Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Dunstan Luka Kitandula (31 total)

MHE. YUSTINA A. RAHHI aliuliza: -

Je, lini Serikali itaanzisha Mfuko wa Fidia kwa wahanga wanaoathirika na wanyamapori wakali na waharibifu?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la kama ulivyonielekeza.

Mheshimiwa Spika, kwa hii ni mara yangu ya kwanza kusimama mbele ya Bunge lako tukufu baada ya Mheshimiwa Rais kunipa heshima hii ya kuniteua kuwa Naibu Waziri, naomba nitumie fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye imempendeza niweze kutumika kwenye nafasi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pili nimshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kunipa heshima hii ya kuitumikia nchi yetu. Naahidi kutekeleza majukumu yangu kwa uwezo wangu wote na kwa vipawa vyote alivyonipa Mwenyezi Mungu, naahidi sitamwangusha.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba ushirikiano wako na Wabunge wenzangu nawaahidi ushirikiano naomba tushirikiane. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikilipa kifuta jasho na kifuta machozi kama mkono wa pole au faraja kwa wananchi wanaopata madhara kutokana na wanyamapori wakali na waharibifu. Malipo hayo yamekuwa yakifanyika kwa mujibu wa Kanuni za Kifuta Jasho na Machozi za mwaka 2011 na kwa kadri ya upatikanaji wa fedha hizo.

Mheshimiwa Spika, kanuni hizo zilianza kutekelezwa mwaka 2012 ambapo katika kipindi cha kuanzia 2012/2013 hadi 2022/2023 jumla ya shilingi bilioni 11.3 zimelipwa kwa wananchi walioathiriwa na wanyamapori wakali na waharibifu. Hata hivyo, suala hili limekuwa ni changamoto kubwa kwa nchi nyingi za Afrika ambapo limesababisha baadhi ya nchi kuondokana na utaratibu wa kulipa kifuta jasho na machozi. Lakini Tanzania imeendelea kuona umuhimu wa kuwafuta jasho na machozi wananchi kwa madhara wanayoyapata kutokana na wanyamapori hao. (Makofi)
MHE. MARIAM N. KISANGI K.n.y. MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaondoa popo waliopo maeneo ya Upanga ili kulinda afya za wakazi wa maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kudhibiti popo katika Jiji la Dar es Salaam kwa kuchukua hatua mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kufanya soroveya (survey) ya kuangalia ukubwa wa tatizo, maeneo yaliyoathirika, mbinu gani ambazo ni rafiki kwa mazingira zitumike kudhibiti na pia kubaini aina ya popo wanaosumbua. Imebainika kuwa kuna aina mbili ya popo wanaosumbua, ambao ni popo wanaokula matunda (hawa wanaotumia miti kama maeneo yao ya makazi) na popo wanaotumia mapango au magofu ya nyumba kama makazi yao.

Mheshimiwa Spika, katika kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo, majaribio ya dawa tano za kunyunyizia yalifanyika ili kufukuza popo katika makazi hayo. Kati ya dawa hizo; dawa mbili (Napthalene na Bat CRP) zimeonekana kuwa na uwezo wa kuwafukuza popo hao. Juhudi zaidi zinaendelea kwa kushirikiana na wadau kwenye maeneo husika.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:-

Je, nini mkakati wa Serikali kuvifanya vivutio vya mapango ya Handebezya na jiwe linalocheza kuwa na tija kwa Taifa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Mkundi, Mbunge wa Ukerewe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali inayolenga kuendeleza, kukuza na kutunza vivutio vya utalii vilivyopo Ukerewe vikiwemo Mapango ya Handebezya na Jiwe linalocheza vinavyopatikana katika Kisiwa cha Ukerewe. Mikakati hiyo ni pamoja na kutangaza vivutio hivyo kwa kutumia vyombo mbalimbali vya habari.

Mheshimiwa Naibu Spika, mathalan, Wizara kupitia TTB iliratibu ziara ya Kituo cha Televisheni cha ITV kwenda kutembelea baadhi ya vivutio vya utalii vilivyopo Ukerewe vikiwemo Mapango ya Handebezya na jiwe linalocheza kwa ajili ya kuandaa documentary ambayo itakapokamilika itaonyeshwa katika kipindi cha ITV cha Chetu ni Chetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, mafunzo yanaendelea kutolewa kuhusu uanzishwaji wa utalii wa utamaduni ambapo hadi sasa kuna vikundi vya utalii wa utamaduni vikiwemo Ukerewe (Ukerewe Cultural Tourism Enterprises) na Nansio (Nansio Cultural Tourism Enterprises).

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Maliasili na Utalii imeendelea kushiriki katika maonesho na matamasha mbalimbali yakiwemo Maonesho ya Biashara ya Afrika Mashariki na Tamasha la Bulabo yanayofanyika katika Kanda ya Ziwa kwa lengo la kutangaza vivutio vya utalii na fursa za uwekezaji zilizopo katika ukanda huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Wizara itaendelea kuhamasisha uwekezaji wa miundombinu inayoelekea katika maeneo yenye vivutio vya utalii, ujenzi wa huduma za malazi zenye hadhi pamoja na kuboresha huduma za kijamii, ikiwemo maji, umeme, huduma za kibenki na mawasiliano.
MHE. MOHAMED JUMAH SOUD aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kupunguza upoteaji wa Uoto wa Asili nchini unaosababisha kupoteza hadhi kwa Hifadhi na Mapori ya Akiba?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Jumah Soud, Mbunge wa Donge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, sababu kubwa ya kupotea kwa uoto wa asili katika Hifadhi na Mapori ya akiba ni ongezeko la mimea vamizi katika maeneo hayo. Mimea hiyo husababisha mabadiliko ya aina ya mimea katika maeneo yaliyohifadhiwa kwa kutoa fursa kwa mimea isiyoliwa na wanyamapori kustawi zaidi, kuongezeka na kupunguza uoto wa asili ambao ni tegemeo la wanyamapori. Hadi sasa, tafiti zimebaini aina 47 za mimea vamizi katika maeneo yaliyohifadhiwa. Sababu zinazopelekea kushamiri kwa mimea vamizi ni pamoja na uingizaji wa mifugo kwenye maeneo yaliyohifadhiwa, mabadiliko ya tabianchi, shughuli za binadamu na viumbepori wahamao.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika jitihada za kudhibiti mimea vamizi, Wizara kupitia Taasisi za uhifadhi inatekeleza mkakati wa kukabiliana na mimea vamizi katika maeneo hayo ikiwa ni pamoja na kuondoa kwa kung’oa mimea husika katika hifadhi. Aidha, mikakati mingine ni kuimarisha ulinzi wa maeneo yaliyohifadhiwa kwa kudhibiti shughuli za kibinadamu ikiwemo kilimo na uingizwaji wa mifugo hifadhini sambamba na kuwekeza zaidi katika utafiti ili kupata suluhisho la kudumu.
MHE. DENNIS L. LONDO aliuliza:-

