Questions to the Prime Minister from Hon. Rashid Abdallah Shangazi (7 total)
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi hii.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, Serikali ya Awamu ya Tano imehamasisha sana shughuli za kilimo na wananchi wamehamasika sana, lakini hivi karibuni limetokea tatizo kubwa sana la ufungaji wa mazao kwa mtindo wa lumbesa lakini pia kuwepo na vifungashio ambavyo havina viwango stahiki. Jambo la kusikitisha sana ni kwamba Mamlaka za Serikali, hasa Wakala wa Vipimo na Mizani, pia Serikali katika ngazi za Halmashauri, Wilaya na Mikoa zimeshindwa kabisa kudhibiti tatizo hili la ufungaji wa mazao kwa mtindo wa lumbesa. Je, Serikali ipo tayari kuanzisha operesheni maalum nchi nzima kudhibiti tatizo hili ambalo kwa kweli linawanyong’onyeza wakulima na kuwaletea lindi la umaskini? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shangazi, Mbunge wa Mlalo kule Lushoto, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali imeendelea kusisitiza wakulima wetu nchini wanapolima mazao yao waweze kunufaika kutokana na masoko yaliyo sahihi. Tunaanza kuona baadhi ya wanunuzi kutofuata sheria, kanuni na taratibu za manunuzi ya mazao hayo pindi wanapokwenda kwa wakulima.
Mheshimiwa Spika, nimefanya ziara Wilaya ya Karatu eneo maarufu linalozalisha mazao la Lake Eyasi, eneo la Eyasi kule chini. Moja kati ya malalamiko ambayo wakulima waliyatoa ni kama ambavyo Mheshimiwa Shangazi ameeleza, lakini Serikali imeweka utaratibu wa mazao yote yanayolimwa na kuingia kwenye masoko, lazima masoko hayo yatumie vipimo halisi ili liweze kulipa bei stahiki na mkulima aweze kunufaika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunaposema vipimo stahiki maana yake kuna vipimo ambavyo tunavitumia, inaweza kuwa ni kipimo cha ndoo ambazo tunajua kuna ndoo za lita tano, kumi, ishirini, na ni rahisi pia kukadiria na bei ambayo inawekwa na wakulima inakuwa ndiyo bei sahihi. Pia kuna vifungashio kama vile magunia ya kilo hamsini, kilo mia, nayo pia ni sehemu ya vipimo halisi lakini muhimu zaidi ni kutumia mizani ambayo haina utata.
Mheshimiwa Spika, sasa imetokea wanunuzi kuwalazimisha wakulima baada ya kile kipimo halisi kuongeza tena nundu inayojulikana kwa jina la lumbesa kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameeleza, hii haikubaliki. Tumetoa maelekezo sahihi kwa Wakuu wa Mikoa wote, Wakuu wa Wilaya wote, Wakurugenzi na Maafisa Kilimo na Maafisa Ushirika wanaosimamia masoko kwenye ngazi hizo za wakulima wawe wasimamizi wa biashara inayofanywa na wanunuzi kwa mkulima pindi anapouza mazao yake ili kujiridhisha kwamba vipimo vyote vinatumika na siyo kuongeza nundu zaidi ya kipimo ambacho kinatakiwa, kwa sababu kufanya hivyo tunamnyonya mkulima na mkulima anapata hasara kwenye mazao hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo utayari wa Serikali upo na tumeshatoa maelekezo kwa Wakuu wa Wilaya. Kwa hiyo nirudie tena kutoa wito kwa Maafisa Kilimo, Ushirika, Wakuu Wa Wilaya, Wakuu wa Mikoa kwenye maeneo yao wasimamie biashara hii na kuendesha operesheni kwenye maeneo yote ya masoko ili kujiridhisha kwamba mazao yetu yananunuliwa kwa vipimo kama ambavyo vimekubalika. Huo ndiyo msisitizo wa Serikali na tutaendelea kusisitiza wakati wote. (Makofi)
