza je, ulikuwa ni mkakati wa kuhakikisha thamani ya fedha yetu. Kama nilivyoeleza kwenye jibu langu la msingi moja ya kazi za benki kuu ni kuhakikisha kwamba thamani ya fedha yetu inakuwa imara na katika mikakati ya kuhakikisha hilo, ni kuhakikisha kunakuwa na usimamizi imara na madhubuti wa maduka yetu ya kubadilisha fedha na hilo ndilo lilikuwa lengo la zoezi lililofanyika.
MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mheshimiwa Spika, ahsante, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri na ya kutoshereza kabisa, lakini nina swali moja la nyongeza.

Majibu yake yamejikita sana kwenye maeneo ya miji, swali langu ni kwamba Serikali ina mpango gani, huduma hizi kuzipeleka katika visiwa vidogovidogo kama vile Tumbatu?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema huduma zetu za TPB zimeongezeka kwa kiwango kikubwa na tumeweza kuwafikia wananchi walio wengi na kwa visiwa vyetu kwa Zanzibar tumeshafungua matawi tayari na sasa tunajipanga kwenda kufungua katika visiwa hivi vidogo, wakati huo tukiendelea kuwahudumia kwa kupitia mfumo wa kidigitali.
MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nashukuru Serikali kwa majibu yake mazuri na ya kupendeza. Mheshimiwa Waziri katika jibu lake la msingi amesema kwamba kabla ya kutekeleza suala hili kwanza watafanya utaalam. Je, tathmini hii ya kitaalam itafanyika lini katika kisiwa hiki cha Tumbatu ili kuwapa wananchi manufaa zaidi. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hija, Mbunge wa Tumbatu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, tathmini ya kitaalam ambayo tunategemea kuifanya eneo la kisiwa alichokitaja Mheshimiwa Mbunge litakuwa ni sambamba pamoja na tathmini ya kitaalam ya maeneo yote ya mipakani nchini kwetu Tanzania pamoja na visiwa vyote ambavyo vinahitaji kupata mawasiliano. Tathmini hiyo tunategemea kuifanya kuanzia tarehe Mosi mwezi wa kwanza mpaka 2020 katika maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya kuhakikisha kwamba maeneo hayo ambayo ni muhimu kwa nchi yetu yote yanapelekwa huduma za mawasiliano.
MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri na ya kuridhisha ya Serikali, nina swali fupi la nyongeza: -

Mheshimiwa Spika, ili kuongeza wigo wa usikivu nchini, TBC haioni kwamba kuna haja ya kuwasiliana na redio za kijamii ili kuziwezesha kujiunga na TBC Taifa wakati wa matokeo makubwa kama vile taarifa ya habari na mengineyo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Juma Othman Hija kama ifuatavyo: -


Mheshimiwa Spika, ni mpango wa Serikali kuhakikisha kwamba Shirika la Utangazaji TBC linafanya mahusiano mazuri na Shirika la Utangazaji la Zanzibar. Baada ya kukamilisha katika miradi yetu ya awali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, tuna mpango wa kuja kushirikisha na redio zingine ili pale ambapo Shirika la Utangazaji Tanzania linapokuwa na changamoto ya miundombinu basi iweze kushirikisha redio nyingine ambazo zitakuwa zinasaidiana. (Makofi)
MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali na nimeridhika na majibu hayo ya Serikali, lakini nimepata wasiwasi juu ya ufuatiliaji wa kazi hii. Barua ya hati miliki tu imechukua miaka miwili tangu Aprili, 2020 mpaka leo 2022 hakuna majibu yoyote. Je, Mheshimiwa Waziri ananiahidi nini kunitoa wasiwasi huu juu ya ufuatiliaji wa kazi hii?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Hija, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana naye kwamba si kawaida kuchukua muda mrefu namna hii hasa baada ya Jeshi la Polisi kuwa wamelipa Sh.2,200,000 kwa ajili ya kupata hati ya kiwanja hicho. Tutafuatilia kwa karibu na kupitia hadhara hii, nimwombe Kamishna wa Polisi Zanzibar afanye ufuatiliaji yeye binafsi ili kuhakikisha kwamba hati inapatikana, hatimaye ujenzi kwenye eneo hili uweze kuanza. Nashukuru.
MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa changamoto zinazoikabili mtaji wa sekta binafsi ni viwango vya riba katika benki zetu. Je, Serikali ina mpango gani kudhibiti viwango hivi vya riba? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Juma Othman Hija, Mbunge wa Tumbatu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania ilishatoa trilioni moja kwa benki ili kutoa mikopo hasa ya kilimo kwa riba nafuu, isiyozidi asilimia 10 na zipo Benki zetu kama vile CRDB, NMB katika dirisha la kilimo wapo na single digit. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imezingatia na itaendelea kuangalia viwango vya riba kulingana na hali ya uchumi nchini, ahsante.
MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa wahamiaji haramu bado wamekuwa wakionekana wanaingia nchini na wanapopatikana wanapelekwa katika Magereza yetu ambako wanaongeza gharama za bajeti katika Magereza yetu: Je, Serikali haioni haja ya kuwarejesha kwao mara tu wanapowakamata? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Othman, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli wapo wahamiaji haramu ambao wanapokamatwa hurejeshwa kwenye nchi zao, lakini wapo ambao wakati tunafanya mawasiliano na nchi zao, huwekwa Magerezani na wapo wanaofungwa kutokana na aina ya makosa waliyoyatenda, ahsante sana.