Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Stephen Hillary Ngonyani (29 total)

MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona. Kwa kuwa tatizo la Bukene linafanana kabisa na Korogwe Vijijini hasa kwenye Kata ya Kizara. Mwaka 2012 tulimchukua Naibu Waziri hapa alikwenda mpaka kule akawaahidi wananchi wa Kizara kwamba mwishoni mwa mwaka 2012 mnara utapatikana. Cha kushangaza mpaka leo hii hakuna cha mnara wala namna ya kupata mnara. Je, ni lini sasa Serikali itawapelekea wananchi wa Kizara mnara?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tutagawa fomu kwa ajili ya Waheshimiwa Wabunge wote ambao wanahitaji mawasiliano kwenye vijiji vyao ili na sisi tuwe na database ya uhakika. Pia nataka kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba kijiji chake kama nilivyosema mwaka huu kitapelekwa mawasiliano, kupitia kwa kampuni ya Viettel au Halotel Tanzania. (Makofi)
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na yenye maana. Mwaka jana mwezi wa Sita niliomba Serikali iende mpaka Korogwe ikaangalie maeneo ambayo hayaendelezwi na Serikali iliniahidi kwamba ingekwenda kule na kukagua mashamba ambayo hayaendelezwi ili ufanywe utafiti wa kuwagawia wananchi, hadi leo hii na mimi nilienda kwenye mikutano ya hadhara na kuwaambia wananchi kwamba Naibu Waziri atakuja kuangalia mashamba ambayo hayaendelezwi na watu wakakipa sana kura Chama cha Mapinduzi kwa kujua kwamba viongozi wanafika.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini cha kushangaza mpaka leo hii hawajafika na badala yake nasikitika sana baadhi ya Watumishi wa Halmashauri wanaleta habari ambazo siyo njema, zisizoweza kumsaidia mtu wa aina yeyote. Naomba Waziri, ni lini mimi na wewe tutakwenda mpaka Korogwe Vijijini ukaone huku kudanganywa kwamba ni shamba moja katika mashamba 17 yanayozunguka Jimbo langu hayajapatiwa ufumbuzi.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu niseme kwa Waheshimiwa Wabunge wote kwa kupitia swali la Mheshimiwa Ngonyani.
Mheshimiwa Naibu Spika, ikiwa kama kila Mbunge atataka Waziri afike kwenye eneo lake na kufanya utambuzi wa mashamba zoezi la ukaguzi wa mashamba haya yasiyoendelezwa halitafikia ukomo. Hata hivyo, najua wazi kwamba ni jukumu la Halmashauri zetu husika ambapo na Wabunge ni Wajumbe kuweza kuyatambua hayo mashamba na Wizara inapofika pale, inakuja baada ya kuwa imepata taarifa ili kujihakikishia kwamba kilicholetwa ni sahihi, tutafika pia kukagua, lakini hatuwezi kufanya ile kazi ya mwanzo, unakwenda kila eneo kukagua halafu ndiyo uweze kuchukua hatua, maana utashindwa kuchukua maamuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lazima Halmashauri husika ilete mapendekezo halafu Mheshimiwa Waziri apeleke kwa Mheshimiwa Rais kwa ajili ya ubatilisho. Maamuzi ya matumizi yanafanyika ndani ya Halmashauri kwa sababu ndiyo wenye mamlaka pia ya kugawa mashamba hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe tu Waheshimiwa Wabunge, kwa sababu zoezi hili Mheshimiwa Waziri alishalitolea maelekezo na alitoa barua katika maeneo yote, ni jukumu letu sasa kuanza kukagua yale mashamba tuliyonayo ambayo Halmashauri zetu imeyatoa. Hivyo, Wizara inarahisisha kazi baada ya kuwa imeshapata kutoka kwenu, sisi tutakuja kutambua ili sheria zisikiukwe na kuleta malalamiko kwa Wizara.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Mheshimiwa Ngonyani iwapo itabidi, basi tutafika, lakini kazi hii ni kazi ya Halmashauri.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti,ahsante, kwa kuwa tatizo la Tunduru huko linalingana kabisa na Korogwe Mjini. Ni lini Serikali itaifanya Hospitali ya Magunga iwe Hospitali Teule?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Hospitali ya Korogwe Mjini, juzi nilipita pale katika ziara yangu wakati naenda Arusha nilitembelea Hospitali ile na nikaona kwamba congestion ya watu wa pale na mahitaji yake na kwamba Wilaya iko barabarani, bahati nzuri Naibu Waziri wa Afya juzi alifika pale hali kadhalika Waziri wa Afya alifika pale, naona kwamba haya yote nimeona ni kipaumbele hospitali ile kuwa Hospitali yetu ya Rufaa ya Mkoa ili mradi kufanya hivyo. Ninaamini mchakato unaohitajika ukikamilika na mahitaji yote hasa yanayotakiwa kwamba kuifanya hospitali ya Mkoa kukamilika basi nadhani Serikali haitosita kuhakikisha hospitalki ile inakuwa Hospitali ya Mkoa kwa vigezo vitakavyokamilika na kutokana na maelekezo kutoka Wizara ya Afya.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri Jafo nataka kuongezea kwenye suala la muundo na mgawanyo na set up kwa kuzingatia maeneo katika utoaji wa huduma ya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeongea na Waziri wa Afya, tumeona liko tatizo la catchment areas namna zilivyowekwa na uwiano wa vituo vya afya, hospitali za Wilaya, hospitali za Mikoa na ziko nyingine ambazo maombi yako mengi sana wakiomba zipandishwe madaraja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ingawa utaratibu unaanzia huko chini kuanzia kwenye Kata, kwenye Wilaya, kwa maana ya Halmashauri, hata hivyo tunaona haja ya Serikali kukaa na kufanya sensa maalum ya kuweka mfumo wa utaratibu mzuri ili tuende kwa utekelezaji ambao utastahiki. Kwa mfano, haiwezekani ukakuta catchment area ya kata karibu nne kukawa hakuna kituo cha afya, lakini kituo cha afya kimeelekea upande mmoja. (Makofi)
Kwa kuwa tuna uchache wa rasilimali lakini iko haja ya kufanya sensa hiyo ili baadaye tuje na mpango kazi maalum kwa kushirikiana na Wizara ya Afya tutakapopanga mpangilio mzuri wa vituo vya afya, Hospitali za Wilaya na Hospitali za Mikoa kulingana na mahitaji ya wananchi.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante. Kwanza nikupongeze kwa kuzaliwa juzi Muhimbili na Mama Ulega, Mungu akubariki sana.
