Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Rashid Abdallah Shangazi (15 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwanza, napenda kuwapongeza wananchi wa Jimbo la Mlalo kwa imani yao kubwa ambayo imenifanya leo nasimama mbele ya Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda niungane na Wabunge wenzangu kuchangia Hotuba ya Mheshimiwa Rais kama alivyoitoa tarehe 20 Novemba, 2015.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitaanzia na zoezi zima la utunzaji wa mazingira. Duniani kote sasa hivi tunazungumzia mabadiliko ya tabia nchi. Nadhani tutakubaliana sote kwamba hata haya matatizo ya maji tunayoyazungumza kutoka kwenye Majimbo tofauti yamesababishwa
na namna ambavyo tumeharibu mazingira yetu. Tunapozungumzia utunzaji wa mazingira, tunamaanisha pamoja na utunzaji wa vyanzo vya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitatoa mfano katika Jimbo langu la Mlalo, tunao Msitu wa Asili wa Shagayu mwaka 2012 uliungua moto takribani hekari arobaini na tisa lakini ni hekta kumi na moja tu ndizo ambazo zimepandwa. Cha kusikitisha mvua za Desemba zimesababisha maafa makubwa kwa sababu ardhi imekuwa loose, imesababisha maporomoko na mafuriko katika kata za Mtae, Shagayu, Mbalamo na Mnazi. Hii yote ni kwa sababu ya uoto wa asili ambao umeondoka.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na tatizo la uharibifu wa mazingira katika maeneo ambayo yanazunguka msitu wa Shagayu vilevile kuna tatizo la nguvu kazi. Msitu wa Shagayu unazungukwa na takribani vijiji kumi na tano lakini wako Watendaji wawili pekee na wanatumia
pikipiki moja. Nimuombe Waziri wa Maliasili kupitia Serikali yetu sikivu ahakikishe kwamba anawasaidia Watendaji ili waweze kufanya kazi hii ya utunzaji wa mazingira na misitu kwa ufanisi unaotakiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili nitajikita kwenye kilimo. Kama sote tunavyotambua kilimo ndiyo mhimili wa uchumi wa nchi yetu ya Tanzania. Kwa wakazi wa Jimbo la Mlalo na Halmashauri ya Lushoto kwa ujumla wake, ni takribani asilimia tisini na nane wanategemea
kilimo. Tunaomba kupitia hotuba hii ya Mheshimiwa Rais, Wizara inayohusika itufanyie yafuatayo katika Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto. Tunayo maeneo ya aina mbili, ya milimani ambapo tunaendesha kilimo cha mbogamboga na matunda katika kata za Lukozi, Malindi, Rangwi, Sunga na Shume. Kuna tatizo kubwa la wakulima kunyonywa pindi wanapovuna mazao yao kwa kutumia mtindo wa lumbesa. Lumbesa imekuwa ni sehemu ya unyonywaji wa wakulima, hivyo mwisho wa siku hawaoni faida ya yale mazao ambayo wanayavuna. Hivyo, naomba Bunge lako Tukufu, tuisimamie Serikali kuhakikisha kwamba kunakuwa na udhibiti wa ufungaji wa mazao kwa njia ya lumbesa. Tunatambua Wizara ya Viwanda na Biashara ina Wakala wa Mizani na Vipimo, tunaomba ilisimamie suala hili ili liweze kupatiwa ufumbuzi wa mwisho.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni ukanda wa tambarare. Ukanda huu tunapata changamoto kwamba mvua zinazoshuka katika mabonde yetu na makorongo zinaelekea baharini na maji yanapotea bure. Tunaomba Wizara ya Kilimo ije na mpango wa kutujengea
mabwawa ili tuweze kuhifadhi maji yanayotiririka wakati wa msimu wa mvua. Maji haya yatasaidia wananchi kuendesha kilimo chenye tija kwa msimu mzima wa mwaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika maeneo hayo tunayo mapori mazuri ambayo yakitumika vizuri kwa kuzingatia rasilimali ardhi, tunaweza tukaanzisha benki ya ardhi ambayo itakuwa ni kivutio kimojawapo kwa wawekezaji ambao wanatafuta maeneo ya kuwekeza. Pia
kwa kutumia mipango ya ardhi, tunaweza pia tukawatengea wafugaji ambao nao pia wanapatikana katika eneo hili, wakapata maeneo ili waachane na kasumba ya kuswaga ng‟ombe kila mahali. Tutakuwa tumewajengea uwezo wa kukaa mahali pamoja ambapo hata
Serikali inaweza ikapata kodi yake stahiki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia hotuba hii nzuri ya Rais lazima pia tufungue fursa mpya za kuwawezesha wananchi wetu. Jimbo la Mlalo, Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto inapakana na nchi jirani ya Kenya. Tunao mpaka kule ambao unatumiwa kwa ajili ya shughuli za kupitisha magendo pamoja na kupitisha Wasomali ambao wanapita kwa njia za panya.
Niiombe Serikali ione kwamba hii ni fursa ya kufungua kituo cha mpaka katika eneo la Kata ya Lunguza ili tuweze kufanya biashara na nchi jirani ya Kenya. Ni jambo jema kabisa kwamba ulinzi wa mipaka yetu ni jukumu ambalo halikwepeki lakini tukiweza kuweka kituo cha biashara na mpaka itasaidia wafayabiashara kuweza kwenda nchi jirani na pia itatusaidia na sisi kuuza mazao yetu katika nchi jirani ya Kenya.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua suala zima la umeme vijijini. Tunashukuru umeme vijijini umesambazwa kwa kiwango cha kutosha lakini pia niombe Waziri anayehusika na nishati katika Jimbo langu bado kuna kata zaidi ya nne hazijaguswa na nguzo hata moja. Naiomba
mamlaka inayohusika kupeleka umeme vijijini atambue Kata za Shagayu, Mbaramo, Mbaru na Sunga ili nazo ziweze kupewa kipaumbele katika usambazaji wa umeme vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo napenda kulizungumzia ni rushwa.
Mheshimiwa Rais ameanza vizuri, anapambana na majipu makubwa katika ngazi ya kitaifa. Kupitia Bunge lako Tukufu, naomba pia Waziri wa TAMISEMI, ashuke huku chini katika Halmashauri zetu, miradi mingi inafanywa chini ya utekelezaji uliokusudiwa. Huku nako kuna
mchwa wanatafuna pesa, miradi haina tija, miradi haikamiliki kwa wakati, wanawazungusha Madiwani kwa sababu wanatumia uelewa hafifu wa Madiwani wetu walioko huko vijijini pamoja na Watendaji wa Vijiji. Naiomba Wizara husika ilisimamie hili kwa jicho la karibu zaidi.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hayo naomba kuwasilisha, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchangia katika bajeti ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Mlalo, Tarafa ya Umba ni tambarale hivyo maji yanayotiririka kutoka milimani yanapotea bure kwenda baharini upande wa nchi jirani ya Kenya. Rai yetu ni kupata mabwawa makubwa kwa ajili ya kuanzisha skimu za umwagiliaji katika Kata za Mnazi, Lunguza na Mng‟aro. Hili ndiyo eneo pekee lenye ardhi ya kutosha katika Halmashauri ya Mlalo na Lushoto ambalo bado halijatumika.
Mheshimiwa Naibu Spika, ufugaji pia ni changamoto kwani hakuna hata josho moja. Aidha, hakuna hata mabwawa ya kunywesha mifugo ya wafugaji wa Bonde la Hifadhi ya Mkomazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Mlalo jiografia yake ni Milima ya Usambara na kuwa kikwazo kwa shughuli za uvuvi kwa kuwa hakuna mito na maziwa. Tunaomba Wizara ituweke katika mpango wa kutupatia mabwawa ya samaki ili wananchi wangu waweze kupata bidhaa hii katika ubora na kuondokana na tatizo la kuwa na upungufu wa madini ya chuma.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna tatizo sugu la ufungaji wa mazao kwa mtindo wa lumbesa na kuwanyonya kwa kiasi kikubwa wakulima ambao wengi wao ni wanawake na wanalima kilimo hai ili waweze kupata tija ya mazao yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili tuendeleee tunahitaji mambo manne muhimu nayo ni ardhi, watu, siasa safi (good policy) na uongozi bora. Mheshimiwa Waziri hakikisha kupitia halmashauri nchini tunaweka utaratibu wa kuweka Reserve Land Bank ili wakati tunapopata wawekezaji wa kilimo tuwaelekeze huko.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tuwajengee uwezo watu wetu hasa wafugaji ili kupata namna bora ya kuwashawishi kupunguza idadi ya mifugo na kupata tija wawapo na mifugo michache. Vile vile badilisha sera ambazo siyo rafiki kwa Wizara yako ikizingatiwa Wizara hii ndiyo mhimili wa uchumi wa Taifa, pia ndiyo chachu ya kuelekea Tanzania ya viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama mnataka mali mtaipata shambani.
Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Na mimi napenda kwanza kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa wasilisho lake japo lina upungufu, lakini ndiyo mwanzo wa Serikali yetu ya Awamu ya Tano. Tuko hapa kwa ajili ya kuyaboresha ili angalau bajeti itakayokuja mwaka unaofuata waweze kuyarekebisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza na suala zima la TBC. Kama alivyomaliza kuzungumza mzungumzaji aliyemaliza, mawasiliano ya TBC hasa kwa mikoa ya pembezoni bado hayapatikani na hususan katika Wilaya ya Lushoto ambayo ina population ya watu takribani 500,000 wanapata redio zinazotoka Kenya, hasa Mombasa na Nairobi. Sasa ipo hatari kwamba wananchi hawa watakuwa hawapati huduma za habari la Taifa lao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Nape pamoja na Mkurugenzi wa TBC Dkt. Ayoub Rioba, najua yuko hapa, kule Lushoto hatupati matangazo ya TBC. Mwandishi wa habari, ndugu yangu Suleiman Mkufya, tulikuwa naye kwenye kampeni, kila mahali alipokuwa anakatiza ndiyo swali alilokuwa anaulizwa kwamba mbona TBC Lushoto haipatikani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nizungumzie la soka. Nitatofautiana na wachangiaji waliotangulia kwa maana ya kuipa uhai timu ya Taifa. Naamini katika hii miaka ya karibuni hata tufanye vipi, hakuna miujiza ya kuweza kwenda kwenye mashindano makubwa kwa kupitia crash program. Bila uwekezaji wa maana kufanyika katika soka, soka haina njia ya mkato.
