Supplementary Questions from Hon. Dunstan Luka Kitandula (41 total)
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa na mimi niuliza swali la nyongeza. Mji wa Maramba una tatizo kubwa sana la kukatika kwa umeme kama ilivyo Mji wa Korogwe. Je, Waziri atatuhakikishia kwamba katika mipango hiyo anayoizungumza ina-consider vile vile Mji wa Maramba?
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la kukatikakatika umeme, sababu mojawapo ni miundombinu kuwa inasafirisha umeme mdogo ambao haulingani na matumizi. Kwa hiyo, project kubwa kabisa ambayo tuna nyingine tunaizindua mwezi wa tisa ni kutoka kwenye miundombinu inayosafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 220 kwenda 400.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ndugu zangu wa Tanga, hii inatoka Dar es Salaam inapita Tanga ikielekea Arusha halafu kuna nyingine inatoka Iringa, Dodoma kuelekea Shinyanga. Ni lazima tuwe na umeme mwingi ndiyo tutakomesha ukatikaji wa umeme mara kwa mara na hilo tatizo linatatuliwa. Ahsante.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa hali ya kukamilika kwa vigezo vya kupandisha hadhi miji yetu kule Namanyere iko sawa sawa na kule Maramba ambapo tumetimiza vigezo vya kupata mji mdogo tangu kabla Mkinga haijawa Wilaya. Je, ni lini Mji wa Maramba utapewa hadhi ya kuwa Mji Mdogo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli hawa wenzetu walikuwa na maombi yanayogusa sehemu mbili; walikuwa wanaomba hii Maramba iwe mji mdogo, lakini walikuwa wanaomba eneo hili la Mkinga. Naomba nimwambie Mheshimiwa Mbunge, nadhani maombi haya yamepita muda mrefu sana. Sasa nimwombe na nimwagize Mkurugenzi na timu yake kule Halmashauri wakishirikiana naye kwa sababu kulikuwa na maombi haya na muda mrefu sana umepita, waanze huu mchakato vizuri ilimradi itufikie Ofisi ya Rais, TAMISEMI, mwisho wa siku vile vigezo vikiwa vimefikiwa hatutosita kuhakikisha eneo hili linapandishwa hadhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nimwagize Mheshimiwa Mbunge na wengine wote, maana yeye ni rafiki yangu tupo humu ndani. Namwambia Mkurugenzi na timu yake yote waanze huu mchakato sasa vizuri ilimradi hili jambo lifike Ofisi ya Rais, TAMISEMI na wataalam wetu waende kuhakiki kwa ajili ya vigezo hivyo
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Umuhimu wa kimkakati wa daraja la Wami kwa maana ya usalama wa nchi yetu na uchumi wa Taifa letu unafanana sana na umuhimu wa kimkakati wa barabara ya Mabokweni - Maramba - Bombo Mtoni - Mlalo -Same kwa maana ni barabara inayopita kwenye maeneo ambayo ni mpakani, kwa hiyo, ina umuhimu wa kiusalama. Vilevile ni barabara ambayo inaunganisha mbuga za wanyama na inaunganisha Mkoa wa Tanga na Mkoa wa Kilimanjaro. Je, Serikali kwa umuhimu ule ule wa kimkakati, ipo tayari sasa kuijenga kwa kiwango cha lami barabara hii?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni bahati mbaya kwamba Mheshimiwa Mbunge alipofika ofisini kuleta tatizo la barabara hii au tuseme umuhimu, changamoto ya barabara hii, tuliongea lakini hatukumalizia kwa sababu kulikuwa na mambo mengine yalituvuruga. Mimi naomba sana tukae tena tumalizie ile kazi ya kuijadili hii barabara kwa undani tukiwashirikisha wataalamu wetu ili hatimaye tuwatendee haki wanaotumia hii barabara.
MHE. DUSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri ningependa kujua tumeshuhudia vituo hivi vikijengwa lakini baada ya muda mfupi matumizi yake yanakuwa yamepitwa na wakati kwa sababu inahitajika kujenga eneo kubwa zaidi. Sasa swali kwa nini Serikali isiwe inafanya tathmini ya kina kujua mahitaji halisi ili kukwepa gharama ya kurudia ujenzi mara kwa mara?
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, katika barabara hizi bado wananchi wamekuwa wana malalamiko kwamba fidia wanayopewa inachukua muda mrefu sana kukamilika kama ilivyo kwa barabara ya Tanga - Horohoro, ambayo mpaka leo bado kuna watu wanadai. Je, ni lini Serikali itahakikisha watu hawa wanalipwa stahili zao?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kubadilika matumizi ya eneo la Mizani na kwamba ujenzi tunapoanza tunajenga eneo dogo na baadaye tunalazimika kubadilisha naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ombi lake tumelipokea na nitawataka watu wa TANROADs mikoa yote kuhakikisha kwamba wanapopanga matumizi ya vituo hivi wasiangalie muda mfupi waangalie muda mrefu ni afadhali kutumia gharama nyingi mara moja kuliko gharama kidogo, halafu tunaendelea kurekebisha kila mwaka. Kwa hiyo, tunamshukuru nimepokea ombi lake tutalifanyia kazi.
Kuhusu suala la stahili kwa watu ambao wanatakiwa kufidiwa katika maeneo haya, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge ni nia ya Serikali kuwalipa fidia watu wote wanaostahili katika maeneo yote. Lakini lazima tukiri kwamba ili tuweze kulipa fidia lazima tuwe na uwezo sasa kwa mfano unaweza ukalipa fidia, lakini ukachelewa kuanza kujenga, unaweza ukaanza kujenga watu wanaanza kutumia barabara na baadaye ukalipa fidia kadiri uwezo unapopata.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiria hii njia ambayo Serikali inaitumia, ni njia sahihi, kwanza tuwape huduma watu, baada ya hapo tuendelee kutafuta fedha za kuwalipa fidia na mara fedha zitakapopatikana nakuhakikishia watu hawa watalipwa fidia.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii. Hali ya migogoro iliyoko Serengeti na vijiji vya Ngorongoro inafanana na hali iliyopo katika Wilaya yangu ya Mkinga eneo la Kimuni katika mpaka wetu na Kenya na Pori Tengefu la Umba na Mbuga ya Mkomazi. Wananchi kwa muda mrefu wameomba mgogoro huu ili utatuliwe eneo lile litangazwe kuwa WMA lakini kwa muda mrefu hatujapata majibu, nini suluhisho la jambo hili na Waziri anatuambia nini?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitoe wito kwa Waheshimiwa Wabunge wote ambao wanaishi kwenye maeneo yanayopakana na hifadhi kila mmoja kwa wakati wake tuweze kupata nafasi ya kuwasiliana ili tuweze kuangalia maeneo yake ambayo anaona yana mgogoro ni kweli yameorodheshwa kwenye orodha ninayoizungumzia ambayo imetayarishwa na Serikali. Hilo la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kujibu swali mahsusi la Mheshimiwa Dunstan Kitandula kuhusu eneo la Kimuni, Umba, Mkomazi na hasa kuhusiana na suala la maombi ambayo wameyaleta Serikalini kwa ajili ya kuundwa kwa WMA. Ni kweli WMA inaundwa kwa makubaliano baina ya wananchi wa eneo linalohusika na Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii. Sasa nimpe tu comfort Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kuwa suala hili ni mahsusi itakuwa ni vigumu kukumbuka maombi haya kama yameshatufikia tayari na yako kwenye status gani kwa sasa, nimuombe baada ya kikao hiki mchana tuweze kuwasiliana kwa sababu wakati huo mimi nitakuwa nimewasiliana na ngazi zinazohusika ili kuweza kupata uhakika zaidi ya majibu ya status au hatua gani imefikiwa kuhusiana na maombi ya WMA kwenye maeneo anayoyazungumzia.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana
