Supplementary Questions from Hon. Omari Mohamed Kigua (59 total)
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ni takribani miaka 13 toka Wilaya hii ya Kilindi imeanzishwa. Mheshimiwa Naibu Waziri atakubaliana na mimi kwamba, pana umbali mkubwa sana kati ya Wilaya ya Handeni iliko ofisi ya Mamlaka ya Mapato na Kata mbalimbali za Jimbo la Kilindi hususani katika Kata ya Pagwi. Je, ni lini sasa utafiti huu utakamilika ili wananchi wa Kilindi waweze kunufaika na huduma hii? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa ametaka kujua ni lini utafiti huu utakamilika. Kama nilivyosema katika jibu langu la msingi kwamba pamoja na utafiti huu kukamilika pia tunaangalia potentials ya ukusanyaji yaani cost and benefit analysis ya kuanzisha ofisi hizi kila Wilaya. Kwa sasa hivi nguvu nyingi tunazielekeza katika kuanzisha ofisi za Mamlaka za Mapato katika mikoa mipya ambayo imeanzishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo naendelea kusema kwamba namwomba Mheshimiwa Kigua aendelee kuongea na wananchi waendelee kulipa kodi kupitia Wilaya yao ya mwanzo kabla ya Kilindi kuanzishwa. Pia tutakapokamilisha utafiti huu na tukaona kwamba kuna potential kubwa ya kupata mapato ya kutosha Wilaya ya Kilindi, basi hatutasita kuanzisha ofisi hii katika Wilaya ya Kilindi na wilaya nyingine zote za Tanzania ambazo hazina Ofisi.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, lakini nina swali moja la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, vimetajwa vigezo vingi sana hapa, lakini vigezo hivyo inaweza ikawa ni sababu ya kutoleta maendeleo katika maeneo husuka. Je, Serikali haioni umuhimu kwamba kigezo cha jiografia tu kinaweza kutosha kugawanya Jimbo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA NA VIJANA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Katiba yetu, Ibara ya 75(1) mpaka (6) imezungumzia vigezo na sifa za ugawaji wa Majimbo ndani ya nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vigezo vilivyotajwa ndani ya Katiba ni pamoja na hali ya kijografia, lakini mwaka 2010 Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilikwenda kufanya tafiti katika nchi za SADC na kubaini baadhi ya vigezo vingine ambavyo vinasaidia katika ugawanyaji wa Majimbo.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge katika pendekezo lako hilo, kama Serikali tunalichukua, lakini pia viko vigezo vingine vingi vya ziada ambavyo vilikuwa vikitumika katika ku-determine Majimbo yagawanywe katika mfumo upi, vingine vikiwa ni pomoja na hali ya kiuchumi, lakini settlement pattern na yenyewe huwa ni kigezo cha kuweza kutolewa ili Majimbo haya yaweze kugawanywa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, pendekezo la Mheshimiwa Mbunge tunalichukua kama Serikali, lakini nimpe pia habari ya kwamba tumekuwa tukichukua na vigezo vingine ambavyo vimeainishwa katika Katiba yetu, vilevile na utafiti uliofanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, leo muda wetu umebana kidogo kwa ajili ya shughuli zilizo mbele yetu. Kwa hiyo, tunaendelea na Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mheshimiwa Dkt. Elly Marco Macha, Mbunge wa Viti Maalum, swali lake litaulizwa na Mheshimiwa Amina Mollel.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina swali moja la nyongeza kama ifuatavyo. Serikali imekuwa ikitoa pesa nyingi sana kwa ajili ya miradi ya maji, lakini kumekuwa na tatizo kwamba miradi hii imekuwa inakosa ufuatiliaji; kwa maana kwamba miradi ile, hasa ya maji imekuwa katika kiwango cha chini sana. Je, Serikali iko tayari kuwa na kitengo maalum kwa ajili ya kufuatilia kuhakikisha kwamba fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya maji zinakidhi mahitaji, kwa maana miradi itengenezwe katika viwango vinavyotakiwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa miradi ya maji unafuata mfumo wa D by D. Wizara ya Maji inatoa fedha kupeleka katika halmashauri na halmashauri zinafanya utekelezaji.
Kuhusu suala la kufuatilia utekelezaji wa miradi hii ili kuhakikisha kwamba inakamilika katika viwango vinavyostahili; mwaka huu tulionao Wizara ya Maji imeajiri wahandisi zaidi ya 400 na imewapeleka katika halmashauri ili kwenda kuimarisha utaalam kuhakikisha kwamba sasa utekelezaji wa miradi utakwenda vizuri.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri nina maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na nia na dhamira nzuri ya Serikali juu ya kuwasaidia wachimbaji wadogo wadogo lakini imeonekana kwamba masharti haya hayawasaidii hawa wachimbaji wadogo na tunajua kwamba sasa hivi wimbi kubwa la watu wanaokosa kazi ni vijana. Sasa, je, Serikali iko tayari kupunguza vigezo vile ili watu wengi waweze kunufaika na mpango huu?
Swali langu la pili, je, Naibu Waziri yupo tayari kuambatana nami kwenda Jimboni ili tuweze kuzungumza na wachimbaji wadogo ili wajue dhamira ya Serikali ya kuwasaidia hususan wachimbaji wadogo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Mheshimiwa Kigua kwa kutambua kwamba kulikuwa na vikwazo tulipoanza utaratibu huu. Tumepunguza vikwazo vya kuomba mikopo. Tulipoanza kutoa ruzuku mwaka 2013 ilikuwa siyo ruzuku, ilikuwa ni mikopo. Sasa Serikali imepunguza masharti ya mikopo na badala yake sasa inatoa ruzuku. Hilo ni jambo muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kikwazo cha pili kilikuwa ni lazima wachimbaji wawe na Bankable statement inayoonyesha rasilimali ya madini iliyoko hapo chini. Sasa kulingana na uwezo mdogo wa wachimbaji wadogo, kigezo hicho kimeondolewa. Kwa hiyo, tunashukuru Mheshimiwa na vigezo vinaendelea kupungua ili Watanzania wengi wanufaike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niko tayari kutembelea kwenye Jimbo la Kilindi na hasa maeneo ya Tunguli. Ningependa nifike Tunguli lakini hata Kwa Manga mpaka kule kwenye Kijiji cha Kikunde na Mafulila ambako wanachimba wachimbaji wengi.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa uharibifu wa mazingira umekuwa ni tatizo sugu sana hususan katika Jimbo langu la Kilindi katika Kata za Negero, Mkindi, Kilindi Asilia pamoja na Msanja kutokana na shughuli za kibinadamu; je, Waziri yuko tayari kwa kushirikiana na Wataalamu wetu wa Chuo Kikuu cha SUA, kwa mfano, tuna Watalamu wazuri, akina Profesa Dhahabu na Mariondo kwa ajili ya kupeleka timu kule kuweza kufanya tathmini kubwa? (Makofi)
Swali la pili, suala hili la mazingira limekuwa ni sugu sana; je, Serikali iko tayari sasa kwa kushirikiana na Halmashauri kuhakikisha kwamba inapeleaka wataalamu wa kutosha wa mazingira kulinda maeneo yetu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshindwa kujizuia kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake zuri, Mheshimiwa Omari Mohamed Kigua. Nampongeza kwa swali lake zuri sana leo la mazingira hapa Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali yake ya nyongeza naomba niyajibu kama ifuatavyo:-
Moja, kwanza ofisi yangu inashirikiana vizuri sana na wataalam wa mambo ya mazingira hasa katika mambo ya hewa ya ukaa ambao wako pale SUA. Nimhakikishie kwamba ofisi yangu haina kipingamizi chochote cha kuja kufanya tathmini ya maeneo yaliyoathirika katika Kata alizozitaja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaunda hiyo timu, itakuja na hao wataalam na nimhakikishie kwamba Ofisi ya Makamu wa Rais ina watalaam waliobobea katika mambo ya mazingira vizuri sana, kwa hiyo, hakuna kitu ambacho kitaharibika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni kwamba wasiwasi wake kuhusu wataalam wa mazingira ambao anahisi kwamba Halmashauri nyingi hazina wataalam na sekta nyingine, nimhakikishie tu kwamba hivi karibuni Waziri wangu anakamilisha orodha ya wataalam ambao tutawateua ambao ni Wakaguzi wa Mazingira (Environmental Inspectors) zaidi ya 400 hapa nchini na watasambazwa kwenye sekta mbalimbali. Hivyo basi, tatizo hili na kiu kubwa ya kuwahitaji wataalam hawa watakuwepo katika sekta kama Mheshimiwa Mbunge ambavyo ameomba.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, ahsante pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ni ukweli usiopingika kwamba swala la changamoto ya maji ni tatizo kubwa nchini.
Je Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuchukua ushauri kwamba ili kutatua tatizo hili tuweke utaratibu wa Serikali kushirikiana na sekta binafsi kwa mpango wa PPP ili kuondoa suala la changamoto ya maji nchi?
Swali la pili, je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kuchukua ushauri wa Mheshimiwa Mbunge kwamba kuna umuhimu sasa umefika ili kupata thamani ya fedha katika miradi yetu ya maendeleo ya maji kuhakikisha kwamba mnaanzisha kitengo cha ufuatiliaji pale Wizarani ili msitoe tu fedha lakini fedha zile ziwe zinamaana katika miradi yetu mbalimbali katika Halmashauri zetu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NAUMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, ushauri wake kwanza ni mzuri kwamba kuna haja Serikali kuangalia utekelezaji wa miradi na uhusishe sekta binafsi kupitia mpango wa PPP. Kweli hilo suala ni zuri lakini Waheshimiwa Wabunge na naona wengi wanazungumza sana hili suala la PPP. Suala hili tumeshalifuatilia na tumelijadili sana, lina changamoto zake tumefanikiwa kwenye Daraja hili la Kigamboni kwa sababu tumetumia taasisi ya ndani lakini unapokuja kutumia taasisi ya nje repayment program ndio inaleta shida sana kwenye hii miradi ya PPP. Usiopoangalia unaweza ukajikuta kwamba nchi unaipeleka pabaya kwa sababu pia na sisi kama Serikali tunatakiwa kuweka viwango ambavyo mwananchi atavimudu. Unaweza ukaweka viwango vya kulipa wakati wa matumizi ya hiyo huduma ikawa ni kubwa mno wananchi wasiweze ikatuletea shida lakini tunalipokea hili na nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunaendelea kulifanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, kitengo cha ufuatiliaji wa miradi Mheshimiwa Mbunge nakushukuru sana na kweli kitengo hiki tumeanza kukiunda na iko mifano, nilitembelea Handeni nikaunda tume imefanya kazi nzuri imebaini mapungufu mengi sana katika utekelezaji wa ile miradi. Pungufu moja wapo ikiwa ni kwamba tumekosa kitengo ambacho kinasimamia moja kwa moja utekelezaji wa miradi, matokeo yake sasa hii hela hatupati ile value for money. Kwa hiyo, nikushukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwamba suala hili tayali Wizara inalifanyia kazi ili usimamizi wa miradi uweze kuwa mzuri zaidi.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri wa Ujenzi, napenda kuuliza swali moja la ziada kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika kwamba barabara hii ni muhimu sana kiuchumi na ukizingatia kutoka Makao Makuu ya Wilaya ya Kilindi kwa maana ya Songe hadi Gairo ni kilometa hizo alizotaja. Barabara hii nyakati za mvua ina changamoto kubwa sana na ni juzi tu Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya alipokuwa anakuja Makao Makuu ya Wilaya, alikwama maeneo ya Chanungu pale kwa takribani saa mbili.
