Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Dunstan Luka Kitandula (17 total)

MHE. DUNSTAN L. KITANDULA aliuliza:-
Serikali iliweka Wilaya ya Mkinga kuwa miongoni mwa Wilaya za kipaumbele kujengewa Chuo cha VETA.
Je, ni lini sasa Serikali itatekeleza ahadi ya kujenga Chuo cha VETA Wilayani Mkinga?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijajibu swali naomba kama itakupendeza, kupitia Bunge lako tukufu niwapongeze na kuwatakia kila la kheri vijana wetu 960,202 wanaofanya mitihani ya darasa la saba leo kwenye shule tofauti 16,845. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dunstan Luka Kitandula, Mbunge wa Mkinga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi kwa ajili ya kuandaa rasilimaliwatu watakaotumika katika viwanda na shughuli nyingine za uzalishaji, hasa wakati huu ambapo Serikali imeazimia kufanya nchi yetu kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Vyuo hivi vitasaidia kuwaandaa vijana ili waweze kujipatia ajira kwa kujiajiri au kuajiriwa ikizingatiwa kuwa kundi kubwa la vijana wetu halipati fursa ya kuendelea na masomo ya elimu ya juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na mpango wake wa ujenzi waVyuo vya Ufundi Stadi vya Mikoa na Wilaya, ikiwemo Wilaya ya Mkinga, kutegemeana na upatikanaji wa fedha. Lengo ni kila Mkoa na Wilaya kuwa na Chuo cha Ufundi Stadi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Wizara inaendelea na utekelezaji wa Mradi wa Stadi za Kazi (Education and Skills for Productive Jobs – ESPJ) ambapo kupitia Mradi huu Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDC’s) vitakarabatiwa ili kuongeza fursa za mafunzo. Hivyo, katika kipindi hiki ambacho Serikali inaendelea na jitihada hizi, nashauri wananchi wa mikoa na wilaya zote ambazo hazijawa na Vyuo vya VETA kutumia Vyuo vya Ufundi vilivyopo nchini, hususan kwenye mikoa na wilaya jirani ili vijana wetu waweze kupata ujuzi na stadi muhimu kwa maendeleo ya nchi kwa ujumla.
MHE. DUSTAN L. KITANDULA aliuliza:-

Katika kuimarisha ulinzi wa mipaka yetu na nchi jirani ya Kenya, Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) limechukua mashamba ya baadhi ya wananchi wa Kata ya Mwakijembe:-

Je, ni lini wananchi hao watapewa fidia kwa ajili ya ardhi/mashamba yao yaliyochukuliwa na Jeshi?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dunstan Luka Kitandula, Mbunge wa Mkinga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania limeanzisha Kituo cha Ulinzi katika eneo la Kata ya Mwakijembe, Wilaya ya Mkinga lenye hekari moja mwaka 2017. Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga iliona umuhimu wa kutenga eneo hilo kwa matumizi ya Jeshi ili kuimarisha ulinzi kwenye maeneo ya mpakani. Eneo hilo awali lilikuwa ni shamba darasa la mradi wa umwagiliaji uliokuwa unaendeshwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa eneo hili lilikuwa linasimamiwa na uongozi wa Wilaya kabla ya Jeshi kuingia hapo, ni busara suala la fidia kama lipo likawasilishwa kwenye uongozi wa Wilaya ya Mkinga.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA (K.n.y. MHE. DUNSTAN L. KITANDULA) aliuliza:-

Kata za Kigongoi, Mhinduro na Bosha Wilayani Mkinga zinalima kwa wingi viungo vya chakula kama vile hiliki, mdalasini, pilipili manga na karafuu:-