kwa kunipa fursa hii ili niulize swali moja la nyongeza. Kwa kuwa Serikali iliwahi
kutoa orodha ya Wilaya za kipaumbele za ujenzi wa vyuo vya VETA na katika
orodha ile Wilaya ya Mkinga ilikuwa ni miongoni mwa Wilaya hizo. Je, ni lini sasa
Serikali itatekeleza ahadi yake ya kujenga chuo kile kule Mkinga?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu
Spika, ni kweli Serikali inatambua hilo na hata tunapojibu maswali ya VETA
tunajua tutapambana nna swali la Mkinga. Nimfahamishe tu kwamba katika
vipaumbele vya Serikali bado Mkinga iko pale pale. Tukipata fedha tunaamini
kwamba tutatekeleza.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Zaidi ya nusu ya Vyama vya Ushirika nchini havijafanyiwa ukaguzi kazi ambayo ilipaswa kufanywa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika. Kutokana na uwezo mdogo wa Tume yetu wa kifedha na watendaji tumeshindwa kufanya hivyo. Serikali ina mkakati gani wa kuiwezesha Tume ya Ushirika iweze kufanya kazi yake kikamilfu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge kwamba kumekuwepo na changamoto ya kufanya ukaguzi kwenye Vyama vyote vya Ushirika. Kwa sasa Wizara na Tume ya Ushirika imejipanga kuhakikisha kwamba katika mwaka unaokuja wa fedha Vyama vyote vya Ushirika vinakaguliwa, lakini zaidi kuweka mfumo ambapo utaratibu wa ukaguzi utakuwa unafanyika mara kwa mara bila kukosa.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya Skimu ya Umwagiliaji ya Ulumi inafanana sana na Skimu ya Umwagiliaji ya Mwakijembe. Mwaka 2010 Serikali ilitumia shilingi bilioni 1.2 kujenga Skimu ya Umwagiliaji ya Mwakijembe, lakini bahati mbaya sana skimu ile mifereji haikujengewa wala hakuna bwawa lililojengwa kuvuna maji. Matokeo yake, leo hii tunapozungumza its hardly 10 percent ya mradi ndiyo imetumika. Nini kauli ya Serikali kuhakikisha skimu ile inafanya kazi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa, ndiyo maana Serikali kwa kupitia msaada wa Serikali ya Japani sasa hivi mhandisi mshauri anapita nchi nzima ili kubaini matatizo ya miradi ya umwagiliaji ambayo imefanya efficiency ya miradi ya umwagiliaji isiwe nzuri. Ni kweli kabisa kwamba miradi mingi imejengwa lakini imekuwa na matatizo kwamba inalimwa mara moja tu, kipindi cha masika, baada ya hapo kilimo hakuna, kunakuwa hakuna maana. Ndiyo maana mpango huu unaoendelea wa mwaka 2002 kupitia miradi yote ya umwagiliaji kubaini shida ni nini ndipo tutagundua kwamba kumbe skimu zilijengwa lakini hazina maji kwa hiyo tuna mpango wa kujenga mabwawa. Lakini tusubiri ripoti ya wahandisi washauri, watakapokuwa wameikamilisha ndipo tutaendelea sasa kurekebisha mapungufu yote ili miradi hii iweze kufanya kwa uwezo mkubwa ule unaotarajiwa.
MHE. DUNSTAN. L. KITANDULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Serikali ilihaidi kwamba Kata ya Mwakijembe ambayo iko mpakani na Kenya vijiji vyake vilisahaulika lakini kuna umuhimu wa kiulinzi vijiji vile kupata umeme. Serikali ilihaidi kwamba kabla mkandarasi hajaondoka kufanya survey wataagizwa ili jambo hilo lifanyike. Je, ni lini jambo hili litakamilika?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kata anayoitaja Mheshimiwa Mbunge ya Mwakijembe ni kata ambayo iko mpakani, laikini kama alivyosema aliliwasilisha ombi lake hilo. Kwa kutambua umuhimu wa maeneo ambayo yako mpakani suala lake linashughulikiwa na mkandarasi wa Mkoa wa Tanga katika maeneo ambao Wilaya ya Mkinga na Wilaya zinginezo ni Delimiki Electric Company Limited yupo site anaendelea na hiyo kazi. Kwa hiyo nimtoe wasi wasi Mheshimiwa Mbunge, kwamba Serikali inashughulikia. Na kwa kuwa nia yetu ni kusambaza umeme katika maeneo yetu hilo jambo litafanikiwa, ahsante.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa miaka kumi mfululizo ulimwenguni sekta inayokua kwa kasi katika sekta ya kilimo ni sekta ya samaki. Serikali ipo tayari sasa kuwasaidia wavuvi walioko Ukanda wa Pwani kuondokana na umaskini kwa sababu sekta hii imeonekana ni sekta inayokua kwa kasi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iko tayari kuwasaidia wavuvi kusonga mbele.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Barabara ya Tanga – Mabukweni – Malamba – Bombo Mtoni – Mlalo mpaka Same ni barabara inayounganisha Mkoa wa Tanga na Mkoa wa Kilimanjaro; na kwa mara kadhaa barabara hii imeahidiwa kujengwa kwa kiwango cha lami. Ni lini sasa barabara hii itajengwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe Mheshimiwa Dunstan Kitandula tukutane ofisini na wataalam ili tuweze kujadili kwa kina suala hili ili huu usumbufu usiendelee, tuwe na lugha moja kati yetu sisi wataalam katika kuhakikisha kwamba wananchi na hasa wa Jimbo la Mkinga wanaotumia barabara hii waondokane na adha ambazo wanazipata kwa sasa. Nikuombe tukutane na wataalam, Katibu Mkuu pamoja na watu wa TANROADS tulijadili kwa kina na hatimaye tupate majibu sahihi na majibu ambayo wote tutakuwa tunaelewa kwa pamoja na hatimaye tuchukue hatua.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Tatizo la maji la Songea linashabihiana na kwa kiasi kikubwa na tatizo la maji katika Wilaya ya Mkinga. Hivi karibuni tumewasilisha taarifa ya Maafa kwa kuharibika mabwawa takribani saba katika Wilaya ya Mkinga na kwamba watu wanashida kubwa ya maji. Je, ni nini kauli ya Serikali kwa tatizo hili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na uharibifu mkubwa ulioharibu miundombinu ya maji Mkoa wa Tanga kutokana na mvua, Mheshimiwa Mbunge nimuahidi kwamba, ni kweli taarifa niliipokea ambayo imeandikwa kwenda upande wa maafa na mimi ninayo, lakini kabla hatujachukua hatua, basi baada ya Bunge tu naomba mimi na yeye mguu kwa mguu, twende nikajionee kule na nitakuwa na wataalam ili tuweze kuona sasa tutafanya nini. (Makofi)
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza swali dogo la nyongeza:
Mheshimiwa Naibu Spika, Taifa letu linakabiliwa na tatizo kubwa ambalo kimsingi ni janga la utapiamlo na lishe iliyopitiliza, hii lishe iliyopitiliza ndiyo chimbuko sasa la magonjwa kama kisukari na magonjwa ya moyo.
