Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Lolesia Jeremia Maselle Bukwimba (28 total)

MHE. LOLESIA J. M. BUKWIMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Kwanza nianze kwa kutoa shukrani kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa sababu utekelezaji utaanza mara moja mwaka huu Julai, 2016. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kuna hizi huduma za jamii, shule za sekondari, zahanati, vituo vya afya ambavyo pia ni muhimu kuweza kupatiwa umeme. Napenda kujua sasa, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba pia vituo vya afya pamoja na zahanati na shule za sekondari zinapatiwa umeme huu? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, katika Bunge lililopita, la Kumi, Serikali iliahidi kwamba ingehakikisha vile vijiji vyote ambavyo vinapitiwa na nguzo za umeme juu, zinapatiwa umeme, lakini mpaka sasa hakuna hatua zozote zinazoendelea kuhakikisha wanapatiwa umeme. Katika Jimbo la Busanda pia kuna vijiji ambavyo vimepitiwa na nguzo juu lakini hazina umeme. Napenda kujua:-
Je, Serikali ina mpango gani sasa kuhakikisha kwamba vijiji hivi ambavyo vikiwemo Kijiji cha Buziba, Bunekezi na Naruyeye vinapatiwa umeme ili wananchi waweze kunufaika na huduma ya umeme? (Makofi)
NAIBU WAZIRI NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa kuna maeneo mengi ya ustawi kwa jamii ambayo pia yangepewa kipaumbele cha umeme kwenye mpango huu.
Niseme tu kwamba kwenye awamu ya kwanza na awamu ya pili ya (REA-Phase I na REA-Phase II), maeneo mengi sana ya Shule za Sekondari pamoja na hospitali yamepitishwa umeme. Hata hivyo kwenye REA-Phase III inayoanza mwezi Julai, naomba tu niungane na Mheshimiwa Bukwimba kwamba kama kuna shule za sekondari pamoja na vituo vya afya ambavyo havimo kwenye mpango huo na havikufanyiwa kazi kwenye awamu ya pili, naomba tufuatane naye baada ya Bunge lako ili tukabainishe maeneo hayo. Ahsante sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba sasa nijibu swali la pili la Mheshimiwa Lolesia Bukwimba, kuhusu vijiji vilivyopitiwa na nyaya za umeme lakini hazina umeme. Namhakikishiae Mheshimiwa Lolesia Bukwimba kwamba kwenye awamu inayokuja awamu REA-Phase III, kuna underground REA-Phase III. Maeneo ambayo yalipitiwa na nguzo za umeme lakini hayakupata umeme na yamo kwenye mpango wa umeme, yamekadiriwa kwenye nguzo za umeme under REA- Phase III, under REA Line, ambao pia ambapo itahusisha Vijiji vya Buziba, Bunekezi na maeneo ya jirani.
Mheshimiwa Spika, pia namwomba Mheshimiwa Bukwimba, kwa sababu tumeshirikiana naye sana kwenye masuala ya umeme kwenye Mkoa wa Geita, kama kuna vijiji vingine ambavyo havimo kwenye mpango huu, kadhalika baada ya Bunge hili, nionane naye ikiwezekana tukae sisi wawili tu, tujifungie, kuainisha maeneo hayo. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Kicheko)
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nianze kwa kuishukuru Serikali kwa kupeleka hizo fedha kwa ajili ya kukamilisha miradi. Hata hivyo, wananchi wa Busanda wangependa kujua kwamba ni lini sasa miradi hii itakamilika, maana imekuwa ni miradi ya muda mrefu sana na utekelezaji wa miradi hii ya Benki ya Dunia imekuwa ni ya muda mrefu sana?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa, Jimbo la Busanda linagusa Ziwa Viktoria katika maeneo ya Bukondo na sehemu zingine, ningependa kujua sasa mkakati wa Serikali, ni lini mtahakikisha wananchi wanapata maji ya uhakika kwa kuvuta maji kutoka Ziwa Viktoria?
NAIBU WAZIRI WA TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, kwa suala la lini naomba nizungumze wazi, bahati nzuri tumeshapeleka fedha nilivyozungumza pale awali, shilingi bilioni 1.144. na hili naomba nimuagize Mkurugenzi wa Halmashauri husika kuhakikisha katika Mwaka huu wa Fedha, kwa sababu fedha zimeshafika hakuna sababu ya wananchi kuendelea kupata shida.
Hili Mheshimiwa Mbunge naomba nikwambie, nadhani tulikuwa pamoja katika kuzindua mradi mkubwa wa maji pale Geita. Katika hili nasema kwamba, tutarudi tena kule Geita kuangalia tatizo hili la maji, kama pesa zimefika nitashangaa sana kuwaona Wataalam wetu wanashindwa kuzitumia fedha hizi vizuri ili wananchi wapate huduma ya maji.
Mheshimiwa Spika, lakini ajenda ya pili, ni kwa nini sasa tusitumie suala la Ziwa Viktoria, nadhani siku ile ya Mkutano Mkubwa tulisema wazi kwamba wale wananchi wote wanaopakana na Ziwa Victoria, Serikali katika awamu ya pili itaangalia ni jinsi gani ya kufanya badala ya wakati mwingine kuchimba bore hole, twende sasa kutumia hii rasilimali adimu tuliyokuwanayo ya Maziwa yetu.
Mheshimiwa Lolesia nikwambie kwamba, Serikali katika huu mpango wa maji wa awamu ya pili ambao ulianza Januari iliyopita, tunajipanga kuhakikisha kuwa tutafanya matumizi mazuri ya Ziwa Victoria, siyo Busanda peke yake bali vijiji vyote na maeneo yote yanayozunguka Ziwa Viktoria, wakiwepo ndugu zangu wa Magu ambao mwezi uliopita nilikuwa kule.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona.
Katika Hospitali yetu ya Wilaya ya Geita ambayo imepandishwa hadhi kuwa hospitali ya Mkoa kuna msongamano mkubwa sana wa watu kiasi kwamba kwa kweli changamoto ni kubwa sana. Ningependa hasa kujua kwa sababu tunatakiwa tujengewe Hospitali mpya ya Rufaa ya Mkoa.
Ni lini sasa Serikali itaanza ujenzi rasmi katika hospitali ya Mkoa ambayo itakuwa ni Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, suala la ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Mheshimiwa Bukwimba tulikuwa na Mheshimiwa Makamu wa Rais tulifungua hospitali ile ya Geita, kweli kuna msongamano mkubwa, na pale ni kipaumbele, nadhani mchakato wa Serikali tutafanya mambo haya kwa haraka kuangalia bajeti ya mwaka wa fedha unaokuja, tuweke mipango ya pamoja ya Kiwilaya na Kimkoa na mwisho wa siku tujenge hospitali yetu ya rufaa ya Mkoa wa Geita.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Kama ilivyo Mji Mdogo wa Namanyere, katika Wilaya ya Geita kuna Mji Mdogo wa Katoro ambao una hadhi na umetimiza vigezo vyote. Napenda kujua sasa ni lini Mamlaka ya Mji Mdogo huu wa Katoro utapandishwa kuwa Mamlaka ya Mji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kweli Mji wa Katoro unakua sana hasa katika eneo lile la Mkoa wa Geita. Kutokana na suala la Sekta ya Madini, hali ya miji imekuwa ikikua kwa kasi sana ukiwemo na mji wa Katoro. Kwa hiyo, nipendekeze tu kwa sababu katika database yangu hapa nikiangalia Mji wa Katoro siuoni, kwa hiyo Mheshimiwa Lolesia, kama walishaleta Ofisi ya Rais, TAMISEMI nitakwenda ku-cross check, lakini kama bado hawajaanza huo mchakato, naomba nielekeze sasa jinsi gani tutafanya katika eneo la Halmashauri yao, wahakikishe kwamba wanaanza mchakato wa kawaida kwanza katika Vijiji, katika u-DC, Baraza la Madiwani na baadaye RCC, yale maombi yaje Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tutayatathmini, mwisho wa siku ni kwamba, eneo hili litapandishwa kwa vigezo vitakavyokuwa vimefikiwa.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Ni kweli kwamba Serikali imeweza kujibu kwamba itawapa maeneo wachimbaji wadogo katika maeneo hayo, lakini imekuwa ni ahadi ya muda mrefu sana hasa katika eneo la Nyarugusu maeneo ya STAMICO, kila wakati Serikali imekuwa ikiahidi kwamba itawapatia maeneo na wananchi wanahitaji kujua kwamba ni lini sasa Serikali itawapatia maeneo haya ya wachimbaji wadogo hasa maeneo ya Nyarugusu? (Makofi)
