Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Omari Mohamed Kigua (10 total)

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021
MHE. OMAR M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Awali ya yote kabla sijaanza kuchangia juu ya Mpango huu wa Serikali, napenda kwanza nikushukuru wewe na niwashukuru Wanakilindi walionipa fursa hii ya kuweza kuwa Mbunge wao wa Jimbo la Kilindi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimepitia Mpango huu, una mambo mengi mazuri, nami naamini kabisa nia ya Serikali hii ni kuleta maendeleo ya dhati kwa wananchi wa nchi hii ya Tanzania. Mpango huu umeangalia mambo muhimu sana ambayo kwa muda mrefu yalikuwa hayaendi sawasawa, sasa basi ni mambo gani ambayo nayadhamiria kwa leo kuyazungumzia? Nitaanza moja kwa moja kwenye Sekta ya Mawasiliano tunapozungumzia barabara.
Mheshimiwa Spika, suala la miundombinu ni suala muhimu sana, nikiamini kwamba miundombinu ikiwa ni mizuri, basi maendeleo ya maeneo mbalimbali na ya nchi kwa ujumla yataweza kufanikiwa. Katika eneo la barabara, naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuliwekea uzito unaostahili kwa sababu maeneo mengi yalikuwa hayapitiki hususan barabara katika kiwango cha lami. Hili limeweza kufanikiwa, nami naomba niipongeze Serikali katika suala hili.
Mheshimiwa Spika, katika eneo langu ambalo nimetoka katika Jimbo la Kilindi, kuna mpango wa kuijenga barabara ile kwa kiwango cha lami ambapo barabara ile itaanzia Handeni kwenda Kibirashi hadi Kiteto kupitia Namrijo Juu pamoja na Jimbo la Mkoa wa Singida.
Mheshimiwa Spika, nataka nilizungumzie suala hili kwa sababu kama nilivyozungumza awali kwamba mawasiliano ni kitu muhimu sana, katika eneo langu ninalotoka kuna mazao yanalimwa hususan mahindi na utakuta hata nchi jirani mazao mengi yanakuja kuchukuliwa Jimbo la Kilindi, lakini kwa sababu miundombinu siyo mizuri, unakuta mazao mengi yanaishia kuozea katika mashamba.
Mheshimiwa Spika, namshauri kaka yangu, Mheshimiwa Profesa Mbarawa pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri waliangalie hili, japokuwa najua kwa mwaka huu wa fedha unaoanza Julai hautakuwepo Mpango huu, lakini barabara hii ipewe kipaumbele cha hali ya juu kwa sababu italeta maendeleo ya dhati kwa wananchi wa Kilindi na Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, sehemu nyingine ambayo ningependa kuchangia ni Sekta ya Madini. Nimeona imezungumziwa hapa; na tunapozungumzia madini, tunazungumzia Sekta ya Nishati. Ni kweli kwamba umeme ndiyo kila kitu na Mheshimiwa Waziri hususan Waziri wa Nishati na Madini, ameweza kuweka mipango mizuri sana juu ya nishati, lakini nishati hii haijafika maeneo mengi hususan katika vijiji.
Mheshimiwa Spika, nitolee mfano tu katika Jimbo langu la Kilindi. Tunavyo vijiji kama 102, lakini vijiji vichache sana ambavyo vimenufaika na huduma hii ya umeme kwa maana ya REA, ushauri wangu ni kwamba, yale maeneo ambayo kwa asilimia kubwa wameshapata huduma hii, basi waangalie maeneo mengine ambayo hayajanufaika na huduma hii, kwa sababu wananchi hususan wa vijijini wanahitaji umeme kwa ajili ya maendeleo, wanahitaji umeme kwa ajili ya shughuli mbalimbali. Ni imani yangu kwamba Serikali italiangalia hili kwa umuhimu wa juu sana.
Mheshimiwa Spika, lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni suala la maji. Maji imekuwa ni kilio, kila Mbunge anayesimama hapa anazungumzia suala la maji. Labda tu nizungumzie kwa eneo ninalotoka mimi. Ni kwamba eneo lile lina maji mengi sana lakini hatuna visima na miundombinu kwa kweli ni ya muda mrefu kiasi kwamba maji imekuwa ni tatizo kubwa sana.
Mheshimiwa Spika, ushauri wangu kwa Mheshimiwa Waziri wa Maji ni kwamba, maji yanapotea sana. Kuna Mpango kule wa bwawa katika Kata ya Kibirashi; utaratibu ule wa kuhifadhi maji kwa njia ya mabwawa ni utaratibu mzuri sana. Badala ya kuchimba visima tuwe na njia ya kuweza kuhifadhi maji kwa njia ya mabwawa. Nadhani utaratibu huu ni mzuri sana. Ni utaratibu ambao unaweza ukaisaidia Serikali kupunguza kero ya maji kwa muda mrefu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, utakuta sasa hivi mvua zinanyesha kule lakini maji mengi yanapotea kwa sababu hatuna utaratibu mzuri wa kuhifadhi maji. Nadhani muda umefika sasa, tuone namna ya kuwashirikisha wananchi pamoja na Serikali juu ya kuweka visima au kuweka mabwawa ambayo yanaweza kuhifadhi maji kwa muda mrefu. Kwa sababu ukiangalia katika eneo langu, siyo rahisi kusema labda maji yatoke Ruvu yafike Kilindi; lakini njia mbadala ambayo inaweza kusaidia kutatua tatizo hili la maji ni kuhakikisha kwamba tunakuwa na mabwawa.
Mheshimiwa Spika, naishukuru Serikali yangu kwamba imeweza kuliona hili, tuna bwawa la mfano kabisa ambalo halijakamilika, liko Kata ya Kibirashi. Bwawa hili litawanufaisha wafugaji pamoja na wakulima, naishukuru sana Serikali yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo ningependa kugusia ni suala la viwanda. Nimeona Serikali yetu ina mpango mzuri sana wa viwanda hususan kufufua viwanda vya zamani pamoja na viwanda vipya. Naomba niipongeze Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi katika hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa kinachonishangaza hapa, ukiangalia upande wa Tanga ambapo tulikuwa na viwanda vingi sana; tulikuwa na viwanda vya matunda, lakini viwanda vile vimekufa. Nashauri kwamba muda umefika wa kuvifufua viwanda vile pamoja na kuanzisha viwanda vingine.
Mheshimiwa Spika, eneo ninalotoka kuna wafugaji wengi sana, lakini nikiangalia Mpango huu, sioni namna ambavyo wananchi hususan wafugaji wa Wilaya ya Kilindi wanaweza kunufaika na Mpango huu wa viwanda vidogo vidogo. Sasa najiuliza, mifugo hii ambayo Wanakilindi wanayo, watanufaika na nini katika hili? Namshauri kaka yangu Mheshimiwa Waziri wa Viwanda pale aangalie namna ambavyo tunaweza na sisi wananchi wa Kilindi tukaweza kupata kiwanda kidogo cha kuweza hata kutumia maziwa haya mengi ya mifugo ya Wilaya ya Kilindi ili wananchi waweze kunufaika na fursa hii ambayo wanapata wananchi wa sehemu nyingine.
Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo ningependa kuchangia ni suala la utalii kwa ujumla. Ni kwamba eneo la utalii ni eneo muhimu sana ambalo naamini Serikali yetu lazima itie msisitizo wa hali ya juu sana. Wengi wamezungumza hapa kwamba watalii wanafika Kenya, halafu wana-cross wanakuja Tanzania. Hili limeelezwa kwamba mpango mzuri wa Serikali ni kununua ndege kusaidia kufanya watalii waweze kufika nchini kwetu kwa urahisi zaidi.
Mheshimiwa Spika, napongeza mpango huu, ni mzuri na wale ambao wana-discourage suala hili, naona hawako pamoja na sisi. Naomba Serikali yangu iendelee mbele na utaratibu huu. Pia kuna maeneo ambayo Mheshimiwa Waziri wa Utalii naona hawajafika maeneo mengi, labda nitoe mfano mmoja, katika eneo ninalotoka, kuna Mbuga ya Wanyama ya Saunyi. Mbuga ya Saunyi ina wanyama wa aina mbalimbali, lakini nina wasiwasi kama Serikali inajua kama kule kuna mbuga za wanyama.
Mheshimiwa Spika, fursa ile inawezekana hata wanyama ambao wanachukuliwa kwenda nje ya nchi, wanachukuliwa kutoka kule kwa sababu sijawahi kusikia hata siku moja watu wanaizungumzia Mbuga ya Saunyi.
Mheshimiwa Spika, nashauri kwamba ili tuweze kuimarisha utalii, ni kwamba Serikali iwe na utaratibu mzuri wa kuhakikisha kwamba kila fursa ya utalii iliyopo, inatumika vizuri. Haya ni mambo ya msingi ambayo wenzetu wa nchi jirani wameweza kuzitumia na kwa hakika uchumi wao umeweza kwenda juu sana kwa kutumia utalii vizuri. Nina imani kwamba tunavyo vivutio vingi sana lakini Serikali haijatumia vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia napenda kuchukua fursa hii kuzungumzia changamoto ambazo tunazipata katika madini. Ni kwamba nchi yetu ina madini mengi sana, maeneo mengi yana madini na Wilaya ninayotoka mimi, Jimbo langu la Kilindi lina maeneo mengi sana yenye madini, lakini wachimbaji wadogo hawajaweza kunufaika na Mpango huu. Hawajanufaika pengine kwa sababu ya sheria zilizopo.
Mheshimiwa Spika, nitoe mfano mmoja tu kwamba hawa wachimbaji wadogo wadogo ndiyo watu wa kwanza ambao huwa wanagundua wapi pana madini. Mchimbaji huyu mdogo akishapatiwa license, inapokuwa muda wake umepita, hapewi fursa mchimbaji huyu kwa sababu hana uwezo. Unakuta license hizi wanaopewa watu wengine wenye uwezo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo hili limeleta malalamiko makubwa sana na namwomba kaka yangu Waziri wa Nishati na Madini aliangalie tena na atakapoleta Muswada wake hapa tuangalie upya sheria hizi zinazohusu wachimbaji wadogo wadogo kwa sababu naamini Serikali ina nia nzuri ya kuwawezesha wananchi wadogo ili waweze kusimama vizuri kiuchumi.
Mheshimiwa Spika, haya mambo ni ya msingi sana kwa sababu sisi kama Wawakilishi wao tunapata malalamiko mengi sana hususan katika maeneo ambayo yana wachimbaji wadogo wadogo. Ni imani yangu kwamba itakapofika muda wa kuchangia Bajeti ya Nishati na Madini, hili tutalichangia kwa nafasi nzuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala lingine ni elimu. Elimu ni kila kitu. Elimu imezungumzwa hapa na nashukuru kwamba Serikali imeliangalia kwa kulipa kipaumbele. Kama alivyozungumza Mheshimiwa mwingine aliyepita hapa, amezungumzia juu ya kuvipa kipaumbele hivi Vyuo vya VETA. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Vyuo vya VETA vimeweza kuinufaisha nchi hii kwa muda mrefu sana hususan wanafunzi ambao hawajapata fursa kwenda Sekondari. Nashauri kila Wilaya, kila Mkoa, ikiwezekana tuwe na VETA ili iweze kuwasaidia vijana wetu, kwa sababu tumezungumzia kwamba tunataka tuwe na viwanda. Viwanda hivi watendaji au wafanyakazi hawatakuwa ni ma-graduate peke yake, ni lazima tutahitaji kada za katikati ambazo zitazalishwa kutokana na VETA.
Mheshimiwa Spika, katika Jimbo langu nilikuwa nafuatilia kabla sijawa Mbunge, ni kwamba kulikuwa na ahadi ya kujenga Chuo cha VETA katika Jimbo la Kilindi Kata ya Kibirashi. Bahati mbaya ahadi hiyo imekuwa ni hewa, lakini naamini kabisa Serikali yangu ni sikivu, watanisikiliza na wataweza kutimiza wajibu wao katika hili, kwa sababu wananchi wanahitaji VETA kwas ababu watoto wengi hawapati fursa ya kupata mafunzo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimezungumzia hili kwa uchungu mkubwa sana kwa sababu maeneo tunayotoka sisi, wananchi vipato vyao ni vya chini sana na sio wote ambao wana uwezo wa kupeleka watoto wao sekondari. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, labda nikwambie tu, Wilaya yangu ya Kilindi kwa mwaka huu imekuwa ni Wilaya inayoongoza kimkoa katika matokeo ya Kidato cha Nne mwaka 2015. Naomba kwa niaba ya Halmashauri ya Kilindi, nimshukuru pia Waziri wa Elimu kwamba amefanya jitihada kubwa sana kuhakikisha kwamba pamoja na changamoto nyingi tulizonazo tumeweza kusonga mbele.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. OMAR M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote naomba nikushukuru kwa kunipa fursa jioni ya leo niweze kuchangia bajeti ya Wizara ya Sheria. Kwanza naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri husika wa Wizara hii kwa bajeti nzuri sana ambayo ameiwasilisha kwa siku ya leo. Bajeti hii imechukua mambo mengi sana ambayo yalikuwa ni kilio cha wananchi, nikiamini kabisa kwamba imeweza kujibu kilio cha wananchi wa maeneo mbalimbali, hususan wa Jimbo la Kilindi ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakililia Mahakama ya Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa hatua zake anazochukua za kutumbua majipu.
