Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Lolesia Jeremia Maselle Bukwimba (20 total)

MHE. LOLESIA J. M. BUKWIMBA aliuliza:-
Je, ni lini miradi ya usambazaji wa umeme katika Kata za Kamena, Nyamalimbe, Busanda, Nyakamwaga, Nyakagomba, Nyaruyeye, Kaseme, Magenge, Nyalwanzaja na Bujula katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita utaanza rasmi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa napenda kujibu swali la Mheshimiwa Lolesia Jeremiah Maselle Bukwimba, Mbunge wa Jimbo la Busanda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Kanda za Busanda na Nyakamwaga zinafanyiwa tathmini ya Kampuni ya Ramaya International Tanzania Limited na zimewekwa kwenye Mpango wa Mradi wa Geita – Nyakanazi Transmission Line.
Mheshimiwa Spika, kazi ya kupeleka umeme kwenye Kata za Busanda na Nyakamwaga, itajulimsha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 23.7; pamoja na ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 0.4 wenye urefu wa kilomita 18.5; lakini kadhalika, ufungaji wa transfoma sita ambapo transfoma moja ina ukubwa wa kVA 50; transfoma mbili mbazo zina ukubwa wa kVA 100 na transfoma tatu zenye ukubwa wa kVA 200.
Mheshimiwa Spika, gharama ya kazi hii inakadiriwa kuwa shilingi bilioni 1.6. Kazi inatarajia kuanza mwezi Oktaba mwaka huu wa 2016 na itakamilika mwaka 2018.
Mheshimiwa Spika, Kata za Kamena, Nyamalimbe, Kaseme pamoja na Nyarwanzaga, zimefanyiwa tathmini na kubainika kuwa kazi ya kupeleka umeme kwenye Kata hizo itajumuisha ujenzi wa njia ya umeme msongo kilovoti 33 yenye urefu wa kilomita 50.8. Kadhalika ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilomita 25, pamoja na ufungaji wa transfoma 11 ambapo transfoma tatu zaina ukubwa wa kVA50; transfoma sita zina ukubwa wa kVA 100 na tranfoma mbili zenye ukubwa wa kVA200. gharama ya kazi hii ni shilingi bilioni 2.87.
Mheshimiwa Spika, Kata hizi zimo pia katika mpango wa awamu ya tatu ya kusambaza umeme vijijini yaani REA - Phase III unaotajariwa kukamilika mwezi Julai, 2016.
Mheshimiwa Spika, tathmini ya mahitaji halisi kwa ajili ya kupeleka umeme katika Kata za Nyaruyeye, Magenge, Nyakagomba na Bujula inafanywa na TANESCO na itakamilika mwezi Machi, mwaka huu ili kujumlishwa katika Mradi wa Awamu ya Tatu wa Kusambaza Umeme Vijijini yaani REA-Phase III unaotarajiwa pia kuanza mwezi Julai, mwaka 2016.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kumaliza tatizo la maji katika Jimbo la Busanda katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita?
NAIBU WAZIRI WA TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lolesia Jeremiah Bukwimba, Mbunge wa Jimbo la Busanda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ili kutatua tatizo la maji katika Jimbo la Busanda, Serikali katika Bajeti ya Mwaka 2015/2016, imefanikiwa kupeleka shilingi bilioni 1.144 ambazo zinatumika kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa miradi ya maji katika Vijiji vya Luhuha, Nyakagomba, Chankolongo, Kabugozo, Chikobe, Chigunga, Inyala na Katoro, ambayo inaendelea kutekelezwa. Miradi hii ikikamilika itachangia kwa kiwango kikubwa kutatua tatizo la maji linalowakabili wananchi wa Jimbo la Busanda.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuboresha huduma ya maji katika Jimbo la Busanda na Maeneo mengine nchini kwa kadiri rasilimali fedha zinavyopatikana.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itawapa maeneo ya uchimbaji wachimbaji wadogo wa Kata za Nyarugusu, Nyaruyeye na Kaseme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Lolesia Jeremiah Bukwimba, Mbunge wa Busanda kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2001 Wizara ilitenga eneo lenye ukubwa wa hekta 533.55 kwa ajili ya wachimbaji wadogo katika eneo la Nyarugusu. Pamoja na hatua hiyo, wachimbaji wadogo wameendelea kuomba kumilikishwa maeneo hasa ya Buziba yanayomilikishwa na Kampuni ya Buckreef Gold Ltd, kupitia leseni namba PL 6545/2010. Leseni hii itaisha muda wake tarehe 11 Julai, 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo ya Nyaruyeye na Kaseme pia yana leseni hai ya utafutaji wa madini yenye leseni RL 0007/2012 ya Kampuni ya ARL ambayo pia itaisha muda wake tarehe 20 Septemba, 2017. Kwa sasa Serikali inafanya mazungumzo na kampuni hizo ili kuona uwezekano wa kuachia maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea na utaratibu wa kutenga maeneo kwa ajili ya shughuli za wachimbaji wadogo hapa nchini. Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) wanaendelea kutathmini maeneo mbalimbali ili kuona kama maeneo hayo yana mashapo ya kutosha kwa ajili ya wachimbaji wadogo.