Nawapongeza sana wenzetu wa Alliance Academy wale wa Mwanza, vile ndiyo vitalu ambavyo vinaweza vikatufanya siku za usoni tuweze kuheshimika katika medani za soka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna Chuo cha Michezo cha Malya. Chuo hiki kilikuwa kinatoa elimu za michezo lakini kinatoa ngazi ya preliminary. Tunaomba Mheshimiwa Waziri alifanyie kazi, waanze kuongeza, angalau kitoe mpaka ngazi ya diploma pamoja na ngazi ya Shahada. Tutakapokuwa na walimu wa michezo wa kutosha na tukawatawanya kwenye shule, ndiyo hawa baadaye wanaweza wakaleta tija kwenye ulimwengu wa michezo katika Tanzania yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hivi kama tunataka mafanikio ya njia ya mkato, basi tutayapata kupitia timu ya wanawake ya Twiga Stars. Twiga Stars ilikuwa inafanya vizuri sana na mara zote ilikuwa inafika hatua ambayo kama kungekuwa na uwekezaji wa maana, kama ingekuwa inatafutiwa wafadhili kama ambavyo zinatafutiwa timu za wanaume, naamini timu hii ingekuwa imeshafika katika fainali za Afrika. (Makofi)
Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Waziri na wenzetu wa TFF, Mheshimiwa Kadutu yuko humu ndani, kwamba tujaribu kuweka uwekezaji kwenye timu ya Twiga Stars. Timu hii inaweza ikatutoa kwenye suala la crash program, kwa muda mfupi tunaweza tukaenda mahali fulani na tukafanikiwa. (Makofi)
Suala lingine ni kuhusu Baraza la Sanaa la Taifa. Baraza hili linafanya kazi kama wenzetu wa TFDA kwamba wanasubiri bidhaa ziko sokoni ndiyo wanaenda kukamata wauzaji wa zile bidhaa. Nawaomba wasifanye kazi kwa namna hiyo. Tumeona video ya chura ambayo imekuwa kwa kweli inadhalilisha, nashangaa bado hatujapata matamko kutoka kwa akina mama, lakini video ile haistahili kuangaliwa na Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tuna tamaduni zetu. Ni vizuri Baraza la Sanaa la Taifa likasimamia wasanii wetu kuhakikisha kazi wanazofanya lazima ziwe zinazingatia maadili na tamaduni zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la uandishi na utangazaji; ni kweli kabisa kwamba waandishi wetu wanafanya kazi katika mazingira magumu, wakati mwingine habari hizi wanazozitafuta hasa habari za uchunguzi, zikiwemo za mauaji ya vikongwe, albino pamoja na habari za huko mikoani, nyingi wanazifanya katika mazingira hatarishi. Ni vizuri Wizara ikaja na sera maalum ya kuweza kuwalinda waandishi wa habari ili waweze kupata bima ili wanapokuwa katika kazi zao, waweze kuwa na uhakika wa maisha yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine pia tuhakikishe kwamba kuna chombo cha kupima weledi wa waandishi wa habari, kwa sababu wapo wenzetu waandishi wanageuza baadhi ya watu kuwa bidhaa. Unashangaa gazeti kila siku linaandika habari za mtu mmoja ambazo ni habari za kutunga, wakati mwingine hazina uhakika wowote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, weledi katika uandishi uzingatiwe, tuepuke uchochezi. Watangazaji nao siku hizi kunakuwa na mipasho mingi kwenye vyombo vyetu vya habari, hawaongei mambo ya msingi, hasa katika vipindi vya taarabu, wanazungumzia mambo ya mitaani ambayo hayana tija sana kwa Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa mwenyekiti, suala lingine ndugu zangu, nilikuwa naongelea suala zima la deni la Serikali. Serikali imekuwa inakwenda pale TFF na kuingia kwenye akaunti zao na kuchukua pesa. Mwanzo wa mambo yote haya ni katika mechi ile ya Tanzania na Brazil. Mechi ile kwa tunaofahamu ni kwamba iliandaliwa chini ya Serikali ya Awamu ya Nne kupitia Ikulu na zilitolewa takribani shilingi bilioni tatu kwa maandalizi ya mechi ile. Mapato yaliyopatikana kwenye mechi, nadhani ni kama shilingi bilioni 1.8, hizo nyingine hatujui kwamba Mheshimiwa Rais alizitoa wapi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo TRA walikuwa mara kwa mara wanaingia katika akaunti za TFF na kuchukua pesa. Sasa msingi ni kwamba mechi ile iliandaliwa na Kamati maalum, haikuandaliwa na TFF. TFF walikuwa tu ni waendeshaji wa mpira lakini katika mechi ile hawakuhusika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine katika hilo hilo, ni kwamba kulikuwa na mshahara wa kocha ambaye aliletwa na Serikali ya Awamu ya Nne, Marcio Maximo. Kwanza tunamshukuru sana kocha huyu kwa sababu alileta hamasa kubwa sana katika mpira wa Tanzania, aliifanya TFF ya Rais Leonard Chila Tenga kuwa taasisi ambayo iliheshimika sana na mwamko katika nchi uliongezeka sana. Kocha huyu alikuwa analipwa pia kupitia Serikali. Sasa tunashangaa baada ya muda TRA wanadai kodi ya mapato ya mshahara wa kocha wa TFF. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuishauri Serikali kwamba hebu ilifanyie kazi suala hili TFF inajiendesha yenyewe kupitia mapato ya mlangoni, haina ufadhili wa kutosha. Sasa hivi tumeiachia pia jukumu la kuandaa timu ya Taifa ambapo kimsingi wenzetu wa Afrika Magharibi timu hizi zinaandaliwa na Serikali. Bila Serikali kuweka mkono katika timu ya Taifa, tusitarajie miujiza yoyote kama tunaweza tukaenda huko ambako tunatabiri kwenda. Ni lazima Serikali iweke uwekezaji wa kutosha lakini wakati huo huo iwa-support wenzetu wa TFF, wanayo kazi ngumu, zipo timu zaidi ya nne ambazo wanatakiwa kuziandaa, wao peke yao hawatoshi. Hiki kidogo ambacho tunakipata, bado Serikali inaenda inakichukua ilhali suala la mshahara wa kocha lilikuwa limetokana na mshahara ambao Rais aliahidi kwamba atatoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine naomba kwa mara ya kwanza leo nimpongeze Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Mheshimiwa Sugu, amezungumzia suala zima la miziki ya ndani kupigwa kwa asilimia 80. Mimi nasema, isiwe 80, twende hata mpaka 90. Sasa hivi hata hao wasanii wetu wanakuwa wa Marekani zaidi ama wa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, ahsante sana na naunga mkono hoja
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Nami naomba kwanza nitoe shukurani za dhati kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa Hotuba yake nzuri ambayo ime-reflect Mpango wa Serikali wa Miaka Mitano; lakini vile vile imejikita katika Hotuba ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa Novemba, wakati anazindua Bunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza na kumpongeza sana Waziri wa Nishati Profesa Sospeter Muhongo, kwa kupigana na kuwezesha Serikali yetu kupata mradi ule wa bomba la mafuta kutoka Ziwa Albert kule Uganda hadi katika Bandari ya Tanga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ile ni fursa nzuri kwa sisi Watanzania kuitumia kama comparative geographical advantage kwamba isiishie tu kwenye kusafirisha mafuta ghafi; lakini iendane sambamba na upanuzi wa Bandari ya Tanga ili iweze kuwa hub ya mizigo ya nchi ya Uganda na pia ushirikiano na wenzetu wa Sudani ya Kusini ambao wamejiunga katika Jumuiya Afrika Mashariki. Tukiitumia fursa hiyo vizuri ya kupanua Bandari ya Tanga kuboresha miundombinu ya reli kutoka Tanga, Moshi, Arusha hadi Musoma; pia sambamba na kuboresha Bandari ya Ziwa Victoria katika bandari ya Musoma, itaweza kuleta tija zaidi kwa Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiwa katika bajeti ya TAMISEMI kama ambavyo iko mbele yetu, naomba na mimi nichangie katika maeneo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza, nitajikita katika eneo la ugatuzi wa madaraka, maana dhana nzima ya ugatuzi ni kuweza kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi, lakini ninavyozungumza hapa mimi ni Mbunge wa tatu wa Jimbo la Mlalo, tunayo maombi yetu Wizara ya TAMISEMI ya kutaka tupate Halmashauri ya Mlalo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Mlalo linaundwa na tarafa tatu, kata 18, vijiji 78, vitongoji 599, sekondari 29, shule za msingi 93. Tunao mwingiliano wa mabasi ya kwenda Arusha, Dar es Salaam na kadhalika. Tunayo magulio makubwa ambayo yanaweza yakaleta watu wengine kutoka Zanzibar, Comoro na Mheshimiwa Ally Salehe pale Mbunge wa Malindi; naye alitoa mchango wake kushuhudia katika hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ombi letu sisi ni kuweza kupata Halmashauri, ili tuweze kuhudumia wananchi kwa ukaribu. Tunavyo vituo vya afya vya kutosha zaidi ya vinne, na viwili tayari vinafanya shughuli ya upasuaji, kwa hiyo, ni imani yangu kwamba Wizara husika italichukua hili na italifanyia kazi kadri inavyowezekana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sikupata fursa ya kuchangia kwenye bajeti ya Waziri Mkuu, kulikuwa na suala zima la Baraza la Uwezeshaji la Taifa. Kama ambavyo Hotuba ilivyotoka Baraza hili ndilo litakalohusika na dhana nzima ya hizi shilingi milioni 50 kwa kila kijiji na kwa kila mtaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu ni kwamba, ahadi ya milioni 50 imetokana na zao la kisiasa, kwamba ni utekelezaji wa Ilani ya Chama lakini kwa kuwa tuna uzoefu na mamilioni ya JK; kwamba hayakuwafikia walengwa waliokusudiwa, nitoe rai kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu na Baraza zima hili wa Uwezeshaji kwamba pesa hizi zipitie kwenye mabenki. Mabenki ambayo yana network mpaka kwenye vijiji hata kama ni microfinance pesa hizi zitengenezewe utaratibu tusije tukajidanganya tukazipeleka kwa Makatibu wa Vijiji, ama zikaishia kwenye halmashauri halafu wao ndio wazipeleke huko; tunaweza tukakumbana na kadhia kama ambayo tumekutana nayo katika mamilioni ya JK.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo nataka kuchangia ni suala zima la mazao ya kilimo. Serikali ya Awamu ya Tano imejipambanua wazi kwamba tunataka kwenda kwenye uchumi wa kati wa viwanda, ni jambo zuri. Yako mazao ambayo hayapo katika utaratibu huo wa kuwa kwenye viwanda vikubwa; mfano mazao yanayotokana na mbogamboga. Mazao haya kwa halmashauri ya Wilaya ya Lushoto ni kama viazi, kabichi, karoti, nyanya, vitunguu na kadhalika. Mazao haya huwa wanatumia mfumo wa lumbesa kuyapeleka masokoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo huu ulikuwa ni wa unyonyaji sana kwa wakulima. Kwa hiyo, mwisho wa siku mkulima hawezi kupata tija kwenye mazao ambayo anatumia muda mrefu kuyazalisha. Niiombe Serikali kupitia halmashauri waweke utaratibu mzuri wa kuzibana halmashauri zote ziweze kudhibiti huu ufungaji wa mazao kupitia lumbesa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu huu utawasaidia hao wananchi ambao hawawezi kwenda kwenye uchumi wa viwanda; waweze kupata mazao yao katika ubora mzuri wa kupata tija ya faida ya mazao ambayo wanayazalisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la uwezeshaji wa wananchi kupitia miundombinu ya masoko. Huko vijijini masoko bado ni tatizo kama ambavyo nimetangulia kusema kwamba Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto inapokea wageni kutoka maeneo mbalimbali kutoka Zanzibar na Comoro, lakini bado hatuna miundombinu mizuri ya masoko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe rai kwa Baraza la Uwezeshaji la Taifa kwamba watujengee masoko na kwa kupatikana masoko; inaweza ikawa ni tiba mojawapo ya kupunguza haya matatizo ya lumbesa kwa sababu naamini wakulima watakuwa wanauza mazao yao katika masoko yaliyoko karibu na maeneo yao, hawatakuwa na haja ya kuwauzia wachuuzi ambao huwa ndiyo wanapeleka katika mtindo wa lumbesa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la utawala bora; nimefarijika kuona katika Hotuba ya Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora wamezungumzia suala zima la uanzishaji wa Idara ya Mikataba na Utendaji Kazi Serikalini. Jambo hili ni jema, tunaomba lifanyiwe kazi na utaratibu uanze mara moja ili mwisho wa mwaka waweze kupima tija ya wafanyakazi wa umma pamoja na wafanyakazi katika idara mbalimbali za Serikali. Hii itazidi kuongeza uwazi na uwajibikaji miongoni mwa Taasisi na Idara za Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la chaguzi zetu ambazo tumekuwa tunaendelea kuzifanya. Lazima tukumbuke kwamba chaguzi hizi zinafanywa kwa mujibu wa sheria, lakini pia zipo tume ambazo zinasimamia, ni vizuri sana tusilitumie Bunge kama sehemu ambayo kila siku tunaongelea jambo ambalo limekuwa linatolewa ufafanuzi mara kwa mara. Tunapozungumza dhana zima ya utawala bora pamoja na utumbuaji wa majipu tusijaribu kuegemea upande mmoja hata kwenye vyama vyetu ni lazima tuhakikishe kwamba dhana nzima ya utawala bora pia inapatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mfano ambao nisingependa sana kuutumia kwa jinsi ambavyo namuheshimu kaka yangu Mheshimiwa Zitto Kabwe, lakini naomba tu niutumie, kwamba hata yeye alipokuwa na kesi na chama „X‟ siku ambayo hukumu imesomwa basi wamemtangazia pale pale mahakamani kwamba kuanzia wakati ule sio mwanachama wa chama kile, hawajampa hata muda wa kufanya hiyo natural justice. Sasa haiwezi ikawa akijisaidia kuku ndiyo kajisaidia, lakini akijisaidia bata basi inakuwa ni matatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Ezekiel Wenje Mbunge wa Nyamagana kwenye Bunge lililopita, alizungumza sana kuhusu suala la Mheshimiwa Kabwe ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, sasa leo anatumbuliwa hadharani bado watu tunahoji kwa nini huyu mtu hapewi haki ya kusikilizwa. Niwaombe tunaposema upinzani, tunataka kwamba tuwe na Serikali mbadala na naamini kwamba upinzani wa kweli umeondoka na Mheshimiwa Zitto Kabwe na Mheshimiwa Dkt. Willbroad Slaa, uliobaki Bungeni sasa hivi ni upingaji sio upinzani, tumeona kete moja ya ACT Wazalendo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Na mimi naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri, ameitendea haki Wizara hii tangu Serikali ya Awamu ya Nne na hii ya Tano. Vilevile nampongeza Dkt. Yamungu Kayandabila, nadhani hii ni hotuba ya kwanza ambayo tumekuja humu ndani tukiwa very comprehensive; ina information za kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nampongeza na Naibu Waziri Mheshimiwa Dkt. Angeline Mabula, naye naamini kwamba ameitendea haki nafasi ya wanawake katika uongozi. Mheshimiwa Waziri pamoja na watendaji wote wa Wizara yako, kwa kweli lazima tuwatendee haki; na kama ambavyo Mheshimiwa Rais anasema tumuombee dua, naamini Watanzania wote watakubaliana na mimi kwamba dua hizo pia tuzielekeze katika Wizara yako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, Wizara yake inapambana na mapapa wakubwa wa ardhi, lakini tumeona anavyothubutu na kuchukua maamuzi ambayo yana tija kwa wananchi walio wengi. Mimi binafsi napenda nimpongeze kwa kutupatia Halmashauri ya Lushoto Baraza la Ardhi, hiki kilikuwa ni kilio cha miaka mingi na tunaposema Baraza la Ardhi wote tunafahamu kwamba wanaoathirika zaidi na masuala ya ardhi ni akinamama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zamani wanawake kule Lushoto hasa wale wajane ilikuwa ni lazima wasafiri kwenda mpaka Korogwe wakati mwingine anaambiwa aje na mashahidi wasiopungua sita, sasa yeye ni mjane anaambiwa leta mashahidi, awasafirishe, wakati mwingine awalaze. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri amesikia kilio chetu kwa haraka sana na amechukua hatua na ofisi ile imefunguliwa rasmi Mei 13, tunamshukuru sana na naamini dua hizi za wajane pia zitaelekea kwake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwenye hii orodha ya mashamba na migogoro ya matumizi bora ya ardhi, katika Wilaya ya Lushoto ameainisha maeneo mawili. Kuna shamba namba 902/3 lakini pia kuna eneo la Kijiji cha Shumenywelo pamoja na shamba la misitu ya hifadhi la Shume. Mgogoro ule ni wa siku nyingi, namwomba sana afike Lushoto akatatue mgogoro huu, umechukua muda mrefu sana na naamini kwa kasi hii ambayo ameanza nayo na ambayo naamini kwamba sio nguvu ya soda atafika maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo tunalo tatizo la shamba la Mnazi, Mnazi Sisal Estate, lilikuwa chini ya mamlaka ya mkonge. Kama yalivyo mashamba mengine yote na lenyewe limebinafsishwa. Shamba hili lina ukubwa wa takriban hekari 6,000 na ndani yake yapo mashamba matatu. Amepewa mwekezaji mmoja kutoka nchi jirani ya Kenya. Wakati anakabidhiwa shamba hili, amekabidhiwa hekari 1,500 zenye mkonge. Hivi ninavyozungumza hapa, hekari ambazo zina mkonge ni 45 tu. Kwa hiyo, kadri muda unavyozidi kwenda ndiyo anavyozidi kushusha uzalishaji. Nimwombe Mheshimiwa Waziri, shamba hili tulirudishe kwenye miliki ya Serikali halafu tutalitafutia uwekezaji mwingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, shamba hili pia lina migogoro na vijiji vinavyolizunguka, kipo Kijiji cha Kwemng’ongo na Kijiji cha Kwemkazu. Hawa kuna wakati fulani mwekezaji huyu aliwapa hekari 750, lakini baadaye amewanyang’anya kwa hiyo, naomba sana suala hili tulifanyie kazi kwa sababu ardhi hii imekaa haina kazi yoyote na Wilaya ya Lushoto kwa ujumla ina matatizo ya ardhi na hii ndiyo ardhi pekee ambayo tunaweza tukaipata kubwa ya kuweza kutusaidia katika masuala mazima ya uwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo Wilaya ya Lushoto maeneo mengi sana yanamilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania. Kwa ukweli wanayamiliki kihalali, lakini yapo baadhi ya maeneo ya Taasisi haswa shule pamoja na vituo vya afya yapo katika maeneo haya. Nimwombe Mheshimiwa Waziri kwamba, kwa busara anaweza akatukutanisha nao ili angalau yale maeneo ambayo yanatumiwa na umma waweze kuyatoa kwenye hati zao ambazo wanazimiliki kwa mujibu wa taratibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni suala zima la land bank, kwamba Halmashauri zetu nyingi hazina hifadhi ya ardhi na huko kwenye Halmashauri wanatoa ardhi hovyo hovyo hasa kwa watu ambao wanakuja mara nyingi kwa kigezo cha uwekezaji. Sasa niombe Wizara kupitia sera ije na sera mahsusi ambayo inazitaka Halmashauri zetu zitenge maeneo mahsusi kwa ajili ya uwekezaji, kwamba yawepo tu, yawekwe kama hifadhi ya ardhi kwa ajili ya uwekezaji wa siku za usoni. Kama ambavyo juzi Mheshimiwa Mbowe alikuwa anazungumzia suala la hekta 11,000 – zile kwenye suala la uwekezaji wa ardhi ni chache sana. Kwa hiyo, nataka niseme kwamba ni lazima kuwe na sera madhubuti ambayo inalizungumzia suala hili ili tunapo zungumza kwamba tunataka maendeleo tuwe na ardhi, watu na siasa safi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siasa safi hapa ni good policy. Policy ambazo ni nzuri za kuweza kuwa na matumizi bora ya ardhi ili iweze kuleta tija kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo, naomba nikushukuru sana na niwapongeze pia timu ambayo inamsaidia Mheshimiwa Waziri, tunawatakia kazi njema na ufanisi mwema. Ahsanteni sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona na mimi nichangie katika bajeti hii muhimu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nianze na suala la Mkaguzi na Mdhibiti wa Serikali (CAG) kwamba pesa alizotengewa shilingi bilioni 44.7 ni pesa ambazo haziwezi zikamfanya afanye kazi yake kwa ufanisi. Tunapozungumza matatizo yaliyoko kwenye Halmashauri zetu tunayatambua na Serikali ya Awamu ya Tano imejipambanua kwamba ni Serikali ambayo imekuja kudhibiti ufisadi, sasa huyu mtu ambaye ndiye anayetambua ngazi ya mafisadi katika ngazi ya Halmashauri na kwenye taasisi tunapompa fungu dogo maana yake tusitarajie kwamba hata yale majipu yatakuja kupasuliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tumeona kwamba ofisi hii tangu imeanza kufanya kazi imekuwa inafanya kazi nzuri sana, kazi ambayo kila mwaka ilikuwa inatoa tija na ilikuwa inaleta mwanga hata kwenye Halmashauri zetu na walikuwa wanatujengea uwezo hata Waheshimiwa Wabunge kupitia Kamati hizi za LAAC namna ambavyo tunaweza kudhibiti mianya ya pesa za Serikali ambazo zinapotea kupitia Halmashauri zetu.
Kwa hiyo, nitoe rai kwa Waziri wa Wizara husika aliangalie suala hili kwa jicho la tahadhari sana kwamba kama tutamnyang’anya CAG uwezo maana yake ufisadi uliotamaliki katika Halmashauri zetu utaendelea zaidi kutafuna miradi mbalimbali inayoelekea katika Halmashauri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili nizungumzie suala la gratuity (mafao haya ya Ubunge). Mimi niseme kwamba Mheshimiwa Waziri amewahisha shughuli, suala la mwaka 2020 analizungumza leo, niungane na wenzangu kusema kwamba anatu-beep Wabunge. Niseme Sheria Namba 4 ya mwaka 1999 inazungumzia wigo mpana wa hawa wanasiasa ambao walikuwa wamesamehewa hii kodi. Kwa nini wawe Wabunge peke yao, hili ni suala la kutufanya tuamini kwamba kweli anatu-beep. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niseme kwa kuwa kodi hii ya mwendo kasi ambayo anajaribu kwenda nayo atukimbize kwa miaka minne ambayo haina tija kwa bajeti ya mwaka huu basi alitafakari kwa kina sana na aangalie hivi vilio vya hawa Waheshimiwa Wabunge sisi huko majimboni kila jambo ni la kwetu.
Vipaimara vinatuhusu, Maulid tunamaliza sisi, kukiwa na watoto kwenye chanjo, kwenye mwenge, kwenye kila kitu sisi ndiyo tunaohusika. Kwenye majimbo huko michezo inabembwa na Wabunge na hata ukitoka kwenye mageti yetu sasa hivi pale unakuta wauza mipira wote wamejaa kwenye mageti wanasubiri zianze Jimbo Cup, utashangaa mara Mhagama Cup, Mwinyi Cup, Cosato Chumi Cup yote haya ni matatizo ambayo yanawasibu Wabunge. Naamini hata kule Mbeya mwaka huu utasikia Tulia Ackson Cup. Sasa Mheshimiwa Waziri tunakuomba sana uliangalie hili kwa jicho la tahadhari. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye tozo ya utalii ya asilimia 18 kwenye VAT kwenye suala la usafirishaji, hili nalo ni eneo ambalo lazima tuliangalie kwa jicho la tahadhari sana. Wenzetu Kenya miundombinu yao ya utalii ni wezeshi sana, Shirika la Ndege linawa-support sana katika utalii sisi bado ndiyo kwanza tumepanga tununue ndege tatu za kuweza ku-boost eneo letu la utalii.
Ningemshauri Waziri kwamba angalau tuende taratibu, hii VAT tunayotaka kuiweka kwenye tozo ya usafirishaji ya utalii hebu kwanza twende kwa tahadhari. Sasa hivi kutokana na nchi jirani ya Kenya kutokuwa na usalama wa kutosha kutokana na mashambulizi ya magaidi wa Al-Shabab sisi tuna advantage nzuri ya kuteka hili soko. Kwa hiyo, ni vizuri tusiongeze gharama za ziada, twende hivi hivi kwanza soko letu liwe madhubuti mbele ya safari huko tunaweza tukaangalia maeneo gani tunaweza tukaboresha.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala zima la reli ya Tanga – Moshi - Arusha - Musoma. Tunapozungumzia msongamano mkubwa wa mizigo na magari katika Bandari ya Dar es Salaam tiba pekee ni kuiwezesha reli ya Tanga kufanya kazi inavyotakiwa. Tunashukuru tumepata neema ya bomba la kusafirisha gesi ghafi kutoka Ziwa Albert kule Uganda mpaka Bandari ya Tanga. Sambamba na hili bomba la mafuta tungeweza kuboresha Bandari ya Tanga ili mizigo ya nchi ya Uganda pamoja na Sudan Kusini iweze kupitia Bandari ya Tanga. Tukipitisha mizigo katika bandari hii tutakuwa tumeimarisha uchumi wa Mikoa ya Kanda ya Kaskazini mpaka kule Musoma na tutakuwa tumewawezesha wananchi wote ambao wanapitiwa na hii reli ya Tanga - Arusha - Musoma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la afya. Afya yetu ya msingi inaanzia katika ngazi ya zahanati, lakini pia tunavyo vituo vya afya vingi sana katika nchi yetu. Pamoja na nia nzuri ya Wizara ya Afya kwamba watakuwa wanaleta sera kwamba kila Halmashauri iwe na hospitali ambayo inaweza ikawa na ngazi ya Hospitali ya Wilaya basi lazima pia waviangalie vituo vyetu vya afya. Kule Mlalo tunacho kituo kikubwa cha afya kinatoa huduma za upasuaji, lakini kinakosa miundombinu ya wodi za wagonjwa lakini pia miundombinu wezeshi kama ambulance kwa ajili ya kuwasafirisha hawa wagonjwa wanaofanyiwa operesheni kama ita-fail katika kituo kile cha afya.