Vilevile nimpe moyo kwa changamoto anazozichukua kwa wale watendaji ambao kwa muda mrefu wamekuwa ni matatizo ya nchi hii, ninaamini kabisa Waheshimiwa Wabunge na hata wale wa upande mwingine wanajua Mheshimiwa Rais anachukua msimamo ulio sahihi kabisa. Mambo haya ni ya msingi tukiweza kuyazungumzia kwa mustakabali wa nchi yetu hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijielekeze moja kwa moja kuchangia hususan kwenye Mahakama zetu. Tanzania hii ina Mahakama za Mikoa, Mahakama za Rufaa na Mahakama za Mwanzo, lakini ninaamini kabisa changamoto za Mahakama hasa hizi za Mwanzo na Wilaya zimekuwa ni kubwa sana, kwa maana kwamba mahakama nyingi zimekuwa chakavu na hazijafanyiwa ukarabati wa muda mrefu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna maeneo ambayo yana Wilaya lakini hayana Mahakama za Wilaya. Mfano katika Jimbo langu la Wilaya ya Kilindi ni takribani miaka 13 toka tumepata Wilaya lakini hatuna Mahakama za Wilaya. Jambo hili limekuwa ni kero kubwa sana kwa sababu wakazi wa Jimbo la Kilindi wamekuwa wakifuata huduma hii ya Mahakama kwa takribani kilometa 200 au 190 kutoka Wilaya moja hadi Wilaya nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Kilindi kwa ujumla ina changamoto nyingi sana za migogoro hasa ya wakulima na wafugaji. Kwa hiyo, unakuta kwamba, jambo hili limekuwa ni kero ya muda mrefu na hata Mbunge aliyepita alikuwa akilipigia kelele suala hili, lakini ninamshukuru Mheshimiwa Waziri husika kwenye bajeti yake ameweza kuliona hili na miongoni mwa Wilaya 12 ambazo zimetengewa hela kwa ajili ya kujengewa Mahakama ya Wilaya basi na Wilaya ya Kilindi imepata fursa hiyo. Naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala lingine ni suala la Mahakama hizi za Wilaya kutokuwa na Mawakili wa Serikali. Mawakili wa Serikali wamekuwa ni msaada mkubwa sana kwa wananchi ambao hawana uelewa wa elimu ya sheria. Nashauri hususan kaka yangu Waziri, Mheshimiwa Mwakyembe kwamba muda umefika sasa hivi wa kuwa na Mawakili katika kila Mahakama ya Wilaya, kwa sababu watu hawa wanawasaidia wananchi wasiokuwa na uwezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, labda niseme jambo moja, Mawakili katika kitabu chako umeeleza hapa kwamba mna mpango wa kupunguza idadi ya mrundikano ya kesi, kwa maana ya kwamba zero case backload! Mheshimiwa Waziri hebu nikuulize swali moja pengine utanipa maelezo wakati unajibu hoja hizi kwamba unatarajia Mahakama ya Wilaya at least iweze kujibu kesi 250 kwa mwaka, sasa Hakimu wa Wilaya ambaye anabeba Wilaya mbili kwa maana ya Wilaya ya Kilindi na Wilaya ya Handeni anawezaje kutatua kesi hizi kwa kipindi cha mwaka mmoja? Haya ni mambo ya msingi kabisa na unaweza tu ukaenda ukauliza pale Mahakama ya Wilaya ya Handeni kwamba, Hakimu ana idadi kiasi gani ya kesi za kutoka Wilaya hizi mbili?
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri kwamba wakati tunasubiria kujenga Mahakama ya Wilaya, sisi tunayo majengo katika Jimbo la Kilindi tunaweza tukapewa Hakimu wakati tunasubiri jengo likijengwa. Mimi nadhani fursa hii ni nzuri, ili tuweze kuwapa haki wananchi wa Wilaya ya Kilindi. Ninadhani changamoto hii haipo katika Jimbo langu tu, ipo katika Wilaya mbalimbali ambazo hazina Mahakama za Wilaya, nikiamini kwamba wananchi wanayo haki ya kuwa na huduma hizi za kimsingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo ningependa kuchangia siku ya leo ni suala la Serikali kupoteza kesi. Serikali inapokuwa inawashtaki watu mbalimbali mara nyingi huwa inapoteza kesi! Sasa tunatakiwa tujiulize sababu za msingi ni kwa nini Serikali inapoteza kesi? Haya ni mambo ya msingi kwa sababu wakati mwingine Serikali inashtaki mambo ambayo watu wamehujumu nchi! Tuchukulie mfano wa kesi ya samaki wale, Serikali imepoteza na inatakiwa kulipa fidia. Sasa ni nini kilichosababisha Serikali ikapoteza kesi hiyo wakati Serikali inao wataalam, inao Waendesha Mashitaka wa kutosha na wenye elimu yakutosha! Nadhani imefika muda sasa tuangalie utaratibu mzuri wa namna gani tunaweza kupata watu ambao wamebobea wanaoweza kuishauri Serikali katika mambo ya kesi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo ningependa kulichangia ni juu ya bajeti ya Wizara hii. Mheshimiwa Waziri husika wa bajeti hii amezungumza sana kwamba ana changamoto ya bajeti, nadhani kwa sababu Wizara hii inahusika na mambo ya sheria na mambo ya mahakama ifike wakati kwamba, Wizara hii yenyewe tuiongezee hela ili tuweze kuondokana na changamoto mbalimbali kwa ajili ya kutatua kesi za wananchi na kutoa haki kwa wananchi wa Tanzania kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ningependa kuchangia katika upande wa Mahakama za Mwanzo. Nichukulie mfano katika Jimbo langu la Kilindi, Mahakama za Mwanzo ziko chache sana! Jimbo lenye Kata 21 na vijiji visivyopungua 102, Mahakama za Wilaya nadhani ziko kama tatu kama siyo nne! Maana yake ni kwamba wananchi wanakosa haki zao za kimsingi. Kwa hiyo, imefika wakati Mheshimiwa Waziri husika ahakikishe kwamba ule mpango wa kuwa na Mahakama za Mwanzo katika kila Kata, basi mpango huo Serikali kwa dhati ya moyo wake ihakikishe kwamba mahakama hizo zinaanzishwa na zinakuwa na Mahakimu wa kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ningependa kushauri ni juu ya idadi ya Mahakimu katika Mahakama zetu. Sehemu nyingi sana utakuta utakuta kwamba, hatuna Mahakimu, lakini tunacho Chuo cha Mahakama Lushoto! Kwa nini Serikali isingetia nguvu pale tukahakikisha kwamba wataalam wengi wanapatikana, Mahakimu wanapatikana, ili Mahakama zetu ziweze kuwa na Mahakimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mpango huu kuna uanzishwaji wa Mahakama ya Mafisadi ambayo inatarajiwa kuanza mwaka wa fedha huu. Jambo hili nataka niipongeze sana Serikali hususan Mheshimiwa Rais kwa uamuzi wa dhati wa kuanzisha Mahakama hii. Mimi naamini kabisa kwamba muda umefika sasa hivi wa kuwa na Mahakimu wa kutosha katika kila Wilaya, kila Kata, ili wananchi wetu waweze kupata haki za msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ningependa kuchangia juu ya ukusanyaji wa maduhuli katika mahakama zetu. Nadhani utaratibu uliopo sasa hivi ni mzuri lakini inabidi uboreshwe sana. Uboreshwe kwa sababu mahakama hizi zina mahitaji mengi sana, wakitegemea OC ya Serikali maana yake uendeshaji wa mahakama hizi hautakwenda vizuri. Mimi ni imani yangu kwamba Serikali imesikia haya na imesikia michango ya Waheshimiwa Wabunge mbalimbali tukiamini kwamba muda umefika wa kuweza kutoa haki kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema maneno hayo machache, naomba kuunga mkono hoja ya bajeti hii. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia hotuba hii ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kama ifuatavyo:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi kubwa wanayoifanya. Kwa mwelekeo wa bajeti hii inayoonesha wazi Serikali imedhamiria kuboresha elimu kuanzia ngazi ya shule ya msingi hadi elimu ya juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze uamuzi wa Serikali kuhamishia Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDC) kuhamishwa Wizara ya Elimu kwa dhana ya dhamira ya kuvifanya vyuo hivi kutoa elimu ya ufundi, jambo hili litasaidia sana kuwezesha vijana wetu wengi ambao hawajapata fursa ya elimu ya sekondari wapate elimu ya ufundi ambayo wataweza kujiajiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vyuo hivi kwa muda mrefu vimekuwa vikiendeshwa katika mazingira magumu sana, vimekuwa havipati fedha za kutosha, dhamira ya kutoa elimu imefikiwa kwa kiasi kidogo.