Swali la pili, mwaka 2015 Serikali ilizindua mradi mkubwa sana wa wachimbaji wadogo pale Rwamgasa na tuliuzindua mradi huu kwa vigelele na shangwe, lakini sasa hakuna kinachoendelea mpaka sasa. Ni mradi wa World Bank! Napenda kujua, ni lini sasa mradi huu utaanza rasmi ili wachimbaji wadogo waweze kunufaika?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa Serikali imekuwa ikikusudia kuwatengea maeneo wananchi, hasa wa eneo la Mheshimiwa Bukwimba. Kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Bukwimba, amekuwa akifuatilia sana maeneo ya wachimbaji wadogo katika eneo lake.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimkumbushe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, mwaka 2015 kwa juhudi zake ambazo aliomba wananchi wachimbiwe maeneo, walitengewa maeneo 95, eneo la Rwanyamgaza. Kadhalika, maeneo ya Kaseme, walitengewa maeneo 43.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba tu Mheshimiwa Bukwimba awahamasishe wananchi, kwa sababu kati ya maeneo 95 aliyotengewa, ni maeneo 25 tu kule Rwanyamgaza yanafanya kazi; na kati ya maeneo 43 kule Kaseme ni maeneo 17. Hata hivyo Mheshimiwa Bukwimba kwa juhudi zako bado tunakutengea maeneo mengine ambayo yanaachiwa wazi na wananchi hasa eneo la Buziba. Buckreef itaachia hekta 200, lakini bado Kampuni ya ARL itaachia hekta 100; bado Kampuni ya Bismak itaachia hekta 120, lakini na Ernest Masawe ataachia hekta 90, hiyo ni kwa ajili ya wananchi wako Mheshimiwa Bukwimba. Kwa hiyo, bado tunakutengea maeneo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini sasa? Mwezi wa Kumi tunaanza kutenga maeneo rasmi. Hii ni kwa nchi nzima ikiwemo eneo la Igunga kule Iborogero, maeneo ya Kibao kwa Mfipa, maeneo ya kule Mkuranga kwa ajili ya Waziwazi lakini na maeneo mengine ya Busiri, pamoja na Londani Sambalu kule Singida kwa Waheshimiwa Wabunge. Kwa hiyo, bado tunaendelea kutenga maeneo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala lake la pili ni kwamba Kituo cha Kuchenjua Madini kwa ajili ya wachimbaji wadogo, kimechukua muda mrefu. Mheshimiwa Bukwimba nakupongeza sana, tuna kituo kimoja tu cha mfano cha kuchenjua madini hapa nchini na ndiyo kituo cha Rwamgasa ambao Mheshimiwa Bukwimba, mwaka 2015 na mwaka 2014 ulihangaika sana. Mheshimiwa Bukwimba nakupongeza sana, utakuwa ni Mbunge wa mfano kwa sababu ndiyo eneo tunalofungua Kituo cha Kuchenjua cha Mfano hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini kinakamilika sasa? Leo tumefungua tenda kwa ajili ya kumpata mjenzi na kazi ya kujenga itaanza mwezi Septemba mwaka huu na mradi ule utakamilika mwezi Mei mwakani. Gharama yake ni hela nyingi kidogo, ni Dola 800,000, tutazitenga ili kituo hiki kianze kufanya kazi. Pia nawapongeze mgodi wa GGM nao wanachangia Dola 200,000. Kwa hiyo, kituo hiki kitaanza kufanya kazi lakini mantiki ya kituo hiki kitasaidia sana wachimbaji wadogo kujua thamani sasa ya dhahabu wanayochimba hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawahamasisha wananchi wote ambako madini yanachimbwa sasa wote tupeleke kwenye eneo hili la Rwamgasa ambacho Mheshimiwa Bukwimba amekifungua ili wananchi wetu sasa wanufaike na rasilimali yetu ya dhahabu.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuuliza swali la nyongeza. Tatizo la barabara hasa katika Halmashauri zetu ni kubwa sana ikiwemo hata Halmashauri ya Wilaya ya Geita na wananchi wanashindwa kwenda sehemu mbalimbali, wanashindwa kusafirisha mazao yao kwa sababu tatizo la barabara ni kubwa sana. Napenda kupata kauli ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba mnasemaje sasa kuhusu kupeleka fedha hizi ili barabara ziweze kutengenezwa kwa wakati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema awali, nakiri wazi kwamba barabara nyingi sana ziko katika hali mbaya na nakiri wazi kwamba mvua iliyonyesha sasa hivi, zile barabara ambazo zilikuwa katika hali mbaya, sasa hivi hali imekuwa ni mbaya zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana nimesema pale awali wakati nilipokuwa najibu swali la Mheshimiwa Pudenciana kwamba jukumu letu kubwa ni kujielekeza sisi kama Serikali. Haya makusanyo ambayo sasa hivi yanakusanyika, basi katika bajeti ya fedha ambayo mwaka huu tunaondoka nayo, ziweze kufika Majimboni.
Mheshimiwa Naibu Spika, imani yangu ni kwamba, tunaposukuma fedha hizi, japokuwa ni kipindi kifupi kilichobakia, lakini zitasaidia hasa kukwamua barabara zenye changamoto kubwa. Nakiri wazi kwamba kweli barabara hali yake siyo nzuri na Mheshimiwa Lolesia nakiri kwamba nami nimeshafika kule Jimboni kwake kipindi naenda kuzindua mradi wa maji. Nimetembelea na nimeona barabara zile jinsi gani zilivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naahidi tutashirikiana ilimradi kinachopatikana siyo katika Jimbo lake peke yake isipokuwa katika maeneo mbalimbali ambayo yana changamoto kubwa, kama nilivyosema jana katika swali la msingi. Tutajitahidi ili hizi fedha ziweze kwenda na miradi iweze kutekelezeka.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mehshimiwa Naibu Spika, asante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Nashukuru kwa jibu la Mheshimiwa Waziri japokuwa majibu aliyonipa inaonesha kwamba ni mipango ya baadaye sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Gati la Bukondo kwa sasa hivi ninavyosema liko katika hali mbaya sana kiasi kwamba watu kuvuka kwenda kupanda meli inabidi waogelee kwanza ndipo waikute meli, kwa hiyo hali ni mbaya sana. Sasa ningependa kujua Mheshimiwa Waziri kwamba ni lini watakwenda kufanya ukarabati kwa sababu katika swali langu la msingi nimeuliza ukarabati wa hilo gati?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Ziwa Victoria katika Halmashauri ya Ziwa Victoria pamoja na Chato tunategemea sana usafiri wa majini hasa kwa MV Chato ambayo inatoka Chato - Bukundo kwenda mpaka Nkome. Na Nkome pia gati lake liko katika hali mbaya sana, ningependa kujua nini mkakati wa Serikali kuhakikisha ya kwamba inakarabati magati yote hayo ili wananchi waweze kupata usafiri wa kutosha?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Lolesia Jeremiah Bukwimba kwa namna anavyofuatilia maendeleo ya wananchi wake wa Bukwimba na wa Geita kwa ujumla. Amefika ofisini Dar es salaam na amefika vilevile Dodoma kumfuata Waziri wangu. Tumejadiliana hilo kwa kirefu na tulimuahidi kwamba tutawasiliana na wataalam wanaohusika na masuala haya ya gati ili hatimaye tuweke msukumo ili hili hitaji lake liweze kutekelezwa na wananchi wapate huduma wanayokusudia.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naomba kurudia kile ambacho Waziri wangu alimuahidi, na mimi nilikuepo wakati anaahidiwa, na sisemi asije tena, aendelee kufuatilia, najua mambo mengi sana anafuatilia. Naomba uendelee kufuatilia, lakini kwa hili suburi tutakapokamilisha yale mawasiliano kati yetu na taasisi zinazohusika ili upate majibu sahihi na sisi tutafanya msukumo unaohitajika ili hatimaye kile kinachokusudiwa katika swali lako kiweze kukamilika.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niulize maswali mawili ya nyongeza.
Kwanza kabisa nianze kumshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake, hata hivyo napenda kusema kwa mfano wananchi wa Nyarugusu ni kipindi kirefu sana ni ahadi Awamu ya Nne ya Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete aliahidi wananchi hawa waweze kupewa eneo hili na harakati mbalimbali, viongozi wengi wamekuja katika eneo hilo kuahidi lakini hakuna kilichofanyika kwa hiyo wananchi wote wa Nyarugusu wanahitaji kusikia kwamba ni lini sasa wataweza kupewa eneo hilo la STAMICO?
Swali la pili, wananchi wa Geita wanategemea sana shughuli za uchimbaji ndio maana Wanyamatagata pamoja na Sami na maeneo mengine kama vile Mkaseme maeneo ya Magenge wananchi wanahitaji kupewa maeneo ya uchimbaji, ningependa kujua sasa nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba wananchi hao wanapewa maeneo ya uchimbaji? (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, na ndugu zangu wa Nyarugusu, nadhani unataka tutoe jibu la ukweli kabisa na hili ndiyo litakuwa la ukweli.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba hilo eneo ambalo Mheshimiwa Mbunge analiongelea ni leseni kati ya STAMICO na kampuni ambayo kuna Watanzania na Wacanada, kilichotokea ni kwamba kuna mgogoro mkubwa kweli na Mheshimiwa Naibu Waziri nilivyomuagiza aende kule alivyotoa tamko tu, lile tamko likasambazwa dunia nzima.
