HE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa na mimi niweze kumuuliza swali Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingikakwamba Serikali hii ya Awamu ya Tano imefanya mambo mengi sana; tumeona imepunguza matumizi mengi, uchumi unakwenda vizuri, Sekta ya Madini inakwenda vizuri.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, watumishi wa Serikali au watumishi wa Umma wana malalamiko muda mrefu sana, na malalamiko yao makubwa ni juu ya mishahara. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri Mkuu ninapenda nikusikie uwaambie Watanzania ni lini Serikali itapandisha mishahara ya watumishi? Ahsante.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kigua, Mbunge wa Kilindi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, na mimi nakiri kwamba wafanyakazi wanahitaji kuboreshewa maslahi yao, eneo hili la mishahara likiwa ni moja kati ya maeneo muhimu. Kama ambavyo tumekuwa tukitoa majibu kwenye maswali ya msingi kupitia vipindi vyetu kwa Mawaziri husika, lakini pia nyakati kadhaa kueleza nia ya Serikali ya kuboresha maslahi ya watumishi. Maslahi ya watumishi ni pamoja na kuweka stahili zao za kila siku, madeni yao, kupanda kwa madaraja na malimbikizo yao pamoja na nyongeza ya mishahara ni miongoni mwa mambo ambayo Serikali imedhamiria kuyafanya.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais alitoa ahadi ya kuboresha maslahi ya watumishi wakati wa sherehe ya Mei Mosi na aliwaambia wafanyakazi wote. Sasa Serikali kuanzia mwezi wa sita tunaendelea kuhakikisha kwamba tunakamilisha taratibu za kimsingi ambazo zitaiwezesha sasa Serikali kuanza kutoa malipo kwenye maeneo haya.
Mheshimiwa Spika, lakini eneo la kwanza ni lile la madeni, eneo la pili kwa muda mrefu tulisitisha madaraja ambalo sasa tumeanza kuwapandisha madaraja watumishi ambao hawakupanda madaraja kwa muda mrefu tunawafikisha mahali pao, na tunapobadilisha madaraja haya inabidi tulipe malimbikizo yake. Pia kuna ambao walishapanda, walikuwa hawajalipwa malimbikizo, sasa tunaanza uratibu. Na hapa juzi tumetenga shilingi bilioni 147 kwa ajili ya kulipa na Mheshimiwa Rais alishaeleza nia ya kulipa maslahi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tukishakamilisha haya, ni pamoja na yale mambo ambayo tulianza nayo, uhakiki wa watumishi, vyeti fake, ili kuondoa watumishi tusije tukawalipa watu ambao sasa hawastahili. Eneo hilo tumelimaliza, madeni tumeendelea kuhakiki, na kwa sababu madeni yanaendelea kila siku nayo tunaendelea kuyahakiki lakini yale ya muda mrefu tayari, na tumeanza kulipa. Na madeni haya yanalipwa kupitia mishahara yao. Tusingependa tuwe tunatangaza leo tumelipa, hii inaweza ikaleta athari kwenye eneo la mabadiliko ya kiuchumi.
Mheshimiwa Spika, lakini Serikali inalipa ingawa inalipa kwa awamu, lakini tutahakikisha kwamba madeni yote ya watumishi tunamaliza, waliokosa kupanda madaraja kwa muda mrefu tunawapandisha na kulipa stahili yao mpya halafu sasa tuje tuongeze mishahara. Tutakuwa tayari Serikali tunajua tuna watumishi wangapi, tutahitaji fedha kiasi gani za kulipa nyongeza ya mshahara, na wakati huo itakapokuwa imekamilika, nataka niwahakikishie watumishi tutaendelea na uboreshaji likiwemo na eneo la uongezaji wa mishahara.
Mheshimiwa Spka, kwa hiyo nawasihi sana wafanyakazi wenzetu kote wawe na imani na Serikali yao na huku tukiendelea kuratibu vizuri. Tunachotaka sisi tusije tukapoteza fedha tukawalipa watu ambao hawastahili, lakini pia lazima tujiridhishe ni kiwango gani cha fedha kinahitajika kulipa kwenye eneo hili ili kila mtumishi apate stahili yake na kila mtumishi tunapoboresha mishahara apate kima ambacho angalau kinaweza kukidhi mwenendo wa maisha ya kila siku na huo ndiyo utaratibu ambao Serikali imejiwekea. Ahsante sana.