Swali langu ni kwamba, kwa kuwa baraza la ardhi la Wilaya ya Korogwe linafanya kazi katika mazingira magumu. Kuna kesi nyingi za kutoka mwaka 2009 mpaka leo hazijamalizika.
Je, ni lini Serikali itaongeza Watumishi pale ili kesi zile ambazo zimekaa kwa muda mrefu katika Baraza la Ardhi la Korogwe ziwe zimepata ufumbuzi wa haraka ili wananchi waone umuhimu wa Serikali yao?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, hii ndiyo sababu tumetenganisha yale Mabaraza na kuunda Baraza jingine la Lushoto, kwa sababu kesi nyingi zilizokuwa zinakuja Korogwe ni za Lushoto na Wilaya nyingine. Kwa hiyo tumeunda Baraza la Lushoto, tutakwenda kuunda Baraza jingine la Kilindi. Kwa kufanya hivyo tutakuwa tumepunguza mzigo wa Korogwe na hivyo Baraza lile litakuwa limepunguziwa mzigo wa kuhudumia.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tukichukua hatua hizo Baraza lile litahudumia watu wachache zaidi na hasa wananchi wa Korogwe.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Katika Jimbo la Korogwe Vijijini kulitokea kampuni ambayo sio mali ya Serikali, UNDP, ilinipa milioni 243 nikachimba visima tisa. Baada ya kuchimba visima hivyo walikuja wataalamu wa Serikali wakasema sehemu hizi tukichimba tutapata maji safi, lakini cha kusikitisha baada ya kuchimbwa maji yale yalivyokwenda Serikalini kuleta majibu nikaambiwa maji yale hayafai kutumika kwa binadamu na hela tayari zimeshatumika shilingi milioni 243.
Je, hii hasara ambayo wameipata wananchi wa Jimbo la Korogwe Vijijini italipwa na nani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani Naibu Waziri Wizara ya Maji siku ile kama mtaalam wa maji, amezungumza hapa kwamba, mara nyingi sana taaluma zetu hizi za maji wakati mwingine unaweza kufanya survey, lakini hujui kiwango gani cha maji utakipata! Lakini sio kiwango cha maji, hata ule ubora wa maji wa kiasi gani!
Mheshimiwa Naibu Spika, na ndio maana ukiangalia, kwa mfano katikati tulikuwa na mradi kutoka China, tulipata visima kwa Wilaya ya Kilosa na Wilaya ya Kisarawe. Katika visima vilivyochimbwa ikaonekana kwamba kiwango cha madini ya chuma yako mengi zaidi ya madini ya aina mbalimbali maji yale hayafai kunywa! Halikadhalika katika eneo lako, kwanza nikupongeze kwa sababu umefanya initiative ya kupata watu ambao wanakusaidia kuchimba maji, maji yamechimbwa, lakini ubora wa maji bado hauko sawasawa! Naomba nikwambie itakuwa ni jambo la ajabu kusema kwamba gharama ile italipwa na nani!
Mheshimiwa Naibu Spika, itakuwa ni jambo la ajabu ni kwa sababu, maji yamepatikana, lakini mtaalamu wa maji hata anavyofanya survey hawezi kusema maji haya nikiyatoa hapa yatakuwa matamu au ya chumvi! Jambo hilo bado ni gumu na wataalam wote wanakiri hivyo. Kwa hiyo, nini cha kufanya; cha kufanya ni kwamba kwa sababu visima vile maji hayajawa na ubora uliokusudiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni jukumu la Serikali sasa tuweke mipango mipana jinsi gani tutawasaida wananchi wa Jimbo lako waweze kupata huduma huduma ya maji kama sera ya maji inavyoelekeza hivi sasa kwamba wananchi waweze kupata maji. Mbunge nakujua kama ni mpiganaji na hili litawezekana katika maeneo yetu.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Namshuruku Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri yenye matumaini kwa wananchi wa Mombo lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mradi huu sasa hivi una muda mrefu na tatizo la maji la Mombo ni la muda mrefu na wananchi wameanza kukata tamaa; na kwa kuwa halmashauri mbili zilishakubaliana, ya Bumbuli na Korogwe kwamba maji yale yapitie katika vile vijiji vinavyolinda chanzo cha maji, ni wakati gani wananchi wale wa Korogwe Vijijini na Bumbuli wataanza kupata maji?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa sasa hivi Serikali imetutengea shilingi bilioni 1.9 kwa ajili ya mradi wa maji wa Korogwe Vijijini; kuna mradi wa maji wa Bungu, mradi huu hatukuwa tunatumia hela za Serikali, mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yalitumia hela zao kukamilisha mradi huu ambao ulikuwa ni kwa ajili ya vijiji saba. Kati ya vijiji hivyo saba vijiji vinne tu ndivyo vimepata maji. Serikali iliombwa shilingi milioni 410 ili mradi huu ukamilike lakini mpaka sasa hivi hela hiyo haijapatikana. Vijiji ambavyo vimekosa ni Mlungui, Kwemshai na Ngulwi. Naomba sasa Serikali mtenge hela za dharura ili tukakamilishe mradi huo ambao haukutumia hela za Serikali, ni mashirika binafsi yaliamua kujenga mradi huo. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Nganyani kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza linaonesha Mheshimiwa Mbunge unawapenda wananchi wako na unataka hatua za haraka kuhakikisha kwamba wanapata maji. Wizara ya Maji na Umwagiliaji, wewe mwenyewe Mheshimiwa Mbunge na halmashauri yako naomba tushirikiane, tukutane ili tuone tunafanyaje kuhakikisha kwamba tunachukua hatua za haraka ikiwa ni pamoja na fedha ambazo umetengewa katika bajeti inayoanza Ijumaa tarehe 1 Julai, kuhakikisha wananchi watapata maji kwa haraka.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali namba mbili, kuhusu Mradi wa Maji wa Bungu ambao umefadhiliwa na marafiki zetu lakini hawakuukamilisha. Katika vijiji vilivyotarajiwa ni vijiji vinne tu ambavyo vimepata maji vingine bado, tufanyeje?
Naomba pia hili tushirikiane, Mkurugenzi wa Halmashauri atuletee taarifa. Tumeahidi katika bajeti inayokuja, miradi yote iliyokuwa inaendelea, ili mradi tu ililenga kuwapatia wananchi maji, hata kama ilikuwa inafanywa na wewe mwenyewe na umefikia ukomo tupe taarifa Serikali itatoa hela ili tuweze kukamilisha miradi hiyo wananchi wapate maji.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Tanzania nzima ili iwe barabara ni lazima kuwepo na madaraja. Katika Wilaya yangu ya Korogwe Vijijini wakati wa mvua barabara za Mkoa zote zimevunjika madaraja na hakuna magari yanayoweza kupita katika barabara ya Mkoa kutoka Korogwe kwenda Mnyuzi kwa kupitia Muheza; na barabara ya kutoka Korogwe kwenda Magoma kwa kupitia Maramba hadi Daruni.
