Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Rashid Abdallah Shangazi (124 total)

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona. Pamoja na majibu mazuri yenye kutia matumaini ya Naibu Waziri, naomba niulize swali la nyongeza kama ifuatavyo:-

Je, ni lini Serikali itakuja na mpango wa muda mfupi wa kuwapatia japo huduma ya visima virefu wakazi wa vijiji vya Maseleka, Madala na Tema wakati wanasubiri utekelezaji wa mradi huu mkubwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, kwanza Mheshimiwa Shangazi nadhani ni Mbunge kijana na ni mara yake ya kwanza ameingia Bungeni lakini ameonesha ni wazi kwamba kuingia kwake moja kwa moja ameenda katika ajenda kubwa ya suala zima la matatizo ya wananchi kuhusu suala la maji.

Mheshimiwa Spika, kutokana na ajenda hiyo naomba Serikali ichukue wazo hili, naomba tuangalie kwamba ni jinsi gani tutafanyakazi kwa pamoja ili wananchi wa Mlalo waweze kupata huduma hii ya maji. Naomba nichukue jambo hilo na naomba nimuahidi kwamba Ofisi yetu, Mheshimiwa Waziri wangu nadhani ataniruhusu nitafika kule Mlalo, licha ya ajenda ya maji nadhani ana changamoto nyingi kama Mbunge kijana lazima tumsaidie ili Jimbo lake liende vizuri.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona.
Naomba kumwuliza Waziri, kwa kuwa mbuga ya Hifadhi ya Mkomazi iko katika Wilaya za Same, Mwanga na Lushoto na kwa kuwa lengo la hifadhi hizi ni kuongeza Pato la Taifa. Je, ni lini Serikali itajenga mlango wa kuingilia katika mbuga ya Hifadhi ya Mkomazi katika eneo la Kivingo, Kata ya Lumbuza ili na Wilaya ya Lushoto nayo iweze kuchochea Pato la Taifa? Ahsante.
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu inafanya study hivi sasa ya kuangalia namna ya kuongeza milango ya kuingia katika Pori la Mkomazi na iko tayari kufungua mlango wa kuingia Mkomazi kutoka katika Jimbo la Mheshimiwa Mbunge.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu ya Waziri, lakini ninayo maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Kwa kuwa skimu ambazo amezitaja zinapita nje ya Vijiji vya Langoni A, Langoni B, Mkundyambaro na Mkundyamtae, je, Serikali haioni sasa kwamba kuna umuhimu wa kipekee wa kuwapa wananchi wa vijiji hivyo bwawa la kuhifadhia maji?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne tarehe 10 Julai, 2014, alipita katika Kata ya Mng‟aro na akatoa ahadi kuboresha miundombinu ya maji ambayo ni chakavu toka mwaka 1972. Upembuzi yakinifu umefanyika, gharama ya ukarabati ni shilingi 157,200,050/=Mheshimiwa Mwenyekiti, . Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kutimiza agizo hilo la Rais? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Rashid Shangazi, tangu niteuliwe kuwa Naibu Waziri ameshakuja ofisini mara nne kwa ajili ya kufuatilia miundombinu ya umwagiliaji pamoja na maji ya kunywa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu kwenye swali la msingi, swali (a) kwamba Serikali inafanya upembuzi wa awali ili kuweza kubaini maeneo mengine yanayoweza kujengwa mabwawa. Kwa sababu hiyo, kwenye utafiti huo utahusisha pia vijiji ambavyo Mheshimiwa Shangazi amevitaja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kuna ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne ya kukarabati miundombinu ambayo imefanya kazi kwa muda mrefu na inaelekea kupunguza ufanisi wake. Mheshimiwa Rais aliahidi kutoa shilingi milioni 152 kwa ajili ya ukarabati huo. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ahadi hiyo tumeipokea na tutaifanyia kazi.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Naomba niulize swali kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Mlalo kama ifuatavyo:-
Je, ni lini Serikali itatuletea huduma za X-ray katika Kituo cha Afya cha Mlalo ambacho kinahudumia zaidi ya wakazi elfu sitini wa Jimbo la Mlalo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii na namshukuru Mheshimiwa Rashidi Shangazi, Mbunge wa Jimbo la Mlalo, kwa swali lake la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, majibu ni kwamba, Serikali yetu ya Tanzania imeingia mkataba na Serikali ya Uholanzi ku-embark kwenye mradi mkubwa unaojulikana kama mradi wa sekta ya afya wa ORIO ambapo Serikali yetu itakuwa tayari kuchangia nusu ya Euro 22,000,000 kwa ajili ya kununua vifaa vya kufanyia uchunguzi wa magonjwa na kusambazwa kwenye hospitali zote nchi nzima. Tulikuwa tumelazimika kuchangia takribani Euro milioni 2.2 na mpaka tunavyoongea tulikuwa tumepungukiwa na kama Euro 818,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini wiki iliyopita, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dokta John Pombe Magufuli amemwelekeza Waziri wa Fedha kwamba fedha zilizokuwa zitumike kwa ajili ya semina elekezi kwa Mawaziri zielekezwe kwenda kukamilisha deni hilo la Euro 818,000 kwa ajili ya kukamilisha mchango wetu kwenye mradi huu mkubwa wa kununua vifaa. Hivyo, naamini kwamba hospitali mbalimbali nchini ikiwemo Hospitali ya Mlalo zinaweza zikapata vifaa hivyo pindi tutakapoanza utekelezaji wa mradi huu.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuuliza swali la nyongeza, kwa kuwa Kituo cha Afya cha Mlalo ndiyo kituo pekee kinachofanya huduma ya upasuaji katika Jimbo la Mlalo.
Je, ni lini Serikali itakipatia kituo hiki gari la wagonjwa ili pale ambapo upasuaji unakwama waweze kupelekwa Hospitali ya Wilaya ya Lushoto? Ahsante!
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshmiwa Naibu Spika, ni kweli Kituo cha Afya cha Mlalo kina changamoto ya gari. Lakini wiki iliyopita nilizungumza kwamba wakati mwingine hizi changamoto ni kweli, naomba ikiwezekana tuweke priority katika mchakato wa bajeti. Mheshimiwa Shangazi kwa sababu najua ni mfuatiliaji sana katika maeneo yako haya, tukiri kwamba mwaka huu Mlalo hawajapanga hii bajeti kwa ajili ya ununuzi wa gari, lakini naomba niwasisitize kwamba Ofisi ya Rais, TAMISEMI itakuwa nanyi kwa karibu kuhakikisha katika bajeti ya mwaka wa fedha unaokuja Mlalo inapewa kipaumbele au tukipata fursa yoyote ya upatikanaji wa gari basi Mlalo iwe kipaumbele kwa sababu eneo lake na jiografia yake mpaka kuja huku Mjini changamoto yake ni kubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba tulichukue hilo kama Ofisi ya Rais TAMISEMI tukishirikiana nanyi kwa pamoja kuhakikisha watu wa Mlalo baadaye wapate gari la wagonjwa ili akina mama na watoto waweze kupata huduma ya kutosha.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amesema kwamba wametenga pesa kwa ajili ya uanzishaji wa Mahakama nyingi za Wilaya na kama alivyozitaja, lakini napenda kumuuliza, ni lini sasa Wilaya ya Temeke ambayo inatumia majengo ya Halmashauri ya Manispaa ya Temeke itakuwa na majengo yake?
Mheshimiwa Naibu Spika, je, kwa Wilaya mpya ya Kigamboni ambayo imeanzishwa ni lini itapatiwa Mahakama?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
WAZIRI WA SHERIA NA KATIBA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika mpango wa miaka mitano wa ujenzi na ukarabati wa Mahakama zetu, Mahakama ya Tanzania ina mpango mzuri kabisa wa kujenga Mahakama ya Wilaya Temeke. Vile vile Mahakama Kigamboni Mheshimiwa Shangazi tayari imeshajengwa, tupo katika kumalizia tu na ni Mahakama ya kisasa ambayo ningeomba tu utakapomaliza Bunge hili ukaiangalie ndiyo mfano wa Mahakama ambazo tutakuwa tunajenga Tanzania kwa Mahakama zote za mwanzo.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa dhumuni la REA Phase One ilikuwa ni kupekeka umeme kwenye kila makao makuu ya kata na kwa kuwa Kata ya Hemtoye, Mbaramo, Mbaru pamoja na kata ya Shagayu bado hazina umeme.
Je, ni lini Serikali itapelekea umeme katika maeneo hayo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda nisahihishe kidogo, siyo kweli kama Phase One ya REA ilikuwa inapeleka kata zote ni Kata chache. REA II pia ilichagua Mikoa na Kata na maeneo ya kati. Jibu la uhakika sasa kama alivyosema ni lini sasa atapewa, REA ya Awamu ya Tatu inayoanza mwezi wa saba ndiyo itakayopeleka umeme kwenye Vijiji vyote pamoja na vya Mheshimiwa Mbunge ambavyo havijapata umeme hadi sasa.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona.
Kwa kuwa ukikaa karibu na waridi unanukia basi na mimi naomba niombee barabara yangu ya kutoka Mkomazi kwenda Mnazi, Lunguza hadi Mng‟aro sasa ifikiriwe kujengwa kwa kiwango cha lami. Naomba Mheshimiwa Waziri atuambie ni lini barabara hii itaingia katika mchakato huo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Mbunge kwamba tumepokea ombi lake na tutaenda kulifanyia kazi, muda siyo mrefu tutamletea majibu yaliyo sahihi.
MHE.RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, lakini ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa kiwanda hiki inaonekana ni teknolojia ya zamani ambayo wenzetu wa SIDO ndio ambao wameitengeneza kama alivyosema Mheshimiwa Waziri. Je, ni lini sasa Serikali itakwenda na wakati na kuwaletea wananchi hao kiwanda ambacho kinaendana na teknolojia ya kisasa ili pia kiweze kuwanufaisha wananchi wa Kata za Lugulu, Mpinji, Bombo, Vunje Maole na Ndungu?
Swali la pili, kwa kuwa katika Jimbo la Mlalo pia ni wakulima wazuri wa tangawizi na Mheshimiwa Naibu Waziri amejibu kwamba Kampuni ya Lion Wattle inanunua tangawizi, na mimi nataka nimwambie kwamba sio ukweli.
Je, Serikali ina mpango gani wa kututafutia wafanyabiashara wanaoeleweka ambao watakuja kununua mazao haya ya tangawizi katika Kata za Mbaramo, Mnazi, Wangwi pamoja na Honde?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu teknolojia inayotumika katika kiwanda cha Same, nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba tuko tayari kupitia upya na kufanyia tathimini kiwanda kile ili kuangalia kama teknolojia yake imepitwa na wakati; na ikionekana hivyo tuko tayari kuwasaidia wana ushirika ili kuweza kutafuta fursa ya kuweza kutafuta kiwanda na teknolojia ambayo inaendana na wakati. Tunaamini kwamba hii itatusaidia katika kupanua uwezo wa kiwanda ili iweze vile vile kuchukua na kusindika tangawizi kutoka maeneo mengine ikiwemo maeneo ya jirani kama Lushoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la nyongeza la pili, kuhusu kampuni ya Lion Wattle, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Ofisi yangu iko tayari kukaa na yeye. Tujadiliane kuhusu hoja hii anayoileta sasa kwamba ana wasi wasi na ukweli kwamba hiyo kampuni inanunua tangawizi. Kwa hiyo tuko tayari vizuri ni mtu ambaye anakuja ofisini kwangu mara kwa mara. Namkaribisha tena tuongee tupitie na tufananishe taarifa tulizonazo, lakini tuko tayari vilevile kuwasaidia wakulima wa Jimboni kwake Mlalo ili kuweza kupata masoko ya tangawizi ikiwa ni pamoja na yale makampuni mengine ambayo nimeyataja.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Napenda kuuliza swali la nyongeza kwa Mheshimiwa Waziri. Kumekuwa na ongezeko kubwa la akina mama wanaojifungua kwa operesheni, na suala hili lilikuwa linahusishwa pia na maadili ya madaktari wetu. Je, Serikali ina tamko gani kwamba suala hili ni suala la kitaalam au ni mmomonyoko wa maadili miongoni mwa madaktari? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, kujifungua kwa operation ni jambo ambalo haliwezi kuwa la kukiuka maadili, bali ni jambo la kitaalamu. Kuna sababu na vigezo mahususi ambavyo hupelekea daktari akafanya uamuzi wa kumpeleka mama mjamzito kwenda kujifungua kwa njia ya operation (caesarean section) na kitu chema sana kufanya uamuzi huo kwa sababu huokoa maisha ya mama na mtoto kuliko kusubiria kujifungua kwa njia ya kawaida ambapo mama mjamzito anaweza akaingia kwenye hali hatarishi.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri napenda kumfahamisha kwamba tunakwenda kwenye Tanzania ya viwanda na kule Mlalo tunalima kabichi, karoti, viazi, hoho pamoja na mazao mbalimbali ya mboga mboga. Je, haoni kwa kuwa sisi tutakosa viwanda wakatutafutia soko zuri la kuweza kupata tija kwenye mazao haya?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa mazao na bidhaa nyinginezo zinafungwa katika vipimo ambavyo vinaeleweka, haoni sasa ni wakati wa Serikali kuweka mkazo kwamba na mazao ya wakulima nayo yaweze kufungwa katika utaratibu ambao utawaletea tija wakulima? Ahsante.
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu soko la mazao, katika maelekezo ambayo Serikali imetoa na Mheshimiwa Waziri Mkuu katika hotuba yake amesisitiza ni kwamba Halmashauri zote kuanzia ngazi ya Kijiji, Kata mpaka Wilaya tunapaswa kutenga maeneo ambayo moja itakuwa sehemu ya kujenga viwanda vidogo, pili itakuwa sehemu ya kujenga hifadhi na tatu itakuwa sehemu ya kufanyia biashara. Kwa kutengeneza zile business centers, wateja wataweza kufika na kuweza kununua mazao yenu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mazao ya wakulima yakifungashwa vizuri yatapata soko, nakubaliana na hilo. Jambo la kufanya ni kwamba tunapohimiza ujengaji wa viwanda huko vijijini vinaongeza thamani na unapoongeza thamani ya bidhaa inahusisha pamoja na ufungaji. Kwa mfano, tungependa watu wa Lushoto na Tanga zile tangawizi na hiliki mkishazichakata kwenye viwanda vidogo pale ndiyo zinaingia kwenye packaging ambayo itakuwa inaeleza kama ni kilo au ni volume gani.
Mheshimiwa Shangazi tutawasiliana zaidi kusudi niweze kukupa maelekezo ya kiutendaji.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona. Kwa kuwa katika Wilaya yetu ya Lushoto tuna pakana na nchi jirani ya Kenya na Kituo cha Polisi cha Mnazi kina upungufu mkubwa wa vitendea kazi zikiwemo pamoja na silaha.
Je, Serikali inatoa tamko gani kuhusu suala hilo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, hili jambo niseme tu kwamba tutalichukua tuangalie upungufu huo ambao anauzungumzia Mheshimiwa Mbunge kwa kushirikiana na yeye tuone hatua muafaka ya kuchukua ikiwemo kuongeza vitendea kazi kadri ya mazingira na hali halisi na ushauri wa kitaalamu utakapokuwa unaruhusu. Maana yake wakati mwingine uwekaji wa vitendea kazi hivi unazingatia vigezo vingi ikiwemo silaha, kwa hiyo, kuna haja ya kukaa na wataalam kwa maana ya Jeshi la Polisi kushauriana ni sababu gani ambazo zimesababisha eneo hilo liwe na upungufu halafu tuchukue hatua stahiki kwa wakati muafaka.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto ina Majimbo mawili; Mlalo na Lushoto, na tunalo ombi katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI la kupata Halmashauri ya Mlalo.
Je, ni lini sasa Serikali itatupatia Jimbo la Mlalo Halmashauri kamili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika kumbukumbu zetu, namshukuru Mheshimiwa Mbunge alishawahi kufika mpaka ofisini na katika kufanya rejea katika documents zetu, tumeona kwamba kuna vitu fulani vilikuwa bado havijakidhi vigezo kule Mlalo; na maelekezo tuliyoyatoa ni kwamba, wafanye ule mchakato kuangalia vile vigezo viweze kukamilika, halafu maombi yale yawasilishwe rasmi katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI, ilimradi eneo hilo sasa wataalam watakapokuja kufanya uhakiki; ikionekana eneo hilo sasa linatosha kuanzisha Halmashauri mpya, basi hakuna shaka, Ofisi ya Rais, TAMISEMI haitosita kufanya hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshatoa maelekezo katika suala zima la Mlalo na Mheshimiwa Shangazi amekuwa akilifuatilia kwa ukaribu sana suala hili. Sasa naomba nitoe msukumo katika maeneo husika, ule mchakato na vile vigezo mwanzo vilikuwa havijakamilika vizuri, tuweze kuvikamilisha na maombi hayo sasa yawasilishwe katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa ufanisi wa hali ya juu katika maeneo hayo.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ambayo yanamhusu Mbunge wa mwendokasi aliyetoka, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa Wizara ya Utumishi, imeshindwa kutoa vibali kwa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto ambayo inatugharimu takribani milioni 28 kuhudumia watumishi 58. Je, ni lini Wizara hii itatoa kibali kwa Halmashari ya Wilaya ya Lushoto?
Swali la pili, kwa kuwa pesa hizi ambazo Halmashauri ya Lushoto inazitumia, kulipa mishahara zilikuwa ziende kwenye makundi maalum hasa ya vijana na akinamama, zile asilimia tano. Je, Wizara haioni kwamba pesa hizi kutumika kulipa watumishi inakinzana na dhana nzima ya utawala bora?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba maswali haya naona yametoka nje kabisa na swali hili la msingi. Kuhusiana na lini sasa Ofisi ya Rais, Utumishi itatoa kibali kwa Halmashauri ya Lushoto, kwa ajili ya kibali cha ajira, niseme tu kwamba kwa sasa Serikali bado inaendelea na mchakato na pindi vibali hivyo vitakapokuwa tayari, basi taasisi husika zitaweza kufahamishwa na wataendelea na michakato hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la pili, kwamba kutokana na vibali hivi kuchelewa, imepelekea Halmashauri ya Wilaya yake kuweza kutumia mapato yake ya ndani au own source kwa ajili ya kulipa mishahara. Niseme tu kwamba kila mwaka na Halmashauri zote na mamlaka za ajira wanafahamu mchakato wa ajira, kila mwaka mamlaka ya ajira inatakiwa iwasilishe ikama yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, tumekuwa tukishuhudia huwa wanawasilisha ikama, ikama inaidhinishwa na baadaye Halmashauri inaenda kinyume kabisa na kuwaajiri watu wake kwa kupitia fedha zao za ndani. Niseme
tu kwamba kwa kweli suala hili limekuwa likileta changamoto na tuombe sana Halmashauri zijikite zaidi katika ikama ambazo zinaidhinishwa na Serikali kwa kutumia mishahara ya Serikali.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini bado nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, kwa kuwa iliyokuwa NBC, Benki iliyokuwa inamilikiwa na Serikali ilikuwa na tawi pale mlalo na ilikuwa inahudumia wakazi wa Mlalo, Mbaramo, Mtae mpaka Mlola; je, kwa nini NMB iliyochukua nafasi ya NBC isitekeleze wajibu huo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa, Mheshimiwa Waziri amesema sehemu ambazo zina mzunguko mkubwa wanaweza wakaongeza ushawishi wa kutengeneza Community Bank; na Jimbo la Mlalo lina mzunguko mkubwa wa fedha; je, ni lini kwa kushirikiana na SACCOS ya Kumekucha Mwamko SACCOS Ltd. wanaweza wakawajengea uwezo ili tuweze kuanzisha hiyo Community Bank? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi ni kwamba Serikali ilijitoa moja kwa moja kuendesha shughuli hizi, lakini Serikali kupitia Wizara yangu itaendelea kuhimiza mabenki kuendelea kusambaza huduma zao kwa wananchi wa vijijini likiwepo na Jimbo la Mlalo. Pia nitalifikisha ombi hili katika Benki yetu ya NMB na kuwashauri kuhusu ombi hili la Mheshimiwa Rashid Shangazi ili tuone sasa NMB inaweza kurejesha huduma ambayo mwanzo ilikuwa ikiendeshwa na Benki yetu ya NBC. Kwa hiyo, nitakaa nao, nitaongea nao na namwomba Mheshimiwa Mbunge tushirikiane naye ili tuweze kuongea na Menejimenti ya NMB ili kurejesha huduma hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili, napenda kumthibitishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania ipo tayari kabisa kutoa ushauri wa kitaalamu na namna ya kuanzisha benki za kijamii. Ninafahamu pale Mlalo hasa maeneo ya Lukozi, maeneo ya Rangwi, Mlalo yenyewe, Shume na Mlola kuna huduma nyingi za kiuchumi, hivyo niko tayari kabisa kuishauri Benki Kuu kwamba sasa tukatoe huduma hizi za kitaalamu kwa wajasiriamali wetu hawa ili waweze kuanzisha Benki ya Kijamii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli, kuna society nzuri pale ambayo tukishirikiana nao na mtaji unaotakiwa kuanzisha Community Bank ni shilingi bilioni mbili tu, kwa taarifa nilizonazo, taasisi hii iliyopo pale ina zaidi ya shilingi bilioni moja sasa. Kwa hiyo, wamebakiza sehemu ndogo tu waweze kuanzisha Community Bank. Mheshimiwa Rashid Shangazi tushirikiane ili tuweze kuanzisha Community Bank pale Mlalo.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Kwa kuwa pamoja na upungufu uliopo katika kodi hii, lakini pia baadhi ya wananchi ambao sio waaminifu walikuwa wanatumia mwanya huo kutengeneza sticker ambazo ni feki: Je, Serikali ina mpango gani wa kuja na sticker madhubuti ambazo siyo rahisi kufojiwa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa wapo wananchi ambao wanatenda vitendo viovu vya kufoji sticker hizi. Kama nilivyosema, lakini naomba pia tufahamu kwanza Waheshimiwa Wabunge, katika sehemu ambako tumeboresha kwa kiasi kikubwa ni utoaji wa sticker hizi ambapo kwa sasa hivi mwananchi yeyote anaweza kulipia gari yake popote alipo na akaenda kuchukua risiti yake katika Ofisi zetu za Mamlaka ya Mapato popote pale alipo huku akiwa amepewa control number. Kwa hiyo, tumeweza kutoka katika manual work na sasa tunatumia teknolojia katika kutoa huduma hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na maboresho hayo, kama nilivyosema, tusubiri Finance Bill itakapokuja, tutaona sasa kutakuwa hakuna mkono wa mtu yeyote kuingia katika ukusanyaji na utoaji wa sticker hizi kwa sababu itakuwa ni mfumo wa automatic ambao hakuna yeyote atakayeweza kuuingilia na kuweza kutoa sticker ambazo ni feki.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, japo hayaridhishi sana, napenda kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa miti ya asili huwa ukuaji wake siyo wa kasi na wameshaanza kupanda miti katika hizi hekta 11, kwa nini wasione umuhimu wa kumalizia hizi hekta 38 ili ku-cover eneo hili la msitu kwa sababu msitu huu una vyanzo zaidi ya vinne vya mito ambayo inatiririsha maji kuelekea katika mbuga ya Mkomazi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, mvua za mwaka jana, zilisababisha uharibifu mkubwa kutokana na maporomoko yaliyosababisha uoto wa msitu kupotea, hivyo kusababisha uharibifu mkubwa katika barabara za Kata ya Shagayu, Mbaramo na Sunga. Je, Wizara haioni sasa kuna umuhimu wa kipekee wa kuwaunga mkono wakazi wa maeneo haya ili kuweza kuboresha miundombinu hii ya barabara iweze kusaidia hata wakati mwingine wanapakuwa na dharura za moto waweze kufika katika eneo husika kwa haraka zaidi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze kwa kutambua kwamba misitu inachangia kiasi kikubwa au ndiyo msingi kwa kweli wa kuweza kuboresha vyanzo vya mito. Ana mito minne, na kwamba yote minne chanzo chake kikubwa ni misitu hii tunayoizungumzia.
Kwa hiyo, kwa kutambua hivyo nampongeza lakini nataka elimu hiyo pia aweze kuifikisha kwa wananchi kwenye eneo lake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali kwa nini sasa tusipande miti kwenye lile eneo ambalo lina hekta 38 tulizosema tuache miti ikue kwa utaratibu wa asilia. Kwanza, nimfahamishe tu kwamba, mimea ikiwemo hiyo miti kwa kawaida huwa kuna mimea ambayo ni rafiki kukua pamoja na mimea mingine si rafiki kukua kwa pamoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wazo lake siyo baya lakini tunapaswa kufanya kwanza utafiti wa kitaalam, na nitafanya utaratibu wa kufika kwenye eneo lile na wataalam ili tuweze kuona miti iliyopo ni miti gani inayotakiwa kukua asilia, halafu tuone kama kuna miti rafiki inayoweza kupandwa ilimradi tusichague miti ambayo itaathiri ile miti ambayo inatakiwa kukua asilia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili, uwepo wa barabara ambazo zinasaidia kutumika wakati wa dharura za moto na matumizi mengine ambayo ni rafiki kwa utunzaji wa misitu.
Kwanza ni dhahiri kwamba hiyo pia ni interest yetu pia sisi kama Serikali, lazima tuwe na barabara ambazo zinaweza kutusaidia wakati wa dharura kama moto utatokea, na kuwa ni jukumu letu kushirikiana na wananchi, na mamlaka za Wilaya zilizopo kuweza kuhakikisha kwamba barabara hizi zinatengenezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni suala la kuangalia hali ya kibajeti, lakini pamoja na hayo katika safari hiyo nitakayokwenda nitakwenda pia kuangalia hali ya barabara na kuweza kuona namna gani tunaweza kuweka kwenye mipango yetu.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Kwa kuwa katika Kata ya Mnazi, Tarafa ya Umba, kuna tatizo linalofanana na huku Newala Mjini; kuna kiwanja cha ndege (air stripe) ambayo ni ya muda mrefu sana haitumiki na sisi tupo karibu na hifadhi ya Mkomazi: Je, Serikali haioni kwamba ni wakati muafaka sasa kukifufua kiwanja hiki ili kiweze kuchochea utalii katika hifadhi ya Mkomazi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimepokea ombi la Mheshimiwa Shangazi na nitawasiliana na Waziri wa Maliasili na Utalii ambao kiwanja hiki ilikuwa ni mali yao na ni kwa ajili ya shughuli za utalii ili tuone namna gani kiwanja hicho kitafufuliwa na kama kuna shughuli za kiuchumi zitakazowezesha kiwanja hiki kujilipa.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niipongeze
Wizara hii imekuwa ni sikivu sana. Katika Jimbo la Mlalo karibu Kata zote sasa
mawasiliano yapo, isipokuwa katika Kata ya Rangwi na Kata ya Malindi hasa
eneo la Makose. Je, ni lini sasa katika hii Kata ya Rangwi na Malindi mawasiliano
ya simu za mkononi yatapatikana?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa
Naibu Spika, naomba nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rashid
Shangazi kwa namna anavyofuatilia mambo mbalimbali, hususan barabara
pamoja na mawasiliano katika Jimbo lake. Nimhakikishie, kama ambavyo
nimekuwa nikimweleza wakati anakuja ofisini kufuatilia shughuli za wananchi
wake kwamba, haya maeneo machache ya hizi Kata mbili za Malindi, Rangwi,
Serikali itaangalia uwezekano wa kuyafikia na hasa kwa kushirikiana na wadau
wetu kwa maana ya makampuni ya mawasiliano ya simu.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa vitendo hivi vya uhalifu vipo nchi nzima na kule Jimboni Mlalo mwezi wa nane/tisa vikundi vya ugaidi vimeua watu wawili na kuchoma mabweni ya Chuo Kikuu cha SEKOMU. Je, ni lini Serikali itaimarisha ulinzi katika maeneo ya Jimbo la Lushoto ikiwa ni pamoja na kujenga seliya kuwekea silaha katika Kituo cha Mlalo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuna kazi kubwa imefanyika ya kuweza kupambana na ujambazi katika maeneo mbalimbali ikiwemo Mkoa wa Tanga. Kimsingi nchi yetu haina ugaidi, tunasema tunavimelea vya ugaidi. Kwa hiyo, kilichofanyika Tanga na ninyi ni mashahidi katika maeneo ya Amboni na kwingineko ni kazi kubwa sana ambayo imefanyika kwa mafanikio makubwa na hakika kwamba mafanikio yale ndiyo ambayo yamesababisha mpaka sasa hivi Mkoa wa Tanga kwa ujumla wake ikiwemo Lushoto kuendelea kuwa katika hali ya usalama. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kuwa suala la uhalifu ni suala ambalo linaendelea kuwepo, tutaendelea kuhakikisha kwamba tunaimarisha kazi hiyo ifanyike zaidi na zaidi ili kutokomeza kabisa uhalifu katika maeneo ambayo yamesalia katika nchi yetu.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona. Kwa kuwa tatizo lililopo katika misitu ya Geita linafanana sana na tatizo lililopo katika Msitu wa Shume ambapo katika vijiji vya Shume, Nywelo na Mkuhnyi ambavyo vipo katika Kata ya Manolo navyo eneo la Msitu wa Hifadhi wa Shume umeingia katika maeneo ya vijiji ambako wananchi mara nyingi ndiko wanakofanya shughuli zao za kiuchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, na tatizo la mgogoro huu pia limeripotiwa katika Randama ya Wizara ya Ardhi. Je, ni lini sasa Serikali itakaa na wananchi hawa wa vijiji vya Shume, Nywelo pamoja na Mkunki ili angalau waweze kutatua tatizo hili?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, tumesikia, tumepokea shamba la msitu wa kupandwa wa Shume uliopo katika maeneo yale ya vijiji alivyovitaja vya Shume, Nywelo na Mkunki. Ni suala ambalo kama alivyosema mwenyewe limeorodheshwa kwenye
orodha ya maeneo ambayo yanatakiwa kushughulikiwa chini ya orodha ya migogoro ya ardhi iliyoandaliwa na Wizara ya Ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana kwa
kutukumbusha licha ya kwamba lipo kwenye orodha na kwa kweli kwa namna ambavyo anaweza kuwasemea wananchi ya maeneo haya kama mwakilishi wao na nimuahidi sambamba na kazi inayoenda kufanyika chini ya kamati iliyoundwa; mimi na yeye tutapanga tutaweza kwenda kwenye hili eneo tukaangalie uhalisia ili tuweze hata kuishaurihiyo kamati.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona. Kwa kuwa tatizo lililopo Njombe linafanana kabisa na tatizo lililopo katika Kata ya Mtae Jimbo la Mlalo Wilayani Lushoto. Je, ni lini Serikali itayakarabati majengo yale machakavu ya Mahakama ile ya mwanzo Mtae?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwanza kabisa nimhakikishie tu kwamba, azma ya Serikali kupitia Mahakama ni kuhakikisha kwamba tunasogeza huduma za mahakama karibu zaidi na wananchi. Ukiangalia tu katika mwaka huu wa fedha ambao tunaumaliza Serikali ilitenga zaidi ya Shilingi bilioni 46.5 na hata katika mwaka huu wa fedha ambayo bajeti yake tunaanza nayo zaidi ya Shilingi bilioni 18.1 pia zimetengwa kwa ajili ya kujenga mahakama mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaliona suala hili, tutakwenda kuliangalia; lakini katika mahakama ambazo ziko katika utaratibu kwa mwaka huu tunaomalizana nao ni ujenzi wa Mahakama Kuu, Tanga ambako na yeye pia anatoka, tunakamilisha ukarabati huo. Vile vile tunakamilisha ukarabati katika
Mahakama Kuu, Dar es Salaam lakini pia tunaanza ujenzi katika Mahakama Kuu, Mara pamoja na Kigoma na vile vile tunakamilisha ujenzi wa Mahakama za Wilaya Bagamoyo, Kigamboni na Mkuranga.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Mahakama za Mwanzo tunakamilisha ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo
Kawe pamoja na Kinyerezi, vile vile katika mwaka huu wa fedha, zaidi ya Mahakama za Mwanzo 10 zitaweza kujengwa na kukarabatiwa.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, yapo pamoja na majibu ya Serikali ambayo kimsingi hayajatatua tatizo lengo lilikuwa ni Serikali itutue huu mzigo. Kama utakumbuka ni kwamba mapato ya ndani yanatakiwa yaende kwenye makundi maalum ikiwepo wanawake na vijana zile asilimia 10. Sasa Halmashauri inapotumia pesa zote hizi kwa ajili ya kulipa watumishi ambao ni jukumu la Serikali, je, Serikali haioni kwamba hili linaendana na kinyume na dhana nzima ya utawala bora?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa uhitaji huu
wa kutumia own source kulipa watumishi wa ndani bado unaonekana mahitaji yapo kwa sababu Serikali Kuu haiajiri na kwa sasa wakati wa zoezi zima hili la uhakiki wa vyeti Halmashauri ya Lushoto imepoteza zaidi ya watumishi 115. Serikali inatoa tamko gani la kufidia hili pengo ambalo wafanyakazi hawa wametoka?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa, pamoja kwamba anasema kwa upande mmoja alikuwa hajaridhika, nimpongeze kwa namna ambavyo amekuwa akifuatilia suala zima la ajira hizi zinazofanyika kwa kutumia mapato ya ndani.
Mheshimiwa Spika, kwanza nipende kusema yafuatayo; kama Serikali hatu-entertain sana ajira hizi kwa kutumia mapato ya Halmashauri. Tunatambua kwamba mapato haya ya Halmashauri au own source yanatakiwa kwenda katika vipaumbele vingi na ndiyo maana tuaendelea kusisitiza ni vema Halmashauri zetu kupitia kwa waajiri ambalimbali na Maafisa Utumishi wahakikishe wanaweka mapendekezo yao na makisio yao ya Ikama ili kipindi ambapo tunaajiri basi waweze kupata mgao wa ajira kwa wakati sahihi bila kuathiri uwezo wao Halmashauri katika kulipa.
Mheshimiwa Spika, tumekuwa tukipata changamoto nyingine, wako ambao walikuwa wakiajiri kupitia hizi own source lakini unakuta hawafuati taratibu. Nipende kuweka angalizo kupitia Bunge lako, mchakato wa ajira hizi za own source unatakiwa usitofautiane na mchakato wa ajira zingine kama zinazofanyika katika Serikali Kuu na kulipiwa na Serikali Kuu, lakini vilevile hata katika sifa na miundo ya kiutumishi inatakiwa pia isiwe compromised, sifa zile zile kwa mujibu wa miundo ya maendeleo ya kiutumishi. Kwa hiyo, nimeona niseme hayo kwanza kabla sijajibu swali lake kwa undani.
Mheshimiwa Spika, nipende kumtoa hofu Mheshimiwa Shangazi, wao walipoleta haya mahitaji walionekana wanauweza kulipa, lakini nimuhakikishie tu katika mwaka huu ujao wa fedha 2017/2018 kwa Halmashauri ya Lushoto tumewatengea ajira nafasi 252 ambapo kati ya hizo kwa kada za afya tumewatengea nafasi 54, kwa upande wa elimu nafasi 132 kilimo nafasi 10, mifugo nafasi tano na nafasi nyinginezo 51.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa watumishi walioathirika katika zoezi la vyeti fake, kama nilivyosema katika siku nne zilizopita, tayari tumeshatenga nafasi 15,000 kwa ajili ya kuzibia zile nafasi 9,932 pamoja na nafasi zingine za ziada zaidi ya 5,000 katika maeneo mbali mbali yenye upungufu mkubwa na mahitaji.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa tatizo lililopo Serengeti linafanana kabisa na tatizo lililopo katika Tarafa ya Mtae, Shagayu, Sunga na Rangu, wananchi wamehamasika kuchangia huduma za CHF lakini wanapokwenda kwenye Kituo cha Afya cha Mtae huduma hakuna. Je, Serikali inawambiaje wananchi hawa wa Tarafa Mtae?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niweke rekodi sawa kwamba bahati nzuri tulikuwa na Mheshimiwa Mbunge katika Jimbo lake kipindi kile wakati nilipokwenda kutembelea Wilaya ya Lushoto. Ni kweli kwa sababu tumegundua changamoto ya afya ipo kubwa zaidi ndio maana katika vipaumbele vyetu tumeamua kukiteua hiki Kituo cha Afya cha Mtae ni miongoni mwa vituo ambavyo ndani ya mwezi huu mmoja unaokuja tutaenda kufanya ujenzi wa maternity ward pale na kufanya ukarabati mkubwa lengo kubwa wananchi wa Mtae na maeneo ya jirani waweze kupata huduma nzuri katika eneo lile.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante nami nataka kujua hapo kwamba kwa kuwa wakati shisha linapigwa marufuku, huku nyuma kuna watu walikuwa wamepewa leseni ya kufanya hiyo biashara kwa sababu ilikuwa inaonekana ni biashara halali. Je, Serikali inatoa tamko gani kuhusu hilo? (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, masuala yote yanayohusu afya za Watanzania ni kipaumbele cha Serikali na kwa kuwa ni kipaumbele cha Serikali, jambo la kwanza tunalofanya ni kuokoa maisha ya Watanzania. Wakati tunafanya hivyo, ndiyo maana tunasema tunaliwekea utaratibu mzuri wa Kisheria na hivi tunavyoongea, ukienda kwenye ukurasa wa 15 wa kitabu cha hotuba ya Waziri wa Afya, ameongelea utaratibu ambao utachukuliwa na tayari alishatungia kanuni. Kwa hiyo, inasubiria mashauriano ya mwisho ndani ya Serikali ambayo yanazingatia concern aliyoitoa Mheshimiwa Shangazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Shangazi, n kwa kutambua kwamba hilo jambo lilikuwepo lakini ni lazima tuzingatie afya za Watanzania na tuzingatie utaratibu ambao utaweka utaratibu wa kisheria wa kudumu ili kuweza kuhakikisha kwamba afya za Watanzania zinalindwa. (Makofi)
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Wakati anajibu suala la Mbuga ya Mkomazi na Mbuga ya Mkomazi kwa Mkoa wa Tanga kuna Wilaya ya Lushoto, Korogwe na Mkinga. Tatizo la mipaka hata kule linatuathiri na kuna timu sasa inapita kutathmini hilo tatizo, nataka nitambue, je, Serikali kupitia Wizara ya Maliasili imeshirikiana na hawa watalaamu ambao wanapita kutathmini ile mipaka, hasa katika eneo la Mwakijembe Wilaya ya Mkinga?