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ilani ya Chama chetu cha Mapinduzi iliielekeza Serikali kuhakikisha kwamba usambazaji umeme vijijini unakamilika kufika mwaka 1922. Na Mheshimiwa Waziri Mkuu hivi karibuni kupitia Bunge hili Waziri mwenye dhamana ya nishati amekuwa akitueleza kwamba jukumu hili litakwenda kukamilika 2022 lakini pia ametupa mpaka namba za wakandarasi ili tufuatilie mwendelezo wa usambazaji umeme vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninayo masikitiko makubwa kwamba pamoja na agizo hilo, lakini sio vijiji vyote ambavyo vimeingizwa katika mpango huu; hivi tunavyozungumza wakandarasi wapo site lakini wanaruka baadhi ya vijiji kwa maana kwamba hawajapewa scope. Na zaidi ya hilo, badala ya nguzo 40 ambazo zilikuwa zinatolewa kwenye kila Kijiji sasa wanatoa nguzo 20. Sasa nilitaka kufahamu ni ipi kauli ya Serikali kuhakikisha kwamba ifikapo mwaka 2022 nchi nzima itakuwa inawaka umeme? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Shangazi, Mbunge wa Mlalo kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali imeazimia kupeleka umeme kwenye vijiji vyote na bado tumeweka dhamira ya kupeleka umeme mpaka vitongojini ikiwemo na maeneo ya visiwani. Utaratibu ambao tumeuweka ndani ya Serikali kwa zoezi hilo la kusambaza umeme, tunaenda kwa awamu na sasa tupo kwenye awamu ya tatu na hii awamu ya tatu tumeigawa kwenye awamu mbili; awamu ya tatu moja na awamu ya tatu mbili. Awamu ya tatu mbili imeanza siku za karibuni na wakandarasi tumeshawasambaza kwenye halmashauri zote ili kukamilisha vijiji vyote vilivyobaki vipate umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwenye awamu ya tatu hii mbili tumeongeza mkakati ambao nimeueleza awali wa kupeleka umeme kwenye vitongoji na kwenye visiwa kama vile kule Ukerewe, Mafia na maeneo mengine ya visiwa. Mkakati huu tayari umeshatangazwa, zabuni zimetolewa, wakandarasi wamepatikana, ujenzi wa umeme utaanza kazi mara moja. Lengo letu ni kupeleka umeme kila Kijiji na kupeleka umeme kwenye vitongoji vyote ikiwemo na visiwani ambapo tunaweza tukapeleka umeme jua ili nao wapate pia umeme kwa ajili ya matumizi ya kila siku. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, dhamira ya Serikali bado imebaki palepale na nakumbuka mwezi wa pili nilikuwa Mlalo kwa Mheshimiwa Shangazi kwa hiyo inawezekana ameuliza swali hili kama alivyokuwa amechangia siku ile kwenye mkutano wa hadhara na nikamhakikishia kwamba Serikali itapeleka umeme kwenye Jimbo la Mlalo lote, vijijini mpaka vitongojini. hivyo ni pamoja na nchi nzima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote kwamba mkakati wa Serikali wa kupeleka umeme vijijini uko imara na sasa hivi tume-cover sehemu kubwa sana; tumebaki na vijiji vichache sana ili tuweze kuvimaliza vijiji vyote, kazi inaendelea na kwa kweli kazi inaendelea. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ili niulize swali la kwanza kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sera yetu ya Elimu hasa elimu ya msingi imeelekeza kwamba elimu ya msingi ni bure kuanzia ngazi ya msingi; na zoezi hili lilikuwa linafanyika vizuri sana, tunaipongeza sana Serikali kwa hatua hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu nilitaka kuufahamu, ni upi mkakati wa Serikali katika Sera ya Afya angalau sasa katika afya msingi kwa maana ya zahanati na vituo vya afya kuweka eneohili tupate huduma za afya bure?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shangazi, Mbunge wa Mlalo kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Serikali yetu imeandaa sera upande wa elimu na kuifanya elimu sasa ipatikane bure kuanzia elimu ya awali mpaka kiwango cha sekondari, kidato cha nne na mkakati huu unasaidia sana kuwapunguzia wazazi gharama za kumpeleka mtoto shule na huku tukiwa pia tumeweka ulazima wa kila mtoto wa Kitanzania kupata elimu ya msingi ambayo kwa sasa inaenda mpaka kidato cha nne.