Sasa Serikali iongeze bajeti kwenye vyuo hivi viweze kutoa elimu bora na wanafunzi bora, yale maeneo ambayo hayana vyuo hivi vya FDC‟s basi Serikali ijenge vyuo vya VETA. Mfano ni Jimbo langu la Kilindi halina FDC‟s wala VETA japo kwa mwaka wa fedha unaoanza Julai 2016 Serikali imedhamiria nasi tupate chuo cha VETA. Naomba nipate uthibitisho wa dhamira ya Serikali katika hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nizungumzie juu ya upungufu wa walimu katika shule zetu za msingi na Serikali, japo Serikali kwa sasa inaonesha kutatua tatizo hili hususani katika masomo ya sayansi, hisabati, fizikia na kadhalika. Mfano, katika Jimbo langu la Kilindi shule za sekondari Mafisa, Kibirashi, Kikude hazina walimu wa kutosha, nitaleta ofisini kwa Mheshimiwa Waziri upungufu wa walimu ili Serikali ione namna ya kutatua tatizo hili vinginevyo kiwango cha elimu katika Wilaya ya Kilindi kitashuka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nieleze juu ya suala la Maafisa Elimu na Walimu kukaa katika eneo moja la kazi. Jambo hili kwa kweli halileti ufanisi katika utendaji. Mtumishi kukaa eneo moja kwa muda mrefu kunamfanya mtumishi kutojifunza changamoto na morali ya kazi kwa mfano, katika Jimbo langu la Kilindi, Afisa Elimu Sekondari na Elimu ya Msingi wamekaa muda mrefu, Wizara kwa kushirikiana na TAMISEMI, tupate watumishi wapya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba suala la Wilaya kupata High School lipo chini ya Serikali za Mitaa lakini bado Wizara hii inalo jukumu la kusimamia Wilaya ambazo hazina kabisa shule za kidato cha tano na cha sita zinapewa fursa hizo. Mfano katika Wilaya yetu ya Kilindi hatuna hata shule moja, hii inanyima fursa kwa vijana ambao wazazi wao hawana uwezo kujiunga na shule ambazo zipo mbali na Wilaya ya Kilindi. Wazazi, uongozi wa maeneo hawana nguvu za kiuchumi. Wanafunzi wanachaguliwa mbali na Wilaya ya Kilindi mara nyingi hawaendi. Wizara ituone nasi, itusogezee shule ya wavulana na wasichana katika ngazi za kidato cha tano na cha sita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa dhamira yake ya kutoa elimu bure kwa wananchi. Wananchi wa Tanzania na wa Kilindi wamenufaika sana na fursa hii. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia hotuba hii kwanza kwa kumpongeza Waziri na Naibu Waziri wa Wizara hii kwa kazi kubwa wanayoifanya kumsaidia Rais, Mheshimiwa John Pombe Magufuli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa leo nitachangia kwenye maeneo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, usikivu wa redio Tanzania ni mdogo sana kwenye maeneo mengi ya nchi yetu ya Tanzania. Redio hii kwa jina TBC ndiyo wananchi wengi wanaitegemea kwa ajili ya taarifa za uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano katika Jimbo langu la Kilindi kwa kweli, wananchi wa eneo hili kwa muda mrefu wamekuwa wakililia kupata haki yao ya kupata taarifa, hususan za TBC, japo zipo baadhi ya redio zinasikika. Naishauri Wizara hii na Wizara ya Mawasiliano wahakikishe mawasiliano ya uhakika ya redio yanapatikana katika Jimbo langu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningependa kuchangia suala la michezo hususan mpira wa miguu. Mchezo huu muhimu ni sehemu ya ajira kwa vijana wetu. Utaratibu wa Shirikisho la Mpira Tanzania (TFF) katika kuandaa soka letu Tanzania siyo mzuri. Hatuna utaratibu wa kupata timu ya Taifa, hususan timu ya vijana, Serikali haina budi kuwekeza zaidi kwenye soka la vijana kuanzia soka la vijana chini ya miaka 14, miaka 17 na chini ya miaka 20 huko ndiko tunakoweza kuwekeza soka la uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali kwa kushirikiana na Shirikisho la Mpira (TFF) ni lazima tuwekeze kwenye mpira kwa kushirikiana na makampuni mbalimbali ambayo yatatoa udhamini mkubwa ili Taifa liweze kusonga mbele. Nchi za wenzetu za Afrika kama Nigeria, Algeria, Ivory Coast na kadhalika wamefika mbali kwa nchi zao kuweza kuwekeza katika soka la vijana. Vilevile Wizara ya Elimu ihakikishe kuwa michezo shuleni inarudishwa kwa kasi kubwa kwani huko ndiko waliko vijana wengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ningependa kujielekeza kwenye upatikanaji wa vifaa vya michezo kwa bei nafuu. Vifaa vingi vya michezo vipo bei ya juu sana, Serikali ilione suala hili kwa kusimamia bei za vifaa vya michezo ili wananchi wengi hususan vijana waweze kupata vifaa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ni muhimu katika michezo nchini ni suala la uchaguaji wa timu ya Taifa. Timu ya Taifa imekuwa na utaratibu mbovu sana, timu hii ya Taifa imekuwa haiangalii wachezaji kutoka Wilayani na Mikoani kama ambavyo miaka ya nyuma ambapo timu ya Taifa ilitazama uwezo wa mtu na siyo timu kubwa tatu za Dar es Salaam, Simba, Yanga na Azam. Wakati umefika sasa pawepo na Kamati ya wachezaji wa zamani waliocheza timu ya Taifa kuhusishwa na utafutaji wa vipaji mikoani kuanzia ngazi ya vijiji, wilayani na mkoani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hotuba.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante kwa kunipa fursa hii. Awali ya yote naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba hii ya Wizara ya Ujenzi lakini pia nimshukuru Mheshimiwa Waziri husika wa Wizara hii kwa mara ya kwanza ameweza kuona umuhimu wa Jimbo la Kilindi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nataka nianze kwa kuchangia hususani katika upande wa barabara kwenye dhana ya kuunganisha mikoa kwa mikoa kwa maana ya barabara kiwango cha lami. Nikienda ukurasa wa 41, hapa nataka nizungumzie barabara inayoanzia Handeni kwenda Kibirashi, Kijungu, Kibaya, Njoro, Chemba, Kwa Mtoro hadi Singida, ina urefu wa kilometa 460. Dhana hii ya kuunganisha mikoa ni dhana pana na ina maana kubwa sana kwa sababu inalenga katika uchumi wa mwananchi mmoja mmoja, Wilaya, Mkoa hadi Taifa. Unapofungua barabara maana yake unaruhusu mazao yauzwe kwa wepesi, unaruhusu movement za watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Wizara hii katika mwaka wa fedha unaoanza 2016/2017 wametufikia katika stage ya visibility study na detailed design. Mimi nataka niamini kabisa kwamba barabara hii ni muhimu sana kwa sababu inaunganisha mikoa minne, Mkoa wa Tanga, Mkoa wa Manyara, Singida pamoja na Dodoma. Muda umefika wa kuweza kuitengeneza barabara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lingine ambalo limezungumzwa na Wabunge wa Mkoa wa Tanga na mimi lazima nizungumze, hususani suala la reli ya Tanga kwenda Moshi hadi Musoma, na pia nataka nizungumzie habari ya bandari. Mambo yote haya ni ya msingi kwa sababu yanalenga kuinua uchumi wa Tanga. Waziri wa Viwanda alizungumza hapa kwamba kuna wawekezaji ambao wanataka kufungua viwanda katika Mkoa wa Tanga. Sasa kama unataka kufungua Mkoa wa Tanga maana yake nini, ni lazima uwe na bandari na reli iliyo imara ili uweze kusafirisha cement ile katika mikoa ya pembezoni mwa nchi. Mimi naomba Mheshimiwa Waziri hili ulitie mkazo mkubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kuchangia kwa sababu muda hautoshi ni juu ya wakandarasi wetu ambao wanatengeneza barabara. Barabara nyingi hususani katika Halmashauri zinatengenezwa chini ya kiwango na wakati mwingine mkandarasi anatengeneza barabara haweki matoleo. Hili linasababisha barabara hizi kuharibika hasa wakati wa mvua. Mfano katika Jimbo langu la Kilindi lenye squire meter 6,125, Mheshimiwa Waziri nikuambie barabara hizi sasa hivi hazipitiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wamenituma kwamba tuangalie ni namna gani mfuko huu wa TANROADS unaweza kusaidia kuikarabati barabara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine ni ushauri tu katika Wizara hii kwamba pawepo na performance audit katika miradi yetu mikubwa ya barabara. Miradi hii wakandarasi wanapewa hela nyingi sana, lakini baada ya mwaka mmoja, miezi sita barabara hazipitiki. Hii haiwezekani, Serikali lazima iwe very serious na hili, ili fedha za Watanzania ziwe na maana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala lingine ambalo ningependa kuchangia ni suala la mawasiliano…
MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa jioni ya leo niweze kusema machache, hususani katika Wizara hii iliyopo mbele yetu. Naomba nichukue fursa hii kwanza, kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuiletea maendeleo nchi yetu. Watanzania ni mashahidi kwamba, Profesa Muhongo na Naibu wake wanafanya kazi iliyotukuka na sote hatuna budi kumpa pongezi na kum-support afanye kazi ya ziada. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, itakuwa sio busara pia, kutokumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kuhakikisha kwamba, Tanzania inapata bomba lile ambalo linatoka Uganda hadi Tanga. Bomba hili litatoa fursa ya ajira kwa vijana wetu, ndugu zetu, kabla na baada. Naomba niseme kwa niaba ya wachangiaji au Wabunge wa Mkoa wa Tanga, nikupe shukrani za dhati sana katika hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo sasa naomba nichangie kuhusu REA, Umeme Vijijini; Waziri na Naibu Waziri ni mashahidi, mara nyingi nimekuwa nikizungumza nao na kupeleka ushahidi kwamba, Jimbo la Kilindi lina vijiji visivyopungua 102, lakini katika vijiji hivyo ni vijiji 20 tu, tena vilivyopo usoni mwa Makao Makuu ya Kata. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anaangalia suala la umeme wa REA vijijini, basi ajue Wilaya ya Kilindi wana changamoto kubwa sana. Naomba vijiji vilivyobaki, kama siyo vyote, tuweze kupata hata nusu ya vijiji hivyo kwa sababu, wananchi wa Jimbo la Kilindi wanahitaji umeme kwa ajili ya maendeleo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala lingine ambalo ningependa kulizungumzia sambamba na mambo ya umeme hapo hapo, ni kwamba umeme uliopo Kilindi uliletwa kwa ajili ya wakazi wachache sana. Jimbo lile sasa hivi lina wakazi takribani laki tatu, umeme ule unakatika mara kwa mara, wakati mwingine hata wiki umeme unakuwa haupatikani! Nashauri basi, kwamba Wizara iangalie namna gani inaweza ikaboresha ili wananchi wa Wilaya ya Kilindi waweze kupata umeme wa uhakika. Najua hilo kwamba, kuna utaratibu wa kuleta umeme kwa kiwango kikubwa, basi na Wilaya ya Kilindi kwa ujumla iweze kunufaika na mpango huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, napenda kuzungumzia suala la madini. Wilaya ya Kilindi imebahatika kuwa na madini ya dhahabu na ruby yanapatikana kwa kiwango kikubwa sana pale, lakini nimepitia kitabu hiki cha hotuba ya Mheshimiwa Waziri, sijaona ni wapi! Sasa Serikali inatia msisitizo kuweka nguvu ili wananchi wa Kilindi waliobahatika kwa nguvu ya Mwenyezi Mungu kupata madini yale waweze kunufaika na madini yale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona kwamba kuna utaratibu wa kupima, Mheshimiwa Waziri, Ukanda wa Ziwa unajulikana kwamba ni Ukanda wa Green Belt. Mzungumzaji aliyepita hapa amezungumza kwamba, migodi mingi kule inafungwa, Kilindi ina dhababu nyingi sana, kwa nini sasa tusiharakishe upimaji katika Jimbo la Kilindi ili wawekezaji wanaokuja kwa ajili ya dhahabu na ruby wakimbilie katika Wilaya ya Kilindi, hivyo wananchi wa Kilindi wanufaike na Taifa kwa ujumla. Naomba, Mheshimiwa Waziri aliangalie hili kwa jicho la tatu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile ningependa kuzungumzia juu ya Sheria za Madini, Wilaya ya Kilindi kuna migogoro mingi; Mheshimiwa Waziri kwa sababu, utaratibu wa kutoa license mtu anaweza kupata license yupo Mwanza, yupo popote pale, lakini naamini na anafahamu hilo kwamba, wagunduzi wa madini mara nyingi ni wananchi au wakulima wa maeneo yale. Sasa inapokuwa mtu huyu kaja na license, amemkuta mwenyeji pale ambaye vizazi vyote kazaliwa pale, kazeekea pale, halafu anamwambia azungumze naye namna ya kumpisha ili aweze kuchukua madini pale ardhini! Mtu alikuwa analima mahindi, leo kaambiwa kwamba, pana dhahabu, hivi ni rahisi kuondoka eneo hilo? Siyo rahisi!
