Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Rashid Abdallah Shangazi (17 total)

MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaharakisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wa Kata za Manolo, Shume, Sunga na Mbaru ili kuwaondolea usumbufu Wananchi wa maeneo hayo ikiwemo ushiriki hafifu kwenye shughuli za kiuchumi?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais- TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Shangazi, Mbunge wa Mlalo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Jimbo la Mlalo linakadiriwa kuwa na wakazi wapatao 196,258 kati yao ni asilimia 69 tu wanaopata huduma ya maji safi na salama. Aidha, kwa kutambua tatizo hilo, Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto ina mradi wa maji wa Shume, Madala na Manolo. Mradi huu unatarajiwa kugharimu jumla ya shilingi bilioni 2.96 hadi kukamilika ambapo kampuni ya Orange Contractor Ltd. kwa kushirikiana na Linda Technical Service Ltd. kutoka Mjini Lushoto na tayari mkataba umesainiwa. Hata hivyo, kazi hii inasubiri upatikanaji wa rasilimali fedha. Mradi huu unatarajia kuhudumia wananchi wapatao 33,541 katika Kata hizo. Mradi huu utakuwa na urefu wa kilomita 55, vituo 70 vya kuchotea maji pamoja na matenki matatu ya kuhifadhia maji.
Mheshimiwa Spika, katika Kata ya Mbaru, Halmashauri kwa kushirikiana na Shirika lisilo la Kiserikali la CHAMAVITA liliufanyia ukarabati mradi mkubwa wa maji wa Rwangi. Kwa mwaka wa fedha 2013/2014 CHAMAVITA ilitumia shilingi bilioni 96.0 kwa ajili ya kuboresha mradi huo kwa kupanua mfumo huo kutoka Kijiji cha Nkelei hadi Vijiji vya Mamboleo na Kalumele ambavyo vipo Kata ya Mbaru. Wananchi wa Vijiji hivi wanapata maji kutoka kwenye tanki la maji kwa Kwekidevu lenye ujazo wa lita 22,500.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Kata ya Sunga yenye Vijiji vitano vya Sunga, Kwemtindi, Masereka, Nkukai na Mambo inakadiriwa kuwa na wakazi wapatao 12,122. Huduma ya maji kwa Kijiji cha Mambo inapatikana kupitia visima vifupi viwili vyenye pampu ya mkono pamoja na vituo vinne vya kuchotea maji kutoka kwenye Mradi Mdogo na Mserereko ambao hauna tanki la kuhifadhia maji. Mradi huu mdogo ulijengwa na Mwekezaji wa Mambo View Hotel kwa gharama ya shilingi milioni 5.0. Katika mwaka wa fedha 2012/2013. Kwa wastani Kata ya Sunga wananchi wanaopata huduma ya maji safi na salama ni asilimia 16 tu.
Mheshimiwa Spika, vijiji vya Sunga, Kwemtindi, Masereka, Nkukai na Mambo katika Kata ya Sunga vitapewa kipaumbele mara tu baada ya vijiji kumi vya awamu ya kwanza ya programu ya maji kukamilika. Aidha, Serikali itaendelea kuboresha huduma ya maji katika Jimbo la Mlalo na maeneo mengine nchini kadri rasilimali fedha zinavyopatikana.
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:-
Kilimo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wetu na Watanzania zaidi ya 75% wanategemea kilimo kama ajira ya kuendesha maisha yao:-
Je, ni lini Serikali itaanzisha miradi mikubwa ya kuhifadhi maji (water reserves) ili kuwa na scheme itakayowezesha wakazi wa Kata za Mnazi, Lunguza na Mng‟aro kuendesha shughuli zao za kilimo msimu mzima?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Shangazi, Mbunge wa Mlalo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuendeleza kilimo cha umwagiliaji, Serikali inayo mikakati ya kujenga na kuboresha miundombinu ya umwagiliaji katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyataja, Serikali ilishajenga skimu ya umwagiliaji ya Kitivo yenye eneo la hekta 500 kwenye miaka ya 1990. Vilevile mwaka 2013, Serikali ilijenga banio kwa ajili ya skimu ya Kwemgiriti yenye jumla ya hekta 800 na Kituani Mwezae yenye jumla ya hekta 600.