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge anataka kujua nini mpango wa Serikali wa Sera aina ile ile ya elimu kuifanya pia kwenye sekta ya afya ili tuweze kutoa huduma za afya bure.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka tu kueleza kwamba tunaendelea kufanya mapitio ya sera zetu na hasa kwenye sekta ya huduma za jamii ili Serikali yetu iweze kutoa ikiwezekana unafuu mkubwa kwenye utoaji wa huduma za jamii kwa Watanzania ikiwemo na sekta ya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, pindi tutakapofanya mapitio haya na kukamilisha kuona uwezo wa kifedha wa kugharamia kwa upande mwingine, kwa maana ya kupata vifaa tiba, utafiti na maeneo mengine yote, Serikali itatoa tangazo wakati pale tutakapokuwa tumekamilisha utafiti huo ambao sasa hivi wataalam wetu wanaufanyia mapitio, ahsante sana. (Makofi)
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, nishati ya mafuta ni nishati ambayo ni muhimu sana kwa Taifa letu, kwanza kwa sababu ni sehemu ya ulinzi na usalama wa nchi, lakini pili pia ni sehemu ambayo inachangia kwa mawanda mapana shughuli zote za kiuchumi katika nchi yetu. Lakini miezi ya hivi karibuni kuanzia Mwezi wa Saba, Mwezi wa Nane na hata Mwezi huu wa Tisa kumekuwa na sintofahamu kwenye eneo hili la sekta ya nishati. Upatikanaji wa mafuta umekuwa ni wa mashaka pia bei zimekuwa zikibadilika bila ya kuwa na mpangilio maalum. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika hali ambayo ni ya kushangaza zaidi ni kwamba wiki moja ama mbili kabla ya kutangazwa bei ya mafuta kama utaratibu ulivyo kwamba kila Jumatano ya kwanza ya mwezi mpya bei ya mafuta zinatangazwa, mafuta huwa hayapatikani, bei ikishatangazwa tayari mafuta yanaanza kupatikana.
Mheshimiwa Spika, nataka kufahamu ni upi mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba Taifa linakuwa na mafuta wakati wote, lakini pia kuhakikisha kwamba yanapatikana kwa bei ambayo Watanzania kote nchini wanaweza kuimudu? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, kwanza ninakiri kwamba tunazo changamoto za upatikanaji wa mafuta nchini, kwa sababu baadhi ya vituo kwenye maeneo mbalimbali vimekuwa vikikosa mafuta na Watanzania wanaohitaji huduma hii maeneo kadhaa tumeona wakiwa wanalalamika kukosekana kwa mafuta.
Mheshimiwa Spika, ziko jitihada kadhaa zinafanywa na Serikali kupitia mifumo yetu ya upatikanaji wa mafuta, Wizara imekuwa ikifanya jitihada pia za kuona upatikanaji wa nishati hii unakuwepo, pia hata Kamati ya Bunge ya Nishati imekaa mara kadhaa na Wizara kuona mwenendo wa upatikanaji wa nishati hii. Nasi tunajua nishati hii ina msaada mkubwa kwenye maeneo mengi na ndiyo inasaidia pia kufanya shughuli za kiuchumi ziweze kwenda.
Mheshimiwa Spika, kufuatia mabadiliko ya Mheshimiwa Rais aliyoyafanya juzi, tumeanza kumwona Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu akifanya vikao kadhaa ndani ya Wizara kukutana na wadau. Sasa kwa kuwa ameshaanza hii kazi, niendelee kumuagiza Naibu Waziri Mkuu kushughulikia hili. Muhimu zaidi nishati yenyewe ipatikane nchini, suala la bei tunajua bei zinabadilika wakati wowote, lakini kwanza nishati ipatikane kwenye vituo vyote na maeneo yote nchini. Pili Watanzania wapate hii huduma na upatikanaji huu ni muhimu kuhusisha pia taasisi zote za mafuta, EWURA na taasisi nyingine zote wale wanunuaji wa mafuta kwa bulk, lakini pia Taasisi ya Ununuaji wa Mafuta tutengeneza kikao kikubwa na Wizara kadhaa zinazohusika, Wizara ya Fedha, Ofisi ya Uratibu, Ofisi ya Waziri Mkuu mkae pamoja, muone namna ya upatikanaji wa mafuta, suala la bei tutaanza kuliangalia hapo baadae kwa sababu bei zinabadilika kutegemeana na upatikanaji.