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri sheria hii iangaliwe kwa jicho lingine tena kwa sababu, wananchi wa maeneo haya wanadhani ndio wanapaswa kupata fursa ya kunufaika na madini yale. Hatukatai kwamba, wawekezaji wasije Tanzania, lakini utaratibu uwape fursa wananchi wa maeneo yale kwa sababu, migogoro ya mara kwa mara imetokea na Mheshimiwa Waziri ni shahidi. Nimeshakwenda ofisini kwake nikamwambia kwamba, tunahitaji Ofisi ya Madini katika Wilaya ya Kilindi ili iweze kusimamia taratibu za madini Wilaya ya Kilindi. Ni kwamba, ofisi ya madini ipo Handeni, lakini umbali kutoka Wilaya ya Handeni mpaka Wilaya ya Kilindi ni umbali mkubwa unahitaji gharama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri tu hakuna ulazima wa kujenga ofisi pale, tusogezee maafisa watakaoweza kuwahudumia wananchi kwa sababu, wananchi wa Kilindi na wenyewe wanayo fursa ya kupata huduma ya madini pale. Hii pia itapunguza migogoro ya ardhi ya mara kwa mara. Mheshimiwa Waziri naomba wakati ana-wind up aweze kunipa majibu katika hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo napenda kuchangia ni suala la REA. Inavyoonekana hapa wale wakandarasi, makampuni yale yanayosambaza umeme vijijini, inaonekana wamepewa maeneo mengi sana. Nilipokuwa nazungumza na Meneja wa Wilaya ya Kilindi aliniambia, mtu anayesambaza umeme vijijini amepewa Mkoa wa Morogoro na Mkoa wetu wa Tanga na Mkoa mwingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani wakati umefika wa kuwapunguzia wale work load ili waweze kufanya kazi hizi kwa ufanisi wa hali ya juu sana. Wakati mwingine tutakuwa tunawalaumu hawa watu, lakini hawafanyi kazi kwa ufanisi kwa sababu, kazi hizi wanazopewa vijiji vinakuwa vingi sana. Nashauri na naamini kabisa kwamba, kwa phase ya tatu, basi kazi zitakwenda kwa haraka ili wananchi waweze kufaidika na umeme huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia suala la kumsaidia Mheshimiwa Rais na Serikali kwa ujumla kwamba, tunatakiwa tuongeze wigo wa mapato. Wigo wa mapato upo katika maeneo haya ambayo nayazungumzia, hususani ya madini. Siku moja Mheshimiwa Waziri nimeshawahi kumwambia kwamba, watu wanagawana milioni 200, mia 300 Kituo cha Polisi, maana yake Serikali inapoteza mapato! Hebu, Wizara ya Madini ione namna ya kuweka utaratibu mzuri wa kuhakikisha kwamba, mapato haya yanayopotea ya Serikali, basi yanadhibitiwa. Haiwezekani mtu anayechimba pale, mwekezaji mdogo apate milioni 300 wakagawane Kituo cha Polisi, usalama hapo uko wapi? Wizara ya Madini iko wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani wakati umefika, Mheshimiwa Waziri aone na kunisikiliza kwa sababu maneno haya ninayozungumza siyo yakwangu mimi, ni ya Wapigakura wa Wilaya ya Kilindi. Naamini wananisikiliza na wanajua Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi itawasikiliza na itawaletea Ofisi Wilaya ya Kilindi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kulizungumzia ni juu ya hawa wachimbaji wadogo wadogo na wakubwa wa madini, wamekuwa wakifanya shughuli hizo wakati mwingine wakiathiri mazingira. Kwa mfano, katika Kata ya Tunguli, kuna mwekezaji pale ambaye anafanya shughuli za madini, lakini kwa taarifa nilizonazo ni kwamba, maji yanayomwagika…
MWENYEKITI: Ahsante, muda wetu ndio huo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia hotuba iliyopo mbele yangu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wake kwa kazi kubwa na umahiri wa hali ya juu katika Wizara hii nyeti kwa jinsi wanavayojitoa kulitumikia Taifa hasa katika kusimamia huduma ya umeme kwenye maeneo yote ya nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, naomba kuchangia katika huduma ya umeme vijijini (REA). Huduma hii ni nyeti na imelenga kusambaza umeme kote nchini, lakini zipo changamoto kwa baadhi ya maeneo nchini. Mfano, katika Jimbo langu la Kilindi lenye ukubwa wa sm2 za mraba 6,125 vijiji 102 na kata 21 ni vijiji 24 tu ambavyo vimepata umeme, tena ni maeneo ya Bura. Je, Waziri na Wizara kwa ujumla, ni lini vijiji vilivyobaki vitapata umeme?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa yapo maeneo yenye huduma za kijamii hatuna umeme, mfano zahanati, shule za sekondari na shule za msingi. Ni imani yangu Serikali italitazama suala hili katika awamu ya tatu ili maeneo nyeti yaliyobaki yapate umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, katika Wilaya ya Kilindi kuna tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara, hali hii imetokana na umeme mdogo, miundombinu chakavu na ukosefu wa transformer. Umeme uliopo ulilenga kutoa huduma kwa wananchi wachache na wakazi 300,000. Nishauri hatua za haraka za dhati zichukuliwe ili wananchi wapate huduma hii kwa uhakika.