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mbuga ya Mkomazi kwa Mkoa wa Tanga iko katika Wilaya za Lushoto, Korogwe na Mkinga na hili tatizo la mipaka sasa hivi kuna timu ya ambayo iko chini ya RAS kwa kule Tanga inafuatilia haya maeneo yenye migogoro ambayo wananchi na mbuga wanakinzana hasa eneo la Mwakijembe katika Halmashauri ya Mkinga, je, Wizara ya Maliasili na Utalii inatambua uwepo wa hii timu ambayo inakagua mipaka?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua uwepo wa timu hiyo inayokagua mipaka.
Lakini Mheshimiwa Mbatia nafikiri wakati nikiwa namjibu swali alikuwa anasisitiza lini nilimuona wakati anataoka alikuwa anaendelea kuongea anauliza lini, sasa Mheshimiwa Mbatia tukimaliza kikao hiki cha Bunge (Kamati ya Fedha hivi) mimi na wewe tuambatane tukaangalie uhalisia ulivyo halafu tuweke ratiba ya kushughulikia suala hilo.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Kwa kuwa suala la lililopo kule Masengwa linafafanana kabisa na bwawa ambalo Serikali imetuahidi katika Kata ya Mnazi na Kivingo kule Lushoto. Je, ni lini sasa Serikali itatenga fedha kuanza mradi huo wa uchimbaji mabwawa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza eneo la Lushoto ni zuri sana, ni green, lina mvua za kutosha na linafaa kwa kilimo cha umwagiliaji. Sasa hivi Wizara yetu imepata fedha kutoka Serikali ya Japan na inashirikiana na wataalam wa Serikali ya Japan kupitia mpango kabambe wa kuhakikisha kwamba unaainisha maeneo yote yaliyotambuliwa kwa kilimo cha umwagiliaji ili uweze kuweka mkakati na kuweka mbinu kama nilivyozungumza kwenye swali moja la msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, katika huo mpango ambao tunatarajia ukamilike mwaka 2018 maeneo yote yataainishwa na matatizo mengi ambayo yamejitokeza yataangaliwa ili tuhakikishe tunajenga miundombinu ambayo itawezesha kilimo cha umwagiliaji. Nimhakikishie Mheshimiwa Shangazi kwamba katika kazi hii inayoendelea tutahakikisha kwamba tunafika mpaka Lushoto.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tatizo lililopo kwenye barabara ya Makambako – Songea linafanana kabisa na tatizo lililopo Mombo – Soni - Lushoto kilometa 36 na juzi baada ya zile mvua kubwa imesababisha uharibifu mkubwa wa barabara ile. Je, ni lini sasa Serikali itaifanyia ukarabati mkubwa barabara hii ya Mombo – Soni - Lushoto kilometa 36?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rashid Shangazi kwa sababu yeye alikuwa wa kwanza kunijulisha matatizo yaliyotokea katika barabara hii anayoongelea kabla hata ya wataalam wangu hawajaniambia. Nadhani sasa anafahamu kwamba barabara hiyo imeanza kupitika kwa sababu kazi imefanyika ya kurudisha mawasiliano na kutengeneza pale ambapo mawe yaliteremka na kuziba barabara. Tunashukuru barabara hiyo sasa inaanza kupitika baada ya matengenezo kukamilika na tutaendelea kuifanyia marekebisho pale ambapo tutaona panahitajika. Nakushukuru sana Mheshimiwa Shangazi. (Makofi)
MHE. RADHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu ya Serikali lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
(a) Kwa kuwa katika majibu ya Serikali inaonyesha kwamba mifereji imejengewa na mimi ninatoka kule ninafahamu kama mifereji hii haikujengewa.
Je, Waziri yuko tayari kuungana na mimi kwenda kukagua ili aweze kujionea kabla ya hiyo bajeti ya mwaka 2018/2019?
(b) Kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto ni sehemu ya ushirika huu, haoni kwamba ni vizuri wakaguzi hawa wakatoka Serikali kuu ili kuondoa mgongano wa kimaslahi lakini pia kuweza kuleta uwazi na uwajibikaji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILAJI: Mheshimiwa Spika, sasa hivi tayari kuna timu ya Mhandisi Mshauri ambaye anapitia skimu zote za umwagiliaji nchini na ndiyo maana tumeonesha kwamba kuanzia bajeti ya mwaka 2018/2019 tutangiza kwenye bajeti.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, baada ya kumaliza hiyo taarifa tutaangali hicho kitu kinachozungumzwa, kwamba mifereji ipo lakini haipo, basi tutaainisha; lakini pia na mimi niko tayarai kuongoza na Mheshimiwa Mbunge ili tuende tukaangalie; lakini la msingi tusubiri hiyo taarifa ya Mhandisi Mshauri.
Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la ukaguzi; Mheshimiwa Mbunge kwa sasa hatuwezi kusema tutamtuma nani kwa sababu tayari tutakuwa tumewaonyesha wale wabadhirifu kwamba ni yupi wanaweza wakamuwahi. Hata hivyo nikuhakikishie kwamba tutaunda timu makini sana ambayo itakuja kufanya ukaguzi na itatuletea taarifa ambayo ni ya uhakika kabisa na wewe mwenyewe utaifurahia.
Mheshimiwa Spika, pia katika hiyo shughuli nitaendelea kushirikiana na wewe ili kuhakikisha kwamba hatua stahiki, ukaguzi unaostahili umefanyika ili Serikali iweze kushauriwa ipasavyo.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Barabara inayotoka Lushoto kwenda Mlalo, kilometa 42, ambayo ndiyo inayounganisha Majimbo haya imekuwa ikijengwa na Wakala wa Barabara (TANROADS) kwa kilometa mbili mbili kwa kila mwaka. Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuitengea fedha barabara hii ili iweze kurahisisha mawasiliano kati ya Mlalo, Mtae na Lushoto?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Lushoto – Mlalo ni barabara ambayo inahudumiwa na TANROADS Mkoa wa Tanga na inapitika siku zote, mwaka mzima, haina matatizo makubwa. Kazi iliyopo mbele yetu sasa hivi ni kutafuta fedha ili tufanye feasibility study na detailed engineering design ili huko baadaye tuweze kutafuta pesa kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Mheshimiwa Shangazi kwamba, tutakaa pamoja tutazungumza ili kuhakikisha tunampa mpango mzima ambao tutaweza kuutekeleza ili kuhakikisha barabara hii inajengwa kwa kiwango cha lami.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Kwa kuwa msiba uliopo huko Lupembe wa kiwanda kufungwa ni sawa kabisa na msiba ulioko kule Bumbuli Kiwanda cha Mponde sasa ni miaka mitano chai inashindwa kuzalishwa na wananchi hawa wanapata hasara.
Je, Serakali inatoa tamko gani kuhusu msiba huo wa watu wa Bumbuli?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, aya ya mwisho katika swali nililolijibu nilisema Serikali inafuatilia hizi changamoto au migogoro kwenye viwanda vya chai. Sitaki kusema zaidi, lakini yule aliyeleta mgogoro, aliyehusika kwenye mgogoro wa Lupembe ndiyo yule anayehusika na kwenye mgogoro wa Mponde. Sasa sijui kuna nini! Niko chini yangu na juzi nilikuwa Tanga, nimewaeleza kwamba tutalifuatilia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpe taarifa Mheshimiwa Shangazi kwamba katika Wilaya yake, Halmashauri sasa inakwenda njia ya pili kuanzisha kiwanda. Nimewaelekeza waende TIRDO wawaongoze namna ya kutengeneza kiwanda kingine, lakini Serikali inafuatilia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, jambo la kusikitisha, anayelalamikiwa Kusini, ndiye anayelalamikiwa Mashariki.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shamba la Mnazi Estate kule Lushoto - Mlalo limevamiwa kwa sababu Mmiliki ambae alikuwa anendelea kulimiliki ameshindwa kuliendesha. Je, pamoja na mchakato ambao tulikuwa tumeuanza wa kufuta, Serikali imefika hatua gani ya kumuondoa mmiliki katika ardhi hiyo?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwenye kijiji cha Mnazi kuna Kampuni inatiwa Lemash Enterprise ambayo ilikuwa inamiliki shamba la Mkonge lenye hekta 1,275 lakini nataka nimhakikishie Mheshimiwa Shangazi kutokana na jitihada zake za kuondoa kero ya wananchi na katika kutekeleza spirit ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli walitimiza wajibu wao na nataka kumhakikishia kwamba na Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli naye ametimiza wajibu wake. Tarehe 4 Septemba, 2017 shamba hilo limefutwa rasmi na mmiliki ameshaambiwa, nimeshachukua hatua ya kulitangaza kwenye Gazeti la Serikali kwa order ya Rais na hivi sasa nimeshamwandikia Mkuu wa Mkoa wa Tanga ili atupe mapendekezo mazuri zaidi ya namna ya kulitumia shamba hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo nakuomba Mheshimiwa Shangazi kwa kuwa umelianza, basi naomba ushirikiane na Mkuu wa Mkoa wa Tanga kulimalizia mlete mapendekezo mazuri yatakayowezesha kutumika shamba hilo kuinua uchumi wa wananchi wa Mnazi. Tungependa shamba hili liendele kuwa shamba la Mkonge lakini ninyi watu wa Tanga muamue nani aendesha kilimo hicho kwa ajili ya kuongeza tija ya ajira na uchumi wa Taifa. (Makofi)
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu ya Serikali ambayo yanatia matumaini, nina maswali madogo ya nyongeza.
Swali la kwanza, wakati redio ya TBC wanatumia mawimbi ya short wave na medium wave mawasiliano yalikuwa mazuri. Je, hawaoni kwamba kuhamia kwenda digital inaweza ikawa ni changamoto hata kwa maeneo mengine yaliyoko pembezoni katika Taifa letu? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa kwa mujibu wa Katiba Ibara ya 18(b) tunayo haki ya kupokea na kupata taarifa, sasa anawaambia nini wakazi wa Mlalo ambao wako pembezoni mwa nchi jirani ya Kenya ambao hawapati habari za Taifa lao na je, hawaoni kwamba hii inahatarisha usalama wa Taifa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nichukue nafasi hii ya kuweza kumpongeza kwa dhati kabisa Mheshimiwa Rashid Shangazi kwa namna ambavyo amekuwa akifuatilia kwa umakini kabisa matatizo ya wananchi wa Jimbo la Mlalo.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwamba baada ya kupokea majibu mazuri kabisa ya Serikali nilitegemea kwamba Mheshimiwa Shangazi atakuwa hana maswali ya nyongeza. Kwa sababu ameuliza maswali mawili, naomba nimjibu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo kweli kwamba kuhama kutoka kwenye mfumo wa analogy kwenda kwenye digital imepelekea kuweza kupunguza usikivu wa redio hii ya TBC. Changamoto kubwa ambayo ilikuwepo ni kwamba mitambo mingi ambayo ilikuwa inatumika ilikuwa ni mitambo ambayo imechoka, mibovu ukizingatia kwamba mitambo hiyo ilikuwa ni ya muda mrefu sana.
Kwa hiyo, hata linapokuja suala zima la kutafuta vipuri kwa ajili ya kufanya marekebosho ya mitambo hiyo, ilikuwa ni ngumu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimtoe hofu Mheshimiwa Rashid Shangazi kwamba tatizo hilo kwa sasa hivi TBC imelichukua kwa kina na inalifanyia kazi na mpaka sasa hivi katika mikoa ya Arusha, Dodoma, Mwanza pamoja na Kigoma tumeanza utaratibu wa kuboresha mitambo hiyo ili kuhakikisha kwamba matangazo haya ya TBC Taifa pamoja na TBC FM yanawafikia wananchi kama ambavyo inatakiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali lake la pili, ametaka kujua umuhimu wa chombo hiki cha Taifa, TBC kwa maeneo ambayo ni ya mipakani. Mheshimiwa Shangazi, Serikali hii ya Awamu ya Tano inatambua kabisa kwamba wananchi wote ambao wanakaa maeneo ya mipakani wana haki ya kupata taarifa kama ambavyo wananchi wengine wanakaa katika maeneo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia hilo, kuna mkakati wa TBC ambao umeshaanza kufanyika katika maeneo ya mpakani, nikianza na eneo la Rombo, lakini ukienda na eneo la Namanga, Tarime pamoja na Kakonko, tayari ufungaji wa mitambo mipya ya TBC umeanza kufanyiwa kazi. Tunaamini kwamba mitambo hii itakapokamilika, kwa kiasi kikubwa sana itasaidia kumaliza tatizo hili za usikivu kwa chombo hiki cha TBC.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Mheshimiwa Shangazi aliuliza kwa upande wa Lushoto. Kama ambavyo nimejibu kwenye jibu langu la msingi, ni kwamba tayari shilingi milioni 50 imeshatengwa kwa ajili ya kumaliza tatizo la usikivu katika Wilaya hiyo ya Lushoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie kabisa Mheshimiwa Shangazi kwamba eneo hili la Kwamashai ambalo limechaguliwa kuhakikisha kwamba mtambo huu unawekwa, ni eneo ambalo limefanyiwa utafiti wa kina na imeonekana kabisa kwamba mtambo huo ukijengwa hapo, basi maeneo yale ya Lukozi, Mnazi pamoja na Lunguzi ambako imepakana kwa ukaribu kabisa na kijiji ambacho kiko kwenye nchi ya Kenya watapata matangazo ya TBC kama inavyotakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya kutoka Lushoto kwenda Mlalo, lakini pia kutoka Mlalo kwenda Bombo Mtoni hadi Maramba ni ya muda mrefu sana na inakuwa inajengwa kwa kiwango cha kilometa mbili mbili kila mwaka. Je, ni lini sasa Serikali itaweka nguvu ili barabara hii ya kutoka Lushoto - Mlalo na kutoka Mlalo kwenda mpaka Maramba ijengwe kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J.KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Shangazi amekuwa akifuatilia sana barabara pamoja na maendeleo mbalimbali katika Jimbo la Lushoto. Ninatambua mahitaji ya barabara katika maeneo haya ambayo ameyataja maeneo ya kiunganishi cha Lushoto - Mlalo na ile barabara ya Mlalo kupita Maramba kwenda Mkinga na Mheshimiwa Kitandula amekuwa akifuatilia hii.
Kwa hiyo, kama nilivyojibu pale awali kwamba tunaendelea kutafuta fedha kama Serikali inavyokusanya fedha vizuri tutaendelea kujenga barabara mbalimbali. Kwa hiyo, niwaombe tu wananchi wa Mlalo, Maramba Mkinga na wananchi wa Lushoto kwa ujumla na watanzania wote kwamba waendelee kuvuta subira tu kadri fedha zinavyopatikana tutaendelea kuboresha barabara zote nchini ili ziweze kutoa mchango mkubwa katika ujenzi wa uchumi wa nchi yetu.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri kuna maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa kama tunavyofahamu Jiji la Dar es Salaam linazidi kupanuka na maeneo ya pembezoni zipo sekondari nyingi ambazo mwisho wake ni kidato cha nne; na kwa kuwa katika Jimbo la Segerea hasa katika eneo la Kinyerezi na Kipawa, bado hakuna Sekondari za kidato cha tano na sita. Je, Serikali haioni kwamba ni wakati sahihi sasa wakupeleka hizi shule za kidato cha tano na sita katika maeneo ya pembezoni?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa swali hili linafanana kabisa na kule Lushoto, hasa Jimbo la Mlalo. Tunazo Tarafa tano katika Halmashauri yetu ya Lushoto, lakini ni Tarafa nne pekee ndio zenye sekondari ya kidato cha tano. Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka Tarafa ya Umba na Mlola nazo zipate sekondari za kidato cha tano? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama anavyosema Mheshimiwa Mbunge kwamba Jiji la Dar es Salaam linapanuka, na shule nyingi nyingine zimejengwa pembeni mwa Jiji la Dar es Salaam especial maeneo ya kule Mbondole, Zingiziwa na maeneo mengine. Kwa hiyo nimesema kama ni ile mikakati wa Kiserikali, kwa sababu Halmashauri wenyewe wana mkakati wa kujenga takribani shule sita mpya za sekondari. Sisi Serikali katika hilo tutawaunga mkono shule hizi, na mara baada ya kukamilishwa kwake tutaweza kuzisajili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo kubwa vijana wetu ambao wanapata nafasi baada ya kumaliza kidato cha nne waweze kupata nafasi ya kidato cha tano na sita. Kuhusu suala la shule za kule Mlalo, Mheshimiwa Shangazi kama mtakuwa mmeianzisha hii mipango kule Mlalo katika Halmashauri yenu ya Lushoto, naomba nikuhakikishie kwamba Serikali haitosita kushirikiana nanyi. Kwa sababu hata nilipokuwa ziarani kule mlinipeleka shule moja ya sekondari ambayo mmeniambia kwamba watoto wanafaulu kwa kiwango kikubwa sana. Kwa hiyo Serikali itaungana na ninyi, lakini ni mara tu baada ya kuanza michakato hii mliyoianza ya ujenzi wa sekondari za kidato cha tano na sita. Serikali tutaungana na hilo ili kuwafanikisha wananchi wa Mlalo na Wilaya ya Lushoto kwa ujumla ili waweze kupata fursa hii ya elimu ya kidato cha tano na cha sita. (Makofi)
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante, majibu ya Wizara yanaonekana ni mepesi sana kwa sababu nchi nyingi anazozitaja ni nchi za kiafrika na lengo mahususi ya hili swali tulikuwa tunataka tujue nchi zote ulimwenguni lakini natambua kwamba nchi zilizopo chini ya Umoja wa…