Mheshimiwa Spika, pia tupanue wigo wa waagizaji wa mafuta ili tuwe na mafuta mengi nchini kwa usalama wa Taifa letu. Kama hili litafanyika ndani ya wiki moja tutakuwa tumeshapata majibu na tutawapa taarifa Watanzania, lakini tutahakikisha kwamba nishati hii ya mafuta inapatikana na Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu atashughulikia hilo. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii ya kuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Waziri Mkuu kumekuwa na ongezeko la wanyama wakali hasa tembo ambao wamekuwa wakivamia maeneo ambayo yako mbezoni mwa Hifadhi za Taifa, lakini pia na mapori tengefu.
Mheshimiwa Waziri Mkuu wanyama hawa kwa nyakati tofauti wamekuwa wakiathiri shughuli za kijamii, kiuchumi lakini pia wakati mwingine kusababisha hata vifo.
Mheshimiwa Waziri Mkuu suala la ulinzi wa mali na usalama wa raia ni jukumu la Serikali. Je, ni kwa kiasi gani Serikali itawahakikishia wananchi hawa walioko pembezoni mwa hifadhi hizi usalama wao ili wasiendelee kupata athari zinazosababishwa na wanyama hao? Ahsante.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, nimeona nilijibu hili swali la Mheshimiwa Shangazi, Mbunge kutoka Lushoto kwa sababu pia nimefanya ziara maeneo mengi na nimekuwa nikilalamikiwa na Watanzania wanaoishi kwenye maeneo yaliyo kando kando na maeneo ya hifadhi kwa maslahi ya Taifa.
Nikubaliane naye kwamba Serikali inao wajibu wa kulinda mali lakini pia usalama wa raia ndani ya nchi. Pia nikiri kwamba tuna ongezeko kubwa la wanyamapori hasa baada ya kuwa tumeimarisha ulinzi kwa maana ya uvamizi, uwindaji haramu, kwa hiyo wanyama wengi wameongezeka na tembo nao pia wameongezeka sana.
Mheshimiwa Spika, huu mjadala huu nimeusikia sana pia hapa Waheshimiwa Wabunge wakichangia wakati wa bajeti ya Maliasili na Mheshimiwa Waziri amejitahidi kueleza namna Serikali inavyojitahidi kudhibiti wanyamapori wanaoingia kwenye maeneo ya makazi ya watu, lakini mashamba na kusababisha pia upotevu, uharibifu wa mali pia hata vifo kwa baadhi ya Watanzania ambao wako karibu sana na maeneo haya ya hifadhi.
Mheshimiwa Spika, ziko jitihada za Serikali zinafanyika sasa za kuhakikisha kwamba tunapunguza au kuondoa kabisa madhara haya kwa yale maeneo yaliyo pembezoni ikiwemo kwenye Jimbo la Mlalo anakotoka Mheshimiwa Shangazi ambalo linakaribiana sana na Mbuga ya Mkomazi.
Mheshimiwa Spika, na ziko Wilaya kadhaa, nimeenda Liwale, Mkoani Lindi, nimefanya ziara Wilayani Kilwa, Mkoani Lindi na hata Lindi Vijijini pia. Nimefanya ziara Mkoani Ruvuma maeneo ya Tunduru Jimboni kwa Mheshimwia Mpakate. Nimefanya ziara pia Meatu, Bariadi maeneo ambayo yamekaribiana sana na Mbuga wa Serengeti pia hata Wilaya ya Serengeti kote huko nimepita na moja kati ya vilio vya Watanzania ni ongezeko la Tembo ambao pia wanakuja hapa. Na kwenye mjadala hapa nilimsikia hata Mheshimiwa Mulugo akirejea misahafu na biblia juu ya jambo hili. (Makofi)
Sasa jitihada ambazo tumezifanya ni kwanza tumeongeza idadi ya askari wa wanyamapori na askari hawa tunawapeleka kwenye maeneo yote yaliyo karibu na makazi ya watu kwenye mbuga hizi ambazo ziko karibu na watu.