Je, mchakato wa ujenzi wa geti jipya la kuingilia Hifadhi ya Mikumi kutokea Kilangali na Tindiga umefikia hatua gani?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dennis Londo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha tathmini ya awali kwa ajili ya kujenga lango la kuingilia watalii kupitia maeneo ya Kilangali na Tindiga Wilaya ya Kilosa. Kufuatia tathmini hiyo, gharama za ujenzi wa lango hilo na miundombinu ambata ya lango husika ni jumla ya shilingi bilioni 2.8. Aidha, michoro pamoja na BOQ imekamilika. Hatua inayoendelea kwa sasa ni kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa lango hilo. Kwa ujumla, lango husika litafungua fursa za watalii watakaosafiri na treni ya mwendokasi kutoka Dar es Salaam na Dodoma kuingia Hifadhi ya Taifa ya Mikumi kwa urahisi.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, Serikali kwa kuona umuhimu wa hifadhi hiyo imejipanga kuongeza malango ya kuingilia watalii katika maeneo yote muhimu ambapo kwa sasa kupitia Mradi wa Kukuza Utalii Kusini (REGROW), malango mawili ya kisasa yanajengwa kwa ajili ya kuingilia watalii katika maeneo ya Doma na Kikwaraza (Mji mdogo wa Mikumi). Ujenzi huo umeanza mwezi Agosti, 2023 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Novemba, 2024.
MHE. VENANT D. PROTAS aliuliza:-

Je, lini Serikali itapeleka Askari na kulipa fidia kwa Wananchi waliovamiwa na Tembo kwenye makazi na mashamba yao Jimbo la Igalula?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Venant Daud Protas, Mbunge wa Jimbo la Igalula, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imeweka askari sita wakiwemo askari wa uhifadhi wawili na askari wa vijiji (VGS) wanne katika kituo cha kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu cha Ndala kilichopo katika Wilaya ya Nzega mkoani Tabora. Aidha, askari hao wamepewa vitendea kazi ikiwemo pikipiki mbili na silaha ambavyo vinawawezesha kudhibiti wanyamapori hao popote wanapoonekana ikiwemo Jimbo la Igalula.

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikilipa kifuta jasho na kifuta machozi kwa wananchi wanaopata madhara kutokana na Wanyama pori ambapo kwa upande wa Wilaya ya Uyui ambayo inajumuisha Jimbo la Igalula Wizara imepokea maombi ya wananchi 17 waliopata madhara ya wanyama pori wakali na waharibifu, maombi hayo kwa sasa yanaendelea kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Spika, kupitia Bunge lako tukufu niendelee kutoa rai kwa wakurugenzi wa Halmashauri wa wilaya hususan zenye changamoto za wanyama pori wakali na waharibifu kuharakisha kuwasilisha maombi yanayotokana na madhara ya Wanyama pori hao Wizarani ndani ya siku saba ili kuiwezesha Serikali kufanya malipo ya kifuta jasho na kifuta machozi kwa wakati.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaona umuhimu wa kukitangaza vya kutosha Kivutio cha Maporomoko ya Maji Rusumo ili kuchangia pato la Taifa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oliver Daniel Semuguruka, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Wizara inaendelea kushirikiana na Halmashauri za Wilaya kubaini vivutio mbalimbali vya utalii nchini kwa lengo la kuongeza wigo wa mazao ya utalii, katika kutekeleza hilo mwaka 2021 wataalam wa Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Ngara walibaini vivutio vya utalii na fursa mbalimbali za uwekezaji na shughuli za utalii katika Mkoa wa Kagera.

Mheshimishiwa Spika, miongoni mwa vivutio vilivyobainishwa ni Maporomoko ya Maji ya Mto Rusumo ambayo yanatoa fursa ya uendelezaji wa shughuli za utalii. Hata hivyo, tathmini ya awali iliyofanywa na watalaam wa Wizara imebaini kwamba kiasi kikubwa cha maji ya maporomoko hayo kimechepushwa kwa ajili ya uzalishaji wa umeme na hivyo kupunguza mvuto wa utalii wa maporomoko pekee.

Mheshimishiwa Spika, kwa mujibu wa ushauri wa watalaam, mara baada ya kukamilika kwa mradi wa uzalishaji wa umeme na kukabidhiwa Serikalini, tathmini mpya itafanyika ili kuunganisha utalii wa maporomoko ya maji na utalii wa uzalishaji wa umeme. Endapo tathmini hiyo itaonesha uwezekano wa eneo hilo kutumika kama kivutio cha utalii wa maporomoko ya maji na utalii wa uzalishaji umeme, Serikali itajielekeza kwenye kufanya maboresho ya miundombinu katika maporomoko hayo na kuyatangaza ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuvutia watalii kutembelea katika kivutio hicho.

