Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Mary Pius Chatanda (10 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kunipatia nafasi nami niweze kuchangia hotuba ambayo aliitoa Mheshimiwa Rais alipokuwa anafungua Bunge hili.
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu na kuwashukuru wananchi wa Wilaya ya Korogwe Mjini kwa kunipa nafasi ya kuwawakilisha katika Bunge hili Tukufu. Mwenyezi Mungu awabariki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii vilevile kumpongeza Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo kwa nafasi aliyoitumia jana usiku kupitia vyombo vya habari alipotoa ufafanuzi juu ya jambo ambalo wenzetu wameamua kufanya upotoshaji wa makusudi kabisa. Ni ukweli usiopingika kwamba Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo ameeleza wazi nia na madhumuni ya Shirika letu la TBC kusitisha matangazo kwa maana ya kutaka MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kunipatia nafasi nami niweze kuchangia hotuba ambayo aliitoa Mheshimiwa Rais alipokuwa anafungua Bunge hili.
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu na kuwashukuru wananchi wa Wilaya ya Korogwe Mjini kwa kunipa nafasi ya kuwawakilisha katika Bunge hili Tukufu. Mwenyezi Mungu awabariki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii vilevile kumpongeza Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo kwa nafasi aliyoitumia jana usiku kupitia vyombo vya habari alipotoa ufafanuzi juu ya jambo ambalo wenzetu wameamua kufanya upotoshaji wa makusudi kabisa. Ni ukweli usiopingika kwamba Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo ameeleza wazi nia na madhumuni ya Shirika letu la TBC kusitisha matangazo kwa maana ya kutaka wao. Kila mwananchi hivi sasa ikishafika kipindi cha taarifa ya habari saa moja, saa mbili, hata kama mtu hana TV anakimbia kwa jirani yake kwenda kusikiliza leo kunafanyika kitu gani, leo Rais atasema nini, leo Mawaziri watasema nini, jinsi walivyokuwa na hamu na utekelezaji wa hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niendelee kupongeza sana jitihada za Mheshimiwa Rais ambazo ameshaanza kuzichukua. Nawapongeza pia Mawaziri kwa kazi nzuri ambayo na wenyewe wameanza kufanya kazi, msirudi nyuma kazeni buti. Achene kuwasikiliza watu wachache wanaosema inawezekana huu ni moto wa kifuu, huu siyo moto wa kifuu utaendelea kuwaka na hautazimika ili kuweza kuwaletea maendeleo wananchi wetu wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nieleze juu ya kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwamba Tanzania yenye viwanda inawezekana. Mimi nafikiri kauli hii ya Mheshimiwa Rais ya Tanzania na viwanda inawezekana, itawezekana endapo tutaondokana na urasimu ambao unazaa rushwa. Wapo wawekezaji wengi ambao wanapenda kuwekeza katika nchi yetu, lakini wanapofika kwenye ofisi zetu za Serikali wanakutana na urasimu mkubwa. Urasimu ule unaashiria rushwa. Rais wetu amesikitishwa sana na suala la rushwa lililoko serikalini. Kwa hiyo, niwaombe ndugu zangu suala la urasimu tukiliacha Tanzania ya viwanda inawezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niunge mkono vilevile kauli ya Mheshimiwa Rais ya kukemea suala la rushwa. Shughuli zetu hata kwenye Halmashauri zetu zimeingiliwa sana na suala la rushwa hasa kwenye kitengo hiki cha ugavi, cha ukusanyaji wa mapato, watu wanafanya vile ambavyo wanataka wao.
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe basi Waziri anayehusika kwenye hizi Serikali zetu za Mitaa, hebu tuingie kwenye vitengo hivi vya ugavi na ukusanyaji wa mapato, watu hawa wanatusababishia Serikali kukosa mapato katika Halmashauri zetu. Wanatumia vitabu vya aina mbalimbali katika ukusanyaji wa mapato, wanakubaliana na wafanyabiashara hawawatozi ushuru ambao unatakiwa. Kwa hiyo, niombe sana kama tunatumbua majipu hebu sasa tufike mpaka huku chini kwenye hizi Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la elimu. Suala la elimu bila malipo ni mpango mzuri ambapo wananchi wameufurahia sana. Nitoe ushauri kwenye Serikali mpango huu uende sambamba na kuwajengea mazingira bora walimu. Bila kuwajengea mazingira bora walimu mpango huu unaweza ukasuasua. Walimu wana matatizo mengi, wanatakiwa waandaliwe mazingira kama vile vitendea kazi, nyumba za kuishi, kuwalipa stahiki zao zile ambazo wanadai ikiwa ni pamoja na malimbikizo ya likizo.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze kwa kuunga mkono jitihada za Mheshimiwa Rais wa Jahmuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Waziri Mkuu na Mawaziri kwa kazi nzuri ambayo wamekuwa wakiifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wameshuhudia juhudi zao katika kutekeleza dhamira ya uwajibikaji na maadili kwa viongozi, watendaji na watumishi wasiyo waadilifu kwa kuwatumbua majipu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ikishafika sasa hivi saa moja kwenye taarifa ya habari, ikifika saa mbili kwenye taarifa ya habari wananchi wanakimbia kwenda kusikiliza leo kunatokea kitu gani. Wananchi walikuwa wameshachoka na tabia ya baadhi ya watendaji wa Serikali ambayo walikuwa wakiifanya, kwa hiyo, sasa wanafurahia juhudi ya Serikali ambayo inafanya ya kuhakikisha kwamba hakuna matabaka kati ya walio nacho na wasiyo