Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Mboni Mohamed Mhita (6 total)

MHE. MBONI M. MHITA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kutokana na changamoto za daraja la Wami kufanana sana na changamoto za madaraja ambayo yanaunganisha barabara inayotoka Handeni kwenda Turiani, je, ni lini Serikali itaanza mchakato wa ujenzi wa madaraja haya ili barabara inayounganisha Handeni na Mkoa wa Morogoro iweze kufanya kazi na kupitika? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, barabara anayoongelea Mheshimiwa Mboni Mhita pamoja na madaraja ambayo yamo katika barabara hiyo ni sehemu ya barabara iliyotolewa ahadi na viongozi wetu wa Kitaifa ijengwe kwa kiwango cha lami. Nami naomba nimhakikishie, tupo hapa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ambapo kazi yetu kubwa ni moja tu kuwajengea miundombinu Watanzania kwa kuhakikisha kwamba ahadi zote za viongozi wetu wakuu zinatekelezwa. Pamoja na kwamba madaraja haya na barabara hii kama alivyoona katika bajeti tuliyoipitisha haikuwekewa fedha ya kutosha, nimhakikishie baada ya kukamilisha madaraja na barabara ambazo tayari wakandarasi walikuwa site kuanzia Awamu ya Nne, tutaanza kushambulia ahadi ambazo zilitolewa na viongozi wetu na ahadi zote zilizopo katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi kuhakikisha kwamba tunazikamilisha katika miaka inayofuata.
MHE. MBONI M. MHITA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuweza kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Jimbo la Handeni Vijiji kwenye Kata ya Kang‘ata eneo la Magambazi, kuna mgogoro kati ya wananchi na mwekezaji lakini kwa sasa mgogoro huo unasubiri maamuzi kutoka kwenye Wizara ya Nishati na Madini. Lakini wakati huo huo mgogoro huo umeweza kusimamisha shughuli nyingi ambazo kwa namna moja ama nyingine zingeweza kunufaisha wananchi wa Kata ya Kang‘ata na eneo la Magambazi. Je, ni lini Wizara itatoa maamuzi juu ya utatuzi wa mgogoro huu ili shughuli ziweze kuendelea? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli maeneo ya Handeni pamoja na maeneo mengi ya Kilindi kuna migogoro mingi sana kati ya wachimbaji wadogo, wananchi pamoja na wawekezaji kutoka nje. Lakini kwa jitihada ambazo tumechukua hasa kwa maeneo ya Handeni wiki iliyopita tulimtuma mkaguzi wa migodi kwenda kukagua migogoro iliyopo kati ya wananchi wa Magambazi pamoja na wawekezaji wanaochimba pale. Hivi sasa kampuni ambayo ilikuwa inachimba pale Kampuni ya Scanda ambayo pia ilifanya utafiti haijakamilisha kazi zake. Lakini nimhakikishie tu timu yetu ipo pale sasa na tukitoka hapa Mheshimiwa wa Handeni tukae tukubaliane tufuatilie timu imefikia hatua gani lakini tumeipa muda wa wiki mbili na wiki ijayo wataleta taarifa na taarifa hiyo tunahakikisha kwamba itatoa suluhisho na mgogoro wa wananchi wa Handeni pamoja na wachimbaji hao.
MHE. MBONI M. MHITA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri kwamba Jimbo la Handeni Vijijini ambalo kwa upande mmoja ni barabara kubwa ya Mkata kupitia Korogwe kuja mpaka Misima; ila askari wa Jimbo la Handeni ama Wilaya nzima ya Handeni hawana usafiri wa ku-patrol, jambo ambalo naamini kama wangeweza kuwa na usafiri huo kwa namna moja ama nyingine wangeweza kupunguza idadi ya ajali ambazo zinatokea. Lakini pia, swali langu la pili…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mboni, swali la nyongeza huwa ni moja.
MHE. MBONI M. MHITA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali hili nalo vilevile tumelichukua. Tutaangalia vilevile utaratibu na hali halisi ilivyo na changamoto ya eneo la Handeni na changamoto za maeneo mengine na idadi ya magari ambayo tutayaingiza kwa awamu inayokuja. Pia tutalipa uzito kwa kutilia maanani changamoto ambazo ametueleza Mheshimiwa Mbunge.