Kwa hiyo, naomba wananchi wafahamu kwamba eneo hilo halitatolewa mpaka hiyo kesi iishe. Watanzania tuwe makini sana, tumesaini mikataba na makampuni na mkataba mkubwa ni ule MDA (Mineral Develepment Agreement), tukicheza na hiyo kesi na Wabunge kama wanataka tuandikishiane na Wabunge kwamba Serikali ikishtakiwa Wabunge husika watabeba gharama za hiyo kesi kwenye mahakama za nje ya Tanzania. Kesi bado ipo, wananchi wavute subira mpaka hiyo kesi ikamilike kuhusu huo mgodi wa Nyarugusu na huo ndiyo ukweli. Kwa hiyo, ahadi zitatolewa, ahadi zisitolewe tena hapa mpaka hiyo kesi iishe.
Mheshimiwa Naibu Spika, wachimbaji wadogo sasa wa Geita na sehemu zingine, ni kwamba tunatoa maeneo kwa wachimbaji wadogo, na hivi juzi nilikuwa naenda kutoa ruzuku ya awamu ya tatu, lakini tumegundua kwamba ruzuku awamu ya pili waliochukua fedha kwa kupitia TIB hawakuchukua fedha walipewa vifaa, vile vifaa vingine havipo huko kwenye migodi.
Kwa hiyo, kabla hatujatoa ruzuku ya awamu ya tatu imesimamishwa mpaka tufanye tathmini ya awamu ya pili na awamu ya kwanza, hapo ndipo tutaenda kutoa ruzuku ya awamu ya tatu. Lakini wachimbaji wadogo Serikali ina dhamira kubwa kwelikweli ya kuwaendeleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania tuheshimu sheria, na ninawaomba Wabunge, tuna Sheria ya Madini ya mwaka 2010 inatambua utoaji wa leseni na MDAs hizo. Sasa Wabunge wenyewe hatuwezi kushabikia kuvunja sheria ambazo tuliziweka. Ahsante. (Makofi)
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nianze kushukuru kwa ajili ya majibu, vilevile maandalizi ya ujenzi wa hiki Chuo cha VETA, Mkoa wa Geita ni wa muda mrefu, ni tangu awamu iliyopita, lakini mpaka sasa ujenzi haujaanza. Ningependa kujua Mheshimiwa Waziri amesema utaanza hivi mapema, ni lini? Je, ni katika mpango wa mwaka huu wa 2016/2017?
Swali la pili, kwa kuwa tunaelekea kwenye viwanda, Awamu ya Tano ni awamu ya viwanda na vijana wetu hasa katika Mkoa wa Geita na Wilaya ya Geita hawana ujuzi kabisa, Serikali inasemaje kuanzisha program maalum kupitia SIDO, kwamba vijana wetu sasa waanze kuelimishwa ili viwanda vikianza waweze kuajiriwa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kumshukuru kwa shukrani alizotupa. Pili, nikubaliane naye kwamba mchakato huu umeanza muda mrefu, hata hivyo tunapozungumzia kuanza kwa ujenzi, nina maana ni hatua zote zinazohusika ili kuwezesha ujenzi huu. Kama ambavyo tumekuwa tukizungumza hapo awali, chuo hiki kinategemewa kujenga kwa fedha za mkopo kutoka ADB, kwa hiyo, kuna taratibu ambazo lazima zifuatwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza la muhimu ilikuwa ni kupata hati na kiwanja ambacho kiko mahali pazuri ambapo wanachuo wengi watapenda kwenda hapa na pia itakuwa rahisi kufikika kazi hiyo imekamilika, sasa hivi tunaendelea na hatua za kumpata mshauri elekezi, tunaamini hatua hizi hazitakuwa na utata mkubwa kwa sababu ziko wazi na zinakwenda kwa taratibu zilizopo tukishakamilisha ndipo tukakapoanza ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili kuhusiana na tatizo la upungufu wa wataalam hasa katika azma ya kwenda uchumi wa viwanda. Ni kweli kabisa vijana wetu wengi wanamaliza darasa la saba, form four na vyuo, wanahitaji ujuzi. Kupitia ziara hiyo niliweza kutembelea maeneo mbalimbali vikiwemo Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi ambavyo navyo vinaonekana kuwa na mchango mkubwa katika kutoa mafunzo haya ya ufundi. Wizara tumeshajipanga kuona kwamba vyuo hivyo vinakarabatiwa na kuongezewa vifaa ili vijana wengi zaidi waweze kunufaika.
MHE. LOLESIA J. M. BUKWIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuweza kuuliza swali la nyongeza. Kulingana na majibu ya Mheshimiwa Waziri ni kwamba, hivi karibuni tutapata mikopo kutoka Benki ya Dunia na sehemu mbalimbali kwa ajili ya kuwezesha kuwa na unafuu, niseme tu kwamba, Benki hii ya TADB kwanza iko kwenye Kanda, kwa mfano katika Kanda ya Ziwa iko Mwanza. Wakulima kwenda mpaka Mwanza kufuatilia mkopo huu kwa kweli inakuwa ni tabu na wanatumia gharama kubwa.
Je, Serikali haioni sasa ni wakati iweze kuhakikisha Benki hii inafika mpaka vijijini au kwenye Makao Makuu ya Wilaya ili kuwawezesha wananchi wengi kufaidika?
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda tu niseme kwamba Serikali inaona umuhimu wa kupeleka huduma za benki hii kutoka kwenye Kanda mpaka katika ngazi za chini zaidi na ndiyo dhamira ya Serikali, lakini ni vema twende taratibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya kwanza ambayo inafanywa na Serikali sasa hivi ni kuiongezea mtaji benki hiyo, kazi ya pili ambayo sikuisema mwanzo ni kuimarisha Management ya TADB yenyewe ili iweze kufanya kazi hiyo, yote mawili yakifanyika kwa pamoja hakika tutahakikisha kwamba benki hiyo inajitanua mpaka katika ngazi husika kuwafikia wananchi.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Katika majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri amekiri kabisa kwamba tatizo hili la Kifua Kikuu ni kubwa sana na hasa
katika maeneo ya wachimbaji wa madini ikiwemo Geita. Ningependa kujua sasa kwamba Serikali ni lini itaweza kufanya utafiti wa kina hasa katika maeneo ya wachimbaji ili kubaini ukubwa wa tatizo hili katika maeneo haya na hatimaye kuweza kupatiwa ufumbuzi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa
nchini Tanzania tatizo hili la kifua kikuu ni kubwa sana, katika takwimu za dunia inaonesha kwamba mwaka 2015 watu 160,000 waliweza kupata tatizo hili la kifua kikuu. Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuwa na sera pamoja na mikakati ili kuweza kupambana kutokomeza ugonjwa huu wa kifua kikuu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza kwamba ni lini Serikali itafanya utafiti kwenye maeneo haya, naomba nimuahidi tu kwamba, Serikali itaendelea kutekeleza mikakati hii kama ambavyo imeweka
mpango wake wa bajeti wa kila mwaka na tutakapopata pesa mahususi kwa ajili ya tafiti mbalimbali, tutahakikisha tunatoa kipaumbele kwenye eneo hili la maeneo ya migodi kwenye magonjwa haya ya kifua kikuu pamoja na magonjwa ya silicosis.
Mheshimiwa Naibu Spika, sina tarehe mahususi
kwamba ni lini tunaweza tukafanya hivyo lakini dhamira yetu ni njema na kwamba tutakapopata pesa basi tutazielekeza kwenye tafiti kwenye maeneo haya ya migodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili kwamba kwa nini Serikali isilete sera kwa ajili ya Kifua Kikuu; naomba nimjulishe tu kwamba sera tunayo na infact mapitio ya sera yanatuelekeza sasa hivi ndani ya Serikali kutekeleza miradi
ya Kifua Kikuu, uchunguzi pamoja (case detection) mpaka kwenye ngazi ya jamii, kwenye ngazi ya kaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ufuatiliaji wa kesi mbalimbali za kifua kikuu kwa sera hii tuliyonayo sasa unafanyika mpaka kwenye ngazi ya community kwa maana ya kwamba tunakwenda mpaka kwenye kaya, kwenye household. Kwa hiyo sera tunayo na tunaendelea kuitekeleza na kwa kiasi kikubwa katika miaka ya karibuni maambukizi ya kifua kikuu yameendelea kupungua.