Aidha, Serikali itaendelea kujadiliana na kampuni zinazomiliki leseni za madini kwa wachimbaji hapa nchini kwa ajili ya kuwagawia wachimbaji wa maeneo ya Nyarugusu, Nyaruyeye pamoja na Kaseme.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, katika kutenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo, vigezo vinavyozingatiwa ni pamoja na uwepo wa eneo lililo wazi kwa ajili ya kuwagawia wachimbaji kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya mwaka 2010.
MHE. LOSESIA J. BUKWIMBA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itafanya ukarabati wa gati la Bukondo katika Halmashari ya Wilaya ya Geita?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini ninajibu swali namba 405 na naomba kujibu swali namba 405 la Mheshimiwa Lolesia Jeremiah Bukwimba, Mbunge wa Busanda, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari katika mwaka wa fedha 2016/2017, itafanya tafiti za eneo la gati (Geotechnical Survey na Bathymetric Survey) pamoja na usanifu wa kina (detailed design) kwa kutumia wataalam wa Mamlaka wa Usimamizi wa Bandari.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali imepanga kuanza taratibu za kumilikishwa eneo na Halmashauri ya Wilaya ya Geita kwa ajili ya matumizi ya bandari ikiwemo ujenzi wa Gati la Bukondo. Baada ya kukamilika kwa maandalizi ya ujenzi Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi ya Bandari itatenga fedha za ujenzi wa gati hili katika bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO (K.n.y. MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA) aliuliza:-
Rais wa Awamu ya Nne aliahidi kujenga barabara ya Geita – Bukoli - Kahama kwa kiwango cha lami.
Je, ni lini Serikali itaanza utekelezaji wa ahadi hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lolesia Jeremia Bukwimba, Mbunge wa Busanda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) tayari imeanza maandalizi ya kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya Geita – Bukoli – Kahama yenye urefu wa kilometa 139, kwa kukamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hiyo. Ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara hii utaanza kulingana na upatikanaji wa fedha. Aidha, TANROADS itaendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali ili barabara hii iweze kupitika majira yote ya mwaka
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA aliuliza:-
Ni Sera ya Taifa kuwa na Chuo cha Ufundi katika kila Wilaya:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Chuo cha Ufundi katika Wilaya ya Geita?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Lolesia Bukwimba, Mbunge wa Busanda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeanza maandalizi ya ujenzi wa Chuo cha Ufundi Standi cha Mkoa wa Geita kitakachohudumia Wilaya zote za Mkoa huo pamoja na maeneo mengine ya nchi. Mnamo tarehe 6 Agosti, 2016 nilifanya ziara katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa, moja ya maeneo niliyotembelea ni eneo la Magogo katika Mji wa Geita mahali ambapo chuo hicho kitajengwa. Lengo lilikuwa ni kutoa msukumo wa upatikanaji wa hati miliki ya eneo hilo ili hatua za ujenzi zianze mapema kama ilivyopangwa katika bajeti ya mwaka huu wa 2016/2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo furaha kukuthibitishia kuwa hatimiliki ya kiwanja Namba 177 kitalu E, chenye ukubwa wa hekta 27.27 yaani ekari 68.17 kwa umiliki wa miaka 99 imepatikana. Kazi inayofuata ni kumpata Mshauri Elekezi na Mkandarasi ili ujenzi uweze kuanza mapema iwezekanavyo.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA aliuliza:-
Katika Mkutano wa SADC uliofanyika Nchini Swaziland pamoja na mambo mengine suala zima la kupambana na Ugonjwa wa Kifua Kikuu na Silicosis lilijadiliwa. Ugonjwa huo unaathiri sana watu wanaojihusisha na shughuli za uchimbaji wa madini na wale wanaoishi kandokando na maeneo ya uchimbaji:-
(a) Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi wanachama wa SADC; je, inalifahamu tatizo hilo?