nacho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nianze kwa kunukuu maneno aliyosema Kitilya Mkumbo kwenye mtandao wa twitter amesema; “Tunahitaji upinzani utakaojikita katika sera mbadala. Upinzani unaotegemea makosa ya Serikali ya CCM pekee unaweza kupwaya sana katika kipindi hiki.” Mwisho wa kunukuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona ninukuu hili la Mkumbo kutokana na kitendo cha Kiongozi wa Kambi ya Upinzani kutowasilisha hotuba ya bajeti ya Kambi ya Upinzani na hasa ukiangalia bajeti yetu sisi ya Waziri Mkuu ina karatasi kama 100 kitu hivi lakini ya mwenzetu huyu amekuja na karatasi tatu. Matokeo yake kwa sababu kashindwa kuiandika bajeti anashawishi wenzake watoke nje. Hoja ya Kitilya Mkumbo iko sahihi kabisa hawa watu wamefilisika na wamepwaya kisiasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nichukue nafasi hii kuishukuru Serikali ya Tanzania kwa kupata mradi mkubwa wa bomba la mafuta kutoka Uganda kuja Tanzania hususani Mkoa wa Tanga. Ni matarajio yangu kwamba fursa hii ambayo tumeipata tutaisimamia vizuri na kuweza kuanza kufanya maandalizi ya maeneo ambayo mradi huu utapita kwa kutoa elimu kwa wananchi wa maeneo yale na hatimaye kuanza kufanya maandalizi ya fidia kwa maeneo yale yatakayokuwa yamepitiwa na mradi kama kwenye mashamba na nyumba ili kuondoa usumbufu katika utekelezaji wa mradi huu. Ni matarajio yangu kwamba watatoa elimu kwa wananchi ili waweze kutambua faida ya mradi huu ambao umepatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikubaliane kabisa na kaulimbiu kwamba Tanzania kuwa ya viwanda inawezekana. Ili kufanikisha jambo hili ni vizuri tukaimarisha suala la kilimo. Tukiimarisha kilimo vizuri tukakipa kipaumbele kitaweza kuzalisha malighafi ambazo ndizo zitakazoweza kulisha hivyo viwanda.
Tusiposimamia vizuri kuhakikisha kwamba kilimo tunakipa kipaumbele tunaweza tukajenga viwanda na hatimaye tukakosa malighafi, viwanda vikawa vipo na havifanyi kazi na ile kauli mbiu ya kwamba Tanzania iwe ya viwanda ikawa ni kazi bure. Hivyo, naishauri Serikali tusimamie na tuhakikishe kwamba kilimo kinapewa kipaumbele, kiende sambamba na upatikanaji wa maji. Kama maji hayapo kiwanda hakiwezi kufanya kazi, kama hakuna umeme wa uhakika kiwanda hakiwezi kufanya kazi, kama miundombinu hakuna, kiwanda kinaweza kikafanya kazi lakini usafirishaji wa hayo mazao itakuwa ni shida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, miundombinu ni pamoja na reli. Tunapozungumzia reli kama ambavyo wezangu wengine wametangulia kuzungumza reli ni kitu muhimu sana. Reli inapunguza uharibifu wa barabara, magari makubwa yanapita yanaharibu barabara kila siku inafanyiwa matengenezo. Reli ikitengenezwa nadhani mizigo yote itapita kwenye reli na viwanda vyetu vitakapokuwa vimezalisha mazao yatapitishwa kwenye reli, hivyo angalau shughuli za uzalishaji na mali kupeleka kwenye mikoa kupitia reli. Napozungumzia reli basi naomba ifahamike kwamba ni pamoja na reli ile ya kutoka Tanga - Kilimanjaro - Arusha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nizungumzie suala zima la Mfuko wa PSPF. Huu Mfuko wa PSPF unachelewesha mno mafao ya watumishi waliostaafu. Niiombe Serikali, watumishi hawa ambao wanakuwa wamestaafu hizi fedha zao ndizo zinazowasaidia kuweka maisha yao vizuri. Inapokuwa wanacheleweshewa kupata mafao yao inakuwa ni shida. Kwanza, inawapa ugumu wa maisha kwa sababu ameshajipanga kwamba amestaafu kuna hizo fedha anategemea kufanya shughuli ambazo zitamwezesha kupata kipato, lakini anacheleweshewa kupata fedha hizi. Niombe Serikali, hawa wastaafu wanapostaafu basi iwe ni muhimu sana kuwaandalia mafao yao mapema ili waweze kutoka wakiwa na fedha zao na hatimaye waweze kuishi muda mrefu kuliko ilivyo hivi sasa. (Makofi)
Mheshimwa Mwenyekiti, suala la walimu. Lipo tatizo kwa walimu kuhusiana na upandishwaji wa madaraja. Walimu wamekuwa wanachukua muda mrefu kwenye kupandishwa madaraja na hata wakipandishwa mishahara yao kwa maana ya stahiki zao zile zinachelewa sana kufanyiwa marekebisho, inachukua hata miezi sita mtu hajarekebishiwa. Niombe wanapopandishwa madaraja basi na zile stahiki zao ziwe zimeandaliwa. Kule Korogwe wapo baadhi ya walimu wanadai malimbikizo toka 2010 hadi hivi sasa hawajalipwa na wamepandishwa madaraja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iangalie upya suala la posho ya kufundishia (teaching allowance) kwa walimu. Tuseme tusemavyo walimu wana jukumu kubwa sana, wanafanya kazi kuliko mfanyakazi mwingine yeyote.
Tukirudisha teaching allowance kwa walimu haki ya Mungu hii elimu itakwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe Serikali hebu tulitazame jambo hili. Walimu hawa wamekuwa wakitoka shuleni wakifika nyumbani ni kazi ya kuanza kufanya maandalizi, kusahihisha mitihani, kusahihisha madaftari na kuandaa maandalio ya kesho. Kwa bahati mbaya sasa itokee mama ndiyo mwalimu, baba labda ni mhasibu, yule mama anakaa kufanya kazi ya ualimu pale nyumbani mpaka saa nane ya usiku hebu niambie, baba amelala yupo kitandani. Unatarajia hiyo nyumba ya mwalimu na huyo mumewe inakuwaje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Serikali hata kama atafanya kazi kwa o kwa muda huo…
MWENYEKITI: Mheshimiwa umemaliza muda wako naomba ukae!