Je, Serikali ipo tayari kuwawezesha Wakulima hao kupata mbegu bora ili waweze kuongeza uzalishaji wa mazao yao?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dunstan Luka Kitandula, Mbunge wa Mkinga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuwekeza katika mazao mbalimbali ya kilimo yakiwemo mazao ya viungo ambayo mahitaji yake yanaendelea kuongezeka ndani na nje ya nchi. Kwa kutambua umuhimu huo, Serikali kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) imeanza kufanya utafiti wa kupata mbegu bora za mazao ya viungo na mazao mengine ya bustani aina ya horticulture ili kuongeza uzalishaji na tija.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo inapitia Sera ya Kilimo ya Mwaka 2013 ambapo sekta ndogo ya mazao ya bustani ni miongoni mwa maeneo muhimu yanayozingatiwa. Vilevile, kutokana na umuhimu wa mazao hayo, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo itafanya kikao cha wadau wa mazao hayo tarehe 8 Novemba, 2019 ili kuandaa Mkakati wa Miaka Mitano wa Kuendeleza Mazao ya Bustani. Mkakati huo unalenga kuongeza uzalishaji, ubora wa mazao na kuimarisha mifumo ya masoko ya mazao hayo. Aidha, mkakati huo utakuwa ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa unaolenga Taifa letu kufikia uchumi wa kati mwaka 2025.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hatua hizo, Serikali inaendelea kutoa elimu ya kilimo bora cha mazao ya viungo na mazao mengine; uhifadhi, usindikaji na masoko kwa kushirikiana na Sekta Binafsi kikiwemo Chama cha Wadau wa Mazao ya Viungo Tanzania (Tanzania Spices Association – TASPA), Sustainable Agriculture Tanzania (SAT) na vyama vingine vya wakulima.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA aliuliza:-

Je, ni lini mradi wa maji kutoka chanzo cha Mto Zigi kwenda Mkinga na Horohoro utaanza?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dunstan Luka Kitandula, Mbunge wa Jimbo la Mkinga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeshaanza maandalizi ya mpango wa utekelezaji wa mradi wa kutoa maji Mto Zigi kwenye mji wa Kasera ambao ni Makao Makuu ya Wilaya ya Mkinga, pamoja na Mji wa mpakani wa Horohoro. Kwa sasa taratibu za kumpata Mtaalam Mshauri atakayefanya upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na uandaaji wa makabrasa zabuni zinaendelea. Matarajio ni Mtaalam Mshauri atakayepatikana atakamilisha kazi hiyo mwezi Septemba, 2019. Ujenzi wa mradi huo unatarajiwa kuanza baada ya kukamilika kwa usanifu.

Mheshimiwa Spika, wakati tunasubiri usanifu wa mradi wa kutoa maji Mto Zigi kukamilika, Serikali imeandaa mradi wa uboreshaji wa huduma ya maji kwa mpango wa muda mfupi katika Mji wa Horohoro kwa gharama ya kiasi cha shilingi milioni 595. Kazi zitakazotekelezwa ni ulazaji wa bomba, ujenzi wa mtambo mdogo wa kusafisha na kutibu maji, ukarabati wa tanki la maji na ujenzi wa vituo vitano vya kuchotea maji. Mradi huo unatarajiwa kuanza mwezi Juni, 2019 na kukamilika baada ya miezi sita.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itapeleka umeme wa REA III katika Kijiji cha Hemsambia na Vitongoji vyake vyote?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dunstan Luka Kitandula, Mbunge wa Mkinga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Vijiji vya Hemsambia na Kindundui ni miongoni mwa Vijiji vya Kata ya Kigongoi, Wilaya ya Mkinga vilivyofaidika na Awamu ya Tatu ya utekelezaji wa Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini, REA III, mzunguko wa kwanza. Mkandarasi Kampuni ya Ubia ya JV Radi Service Limited, Njarita Contractor Limited na Aguila Contractor Limited yuko site anaendelea na kazi ya kusambaza umeme katika maeneo husika.

Mheshimiwa Spika, kazi za kupeleka umeme katika Vijiji vya hemsambia na Kindundui imejumuisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 2.1, njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilometa mbili, ufungaji wa transfoma mbili za KVA 50 pamoja na kuwaunganishia umeme wateja wa awali 62. Gharama ya mradi ni shilingi milioni 184.23.