(b) Je, Serikali ina mkakati gani wa makusudi wa kupambana na Ugonjwa huo wa Kifua Kikuu na Silicosis, hasa katika maeneo yenye shughuli za uchimbaji wa madini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lolesia Jeremiah Bukwimba, Mbunge wa Jimbo la Busanda, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania inafahamu changamoto ya uwepo wa Magonjwa ya Kifua Kikuu na Silicosis katika maeneo ya wachimbaji. Kwa upande wa Kifua Kikuu inakadiriwa kuwa ukubwa wa tatizo hili ni kubwa zaidi ikilinganishwa na hali halisi katika maeneo mengine na kwa upande wa Silicosis kumekuwepo na ripoti za wagonjwa wachache katika hospitali za Serikali ikiwemo Kibong’oto
kuhusu wachimbaji wadogowadogo kutoka maeneo ya migodi. Kupitia ufadhili wa Mfuko wa Dunia wa Kupambana na Magonjwa ya UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria (Global Fund to Fight AIDS, Tuberculosis and Malaria), nchi kumi wanachama wa Jumuiya ya SADC ikiwemo Tanzania zipo katika utekelezaji wa mpango wa kudhibiti kifua kikuu na magonjwa ya mfumo wa hewa yatokanayo na uchimbaji madini ikiwemo Silicosis.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia halmashauri zilizo katika maeneo ya migodi imeanza kuweka mikakati ya kudhibiti magonjwa haya kama vile kutoa elimu kwa wachimbaji ya namna ya kujikinga na vumbi na kutumia njia sahihi za uchimbaji. Vilevile, katika mpango huu wa
Global Fund to Fight HIV AIDS, Malaria and Tuberculosis kuna afua (intervention) itakayoshughulika na Sera za Udhibiti wa Vumbi katika Maeneo ya Wachimbaji (The Dust Control Policy) ambayo itawabana wachimbaji kudhibiti vumbi wakati wa shughuli za uchimbaji. Aidha, Serikali itaongeza wigo wa huduma katika vituo vya afya kwenye maeneo yaliyoathirika ikiwemo Mkoa wa Geita ili vituo viwe na uwezo wa
kuchunguza na kutibu magonjwa hayo na kuwajengea uwezo wataalam wa afya katika kuhudumia wagonjwa katika maeneo ya migodi.