Mheshimiwa Spika, kupitia Bunge lako tukufu niendelee kuwahamasisha Watanzania wenzangu kuwa na utamaduni wa kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii. Aidha, nitoe wito kwa Mheshimiwa Mbunge, uongozi wa Mkoa na wadau wengine kwa ujumla kuhamasisha uwekezaji wa huduma ikiwemo huduma za malazi na miundombinu mbalimbali katika vivutio vya utalii vilivyopo katika Mkoa wa Kagera.
MHE. EMANNUEL L. SHANGAI aliuliza:-

Je ni sheria ipi inawaruhusu Watumishi wa TANAPA, TAWA na NCAA kutoza mifugo shilingi 100,000 pindi iingiapo hifadhini?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emannuel Lekshon Shangai, Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Taasisi za Uhifadhi za TANAPA, NCAA na TAWA zinaongozwa na Sheria mahususi za kusimamia rasilimali za wanyamapori. Mathalan, Sheria ya TANAPA Sura 282 Kifungu cha 28(1)(a) kama kilivyorekebishwa na Sheria ya Marekebisho Mbalimbali (Na. 11) ya mwaka 2003 ambayo imeongeza kifungu 20A cha Sheria hiyo kwa kuwapa mamlaka watumishi wa TANAPA kutoza faini isiyozidi shilingi 100,000 kwa kila kosa pale mkosaji anapokiri na kukubali kwa maandishi kulipa faini kwa kosa husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kifungu cha 116 cha Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori, Sura ya 283 hutumika katika kutoza faini pindi mifugo inapoingizwa kinyume cha sheria, ndani ya mapori ya akiba. Kifungu hiki kimebainisha utaratibu wa kulipa faini ambapo mkosaji atalipa faini mara baada ya kukubali na kukiri kosa. Aidha, sheria imeelekeza kuwa kiwango cha faini hakitapungua shilingi 200,000 na hakitazidi shilingi 10,000,000. Mkosaji hukiri kosa kwa maandishi na kulipa faini hiyo, na endapo hatakuwa tayari kulipa faini, hufikishwa Mahakamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge na Wananchi kwa ujumla kuwa Serikali itaendelea kuhifadhi na kusimamia rasilimali za wanyamapori kwa kushirikiana na jamii. Hivyo, tunawaomba wote watoe ushirikiano katika kufanikisha jukumu hilo na kuwasihi wazingatie sheria ili kuepusha migongano isiyo ya lazima baina yao na Wahifadhi.
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI aliuliza: -

Je, lini Serikali itafanya mapitio ya viwango vya malipo ya ujira kwa wapagazi, wapishi na waongoza watalii Mlima Kilimanjaro?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu,

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Charles Stephen Kimei, Mbunge wa Vunjo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua changamoto ya viwango vya malipo ya ujira kwa wapagazi, wapishi na waongoza watalii katika Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro. Aidha, katika kutatua changamoto hizo, Wizara kwa kushirikiana na vyama vya mawakala wa utalii yaani waajiri imeanza kutekeleza mikakati mbalimbali kwa ajili ya kufanya maboresho ya viwango hivyo vya malipo ya ujira.

Mheshimiwa Spika, kufuatia hatua hiyo, Wizara imefanya kikao na Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu na kujadili kuhusu viwango vya ujira kwa wapagazi, wapishi na waongoza watalii.

Mheshimiwa Spika, hatua inayofuata ni Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kufanya kikao kazi baina ya wadau hao na waajiri wao kwa lengo la kupendekeza viwango stahiki, ili viweze kuwasilishwa katika Bodi ya Utatu yenye dhamana ya kumshauri Waziri mwenye dhamana ili makubaliano hayo yawe ya kisheria. Kikao hicho kinatarajiwa kufanyika katikati ya Novemba, 2023 kule Arusha.
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH aliuliza:-

Je, kuna mkakati gani wa kupunguza athari hasi zitakazojitokeza kutokana na kuondolewa kwa buffer zone katika hifadhi na mapori?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Soud Mohammed Jumah, Mbunge wa Donge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, maeneo ya kinga za hifadhi za wanyamapori husaidia wanyamapori kupata mahitaji yao ikiwemo malisho na hivyo kupunguza migongano baina ya binadamu na wanyamapori.

Mheshimiwa Spika, katika kupunguza athari za kutokuwa na maeneo ya kinga, Wizara kupitia taasisi zake za uhifadhi (TANAPA, TAWA na NCAA) inatoa elimu kwa wananchi kuhusu kutokuanzisha shughuli za kibinadamu kama vile kilimo na makazi kwenye maeneo ya karibu na hifadhi ili kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na wanyamapori.

Vilevile kuwaelimisha kuanzisha shughuli rafiki kama vile ufugaji nyuki kwenye maeneo hayo. Sambamba na hatua hiyo, jitihada za kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu zinafanyika ili kulinda wananchi na mali zao.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU aliuliza: -

Je, Serikali haioni umuhimu wa kugawa mizinga ya nyuki ili kubadili shughuli za kiuchumi zinazoharibu mazingira kama kukata miti na mkaa Iringa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jesca Jonathani Msambatavangu, Mbunge wa Iringa Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ugawaji wa mizinga na vifaa vingine ni mojawapo ya mikakati ya Serikali katika jitihada za kuwezesha makundi mbalimbali ya kijamii kushiriki katika shughuli za ufugaji wa nyuki hapa nchini. Zoezi la ugawaji wa mizinga lina lengo la kuchochea ufugaji nyuki kwa jamii hasa zile zinazoishi jirani na maeneo yaliyohifadhiwa ili ziweze kujipatia kipato na kuachana na shughuli zinazoharibu mazingira kama kukata miti na kuchoma mkaa.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuimarisha uhifadhi wa maeneo mbalimbali ambapo kupitia Mradi wa REGROW imetoa elimu ya Ufugaji nyuki kwa jamii ya Tungamalenga na kwa mwaka wa fedha 2023/2024 imepanga kuwagawia mizinga 50 kwa kikundi cha Subira kilichopo Wilaya ya Iringa. Vilevile elimu ya ufugaji nyuki imeendelea kutolewa kwa jamii zinazozunguka hifadhi ambapo kupitia elimu hiyo wananchi wamefundishwa namna bora ya kufanya shughuli za ufugaji nyuki kwa tija.