Kwa hiyo, niiombe Wizara pamoja na kwamba safari hii wametenga takribani shilingi trilioni 1.9 ambayo ni sawa na asilimia 92 basi tujitahidi bajeti inayokuja mwakani angalau tufike asilimia 15 ili kufikia yale Maazimio ya Abuja ili tuweze kuhudumia wananchi wetu vile ambavyo inapaswa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza pia Wizara kwa kukufuta kodi kwenye vifaa vya walemavu. Mwalimu Nyerere aliwahi kusema ukitaka usawa wa binadamu ndugu zetu walemavu tuwaajiri. Kwa hiyo, niipongeze Wizara kwa kuliona hili, lakini tunaomba kwamba misaada hii waisimamie ili iende kwa wale ambao wanakusudiwa. Miundombinu hii isiishie tu kwenye wheelchair na vitu vingine vya kawaida, lakini ifike pia kwenye zile facilities kwa mfano wale ambao wanauoni hafifu vifaa vyao vyote viweze kupatikana kwa urahisi. Aidha, isingekuwa tu kuwaondolea kodi lakini pia Serikali ingeenda mbali zaidi hata kuweza kuwajengea uwezo wa kupata hivi vifaa bure kabisa kwa watu wale ambao wana ulemavu mahsusi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo nataka kulizungumzia ni suala zima la maji. Tumeona kwenye bajeti iliyopita maji yameelekezwa zaidi mjini. Tunaiomba Serikali ihakikishe kwamba pesa zilizotengwa kwa ajili ya miradi ya maji vijijini safari hii zote zinaenda.
Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Makamu wa Rais wakati wanapita kuomba kura walikuwa na kauli mbiu ya kumtua mama ndoo kichwani. Ninachoamini kwamba akina mama ambao wanabeba ndoo kichwani ni wale ambao wako vijijini, mijini maji mengi yanachotwa kwa mabomba tu nje hatua chache. Ili kumtua mama wa kijijini ndoo kichwani ni lazima tuhakikishe kwamba pesa zilizotengwa katika bajeti hii zinakwenda katika maeneo mahsusi na Wizara inasimamia miradi yote ili wananchi hao waweze kufaidika na huduma za jamii katika nchi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mwisho nimalizie kodi kwenye muamala wa simu. Hili suala nalo ni muhimu, naomba Waziri atakaposimama ku-wind up alitolee ufafanuzi maana wapo baadhi ya wanasiasa wanalipotosha huko nje kwa wananchi. Kwa hiyo, hapa inatakiwa lielezwe kwa ufasaha. Vilevile pia Wizara itumie nafasi hii kuwabana hawa wenye makampuni za simu kwa sababu wengi wanaofanya miamala ni wananchi wa kawaida na hata wale wanaofanya biashara hii ya uwakala pia ni wananchi wa kawaida ambao wanatumia mitaji yao wenyewe lakini gharama ambazo mashirika haya yanachukua ni kubwa zaidi kuliko wale mawakala wanachokipata. Unakuta wakala anapata pesa ndogo sana wakati mtaji ni wake, wafanyakazi ni wake, yeye ndiyo analipa kodi lakini makampuni haya yanachukua gawio kubwa zaidi kuliko hao mawakala ambao ndiyo wanaofanya kazi kubwa zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia katika Wizara hii muhimu kwa kukuza uchumi wa nchi yetu. Msitu wa Shagayu uliopo Wilaya ya Lushoto uliungua mwaka 2012 ambapo hekta 49 ziliungua hata hivyo mpaka sasa ni hekta 11 tu ambazo zimepandwa katika eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuungua kwa eneo la msitu huo lilisababishwa ardhi kutokuwa na vizuizi vya maji, hivyo mvua za mwaka 2015 zilisababisha maafa makubwa ya maporomoko na mafuriko katika maeneo yanayozunguka msitu huu. Mheshimiwa Waziri pamoja na eneo kubwa la msitu ambao unazungukwa na vijiji 15, lakini msitu una wafanyakazi wawili tu ilhali unazo nyumba za kutosha familia sita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo tunaomba Idara ya Misitu kupitia Wizara watuongezee watumishi wanne kufikia sita ili waweze kuhudumia vizuri eneo la msitu ikiwa ni pamoja na kuwapatia usafiri wa pikipiki kwani kwa sasa ipo pikipiki moja tu. Tunaomba ziongezwe pikipiki mbili zaidi ili ziweze kuleta tija katika kuhudumia msitu huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miundombinu inayozunguka maeneo ya msitu wa Shagayu sio rafiki, tunaomba Wizara kupitia Wakala wa Misitu ya Asili ili kuboresha miundmbinu hasa ya barabara ili isaidie kukabiliana na majanga hasa ya moto pale unapojitokeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Mbuga ya Mkomazi iliyopo katika Mikoa ya Tanga na Kilimanjaro, lakini Mlanga (lango) la kuingilia hifadhini lipo katika Wilaya ya Same, hivyo kuwasumbua watalii wanaotembelea Wilaya ya Lushoto na vivutio vyake kulazimika kwenda mpaka Same.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Wizara kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa na hususani Hifadhi ya Mkomazi kutuwekea mlango wa kuingia hifadhini kupitia Wilaya ya Lushoto katika Kata ya Lunguza, Kijiji cha Kiringo ili kukuza na kuchochea shughuli za utalii katika eneo hili la Tarafa ya Umba ili kusaidia kupunguza umaskini na kuchochea maendeleo ya watu wa Lushoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uhifadhi na ujirani bado unasuasua katika Hifadhi ya Mkomazi, hivyo kuweka mazingira hafifu ya ushirikiano baina ya hifadhi yetu na wananchi wa maeneo husika. Tunaiomba Wizara ihakikishe ile asilimia saba ya mapato yatokanayo na makusanyo ya hifadhi husika basi yaelekezwe kwenye vijiji na jamii inayozunguka hifadhi ili kuchochea shughuli za maendeleo na kupunguza uhasama baina ya hifadhi na wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro ya ardhi baina ya hifadhi zetu bado ni jambo linalosumbua sana hasa katika Kijiji cha Kiringo ambapo mpaka upo jirani sana na makazi ya watu hivyo kuleta misigano isiyokuwa ya lazima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Operesheni Tokomeza katika Wilaya ya Lushoto umeacha ardhi ya watu wakiwa na athari za kimwili, kiafya na kiuchumi. Silaha ambazo zimechukuliwa toka kwa wananchi waliopo jirani na hifadhi lakini hazikuhusika katika shughuli haramu za ujangili zirejeshwe kwa wamiliki halali ili waweze kujilinda kwa usalama wao kama walivyoziomba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni matarajio yetu kuwa uhifadhi wa misitu na mbuga zetu utaenda sambamba na ustawi wa jamii yetu ya Kitanzania kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata fursa hii ya kuchangia katika hoja ambayo ipo katika Bunge lako Tukufu. Moja kwa moja ningependa kuanza na suala la himaya ya pamoja ya ushuru wa forodha (single customs territory). Hii single customs territoryilianza mwaka 2013 lakini utekelezaji wake katika nchi za Afrika Mashariki ulianza mwaka 2014, Kenya na Uganda walianza Januari lakini ilivyofika Julai Tanzania na Rwanda nazo zikaanza utekelezaji wake hadi hivi ninavyozungumza wenzetu wa Burundi bado hawajaanza kutekeleza hii dhana nzima ya single customs territory.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanini nasema haya? Nayasema haya kwa sababu hili ni eneo mojawapo ambalo sisi kama Tanzania inawezekana ikawa tumepigwa goli kwa sababu hii mizigo ambayo inakwenda Kongo sisi tunapo-charge hapa katika Tanzania halafu wengine hawafanyi hivyo ndio hii sasa ambayo wenzetu wanatumia mwanya kupitisha bandari nyingine hizo ili kukwepa hii single customs territory.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninaomba nitoe ushauri kwa Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana na Serikali kwa ujumla kwamba kwa kuwa hii single customs territory imeanza kwa nchi za Afrika Mashariki na nchi ya Kongo walivyoona kwamba ina manufaa wakaomba wao wenyewe kwamba bidhaa zinazokwenda katika nchi yao zitozwe kodi katika maeneo yetu. Basi naiomba Serikali sasa iweze kuwaandikia Kongo ikiwezekana pia wawaombe na Mozambique nao waingie katika huu utaratibu ili kwamba bandari zote ziwe fair. Lakini kama sisi tutaendelea kutekeleza wakati Mombasa hawatekelezi kwa asilimia 100 na kule Beira hawamo kabisa katika mpango huu na kule Walvis Bay kule Namibia pia hawamo katika mpango huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hili ni jambo la Serikali kwa kuwa limeamuliwa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki basi warudi kule wakahakikishe kwamba mambo haya yanatekelezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo lina faida ambayo faida yenyewe imejificha sana sio rahisi kuonekana kwa jicho la karibu. Faida namba moja ni kwamba kabla ya utaratibu huu haujaanzishwa mizigo mingi ya kwenda Kongo ilikuwa inakuwa dumped katika nchi yetu, mizigo ambayo inatakiwa kwenda transit haiendi inabaki katika soko la ndani, matokeo yake ni kwamba nchi inakosa uwezo wa kukusanya kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hiyo, pia wakati huo hata wasafirishaji waliokuwa wanapeleka mizigo Kongo unaweza ukakuta lori limefika Kongo, akaa zaidi ya mwezi mwenye mzigo hajalipa mwezi mwenye mzigo hajalipa kodi kwa hiyo anashindwa kushusha, unakuta unatumia muda mrefu nina ushahidi wa wazi kabisa mimi ni-declare interest nilikuwa ni mdau katika eneo hili, yapo malori ambayo yanaweza yakafanya trip mbili kwa mwaka huko nyuma, lakini baada ya hii single customs territory kuanza kila mtu anaondoka hapa na mzigo ambao umelipiwa kodi anashusha kwa wakati na anarudi na tumekuwa tunatengeneza mpaka trip nane kwa mwaka. Kwa hiyo, ni jambo zuri lakini lazima lifanyiwe utafiti vizuri tuhakikishe kwamba utekelezaji wake usiwe wa nchi moja bali uwe wa Jumuiya nzima ya Afrika Mashariki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sambamba na hilo pia nizungumzie suala zima la mpango pamoja na dhana nzima ya kilimo, kwamba ni kweli kwamba huoni connection ya moja kwa moja kati ya kilimo na hii dhana nzima ya uanzishwaji wa viwanda. Kwa hiyo, ningependa kuwashauri Serikali kwamba sasa hebu ije na comprehensive information ya kuweza kufanya integration kati ya kilimo kitaungana vipi kwenda kwenye viwanda. Hivi viwanda ambavyo mjomba wangu Mheshimiwa Mwijage anavinadi lazima tupate tafsiri ni viwanda vya namna gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ninavyofahamu mimi kwa Tanzania yetu kwa sababu sisi ni wakulima basi viwanda hivi vinatakiwa viwe vingi vya maeneo yanayoendana na mazao ya kilimo ili tutengeneze wigo mpana wa kuwasaidia wananchi wetu. Hatutarajii kuwa na kiwanda pekee kitakacho ajiri watu 500 lakini tunataka tuwe na kiwanda ambacho kitaajiri watu 500 kwenye kiwanda wafanye kazi za kiwanda, lakini hawa outgrowers huku nje nao waweze kuwa supported, watu wawe busy kwenye mashamba na wawe na masoko ya uhakika kupitia hivi viwanda ambavyo tunakusudia kuvianzisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika hili ni lazima hata tafiti za kilimo zifanyike upya. Sasa hivi wakulima wetu wengi wanafanya kazi hizi za kilimo kwa mazoea, tunazungumzia tatizo