Je, Serikali ipo tayari kwa maksudi kabisa kuandaa semina kwa Bunge zima ili Wabunge hawa wakielimika iwe chachu ya kutoa elimu kwa jamii nchini?(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Kitandula ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Wabunge, Masuala ya Lishe, kwa kusimamia vizuri masuala ya lishe.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tumekuwa na changamoto kubwa sana ya utapiamlo pamoja na suala la lishe iliyopitiliza ambayo kwa lugha ya kitaalam tunaita viribatumbo (obesity) na sisi kama Serikali tumeweka mkakati ambao ni jumuishi na ambao ulizinduliwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu mwaka jana, ambao unashirikisha sekta zote kuhakikisha kwamba tunajenga Tanzania yenye lishe. Wizara tupo tayari kutoa semina kwa Wabunge ili kuwajengea uwezo na uelewa na wao kwenda kusemea masuala ya lishe na viribatumbo katika jamii wanazotoka.(Makofi)
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Hali ya ahadi kwa barabara za Dar es Salaam inafanana sana na ahadi ya barabara ya Tanga - Mabokweni - Maramba - Bombo Mtoni - Kitivo hadi Same ambapo barabara hii ilikuwa kwenye mpango wa kujengwa kwa kiwango cha lami kupitia fedha za MCC II, lakini mradi ule ukashindikana. Sasa ni lini Serikali itaanza usanifu wa barabara hii ili iweze kujengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge, najua suala la barabara hii ya Tanga - Maramba Mawili- Bombo Mtoni kupanda mpaka kwenda upande mwingine tunakwenda Same na upande mwingine tunapita Lushoto, barabara hii nimeipita nimeiona.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile ilikuwa kwenye mpango hauku-mature nimwombe tu Mheshimiwa Mbunge na mara nyingi nampa feedback kwamba tunaitazama sasa ili tuone namna bora ya kuweza kuitengeneza barabara hii muhimu. Wananchi wa Maramba kwa kweli barabara hii nilipita niliiona wana shauku kubwa sana ya barabara hii. Mheshimiwa Mbunge naomba avute subira na nitaendelea kumpa mrejesho namna tunavyoweza kujipanga kuitengeneza barabara hii.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, majibu haya hayaridhishi hasa ukizingatia kwamba ahadi hii ya Serikali ni ya muda mrefu takriban miaka saba sasa. Pale Mkinga tunategemea uwekezaji mkubwa sana wa kiwanda kikubwa cha cement, uwekezaji wa takriban dola bilioni tatu. Uwekezaji ambao utavutia takriban viwanda 11. Sasa kwa muktadha huo, nini mkakati wa Serikali wa kuleta Chuo cha Ufundi pale Mkinga ili vijana waweze kupata stadi zitakazowawezesha kuingia kwenye uchumi huu wa viwanda? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wenzetu wa Singapore kwa kutambua changamoto ya ajira katika nchi yao, wametumia mfumo ambao umewawezesha kuondoka kwenye tatizo, mfumo wa ku-link mafunzo ya VETA na maeneo ya kimkakati ya uzalishaji (industrial park) je, Serikali iko tayari kujifunza kutoka kwa wenzetu ili tuondokane na tatizo tulilonalo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naelewa sana Mheshimiwa Kitandula anaposema jibu langu la msingi halijamridhisha kwa sababu kwa kweli kwa miaka mitatu sasa amekuwa kila wakati yupo Wizarani akifuatilia ujenzi wa VETA ya Wilayani kwake Mkinga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kupitia Bunge lako Tukufu nimhakikishie Mheshimiwa Kitandula kwamba tayari mchakato wa kujenga Chuo cha VETA Mkinga umefikia katika hatua za mwisho. Serikali kwa kushirikiana na kampuni ya Dubai inayoitwa Planet Core iko katika hatua za mwisho za kuingia mkataba wa PPP ili waweze kujenga vyuo kumi nchini kikiwepo Chuo cha VETA cha Mkinga. Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba awe na subira kidogo tu kwa sababu kile ambacho amekuwa akitafuta kwa muda mrefu sasa kiko mbioni kutekelezwa. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ya kuuliza swali moja dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Skimu ya Mwakijembe ambayo imetumia fedha nyingi kujengwa, zaidi ya shilingi bilioni moja, mpaka leo hii haijakamilika kwa kukosa mifereji ya umwagiliaji lakini vilevile kukosa bwawa na sasa tunashuhudia maeneo ya wananchi yakichukuliwa na Jeshi bila fidia yoyote. Je, Waziri yuko tayari kuja kufanya ziara mahsusi Jimboni Mkinga ajionee hali hii ili kuweza kutatua tatizo linaloikabili skimu ile?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishie kaka yangu, Mheshimiwa Dunstan Kitandula, mimi kama Naibu Waziri wa Maji nipo tayari.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya mwaka huu tumetenga fedha kwa ajili ya kufanya usanifu wa Mradi wa Kupeleka Maji Makao Makuu ya Wilaya ya Mkinga kutoka Mto Zigi kuelekea Horohoro lakini mpaka sasa hakuna dalili yoyote ya jambo hili kufanyika. Ni lini usanifu huu utaanza?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Mkinga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba usanifu huo utaanza mara moja, tunajipanga kuhakikisha kwamba tunatafuta wataalam ili wakafanye kazi hiyo.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, hali ilivyo Chemba inafanana vilevile na kule Mkinga. Tunaishukuru Serikali katika kipindi hiki imetuwezesha kuanzisha sekondari za kidato cha tano na sita kwa Shule ya Mkinga Leo na Maramba Sekondari. Shule hizi zinakabiliwa na tatizo kubwa sana la maji na kukamilika kwa vyumba vya madarasa na mabweni. Je, nini kauli ya Serikali kuwezesha kukamilika kwa nia njema hii ya kuwa na sekondari za A-Level ili ziweze kutoa elimu stahiki kama walivyokusudia?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda sana nimpongeze Mheshimiwa Jumaa Aweso kwa majibu yake mazuri. Pengine hakumalizia tu kwamba Wizara ya Maji na Umwagiliaji inakamilisha mchakato wa mwisho kabisa wa kupata dola milioni 350 ambazo ndani yake kuna programu nzuri sana ya kupeleka huduma za maji katika shule za sekondari na za msingi zote nchini ambazo hazina huduma ya maji, pamoja na hizo alizotaja Mheshimiwa Kitandula, Shule za Maramba ambayo ni shule ya zamani sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimhakikishie kwamba tumeshatoa agizo kwa Wakurugenzi wa Halmashauri wote akiwemo Mkurugenzi wake, kuhakikisha kwamba shule ambazo wamezipangia kwamba zitaombewa kibali ziwe kidato cha tano na sita wanaweka kipaumbele cha haraka ili kusudi miundombinu yake iweze kukamilika, maombi yake yaweze kufikishwa Wizara ya Elimu ili zipate kibali ili angalau mwakani ziweze kuanza kuchukua vijana wa kidato cha tano na sita.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza swali moja la nyongeza. Wilaya ya Mkinga, Muheza, Korogwe na Lushoto ni maeneo ambayo yanalima kwa wingi mazao ya spices, lakini kwa muda mrefu maeneo haya yamekabiliwa na changamoto ya ukosefu wa huduma za Ugani, masoko duni ya bidhaa hizi na vilevile mazao haya kuuzwa kwa bei ya chini sana. Je, Waziri yuko tayari na wataalam wake kuja kwenye maeneo haya kujionea hali halisi ili kuweza kuondoa changamoto zinazowakabili wakulima wetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Dunstan Kitandula kwa namna anavyofuatilia masuala ya spices kwa niaba ya wakulima hapa nchini ikiwemo Jimboni kwake. Nimeshamhakikishia kwamba Serikali kwa kutambua kwamba spices hizi zina potential kubwa ya kutuingia fedha za kigeni, niko tayari kwenda Mkoa wa Tanga na kufika maeneo ambayo ameyataja kuhakikisha wakulima hawa tunawasaidia kwenye upande wa kuzalisha kwa tija.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo tunawasaidia kwenye mambo ya branding na mikakati ya kimasoko ili kilimo chao kiweze kuwasaidia kuwakwamua kutoka kwenye umaskini, lakini uzalishaji wao usaidie kuchangia kwenye fedha za kigeni za nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. (Makofi)
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza:-
Mheshimiwa Spika, nianze kwa kueleza masikitiko yangu kwa jinsi ambavyo wataalam wetu wanawapotosha Mawaziri wetu. Eneo tunalolizungumzia ni sehemu ya skimu ya umwagiliaji inayogusa vijiji vitatu katika Kata ya Mwakijembe yenye ukubwa wa takribani hekta 450 na tayari Serikali imetumia zaidi ya shilingi bilioni 1.2 kuendeleza skimu hii. Kwa hiyo, siyo kweli kwamba sehemu tunayoizungumzia ilikuwa ni shamba darasa isipokuwa ni sehemu ya skimu ya umwagiliaji.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, eneo lililochukuliwa siyo hekari moja kama inavyozungumziwa bali ni takribani hekari 50, watu takribani 28 wamekumbwa na kadhia hii. Kwa sababu Waziri amepotoshwa, je, yupo tayari kuja kujionea yeye mwenyewe kule Mkinga ili wananchi hao watendewe haki?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa jambo hili nimekuwa nikilizungumza mara kwa mara hasa kwenye michango yangu ya maandishi nimekuwa nikitoa na takwimu ya uonevu huu na mara ya mwisho nilisema ni watu 14 na hii ilikuwa mwaka jana sasa imeongezeka wamekuwa watu 28 na sasa ni hekari karibu 50 zimechukuliwa. Je, Waziri yuko tayari kutoa tamko hapa la zuio kwamba kikosi kile kilichopo kule kiache tabia hii ya kuchukua ardhi ya wananchi bila ridhaa ya kijiji?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa takwimu zilizopo katika Wizara yangu na zile anazotoa Mheshimiwa Mbunge zinapishana, nadhani ni busara tukafanya kile alichoomba kifanyike nacho ni mimi kufanya ziara katika eneo hilo ili kukagua kwa pamoja kati ya upande wetu sisi kama Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa tukifuatana na wataalam wa Jeshi pamoja na watu wa Wilaya na Kijiji husika ili tuthibitishe ukubwa wa eneo lililochukuliwa na nani anayewajibika kulipa fidia. Endapo itathibitika kwamba Serikali kwa upande wetu Wizara ya Ulinzi inalazimika kulipa fidia basi tutafanya hivyo.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Mwenyekiti ninakushukuru, ninaomba niulize swali dogo moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ipo kwenye hatari kubwa la kupoteza fedha takribani shilingi bilioni moja na milioni 600 kutokana na mkandarasi wa Mradi wa Mbuta kuvunja mkataba, lakini vilevile mkandarasi wa Mwakijembe kuamua kusimama kufanya kazi kwa sababu ya uchelewashaji wa fedha.