Je, Serikali hamna mpango wa dharura kutusaidia madaraja haya ambayo wananchi wamepata taabu kwa muda mrefu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, nilishasema huko nyuma kwamba baada ya mvua kwisha kipaumbele cha kwanza ni kufungua mawasiliano katika yale maeneo ambayo yalikuwa yamekatika na tulishawaelekeza viongozi wa TANROAD Mikoani kwamba wahakikishe tunafungua mawasiliano pale ambapo yalikatika. Naomba Mheshimiwa Stephen Nganyani tuwasiliane pamoja na TANROAD Mkoa ili tuone kitu gani kinaweza kufanyika kutekeleza kile ambacho nilikisema humu Bungeni.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa kuwa, Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne aliahidi kujenga barabara ya lami kilometa 1.5 katika Mji wa Mombo na Rais wa Awamu ya Tano ameahidi vilevile kujenga barabara hiyo kilometa moja, lakini cha kushangaza mpaka leo hii hela hazijaingia katika Mfuko wa Mkoa. Je, ile barabara ambayo imeahidiwa na Marais wawili itajengwa lini kwa kiwango cha lami kule Mombo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, naomba kumhakikishia kwamba ahadi za viongozi wetu, Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne na Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, tuliopewa dhamana tutaitekeleza.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona. Kwanza nianze kwa kuishukuru Wizara ya Ardhi kwa kazi nzuri wanayoifanya. Kwa kuupendelea Mkoa wa Tanga, Wizara ya Ardhi ilitoa shilingi milioni 50 kwa ajili ya kuangalia mashamba ambayo hayaendelezwi lakini fedha ziko mikononi mwa mtu na Korogwe hawajafika na hawajafanya utafiti wowote na badala yake wanakwenda pale kwa ajili ya kumdanganya danganya tu Waziri wa Ardhi. Je, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari twende wote mpaka Korogwe tukaangalie yale maeneo ambayo hawajapewa wananchi na yameachwa kama misitu ili atusaidie kutatua tatizo la wananchi wa Korogwe?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Profesa Maji Marefu ambaye ni mtani wangu, amekuwa akifuatilia sana suala hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spka, ni kweli katika utoaji wa pesa kwa ajili ya kubaini mashamba ambayo pengine hayajaendelezwa ili tuweze kuyatwaa, Korogwe walipewa shilingi milioni 50 kwa ajili ya kazi hiyo. Cha kusikitisha ni kwamba, pamoja na pesa ile kupelekwa lakini kazi iliyokusudiwa ni kama haijafanyika kama tulivyotarajia. Hata Waziri alipokwenda alipewa taarifa za maeneo mengine na haya mashamba yaliyoko Korogwe taarifa ile haukutolewa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niseme kupitia Bunge lako hili, Wizara inapotoa pesa kwa nia njema ya kutaka kumaliza migogoro ya watu iliyoko katika maeneo hayo, tunaomba sana wale Maafisa wanaopokea hizo pesa wawatendee haki wananchi ambao wamekuwa na kero ya namna hiyo. Kwa hiyo, kwa suala la kutaka kwenda kujiridhisha katika hilo na kwa sababu Wizara ilishapeleka pesa, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Stephen Ngonyani kwamba tutakuwa tayari kwenda kufuatilia suala hilo ili tuweze kujua zile shilingi milioni 50 zimetumikaje ili hatua za kinidhamu ziweze kuchukuliwa ikiwa kama kulikuwa na ufujaji wa pesa.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Tatizo la Maswa Mashariki linalingana kabisa na tatizo la Mji wa Mombo, katika Halmashauri ya Korogwe Vijijini. Rais wa Awamu ya Nne aliaahidi kwamba atajenga kiwango cha lami barabara kilometa 1.5 na Rais wa Awamu ya Tano alivyokuja vilevile alitoa ahadi hiyo kwamba atatekeleza ahadi ya ambayo imeachwa na Rais Mstaafu. Lakini mpaka leo hii hakujafanyika kitu cha aina yoyote, je, Serikali inasemaje kuhusiana na Mji wa Mombo ambao wananchi wake wanategemea sana mpaka sasa hivi kungekuwa na barabara ya lami lakini hakuna kinachoendelea
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli ahadi hii ilikuwa ni ahadi ya Mheshimiwa Rais lakini tunaona kulikuwa na faraja kubwa sana, wakati Rais Mstaafu anatoa ahadi hiyo Waziri wake wa Ujenzi ni Dkt. John Pombe Magufuli. Then katika uchaguzi wa mwaka huu sasa yule aliyekuwa ni Waziri wa Ujenzi sasa hivi ndio Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kama tukisema ndugu zetu wa Korogwe Vijijini ni watu ambao mmelamba dume katika mchezo wa karata. Naomba nikuambie hii ahadi ya Rais itakuwepo pale pale na ndio maana ukiangalia katika harakati hizo juzi juzi nilipita Korogwe kwa mama yangu, jinsi ujenzi wa kituo kikubwa cha mabasi kinavyofanyika. Maana yake ni kazi kubwa inafanyika na siyo kituo cha mabasi maana yake ni suala zima la ujenzi wa miundombinu ya barabara ya lami. Maana yake mambo haya yote katika Mkoa wa Tanga kama ilivyoahidiwa na Mheshimiwa Rais kwa kweli yatatekelezwa tufanye subira tu.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza niishukuru Serikali kwa kutoa maneno mazuri ndani ya Bunge hili ila nilikuwa na swali moja la nyongeza. Kwa kuwa suala la utalii ni suala muhimu sana kwa Watanzania na kwa kuwa Zanzibar na Pemba na Tanga watalii wengi walikuwa wanakwenda kwa ajili ya kuogelea ndani ya bahari. Pia kwa kuwa tatizo hili limewaathiri kwa kiwango kikubwa sana watalii wanaotoka nje kwa ajili ya kuja kufanya utalii katika eneo la pembezoni mwa bahari. Je, Serikali inaweka hatua gani ya dharura kwa kuhakikisha suala hili linachukuliwa maamuzi ya haraka ili watalii waendelee kuwepo katika eneo la bahari?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa biashara au uvuvi wa kutumia mabomu unaathiri sana biashara ya utalii na hususani katika Ukanda wa Pwani ambao Mheshimiwa ametaja. Kama nilivyosema Serikali imeamua sasa kuchukulia suala la uvuvi haramu kwamba ni suala la kiusalama; niwafahamishe tu Waheshimiwa Wabunge kwamba kuna uhusiano wa karibu sana kati ya ugaidi, uvuvi wa kutumia mabomu lakini vilevile kutumia mabomu au vilipuzi ambavyo havina leseni katika machimbo yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Serikali imeamua kuchukulia hili suala kwamba sio suala la uvuvi; kwa sababu hamna uvuvi unaitwa uvuvi wa mabomu, pale mtu anapotumia mabomu kuvua hapo anakuwa anafanya maangamizi ya samaki na viumbe vingine baharini na sio uvuvi. Kwa hiyo, tumeamua kulichukulia kwamba ni suala la usalama na ndiyo maana kwa sasa halishughulikiwi moja kwa moja au peke yake na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi lakini vile vile linashughulikiwa na vyombo vya usalama.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kufanya hivyo; Serikali imeanzisha vituo vitano vya kudhibiti uvuaji wa samaki wa aina hii na moja kati ya vituo iko Tanga na Pemba ili kuhakikisha kwamba udhibiti unafanyika wa karibu sana. Naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tokea utaratibu huu uanze mwaka 2015 tayari kuna maendeleo makubwa sana na uvuaji wa kutumia mabomu umepungua kwa kiasi kikubwa. Kwa hiyo, Serikali itaendelea kuhakikisha kwamba linafanyiwa kazi ili liweze kwisha moja kwa moja.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Kwanza nianze kwa kuipongeza Serikali kwa juhudi zake kubwa mnazofanya za kusambaza mawasiliano nchi nzima.