Mheshimiwa Spika, mathalan kwa mwaka wa fedha 2022/2023, Wizara ilitoa mizinga 269 yenye thamani ya shilingi milioni 26.9 kwa vikundi 19 vya wafugaji wa nyuki katika Wilaya za Iringa, Kilolo na Mufindi. Vilevile Mfuko wa Misitu Tanzania umetoa ruzuku ya shilingi millioni 20 kwa vikundi viwili vya ufugaji Nyuki vilivyopo Wilaya ya Iringa. Pia, wadau wa maendeleo wametoa mizinga 260 kwa wafugaji nyuki katika Mkoa wa Iringa.

Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na sekta binafsi pamoja na wadau wa maendeleo, itaendelea kutoa elimu ya uhifadhi na mbinu bora za ufugaji nyuki ili jamii iweze kufuga nyuki kibiashara. Aidha, Mfuko wa Misitu Tanzania umekuwa ukitoa tangazo na kupokea maombi ya ruzuku zitolewazo kwa wadau wa misitu na ufugaji wa nyuki. Hivyo, Mfuko unaendelea kupokea maombi ambayo yanachakatwa ili waombaji waweze kunufaika na ruzuku hizo ikiwemo kupatiwa mizinga ya kufugia nyuki.
MHE. ERIC J. SHIGONGO aliuliza: -

Je, lini Serikali itawamegea eneo Wananchi wa Visiwa vya Maisome katika Hifadhi ya Kisiwa cha Maisome?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mhehimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Eric James Shigongo, Mbunge wa Buchosa, kama ifuatavyo: -

Mhehimiwa Mwenyekiti, katika kutatua changamoto ya mwingiliano wa shughuli za uhifadhi na zile za kibinadamu, Serikali iliwasilisha taarifa ya umuhimu wa kumega hifadhi hiyo kama sehemu ya utatuzi wa migogoro ya Vijiji 975. Katika maelekezo ya Baraza la Mawaziri; Baraza liliridhia hifadhi imegwe na vijiji kupatiwa maeneo ya kuendeshea shughuli zao kwa uhuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeshachukua hatua katika kutekeleza maelekezo ya Baraza la Mawaziri kwa kufanya mapitio ya mpaka wa msitu wa Hifadhi ya Maisome ambapo hekta 2,943.8 zimetolewa kwa wananchi na eneo hilo na kubakiwa na hekta 9,319.2. Kwa sasa taratibu za kubadili mpaka kisheria na kupata ramani mpya zinaendelea. Mara zoezi hilo litakapokamilika, Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi watajulishwa ambapo watakuwa na muda wa siku 90 kutoa maoni yao kabla ya tangazo rasmi la kutangaza eneo jipya la hifadhi baada ya mabadiliko niliyoyasema hapo juu.
MHE. FRANCIS K. NDULANE aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga Jengo la Makumbusho katika Kijiji cha Nandete ili kuhifadhi kumbukumbu za Vita vya Majimaji?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Francis Ndulane kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa makumbusho unahitaji utafiti wa kina wa historia ya eneo husika ili kuweza kupata taarifa na mikusanyo itakayowekwa kwenye makumbusho tarajiwa. Kwa kutambua umuhimu wa historia ya vita vya Majimaji katika eneo la Nandete, Serikali kwa kushirikiana na wadau imeanza kufanya utafiti kwenye eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na jitihada hizo mwaka 2022 Serikali imefanya maboresho ya Sheria ya Mambo ya Kale, Sura ya 333 ili kuruhusu watu binafsi na taasisi mbalimbali kuanzisha makumbusho binafsi kwa lengo la kuhifadhi na kuendeleza utalii unaohusiana na utajiri wa kihistoria uliopo. Natoa wito kwa wadau wetu kutumia fursa hiyo kujenga makumbusho kwenye maeneo ya kihistoria hapa nchini ili kuendeleza historia na kujipatia kipato.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE K.n.y. MHE. SEIF K. GULAMALI aliuliza:-

Je, ni adhabu gani inatolewa kwa Watumishi wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) wanaobainika kudhuru raia na mali zao?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Misitu Sura 323 imeweka makatazo ambayo mtu yeyote anayekiuka makatazo hayo anakuwa ametenda makosa ya jinai na hivyo kulazimika kuchukuliwa hatua za kisheria. Aidha, katika utekelezaji wa majukumu hayo, watumishi wanatakiwa kuzingatia sheria, kanuni na misingi ya haki za binadamu. Hivyo, endapo mtumishi atabainika kudhuru raia au mali zake, atakuwa ametenda kosa kwa mujibu wa Sheria za Utumishi wa Umma za mwaka 2022 na kanuni zake pamoja na Amri za Kudumu za Jeshi la Uhifadhi wa Wanyamapori na Misitu za Mwaka 2022.

Mheshimiwa Naibu Spika, endapo mtumishi wa TFS atabainika kukiuka masharti ya kazi na kama atakuwa ametenda kosa la kijinai na kinidhamu, mwajiri atamfungulia mashtaka kwa mujibu wa Kanuni za Utumishi wa Umma zikisomwa pamoja na kifungu cha 9(3) cha Amri za Jeshi la Uhifadhi za Mwaka 2022. Pindi mtumishi huyo akikutwa na hatia, anaweza kufukuzwa kazi, kupunguziwa mshahara au kushushwa cheo na mshahara.
MHE. INNOCENT E. KALOGERIS K.n.y. MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI aliuliza:-