Ni lini Serikali itachukua hatua za haraka kuhakikisha inaokoa fedha hizi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kaka yangu Dastan Kitandula kwa kazi kubwa ambayo anaifanya katika jimbo lake pale Mkinga.
Mheshimiwa Mwenyekiti sisi kama Wizara ya Maji tulishasema kwamba hatukuwa na kisingizio chochote, kwamba sasa hivi mmetupa rungu kwa maana uazishwaji wa RUWASA kwa maana Wakala wa Maji Vijijini na tumejipanga vizuri kwa maana agizo la Mheshimiwa Waziri kwa maana baadhi ya miradi ya tutaifanya kwa kutumia wataalamu wetu wa ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kumhakikishi katika Mkandarasi yule aliyeondoka site hatuna nafasi tena ya kubembelezana ile kazi tutaifanya kupitia wakala wetu wa maji kwa maana ya Uchimbaji wa Maji Visima (DDCA) nawaagiza waende kuifanya kazi ile mara moja ili wananchi waweze kupata maji. Lakini kuhusu mkandarasi ambaye ametekeleza mradi hajalipwa certificate, nataka nimhakikishie ndani ya mwezi huu wa tisa tutamuweka katika orodha ili kuhakikisha kwamba tunamlipa ili wananchi waendelee kutekelezewa mradi wa maji, ahsante sana.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, na kama ulivyosema, ni kweli kwamba swali hili ni la muda mrefu. Kwa kuwa wananchi wa Mkinga wanazo taarifa kwamba mtaalam huyu amekwishapatikana tangu mwezi Novemba, na ilikuwa waingie mikataba lakini yakawa yanafanyika majadiliano yaliyokuwa na lengo la kupunguza scope ya kazi kwa vijiji vile 37, jambo ambalo limeleta taharuki. Je, Waziri yuko tayari kutuhakikishia kwamba hayo majadiliano hayatapunguza wigo ambao utawahakikishia wananchi wa Mkinga vijiji vile 37 vyote vipate maji? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa mradi wa Horohoro umepigiwa kelele sana kwa muda mrefu na sasa unakwenda kutimia, kutekelezwa, na mwezi wa sita sio mbali. Je, Waziri yupo tayari mwezi wa sita utakapofika atoe ahadi kwamba ataandamana na mimi kwenda kuweka msingi wa kuanza ujenzi wa mradi ule kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kiukweli nitumia nafasi hii, dhati ya moyo wangu kwanza kumpongeza Mheshimiwa Mbunge, amekuwa mfuatiliaji mkubwa sana si kuchangia tu Bungeni lakini hata ofisini amekuwa akija mara kwa mara kuhusu suala zima la mradi huo.
Mheshimiwa Spika, sisi kama viongozi wa Wizara tulikwishasema kwamba hatutakuwa kikwazo kwenye utekelezaji wa miradi ya maji. Wakati mwingine tunatumia muda mrefu sana kwa kuwatumia wakandarasi wetu, sisi kama viongozi tumejadiliana tumeona haja sasa kazi zile zifanywe na wataalam wetu wa ndani ili kuhakikisha kwamba hii kazi inafanyika kwa haraka na wananchi wake waweze kupata maji safi na salama katika kuhakikisha kwamba tunamtua mama ndoo kichwani.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, pamoja na majibu mazuri ya Wizara ambayo yanatupa matumaini, nina maswali mawili ya nyongeza:-
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa survey iliyofanyika Hemsambia ilifanyika kwa vitongoji viwili na kuacha vitongoji vingine vitano. Je, Waziri anatuthibitishia kwamba, kwa azma ile ya kuhakikisha kwamba, kila kijiji kinapofikiwa lazima kijiji chote kipate umeme; Je, vitongoji hivi vitajumuishwa kwenye kupatiwa umeme?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, wakati tunapeleka umeme kwenye Kata ya Bosha maeneo ya Vitongoji vya Miyongwe, Kwemsakazi, Kwashemwaondwa na Kibago B yalirukwa, lini maeneo haya yatapatiwa umeme?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya swali la msingi la Mheshimiwa Kitandula, lakini pia nimpongeze sana Mheshimiwa Luka Kitandula, Mbunge wa Mkinga na pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Nishati.
Mheshimiwa Spika, katika maswali yake mawili ya nyongeza kwanza ni kweli, kwenye Kijiji cha Hemsambia tulifanya survey vitongoji viwili na tukabakiza vitongoji vitano ambavyo tayari wakandarasi tumeshaviingiza kwenye
marekebisho na yanafanyiwa kazi. Na hivi sasa Mheshimiwa Mbunge, pamoja na kupongeza, tulipokuwa katika jimbo lako wiki iliyopita tulitoa maelekezo na wakandarasi wameshaanza kuyafanyia kazi. Kwa hiyo, niwape taarifa tu Wananchi wa vitongoji vitano vya Kijiji cha Msambia kwamba, vitongoji vyote katika kijiji hicho vitafanyiwa kazi na vitakamilika mwezi Septemba mwaka huu.