kubwa la mabadiliko ya tabia nchi duniani. Hali ya hewa imebadilika, tunaona hata mvua zinachelewa sio kwa wakati kama ilivyokuwa zamani. Kwa hiyo, hii yote inategemea pia na watu wa tafiti nao waende mbali zaidi watafiti kwa hali ya hewa iliyopo sasa ni mazao gani tuyapande yanayoendana na hali ya hewa husika? Kwa hiyo, niishauri Serikali kwamba eneo hilo ni lazima walifanyie mkazo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo mazao ya biashara, mkonge, kule kwetu Mkoa wa Tanga tunalima sana mkonge na takribani mashamba 56 yaliyopo nchini, mashamba 36 yapo Mkoa wa Tanga. Kwa hiyo, naomba eneo hili pia lipewe kipaumbele ili kuweza kukuza uchumi wa Mkoa wa Tanga na nchi kwa ujumla. Ahsante sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, single customer territory imeanza utekelezaji wake mwaka 2014 Januari, kwa nchi za Kenya na Uganda na kwa Tanzania imeanza rasmi Julai, 2014. Changamoto mpaka sasa kwenye himaya hii ya forodha ya pamoja ni kwamba kati ya nchi zote tano za Afrika Mashariki ni Tanzania na Rwanda pekee ambazo zinatekeleza makubaliano haya kwa asilimia mia moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, Uganda na Kenya bado wanakusanya kwenye baadhi ya bidhaa tu, huku Burundi ikiwa haijawahi kutekeleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, dhana hii ya SCT ni njema sana kama itakuwa inatekelezwa na nchi zote wanachama. Ndio maana nchi ya Congo DRC imeomba iingizwe katika utaratibu huo. Ni jukumu la Serikali kuhakikisha kuwa nchi zote zilizoridhia SCT zinatekeleza ili kudhibiti unyonyaji wa mapato kutoka kwa baadhi ya nchi ambazo hazitekelezi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Serikali yetu iwasiliane na Serikali ya Jamhuri ya Mozambique ili kupitia bandari ya Beira pia utaratibu huu uweze kutumika. Hii itasaidia kuwadhibiti wale wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, faida za SCT; kudhibiti ukwepaji kodi kupitia mizigo ya transit, hapo awali kabla ya utaratibu huu mizigo mingine ilikuwa inashushwa ndani ya nchi yetu, hivyo kuwepo na ukwepaji kodi na kuikosesha Serikali mapato.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushindani hafifu wa kibiashara, kwa sababu wafanyabiashara hasa wakubwa walikuwa favored na utaratibu huo, kuliko wajasiriamali wadogo. Wasafirishaji wa mizigo kwenda Congo wamekuwa wakifanya trip nyingi zaidi baada ya utaratibu huu wa SCT kwa kuwa hakuna usumbufu, tofauti na ilivyokuwa huko nyuma; ilikuwa inawagharimu wasafirishaji zaidi ya miezi miwili hadi minne kusafirisha na ku-clear mizigo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo; ufufuaji wa zao la Mkonge katika Mikoa ya Tanga, Morogoro na baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Pwani, zao la mkonge limepanda thamani sana duniani na kati ya mashamba 56 yaliyopo nchini mashamba 37 yapo Mkoa wa Tanga na mengi yamekuwa mapori.
Mheshimiwa Naibu Spika, Bandari, Bandari ya Tanga ifufuliwe na kupanuliwa ili iende sambamba na ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Uganda–Ziwa Albert hadi katika Bandari ya Tanga. Hii itasaidia pia usafirishaji wa mizigo kutoka Tanga Tanzania hadi Uganda na nchi jirani ya Sudani Kusini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Viwanda, Kiwanda cha Afritex kilichokuwa kina uwezo wa kuajiri wafanyakazi 2000, kimefungwa na kipo Mkoani Tanga kikitengeneza aina mbalimbali za bidhaa za nguo. Serikali inakosa mapato, lakini pia ajira inapungua kwa kiasi kikubwa. Ahsante.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia jambo ambalo liko mbele ya Bunge letu Tukufu. Nitaanza na suala zima la kuchangia katika Kamati ya Katiba na Sheria ambayo na mimi ni Mjumbe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati yetu haikufanya kazi vizuri kwa sababu bajeti ilikuwa ni finyu. Kuna maeneo ambayo tulipaswa kwenda kufanya ili tuweze kuona uzoefu na pesa ambazo zimekwenda kwenye miradi lakini tumeshindwa kufanya hivyo. Jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba, kama utakumbuka Bunge letu Tukufu liliridhia kwamba na sisi tutoe mchango kwa wenzetu wale waliopatwa na tetemeko kule Kagera lakini pia Kamati yetu ambayo inaitazama Ofisi ya Waziri Mkuu tulishindwa kwenda hata kuwaona wenzetu wale waliokumbwa na ile kadhia. Kwa hiyo, nitarajie kwamba jambo hili tuliangalie kwa kina katika bajeti zijazo, Kamati hizi ziweze kupewa uwezeshaji wa kutosha ili zifanye kazi yake kamili ya kuisimamia Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika katika Wizara ya Sheria na Katiba, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora; Tume hii haikutengewa fedha kabisa ya kufanya kazi, zaidi ya mishahara na OC hakuna kingine ambacho kimewekwa katika Tume hii. Sasa tutakubaliana kwamba sasa hivi kwa kadri utandawazi unavyoongezeka na kadri ambavyo hata shughuli za kiuchumi zinazidi kupanuka, uwekezaji unaongezeka katika nchi yetu, basi pia matukio ya uvunjaji wa haki za binadamu nao unaongezeka. Kwa hiyo, tulitarajia kwamba, Tume hii iongezewe nguvu ya kifedha ili iweze kufanya kazi. Matukio yale yalilyokuwa yanatokea mwanzo siyo yanayotokea sasa. Sasa hivi teknolojia jinsi inavyokua na matukio nayo ya unyanyasaji na uvunjifu wa haki za binadamu nayo ndivyo yanavyozidi kuongezeka. Kwa hiyo, natarajia kwamba ofisi hii itaongezewe uwezo ili iweze ikafanya kazi yake vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tulipotembelea Ofisi ya Waziri wa Sheria, tulikutana na changamoto kwamba hata jengo la ofisi liko katika mazingira ambayo siyo mazuri sana. Mheshimiwa Mshua ambaye niko naye hapa karibu aliweza hata kupoteza fahamu tukiwa ndani ya ofisi ya Waziri wa Sheria na Katiba, kwa maana kwamba ofisi haikuwa hata na mazingira mazuri kiasi kwamba hata watumishi pale sijui hata afya zao zitakuwa katika hali gani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo niendelee katika Ofisi ya Rais, Utumishi pamoja na Serikali za Mitaa, kwamba tuna tatizo katika Halmashauri ya Lushoto. Pesa ambazo tunazipata kutokana na own source tunazipeleka kulipa Watumishi wa Serikali ambao bado hawajapata vibali vya ajira kutoka Serikali Kuu. Takribani shilingi milioni 28 zinatumika kulipa Watumishi wa Halmashauri. Kwa hiyo hii inachangia kwamba pesa hizi ambazo zilipaswa kwenda kwenye asilimia tano ya akinamama na asilimia tano ya vijana na pia asilimia 20 kwa ajili ya kuwawezesha Wenyeviti wa Serikali za Vijiji kupata posho zao zinashindwa kwenda katika eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo limekuwa ni tatizo, Wenyeviti wa Vijiji katika Halmashauri yangu wana miaka zaidi ya 10 hawajawahi kupata fedha, hili ni tatizo kubwa linawafanya sasa wanashindwa hata kutekeleza wajibu wao. Kwa hiyo, niiombe Wizara hii ya Utumishi ihakikishe kwamba inatupokea mzigo wa watumishi hawa ili angalau pesa hii iende kwenye maeneo ambayo yanahusika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala zima la watumishi pia linaenda katika Idara ya Afya. Tumejenga zahanati 10 ambazo ziko tayari lakini hazina watumishi. Tumeiunga kauli mbiu ya Serikali ya Awamu hii ya Tano ya kujenga zahanati kwa kila kijiji, lakini sasa zahanati zile zinaanza kuchakaa bila kutumika. Kwa hiyo, tunaiomba Serikali ihakikishe kwamba hawa watumishi wa afya wanaajiriwa kwa haraka ili waende kuwatumikia wananchi hawa wa Halmashauri ya Lushoto. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la ufungaji wa mazao kwa mtindo wa Lumbesa. Namwomba ndugu yangu Mheshimiwa Simbachawene kwamba hili tangazo bado halijaenea vizuri huku katika Halmashauri. Huku kwenye Halmashauri bado wanasubiri hawa wanaofunga Lumbesa kwenye yale mageti ya kukusanya ushuru, nadhani kwamba ingependeza zaidi kwa sababu hawa wanaofunga haya mazao wanafunga kutoka kwenye magulio na kwenye vijiji basi hii kazi wapewe Watendaji wa Vijiji wakishirikiana na Wenyeviti, kule kule wanakofungasha haya mazao ndiko ambako waanze kuwabana ili angalau hili tatizo liweze kuondoka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumza tatizo hili tunamaanisha kwamba akinamama ndiyo wanaoathirika sana kwa sababu ndiyo wazalishaji wakubwa katika halmashauri zetu. Utakuta wameshavuna viazi, wameshavuna nyanya na karoti halafu anakuja mwanaume anafunga kwa kadri anavyoweza, gunia moja linafungwa mpaka debe 10. Kwa hiyo, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri kwamba, ule waraka ambao ameutoa basi aendelee kuukazia ashuke mpaka katika ngazi za vijiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la TASAF; TASAF nayo ina changamoto kwa sababu vile vigezo ambavyo vimeainishwa vya kaya maskini inawezekana katika zile hatua za awali, wananchi hawakujitokeza vizuri kwenye mikutano, kwa hiyo wakajiangalia walioko kwenye mikutano maskini ni nani wakaandika wale walioko kwenye mikutano, lakini baada ya uhakiki, inaonekana kabisa kwamba maskini halisi waliachwa majumbani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naiomba Serikali pamoja na nia njema hii ya kuhakiki, naomba niendelee kwa sababu hata mimi katika pitapita zangu kuna mmoja ambaye alikuwa ni mnufaika wa TASAF yeye alikuwa siku za TASAF ndiyo ambazo ananunua bia na tulivyombaini tukatoa taarifa na akaondolewa kwenye ule mpango. Kwa hiyo, tuendelee kufanya utafiti ili watu hawa ambao hawastahiki wasiwepo katika hilo eneo la kupata hizi fedha za uwezeshaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo niongelee kuhusu asilimia tano kwa vijana na akinamama kwamba Halmashauri nyingi zinashindwa kutenga hii pesa katika Halmashauri zao na sababu ziko wazi. Huko nyuma, Serikali ya Awamu ya Nne ilikuwa imetoa matamko mengi ya kujenga haya majengo ya sekondari ambayo hakukuwa na mafungu, kwa hiyo Wakurugenzi nao kwa kuwa wanabanwa wakawa wanatafuta mahali gani wataweza kupata hizi pesa. Kwa hiyo, niombe kwamba sasa hivi hizi pesa hebu tuzitengenezee utaratibu mzuri Halmashauri wakati zinakaguliwa hasa na Kamati ile ya Serikali za Mitaa, tuangalie ni asilimia ngapi wametoa kwa ajili ya hawa vijana, ni asilimia ngapi zimetoka kwa ajili ya akinamama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama itapendeza kutokana na hili lindi la watu wenye ulemavu kuongezeka kwenda mijini, nashauri Bunge hili kwamba tufike mahali kwa nini tusipunguze japo asilimia moja katika hizi, tukatoa asilimia moja kwa vijana na asilimia moja kwa akinamama ili tukatengeneze asilimia mbili zikaenda kwa wenzetu walemavu kwa sababu huko kwenye Halmashauri ikiwa tunaweza kuwatambua itakuwa ni eneo zuri pia la kupunguza wao wasiende mijini. Kwa hiyo, kama tutaona linafaa tunaweza tukaliingiza, hizo asilimia angalau na wenzetu hawa wenye ulemavu waweze kupata asilimia hii kutoka katika mapato ya halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho nikazie kwenye asilimia 20 ambayo inapaswa kwenda kwa Wenyeviti wa Vijiji na Serikali za Mitaa. Hizi pesa Mheshimiwa Waziri Simbachawene haziendi. Halmashauri hazitengi hizi pesa, Wenyeviti hawapati posho na wakati mwingine inakwamisha hata tunapohamasisha shughuli za maendeleo, wanakosa nguvu ya ushawishi. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri akazie hili kwamba Halmashauri ziwatengee pesa hizi za posho Wenyeviti wa Serikali za Mitaa na Wenyeviti wa Vijiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami naomba nichangie kwenye Kamati hii ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama. Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza na suala zima la tozo ile ya fire. Tunapolipia road licence kuna shilingi karibia Sh.30,000 mpaka Sh.40,000 zinakwenda kwenye huduma za zimamoto kwa maana ya fire. Sasa nataka kujua kupitia Kamati na Wizara kwamba pesa hizi zinatumika katika eneo gani? Kwa sababu huduma za zimamoto katika miji mikubwa kama Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Tanga na Mbeya bado tunaona wanatumia magari ambayo hayana uwezo wa kutoa huduma hii katika maghorofa marefu zaidi. Mheshimiwa Mwenyekiti, ni matarajio yangu kwamba kwa sababu pesa hizi zinakusanywa kupitia TRA na zina uhakika wa kupatikana sasa zingekwenda kuboresha huduma ya hivi vyombo vya kuzimia moto katika manispaa zote ili angalau tuwe na vyombo vya zimamoto vya kisasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo kwa Jiji la Dar es Salaam ambalo sasa hivi tuna huduma ya mabasi yaendayo kasi, ni kweli tumeingia katika dunia ya ushindani wa teknolojia lakini gari hizi zinazobeba magari yaliyoharibika kwa maana ya breakdown bado wanaendelea kutumia land rover ambazo mara nyingi zinasababisha kuharibu zaidi hata hayo magari. Kwa sababu siyo magari yote yanayovutwa na breakdown ni mabovu, mengine labda wame-pack katika maeneo ambayo sio sahihi, kwa hiyo wakati wanayavuta haya magari wanasababisha uharibifu kwa magari yanayovutwa. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya Mambo ya Ndani kwamba yeye ni kijana wa kisasa hebu alete huu usasa katika hizi breakdown tupate ambazo zinaendana na wakati tuliokuwa nao. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nizungumzie suala zima la ulinzi na usalama hasa katika Mkoa wetu wa Tanga ambapo tulikumbwa na tukio moja ambalo lina harufu ya ugaidi. Mwezi wa Nane na wa Tisa yalitokea mapigano, watu wenye silaha walivamia baadhi ya vijiji katika Jimbo la Mlalo na Lushoto wakafikia hatua wakachoma bweni la Chuo cha SEKOMU. Kwa hiyo, ni rai yangu kwamba kwa kuwa Mkoa wa Tanga uko pembezoni mwa nchi jirani ya Kenya na tunajua kabisa kwa kule upande wa Kenya kuna tishio la Al-shabaab, basi nataraji kwamba zile harufu lazima zitakuwa zinapenya katika maeneo yetu. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia wapo askari hodari ambao wameweza kupambana katika tukio hili, kuna Inspector Joram ambaye mara ya mwisho alifanikiwa kukamata magaidi wawili wa Kisomali katika hilo kundi na hawa ndiyo waliokwenda kuonesha silaha zaidi ya tisa zilizokuwa zimefichwa kwenye kaburi na wakasaidia angalau kuufuatilia ule mtandao. Nitoe rai kwa Waziri mwenye dhamana awaone hawa vijana ambao wanafanya kazi nzuri waweze kupongezwa kwa sababu kazi waliyofanya ni kazi ya kishujaa na kizalendo. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kwa upande wa magereza tunalo gereza kongwe sana linaitwa Gereza la Kilimo la Mngalo, ni miongoni mwa magereza ya mwanzo kabisa yanayojishughulisha na kilimo. Hata hivyo, gereza hili linatumika chini ya kiwango kwa sababu lina uwezo wa kubeba wafungwa 100 lakini wapo 38. Niombe kule kwenye msongamano ikiwemo Rorya, Tarime na kwingineko basi unaweza ukawasogeza huku Mlalo waweze kutusaidia katika shughuli za kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia mwelekeo wa bajeti kwa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2017/2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianzie alipoishia Mheshimiwa Mhagama kwenye suala zima la kilimo. Naanzia hapo kwa sababu huyu ni pacha mwenzangu naye anaendesha kilimo cha tangawizi kama ambavyo mama yetu Mheshimiwa Anne Kilango amesema sasa ni zamu ya
tangawizi. Napenda kuliambia Bunge lako Tukufu kwamba kule Mlalo, Kata ya Mbaramo, Lunguza, Mnazi na lakini kule katika Jimbo la Madaba na Jimbo la Same Mashariki na Same Magharibi kule ndiko tangawizi inalimwa kwa kiasi kikubwa. Tena sisi tunalima ile tangawizi ambayo ni kilimo hai, tunatumia mbolea ya samadi ambayo inakubalika hata kimataifa. Kwa hiyo, kwa kuungana pamoja na mama yetu Mheshimiwa Anne Kilango naamini jambo hili litapiga hatua kubwa zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa hatuwezi tukawa na kilimo endelevu kama hatutawekeza kwenye kilimo cha umwagiliaji. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo ni kwamba ni asilimia moja tu ya ardhi yote ya Tanzania ambayo ni kilimo cha umwagiliaji. Ina maana Serikali inapaswa kuja na mikakati madhubuti kuhakikisha kwamba sasa kilimo chetu kisitegemee mvua. Kutokana na mabadiliko ya tabia nchi mvua zetu zimekuwa sio za uhakika tena. Kwa hiyo, ni wajibu wa Serikali kuhakikisha kwamba tunawekeza miundombinu ya mabwawa katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri zetu ili kilimo hiki kiende kutoa ajira iwasaidie Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sambamba na hilo wakati mwingine namshangaa Waziri wa Viwanda na Biashara kwa sababu viwanda anavyozungumza bado haviendi kutatua tatizo kubwa la ajira. Tunahitaji tupate viwanda ambavyo ni shirikishi, viwanda ambavyo vitasaidia kunyanyua soko la bidhaa za mazao. Tukiwa na viwanda vya vigae na malighafi hizi za ujenzi pekee bado wananchi hawa hawatakuwa na uwezo wa kununua hivyo vitu lakini bado hatutatatua tatizo la ajira. Kilimo pekee… (Makofi)
TAARIFA...
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hiyo ni nzuri lakini mimi sikuwa nazungumzia kiwanda kimoja specific, nilikuwa nazungumzia kwa maana ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ninavyozungumza pale Tanga pana kiwanda kinaitwa AFRITEX kilikuwa kinatengeneza nguo, ni mwaka wa pili sasa kimefungwa.
Mheshimiwa Waziri kila anaposimama anazungumzia viwanda vipya, hivi vya zamani vinavyokufa anavisimamia kwa namna gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia Kiwanda cha Nguo tunamaanisha kwamba wakulima wa pamba ndiyo watakaoweza kulisha pamoja na kupata soko kupitia viwanda hivi. Kiwanda cha AFRITEX pale Tanga kilikuwa kimeajiri watu zaidi ya 2,000 sasa hivi watu wale hawana ajira. Kwa hiyo, lengo langu ni kusema kwamba, pamoja na ajira za viwandani lakini pia ajira hizi zitokane na mazao yanayozalishwa na wananchi katika maeneo mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia Kiwanda cha Rhino Cement palepale Tanga kina tatizo la kupata malighafi. Tatizo lile ambalo alikuwa anakumbana nalo Dangote, Tanga Rhino Cement pia wana shida hiyohiyo. Malighafi wanayopata kutoka kwenye makaa ya mawe kule haitoshi. Uwezo wa kiwanda ni mahitaji ya malighafi tani 20,000 kwa mwezi lakini hawana uwezo wa kupata tani hizo wanaendesha kiwanda mara moja kwa wiki na kiwanda kile wakisimamisha uzalishaji kwa siku moja ina maana ajira zaidi ya watu 700 zitatetereka. Kwa hiyo, pamoja na hiyo nia nzuri lakini tunaomba kwamba viwanda vilivyopo pia viweze kuimarishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiwanda cha Chai Mponde, ni mwaka wa tano sasa hakifanyi kazi kiko kule Bumbuli. Kwa taarifa yako Jimbo la Bumbuli lina kata 18, kata 15 zote wanalima chai lakini ni mwaka wa tano sasa kiwanda kimefungwa, wananchi hawana shughuli zozote za uzalishaji kule. Maana yake ni kwamba hata Halmashauri sasa haiwezi kupata mapato kwa sababu ndani ya Halmashauri yenye kata 15 zinazolima chai, leo chai ile haina soko kwa sababu kiwanda kimefungwa. Mheshimiwa Mwijage anafahamu, Ofisi ya Waziri Mkuu hili wanalifahamu, kwa sababu PPF na NSSF wamekwenda kule lakini mpaka sasa hivi hakuna matumaini. Mheshimiwa Mwijage, sisi ni wajomba zako kule, tunakuomba utunusuru katika hili, Kiwanda cha Chai Mponde kifunguliwe ili wananchi wapate ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni Kiwanda cha Sabuni cha Foma pale Tanga. Kiwanda hiki kimenunuliwa na mwekezaji Haruna Zakaria lakini amekifunga, kimepoteza ajira zisizopungua watu 1,000. Tunaomba Serikali ikae na mwekezaji huyu kujua kwa nini amekinunua kiwanda na amekifunga, kwa sababu mitambo ipo pamoja na nyenzo nyingine zote zipo pale lakini amefunga. Sasa inawezekana wakati mwingine ni mambo haya ya kodi lakini ni vizuri sasa Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana akaenda kukutana na watu hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine niongelee suala la miundombinu ya barabara katika Mkoa wetu wa Tanga. Mkoa wa Tanga, Wilaya za Pangani na Handeni ni sehemu ambayo Mbuga ya Saadani pia inapatikana, siyo kwamba Saadani inapatikana kwa Wilaya ya Bagamoyo pekee. Ili tuweze kuimarisha utalii katika Mkoa wa Tanga, ambapo pia kuna Mbuga ya Hifadhi ya Mkomazi iliyopo katika Wilaya za Kilindi na Lushoto kwa upande wa Tanga, ni lazima sasa ile barabara ya kutoka Pwani - Pangani - Tanga iunganishwe na barabara ya kwenda Maramba – Bombomtoni – Mlalo - Same Mashariki iweze kunyanyuliwa. Hii barabara iko chini ya Wakala wa Barabara wa Mkoa, tunaomba sasa ianze kufikiriwa kuingizwa katika mpango wa kuwekewa lami. Sambamba na hilo, barabara ya kutoka Lushoto - Mlalo – Mnazi - Same kule Ndungu kwa mama yangu Mheshimiwa Anne Kilango pia lazima na yenyewe ifikiriwe kwanza kuwekwa lami. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nayazungumza haya kwa sababu uzalishaji mkubwa wa mazao ya mbogamboga na matunda katika Wilaya ya Lushoto unategemea sana barabara. Inawezekana kabisa kwamba kama kutanyesha mvua barabara ikasumbua ndani ya siku moja unaweza