Mheshimiwa Spika, lakini pia tumeimarisha na tunaendelea kujenga amary ya hivyo vituo ambavyo vinatunza silaha ambazo zitasaidia pia angalau kuwaondoa hawa tembo warudi kwenye maeneo yao. Na sasa hivi Wizara inaendelea kuratibu ujenzi wa vituo vile 32 kando kando ya maeneo yote haya. Hata nilipokuwa Mkoani Lindi, eneo la Rondo zamani ilikuwa ni Kituo cha Maliasili ambao walikuwa wanasaidia sana kupunguza idadi ya wanyama hatari wanaoingia kwenye makazi ya watu kwa Wilaya za Lindi Vijijini, lakini pia Kilwa maeneo ya Kilanjelanje na maeneo mengine. Kwa hiyo tunarudisha vile vituo uhai wake ili tupeleke hawa askari ambao tunawapeleka kwenye maeneo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wanyama tembo pamoja na ongezeko lake Serikali haikusudii kuvuna, lakini kusudio hasa na ndio kazi kubwa tuliyonayo ni kuzuia wanyamapori kuingia kwenye makazi. Tembo yuko kwenye kundi la top five ya wanyama ambao wenyewe kazi yetu ni kuhifadhi kama sehemu ya nyara za Taifa. Tembo wenyewe, tuna simba, tuna twiga, chui na faru hawa wako kwenye top five ambao Serikali kwa namna yoyote ile itaendelea kuwahifadhi waendelee kuwa ni tunu ya Taifa letu. (Makofi)
Kwa hiyo, niwahakikishie wananchi wote wanaoishi kwenye maeneo ya pembezoni mwa mbuga ambao wameendelea kupata tatizo la tembo kwamba mkakati wa Serikali wa kuongeza askari wengi watakaokaa kwenye maeneo hayo na wakafanya kazi hiyo na tumewakabidhi TAWA wasimamie kwa kina wahakikishe kwamba madhara haya hayajitokezi tena.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tutaendelea kufanya tathmini kadri tunavyoendelea ili kupunguza athari hiyo na Mheshimiwa Shangazi eneo lile mimi nimefanya ziara Wilayani Same kwa Mheshimiwa Kilango, lakini pia nilikuja mpaka mpakani mwa vijiji vyako nimeona hiyo na nimepata malalamiko hayo. Kwa hiyo, tutaendelea kudhibiti maeneo yale ya vijiji vyako vile ambavyo tembo wanaingia kwako kutoka Mkomanzi ili wananchi waweze kuishi kwa amani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niliona nilijibu hili nifafanue niwahakikishie Watanzania kwamba Serikali inaimarisha mifumo ya kuzuia madhara haya kwa kuhakikisha tunaongeza askari wanaoweza kusaidia kuwazuia tembo wasiingie kwenye makazi ya watu. Tathmini itatuonesha zaidi nini tufanye baada ya zoezi la awali tunalotekeleza sasa, ahsante sana. (Makofi)
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi hii.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwanza nikupongeze sana kwa wasilisho zuri ambalo kwa kweli limekuja wakati muafaka katika kusimamia tasnia nzima ya Sekta ya Elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu ametaja wadau muhimu katika ushirika huu, lakini hadi hivi ninavyozungumza hakuna chombo maalum kinachoisimamia Sekta Binafsi ya Elimu, hivyo kuwa na sauti ya pamoja pale inapotimiza majukumu yake ya kutoa elimu. Tutakumbuka kwamba shule za Serikali zipo chini ya TAMISEMI na zinapokea miongozo yote kutoka TAMISEMI, lakini Shule za Sekta Binafsi na Vyuo vya Sekta Binafsi na vya Kidini hawa hawana chombo ambacho kinawaunganisha kwa pamoja. Sasa nataka tu kufahamu kwamba ni upi mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba sekta hii nayo inakuwa na chombo ambacho inaweza ikakisimamia? Ahsante.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shangazi, Mbunge wa Mlalo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Sera yetu ya Elimu imetoa nafasi kutekelezwa kupitia Sekta ya Umma ambayo ni ya Serikali, lakini pia Sekta Binafsi na ndio kwa sababu leo Taasisi za Kidini zimeanzisha shule za msingi, sekondari hata vyuo, mtu mmoja mmoja ameweza kuanzisha shule ya msingi, sekondari na vyuo na wote hawa wako kwenye utekelezaji wa Sera ya Elimu kwa pamoja.