Nchi zilizopo chini ya Umoja wa Madola (Commonwealth) tuna utaratibu huu wa visa on entry or visa on arrival. Je, kwa nini wananchi wa India wanapokuja Tanzania wanakuja kwa visa on arrival, lakini sisi tunapokwenda nchi kama India lazima uombe visa hasa ikichukuliwa kwamba Watanzania wengi wanakwenda India kwa ajili ya kupata huduma za matibabu?
Swali la pili, zipo nchi za Afrika Magharibi ambazo wanaingia kwa visa ya referred visa ikiwemo Cote d’voire, Senegal na Mali. Je, kwa nini sasa isiwe ni wakati muafaka wa kuiunganisha Nigeria katika nchi hizi kwasababu inaonekana kwamba mara nyingi wanapoingia huku kwetu wanahatarisha usalama wa nchi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli nchi za Jumuiya ya Madola zina utaratibu wa wananchi wake kutembeleana bila visa. Lakini kama nilivyojibu katika swali langu la msingi kwamba ushirikiano na matengamano hayo ikiwemo la Jumuiya ya Madola, utaratibu wake unaweza kubadilika kulingana na mahusiano pamoja na hali za kiusalama. Kwa hiyo, sio jambo la kushangaza kuona India na Nigeria juu ya kwamba zote mbili ni wanachama wa Jumuiya ya Madola lakini utaratibu wa visa on arrival ukawa hautumiki.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Wakati anajibu suala la Mbuga ya Mkomazi na Mbuga ya Mkomazi kwa Mkoa wa Tanga kuna Wilaya ya Lushoto, Korogwe na Mkinga. Tatizo la mipaka hata kule linatuathiri na kuna timu sasa inapita kutathmini hilo tatizo, nataka nitambue, je, Serikali kupitia Wizara ya Maliasili imeshirikiana na hawa watalaamu ambao wanapita kutathmini ile mipaka, hasa katika eneo la Mwakijembe Wilaya ya Mkinga?

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mbuga ya Mkomazi kwa Mkoa wa Tanga iko katika Wilaya za Lushoto, Korogwe na Mkinga na hili tatizo la mipaka sasa hivi kuna timu ya ambayo iko chini ya RAS kwa kule Tanga inafuatilia haya maeneo yenye migogoro ambayo wananchi na mbuga wanakinzana hasa eneo la Mwakijembe katika Halmashauri ya Mkinga, je, Wizara ya Maliasili na Utalii inatambua uwepo wa hii timu ambayo inakagua mipaka?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua uwepo wa timu hiyo inayokagua mipaka.
Lakini Mheshimiwa Mbatia nafikiri wakati nikiwa namjibu swali alikuwa anasisitiza lini nilimuona wakati anataoka alikuwa anaendelea kuongea anauliza lini, sasa Mheshimiwa Mbatia tukimaliza kikao hiki cha Bunge (Kamati ya Fedha hivi) mimi na wewe tuambatane tukaangalie uhalisia ulivyo halafu tuweke ratiba ya kushughulikia suala hilo.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa uwepo wa Msitu wa Shengena, Msitu wa Shangai na Msitu wa Bombo ndiyo unaosaidia uwepo wa Hifadhi ya Mkomazi; lakini katika Msitu huo wa Bombo kuna uvamizi mkubwa unaofanywa na wananchi. Je, ni lini sasa Serikali itaweka mipaka (beacons) kutenga eneo hili la Msitu wa Bombo ambao ni msitu maalum wa kuvuta mvua? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kweli kabisa msitu wa Bombo ni msitu muhimu sana kwa ajili ya Hifadhi ya Mkomazi, lakini pia kwa ajili ya ikolojia nzima ya eneo la Mkomazi. Sasa lini Serikali itaweka beacons?
Mheshimiwa Mwenyekiti, zoezi la uwekaji wa beacons linaendelea nchi nzima na nataka nimhakikishie kwamba kama bado hatujafika Mkomazi, nitakwenda kuangalia ratiba na kuona lini tunafika huko ili niweze kumpa tarehe kabisa, lini tunaweka katika hifadhi hiyo. Kwa hiyo, tuonane baada ya hapa, tuweze kuona ni lini beacons zinawekwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huo ni mpango wa Serikali ambao unaendelea sasa hivi kuweka beacons au kuweka alama za mipaka katika hifadhi zote nchini.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mheshimiwa Waziri anajibu swali hapo amezungumza kwamba upo mkakati wa kuzishirikisha Halmashauri na kuweza kuingia katika uzalishaji huu wa samaki.
Sasa kwa bahati mbaya sana mimi natokea katika Milima ya Usambara ambako huko hakuna mito, hakuna mabwawa, hakuna chochote, sisi samaki tunamuona kwenye picha na wenzangu Wapare kule Same. Sasa anatuambia nini, Wizara ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba hizi Halmashauri ambazo hazina mito wala maziwa zinafaidika na huu uzalishaji wa samaki? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi hii ya kumjibu Mheshimiwa Shangazi swali lake la nyongeza na anauliza Wizara ina mkakati gani wa kuwasaidia watu wa milimani ambao hawana maziwa, hawana mabwawa wala hawana maji yanayotiririka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao mpango mzuri sana na hivyo nampongeza sana Mheshimiwa Shangazi na ni ukweli kwamba samaki ni chanzo cha protein, lakini vilevile na madini yaliyo muhimu kabisa katika mwili wa binadamu yanayoenda kuimarisha mifumo ya mifupa na mengineyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimechukua ombi lake Mheshimiwa Shangazi la kutaka watu wa kule Mlalo waweze kupata mabwawa ya samaki ili waweze kufuga samaki ili waweze kupata faida ya kupata protein na virutubisho vingine.
Namhakikishia ya kwamba tutampatia wataalam watakaoweza kushirikiana na halmashauri yake, watakaoweza kwenda kufanya mapinduzi haya ya ufugaji wa samaki na watapata na vifaranga pia tena si vifaranga tu, vifaranga bora.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Napenda kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa kilichokuwa Kiwanda cha Mbolea cha Tanga kimebinafsishwa na sasa zinaendelea shughuli nyingine pale ambazo hazihusiani na mbolea. Kwa mahitaji haya ambapo bado mbolea inahitajika nchini, je, Serikali haioni ni wakati muafaka sasa wa kukirejesha kiwanda kile ili kiweze kuzalisha mbolea?
NAIBU WAZIRI VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimshukuru kwa jinsi ambavyo anafuatilia shughuli zetu za viwanda na kulifanya swali letu kuwa makini katika eneo husika. Niseme tu kwamba ni kweli eneo hilo ambalo lilikuwa Kiwanda cha Mbolea Tanga kimebadilishwa na sasa kinashughulika na shughuli za mafuta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba lengo la kubinafsisha ilikuwa si tu kwamba lazima kuendeleza kiwanda kile kilichopo hata kama mashine zilizopo zilikuwa hazifai. Kimsingi mashine zile zilikuwa zimezeeka sana na mwekezaji alitoa mapendekezo akaandika umuhimu wa kuwekeza katika mafuta kwa misingi ya kupokea mafuta, kuhifadhi na kusambaza na sasa hivi ana uwezo wa kusambaza mafuta kufikia lita za ujazo milioni 126.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli imekuwa ni mkombozi kwa wananchi na wafanyabiashara wote wa maeneo ya Tanga, Arusha na maeneo ya Kaskazini hata Kigoma. Kwa hiyo, binafsi nampongeza kwa uwekezaji huo kwa sababu lengo letu sisi ni kuongeza tija katika shughuli zote za kiuwekezaji.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya maswali mawili ya nyongeza. Kwanza, napenda kuiuliza Serikali, je, imepangaje kusaidia vyuo vikuu vijiendeshe kwa mujibu wa sheria za nchi lakini bila kuathiri uhuru wa utoaji wa taaluma?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ubora wa elimu inayotolewa na vyuo vikuu vyetu imekuwa ni ya kutia mashaka na inashindwa kuwaandaa vijana kujiajiri lakini pia kushindana kimataifa. Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuboresha mitaala ya elimu ya vyuo vikuu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaheshimu uhuru wa vyuo vikuu (academic freedom) na mara nyingi sana Serikali haitaingilia namna vyuo vikuu vinavyoendeshwa. Hata hivyo, uhuru huo lazima ufanyiwe kazi ndani ya sheria. Kwa hiyo, vyuo vyote vinatakiwa viwe na uhuru lakini uhuru wake uko kwenye mipaka ambayo imewekwa na sheria, kanuni na taratibu. Ndiyo maana chuo kikuu chochote, kiwe cha Serikali au binafsi ambacho hakifuati sheria, kanuni, taratibu na miongozo hatutasita kukichukulia hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili kwamba ni namna gani tunajaribu kuboresha quality ya elimu katika vyuo vikuu vyetu, jibu lake linafanana na hilo ambalo nimeshatoa kwamba Tume ya Vyuo Vikuu ambayo ndiyo hasa imepewa kazi ya kuhakikisha kwamba inadhibiti ubora wa elimu katika vyuo vyetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia itaendelea kuhakikisha kwamba taratibu zile zinafuatwa na ndiyo maana tunafanya tathmini ya kila mara na vyuo vikuu vile ambavyo havitakuwa vimefuata taratibu zile vitafungiwa. Ndiyo maana kwa mwaka huu vyuo 19 vimefungiwa na programu 75 za vyuo 22 zimesitishwa. Tunachosema tu ni kwamba ili tuweze kuwa na ubora unaotakiwa, tutaendelea kuchukua hatua ili elimu yetu iendelee kuwa bora.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali ninayo maswali ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa amesema lengo la chuo hiki cha mahakama ni kutoa elimu ambayo inasaidia watumishi walioko makazini waweze kuboresha ufanisi na utendaji wao; je, haoni sasa ni muhimu kwa chuo hiki pia kuanzisha kozi maalum kwa watumishi wengine wa Idara ya Mahakama wakiwemo makarani na wakalimani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Serikali imeanzisha msaada wa huduma ya msaada wa kisheria na kwa kuwa kule Lushoto nako tuna watoa msaada wa kisheria; je, haoni kwamba ni muhimu chuo hiki kikasaidia watoa msaada wa kisheria katika Halmashauri ya Lushoto kuwajengea uwezo ili waende kuwasaidia wananchi huko vijijini? (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kuhusu kutoa elimu kwa ngazi ya makarani na watu wa masijala ya mahakama, nakubaliana naye kabisa kwamba wakati umefika na maadam chuo kimeweka kikosi kazi cha kupitia upya mitaala na mafunzo mbalimbali ya kozi mbalimbali katika chuo hicho, nachukua maoni yake na nitawasilisha katika kikosi kazi hicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la kutoa elimu kwa paralegal kwa ajili ya msaada wa kisheria pia wazo hilo ni zuri na siyo tu kwa Lushoto, nadhani kwa maeneo yote ya Mikoa ya Kaskazini ambayo yako karibu na Chuo cha Lushoto.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo TAMISEMI na Waziri anafahamu, Halmashauri ya Lushoto ina upungufu wa Walimu 826 wa shule za msingi. Sasa Serikali inatuambia nini kuhusu huu usumbufu ambao umesababishwa na Wizara yenyewe? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Rashid Shangazi, ambaye juzi alikuwa Singida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda nikanushe kwamba upungufu wa Walimu haujasababishwa na Wizara yetu kwa sababu upungufu wa watumishi uko kwenye kila sekta na si sekta ya elimu peke yake. Tunafanya jitihada mbalimbali kuhakikisha kwamba tunapunguza upungufu wa watumishi kwa Serikali nzima kwa sekta zote. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Shangazi kwamba tutakapokuwa tunaajiri na tutakapokuwa tunahamisha Walimu Halmashauri yake na Jimbo lake la Lushoto hatutaliacha nyuma.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi hii.
Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, lakini hapo utaona amesema kwamba muda mfupi ujao watakuwa wamekamilisha ukusanyaji wa maoni ya wadau.
Swali langu la kwanza, je, wadau ambao ni Waheshimiwa Wabunge na ambao ni wawakilishi wa wananchi mpaka sasa naona bado hatujashirikishwa, haoni kwamba kuliacha kundi kubwa kama hili kunaweza kukaweka matobo tena kwenye sera ambayo inarekebishwa?
Swali la pili, je, ni kwa kiasi Serikali itachukua wajibu hasa kuhakikisha kwamba michezo ya kubahatisha inakuwa sehemu katika sera hii mpya ili kutanua mfuko wa michezo na kuweza kutoa udhamini wa kutosha katika michezo ili hata hawa wanamichezo wasiwe wanajiandaa wenyewe na wakati wakileta sifa za Taifa tunazipokea kama nchi? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba rasimu ya sera imejadiliwa na wadau mbalimbali, lakini hatujaleta Bungeni na siyo kawaida. Kutokana na umuhimu wa Bunge hili na vilevile mchango ambao kwa kweli mara nyingi unakuwa umefanyiwa kazi na Waheshimiwa Wabunge tutaangalia uwezekano wa kabla ya kufikia mwisho tuweze kupata mawazo ya Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Spika, pili kuhusu michezo ya kubahatisha ni kweli kabisa katika sera tuliyonayo sasa hivi ya mwaka 1995, michezo ya kubahatisha siyo sehemu ya michezo na tumechukua hatua ya kuingia katika mabadiliko ya sheria mbalimbali ambayo yatawasilishwa leo Bungeni hapa tunafanya mabadiliko ya sheria hiyo ili michezo ya kubahatisha nayo iwe sehemu ya michezo na iweze kuchangia katika maendeleo ya michezo nchini.
MHE. RASHID R. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Mimi naona wivu wenzangu wanapotoa pongezi kwamba maeneo yao umeme umeshapatikana, sasa mimi nina masikitiko makubwa kwamba bado katika Jimbo la Mlalo, Halmashauri hiyohiyo ya Lushoto, kata nne bado umeme haujawaka katika Kata za Mbalamo, Shagayu, Mbalu na Hemtoe. Barua ya kutoka REA kwenda kwa mkandarasi imetoka tangu mwaka jana. Nataka Mheshimiwa Waziri anipe commitment ni lini katika kata hizi na zenyewe umeme utawaka katika Jimbo la Mlalo, Halmashauri ya Lushoto?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Shangazi kwa maswali yake mazuri na kweli naungana na yeye kwamba kati ya maeneo ambayo mkandarasi alikuwa hajaanza kazi rasmi ni pamoja na Jimbo la Mheshimiwa Shangazi. Tunapoongea hapa na leo asubuhi tumeongea na Mheshimiwa Shangazi na mkandarasi ameshapeleka makundi manne, ni matarajio yetu atafanya kazi vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimuahidi Mheshimiwa Shangazi kwa niaba ya wananchi wake, mimi baada ya Bunge hili kuisha Mheshimiwa Shangazi tutafuatana mimi na naye tutakwenda kusimamia mguu kwa mguu mpaka vijiji vyake vyote ambavyo havijapatiwa umeme sasa vitapatiwa umeme. Awape uhakika wananchi wake kwamba Serikali hii haina mchezo kwenye suala la umeme vijijini.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu ya Serikali lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa hapa swali alilouliza lilikuwa ni kuhusu kupandisha hadhi Kituo cha Afya na amesema wana mpango wa kujenga Hospitali ya Wilaya ambayo wanazidi kuiboresha, je, ni lini sasa kituo hiki ambacho Mheshimiwa amekitaja kitapewa uwezeshaji kama ambavyo tumeona katika vituo mbalimbali nchini ili na chenyewe sasa kiweze kujitosheleza?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa katika Jimbo la Mlalo Halmashauri ya Lushoto, Zahanati ya Malindi na Zahanati ya Manolo zina miundombinu inayotosheleza kuwa na hadhi ya Vituo vya Afya na ukizingatia kwamba hizi ziko katika Tarafa ya Mtae ambayo haina hata kituo kimoja cha afya. Je, lini sasa Serikali itahakikisha inatusaidia katika ule mpango wa shilingi milioni mia nne mia tano ili Tarafa hii iweze kupata kituo cha afya chenye uhakika.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali la msingi linauliza likiwa linataka suala zima la Hospitali ya Wilaya na katika majibu ambayo nimeyatoa nimeeleza jitihada ambazo zinafanywa na Serikali katika kujenga Hospitali ya Wilaya ndiyo maana kimetengwa kiasi cha shilingi bilioni 1.5 ili ujenzi wa hospitali hiyo ambayo eneo tayari limeshatengwa ekari 40 ianze kujengwa. Sasa katika swali lake la msingi anataka hicho kituo cha afya ambacho kina hadhi ya kituo cha afya, labda Mheshimiwa Mbunge anadhani kwamba hakijakamilika. Kituo cha Afya kimekamilika na ndiyo maana kimekuwa kikitumika kama Hospitali ya Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la msingi la pili, kuhusiana na Jimboni kwake ambalo angependa zahanati ambazo ziko na zinafanya kazi zipandishwe hadhi zifanane na vituo vya afya au kuanza ujenzi wa vituo vya afya. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ni adhma ya Serikali kuhakikisha kwamba zahanati zinaendelea kuwepo lakini pia haiondoi haja ya kuwepo vituo vya afya. Wakati wowote ambapo pesa itapatikana hatutaacha kutizama maeneo ya kwake na ninaamini tutapata fursa pia kutembelea eneo la kwake.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Swali langu lilikuwa very specific kwa Gereza la Mng’aro, lakini naona Waziri ananijibu na magereza mengine nchini. Sasa gereza hili limejengwa kwa miti pamoja na udongo na linahatarisha hata usalama wa wafungwa ambao wako pale. Je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kuhakikisha kwamba, badala ya kusubiri changamoto za nchi nzima, kuwa na mpango wa muda mfupi wa kukarabati gereza hili?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa, gereza hili ni la kilimo na liko katika Skimu ya Kilimo ya Mng’aro ambayo ni kilimo cha mpunga na lilikuwa na uwezo wa kulisha magereza yote ya Mkoa wa Tanga. Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka kulipa zana bora za kilimo ili liweze kuzalisha zaidi na kuweza kulisha magereza yote ya Mkoa wa Tanga?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge, mara nyingi amekuwa akifuatilia sana maendeleo ya vyombo hivi vya usalama vilivyopo chini ya Wizara yetu ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Leo hili swali lake lake linaonesha msingi wa dhamira yake hiyo ya dhati.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusiana na swali lake la kwanza ambalo ametaka kujua kuhusu mpango mahususi wa ukarabati wa Gereza la Mng’aro; naomba nijibu swali hili pamoja na swali la pili kwa sababu yanaingiliana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Shangazi na Waheshimiwa Wabunge wengine, kwamba tumekuwa tukifanya jitihada mbalimbali ambazo zinasaidia kuboresha magereza yetu ambayo yako katika hali mbaya, ukiachilia mbali jitihada za Serikali kupitia bajeti kuu ambayo hata mwaka huu wa fedha tumetenga fedha hizo. Mifano iko mingi tu ambayo mimi binafsi nimefanya ziara maeneo kadhaa na tumeweza kushirikiana katika kuhakikisha kwamba tunafanya ukarabati kwa kutumia rasilimali katika maeneo husika. Naomba nichukue fursa hii kwa kutumia mfano huohuo ambao nimeweza kuona kwamba, umefanya kazi katika maeneo mengine ili tuupeleke Mlalo.
Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri hivi karibuni nilipofanya ziara katika Mkoa wa Lindi, watu wa Magereza wa Mkoa wa Lindi waliniambia kwamba, wangekuwa wamepata mashine za kufyatulia matofali ingerahisisha huu mchakato ambao tunauzungumza hapa. Nichukue fursa hii kumpa pongezi sana Kaimu Mkurugenzi wa National Housing Corporation ambaye baada ya kutoka Lindi nilimwandikia barua kumwomba mashine hizo na ametupatia mashine 10 kwa kuanzia ambazo nitazipeleka Lindi, lakini nitatumia mamlaka niliyokuwanayo kuchukua mashine moja ile kuipeleka kwa Mheshimiwa Shangazi, Mlalo, tukafanye kazi ile ya kuweza kuanza kufanya kazi ya ukarabati wa gereza letu lile kwa kutumia rasilimali za pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hiyo itasaidia vile vile kuhamasisha ujenzi wa mabweni ya ziada, kwa sababu suala la kilimo, kama swali lake la pili ambalo amelizungumza, linategemea vile vile nguvukazi ya wafungwa; ambapo kwa kiwango cha wafungwa waliopo Mng’aro sasa hivi na aina ya ukubwa wa shamba lile la karibu ekari nadhani zaidi ya 300 wafungwa wale hawatatosheleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tutafanya jitihada za kuongeza mabweni, ili tupate wafungwa zaidi na wakati huohuo nimuahidi pia Mheshimiwa Shangazi kwamba tuna mpango vile vile wa kupata matrekta sita mapya ambayo tutayagawa katika magereza ambayo ni ya kilimo makubwa. Vile vile kule kuna matrekta ambayo ni chakavu, kwa hiyo tutachukua trekta moja chakavu tutalitengeneza vizuri tuweze kulipeleka Mng’aro. Tukifanya hayo tutakuwa tumetatua matatizo yote mawili kwa pamoja, tutakuwa tumeimarisha miundombinu wakati huohuo suala la kilimo cha mpunga katika eneo lile litakuwa limepatiwa ufumbuzi.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Lushoto yenye tarafa tano ina Vituo vya Afya katika Tarafa ya Mlola, Mlalo, Mnazi pamoja na Lushoto Mjini; je, ni lini sasa Serikali itajenga Kituo cha Afya katika Tarafa pekee iliyobaki ya Mtae?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Naibu Waziri kwa majibu mazuri sana ya maswali yote ya awali. Mheshimiwa Shangazi alishafika ofisini kwetu mara kadhaa kuhusu kituo hiki na ndiyo maana tumeanza katika awamu hii kupeleka pale Mnazi. Naomba nimhakikishie kwa sababu wananchi wa Mtae wanapata shida, katika kipindi kinachokuja tutafanya kila liwezekanalo, kuhakikisha eneo lile tunalipatia Kituo cha Afya. Lengo letu ni kupunguza vifo vya mama na watoto. (Makofi)
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu ya Serikali, ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa, Serikali imenyang’anya vyanzo vya mapato vya halmashauri lakini pia imeshusha asilimia za mazao hasa ya kibiashara kutoka asilimia 5 mpaka 3, hivyo halmashauri nyingi kushindwa kutoa hii asilimia 10. Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka kusaidia kuongeza ruzuku katika eneo hili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa, zipo halmashauri ambazo zinategemea mazao ya kilimo pekee, kwa mfano Halmashauri ya Lushoto, Halmashauri ya Handeni na nyinginezo na zipo halmashauri ambazo zina rasilimali kama madini, hivyo mfuko huu unakuwa hauna ulingano kwa maana kwamba yapo maeneo ambayo wanapata mapato makubwa na mengine wanapata mapato kidogo sana. Hatuoni kwamba kwa kufanya hivi tunaleta misingi ya ubaguzi katika pato la Taifa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Rashid Shangazi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la kwanza amesema kwamba, kuna baadhi ya vyanzo vya mapato halmashauri zimenyang’anywa. Nataka nimhakikishie kwamba, utaratibu wa Serikali ni mzuri. Katika baadhi ya vyanzo ambavyo vimechukuliwa, kwa mfano, vinavyokusanywa na TRA, bajeti ya halmashauri inakuwa iko palepale na baada ya ukusanyaji bajeti ambayo ilitengwa huwa inarudishwa kwa halmashauri. Kuhusu kwamba kwa nini tusiweke ruzuku maalum ili kufidia, nadhani ni wazo ambalo tunaweza tukalifanyia kazi kwa mwaka ujao wa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili kwamba baadhi ya halmashauri mapato ni kidogo ukilinganisha na halmashauri nyingine. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Shangazi na Waheshimiwa Wabunge kwamba katika ukokotoaji ambao tutaufanya hivi karibuni, kama sehemu ya kuweka utaratibu mzuri zaidi wa kuziangalia hizi halmashauri zetu. Tutaangalia utaratibu ambao ni mzuri zaidi ili kusudi halmashauri ambazo zina uwezo mkubwa na halmashauri ambazo hazina uwezo kabisa tuangalie namna ya kutekeleza agizo hilo.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza nitoe shukurani kwa Wizara hii kwa sababu wametujengea mtambo katika eneo letu la Kwemashai kule Lushoto; lakini bado usikivu haupo vizuri. Sasa, je, ni lini Serikali itahakikisha kwamba usikivu wa TBC katika Wilaya ya Lushoto na leo wenyewe wapo hapa wamekuja kufuatilia jambo hili utakuwa na usikivu unaoeleweka?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa napenda kumpongeza Mheshimiwa Rashid Shangazi kwa sababu yeye amekuwa ni mdau mkubwa wa TBC ndani ya Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. Hata hivyo, kama ambavyo ametoa pongezi na mimi kwa niaba ya Serikali napenda kupokea pongezi hizo, kwamba TBC sasa hivi tumekwisha kuweza kujenga Mtambo katika Wilaya yake ya Lushoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto kubwa ambayo ipo katika Wilaya hiyo ya Lushoto ambayo inasababisha usikivu kutokuwa mzuri ni kwamba mitambo hii inapofungwa lazima kuwe kuna muda kidogo wa kuweza kufanyia maboresho. Kwa hiyo, nichukue nafasi hii kuweza kumhakikishia Mheshimiwa Shangazi, pamoja na wananchi wote wa Wilaya ya Lushoto ambao wapo ndani ya Bunge hili, kwamba ndani ya miezi miwili nilishaongea na Mkurugenzi wa TBC ameniahidi kwamba atatuma timu yake ya wataalam kwenda kufanya maboresho katika mtambo huo ili basi usikivu wa TBC uwe mzuri. Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
(a) Pamoja na majibu ya Serikali ambayo kwa kweli hayaridhishi sana na hayaendani hata na swali lilivyoulizwa, naomba tu sasa nipate kuuliza kulingana na majibu yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shilingi milioni 4.8 alizotenga kwa ajili ya majosho katika vijiji vya Mkundi - Mtae na Kiwanja, haoni kwamba ni fedha chache sana kulinganisha na hizi shilingi milioni 12 zilizotengwa kwa ajili ya Vijiji vya Kamba na Kivingo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mtazamo huo, Serikali haioni kwamba haina dhamira ya kweli ya kuondoa kero kwa wafugaji?
(b) Kwa kuwa hakuna maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya maeneo ya malisho, hili nalizungumza mwezi wa Ramadhani nikiwa na uhakika; hizi beacon Serikali inazotaka kwenda kuweka, inaenda kuziweka katika maeneo gani? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi kwa namna ambavyo anawapigania wananchi wake hasa kundi hili muhimu la wafugaji katika Jimbo lake. Swali lake la kwanza anataka kujua juu ya dhamira ya dhati ya Serikali katika kuwasaidia wafugaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishie kwamba Serikali inayo dhamira ya dhati ya kuwasaidia wafugaji na ndiyo maana katika bajeti yetu ya mwaka huu 2018/2019 ziko pesa tulizozitenga kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunatengeneza miundombinu ya mifugo na kwa upande wa swali la pili, anasema wapi tunakwenda kuweka hizo beacon?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mipango ya matumizi bora ya ardhi ipo katika Halmashauri na ardhi za vijiji zipo kwa mujibu wa Sheria Na. 5 ya Sheria ya Ardhi na Sheria Na. 6 ya Matumizi ya Ardhi. Kwa hiyo, namna ya kupanga na namna ya kutumia bado ipo katika mamlaka ya Serikali za Mitaa wao wenyewe ikiwa Mbunge yeye ni mmojawapo katika Madiwani ambao wanapaswa kwenda kusimamia na kushiriki katika upangaji wa matumizi bora ya ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimwambie kwamba kwa upande kama Serikali Kuu tunayo sheria inayolinda maeneo hayo hasa ya malisho, Sheria Na. 13 ya mwaka 2010 inayohusu malisho ya mifugo. Kwa hiyo, nataka nimhakikishie kwamba sisi kama Serikali tuna nia dhahiri na ya dhati kabisa ya kuwasaidia wafugaji.
MHE. RASHID A SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Halmashauri ya Lushoto na hospitali ya Wilaya ya Lushoto inahudumia Majimbo matatu na Halmashauri mbili kwa maana ya Lushoto na Bumbuli na inakabiliwa na msongamo mkubwa sana wa wagonjwa. Je ni lini sasa Serikali itaipa fedha ili kupanua huduma hizi za afya katika Wilaya ya Lushoto?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba Wilaya ambayo Mheshimiwa Mbunge anaitaja ina population kubwa. Pia ni ukweli usiopinga kwamba Halmashauri wanajua uhitaji, naomba kwa kushirikiana na Halmashauri na hasa Mheshimiwa Mbunge akiwa wa kwanza kuelekeza namna iliyo bora ya kuhakikisha maeneo mengi vituo vya afya vinajengwa hasa kwa kushirikisha wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ni vizuri kama ni suala la ujenzi wa vituo vingine ili kuweza kutoa nafasi kwa hospitali ya Wilaya, wazo hilo jema ni vizuri likaanza kwao na sisi Serikali tutaunga mkono jitihada za wananchi.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu ya Serikali yenye kutia matumaini, nina maswali mawili madogo ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa eneo hili la Mkomazi lina barabara ambayo inaunganisha utalii wa ukanda wa juu na ukanda wa chini kwa maana ya barabara ya Hekicho – Kwekanda - Lugulua, je, Wizara hii iko tayari kukaa na wenzetu wa TAMISEMI kupitia TARURA ili waweze kuboresha miundombinu wageni waweze kufika kwa urahisi katika geti hili ambalo tunakusudia kulifungua?