MHE. LOLESIA J. M. BUKWIMBA aliuliza:-
Je, ni lini mradi wa maji wa Chankolongo katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita utakamilika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lolesia Jeremia Maselle Bukwimba, Mbunge wa Busanda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Geita ilianza kutekeleza mradi mpya wa maji wa Chankolongo mwaka 2014/2014 ukiwa ni mojawapo ya miradi ya vijiji 10 kwa kufanya usanifu upya na kusaini mikataba ya ujenzi mwezi Machi, 2014 wenye thamani ya shilingi bilioni 4.39 baada ya mradi wa awali wa Nyakagomba kushindikana hadi kuchakaa kwa miundombinu yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi unalenga kutumia chanzo cha Ziwa victoria na utahudumia vijiji vinne vya Chankolongo, Chikobe, Chigunga na Kabugozo vyenye wakazi wapatao 24,724. Kazi yote ina mikataba sita iliyoandaliwa na kusimamiwa na COWI (T) Consulting Engineers and Planners kwa kushirikiana na Association with Environmental Consult Limited. kama Mtaalam Mshauri. Malipo yaliofanyika hdi ssa ni kiasi cha shilingi bilioni 1.99 ambayo ni sawa na asilimia 45.3 ya gharama ya mradi, ambapo utekelezaji umefikia asilimia 50.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu ulikumbwa na changamoto kutokana na uwezo mdogo wa mkandasi (Fare Tanzania Limited) aliyekuwa akijenga choteo na kusambaza mabomba. Hata hivyo, Halmashauri ya Wilaya ya Geita imesukuma utekelezaji wa mradi huu ambapo mkandarasi (Fare Tanzania Limited) ameingia makubaliano (sub contract) na kampuni nyingine iitwayo Katoma Motor Factors Limited ambayo inaleta mabomba yote ya mradi pamoja na pampu ndani ya mwezi huu wa Julai 2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hali ya sasa mradi huu unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Desemba, 2017.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itawalipa walimu madai yao ya kusimamia mtihani wa kidato cha nne mwaka 2015 na mtihani wa kidato cha pili mwaka 2016?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lolesia Jeremiah Bukwimba, Mbunge wa Busanda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, walimu waliosimamia mtihani wa Taifa wa kidato cha nne mwaka 2015 wanadai jumla ya shilingi bilioni 1.6 na walimu waliosimamia mitihani ya kidato cha pili mwaka 2016 wanadai jumla ya shilingi bilioni 3.2. Hivyo, jumla ya madai kwa mitihani yote miwili ni shilingi bilioni 4.89.
Mheshimiwa Spika, madeni hayo yamewasilishwa Hazina kwa ajili ya uhakiki ili walimu hao wapewe madai yao.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA aliuliza:-
Je, ni lini mradi wa umeme wa REA utaanza kutekelezwa katika Jimbo la Busanda?
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Lolesia Jeremia Bukwimba, Mbunge wa Busanda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa Mradi Kabambe wa Usambazaji Umeme Vijijini Awamu ya Tatu umeanza rasmi nchi nzima tangu mwezi Machi, 2017. Mradi huu unajumuisha vipengele-mradi vya densification, grid extension na off-grid renewable. Mradi huu unalenga kuongeza wigo wa usambazaji umeme katika vijiji vyote vilivyobaki nchi nzima, vitongoji vyote, taasisi zote za umma na sehemu za pembezoni ikiwa ni pamoja na maeneo vya visiwa. Usambazaji wa umeme katika Jimbo la Busanda utafanyika kupitia vipengele-mradi vya densification na grid extension utakaokamilika mwaka 2020/2021.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya kupeleka umeme katika Jimbo la Busanda pamoja na Wilaya yote ya Geita itajumisha ujenzi wa njia ya umeme msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 184.7; ujenzi wa njia ya umeme msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilometa 582 na ufungaji wa transfoma 109. Mradi huu utaunganisha wateja wa awali 8,834. Gharama za mradi huu ni shilingi bilioni 25.6. (Makofi)
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA aliuliza:-
Tatizo la uhaba wa watumishi katika sekta ya afya kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Geita ni kubwa sana.