Mheshimiwa Spika, sasa suala la chombo kwa Sera ya Elimu inavyotekeleza, Wizara ya Elimu ndio msimamizi wa sera na yeye ndio anayeshughulikia na udhibiti ubora wa elimu hapa nchini wakati usimamizi wa shughuli za kila siku kwa shule za msingi na sekondari inafanywa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Kwa hiyo matatizo yote na shughuli zote za Elimu ya msingi na sekondari zinasimamiwa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Wanapofanya hivi pamoja na Sekta ya Elimu ambayo inatambua Sekta Binafsi ambayo inafanya kazi ya kutoa elimu nchini inaingia kwenye utaratibu huo huo. Watatekeleza sera ya nchi, lakini pia watakaguliwa kwa mifumo iliyopo nchini, lakini utendaji wa kila siku utaendelea kufuatiliwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa sababu shule zote za msingi na sekondari za sekta binafsi ziko kwenye Halmashauri husika na msimamizi ni Mkurugenzi wa Halmashauri.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Mkurugenzi na Idara yake ya Elimu wataendelea kufuatilia mwenendo wa utoaji elimu nchini kupitia Idara ya Elimu watakwenda kwenye shule za sekta ya umma za Serikali watakwenda na kwenye shule za sekta binafsi ili kuona kuwa mwenendo wa utoaji wa elimu unakuwa mmoja na ndio kwa sababu wanafuata ratiba ya Serikali hata Sekta Binafsi, wanafanya mitihani ya Serikali chini ya Baraza la Mitihani pia ni pamoja na Sekta Binafsi.
Mheshimiwa Spika, hii sasa inaweza wakajua sasa sekta binafsi kwamba wanawajibika kwa Mkurugenzi wa Halmashauri husika. Suala la kuwa na chombo maalum cha sekta binafsi kwa kuwa tumesema shule za msingi, sekondari zote zinawajibika kwa Mamlaka ya Serikali za Mitaa hicho ndio Chombo chao ambacho inatakiwa kuripoti matatizo yao, mafanikio yao na kama kuna changamoto nyingine zozote zile wataripoti kwa Wakurugenzi wa Halmashauri. Shule hizo za Binafsi zinakaguliwa na Mkurugenzi wa Halmashauri kupitia chombo cha Wizara ya Elimu cha Udhibiti Ubora tulichokipeleka kwenye Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Spika, hii inafanya uendeshaji wa elimu kwa ujumla wake kuwa hauna matatizo na tumewaruhusu pia Sekta Binafsi kuanzisha umoja wao, watajadili mafanikio yao, watajadili mapungufu yao na watapeleka kwenye ngazi husika za Serikali pale ambapo wanaona kuna umuhimu wa kushirikiana na Serikali. Kwenye maboresho ya Sera hii ambayo leo tunaisoma hapa na kwamba tumeshakamilisha, tunasubiri kuzindua. Sekta Binafsi wameshirikishwa kikamilifu na waliitwa wote hapa Dodoma wamezungumza kwa pamoja, wamekubaliana, wamerudi wakiwa wameridhika na naamini wako Waheshimiwa Wabunge hapa nao wamejikita kwenye utoaji wa elimu na wao pia wanajua kwamba walishirikishwa na Serikali.