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Wilaya Lushoto ina vivutio vingi vya utalii na vingi bado havijatambulika ikiwemo utalii wa maliasili lakini pia na utamaduni ikiwemo makazi yale ya Chifu Kimweri, Waziri uko tayari kuongozana nami kwenda Lushoto ili angalau waweze kuvibaini vivutio hivi viweze kugeuka kuwa fursa ya kiuchumi kwa wananchi wa Lushoto?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, baada ya kuwahakikishia ufunguzi wa lango hili, TANAPA watashirikiana na TAMISEMI kuona
namna kurekebisha barabara hii ambayo Mheshimiwa Mbunge anaomba kutoka Hekicho kwenda Kwekanda ili kuweza kufungua pia lango la utalii kwenye maeneo haya ya misitu.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu kuvitambua vivutio vya utalii ambavyo bado havijatambuliwa, niko tayari kuongozana na Mheshimiwa Mbunge kwenda kuangalia vivutio hivi na kuviweka kwenye package ya pamoja kuhamisha watu wa TANAPA waweze kuvitangaza.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu ya Serikali ninayo maswali mawili ya madogo ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa Sera ya elimu ya mwaka 2014 imetamka wazi kwamba elimu ya msingi itaishia darasa la sita na hadi hivi tunavyozungumza Serikali bado haijatekeleza katika eneo hilo. Je, Serikali inatuambiaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni kwa kiasi gani Sera hii ya Elimu inazingatia ubora wa elimu, hasa ukizingatia kwamba miongoni mwa mikoa ambayo huwa haifanyi vizuri katika mitihani mbalimbali ni Mkoa wa Tanga. Sasa nataka kujua ni kwa kiasi gani Sera hii ya elimu inazingatia suala zima la ubora wa elimu kwa maana ya quality assurance? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Rashid Shangaz, Mbunge wa Mlalo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kujibu, naomba nitumie nafasi hii kusema kwamba Mheshimiwa Shangazi amekuwa akifuatilia suala hili na masuala yote yanayohusiana na elimu na kwa kweli kwa nafasi yake hakuna ubishi kwamba ni moja kati ya Wabunge bora kabisa ambao wamewahi kutokea katika Bunge hili. Swali lake la kwanza ni hilo kwamba kwa nini hatujatekeleza wazo lile la Sera la kuishia darasa la sita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jibu letu ni kwamba Sera siyo Msahafu, kwa hiyo Serikali inabadilisha Sera kadiri inavyoona kwamba inafaa kulingana na mahitaji ya wakati huo. Kwa sasa busara imetujia upya kwamba elimu kuanzia darasa la kwanza mpaka la saba siyo kitu kibaya, kwa hiyo hatuna haja ya kubadilisha na ndiyo maana tumebakia na mfumo wa zamani na hatujavunja sheria, Sera siyo lazima itekelezwe, Sera unatekeleza na unabadilisha kadiri unavyoona inafaa. Kwa sasa tuko kwenye mapitio na ni moja ya mambo ambayo tuliona kwamba hatutatekeleza na tutaendelea na utaratibu wa zamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuhusiana na ubora wa elimu ni kweli kwamba Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, imeweka msisitizo mkubwa katika masuala ya udhibiti ubora wa elimu na ndiyo maana kumetokea mabadiliko makubwa sana katika mfumo wetu wa udhibiti ubora. Zamani tulikuwa tunasema ni ukaguzi wa elimu lakini siku hizi tunadhibiti ubora, lakini vile vile mtindo mpya wa kudhibiti ubora ni wa kiushirikishwaji zaidi unawaleta wadau wote kushiriki katika kudhibiti ubora wa elimu, lakini vilevile kama wote mnavyojua sasa tuko katika mikakati mikubwa ya kuhakikisha kwamba Wadhibiti Ubora wanawezeshwa kwa kupata vifaa na ofisi. Kimsingi tumeweka mikakati mikubwa sana ya kuhakikisha kwamba elimu yetu inakuwa bora. Moja kati ya masuala ambayo tunayafanyia kazi katika mapitio ya Sera ni kuendelea kuweka mifumo ambayo itawezesha kudhibiti ubora wa elimu.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Katika Kijiji cha Mkundi ya Mtae, Tarafa ya Umba ambayo kimsingi Tarafa hii karibu eneo kubwa ni wafugaji, pana migogoro ya ardhi ambayo ni baina ya wakulima na wafugaji na mara kadhaa nimejaribu kuwasiliana na Wizara kuona namna bora ya kutatua mgogoro katika eneo hili ambalo kimsingi eneo hili lilikuwa ni eneo la wafugaji. Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuboresha maeneo haya hasa katika sekta nzima ya ufugaji?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Shangazi, Mbunge wa Mlalo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imejipanga vyema katika kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji na tumeunda Kamati ambayo inatembea nchi nzima katika kuhakikisha kwamba migogoro ya wakulima na wafugaji inapatiwa suluhu na kwisha kabisa. Kijiji alichokitaja cha Mkundi Mtae ambapo kipo katika Tarafa nzima ya Umba ambayo sisi kama Wizara ya Mifugo tumekitambua kijiji hiki na maeneo mazima ya Tarafa ya Umba kuwa ni maeneo yanayoshughulika zaidi na shughuli za ufugaji. Nataka nimhakikishie Wizara yetu inayo mipango mizuri ya kuhakikisha kwamba fursa na uwekezaji katika mifugo inapatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yeye Mwenyewe Mheshimiwa Mbunge Rashid Shangazi ameleta maombi ya kuboresha majosho yaliyoko katika eneo hili. Naomba nimhakikishie kuwa, majosho yale yamechukuliwa na Wizara yetu na yapo katika mpango wa kuhakikisha yanarekebishwa na yatakapokuwa tayari yamerekebishwa sisi katika Wizara tutakuwa pamoja na yeye kwenda nae pale kwenda kuyazindua kwa ajili ya kuboresha sekta yetu ya mifugo.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa majibu hayo, lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

(a) Kwa kuwa barabara hii ya Mtii – Mtae – Mnazi, kilometa 12.7 pamoja na Kwekanda – Hekcho – Rugulu hadi Mkomazi kilometa 17.5, zote hizi tumeziweka katika bajeti ya Mwaka wa Fedha 2019/2020 na bajeti tayari tumeshapitisha. Je, Serikali inatoa tamko gani kwa wananchi wa Mlalo?

(b) Kwa kuwa, barabara hizi siyo tu kwamba zinaunganisha Tarafa za Umba – Mlalo na Mtae, lakini pia zinaunganisha wilaya jirani za Korogwe na Same: Je, Serikali haioni kwamba kwa kutofanya wepesi wa kurekebisha barabara hizi inakuwa ni kikwazo kwa fursa za kiuchumi kwa wananchi wa Mlalo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, kipekee kwanza naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Shangazi, amekuwa akipigia kelele sana kuhusu barabara hii ya kwenda Mtae na mara nyingi sana amefika ofisini kwetu. Naomba nimpongeze katika hilo.

Mheshimiwa Spika, katika swali lake anaulizia kwamba tayari bajeti imeshapitishwa, nini tamko la Serikali kuhusiana na ujenzi wa barabara hiyo? Bajeti ambayo imepitishwa kwa ajili ya Wilaya ya Lushoto ni jumla ya shilingi bilioni 1.8. Kama katika bajeti yao na barabara hii ipo, ni vizuri wakahakikisha kwamba barabara hii ni muhimu ikaanza kutengenezwa mapema.

Mheshimiwa Spika, kwa vile bajeti inahusu shilingi bilioni 2.5 ambayo siyo rahisi, Bajeti ambayo imepitishwa ni
1.4 na wao wanahitaji shilingi bilioni 2.5; na kilometa katika Wilaya ya Lushoto ni jumla ya 935. Naomba Meneja wa TARURA ahakikishe katika vipaumbele vya barabara za kutengenezwa iwe pamoja na barabara hii.

Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili, anaulizia je, Serikali haioni umuhimu wa kutengeneza barabara ya kuunganisha kwenda Lushoto na wilaya nyingine kwa maana ya fursa ya kiuchumi? Ni ukweli usiopingika kwamba maeneo ambayo barabara haipitiki tunakuwa tunawanyima wananchi fursa ya kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika pia kwamba bajeti yetu haiwezi ikakidhi kwa mara moja maeneo yote. Naomba Mheshimiwa Mbunge aendelee kuvuta subira na yeye mwenyewe ni shuhuda, tangu tumeanzisha chombo cha TARURA kazi inayofanyika ni nzuri na hakika na barabara hii itawekwa kipaumbele ili iweze kutengenezwa.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante kwa kunipa nafasi hii. Hospitali ya Mkoa wa Tanga Bombo ni miongoni mwa hospitali kongwe hapa nchini na inahudumia zaidi ya halmashauri 11 pia inahudumia kisiwa kizima cha Pemba. Miundombinu yake imechakaa sana kiasi kwamba sasa hivi hata sio rafiki kwa wagonjwa lakini pia kwa wenzetu wenye ulemavu kwa sababu hakuna lifti katika wodi za wagonjwa.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha miundombinu ya hospitali hii kongwe?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali tunakiri miundombinu ya hospitali ya Bombo ni hospitali moja kongwe sana ndani ya nchi na nimepata fursa ya kuitembelea hospitali hii na kuona hizo changamoto hususani klatika jengo la wazazi ambapo wagonjwa hakuna lifti pale na imekuwa inaleta adha kidogo kwa wagonjwa kuweza kufika kule juu gorophani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali tumeliona hilo na kama nilivyosema katika jibu langu la msingi Serikali tumekabidhiwa hospitali hizi za rufaa za mikoa, makusudio yetu ni kuziboresha hospitali zetu zote hizi za rufaa kwa kuanza tunataka tujielekeze katika huduma za dharura, huduma za ICU, huduma za theatre, na majengo ya akina mama na watoto. Kwa hiyo tathmini tumeshafanya na kadri fedha zitakapopatikana tutaendelea kufanya maboresho haya na kuhakikisha kwamba hospitali hizi za rufaa za mikoa ikiwa ni pamoja na Bombo zinafanyiwa marekebisho yanayostahiki.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu ya Serikali lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kwa mujibu wa Katiba Ibara ya 18(d) haki ya kupata taarifa ni haki ya msingi kabisa na imetajwa kwenye Katiba na Tanzania siyo kisiwa kwa maana kwamba tunatakiwa na sisi mambo yetu yafahamike kimataifa.

Je, Serikali haioni kwamba kuzizuia hasa Azam kuonesha matangazo haya ni kunyima fursa ya habari za ndani kujulikana kimataifa?

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima kuwa wazalendo ni kupenda vya nyumbani na hawa Azam tumeona wakifanya kazi kubwa sana ya kuelimisha Taifa na kutoa taarifa mbalimbali za kijamii na mara nyingi hata matangazo ya Live ya Mheshimiwa Rais yanaonekana kupitia Azam.

Sasa Serikali ina mkakati gani mahsusi wa kuangalia hizi sheria na kanuni ili kuweza kuruhusu Azam TV iweze kuruka ndani na kuweza kuonekana katika ving’amuzi hivi tupate taarifa za channel zote za ndani zionekane katika Azam TV.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Rashid Shangazi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana kwa kuwa amekuwa ni mmoja kati ya wadau wa tasnia ya habari kwa jinsi anavyofuatilia masuala haya ya visimbusi au ving’amuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kujibu maswali yake mawili ni kwamba ni kweli tunakiri kwamba kila Mtanzania anayo haki ya kupata habari na ndiyo maana kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania tulitengeneza utaratibu wa kutoa leseni za aina mbalimbali kwa watoa huduma za matangazo kuweza ku-apply. Watu wa StarTimes, Ting na Continental wali-apply leseni ambazo zinawawezesha kuonesha free to air channels lakini Azam, Zuku na wengine wali-apply leseni ambazo zinawaruhusu kuonesha matangazo kwa njia ya kulipia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama Serikali tuliwaambia kabisa madhara au faida ya kuchukua leseni za aina hiyo ambazo hata gharama ya ulipiaji kwa mwaka ni tofauti. Azam waliamua kuchukua ile ya kimataifa kwa sababu walitaka mtu anayetaka kuona habari kupitia Azam aweze kulipia; kitendo cha wao kuanza kuonyesha channels za free to air, zile ambazo zinamruhusu mwananchi yeyote hata kama hela imeisha kwenye king’amuzi aone, haikuwa ni sehemu ya masharti ya leseni yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kwa swali lake la pili, nimuondoe wasiwasi kwamba kati ya watu walio-apply leseni za kuonesha na free to air channel Azam wapo na nimuondoe wasiwasi kwamba jana wamepokea hiyo leseni na wametuhakikishia kama Serikali kwamba ndani ya miezi saba watakuwa wameshajenga DDT eneo lote la nchi yetu kwa ajili ya kurusha hizo channels za bure.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mheshimiwa Naibu Waziri alikuwa Mlalo mwezi wa 12 baada ya zile mvua kubwa ambazo zimesababisha mafuriko na maporomoko makubwa sana kule na ameona barabara ile na hali ilivyo. Je, anatupa majibu gani ya haraka kuhakikisha kwamba fedha zinapatikana na pia waongeze ujenzi angalau kwa kilometa 10 kila mwaka?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; barabara ya kutoka Maramba kwenda Mnaro – Lunguza hadi Mnazi na yenyewe pia ni ni ya Wakala wa Barabara wa Mkoa. Halikadhalika, barabara ya kutoka Lukozi kwenda Mtae kupitia Manoro lakini pia kupitia Makose zote hizi ni barabara ambazo zinahudumiwa na Wakala wa Barabara wa Mkoa. Mpaka sasa hivi ninavyozungumza barabara hizi hazipitiki kwa maana kwamba wananchi wanapata, shida inabidi watumie usafiri wa bodaboda na kutembea kwa miguu. Serikali inatuhakikishia msaada gani wa haraka wa kuhakikisha kwamba barabara hizi zinapitika haraka inavyowezekana? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza uniruhusu nitoe pole kwa Mheshimiwa Shangazi na wananchi wa Mlalo kwa sababu wakati ule wa mvua nyingi za mwezi wa kumi na mwezi wa kumi na moja tulipata maporomoko ya udongo ambayo pia yalisababisha vifo vya watu kama watano hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uniruhusu nimpongeze pia Mheshimiwa Mbunge, Mheshimiwa Shangazi kwa kweli ni mahiri kwa kushughulikia mambo na nafikiri wananchi wa Mlalo hawakufanya makosa kumchagua kwa sababu Mheshimiwa Shangazi utamuona anazungumzia juu ya barabara lakini sio barabara yake, amezungumza juu ya barabara ambazo zinaunganisha na maeneo mengine. Pia tumeona kwa umahiri wake hapa akishughulika na masuala ya michezo, wote tunafahamu. Mheshimiwa Shangazi pia ni coordinator mzuri kwenye upande wa chama, kwa hiyo, Mheshimiwa Shangazi nakupongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lako la barabara ya Mlalo, nafahamu kwamba kwenye mafuriko yaliyotokea hata eneo kubwa la uchumi kwenye eneo lako la umwagiliaji kule Mlalo ulipata shida na barabara haipitiki na ndio maana nilitembelea maeneo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Shangazi kwamba kwa jinsi nature ilivyo, tulikubaliana na tumetoa maelekezo kwamba angalau tuongeze kidogo kwenye bajeti zetu ndio mkakati wetu ili angalau maeneo yale yote yaliyo makorofi kama kilometa 10 hivi tuweze kuya-cover ili wananchi wasiendelee kupata shida tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nikuhakikishie tunajitahidi kadri tutakavyoweza kupata nafasi kwenye bajeti yetu tupatazame eneo hili ili wananchi wa eneo hili la Mlalo waweze kupata huduma vizuri na hasa ukianzia kule Mlalo kuelekea Lushoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili, kama nilivyosema Mheshimiwa Shangazi anafuatilia kuona wananchi wa Mlalo wanaweza kusafiri kwa vizuri kabisa kuja huku Lushoto lakini wanaweza wakasafiri vizuri kabisa kwenda kule Malamba na Same kupitia kule Bondeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Shangazi nikuhakikishie kwa wananchi wako wa Malamba, Lunguza, Mnazi, Lukozi, Manolo na hadi kule Mtai kwa jinsi tulivyoona hali ilivyo na tumetoa maelekezo kwa Meneja wa TANROAD Mkoa wa Tanga kwamba tuweze kuweka fungu la kutosha kwa sababu hizi barabara angalau tuziboreshe ili madaraja yaweze kukaa vizuri, tuweke changarawe katika maeneo haya ili barabara ikae vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Shangazi vuta subira tu kwa sababu maeneo haya yote nimeyatembelea, nitakuwa na umakini mkubwa kuhakikisha kwamba wakati tunaangalia bajeti yetu basi wananchi wa maeneo haya wanapitika vizuri. Kwa sababu kisera lazima tuhakikishe wananchi kwanza wanapita halafu tuendelee ku-deal na uboreshaji wa makalavati na madaraja ili wananchi hawa waweze kuwa supported kwenye hali ya uchumi katika eneo hili, ahsante sana. (Makofi)
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, asante kwa nafasi hii, katika Halmashauri ya Lushoto, Kata ya Manolo kuna mradi ambao umesainiwa tangu mwaka 2013, tunavyozungumza hadi sasa Serikali imeshalipa hela zote kwa mkandarasi, lakini jambo dogo la shilingi milioni 82 za VAT Serikali imeshindwa kuondoa na mpaka sasa hivi wananchi wale wanapata shida tangu mwezi wa sita mpaka sasa hivi shilingi milioni 82 imekuwa ni kikwazo cha Wananchi wa Manolo kupata maji safi na salama.

Je, Serikali inatoa kauli gani kwa Wananchi hawa wa Manolo ambao wanaendelea kuteseka kwa kukosa maji safi na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge. Kiukweli Mheshimiwa Shangazi mradi huu umeupigania sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya changamoto ilikuwa ni suala la fedha, mkandarasi alikuwa akidai takribani milioni 600 na sisi kama Wizara ya maji tulitengeneza commitment na tukamlipa ile fedha. Sasa hii changamoto ya VAT nataka nimhakikishe Mheshimiwa Mbunge Serikali haijawahi kushindwa, sisi kama Wizara ya Maji tupo tayari tutakaa na Wizara ya Fedha haraka katika kuhakikisha changamoto hii tunaitatua kwa haraka, ili Wananchi wako waweze kupata huduma ya maji safi na salama, ahsante sana.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafsi hii. Mvua zinazoendelea kunyesha katika Wilaya ya Lushoto zimefanya uharibifu mkubwa sana wa miundo mbinu ya skimu za umwagiliaji, Skimu ya Mng‟alo Kitivo pamoja na skimu kiwani mwezae kwa Mgiriki Kata ya Lunguza nakufanya sasa kilimo cha mpunga kiwe shakani.

Je, serikali ina mpango gani mahususi wa haraka kwenda kuondoa mawe ambayo yamenasa katika kingo za mto umba ambao ndio unapeleka maji katika skimu hizi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Rashid Shangazi Mbunge wa Mlalo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kweli kwamba tumepata taarifa; kwanza kutoka kwa Mheshimiwa Mbunge mwenyewe kwamba alishatuambua, lakini pia kutoka kwa katibu Mkuu wa Chama Chama Mapinduzi, anayesimamia ilani, Dkt. Bashiru Ally. Alifika mwenyewe kwenye skimu hiyo na alitupigia simu kujua namna gani tunakwenda kusimamia utekelezaji wa ilani katika Jimbo hilo la Mlalo huko Lushoto.