Je, Serikali ina mkakati gani wa dharura wa kuliondoa tatizo hilo?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu wali la Mheshimiwa Lolesia Jeremiah Bukwimba, Mbunge wa Busanda kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Geita ina mahitaji ya watumishi wa sekta ya afya 465 ambapo waliopo ni 235 na upungufu ni 240. Upungufu huu umetokana na sababu mbalimbali ikiwemo uhamisho, vifo, kustaafu pamoja na zoezi la Kiserikali la kuondoa watumishi hewa na wale waliokuwa na vyeti fake. Hata hivyo, baada ya kukamilisha mazoezi hayo, Serikali imeanza kutoa vibali vya kuajiri kada mbalimbali ikiwemo kada ya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mgao wa watumishi wa nchi nzima mwaka 2017, Halmashauri ya Wilaya ya Geita ilipata jumla ya watumishi 22 kati yao ni madaktari wawili. Watumishi hao wote wameripoti kwenye vitu na wanaendelea na kazi. Aidha, kwa mwaka wa fedha 2018/2019, Halmashauri ya Wilaya ya Geita imetenga katika bajeti na kuomba kibali cha kuajiri watumishi 121 katika sekta ya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuhamasisha Halmashauri kutenga bajeti kwa ajili ya kuajiri wataalam zaidi ili kutatua changamoto ya uchache wa watumishi katika wilaya hiyo.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA aliuliza:-
Ni Sera ya Taifa kuwawezesha Wavuvi ili wafanye shughuli zao kwa tija:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwawezesha Wavuvi katika Ukanda wa Ziwa Victoria?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lolesia Jeremiah Bukwimba, Mbunge wa Busanda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ili kuwawezesha wavuvi hususan kununua vifaa kwa bei nafuu, Serikali imeondoa kodi ya ongezeko la thamani yaani VAT kwa engine za kupachika, nyuzi za kushonea nyavu, vifungashio na nyavu zenyewe. Pia kulingana na chapisho la Afrika Mashariki kuhusu ushuru wa pamoja la mwaka 2007 - 2012, engine za uvuvi, malighafi zinazotumika kutengeneza zana mbalimbali za uvuvi na viambata vyake vinavyonunuliwa katika Soko la Afrika Mashariki hupewa punguzo la kodi ama kufutiwa kodi kabisa.
Mheshimiwa Spika, hatua hii itasaidia kupungua kwa bei za zana za uvuvi ambapo wavuvi wataweza kunufaika na mpango huo hatimaye kumudu kununua zana za uvuvi.
Mheshimiwa Spika, Serikali pia imeanzisha Benki ya Kilimo ambayo inatoa fursa kwa wavuvi kupata mikopo kwa ajili ya kununua zana za uvuvi. Aidha, Serikali inaendelea kuwahamasisha wavuvi kujiunga kwenye Mifuko ya huduma za kijamii ikiwemo Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, kama vile NSSF ambapo Mfuko wa NSSF umeanzisha utaratibu unaojulikana kama Wavuvi Scheme ili kuwawezesha wavuvi kupata huduma za kijamii zinazotolewa na mfuko huu kama vile huduma za afya pamoja na kupewa malipo ya uzeeni.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na operesheni ya kudhibiti uvuvi haramu na biashara ya haramu ya mazao ya samaki inayokwenda kwa jina la Operesheni Sangara. Operesheni hii inalenga katika kuhakikisha rasilimali za uvuvi zinalindwa ili ziweze kuwasaidia wananchi na Taifa kwa ujumla katika kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja na kuongeza Pato la Taifa. Pia inalenga katika kutunza rasilimali na mazingira kwa ajili ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA aliuliza:-
Lengo la Serikali ni kuhakikisha kila kijiji kinapata umeme wa REA; je, ni lini sasa vijiji vyote vya Jimbo la Busanda vitapata umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Lolesia Jeremiah Bukwimba, Mbunge wa Busanda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Busanda lina jumla ya Kata 22 na vijiji 83 ambapo kati ya hivyo 14 vimepatiwa nishati ya umeme; vijiji nane vitapata umeme kupitia mradi wa REA awamu ya tatu mzunguko wa kwanza ambapo vijiji vya Bugogo, Ntono, Ihega, Butobela na Ngula ni miongoni wa vijiji vitakavyonufaika na mradi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkandarasi wa Kampuni ya White City International Contractors Electrical Power Engineering Co. Ltd ameshaanza utekelezaji wa kazi za mradi na kazi hiyo itakamilika mwezi Juni, 2019.