Mheshimiwa Mwenyekiti, skimu hizi zinanufaisha wananchi wa maeneo ya Kata za Mng‟aro, Lunguza na vijiji vinavyozunguka Kata hizo. Chanzo cha maji ya umwagiliaji katika skimu hizo ni Mto Umba ukiunganishwa na Mto Mninga. Taarifa iliyopo kwa sasa inaonesha kuwa wingi wa maji katika Mto Umba umepungua kutokana na shughuli za kibinadamu zinazoendelea katika maeneo ya vyanzo vya mito pamoja na uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabia nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kata ya Mnazi kuna skimu ya Kwemkazu yenye eneo la hekta 150 ambayo ilifanyiwa maboresho ya miundombinu mbalimbali kati ya mwaka 2009 hadi mwaka 2013. Skimu hii inapata maji kutoka Mto Mbarama. Tatizo ambalo limejitokeza kwa sasa, mto huu unakuja na mchanga mwingi sana unaoathiri ufanisi wa banio. Tatizo hili linasababishwa na shughuli za kibinadamu na uharibifu wa mazingira kwenye vyanzo vya mto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuboresha wingi wa maji katika skimu zilizotajwa hapo juu, Serikali itafanya uchunguzi wa awali katika maeneo husika ili kuangalia kama kuna maeneo yanayofaa kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa mapya.
Aidha, namshauri Mheshimiwa Mbunge kushirikiana kwa karibu na Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto kuangalia namna bora inayoweza kufanywa kuhifadhi mazingira katika vyanzo vya mito ili kuiwezesha kutiririsha maji vizuri na kupunguza tatizo la mchanga.
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itasimamia kwa dhati sheria zake na kuondosha unyonyaji na ukandamizaji unaofanywa na wachuuzi kwa kununua mazao ya wakulima kwa utaratibu wa kufunga lumbesa?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Shangazi, Mbunge wa Mlalo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuondokana na unyonyaji na ukandamizaji unaofanywa na wachuuzi, Serikali imeamua kufanya mapitio ya Sheria ya Vipimo, Sura ya 340 ili iendane na mazingira ya sasa. Lengo la Serikali ni kumlinda muuzaji kwa kuwadhibiti wanunuzi wanaotumia njia za udanganyifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mapitio ya sheria tajwa kwetu ni suala la kipaumbele. Katika kipindi kifupi kadri iwezekanavyo Wizara yangu itawasilisha mabadiliko hayo Bungeni ili Bunge lako Tukufu lifanye marekebisho yanayostahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na marekebisho ya Sheria ya Vipimo yaliyotajwa hapo juu, Wakala wa Vipimo imewasilisha kwa Ofisi ya Rais - TAMISEMI, mapendekezo ya kutungwa kwa sheria ndogo (by laws) katika Mamlaka za Serikali za Mitaa zitakazowaongoza wakulima na wafanyabiashara kufungasha mazao kwa mujibu wa Sheria ya Vipimo na Kanuni zake. Ili kurahisisha usimamizi wa matumizi ya vipimo rasmi katika ununuzi wa mazao, Mamlaka za Serikali za Mitaa zitaainisha vituo maalum (buying and selling centre) katika vitongoji nchi nzima na kwa mazao yote na hivyo hakuna mfanyabiashara atakayeruhusiwa kusafirisha mazao ambayo yamefungashwa kinyume na Sheria ya Vipimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Wakala wa Vipimo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali za Mitaa itaanzisha vituo maalumu vya ukaguzi bila kusababisha usumbufu katika ufanyaji biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutumia fursa hii kuwatangazia Wakurugenzi wote wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuunga mkono juhudi za kupiga vita matumizi ya vipimo batili katika ununuzi wa mazao ya wakulima ikiwa ni pamoja na kutenga na kuyasimamia maeneo maalum ya kuzuia mazao (buying and selling centres). Maafisa Ugani walioko vijijini watumike kusimamia matumizi ya vipimo rasmi katika vituo hivyo na kutoa taarifa zote muhimu kwa Wakala wa Vipimo.