Mheshimiwa Spika, Serikali tupo tayari, na nichukue nafasi hii kuwaelekeza Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kanda ya Kilimanjoro, viongozi wa mkoa na wilaya kwenda haraka iwezekanavyo katika skimu hii katika banio la Ng‟alo Kitivo pamoja na Skimu ya Lunguza ili kuangalia mapungufu haya na uharibifu mkubwa wa mawe tuone namna gani tunaweza kuondoa haraka iwezekanavyo. Nami nikuahidi pia baada ya Bunge hili, kwa sababu nilishafika miezi miwili iliyopita, nitarudi tena huko ili kuona namna gani tunaweza kuwaidia watu wa Mlalo.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa nafasi.

Mheshimiwa Spika, tarafa ya Mtae katika Halmashauri ya Lushoto ambayo ina kata tano ndiyo pekee mpaka sasa hivi haijapata kituo cha afya. Je, ni lini Serikali itatimiza ahadi yake ya kujenga kituo cha afya katika Tarafa ya Mtae?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la ndugu yangu Mheshimiwa Rashid Shangazi, Mbunge wa Mlalo, kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo hili amelileta kwa muda na alikuwa na changamoto pale Mnazi na Mtae na ndiyo maana tukaona tuanze katika eneo lingine lakini hii eneo la Mtae lipo katika mpango kazi wetu. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ajenda yetu ipo palepale katika mgao wa fedha tutakaoupata tutahakikisha suala la Mtae linapata kituo cha afya. Kwa hiyo, wala asiwe na hofu, ni jukumu letu kutatua changamoto kwenye maeneo mbalimbali. Kwa hiyo, Mheshimiwa Shangazi wala asihofu suala hilo liko katika mpango wetu wa kazi.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, pamoja na majibu ya Serikali kwanza tunashukuru kwamba, wameweza kutupatia gari la canter kwa ajili ya kubeba mahabusu katika Wilaya ya Uvinza, lakini tunaomba sasa ni lini Serikali itampatia OCD wa Wilaya ya Uvinza gari la kufanyia patrol kwa sababu kwa kipindi kirefu sana hakuna gari la kwa ajili ya kufanya patrol?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Katika Wilaya ya Lushoto ambayo ndio wilaya kongwe ya kipolisi nchini jengo la utawala ambalo anatumia OCD limesimama kwa muda mrefu sasa na jengo hili linajengwa kwa msaada wa fedha za DFID. Je, ni lini jengo hili la Polisi Wilaya ya Lushoto litakamilika?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na gari la OCD, kama ambavyo nimejibu katika swali la msingi Uvinza, lipo gari aina ya Land Cruiser ambayo anatumia OCD kwa sasahivi. Ingawa tukipata gari jingine tutaongeza tunatambua umuhimu wa mahitaji ya gari hasa katika Wilaya ya Uvinza na Mkoa wa Kigoma kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na hoja ya kituo cha Polisi ambacho ujenzi wake umesita kule Lushoto; kimsingi nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kituo hiki ambacho kilikuwa kinajengwa chini ya ule mradi pesa za ufadhili kutoka mradi wa STAKA pamoja na Serikali, ilisita kwa muda, hata hivyo tumeshafanya tathmini na kugundua kwamba, zinahitajika fedha kwa ajili ya kukamilisha kituo hiki na ninadhani takribani kama shilingi milioni 300 si pesa nyingi. Fedha hizi tunatarajia kuzipata kupitia kwenye mfuko wa Tuzo na Tozo, hivyo tutakapokamilisha kupata fedha hizo tutamaliza kituo hiki kiweze kutumika.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu ya Serikali lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa bahati Mheshimiwa Naibu Waziri ameanza kwa kusema kwamba Serikali ya Awamu ya Tano ni mwendelezo wa Serikali zilizopita.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, zao la kahawa linaelekea kupotea kwa kasi kubwa sana na sababu kubwa inalolifanya zao hili hili lipotee ni mabadiliko ya tabianchi. Je, Serikali ina mkakati gani wa kufanya utafiti upya ili kuleta mbegu ambazo zitaendana na hali ya hewa ambayo ipo sasa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mheshimiwa Waziri amesema kwamba mazao haya yalikuwa ni mkakati kwa ajili ya malighafi za viwanda. Sasa nataka aniambie, tulikuwa na kiwanda cha VOIL pale Mwanza, Kiwanda cha Magunia Morogoro, Kiwanda cha Magunia Moshi, tulikuwa na Kiwanda cha Nyuzi Tabora. Hivi viwanda havipo ilhali wananchi wanaendelea kuzalisha: Je, hizi malighafi wananchi wanazozalisha, zinakwenda katika viwanda vipi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE): Mheshimiwa Spika, suala la mabadiliko ya tabianchi ni challenge ambayo inaikabili nchi yetu na dunia kwa ujumla. Wizara ya Kilimo kupita taasisi yake ya TARI sasa hivi tunafanya utafiti wa kuwa na mbegu sitakazokabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Hii imeonekana katika korosho ambapo tumepunguza muda wa mpaka zao la korosho kuja kuzalisha matokeo. Kwa hiyo, tunafanya hivyo hivyo katika mazao yote ya kimkakati na hata mazao ya chakula.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, utafiti huu unaendelea pamoja na soil profiling ili kuweza kujua kwamba eneo hili ambalo tunalima kahawa je, bado litaweza kuhimili zao la kahawa au ama tuweze kuwashauri wananchi jambo lingine? Sasa hivi Wizara kupitia taasisi yake ya TARI inaendelea na utafiti katika vyuo mbalimbali lakini wakati huo huo tunafanya suala la soil profiling.

Mheshimiwa Spika, pamoja na changamoto ya tabianchi, zao la kahawa linakabiliana na changamoto nyingi ikiwepo mfumo wa uzalishaji na mfumo wa uuzaji kupitia ushirika, Wizara inapitia mfumo mzima wa kuanzia uzalishaji mpaka uuzaji wa mazao yote ili kuweza kuleta tija kwa mkulima.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la viwanda ni ukweli usiofichika kwamba Taifa letu limepitia nyakati mbalimbali na viwanda vyetu vingi vimepitwa na teknolojia. Sasa hivi Wizara ya Kilimo na Wizara ya Viwanda na Biashara tunafanya mapping na ku-develop new strategy ili ku-attract investors ili waje kuwekeza katika Sekta ya Viwanda ili waweze ku-take off mazao ya wakulima.

Mheshimiwa Spika, Kiwanda cha Nyuzi Tabora na viwanda alivyovitaja Mheshimiwa Waziri vikiwemo viwanda vya pamba, sasa hivi vingi vimepitwa na teknolojia. Tunaposema tunafufua, sisi kama Wizara ya Kilimo na Wizara ya Viwanda tumekubaliana mkakati wetu siyo suala la kufufua tu ni ku-attract uwekezaji mpya utakaoendana na teknolojia ya sasa ili mazao ya kilimo yaweze kupata tija na kuweze kupata masoko ya uhakika. (Makofi)
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo Naibu Waziri amesema kwamba swali hili liliulizwa kuhusu Tanga wiki iliyopita ningependa kujua Mkoa ambao una halmashauri 11 na tunaposema pamoja na kupeleka maendeleo karibu na wananchi lakini lengo haswa ni kuboresha huduma. Huoni kama ni mzigo kubwa sana kwa mkoa mmoja kuwa na halmashauri nyinigi wakati baadhi ya mikoa halmashuri zake hazizidi nne hadi tano?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri nimewahi kuwa katibu wa vijana wa Chama cha Mapinduzi wa Mkoa wa Tanga, nina zifahamu halmashauri 11 na ukiangalia jiografia kwenda mpaka kule kilindi mpaka Tanga kule Nkinga ni jiografia kubwa. Lakini tunajua kuna mikoa mingine pia ni mikubwa sana ukiangalia kwa mfano Lindi, Ruvuma kule kwa kweli kuna maeneo makubwa sana kiuongozi labda kwa jibu la jumla tu ni kwamba msimamo wa Serikali ni kwamba kwa gharama iliyopo kama ilivyotajwa kwenye REA ujenzi wa miundombinu ya mkoa na wilaya ni kubwa sana ni mabilioni ya fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tulipokee tushauriane ndani ya Serikali tuone kama tunaweza kulifanya kesi by kesi kulingana na ukubwa wa eneo hili tuone kama tunaweza kulifanyika kazi kwa sasa siwezi kuahidi kama tutafanya kesho. Tunaona ile ku-concern ya huduma karibu na wananchi jiografia yetu kubwa mikoa ni mikubwa lakini tulipokee kama maoni ya Wabunge tuendelee kuyafanyia kazi wakati ambapo ikiwa wakati muafaka hili litatekelezwa. Lakini hayo ndio majibu ya Serikali kwa sasa.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa hapa amebainisha wazi kwamba kitambi kinasababishwa zaidi na vyakula vilivyopitiliza hasa vyenye wanga na kwa tamaduni zetu watanzania karibia vyakula vyote tunavyovitumia ni vya wanga. Je, Serikali inatushauri watanzania tule vyakula gani ili kuepukana na vitambi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini la pili, utakuwa ni shahidi kwamba sasa hivi kuna ongezeko kubwa sana la uzito uliopitiliza kwa watoto, vijana lakini hata kwa akinamama na hapa tunapozungumza hivyo vitambi pia hata kina mama wanavyo. Sasa tunataka tuone kwamba Serikali ina mkakati gani mahususi, hapa wamezungumzia habari ya chanjo lakini pamoja na hizo elimu wanazotoa, ni nini kifanyike ili tatizo hili lisiendelee kuathiri haswa malika haya madogo ambayo nimeyataja? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, wanga kwa nini ndiyo unaosababisha na Serikali ina ushauri gani? Kwa ruksa yako naomba niwakumbushe hatua za kibailojia kidogo Waheshimiwa Wabunge, wanga ni mzuri kwa mwili, lakini kazi ya wanga ni kuzalisha nguvu tu, unapoliwa ukapitiliza kwa wale ambao mnakumbuka somo ya biolojia wanga uliozidi unageuzwa kwenda kuwa complex compound inayoitwa glycogen haya ni mafuta. (Makofi)

Mheshimwia Spika, sasa glycogen katika mwili wa binadamu hasa mtu mzima hauna kazi nyingine yoyote isipokuwa ni kuhifadhiwa, na huu hii glycogen ambayo kiasili ni protini inahifadhiwa katika maeneo mbalimbali ya mwili wa binadamu ikiwa ni pamoja na mishipa ya kupitisha damu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana tunasema pamoja na appetite ambayo inaweza kukufanya ule ugali mwingi sana, lakini ni vizuri ukala kiasi kile ambacho kitakwenda kuzalisha energy kwa maana ya nguvu ya kuusukuma ule mwili wenyewe, unapokula ziada ndiyo huleta matatizo.

Sasa sisi ushauri wetu kama Serikali nini, kwanza ni kula ulaji ambao unazingatia mlo wenye tunaita mlo bora na hasa protini na katika upande wa protini pamoja na ubora wote wa protini za nyama, lakini protini iliyo bora zaidi ni ile protini inayotokana na mimea. Ushauri wetu Waheshimiwa Wabunge mle zaidi protini na hasa protini zinazotokana na mimea.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili Mheshimiwa Mbunge Rashid Shangazi anauliza nini kifanyike ili hili rika ambalo linaonekana linaathirika zaidi kama vile vijana na hata wakinamama amewataja. Sisi Serikali tunashauri, kwa kawaida kisayansi inakubalika kwa watu wazima kuwa ndiyo waathirika zaidi wa upatikanaji wa vitambi, wanapopata vijana ni jambo lisilokuwa la kawaida. Sasa vijana wanachoshauriwa ni kubadilisha lifestyle namna ya uendaji katika maisha, ulaji wa chipsi uliopitiliza, na unywaji wa pombe uliopitiliza haya ndiyo yanayopelekea matatizo haya…

SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Naibu Waziri.

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, lakini na ufanyaji wa mazoei pia, ninashukuru.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante nashukuru sana kwa nafasi.

Mheshimiwa Spika, napenda kumuuliza Mheshimiwa Waziri kwa kuwa, kule Lushoto sisi tayari tumeshajiandaa na tuko tayari tunavuna matunda mengi sana, lakini masoko yake kwa kweli sio mazuri kiasi kwamba yanashawishi vijana kuachana na kilimo cha matunda na kwenda mjini.

Je, Serikali ina mkakati gani kusaidia kutupatia masoko ya uhakika wakulima wa matunda kule Lushoto?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA: Mheshimiwa Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa namba ambavyo anawapigania vijana katika eneo lake na niseme tu kwamba katika majibu yangu ya awali niliyoyasema eneo mojawapo ambalo pia tutalifikia ni eneo la Lushoto lenye matunda mengi sana na tayari tumeshaanza mazungumzo na mwekezaji mkubwa kabisa Ndugu Bakhresa kwa ajili pia ya kuona namna ambavyo tunaweza tukasaidiana naye tukapata mahitaji ya matunda ambayo anayahitaji kule kiwandani, ili vijana wa Lushoto kupitia utaratibu ambao tumeuweka tuwawezeshe waweze kulima na baadae soko liwe ni kupitia Ndugu Bakhresa na kampuni nyingine za vinywaji hapa nchini.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali lakini nina maswali madogo mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, Mheshimiwa Waziri, hivi karibuni alikuja Lushoto ambako kulikuwa na tatizo la upangaji wa ardhi katika Mji Mdogo wa Mnazi ambapo pesa ambazo zimetumika vibaya nje ya utaratibu na ulitoa maagizo. Sasa nataka kujua ni kwa kiasi gani jambo lile Ofisi ya Rais, TAMISEMI imelishughulikia?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mji Mdogo wa Lushoto umeshatangazwa takribani miaka tisa, lakini mpaka sasa mamlaka ile bado haijaanza kazi, bado inapatikana ndani ya Halmashauri ya Lushoto. Sasa je, ni lini sasa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Lushoto itaanza kufanya kazi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, asante. Naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Shangazi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli nilifanya ziara katika Wilaya ya Lushoto, Mkoa wa Tanga na nikakuta kuna matumizi mabaya ya fedha shilingi zaidi ya milioni 300. Nikatoa maelekezo kwa Mkuu wa Wilaya, namshukuru uchunguzi umeshafanyika, tumeshapokea taarifa ile watu wote waliohusika namhakikishia Mheshimiwa Mbunge watashughulikiwa kwa mujibu wa tararibu za kisheria, tunalifanyia kazi jambo hilo, naomba tupeane muda, tuvute subira kidogo.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mheshimiwa Mbunge anaulizia habari ya Mji Mdogo ambao ulitangazwa na haujawa mamlaka kamili. Nimejibu maswali haya mara kadhaa, nirudie tu kusema kwamba kama jambo hili haliongezi gharama za kuendesha Serikali, tumeelekeza na ni msimamo wa Serikali kwamba kwa sasa tujielekeze kuboresha maeneo na kukamilisha maeneo ambayo yalishaanzishwa kabla ya kuanzisha maeneo mengine ya mji.

Mheshimiwa Spika, sasa kama hili linaongeza gharama, kuongeza watumishi, majengo ya Serikali na bajeti kuongezeka, kwa kweli Serikali haitakuwa tayari kufanya kazi hiyo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hayo ndiyo majibu ya Serikali na Mheshimiwa Mbunge aendelee kutoa ushirikiano. Kadri tutakavyopata fedha ya kutosha, yale maeneo ambayo yameshaanzishwa yakaimarishwa vizuri kwa kupeleka huduma muhimu, vifaa, watendaji wa kutosha, basi maeneo mengine mapya yataanzishwa ili kupeleka huduma karibu na wananchi wetu. Ahsante.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri na Serikali wamekiri kwamba takriban skimu 70 zina changamoto na kule Mng’aro hivi tunavyozungumza ni msimu wa mpunga lakini wanashindwa kwenda mashambani kwa kuwa skimu haiwezi ikaririsha maji kuelekea mashambani. Je, Serikali ina mpango gani wa haraka sana kuhakikisha kwamba skimu hii ya Mng’aro inatiririsha maji kuelekea mashambani?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kulikuwa na maelekezo ya Mheshimiwa Katibu Mkuu wa Chama alipotembelea Mkoa wa Tanga kwa maana kwamba Wizara ya Kilimo itembelee ikaone skimu hizi. Kwa sababu kuamini ni kuona, je, Waziri yuko tayari sasa kutenga muda na nafasi kwenda kuziona skimu hizi ambazo ni muhimu sana kwa uzalishaji wa mpunga katika Mkoa wa Tanga?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya ngonyeza ya Mheshimiwa Rashid Shangazi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la Wizara ya Kilimo kwenda Mlalo, hivi karibuni tulikuwa Mkoa wa Tanga na Mheshimwia Waziri Mkuu lakini bahati mbaya hatukuweza kufika Jimbo la Mlalo. Nakata nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa mimi mwenyewe niko tayari tukutane tupange ili tuweze kwenda pamoja katika maeneo ya Mlalo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusu suala la kukarabati skimu hizi tatu tulizozitaja, kwanza practically sasa hivi ni kipindi cha mvua kwa hiyo ukarabati itakuwa ni vigumu sana kuufanya. Nataka nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tumetenga fedha kupitia Tume ya Umwagiliaji kiasi cha shilingi milioni 30 kwa ajili ya kurekebisha skimu za Mlalo.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada tu ya msimu huu wa mvua kuisha Wizara ya Kilimo tutatumia mfumo ambao tumeutumia kama majaribio maeneo ya Ruaha na Jimbo la Mheshimiwa Lukuvi kwa kutumia force account kufanya marekebisho ya skimu hizi na wala hatutotumia wakandarasi, tutatumia vifaa vyetu wenyewe. Tutaenda kufanya hivyo immediately baada ya msimu wa mvua kuisha na tumetenga fedha kwa ajili ya skimu zake tatu.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Lushoto ina uhaba mkubwa sana wa watumishi katika sekta ya elimu na afya. Katika sekta ya elimu, msingi peke yake ambapo tuna shule 168, tuna uhaba wa watumishi 1,274. Tuna vituo 63 vya kutoa huduma za afya lakini tuna uhaba wa watumishi 1,218. Ni lini Wizara hii itaiangalia Halmashauri ya Lushoto kwa jicho la huruma na kutuondoa katika kadhia hii ambayo wananchi wanaendelea kupata?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shangazi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kuajiri walimu kadri bajeti itakavyoruhusu. Katika bajeti ya mwaka 2021, Serikali ilitenga bajeti ya ajira 9,500 kwa walimu na watumishi katika kada ya afya 10,467. Hivyo basi, pale Serikali itakapoanza kuajiri hawa, tutaangalia pia na Mlalo kule ili aweze kupata watumishi hawa. Ahsante. (Makofi)
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, asante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Swali la kwanza; barabara hii ni muhimu sana kwa shughuli za uchumi wa wananchi wa Lushoto, hasa ukizingatia kwamba, mazao tunayozalisha kule ni mbogamboga na matunda ambayo ni rahisi kuharibika. Kulikuwa na ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba, angalau sasa barabara hii ijengwe japo kwa kiwango cha kilometa 10 kwa mwaka. Je, tunapoelekea kutengeneza bajeti Serikali haioni ni muhimu kutenga kiwango hicho cha kilometa 10 kwa kila mwaka?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa barabara hii imeendelea kutia hasara wananchi wa Mlalo, hasa nyakati za mvua. Je, Serikali sasa iko tayari kuwalipa fidia mara ambapo wananchi wanapata hasara ya mazao yao kuoza barabarani?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Shangazi, Mbunge wa Mlalo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa barabara hii ambako kunazalishwa sana matunda na mbogamboga. Kwa kutambua umuhimu huo ndio maana Serikali tayari imeshakuwa na mpango wa kujenga hii barabara. Tunatambua pia kwamba, Serikali ilitoa ahadi kwamba, itaendela kujenga hii barabara walao kwa kilometa 10.

Mheshimiwa Naibu Spika, ameuliza kama kwenye bajeti ijayo je, tutajenga. Itategemea pia na upatikanaji wa fedha na kama itapatikana si tu kilometa 10 bali inawezekana ikawa ni kukamilisha kabisa barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; endapo kama tutatoa fidia kwa wale wanaopata matatizo hasa pale ambapo mazao yao yanaharibika. Tumeshaongea na Meneja wa TANROADS Mkoa wa Tanga, ili badala ya kuendelea kutengeneza kile kipande wanachokiendeleza, basi atengeneze yale maeneo ambayo ni korofi, ili yaweze kuimarika na kusitokee tatizo kama hilo. Kama kuna changamoto nyingine basi namwomba Mheshimiwa Shangazi, Mbunge wa Mlalo, anipatie. Nimwahidi Mheshimiwa kwamba, nitafika kuona hizo changamoto ambazo anazisema. Ahsante. (Makofi)
MHE. RASHIDA A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Matatizo ya usambazaji wa umeme vijijini yaliyopo Handeni ni sawa kabisa na yaliyopo kule Lushoto katika Jimbo la Mlalo. Hivi ninavyozungumza tunapoelekea kwenye robo ya tatu ya mwaka wa fedha ambao unakaribia kwisha hakuna hata kijiji kimoja ambacho REA wamesambaza umeme. Sasa tunataka kujua, wananchi wa Lushoto hususan Jimbo la Mlalo wameikosea nini hii Serikali hii ya Awamu ya Tano?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shangazi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Soika, kama nilivyotangulia kujibu kwenye swali la msingi. Maendeleo ni hatua, na tulianza na vijiji vichache na tunazidi kuongeza, na katika awamu ya tatu mzunguko wa pili wa REA vijiji vyote ambavyo vilikuwa havijapata umeme vitapatiwa umeme.

Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Shangazi kwamba kabla ya mwaka 2022 Disemba vijiji vyote vya kwenye Jimbo lake la Lushoto viitakuwa vimepatiwa umeme kama nilivyotoa majibu kwenye swali la msingi.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Skimu ya Pawaga, Ruaha Mbuyuni na Mlalo kule Lushoto tuliahidiwa kwamba zingetengewa fedha baada ya kuharibiwa na mafuriko makubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, mpaka sasa ninavyozungumza wenzetu wa Pawaga na Ruaha Mbuyuni wameshapewa fedha lakini sisi milioni 30 ambazo zimeahidiwa na Tume ya Umwagiliaji mpaka sasa hazijafika katika Halmashauri ya Lushoto kwa ajili ya Skimu ya Mlalo. Je, Serikali inatoa commitment gani kwa pesa hizi kwenda katika Skimu hii ya Mlalo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shangazi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Skimu za Mnaro, Pawaga na Ruaha zilikuwa zimeathirika kwa kiwango kikubwa na mvua za mwaka jana na mvua zilizoendelea mwaka huu. Kama Wizara tuliamua kwamba badala ya kupeleka fedha tutumie equipment tulizonazo wenyewe za Tume ya Umwagiliaji na kutupunguzia gharama.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba Skimu za Pawaga na Ruaha zimeshafanyiwa kazi, Skimu inayofuatia kupeleka vifaa ni ya Mlalo ambayo anatoka Mheshimiwa Shangazi na naamini kwamba kabla ya msimu ujao wa mvua tutakuwa tumeshairekebisha na tutatumia vifaa vyetu na Tume watapeleka vifaa wenye kwenda kufanya hiyo kazi badala ya kupeleka fedha. Kwa sababu tukitumia force account tutatumia nusu ya bajeti iliyokuwa imeletwa na halmshari yake.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri ya Serikali ambayo kwa kweli yanatia Faraja, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ukurasa wa 150 Ibara ya 100 imeweka bayana kwamba, tunataka tupeleke maji vijijini kwa asilimia 85 lakini mijini kwa asilimia 95. Na kinachoonekana hapa kinakosekana ni elimu kwa wananchi, je. Wizara iko tayari sasa kuja na mpango Madhubuti wa kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi ili wawe na utaratibu huu mzuri wa kuvuna maji? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa, maji yanapotiririka yanaharibu miundombinu kwa kiasi kikubwa na mara nyingi ni miundombinu ya barabara, reli lakini pia wakati mwingine na mabwawa na scheme za umwagiliaji. Na kwa mfano, katika eneo la Kongwa mara kadhaa tumeona kwamba, barabara inasombwa na maji lakini pia, kule katika Mto Mkondoa eneo la Kilosa, reli mara kadhaa inasombwa na maji. Sasa kwa nini Serikali isije na mkakati mahsusi wa kuhakikisha kwamba, tunakuwa si tu, na mabwawa machache lakini tutafute mabwawa mengi nchi nzima ambayo yatakuwa yanazuia maji ambapo maji haya yatatumika kwa matumizi ya kunywa lakini pia, kwa ajili ya matumizi ya kilimo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Ilani inatutaka kufika mwaka 2025 vijijini kote maji yawe yamefika kwa asilimia 85 na maeneo ya Miji kwa asilimia 95. Wizara inaendelea kutekeleza Ilani kwa ufasaha sana na maelekezo ya Mheshimiwa Waziri wetu wa Maji ni kwamba, maji haya ya mvua kwetu sisi tunayachukulia kuwa ni fursa na sio laana. Hivyo, nipende kumwambia Mheshimiwa Shangazi kwa umahiri alionao, Wabunge wote humu ndani tunafahamu umahiri wa Mheshimiwa Shangazi vile ni Mwenyekiti wa Simba Sports Club humu Bungeni. Lakini vile vile, ni Katibu wetu sisi Wabunge tunaotokana na Chama Cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninafahamu tutaendelea kushirikiana lakini Wizara tutaendelea kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi namna bora ya uvunaji wa maji katika makazi yetu na kama Wizara ya Maji, tutaendelea kushirikiana na Wizara ya TAMISEMI, ili tuweze kuunganisha nguvu ya pamoja kuona wananchi tunawapa elimu, namna bora ya kufanya design, namna pale wanapojenga makazi yao. Kwasababu, mvua hizi tukiweza kufanya ni zoezi la shirikishi, maji yatakuwa ni mengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, na hata kwenye mashule yetu kama nilivyojibu kwenye jibu langu la msingi tutahakikisha na wao tunaendelea kutoa elimu kwa wakuu wa shule, ili kuona hata kwenye mashule yetu, watoto wasiendelee kuteseka. Maji hayana sababu ya kwenda kuharibu miundombinu mingine ambayo tunahitaji katika maisha yetu ya kila siku na maji haya tuweze kwenda kuyatumia vyema. Lakini vile vile, tutaendelea kuona namna bora ya kupata matenki ya bei nafuu kwa maeneo ya vijijini, ili ikiwezekana basi maji haya yaweze yakavuliwa kwa ushiriki wa pamoja na isije ikapelekea tena kuwa ni gharama kwa mwananchi mmoja mmoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, na katika swali lake la pili, kama Wizara nipende tu kusema nimepokea ushauri huu tutaendelea kuufanyia kazi Mheshimiwa Shangazi tutaonana, ili tuweze kuendelea kushauriana vema na Wizara tutakwenda kutekeleza vema. (Makofi)
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali ambayo yanaonesha mwanga wa kupambana na rushwa katika michezo, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, je, ni hatua gani zimechukuliwa kwa watu ambao wamebainika kujihusisha na vitendo vya rushwa katika michezo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, ni mkakati gani Serikali itatumia kuboresha mifumo ya uuzaji tiketi na kukusanya mapato, lakini pia kuziba mianya ili kuongeza mapato zaidi katika sekta hii ya michezo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, Serikali imechukua hatua mbalimbali katika kuhakikisha kudhibiti mianya ya rushwa katika soka nchini, lakini vilevile imekuwa ikichukulia hatua watuhumiwa waliokutwa na hatia katika kujishughulisha na masuala ya rushwa. Ikumbukwe kwamba mwaka 2017 kuna watuhumiwa ambao walifikishwa mahakamani na kukutwa na hatia na hatimaye kulipishwa faini.