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya kupeleka umeme katika Jimbo la Busanda, itajumuisha ujenzi wa kilometa 21.44 za njia ya umeme wa msongo kilovoti 33 na kilometa 26 za njia ya umeme wa msongo 0.4 kilovoti, ufungaji wa transfoma 14 na uunganishaji wa wateja wa awali 404. Gharama za mradi ni shilingi bilioni 1.56.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, vijiji vitano vya Buyagu, Nyalwanzaja, Kamena, Nderema na Imalampaka vitapata umeme kupitia mradi wa ujenzi wa njia ya msongo wa 220KV wa Bulyanhulu – Geita ambapo Mkandarasi anatarajiwa kufika site mwezi Mei, 2018. vijiji 56 vilivyobaki vitapata umeme kupitia mradi wa REA Awamu ya Tatu, mzunguko wa pili unaotegemewa kuanza mwezi Julai, 2019 na kukamilika mwezi Juni, 2021. Ahsante. (Makofi)
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itajenga barabara ya Geita – Bukoli – Kahama kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lolesia Jeremia Bukwimba, Mbunge wa Busanda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Geita – Bukoli - Kahama yenye urefu wa kilometa 120 ni barabara ya mkoa inayohudumiwa na Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS). Mpango wa kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami umeanza ambapo kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina imekamilika tangu mwaka wa fedha 2014/2015.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu kupitia TANROADS imepanga kutekeleza ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami katika sehemu kuu mbili. Sehemu ya kwanza (Lot.1) ni Geita – Nyarugusu – Bulyanhulu Junction (km 58.3) na sehemu ya pili (Lot.2) ni Bulyanhulu Junction – Kahama (Km 61.7). Utekelezaji wa ujenzi utaanza mara fedha zitakapopatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Serikali inaendelea kutafuta fedha, TANROADS itaendelea kuimarisha barabara hii kwa kuifanyia matengenezo ya aina mbalimbali ili iweze kupitika majira yote ya mwaka. (Makofi)
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBAaliuliza:-
Je ni lini Serikali itapeleka gari la wagonjwa kwenye Kituo cha Afya Bukoli?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lolesia Bukwimba, Mbunge wa Busanda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Geita ina gari saba zinazotoa huduma kwa wagonjwa (ambulance). Gari tano zinatoa huduma katika Vituo vya Afya vya Katoro, Nzera na Chikobe ambavyo vimeanza kutoa huduma za upasuaji. Gari mbili zinatoa huduma katika vituo vya afya vinavyobaki kikiwemo Bukoli ambacho kipo katika ukarabati ili kukiwezesha kutoa huduma za upasuaji. Halmashauri inashauriwa kuweka kipaumbele na kutenga bajeti kwa ajili ya ununuzi wa gari za wagonjwa kulingana na mahitaji.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji wa Katoro- Buseresere unaokusudia kutoa maji Ziwa Victoria?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lolesia Jeremia Bukwimba, Mbunge wa Jimbo la Busanda, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Tano inaendelea kutekeleza miradi ya maji ambayo lengo lake ni kufikisha huduma ya maji kwa asilimia 95 ya wakazi wa mijini na asilimia 85 ya wakazi wa vijijini hadi ifikapo mwaka 2020. Malengo hayo yanahusu pia maeneo ya Katoro na Buseresere.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeanza maandalizi ya utekelezaji wa mradi wa Majisafi kutoka Ziwa Victoria kwenda Miji ya Katoro na Buseresere ambapo hadi hivi sasa mazungumzo ya awali kati ya Serikali kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) na wafadhili kutoka Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB) yamefanyika. EIB wameonesha nia ya kufanya mradi wa maji kwa ajili ya miji hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, andiko ya mradi wa maji kwa ajili ya miji ya Katoro na Buseresere limeshawasilishwa Wizara ya Fedha na Mipango ili maombi yaweze kuwasilishwa rasmi EIB.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Gati katika Kijiji cha Bukondo Halmashauri ya Wilaya ya Geita?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Lolesia Jeremiah Bukwimba, Mbunge wa Busanda, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania ina mpango wa kufanya upembuzi yakinifu kwenye Maziwa yote Makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa ili kutambua maeneo yanayofaa kujenga magati. Zabuni kwa ajili ya kumpata mtaalam mwelekezi wa kufanya kazi ya upembuzi yakinifu ilitangazwa na kupata kampuni ya RINA kutoka nchini Italia mwezi Desemba, 2018 kwa ajili ya kufanya kazi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kumpata mshauri mwelekezi huyo kumekuwa na mazungumzo ya maridhiano ya bei ya kufanya kazi ambayo yalikamilika mwezi Desemba, 2019. Kazi ya Upembuzi Yakinifu inatarajiwa kuanza mwezi Februari, 2020 na kukamilika ndani ya miezi