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nimesimama kutoa msisitizo kwa swali la Mheshimia Lolesia Bukwimba, ni kweli tuna wagonjwa takribani 160,000 wa kifua kikuu nchini lakini changamoto yetu kubwa ni kuwafikia wagonjwa wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeweza kuwafikia
wagonjwa takribani 62,000 tu, kwa hiyo nitoe wito kwa Waheshimiwa Wabunge, tunapokwenda katika majimbo yetu tuwahamasishe wananchi kupima kifua kikuu, takribani wananchi 100,000 tunao katika majumba yetu, katika kaya zetu, katika shule zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo kubwa ambalo
tumelifanya, kila mama mjamzito na mtoto mwenye umri wa chini ya miaka mitano anayekwenda hospitali sasa hivi atapimwa kifua kikuu na watu ambao pia wana maambukizi
wa VVU. Kwa hiyo, nawaomba sana kifua kikuu kiwe ni agenda yenu ya kila siku mnapokuwa katika majimbo yenu. Mtu ambaye hajapata matibabu ana uwezo wa kuambukiza mpaka watu 20 kwa mwaka mmoja, tusipochukua hatua Kifua Kikuu kitakuwa ndicho kinachoongoza kuua kuliko Malaria au HIV/AIDS.
Mheshimiwa Naibu Spika, niliona nisimame ili
kuwahamasisha Waheshimiwa Wabunge kushiriki katika mapambano ya kifua kikuu.
MHE. LOLESIA J. M. BUKWIMBA: Ahsante sana Mheshimiwa Naibu kwa kunipa nafasi niuliza maswali mawili ya nyongeza. Kutokana na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri ni kweli kwamba changamoto bado ni kubwa sana katika Mradi huu wa Chankolongo. Pia kutokana na majibu yake na yeye mwenyewe amewahi kufika kwenye huo mradi, mradi huu ni wa muda mrefu sana kiasi kwamba wananchi mpaka sasa hawaelewi kinachoendelea juu ya mradi huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ningependa pia Mheshimiwa Waziri awahakikishie wananchi kwamba, je, ni kweli mwezi Desemba mwaka 2017 mradi huu utakamilika kutokana na changamoto zilizopo?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa mradi huu unakusudia kuvuta maji kutoka Ziwa Victoria na ndani ya Jimbo la Busanda wananchi wana tatizo kubwa sana la maji na maji mengi yanayotumika kwa ajili ya uchenjuaji wa dhahabu ni machafu na wananchi wanapenda kupata maji safai na salama; je, mradi huu utawezesha kufikisha maji na katika Jimbo zima la Busanda?Napenda kupata majibu hayo. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli mimi na yeye Mbunge tulikwenda jimboni kwake ili kuukagua mradi huu na ni kweli mradi huu tumeukuta una changamoto nyingi sana na ndiyo maana kwa hatua tulizozifanya pale na kutoa maelekezo nilipofika site mpaka Engineer pale pamoja na Afisa Manunuzi amesimamishwa majukumu kutokana na mradi huu, kwa hiyo hatukulala kwenye mradi huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, miezi michache iliyopita tulitoa maagizo kwamba choteo liweze kukamilika na mabomba yaweze kupatika. Kwa taarifa nilizozipata juzi ni kwamba lile choteo limekamilika maji yanatoka katika ziwa mpaka yanafika pale katika intake yenyewe, lakini usambaji wa mabomba umekuwa ukisua sua. Ndiyo maana Halmashauri ilivyosukuma, huyu sasa ameingia na hii kampuni nyingine ya Katoma Motor Factors Limited ambayo imefanya commitment ya kuleta mabomba yote bila hata ya kulipwa hata senti tano. Kwa hiyo mabomba yatafikishwa site ndani ya mwezi huu wa saba.
Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa nilizozipata ni kwamba tayari mabomba haya yapo ndani ya meli na kwamba muda wowote yatafika hapa site. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge naomba nikuhakikishie kwamba kwa jinsi nilivyoongea na watendaji katika Halmashauri ya Geita ni kwamba tutasukuma ndani ya mwezi wa 12 mradi huu uweze kukamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu agenda ya pili, kwamba mradi huu ikiwezekana ufike kwenye maeneo mengine; wazo ni jema lakini naona kwanza jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba mradi huu unaweza kukamilika katika vile vijiji vya awali. Jambo hili likishakamilika hapa tutaweka mipango mingine ya namna ya kufanya; kwa sababu chanzo hiki ni kikubwa sana ili kiweze kusaidia wananchi wa Busanda waweze kupata maji kama Mbunge wao anavyohangaika siku zote.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa jibu la Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini napenda tu kujua, maana sasa wamesimamia kwa muda mrefu tangu mwaka 2015/2016 ni muda mrefu sasa.
Je, ni lini sasa uhakiki huu utaweza kukamilika ili walimu waweze kulipwa madai yao? (Makofi)
Swali la pili, katika madai hayo, walimu tu Wilaya yetu ya Geita wanadai zaidi ya shilingi milioni 120, napenda pia kujua ni lini walimu hawa wanaotoka Wilaya yangu ya Geita wataweza kulipwa madai yao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, katika level mbalimbali, mchakato huu wa uhakiki wa deni umeshakamilika. Kwa hiyo, nadhani Hazina sasa hivi wanajipanga, wakati wowote deni hili litaweza kulipwa ili mradi kila mtu haki iweze kupatikana.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo najua Mheshimiwa Bukwimba ni mpiganaji mkubwa sana wa watumishi wake katika jimbo lake, lakini siyo jimbo lake peke yake isipokuwa katika maeneo mbalimbali. Katika eneo la Jimbo lako kwamba lini watalipwa mgao huu wa deni hili ambalo Hazina wanalishughulikia, likilipwa lote litalipwa kwa pamoja.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba tuvute subira kwa sababu Hazina ndiyo walikuwa wanafanya uhakiki wa madeni mbalimbali siyo wa walimu ni mchakato wa kulipa madeni mbalimbali. Jambo hili litakamilika na wananchi wa Busanda kule katika jimbo lako Geita wananchi wa eneo lile watapata hasa hasa watumishi wa Serikali ambao ni walimu watapata madai yao kama ilivyokusudiwa.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kumshukuru Mheshimwia Naibu Waziri kwa majibu mazuri lakini ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa kwa muda mrefu sana kuna baadhi ya sehemu kwa mfano ndani ya Jimbo la Busanda wana umeme, lakini katika Taasisi za Serikali na za Umma hazijaweza kufikiwa na umeme huo. Nikitoa mfano, Kituo cha Afya Bukoli, Kituo cha Afya Lwamgasa, Shule ya Sekondari ya Bukoli, Shule ya Sekondari Lwamgasa, Shule ya Sekondari Chigunga na kwenye Zahanati ya Chigunga umeme huu haujafika.
Je, Serikali inasemaje sasa kuhusu mpango wa kuhakikisha kwamba Taasisi zote za Umma pamoja na sehemu za kuabudia zinafikiwa na umeme wakati utekelezaji unapoendelea? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tumeona katika vyombo vya habari katika mikoa mbalimbali umeme ukizinduliwa ili Awamu ya Tatu ya REA iweze kuanza kufanya kazi lakini katika Mkoa wa Geita sijaona jambo hili likifanyika. (Makofi)
Je, ni lini sasa Serikali itazindua rasmi umeme wa REA Awamu ya Tatu katika Mkoa wa Geita ili wananchi waweza kuanza kuona utekelezaji wake? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nianze kumpa pole sana Mheshimiwa Bukwimba kwa wananchi wake wanne walioangukiwa na kifusi kwenye machimbo ya kule Nyamalimbe, pole sana Mheshimiwa Bukwimba kwa niaba ya wananchi wa Geita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyouliza Mheshimiwa Bukwimba, nianze kwanza kumpongeza anavyouatilia maendeleo ya umeme kwa wananchi wa Jimbo la Busanda. Hata hivyo, mradi kabambe wa REA Awamu ya Tatu, kama nilivyoeleza kwenye jibu langu la msingi unalenga kupeleka umeme katika vijiji vyote vilivyobaki lakini katika vitongoji vyote vilivyobaki na taasisi za umma. Nisisitize katika hili, Taasisi za Umma ninamaanisha vituo vya afya, shule, misikiti, masoko na kadhalika, haya yote yatafikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Bukwimba, vijiji vyake vya Nyaluyeya ambavyo vituo vya afya havina umeme sasa vitawekewa umeme. Kule Nyamalimbe vituo vya afya pamoja na shule vitawekewa umeme. Shule za Bukoli, shule za Kamena, Kaseme pamoja na vituo vya kwa Mheshimiwa Musukuma, kisiwa chake cha Izumachele tutaenda mpaka huko.
Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa wa Busanda kwamba vitongoji vyote ambavyo vina zahanati tutawekea zahanati umeme pamoja na shule. Umeme mwingine mbadala, kwenye taasisi za umma tutawawekea pia umeme wa solar. Hii ni kwa sababu ikitokea kuna hitilafu ya umeme basi umeme wa solar uweze kufanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, ni lini sasa tunazindua, nitumie nafasi hii kusema kwamba ni kweli tumezindua mikoa kumi tu nchi nzima, tunaendelea kuzindua mikoa yote 15 iliyobaki ya Tanzania Bara, mkoa mmoja hadi mwingine na mahali pengine ikilazimika tutazindua kila wilaya ili wananchi waweze kujua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumueleza Mheshimiwa Lolesia Bukwimba kuanzia mwezi wa saba tutaanza uzinduzi, kwa hiyo, mwezi wa saba Mheshimiwa Bukwimba tufuatane ili tukazindue umeme wa REA Awamu ya Tatu katika Jimbo lako.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kutokana na jibu la Mheshimiwa Naibu Waziri inaonesha kabisa kuna upungufu mkubwa wa watumishi 240. Katika mwaka 2017 wameajiri watu 22 vilevile mwaka ujao wanapanga kuajiri watu 121, hii inaonesha ni mkakati wa kawaida tu na kwa sababu hiyo hawajaweza kukidhi kile ambacho mimi nilikuwa nahitaji kujua. Mimi ninachotaka kujua, ni lini sasa Serikali itakuwa na mkakati wa dharura wa kuhakikisha kwamba Halmashauri ya Wilaya ya Geita inapata watumishi wa kutosha ili waweze kuwapatia wananchi huduma inayostahiki? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, katika Halmshauri ya Wilaya ya Geita hasa katika Jimbo la Busanda kuna baadhi ya vituo vya afya ambavyo kwa kweli vina upungufu mkubwa sana hasa katika Kituo cha Afya Katoro ambapo kuna idadi kubwa ya watu vilevile kituo hicho kinahudumia pia na Kata zingine jirani kama Rwamgasa, Busanda pamoja na Kasemye. Kitu hiki kina upungufu mkubwa sana wa wataalam kiasi kwamba inasababisha hata wakati mwingine watu kupoteza maisha yao. Ni lini sasa Serikali itahakikisha inapeleka watumishi kwa dharura katika kituo hiki cha afya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza anauliza mkakati wa dharura, ni ukweli usiopingika kama tulivyokiri kwenye jibu letu kwamba upo upungufu mkubwa sana na namna pekee ni kuweza kuajiri na suala la kuajiri ni pamoja na bajeti inaporuhusu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi tukubaliane kwamba kwa kuanzia na hao ambao tumewataja 121 si haba na kwa sababu katika majibu yangu kwenye swali la msingi nimemueleza sababu zilizosababisha upungufu huu mkubwa, siyo rahisi kwamba kwa mara moja tutaweza kuziba pengo hili kwa sababu suala lenyewe lina budget implication.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiopingika kwamba Katoro pale idadi ya watu ni kubwa na iko haja ya kuhakikisha kwamba pamoja na hospitali iliyopo vijengwe na vituo vingine vya afya ili kuweza kuongeza maeneo ya afya kuweza kutibiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe kwa kupitia Halmashauri yake wana uwezo wa kuweza kufanya allocation ndani kutazama maeneo yapi ambayo staff wako wengi ili ndani kwa ndani kwanza kupunguza wakati wanasubiri ajira kutoka Serikali kuu. (Makofi)
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwanza nitoe shukrani kwa kupeleka madaktari wanane kwa awamu, watano halafu watatu. Hata hivyo, kuna tetesi kwamba kuna daktari mmoja atahamishwa hivi karibuni. Napenda kujua kama ni kweli na kama siyo kweli basi nipate ufafanuzi kutoka kwa Mheshimiwa Waziri kwamba kama wakimhamisha yule watatuletea tena lini daktari mwingine? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa changamoto katika Hospitali ya Wilaya ya Bukombe ni sawa kabisa na changomoto iliyoko katika Halmshauri ya Wilaya ya Geita, tuna upungufu mkubwa sana wa madaktari pamoja na wauguzi. Je, Serikali inasemaje kuhakikisha kwamba Serikali inaleta watumishi wa afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, suala la kwamba kuna tetesi za kuhamishwa hivi karibuni kwa daktari mwingine labda kwa sababu anajua ambayo Waheshimiwa Wabunge wengi hawajui na labda pengine kwa sababu ya kuweka sawa niweke vizuri kwamba hata ule uhamisho wa mwanzo tulioufanya ulikuwa ni kwa sababu kulikuwa kuna shida ya kutafuta madaraka hali iliyopelekea daktari mmoja aliyekuwa anakaimu nafasi ile akashambuliwa mtaani ambapo ilionekana kama ni kutokana na mazingira hayo. Ndiyo maana tukafanya ule uhamisho na baadaye tukapeleka madaktari wengine. Kwa hiyo, kama ni tetesi zenye dhana ile ile na pengine hatua hizi zitakuwa zina sababu ile ile atahama, lakini haina maana kwamba hatutapeleka daktari mwingine kuziba nafasi hiyo.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ameuliza kuhusu upungufu wa madaktari kwa maeneo yote sasa siyo tu Bukombe na Geita, lakini pia najua tuna upungufu wa madaktari na wauguzi katika maeneo mengi. Mheshimiwa Rais ametoa kibali cha ajira za watumishi wengine 15,000 ambao wataziba nafasi ya hawa watumishi hewa waliokuwa na vyeti fake ambao wameondolewa. Kibali hicho kinaendelea na katika kibali hicho pia tuna idadi kubwa tu ya wataalam wa afya ambao watakuja kwa ajili ya ku-replace lakini tuna ajira zingine 54,000 ambazo ni za mwaka huu wa fedha ambazo na zenyewe tunaamini katika kufanya hivyo tutaziba eneo kubwa sana la upungufu siyo tu wa idara hii ya afya lakini pia na idara nyingine kwa ujumla wake.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri na jinsi ambavyo Serikali imejipanga kuwawezesha wavuvi. Vilevile wapo wavuvi ambao hawana uwezo kabisa, wanahitaji kuwezeshwa na Serikali. Ningependa kujua sasa nini mkakati wa Serikali wa kuwapatia ruzuku wavuvi hawa ili waweze kujikwamua kiuchumi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; wavuvi walioko katika Mkoa wa Geita hasa katika Jimbo la Busanda katika maeneo ya Bukondo, Nyakasamwa pamoja na Nungwe wanazo changamoto nyingi. Ningependa kujua Mheshimiwa Waziri ni lini atakuja kututembelea katika Jimbo la Busanda ili kubaini changamoto hizi na kuweza kuzitafutia ufumbuzi wa kutosha? Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza linahusu ruzuku kwa wavuvi. Wizara inayo program maalum ya kuwawezesha wavuvi ambao wapo katika utaratibu wa vikundi ambapo tunatoa mashine za ruzuku, wao wenyewe wavuvi wanachangia asilimia 60 na Wizara tunachangia asilimia 40.
Mheshimiwa Spika, hivyo, shime Mheshimiwa Mbunge aende akawahamasishe wavuvi wake waweze kuwa katika vikundi, wapitishie barua zao za maombi kwa Halmashauri ya Wilaya kwa maana ya Mkurugenzi na hatimaye azilete Wizarani, tunamhakikishia Mbunge kumsaidia kuweza kupata mashine hizo kwa ajili ya vikundi vyake.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mheshimiwa Lolesia Bukwimba, bibi yangu huyu anaomba niende kuwatembelea babu zangu kule Busanda. Nataka nimhakikishie kwamba baada ya Bunge hili mimi na yeye mguu kwa mguu mpaka Busanda kuhakikisha nakwenda kukutana na wavuvi wa kule Busanda. Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa, tatizo la upungufu wa Walimu katika Shule za Msingi Magu ni sawa kabisa na katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita. Je, Serikali inasemaje sasa kuweza kuhakikisha kwamba, suala hili linafanyiwa kazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu katika majibu yaliyopita, ni kwamba chini ya usimamizi wa Mheshimiwa Rais wetu tunafanya jitihada za kutosha kuhakikisha kwamba tunapunguza kabisa tatizo la upungufu wa Walimu. Hatuwezi kulipunguza kwa siku moja au kwa mwaka mmoja kwa sababu mahitaji ni makubwa sana kulingana na payroll ya Serikali, lakini tunajitahidi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano tunataka tuondokane na upungufu wa Walimu wa sayansi, hadi mwaka 2020/2021 tuwe hatuna upungufu wa Walimu wa sayansi. Kwa upande wa shule za msingi tunataka tupambane kuhakikisha kwamba ndani ya miaka michache ijayo tumepunguza kabisa upungufu wa Walimu wa shule za msingi katika halmashauri zote, ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Geita.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Menyekiti, kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu. Inaonesha kwamba amefuatilia kweli katika Halmashauri ya Wilaya jinsi ambavyo imefanya kazi imekaa na GGM. Lakini vilevile niishukuru GGM kwa kuanza kutekeleza uwajibikaji wa Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na marekebisho yake ya mwaka 2017 katika kipengele cha 105.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sasa kuna baadhi ya makampuni ya uwekezaji katika sekta ya madini ambayo mpaka sasa hayajaanza kufanya utekelezaji wa sheria hii. Kwa mfano Mgodi ule wa Bacliff pale hawajaanza kufanya utekelezaji. Je, Serikai inasemaje sasa kwa makampuni ambayo hayajaanza kufanya utekelezaji wa sheria hii mpaka sasa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Mgodi wa Bulyanhulu ambao uko Kahama umepakana sana na Halmashauri ya Wilaya ya Geita, hasa katika Jimbo la Busanda katika Kata ya Butobela kule Nyakagwe pamoja na Kata ya Bukoli na wananchi walioko jirani na maeneo haya wananufaika, hasa wale wa Kahama, lakini wale wa upande wa Geita sasa ambao nimewataja wa Nyakagwe na Bukoli ni kilometa mbili tu kutoka kwenye mgodi ule lakini hawanufaiki chochote.