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya mwanzo ili niweze kuchangia. Kwanza kabisa naomba niuunge mkono hoja juu ya bajeti aliyowasilisha Waziri wa Elimu kwamba, amewasilisha kiufundi kabisa, nampongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi ya kumpa pole Naibu Waziri wa Elimu kwa msiba ambao umempata. Basi, namwombea kwa Mwenyezi Mungu amtie nguvu na Marehemu Roho yake iweze kuwekwa mahali pema peponi. Amina.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Waziri na Naibu Waziri, Wakuu wa Wizara kwa kazi ambayo wamekuwa wakiifanya pamoja na changamoto nyingi ambazo wanakabiliana nazo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwa kusema kwamba, elimu ndiyo ufunguo wa maisha. Bila elimu hakuna viwanda, bila elimu hakuna kilimo chenye tija, bila elimu hakuna afya bora na kadhalika. Hivyo, ningeomba sana, Wizara ya Elimu ifanye kazi ya kuboresha suala zima la elimu. Suala zima la elimu likiboreshwa, tunaweza tukawapata wasomi wazuri, watakaoweza kuendesha nchi hii na kuweza kuingia kwenye soko la ajira.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishauri Wizara ya Elimu, kwa kuanza kutazama upya ufaulu wa darasa la saba. Ufaulu wa darasa la saba uanze sasa kwak kuzingatia vigezo vya kuingia kwenye elimu ya sekondari. Utaratibu wa mitihani wa kuchagua alama za a, b, c, d, tunawapata wanafunzi ambao wanakwenda sekondari wasiojua kusoma na kuandika. Hawa wanafunzi ambao wengine wana vipaji vile vya kubahatisha, wanabahatisha halafu wanaingia kwenye elimu ya sekondari.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakiingia kwenye elimu ya sekondari wanawapa tabu Walimu wa sekondari namna ya kuwafundisha, kwa sababu inabidi sasa waanze kuwafundisha kwa uelewa zaidi, masomo yale ambayo yalikuwa ni ya darasa la saba wanaanza kuwafundisha huku sekondari. Kwa hiyo, naomba sana utaratibu ule wa awali, uliokuwepo mara ya kwanza uweze kurejewa ili kuondoa usumbufu kwa Walimu wa shule za sekondari kuanza kuwafundisha wale wanafunzi ambao hawakufaulu vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Wizara irejeshe utaratibu wa zamani wa kufanya masomo kwa kufikiri badala ya kufanya masomo kwa kuchagua. Wakifanya hivyo tutawapata watoto wanaojitambua, itawarahisishia Walimu kuwa na watoto wenye uelewa na ufaulu wenye tija kuliko ilivyo sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sasa uboreshaji wa elimu uende sambamba na uboreshaji wa maslahi ya Walimu na stahiki zao. Baadhi ya stahiki za Walimu wala hazihitaji kuwa na shida kiasi kwamba Walimu wanapata matatizo, wanapata shida za kuhangaika kufuata stahili zao. Walimu inajulikana siku zao za likizo, mwezi wa Sita ni mapumziko na mwezi wa 12 ni mapumziko, hivyo niiombe Wizara, kinapofika kipindi hicho, wanapojua kwamba Walimu wanataka kwenda likizo mwezi wa Sita, wale Walimu wanaotakiwa kwenda wawe wameandaliwa tayari nauli zao miezi miwili kabla, fedha zao zipelekwe kwenye Halmashauri ili Walimu hawa wanapokuwa wanakwenda likizo, wapewe nauli zao badala ya kuwakopa kwamba waende halafu watakuja kurudi ndipo wapate nauli zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala la teaching allowance. Walimu hawa, ndugu zangu, wanafanya kazi kubwa, wanafanya kazi kiasi kwamba hawana nafasi ya kupumzika, hawana nafasi ya kufanya shughuli nyingine za kuwaongezea kipato. Kwa hiyo, naiomba Serikali iangalie utaratibu wa kurejesha teaching allowance ili Walimu hawa wapate moyo wa kufanya kazi, kwa sababu hawana njia nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, watumishi wengine wanapata muda wa kwenda kufanya kazi kujiongezea kipato, lakini Walimu hawana nafasi ya kufanya hivyo kwa sababu wanakuwa na shughuli nyingi ambazo zinawafanya waendelee kufanya maandalizi kwa ajili ya wanafunzi kwa kesho yake. Kwa hiyo, ni matarajio yangu kwamba Serikali, ombi hili ni la muda mrefu, ni vizuri basi wakaliangalia ili Walimu hawa walipwe hiyo teaching allowance ili iweze kuwasaidia katika kujikimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala zima la madarasa haya ya awali. Madarasa ya awali, Serikali kwa kweli imefanya kazi kubwa kuona kwamba watoto wote waende shule. Hata hivyo, niombe basi kwa kuwa Walimu hakuna wa madarasa la awali, sana sana wanawachukua wale Walimu ambao ni watu wazima ndiyo wamewapangia kufundisha madarasa ya awali. Niombe sasa waandaliwe Walimu maalum watakaokuwa wanafundisha madarasa haya ya awali, badala ya kuwatumia wale Walimu ambao wanaona ni watu wazima waliopo kwenye madarasa mengine na kuwaleta kwenye madarasa haya ya awali. Vile vile iende sambamba na suala zima la kuwapa vile vitendeakazi vya kufundishia.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba sana Serikali, kwa sababu ruzuku inapelekwa kwa wanafunzi wale wa shule za msingi, basi ruzuku vile vile ya watoto wa shule ya awali, iunganishwe kwa kupelekwa kwenye shule za msingi ili angalau na wenyewe waingie kwenye hesabu, kwa sababu safari hii walipokuwa wamepeleka zile ruzuku, hawakuingiza kwenye orodha ya watoto ambao wako shuleni.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tena nizungumzie suala la upandishwaji wa madaraja. Naomba upandishwaji wa madaraja uende sambamba na mabadiliko ya mishahara ya Walimu…