Swali langu linakuja, je, ni lini sasa Mheshimiwa Naibu Waziri atahakikisha kwamba watu wa TANROADS Mkoa wa Tanga wanasimamia kwa dhati matengenezo maeneo yafuatayo, kwa maana katika Bonde la Chanungu, Kijiji cha Mafulila pamoja na eneo la Kikunde, karibu kabisa na Kijiji cha Gairo hapa kuhakikisha kwamba barabara hii inapitika kwa msimu mzima wa mwaka? Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nilieleza katika jibu la swali la msingi, barabara hii ni muhimu sana na Serikali inalifahamu hilo.
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nilisema, tunatenga bajeti ya fedha na mwaka huu zimetengwa kuhakikisha kwamba barabara hii inapitika majira yote. Kwa sababu hiyo, nawaelekeza TANROADS Mkoa wa Tanga na TANROADS Mkoa wa Morogoro kuhakikisha barabara hii inapitika majira yote. (Makofi)
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Napenda kuuliza swali la nyongeza kwa Mheshimiwa Naibu Waziri, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya mawasiliano katika Kisiwa cha Pemba ni sawa kabisa na Wilaya ya Kilindi, baadhi ya maeneo hayana mawasiliano kabisa. Nini kauli ya Mheshimiwa Naibu Waziri kuhusu wananchi wa Kata ya Saunyi, Kata ya Loane na baadhi ya maeneo ya Kata ya Kimbya ambao hawana mawasiliano kabisa katika Wilaya yangu ya Kilindi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imejikita kupeleka mawasiliano sehemu zote ambazo hazina mawasiliano kabisa. Tunapata changamoto kwa baadhi ya vijiji ambavyo vina mawasiliano, lakini wananchi wanataka kutafuta mawasiliano ya ziada. Katika maeneo hayo, mipango ipo, lakini siyo ya haraka.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mgumba nafahamu kwenye Kata ya pili uliyoitaja baada ya Saunyi, kuna mawasiliano ya aina moja na wananchi wanataka mawasiliano ya aina nyingine. Nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea kuwasiliana na watoa huduma za mawasiliano, watakapoona kuna faida kwao, watapeleka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali tumejikita kupeleka vile vijiji ambavyo wale watoa huduma lazima tuwashawishi kupeleka huduma za mawasiliano. Sile sehemu ambazo hakuna mawasiliano kabisa, hizo ndiyo tumejikita kama Serikali kuhakikisha kwamba wananchi wa eneo hilo, wanawasiliana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ndani ya vijiji hivi ambavyo nimevitaja, kama sehemu mojawapo ambako vinasomeka, tutahakikisha tunapeleka mawasiliano ili wananchi wa Tanzania wote wawasiliane.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru. Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Kilindi ina takribani miaka 20 toka imeanzishwa lakini hali ya kusikitisha ni kwamba kituo kinachotumika ni kama post wakati ikiwa ni Wilaya ya Handeni zamani. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri au Waziri yuko tayari kutembelea Jimbo la Kilindi ili kujionea hali halisi ya jinsi ambavyo hata OCD anakaa guest house mpaka leo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumjibu Mheshimiwa Shekilindi, Mbunge wa Kilindi kuwa....
Samahani Mheshimiwa Kigua, Mbunge wa Kilindi kuwa tutakuja Kilindi.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nina swali moja au mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni imani yangu kwamba dhamira ya Serikali ni kuwahudumia wananchi na kuwapelekea huduma iliyo imara, lakini swali la msingi ilikuwa ni kueleza changamoto ya miradi hii.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari kufanya ziara kupitia miradi yote ambayo nimeitaja hapo juu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mwenda kwao haogopi kiza na Kilindi ni nyumbani, nipo tayari kwenda Kilindi. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Elimu lakini nina maswali madogo mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, natambua jitihada za Wizara ya Elimu za kuanzisha Shule za Sekondari za Kata lakini ni ukweli usiopingika kwamba wananchi wengi baadhi ya maeneo wanashindwa kupeleka watoto wao maeneo ya mbali, mfano Jimbo la Kilindi ambako wazazi hawana uwezo wa kupeleka watoto wao kidato cha tano na cha sita. Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kushirikiana na halmashauri yetu ambapo tumeshafanya jitihada kubwa kutembelea Shule za Sekondari za Kilindi Girls, Kikunde na Mafisa ambazo tayari zina miundombinu kwa ajili ya kupata sifa ya kuwa na kidato cha tano na sita? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kigua, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kama niko tayari katika kutembelea shule za jimboni kwake kama alivyotaja, mimi niko tayari kuzitembelea lakini naomba tu niendelee kusizisitiza kuwa Shule za Kidato cha Tano na Sita ni shule za kitaifa. Kwa hiyo, hata kama tukijenga Kilindi bado haitakuwa kwa ajili ya wanafunzi wa kutoka Kilindi tu, watatoka wanafunzi Tanzania nzima.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, kwanza nampongeza na niwapongeze TAMISEMI kwa kutupatia kiasi kilichotajwa kwa ajili ya shule zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika kwamba Halmashauri zetu nyingi hazina uwezo wa mapato, lakini natambua dhamira ya Serikali ya kutoa elimu bure. Nina maswali mawili ya nyongeza:-
Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kukarabati shule kongwe ambazo ni za muda mrefu? Kwa mfano, Shule ya Msingi Masagali ya mwaka 1940 na Shule ya Msingi Songwe 1952? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kutembelea hizi ili ajionee hali halisi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA C. WAITARA):
Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Kigua kwa kazi nzuri ambayo anaifanya kutetea wananchi wake na hasa kuboresha miundombinu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nimwarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba tunavyozungumza hapa kwenye mgawo ambao umeishia awamu ya saba ya EP4R amepata mgawo wa shule mbili; Shule ya Kikunde mabweni mawili, matundu sita ya vyoo, vile vile na Shule ya Mafisa ambayo imepata madarasa manne na bweni moja na matundu sita ya vyoo.
Mheshimiwa Spika, vilevile swali lake la kwanza ni kwamba Serikali ya Awamu ya Tano imejitahidi sana, tumekarabati shule 45 kwa zile shilingi bilioni 60, lakini sasa tunaenda awamu ya pili, tunakarabati shule 17 kwa zaidi ya shilingi bilioni 17. Sasa shule aliyoitaja, tutaangalia kwenye orodha yetu, lakini tutaendelea kadiri itakavyowezekana. Ni nia ya Serikali kukarabati shule zote 89 hizi kongwe, zikamilike, lakini tumeanza zile ambazo tulizirithi kutoka kwa Wakoloni, ili tumalize twende na nyingine zote pamoja na hizi za kisasa ambazo wananchi wanachangia pia.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, naomba nimwarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba Mkutano huu ukimalizika tarehe 11 nitakuwa Tanga na Kilindi ni mojawapo. Tanga, Arusha na kuendelea. Kwa hiyo, niko tayari kutembelea shule hizi na kupata maelezo ya ziada. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini nina maswali mawili, kama ifutavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, changamoto ya hosteli ambayo imejitokeza katika Jimbo la Mufundi Kusini haitofautiani sana na hali iliyopo katika Jimbo la Wilaya ya Kilindi. Ni ukweli usiopingika kwamba suala la hosteli ni kitu muhimu sana kwa sababu linachangia katika ufaulu wa watoto wetu. Je, Serikali iko tayari sasa kuhakikisha kwamba shule zote za vijijini ambazo watoto wanatembea kwa umbali mrefu zinakuwa na hosteli?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni kwamba katika Jimbo la Kilindi ipo Shule ya Kwamkalakala ambayo ni miongoni mwa shule kumi za mwisho ambazo zimefanya vibaya kutokana na kutokuwa na hosteli. Je, Serikali ipo tayari kutoa msaada maalum kuhakikisha kwamba shule ile inajengewa hoteli? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge wa Kilindi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza anataka kujua kama Serikali iko tayari kujenga hosteli kwenye shule zote za sekondari. Ni ukweli usiopingika kwamba hakuna mtu ambaye anapinga kutokuwa na hosteli katika shule zetu, zimeonesha tija na hasa kusaidia watoto wa kike waweze kupata muda mwingi wa kujisomea na kuweza kufanya vizuri katika masomo yao ambao pia wamekuwa wakifanya vizuri wale ambao wamebahatika kusoma vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunao mpango kupitia EPforR, tumepeleka fedha katika hosteli zetu na Kilindi wamepata hosteli moja ambayo nilienda kuitembelea. Tutaendelea kufanya hivyo kwa mwaka wa fedha huu ambao tumeleta bajeti leo mezani kwenu, Waheshimiwa Wabunge watuunge mkono ikishapita tutaangalia namna ya kuboresha.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, tunawaomba wadau wote na Watanzania popote walipo hili jambo la kujenga hosteli za watoto wa kike katika shule zetu ni jambo shirikishi. Sisi Wabunge tushirikiane na wananchi wengine na Serikali tutasaidia kadri tutakavyokuwa na uwezo wa fedha wa kufanya jambo hilo.
MHE. OMARI M. KIGUA: Ahsante Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli kabisa nami naungana na Serikali kwamba kuna umuhimu wa Serikali kushirikiana na sekta binafsi katika kuwaletea Watanzania huduma. Pamoja na hali hiyo, zimejitokeza changamoto nyingi sana sana katika Hospitali hii ya KKKT mojawapo ni suala la utawala.
Swali: Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari sasa kuangalia utaratibu ulio mzuri ili dhana hasa ya ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi iweze kufikiwa?