Mheshimiwa Spika, vijiji vingine vya Kata ya Kigongoi vya Vuga, Kwekuyu, Kindundui, Mgambo Shashui na Bombo Mbuyuni vitapatiwa umeme kupitia Mradi wa REA III Mzunguko wa Kwanza unaoendelea kutekelezwa Wilayani Mkinga na kukamilika mwezi Juni, 2020. Ahsante sana.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA aliuliza:-

Kijiji cha Segoma Wilayani Mkinga ni miongoni mwa vijiji vitakavyopata umeme wa REA III.

Je, kwa nini Serikali isitumie fursa hiyo kuunganisha umeme katika Sekondari ya Lanzoni iliyopo karibu na Kitongoji cha Darajani?
WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dunstan Luka Kitandula, Mbunge wa Mkinga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) pamoja na Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) inatoa kipaumbele kupeleka umeme katika Taasisi za umma na za kijamii ikiwa ni pamoja na Shule za Awali, Msingi na Sekondari, Vyuo vya Ufundi Stadi, Vituo vya Afya, Zahanati, Visima vya Maji na Nyumba za Ibada.

Mheshimiwa Naibu Spika, Katika Mwaka wa fedha 2019/2020 Serikali kupitia TANESCO inaendelea na kazi ya kusambaza umeme katika Vijiji vya Mgamboshashui, Kumbamtoni na Mpale. Kazi hiyo inahusisha kupeleka umeme katika Shule za Sekondari Duga na Lanzoni zilizopo katika Jimbo la Mkinga.

Mheshimiwa Naibu Spika, Gharama ya kazi ya kupeleka umeme katika vijiji hivyo vitatu pamoja na shule hizo za Sekondari ni Shilingi Milioni 91. Utekelezaji wa kazi hiyo ulianza mwezi Machi, 2020 na utakamilika mwezi Mei, 2020. Jumla ya wateja wa awali zaidi ya 175 wataunganishiwa umeme.
MHE. MWANTUMU M. ZODO K.n.y. MHE. DUNSTAN L. KITANDULA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itafanya zoezi la kuhakiki na kuweka alama kwenye mpaka wa Tanzania na Kenya kwa eneo la nchi kavu na baharini ili wananchi wa mpakani Wilayani Mkinga waondokane na kero ya muda mrefu ya kukamatwa na kutaifishiwa mali zao na askari wa Kenya?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dunstan Luka Kitandula, Mbunge wa Mkinga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mpaka wa kimataifa kati ya Tanzania na Kenya una jumla ya urefu wa kilometa 817.71 ikiwa kilometa 758 ni nchi kavu na kilometa 59.71 ni ndani ya maji. Eneo la nchi kavu la mpaka huo linaanzia Ziwa Victoria, Wilaya ya Rorya Mkoani Mara hadi Jasini, Wilaya ya Mkinga Mkoa wa Tanga.

Mheshimiwa Spika, hadi sasa, sehemu ya mpaka wa Tanzania na Kenya yenye urefu wa kilometa 172 kutoka Ziwa Victoria hadi Ziwa Natron umeimarishwa na kuwekewa
alama 1,135. Kati ya alama hizo, alama 162 zimejengwa na kukarabatiwa na alama 973 zimejengwa kwa umbali wa mita 100 hadi 200 ili kuwezesha wananchi kuubaini mpaka kwa urahisi. Zoezi la kuimarisha mpaka kati ya Ziwa Natron hadi Namanga wenye urefu wa kilometa 128 kwa mwaka 2019/ 2020 liliahirishwa kutokana na kuzuka kwa ugonjwa wa Covid-19. Kutokana na uwepo wa ugonjwa huo, zoezi la kuimarisha mpaka uliobaki kati ya Tanzania na Kenya wenye urefu wa kilometa 586 kwa nchi kavu na kilometa 59.71 ndani ya maji limesimama hadi hapo nchi hizi mbili zitakapokubaliana. Urefu wa Mpaka katika Wilaya ya Mkinga katika mpaka huu ambao haujaimarishwa ni kilometa 52.96 ambayo ni nchi kavu.