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi nami niweze kuchangia hotuba iliyowasilishwa na Waziri wa Mambo ya Ndani. Kwanza kabisa nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri wa Mambo ya Ndani kwa kazi kubwa anayoifanya akishirikiana na viongozi wakuu kwa maana watendaji wakuu wa Wizara hizo pamoja na changamoto mbalimbali ambazo wanakabiliana nazo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeanza na suala zima la magereza. Tumesema kwamba Serikali yetu tunataka nchi hii safari hii iwe nchi ya viwanda; ukiangalia kwenye taarifa ya Kamati imetoa ushauri kwa kuishauri Serikali kwamba tuiwezeshe magereza ili iweze kufanya kazi yake vizuri. Ninavyokumbuka, nilipokuwa nikikua, magereza wamekuwa wakilima mashamba kwa mfano yale magereza ya kilimo walikuwa wakilima mashamba na kuweza kutosheleza mazao ya chakula na ziada.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kinachotakiwa hapa ni kurejesha ule utaratibu wa zamani ili magereza waweze kupatiwa zana za kufanyia kazi, waweze kupatiwa mtaji, kwa ajili ya uzalishaji. Magereza wakizalisha mazao ya kutosha inaweza ikapatikana malighafi ya kupeleka kwenye viwanda ambavyo tunasema tunataka tuwe na viwanda ili kusudi viweze kulishwa na malighafi itakayokuwa imezalishwa na magereza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi hii inawezekana kwa magereza kwa sababu wenzetu tayari wana rasilimali watu, tukiwawezesha magereza tukawapa mtaji wa kutosha hakuna kitakachoshindikana. Magereza zamani walikuwa wanafuga mifugo kwa maana ya ng’ombe wa maziwa. Nakumbuka nilipokuwa pale Mafinga yalikuwa yanatoka maziwa kwenye gereza la Isupilo, yanaletwa huku ukiuliza yametoka wapi, wanasema maziwa yanatoka Gereza la Isupilo. Kwa hiyo, kama tutataka kuanzisha viwanda vya maziwa, magereza hawa tukiwawezesha watafuga vizuri na viwanda hivyo vitaweza kufanya kazi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishauri Serikali yangu ili tuweze kuufufua huu uchumi tunaouzungumza wa kutaka tuwe na viwanda tuweze kuwawezesha magereza kwa kuwapa mtaji na hatimaye kuwawezesha kwa zana za kufanyia kazi ili kusudi wao wenyewe waweze kuzalisha kwa maana ya kulisha magereza yao, kuachana na kuendelea kuitegemea Serikali. Wakati huo huo ziada itapatikana kwa ajili ya kuuza na hatimaye kuweza kupata fedha ambazo zitapatikana kama sehemu ya maduhuli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Kamishna Mkuu wa Magereza kule kwangu Korogwe kwenye gereza moja la Kwa Mngumi ameanza kufufua mabwawa 30 ya ufugaji wa samaki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mabwawa yale ni makubwa na ameshaanza kupanda samaki mle ndani, lakini anachohitaji hapo kuna changamoto, nimwombe Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi aweze kutembelea lile gereza ili aende akaone yale mabwawa ambayo ameyaanzisha huyu Kamishna Mkuu wa magereza ili aweze kuona ni namna gani ambavyo anaweza kuwasaidia ili kusudi waweze kufanikisha kukamilisha ule mradi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende sasa kama walivyosema wenzangu suala la maslahi ya askari. Lipo tatizo pamoja na kwamba tunasema bajeti inakuwa ndogo, lakini inakuwa ndogo kwa hawa askari wa ngazi ya chini tu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, askari wa ngazi ya chini wanapata shida, wanakwenda likizo bila malipo ya likizo yao, hata wakirudi kutoka likizo wakiomba fedha hizo kulipwa hawalipwi. Niiombe Serikali katika bajeti ile ambayo inatengwa kwa ajili ya Wizara hii ni vizuri tukawapa fedha zote ili kusudi waweze kulipa madeni wanayodaiwa na askari wa ngazi za chini walipwe madai yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo jambo lingine ambalo askari wa ngazi ya chini wanapata shida, suala la upandishwaji wa vyeo, wana utaratibu wa kila baada ya miaka mitatu askari wa ngazi ya chini anatakiwa kupandishwa cheo, lakini hawapandishi kwa wakati na hata wakipandishwa hawalipwi mshahara kulingana na cheo alichopandishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana tusiwafishe moyo vijana hawa askari wa ngazi ya chini hawa mishahara yao ni midogo, wanapandishwa vyeo halafu hawalipwi kulingana na vyeo walivyopewa, wapewe kulingana na vyeo vyao walivyopewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima la kufiwa, askari wa ngazi ya chini akifiwa nitaomba Waziri anipe majibu anapo-wind up hivi ni kweli kwamba akiwa na baba yake mzazi, mama yake mzazi anakaa naye pale nyumbani na tuseme bahati nzuri huyu askari yeye kwao labda ni Musoma amefiwa na baba yake alikuwa akimlea hapo nyumbani alikuwa anaugua, askari yule hawezi kusafirisha na mzazi wake yule kupelekwa nyumbani, askari yule anahangaika anatafufa fedha za kusafirisha mwili ule hivi ni kweli?
Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu askari si mtumishi wa Serikali inakuaje watumishi wa Serikali wengine wazazi wao wakifariki wanasafirishwa iweje askari polisi anafanyiwa kitu cha namna hiyo? Nitaomba majibu kama ni kweli, utaratibu ni huo naomba utaratibu huo ubadilishwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nyumba za Polisi, wenzangu wamezungumza sana, nimefanya ziara yangu nilitembelea taasisi ikiwemo Polisi, Magereza kama walivyosema wenzangu inasikitisha. Askari wa Korogwe Mjini wana nyumba chumba kimoja na sebule, ana watoto watano, wa kike wawili, wa kiume watatu, wote wana umri mkubwa hebu niambieni sasa maadili yako wapi hapo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali, nimeona hapa mnazungumzia suala zima la Serikali kupitia mkopo wa China, sasa nimwombe Waziri atakapokuja ku-wind up aniambie huu ni mkopo ambao umeshapatikana au wanakusudia kupewa hizi fedha, naomba waje waniambie. Kama mkopo huu umepatikana, niwaombe askari wa Korogwe wawemo katika mpango wa nyumba hizi 4,136. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba nichukue nafasi tena kumpongeza Waziri kwa kuwasilisha taarifa yake vizuri na haya mengine ni mapito, yeye apige mwendo, mti wenye matunda mazuri siku zote huwa unapigwa mawe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Naikumbusha Serikali suala la ujenzi wa bandari kavu ya Korogwe Mjini, eneo la Old Korogwe. Mheshimiwa Rais alipokuwa akiomba kura Korogwe, alikutana na hoja hii kutoka kwa wananchi na kuwaahidi atalifanyia kazi jambo hili, lakini kwenye vitabu vya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi hakuna mahali palipozungumzia suala hili la bandari kavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Mheshimiwa Rais alitoa ahadi ya lami Korogwe Mjini, kilometa tano, lakini ndani ya makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti hii, Korogwe haijaguswa. Niiombe Wizara hii kuona ni namna gani itatekeleza ahadi hii ili wananchi waendelee kuwa na imani na Serikali yao. Naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika hotuba iliyowasilishwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, napenda kumpongeza Waziri wa Ardhi na Naibu wake, pamoja na watendaji wote wa Wizara kwa majukumu makubwa waliyonayo na utendaji wao mzuri ambao wameanza katika kipindi hiki cha uteuzi wa Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Mafuguli. Nawapongezeni sana kwa kazi nzuri pamoja na changamoto kubwa ambazo mnakabiliana nazo za migogoro ya ardhi iliyopo hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo Kamati yetu imesema, Serikali imekuwa haitoi fedha zilizoombwa katika bajeti ambayo ilikuwa imetengwa ya Wizara ya Ardhi. Kutotoa fedha kwa wakati na kutotoa fedha zote, kumechangia Wizara hii kutotekeleza majukumu yake vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali itambue kwamba Wizara hii ina majukumu makubwa, imebeba mambo makubwa yanayohusiana na wananchi juu ya migogoro ya ardhi. Kwa hiyo, kutowapa fedha, kutopeleka fedha kwa wakati na kutopeleka fedha zote kunachangia kutotekeleza majukumu yao vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naishauri Serikali ihakikishe kwamba katika bajeti itakayokuwa imetengwa safari hii, wapewe fedha zao zote na kwa wakati ili waweze kutimiza majukumu yao vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kuonyesha masikitiko yangu ambayo yamefanywa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuchelewesha mchakato wa maamuzi ya usimikaji wa Mfumo wa Utunzaji wa Kumbukumbu. Ucheleweshaji huu umekuwa ni wa miaka miwili na nusu. Tulipokuwa kwenye Kamati, tuliwaita Ofisi ya Waziri Mkuu tukataka watuambie, ni kwa nini wamechelewesha tender kwa ajili ya usimikaji wa mfumo huu wa kumbukumbu za ardhi? Majibu yaliyotolewa pale, yalikuwa ni ya ubabaishaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sasa Ofisi ya Waziri Mkuu ifanye haraka suala la mchakato, ikamilishe mchakato huu haraka ili kusudi suala hili la usimikaji uweze kufanya kazi mapema ili kusudi matatizo yaliyopo ya ardhi yaweze kutatuliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala zima la uendelezaji wa mji mpya wa Kigamboni. Naungana na maoni ya Kamati yetu kwamba wenzetu waliopo pale katika ofisi ile ya uendelezaji wa mji wa Kigamboni hawana kazi ya kufanya. Hata ukiangalia kwenye bajeti safari hii hawana fedha za maendeleo. Hata kipindi kilichopita, hawakuwa na fedha za maendeleo. Watu hawa wanapewa bajeti ya mishahara tu. Kwa hiyo, wanalipwa mishahara pasipo kazi. Hakuna haja ya kuendelea kuwepo na ofisi kule Kigamboni ya uendelezaji wa eneo lile wakati watu hawafanyi kazi. Ni vizuri watu hawa wakarejeshwa basi kwenye maeneo mengine wakaendelea kufanya kazi zao. Walipwe mshahara wakifanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wamepanga jengo kubwa lenye gharama kubwa, wanakwenda wanasaini, wanatoka zao. Hata Biblia imesema asiyefanya kazi na asile. Iweje hawa wenzetu wanakuwepo katika kipindi cha miaka nane hakuna kazi inayofanyika pale na wala hakuna fungu la maendeleo! Tulipokuwa tunauliza, bahati nzuri Mheshimiwa Waziri alikuwa anawatetea kidogo, anasema waacheni tu, tutaangalia, tutatafuta fedha; utatafuta wapi wakati humu ndani ya bajeti hii ya maendeleo haipo? Fedha za kutafuta kuokoteza, zinatafutwa wapi? Ni vizuri watu hawa wakasambazwa kwenye maeneo mengine kwa sababu Wizara hii ina upungufu wa