Kwa kuwa tatizo la mawasiliano katika Jimbo la Korogwe Vijijini ilikuwa ni Kata nyingi hazina mawasiliano; na kwa kuwa Serikali hii ni sikivu; kuna Kata ambazo hazina mawasiliano kabisa, kwa mfano, Kata ya Dindira katika Kijiji cha Kwefingo, Kata ya Chekelee katika Kijiji cha Bagai, Kata ya Mkalamo katika Vijiji vya Kweisewa na Toronto, Bungani na Kata ya Kerenge katika Kijiji cha Makumba:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini vijiji hivi navyo vitajengewa minara ili nao wanufaike na Serikali hii ya Awamu ya Tano?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Stephen Hillary Ngonyani (Profesa Maji Marefu) kwa kunijulisha kwamba katika jibu langu la msingi la ujenzi wa mnara, ni kwamba kumbe tayari kazi imekamilika na umeme unawaka. Kilichobaki ni kutoa taarifa kwetu ili na sisi Wizara rekodi yetu tuweze kuirekebisha kuonesha kwamba umeme umewaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Profesa Maji Marefu na namhakikishia kwa kazi hii kubwa anayoifanya ya kufuatilia masuala haya na kutupa taarifa za uhakika katika maeneo mbalimbali ya eneo lake, kwa mfano: katika Kata ya Kerenge anafahamu mnara umejengwa katika Kijiji cha
Makumba, lakini vile vile Kata ya Dindira mnara umejengwa katika Kijiji cha Kwefingo ambacho ndiyo Makao Makuu ya Kata; anafahamu vile vile Kata ya Chekelei katika Kijiji cha Kwamkole nako mnara umejengwa; na mwisho Kata ya Mkalamo, Vijiji vya Kweisewa na Toronto Bungani, Minara imejengwa.
Hii yote hii ni kwa sababu ya juhudi zake za kufuatilia kwenye Makampuni yanayojenga minara; siyo Wizarani tu, bali na kwenye Makampuni yanayojenga minara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Ngonyani na naomba ajaribu kuambukiza hiki kitu anachokifanya katika eneo lake kwa Waheshimiwa Wabunge wengine na hasa mimi mwenyewe.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona. Tatizo la Lushoto linalingana kabisa na Korogwe Vijijini hasa kwenye Mji Mdogo wa Mombo. Serikali kwa kupitia Benki ya Dunia ilitenga milioni 900 kwa mradi wa maji ambao unakwenda kutoka Vuga mpaka Mombo kwa kupitia Mombo kwenda Mlembule. Mradi huu umekamilika kwa asilimia 80, tatizo ni kwamba, wananchi wanaolinda chanzo cha maji katika Wilaya ya Bumbuli au katika Mji wa Bumbuli ambao wanatoka Vuga walikuwa wanaomba wapatiwe maji na sasa hivi Serikali iliahidi kwamba, wale wananchi wanaolinda chanzo cha maji watapatiwa maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini mradi huu wa Mombo ambao Serikali imetumia gharama zaidi ya milioni 900, lakini mpaka sasa hivi haujakamilika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Maji na Umwagiliaji katika Sera yake na katika mipango yake imeweka mpango kwamba, Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2016/2017 kwanza inakamilisha miradi iliyokuwa inaendelea kabla haijaingia katika miradi mipya. Kwa hiyo, mradi wako Mheshimiwa Mbunge ambao umeuita ni mradi wa Benki ya Dunia na imebakia kidogo mradi huo utakamilika, lakini pia ni sambamba na kuwapelekea maji wananchi wa eneo ambalo ni chanzo cha maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yetu imepanga kwamba, maeneo yote ambayo maji yanatoka katika lile eneo, basi maji lazima na huko yapatikane. Kama utaratibu huo haukuwepo, naomba Mheshimiwa Mbunge pamoja na
Halmashauri washauriane ili mwaka wa fedha 2017/2018 tuweze kutenga fedha kuhakikisha wale wananchi wa kwenye chanzo cha maji wanapata maji.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru sana Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri sana yenye matumaini kwa wananchi wa Jimbo la Korogwe Vijijini, pia nimpongeze kwa safari alizofanya katika Jimbo langu. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa Naibu Waziri umefika na kuliona shamba hili ambalo limetelekezwa zaidi ya miaka 22, ni kwa nini sasa Serikali isiwakabidhi wananchi wakalitumia kwa shughuli zao mbadala? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa mashamba mengi yamechukuliwa mikopo kwenye mabenki na sasa hivi yametelekezwa, nini kauli ya Serikali kwa yale mashamba ambayo yalichukuliwa mikopo, hayaendelezwi na yametelekezwa mpaka muda huu?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza anataka kufahamu ni lini Serikali itakabidhi sasa wananchi hao mashamba hayo ambayo yametelekezwa muda mrefu ili waweze kuyatumia.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, ni kwamba utaratibu ili uweze kumnyang’anya mtu huyu ni lazima ule utaratibu wa kisheria ufwatwe, na ndiyo maana nimesema katika hatua za awali ambazo Serikali imechukua ni kutoa notice kwa hawa ambao wametelekeza mashamba na siyo huyo mmoja tu, yapo mashamba zaidi ya 22 ambapo baada ya ziara yangu wamepewa notice.