Je, Serikali inasemaje sasa kuhakikisha kwamba wananchi wa Jimbo la Busanda pia, hasa wa maeneo ya Bukoli pamoja na Nyakago wanafaidika na mgodi uliopo Bulyanhulu ambao uko jirani sana na sisi?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza ni kwamba Mgodi wa Bacliff ni kweli kabisa haujatoa CSR Plan yao kutokana na mujibu wa sheria inavyosema. Lakini nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Mgodi ule wa Bacliff mpaka sasa hivi hawajaanza uzalishaji. Kwa hiyo watakapokwenda katika uzalishaji ni lazima watupe CSR Plan yao na CSR Plan yao lazima iwe shirikishi kwa kushirikiana na Halmashauri husika waangalie namna gani wataweza kui- finance miradi mbalimbali ya maendeleo katika Wilaya au Halmamshauri hiyo.
Kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba asiwe na wasiwasi, mradi huu wa Bacliff utakapoanza kufanya kazi basi lazima sisi kama Wizara tutahakikisha kwamba wamekuja na CSR Plan yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile kwa kampuni yoyote, nipende kutoa wito kwa makampuni yoyote ya uwekezaji, makampuni yote ambayo yanawekeza katika sekta ya madini ni lazima yatii sheria na taratibu zilizowekwa. Sheria ya mwaka 2017 na Kanuni zake za mwaka 2018 zinahitaji kila kampuni ilete CSR Plan yao kuhakikisha kwamba wanashirikiana na jamii au Halmshauri husika katika kuratibu na kuhakikisha kuwa wanatoa fedha katika kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo katika halmashauri husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kanuni za mwaka 2018 zinasema kuna masuala ya local content plan pamoja na kile kiapo cha uaminifu. Ni lazima kila kampuni ikamilishe yale mambo ambayo yameainishwa katika kanuni za mwaka 2018, bila kufanya hivyo sisi kama Wizara hatutasita kuchukua hatua katika kampuni zinazohusika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, kuhusiana na wale watu ambao wamepakana na Wilaya ya Kahama na hasa ambao wapo karibu na Mgodi wa Bulyankulu, sisi tunafuata sheria. Sheria ndiyo zinazosema kwamba halmashauri husika iweze kufaidika kwa maana ya kupata service levy. Lakini vilevile nitoe tu wito kwa Mgodi wa Bulyankulu, kama inawezekana kata ambazo ziko karibu na mgodi huo basi waweze kuwasaidia wananchi wa maeneo hayo kwa kuwapa ajira kupitia ile kanuni yetu sisi ya local content kwa maana ya kuwajali Watanzania wanaoishi karibu na maeneo yale kwa kuwapa ajira lakini vilevile kuwapa fursa ya kuweza kuuza bidhaa na kuuza huduma mbalimbali katika mgodi huo. Ahsante.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Waziri amezungumza vizuri sana kuhusiana na habari ya kupeleka umeme katika Jimbo Busanda, lakini vijiji hivi ambavyo amevitaja bado hatujamwona mkandarasi, hajafika. Napenda kujua ni lini sasa mkandarasi ataanza rasmi kufanya kazi katika vijiji hivyo vya Ntono na Bugogo ambavyo amevitaja katika jibu la msingi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, sera ya nchi ni kwamba mahali popote ambapo nguzo zinapita na nyaya juu, lazima wananchi waweze kupata umeme. Kwenye Jimbo la Busanda kuna vijiji ambavyo vimepitiwa na nguzo; kwa mfano, Nyaruyeye pamoja na vijiji vingine sehemu za Busaka vimepitiwa na nguzo juu lakini havina umeme. Ndiyo maana nilimfuata Mheshimiwa Waziri ofisini nikapeleka vijiji 30 vya nyongeza kwa ajili ya kupatiwa umeme, lakini hapa sijavisikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujua sasa Wizara inasemaje kuhusu kuvipatia umeme vijiji 30 ambavyo nimeongea na Mheshimiwa Waziri?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Mheshimiwa Bukwimba kwa kufuatilia masuala ya umeme katika Jimbo lake akiwa Mbunge mwanamke wa Jimbo pia. Ameulizia ni lini mkandarasi ataripoti katika Jimbo lake?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nirejee kama nilivyosema awali, tutakutana nao wakandarasi tena kwamba maelekezo ni yale yale, mkandarasi asikae sehemu moja. Kwa hiyo, pengine kama yuko katika maeneo mengine, tumesema wawe na magenge na kila Wilaya wakandarasi kazi ionekane imeanza kwa sababu hakuna kikwazo tena.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, nataka nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kutokana na changamoto iliyokuwepo ya uwepo wa vijiji ambavyo vimepitiwa na miundombinu ya umeme na umeme hakuna, imekuja densification ya awamu ya pili ambapo Geita ni Mkoa mmojawapo katika densification ya awamu ya pili pamoja na mikoa mingine, jumla 11.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba la hilo, vijiji vyake 30 tumeviwasilisha REA kwa ajili ya mchakato na ninamthibitishia vitakuwepo katika hiyo orodha kama ambavyo amefuatilia Mheshimiwa Mbunge. Nakushukuru.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu, japokuwa niseme tu kwamba barabara hii imekuwa kwenye mpango kwa muda mrefu sana. Kulingana na majibu yake ni kwamba upembuzi yakinifu umekamilika tangu 2014/2015, ni muda mrefu sasa inakaribia miaka minne. Barabara hii inaunganisha Mkoa wa Geita na Mkoa wa Shinyanga na ni muhimu kiuchumi. Mimi na wananchi tungependa kujua ni lini fedha itapatikana ili utekelezaji uanze mara moja? Hilo ni swali langu la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2015, Mheshimiwa Rais akiwa pale Katoro aliweza kuahidi kilomita 10 za lami; kilometa 5 Katoro na kilometa 5 Buseresere lakini mpaka sasa hakuna chochote kinachoendelea. Je, ni lini sasa utekelekezaji huu utaweza kuanza? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA):
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Lolesia Bukwimba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba uniruhusu nimpongeze sana dada yangu Mheshimiwa Lolesia Bukwimba kwa sababu amekuwa akifuatilia sana juu ya maendeleo katika Jimbo lake. Niseme tu kwamba barabara hii tumezungumza naye sana nje ya Bunge lakini naona pia anavyoshirikiana na pia na Wabunge wengine kwa sababu barabara hii inagusa maeneo mengi na kama alivyosema inaunganisha Mkoa wa Shinyanga na Mkoa wa Geita. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mpango wa kuitengeneza barabara hii na niseme kweli imekuwa ni muda mrefu tangu usanifu ukamilike na kwa kuwa Serikali inaendelea kutafuta fedha, nimjulishe tu Mheshimiwa Lolesia Bukwimba juhudi zake zimesababisha angalau kwa kuanza katika mwaka wa fedha 2018/2019, Bunge lako limetenga shilingi bilioni 13 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hii. Wakati tunatafuta fedha za kutosha lakini juhudi zimeshaanza kwa kuweza kupata hizi fedha ambazo Bunge limepitisha ili kuanza kuitengeneza hii barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie tu Mheshimiwa Lolesia Bukwimba pamoja na wananchi wa Jimbo la Kahama Mjini, Jimbo la jirani yangu pale Mheshimiwa Maige kule Msalala pamoja na Jimbo lake la Busanda pamoja na Geita na wananchi wote wa Nyarugusu, Bukoli, Bulyankulu, Itobo, Busoka na Kahama Mjini kwamba ujenzi sasa unaanza na tunaendelea kusukuma ili tuweze kupata fedha za kutosha kujenga barabara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ahadi ambayo ilitolewa na Mheshimiwa Rais katika Mji wa Katoro na Buseresere, Serikali inatambua kilometa kumi ziko kwenye ahadi, kilomita 5 ziko Katoro na kilomita nyingine 5 ziko Buseresere. Niseme tu kwamba tumefanya uratibu ili kuweza kuzitambua barabara zote ambazo zimeahidiwa na Mheshimiwa Rais nchi nzima. Tumeendelea kuzipanga zile zinashughulikiwa na TARURA na TANROADS na tunaendelea kuhakikisha kwamba kwenye ule mpango mkakati wa Wizara basi barabara zote ambazo Waheshimiwa viongozi wametoa ahadi zinatekelezwa. Kwa hiyo, nimtoe hofu, tunazisimamia kwa nguvu kuhakikisha kwamba ahadi hizi za Mheshimiwa Rais na zilizopita katika awamu nyingine tunaendelea kuzishughulikia ili tuweze kutengeneza barabara hizi. (Makofi)
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza kabisa, takwimu zinaonesha kwamba katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa ikiwemo Geita kuna changamoto kubwa sana ya vifo vya akinamama wakati wa kujifungua; na kwa sababu hiyo wengi inatokana na kwamba wakati wa kujifungua, pale wanaposhindwa kuwapeleka hospitali ya rufaa ya Mkoa inakuwa ni vigumu kwa sababu hakuna usafiri. Kwa hiyo, ni muhimu sana kituo cha afya cha Bukoli kipatiwe kwa kweli gari la wagonjwa. Je, Serikali ina mkakati gani sasa wa kuona umuhimu huo wa kupatiwa gari la wagonjwa katika kituo cha afya cha Bukoli? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vile vile sambamba na gari la wagonjwa kuna upungufu mkubwa sana wa watumishi, hasa katika vituo hivi vya afya ikiwemo cha Bukoli pamoja na kituo cha Katoro, Chikobe, vyote hivyo. Je, Serikali ina mkakati gani sasa wa kuhakikisha kwamba inapunguza tatizo hili?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba nimshukuru sana Naibu Waziri kwa majibu mazuri yale ya awali. Nafahamu changamoto kubwa inayolikabili Jimbo la Busanda hali kadhalika Mkoa mzima wa Geita.
Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ombi lake tunalichukua, pale inapopatikana fursa tutaangalia nini cha kufanya kwa ajili ya kuweza kulishughulikia eneo hilo.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kwa ajili ya kupunguza hili tatizo la vifo vya akinamama na watoto; na hasa tuna kesi kubwa sasa hivi ya akinamama wengi kupata fistula kwa sababu ya kuwapeleka maeneo mbalimbali kwa kuwa referral system inapatikana mbali; ndiyo maana tumejielekeza katika kuimarisha vituo hivi vya afya.
Mheshimiwa Spika, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali yetu imejipanga; na mpango mkakati wa hivi sasa ni kwamba tunatarajia kukamilisha vituo vya afya 350 kwa lengo kubwa la kupunguza tatizo hili. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wote kwamba Serikali itafanya kila liwezekanalo; hata kule sehemu ya Songambele na sehemu ya Mkoka jambo hili lipo katika kipaumbele chetu kuhakikisha wananchi wanapata huduma vizuri.

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Jafo; lakini nimesimama kwa sababu ya hoja ya Mheshimiwa Lolesia Bukwimba, kwamba Geita ni moja ya mikoa yenye idadi kubwa ya vifo vitokanavyo na uzazi. Kwa hiyo nakubaliana, nataka tu kuongeza majibu ya Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI.
Mheshimiwa Spika, sambamba na ujenzi au ukarabati wa vituo vya afya tunajikita pia katika kuboresha huduma ambazo akinamama wajawazito wanapatiwa. Kwa mfano tumeifanya tathmini, wanawake ambao wanakwenda katika vituo vya kutoa huduma za afya hawapimi, hawafanyiwi vipimo muhimu; kwa mfano wingi wa damu, labda mkojo na shinikizo la damu. Hivi leo Mheshimiwa Makamu wa Rais anazindua kampeni ya Kitaifa ya kuhimiza uwajibikaji katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi; na kipaumbele tumeweka Geita, Kigoma, Kagera na mikoa yote ya Kanda ya Ziwa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, suala la kupunguza vifo halitamalizika kwa kujenga majengo tu, pia tunataka kusimamia ubora wa huduma anazopewa mama mjamzito pamoja na vitoto vichanga. Tunasema jiongeze tuwavushe salama.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili nami niulize swali la nyongeza. Kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Geita ina Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katoro ambao una population kubwa sana: Je, Serikali inaonaje sasa hii mamlaka ya mji mdogo iwe mamlaka kamili ya mji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kama nilivyosema, mchakato huu wauanzishe wenyewe watu wa Geita na hususan Busanda; nasi Ofisi ya Rais TAMISEMI tutapokea mapendekezo yao na tutawahisha jambo hili kadri itakavyohitajika kulingana na ukubwa wa bajeti na upatikanaji wa fedha.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Kwanza naipongeza Serikali kwa hatua ambayo imechukua kuweza kuhakikisha kwamba kuna mradi wa maji wa kutoka Ziwa Victoria, Katoro, Buseresere. Wananchi wanahitaji kujua ni lini utekelezaji utaanza rasmi?

Swali la pili; kwa kuwa azma ya Serikali mpaka mwaka 2020 ni kuhakikisha kwamba mijini asilimia 95 ya maji, asilimia 85 vijijini, jambo ambalo nikiangalia hali halisi, kwa mfano katika Mkoa wa Geita Jimbo la Busanda, naona hali iko chini sana. Napenda kujua sasa kwamba nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba tunapata maji kwa asilimia 85 katika Jimbo Busanda na asilimia 95 Mji wa Geita ambapo sisi wananchi wote ni Makao Makuu ya Mkoa wetu wa Geita?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nampongeza sana Mheshimiwa Lolesia kwa kazi nzuri sana ya kuwapigia wananchi wake. Kubwa, tunatambua kabisa maji hayana mbadala. Ndiyo maana sisi kama Wizara ya Maji tumefanya jitihada ya kuwasilisha hili andiko kwa Wizara ya Fedha ili waweze kuwasilisha EIB. Wizara ya Maji itafanya ufatiliaji wa karibu katika kuhakikisha jambo hili linakamilika kwa wananchi wake ili mradi uweze kuanza kwa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha azma ya Mheshimiwa Rais ya kumtua mwanamama ndoo kichwani na kutimiza Ilani ya Chama cha Mapinduzi asilimia 85 ya upatikanaji wa maji vijijini na asilimia 95 ya upatikanaji mijini, tumeshakamilisha miradi zaidi ya mitatu katika Jimbo lake. Moja, Nyakagongo, Luhuha pamoja na Mharamba katika kuhakikisha wananchi wale wanapata maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati uliokuwepo sasa hivi ni katika kuhakikisha tunakamilisha mradi wa zaidi ya shilingi bilioni nne wa Nachankorongo ili mradi ule ukamilike kwa wakati na umeshafikia zaidi ya asilimia 90 upo katika muda tu wa matazamio.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa na la msingi kabisa, sasa hivi tunakamilisha mradi wa Lamugasa na tunajenga mradi wa maji Nkome, Nzela ambao ni wa zaidi ya shilingi bilioni 25 katika kuhakikisha tunatatua tatizo la maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, sisi kama Wizara ya Maji katika miji 25 katika mpango wa kutatua tatizo la maji, Mkoa wa Geita tumeuangalia kwa ukaribu zaidi na tunafanya jitihada kubwa ya kutatua tatizo la maji.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize maswali ya nyongeza:

Mheshimiwa Spika, kwanza niipongeze sana Serikali kwa kupeleka jenereta tena kwa ajili ya kuendeleza huduma katika hospitali ya Mkoa wa Geita, lakini bado kuna changamoto nyingine pia kwamba hospitali ya Mkoa wa Geita pia ina upungufu mkubwa sana wa watumishi. Je, Serikali inasemaje kuhakikisha kwamba watumishi hawa wanapatikana? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kama ilivyo hospitali ya Mkoa wa Geita pia katika vituo vingi vya kutolea huduma kwenye Mkoa wa Geita hakuna nishati ya umeme na hii inasababisha huduma kutolewa lakini pia kupata changamoto hasa kwa akina mama wajawazito wakati wa kujifungua usiku;

Je, Serikali inasemaje kuhakikisha kwamba vituo vya afya vinapatiwa huduma ya umeme maeneo yote katika Mkoa wa Geita? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, ni kweli tunakiri kwamba katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita tuna changamoto ya rasilimali watu, watumishi waliokuwepo pale ni takriban asilimia 50 ya watumishi wote ambao wanahitajika. Serikali imeliona hilo na inaendelea kuongeza watumishi kadri vibali vya ajira vinavyopatikana. Sambamba na hilo, tunaendelea kusomesha wataalam mbalimbali kuhakikisha kwamba zile huduma za kibingwa basi zinapatikana katika Mkoa huu wa Geita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ameulizia kuhusu suala la umeme katiak vituo vyetu vya kutolea huduma za afya. Wizara ya Afya tumekuwa tunafanya kazi kwa karibu sana na Wizara ya Nishati kupitia mpango wa REA na moja ya mkakati katika mradi huu ni kuhakikisha kwamba vituo vyote vya kutolea huduma za afya na shule vinapata umeme. Kwa hiyo nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara ya Afya kushirikiana na Wizara ya Nishati kupitia mradi wa REA itahakikisha kwamba maeneo yote ambayo yanapitiwa na mradi wa REA basi nayo yanapata umeme.