watumishi katika maeneo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Wizara iweke utaratibu sasa wa kuweka mabaraza ya ardhi kwa kila Wilaya. Ipo shida, pale kwangu Korogwe kuna Baraza la Ardhi, ni kero kubwa. Kesi za mabaraza ya ardhi haziishi, zimesongamana, ni nyingi. Baraza la Korogwe pale, linachukua Handeni, Kilindi, Lushoto na Korogwe yenyewe. Kuweka mlundikano wa kesi nyingi katika baraza lile, kunasababisha rushwa kubwa. Wananchi wanalalamika. Naiomba sana Wizara, ihakikishe kwamba kunafunguliwa mabaraza mengine, ikiwezekana kule Kilindi na Handeni wawe na baraza lao, Korogwe wawe na baraza lao na Lushoto wawe na baraza lao ili kuondoa usumbufu ambao wanaupata wananchi kuja kutoka Handeni kuja Korogwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie kuhusu mashamba makubwa ya wawekezaji. Naomba hawa wawekezaji ambao wanapewa maeneo kwenye vijiji, basi waone umuhimu wa kuchangia masuala ya maendeleo kwa wananchi wa vijiji vile ambavyo wanaishi. Hiyo itajenga mahusiano mazuri na wanavijiji. Kutowasaidia kufanya hivyo, ndiyo unasikia migogoro mingine kwenye maeneo hayo, wawekezaji mara wanafukuzwa na wanavijiji, mara wanaingiliwa kuchomewa mali zao. Ni vizuri wakajenga mahusiano mzuri na wana vijiji ili kusudi wakiwasaidia kwa mfano miradi ya maji, ujenzi wa shule na mambo mengine mengi, hakutakuwa na matatizo na kero ambazo zinatokea sasa hivi kwa wawekezaji na wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa Wizara ianze kuangalia namna ya kuwapa wawekezaji maeneo. Tuangalie maeneo ambayo yako wazi, tusiende kuwapa wawekezaji maeneo ambayo ni mashamba wa wananchi na makazi ya wananchi ili kuondokana na migogoro ya ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ningependa kuishauri Serikali yangu sasa waanze kuona umuhimu wa kuanza kuwapatia wawekezaji maeneo ambayo sio makazi ya wananchi na siyo mashamba ya wananchi ili kuondoa migogoro ya ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja lakini naishauri Serikali bajeti inayotengwa itolewe yote na kwa wakati hasa ikizingatiwa Wizara hii inakabiliana na changamoto nyingi zinazohusiana na migogoro ya ardhi na maendeleo yanayohusiana na upimaji na uboreshaji wa mipango Miji na Majiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Waziri Mkuu ikamilishe haraka mchakato wa ununuzi wa vifaa vitakavyotumika kwenye mfumo wa utunzaji wa kumbukumbu za ardhi yaani Intergrated Land Information Management System, kutofanya haraka kunazorotesha ufanisi katika utawala wa ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mabaraza ya Ardhi ya Wilaya kuna mlundikano wa kesi nyingi kutokana na kushindwa kuhimili, kushughulikia zaidi ya Wilaya nne. Kwa mfano, Baraza la Ardhi la Korogwe linashughulikia Wilaya za Kilindi, Handeni, Lushoto, Korogwe Vijijini na Korogwe Mjini. Kwa kushika zaidi ya Majimbo na Wilaya tano kunasababisha uwepo wa rushwa jambo ambalo linazuia haki za wananchi.
Naishauri Serikali kuanzisha Mabaraza mengine kwa Wilaya ya Kilindi, Handeni, Korogwe Vijijini iwe na Korogwe Mjini na Lushoto iwe peke yake kulingana na ukubwa wa Wilaya hiyo yenye Majimbo makubwa matatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa uendelezaji Mji wa Kigamboni haujatekelezwa muda mrefu na hata haina bajeti ya maendeleo zaidi ya kuwa na bajeti ya mishahara na ulipaji wa pango la ofisi bila ya uwepo wa majukumu ya kufanya. Naishauri Serikali kuifunga ofisi hiyo na watumishi wapelekwe maeneo mengine yenye upungufu wa watumishi wa ardhi kwenye Miji na Majiji hadi Kata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kuanza kuona umuhimu wa kutoa maeneo ya wawekezaji nje ya maeneo ya mashamba ya wananchi au makazi ya wananchi ili kuepuka ulipaji wa fidia. Wawekezaji wanaofaidika kupata maeneo kwenye Vijiji au Halmashauri wawe na mahusiano mazuri na wananchi katika maeneo yao kwa kuvisaidia vijiji huduma za jamii kwa maendeleo ya vijiji hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uwepo wa master plan za vijiji, miji na majiji ni vema elimu ikatolewa kwa wananchi kabla ya ujenzi holela ambao unapoteza maana ya miji kwa kutokuwa na miundombinu ya barabara mifereji ya maji taka, maji ya mvua mabomba ya maji, viwanja vya michezo na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze juhudi za NHC kwa kazi nzuri wanayoifanya ya ujenzi wa nyumba bora na kauli mbiu yao ya maisha ni nyumba. Naishauri Serikali shirika hili lianze kuona umuhimu wa kujenga nyumba zenye bei nafuu ili kuwawezesha hata wale wenye kipato cha chini waweze kununua nyumba hizo. Aidha, Serikali ione namna itakavyoweza kuondoa VAT kwenye vifaa vya ujenzi wa nyumba hizi za NHC kwa lengo la kuwawezesha kufanikisha ujenzi wa nyumba zenye bei nafuu.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MARY P.CHATANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nianze kwa kuunga mkono hotuba ya Waziri wa Fedha. Nipongeze jitihada za Serikali katika ukusanyaji wa mapato, lakini bado tuna safari ndefu ya kuendelea kutoa elimu kwa wananchi wetu juu ya kudai risiti pale wanapokuwa wamenunua bidhaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile niendelee kuishauri Serikali kwamba ni wakati muafaka sasa katika jambo hili la ukusanyaji wa mapato au kutoa elimu, tuanze kutoa kwa shule zetu za msingi na sekondari ili watoto wetu waweze kufahamu mapema juu ya suala la ulipaji wa kodi na kudai risiti pale wanaponunua bidhaa kwenye maduka.