Mheshimiwa Spika, sehemu ya mpaka ndani ya Bahari ya Hindi kutoka Jasini hadi kwenye alama ya utatu kati ya nchi ya Tanzania, Kenya na Ushelisheli ina mkataba wa makubaliano kati ya nchi hizi tatu… katikati ya Kenya na Tanzania ambao ulitiwa saini tarehe 23 Juni, 2009 Jijini Dar es Salaam isipokuwa alama zake za maboya hazijawekwa. Kazi ya kuweka maboya katika mpaka huu itafanyika baada ya kukamilika uimarishaji wa mpaka katika eneo la nchi kavu.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itafuta hati ya mashamba yaliyotelekezwa kwa zaidi ya miaka 20 Wilayani Mkinga hususan shamba la Kwamtili ili ardhi hiyo igawiwe kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Dunstan Luka Kitandula, Mbunge wa Mkinga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi (Sura 113), kila mmiliki wa ardhi anapaswa kuendeleza ardhi yake aliyomilikishwa kwa kuzingatia masharti yaliyoainishwa katika nyaraka za umiliki. Kwa wamiliki wanaobainika kukiuka masharti ya umiliki, sheria hiyo imeelekeza hatua mbalimbali za kuchukua ikiwemo kubatilisha milki husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa mashamba yenye milki za hati Na. 14501 (Ekari 2,841) na hati Na. 4722 (Ekari 58) Kwamtili, Wilayani Mkinga yanayomilikiwa na Kampuni ya Kwamtili Estate Limited kwa matumizi ya kilimo yana ukiukwaji wa masharti ya umiliki ikiwemo wamiliki kushindwa kuyaendeleza na kukwepa kulipa kodi ya ardhi kikamilifu. Hata hivyo, imebainika kuwa, katika Daftari la Kumbukumbu la Msajili wa Hati, hatimilki za mashamba hayo zimewekwa rehani kwa kukopeshwa fedha na hivyo kuwa na third part interest (maslahi ya mtu wa tatu).

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara imeelekeza Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga kuanza kuchukua hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kutuma Ilani ya Ubatilisho kwa wamiliki. Hatua hiyo ikifanyika sambamba na kuwasiliana na Benki iliyotoa mkopo kama dhamana kuwataarifu wahusika kutafuta dhamana nyingine kutokana na masharti ya mashamba hayo kukiukwa. Mara baada ya milki za mashamba hayo kubatilishwa, hatua za kuyapanga, kuyapima na kuyagawa upya kulingana na mahitaji halisi sasa zitaendelea.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara ya Tanga – Mabokweni – Maramba – Daluni – Mtoni – Bombo – Magoma hadi Korogwe?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Dunstan Luka Kitandula, Mbunge wa Mkinga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Tanga – Mabokweni – Maramba – Daluni – Bombo Mtoni – Korogwe yenye urefu wa kilometa 127.69 ni barabara ya mkoa inayohudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS). Aidha, Sehemu ya barabara ya Tanga – Mabokweni yenye urefu wa kilometa 11.2 tayari imejengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kiuchumi wa barabara ya Tanga – Mabokweni – Maramba – Daluni – Bombo – Korogwe kwa wananchi wa maeneo ya Mashewa, Mabokweni, Maramba, Bombomtoni, Magoma na Daluni. Kwa kutambua umuhimu huo, Wizara imetenga fedha katika bajeti ya mwaka wa fedha ujao 2021/ 2022 kiasi cha shilingi milioni 1,275.4 ambayo ni sawa na bilioni 1.2754 ili kuanza upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hii. Mara baada ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kukamilika, Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii. Aidha, barabara hii itaendelea kufanyiwa matengenezo mbalimbali ili iweze kupitika majira yote ya mwaka. Ahsante.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA aliuliza: -

