Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Jumaa Hamidu Aweso (4 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JUMAA H. AWESO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwanza kwa kunipa nafasi hii adhimu na mimi nichangie hotuba ya Waziri Mkuu iliyopo mbele yetu. Pia naomba niipongeze Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kazi kubwa inayoifanya. Lakini pia nimpongeze Dkt. John Pombe Magufuli ni jembe, tena ni jembe la palizi ambalo limekuja kwa ajili ya kuwasaidia Watanzania. Pia nimpongeze pia Waziri Mkuu kwa kazi kubwa anayoifanya, najua zipo changamoto nyingi lakini nasema bahari kubwa ndiyo ivukwayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchangia katika suala zima la uwezeshaji wa wananchi kiuchumi. Pamoja na mafanikio ya kukuza uchumi katika Taifa letu, pia kuna changamoto kubwa ya umaskini wa watu wetu, ninaiomba Serikali ihakikishe kwamba inatengeneza mazingira ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ili kuhakikisha kwamba inawasaidia katika kuepukana na umaskini uliokithiri katika jamii yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali yetu imeahidi katika Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi kutenga shilingi milioni 50 katika kila kijiji, hii itakuwa ni solution ya kuwasaidia Watanzania kwa sababu wapo mama lishe, wapo wajasiriamali wadogo wadogo wakiwemo bodaboda, kilio chao kikubwa ni mitaji, leo ukitaka mtaji unawaambiwa upeleke hati ya nyumba, kiwanja huna hiyo hati utaitoa wapi! Naamini kupitia Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya shilingi milioni 50 katika kila kijiji itasaidia sana Watanzania na wananchi wa Pangani.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ningependa nilizungumzie ni suala zima la kilimo. Watanzania wanategemea sekta ya kilimo, lakini kilimo kilichopo sasa, ukuaji wake ni wa kusuasua na kutegemea kudra za Mwenyezi Mungu. Ninaiomba Wizara ya Kilimo ihakikishe kwamba inajikita katika sekta ya kilimo cha umwagiliaji kwa sababu nchi yetu Mwenyezi Mungu ameijaalia, kuna mito na maziwa mengi tukijikita katika kilimo cha umwagiliaji nadhani suala la chakula kwetu litaisha kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mji wetu wa Pangani tumejaaliwa kuwa na Mto wa Pangani ambao unamwaga maji baharini, ninamwomba kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu Nchemba ahakikishe kwamba anatutengenezea scheme ya umwagiliaji ili kuhakikisha kwamba jamii yetu ya Pangani tunajikita katika kilimo cha umwagiliaji ambacho kitakuwa katika mazao ya mbogamboga ambayo itaweza kulisha Wilaya ya Pangani na Mkoa wa Tanga pia tunachangia Pato la Taifa katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ninapenda kulizungumzia ni suala zima la miundombinu ya barabara. Ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya barabara ni kichocheo cha maendeleo katika jamii yoyote. Lakini katika Wilaya yetu ya Pangani, barabara yetu imekuwa ni ahadi ya muda mrefu lakini mpaka sasa barabara hii imeweza kuzorotesha maendeleo katika jamii yetu ya Pangani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaiomba Serikali ya Awamu ya Tano iangalie kwa jicho la huruma kuhakikisha kwamba inajenga barabara hii ya Pangani, Tanga - Pangani - Sadani ili kuweza kuinua uchumi wa Pangani.