Mheshimiwa Naibu Spika, mbali ya hiyo Serikali imefanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato, lakini bado kuna ukwepaji wa kodi kwa baadhi ya vituo vya mafuta. Viko vituo vya mafuta ambavyo vyenyewe vinatumia ile mashine, ukienda kununua mafuta unapomdai risiti anakwambia mashine nimeipelekea kwenye chaji, unamwambia sasa inakuwaje umeshaniwekea mafuta, anakwambia sasa nifanyaje nimeipeleka kwenye chaji.
Kwa hiyo, pale hupati risiti kwa sababu ameshakwambia amepeleka kwenye chaji. Sasa niombe Serikali tuendelee kuwasimamia hawa wafanyabiashara wazifunge zile mashine kwenye zile mashine zinazotoa mafuta ili anapotoa mafuta na risiti inajitoa badala ya hizi mashine ambazo wanasema zinakwenda kuchajiwa huko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapoteza mapato kwenye vituo vya mafuta kwa ujanjaujanja huo, kwamba wanapeleka kuchaji zile mashine.
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye suala la TRA kukusanya mapato. Nakubaliana na jambo hilo lakini sasa tunaliwekaje kwa sababu Halmashauri zetu katika bajeti zao hususani Halmashauri yangu ya Korogwe ni sehemu ya own source ya mapato yao ya ndani kwa ajili ya shughuli za maendeleo katika Halmashauri. Sasa endapo TRA itakusanya mtatuwekea utaratibu gani wa kurejesha zile pesa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, bado nina uzoefu wa huko nyuma, viko vyanzo ambavyo Serikali ilivizuia kwamba Halmashauri isikusanye kwamba Serikali kuu itafidia, lakini bado kumekuwa na usumbufu na ucheleweshaji wa fedha hizo kurejeshwa kwenye Halmashauri baada ya kuwakataza kwamba wasikusanye yale mapato.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Mheshimiwa Waziri aniambie baada ya kuwa TRA imekusanya fedha hizi na hasa ikizingatiwa kwamba ndiyo chanzo cha mapato katika Halmashauri zetu, watakuwa wanarejesha kwa wakati ili hizi fedha zikafanye kazi za maendeleo katika Halmashauri zetu? Nitamwomba Waziri aniambie atakapokuwa anafanya majumuisho. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yako maeneo mengi ambayo yanapoteza mapato, tukikusanya vizuri hata upande huu wa madini tukiangalia vizuri hii mikataba ndugu zangu inaweza ikatusaidia kupata mapato ya kutosha tukaachana na hili suala hata la kutaka kukata kodi kwenye kiinua mgongo cha Wabunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kukata kodi kwenye viinua mgongo hatukatwi Wabunge tu, nimeona kumbe wanakatwa mpaka Watumishi wa Serikali. Watumishi hawa wa Serikali na sisi Wabunge tunakatwa tayari kwenye mishahara yetu, sasa inakuwaje tena tunaendelea kukatwa kwenye kiinua mgongo? Niiombe Serikali iliangalie jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye Mfuko wa Maji na naungana na Kamati ya Bunge ambayo ilitoa taarifa yake kwamba iongezwe tena angalau Sh. 50/= kusudi iwe Sh. 100/=, ikiwa Sh. 100/= maana yake itatusaidia kwenye Mfuko wa Maji, lakini wakati huo huo zikajengwe zahanati na vituo vya afya. Wanawake wajawazito na watoto wanapata shida, endapo hatutajenga zahanati, endapo hatutakamilisha zahanati zilizokuwa zimejengwa na vituo vya afya, wanawake wataendelea kupata shida kwenda mwendo mrefu kwa ajili ya kwenda kujifungua na kwa ajili ya kuwapelekea watoto kupata matibabu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niombe Serikali yangu ikubaliane na suala la kuongeza Sh. 50/= ili iwe sh. 100/= na hatimaye fedha zile zigawanye ziende kujenga vituo vya afya pamoja na zahanati. Ukiangalia pale kwangu Korogwe Mjini sina hospitali ya Wilaya, nina zahanati pale ya Majengo, nakusudia sasa ile zahanati iwe ndiyo kituo cha afya ambacho kitakuwa kama sehemu ya Hospitali. Sasa kama hakijatengewa fedha hawa wananchi wangu wa Korogwe wanatibiwa wapi? Niombe Serikali tukubaliane kwa hili ambalo limependekezwa na Kamati ili kusudi fedha hizi ziweze kusaidia kujenga zahanati pamoja na vituo vya afya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha standard gauge, nakubaliana na naunga mkono kwa asilimia mia, lakini hebu tuitazame na reli ya Tanga, kwa sababu sasa hivi tunasema litajengwa bomba la mafuta kutoka Uganda hadi Tanga. Hebu tuiangalie na reli ya Tanga kuweza kuipa fedha ili kusudi iweze kujengwa kwa kiwango cha standard gauge.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni matumaini yangu kwamba Waziri naye ataliangalia hili kwa sababu tumekubaliana bomba hili linaanza kujengwa hivi karibuni, ni kwa nini sasa Tanga haijatengewa fedha kwa ajili ya kujenga reli kwa kiwango cha standard gauge? Wamesema hili bomba kwa taarifa nilizonazo litakuwa linapita kando kando mwa reli mle, niombe sana Serikali yangu iliangalie hilo kuona kwamba ni namna gani ambavyo inaweza ikajenga reli ya Tanga kwa kiwango cha standard gauge.