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchangia juu ya sheria ya utoaji wa leseni kwa wachimbaji wa madini. Sheria hii imesababisha migogoro ya mara kwa mara kwa kuwa Sheria hii ya Madini na Sheria ya Ardhi zinafofautiana. Mwenye leseni anapotaka kuchimba madini ni lazima akubaliane na mwananchi aliye katika eneo husika kwa ajili ya fidia. Sasa, inakuwa vigumu mwananchi kuondoka eneo hilo pale anapojua dhahabu au aina nyingine ya madini yamegundulika eneo hilo, hususani pale inapotokea fidia inayotolewa ni ndogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kuna changamoto kwa Ofisi ya Madini ya Handeni inayohudumia Wilaya ya Kilindi kutoa leseni kwa watu waliopo nje ya Kilindi na kuwaacha wazawa wa wilaya husika. Hali hii imechangia migogoro ya mara kwa mara. Naishauri wizara isogeze huduma ya ofisi wilayani Kilindi, naomba jibu kwa Wizara husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimepitia kitabu chote cha hotuba ya Mheshimiwa Waziri sijaona sehemu ya hotuba yake inayoonesha dhamira ya Serikali katika kuwasaidia wachimbaji wadogo wadogo katika Jimbo la Kilindi. Naomba majibu ya kuridhisha kutoka kwa Mheshimiwa Waziri. Aidha, kama Serikali ikitoa ruzuku basi fedha hizo hazifiki kwa walengwa. Nashauri kila Mbunge anayetoka kwenye eneo lenye madini ahusishwe katika kusimamia zoezi hili ili walengwa wanufaike na nia nzuri ya Serikali katika kuwasaidia wananchi wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kuchangia hotuba hii juu ya kutokuwa na ofisi yenye hadhi ya wilaya, kwa maana ofisi ya TANESCO. Watumishi wa TANESCO kiukweli ni wachache, hawana vitendea kazi vya kutosha kuweza kuwafikia wananchi wenye jiografia ngumu. Naomba Waziri ashirikiane na Shirika la Umeme tupate ofisi bora na watumishi wa kutosha wa kuwahudumia wananchi wa wilaya hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa jitihada kubwa alizofanya za kufanikisha upatikanaji wa mkataba wa kujenga bomba la mafuta kutoka Uganda hadi Tanga litakalosaidia kukuza uchumi wa Mkoa wa Tanga na Taifa kwa ujumla; ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa ajira wakati wa ujenzi na baada ya ujenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watumishi wote wa Wizara hii kwa jitihada kubwa wanazochukua katika kusimamia ardhi ya nchi hii pamoja na dhamira ya dhati katika kutatua migogoro mbalimbali ya ardhi nchini kwetu. Nimepitia hotuba hii na kuona dhamira ya Wizara hii na ilivyojipanga kuona namna gani ambavyo Serikali yetu inasimamia ardhi yetu kwa kuithaminisha kwa taratibu na sheria zilizopo, hili ni jambo jema sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuchangia juu ya migogoro ya ardhi. Suala hili limekuwa likichukua muda mwingi wa wananchi wa kufanya shughuli za kiuchumi badala yake wanakuwa wakitumia kutatua migogoro ya ardhi. Mfano mzuri ni mgororo wa ardhi wa mpaka baina ya Wilaya ya Kilindi na Kiteto, mgogoro huu umechukua muda mrefu sana. Naomba kauli ya Mheshimiwa Waziri hivi ni lini mgogoro huu utakwisha. Naamini mgogoro huu umeasisiwa na watumishi wa Halmashauri wasio waaminifu walioshirikiana na baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Kiteto. Ili wananchi waone Serikali yao inawajali muda umefika sasa kupata suluhu ya kudumu ya mgogoro huu. Nashauri Serikali iwachukulie hatua watumishi wote waliobadili ramani ya mipaka ya Wilaya hizi mbili kwani awali mgogoro huu haukuwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha kuna migogoro ya wafugaji na wakulima, hii pia imekuwa ni migogoro ya muda mrefu. Wafugaji wamekuwa wakigombana na wakulima mara kwa mara kwa wafugaji kulisha mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima na wakulima kulima maeneo ya wafugaji. Nashauri maeneo haya yapimwe na wafugaji wawe na maeneo yao na wakulima wawe na maeneo yao ili kupunguza migogoro hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, uwepo utaratibu wa kuwa na maeneo ya kufuga na kunyweshea ili wafugaji wapate malisho ya uhakika kwani imeonekana hili ndilo tatizo kubwa kwa sababu wafugaji wamekuwa wakihamahama kutoka sehemu moja kwenda nyingine kutafuta malisho ya mifugo yao. Vilevile wafugaji wasihame na mifugo yao kutoka Wilaya moja kwenda nyingine bila kuwa na kibali maalum.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia suala la watumishi hasa wale wanaopima maeneo ya ardhi. Nashauri watumishi hawa wasikae kwenye vituo vyao vya kazi kwa muda mrefu. Mfano katika Kata ya Newiro watumishi wa Halmashauri wameuza kwa wafanyabiashara maeneo mengi ya kata hii, leo hii hakuna hata eneo la wazi, maeneo yote yameuzwa. Wasiwasi wangu vizazi vijavyo vitakosa mashamba ya kulima. Mashamba haya yamepimwa na Wizara kutoa hati. Nitaleta hati hizo zenye maeneo makubwa ambayo hayakufuata utaratibu unaotakiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, naomba Wizara hii ifute hati ya shamba la Tanzania Leaf Tobacco Company Ltd., lenye ukubwa wa hekari 2,133 lililopo Kata ya Kwadibona. Shamba hili limetelekezwa kwa muda mrefu sana, takribani miaka 20 bila kuendelezwa. Nashauri hati hii ifutwe ili eneo hili litengwe kwa ajili ya wawekezaji. Barua ya kufuta hati hii imekwishafika Wizarani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa kujibu kilio cha muda mrefu sana cha Baraza la Ardhi. Kwa niaba ya wananchi wa Kilindi tunashukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu wake pamoja na uongozi mzima wa Wizara hii kwa jitihada na kazi kubwa wanayofanya katika kusimamia majukumu makubwa ya Wizara hii. Wizara hii inasimamia majukumu ya rasilimali muhimu ya nchi yetu kwa maana mbuga zetu za wanyama, misitu yetu ya asili pamoja na vivutio vya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii inachangia kwa kiasi kikubwa Pato letu la Taifa kutokana na ujio wa utalii, mazao mbalimbali ya asili mfano magogo ya mbao, lakini bado jitihada za dhati zinahitajika ili kusimamia maeneo haya pamoja na kuongeza usimamizi wa uvunaji wa misitu yetu, Serikali inapoteza fedha nyingi kutokana na watu wengi wasio waaminifu wanaoshirikiana na Watanzania wasio wazalendo kuhujumu misitu yetu. Lazima Wizara ihakikishe udhibiti mkubwa unafanyika. Mfano katika Jimbo langu la Kilindi, Kata ya Msanja, Kitongoji cha Twile kuna uharamia