Kwa hiyo, niseme tu kwamba taratibu za Serikali zinaendelea, muda ule ukishakwisha ni jukumu la Halmashauri husika kuweza kupendekeza kwa Mheshimiwa Waziri ili na yeye aweze kumshauri Rais kubatilisha, ni lazima ule mchakato wa kisheria utimizwe. Kwa sababu wenzetu wa Korogwe wameshaanza nina imani litafikia mahali pazuri.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili anasema mashamba mengi yamekuwa mapori lakini pia inafahamika kwamba mengine yamechukuliwa mikopo mabenki na nini sasa Serikali inasema nini.
Mheshimiwa Spika, niseme haya yamekuja kuahamika na kuthibitika rasmi baada ya Wizara yangu kuanza kutoa ilani kwa wale ambao wameyatelekeza mashamba yao, lakini kama Serikali tunachofanya sasa ni kuhakikisha tunafanya kazi sambamba na mabenki ili fedha za umma zisipotee, kwa sababu dhamana za hati zile zimewekwa na zimechukuliwa mikopo, lakini pengine mikopo ili haikwenda kunufaisha katika yale maeneo.
Kwa hiyo, jukumu letu sisi tunalofanya, pamoja na ilani zinazotolewa katika mashamba haya, lakini bado kama Serikali tunafanya kazi kwa karibu sana na mabenki ili kuhakikisha kwamba kama zile dhamana walizokuwa wameweka pengine zinakwenda kubatilishwa sasa tujue ni namna gani yale mabenki yataweza kupata pesa zake. Kwa hiyo hili tunalifanya kwa uangalifu ili kuona kwamba pesa za Umma hazipotei lakini pia haki ya wananchi au ya wamiliki wale pia inakwenda sambamba kisheria ili tusijikute kwamba tumekwenda nje ya utaratibu. (Makofi)
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa tatizo la Busokelo linalingana kabisa na Korogwe Vijijini. Kwanza nianze kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri wanayonifanyia kule Korogwe kwa kujenga daraja la Magoma. Barabara ya kutoka Old Korogwe kwenda Maguzoni ni barabara ya Mkoa, lakini daraja lake lilibomoka toka mwanzo wa mwaka huu.
Je, Serikali ina mpango gani wa dharura wa kujenga daraja hili ili wananchi waliokuwa wapo kwenye kisiwa waitumie barabara yao?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa daraja hilo tutalishughulikia na kwa nafasi hii nawataka TANROADS Mkoa wa Tanga walete taarifa kamili ya lini wamepanga kukifanya ili tuweze kutekeleza kile ambacho Mheshimiwa Mbunge na ambacho wananchi wa Korogwe wanakitaka.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mradi huu unagusa hasa sehemu za tambarare peke yake, ni lini sehemu za milimani kama vile Suji, Mkomazi, Manga Mtindilo, Mikocheni na Bwiko mradi huu nao utatekelezwa huko kwa sababu wakati wa mwanzo tuliambiwa hela zipo na mradi unaanza? Naomba kujua ni lini sehemu zile za milimani na zenyewe zitapata maji?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji ambavyo vitapewa maji katika mradi huu wa Same-Mwanga ni Bwiko, Mkomazi, Nanyongie, Manga Mtindilo na Manga Mikocheni, hii ndiyo ipo kwenye mpango. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba mradi umechukua muda mrefu na sababu kubwa ni kwamba mradi huu unategemea ufadhili wa nchi za Kiarabu. Sasa fedha ambazo unategemea mtu mpaka akupe huwa inachukua muda mrefu. Hata hivyo, Serikali tumeamua katika mwaka wa fedha unaokuja ule upungufu wa bajeti ambao upo tutaweka kwenye fedha zetu za ndani. Kwa hiyo, nitaomba sana Waheshimiwa Wabunge tuweke fedha za kutosha kwenye fedha za ndani ili mradi huu tuweze kuukamilisha.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri wa Kilimo. Nilikuwa na swali dogo tu la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa zao la mkonge ni moja ya mazao yanayoiingizia nchi yetu kipato, na kwa kuwa wakulima wa mkonge katika Jimbo la Korogwe Vijijini na hasa Mkoa wa Tanga wamekuwa wanajitahidi sana kulima mkonge ili wajinufaishe wao na familia zao na kuwasomesha watoto wao, je, Serikali itawasaidiaje ili wapate kulipwa haraka fedha walizokuwa wanadai kwenye Mamlaka ya Mkonge au Katani Limited ili ziweze kuwasaidia kuendesha na kustawisha zao la mkonge hapa nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba zao la mkonge ni zao muhimu sana na linaloingizia wakulima pamoja na nchi fedha nyingi. Kwa taarifa tuilizonazo ni kwamba mwaka 2014/2015 mkonge uliingizia nchi dola za Kimarekani milioni 35.4 na kwa sasa uzalishaji umefikia kiwango cha tani 40,000. Kwa sasa sisi ni nchi ya pili baada ya Brazil inayozalisha tani 150,000 za mkonge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itahakikisha kwamba wakulima wanaendelea kufaidika na kuinuka tena kwa zao la mkonge fahari ya watu wa Tanga ambapo kwa sasa tunafuatilia kuhakikisha kwamba wakulima wanalipwa fedha zao miezi mitatu na ndiyo maana nimemueleza Mheshimiwa Mbunge kwamba fedha zinategemewa kulipwa mwezi huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nieleze tu kwamba kilio hiki cha wakulima kucheleweshewa fedha siyo cha Mheshimiwa Ngonyani peke yake, Wabunge karibu wote wa Mkoa wa Tanga wamekuwa wakiulizia kuhusu hizi fedha, na Mheshimiwa Mbunge wa Pangani amelalamika sana kuhusu hili na nimuahidi Mheshimiwa Nyonyani na Wabunge wote wa Tanga baada ya Bunge hili mimi mwenyewe naondoka naelekea Tanga kwenda kushughulikia kwa karibu zaidi kuhakikisha kwamba fedha za wakulima zinalipwa.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nampongeza ndugu yangu Naibu Waziri kwa kazi nzuri anayoifanya na hasa ya kushughulikia matatizo ya wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika tatizo la kule Mbulu hasa kule Haydom, inalingana kabisa na Korogwe Vijijini