Swali la pili, kwa kuwa Kilindi haina Hospitali ya Wilaya: Je, Serikali iko tayari sasa kuitengea fedha Wilaya ya Kilindi ili iweze kupata Hospitali ya Wilaya? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni azma na lengo la Serikali kuhakikisha kwamba zile hospitali ambazo tunashirikiana katika kutoa huduma kwa maana ya DDH, suala la utawala bora inakuwa ni kipaumbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawe ni shuhuda kwamba katika swali lake amesema kuna tatizo la utawala. Sasa ni vizuri Mheshimiwa Kigua tukitoka hapa tuelekezane hasa tatizo ni nini ili tuweze kutoa ufumbuzi ili wafanyakazi nao waweze kuona ni sawa na ambavyo wanafanya katika hospitali zetu za Wilaya. Kwa sababu suala la kuwa na utawala bora ni jambo la msingi kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Kigua atakubaliana na Serikali kwamba azma ya kuhakikisha kwamba hospitali zinajengwa katika maeneo yote ambayo Halmashauri hazina Hospitali za Wilaya inafikiwa. Kwa kuanzia, yeye mwenyewe ni shuhuda, katika bajeti ambayo Bunge lako Tukufu limetupitishia, tumeweza kuwatengea kwa kuanzia shilingi milioni 200 kwa ajili ya kujenga Kituo cha Afya cha Msente. Naamini baada ya kuhakikisha kwamba tunakamilisha ujenzi wa hospitali 67 tulizoanza nazo na 52, hakika naomba nimtoe shaka kwamba na Kilindi tutakwenda.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, binafsi namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu yenye ufasaha wa hali ya juu sana. Ni majibu ambayo yanatoa matumaini makubwa siyo kwa Wilaya ya Kilindi tu, lakini maeneo mengine ya Tanzania kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, pamoja na shukurani hizo, nina swali moja la nyongeza. Mheshimiwa Waziri amekiri kwamba Mahakama hizi ni chakavu na Mahakana zinazofanya kazi ni tatu tu.
Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari sasa kuanzisha hata Mahakama za Mwanzo I Mean kuanzisha hata ofisi ndogo ili huduma hii ipatikane kwa muda mfupi wakati tukisubiria ujenzi wa Mahakama hizi za Mwanzo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, kwanza nataka nitoa shukurani za pekee kwako. Jana ulikwenda kufungua Mahakama ya Wilaya ya Kondoa na ulifuatana na Jaji Mkuu. Katika hotuba yako ulidhihirisha kwamba ni jitihada za Serikali kujenga Mahakama, kuboresha Mahakama na kujenga Mahakama za karne ya 21 ambazo zina TEHAMA na vifaa vya kisasa vya kielektroniki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka kuwahakikishia Waheshimiwa Wajumbe kwamba kwanza kuna huu mpango mahususi wa Mahakama ya Tanzania ya kujenga Mahakama katika ngazi zote mwaka huu na mwaka ujao. Nataka kuwahakikishia kwamba kitendo cha sisi kuamua kupeleka mashauri kutoka Mahakama hizo chakavu na kwenye maeneo ya awali na ya muda, utaendelea kuboreshwa.
Mheshimiwa Spika, nataka kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba hiyo haitasimamisha hata kidogo usikilizaji wa mashauri katika Mahakama hizo na jitihada za uboreshaji na ujenzi tutazikamilisha katika mwaka huu wa fedha na kuendelea katika mwaka ujao wa 2021. Ahsante. (Makofi)
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza niipongeze Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kujenga daraja la muda la Nderema ambalo linaunganisha Wilaya ya Kilindi na Handeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuipongeza Serikali, naomba niulize swali la nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mvua hizi hazikutegemewa na zimeharibu sana barabara kuanzia Handeni – Kibirashi - Songe – Gairo. Je, Serikali iko tayari kutuma wataalamu kwenda kuangalia hali ya uharibifu ili kuweza kurejesha mawasiliano katika eneo hili? Ahsante.
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja dogo la Mheshimiwa Kigua, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nitoe taarifa kwamba kwa mujibu wa usanifu wa barabara mvua zina return period tatu; kuna ya miaka kumi, hamsini na miaka mia moja. Mvua iliyonyesha juzi Tanga inaonekana ina return period ya miaka mia moja na ambayo design huwa haijumuishi returned period hizo lakini kwa mujibu wa swali lako Mheshimiwa Mbunge tuko tayari.
MHE. OMARY M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza. Barabara ya Handeni- Kibirashi hadi Kiteto imekwisha na hatua zote za mwisho zimeshakamilika; na kwa kuwa barabara hii ni barabara ya kimkakati inaunganisha mikoa minne kwa maana ya Mkoa wa Tanga, Manyara, Singida na Dodoma. Je, Serikali sasa haioni umuhimu kuanza kutengeneza barabara hii kwa kiwango cha lami ili kuondokana na kero hii ya mara kwa mara? Hivi ninavyosema muda huu barabara hii haipitiki kwa wiki sasa.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kigua, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Serikali inafahamu umuhimu wa barabara hii ndio maana usanifu wa kujenga barabara hii kilometa 461 kutoka Handeni kwenda hadi Singida umeshakamilika. Kwenye bajeti yetu tumetenga fedha kuanza ujenzi wa lami wa barabara hii kilometa 50, kwa hiyo Mheshimiwa Kigua naomba avute subira na kwamba tukipata fedha tutaanza ujenzi. Hata hivyo, kuna maeneo yalikuwa yameathirika na mvua kama nilivyojibu swali langu la msingi, ni kwamba tumejipanga kurejesha maeneo yote ambayo ni korofi na kama mvua zitaendelea kunyesha maeneo yoyote yatakayoonekana kuwa ni korofi tutakwenda maeneo hayo kufanya marejesho ya barabara.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la msingi namba 358 limetaja barabara hii ambayo inaunganisha Wilaya ya Gairo na Kilindi, swali langu la nyongeza ni kama ifuatavyo; mwaka 2010 Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne alitoa ahadi ya kujenga barabara hii kw akiwnago cha lami. Je, ni lini Serikali itatimiza ahadi hii? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Kigua kwa sababu tumezungumza sana juu ya barabara hizi ambazo zinaunganisha Wilaya ya Kilindi na hii barabara ambayo nilikuwa nimeijibia swali kutoka Gairo kwenda Kilindi kama Mheshimiwa Kigua anavyosema ni barabara ambayo tunaitegemea siku za usoni na kutokana na ahadi ya Mheshimiwa Rais tutaiunganisha na barabara hii muhimu ambayo kwa hatua za ujenzi zimeshaanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivyo kwa sababu tukishaanza kufanya usanifu hata barabara hii kubwa ukitoka Handeni unapita eneo la Kibirashi ambapo ndiyo barabara hii anaitaja Mheshimiwa Mbunge, itaungana na hii barabara tukiendelea kwenda kule Chemba hadi Singida. Kwa hiyo unafahamu kabisa tuko kwenye hatua ya ujenzi wa barabara ile. Niombe uvute subira, mahitaji ya ujenzi wa barabara ni mengi, tutaenda kidogo kidogo kadri fedha zinavyoruhusu ili tuweze kuendelea kufanya ujenzi huu na ahadi itakuwa inaendelea kutekelezwa hivyo. Kwa hiyo, vuta subira barabara ile kubwa itakwenda na hii ambayo itatuunga kutoka barabara kubwa ya kutoka Dar es salaam – Morogoro kuja Dodoma kwa maana ya Gairo kwenda Kilindi itaungana na hii barabara. Tunafahamu hivyo, kwa hiyo naomba uvute subira tu, usiwahishe shughuli, siku za usoni tutakwenda kujenga barabara hii.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri juu ya tatizo hili, nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo;
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la migogoro ya ardhi imekuwa ni changamoto kila eneo katika nchi hii na kama swali la msingi linavyosema kwamba katika Jimbo la Wilaya ya Handeni kuna changamoto ya migogoro ya ardhi. Je, nini mpango mkakati wa Serikali hususan kwa kupima maeneo haya ya ardhi kwa kuainisha maeneo ya wakulima na wafugaji?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, changamoto hii ya migogoro ya ardhi iliyopo Handeni inafanana sana na changamoto iliyopo kuna mgogoro baina ya Wilaya ya Kilindi na Wilaya ya Kiteto ambayo imedumu muda mrefu sana. Je, nini kauli ya Serikali kuhakikisha kwamba inatatua mgogoro huu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba nijibu maswali ya nyongeza mawili ya Mheshimiwa Mbunge wa Kilindi kwa niaba ya Mbunge wa Handeni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kuna maeneo mengi ambayo hayajapimwa katika Halmashauri zetu na katika Tawala za Mikoa, lakini bahati nzuri Serikali imepunguza sana gharama za upimaji na najua wapo wadau mbalimbali ambao wanaendelea katika maeneo mbalimbali ya kupima maeneo yetu. Mimi naomba nitoe maelekezo kwa viongozi na ushauri kwa wananchi kwamba ukipima eneo lako thamani yako inapanda, unaweza ukakopesheka na ukapata fedha ili kujiendeleza katika eneo lako. Kwa hiyo, wale watu muhimu ambao wanafanya huo upimaji katika maeneo yetu ambao unatambuliwa na viongozi wetu wa vijiji, mitaa, kata, halmashauri na mikoa wawape ushirikiano na wapime maeneo yao ili kuweza kupata hati lakini pia kuweza kupata fedha katika benki mbalimbali katika kuendeleza maeneo yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili anauliza suala la mgogoro ambao upo kati ya Kilindi na Kiteto. Yako maeneo mbalimbali ambayo tumepokea malalamiko yao, iko migogoro ambayo ipo katika Wizara ya TAMISEMI ya mipaka, tunaishughulikia na tunafanya hivyo kwa sababu mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili angalau maeneo haya yaweze kutambulika vizuri na uchaguzi usiwe na maneno maneno mengi ya kuhusu mipaka. Yapo mambo ambayo yanahusiana pia na matumizi ya ardhi ambayo yapo kwenye Wizara ya Ardhi, haya pia tunashirikiana na wenzetu wa WIzara ya Ardhi ili kuweza kuyatatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kama kuna mgogoro ambao ameutaja hapa sasa tuwasiliane baadae ili tuweze kupata details/taarifa sahihi za eneo hili na ninamhakikishia tutafanya kazi nzuri kuweza kuhakikisha kwamba eneo hili mgogoro unamalizika na watu wetu waendelee kuishi kwa amani na kushirikiana kama ni wafugaji au wakulima, Mheshimiwa Rais tayari ameshatoa maelekezo ili maeneo yatengwe na kuheshimiwa ili watu wetu wafanye kazi bila kugombana kwa kuleta maendeleo katika nchi yetu. Ahsante.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na maelezo ya Naibu Waziri juu ya swali langu Namba 24, napenda kuuliza maswali ya nyongeza mawili kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ni uchumi, barabara ndiyo kila kitu. Swali hili naliuliza kwa mara ya pili katika Bunge lako tukufu lakini majibu ni yale yale.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la kwanza: kwa kuwa barabara hii kipindi cha mvua imekuwa hapitiki na ndiyo maana nimekuwa naomba muda mrefu kwamba barabara hii itengenezwe kwa kiwango cha lami, ni kwa sababu ni barabara ambayo ina uchumi wa hali ya juu sana; barabara hii ina ahadi ya Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete; kwa maelezo ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba bajeti haitoshi, fedha hakuna.