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia Wilaya ya Pangani ilivyo ni kama kisiwa, ili uende Pangani lazima uende kwa makusudio maalum, unaenda kuzika au umesikia kuna kitchen party ndiyo watu waweze kwenda, madhara ya barabara hii ni makubwa, ingawa tumekuwa na fursa nyingi ya kiutalii, tuna uvuvi bahari kuanzia mwanzo wa mji mpaka mwisho wa mji. Ninaiomba Serikali itengeneze barabara hii ya Pangani ili kuhakikisha kwamba uchumi wa Pangani unapaa, badala ya kuwa pangoni, sasa tupae angani. Ninaamini Serikali hii kwa kazi inayofanya barabara hii itatengenezewa kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo nataka nilizungumzie ni sekta ya uvuvi. Jamii yetu ya Pangani tunategemea sekta ya uvuvi, Lakini uvuvi tunaoufanya ni wa kutumia zana duni na ukitaka kwenda kuvua lazima utegemee ndoano na chambo; hivi samaki akishiba huyo samaki utamvua wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Wizara ya Uvuvi iangalie sasa suala la uvuvi ili kuhakikisha kwamba inawasaidia wavuvi wa Pangani kwa kuwapatia pembejeo na zana na kuhakikisha tunatengenezewa bandari ya uvuvi kwa ukanda wa Pangani na Tanga ili kuhakikisha kwamba wavuvi wa Pangani wanafaidika ni rasilimali bahari tuliyonayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo napenda nizungumzie ni suala la afya. Huduma ya afya bora ni njia nzuri ya kuinua uchumi katika jamii yoyote, lakini katika sera ya Serikali inasema kwamba itajenga zahanati katika kila kijiji na kituo cha afya katika kila Kata, lakini Pangani tuna kituo kimoja tu cha afya na asilimia kubwa ya wananchi wanakaa ng’ambo ya Mto Pangani ambapo hutegemea huduma katika hospitali yetu ya Wilaya ya Pangani. Hospitali ya Wilaya ya Pangani bado haijajitosheleza, ukitazama x-ray hakuna, bado dawa ni shida, leo ukitaka x-ray mpaka uende Tanga.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaiomba Serikali ya Awamu hii ya Tano katika bajeti yake ihakikishe kwamba inashirikiana na sisi kuhakikisha tunatengeneza vituo vya afya vya ziada ili kuisaidia jamii yetu ya Pangani katika suala zima la afya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo ningependa kusema kwamba wapo watu ambao wanajigeuza bundi kukitakia Chama cha Mapinduzi mabaya kife, lakini nasema watakufa wao na ofisi zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi iliyofanya Chama cha Mapinduzi ni kubwa, ukiangalia katika Wilaya yetu ya Pangani mpaka mwaka 2005 tulikuwa na shule mbili tu za Serikali, lakini sasa hivi tuna shule saba hata mimi mtoto wa mama ntilie nimefika Chuo Kikuu, dogo hilo? Mungu atupe nini, hata Mwenyezi Mungu anasema katika vitabu vya dini waamma biniimati rabbika fahadith (zielezeeni neema za Mwenyezi Mungu kwa kushukuru). Sasa leo usiposhukuru kidogo unataka ukashukuru wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imefanya kubwa lakini ninachokiomba iendelee kutengeneza miundombinu ya elimu, vilevile kuboresha maslahi ya elimu kwa watumishi ili kuhakikisha wanafaidika na kazi wanazozifanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo sina maneno mengi ya kusema, naunga mkono hoja asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. JUMAA H. AWESO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwanza kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia hotuba iliyokuwepo mbele yetu. Lakini pia niungane na Mbunge wa Muheza kuhusu malalamiko yetu na masikitiko yetu kwa Wizara hii kwa namna mkoa wetu ulivyosahaulika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapata uchungu leo kuona baadhi ya maeneo ya wenzetu yanatekelezewa miradi mbalimbali lakini sisi Mkoa wetu wa Tanga tunasahaulika. Leo tunaona wenzetu wanashangilia wanakaa safu za mbele lakini sisi mkoa wetu wa Tanga tunawekwa katika jiko kazi yetu kusugua masufuria na sisi Mkoa wetu lazima atutizame kwa jicho la huruma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi watu wa Tanga tumekuwa watu wa kupembuliwa tu. Ukiangalia bandari tunapembuliwa, ukiangalia sijui nini tunapembuliwa hivi sisi ni lini tutatekelezewa