Mheshimiwa Spika, nataka niwahakikishie wadau wote wa utoaji elimu kwa Umma kwamba Sera yetu inalenga kufanya maboresho makubwa. Dhamira ya Rais wetu katika kuanzisha mchakato huu, lakini michango ya Waheshimiwa Wabunge imepelekea kukamilika kwa Sera hii na Wadau wa Sekta Binafsi ambao wamechangia, yote inapelekea kwenda kuimarisha Sera hii na iweze kutekelezeka. Kwa hiyo wajibu wetu sasa ni kuipokea na kuanza maandalizi ya kutekeleza Sera hii. Hayo ndio majibu ya msingi. (Makofi)
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, pamoja na maelezo ambayo umeyatoa ambayo yanaonesha msimamo wa Serikali lakini Ibara ya 15 (1) ya Katiba inatoa uhuru na inasema: “Kila mtu anayo haki ya kuwa huru na kuishi kama mtu huru”. Katika maelezo yako umesema kutaandaliwa kambi maalumu ya kuwaweka watu wenye ualbino. Sasa huoni kwamba kuwaweka katika makambi ni kuwanyima haki yao ya kuwa huru?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shangazi, Mbunge wa Mlalo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Sera yetu ya Serikali ni kuanza kuwalinda hawa wote wenye ulemavu wa aina yoyote ile ili pia na wao waweze kushiriki kwenye maendeleo ya Taifa letu wakiwa salama. Tunaendelea kutafuta njia mbalimbali ambazo zinaweza kuwafanya hawa kuwa salama zaidi, huku tukiimarisha ulinzi wao kwenye vyombo vyote vya ulinzi na usalama, hapa malengo yetu ni kutoa uhakika wa maisha yao wakati wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, njia hizi mbalimbali tunazozitafuta wakati mwingine tunafikiria kwamba tukiwaweka pamoja wanakuwa salama zaidi, tukiwaweka pamoja tuna tatizo la kisaikolojia la kujiona wao ni walemavu. Tumeanza kufanya marekebisho ya vijana wote wenye ulemavu kote nchini kwamba, badala ya kuwapeleka kwenye shule maalumu ya watoto wenye ulemavu wa aina hiyo, tunajaribu sasa kuwachanganya kwenye shule za msingi na sekondari pamoja ili na wao washiriki pamoja kwenye shughuli mbalimbali za kijamii, michezo wakiwa darasani na kila mmoja kwa ulemavu wake na sasa tumeanza kuona na tunaanza kupata mafanikio.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tunapoelekea kujaribu hili na kuona mafanikio haya pia Serikali imekwishaanza kutoa ruzuku kwa maana kunaongeza kwenye bajeti ya Wizara ya TAMISEMI kwenye kila Halmashauri. Tumewapelekea fedha katika kila Halmashauri ili fedha hii iende kwa wanafunzi walioko shuleni wenye uhitaji maalumu. Kwa mfano, tukiwa na mwanafunzi mwenye uono hafifu, fedha ile itatumika kununua fimbo lakini pia ule mtambo braille ya kuandikia na sasa hivi tuna kompyuta. Kwa hiyo, kila Halmashauri inawajibika kununua fimbo na braille kwa ajili ya vijana wetu ambao wana uono hafifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa wenye ualbino tunanunua lotion (mafuta ya kupaka ngozi) na kununua kofia zinazosaidia kuzuia mionzi ya jua. Hili linaendelea kutekelezwa. Vilevile, kwa wale ambao wana tatizo la viungo (hawawezi kutembea) Halmashauri inawajibika kununua baiskeli kupitia fedha ile ili mtoto aweze kutembea, kushiriki na wenzake. Hata kwenye michezo tunaona pia kuna baiskeli za walemavu wanacheza michezo kama basketball na baseball. Kwa hiyo, tunaendelea kufanya haya tukijaribu kuona ni njia ipi itaweza kufanikiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge aendelee kutupatia nafasi Serikali tuendelee kufanya tafiti na tathmini ni njia ipi nzuri zaidi inayoweza kuifanya jamii ya wenye ulemavu kushiriki kikamilifu pamoja na jamii husika kwenye shughuli mbalimbali za maendeleo, ahsante sana. (Makofi)