Je, ni lini wananchi wa Kata ya Mwakijembe ambao mashamba yao yalitwaliwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) watalipwa fidia?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dunstan Luka Kitandula, Mbunge wa Mkinga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania lilianzisha Kituo cha Ulinzi mwaka 2017, eneo la Kata ya Mwakijembe. Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga iliona umuhimu wa kutenga eneo hilo kwa matumizi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania ili kuimarisha ulinzi kwenye maeneo ya mpakani. Aidha, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ilitembelea eneo husika mwaka 2017 kujionea hali halisi. Eneo husika awali lilikuwa ni la mradi wa Serikali wa umwagiliaji maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Kata ya Mwakijembe wanaombwa wawe na subira pindi taratibu za kisheria za utwaaji wa eneo zikikamilika. Serikali italipa fidia kwa wananchi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia sababu zilizotolewa hadi Jeshi kukabidhiwa eneo hilo, Jeshi litaendelea kutumia eneo hilo wakati taratibu za ulipwaji wa fidia zinaendelea.
MHE. JOHN M. SALLU K.n.y. MHE. DUNSTAN L. KITANDULA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya kuvipatia maji kutoka mradi wa Mapatano Vijiji vya Kwangena, Bantu na Machimboni Wilayani Mkinga?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dunstan Luka Kitandula Mbunge wa Jimbo la Mkinga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, jukumu la Serikali ni kuhakikisha maeneo yote ya vijijini huduma ya upatikanaji wa maji inaboreshwa. Ambapo katika mwaka wa fedha 2021/2022 kazi ya upanuzi wa skimu ya maji ya Mapatano inafanyika. Ili kufikisha maji katika vijiji vya Kwangena, Bantu na Machimboni ambavyo mahitaji ya maji ni lita 251,000 kwa siku.

Mheshimiwa Spika, katika upanuzi huo kazi zitakazofanyika ni kulaza mabomba Kilomita 29 na kujenga matenki mawili (2) ya kuhifadhi maji lita 45,000 na lita 135,000. Kazi hii inatarajiwa kukamilika mwezi Agosti, 2022 na utanufaisha wananchi takriban 11,000.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwawezesha wakulima wa mazao ya viungo kama Iliki, mdalasini, pilipili manga na karafuu wa Kata ya Kigongoi, Mhindano na Bosho Wilayani Mkinga ili waweze kuongeza uzalishaji wa thamani ya mazao hayo?
WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dunstan Luka Kitandula, Mbunge wa Mkinga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, mazao ya viungo yanayojumuisha Karafuu, Pilipilimanga, Pilipili Kali, Mdalasini, Hiliki, Tangawizi na jamii hiyo ya mazao ya viungo, hulimwa zaidi katika Mikoa ya Tanga, Morogoro, Mbeya, Kilimanjaro, Kigoma na Ruvuma. Aidha, katika Mkoa wa Tanga Wilaya ya Mkinga na katika Kijiji cha Kigongoi na vijiji vidogo jirani yake ndiyo wanazalisha mazao ya viungo zaidi ikiwemo Hiliki, Mdalasini na Pilipilimanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kutambua umuhimu wa kuendeleza mazao ya bustani yakiwemo mazao ya viungo, inatekeleza Mkakati wa Kuendeleza Mazao ya Bustani wa Mwaka 2021 - 2031 wenye lengo la kuongeza uzalishaji kwa kutumia teknolojia bora na kuimarisha usimamizi na uratibu. Aidha, mikakati mingine ni pamoja na kutoa mafunzo ya wataalam na wakulima kuhusu kanuni za uzalishaji wa mazao ya viungo, kuunganisha wakulima na wanunuzi wakubwa, na kuanzisha vitalu vya kisasa vya miche ya viungo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na chama cha wasindikaji wa viungo (TASPA) na wasindikaji wa mazao ya viungo wameanza kuwashirikisha wakulima wa viungo Wilaya ya Mkinga kwa kuanzisha vitalu vya kisasa vya viungo. Mfano, Kampuni ya Trianon Investment Ltd yenye Kiwanda cha Viungo Lusanga – Muheza tayari imeanza kununua mazao kwa wakulima wa viungo Mkinga na imedhamiria kugawa miche bora kutoka katika bustani bora ya kuzalisha miche iliopo kiwandani.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika imeanza kuhamasisha wakulima kuanzisha na kujiunga na Vyama vya Msingi vya Ushirika ili kukuza uwezo wao wa kifedha kupitia mikopo na kuwa na nguvu ya pamoja katika soko; na pia Serikali kuweza kuwapatia mafunzo ya uzalishaji bora na uongezaji thamani wa mazao yao. (Makofi)
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA aliuliza: -