18. Hivyo, ujenzi wa gati katika eneo la Bukondo utategemea mapendekezo ya taarifa ya mshauri mwelekezi.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA aliuliza:-

Katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita kuna upungufu mkubwa wa watumishi wa sekta ya afya:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lolesia Jeremiah Bukwimba, Mbunge wa Busanda, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2016/2017 hadi 2018/2019, Serikali imeajiri watumishi 8,444 wa sekta ya afya nchini ambapo watumishi 45 walipangwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita. Katika mwaka wa fedha 2019/2020, Ofisi ya Rais, TAMISEMI imepata kibali cha kuajiri watumishi 550 wa sekta ya afya na taratibu zinakamilishwa ili waweze kupangwa kwenye vituo vya kutolea huduma kote nchini ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Geita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuajiri watumishi wa kada mbalimbali za afya kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE (K.n.y. MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA) aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itapeleka umeme wa REA III katika Kata za Bujula, Nyamalimbe, Kamena, Nyalwanzaka, Nyakamwaga, Busanda Kaseme, Magenge, Butindwe na Nyaruyeye?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la mhesimiwa Lolesia Jeremiah Bukwimba, Mbunge wa Busanda, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inapeleka umeme katika Jimbo la Busanda kupitia Mradi wa REA III Mzunguko wa Kwanza ambapo Kata ya Nyaruyeye itapatiwa umeme kupitia Mkandarasi Kampuni ya JV White City International Contractors. Na kazi ya kupeleka umeme katika Kata ya Nyaruyeye itakamilika mwishoni mwa Mwezi Mei, 2019 ambayo ni wiki hii.

Mheshimiwa Spika, katika Kata nyingine za Nyalwanzaja, Kamena, Busanda na Nyakamwaga zitapata umeme kupitia utekelezaji wa mradi wa kusambaza umeme katika vijiji vinavyopitiwa na mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa Gridi ya Taifa ya Msongo wa Kilovoti 220 kutoka Bulyanhulu hadi Geita. Hadi mwezi Mei, 2019 mkandarasi amekamilisha kazi za kufanya survey na kazi za ujenzi wa mradi zinatarajiwa kuanza mwezi Julai, 2019 na kukamilika mwezi Januari, 2021. Katika Kata zilizobaki za Magenge, Nyamalimbe, Bujula na Kaseme zitapatiwa umeme kupitia Mradi wa REA III Mzunguko wa Pili unaotarajiwa kuanza Mwezi Julai, 2019.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itapandisha hadhi barabara ya Katoro – Busanda – Nyakamwaga – Nyubululo – Kamena - Nyamalimbe – Mwingiro kuwa barabara ya Mkoa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano napenda kujibu swali la Mheshimiwa Lolensia Jeremiah Bukwimba, Mbunge wa Busanda, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kufuatia kuanzishwa kwa Wakala wa Barabara, Vijijini na Mijini (TARURA) barabara ya wilaya ikiwemo barabara ya Katoro Busanda – Nyakamwanga – Nyabululo – Kamena – Nyanalimbe – Mwingiro kilometa 68 zinahudumiwa na TARURA iliyoanzishwa mahususi kwa ajili hiyo. Hivyo zoezi la upandishwaji hadhi barabara kutoka barabara za Wilaya kuwa barabara za Mikoa ikiwemo kukasimu (designation) limesimamishwa kwa muda na Serikali kwa nchi nzima ili kuipatia TARURA fursa ya kutekeleza jukumu hilo mahususi la kuanzishwa kwake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia maelekezo hayo, namshauri Mheshimiwa Mbunge ashirikiane na Ofisi ya Rais TAMISEMI na TARURA katika kusimamia mipango yao kuhusu barabara hii. Hata hivyo, taratibu za kuomba kupandishwa hadhi barabara imeainishwa kwenye Kanuni Na. 43 na 44 za mwaka 2009 za Sheria ya Barabara Na. 13 ya Mwaka 2007 ambapo Bodi ya Mkoa ya Barabara (Regional Roads Board) huwasilisha maombi kwa Waziri anayehusika na barabara iwapo barabara tajwa itakuwa imekidhi vigezo vya kupandishwa hadhi.