ukamtia mtu hasara kubwa sana kwa sababu mazao haya yanaharibika kwa haraka. Kwa hiyo, mpango pekee ni kuhakikisha kwamba barabara hii inawekewa lami ili iweze kuwa na uhakika wa kufikisha mazao ya wananchi masokoni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho niongelee suala la MIVAF. Tumetembelea miradi mbalimbali iliyoko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kule Pemba na Unguja. Nishukuru kwamba MIVAF ni mradi ambao umesaidia sana lakini unakwisha mwaka huu mwezi Desemba. Niiombe Serikali, kuna tetesi kwamba andiko la miradi hii lipo kwenye Ofisi ya Wizara ya Fedha, tunaomba sasa wasisite waweze kuhakikisha kwamba wanasaini hii mikataba ili angalau tuweze kupata na MIVAF II. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, kule Jimboni Mlalo, tulipata mradi mmoja wa soko kupitia MIVAF lakini nasikitika kusema kwamba soko lile ni dogo sana. Sisi uzalishaji wetu wa viazi, Mheshimiwa Mhagama ni mkubwa sana, tunazungumzia takribani fuso 40 kwa kila wiki zinaingia Dar es Salaam. Bila Lushoto Dar es Salaam chipsi zitakuwa ni adimu sana. Kwa hiyo, tunaomba pamoja na mambo mengine lakini soko lile pale kwenye Kata ya Malindi ambalo limejengwa kwa fedha za MIVAF liongezewe uwezo liwe kubwa zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja iliyoko mbele ya Bunge lako Tukufu. Nami nianze kushukuru na kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Harrison Mwakyembe pamoja na Naibu wake kwa kazi nzuri ambayo ameleta. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme kwamba Wizara hii pamoja na ufinyu wa bajeti, lakini ni Wizara ambayo inaweza ikajitengenezea fedha katika maeneo mbalimbali. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mwakyembe anao wajibu wa kuhakikisha kwamba anakuwa celebrity katika hii Wizara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na Shirika la Utangazaji la Taifa TBC. Bajeti iliyopita TBC kupitia Wizara walituahidi kwamba Halmashauri 81 ambazo TBC ilikuwa haisikiki kwamba wanatafuta fedha na watahakisha kwamba katika bajeti ya mwaka huu maeneo hayo yatakuwa yamefikiwa; nasikitika kwamba mpaka sasa TBC haisikiki katika maeneo ya mbali hasa ya pembezoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejipa kazi ya kufanya utafiti, ukiondoa kule Mlalo ambako tunapakana na nchi jirani ya Kenya, lakini kule Rombo kwa Mheshimiwa Selasini pia haipatikani. Juzi nilikuwa Peramiho kwa Mheshimiwa Mhagama, nako huko wanapata redio za Msumbiji. Huko Nkasi kwa Mheshimiwa Keissy anapata redio za Kongo; ukienda Kakonko Kigoma, wanapata redio za Burundi. Sasa hii ni hatari sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposema dhima na dira ya Wizara hii ni pamoja na kuwa na Taifa linalohabarishwa vizuri linaloshamirika na kiutamaduni lenye kazi bora za sanaa na lenye umahiri mkubwa katika michezo ifikapo 2025. Bila kuwa na chombo cha habari cha Taifa ambacho kinafikia hayo maeneo, hii itakuwa ni ndoto. Kwa hiyo, naomba sana Wizara ihakikishe kwamba TBC inafanya kazi kwa ufanisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mlata hapa alikuwa anaelezea namna ambavyo Clouds FM wameanza ambayo sasa hivi ni Clouds Media. Walianza kwenye chumba kimoja, lakini sasa hivi Clouds ipo nchi nzima, inasikika kwa mawimbi haya ya FM. Tatizo la TBC ni nini? Kama tatizo ni hii teknolojia mpya kwa nini tusirudi kwenye teknolojia ya zamani? Maana wakati ule wakati wa short wave, medium wave na AM ilikuwa inapatikana nchi nzima. Hawa wasanii akina Mzee Jangala, Majuto na wengineo wote tulikuwa tunawasikiliza kwenye vipindi, hatuwaoni lakini tuna-enjoy. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tunaona kabisa huu ndiyo utamaduni wa Kitanzania; walikuwa na vipindi vizuri vya kuelimisha wakati wa Kampeni za Malaria, Kampeni za Chaguzi na kampeni mbalimbali za nchi hii. TBC sasa hivi nao wanaigiza kwenye redio hizi za kizazi kipya. Nataka nitoe tahadhari kwamba tusipokuwa makini, hata Millad Ayo ambaye ameanza juzi juzi hapa, anaweza akaja akaizidi TBC. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala zima la michezo. Mheshimiwa Waziri ameeleza michezo kwa mapana, lakini nasikitika kwamba bado michezo inaonekana kwamba ni mpaka wadau washiriki. Hakuna jitihada Mahususi za Wizara yenyewe kutenga fedha kwa ajili ya kwenda kuhuisha michezo kwenye mashule, vyuo na hata huko mitaani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasikitika sana kuona kwamba wakati wa Mwalimu Nyerere vyanzo vyetu vya bajeti vilikuwa ni vichache sana, tena tulikuwa tunategemea zaidi mazao ya kilimo, yeye aliwezaje? Wale Marijendali wote uliowataja ni wa wakati wa Mwalimu. Inashindikana vipi sasa hivi wakati michezo hii imekuwa ni kama biashara? Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, aanze kuwatambua wadau lakini pia lazima Serikali na yenyewe iweke bajeti mahususi kwa ajili ya kuhuisha michezo mashuleni, vyuoni na katika maeneo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hili, naomba nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Naibu Spika Tulia Ackson, yeye ameanzisha mashindano kule Mkoani Mbeya pamoja, Wilayani Kyela. Kwanza alianza na utamaduni na hili ndiyo eneo ambalo lipo katika Wizara ya Mheshimiwa Waziri. Pia kuna mashindano, anashindanisha ngoma za asili za makabila mbalimbali yaliyopo ukanda ule wa Mbeya. Mwaka huu kuna mpango wa kufanya mashindano haya yawe ya Kitaifa, tuone ngoma kutoka Pemba, kutoka Tanga na pengine popote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wadau kama hawa ni vizuri sana tukawaunga mkono ili angalau Watanzania hawa wa kizazi kipya ambao wanaanza kusahau mila na desturi zao waweze kujua kwamba nchi hii ina utamaduni na ina desturi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, mwaka huu pia kulikuwepo na mashindano ya Tulia Marathon,

yamefanyika katika Jiji la Mbeya. Haya ni mashindano ambayo nayo yanapaswa kuungwa mkono. Kwa sababu sasa hivi Marathon pekee tunayoitumia hapa Tanzania inayotambulika duniani ni hii ya Kilimanjaro Marathon. Kilimanjaro Marathon tayari imeshaanza kuzidiwa, sasa hivi washiriki wamekuwa ni wengi sana kiasi kwamba sasa wakati mwingine wanakosa nafasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuitumie fursa hii. Pamoja na jitihada nzuri pia za kutangaza Utalii wa Kusini, tunayo Mbuga yetu ile ya Kitulo, tunayo Ruaha, lakini hizi Mbuga hazijatangazwa vizuri. Kwa kutumia michezo hasa kutumia hii Tulia Trust tunaweza tukazitangaza vizuri kupitia Marathon, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, Wizara yake iweze kukaa na Mdau huyu kuona hii Marathon inaweza ikatambulika Kimataifa ili tupate washiriki mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala zima la michezo hasa mpira wa miguu. Mpira wa miguu sisi bado tumekuwa ni washindani wa kubahatisha. Hawa vijana wa Serengeti Boys ambao tunawapongeza sasa, huwezi ukaona successful plan ambayo inaandaa wengine. Inatokea tu kwamba ni bahati, vipaji vimekusanywa kwa wakati mmoja hasa kupitia wenzetu hawa wa Airtel Rising Star. Kwa hiyo, naomba kwamba lazima tuweke mkakati ambao utasaidia tuanze kuandaa vijana wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na kuandaa vijana wengine, tuandae sasa hii ndio iwe dira yetu ya Timu ya Taifa inayokuja. Hawa vijana tutakapomaliza mashindano haya na tukawaacha wakaingia kwenye vilabu hivi vya Kitanzania ambavyo tunajua namna ambavyo wanawalea wachezaji, tutawaharibu. Kwa hiyo, nitoe rai kwa Mheshimiwa Waziri kwa kushirikiana na TFF tuhakikishe kwamba vijana hawa tunawatunza vizuri, tutafute Mawakala wazuri wa Kimataifa, vijana hawa waweze kupata exposure ya kwenda kucheza soka nje ya nchi ili baadaye waweze kuja kusaidia Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, uendeshaji wa mpira wa miguu bado una wasiwasi mwingi. Baada ya kuondoka Rais aliyepita, Leonard Chila Tenga sasa hivi TFF pameyumba sana. Maamuzi mengi yanafanyika kwa upendeleo, kwa hila; ni hivi juzi tu hapa timu ya Simba imenyang’anywa points zake tatu nzuri kabisa. Sasa sheria ziko wazi kwamba mchezaji akiwa na kadi za njano zaidi ya tatu, haruhusiwi kucheza mchezo unaofuata. Matokeo yake yametoka maamuzi mengine bila kugusia kwamba: Je, kadi ilikuwepo ama haikuwepo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri, tuwaangalie TFF kwa jicho la karibu hasa ukizingatiwa kwamba FIFA ya wakati huu inaruhusu Serikali kuanza kuingilia kuangalia maendeleo katika nyanja hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, Mheshimiwa Waziri amezungumza hapa kwamba timu ya Everton inakuja kucheza na miongoni mwa timu moja ya Tanzania. Nataka niseme wazi kwamba Simba Sport Club ndiyo timu pekee inayoweza ikatoa uwakilishi mzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi kuishindanisha Simba na Timu ambayo imefungwa na Mbao FC.

Kwa hiyo, naombe sana Mheshimiwa Waziri kwamba hakuna haja ya kushindanisha, Simba Sport Club ndiyo wanatutoa kimasomaso kwenye mashindano ya Kimataifa, hii ni nafasi pekee.
The Written Laws (Miscellaneous Amendment) Bill, 2016
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba nitoe mchango wangu kidogo kwenye suala lililopo mbele ya Bunge lako Tukufu. Kwanza nami nipongeze mapendekezo haya yaliyoletwa na AG, amefanya kazi nzuri, japo yapo maboresho madogo, lakini dhamira yake inaonekana ni njema kabisa kwa Taifa letu hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niongelee kwenye Division ya Mahakama hii ya Uhujumu Uchumi ama Mahakama ya Mafisadi kama ambavyo imezungumzwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nami concern yangu mwanzoni ni kwenye shilingi bilioni moja kama ndiyo kianzio, lakini kwa kuwa niko kwenye Kamati ya Sheria na Katiba hata wale wadau ambao tumewaita pale kama Tanganyika Law Society wamekuja na wazo angalau ifike milioni 500. Sisi kwenye Kamati tukasema basi, kwa kuwa ufisadi umejaa zaidi katika Halmashauri zetu na huko wakati mwingine pesa zilizoko kule inawezekana ni milioni 100, 50, inaweza ikawa bado na athari kubwa sana za uchumi kwa wananchi wa maeneo husika, basi tutake tu kwamba Ofisi ya DPP, iweze kuangalia hata kesi ambazo hazijafika kiwango cha bilioni moja, lakini zina madhara makubwa kwenye jamii, basi zipate nafasi kwenye Mahakama hii Maalum.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni separation of power. Suala hili pia lilikuwepo kwenye Kamati na bado naamini kwamba, tunaposema kwamba Rais atashauriana na Mkuu wa Mahakama, haimaanishi kwamba Rais, anaingilia uhuru wa Mahakama. Kwa sababu hapa ni suala la kisera na ni suala la kiuongozi na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hii ya mwaka 77 ambayo tuko nayo, Ibara ya 33 inasema:-
(1) “Kutakuwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano.