mkubwa wa ukataji wa miti na magogo hivi hawa Wakala wa Misitu (TFS) wanafanya kazi gani? Mimi nadhani kama hawashirikiani na wahalifu hawa basi hawajui makujumu yao, mara nyingi wanapokamata magogo haya yanapelekwa Handeni badala ya kusafirishwa Kilindi, huu ni utaratibu gani? Nashauri Wakala hawa pia ofisi zao zihamishwe au zianzishwe ama kufunguliwa Wilayani Kilindi, eneo hili la uharibifu wa misitu halina usimamizi wa dhati. Nashauri Wizara husika iangalie namna ya kuwa na njia sahihi ya kuwasimamia watumishi wasio waaminifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa pia kuchangia namna ambavyo Wizara inaweze kupanua maeneo ya utalii kwa kuongeza maeneo ya utalii. Mfano, katika Jimbo langu la Kilindi yapo maeneo mengi ya utalii ambayo tanaweza kuchangia pato la Wizara hii, mfano pori tengefu la Handeni milima ya asili ya Kimbe, milima ya Kilindi asilia, milima ya Lulago yenye miti na uoto wa asilia haya yote ni maeneo muhimu sana ambayo wataalam wake tuijenge nchi. Nashauri ijenge utaratibu wa kufuatilia haya tunapowaambia kwani yana lengo la kuchangia pato la nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kuchangia ni upungufu wa wafanyakazi katika Wizara hii ambao wangekuwa na jukumu la kusimamia na kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa misitu na rasilimali ya nchi yetu, mfano katika Jimbo na Wilaya yangu ya Kilindi hatuna Afisa wa Wilaya anasimamia misitu, aliyepo ni Afisa katika ngazi ya Kata, Wizara ituletee mtumishi haraka kwani maeneo mengi katika Wilaya yanaharibiwa kwa kukosa usimamizi wa dhati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni juu ya maeneo ya hifadhi za misitu yaliyopo karibu kabisa na mijini, hifadhi hizi pamoja na faida tunayopata ya kuhifadhi mazingira na kupata mvua lakini maeneo haya yamekuwa ni maficho ya wahalifu hasa majambazi. Mfano msitu wa pale Kipala mpakani Wilaya ya Mkuranga hifadhi hii majambazi yametumia kama mafichio na hata askari zaidi ya sita wameuwawa pale kwenye check point. Nashauri Wizara sasa isafishe kwa kukata miti kwa mita 50 ili kuleta ulinzi na usalama kwa wakazi wa eneo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa kabla sijachangia mpango huu wa Serikali naunga mkono hoja. Nimpongeze Waziri wa Fedha na Naibu wake pamoja na watumishi wote wa Wizara ya fedha walioshiriki katika kuandaa mpango huu ambao unalenga katika kuinua uchumi wa Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimepitia mpango huu mambo mengi yaliyomo ndani mpango huu yana nia ya kuinua uchumi wa nchi yote kwa leo. Nitajikita kwenye maeneo machache ambayo yanahitaji usimamizi na mkakati wa hali ya juu. Maeneo hayo ni Sekta ya Kilimo cha Umwagiliaji, Sekta ya Utalii pamoja na kutazama upya aina ya kodi mbalimbali zinazotozwa na Mamlaka ya Mapato (TRA) hususan kwa wafanyabiashara wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sekta ya Kilimo ni muhimu sana ikisimamiwa kwa karibu na kwa njia za kisasa ni eneo ambalo kwa kiasi kikubwa itachangia pato la Taifa letu. Eneo ninalosisitiza hapa ni kilimo cha umwagiliaji, nchi yetu imebahatika kuwa na ardhi nzuri yenye rutuba, pia na mabonde mengi. Je, Serikali haioni umefika muda badala ya kutegemea kilimo tulichozoea cha kutegemea mvua, tutumie fursa za mabonde yetu kuzalisha mazao mbalimbali ya chakula na biashara. Aidha, kupitia mpango huu tunaweza kuchimba mabwawa makubwa pamoja na visima virefu ili kilimo chetu kisitegemee mvua tu. Ni muhimu sana kwani ni Mataifa mengi yameweza kupiga hatua, aidha tatizo la vifaa la kila wakati litatuliwa
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo ningependa Waziri wa Fedha alitazame katika kuinua pato la nchi yetu ni Sekta ya Utalii. Nchi yetu ina maeneo mengi ya utalii kwa maana mbuga mbalimbali za utalii, lakini bado sekta hii inachangia kiasi kidogo si kwa kiwango ambacho kama Wizara husika ingekuwa na mkakati na mpango thabiti, Taifa lingefaidika sana. Bado naamini hatujaweza kutangaza sekta hii ipasavyo, aidha, gharama au tozo tulizoweka katika utalii zimepunguza ujio wa watalii ni vema tukubaliane wenzetu wa nchi jirani nao wana fursa kama yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mbuga zetu zina wanyama wengi, hivyo tuweke mkazo katika eneo hili, niipongeze Serikali kwa kununua ndege mpya nikiamini zitasaidia ujio wa watalii ambao awali walikuwa wakifikia nchi jirani. Niiombe Serikali yetu pia iboreshe huduma katika mahoteli ambapo watalii wanafikia, pia kodi kwa watalii ipunguzwe kwani imepunguza idadi ya watalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ningependa kutoa mchango juu ya kodi mbalimbali zinatozwa na Mamlaka ya Mapato (TRA), nchi yoyote duniani haiwezi kusonga mbele bila ya kodi; mipango yote ya maendeleo inategemea kodi hata nchi yetu bila ya kodi haiwezi kusonga mbele. Naunga mkono suala la kodi ila nina mawazo tofauti juu ya utitiri wa kodi na juu ya ukadiriaji wa kodi, eneo hili lina matatizo kwani ukadiriaji huu hauna uhalisia, aidha watumishi wote wa TRA wanakosa njia iliyo sahihi ya ukadiriaji kwani wananchi wengi wamekuwa wakilalamika sana kukadiriwa kiwango kikubwa ambacho hakilingani na uhalisia wa biashara zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Serikali ione njia nzuri ya kupitia TRA ili ipunguze malalamiko haya. Wananchi wengi wana nia ya kulipa kodi, tusiwakatishe tamaa wananchi wote nikiamini kabisa bila kodi hakuna uhai. Ni imani yangu Mheshimiwa Waziri na Serikali watayapokea maoni haya.