miradi yetu ya maendeleo? Kwani tumemkosea nini Mwenyezi Mungu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumza haya kwa masikitiko makubwa kwa kuwa kila kukicha sisi tumekuwa watu wa kupewa ahadi tu. Wali ni mtamu sana kwa maini lakini ukikaa sana unakuwa kiporo na kiporo kikaa sana kinachacha na kikichacha kinaumiza tumbo, leo wananchi wa Tanga tunaumizwa kutokana na kutotelekelezwa miradi mbalimbali, inakuwa kazi ya kusuasua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine nataka nizungumzie kwa masikitiko makubwa barabara yetu ya Pangani – Tanga – Saadani. Barabara hii mimi tangu sijazaliwa, nimezaliwa, nimesoma msingi, sekondari mpaka Chuo Kikuu leo nimefika na mimi nimekuwa Mbunge lakini barabara yetu tumekuwa watu wa ahadi tu. Amekuja Mheshimiwa Rished miaka 15 tunaambiwa itajengwa, Mheshimiwa Pamba akaambiwa ipo kwenye upembuzi, mimi leo naambiwa pia barabara yetu African Development Bank wameonyesha nia sasa hii nia inaisha lini ili barabara hii sasa itengenezwe? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Pangani tupo pangoni, tuna fursa nyingi katika Wilaya yetu ya Pangani, leo tuna Mbuga Saadani ambayo ni kichocheo kikubwa cha kiutalii, ni mbuga pekee katika Afrika ambayo imeungana na bahari. Barabara hii ya Tanga - Pangani ndiyo inaunganisha na Mkoa wa Tanga na nchi jirani ya Kenya, tukijenga barabara Tanga - Pangani - Saadani tutaweza kuinua sekta ya utalii katika Wilaya ya Pangani na Mkoa wa Tanga. Lakini kwa kuwa tuna mahusiano vizuri na Zanzibar na Mombasa, Kenya ina maana tutainua sekta ya utalii katika Wilaya ya Pangani, lakini pia tutaweza kunyanyua sekta mbalimbali za kiutalii, uvuvi na kilimo kutokana na barabara hii ya Tanga - Pangani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sina maneno mengi sana ya kusema, ila nilikuwa namwomba Waziri katika majumuisho yake atuambie amejipanga vipi kuhakikisha kwamba atatutekelezea barabara hii ya Tanga - Pangani, Bandari ya Tanga pamoja na reli ya kutoka Tanga - Arusha na Musoma ili tuchangie katika pato la Tanzania.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. JUMAA H. AWESO: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru, ila nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Profesa Sospeter Muhongo pamoja na timu yake kwa kazi nzuri na uwajibikaji uliotukuka katika kuwatumikia wananchi wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nijielekeze kuchangia katika Usambazaji wa Umeme Vijijini (REA) katika hotuba iliyokuwepo mbele yetu. Nchi yetu ina malengo ya kuwa nchi ya viwanda na kufikia katika azma ya uchumi wa kati. Pamoja na jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali, lakini ukweli ni kwamba, tuna changamoto kubwa ya vikwazo vya uchumi kimojawapo ni kukosekana kwa nishati ya uhakika ya umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, asilimia kubwa ya wananchi wetu wanaoishi vijijini wanakosa huduma hii muhimu ya nishati ya umeme ambao ni kichocheo kikubwa cha maendeleo ya watu wetu. Niiombe Serikali iongeze kasi ya usambazaji na kuiongezea fedha za kutosha Wizara ya Nishati kuhakikisha inasambaza umeme kwenye vijiji vingi na kwa wakati muafaka pia, kukamilisha miradi ya umeme ambayo haijakamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukisambaza umeme vijijini tutawezesha wakulima kuongeza thamani ya mazao kwa kufungua viwanda vidogo vidogo, tukisambaza umeme vijijini wavuvi watahifadhi samaki; pia, itawawezesha wafugaji kuhifadhi nyama kwa muda mrefu, sambamba na kuongeza ajira kwa vijana kwa kuanzisha shughuli mbalimbali za kijasiriamali; mfano saluni za kike na za kiume, uuzaji wa vinywaji baridi, viwanda vya kuchomea vyuma na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, nitumie nafasi hii kumwomba Mheshimiwa Waziri katika bajeti hii ahakikishe vijiji vifuatavyo katika Jimbo la Pangani vinapatiwa umeme huu wa REA; Kigurusimba Misufini, Mivumoni, Matakani, Kidutani, Jaira, Kikokwe, Langoni, Mtango, Mtonga.