Mheshimiwa Spika, vilevile, mwaka 2018 kuna kesi moja ambayo ilikuwa ni maarufu sana hapa nchini, ambapo kuna mtuhumiwa alikutwa na hatia ya kula shilingi milioni 90 za Chama cha Mpira wa Miguu nchini TFF na yeye vilevile, alifunguliwa mashitaka ikiwemo ya uhujumu uchumi, lakini na baadaye kuweza kulipa fedha hizo kuzirudisha katika TFF. Kwa hiyo, tutaendelea kushughulika na watuhumiwa wa aina hii.

Mheshimiwa Spika, nikijibu swali la pili la Mheshimiwa Shangazi, ili kuziba mianya sote tunafahamu kwamba sasa tunaenda kwenye ulimwengu wa teknolojia, hivyo basi, niwaase wenzetu wa TFF na timu za mipira za miguu kwamba sasa waende katika kuachana na tiketi zile za vitini vya kuchana na waweze kwenda kwenye electronic ticket, hii itasaidia sana upungufu na upotevu wa mapato, itaongeza mapato kwa timu zao, lakini vilevile kwa TFF.

Mheshimiwa Spika, vilevile niwaagize kwasababu e-government (eGA) ipo chini ya Ofisi yetu niwaagize hapa mbele ya Bunge lako Tukufu washirikiane na wenzetu wa TFF ili kuweka mfumo bora wa kukata tiketi za kuingia katika michezo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kusema katika hii trend tulioiona mwaka 2019 ya mwezi Januari kupata shilingi milioni 122 na mwezi Machi, mechi zote hizi zilikuwa ni za timu ya mpira ya Simba; kwa hiyo, kumeonekana kukiwa na timu ya Simba inacheza uwanja unajaa sana, lakini bado mapato yanakuwa hafifu, ukilinganisha na timu nyingine ambayo ni kubwa Afrika Mashariki na Kati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, pamoja na majibu ya Serikali, lakini ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; kwa kuwa sasa Serikali ipo katika mchakato wa ajira hizi mpya ambazo amezitaja 6,979 hivi na sisi upungufu wetu ni walimu 1,270.

Je, haoni sasa kuna umuhimu angalau Halmashauri kama ya Lushoto ikapewa kipaumbele angalau kwa kusogeza hata kupata walimu japo 200?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa wapo walimu ambao asili yao ni Lushoto na Tanga kwa ujumla na wapo katika maeneo mbalimbali ya nchi hii na hawa wapo tayari kurudi Lushoto kuungana na wananchi wa Lushoto katika kutoa huduma hii ya elimu lakini changamoto za uhamisho ndio zinazowakwamisha.

Je, Serikali iko tayari kushirikiana na mimi kuwabaini wale wote ambao wapo tayari kurudi Lushoto ili kwenda kusaidia jukumu hili na kuondoa huu uhaba mkubwa wa walimu katika Halmashauri yetu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS . TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi, Mbunge wa Mlalo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi ni kweli kwamba katika Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, lakini pia katika Jimbo la Mlalo kuna upungufu wa watumishi kwa maana ya walimu na Serikali kama ambavyo nimejibu katika jibu langu la msingi imeendelea kuwaajiri kwa awamu walimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto. Naomba nimhakikishie kwamba katika ajira hizi 6,900 ambazo zinakwenda kutolewa hivi sasa ambapo tayari taratibu za kuwa-shortlist na kuwapata walimu hao zinaendelea, tutakwenda kuhakikisha tunampa kipaumbele cha hali ya juu sana Mheshimiwa Shangazi na Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto kwa ujumla wake. Kimsingi namhakikishia kwamba tutaendelea kulifanyia kazi kwa karibu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili; walimu wenye asili ya Lushoto ambao wanapenda kurudi kufanya kazi katika Halmashauri hiyo, utaratibu wa Serikali uko wazi na walimu na watumishi wote kote nchini wanaruhusiwa kufanya kazi sehemu yoyote, lakini wale ambao wana sababu za msingi za kuomba kurudi katika Halmashauri yoyote ile ikiwemo Lushoto bila kujali wanatokea ama hawatokei Lushoto wanaruhusiwa kufuata taratibu za Serikali za kuomba uhamisho na sisi kama Serikali tuna vigezo ambavyo tutavitazama na kuona walimu wale wanapata vibali vya kuhama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie kwamba kama wapo wanaohitaji tunawakaribisha, lakini kwa kufuata vigezo na taratibu zile za Serikali, nakushukuru. (Makofi)
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa maji katika Kata ya Mnazi, Tarafa ya Umba ni takribani miezi miwili sasa RUWASA wamepeleka saruji na mipira ile midogo, lakini mpaka sasa tunasubiri mabomba. Ni lini mabomba haya yatapelekwa ili maji katika Mji wa Mnazi na viunga vyake yaweze kupatikana kwa urahisi? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Shangazi, kaka yangu ambaye anafanya kazi kubwa sana katika Jimbo lile la Mlalo.

Mheshimiwa NaibU Spika, nataka nimhakikishie maji hayana mbadala na sisi kama Wizara ya Maji umuhimu wetu na jukumu letu ni kuhakikisha tunalinda uhai wa wana Mlalo na wana Mnazi. Natoa maelekezo kwa Mhandisi wa Maji wa pale Lushoto kuhakikisha mpaka Jumatatu mabomba yamefika na kazi ianze mara moja. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu ambayo siyo ya matumaini sana kwa wananchi wa Tarafa ya Umba, hasa Kata ya Mnazi na Lunguza, tunayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; kwa kuwa shughuli za wananchi hawa wanaozungukwa na hifadhi ya Taifa Mkomazi sehemu yao kubwa ni ufugaji na eneo lao ni dogo, lakini uanzishwaji wa hifadhi haujawatendea haki kwa sababu hakuna mlango hata mmoja wa kuingilia hifadhini kutokea upande huu wa Lushoto.

Je, ni lini sasa Serikali itatekeleza ahadi yake ya kujenga geti la kuingia Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi katika eneo la Kamakota, Kijiji cha Kivingo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa ukaribu huu wa Hifadhi na makazi ya watu unasababisha mara kwa mara wanyama waharibifu, hasa tembo, kuvamia mashamba katika Vijiji vya Mkundo- Mbaru, Mkundi-Mtae, kiasi kwamba zaidi ya ekari 3,000 za matikiti maji na mkonge zimeharibiwa vibaya na tembo.

Je, Waziri yuko tayari sasa kuwatembelea wananchi wale ili angalau akawaone na kuweza kuwafariji?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Rashid Shangazi, Mbunge wa Mlalo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Shangazi kwa kuendelea kuhamasisha utalii, hasa katika maeneo ya Jimbo lake la Mlalo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivyo kwa sababu Wilaya ya Lushoto ni eneo moja wapo ambalo linasaidia sana kuongeza mapato ya Serikali, hasa kisekta, na Mheshimiwa Shangazi amekuwa mara nyingi akitutembelea katika ofisi zetu kuelezea changamoto za maeneo hayo. Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba Serikali inatambua mchango wkae, lakini pia tuko bega kwa bega kuhakikisha kwamba utalii unasonga mbele, ikiwemo eneo hili la Mlalo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo ameomba kuhusu kuweka geti katika eneo la Kamakota, nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba katika bajeti hii ambayo mmetupitishia, geti hili litafunguliwa ili kurahisisha watalii wanaoelekea maeneo ya Lushoto, hususan Mlalo, basi iwe rahisi sana kupita katika eneo hili la Kamakota.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, utalii tutaufungua katika eneo hilo na tuna uhakika kwamba tutaweza kupata mapato mengi yanayotokana na Hifadhi yetu hii ya Mkomazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ameuliza kama Waziri yuko tayari; nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba nitafika Mlalo, kama siyo basi atakuwa ni Waziri, kuongea na wananchi na kuendelea kuwapa pole hata wananchi wengine wenye maeneo ambayo wanakutana na changamoto hizi za wanyama wakali na waharibifu kama tembo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu haya ya Serikali ambayo kwa kweli yanaonyesha bado tuko nyuma sana, maana kati ya 140,000 kwa Afrika sisi tuna 5,000 sawa na asilimia 4.2: Sasa ni upi mkakati wa Serikali katika kuhuisha sera na sheria ambazo wakati mwingine ndiyo zinazokuwa kikwako katika ukuaji wa mitaji wa kibiashara na uwekezaji?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili: Mheshimiwa Waziri ametaja sekta mbalimbali ambazo mabilionea hawa aliowataja wanatoka, lakini kwa masikitiko makubwa hakuna hata mmoja anayetokana na Sekta ya Kilimo na Mifugo na Uvuvi. Haoni kwamba kwa stahili hiyo wakulima, wafugaji na wavuvi wataendelea kuwa wasindikizaji katika eneo zima hili la kiuwekezaji wa mitaji? (Makofi)
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Shangazi kwa swali lake nzuri. Nampongeza kwa jana niliambiwa alikuwa anashabikia moja ya timu iliyoshinda kwa mbinde sana. Taarifa alizonipa Mkuchika anasema, basi timu yake isingeshinda, mpaka sasa mpira ule ungekuwa bado unaendelea kuchezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mabilionea hawa tuliotaja, tumewataja tu kwa mfano. Tumetoa tu mifano ya baadhi ya sekta ambazo tumeweza kuziainisha, lakini haina maana kwamba kwenye Sekta ya Kilimo na Mifugo hakuna mabilionea. Hata Sekta ya Mifugo na Sekta ya Kilimo wapo mabilionea na takribani kila mkoa kwenye sekta hiyo ya kilimo mabilionea wapo kuanzia ngazi zote; kuanzia kwenye kulima kwenyewe wapo ambao wako ngazi ya processing ambazo ziko ngazi ya viwanda, lakini wapo pia wa ngazi ya export. Kwa hiyo, hii tulitolea tu mifano ya baadhi ya maeneo ambayo yapo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sekta nyingine zipo ambazo hatujazitaja kwa kiwango kikubwa na zenyewe zina mabilionea ambao wako. Kwa mfano, King Musukuma pamoja na wengine ambao na wenyewe wapo katika makundi yale.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la kwamba tuna sera gani? Serikali ina sera na moja ya maeneo ambayo tumeyapa uzito mkubwa ni kutengeneza mazingira bora kabisa ya ufanyaji biashara ambapo tunahamisha watu kutoka kundi moja la kipato kwenda kipato kingine na mkakati huo unaanza na biashara kuanzia zile zilizo ndogo kwenda biashara zilizo kubwa na zilizo kubwa kwenda kwenye ngazi ya mabilionea ili Tanzania iweze kuwa na mabilionea wengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo tamko lilitolewa siku siyo nyingi sana, hata Wabunge wanakaribishwa waungane na King Musukuma kwenye kundi lile la mabilionea ili waendelee kuongozwa kwa mfano kwa wananchi hao wanaowaongoza. (Kicheko/Makofi)
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami pamoja na majibu mazuri kabisa ya Daktari msomi, mwanasayansi Mheshimiwa Mollel, nina swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huko nyuma tulikuwa tunaona Serikali ikishiriki katika kampeni mbalimbali tunapokuwa na magonjwa haya ya mlipuko na magonjwa mengine. Kwa mfano tuliwahi kuwa na kampeni ya kutokomeza Malaria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kufahamu, ni upi mpango wa Serikali kutumia wasanii wetu katika kuhamasisha, lakini pia kutoa elimu zaidi kwa wananchi hasa makundi ya vijana katika kupambana na Ugonjwa huu wa Uviko-19? Kwa sababu tunaona katika awamu hii kama wasanii hawajatumika sana katika eneo hili? Ni upi mpango wa Serikali?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la Mheshimiwa Mbunge ni muhimu sana; na kweli kwa kutumia wasanii wanaweza wakatufikishia vizuri sana ujumbe, lakini kikubwa ambacho kinaendelea sasa hivi ni kuhakikisha kwamba badala ya kutumia wasanii kutoka juu, tunapeleka kabisa huduma iende ikafanyike na jamii yenyewe kule chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, imeonekana kwamba, ukiangalia fedha tulizonazo, ukitumia sana wasanii hawa wakubwa, ambao bado tunaendelea kuwatumia na tutawatumia jinsi watakapohitajika, lakini kwa kupeleka kule chini huduma inafika kwa urahisi zaidi kwa lugha inayoeleweka na watu wa jamii iliyoko eneo husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana tumesema tutakwenda kule na tukifika kule Umasaini tutawatumia wasanii walioko kule, lakini tutatumia redio na lugha zilizoko kule ili waweze kupata kirahisi na ili ujumbe ufike. Ila hatuna lengo la kuwaacha wasanii, isipokuwa tunatafuta namna ya kutumia hela kidogo kwa kufanya kazi kubwa zaidi. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Katika skimu ya Mng’aro ambayo Mheshimiwa Waziri mara kadhaa hapa alikuwa anaitolea maelezo; na nimeiuliza lakini bado mpaka sasa fedha zile ambazo mmezitenga shilingi milioni 30 hazijafika kuboresha banio na sasa tunaelekea kuanza kwa msimu wa kilimo: -

Je, ni nini commitment ya Serikali katika jambo hili?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shangazi. Kwanza nimpongeze sana yeye binafsi pamoja na Diwani wake Ndugu Jambia Juma Shehoza kwa kuifuatilia Skimu ya Mnga’ro.

Nataka tu nimwambie kwamba tumeshatangaza tender na tarehe 18 Novemba, 2021 tender hiyo inafunguliwa ili kupatikana Mkandarasi wa kuweza kwenda kuifanya kazi na kurekebisha tatizo la skimu hiyo. (Makofi)
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Wilaya ya Lushoto ina tarafa 8 lakini tuna vituo 5 tu vya Polisi, lakini katika Kata ya Lukozi na Lunguza ambazo ni miji midogo na hii Lunguza ipo karibu kabisa na mpaka wa nchi jirani ya Kenya, wananchi wale wametenda maeneo na wanataka kulikabizi Jeshi la Polisi ili kwa kushirikiana nao tuweze kujenga vituo vya Polisi. Je, Waziri yuko tayari kumuagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga aje akabaini yale amaeneo na shughuli za ujenzi zianze? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rashidi Shangazi Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya miongoni mwa azma kubwa ya Serikali ni kuhakikisha kwamba wananchi wanaishi kwa amani na utulivu katika maeneo yao hasa baada ya kupata ushirikiano kutoka kwa Jeshi la Polisi na vyombo vyengine vya ulinzi na usalama, na zaidi pale wananchi wanapoamua kwamba wao wenyewe wameshajitolea wako tayari kujenga kituo cha Polisi, sisi kama Serikali kama Wizara kama Jeshi la Polisi tupo tayari kutoa ushirikiano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nichukue fursa hii kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi nimuagize RPC Mkoa wa Tanga kwa kushirikiana na OCDs wake na baadhi ya mastafu wake, wahakikishe kwamba wanakwenda kutoa ushirikiano kwa wananchi ili lengo namadhumuni kituo hiki cha Polisi kijengwe ili wananchi waweze kupata huduma ya ulinzi na usalama. Nakushukuru.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. pamoja na majibu ya Serikali, na kwa kuwa amekiri kwamba Muswada huu umeshasomwa kwa mara ya kwanza Bungeni, ni commitment gani anatoa kwa maana Muswada huu uweze kuja kwa mara ya pili, hatimaye mara ya tatu ili hii sheria iweze kuboreshwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973 ilikuwa haitambui usafiri wa pikipiki, almaarufu kama bodaboda, kama ni chombo rasmi cha kusafirisha abiria na chombo hiki sasa hivi kinatumika kwa Watanzania walio wengi nchini. Kama sheria hii itaendelea kuchukua muda, Serikali haioni umuhimu wa kuleta kwa hati ya dharura hata katika sheria ya mabadiliko mbalimbali ili jambo hili liweze kuwa katika sheria zetu za nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi, Mbunge wa Mlalo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu commitment ya Serikali, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika vikao vijavyo ambavyo tutaruhusu marekebisho ya sheria tutaangalia uwezekano wa kuileta sheria hiyo ili iweze kupitishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hili suala la usafiri wa pikipiki, hili ni pamoja na mambo mengine ambayo yalijitokeza na hususan maoni ya Kamati ya NUU, yalibaini kwamba pana mambo mengine ya kuhitaji kuzingatiwa ukiwemo usafiri wa pikipiki. Kwa hiyo ni ahadi yetu kwamba muswada huo utakapoletwa humu utakuwa pia umezigatia masuala ya usafiri wa bodaboda. Ahsante. (Makofi)
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi hii.

Mheshimiwa Spika, kiwanda kinachotajwa hapo malighafi yake inatoka katika Shamba la Misitu Shume ambayo ipo Lushoto na ninavyo fahamu mimi kiwanda hiki kwa sasa Msajili wa Hazina amekikodisha kwa mwekezaji mdogo wa pale Korogwe.

Je, kwa nini wasiboreshe mkataba ulipo sana na mwekezaji huyu mdogo ili angalau kuweza kuwasaidia wananchi wa Korogwe na Lushoto kwa ujumla?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika nakushukuru sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Rashid Shangazi, Mbunge wa Mlalo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali wakati inaangalia namna ya kuweza kukifufua kiwanda hiki ilikodisha kwa mwekezaji anayezalisha nguzo ambazo kama anavyosema Mheshimiwa Mbunge zinatoka Lushoto.

Kwanza nia ni kuona kile kiwanda hakiharibiki kwa maana miundombinu ile iweze kuendelea kuwa bora. Lakini kama nilivyosema kwa sababu bado hatujamaliza mchakato wa kukirudisha rasmi Serikalini kwa hiyo hatuwezi kumpa mwekezaji mwingine mpaka tukamilishe taratibu za kisheria ili tusiwe na migogoro mingine na wawekezaji ambao wataingia katika kiwanda hivho. Nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu ya Serikali, nina maswali madogo mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza; kwa kuwa kwa mujibu wa Sheria hii ya PPP kwa maana ya Sheria Sura namba 210, kiwango cha mtaji kwa wazawa ni dola milioni 20. Je, Serikali haioni kwamba kiwango hiki ni sehemu ya kikwazo cha utekelezaji wa sheria hii?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Serikali ina mpango gani wa kupunguza masharti ya kimkataba katika miradi hii inayoibuliwa na sekta binafsi ili iweze kutekelezwa kwa ufanisi kupitia PPP? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Sheria ya PPP ipo katika mchakato wa kufanyiwa marekebisho na sasa ipo ngazi ya kukusanya maoni kutoka kwa wadau. Kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Mbunge awe na subira mpaka mchakato huo utakapokamilika bila shaka hiki hakitokuwa kikwazo kwa utekelezaji wa sheria hiyo.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, masharti hayo ambayo yapo pia ni kwa mujibu wa sheria na taratibu, kwa hiyo pia nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge masharti hayo huenda yakapungua baada ya kupata mapendekezo kutoka kwa wataalam wetu ambao wanakusanya maoni hayo. Ahsante.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Barabara ya kutoka Mlalo kwenye Ngwelo, Mlola, Mashewa hadi Korogwe inaunganisha wilaya mbili; na barabara hii iko chini ya wakala wa barabara vijijini kwa maana ya TARURA na imeshaanza kujengwa kwa kiwango cha lami kwa kilomita 2.7: Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuipandisha hadhi hii barabara na kuwa ya mkoa?
NAIBU WAZIRI WA TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Rashid Shangazi, Mbunge wa Mlalo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua kazi nzuri ambayo inafanyika katika Jimbo la Mlalo, hususan hii barabara ya Mlalo – Nachiwa mpaka Korogwe na ndio maana sisi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, tulitenga fedha kwa ajili ya kuanza sasa kutekeleza kwa ujenzi wa lami. Sasa kwa kuwa, maombi yao ni kupandisha hadhi, nafikiri tutaiagiza Halmashauri ya Mlalo ifuate taratibu kama ambavyo tumeiagiza Halmashauri ya Tunduru, ili barabara hiyo nayo iweze kufikia hivi viwango ambavyo Mheshimiwa Mbunge anahitaji. Ahsante sana.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri na bora kabisa ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa sisi tayari tunalo eneo letu la kibiashara: Je, ni kwa kiasi gani Serikali imejiridhisha juu ya uwezo wa ufanisi na uwezo wa mtaji wa Kampuni ya DP World ili kuja kuongeza soko katika bandari zetu?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, ni kwa kiasi gani Serikali imejiridhisha uwezo wa kuweza kuongeza ushindani kwa kuwa tayari tunazo Bandari za Beira (Msumbiji), Mombasa (Kenya), na Durban (South Africa) ambazo tunashindana nazo? Mmepima uwezo wa DP World kuja kuongeza ushindani katika eneo hili la ukanda wa SADC na ukanda wa Afrika Mashariki?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Abdallah Shangazi, Mbunge wa Mlalo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali pasi na shaka imejiridhisha kwamba DP World Port ina uwezo wa kuendesha bandari zetu nchini hususan Bandari yetu ya Dar es Salaam. Tumejiridhisha kwa maana ya kwamba, kwanza, inafanya kazi katika mataifa yasiyopungua 69 duniani, na pia wataalamu wetu wametembelea mataifa hayo ikiwemo Uingereza, Canada, India, Dubai kwenyewe na mataifa mengine.

Mheshimiwa Spika, vile vile Bandari hii ya Dar es Salaam hivi sasa inapata wateja wake kwa njia ya mfanyabiashara kuleta meli yake, lakini kupitia DP World, wao wana connection, au mtandao mpana wa kibiashara huko duniani, kwa hiyo, watatutafutia masoko. Zaidi ya yote, wamejenga bandari kavu katika nchi ambazo tunahudumia kama Taifa hususan kule Congo pamoja na Rwanda.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, Mheshimiwa Mbunge anataka kujiridhisha kuhusu ushindani na uwekezaji ambao atafanya DP World. Ni kweli kwamba ushindani katika bandari zetu ni mkubwa hususan katika ukanda wetu wa Bahari ya Hindi. Tuna Mombasa, ni washindani wetu; tuna Beira (Msumbiji), pamoja na Durban (Afrika Kusini). Kupitia DP World, Bandari ya Dar es Salaam, itaongeza ufanisi kwa ushindani kwa sababu kwanza ataleta vifaa na vyombo vya kisasa.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, mifumo ambayo tumekuwa tukizungumza miaka mingi katika Bandari yetu ya Dar es Salaam ili taasisi zionane kupitia mifumo ya electronic single window system, pia itawekezwa na itakuwa automated ili kuongeza ufanisi. Sasa hivi ukienda bandarini utakuta meli ni nyingi lakini muda wa kupakua na kushusha mizigo ni mrefu. Hili ndilo tunataka sasa tuongeze ufanisi kwa kupunguza huo muda ili Bandari yetu ya Dar es Salaam iendane na ushindani wa bandari hizi nyingine ambazo nimezitamka.

Mheshimiwa Spika, tunakushukuru. (Makofi)
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi.

Mheshimiwa Spika, barabara ya kutoka Mkomazi – Mnazi - Umba junction Maramba hadi Tanga iko katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ukrasa wa 177 kwamba ijengwe kwa kiwango cha lami; je, ni lini sasa mchakato wa kuanza upembuzi yakinifu utaanza katika barabara hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shangazi, Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara aliyoitaja inayounganisha Mkoa wa Tanga na Mkoa wa Kilimanjaro iko kwenye Ilani na utekelezaji wa Ilani unaendelea. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tunahakika kwamba tutaanza usanifu wa kina baada ya kufanya upembuzi katika kipindi hiki cha miaka mitano katika utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi, ahsante.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi hii. Serikali iliwaahidi wananchi wa Kijiji cha Kivingo Kata ya Lunguza ambao wako pembezoni mwa hifadhi ya Taifa Mkomazi, kuwajengea bwawa kwa ajili ya shughuli za kilimo na lambo kwa ajili ya shughuli za ufugaji; na Mamlaka ya Hifadhi Tanzania (TANAPA) ilikuwa imeanza huo mchakato. Sasa ni lini Serikali itahakikisha kwamba bwawa hili linachimbwa na lambo kwa ajili ya mifugo linapatikana?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali zuri la Mheshimiwa Rashid Shangazi, Mbunge wa Mlalo juu ya ahadi iliyotolewa na Shirika letu la TANAPA kuhusu kujenga lambo katika Kijiji cha Kizingo pembeni ya hifadhi ya Taifa ya Mkomazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali tunafanya kazi kwa pamoja na TANAPA ni chombo chetu, naomba nimwahidi Mheshimiwa Mbunge ya kwamba nitazungumza na Mheshimiwa Waziri wa Maliasiri na Utalii tuwakumbushe TANAPA tuweze kuifanya kazi hii ya wananchi. Ahsante.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ukurasa 177, ipo barabara ya kutoka Same – Mkomazi - Umba Junction - Maramba hadi Tanga.