Je, lini Serikali itaanza kulipa fidia wananchi wa Kijiji cha Ngombo waliopisha Hifadhi ya Pori Tengefu la Kilombero?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Kijiji cha Ngombo kipo katikati ya eneo la ardhi oevu ndani ya Pori Tengefu Kilombero. Uwepo wa kijiji hiki pamoja na vijiji vingine ndani ya pori hilo ulifanya ukubwa wa eneo la pori kupungua kwa 61.5% kutoka kilometa za mraba 6,500 hadi kilometa za mraba 2,500. Hali hiyo ilipelekea Serikali kupitia Kamati ya Mawaziri Nane kuelekeza Kijiji cha Ngombo kufutwa na wananchi wake kuhamishiwa maeneo mengine sambamba na eneo la Pori Tengefu Kilombero kupandishwa hadhi kuwa Pori la Akiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, kufuatia hatua hiyo, Serikali imeshakamilisha zoezi la uthamini kwa wananchi wa Kijiji cha Ngombo kwa vitongoji vyote vitatu vinavyounda Kijiji hicho ambavyo ni Idenge, Ikwachu na Ifuru. Aidha, jumla ya shilingi 7,351,097,480.46 zimeainishwa kwa ajili ya kulipa fidia kwa wananchi hao. Wizara inasubiri fedha kutoka Hazina ili iweze kulipa fidia kwa wananchi ili waweze kuondoka katika eneo la hifadhi na eneo hilo kuendelea kusimamiwa kama Pori la Akiba Kilombero kwa mujibu wa Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Sura ya 283.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE aliuliza:-

Je, lini Serikali itafika katika Kata ya Kagerankanda kutatua mgogoro wa mpaka baina ya vijiji na TFS?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Kagerankanda inaundwa na vijiji viwili vya Mvinza na Kagerankanda. Kata hiyo inapakana na Hifadhi ya Msitu wa Makere Kusini uliohifadhiwa kwa TSN ya tarehe 10 Agosti, 1953. Kwa sasa hifadhi hii ina ukubwa wa hekta 65,178 kutoka hekta 75,190 zilizokuwepo awali. Kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya jamii hasa ardhi kwa ajili ya kilimo, makazi na malisho ya mifugo, hifadhi hii ilikumbwa na uvamizi kwa ajili ya shughuli mbalimbali. Hivyo Serikali iliridhia maombi ya wananchi ya kumega sehemu ya eneo lake kwa ajili ya kutumiwa na jamii hizo. Taratibu hizi zilikamilika kwa kupitia TSN 718/2018.

Mheshimiwa Naibu Spika, umegaji wa hifadhi hii ulifanyika kwa kuzingatia maelekezo ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mwaka 2017. Kufuatia maelekezo yake, Hifadhi ya Makere Kusini iliondolewa jumla ya hekta 10,012 na kugaiwa kwa wananchi wa maeneo hayo pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu na katika eneo lililomegwa, Kijiji cha Kagerankanda kilipata jumla ya hekta 2,496, Kijiji cha Mvinza hekta 2,174 na Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu kupewa jumla ya hekta 5,342.16.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU aliuliza:-

Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Kituo cha Utalii Kihesa, Kilolo chini ya mradi wa REGROW?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 26 Januari, 2024 Wizara ya Maliasili na Utalii ilisaini mkataba kwa ajili ya ujenzi wa jengo la utalii katika eneo la Kihesa Kilolo, Mkoani Iringa kupitia Mradi wa REGROW. Aidha, tarehe 27 Januari, 2024 mkandarasi alikabidhiwa eneo la ujenzi na kuanza kazi. Mkataba huo ni wa miezi 12 na unatarajiwa kukamilika mwezi Januari, 2025. Hadi kufikia mwezi Mei, 2024 ujenzi wa jengo hilo umefikia 15% na ujenzi unaendelea.
MHE. DKT. THEA M. NTARA aliuliza: -

Je, Chuo cha Utalii Dar es Salaam na Vyuo vingine vya utalii vimetoa wafanyakazi wangapi ngazi ya Menejimenti katika Hoteli za Serengeti na Ngorongoro?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo la Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro zipo hoteli zinazotoa huduma za malazi za kudumu 13. Kati ya hizo, 12 zimeajiri Mameneja wazawa na moja imeajiri Meneja ambaye ni raia wa kigeni. Kwa upande wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, kati ya hoteli 31 zinazotoa huduma za malazi za kudumu 22 zimeajiri Mameneja wazawa na tisa zimeajiri baadhi ya Mameneja ambao ni raia wa kigeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) kinatoa mafunzo katika ngazi ya Cheti na Diploma ambayo yanawezesha wahitimu wengi kuajiriwa katika kada ya utendaji na baadhi katika kada za usimamizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kwa kuwa Chuo cha Taifa cha Utalii kwa sasa hakitoi mafunzo kwa ngazi ya shahada na kimekuwa na changamoto ya kutoa wafanyakazi katika ngazi ya menejimenti kwenye hoteli, kwa hali hiyo, hoteli nyingi zinazotoa huduma za malazi zimeajiri Watanzania katika ngazi ya menejimenti waliomaliza kozi za utalii katika vyuo vingine nchini ikiwemo Chuo Kikuu cha Dodoma, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine na Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE aliuliza: -

Je, lini Kimondo cha Ivuna kitarejeshwa nchini na kutumika kama kivutio cha utalii?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua kuwepo kwa kimondo kilichoanguka Kijiji cha Ivuna, Mkoa wa Songwe mwaka 1938 kikiwa na ujazo wa tani 0.0077 sawa na asilimia 0.0044% ya kimondo cha Mbozi kilichopo katika Kijiji cha Isele Mkoani Songwe chenye tani 16.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Kimondo cha Ivuna kinahifadhiwa kwenye Makumbusho ya Historia ya Asili iliyo katika Mji wa London Nchini Uingereza. Aidha, Wizara kwa kutambua umuhimu wa malikale zilizochukuliwa nchini kabla na baada ya uhuru kwa sababu mbalimbali kikiwemo Kimondo cha Ivuna, imeunda Kamati ya Kitaifa inayoratibu namna bora ya kurudisha au kunufaika na malikale hizo zilizopo nje ya nchi. Kamati inafuatilia taarifa zake ili kuweza kuishauri Serikali njia sahihi za kukirudisha.
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza:-