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ninayo maswali mawili ya nyongeza. Gati hili la Bukondo siyo kwamba ni jipya, lipo, ila tu limeharibika kiasi kwamba meli zinapotua pale kwenye gati zinashindwa kutua vizuri, wananchi ni lazima wakanyage maji ndio wanaingia kwenye ferry. Kwa hiyo, siyo kwamba gati halipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye bajeti za Serikali kila mwaka huwa naiona inawekwa kwenye lakini utekelezaji tu wa ujenzi sijaona ukifanyika. Napenda kujua sasa, ni lini Serikali itafanya ukarabati wa lile gati kwa sababu tayari lipo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kwa kuwa kuna barabara ambazo huwawezesha wananchi kufika kwenye gati hilo; barabara hizo nazo hazipitiki vizuri hasa katika kipindi hiki cha mvua; napenda kujua hatima ya hizi barabara. Kuna barabara ya kutokea Katoro - Inyara kwenda mpaka Bukondo; pia kuna barabara ya kutoka Nyarugusu kwenda Rwamgasa mpaka Katoro na nyingine ya kutokea Kahama ambayo tayari Serikali imeshaiweka kwenye bajeti ya kuweza kutengenezwa kwa kiwango cha lami; napenda kujua hizo barabara zitatengenezwa lini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, katika majibu yangu ya awali nimeeleza kwamba Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari ina mpango wa kufanya upembuzi yakinifu kwa ajili ya kujenga magati kwenye maziwa yote makuu. Kwa kusema hivyo siyo kwamba hatujui kwamba kuna gati katika eneo hilo. Gati katika eneo hilo lipo na gati hilo mpaka sasa hivi linamilikiwa na Halmashauri pamoja na GGM.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu gati hilo kwamba linatakiwa kupata matengenezo na usimamizi maalum na ndiyo maana kwa ridhaa ya Bunge tulifanya marekebisho ya sheria kwenye Bunge lililopita kuhakikisha sasa kwamba Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari inaweza kumiliki bandari zote ambazo ziko kwenye maziwa makuu na eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba taratibu zinaendelea na upembuzi yakinifu unafanyika, siyo kwa eneo hilo peke yake, ni kwa maeneo yote nchi nzima; maeneo ya bahari pamoja na maziwa makuu. Tutakapokuwa tumekamilisha huo upembuzi yakinifu, basi tutaichukua na bandari hiyo tutairekebisha ili kuiwekea miundombinu stahiki ya kuweza kuirekebisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali lake la pili ameulizia kuhusu ujenzi wa kurekebisha barabara ambazo zinaingia kwenye eneo hilo la gati. Ni kweli katika mvua hizi zinazoendelea kumekuwa na uharibifu mkubwa sana wa miundombinu hasa ya barabara maeneo mbalimbali. Eneo hilo tunalifahamu na limeshatengewa katika zile shilingi bilioni tisa ambazo zimetengwa za dharura na lenyewe litazingatiwa kwa ajili ya kurekebishwa.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza kabisa, nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Rais alipokuja Geita aliweza kunipatia Hospitali ya Wilaya itakayojengwa Kata ya Buseresere.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukrani hizo, naomba niulize swali la nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, naipongeza Serikali kwamba imekusudia kuajiri watumishi 550 lakini kwa kuwa Halmashauri ya Geita tuna upungufu mkubwa sana tungependa kujua ni lini sasa hao watumishi wataletwa ili waweze kuanza kufanya kazi katika Halmashauri ya Geita? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa katika Jimbo la Busanda kuna vituo vya kutolea huduma viwili ambavyo vimekamilika kabisa, vinatakiwa tu kufunguliwa, Buziba pamoja na Magenge. Napenda kupata kauli ya Serikali ni lini sasa watahakikisha vituo hivi vimefunguliwa kwa sababu vimekamilika kabisa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE):

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Lolesia Bukwimba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Serikali, naomba nipokee pongezi ambazo Mheshimiwa Mbunge amezitoa kwa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la kwanza anauliza ni lini watumishi watapelekwa ili kuweza kuziba pengo la upungufu huo mkubwa. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge mchakato uko kwenye hatua za mwisho kabisa kwa sababu katika suala la kuajiri lazima taratibu zote zifuatwe. Namwondoa mashaka muda si mrefu watumishi wataweza kupelekwa huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili anaongelea vituo vyake vya afya viwili ambavyo tayari vimeshakamilika, anachotaka kujua ni lini vituo hivyo vitafunguliwa. Kama azma ya Serikali ilivyo kwamba vituo vile vya afya vinajengwa ili vianze kutoa huduma, sina uhakika kama tayari kama vifaa vyote vilishapelekwa. Kama vifaa vilishapelekwa ni jambo jema kinachotakiwa ni kupeleka watumishi ili vituo hivyo vifunguliwe vianze kutoa huduma. Ndiyo makusudi ya Serikali na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, ni kwamba Serikali imesema kwamba hakuna fidia katika miradi hii ya umeme wa REA. Ningependa kujua sasa kwamba je, Serikali ipo tayari kuwaelimisha wananchi kujua kwamba hakuna fidia kabla miradi ile haijaanza kutekelezeka? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa kuna vijiji vingi sana hapa Tanzania ambavyo vimepitiwa na nguzo juu lakini umeme haujashuka kwenye vijiji vile na katika nchi yetu ya Tanzania pia hata katika Jimbo langu limeshuhudia kuna vijiji mpaka sasa mradi wa umeme ulipita tangu mwaka 2014, nguzo zimepita juu lakini wananchi hawajashushiwa umeme.

Je, Serikali ipo tayari sasa kuangalia vijiji hivyo vyote Tanzania nzima na kuhakikisha kwamba vijiji hivi vinapatiwa umeme vikiwemo vile vya Jimbo la Busanda ambavyo vipo vingi Nyaruyeye na Busaka hawajapata umeme? Niombe Serikali iweze kunijibu. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Lolesia kwa kazi nzuri anayoifanya lakini maswali yake amejielekeza kwenye namna gani Serikali itaelimisha wananchi. Nichukue fursa hii kwanza kuwashukuru Watanzania wote kwa maeneo mbalimbali ambapo miradi hii ya REA inatekelezeka, kwa kweli Serikali, REA,TANESCO hata na Wizara yenyewe ya Nishati haijapata changamoto kubwa ya madai ya fidia.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwanza Watanzania wenyewe wapo tayari, lakini sisi tutaendelea kuelimisha kadiri tutavyopata fursa kwenye ziara mbalimbali za Mikoa na Wilaya ikiwemo kwenye Jimbo lake la Busanda kwamba wananchi kwa kweli kwa kuwa Serikali inalipia gharama zote na wao wanalipia VAT tu shilingi 27,000 na haijawahi kuwa kikwazo, tutaendelea kutekeleza mradi huu na tunawaomba watupe nafasi zaidi na waiunge mkono Serikali yetu ya Awamu ya Tano yenye nia ya kuhakikisha ifikapo mwaka 2021 vijiji vyote 12,268 vinapata umeme.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ameuliza katika vijiji ambavyo vimepitiwa na umeme wa msongo mkubwa lakini havijashushiwa umeme, nikiri kweli tatizo hilo lipo na hivi karibuni Mheshimiwa Waziri wa Nishati alivyofanya ziara katika maeneo mbalimbali ya hapa Dodoma, maeneo ambayo miundombinu ya umeme mkubwa imepita lakini hawajashushiwa, wametoa maelekezo kwa TANESCO kwamba ifikapo Desemba 2019 maeneo yote yaliyopitiwa na miundombinu ya umeme haijashushwa umeme, ishushwe kwa sababu katika maeneo hayo kinachofanyika ni ujenzi wa line ndogo LV na kuweka transfoma na kuwaunganishia wananchi umeme kwa bei ileile ya shilingi 27,000. Kwa hiyo, nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge ikiwemo vijiji alivyota kwenye Jimbo lake la Busanda, Mkoa wa Geita na mikoa mingine yote nchini kwamba tatizo hilo kwa kweli tunaliona na tumeshaliwekea mikakati kama miradi ya Quiq Wins katika kupelekea utekeezaji wa mradi huo. Nakushukuru sana.