katika Mji Mdogo wa Hale na wewe mwenyewe umeshafika pale; je, Serikali Serikali ina mpango gani wa kupandisha hadhi Kijiji cha Hale kuwa Mji mdogo kule Korogwe Vijijini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tuliweza kufika pale kwa sababu walikuwa na concern ya Mji wa Mombo. Hayo yote, hata timu yetu tuliituma, waliweza kufika kule na kufanya assessment na wataalamu wameshafanya jukumu lao, iko katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI sasa inafanyiwa kazi. Kwa hiyo, mchakato ukikamilika, basi mtapata mrejesho nini kimepatikana katika eneo hilo.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kazi nzuri anayofanya. Mimi nilikuwa nataka kujua ule Mradi wa Vuga - Mlembule - Mombo ambao yeye ameutembelea kwa muda mrefu sana na kuona matatizo yake na kuwaahidi wananchi wa Mombo kwamba ikifika mwezi wa sita watapata maji. Ni lini Mradi huu utakuwa umekamilika na wananchi wale wafurahie mradi ule mkubwa wa maji ambao unagharimu zaidi ya shilingi 900,000,000?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuhakikishie kwamba wananchi wa Mombo watapata maji. Nilifanya ziara nimeenda Vuga, nimeongea nao na tumekubaliana kwamba sasa tuongeze fedha pamoja na hiyo milioni mia tisa, tunaongeza fedha katika bajeti ya 2017/2018. Na tumeweka utaratibu, eneo lolote lenye chanzo tunapofanya mradi lazima tuhakikishe kwamba wananchi wanaozunguka hilo eneo wapate maji kabla ya kupeleka Kijiji cha mbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunatenga fedha itakayohakikisha kwamba wananchi wa Vuga wanapata maji, na bomba lingine linakuja moja kwa moja mpaka eneo la Mombo na maeneo mengine yatakayopitiwa na hilo bomba. Kwa hiyo nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunaendelea na juhudi kuhakikisha kwamba wananchi wa Mombo wanapata maji kutoka Vuga.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri, lakini nina swali moja la nyongeza kufuatana na Wizara hii kufanya kazi vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, REA ya Awamu ya Pili ilikuwa ina sehemu ambayo imepima lakini sehemu hizo mpaka leo hii bado hazijapata umeme. Mfano ni katika kata ya Magoma katika kijiji cha Makangala na Mwanahauya na Pemba na katika kata ya Kerenge katika vitongoji vya Ntakae, Mianzini, Kwaduli, Migombani, Mfunte na Kiangaangazi. Je, Serikali ina mpango gani wa haraka kuhakikisha kwamba vijiji hivi na ile vya Kata mpya ya Mpale vinapata umeme kwa haraka?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Ngonyani kwa jinsi ambavyo anashughulikia maendeleo ya umeme kwa jimbo lake, hongera sana Mheshimiwa Ngonyani.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuonesha tuna mkakati gani kwanza kabisa upatikanaji wa fedha ya mradi huu unakwenda vizuri na ni mkakati mzuri. Nimhakikishie Mheshimiwa Ngonyani vijiji vyake vitapata umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na kwamba ana wasiwasi na Kata ambazo ametaja za Magoma, Kelege pamoja na Mazizini lakini yako maeneo ya Foroforo pamoja na Majimoto Mheshimiwa Ngonyani atapata umeme kupitia mradi huu. (Makofi)
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, asante sana. Kwanza niipongeze Serikali kwa mpango mzuri wa kunipatia fedha shilingi milioni 18. Nina maswali mawili ya nyongeza. Ukiacha fedha ambayo napewa na Serikali milioni 18 Serikali iliniahidi kunipatia fedha zaidi ya milioni 60 na ikatoa milioni 20 toka 2012 hadi leo hii milioni 40 hawajanipatia. Ni lini ahadi ya Serikali ya milioni 40 ambazo waliniahidi kunipatia ili nimalizie sehemu ya vijiji ambavyo vimebakia vya Kwemshai na Mnungui itatimia?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Shirika Lisilokuwa la Kiserikali liliamua kunipatia fedha na kuchimba visima tisa katika Jimbo langu la Korogwe Vijijini na baadhi ya sehemu Serikali iliamua kuchukua dhamana ya kufunga pampu na kusambaza maji. Katika sehemu hizo Serikali iliamua kwamba katika Kijiji cha Lusanga Mnyuzi, Makuyuni, Kwikwazu pamoja na Kerenge kibaoni kwamba watafunga maji hayo na kuyasambaza. Je, ni lini maji haya yatapelekwa katika vijiji ambavyo Serikali iliamua kwamba watawapelekea maji?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS - TAMISEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli na niweke rekodi sawa kwamba milioni 81 si milioni 18 ambayo tumeweka katika mpango wa Serikali wa mwaka huu. Mradi ule kutokana na tathmini tuliyofanya tunahitaji karibuni milioni 415. Kwa hiyo hii sisi watu wa Pwani tunasema kama kiingilia mbago tu. Nakumbuka tulipokuwa na Mheshimiwa Rais pale Korogwe Mheshimiwa Mbunge alizungumza hoja hii hasa ya maji katika jimbo lake na Mheshimiwa Rais aliibeba kwa ukubwa wake katika Wilaya nzima ya korogwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishie kuwa ni mipango ya Serikali, ukiachana na suala hili la bajeti lakini kwa ahadi ya Mheshimiwa Rais tutafanya kila liwezekanalo ili Wilaya yote ya Korogwe Mjini na Vijijini kama tulivyoelekeza siku ile katika mkutano wetu mambo yatakuwa sawasawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika ajenda nyingine ya wafadhili wetu, tunajua kwamba kuna World Vision kule walifanya kazi na taasisi zingine walifanya kazi kubwa sana. Naomba nimhakikishie, Serikali tumeshaanza kutafuta jinsi ya kufanya ili ahadi ya Serikali juu ya maji iwafikie wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, jana tulisikia kwenye vyombo vya habari, walikuwa wakionesha jinsi wananchi wa jimbo lake walivyokuwa wakishangilia maji kutokana na juhudi kubwa inayofanywa na Waheshimiwa Wabunge wawili katika Wilaya ya Korogwe. Kwa hiyo niwahakikishie kwamba tutatafuta namna ya kufanya ya pamoja kuzishughulikia changamoto tulizobaini kwa kushirikiana na Wizara ya Maji ili ahadi ya Mheshimiwa Rais iweze kutekelezeka na hivyo wananchi wa Korogwe wapate maji safi na salama.