Je, wananchi wa maeneo haya ya Gairo na Kilindi ni liniwatarajie barabara hii kujengwa kwa kiwango cha lami? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili: barabara hii ambayo ina magari mengi na shughuli nyingi za kiuchumi, ina madaraja au mito ya Chakwale, Nguyami na Matale; kipidi cha mvua haipitiki na Serikali kwa kweli imejitahidi mara kadhaa kujenga madaraja.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari sasa kutuma timu yake kwenda kukagua kuona hali halisi, kwa sababu barabara hii kwa sasa hivi haipitiki na wananchi wanapata adha kubwa? Ahsante.
NAIBU WAZII WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Kigua, Mbunge wa Kilindi kwa kuendelea kuwatetea wananchi wa Jimbo la Kilindi ili kuhakikisha kwamba wanapata barabara ya kiwango cha lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, barabara zote ni muhimu sana kwenye masuala ya uchumi, lakini pia katika kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na usafiri wa wananchi. Ndiyo maana tuna ilani ya miaka mitano ambapo katika ilani hiyo tunaamini kwamba katika miaka mitano hatuwezi kutekeleza miradi yote kwa mwaka mmoja. Kwa hiyo, pamoja na kwamba ni kweli ni ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne, nalo tunalijua. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hizi zitajengwa katika kipindi hiki cha miaka mitano mara tu fedha zitakapopatikana na katika bajeti tunazoendelea kuzitekeleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu barabara ya madaraja hayo matatu, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hivi tunavyoongea nimewasiliana na kutaka kupata changamoto za barabara hii. Wiki hii Meneja wa TANROADS wa Tanga na wa Mkoa wa Morogoro, watatembelea hii barabara na kuona changamoto ambazo zinaendelea katika haya madaraja ili tusije tukakatisha usafiri kati ya mikoa hii miwili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hilo suala litafanyika na Mameneja wote kwa sababu ni barabara inayounganisha mikoa miwili. Ahsante. (Makofi)
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri na Waziri wake wa maji kwa kututengea kiasi cha shilingi bilioni 2,146,000,000 kwa ajili ya huduma kwa watu wa Kilindi, baada ya shukrani hiyo ningependa tu nimuulize swali moja tu Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na maelezo mazuri ya kwamba wanafanya tafiti na tafiti hiyo itatoa majibu ndani ya mwezi ujao, sasa nataka tu kupata commitment ya Mheshimiwa Naibu Waziri je, wananchi wa Wilaya ya Kilindi wategemee nini kuhusiana na uhakika wa mradi wa huu ambao utahudumia zaidi ya vijiji 12? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Omari Mohamed Kigua kama ifautavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nipende kupokea pongezi zake kwangu pamoja na Mheshimiwa Waziri kwa hakika tunashirikiana vema na wewe pia nikupongeze kwa sababu unatupa ushirikiano mzuri na tutaendelea kufanya kazi bega kwa bega kuhakikisha suala la maji tunakwenda kulitatua kwa pamoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na lini sasa commitment ya serikali kwenye Mradi huu wa Diburuma ni kwamba tayari kama nilivyoeleza kwenye jibu langu la msingi utafiti unaendelea na hivi punde mwezi ujao tunakwenda kukamilisha usanifu hivyo kutokana na gharama ambayo itapatikana sisi kama Serikali tumejipanga kuhakikisha kutumia chanzo hiki tukiamini kabisa kitakuwa ni chanzo endelevu na sehemu kubwa zaidi ya vijiji 10 ninafahamu zitapitiwa kwa hiyo tutaendelea kushirikiana kuona kwamba chanzo hiki tunakwenda kukitumia tutakitafutia fedha ili kuona kwamba tunatimiza azma ya kuleta maji.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu haya ya kusema kwamba huu wa fedha unaoanza keshokutwa hapo tumetengewa shilingi milioni 182 kwa ajili ya kutengeneza kalavati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la msingi lilikuwa linazungumzia kwamba ni lini Serikali itatengeneza daraja, kama katika maelezo yake alivyosema kwamba eneo hili lina kilometa 38 zinazounganisha Wilaya ya Kiteto na Wilaya ya Kilindi. Eneo hili lina changamoto kubwa kwa sababu daraja ni kubwa sana, kiasi hiki kilichotengwa hakitoshi hata kidogo kwa ajili ya kujenga daraja.
Je, ni lini Mheshimiwa Waziri atakwenda yeye au wataalam wake kwenda kuangalia upana wa daraja hili ili Serikali iweze kutenga fedha za kutosha? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; miaka ya nyuma Serikali ilishatenga pesa kwa ajili ya daraja hili, lakini nina uhakika thamani ya fedha kwenye daraja hili haikufanyika.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari kutuma timu kuona kama fedha hizi zilitumika ipasavyo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Omari Mohamed Kigua Mbunge wa Kilindi kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa anachokieleza Mheshimiwa Mbunge, kwamba daraja lile ni kubwa na Bonde la Mto Sambu kama alivyokuwa amelianisha hapa ni bonde ambalo limeongezeka na linakadiriwa kuwa urefu wa mita 75. Na kwa tathmini ya awali ambayo ilikuwa imefanyika kwenda kufanya matengenezo katika eneo hilo ambalo linahusu hilo daraja, kuna makaravati kama 18, pamoja na drift yaani vile vivuko mfuto vidogo zaidi ya 30 na kitu. Na ilivyofanywa tathmini ya fedha ya awali ni kwamba eneo hilo linahitaji zaidi ya bilioni 2.9 ili kuhakikisha hiyo barabara iwe inapitika muda wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mimi tu niseme kabisa kwamba Mheshimiwa Mbunge kama alivyosema mimi mwenyewe nitafika eneo hilo ili niweze kushuhudia, na vilevile nitaituma timu kutoka Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwenda katika eneo husika. Lakini kikubwa ni kwamba kwa sasa tuna ufinyu wa bajeti ndio maana umeona tumetenge hizi fedha chache. Lakini Bajeti Kuu ya Serikali ikipita, na kile chanzo kipya ambacho tunapelekea fedha kuongezea TARURA ninaamini tutazingatia hili ili barabara hii iweze kupitika kwa wakati wote.
Mheshimiwa Naibu Splika, kwa hiyo tunaomba Waheshimiwa Wabunge mpitishe Bajeti Kuu ya Serikali ili tupate kile chanzo cha uhakika na ninaamini katika mwaka ujao wa fedha hili swali halitaulizwa tena, tutakuwa tumeshalifanyia kazi. Ahsante sana.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Binafsi nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa uamuzi wa busara sana sana wa kununua magari katika halmashauri zote za Tanzania yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi hizo nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza; ni ukweli usiopingika kwamba huduma ya ambulance ni muhimu sana katika kuwahudumia wananchi wa Tanzania. Hata hivyo, huko nyuma imejitokeza changamoto kwamba huduma ya magari haya ya ambulance yanapelekwa sehemu moja mawili, matatu wakati sehemu nyingine hakuna magari kabisa. Sasa nini mpango wa Serikali katika kuepuka hili siku za usoni? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; Serikali imefanya jambo jema sana, inaenda kujenga vituo vya afya kwenye tarafa takribani nchi nzima. Je, nini mpango wa Serikali wa kuhakikisha kwamba tarafa zote hizo pia zinapata magari ya wagonjwa kwa maana ya ambulance? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kwanza nipokee shukrani nyingi ambazo Mheshimiwa Mbunge amezitoa kwa Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na ni kweli Dhahiri, shahiri inaonyesha kazi kubwa sana ambayo Serikali yetu ya Awamu ya Sita inaifanya katika kuboresha huduma za afya katika nchi yetu kwa kasi kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba tumekuwa tunapeleka magari ya wagonjwa katika halmashauri mbalimbali, lakini kuna vigezo ambavyo vimekuwa vikizingatiwa wakati tunapeleka magari na ndiyo maana kumekuwa na utofauti kidogo wa idadi ya magari yanayopelekwa kwenye halmashauri moja ikilinganishwa na magari yanayopelekwa kwenye halmashauri nyingine. Moja ya vigezo ni pamoja na idadi ya wananchi, wingi wa vituo vya afya, lakini pia idadi ya matukio ya magonjwa mlipuko, lakini na ajali za barabarani.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, utaratibu huu ni wa kisera tutaendelea kufanya hivyo, lakini jambo la msingi ni kuhakikisha halmashauri zetu zote zinapata magari ya wagonjwa angalau kutimiza majukumu hayo bila kujali wingi wa wagonjwa na kadhalika, kwa maana ya kuhakikisha kwamba huduma zinapatikana vizuri. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge jambo hili tunalizingatia na mipango yetu ni kuendelea kuboresha.
Mheshimiwa Spika, la pili, katika ujenzi wa vituo vya afya katika kila tarafa; tunahitaji kuwa na vituo vya afya vyenye magari ya wagonjwa na magari haya yataendelea kuwekwa kwenye mipango na kufikishwa kwenye vituo vya afya vinavyojengwa katika tarafa zetu kwa awamu kwa kadri ya upatikanaji wa fedha. Pia kama nilivyotoa taarifa hapa, tuna magari mengi ya wagonjwa yanakwenda kununuliwa mwaka huu wa fedha na hivyo tutaendelea kuboresha utaratibu huo kufikisha magari hayo. Nakushukuru sana.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, binafsi naomba kwanza kuipongeza Serikali kwa kuamua kuanza kujenga hata hizo kilometa 20.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri, inaunganisha mikoa minne, kwa maana ya Mkoa wa Tanga, Manyara, Dodoma na Singida. Kama hiyo haitoshi, ni kwamba barabara hii ni barabara ambayo Bomba la Mafuta kutoka Hoima Uganda hadi Chongoleani Tanga ndiko linakopita. Sasa nataka kuuliza swali.