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba niunge mkono hoja na kushukuru sana kwa kunipa nafasi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Naishauri Serikali, Sheria za Ardhi na Sheria za Uhifadhi, kwa maana ya mipaka inayohusiana na maeneo ya maliasili itazamwe upya kwa lengo la kuondoa migogoro na migongano kati ya wananchi na maliasili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha wataalam wa ardhi, maliasili, kilimo na maji wakutane ili kuisaidia Serikali kumaliza migongano na migogoro ya ardhi kwa kuifanyia uchambuzi wa kina na hatimaye watoe mapendekezo kwa Serikali ili yaweze kupitiwa na kufanyiwa kazi, bila hivyo migogoro hii haitaondoka au haitakwisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mifugo kuingizwa kwenye hifadhi na hifadhi kufanywa malisho halikubaliki. Kuachia jambo hili liendelee litasababisha uharibifu mkubwa wa ardhi, mazingira, kuondoa uoto wa asili kutokana na ng‟ombe kukanyaga hovyo. Misitu itakwisha kwani wafugaji ndio wanaokata miti na kuchoma moto kwa lengo la kutaka nyasi ziote upya kwa ajili ya malisho yao, maliasili itatoweka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la majangili, askari wa wanyamapori waendelee kupatiwa mafunzo na mbinu zitakazowawezesha kukabiliana na majangili. Aidha, vitendea kazi ni lazima vipatikane kwa askari hawa, bila kufanya hivyo kuhimili vishindo vya majangili itakuwa ngumu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kuboresha miundombinu itakayowezesha watalii kutembelea hifadhi kwa urahisi zaidi na kuingizia mapato ya Serikali kwa wingi.
Muswada wa Sheria ya Uthamini na Usajili wa Wathamini wa Mwaka 2016
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi angalau kwa dakika tano hizo, lakini naanza kwa kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kusimamia utawala wa sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania sasa hivi wanazijua mbivu na mbichi, wala watu wengine wasipoteze nguvu bure kwa ndoto za alinacha, wala wasijenge ukuta usiokuwa na matofali. Wamwache Mheshimiwa Rais atekeleze majukumu yake kwa mujibu wa Katiba ya nchi na jinsi ambavyo waliweza kumpa kura wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma kwenye hiki kitabu chao, ni kumzungumza yeye tu kwenye ukurasa wa kwanza, wa pili na wa tatu. Sasa naomba wajue kwamba Rais wetu anasema Hapa Kazi Tu, wala hahitaji ukuta ambao hauna matofali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri pamoja na watendaji wake kwa kuleta Muswada huu ambao unahusu Mthamini Mkuu, Uthamini pamoja na …haya sasa! (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza kwa kuletwa Muswada wa Sheria ya Uthamini na Usajili wa Wathamini wa mwaka 2016. Naungana na mawazo ya Kamati ambayo tumezungumzia na kukubaliana na mapendekezo yaliyoletwa na Serikali. Kwa mfano, katika kifungu cha 5 ambacho kinazungumzia suala la Mthamini Mkuu, kwenye sheria inasema Mthamini Mkuu atateuliwa na Rais, lakini ni miongoni mwa Watumishi wa Umma. Sisi kama Kamati tumekubaliana na wenzetu upande wa Serikali kwamba tupanue wigo zaidi kwa maana ya kuacha nafasi hii iweze kuwa na wigo mpana ili kusudi aweze kupatikana Mthamini Mkuu ambaye ana sifa na vigezo vya kuweza kuteuliwa. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kifungu cha 6 kinachohusu mamlaka ya majukumu ya Mthamini Mkuu, tumeangalia tukaona kwamba ni vizuri kikaongezwa kifungu cha (3) kitakachompa Mthamini Mkuu Mamlaka ya kutekeleza majukumu yake chini ya sheria hii kwa uwazi bila kuingiliwa na kutokuwa na upendeleo wowote. Vilevile tulifikiri ni vizuri basi kifungu hiki kikaendana na kifungu cha 6(1)(h) mbacho kinasema; “Kuandaa na kusababisha kuandaliwa, kusimamia na kuidhinisha taarifa zote za uthamini.” Kwa hiyo, kikiungana na hiki ndiyo kitaleta maana nzuri katika muswada huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia tena kwenye kile kifungu cha 6(1)(e) kinachohusu kuwasilisha report ya uthamini kwa Waziri; nakubaliana na Kamati kwamba report ni vizuri iwasilishwe mara mbili kwa mwaka badala ya miezi mitatu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia sehemu ile ya tatu inayohusu Bodiya Usajili wa Wadhamini, Kifungu kile cha 13(1)(d) kinachohusu muundo wa Bodi; muundo wa Bodi umefanyiwa marekebisho makubwa. Tumeangalia na tumeona kwamba kuna taasisi ambazo zilikuwa zimeachwa, sasa sisi tumefikiri ni vizuri tukaingiza Wawakilishi toka Bodiya Taifa ya Uhasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA) na Wawakilishi toka Chama cha Mabenki Tanzania kwani hawa ni wadau wakubwa namba moja wa uthamini wakati wa kutoa mikopo na wanao uwezo wa kushauri na kutoa mawazo zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi ya kushukuru tena kwa kunipa nafasi, niseme kwamba naungana na mawazo ya Kamati na vilevile naungana na mawazo ya Serikali. Ahsante sana.