Je, lini Serikali itamaliza mgogoro wa muda mrefu wa ardhi kati ya TANAPA Kitulo/TFS na wananchi wa Kata za Ilungu, Igoma na Inyala?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Mbeya Vijijini na uongozi wa kata zilizopakana na Hifadhi ya Taifa ya Kitulo imefanya mikutano 15 kati ya tarehe 17 Mei, 2023 na tarehe 9 Novemba, 2023. Mikutano hiyo ililenga kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa uhifadhi, dhana ya ujirani mwema na kuwashirikisha wananchi katika juhudi za pamoja za kutambua mipaka ya hifadhi kwa faida za hifadhi, jamii na Taifa kwa ujumla. Kufuatia mikutano hiyo, mgogoro huu umemalizika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuendeleza mahusiano mema na jamii zinazozunguka hifadhi, Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia TANAPA kwa kushirikiana na Serikali ya Mkoa wa Mbeya imepanga kuweka vigingi kwenye mpaka wa hifadhi kwa umbali wa kilometa 82 katika mwaka wa fedha 2024/2025 ili kurahisisha utambuzi wa mipaka ya hifadhi na vijiji.
MHE. MAIMUNA A. PATHAN K.n.y. MHE. ALEKSIA A. KAMGUNA aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kupanda miti katika Mkoa wa Morogoro hususani Milima ya Uluguru na kandokando ya Mto Fulua, Mnyera na Kilombero?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aleksia Kamguna, kama ifuatayo:-

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha uhifadhi unaendelezwa katika Milima ya Uluguru, zoezi la kupanda miti limeendelea kufanyika katika Mkoa wa Morogoro hususani katika milima hiyo. Mathalani, kwa kipindi cha Julai, 2023 hadi Machi, 2024, Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kushirikiana na halmashauri na wadau mbalimbali imepanda jumla ya miti 9,026,605 ikiwemo miti 1,000,000 ya mikarafuu kwa ajili ya viungo katika mpaka wa msitu wa Mazingira Asili Uluguru, pamoja na vijiji vinavyopakana na msitu huo na katika Mkoa wa Morogoro kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa maeneo ya Mto Fulua, Mnyera na Kilombero, Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali, wananchi na wadau imeendelea na jitihada za kutunza maeneo hayo kwa kupanda miti rafiki wa maji pamoja na kuendelea kutoa elimu ya umuhimu wa uhifadhi na kupanda miti stahiki katika maeneo ya kingo za mito.
MHE. SALIM A. HASHAM aliuliza: -

Je, lini Serikali itatoa majibu juu ya umiliki wa Msitu wa Hewa ya Ukaa uliopo Kituti hadi Mgolo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kifungu cha 23 cha Sheria ya Misitu kimeweka utaratibu wa uanzishaji na usimamizi wa maeneo ya misitu kisheria. Kupitia Tangazo la Serikali Na. 783/2022, Wizara ilikamilisha taratibu za awali za kutoa notisi ya siku 90 za nia ya Serikali ya kuanzisha rasmi Msitu wa Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga. Kwa sasa Wizara inakamilisha taratibu za kisheria za kuanzisha msitu huo ambao utakuwa chini ya umiliki wa Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kusimamia uhifadhi wa misitu ikizingatiwa kwamba imeandaa na kuzindua biashara ya hewa ya ukaa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania ina takribani hekta za misitu milioni 48.1 ambayo inajumuisha misitu ya Serikali Kuu, misitu ya halmashauri, misitu ya vijiji na misitu binafsi. Aidha, kutokana na kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu kama kilimo cha kuhamahama, uchomaji moto kwenye misitu na ufugaji, nchi yetu inapoteza takribani hekta 469,000 kwa mwaka na hivyo kuchangia kuzalisha gesi joto na hatimaye uwepo wa mabadiliko ya tabianchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, biashara ya kaboni ni mojawapo ya mkakati wa Kimataifa wa kusaidia kupata fedha za uhifadhi wa mazingira na misitu na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Kutokana na umuhimu huo, Serikali imeweka mikakati ya kulinda misitu iliyopo na kuongeza upandaji miti nchini. Serikali imefanya hivyo kupitia mikakati na miongozo mbalimbali ikiwemo Mkakati wa Kuongoa Misitu wa mwaka 2024, Makakati wa Mianzi wa mwaka 2024, Mwongozo wa Kitaifa wa Uandaaji na Utunzaji wa Kitalu cha Miche ya Miti wa mwaka 2024 pamoja na Mkakati wa Kitaifa wa Kilimo Mseto wa mwaka 2024. Hivyo, nitoe rai kwa wananchi kuendelea kuzingatia sheria za uhifadhi zilizowekwa na kutojishughulisha na shughuli za uharibifu wa misitu.
MHE. TUMAINI B. MAGESSA aliuliza:-

Je, lini TFS itawaruhusu Wananchi wa Busanda kufanya shughuli za kiuchumi katika hifadhi ya misitu iliyopo kati ya Geita na Katoro kwani haina miti?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Hifadhi ya Msitu Geita ilihifadhiwa rasmi mwaka 1953 na inasimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania. Hifadhi hiyo yenye ukubwa wa hekta 50,836.535 ilifanyiwa mapitio ya mipaka yake kupitia Tangazo la Serikali Na. 717 la Mwaka 2018 kwa lengo la kupunguza maeneo yaliyokuwa yamevamiwa na wananchi au kutoa maeneo yaliyoombwa kwa shughuli za maendeleo kwa vijiji na mitaa inayopakana na hifadhi hiyo. Mabadiliko hayo ya mipaka yalisababisha kupungua kwa eneo la hekta 4,522.95 kwa malengo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kufuatia uharibifu uliofanyika katika hifadhi ya msitu huo, Serikali imeweka mpango wa kurejesha uoto wa asili uliopotea na kwa mwaka wa fedha 2024/2025. Serikali imetenga fedha za kupanda miti kwenye hekta 100. Hivyo kwa kipindi hiki ambacho Serikali inafanya jitihada za kurejesha uoto wa asili uliopotea, jitihada zozote za kuruhusu kufanyika shughuli za kibinadamu/kiuchumi zitafifisha jitihada za Serikali.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI aliuliza:-

Je, Serikali imechukua hatua gani za muda mfupi wa kati na muda mrefu kunusuru theluji inayotoweka Mlima Kilimanjaro?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Profesa Ndakidemi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, sababu kubwa ya kupungua kwa barafu katika Mlima Kilimanjaro ni kuongezeka kwa joto la dunia kutokana na mabadiliko ya tabianchi yanayochangiwa na ongezeko la shughuli za kibinadamu hususan ukataji wa miti, kilimo, uchomaji wa moto katika maeneo yanayozunguka mlima, uwepo wa mvua chache na vipindi vya ukame na upepo mkavu kutoka Bahari ya Hindi.

Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza mikakati ya muda mfupi Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imepanga kupanda miti takriban milioni nane kwa mwaka katika Mkoa wa Kilimanjaro, sambamba na kutoa elimu kwa umma kuhusu upandaji miti na uhifadhi wa mazingira kupitia vipindi vya redio, televisheni, matamasha na maadhimisho mbalimbali ya kitaifa na kimataifa. Vilevile, Serikali kwa kushirikiana na wadau imezindua kampeni ya kupanda miti zaidi ya bilioni moja katika Mikoa ya Kaskazini ili kunusuru barafu ya Mlima Kilimanjaro.

Mheshimiwa Spika, mikakati ya muda wa kati ni pamoja na kuhimiza matumizi bora ya ardhi na kuimarisha ulinzi katika maeneo yanayozunguka Mlima Kilimanjaro na kutekeleza mipango ya kudhibiti na kupambana na uchomaji moto mlimani. Aidha, katika kutekeleza mikakati ya muda mrefu, Serikali inaendelea kushirikiana na Mashirika ya Kikanda na Kimataifa kutekeleza mikakati ya pamoja ya kuhimili na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ikiwa ni pamoja na kuboresha teknolojia za kilimo, kuongeza ufanisi wa matumizi ya maji, kupunguza uzalishaji wa gesi chafu na kurejesha mifumo ya ikolojia kwenye mlima na maeneo yanayozunguka.
MHE. ERIC J. SHIGONGO aliuliza:-

Je, lini Serikali itatimiza ahadi ya kuwakatia eneo la Hifadhi Wananchi wa Kisiwa cha Maisome kwa kuwa idadi ya wakazi imeongezeka?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Hifadhi ya Msitu wa Maisome ilianzishwa mwaka 1955 kupitia Tangazo la Serikali Na. 355, ikiwa na ukubwa wa hekta 12,191.02. Kufuatia wananchi wa Kisiwa cha Maisome wanaoishi ndani ya hifadhi kuwa na uhitaji wa eneo, kwa ajili ya matumizi kwa shughuli mbalimbali za kijamii, Kisiwa cha Maisome kiliingizwa kuwa sehemu ya utatuzi wa migogoro ya vijiji 975 ambapo Baraza la Mawaziri liliridhia jumla ya hekta 2,871.782 zimegwe kutoka kwenye hekta 12,191.02 za eneo la hifadhi na hivyo, kufanya hifadhi kubakiwa na hekta 9,319.238.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa tayari Wizara imekamilisha zoezi la kupitia mpaka wa hifadhi na kupima upya eneo lililobaki na tayari ramani mpya ya eneo hilo imeandaliwa. Aidha, Wizara imewasilisha Rasimu ya Tangazo la Serikali (Notisi ya Kusudio la Kutangaza Mabadiliko ya Eneo la Msitu wa Hifadhi wa Taifa Maisome ya Mwaka 2024) kwenye Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kwa ajili ya upekuzi ili kukamilisha taratibu za Kisheria za mabadiliko hayo.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA K.n.y MHE. TOUFIQ SALIM TURKY aliuliza:-

Je, Serikali imejipangaje kuhakikisha Watanzania wanashiriki Kongamano la Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Wafugaji mwaka 2027?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Tanzania imechaguliwa kuwa mwenyeji wa Kongamano la Kimataifa la Wafugaji Nyuki Duniani (Apimondia) litakalofanyika mwaka 2027. Serikali imejipanga kwa njia mbalimbali kuhakikisha Watanzania wanashiriki kikamilifu pamoja na kunufaika na Kongamano hilo ikiwa ni pamoja na kuunda Kamati ya Maandalizi ya Kitaifa ambayo inajumuisha wajumbe kutoka Serikalini na sekta binafsi kwa lengo la kuratibu na kufanya maandalizi ya kutosha ili kufanikisha kongamano hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mikakati mingine inajumuisha uhamasishaji wa wananchi katika ufugaji, uzingatiaji ubora na kufungua masoko mapya ya mazao ya nyuki duniani. Serikali pia kwa kushirikiana na sekta binafsi imekuwa ikiandaa maonesho kama hamasa ya maandalizi. Miongoni mwa maonesho yaliyofanyika ni pamoja na siku ya nyuki duniani iliyofanyika tarehe 17 - 20 Mei, 2024 na Maonesho ya Kitaifa ya Asali Tanzania yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 19 hadi 22 Juni, 2024.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI aliuliza:-

Je, Serikali imechukua hatua gani za muda mfupi wa kati na muda mrefu kunusuru theluji inayotoweka Mlima Kilimanjaro?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Profesa Ndakidemi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, sababu kubwa ya kupungua kwa barafu katika Mlima Kilimanjaro ni kuongezeka kwa joto la dunia kutokana na mabadiliko ya tabianchi yanayochangiwa na ongezeko la shughuli za kibinadamu hususan ukataji wa miti, kilimo, uchomaji wa moto katika maeneo yanayozunguka mlima, uwepo wa mvua chache na vipindi vya ukame na upepo mkavu kutoka Bahari ya Hindi.

Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza mikakati ya muda mfupi Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imepanga kupanda miti takriban milioni nane kwa mwaka katika Mkoa wa Kilimanjaro, sambamba na kutoa elimu kwa umma kuhusu upandaji miti na uhifadhi wa mazingira kupitia vipindi vya redio, televisheni, matamasha na maadhimisho mbalimbali ya kitaifa na kimataifa. Vilevile, Serikali kwa kushirikiana na wadau imezindua kampeni ya kupanda miti zaidi ya bilioni moja katika Mikoa ya Kaskazini ili kunusuru barafu ya Mlima Kilimanjaro.