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumalizia, tunaomba Wizara iwe na mkakati maalum wa kuunganisha umeme katika shule za sekondari za kata, zahanati na vituo vya afya, ili kuimarisha huduma za jamii za wananchi wetu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JUMAA H. AWESO: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na kuniwezesha leo kuchangia hotuba iliyoko mbele yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nitumie nafasi hii kumpongeza Waziri Profesa Maghembe kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya katika Wizara hii, kwa kweli anaitendea haki. Waswahili wanasema mzigo mzito mpe Mnyamwezi, naamini Wizara hii Mnyamwezi ni Mheshimiwa Profesa Maghembe na kazi anaifanya. Pamoja na changamoto kubwa anazokabiliana nazo, namwambia songa mbele bahari kubwa ndiyo ivukwayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sina maneno mengi sana ila kubwa nataka nijikite katika suala zima la mambo kale. Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye hazina kubwa ya mali kale. Baadhi ya mali kale zilizopo ni pamoja na majengo ya zamani ambayo yalijengwa na matumbawe katika Miji ya Pwani ikiwemo Pangani, Bagamoyo, Kilwa na Kilindi lakini Serikali haijawekeza katika utalii wa mali kale hizi. Serikali inapoteza mapato mengi kwa kutowekeza kwenye utalii huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe katika bajeti hii itenge fedha za kutosha kuhakikisha kwamba inakarabati majengo yale ili yawe katika hadhi na kuongeza utalii katika mali kale na kuongeza pato la Taifa. Hii iende sambamba na kuajiri watumishi wanaohusiana na mambo ya kale ili kuhakikisha kwamba tunaongeza pato la Taifa katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta hii ya maliasili na utalii ni muhimu na mhimili wa maendeleo katika Taifa letu, lakini mchango wake siyo mkubwa pamoja na fursa zilizopo. Nchi yetu imejaaliwa kuwa na vivutio mbalimbali kama vya wanyamapori na hifadhi mbalimbali, lakini mchango wake umekuwa ni mdogo sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niiombe Serikali itenge fedha na kuhakikisha kwamba inakuwa na mpango mkakati wa kuvitangaza vivutio hivi ili viende kuchangia pato la Taifa. Biashara ya utalii inategemea matangazo. Tunapovitangaza vivutio hivi kwa kasi kubwa, ndiyo tunapoongeza watalii kuja kuvitembelea na kuchangia pato la Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya yangu ya Pangani nataka nizungumzie mbuga ya Saadani. Mbuga ya Saadani ni miongoni mwa mbuga pekee Afrika ambayo imepakana na bahari. Mbuga hii inapata changamoto kubwa ya miundombinu mibovu ya barabara. Nimwombe Mheshimiwa Waziri, ni muda muafaka sasa akae na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi kuhakikisha kwamba wanaiangalia barabara hii ya Tanga - Pangani - Saadani na kuhakikisha inajengwa kwa kiwango cha lami ili kuweza kuwavutia watalii kutoka Kanda ya Kaskazini, Zanzibar pamoja na nchi jirani ya Kenya kuja katika Wilaya ya Pangani na kuinua sekta hii ya utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sina mengi sana ya kusema ila kikubwa tu nimwombe Mheshimiwa Waziri aendelee kufanya kazi na kuweza kuwatumikia Watanzania na sisi kama viongozi vijana tunaendelea kumuunga mkono kuhakikisha kwamba anafikia azma iliyowekwa katika Jamhuri yetu ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.