Je, ni lini upembuzi yakinifu na usanifu wa kina utafanyika kwa barabara hii kuunganisha Mkoa wa Kilimanjaro na Tanga kupitia Wilaya ya Lushoto na Mkinga? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili: Je, ni lini Serikali sasa itakamilisha upembuzi wa kina na usanifu katika kipande cha kutoka Mlalo kwenda Umba Junction kuungana na barabara hii ambayo nimeishaitaja? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Shangazi, Mbunge wa Mlalo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara ya Same - Kisiwani kuja Mkomazi ilikuwa inajengwa kwa vipande. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na Wabunge wa Mkoa wa Kilimanjaro hasa Mheshimiwa Mama Anna Kilango ambaye inamhusu sana barabara hii, kwamba barabara hii ambayo ina urefu usiopungua kilometa 92 inatangazwa yote kujengwa kwa kiwango cha lami na ipo kwenye hatua mbalimbali za kutangaza zabuni.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa swali lake la pili, kuhusu barabara hii ya Mlalo - Umba Junction Serikali inaanza upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ili iweze kujengwa kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mheshimiwa Naibu Waziri anajibu swali la msingi, alitaja viwanja Vinne lakini kwa bahati mbaya kiwanja cha Tanga sijakiona ilihali Tanga tuna ujenzi wa bomba la mafuta na ujenzi huu utahitaji uwanja wa ndege wa Tanga uwe umepanuliwa kwa ajili ya kutoa huduma.

Je, ni upi mkakati wa Serikali kupanua uwanja wa ndege wa Tanga ili kuruhusu shughuli za bomba la mafuta?
NAIBU WAZIRI UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Rashid Shangazi, Mbunge wa Mlalo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanja nilivyovitaja vine vipo kwenye package moja, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Shangazi kwamba Serikali kama bajeti ya mwaka huu tunaokwenda kuipitisha itapita, kuna viwanja vingine ambavyo pia tuna mpango wa kuvipanua na hasa kiwanja alichokisema cha Tanga ambacho katika kipindi hiki ni kiwanja muhimu sana kwa shughuli ambazo zinaendelea katika Mkoa wa Tanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuna uwanja wa Tanza, kuna uwanja wa Lake Manyara, Simiyu, Lindi, ni kati ya viwanja ambavyo tunategemea kama bajeti itapita, vitakuwa ni baadhi ya viwanja ambavyo tutavipanua na kuvifanyia maboresho makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Katika Jimbo la Mlalo, Vituo vya Polisi vya Mlalo na Mtae vipo katika majengo ambayo ni ya Serikali za Vijiji: Je, Serikali ina mpango gani sasa kujenga majengo ya Polisi katika tarafa hizi mbili?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shangazi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Mheshimiwa Shangazi, moja, kwa kujenga mahusiano mema na Serikali za Vijiji hata wakapata majengo ya kuazima. Pia, nikiri kwamba majengo yale hayakidhi haja ya vituo vya kisasa vya Polisi. Nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa vile yeye analo fungu kidogo kwenye Mfuko wa Jimbo, nimshauri aweze kutenga kidogo kwa sababu, tumesema vituo vilivyoko kwenye maeneo ya kijamii kadiri wanajamii wanavyoanza kutoa na Serikali inawaunga mkono kumalizia. Kwa hiyo, akianza tu anipe taarifa na sisi Wizarani tutajipanga ili Jeshi la Polisi liweze kuongezea, vituo hivi vya Mlalo na Mtae viweze kukamilika, nashukuru.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika ahsante, kwa kuwa zao la chikichi linastawi vizuri katika Bonde la Tanganyika na kwa kuwa chikichi inazalisha mafuta, lakini pia malighafi kwa ajili ya kutengenezea sabuni lakini pia mabaki yake yanatumika katika uzalishaji wa chakula cha mifugo.

Je, ni mkakati upi Serikali inauweka kutafuta wawekezaji wakubwa kama wale wa mashamba ya miwa katika bonde hili ili angalau kuziba nakisi hii? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, mkakati wa Serikali ni kuanza kuzungumza na wawekezaji wakubwa walionesha nia kuwekeza katika eneo ikiwemo Kampuni ya Wilmar, Kampuni ya Bakhresa na Mohamed Enterprises na mazungumzo yanakwenda vizuri na wako tayari kufanya uwekezaji huo pindi pale mashamba makubwa yatakapopatikana na tayari mashamba hayo hivi sasa wataalamu wetu wa Wizara ya Kilimo wapo kule kwa ajili ya upimaji wa afya ya udongo ili tukijiridhisha basi tuweze kukaa chini kuzungumza na hawa wawekezaji watumie mashamba hayo makubwa kwa ajili ya uzalishaji wa chikichi.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Serikali ambayo sisi kule mkoani katika hatua ya RCC tulikaa, sasa sijui yalikwamia wapi? Nina maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza: Kwa kuwa mchakato huu huwa unaandaliwa na wataalamu na ambao wako chini ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Je, kama alivyoeleza kwamba hawajapokea wasilisho, hawaoni tu kwamba Mkoa wa Tanga ndiyo mkoa pekee nchini ambao una wilaya nane na una Majimbo ya Uchaguzi 12 na Halmashauri 11? Sasa ni lini Serikali yenyewe tu itaweza kufanya maamuzi ya kuugawa mkoa huu?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, tunaposema utawala bora ni pamoja na upelekaji wa huduma kwa wananchi. Sasa wataalamu hawa katika ngazi za elimu na afya wanapata taabu kubwa sana kwa sababu wanatumikia eneo kubwa la kiutawala: Ni lini sasa Serikali itatenda kama inavyosema kuhusu eneo zima la utawala bora?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi Mbunge wa Jimbo la Mlalo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli tunafahamu Mkoa wa Tanga ni miongoni mwa mikoa yenye Halmashauri nyingi na ni mkoa mkubwa na maana yake kunakuwa na changamoto za aina yake katika uendeshaji. Ila kwa mujibu wa sheria, uanzishaji ni lazima uanzie ngazi ya mkoa wenyewe kama ambavyo sheria hii inaelekeza. Kwa hiyo, pamoja na kwamba Serikali kwa maana ya Serikali Kuu inaona, lakini wajibu wa Halmashauri, mkoa wenyewe, na vijiji utekelezwe ili tuweze kuanzisha mkoa huu kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Spika, pili, kuhusiana na changamoto ya ukubwa wa mkoa ambao unapelekea wataalamu wa afya na elimu kushindwa kutekeleza majukumu yao ya utawala bora, tunaendelea kuwezesha kwa kadri ya ukubwa wa mkoa kwa maana ya miundombinu, usafiri na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, jambo la msingi ni kuleta hoja hiyo ili Serikali iweze kuchukua maamuzi stahiki. Ahsante.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Serikali yenye matumaini kwa wananchi wa Jimbo la Bahi, lakini nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kule Kata ya Mwangoi na Kata ya Dule Mlalo ambako linaunganishwa na Mto Umba, mto ule umehama na kusababisha kina cha maji kushuka chini zaidi na hivyo daraja limezama katika eneo lile, lakini Ofisi ya Rais, TAMISEMI kupitia TARURA wameshafanya tathmini.

Sasa nauliza ni lini ujenzi wa daraja jipya linalounganisha Kata ya Mwangoi na Kata ya Dule katika Kijiji cha Chamlesa litaanza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Rashid Shangazi, Mbunge wa Mlalo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ambayo ameianisha pamoja na hilo eneo ambalo daraja linahitajika, kati ya Mwongoi na Dule, daraja hilo lipo katika mpango na tutalitekeleza katika mwaka wa fedha 2022/2023 yaani mwaka unaofuatia.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kata ya Mbaramo na Shagayo katika Jimbo la Mlalo bado hakuna hata kijiji kimoja kimesambaziwa umeme. Nataka kujua, ni lini Serikali itaanza usambazaji wa umeme katika kata hizo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shangazi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Tanga unao wakandarasi watatu wanaopeleka umeme vijijini na katika Jimbo lake yuko Mkandarasi anaitwa Dem Electric ambaye anapeleka umeme katika maeneo hayo. Nafahamu kwamba mkandarasi huyu anajitahidi kufanya kazi zake vizuri na atakuwepo kwenye maeneo ya kazi, pengine ameanzia eneo lingine ili aje amalizie kwenye hayo maeneo ya kata alizozisema za Mbaramo na Shagayo kama nitakuwa nimezitaja vizuri. Nichukue nafasi hii kumwelekeza yeye pamoja na wakandarasi wengine wagawanye magenge wanayotumia katika kufanya kazi ili kila eneo la Mbunge liweze kuonekana likiwa linafanyiwa kazi kama ambavyo walienda wakaripoti wakaanza kufanya kazi za utekelezaji katika maeneo hayo na eneo hilo liwe mojawapo la kuhakikisha kwamba wanatoka kwenye maeneo waliyofikia sasa kwenda kwenye maeneo mengine ili kufanya kazi na kukamilisha kazi kwa wakati.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi. Katika Halmashauri ya Lushoto yenye shule za msingi 180, ina uhaba wa walimu takribani 1,400, hali inayosababisha sasa angalau wastani wa shule moja kuwa na walimu wanne tu: Je, Serikali ina mpango gani mahususi wa kuhakikisha kwamba inakwenda kuboresha ikama katika Halmashauri ya Lushoto? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza lililoulizwa na Mheshimiwa Rashid Shangazi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba upungufu upo kama nilivyokiri katika jibu la msingi, lakini nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo la ikama la mahitaji ya walimu au madaktari au kada zozote katika maeneo yetu linaanza kwenye mchakato ndani ya Halmashauri zetu. Kwa hiyo, napenda nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Halmashauri yake ya Lushoto ilete mahitaji hayo, nasi kama Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, tutalichukua jambo hili na kwenda kulifanyia kazi na tutakapopata kibali cha ajira, basi tutahakikisha kwamba tunampelekea wafanyakazi kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge anahitaji.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kituo cha Afya Mlalo ni miongoni mwa vituo vikongwe kabisa ambavyo havina huduma ya X-Ray: Je, ni lini Serikali itahakikisha sasa kituo hiki kinapata huduma hiyo ya X-Ray kwa sababu kinahudumia zaidi ya kata tisa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Rashid Shangazi, Mbunge wa Jimbo la Mlalo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, vituo vyetu vyote vya afya kote nchini vimewekwa kwenye mpango mkakati wa kujenga majengo kwa ajili ya huduma za upimaji na huduma za X-Ray na Ultrasound zikiwemo. Kwa hiyo, naomba nilichukue hili ili tuweze kufanya tathmini kwenye Kituo hiki cha Afya cha Mlalo tuone uwezekano wa kupata fedha kwa ajili ya kujenga Jengo la X-Ray na baadaye kuweka mashine kwa ajili ya kuendelea kutoa huduma, ahsante.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. pamoja na majibu ya Serikali, lakini nina maswali madogo mawili ya nyongeza: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; kwenye mapendekezo ambayo ameyataja hapo sikuona suala zima la elimu kwa raia, kwa wananchi, kwa maana Katiba si mali ya wanasiasa pekee ni mali ya wananchi. Je, Serikali imejipangaje kuanzisha elimu japo kwa Katiba hii iliyopo ya mwaka 1977 ambayo wananchi wengi hawaifahamu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; wakati wa rasimu ya Mheshimiwa Warioba, mwaka 2012, mpaka sasa ni takribani miaka kumi na moja, wapo Watanzania ambao wakati ule walikuwa na umri mdogo na sasa wametimiza miaka 18.

Je, Serikali katika mapendekezo hayo itazingatia kwenda upya kutafuta maoni ya wananchi ili kujenga wigo mkubwa wa ukusanyaji wa maoni?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi nijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Shangazi, Mbunge wa Mlalo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kwanza kuhusu elimu kwamba, itolewe ya Katiba iliyopo. Serikali tumejipanga na ndio maana katika bajeti yetu ambayo tuliileta kwenu Waheshimiwa Wabunge tumeweka pia bajeti kwa kazi hiyo. Kwa hiyo Serikali tutatoa elimu ya Katiba iliyopo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, lakini pia Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984. Katiba hizi zote tutapeleka elimu kwa wananchi ili wazifahamu kabla mchakato huu haujaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, amependa kufahamu pia kama wananchi ambao kipindi kile cha rasimu ya Mheshimiwa Warioba hawakushiriki kutoa maoni yao kwa sababu ya umri, kama kipindi hiki watashirikishwa: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wote wa Tanzania watashirikishwa. Tunamshukuru Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuona hili, ndio maana sasa mchakato huu unaanza ili na wale ambao hawakupata nafasi ya kutoa maoni yao basi na wao waweze kutoa maoni yao.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa, Serikali imezipokea halmashauri kulipa ile posho iliyokuwa ya Madiwani.

Je, sasa Wizara haioni kwa nini isielekeze zile posho zilizokuwa zinalipwa kwa Madiwani na Halmashauri ziende zikawalipe Wenyeviti wa Serikali za Vijiji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, hili nalipokea kwa niaba ya Serikali na tutakwenda kuliangalia na kulifanyia kazi na kama tutaona liko viable basi tutachukua hatua.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu ya Serikali lakini ni ukweli usiopingika kwamba maslahi ya watumishi wa idara hii ya Jeshi la Polisi bado yanahitaji maboresho.

Je, Serikali ina mpango gani mahususi wa kuboresha maslahi ya Askari Polisi ili sasa watakapokuwa wanastaafu waweze kupata mafao ambayo yana endana na hali halisi ya maisha?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Rashidi Shangazi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu wa kuangalia maslahi ya askari wa vyombo vya usalama Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameamua kuunda Tume ya Haki Jinai ambayo pamoja na mambo mengine inakwenda kuangalia vilevile eneo hili la maslahi ya askari. Kwa hiyo nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo hilo Mheshimiwa Rais ni katika mambo ambayo anayapa uzito mkubwa sana, na tusubiri pale ripoti ya Tume itakapomaliza ili tione sasa utekelezaji wake utakuwa vipi.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kata ya Manolo, Halmashauri ya Lushoto wameshajenga Wodi ya Mama na Mtoto na wodi mbili za baba na za akinamama, lakini sasa wako katika ujenzi wa theater. Je, Serikali iko tayari kuunga mkono juhudi hizi za wananchi ili sasa tuweze kukipasisha kiwe kituo rasmi cha afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu swali la la nyongeza Mheshimiwa Shangazi la Kituo cha Afya Manolo kule Wilayani Lushoto, Serikali itafanya tathimini katika ujenzi huu wa theater ya pale Manolo na kadri ya upatikanaji wa fedha tutahakikisha kwenye bajeti hii tunayoenda kutekeleza kama ipo tutapeleka fedha kuwasaidia wananchi hawa, lakini kama haipo tutatenga katika bajeti ya mwaka 2024/2025, ili kusapoti jitihada zile za wananchi pale.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; Serikali inakiri kwamba bado haijapata kutambua vizuri kundi hili na ilihali na yenyewe inatambua kwamba ilitoa vitambulisho;

Je, Serikali iko tayari kukiri kwamba vitambulisho vile havikusaidia kutambua kundi hili, haswa kwa teknolojia duni ambayo imetumika?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Ili machinga atoke kwenye hali ya umachinga na Kwenda katika kundi la wafanyabiashara wagodo na wa kati, ni lazima apewe afua mbalimbali za kikodi;

Je, Serikali ina mpango gani sasa kuzibainisha hizo afua za kikodi ili hawa wamachinga waweze kuzitambua na waweze kuingia kwenye kundi la wafanyabiashara rasmi?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Ni kweli moja ya changamoto zilizojitokeza kwa vitambulisho vile vya awali vya kuwatambua wamachinga ilikuwa ni kwamba vinaweza vikatumika na mtu yoyote kwa sababu havikuwa vya kielektroniki. Moja ya kazi kubwa tunayofanya sasa katika bajeti inayokuja ni Serikali Kwenda kutoa vitambuilisho vya kielektroniki ambavyo vitasaidia kuwatambua wajasiriamali walipo, lakini pia pale ambapo watakuwa wamekua, kwa maana kutoka mitaji ile midogo ya 4,000,000 ambayo tunatambua kama wajasiriamali, kwenda juu tutawatambua kama wafanyabiashara halali na kuwarasimisha kwenye kundi halali la wafanyabiashara kutoka wajasiriamlali.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwenye swali la pili; Serikali inafanya kazi kubwa sana. Moja ni kurasimisha kuwatambua wajasiriamali hawa na Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan ametoa fedha 10,000,000 kuanzisha ofisi za wamachinga kila Mkoa. Sasa kupitia hizo tutawatambua na kuwasaidia kupata mikopo nafuu kwenye taasisi zetu za fedha, lakini pia utaratibu unaokuja ni kuona zile fedha asilimia 10 ambazo zilikuwa zinatolewa ziweze kuwa na manufaa kupitia benki ili wajasiriamali hawa wadogo ambao wanahitaji mitaji kwa ajili ya kuendeleza biashara zao wanufaike.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa kuwa, wako watanzania wengi ambao wana ujuzi na stadi mbalimbali na ziko nchi ambazo tunapakana nazo zina uhaba wa kada mbalimbali za utumishi.

Je, Wizara hii iko tayari kuketi na Wizara ya Mambo ya Nje ili kuweza kuwasaidia Watanzania hawa waweze kupata ajira katika nchi hizo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, wazo lililotolewa na Mheshimiwa Mbunge la kuketi na Wizara ya Mambo ya Nje, sisi kama Serikali niseme tunalichukua na tutakaa na wenzetu na kutengeneze miongozo mizuri ya kuona ni jinsi gani tunauza ajira nje ya nchi yetu.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona, kwa kuwa Serikali imeondoa mzigo ule wa kulipa posho za Madiwani kutoka kwenye Halmashauri na Serikali Kuu sasa ndio inayolipa hizo posho; je, Ofisi ya Rais, TAMISEMI iko tayari sasa kuelekeza kwamba zile posho zilizokuwa zinalipwa kwa Madiwani sasa zielekezwe kuwalipa Wenyeviti wa Serikali za Vijiji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kutambua kazi kubwa inayofanywa na Waheshimiwa Madiwani kuanzia mwaka wa fedha 2022/2023 alichukua jukumu la Serikali Kuu kulipa posho za Halmashauri 168 kote nchini na kazi hii inaendelea.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba halmashauri hizi siku za nyuma zilikuwa zinalipa posho za Madiwani, lakini zile fedha zimeendelea pia kupelekwa kwenye maeneo ya miradi mbalimbali. Naomba tuchukue wazo la Mheshimiwa Mbunge kwamba tuone kama zinaweza zikapelekwa kwenye malipo ya Serikali za Vijiji na Mitaa, tutafanya tathmini tuone kama inaweza kutekelezwa ama vinginevyo na tutaleta taarifa rasmi, ahsante.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu ya Serikali, lakini nina maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; kwa kuwa bado kuna idadi kubwa sana ya Walimu wa Masomo ya Sayansi ambao bado hawajapata ajira na Serikali ilikuwa inaendelea kuajiri kidogo kidogo.

Je, ni upi mkakati wa Serikali sasa kuhakikisha kwamba angalau inaongeza wigo wa ajira angalau kuchukua Walimu wote walioko katika soko ambao kwa sasa wako tu hawana shughuli za kufanya?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa suala zima la sayansi pia linaendana na uwepo maabara na wananchi nchi nzima maeneo yote wamejenga sana maboma mengi ya maabara, lakini kulikuwa na kasi ndogo ya ukamilishaji wa miradi hiyo ya Maabara. Je, Serikali ina mpango gani mahususi kuhakikisha kwamba ndani ya kipindi kifupi maboma yote yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi yanakamilika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza yaliyoulizwa na Mheshimiwa Shangazi kwa niaba ya Mheshimiwa Kapinga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, hii idadi ya Walimu ambao bado hawajapata ajira hawa wa sayansi, nimtoe mashaka Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali hii ya Awamu ya Sita itaendelea kutoa kipaumbele katika kuziba mapengo na kuajiri Walimu wengi zaidi kwa sababu kama walivyoona, Wabunge wote ni mashahidi, Serikali hii imejenga miundombinu mingi sana kwenye suala zima la elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hawa Walimu 13,130 ni kwenye mwaka wa fedha huu ambao tunaumaliza, kwa maana ilikuwa 2022/2023 na vilevile Serikali imetenga bajeti kwa ajili ya 2023/2024 na pale ambapo fedha zitaruhusu, basi Serikali itaendelea kuajiri Walimu wengi zaidi na kuwapeleka katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda kwenye swali lake la pili la uwepo wa maabara. Ni kweli Serikali iliweka kipaumbele katika ujenzi wa maabara katika maeneo mbalimbali hapa nchini kwa kupeleka shilingi milioni 30, 30 katika shule nyingi sana hapa nchini kwa ajili ya ujenzi wa maabara hizi. Baada ya ujenzi huu kukamilika sasa Serikali iko katika harakati za kutafuta fedha kwa ajili ya kupeleka vifaa vya maabara hizi. Mara baada ya vifaa hivyo kufika kwenye maabara hizi, vilevile tutaangalia tena namna gani ya kupata fedha kuendeleza ujenzi wa maabara zingine kote nchini.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante Tarafa ya Mlalo yenye kata nne inahitaji kituo kimoja cha kimkakati ambacho kitahudumia Kata ya Lukozi, Malindi, Manolo na Shume.

Je, Serikali ina mpango gani kujenga kituo hiki kwa haraka kwa sababu pia ni ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu alipofanya ziara katika Kata ya Lukozi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru nipende kujibu swali la Mheshimiwa Shangazi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimshukuru kwa namna ambavyo ameendelea kufuatilia maendeleo ya jimbo lake lakini kwa namna ambavyo ameendelea kufatilia utekelezaji wa ahadi za viongozi wetu. Nipende tu kumwakikishia kwamba tunatambua umuhimu na namna ambavyo Kata hii ya Lukozi iko kimkakati. Tunajua kituo hichi endapo kitajengwa kitaweza kuhudumia zaidi ya kata nne ikiwemo Manolo, Malindi, Lukozi yenyewe na nimpe tu uhakika. Kwamba tutakijenga katika mwaka ujao wa fedha 2023/2024 kama ambavyo tutaweza kupanua Kituo cha Afya cha Mlalo vilevile katika Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto kwa Mheshimiwa Shekilindi tutaweza pia nako kujenga kituo cha afya kwa upande Gare, nikushukuru.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu ya Serikali, lakini bado nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mkakati wa Serikali unaonekana hawajafanya utafiti wa kuweza kujua ni kwa kiasi gani uzalishaji wa mbegu unahitajika nchini: -

Je, Serikali ipo tayari sasa kutengeneza mkakati, angalau wa miaka mitano, wa kuhakikisha kwamba wanafanya utafiti wa kujua ni idadi kiasi gani ya mbegu zinatakiwa ili uzalishaji huo wa miche milioni 20 kwa mwaka angalau upande hadi kufikia miche milioni 50?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa TaCRI na Bodi ya Kahawa peke yao hili zoezi hawaliwezi: -

Je, Serikali ina mkakati gani mahususi wa kuhakikisha kwamba inaihusisha sekta binafsi katika eneo hili la uzalishaji wa mbegu ili sasa hili zao la kahawa tuweze kulifufua kote nchini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi, Mbunge wa Mlalo, kwa pamoja kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la utafiti kwenye kahawa ndiyo kazi ambayo imekuwa ikifanyika muda wote kupitia TaCRI ili kuwezesha kuongeza uzalishaji katika zao letu la kahawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uzalishaji wa miche ya kahawa unaendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka kutokana na mahitaji. Kwa hivi sasa tumetoa maelekezo kwa wenzetu wa TaCRI pamoja na wakulima pia kuhakikisha ya kwamba tunang’oa ile mibuni yote iliyofikisha zaidi ya miaka 25 ambayo imezeeka na kupanda miche mipya ili kuongeza uzalishaji. Hivyo, itatulazimu kuongeza uzalishaji mkubwa sana wa miche ya kahawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana sisi kama Serikali peke yetu hatuwezi kufanya, tumewahusisha pia sekta binafsi ili kwa pamoja tuweze kuzalisha miche mingi zaidi, na lengo hapa ni kuwa na miche mingi ya ziada ili wakulima wetu waweze kuipata kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa tumeongeza mkakati mwingine wa kuhakikisha kwamba tunatumia teknolojia ya chupa (tissue culture) kwa ajili ya kuongeza uzalishaji miche mingi zaidi ya kahawa, iwafikie wakulima kwa wakati, na tuweze kuongeza uzalishaji wa zao hili la kahawa hapa nchini.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa kuwa Waziri ametamka wazi kwamba nafasi hizi zinatolewa kwa ushindani, lakini kule vijijini ambako wanafunzi wengi ambao wanaomba hizi nafasi ndiko waliko, Magazeti hayafiki wala mtandao hakuna.

Je, huo ushindani wa haki unapatikanaje katika mazingira ya aina hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Shangazi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba, vilio vinekuwepo hasa katika maeneo ya kule vijijini kabisa, na ni maelekezo yetu kama Wizara kuhakikisha kwamba matangazo yote yanayoletwa ya ajira yanakwenda kwa Wakurugenzi wote wa Halmashauri na kuhakikisha yanafika kwenye vijiji husika, yafike kwenye ofisi za vijiji, yafike kwenye ofisi za kata na maeneo yote yaliyo muhimu kwa ajili ya wananchi kupata taarifa, ili ajira hizi ziendelee kukimbiliwa na Watanzania wote kwa usawa.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, pamoja na majibu ya Serikali nina maswali madogo mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, Mradi wa Rangwi ambao ameutaja hapa ambao una vijiji karibia vinne vya Goka, Nhelei, Kalumele na Mamboleo ni mradi ambao sasa umechakaa, lakini pia eneo la usambazaji limekuwa dogo kwa sababu idadi ya watu imeongezeka. Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuboresha mradi huo?

Pili, katika kata ya Sunga, Tarafa hiyo hiyo ya Mtae vijiji vyote vinne havijawahi kuwa na mradi wowote wa mfumo wa maji ya bomba. Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka na kata hii ya Sunga iweze kupatiwa miundombinu ya maji safi ya bomba?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shangazi kama ifuatavyo;-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tunafahamu mradi ule umechakaa na kama Wizara tayari tumeuweka kwenye mpango wa mwaka 2022/2023 ili kuona kwamba tunakwenda kukarabati na kuweza kuwafikishia wananchi wote wa maeneo aliyoyataja maji mengi, safi, salama na ya kutosha.