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itashawishi Benki za Biashara kuwekeza katika Jimbo la Mlalo ambalo mzunguko wa fedha ni mkubwa sana kutokana na magulio ya mboga mboga na matunda?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi, Mbunge wa Mlalo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuwepo huduma za kibenki katika sehemu zenye shughuli za kiuchumi kama kilimo cha mboga mboga na matunda kama Jimbo la Mlalo. Kwa sababu hiyo, Serikali imekuwa ikijitahidi kuboresha mazingira ya utoaji huduma za kibenki ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara na miundombinu ya umeme ili kuchochea zaidi shughuli za uzalishaji na hatimaye kuvutia mabenki kufungua matawi sehemu hizo. Ikumbukwe kuwa uanzishaji wa huduma za kibenki hutegemea upembuzi yakinifu ambao unazingatia uwezo wa kupata faida pande zote mbili yaani benki na wananchi. Hii pia hutegemea na uchumi wa eneo husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na mabadiliko ya kuendesha mfumo wa kifedha nchini unaotekelezwa kuanzia mwaka 1991, Serikali imekuwa ikitekeleza azma ya kujitoa katika kuhusika moja kwa moja na biashara ya mabenki. Kwa hiyo, Serikali imebaki na jukumu la kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji ili kuiwezesha sekta binafsi kuanzisha benki na kutoa huduma bora za kifedha kwa wananchi wetu, hususan pale ambapo huduma hizo zitaweza kujiendesha. Serikali inaendelea na ushauwishi wake wa Benki za Biashara na taasisi nyingine za fedha kuanzisha huduma za kibenki na kifedha popote ambapo kuna mzunguko mkubwa wa kifedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na ushawishi wa Serikali, tunamwomba Mheshimiwa Mbunge kwa kushirikiana na Serikali yetu, kuwashauri wananchi wa Mlalo kujiunga na kuanzisha Benki za Kijamii (Community Banks) na taasisi ndogo za kifedha (Micro Finance Institutions) zinazozingatia mazingira ya mahali husika ili kukidhi mahitaji ya kibenki ya Jimboni Mlalo.
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:-
Msitu wa Shagayu ndio wenye vyanzo vingi vya mito katika Jimbo la Mlalo, msitu huu uliungua takribani hekari 49 mwaka 2012:-
Je, ni lini Serikali itapanda miti katika eneo lililoungua ili kulinda vyanzo vya maji?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi, Mbunge wa Mlalo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa mwaka 2012 Hifadhi ya Msitu wa Shagayu wenye ukubwa wa hekta 8,296.8 iliungua moto ambapo eneo lililoathirika, karibu na Vijiji vya Sunga, Mtae na Mpanga lina ukubwa wa jumla ya hekta 49 sawa na asilimia 0.6 ya msitu wa Shagayu kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jitihada za kurudisha uoto wa asili katika hali yake ya ustawi kama ilivyokuwa kabla ya kuungua na pengine kuwa bora zaidi, Wizara yangu imefanya yafuatayo:-
(a) Kupanda miti rafiki kwa mazingira kama vile ocotea, mibokoboko, minyasa, markamia na mipodo katika eneo la ukubwa wa hekta 11 kati ya 49 zilizoungua, ambalo liliathirika zaidi.
(b) Kuweka mazingira ya kuruhusu kukua kwa uoto wa asili kwa njia asilia katika eneo la hekta 38, njia ambayo kwa kawaida ndiyo mbinu ya kipaumble kutumika katika uboreshaji wa maeneo ya misitu ya asili yaliyoharibika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge, kuwa hali ya ulinzi katika eneo la hekta 38 zilizoachwa zikue asilia itaendelea kuimarishwa ili kuliwezesha kukua na kurudi katika ubora wake. Aidha, Mheshimiwa Mbunge, anahamasishwa kushirikiana na Serikali na wadau wengine katika kutoa elimu na kuwashawishi wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya uchomaji moto usio rafiki kwa mazingira na hivyo kuepukana na ajali na athari za moto hususan katika misitu.