Je, ni lini barabara hii itaanza kujengwa kwa haraka na kuhakikisha kwamba kilometa zote 461 zinakamilika?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili: Mheshimiwa Naibu Waziri alifanya ziara ya kupita barabara hii mwaka 2021; na kipindi hiki mvua zinanyesha.
Je, yuko tayari kumwagiza Meneja Barabara Mkoa wa Tanga aweze kufanya marekebisho katika maeneo ambayo yameharibika?Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Omari Mohamed Kigua, Mbunge wa Kilindi kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Kigua pamoja na Waheshimia wote ambao barabara hii inawagusa ambao wamekuwa wanaifuatilia.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki wameipitisha barabara hii kama ni barabara ya kipaumbele kutokana na umuhimu wake kwa ajili ya bomba la mafuta. Maana linapopita bomba la mafuta ndiyo barabara hii inakopita. Kwa hiyo, Serikali ina mpango kwa kushirikiana na nchi nyingine kutafuta fedha ili ikiwezekana kilometa zote hizi 461 ziweze kujengwa kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali lake la pili, naomba tu kama tulivyotoa agizo kwa wakuu wote wa TANROADS wa Mikoa ahakikishe kwamba anakwenda kwenye madaraja na maeneo yote ambayo yamepata changamoto ya usafiri katika Mkoa wa Tanga; siyo tu kwa Mheshimiwa Kigua, ni pamoja na barabara zake zote ili kuhakikisha kwamba wananchi hawakwami katika kipindi hiki cha mvua. Ahsante.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri tu lakini nina maswali madogo mawili kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hili la Bondo katika Kata ya Mswaki ni eneo muhimu sana kwa ajili ya mvua, halikadhalika kwa ajili ya mazingira. Lakini eneo hili ni la Serikali na lina GN 341 toka 1960. Swali langu je, nini mpango madhubuti na endelevu wa Serikali wa kulinda maeneo haya ili yasiweze kuvamiwa na wananchi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; moja ya ahadi ya wenzetu wa TFS juu ya eneo hili walikuwa wajenge Kituo cha Afya lakini naipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwamba tayari tumekuwa tukipata Milioni 500 Kituo cha Afya kwenye kijiji cha Mswaki kimejengwa. Je, nini kauli ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba wako tayari sasa kutujengea bwawa kwa ajili ya kitu kinaitwa CSR? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa jinsi ambavyo ametoa ushirikiano kwetu kuhakikisha kwamba eneo hii tunalirudisha Serikalini, wananchi ni kweli walikuwa wamevamia eneo hili lakini kwa kutambua umuhimu wa hifadhi basi tumeanza kuwatoa hawa wavamizi na kuweka vigingi ili maeneo haya yaweze kutambulika rasmi kama ni eneo la hifadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango madhubuti wa Serikali ni kuhakikisha kwamba maeneo yote ambayo ni mazuri na ya muhimu katika kuhifadhiwa vizuri tumeendelea kutoa elimu kwa wananchi, na kwa kutambua kwamba wananchi pia ni sehemu ya uhifadhi, hivyo tumekuwa tukishirikiana na wananchi kuhakikisha kwamba maeneo yote ambayo tunayatambua na ni ya muhimu tunayahifadhi vizuri kwa maslahi ya Taifa. Kwa hiyo nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge Serikali inaendelea kuhakikisha kwamba wananchi wanatambua umuhimu wa uhifadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala lingine ambalo amelisema la Kituo cha Afya, ni kweli Serikali iliwahi kuahidi kuwajengea Kituo cha Afya katika Wilaya ya Kilindi katika Kijiji cha Mswaki na kwa bahati nzuri Serikali imetimiza ahadi hiyo. Kwa kuwa, tumekuwa tukitoa CSR katika maeneo mbalimbali ambayo yanazunguka maeneo yaliyohifadhiwa Mheshimiwa Mbunge nimuombe tulichukue ombi lake tuende tukachakate na hatimay tutampa majibu yaliyo sahihi lakini tuwahakikishie wananchi wa Kilindi na Mswaki kwamba tutahakikisha wanapata CSR kama moja ya wajibu wa Wizara ya Maliasili na Utalii. (Makofi)
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Nataka kumwuliza Mheshimiwa Naibu Waziri, barabara ambayo inaanzia Dumila kupita Turiani kupita Kata ya Negelo hadi Vibaoni Handeni, ni barabara muhimu sana. Kwa upande wa Morogoro imeshakamilika kwa kiwango cha lami: Je, ni lini kilometa 120 kwa kiwango cha lami itakamilishwa?
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Omari Kigua, Mbunge wa Kilindi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, barabara aliyoiainisha imeshafanyiwa usanifu; na Serikali inaendelea kutafuta fedha ili kwa umuhimu wa barabara hiyo iweze kujengwa kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, hapo ni upatikanaji wa fedha tu, once tutakavyopata barabara hii itaanza kujengwa. Ahsante.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, nimshukuru pia Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani kwa majibu yenye kutia matumaini kiasi, lakini nina maswali madogo mawili ya nyongeza. Kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Wazari kwamba Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi imetenga eneo kwa ajili ya Kituo cha Polisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; kwa sababu eneo hilo limetengwa takribani miaka ishirini iliyopita je, ni utaratibu upi au mipango ipi au ni parameter zipi ambazo zinatumika kuhakikisha kwamba mnajenga Vituo vya Polisi kwa kuangalia uhalisia wa mahitaji ya eneo husika? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; Mheshimiwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ambaye sasa hivi ni Waziri wa Mambo ya Ndani alikwishatembelea Wilaya ya Kilindi na kujionea uhalisia wa changamoto ya Kituo cha Polisi jinsi kilivyo.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri, yuko tayari kutoa commitment kwa wananchi wa Wilaya ya Kilindi kwamba mwakani watajenga Kituo cha Polisi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kigua, Mbunge wa Kilindi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kumekuwa na ahadi zinatolewa na zimechukua muda mrefu, hususan kituo hiki, eneo limetengwa muda mrefu kama alivyosema miaka 20, na ametaka tuseme tutazingatiaje uhalisia wa maeneo husika?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba, tunapotaka kujenga eneo lolote lazima tuzingatie uhalisia wa eneo. Ndiyo maana wataalam wetu wanakwenda kule kufanya tathmini ya udongo ili kuweza kujiridhisha vifaa na kiwango gani cha ujenzi utakaohitajiwa. Kwa hiyo, watakapokuwa wanaanza ujenzi, mahitaji halisi ya eneo la Mheshimiwa Mbunge yatazingatiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hili la commitment nimesema, tutatenga kwenye bajeti ya 2023/2024. Sasa bajeti yetu ikishapita hapa, namwomba Mheshimiwa Kigua asome maeneo yatakayojengewa vituo, atajiridhisha kwamba eneo lake litakuwa na mpango huo wa ujenzi. Nashukuru. (Makofi)
MHE. OMAR M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi, ina vijiji 102, vitongoji 611, kata 21 na tarafa nne.
Je, ni lini Serikali italigawa Jimbo hili la Kilindi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba nichukue hoja ya Mheshimiwa Mbunge twende tukajiridhishe na takwimu ambazo amezisema, tuone vigezo na baadaye tuweze kufanya maamuzi, baada ya tathmini hizo tutawapa mrejesho nini hatua inaweza kufuata baada ya tathmini hiyo, ahsante.
MHE. OMAR M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ambayo yanatia moyo kwa wana Kilindi na Watanzania kwa ujumla. Ninayo maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; kwa kuwa Jimbo la Kilindi lina eneo kubwa la utawala; lina vijiji 102, tarafa nne, kata 21 na vitongoji 611, na gari ambalo linatumika sasa hivi ni gari bovu sana. Je, Serikali iko tayari kutuongezea gari lingine baada ya utaratibu huu ambao upo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa utaratibu huu ambao kila Mbunge anaujua hapa kwamba kila halmashauri itapata magari ya wagonjwa kwa mpango wa COVID-19. Je, ni lini utaratibu huo utakamilika ili wananchi wa Tanzania waweze kupata magari hayo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Omar Mohamed Kigua, Mbunge wa Jimbo la Kilindi kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianza kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Omari Kigua kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwasemea wananchi wa Jimbo la Kilindi. Mimi nimhakikishie kwamba Ofisi ya Rais – TAMISEMI, tutaendelea kushirikiana naye ili kuhakikisha wananchi wa Kilindi wanapata maendeleo wanayoyatarajia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na ukubwa wa eneo na uhitaji wa gari jingine, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, katika magari haya yanayonunuliwa, jumla ya magari yote yanayonunuliwa kwa ajili ya huduma za afya katika halmashauri zetu zote, ni magari 407. Kwa hiyo tuna magari 195 kwa ajili ya wagonjwa lakini tuna magari 212 kwa ajili ya ajili ya huduma za usimamizi, chanjo na mambo mengine yanayohusiana na afya. Kwa hiyo, kila halmashauri itakuwa na magari mawili.
Mheeshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie kwamba kutakuwa na magari hayo mapya na ni kabla ya Juni mwaka huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kuhusiana na lini magari hayo yanakuja, taratibu za manunuzi zinaendelea na mpango wa Serikali ni kuhakikisha ifikapo tarehe 30 Juni, magari yawe yamepatikana; au kama atachelewa sana basi ni Julai, lazima magari yatakuwa yamefika kwenye halmashauri zetu, ahsante.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, barabara ya Handeni – Kiberashi – Singida ni barabara muhimu sana na barabara hii nashukuru mkandarasi alikwisha ripoti site lakini kinachoendelea sasahivi ni kwamba kama vile kazi aiendelei Je, tatizo liko wapi? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kigua Mbunge wa Kilindi kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, bahati nzuri wiki iliyopita nimetembelea barabara hii kuangalia changamoto ni nini? Mkandarasi yupo site ameishaanza kazi anakamilisha majengo ya Muhandisi mshauri na kulikuwa na changamoto ndogo ambazo tumeisha zi-sort out na tayari nataka nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuanzia wiki inayoanza hii kasi itaongezeka kwa hiyo barabara inaendelea. Ahsante. (Makofi)
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Wilaya ya Kilindi ina Tarafa Nne, Tarafa Tatu zina vituo vya afya. Je, ni lini Serikali itajenga kituo afya Tarafa ya Kimbe, Kijiji cha Ndegerwa? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Omari Kigua Mbunge wa Jimbo la Kilindi kama ifiatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Tarafa hii ya Kimbe ambayo haina kituo cha afya tayari ilishawekwa kwenye mpango wa Tarafa za kimkakati, sasa fedha tu inatafutwa ikishapatikana itakwenda kujenga kituo cha afya kwa ajili ya kusogeza huduma kwa wananchi. Ahsante.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, barabara inayotoka Handeni kwenda Songe na Kiteto ni siku ya pili sasa hivi haipitiki kutokana na na mvua zinazonyesha, na shughuli zote za uchumi zimesimama. Je, nini kauli ya Serikali juu ya barabara hiyo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kigua, Mbunge wa Kilindi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niwape pole wananchi wa Kilindi kwa adha wanayoipata kwa sababu ya changamoto ya mvua. Napenda nitumie nafasi hii kumuagiza Meneja wa TANROADS Mkoa wa Tanga aweze kufika maeneo yote ambayo yameathirika na kuweza kurejesha mawasiliano kwa muda, na pale ambapo changamoto itakuwa ni kubwa, basi aweze kuwasiliana na TANROADS Makao Makuu kwa ajili ya kutoa msaada mkubwa zaidi, ahsante. (Makofi)
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Ni lini kata ya Mkindi, Kata za Masagaru, Kwekivu na Kimbe vijiji hivi vitapitiwa na minara kwa ajili ya masiliano kwa ajili ya wanachi wa maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika,napenda kujibu swali la Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, mwezi huu wa tano Serikali inatarajia kuingia mkataba na watoa huduma ili kuweza kufikisha huduma ya masiliano katika maeneo 763. Vile vile Serikali imeshaanza kufanya tathmini katika vijiji 2116 vitakavyokamilika. Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kufikisha huduma ya mawasiliano vikiwemo vijiji na kata ambazo Mheshimiwa Mbunge amevitaja, ahsante sana.
Ahsante, Waheshimiwa tunaendelea Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Mheshimiwa Ngasa.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri tu. Lakini pia nitumie nafasi hii kukupongeza wewe Mheshimiwa Mwenyekiti wangu wa Kamati ya Bajeti, hakika uko vizuri kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maswali madogo mawili kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba maeneo madogo ya utawala ni tofauti na maeneo makubwa ya utawala. Sasa je, nini mpango wa Serikali wa kuhakikisha kwamba maeneo madogo hayapewi rasilimali nyingi na watumishi wengi kuliko maeneo makubwa ya utawala? Swali la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; nini mpango mkakati wa kuhakikisha kwamba maeneo yote makubwa ambayo yako sawa na Kilindi ambayo yanahitaji kugawanywa yanafanyiwa mkakati wa haraka ili yaweze kugawanywa? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE NA URATIBU): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Omari Mohamed Kigua, Mbunge wa Kilindi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza kumpongeza sana Mheshimiwa Omari Kigua kwa kazi nzuri anazofanya jimboni, lakini pia niendelee kumhakikishia kwamba Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, tunatambua uwepo wa maeneo haya makubwa na madogo ya kiutawala. Na kama nilivyojibu katika swali la msingi alilouliza, tutaendelea kufanya kazi kuona namna ambavyo tunaendelea kufikisha huduma karibu na wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwa ufafanuzi zaidi, vigezo tunavyovizingatia katika nchi za SADC ikiwemo na Tanzania tutaangalia pia ukubwa wa jimbo husika, mipaka ya kiutawala, hali ya kiuchumi na hali ya kijiografia pamoja na suala la idadi ya watu katika eneo husika, pamoja na uwezo pia wa Ukumbi wetu wa Bunge na idadi ya Wabunge wa Viti Maalum; yote hayo tutayaangalia katika mchakato huu alioulizia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, anasema pia maeneo makubwa; tunatambua na tunafahamu na nimelijibu swali hili hii ni mara ya pili ndani ya Bunge lako Tukufu. Maeneo haya ambayo ni makubwa tume kama ilivyopewa majukumu na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tutafanyia kazi maeneo hayo na tutaomba tuendelee kupata ushirikiano wa kutosha kwa Waheshimiwa Wabunge wote kwa pamoja na wadau wote wa masuala ya uchaguzi, ahsante. (Makofi)
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Wananchi wa Wilaya ya Kilindi wanatambua jitihada za Serikali za kupeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya. Lakini tunazo kata tatu kwenye vituo vya afya vitatu kwenye Kata ya Jaila, Masagalu na kata ya Maswaki tunahitaji at least milioni mia, mia ili kuweza kumalziia vituo vya afya. Je, ni lini Serikali italeta fedha katika maeneo hayo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI):
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhamira ya Serikali kujenga vituo vya afya katika Mkakati ikiwemo kata za kwa Mheshimiwa Kigua kule Kilindi Kata hizi za Jaila, Masagalu na Mswaki na tutaangalia katika mwaka wa fedha kama zimetengwa fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo hivi vya afya na umaliziaji. Kama fedha hizo hazijatengwa nimhakikishie Mheshimiwa Kigua katika mwaka wa fedha 2024/2025 ili Jaila, Masagalu na Mswaki ziweze kupata fedha hizi kwa ajili ya umaliziaji.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwanza nitoe shukrani za dhati sana kwa Serikali yetu kwa kutujengea daraja hili ambalo lilikuwa linaleta usumbufu mkubwa sana kipindi cha mvua. Baada ya shukrani hizo, sasa nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Kata hizi mbili za Songwe na Bokwa kuna ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami; je, Serikali iko tayari kuweka taa katika eneo hilo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kuna Madaraja mawili ya Chakwale na Nguyami ambayo yanunganisha Wilaya za Kilindi na Gairo. Je, ni lini Serikali itajenga madaraja hayo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Omari Mohamed Kigua, Mbunge wa Kilindi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwa sasa barabara zote zinazojengwa na zinazopita kwenye miji mikubwa ama centers kubwa, maelekezo ni kwamba ni lazima tuweke taa kwa ajili ya matumizi ya usiku katika miji yote ambayo ni mikubwa. Kwa hiyo kwa barabara hiyo ambayo inajengwa nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tathmini itafanyika na tutahakikisha kwamba tunaweka taa.
Mheshimiwa Spika, kwenye swali lake la pili, tumeshakamilisha usanifu wa kina mwaka huu wa fedha kwa Madaraja yote mawili ya Chakwale na Nguyami ambayo yanaunganisha Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Tanga, na tumepanga fedha, kwamba mwaka 2023/2024, Madaraja yote hayo mawili ya Chakwale na Nguyami yanakwenda kuanza kujengwa, ahsante. (Makofi)
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, toka mwaka 2015 nilikuwa nikiomba tujengewe Kituo cha Polisi katika Wilaya ya Kilindi. Naomba commitment ya Serikali juu ya ujenzi wa kituo hicho cha Polisi. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimjibu Mheshimiwa Kigua kwa uhakika kabisa kwamba, ni kipaumbele cha Wizara kupitia Jeshi la Polisi kwamba, Wilaya zote ambazo hazina vituo vya Polisi zinajengewa vituo vya Polisi. Nikupe assurance Mheshimiwa tutaangalia kwenye mpango wetu namna gani tunaweza tuka-fast track kutokana na majukumu muhimu ambayo Lindi inakabiliana nayo kwa maana ya uhalifu, mifugo, na kadhalika ili waweze kuwa na kituo cha polisi kumwezesha OCD kutimiza majukumu yake vizuri. Nakushukuru sana Mheshimiwa.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, miaka mitatu iliyopita Serikali katika mpango wake wa maendeleo ilijielekeza kwamba itajenga SGR kwa reli hii ya kuanzia Tanga – Moshi - Arusha hadi Musoma. Je, mpango huo bado upo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kigua, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali itajenga reli hiyo ya Dar es Salaam – Tanga - Moshi mpaka Arusha, lakini kwa sasa tuna awamu mbili ambapo awamu ya kwanza ilikuwa ni kujenga reli ya kutoka Dar es Salaam mpaka Mwanza na awamu ya pili kutoka Dar es Salaam mpaka Kigoma. Mara tutakapokamilisha hizi ndipo tutakapokuja katika hii reli ya kutoka Dar es Salaam – Tanga - Moshi mpaka Arusha na mpango huo uko vilevile.
Kwa hiyo, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge wa maeneo hayo kwamba Serikali ina nia hiyo, lakini kwa sasa tunakamilisha hizi ambazo tumekwishaanza, ahsante.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwanza niipongeze Serikali ya Chama Cha Mapinduzi kwa kutujengea Vituo vya Afya kwenye tarafa tatu. Tuna tarafa nne Wilaya ya Kilindi lakini tuna Tarafa moja ya Kimbe haina kituo cha afya na umbali kutoka tarafa hiyo hadi Makao Makuu ya Wilaya ni takribani kilomita 120;
Je, nini mpango wa Serikali wa kujenga kituo cha afya kwenye tarafa hiyo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nijibu swali la Kigua Mbunge wa Kilindi, kwamba Tarafa ya Kimbe haina na kituo cha afya. Serikali imetenga mwaka wa fedha uliopita zaidi ya bilioni 117 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya vya kimkakati kote nchini ambapo vingine vilikwenda kwa Mheshimiwa Kigua kule Kilindi. Tutakaa na Mheshimiwa Kigua kuona hii Tarafa ya Kimbe nayo tunafanyaje ili iweze kutengewa fedha kupata ujenzi wa kituo cha afya kama vile kata ya kimkakati ili hizi kata zote zinazozunguka tarafa hii ziweze kupata huduma nazo za afya.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na ninaishukuru Serikali kwa majibu mazuri tu. Nina maswali mawili madogo tu ya nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwa sababu barabara hii inaunganisha Kata tatu. Kata ya Msanja, Kata ya Kilindi Asilia na Kata ya Kimbe, ni Kata ambazo zina uzalishaji mkubwa sana wa mahindi na kipindi cha mvua inakuwa ni shughuli kubwa magari kupita. Sasa kwa sababu suala hili liko Serikalini; Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kuelekeza Mkoa sasa kufanya tathmini hiyo na iweze kupandishwa hadhi barabara hiyo?