Mheshimiwa Spika, katika swali la msingi la pili la Mheshimiwa Mbunge, ni kweli tunazo kata tano muhimu sana kwa Mheshimiwa Mbunge, lakini Kata ya Bosha yenye vijiji vinne vikiwemo Kijiji cha Kwashemhonda, pamoja na Kwesekazi, pamoja na Kibango vimeshaanza kufanyiwa kazi na Shirika la Umeme – TANESCO kwa sababu, sasa hivi bei ni ileile 27,000/=. Na jana tumewasiliana na Mheshimiwa Mbunge alikuwa kufuatilia na TANESCO pamoja na wataalamu wameshaingia site kuanzia leo. Kwa hiyo, ni matumaini yetu Mheshimiwa Mbunge na Wananchi wa Mkinga muwe na matumaini kwamba, Kata na Vijiji vyote vya Bosha vinakwenda kupatiwa umeme mwisho wa mwezi Disemba mwaka huu.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naishukuru Wizara kwa majibu haya. Swali la kwanza; kwa kuwa taratibu hizi za Ilani zimekwisha kukamilika na kwamba mmiliki huyu anatumia ardhi isivyo stahili. Je. Waziri anatuambia nini kwa kuwa taratibu hizi zimekamilika ni lini sasa hati ya mashamba haya zitafutwa baada ya kupelekwa kwa mamlaka ya Mheshimiwa Rais? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa barua ya mapendekezo ya kufuta hati ya shamba hili yalizungumzia vile vile Shamba la Mwele ambalo, Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokuja kutembelea Mkinga alitoa maagizo kwamba, ardhi ile imegwe kutoka kwenye shamba la Serikali kwa sababu, limetelekezwa kwa zaidi ya miaka 20. Je. Waziri yupo tayari kufuatilia jambo hili ndani ya Serikali ili agizo lile la Waziri Mkuu liweze kufanyiwa kazi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza amezungumzia kwamba taratibu zile zinazotakiwa kufuatwa katika ubatilishwaji zilishakamilika. Naomba kukiri ni kweli kwasababu barua ya ubatilisho ilitoka tarehe 10 Machi, 2020 maana yake kufikia Juni, 2020 tayari utaratibu ule ulikuwa umekwisha. Lakini wakati huo huo mmiliki huyu alileta utetezi wake akitetea kwamba asiweze kunyang’anywa kwasababu alizokuwa amezilieleza. Lakini baada ya kuangalia pia ilionekana kwamba miliki ile ilikuwa imewekezwa kama dhamana kama nilivyojibu kwenye swali langu la msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Lakini hiyo pia haituzuii kama wizara tumetoa maelekezo kwenye halmashauri kwasababu ile hati imeshawekwa dhamana katika Benki, na Benki yenyewe ni Benki ya Nje kwa hiyo tumeshaelekeza na tayari wamekwisha toa ilani kwa ajili ya kubatilisha tena wamempelekea na yule mmiliki wa Benki ili ajue kwamba dhamana aliyonayo kisheria kwa sheria za Tanzania sasa haitakiwi iwe kule kama ambavyo inapaswa.
Kwa hiyo, tunasubiri hizi siku zikiisha basi tutaweza kufanya kile ambacho kinatakiwa kufanywa kisheria na watu wa Halmashauri ya Mkinga wataweza kufaidika na lile shamba. Namuomba tu Mheshimiwa Mbunge basi awe na subira katika hilo kwasababu tayari taratibu zinafanyika na ilani imekwishatumwa kwenye ile Benki ya Nje pamoja na kwa mmiliki.
Mheshimiwa Naibu Spika, Swali lake la pili anaongelea suala Mweru ambalo lilikuwa na maelekezo pia ya Waziri Mkuu. Kwanza nichukue fursa hii pia kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Dunstan Kitandula kwasababu amekuwa akifuatilia sana. Nakumbuka hata mwaka jana, mwaka juzi kuna shamba la MOA alilipigia kelele taratatibu zilifuatwa likabatilishwa na wakaweza kupewa na sasa wananchi wanalitumia kwa mujibu wa waliyoelekeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika hili naomba nimuhakikishie kwamba, tutachukua speed isiyo ya kawaida tunahakikisha kwamba tunafanya ufuatiliaji na kama umemsikia pia Mheshimiwa Rais wetu wa Awamu ya Sita amesema hana mzaha na wale ambao wana hodhi ardhi bila ya kuzitumia.
Mheshimiwa Naibu Spika, Na sisi kwa kasi ile ile tutaendelea mbali na hilo shamba la Mweru tutaangalia pia na mashamba mengine katika maeneo mengine ambayo wameyahodhi ili tuweze kuchukua hatua stahiki na yaweze kutumika kwa matumizi ambayo yataleta faida kwa wananchi lakini kwa Taifa kwa ujumla. Ahsante.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii imekuwa ikiahidiwa na Marais watatu waliopita. Je, Serikali haioni kwamba kutotekelezwa kwa ahadi za Marais wetu watatu ni kipindi kirefu sana? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; tunaishukuru Serikali kwamba kwa kipindi hiki sasa imetenga bilioni moja kwa ajili ya upembuzi yakinifu na usanifu. Je, Serikali inatuhakikishia kwamba kazi hii itaenda kufanyika na kukamilika kwa kiasi hiki cha fedha? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG.
GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dunstan Luka Kitandula, Mbunge wa Mkinga kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba barabara hii imeahidiwa na Marais watatu kama alivyosema na ni kweli ni muda mrefu, lakini nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge wa Mkinga na wananchi wa Mkinga kwamba wawe na imani na Serikali na ndiyo maana hata fedha tumeonesha kiasi ambacho tumekitenga ili kutimiza ahadi hizo za Marais na awe na imani sana na Awamu hii ya Sita inayoongozwa na Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. Naomba nimhakikishie kwamba itatekelezwa kama tulivyoahidi na tulivyopanga kwenye bajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; nimhakikishie kwamba bajeti iliyotengwa kwa maana ya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina itatosha kufanya kazi hii na kama ilivyopangwa kazi hii ya usanifu na upembuzi yakinifu itakamilika, ahsante. (Makofi)
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kata ya Mwakijembe tuna changamoto kubwa sana ya ukame. Kwa hiyo, eneo hili lililotwaliwa ndilo eneo pekee linalofaa kwa kilimo; na kwa sababu, wananchi hawa wameondolewa kwenye eneo lile.Je, Serikali iko tayari kufanya mchakato wa haraka wa kuwafidia watu hawa ili waondokane na madhila wanayoyapata sasa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili. Kwa kuwa imebainika wazi kwamba eneo hili ni hatarishi; kwa miaka miwili mfululizo yametokea mafuriko makubwa na tumewahatarisha Askari wetu kwenye eneo lile: Je, Serikali ipo tayari kuwahamisha Askari hawa kwenda kwenye eneo la awali ambalo Kamati ya Bunge ililiona ili Askari hawa wakae kwenye eneo ambalo ni salama? (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kitandula, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba, ni dhamira ya Serikali kupitia Wizara yangu kuwalipa fidia wananchi wa maeneo yote ambayo yametwaliwa kwa ajili ya matumizi ya shughuli za kiulinzi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Kitandula kama tulivyowahi pia kuzungumza, ni kwamba tunashirikiana na wenzetu Wizara ya Ardhi na Wizara ya Fedha, na yako maeneo mengi ambayo tayari tumeshalipa fidia; pia uko mpango wa Serikali kupitia Wizara ya Fedha kutupatia fedha na taratibu zikikamilika wananchi hawa nawahakikishia kwamba watalipwa mara moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili, kuona umuhimu wa eneo hili kutumika tena kwa wananchi, niseme tu kwamba, labda kutokana na changamoto za mvua nyingi tulizozipata hivi karibuni, umevutiwa pia kuona uko umuhimu wa wananchi kuendelea kufanya umwagiliaji katika eneo hili; niseme tu kwamba zile sababu za kupewa eneo hili bado zipo. Hata hivyo tunaweza tukalitazama kutokana na maoni ya Mheshimiwa Mbunge kwa sababu, iko kamati maalum ambayo inaendelea kuyapitia maeneo yote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbune kwamba, naelekeza wafanye pia marejeo katika eneo hili kwa kushirikiana na Kamati yetu ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya na pia kwa kushirikiana