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:-
Halmashauri ya Lushoto ina mzigo mkubwa wa kulipa mishahara ya watumishi ambapo inatumia zaidi ya shilingi 28,000,000 kila mwezi kulipa mishahara ya watumishi ambao kimsingi mishahara yao ilipaswa kulipwa na Hazina kupitia Utumishi.
Je, ni lini Serikali itawatua wananchi wa Lushoto mzigo huu?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, nakushukuru na napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi, Mbunge wa Mlalo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika Halmashauri za Wilaya wapo watumishi wanaolipwa kutoka Serikali Kuu na wapo watumishi wanaolipwa kutoka katika vyanzo vya mapato ya ndani ya Halmshauri husika (own source). Utaratibu huu ulianzishwa baada ya kuonekana kuwepo kwa mahitaji maalum yanayowasilishwa na waajiri kutaka kuwaajiri watumishi wa ziada tofauti na ukomo wa bajeti ya mishahara ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto kuna jumla ya watumishi 116 ambao waliajiriwa katika utaratibu huo wa mapato ya Halmashauri (own source) kwa kuwa Halmashauri hiyo iliona inaweza kumudu gharama za kuwalipa mishahara kutokana na vyanzo vyake vya mapato ya ndani.
Mheshimiwa Spika, napenda kutoa wito kwa Halmashauri zote kuzingatia uwezo wao kabla ya kuamua kuajiri watumishi kwa kutumia vyao vyao vya mapato.
MHE. RADHID A. SHANGAZI aliuliza:-
Skimu ya Umwagilaji ya Mng’aro imekuwa haina ufanisi mzuri tangu kuanzishwa kwake.
(a) Je, ni lini Serikali itaboresha miundombinu ya skimu hiyo ili kuleta tija?
(b) Je, ni lini skimu hiyo itakaguliwa ili kuondoa malalamiko ya ubadhirifu wa mali za ushirika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi, Mbunge wa Jimbo la Mlalo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Skimu ya Umwagilaji Mng’aro (Kitivo) ipo katika Kijiji cha Mng’aro Wilaya ya Lushoto na iliibuliwa na wananchi miaka ya 1980 kwa ajili ya kuzalisha mazao ya mpunga, mahindi, maharagwe na mboga mboga. Uzalishaji wa mazao katika skimu hiyo haukuwa na tija kwa kuwa wakulima hawakuwa na miundombinu bora ya umwagiliaji ambayo ilikuwa inasababisha upotevu mkubwa wa rasilimali maji na wakati mwingine kukosa kabisa mavuno kutokana na mafuriko au ukame.
Mheshimiwa Spika, kutokana na hali hii, Serikali iliboresha skimu hiyo kati ya mwaka 1988 na 1995 kupitia fedha kutoka Mfuko wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa kwa kujenga banio kuu la kuchepusha maji kutoka Mto Umba, kuchimba na kusakafia mifereji mikuu ya kupeleka maji mashambani, kujenga vigawa maji na vivuko vya mifereji, kuchimba mifereji ya matupio ambayo ni mifereji ya kutolea maji ya ziada mashambani na kujenga barabra za kupeleka pembejeo na kutolea mazao mashambani.
Mhesmiwa Spika, katika bajeti ya mwaka 2018/2019 Serikali itaingiza skimu hii kwa lengo la kuboresha miundombinu ya umwagiliaji ili wannachi waendelee kuzalisha kwa tija.