Swali la pili ni kwamba barabara hii ina madaraja mengi na ina vivuko vingi sana na kipindi cha mvua haipitiki. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri uko tayari kutoa maelekezo kwa TARURA ili maeneo haya yaweze kurekebishwa na Wananchi wa Wilaya ya Kilindi waweze kupata huduma ya Serikali? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, ninaomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kigua, swali la kwanza kuhusu kuelekeza mkoa; kama nilivyokuwa nimesema kwenye majibu yangu ya msingi kwamba, taratibu za kupandisha au kuteremsha barabara kuwa ya Mkoa ni taratibu za kisheria. Hivyo basi, ningeshauri Mkoa wa Tanga waanze kuchukua hatua stahiki za kupandisha barabara hii kwa kukaa Mheshimiwa Kigua kule Kilindi kupitisha kwenye DCC yao na ikitoka DCC iweze kwend RCC na baadaye kwenda kwenye Bodi ya Barabara ya Mkoa, kisha waweze kuandika kwa Waziri mwenye dhamana ya barabara ambaye ni Waziri wa Ujenzi ili na yeye aweze kutuma timu ya kufanya tathmini ili barabara hii iweze kupandishwa kuwa ya Mkoa. Nitakaa na Mheshimiwa Kigua tuone tunafanya vipi na wenzetu wa Wizara ya Ujenzi ili barabara hii iweze kuanza huu mchakato wa kupandishwa.
Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye swali lake la pili la madaraja na vivuko ambavyo vinahitajika sana. Ni kweli nikiri kwamba barabara hii ni muhimu sana kwa uzalishaji na wananchi wa kule Kilindi kwa ajili ya kutoa bidhaa zao mashambani Mheshimiwa Mbunge amekuwa akilifuatilia sana, tutakaa naye vilevile kuona ni namna gani tutapata fedha kwenye bajeti ya TARURA hii inayokuja 2023/2024 ili kuweza kutengeneza vivuko zaidi kwa sababu tayari katika mwaka huu pekee wa fedha tunaoumaliza tulitengeneza boksi Kalavati 15, drift ndefu yenye mita 15 lakini imechongwa vilevile kilometa 21 kwenye barabara hii, lakini kwa sababu ina urefu wa kilometa 47 tutakaa tuone ni namna gani tunaendelea kutengeneza maeneo hayo yaliyosalia. (Makofi)
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi kwa mwaka wa fedha 2024/2025 inatarajia kutenga au itatenga shilingi milioni 100 kwa ajili ya kumalizia Kitua cha Afya cha Kilindi asilia na shilingi milioni 40 kwa ajili ya hospitali ya wilaya.
Mheshimiwa Spika, sasa, nataka tu nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri, hizi taarifa za kwamba tumetenga shilingi milioni 100 kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa Zahanati ya Masagalu amezipata wapi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Serikali imekuwa na utaratibu wa kuhamasisha wananchi kujenga majengo na wao kutenga milioni 50. Je, Serikali haioni iko sababu ya kutenga milioni 50 na kuwapelekea wananchi wa Masagalu na kumalizia majengo haya? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, nashukuru sana, nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa namna ambavyo ameendelea kuweka kipaumbele katika Baraza la Madiwani ili kuhakikisha kwamba wanatenga fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya ukamilishaji wa majengo ya Zahanati na Vituo vya Afya.
Mheshimiwa Spika, Serikali ni moja. Mkurugenzi wa halmashauri, Katibu tawala wa mkoa wana wajibu wa kupokea maelekezo kutoka katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI, hasa tunapoona vigezo vya ukamilishaji wa majengo hayo vinakidhi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa mujibu wa jengo hili ambalo lina zaidi ya miaka mitano halijakamilika, tumemwelekeza Mkurugenzi na amechukua hiyo commitment kwamba, atenge milioni 100 kama kipaumbele katika Mwaka wa Fedha 2024/2025 kukamilisha boma hili ambalo lina muda mrefu na baadaye tutaendelea na maboma mengine.
Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali ina utaratibu wa kutenga milioni 50 kwa ajili ya kukamilisha maboma na Halmashauri hii ya Kilindi imekuwa ikipata fedha hizo. Pia, nimhakikishie tu kwamba tutaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuhakikisha tunachangia ukamilishaji wa zahanati hiyo. Ahsante.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Ni Septemba niliuliza swali Na. 76 juu ya wananchi ambao wamevamia Msitu wa Bono uliopo Kijiji cha Mswaki kwenye Kata ya Msanja na Serikali ilisema itawaondoa itakapofika Desemba 30, kwa maana ya mwaka 2022. Nataka kujua: Ni nani ambaye anazuia kuondoa wananchi wale ambao wanafanya uharibifu mkubwa na msitu huo tunaoutegemea kwa ajili ya mvua? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, bado Serikali inasimamia maazimio yake yale kwamba wananchi wale wataondolewa kwenye msitu ule. Naomba Mheshimiwa Mbunge, atupe fursa tulifanyie kazi ili tutekeleze kusudio letu.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, kwenye Kata ya Kilindi Asilia na Kata ya Luhande kwenye Vijiji vya Misufini kuna changamoto kubwa ya minara, kwa maana ya mawasiliano yanakatika mara kwa mara.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri, uko tayari kutuma timu yako kuangalia namna ambavyo mawasiliano yanavyopatikana muda wote?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Omari Kigua, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, tuko tayari kama Wizara kutuma wataalamu wetu kwenda kufanya tathmini ili tujiridhishe na uhalisia wa tatizo na kuchukua hatua stahiki, ahsante.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Kilindi haina ofisi au kituo cha polisi na Wizara imekwishaahidi zaidi ya mara tano. Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya Mambo ya Ndani amekwishafika Wilaya ya Kilindi na kujionea ambavyo mazingira siyo mazuri. Mheshimiwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, naomba kupata kauli yako.
Ni lini mtajenga kituo cha polisi katika Wilaya ya Kilindi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kipaumbele cha Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kuhakikisha kwamba maeneo yote ya Mikoa na Wilaya ambayo hayana Vituo vya Polisi kwa ngazi hizo wanajengewa vituo hivyo. Nikupe assurance Mheshimiwa Kigua, kwamba Wilaya yako ya Kilindi, ni moja ya Wilaya itakayopewa kipaumbele mara tutakapopata fedha za maendeleo kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Ngazi ya Wilaya, hasa kwa kuzingatia kwamba umepata wahamiaji wengi kutoka kule Ngorongoro na ni wafugaji wanahitaji kuwa na Kituo cha Polisi chenye hadhi hiyo ili waweze kuhudumiwa ipasavyo. Ahsante. (Makofi)
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Katika Kata ya Mkindi kuna Kijiji cha Kihwenda ambapo panajengwa bwawa kwa ajili ya wafugaji. Ni takribani mwaka wa pili sasa Mkandarasi ameondoka site na bwawa lile ni muhimu sana kwa maji kwa ajili ya wafugaji pamoja na wananchi. Je, nini mpango wa Serikali kuhakikisha kuwa, Mkandarasi anarudi na bwawa lile linakamilika? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli bwawa hilo limesimamishwa ujenzi wake. Nimhakikishie Mbunge tutakwenda kufuatilia, tutaangalia mimi na yeye twende kule, tuangalie na wataalam tuone namna ambavyo tunamrudisha Mkandarasi site ili aweze kukamilisha bwawa hilo na wananchi waweze kupata huduma katika eneo hilo. Ahsante. (Makofi)
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya kwa maelezo mazuri tu kwamba ndege hizi zisizokuwa na rubani ni muhimu kwa ajili ya kutoa huduma za kiafya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hali ambayo Watanzania tumeipata ya Mvua za El Nino ni dhahiri kwamba utaratibu huu ni mzuri na unatija kwa Serikali. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri, mko tayari kuhakikisha kwamba mfumo huu wa kupeleka dawa vijijini unaharakishwa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Naibu Spika, tuko tayari na kweli kwa wakati kama huu njia hiyo ni mkombozi hasa ndani ya Wilaya bila kuzungumzia kwa maana ya kutoka Taifa kwenda kwenye Wilaya, lakini kutoka ndani kwenye Wilaya kwenda kwenye vituo utaokoa sana. Tutaendelea kuharakisha tuone tutafika mahali gani, lakini nisiahidi kwamba kwa kipindi gani, ila tunaendelea, kwa sababu coordinate ni muhimu ili kuongoza lile jambo la network.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri na nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye kipande cha makao makuu ya wilaya kwenye Kata ya Songe na Bokwa ujenzi unaendelea na sehemu zimekamilika, lakini hakuna taa na maeneo hayo yanakuwa yanapata ajali; je, Serikali ni lini itaweka taa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kipande cha Handeni – Kiberashi katika zile kilometa 20 baadhi ya wananchi wamepisha ujenzi wa kiwango cha lami lakini hawajalipwa fidia hadi leo; je, nini mpango wa Serikali wa kuwalipa fidia wananchi hawa? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu wa Serikali kwa sasa ni kuhakikisha kwamba makao makuu ya wilaya tunaweka taa na ndiyo kipaumbele na sasa hivi tunafanya manunuzi ya taa kwa ujumla wake. Nimwombe Mheshimiwa Mbunge tuone kama makao makuu ya wilaya yake ipo kwenye mpango.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ulipaji wa fidia kwa wananchi hawa nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba limekuwa ni suala ambalo Mheshimiwa Mbunge tunajua umekuwa unalifuatilia na sisi kama Wizara tumeshawasiliana na wenzetu wa Wizara ya Fedha ili waweze kukamilisha taratibu za malipo ili wananchi hao ambao wamepisha ujenzi wa mradi huo waweze kulipwa, ahsante.