na Mheshimiwa Mbunge ili tuone kama pia tunaweza tuka-reallocate, tukapata eneo lingine bila kuondoa sababu muhimu za kufanya vijana wetu waendelee kufanya shughuli zao muhimu katika eneo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tu kwamba tutaendelea kushirikiana ili kuona tunaweza kutenda vema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili, kuona umuhimu wa eneo hili kutumiwa tena na wananchi, labda kutokana na changamoto ya mvua nyingi tulizozipata hivi karibuni, Mbunge amevutiwa kuona kwamba upo umuhimu wa wananchi kuendelea kufanya umwagiliaji katika eneo hili. Niseme tu kwamba, zile sababu za kupewa eneo hili bado zipo, lakini tunaweza tukalitazama kutokana na maoni ya Mbunge kwa sababu ipo Kamati Maalum ambayo inaendelea kuyapitia maeneo yote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, nimhakikishie tu Mbunge kwamba naelekeza wafanye pia marejeo katika eneo hili kwa kushirikiana na Kamati yetu ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya lakini kwa kushirikiana na Mheshimiwa Mbunge ili tuone kama tunaweza tuka-reallocate, tukapata eneo lingine bila kuondosha sababu muhimu za kufanya vijana wetu waendelee kufanya shughuli zao muhimu katika eneo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tu kwamba tutaendelea kushirikiana ili kuona tunaweza kutenda vema.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru; hali ya upatikanaji maji Wilaya ya Mkinga kwa sasa ni mbaya sana. Hivi ninavyozungumza mabwawa takribani matano yamekauka, tumeanza kuona dalili za ugonjwa wa homa ya matumbo. Sasa Wizara ilituma wataalam kufanya usanifu wa mradi mkubwa wa kutoa maji Mto Zigi kwenda mpaka Horohoro ambapo kazi hiyo inakamilika kesho. (Makofi)
Je, Serikali iko tayari kwa udharura huu kuhakikisha inaharakisha mchakato wa kupata wakandarasi, ili mradi ule uanze kushughulikiwa haraka iwezekanavyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kitandula, Mbunge wa Mkinga kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tunafahamu maji ni uhai na sisi kama Wizara ya Maji hatupendi kuwa kikwazo na kusababisha milipuko ya magonjwa. Kwa kutambua hilo kama Wizara tunamshukuru Mheshimiwa Rais aliongoza dua na sasa hivi mvua zimeanza kunyesha vizuri, mabwawa yaliyokauka tunayatarajia yarudi katika hali yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika usanifu huu unaoendelea ambao tunautarajia ukamilike kesho, tutaharakisha kuona kwamba lile bwawa ambalo linafanyiwa usanifu na maeneo yale ya Mkinga yote tunakwenda kuyafanyia kazi kwa haraka. Ninawaagiza ile timu iliyotumwa kule na Mheshimiwa Waziri ifanye kadri ya maagizo ya Mheshimiwa Waziri yaliyopo ili kuona tunaharakisha jambo hili. (Makofi)
MHE. DUSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, tija ya kilimo katika mazao haya ipo chini sana kwa sababu ya mbegu duni: Nini kauli ya Serikali katika kuwasaidia wakulima hawa kupata mbegu bora ili kuweza kuongeza tija katika kilimo chao?
Pili, Serikali iko tayari kushirikiana na Mkoa wa Tanga katika kuboresha mnyororo wa thamani wa kilimo cha mazao haya?
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kitandula kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikiri, kama nchi kwa muda mrefu tulikuwa hatujayapa kipaumbele mazao haya ya viungo. Nataka tu nilihakikishie Bunge lako tukufu, kwamba kwanza tumeya-cluster kama sehemu ya mazao ya horticulture, kwa hiyo, yatasimamiwa kwa karibu na idara inayohusika na mazao haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, tumekiagiza kituo chetu cha Mliongano kwamba kianze kufanya kazi ya utafiti na uzalishaji wa mbegu na miche kwa ajili ya mazao ya Hiliki na mazao ya viungo pamoja na mazao ya matunda ya machungwa ambayo yanalimwa kwa wingi katika Mkoa wa Tanga ili kuondoa matatizo yanayowakabili wakulima wetu na kuyapa center stage mazao haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kushirikiana na mkoa, nataka tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, tuko tayari kama Wizara ya Kilimo kukaa nao ili tujadiliane ni namna gani tunaweza kuwasaidia wakulima hawa wadogo kwenye value chain ya mazao kama ambavyo tumeamua kuwasaidia wakulima wa mkonge kwa kuwapatia makorona; na Bodi ya Mkonge itanunua makorona matatu kwa ajili ya kuwapa wakulima wadogo wa maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kama Wizara tuko tayari kukaa nao. (Makofi)
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, hivi tunavyozungumza chuo hiki hakina mkufunzi hata mmoja wala hakina Mkuu wa Chuo. Wakufunzi wanaotegemewa ni kutoka Chuo cha VETA Tanga ambacho na chenyewe kimeelemewa, kinategemewa chuo hichohicho cha Tanga kitoe wakufunzi kwenda Korogwe. Je, Serikali ina mpango gani wa haraka kuhakikisha kinapata wakufunzi ili hayo malengo ya kuanza mwezi wa Kumi yaweze kutimia? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili. Hivi tunavyozungumza vifaa vya ufundi havijapatikana kwenye vyuo hivi vya Mkinga wala Korogwe. Serikali ina mkakati gani wa haraka kuhakikisha vifaa hivi vinapatikana ili mafunzo yaweze kufanyika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba sasa kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kitandula Mbunge wa Mkinga kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza nikiri ni kweli tuna upungufu wa walimu kwenye vyuo vyetu hivi vya VETA hivi sasa tuna Wilaya 77 zenye Vyuo vya VETA vya Wilaya pamoja na mikoa. Lakini nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge katika mwaka wa fedha wa 2021/2022 Wizara imepata kibali cha kuajiri walimu zaidi ya 514. Kwa hiyo, tayari mchakato huu wa kuajiri walimu uko kwenye hatua za mwisho na tutahakikisha sasa miongoni mwa walimu hawa 514 tunaokwenda kuwaajiri basi waweze kwenda kwenye Chuo cha Mkinga lakini pamoja na vile vyuo 25 vya Wilaya pamoja na vyuo vile vinne vya mikoa ambavyo sasa nakamilisha ujenzi wake.
Mheshimiwa Spika, katika eneo la pili amezungumzia suala la vifaa vya kufundishia; ni kweli mchakato wa vifaa unaendelea kwa sababu upo kwenye bajeti 2022/2023 ambao tumeanza kuutekeleza hivi sasa na tuko katika quarter ya kwanza. Kwa hiyo, pindi fedha zitakapokuwa zimekaa tayari tunakwenda kununua hivyo vifaa na kuvipeleka kwenye vyuo hivi ambavyo tayari vimekamilika, lakini upande wa samani zote za vyuo vyote 25 viko tayari kwa ajili ya kupelekwa katika maeneo haya nakushukuru sana.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Barabara ya Mtoni - Bombo kwenda mpaka Bashewa, na barabara hiyo hiyo kutokea upande wa Maramba mpaka Tanga, usanifu wake lini utaanza? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dunstan Kitandula, Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, barabara hii ni barabara ambayo tumeitengea fedha kwa ajili ya kukamilisha usanifu wa kina mwaka huu wa fedha. Kwa hiyo, nina uhakika barabara hii mwaka huu itaanza kufanyiwa usanifu wa kina. Ahsante.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Skimu ya Mwakijembe wananchi wamekuwa wanasubiri kwa takriban miaka 14 sasa. Na kwa kuwa Bunge hili lilipitisha fedha mwaka huu kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu.
Je, Waziri yuko tayari kwenda kusimamia jambo hili ili upembuzi huo na usanifu ukamilike ndani ya mwaka huu tuliotengea fedha na mwaka ujao wa fedha kazi hii ya ujenzi iweze kuanza?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili skimu hii ilitumia zaidi ya bilioni moja na milioni mia mbili, fedha ambazo ni kama zilipotea kwa sababu skimu haijaweza kufanya kazi.