Mheshimiwa Spika, sambamba na juhudi za Serikali, ninawaomba Waheshimiwa Wabunge kwa ujumla kushirikiana na Serikali kuhamasisha wafaidika wakulima wa skimu hiyo ili waweze kuchangia mfuko wao wa uendeshaji na matengenezo ya miundombinu ya umwagiliaji iliyokwishajengwa na Serikali.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, itatuma wakaguzi kukagua nyaraka mbalimvbali cha Chama cha Ushirika cha Skimu ya Mng’aro (Kitivo) Kijiji cha Mng’aro ili kuona kama kuna ukweli juu ya tuhuma za ubadhirifu wa mali za ushirika na hatua stahiki zitachukuliwa kwa wote watakaobainika kufanya ubadhirifu.
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:-
Je, ni lini Wilaya ya Lushoto itaanza tena kupokea matangazo ya Redio ya Taifa (TBC)?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, napenda kujibu la Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi, Mbunge wa Mlalo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kijiografia Wilaya ya Lushoto katika Mkoa wa Tanga ni kati ya Wilaya ambazo zinazozungukwa na milima, mazingira ambayo huzuia mawimbi ya TBC FM pamoja na TBC Taifa, ambayo hurushwa kutokea mitambo ya FM iliyoko katika eneo la Mnyuzi Wilayani Muheza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kutatua changamoto hii, TBC imeamua sasa mtambo wa kurushia matangazo hayo ujengwe katika Wilaya ya Lushoto ili matangazo ya redio yaweze kufika kwa uhakika katika wilaya hii. Ili kufanikisha kazi hii, TBC imetenga shilingi milioni 50 toka bajeti yake ya ndani kwa ajili ya mnara utakaotumika kuweka mtambo wenye nguvu ya watt 500 na viunganishi vyake kwa ajili ya kupokea matangazo hayo. Mtambo huu utafungwa katika eneo la Kwemashai ambako kuna miundombinu ya kuwezesha zoezi hili kukamika kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha.
MHE: RASHID A. SHANGAZI aliuliza:-
Tanzania imeridhia na kuingia mikataba mbalimbali ya kimataifa ikiwemo diplomasia na mahusiano.
Je, ni nchi ngapi na zipi ambazo Watanzania wanaweza kuzitembelea moja kwa moja kwa utaratibu wa visa on entry wakati wa kuingia ukiondoa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi, Mbunge wa Mlalo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa maelezo kwa kuwa visa ni ruhusa inayoambatana na masharti ambayo hutolewa na nchi husika ili kuwaruhusu raia wa kigeni kuingia, kuondoka au kuwepo nchini katika muda maalum. Ruhusa hiyo inapotolewa katika vituo vya kuingilia nchini inajulikana kama visa on arrival.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa utoaji visa on arrival uko katika sura ya makubaliano ama mikataba baina ya nchi na nchi au taratibu zinazotokana na matengamano na ushirikiano wa kimataifa na kikanda. Utaratibu huu unaweza kubadilika kulingana na mahusianao na hali ya usalama kati ya nchi na nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo nchi 16 ambazo Watanzania wanaweza kuzitembelea katika utaratibu wa visa on arrival. Nchi hizo ni Benin, Burkina Faso, Cape Verde, Cote d’voire, Djibout, Gabon, Gambia, Ghana, Guinea, Guinea – Bessau, Liberia, Mali, Mauritania, Niger, Sierra Leone huu wa visa on arrival, pia zipo nchi 67 duniani ambazo Watanzania wanaweza kuzitembelea bila hitajio la visa.
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:-
Chuo cha Mahakama Lushoto (IJA) kinatoa taaluma ya Stashahada za Sheria.
(a) Je, ni lini sasa Serikali itaongeza uwezo wa Chuo hicho ili kitoe elimu ya sheria kwa ngazi ya Shahada?