Mheshimiwa Spika, mikakati ya muda wa kati ni pamoja na kuhimiza matumizi bora ya ardhi na kuimarisha ulinzi katika maeneo yanayozunguka Mlima Kilimanjaro na kutekeleza mipango ya kudhibiti na kupambana na uchomaji moto mlimani. Aidha, katika kutekeleza mikakati ya muda mrefu, Serikali inaendelea kushirikiana na Mashirika ya Kikanda na Kimataifa kutekeleza mikakati ya pamoja ya kuhimili na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ikiwa ni pamoja na kuboresha teknolojia za kilimo, kuongeza ufanisi wa matumizi ya maji, kupunguza uzalishaji wa gesi chafu na kurejesha mifumo ya ikolojia kwenye mlima na maeneo yanayozunguka.
MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:-

Je, lini Serikali itamaliza mgogoro wa mpaka kati ya Hifadhi ya Mpanga Kipengele na Vijiji vya Luduga, Mpanga, Malangali na Wangamiko?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, mgogoro wa mpaka kati ya Hifadhi ya Mpanga Kipengele na Vijiji vya Luduga, Mpanga, Malangali na Wangamiko vilivyopo katika Wilaya ya Wanging’ombe umetatuliwa baada ya kutekeleza maelekezo ya Serikali yaliyotolewa kupitia Kamati ya Mawaziri nane wa kisekta. Maelekezo ya Serikali ilikuwa ni kutoa sehemu ya ardhi ya hifadhi kwa vijiji, kufyeka na kuweka alama za mpaka.

Mheshimiwa Spika, kupitia maelekezo haya, Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Ofisi ya Kamishna wa Ardhi, Mikoa ya Njombe na Mbeya ilifanya mapitio ya mpaka wa Hifadhi ya Mpanga Kipengere na kumega eneo lenye ukubwa wa ekari 18,221.43 na eneo hilo kutolewa kwa wananchi wa vijiji vya Luduga, Mpanga, Malangali na Wangamiko. Aidha, Hifadhi ya Mpanga Kipengere kwa ujumla imemega ardhi yenye ukubwa wa ekari 52,877.602 na kutolewa kwa vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo na hivyo kumaliza migogoro iliyokewepo kati ya hifadhi na vijiji hivyo.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE aliuliza:-

Je, kuna mpango gani wa kuanza kutoa ruzuku vijiji vinavyozunguka Mlima Kilimanjaro kutoka kwenye mapato ya mlima?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro inapakana na vijiji 94 vilivyopo katika Wilaya tano ambazo ni Moshi, Rombo, Siha na Hai, kwa Mkoa wa Kilimanjaro na Longido kwa Mkoa wa Arusha. Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro imeendelea kushirikiana na vijiji vinavyopakana nayo vikiwemo vijiji tisa vilivyopo katika Wilaya ya Hai kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo utekelezaji wa miradi ya maendeleo na utoaji wa elimu ya uhifadhi ili kuwawezesha wananchi hao kunufaika kiuchumi na kimazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania hutekeleza sera ya kugawana faida zitokanazo na uhifadhi kupitia utaratibu wa Miradi ya Ujirani Mwema. Utaratibu huu unawezesha wananchi kuibua wenyewe miradi ya maendeleo na kiuchumi au kimazingira ambayo ni hitaji lao na kipaumbele, kisha hupeleka maombi hifadhini ambapo TANAPA huchangia 90% ya gharama ya mradi na wananchi huchangia 10%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mathalani, katika mwaka wa fedha 2024/2025 jumla ya shilingi 90,550,000.00 zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi minne katika Wilaya ya Hai. Miradi hiyo itahusisha ukarabati wa madarasa manne katika Vijiji vya Foo, Nkuu Ndoo, Ng’uni na Saawe pamoja na mradi wa uwekaji wa mfumo wa gesi katika Shule ya Msingi Lukani.
MHE. ESTHER E. MALLEKO aliuliza:-

Je, kuna mkakati gani wa kuwaongezea bajeti TANAPA na TAWA kwani majukumu yao ni makubwa ikilinganishwa na bajeti inayotengwa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya janga la ugonjwa wa UVIKO - 19 mwaka 2019, ambalo liliathiri shughuli za utalii kwa kiasi kikubwa, Taasisi za uhifadhi hususan TANAPA pamoja na TAWA zilishindwa kupata fedha za kutosha kwa ajili ya kujiendesha hali ambayo iliifanya Serikali kuchukua hatua za makusudi za kunusuru taasisi hizo kwa kugharamia uendeshaji pamoja na kulipa mishahara ya watumishi. Kufuatia hatua hizo, hadi sasa Taasisi za Uhifadhi (TANAPA, TAWA na NCAA) zinapata fedha za uendeshaji kutoka Serikalini kwa utaratibu wa mgao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali iliziongezea taasisi za uhifadhi bajeti ya matumizi ya kawaida (OC). Mathalan, bajeti ya TANAPA iliongezwa kutoka shilingi 106,958,705,429.41 mwaka wa fedha 2022/2023 hadi kufikia shilingi bilioni 118.3 ikiwa ni ongezeko la shilingi 11,348,567,370.59 sawa na ongezeko la 10.61%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile bajeti ya TAWA iliongezwa kutoka shilingi bilioni 45.6 kwa mwaka wa fedha 2022/2023 hadi kufikia shilingi bilioni 62.9 ikiwa na ongezeko la shilingi 17,284,226,400.00 sawa na ongezeko la 37.83%. Aidha, Serikali itaendelea kuboresha bajeti ya taasisi hizo kutegemeana na hali ya ukusanyaji wa mapato ya Serikali ili kuimarisha shughuli za ulinzi na kuboresha miundombinu ya utalii.