MHE. STEPHEN HILARY NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijauliza maswali mawili ya nyongeza kwa ruksa yako naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais, kwa kunipa shilingi bilioni moja kwa ajili ya vituo viwili vya Afya, Kata ya Mkumbala na Kituo cha Afya Bungu, Mungu ambariki sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mwaka 2012 Mahakama hii iliahidiwa kwamba itajengwa, mwaka 2014 iliahidiwa itajengwa, mwaka 2015 iliahidiwa itajengwa, sasa nataka tamko la Serikali mwaka 2020 ni kweli kituo hiki au Mahakama hii ya Mwanzo itajengwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Serikali ilijenga Mahakama ya Mwanzo ya kisasa zaidi pale Magoma katika Tarafa ya Magoma, na nikajitahidi nikakarabati Mahakama moja katika Tarafa ya Bungu, lakini Mahakama hizi mpaka zaidi ya miaka saba hazijafunguliwa.
Sasa naomba Serikali iniambie ni nini sababu zinazuia Mahakama hizi zisifunguliwe wakati wananchi wanapata shida sana kutolewa umbali wa kilometa 30 kwenda kufuata Mahakama sehemu nyingine? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA): Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nichukue fursa hii kuanza kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa jitihada kubwa anazozifanya katika kuhakikisha kwamba huduma hii ya Mahakama inawafikia wananchi wake kwa ukaribu zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lakle la kwanza la nyongeza, nataka nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa mwaka wa fedha wa mwaka 2019/2020 Mahakama hii ya Mwanzo itajengwa na nimuondolee hofu kwa sababu hivi sasa, kupitia Wizara tunashirikiana na Chuo Kikuu cha Ardhi na Baraza la Nyumba la Taifa na sasa tuna mfumo mzuri wa ujengaji wa Mahakama kutumia teknolojia ya moladi ambayo inafanya kazi kukamilika kwa muda mfupi na ukuta kuwa imara zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba kazi hiyo itafanyika na hivi sasa navyozungumza. Tunayo miradi takribani 39 nchi nzima ambayo inatekelezwa na kufikia mwaka wa fedha 2018/2019 tutakuwa tumekamisha Mahakama za Mwanzo na Mahakama za Wilaya na Mahakama za Mkoa takribani 70. Kwa hiyo, nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba hii ni ahadi ya Serikali na jambo hili litatekelezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni kuhusu Mahakama ya Magoma ambayo tayari ukarabati na ujenzi umefanyika lakini mpaka leo haijafunguliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumuagiza Mtendaji wa Mahakama wa Mkoa wa Tanga kuhakikisha kwamba anafuatilia na kutupatia taarifa na sisi tutakwenda kufuatilia na tutampatia majibu Mheshimiwa Mbunge, lakini nataka nimuahidi tu kwamba kama hakuna vikwazo vingine vyovyote basi tutahakikisha kwamba Mahakama hii inafanya kazi na wananchi wa Tarafa ya Magoma wanapata huduma hii stahiki.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tatizo la Karatu linalingana kabisa na tatizo la Korogwe Vijijini hasa kwenye barabara inayotokea Korogwe - Kwashemshi - Bumbuli - Soni imekatika na barabara hii iliamuliwa na Serikali kwamba itajengwa kwa kiwango cha lami na sasa hivi mawasiliano hakuna. Je, Serikali haioni kuna umuhimu wa kuitengeneza barabara hii haraka haraka ikarudisha mawasiliano ya dharura ambayo yalikuwa yameshakatika kwa muda mrefu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu awali, barabara zote ambazo zimekatika hivi sasa TANROADS pamoja na Mameneja wa Mikoa wa TANROADS wote Tanzania nzima waanze kuelekeza nguvu katika kurudisha mawasiliano kwa barabara zile zilizokatika ikiwa ni pamoja na barabara hii ya ndani ya Jimbo la Korogwe Vijijini kwa Mheshimiwa Ngonyani.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na ninamshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri sana, nina maswali mawili ya nyongeza:-
Kwa kuwa wananchi wa Mwanza na Ukelewe wamepata usumbufu zaidi ya miaka mitano kwa kukosa usafiri; na kwa kuwa ni sehemu muhimu sana kwa wavuvi; ni lini sasa Serikali itawapa usafiri wa dharura wananchi wale ili waone umuhimu wa Serikali yao inavyowasaidia?
Swali la pili, kwa kuwa tatizo la Ukerewe linalingana kabisa na Tanga, wananchi wa Tanga, Pemba, Unguja pamoja na Bagamoyo wanahitaji meli kama hiyo ili iwasaidie; je, Serikali ina mpango gani wa kuwahakikishia wananchi wa Ziwa, umetaja Ziwa Nyasa, umetaja Ziwa Victoria, umetaja Ziwa Tanganyika; lakini je, katika Bahari ya Hindi wananchi wa Tanga, Pemba, Unguja na Bagamoyo ni lini na wao watapata meli ili na wao waepukane na kile kimbunga cha kila siku kufariki kwenye meli? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimshukuru Mheshimiwa Stephen Ngonyani, Mbunge wa Korogwe Vijijini kwa namna ambavyo ameniamsha namna ya kufuatilia masuala ya wananchi wa Korogwe Vijijini na mimi vilevile Namtumbo, kwa kweli ninaomba Wabunge wengine wafuate nyayo zake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu dharura nadhani Mheshimiwa anafahamu kwamba tuna usafiri ambao sasa hivi upo, isipokuwa hautoshelezi. Kwa masuala ya dharura usafiri unapatikana, nia yetu kubwa ni kuondokana na meli hizi chakavu, tuzitengeneze na tulete mpya. Kwa hiyo, masuala ya dharura siyo tatizo yamekuwa taken care off.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa swali la pili niliwahi kujibu swali kama hilo katika Bunge hili kwamba katika miaka ya 1980 - 1990 tuliamua kuingiza sekta binafsi katika shughuli za usafiri na kwa upande wa meli tulianzia na upande wa Bahari ya Hindi unafahamu kwamba kuna wasafirishaji binafsi wengi wanafanya shughuli hizo za usafiri. Kama ombi lako maana yake unataka Serikali iondoe hiyo sera ilete sera nyingine tutaliwasilisha Serikalini likajadiliwe tuone hasara na faida yake, kwa sasa naomba tuendelee kupata huduma za meli kutoka kwa wasafirishaji binafsi, TACOSHILI tulishaisimamisha miaka ya 1990.

WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ngonyani hasa sehemu (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi tunavyoongea upo usafiri wa kudumu baina ya Dar es Salaam, Unguja na Pemba. Ipo meli ambayo inaitwa MV Mapinduzi II ambayo ni meli ya kisasa inayosafiri baina ya Unguja na Pemba na tutaongea na Wizara ya Uchukuzi na Mawasiliano huko Zanzibar kuhakikisha kwamba meli hii inasafiri kutoka Pemba kwenda Tanga kama ilivyokuwa hivyo zamani.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Profesa mwenzangu kwa majibu mazuri na yenye msimamo. Nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa Mahakimu wengi wa Mahakama za Mwanzo wanafanya kazi katika mazingira magumu na wanapokwenda kwenye Mahakama za vijijini huwa wanatumia usafiri wa mabasi. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia usafiri kwa ajili ya usalama wao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Mahakimu wengi wanakaa katika nyumba za mtaani za kupangisha. Katika nyumba hizo huwa baadhi yao kuna watuhumiwa wanaowajua sehemu walipo. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha Mahakimu hao wanapata nyumba maalum kwa ajili ya usalama wao? Ahsante sana.
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo wanafanya kazi katika maeneo magumu hasa maeneo ya vijijini yenye matatizo ya usafiri. Kutegemea hali ya bajeti itakavyokuwa inaboreka Serikali ina mpango wa kuwapa vyombo vya usafiri, hasa Mahakimu ambao wanahudumia maeneo makubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu nyumba za Mahakimu Serikali pia inatambua umuhimu wa Mahakimu kuwa na nyumba na kwa kuwa sasa imeanza na mpango wa ujenzi wa Mahakama mara baada ya zoezi la ujenzi wa Mahakama litakapokuwa limefikia mahali pazuri basi Serikali ina mpango pia wa kufikiria kuanza kujenga nyumba za Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo hasa katika maeneo ambayo yana matatizo makubwa. (Makofi)
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza niipongeze Serikali kwa majibu yake mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la Mto wa Mbu lina linalingana kabisa na tatizo la Mji wa Mombo. Mji wa Mombo toka Awamu ya Nne ulihaidiwa na Serikali kwamba utajengwa kiwango cha lami kilometa moja na nusu, na wataalam walienda pale wakapima na wakachukua sample ya udongo, lakini cha kushangaza mpaka leo hii barabara hile ya Mji Mdogo wa Mombo haijafanyiwa utafiti wala haijafanyiwa chochote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nini tamko la Serikali kuhusiana na Mji Mdogo wa Mombo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J.KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge atakubaliana na mimi kwamba amekuwa akilifuatilia suala hili na tumezungumza naye. Nitumie tu nafasi hii nimuelekeze Meneja wa TANROADS Mkoa wa Tanga ili aweze kuharakisha zoezi la kusanifu eneo hili ili sasa tuweze kujenga na kuboresha kama ilivyo kwenye ahadi, ahsante sana. (Makofi)
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona.
Mheshimiwa Waziri wa maji kwanza niwapongeze kwa kazi nzuri mradi wa maji wa Mombo - Mlembule ulikuwa wa Serikali imetenga shilingi milioni 900 lakini cha kushangaza sasa hivi mradi huo umekuwa wa shilingi bilioni nne. Nini tamko la Serikali kuhusiana na mradi wa shilingi milioni 900 mpaka ukafika shilingi bilioni nne? Hizo shilingi bilioni nne ni kwa ajili ya mradi gani mwingine?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tulikuwa na mradi wa shilingi milioni 900, lakini usanifu wake haukuhusisha vijiji vya Mji wa Mombo pamoja na maeneo yanakotoka maji Vuga. Kwa hiyo tukafanya review, hiyo review sasa imekamilika lakini sina taarifa kwamba hiyo review imefikia shilingi bilioni nne.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nikuhakikishie kwamba baada ya Bunge hili leo mimi na wewe twende pamoja, nitakusanya wataalam wangu ili tuweze kuangalia mradi huo uweze kutekelezwa haraka.(Makofi)
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Kambi Mbadala, kwanza niwapongeze Wizara hii ya Maji kwa kufanya kazi vizuri hasa mdogo wangu kwa kubeba ndoo kichwani. Kule Mnyuzi katika Kijiji cha Lusanga kuna mradi mkubwa wa maji ambao upembuzi yakinifu umeshafanyika na maji hayo yangeweza kufika mpaka Shamba Kapori; je, mradi huu mpaka sasa hivi umefikia wapi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana. Hata hivyo, nimpongeze Kaka yangu Mheshimiwa Maji Marefu kwa namna anavyowapigania wananchi wake wa Jimbo la Korogwe Vijijini. Nataka nimhakikishie yeye ni jembe wembe!
Mheshimiwa Naibu Spika, kikubwa kama alivyokuwa amesema, upembuzi yakinifu umeshakamilika, kubwa nimwombe tu Mhandisi wa Maji wa Korogwe Vijijini asilale. Ahakikishe kwamba anatangaza ile kazi ili mwisho wa siku Mkandarasi apatikane na utekelezaji wa mradi uanze mara moja na Wizara ya Maji hatutokuwa kikwazo katika kuhakikisha tunawapa fedha ili mradi ule ukamilike kwa wakati. Ahsante sana.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Profesa mwenzangu. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa Tarafa ya Magoma ina Kata Nane na katika Kata hizi ina Mahakama moja tu ya Mwanzo ambayo ni hiyo ya Mashewa na huu mradi umechukua muda mrefu bila kufunguliwa. Nataka Serikali iniambie ni tarehe ngapi Mahakama hii itakuwa imefunguliwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, maneno anayoelezwa hapo Mheshimiwa Waziri, naomba kama kutakuwa na uwezekano aende. Hayo anayoambiwa kwenye karatasi yanalingana na jinsi Mahakama yenyewe inavyotengenezwa kule nilipo? Nitaomba twende wote ili akahakikishe, aone kwamba imechukua muda mrefu, wanafanya kazi bila kudhibiti na tunapata usumbufu sana kwa walalamikaji na washtakiwa kwenda zaidi ya kilometa 35. (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Kata ile inahitaji Mahakama zaidi na naamini katika mpango utakaofuata wa maendeleo wa miaka 10 wa Mahakama baada ya huu unaoisha 2020 kukamilika, tutatazama tena maeneo ambayo Kata zao ni kubwa na Mahakama ni chache ili katika mpango huo wa awamu ya pili wa ujenzi wa Mahakama nchini maeneo hayo yaweze kuangaliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la pili la kutembelea eneo la Mashewa ili kujionea jinsi Mahakama hiyo inavyojengwa, niko radhi kufika huko na sina wasiwasi Profesa kwa sababu na mimi mjomba wangu ni fundi kama wewe, kwa hiyo nitafika na kuondoka salama. (Kicheko)