(b) Je, ni kwa nini Serikali sasa isione umuhimu wa kukifanya Chuo hicho kiwe Wakala wa Law School ili mafunzo ya uwakili pia yaweze kutolewa chuoni hapo?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi, Mbunge wa Mlalo, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, madhumuni ya kuwepo kwa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto ni kutoa elimu endelevu kwa watumishi wa Mahakama na watumishi wa sekta nyingine za umma wakitokea kazini na siyo kutoa elimu ya sheria kwa ngazi ya shahada. Nia na makusudi hayo inalenga katika kuwaimarisha watumishi hao wanapokuwa kazini kwa kuwapatia mbinu na nyenzo muhimu ambazo ni nadra kupatikana wakati wanapokuwa shuleni/vyuoni na hivyo kuwasaidia katika kutekeleza majukumu yao ya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Wizara bado tunaona kuwa kuna umuhimu wa kuendelea kusimamia lengo la kuanzishwa kwa chuo hicho kwani bado ni la msingi katika kuimarisha kitaaluma watumishi wa Mahakama na sekta nyingine nchini. Hata hivyo, kimeunda kikosi kazi cha kutafiti maeneo mapya ya uanzishwaji wa kozi mpya ikiwemo mafunzo ya ngazi ya Shahada ya Sheria katika Uongozi wa Mahakama (Bachelor of Law in Judicial Administration).
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyotangulia kusema, msingi wa kuanzishwa kwa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto ni kutoa elimu kwa wanaotokea kazini ili kuwapatia nyenzo muhimu kuweza kutekeleza majukumu yao vema. Mafunzo yatolewayo na Chuo cha Uanasheria kwa vitendo yanalenga kumuandaa mhitimu wa shahada ya kwanza kutekeleza kazi ya Uwakili ya Uanasheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Chuo cha Lushoto lengo ni kumwongezea mbinu za kutekeleza kazi za kutoa haki yaani Mahakimu na Majaji, mafunzo ambayo yanatolewa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, nachukua ushauri wa Mheshimiwa Mbunge ili kuangalia namna njema ya kuoanisha mafunzo yanayotolewa na vyuo hivi viwili.
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itapitia upya Sera ya Michezo nchini?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako naomba kabla ya kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi, Mbunge wa Mlalo, nitoe pole kwa ndugu, jamaa na marafiki wa Watanzania wenzetu 11 waliopoteza maisha na wengine 15 waliojeruhiwa katika ajali nyingine mbaya ya Mlima Igawilo, Mkoani Mbeya, Mungu aziweke roho zao pema peponi.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kufa ni wajibu na maisha lazima yaendelee, niruhusu vilevile nielezee kidogo yaliyotokea Uingereza usiku wa kuamkia jana kwa Mtanzania mwenzetu Hassan Mwakinyo wa Tanga kwa ushindi mnono alioupata huko Birmingham, Uingereza, baada ya kumchakaza mwanamasumbwi nyota wa Uingereza Sam Eggington katika raundi ya pili tu kati ya raundi 10. (Makofi)
Kabla ya pambano hili kufanyika bondia wa Uingereza alikuwa bondia namba nane kwa ubora duniani kati ya Mabondia 1,852 wakati Hassan Mwakinya alikuwa ni Bondia wa 174 na sasa hivi kutokana na matokeo haya Hassan ni wa 16 duniani, ni bondia bora wa kwanza Barani Afrika na bondia wa kwanza Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya haya, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi, Mbunge wa Mlalo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Sera ya Maendeleo ya Michezo inayotumika sasa hivi ni ya mwaka 1995, ni dhahiri kuwa katika miaka 23 ya sera tuliyonayo sasa tasnia ya michezo imepitia mabadiliko mengi yanayoleta hitaji la mabadiliko kisera kama vile michezo kuwa chanzo kikubwa cha ajira ya uhakika duniani, kuibuka kwa michezo ya kulipwa, ongezeko la mahitaji ya shule na vyuo mahsusi vya michezo mbalimbali kwa lengo la kulea vipaji toka udogoni kwa wavulana na wasichana, ongezeko la hitaji la viwanja vizuri na vya kutosha ngazi za shule za msingi, sekondari, vyuo, sehemu za kazi na makazi kwa lengo la kuibua viipaji na kupunguza gharama za matibabu kwa magonjwa yanayotokana na mwili kukosa mazoezi, ongezeko kubwa la mahitaji ya vifaa mbalimbali vya michezo na umuhimu wa kujenga uwezo wa ndani kuzalisha vifaa hivyo.