(2) Rais atakuwa ni Mkuu wa Nchi…
Sasa unaposema Mkuu wa nchi; ina maama mihimili yote hii ipo chini yake. Hapa ndiyo Rais anapokuwa Mkuu wa Nchi. Kipengele hicho hicho kinaendelea
….. Kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu.”
Sasa hapo tunamzungumzia Rais kama Mkuu wa Nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Ibara ya 34(4) inasema:-
“Bila ya kuathiri masharti mengineyo ya Katiba hii, madaraka ya Rais wa Jamhuri ya Muungano yatatekelezwa ama na Rais mwenyewe moja kwa moja au kwa kukasimu madaraka hayo kwa watu wengine wenye madaraka katika Utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano.”
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa ndipo tunapoona nafasi ya Mwanasheria Mkuu, nadhani pia hata uwepo wake humu Bungeni ni ku-coordinate kati ya Serikali, Bunge na mhimili mwingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka nitoe mchango wangu katika eneo hilo, kwamba hapa lazima suala hili litaanzia kwenye sera na huko kwenye sera linaanzia kwenye majukwa wakati mwingine ya kisiasa na hata hii Mahakama ya Mafisadi ni suala ambalo Rais alikuwa analizungumza kwenye Mikutano ya Uchaguzi, ina maana ni suala ambalo limetokana na Ilani ya Chama ama limetokana na matakwa ya kisiasa, siyo kwamba Mahakama ndiyo iliyoomba yenyewe kwamba sasa imezidiwa na shughuli pale waanzishe Mahakama hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, huo ndiyo ulikuwa mchango wangu katika eneo hilo. Nakushukuru sana.
Muswada wa Sheria ya Upatikanaji wa Habari wa Mwaka 2016
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Na mimi nashukuru kwa kupata nafasi hii ya kuchangia katika muswada huu. Niseme tu kwamba muswada huu nimeushiriki kwa maana umepita katika Kamati ya Katiba na Sheria ambayo nami nimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Muswada huu wa Sheria ya haki ya kupata taarifa, kuainisha wigo wa taarifa ambazo umma unayo haki ya kupewa, kukuza uwazi na uwajibikaji na wamiliki wa taarifa na kuweka masharti mengine yanayohusika nayo; niseme kwamba ni muswada ambao umekuja wakati muafaka kwa sababu sasa hivi tuna ugatuzi ambapo majukumu mengi yanafanyika katika Mabaraza yetu ya Halmashauri, kwa maana huko Waheshimiwa Madiwani, Wenyeviti wa Vijiji, Vitongoji na kadhalika ndio ambao wako karibu zaidi na wananchi na kuna taarifa ambazo wanapaswa wazipate.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda kwa Kiswahili sahihi tu ni kwamba hapa tunazungumzia haki ya kupata taarifa. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge, tusichanganye; tusijipige chenga wenyewe; kuna suala la taarifa na suala la habari. Ninavyofahamu mimi ni kwamba hata habari inatengenezwa kupitia taarifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hapa tunazungumzia haki ya kupata taarifa na hasa hizi taarifa ambazo kimsingi zinatokana na maamuzi katika Idara za Serikali, Wizara za Serikali, Mashirika ya Umma lakini pia katika Ofizi za binafsi zile ambazo zina maslahi mapana ya umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme kwamba kuna maeneo ambayo nimeyaona yanahitaji yafanyiwe maboresho. Suala la kwanza ni suala zima la siku 30 za kupata taarifa. Tumezungumza na Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana, ameonyesha nia kwamba nia yao ni njema, lakini pamoja na nia yake njema hii tusichukulie zaidi kwa maana inazungumzwa na mtu na hizi Wizara unaweza ukakuta kesho akawekwa mtu mwingine ambaye hana dhamira hiyo kama yeye ambayo ametuaminisha, ni vizuri hizi siku zikatazamwa upya, kwa sababu jambo lenyewe hili siyo suala ambalo kwamba linaoneka ni geni. Ni jambo ambalo sasa hivi ukitazama kwenye website nyingi za Wizara na Idara za Serikali unaona tayari kuna taarifa ambazo zinapatikana. Kwa hiyo, inapotokea kwamba kuna taarifa mahsusi ambayo labda haiko kwenye website ya Wizara ama ya Idara, basi mwananchi angalau apunguziwe siku za kupata hizi taarifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kama tunakusudia kwamba taarifa hii aipate mwananchi yule wa kijijini, sasa inawezekana wakati huo ndiyo greda linapita, linatengeneza barabara na mwananchi huyu anataka ajiridhishe kwamba barabara hii inayotengenezwa inatengenezwa kwa kiwango gani? Atakapohitaji taarifa akaambiwa ni baada ya mwezi mmoja wakati greda limeshapita, ina maana dhana nzima ya kupata taarifa kwa wakati itakuwa haikuzingatiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme pamoja na kwamba sheria hii inakwenda kutengeneza kanuni, lakini basi hizi kanuni ziainishe ni taarifa zipi ambazo siyo lazima mwananchi aziombe? Ziwe tu tayari kwamba Halmashauri zetu zinapofanya maamuzi, zinapoazimia maamuzi fulani, basi ziwekwe kwenye mbao za matangazo, ziwekwe kwenye website, watu wawe tu wanaweza ku-access wakati wowote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, pia ni suala zima la gharama hizi ambapo tunapohitaji taarifa hizi lazima kutakuwa na gharama. Tumejaribu kuainisha kwamba zipo baadhi ya documents ambazo labda ni ya page mbili haina gharama kubwa, lakini inawezekana kuna wengine wanatafuta taarifa hizi kwa ajili ya kufanya tafiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa na wenzetu wa Shirika la SIKIKA ambao walitoa mfano kwamba pale TAMISEMI wakiwa wanahitaji taarifa yoyote ndani ya TAMISEMI wanaipata kwa muda usiozidi siku saba. Kuna taarifa ambazo wamezipata ndani ya siku moja; kuna taarifa ambazo wamezipata ndani ya siku mbili, lakini pia ziko taarifa ambazo zinapatikana kwa maximum ndani ya siku saba. Kwa hiyo, tumeona kwamba hili ni jambo zuri, lakini kwa kuwa wao taarifa hizi nyingi wanazichukua kwa ajili ya kwenda kufanya tafiti, basi ni vyema sana tukaangalia hizi siku 30 angalau Mheshimiwa Waziri pamoja na kanuni za kwenda kutengeneza lakini liangaliwe kwa jicho la upana zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala zima la uwazi na uwajibikaji. Kama tunavyoainisha kwenye suala zima la ugatuzi, maana yake ni kwamba tunaenda kuongeza uwazi na uwajibikaji kwenye Halmashauri zetu lakini kwenye taasisi zetu za umma. Kwa hiyo, hili ni jambo ambalo linapaswa tuliunge mkono na sina tatizo nalo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la muda wa kutoa taarifa kwa yule ambaye taarifa hizo hazipatikani. Kuna eneo ambalo linazungumzia kwamba mwomba taarifa akishamwandikia mtoa taarifa atamjibu ndani ya siku hizo kwamba taarifa hiyo inapatikana au ataipata mahali pengine. Siku hizi nazo bado zinaonekana ni nyingi, tungependa sana kwamba kama taarifa haziko kwa mmiliki wa taarifa aliyoombwa, basi afanye hima kwa haraka amtaarifu mhusika kwamba taarifa hizo anaweza akazipata katika eneo gani lingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo limekuwa na wasiwasi kwa wenzangu nami pia nina wasiwasi nalo ni suala zima la sheria hii kwamba inatokana na Ibara ya 18(d) ya Katiba ambayo inasema kila mtu anayo haki ya kupata taarifa. Sasa kuna maeneo ambayo ametumika kama raia, lakini tukasema kwamba pamoja na kwamba ni mapendekezo ya Kamati pia kwamba ionekane kila mtu anayo haki ya kupata taarifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kwa wenzetu wa nchi ambazo zimeendelea, hata hapa nilipo sasa hivi naweza nika-access information za Marekani na nikapata baadhi ya taarifa. Niseme tu kwamba napingana na wenzangu wanaozungumzia suala la kuweka wazi hizi sheria ambazo zimekatazwa hasa za Usalama wa Taifa, ni vyema tusiziweke taarifa hizi zikawa wazi; ziwe vilevile kwa mujibu wa sheria ile ziendelee kulindwa kwa sababu hatuwezi tukaliweka Taifa letu hadharani kwa kiasi hicho. Mambo ya usalama haya ni lazima tuyazingatie japo tunaamini kwamba yapo maeneo mengine kuna baadhi ya watumishi wanaweza wakatumia kama kichaka cha kuweza kuficha taarifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hili ni lazima wakati tunapambana na uanzishwaji wa sheria hii, lakini vilevie kubadilisha mitazamo na mind set za Watanzania, kwa sababu kuna watu ni wakiritimba tu wa kutoa taarifa hata kama taarifa hizo ni kutaka tu kujua kwamba idadi ya waathirika labda wa ugonjwa fulani katika eneo fulani ni wangapi, lakini bado mtu atakuzungusha pasipo sababu za msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa nataka tusichanganye haya mambo kwamba zipo baadhi ya Idara za Serikali wana ukiritimba tu wa kutoa taarifa, lakini pia ni lazima sana tulinde haki yetu hii ya Sheria za Usalama wa Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni eneo hili la taarifa za Jeshi letu la Polisi. Hapa ndipo ambapo napaona kidogo kuna tatizo japokuwa zipo sheria za uanzishwaji wa Jeshi la Polisi lakini tuangalie hii sheria itafanya kazi vipi kwenye zile taarifa ambazo zinatolewa na polisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo maeneo ambayo labda kumetokea ajali, kumetokea mapigano kati ya wahalifu na polisi, lakini unakuta kila polisi anayeulizwa, Afisa husika anasema mimi siyo mtoa taarifa wa Jeshi la Polisi. Kwa hiyo, kunakuwa na ukiritimba kwamba lazima habari zitoke Makao Makuu labda ya Jeshi la Polisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekana ndiyo ilivyo kwenye kanuni zao, lakini nataka sasa hili tuliangalie kwa upana zaidi, kwa sababu sasa hivi kutokana na uwepo wa mitandao hii ya kijamii, tayari ni kwamba Jeshi linaposhindwa kutoa taarifa hizi kwa wakati, watu mmoja mmoja wanaanza kuzisambaza na baadaye zinaonekana sasa kama ni sababu za uchochezi ama ni sababu ambazo hazina msaada kama ambavyo zingetolewa kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, taarifa hizi pia katika baadhi ya Idara za Serikali, Idara ya Serikali unaikuta iko Wilayani ama Mkoani, lakini bado wanakwambia kwamba taarifa hizi zinapatikana Wizarani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunapozungumza dhana nzima ya ugatuzi ni lazima sasa tusigatue tu mambo ya utawala na fedha lakini pia na hizi taarifa, hao watu walioko huko chini, wamiliki wa taarifa kama ambavyo tumependekeza kwenye Kamati wawe wahakikishe kabisa kwamba kunakuwa na Maafisa wanaotoa taarifa wakati wote na pia kama ambavyo nimependekeza kwamba taarifa zile ambazo ni edible, ambazo zinahitajika tu kwa Umma, zitolewe kupitia hata kwenye website bila kuleta haja ya kuziomba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sitakuwa na mengi, yangu ni hayo machache. Ahsante sana, nakushukuru sana.