MHE. OMAR M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimwulize Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba kwenye Wilaya ya Kilindi kipo Kijiji cha Mgera ambacho kina daraja limekatika takribani miaka mitatu sasa na Serikali haijarekebisha hali hiyo na upande wa pili ndipo ambapo taasisi zote za Serikali zipo huko. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kutoa maelekezo kwa TARURA kwenda kurekebisha daraja hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, katika vipaumbele vya TARURA ni pamoja na kuhakikisha kwamba inahakikisha miundombinu ya barabara hizi haikatiki kimawasiliano. Kwa hoja ya Mheshimiwa Mbunge naomba baada ya kipindi hiki cha maswali na majibu tukutane, tukae, tuweze kufanya mawasiliano na kama ni kweli eneo hili limekata mawasiliano, kuna umuhimu na kipaumbele kikubwa sana ambacho inabidi kitolewe kwa ajili ya kuhakikisha tunarudisha mawasiliano katika eneo hili.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, Kata ya Jaila tunayo zahanati ambayo ina sifa zote za kuwa kituo cha afya, lakini kwa bahati mbaya kuna baadhi ya majengo hayajakamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Mheshimiwa Naibu Waziri upo tayari kutuletea kiasi cha fedha kumalizia majengo hayo na kuwa kituo cha afya? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikifanya jitihada za kuboresha huduma za afya msingi. Katika jitihada hizo imekuwa ikipandisha hadhi zahanati kuweza kutoa huduma za vituo vya afya kwenye maeneo ambayo yanauhitaji, lakini yana mazingira ambayo yanawezesha kuanzishwa kwa kituo cha afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge ametaja eneo hili la Zahanati ya Jaila ambayo imepandishwa hadhi kuwa kituo cha afya. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali inatafuta fedha kuhakikisha hizi zahanati zote ambazo zimepandishwa hadhi kuwa kituo cha afya zinapatiwa fedha ili kuimarishwa ili huduma zitakazotolewa ziendane na huduma zinazotakiwa kutolewa katika vituo vya afya. Kwa hiyo, nikutoe shaka Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali inalifanyia kazi suala hili.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kwanza kuipongeza Wizara ya Maji kwa kazi nzuri sana kwa sababu kata hii ilikuwa ina changamoto kubwa sana ya maji. Sasa, nina swali moja tu la nyongeza. Je, Serikali iko tayari baada ya kukamilisha mradi huu kuhakikisha kwamba wananchi ambao wako pembezoni na kata hii pia wanapata maji? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Omari Kigua, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Chama Cha Mapinduzi inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa takribani shilingi bilioni 39 katika kufanya miradi 13 katika Jimbo la Kilindi. Katika jimbo hili, miradi tisa inafanywa kwa Mfumo wa Wakandarasi na miradi minne wanafanya kwa Mfumo wa Force Account.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaamini kwamba miradi hii 13 itakapokamilika, vijiji 78 vinaenda kunufaika na wakazi takribani 239,810 watanufaika na mradi huo. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pindi miradi hii itakapokamilika Serikali itaenda kuanza kupanua wigo wa upatikanaji wa maji vitongojini kulingana na upatikanaji wa fedha. Nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Wilaya ya Kilindi ni miongoni mwa Wilaya ambazo zina uzalishaji mkubwa sana wa mahindi, lakini hatuna soko la kisasa ambalo lingeweza kusaidia mapato kwa ajili ya Wilaya ya Kilindi. Je, Mheshimiwa Waziri yupo tayari kututengea fedha kwa ajili ya ujenzi wa soko hilo? Ahsante
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitumie nafasi hii kuendelea kumkumbusha mkurugenzi anaweza akafanya tathmini, wakaandika andiko la kuonesha uhitaji, lakini kuonesha kwamba soko hili linaweza likawa lina tija kwa wananchi kama Mheshimiwa Mbunge alivyozungumza, apitishe katika michakato yote na ikikidhi vigezo kwa kweli Serikali italeta fedha kwa ajili ya kuhakikisha soko hili muhimu linajengwa kwa maslahi mapana ya wananchi. Sifa mojawapo muhimu sana katika mchakato huu ni kwamba ni lazima halmashauri iwe ilipata hati safi kwa miaka mitatu mfululizo.
Kwa hiyo andiko hili likikidhi vigezo hivi vyote, basi namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali italeta fedha kwa ajili ya ujenzi wa soko hili.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Kilindi ilipatikana mwaka 2002, lakini toka mwaka 2015 nimeingia hapa Bungeni, nimekuwa nikiomba Kituo cha Polisi cha Wilaya. Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi cha Wilaya?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omari Mohamed Kigua, Mbunge wa Kilindi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua Wilaya ya Kilindi ni Wilaya kubwa na ni kweli haina kituo cha Polisi cha Wilaya. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tunatenga fedha kwa mwaka wa fedha unaokuja 2025/2026, kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Kilindi, ahsante sana. (Makofi)
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Kilindi tunayo shule ya wasichana inaitwa Kilindi Girls na ni kwamba eneo hilo ambalo ipo hii shule ni eneo ambalo linazungukwa at least na msitu. Sasa kwa usalama wa wasichana ni jambo muhimu sana, je, Mheshimiwa Naibu Waziri, uko tayari kulipokea hili na kulifanyia kazi? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, ninampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kuzungumzia masuala ya kuimarisha usalama wa wanafunzi wetu wanapokuwa shuleni. Ninaomba nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge, hili tumelipokea na tutafanya jitihada kwa sababu Serikali imeanza kujenga miundombinu hii kwa awamu. Awamu ya kwanza miundombinu hii ya shule imepatikana na ndiyo maana watoto wameweza kuanza kusoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kila awamu Serikali itakuwa inaleta fedha kwa ajili ya kuendelea kuboresha miundombinu iliyobakia. Kwa hiyo, nimelichukua jambo lako hili Mheshimiwa Mbunge kwa ajili ya kulifanyia kazi.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naipongeza Serikali na kuishukuru sana kwa kutupa kiasi hicho cha fedha ambacho kwa kweli kwa kiasi kikubwa kimeweza kusaidia miundombinu katika Jimbo langu la Wilaya ya Kilindi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina swali moja tu. Hizi shule zote ambazo nimezitaja hapa ni shule za Kidato cha Tano na cha Sita lakini zina uhitaji mkubwa sana sana hususan shule ya Sekondari ya Mkindi na Shule ya Sekondari Vungwe. Hizi shule tuna wanafunzi na kila shule ina wanafunzi 600 na hawana bwalo la kulia chakula. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari kuiona hii kama ni dharura ili kuweza kurahisisha kupata huduma kwa wanafunzi hawa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge, kwa kweli amekuwa akifuatilia sana maslahi mazuri na mapana ya wanafunzi katika jimbo lake kwa kuhakikisha anaendeleza miundombinu hii katika shule hizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa sababu tayari Serikali imeshaanza na kila mwaka inatenga fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu hii. Naomba nimtoe hofu kwamba Serikali inalichukua hili na tutalifanyia kazi kwa ukaribu. Tutazungumza mimi na wewe tuone ni namna gani tunaweza kuhakikisha miundombinu hii muhimu inapatikana kwa ajili ya wanafunzi wetu hawa katika shule hizi alizozitaja Mheshimiwa Mbunge.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa Barabara ya kutoka Handeni hadi Mafleta (kilometa 20) ni takribani mwaka wa pili sasa, lakini wananchi waliopisha barabara hii hawajalipwa fidia. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri ni lini wananchi hawa watalipwa fidia?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, wananchi wale walishafanyiwa tathmini na sisi kama Wizara tulishawasilisha ile tathmini, kwa maana ya thamani ya fidia yao, kwa ajili ya kulipwa. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, wananchi wawe na Subira, Serikali ipo inajipanga kuhakikisha kwamba, wanalipwa hiyo fidia yao. Ahsante.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwenye eneo langu katika Jimbo la Kilindi kuna Kata inaitwa Kata ya Kilwa barabara inayoanzia Kata ya Kwediboma – Kilwa hadi Kwadundwa mvua za El-Nino za mwaka jana zimeharibu miundombinu na kata hiyo sasa hivi haifiki kabisa. Je, Serikali ina mpango mkakati gani wa kuhakikisha kwamba na eneo hilo linapitika kwa sababu lina uzalishaji mkubwa wa bidhaa nyingi sana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu mkubwa wa barabara zetu hizi za TARURA hasa kiuchumi lakini pia kijamii; na inatambua kuwa mvua zilizonyesha za El-Nino zimefanya uharibifu mkubwa. Kwa hiyo, Serikali imekua ikitenga fedha kila mwaka wa bajeti kuhakikisha kwamba inafanya matengenezo na inajenga barabara mpya hizi za TARURA. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaendelea kupeleka fedha katika Jimbo lake kwa ajili ya kuhudumia barabara zake ikiwemo hii aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Je, Wilaya ya Kilindi ni miongoni mwa Wilaya hizi zitakazopata Magari ya Polisi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nchi hii ina Wilaya 139, tumeshagawa magari 71 na tumeagiza mengine 122. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Omari Mohamed Kigua, Mbunge wa Kilindi kwamba, Wilaya ya Kilindi ni moja kati ya Wilaya zitakazopata gari, kwa ajili ya wananchi wake. (Makofi)
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru, kwanza kwa dhati ya moyo wangu na kwa niaba ya Wana-Kilindi ninaomba niipongeze Serikali kwa sababu lilikuwa ni jambo la muda mrefu sana, sana, sana. Niombe tu kwamba Serikali au Wizara ya Mambo ya Ndani iharakishe kwa ajili ya kuanza ujenzi huo, lakini nina swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Kata ya Kikunde wamejenga Kituo cha Polisi na kimefikia 99%. Kwa utaratibu ule ule wa ku-support nguvu za wananchi; je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kutenga kiasi cha fedha ili kuwa-support wananchi wa Kata ya Kikunde?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tunapokea pongezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Kituo cha Polisi cha Kata alichokitaja Mheshimiwa Mbunge, ni kweli tunajenga na kwamba tunamalizia maboma ambayo tayari wananchi wamekwishaonesha juhudi zao za kujenga vituo hivyo. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kituo chake hicho pia tutakichukua tukiongeze kwenye mpango ili tukimalizie na ili wananchi wapate huduma ya ulinzi na usalama katika eneo lao, ahsante sana. (Makofi)
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, kwanza nasikitika sana kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa sababu, msingi wa swali langu ni kwamba tarafa hii ina kata mbili; Kata ya Negero na Kimbe ambapo wananchi wa kata hizi wanapata huduma Wilaya ya Handeni na Wilaya ya Mvomero na kwa kipindi hiki cha mvua ni kwamba wananchi hawapati huduma hiyo. Swali langu ni kwamba, je, Serikali iko tayari kujenga kituo cha afya cha kimkakati katika Kata ya Kimbe?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, namwomba Mheshimiwa Naibu Waziri atume timu yake ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwenda kuangalia adha wanayopata wananchi kwenye huduma hii ya afya katika maeneo hayo, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba tu nimtoe hofu na mashaka Mheshimiwa Omari Kigua kwamba, Serikali inatambua umuhimu wa kujenga Kituo cha Afya katika Kata ya Kimbe kwa sababu, wananchi wengi wanahitaji huduma za afya na kituo cha afya kilicho jirani kiko umbali mrefu sana. Kwa hiyo, ndiyo maana tumemwelekeza Mkurugenzi, ameshatenga fedha shilingi milioni 136 na tayari jengo la OPD liko 92%. Kwa hiyo, utaona tayari tumeanza utekelezaji na ni suala tu la kutafuta fedha, tutaendelea kuhakikisha kwamba tunajenga kituo hicho na kinakamilika mapema iwezekanavyo.
Mheshimiwa Spika, pili, kuhusiana na kutuma wataalamu, tunafahamu, lakini nitamwelekeza Mganga Mkuu wa Mkoa pia Mganga Mkuu wa Halmashauri waweze kuleta taarifa rasmi ili tuweze kuongeza kasi ya kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo hiki cha afya, ahsante.