Mheshimiwa Spika, ni kutokana na hali hii halisi Wizara ilianzisha mwaka jana zoezi la kuipitia upya Sera ya Maendeleo ya Michezo ya mwaka 1995, zoezi ambalo limehusisha ukusanyaji wa maoni kutoka kwa wadau mbalimbali ndani na nje ya nchi. Uandaaji wa rasimu kamili ya Sera mpya ya Maendeleo ya Michezo umefikia hatua za mwisho na ni matarajio ya Wizara kukamilisha zoezi hili ndani ya muda mfupi ujao.
Mheshimiwa Spika, kupatikana kwa sera mpya kutaleta tija na kutuwezesha kuleta mabadiliko chanya katika tasnia ya michezo nchini ikiwa ni pamoja na kutuwezesha kubadili sheria iliyoanzisha Baraza la Michezo la Taifa (BMT) ili iweze kuleta ufanisi katika uendeshaji wa michezo nchini, ikiwa ni pamoja na kuainisha vyanzo rasmi na endelevu vya mapato katika maendeleo ya michezo nchini.
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:-
Gereza la Kilimo la Mng’aro ni miongoni mwa magereza kongwe hapa nchini, lakini gereza hili limekuwa na miundombinu chakavu kutokana na umri wake:-
Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka kulifanyia ukarabati mkubwa gereza hili pamoja na kuongeza uwezo wa kuchukua wafungwa wengi zaidi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Rashid Shangazi, Mbunge wa Mlalo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa Gereza la Kilimo la Mng’aro miundombinu yake ni chakavu kutokana na gereza hilo kuwa la muda mrefu, tangu mwaka 1977 hali ambayo inasababisha gereza hilo pamoja na miundombinu yake kuwa chakavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kukabiliana na changamoto hiyo Serikali linatekeleza mpango wa muda mrefu kwa nchi nzima wa kuboresha majengo hayo kwa kuyafanyia ukarabati mkubwa, ikiwemo Gereza la Mng’aro ili kuimarisha, kuyaboresha na kuyafanyia upanuzi.
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:-
Eneo la tambarare la Tarafa ya Umba na Mkomazi hususan Vijiji vya Mkundi - Mbaru, Mkundi - Mtae lina miundombinu ya majosho ya mifugo na malambo ya kunyweshea mifugo iliyo chakavu.
a) Je, ni lini sasa Serikali itaboresha miundombinu hii ili ipunguze adha ya wafugaji kuhangaika?
b) Kwa kuwa eneo hili ni la wafugaji tangu mwaka 1954, je, ni lini sasa Serikali italiwekea mpaka rasmi ili kupunguza migogoro isiyokwisha ya wafugaji na wakulima?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza uniruhusu nikutakie heri ya siku yako ya kuzaliwa hii leo na baada ya kukutakia heri ya siku yako ya kuzaliwa, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, napenda sasa kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi, Mbunge wa Mlalo, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa 2016/2017 Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto ilijenga birika la maji la kunywea mifugo katika Kijiji cha Kamba kupitia miradi ya maji ya kunywa vijijini. Pia mwaka 2017/2018 Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto kwa kushirikiana na wafugaji ilikarabati josho na birika la kunywea mifugo katika Kijiji cha Kivingo kwa gharama ya shilingi milioni 12.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2018/2019 kiasi cha shilingi milioni 4.8 zilimetengwa kwa ajili ya kukarabati majosho mawili katika Vijiji vya Mkundi-Mtae na Kiwanja ili kupunguza adha ya wafugaji kuhangaika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2018/2019 Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto imetenga shilingi milioni kumi kutekeleza mipango ya matumizi bora ya ardhi katika Vijiji vya Mkundi - Mtae, Mkundi - Mbaru na Kivingo. Aidha, utekelezaji wa mipango ya matumizi bora ya ardhi utahusisha uwekaji wa alama za kudumu kwa maana (beacon) pamoja na uendelezaji wa maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya malisho kwa kuweka miundombinu muhimu ya mifugo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe wito kwa Halmashauri zote nchini kuweka mipango ya matumizi bora ya ardhi ili kupunguza migogoro kati ya wafugaji, wakulima na watumiaji wengine wa ardhi.