Je, Wizara iko tayari kwenda kuangalia kwa kina design itakayofanyika ili design hiyo ihusishe ujenzi wa bwawa la kuhifadhia maji na ujenzi wa mifereji ili skimu iweze kutumika kwa uhakika?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza kwa pamoja ya Mheshimiwa Dunstan Luka Kitandula Mbunge Mkinga kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikiri Mheshimiwa Mbunge amekuwa mfatiliaj mzuri wa jambo hili; na ni kweli skimu hii imekaa muda mrefu. Kulikuwa na changamoto nyingi na hasa kutokana na kwamba katika miaka mingi iliyopita tume yetu haikuwa na uwezo mzuri sana ya kuweza kuisimamia miradi hii mikubwa. Hata hivyo tumefanya mabadiliko makubwa ambapo hivi sasa tumeshamwelekeza Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kuhakikisha ya kwamba wanaipa kipaumbele skimu hii. Lengo letu kubwa ni kuhakikisha tunafanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ili changamoto zilizokuwa zinajitokeza katika miradi iliyopita zisiweze kujirudia, na ikiwemo hoja ambayo Mheshimiwa Mbunge ameisema, ya ujenzi wa mabwawa ili kuhakikisha upatikanaji wa maji wa mwaka mzima na wakulima wa eneo hilo waweze kufanya kilimo kwa mwaka mzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimwahidi Mheshimiwa Mbunge ya kwamba tutasimamia kwa ukaribu kabisa kazi hizi zifanyike mapema ili basi tutenge fedha kwa ajili ya ujenzi na wananchi waweze kunufaika na mradi huu.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ili niulize swali moja dogo la nyongeza. Jiwe la rubi lenye uzito wa kilo 2.8 lipo kwenye maonyesho kwa sasa Dubai na jiwe hili linasadikika linatoka Tanzania na kwamba siku chache zijazo kutakuwa na mnada wa kuuza jiwe hili. Je, kama nchi tunanufaika vipi na mnada huo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Kitandula, Mbunge wa Mkuranga, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli mnamo tarehe 13 Aprili, 2022 Wizara ya Madini ilipata taarifa kupitia mitandao ya kijamii kwamba kuna jiwe la madini ya rubi lenye uzito wa kilo 2.8 na ambalo linadaiwa kuwa na thamani ya dola za Marekani milioni 120, sawa na zaidi ya bilioni 240 za Kitanzania ambalo limepewa jina la Bad All Hamal na ambalo linakwenda kuwekwa mnadani ndani ya siku 30 baada ya mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhan na jiwe hilo kudaiwa kwamba limetoka Tanzania.
Mheshimiwa Spika, mara baada ya kupata habari hizi Wizara ya Maliasili imechukua hatua za haraka kutafuta kama habari hizi ni za kweli na kama kweli jiwe hili kweli limetoka Tanzania na kwa sababu jiwe hili limeshavuka mipaka liko kwenye nchi nyingine, taarifa hizi sasa tunazozikusanya ili tuweze kutoa taarifa sahihi katika Bunge lako Tukufu zinahusisha Nchi ya Dubai na tayari Ubalozi wetu uliopo Dubai na sisi tunafanya mawasiliano kufuatilia ukweli na uhalisia wa thamani ya jiwe hili. Pia baada ya ufuatiliaji wa awali tumebaini kwamba mmiliki halali au tuseme sasa wa jiwe hilo yuko nchini Marekani katika Jimbo la California na mawasiliano naye pia tumeshafanya tangu jana. Hivyo sasa suala hili linazidi kupanua wigo wake kidiplomasia kwamba linahusisha nchi tatu; Nchi ya Tanzania, Dubai na Marekani.
Mheshimiwa Spika, nikuhakikishie tu kwamba tutakapokuwa tumepata nyaraka za usafirishaji wa jiwe hili kama kweli limetoka Tanzania tukapata nyaraka zinazoonyesha thamani na asili ya hili jiwe kwamba limetoka wapi. Tutakapokuwa tumepata na nyaraka za mauzo kati ya mmiliki wa sasa na wa hapo awali, sisi tutaleta taarifa katika Bunge lako Tukufu za uwepo wa jiwe hili na kama ni la kwetu, niwahakikishie Watanzania kwamba haki yao haitapotea sheria, kanuni na taratibu zetu zitatumika kuhakikisha kwamba rasilimali hii inakwenda kunufaisha Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho, sisi Wizara ya Madini tunaendelea kuwahakikishia Watanzania kwamba tumesimama imara kudhibiti na kusimamia rasilimali madini kwa manufaa ya nchi yetu. (Makofi)
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa, naomba niulize swali moja la nyongeza. Mheshimiwa Waziri ulipokuja kutembelea mnada wa Hororo, mojawapo ya changomoto tuliyoizungumza ni ukarabati wa lambo la Ng’ombeni. Je, ahadi iko pale pale, kwamba litakarabatiwa?
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kitandula kama ifuatavyo: -
Ahadi yetu Mheshimiwa Mbunge iko pale pale, na tutafanya hiyo kazi mpaka ikamilike ikiwa ni pamoja na kukamilisha ujenzi wa mnada huo. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge kuwa na uhakika kwamba sisi kazi hiyo tulishaanza kuifanya na kwa hivyo tutaikamilisha kama ambavyo tumepanga. Ahsante sana.
MHE. DUNSTAN KITANDULA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru; naomba niulize swali moja la nyongeza. Ugawaji wa Mkoa wa Tanga ni ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano alipokuja kwenye Mkoa wa Tanga, na hii ilikuwa ni baada ya Wabunge wa Mkoa wa Tanga kumuomba kwamba jambo hili tumeshalijadili kwenye RCC.
Je, hata baada ya ahadi ya Mheshimiwa Rais bado tunatakiwa jambo hili tena kulijadili kwenye mkoa kwa mara nyingine?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dunstan Kitandula kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kadri ya majibu yangu ya jibu la msingi, kwamba kuna taratibu ambazo zipo kwa mujibu wa sheria, na Mheshimiwa Rais alitoa ahadi hiyo, na sisi ahadi hiyo na sisi ahadi za viongozi wetu, Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Makamu Rais, Waziri ni maelekezo ni maelekezo tutafanya kazi hiyo. Hata hivyo niwaombe tufuate utaratibu ule kwa kadri sheria ilivyo.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishukuru Serikali kwa majibu hayo na naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu mradi huu ndio utakuwa mkombozi kwa ukanda wote wa Pwani wa Wilaya ya Mkinga. Je, Serikali inataka kutuambia ni lini hasa mradi huu utaanza?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pili kwa kuwa Waziri anaahidi hapa kwamba mradi huu sasa unaenda kuanza, yupo tayari kuandamana nami twende tukafanye mikutano ya kuwaaminisha wananchi hawa kwamba tatizo lao sasa linaenda kuondoka?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kaka yangu Dunstan Luka Kitandula, kwa kweli hali ya upatikanaji wa maji Mkinga yalikuwa ni changamoto kubwa sana na tumefanya jitihada kama Serikali ya kuchimba visima lakini kwa jiografia ile imekuwa ni changamoto.
Kwa hiyo, maelekezo ambayo tumepata na support ya Mheshimiwa Rais ni kuyatoa maji sasa ya Mto Zigi, Tanga na kuhakikisha tunakwenda kutatua tatizo la maji katika Jimbo la Mkinga. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge sisi kama Wizara ya Maji tumetoa maelekezo itakapofika Juni mkandarasi awepo site kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huu mkubwa na historia itakumbuka wananchi wa Mkinga kwa jitihada unazozifanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini juu ya kuambatana naye, mimi niko tayari kuongozana naye katika kuhakikisha tunaenda kufanya mikutano ili tuweze kuwahabarisha wananchi juu ya utekelezaji wa mradi huu mkubwa katika Jimbo la Mkinga. (Makofi)
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu ya Serikali, naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, nyaraka za kiofisi tulizonazo kutoka Serikalini zilionesha kwamba katika barabara hii, usananifu na upembuzi yakinifu ungekamilika mwezi wa Sita lakini sasa tunaambiwa ni mwezi wa Tisa: Je, Waziri anaweza kuniambia mpaka sasa kazi iliyofanyika, imefanyika kwa kiwango cha asilimia ngapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kutokana na umuhimu wa barabara hii kiusalama na kiuchumi, Wizara ipo tayari kutenga fedha ili ujenzi uweze kufanyika kwenye lots ambazo kazi imeshakamilika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Dunstan Luka Kitandula, Mbunge wa Mkinga, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu asilimia ambayo imefikiwa, naomba baada ya kikao hiki niweze kupata taarifa kamili kwa sasa tuko asilimia ngapi? Hata hivyo nataka tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba pengine kitu muhimu hapa ni lini tutakamilisha hii kazi ambayo kwenye jibu langu la msingi nimesema kazi hii ya usanifu itakamilika mwezi Septemba. Kwa maana ya takwimu, asilimu naomba nitamjulisha Mheshimiwa Mbunge mara baada ya kutoka hapa kupata taarifa kamili.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua kwamba barabara hii ni muhimu sana kiusalama na kiuchumi na ndiyo maana tumeamua kuifanyia usanifu wa kina ili barabara hii iweze kujengwa kwa kiwango cha lami, ahsante. (Makofi)
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba niulize swali moja dogo la nyongeza.
Ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya kuwapatia skimu ya umwagiliaji watu wa Mkinga?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua kwamba lazima tufanye kilimo cha umwagiliaji ili tuweze kuleta tija kwenye kilimo. Katika eneo la Mkinga pamoja na Lushoto tumeanza kufanya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa bonde la Mto Umba ambalo lina hekta zaidi ya 5,560 na tunaamini kabisa kwamba wananchi wa eneo la Mkinga watanufaika na mradi huu mkubwa ambao unakuja kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, wananchi wa Mkinga kwenye kata 13 wamepata athari kubwa ya tembo kutoka Mbuga ya Tsavo, Kenya na Mbuga ya Mkomazi na ili kukabiliana na tatizo hilo Serikali iliahidi kuweka kituo maalum Wilaya ya Mkinga. Lini Serikali itatimiza ahadi hii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante, nimepokea maswali tisa ya nyongeza kwa Waheshimiwa mbalimbali na naomba niyajibu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la Mheshimiwa Londo; ameuliza ni nini kauli ya Serikali? Kama ambavyo nimejibu kwenye swali la msingi. Ni kwamba sasa hivi tunaangalia njia mbadala wakati huo huo tunaendelea kutatua migogoro hii ya wanyama wakali na waharibifu. Tunajenga vituo, tunaajiri VGS, lakini wakati huo huo tumeshaweka sasa mipango kwenye baadhi ya maeneo tuanze kuweka fence ya umeme ili kupunguza hii athari ya wanyama wakali na waharibifu.
Mheshimiwa Spika, kwenye suala la Mheshimiwa Anne Malecela, naomba niahidi mbele ya Bunge lako hili Tukufu kwamba baada ya Bunge hili tutaongozana naye katika maeneo yale. Lakini pia tumeshaanza kuongeza nguvu kwake, tumepeleka askari na tutaendelea kuajiri VGS katika maeneo hayo ili tuweze kushirikiana pamoja. Kwa hiyo, wananchi wa Same kilio chenu kimeshasikika Bungeni na tutaongozana na Mheshimiwa Mbunge (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwenye suala hili la Mheshimiwa Vita Kawawa, ni kweli Mheshimiwa Waziri alitoa ahadi ya ujenzi wa madarasa katika jimbo lake, na huu ulikuwa ni mpango wa CSR si kwa ajili ya fidia ya wanyama wakali na waharibifu. Ni kwamba Mheshimiwa Waziri alifanya ziara katika jimbo hilo na akatoa ahadi ya ujenzi wa madarasa ili kuwafanya wananchi wanaoishi katika maeneo hayo tushirikiane pamoja katika uhifadhi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niendelee tu kuahidi kwamba ahadi ni deni, Wizara itatekeleza. Na kwa kuwa ilikuwa ni kauli ya Mheshimiwa Waziri basi tutafuatilia ili ahadi hii iweze kutekelezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Dunstan, Mbunge wa Mkinga, yeye ameongelea kuhusu kituo; niahidi tu kwamba katika mpango wa fedha wa 2023/2024 uliopitishwa katika Bunge lako hili, tutapeleka kituo katika Jimbo la Mkinga ili tuongeze nguvu ya kudhibiti wanyama wakati na waharibifu.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Justin Nyamoga, madhara makubwa; naomba niahidi tu kwamba tutaendelea kufuatilia katika maeneo haya ili wananchi waweze kulipwa fidia inayotokana na wanyama wakali na waharibifu.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Grace Tendega; naomba tu nilitaarifu Bunge lako, na kwa ridhaa yako, nipe tu nafasi kidogo nitoe ufafanuzi. Tumekuwa na changamoto nyingine imejitokeza katika Mkoa wa Iringa; kuna uvamizi wa simba kwenye baadhi ya maeneo, lakini naomba niwataarifu wananchi, nadhani wameona juhudi za Serikali toka uvamizi huu umejitikeza tumekuwa karibu na wananchi, tunatoa elimu.
Mheshimiwa Spika, naniendelee kutoa elimu kupitia Bunge lako hili, kwamba wakati huu ambapo tunawasaka hawa simba, wananchi wawe na tahadhari ya kutotembea usiku. Lakini pia wenye mifugo wawashe moto kuzunguka maeneo yale ya mifugo ili kuepusha simba wasisogee katika maeneo hayo tunajitahidi sana kulinda maisha ya Watanzania.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niwaombe Wanairinga, Serikali iko kazini na tumeshapeleka helikopta inazunguka usiku na mchana kuhakikisha tunawasaka hawa simba. Tuendelee kushirikiana pamoja ili kuhakikisha zoezi hili tunalikamilisha na simba hawa tunawachukua na kuwarudisha katika maeneo yao.
Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la Mheshimiwa Charles, Mbunge wa Mwibara; kumekuwa na changamoto ya viboko na tembo. Naomba niendelee tu kuahidi, nakumbuka tuliwasiliana na Mheshimiwa Mbunge na tukaongeza nguvu ya askari katika maeneo hayo. Tuendelee tu kuwasiliana, nguvu tutaongeza lakini pia tutaendelea kuajiri VGS ili waweze kusaidia pale inapotokea dharura katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na ombi la Mheshimiwa Jimbo la Tunduru kwamba tuongeze VGS (askari wa vijiji). Tunaomba tulipokee hili na tutaweka priority katika eneo hili, tunajua hii changamoto ya wanyama wakali.
Mheshimiwa Spika, pia kulikuwa kuna shida moja ya mratibu ambaye alihamishwa. Nadhani maelekezo yameshatoka, atarudishwa katika eneo hilo ili aweze kushirikiana na wananchi kudhibiti wanyama wakali na waharibifu.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Matiko tayari nimeshalijibu, kwamba tuko kwenye process ya ku-review hizi sheria na kanuni kuangalia sasa angalau tusogeze kiwango fulani ili wananchi nao waweze kuona umuhimu wa namna ya uhifadhi.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru naomba niulize swali moja dogo la nyongeza.
Mji wa Kasera ambayo ndiyo Makao Makuu ya Wilaya ya Mkinga bwawa lake linalopeleka maji hapo linakaribia kukauka, tumeleta maombi ya dharura takriban shilingi milioni 51. Je, ni lini fedha hizi zitapatikana?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kitandula, Mbunge wa Mkinga, kama ifuatavyo. Tunatarajia wiki ijayo kuwapelekea shilingi milioni 51 kwa ajili ya bwawa hilo. (Makofi)
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pia naishukuru Serikali kwa majibu, naomba kuuliza swali moja tu la nyongeza. Taarifa nilizonazo ni kwamba, mpaka sasa mkataba wa mradi huu haujasainiwa na kwa muda uliobaki Waziri anatuhakikishia kwamba, tutaweza kusaini mkataba huo na ujenzi wa mradi huu uweze kuanza?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dunstan Kitandula, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ndio. Wizara tutaweza kusaini mkataba na kazi zitaanza.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, Kituo cha Afya cha Maramba kinachohudumia kata sita Serikali iliahidi kupeleka X-ray; ni lini Serikali itapeleka X-ray?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dunstan Kitandula kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya cha Maramba ni kweli kwamba kinahudumia kata nyingi na katika mpango ambao tumeuweka nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kituo hiki pia ni miongoni mwa vituo ambavyo tumepanga kitapelekewa X-ray, ahsante.