Swali lake la pili anaulizia kuhusu Kata ya Sunga ambayo ina vijiji vinne ni kweli mtambao wa mabomba kwenye kata hii haukuweza kufikiwa kulingana na jiografia ya eneo lenyewe. Vyanzo ni kweli viko vingi katika eneo lile, lakini vyanzo vingi viko maeneo ya chini na wananchi vijiji viko kwenye miinuko kwa maana kwenye milima hivi kidogo kama tunavyofahamu jiografia ya Lushoto lakini kama Wizara tunaendelea kuona uwezekano wa kupata vyanzo vya kujitosheleza maeneo yale ya juu na hatimaye kabla ya mwaka ujao wa fedha tutahakikisha tunapata na kuweza kuwafikishia maji ya bombani wananchi wote wa Kata ya Sunga yenye vijiji vinne.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, lakini kuna maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa sasa tunakaribia kwenda kusaini mkataba mkubwa wa uchakataji wa gesi asilia wa LNG kule Kusini na sehemu ya uzalishaji wa malighafi za gesi kuwa pia inatengeneza mbolea.

Je, ni upi mkakati wa Serikali kufungamanisha uchakataji wa gesi asilia na uanzishaji wa Kiwanda cha Mbolea katika eneo la Kusini?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Mkoa wa Tanga ndiyo tutakaopokea hifadhi ya mafuta ghafi kutoka Uganda.

Je, Serikali haioni kwamba tunaweza tukatumia eneo la Chongoleani ikiwa ni sehemu pia ya usafishaji ghafi; kwa sababu mafuta haya pia ni malighafi kwa ajili kutengeneza mbolea tukapata Kiwanda kingine cha Mbolea katika Mkoa wa Tanga kama kile kilichokuwepo miaka ya nyuma? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Shangazi, Mbunge wa Mlalo, kama ifutavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Shangazi kwa kufuatilia maendeleo ya ujenzi wa viwanda hasa vya mbolea katika nchi hii na hasa katika Mkoa wa Tanga. Serikali ina mpango wa matumizi ya gesi asilia ambao unatekelezwa kupita Shirika letu la Maendeleo la Petroli (TPDC) lakini pia kwa kushirikiana na Kituo chetu cha Uwekezaji cha (TIC). Kwa hiyo, katika mpango huo tumeshaendelea kuvutia wawekezaji na zaidi ya kampuni tatu ambazo zimeonesha utayari wa kuwekeza katika kuzalisha mbolea kwa kutumia gesi asilia kampuni hizo ni pamoja na Helmik na Ferosta kutoka Ujerumani lakini pia tunayo Polyserve kutoka Misri, lakini zaidi na wengine wanaendelea kufanya tathmini na namna ya kutumia gesi asilia ikiwemo Kampuni ya Dangote.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, katika mpango huo tumeshaendelea kuvutia wawekezaji, na zaidi ya kampuni tatu zimeonesha utayari wa kuwekeza katika uzalishaji wa mbolea kwa kutumia gesi asilia. Kampuni hizo ni pamoja na Helium na Feroster kutoka Ujerumani na pia tunayo Polysafe kutoka Misri. Vile vile na wengine wanaendelea kufanya tathmini ya namna ya kutumia gesi asilia ikiwemo Kampuni ya Dangote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni sahihi kabisa, ni mawazo mazuri kuona namna gani Tanzania inatumia fursa ya mafuta ghafi kutoka Hoima Uganda ambayo yatakuja Tanzania, tuone namna gani ya kutumia mafuta hayo ghafi kuzalisha mbolea ili tukidhi mahitaji makubwa ya nchi hii kutokana na upungu au nakisi ya mbolea kwa ajili ya sekta ya Kilimo. Nashukuru. (Makofi)
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, majibu ya Serikali yamejikita kwenye mfuko mmoja tu ambao ni asilimia 10 ya mapato ya halmashauri, lakini Serikali inamifuko zaidi ya 45 ya kuondoa umaskini.

Je, haioni sasa ni wakati muafaka wa kuanza kuwakopesha wanafunzi kwa kutumia dhamana ya vyeti vyao ambavyo wamevipata vya kitaaluma ili kuondoa hili tatizo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kujibu swali dogo la Mheshimiwa Rashid Shangazi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Mheshimiwa Shangazi amezungumza suala la vyeti na mwanafunzi akishapata cheti haitwi tena mwanafunzi anaitwa muhitimu. Kwa hiyo, naomba nilifanyie marekebisho hapo namna gani wahitimu wetu sasa wanaweza kutumia vyeti vyao kuweza ku-access hiyo mikopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuchukue ushauri wa Mheshimiwa Shangazi, twende tukaufanyie kazi tuufanyie na tathimini ya kina kwasababu sasa ni suala mtambuka si suala la Wizara ya Elimu peke yake hapa itaingia Wizara Fedha, lakini Wizara ya Vijana na Wizara nyingine ambazo zinashughulika na mambo ya vijana na mikopo kwa ujumla.

Kwa hiyo, naomba tuchukue ushauri wa Mheshimiwa Mbunge twende tukaufanyie tathimini ya kina ili tuweze kuangalia je, hivi vyeti vinaweza vikatumika kama bond ya kuwapatia mikopo vijana wetu. Nakushukuru sana.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi, Skimu ya Umwagiliaji ya Kitua Nimwezayo Kongriti iliyoko katika Kata ya Lunguza imeshatengenezewa usambazaji wa maji kutoka kwenye banio hadi kwenye mashamba katika hatua ya awali.

Ni lini hatua ya pili ya kutoa maji kwenye mifereji kuyaingiza kwenye mashamba itaanza?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Shangazi, Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua ya kwanza tuliyoifanya ilikuwa ni kurudisha njia za asili za Mto Umba ambao kazi hiyo imekamilika. Hatua ya pili itakuwa ni kufanya tathmini ya gharama halisi za ukarabati wa mifereji ili tupeleke maji hayo shambani. Nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba hatua ya pili itafanyika ili maji hayo yaweze kufika shambani. (Makofi)
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina swali moja la nyongeza. Kwa kuwa kahawa yenyewe ni bidhaa ambayo ni malighafi, swali langu ni kwamba: Ni upi mkakati wa Serikali kuvutia sekta binafsi katika kuongeza thamani kwa maana ya kuzalisha bidhaa ambazo zitachukua kahawa kama malighafi kwa mfano perfume, dawa na bidhaa nyinginezo ndani ya nchi yetu? Ni upi mkakati wa Serikali kuvutia uwekezaji wa aina hiyo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa swali la msingi ambalo lina tija katika kuongeza thamani katika zao la kahawa. Miongoni mwa mikakati yetu ambayo tulikuwa tumeiweka ni pamoja na kuvutia wawekezaji wengi kuja nchini.
Mheshimiwa Spika, moja ya sababu ambayo tumeiweka hapo, mwekezaji yeyote atakayekuja nchini kuwekeza kwenye viwanda vyetu hususani vya kahawa, maana yake tumepunguza baadhi ya kodi ambazo zilikuwa ni kodi kero kwa wawekezaji ikiwemo kuzuia baadhi ya bidhaa ambazo zinatoka nje, zinazoweza kuua soko la ndani, pamoja na kuwapa vivutio vya muda wa kufanya kazi hizo pamoja na mazingira ya kibiashara kuyaongeza katika soko letu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimwondoe shaka Mheshimiwa Mbunge kwamba moja ya mkakati wa Serikali yetu ni kuvutia wawekezaji na kila mwekezaji atafanya biashara zake hapa katika hali ya usalama zaidi, ahsante sana. (Makofi)
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, vijana wanatofautiana katika sifa, makundi na mahitaji; je, ni kwa kiasi gani programu hizi zimezingatia changamoto hiyo?

Swali la pili, tumeona katika sekta ya elimu sasa tumekuja na mtaala mpya ambapo mafunzo ya stadi kwa maana ya amali yataanza katika ngazi ya msingi; je, katika hayo maboresho ambayo Serikali inakusudia kuyafanya Serikali iko tayari kuzingatia eneo hili la mtaala mpya wa elimu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Rashid Shangazi ambalo kwanza ni kuhusiana na sifa na makundi mbalimbali ya vijana, jinsi ambavyo Serikali imeweka programu za kuweza kuwasaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali tumeweka programu mbalimbali kulingana na mtawanyiko wa makundi pia mikakati imewekwa kwa ajili ya kuangalia namna gani ambavyo vijana hawa wanaweza kufikiwa wote katika Taifa. Moja ya programu ambazo tumeziweka tumeangalia pia programu kisekta, kwa mfano kwenye sekta ya elimu, vijana walio wengi kama viongozi wa baadaye wa Taifa hili wamewekewa programu na Serikali ya kupewa msaada wa elimu bure au elimu bila malipo mpaka Kidato cha Sita na akimaliza Kidato cha Sita ataenda Chuo Kikuu ambako anakutana na mkopo na sasa Dkt. Samia Suluhu Hassan amefikisha mkopo wa elimu ya juu kufikia shilingi bilioni 734.

Mheshimiwa Mwenyekiti, programu nyingine ambayo ipo ya kisekta ni kwenye eneo la uchumi, biashara na uwekezaji. Hapo pia tuna Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, sambamba na hilo kwenye Halmashauri zetu tumeweka programu ya utoaji wa mikopo pia fursa za ajira na mitaji. Katika eneo hilo zile asilimia nne zinaenda kwa ajili ya vijana na watu wenye ulemavu lakini pia wanawake, wanasaidiwa hata awe amemaliza Chuo Kikuu au hayupo kwenye sekta ya kisomo anaweza akapata fedha zikamsaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye sekta ya madini, tumeenda kisekta katika Wizara kuangalia, sekta ya madini pia wapo wale wachimbaji wadogo wadogo vijana, nao wanawezeshwa huko kulingana na programu na miongozo ambayo tumeiweka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sekta ya kilimo pia tuna BBT LIFE ambayo ni Building Better Tommorrow kwa ajili ya kuwasaidia vijana waweze kujifunza namna ya kunenepesha mitamba ya ng’ombe na pia kufanya cage fishing na mafunzo mengine yanayoendana na masuala ya uchumi wa bahari. Zaidi ya hapo kwenye kilimo tuna vijana, tuna BBT LIFE ambayo ni kilimo biashara. Mafunzo yanaendelea na zaidi ya vijana 800 walikuwa wanufaika na programu hizi ni endelevu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna sekta nyingine ya ajira na kazi, tuna kitengo maalum cha ajira kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu cha TAESA, ambapo vijana wanaomaliza vyuo vikuu wanaenda kwa ajili ya mafunzo ya utayari kazini. Pia tuna programu za ukuzaji ujuzi, tuna programu za wanagenzi, zote hizi zinalenga kuwagusa vijana kwenye makundi mbalimbali. Zipo pia programu kwenye sekta ya michezo na sekta nyingine kwa sababu ya muda, lakini uone jinsi gani Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan imewaangalia vijana katika maeneo yote. Hata wale ambao wana-aspire kwenye uongozi wa Taifa kwenye maeneo ya siasa, vyama vya siasa tumefanya mabadiliko ya Sheria hapa kwamba vijana waangaliwe pia katika kupewa fursa kwenye vyama vyao na kuweza kupata fursa za uongozi. Ahsante. (Makofi)
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule katika Jimbo la Mlalo Tarafa ya Umba kwa maana ya Kata ya Mng’aro, Lunguza, Mnazi lakini na Kijiji cha Kivingo tumeshatenga maeneo kwa ajili ya skimu hizi za umwagiliaji;

Je, lini miradi hii itaanza?

NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana naomba nimjibu Mheshimiwa Rashid Shangazi Mbunge wa Jimbo la Mlalo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua kwamba haya maeneo yote ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyataja ya Mng’aro, Lunguza, Mnazi na Kivingo wameshayaandaa kwa ajili ya shughuli hiyo. Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inayafanyia kazi; na tukishamaliza kazi hiyo basi miradi hiyo itatekelezeka. Kikubwa ambacho niwaondoe shaka Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Rais ameweka commitment kubwa kwenye miradi yote ya umwagiliaji na fedha ipo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hii. Kwa hiyo, tutafikia takriban miradi yote nchini, ahsante sana.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, vijana wanatofautiana katika sifa, makundi na mahitaji; je, ni kwa kiasi gani programu hizi zimezingatia changamoto hiyo?

Swali la pili, tumeona katika sekta ya elimu sasa tumekuja na mtaala mpya ambapo mafunzo ya stadi kwa maana ya amali yataanza katika ngazi ya msingi; je, katika hayo maboresho ambayo Serikali inakusudia kuyafanya Serikali iko tayari kuzingatia eneo hili la mtaala mpya wa elimu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Rashid Shangazi ambalo kwanza ni kuhusiana na sifa na makundi mbalimbali ya vijana, jinsi ambavyo Serikali imeweka programu za kuweza kuwasaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali tumeweka programu mbalimbali kulingana na mtawanyiko wa makundi pia mikakati imewekwa kwa ajili ya kuangalia namna gani ambavyo vijana hawa wanaweza kufikiwa wote katika Taifa. Moja ya programu ambazo tumeziweka tumeangalia pia programu kisekta, kwa mfano kwenye sekta ya elimu, vijana walio wengi kama viongozi wa baadaye wa Taifa hili wamewekewa programu na Serikali ya kupewa msaada wa elimu bure au elimu bila malipo mpaka Kidato cha Sita na akimaliza Kidato cha Sita ataenda Chuo Kikuu ambako anakutana na mkopo na sasa Dkt. Samia Suluhu Hassan amefikisha mkopo wa elimu ya juu kufikia shilingi bilioni 734.

Mheshimiwa Mwenyekiti, programu nyingine ambayo ipo ya kisekta ni kwenye eneo la uchumi, biashara na uwekezaji. Hapo pia tuna Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, sambamba na hilo kwenye Halmashauri zetu tumeweka programu ya utoaji wa mikopo pia fursa za ajira na mitaji. Katika eneo hilo zile asilimia nne zinaenda kwa ajili ya vijana na watu wenye ulemavu lakini pia wanawake, wanasaidiwa hata awe amemaliza Chuo Kikuu au hayupo kwenye sekta ya kisomo anaweza akapata fedha zikamsaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye sekta ya madini, tumeenda kisekta katika Wizara kuangalia, sekta ya madini pia wapo wale wachimbaji wadogo wadogo vijana, nao wanawezeshwa huko kulingana na programu na miongozo ambayo tumeiweka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sekta ya kilimo pia tuna BBT LIFE ambayo ni Building Better Tommorrow kwa ajili ya kuwasaidia vijana waweze kujifunza namna ya kunenepesha mitamba ya ng’ombe na pia kufanya cage fishing na mafunzo mengine yanayoendana na masuala ya uchumi wa bahari. Zaidi ya hapo kwenye kilimo tuna vijana, tuna BBT LIFE ambayo ni kilimo biashara. Mafunzo yanaendelea na zaidi ya vijana 800 walikuwa wanufaika na programu hizi ni endelevu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna sekta nyingine ya ajira na kazi, tuna kitengo maalum cha ajira kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu cha TAESA, ambapo vijana wanaomaliza vyuo vikuu wanaenda kwa ajili ya mafunzo ya utayari kazini. Pia tuna programu za ukuzaji ujuzi, tuna programu za wanagenzi, zote hizi zinalenga kuwagusa vijana kwenye makundi mbalimbali. Zipo pia programu kwenye sekta ya michezo na sekta nyingine kwa sababu ya muda, lakini uone jinsi gani Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan imewaangalia vijana katika maeneo yote. Hata wale ambao wana-aspire kwenye uongozi wa Taifa kwenye maeneo ya siasa, vyama vya siasa tumefanya mabadiliko ya Sheria hapa kwamba vijana waangaliwe pia katika kupewa fursa kwenye vyama vyao na kuweza kupata fursa za uongozi. Ahsante. (Makofi)
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kama nilivyosema, shule hii inaitwa Mayaha, naomba hiyo isahihishwe lakini nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Halmashauri ya Lushoto ziko shule kongwe ambazo zimejengwa tangu miaka ya 1950. Shule hizo ni Mbaramo, Fufui, Lwandai, Lunguza na Tema.

Je, Serikali ina mpango gani mahususi shule hizi ambazo si za zamani tu pia ni kongwe na nyingi zimejengwa kwa miti ziweze kufanyiwa ukarabati?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, jambo la kwanza tumepokea hayo marekebisho na kama yalivyoingia katika Hansard ndivyo ambavyo fedha zitakwenda katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili katika shule ambazo Mheshimiwa Mbunge amezitaja za Mbaramo, Fufui, Nyasa, Lwandai, Lunguza na Tema ambazo zimejengwa karibu miaka ya 60 na zinahitaji marekebisho makubwa; kikubwa ambacho Mheshimiwa Mbunge atambue kwamba, Serikali sasa hivi inaendelea na Mradi wake wa BOOST ambao umekusudia kukarabati shule kongwe nchini ikiwemo hizi ambazo amezitaja. Kwa hiyo kila mwaka Serikali itaendelea kuziweka katika bajeti ili kuzirekebisha. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge wathibitishie tu wananchi wako kwamba Serikali ipo kazini na itazifanyia kazi.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kuna ahadi ya muda mrefu ya kupeleka maji katika Kata ya Mnazi katika Vijiji vya Langoni A, Langoni B, Kwemkwazu pamoja na Kiwanja. Ni lini Serikali itakamilisha usanifu na ujenzi wa mradi huu wa maji katika kata hii ya kimkakati kabisa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo, Mheshimiwa Shangazi huu mradi na hasa Kata ya Mnazi natambua kabisa kwamba Serikali kupitia Wizara ya Maji tuna ahadi ya kufika katika kata hii. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tutafika katika kata hii na kuhakikisha kwamba tunasukuma.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo tayari Serikali imeshapata mtaalamu mshauri na gharama ya mradi ya takribani shilingi milioni 800 na tayari mtaalamu mshauri huyu ameshakabidhiwa site kwa ajili ya kuanza kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge mtaalamu wetu atakapokamilika basi tunaamini kwamba mkandarasi atapatikana kwa ajili ya kuhakikisha kwamba mradi huu unatekelezwa kwa haraka iwezekanavyo, ahsante sana.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, Serikali imeboresha miundombinu ya Bandari ya Tanga kiasi kwamba shehena zimeongezeka, lakini reli ya kutoka Tanga kwenda Dar es Salaam na kutoka Tanga kwenda Arusha bado ni chakavu sana, je, kuna mpango wowote wa kuboresha reli hii ili sasa shehena hii iweze kutoka kwa urahisi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Shangazi, Mbunge wa Mlalo na Katibu wa Bunge la CCM kwa swali lake kubwa na zuri la maslahi ya watu wa Tanzania na watu wa Kaskazini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inao mpango mzuri na kabambe kwa sababu inatambua umuhimu wa upande wa Kaskazini kwanza kwenye utalii, kilimo pamoja na sekta nyingine, hivyo katika mwaka wa fedha 2023/2024 tumeshafanya kazi kubwa, tulishasaini mkataba wa kununua materials za kukarabati reli inayotoka Tanga kuelekea mpaka Arusha kilometa 533.

Kwa hiyo, mara baada ya kusaini mkataba huo katika mwaka wa fedha huu unaofuatia tunakwenda kuanza kutoa reli iliyokuwepo, tunataka tuweke reli nzito ambayo itakuwa na capacity ya ratilika 80 kwa yard, iliyokuwepo ilikuwa 45 kwa yard.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii reli iliyopo sasa hivi speed inayokwenda treni ni karibu speed ya 15 - 20 kwa saa moja, hivyo inawachukuwa muda mrefu sana kufika kwenye destination inayotakiwa. Tukifanya maboresho haya speed itaongezeka mpaka 75, kwa hiyo muda kama ilikuwa ni saa 12 tutakuwa tunatumia saa karibu nne. Kwa hiyo, habari njema hii kwa watu wa Kaskazini, Tanga na Watanzania kwa ujumla juu ya maboresho makubwa ya reli ya Kaskazini. (Makofi)
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa majibu mazuri sana ya Serikali. Kwanza, tunashukuru kwa kuona umuhimu wa Hospitali hii ya Magunga. Kwa kweli ni hospitali ya kimkakati kwa sababu ipo katikati ya Mji wa Korogwe, lakini kwenye njia kubwa ya kwenda Arusha na kuja Dar es Salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, nina swali moja la nyongeza, vipo vituo vya afya ambavyo ni vikongwe sana ambavyo vingine pia vilianza tangu wakati wa ukoloni kikiwemo Kituo cha Afya cha Mlalo ambacho na chenyewe kimechakaa sana kinahitaji ukarabati mkubwa. Je, ni lini Serikali sasa itakarabati kituo hiki? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Serikali hii ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka kipaumbele katika kukarabati hospitali zote chakavu ili ziweze kuwa na hadhi ya Hospitali za Halmashauri na kutoa huduma bora kwa wananchi. Kwa hiyo, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba, tayari tulishaainisha hospitali zote kongwe 50 kote nchini. Fedha zinaendelea kutafutwa kwa ajili ya kuzikarabati kwa awamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na Kituo cha Afya cha Mlalo ambacho ni chakavu, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, baada ya kumaliza ukarabati wa hospitali kongwe za halmashauri hizi 19 zilizobaki, tunakwenda kuanza kukarabati vituo vya afya vikongwe. Nimhakikishie Mheshimiwa Shangazi tutakipa kipaumbele Kituo cha Afya cha Mlalo ili kiweze kukarabatiwa na kiweze kutoa huduma bora kwa wananchi. Ahsante sana.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, pamoja na majibu ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza, swali la kwanza; kwa kuwa Serikali imekiri kwamba, kuna athari hasi kwenye michezo hiyo na kwa kuwa vijana wa kiume ndiyo waathirika wakubwa wa michezo ya kubashiri ambayo inachangia ukatili wa kudhuru mwili, ukatili wa kingono, ukatili wa kiuchumi na kusababisha hata matatizo ya afya ya akili. Je, Serikali iko tayari kupitia utoaji leseni wa makampuni haya ya kubashiri hasa yale ya mabonanza ambayo yametapakaa kote nchini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa michezo hii ya kubashiri mtandaoni inafanya vizuri, makampuni kama SportPesa, M-Bet na kadhalika na yako chini ya Wizara ya Fedha ambayo kimsingi ina majukumu mengi na inashindwa kuisimamia kwa ufanisi. Je, Serikali ipo tayari sasa kuihamisha Bodi ya Michezo kutoka Wizara ya Fedha ambayo kwa msingi wa hoja hii imeshindwa kuratibu eneo hili vizuri na kuipeleka kwenye Wizara ya Michezo ambayo kimsingi ndiyo inayosimamia eneo la burudani na sehemu hii ya michezo ya kubashiri ya mtandaoni ni sehemu ya burudani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Shangazi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumpongeza sana kwa kiasi alichofuatilia jambo hili na kimsingi najua dhamira yake ni kuimarisha maadili ya vijana wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali lake la kwanza, nataka nimwambie kwamba, Serikali ipo tayari kupitia na kuangalia uhalali na wale wote ambao watakuwa wanaendesha michezo hii, kinyume na taratibu na sheria zetu basi zitaondolewa leseni zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, Serikali imechukua ushauri wake wataalamu watakaa, wachambue, tukiona upo umuhimu au ipo haja ya kwenda huko, basi Serikali haitasita kuchukua hatua.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Mlalo tunazo sekondari 31 na sekondari za Mkundi, Mtumbi pamoja na Mtaya zote hizi miundombinu yake inaruhusu uanzishwaji wa madarasa ya kidato cha tano na sita. Je, Serikali iko tyari kuzifanyia kazi shule hizi ili ziweze kuwa na kidato cha tano na sita? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kumpongeza Mheshimiwa Mbunge. Mheshimiwa Mbunge amekuwa ni mahiri sana katika kuhakikisha anapambania changamoto za wananchi wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali hili. Kama shule hizi alizozitaja za Mkundi, Mtumbi na Mtale zina miundombinu hitajika basi hatua inayofuata ni Mkurugenzi kuweza kupeleka maombi Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa ajili ya kuomba kupandishwa hadhi kwa shule hizi kwa kidato cha tano na cha sita. Kwa hiyo naomba nichukue fursa hii kumwelekeza Mkurugenzi aweze kufanya tathmini katika shule hizi ili kuona kama zina miundombinu hitajika aweze kupeleka maombi ya kupandisha hadhi shule hizi ili ziweze kuwa shule za kidato cha tano na cha sita.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa mara ya kwanza naomba nikiri wazi kwamba Serikali imejibu maswali kwa ufasaha sana, swali hili limejibiwa kwa ufasaha na hali ndivyo ilivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kipekee nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa namna ambavyo amekuwa akiendelea kujibu kwa ufasaha maswali ya Wabunge hapa Bungeni, namuombea Mwenyezi Mungu aendelee kumbariki na fahamu zake zizidi kukua kwa kiwango kikubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nina swali moja la nyongeza. Barabara hii imekuwa ni mkombozi mkubwa haswa hivi karibuni tulipata mvua ambazo zilifunga barabara kubwa ya TANROADS, barabara hii ikawa ndiyo mkombozi. Lakini zipo kona kali ambazo magari makubwa kuanzia tani nne na kuendelea yanashindwa kupita kwa ufasaha.

Je, Serikali ipo tayari kurekebisha hizi kona takribani tatu ili barabara hii iweze kuwa na ufanisi zaidi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwanza kwa kupokea pongezi za Mheshimiwa Mbunge pia na mimi nimpongeze kwa utumishi wake uliotukuka kwa wananchi wake na hasa kwa sababu amekuwa akifuatilia sana masuala ya miundombinu ya barabara kwenye Jimbo lake.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la nyongeza alilouliza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge TARURA inatambua uwepo wa hizo kona kali tano, ambazo kimsingi zinazuia magari yenye zaidi ya tani nne kuweza kupita. Katika mwaka 2024/2025 Serikali imetenga milioni 328 kwa ajili ya kuanza kurekebisha kona mbili kati ya hizo kona tano ambazo zimebainika ni kali sana.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, katika kipindi cha mwaka 2024/2025 Serikali itatumia hizi fedha milioni 328 kupasua miamba na kuweka tabaka la zege ili magari yaweze yenye ukubwa wa kuanzia tani nne hadi 10 yaweze kupita. Kwa hiyo, nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge Serikali itahakikisha inaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya kuhakikisha inaboresha miundombinu na hasa katika barabara uliyoitaja Mheshimiwa Mbunge.(Makofi)