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya kujenga geti la kuingilia Hifadhi ya Mkomazi katika Kijiji cha Kivingo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII aljibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi, Mbunge wa Jimbo la Mlalo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Hifadhi ya Taifa Mkomazi ipo Wilaya za Same, Mwanga, Lushoto, Korogwe na Mkinga. Kwa sasa wageni wote wanaotembelea hifadhi hii hutumia lango la Zange lililopo katika Wilaya ya Same.

Mheshimiwa Spika, katika mpango na bajeti wa mwaka fedha 2019/2020, Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) limetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa lango la wageni katika eneo la Kamakota, jirani na Kijiji cha Kivingo Wilayani Lushoto. Lango hilo limetengewa kuhudumia wageni wanaotumia barabara ya Tanga – Lushoto - Mlalo - Kihurio na Same.

Mheshimiwa Spika, sanjari na ujenzi wa lango la wageni eneo la Kamakota, Shirika la Hifadhi za Taifa limeweka kwenye mpango wake maeneo yanyotarajiwa kuwekewa malango ambayo ni Njiro (Wilaya ya Same), Ndea (Wilaya ya Mwanga) na Umba (Wilaya ya Mkinga).
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itapitia upya Sera ya Elimu kwa lengo la kuongeza tija na kuendana na mahitaji ya sasa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi, Mbunge wa Mlalo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapitio au maboresho ya Sera hufanyika kwa vipindi tofauti kulingana na mahitaji ya wakati. Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 ni matokeo ya mapitio yia Sera ya Elimu ya mwaka 1995.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuanza utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, Serikali imebaini changamoto katika baadhi ya maeneo na mengine kuwa na upungufu katika utekelezaji wake. Hivyo, Serikali imeanza mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 kwa kufanya majadiliano na wadau/wataalam mbalimbali kwa lengo la kupata maoni yao na kuhakikisha ushirikishwaji wa makundi yote muhimu unafanyika ili Sera hiyo iweze kuendana na mahitaji ya sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchakato huu wa kupitia upya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 unaendelea na kwa wakati muafaka tutawashirikisha Waheshimiwa Wabunge.
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:-

Mafuriko yaliyotokea Mlalo mwaka 1993 yalisababisha uharibifu mkubwa kwa barabara inayounganisha Tarafa za Umba na Mtae:-

Je, ni lini Serikali itatenga fedha za kukarabati barabara hiyo muhimu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi, Mbunge wa Mlalo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara inayounganisha Tarafa za Umba na Mtae yenye urefu wa kilometa 12.7 inajulikana kama barabara ya Mtae – Mtii – Mnazi. TARURA Wilaya ya Lushoto imekamilisha usanifu na tathmini ya kuifanyia matengenezo makubwa, ambapo kiasi cha shilingi bilioni 2.5 kinahitajika.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kugharamia matengenezo hayo kwa kuwa inatambua umuhimu wa barabara hii.
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa barabara ya Lushoto – Mlalo kilomita 45 kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi, Mbunge wa Mlalo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Lushoto – Mlalo yenye urefu wa kilometa 41.93 ni sehemu ya barabara ya Mkoa ya Lushoto – Mlalo – Umba Junction yenye urefu wa kilometa 66.23 inayohudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kutambua umuhimu wa barabara hii, ilianza kuijenga kwa kiwango cha lami kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Hadi kufikia Mwaka wa Fedha 2018/2019, jumla ya kilometa 8.6 zimeshakamilika kwa gharama ya Sh.5,263,802,375. Aidha, katika Mwaka wa Fedha 2019/2020, Serikali imeendelea kuitengea fedha barabara hii kwa ajili ya kuendelea na ujenzi. Sehemu iliyobaki yenye urefu wa kilometa 33 itaendelea kujengwa kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.