MHE. MBONI M. MHITA: Mheshimiwa Naibu Spika, matatizo ya maji katika Jimbo la Lushoto yanafanana sana na matatizo ya Jimbo la Handeni Vijijini. Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuweza kufanya ziara katika Jimbo la Handeni Vijijini na kujionea matatizo ya Maji katika Jimbo hili? Je, yuko tayari ama anatoa commitment gani kwa fedha ambazo amesema zitatoka kwa miradi ya maji katika Jimbo la Lushoto? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na swali la mwisho. Mheshimiwa Naibu Waziri anatoa commitment gani; tayari Bunge lako limeshapitisha bajeti ya Mwaka wa Fedha wa 2016/2017 na katika bajeti hiyo kuna shilingi bilioni 3.4 kwa ajili ya Lushoto, kwa hiyo, hakuna commitment zaidi ya hiyo. Nimwombe tu Mheshimiwa Mbunge sasa ashirikiane na Halmashauri ili kuendelea sasa kufanya matumizi ya hizi fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, matatizo ya Handeni. Tayari tuna mradi wa HTM ambao utekelezaji wake unaanza mwaka wa fedha unaokuja. Ni mradi mkubwa ambao utapitia maeneo mengi katika Mji wa Handeni na hatimaye kuhakikisha kwamba, tunakamilisha mradi huu. Maeneo ambayo hayatafikiwa na mradi huo Halmashauri zihakikishe kwamba, zinatumia fedha iliyopangwa kwa ajili ya ama kuchimba visima au kutengeneza mabwawa kwa ajili ya kuhakikisha kwamba, wananchi wote wa eneo hilo wanapata huduma ya maji. Kama fedha hazitatosha zilizopangwa basi ni wajibu wa Halmashauri kuhakikisha wanaleta maombi ili tuweze kutenga fedha katika Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. MBONI M. MHITA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuniona. Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Handeni Vijijini, Kata ya Mkata tulibahatika kupata mabwawa mawili, moja likiwa Mkata lakini la pili likiwa eneo la Manga.
Mheshimiwa Naibu Spika, mabwawa haya yako chini ya kiwango na mpaka sasa hayajaweza kuanza kutumika. Nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri katika ziara yake katika Jimbo la Handeni Vijijini alipita na kujionea hali halisi ya yale mabwawa. Pia aliweza kutuahidi wananchi wa Jimbo la Handeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakuja hapo. Mheshimiwa Naibu Waziri alituahidi baada ya kuona yale mabwawa kwamba wangefanyia kazi na kuweza kutupa ripoti ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa wale ambao wamefanya ubadhilifu ili kuweza kupata utatuzi wa maji.
Wananchi wa Handeni Vijijini wangependa kujua, je, utatuzi umefanyika na ripoti imeshafanyiwa kazi ili tuweze kujua na hatua stahiki ziweze kufanyika kwa wale ambao wamefanya ubadhilifu huu? Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitembelea kweli eneo hilo la Mkata nikakuta kazi iliyofanyika na kazi hiyo nilizungumza kwenye vyombo vya habari kwamba hata mimi sikuridhika nayo. Baada ya hatua hiyo Katibu Mkuu aliunda Tume ya Wahandisi kwenda kukagua hilo eneo, sasa hivi wanakamilisha kuandaa taarifa ili iweze kuwasilishwa Wizarani ili kuweza kuchukua hatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo lengo letu ni kuhakikisha wananchi wanapata maji. Tuliweka utaratibu mwingine tumeshatangaza tenda tayari kwa ajili ya kupanua mradi wa HTM pale Korogwe ili uhakikishe kwamba unapeleka maji hadi Handeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tulishasema tunaweza tukatumia chanzo cha Wami ili tuweze kuchukua yale maji kuhakikisha kwamba eneo la Handeni Vijijini linapata maji ya kutosha.
MHE. MBONI M. MHITA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuniona. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri swali la nyongeza.
Katika bajeti iliyopita Mheshimiwa Waziri alituahidi wananchi wa Jimbo la Handeni Vijijini kuweza kupata Kiwanda cha Matunda katika Kata ya Kwamsisi na mpaka hivi leo bado wananchi wa Jimbo la Handeni Vijijini wana matumaini makubwa na hakuna ambalo limefanyika. (Makofi)
Je, Mheshimiwa Waziri mko katika hatua gani ili kuweza kuwawezesha wananchi wa Jimbo la Handeni Vijijini kupata kile kiwanda ambacho mlituahidi? Ahsante.
WAZIRI WA VIWANDA BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo, Mradi wa Kiwanda cha Matunda Handeni bado upo. Mwekezaji ambaye anawekeza kiwanda, anayelima Bwana Roy Nightingale ameshaanza kuzalisha ndizi kwa ajili ya kiwanda hicho. Sasa ndizi zake zinauzwa kwenye Kiwanda cha Elven.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nisamehe kitu kimoja, niwaelezee kiwanda cha Elven. Kiko kiwanda kinakausha matunda na matunda hayo yanauzwa Ulaya, kiko sehemu ya Bagamoyo juzi nimekikagua pamoja na Mkuu wangu wa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania mpaka ninapozungumza hatuwezi kutosheleza kiwanda hicho kwa matunda. Kwa hiyo, wakati matunda yenu mtayauza Bagamoyo, Kiwanda chenu cha Nightingale, mwekezaji binafsi kinaendelea. Ni matatizo ya kifedha lakini nitaendelea kusimamia na wewe tushirikiane, kiwanda hicho ningependa kuona kinajengwa na kufanya kazi. (Makofi)