Je, ni lini ujenzi wa Chuo cha VETA unaoendelea Wilayani Mkinga utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Sayansi na Teknolojia, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Dunstan Luka Kitandula, Mbunge wa Mkinga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kukamilika kwa Chuo cha VETA cha Wilaya ya Mkinga pamoja na vyuo vingine ili viweze kutoa mafunzo yatakayowawezesha vijana wetu kujiajiri na kuajiriwa. Kwa sasa ujenzi wa Chuo hiki upo katika hatua za mwisho za ukamilishaji ambapo ujenzi umefikia asilimia 95. Ujenzi wa Chuo hiki unatarajiwa kukamilika kabla ya mwezi Disemba, 2022. Hivyo, Chuo hiki kinatarajiwa kuanza kutoa mafunzo ya muda mfupi kuanzia mwezi Oktoba, 2022 na mafunzo ya muda mrefu mwezi Januari, 2023. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha ujenzi wa Skimu ya Umwagiliaji Mwakijembe pamoja na bwawa la kukinga maji?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dunstan Luka Kitandula Mbunge wa Mkinga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, skimu ya umwagiliaji inakadiriwa kuwa na jumla ya hekta 450. Hekta 200 katika Kijiji cha Mwakijembe na hekta 250 katika Kijiji cha Mbuta ambazo zinafaa kwa kilimo cha umwagiliaji wa mazao makuu yakiwa ni mahindi, maharage na mbogamboga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imeanza kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina katika skimu zilizopo katika Bonde la Mto Umba ikiwemo skimu ya Mwakijembe kwa lengo la kupata gharama halisi za ujenzi. Baada ya kukamilisha zoezi la upembuzi yakinifu na usanifu wa kina skimu hii itaingia katika mpango wa ujenzi wa mwaka wa fedha 2024/2025.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA aliuliza: -

Je, ni lini ujenzi wa Mradi wa Maji Mkinga kutoka Mto Zigi au Kinyatu utaanza kutekelezwa?
WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dunstani Luka Kitandula, Mbunge wa Jimbo la Mkinga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuboresha huduma ya maji kwa wananchi wa Wilaya ya Mkinga pamoja na maeneo ya pembezoni, Serikali imekamilisha usanifu wa mradi wa maji wa Mkinga kwa kutumia chanzo cha maji cha Mto Zigi mwezi Machi, 2022. Aidha, taratibu za kupata mkandarasi zinaendelea na anatarajiwa kuanza kazi mwezi Juni, 2022 na utekelezaji utaendelea katika mwaka wa fedha 2022/2023.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA aliuliza: -

Je, ni lini kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Mabokweni – Maramba – Daluni – Bombomtoni – Magoma – Korogwe utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dustan Luka Kitandula, Mbunge wa Mkinga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania imeanza na inaendelea na kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami kwa Barabara ya Mabokweni – Bombomtoni – Mashewa – Magoma – Kwamndolwa hadi Old Korogwe urefu wa kilometa 127.69. Kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ilianza mwezi Agosti, 2022 na inatarajiwa kukamilika mwezi Septemba, 2023, ahsante.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA aliuliza:-

Je, ni lini Wananchi wa Kata ya Bosha na Mhinduro watapata maji salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dunstan Luka Kitandula, Mbunge wa Jimbo la Mkinga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha usanifu wa Mradi wa Maji wa Mhinduro utakaohudumia Kata za Bosha na Mhinduro na ujenzi utaanza mwezi Juni, 2022 na kukamilika katika mwaka wa fedha 2022/2023.