Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Ahmed Juma Ngwali (3 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. AHMED JUMA NGWALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii japo kwa ghafla.
MWENYEKITI: Niichukue hiyo nafasi nimpe mwingine?
MHE. AHMED JUMA NGWALI: Aah okay, aah usimpe! (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, lakini kabla ya kuchangia Mpango kuna jambo naomba niliweke sawa, japo nilitamani sana Mwanasheria Mkuu angekuwepo tukaenda sawasawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya (1) naomba niisome, inasema: “Tanzania ni nchi moja na ni Jamhuri ya Muungano.” Kwa hiyo, sisi hapa kama Wazanzibari tumo ndani ya Tanzania na ni Watanzania. Hakuna Mzanzibari kwa mujibu wa Katiba kwa sababu Tanzania ni dola moja tu, wala Zanzibar siyo dora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, unaposema Wazanzibari wakatatue matatizo yao, huo ni ubaguzi ambao umekatazwa na Katiba. Haiwezekani tatizo linatokea Arusha, mkasema kwamba tatizo hilo ni la Waarusha tu, haliwahusu watu wa maeneo mengine; linawahusu Tanzania nzima. Kwa hiyo, hili naomba niliweke sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili watu wanasema kwamba Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haihusiki kabisa na masuala ya Zanzibar, lakini naomba niisome Katiba ya Zanzibar… nani kaikimbiza tena! Aah! (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niisome. Ukisoma Katiba ya Zanzibar Ibara ya 119… imechukuliwa bwana! (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 119(14) inasema kwamba; “Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar itashirikiana na Tume ya Taifa katika kuendeleza shughuli zao za uchaguzi.”
Sasa ikiwa Tume ya Uchaguzi ya Taifa ambayo ni ya Jamhuri ya Muungano inashirikiana na Tume ya Zanzibar, kwa hiyo, hata uchaguzi uliofutwa, Tume ya Taifa imeshiriki katika kufuta uchaguzi ule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kitu kimoja cha busara sana; tumetoka mbali sana na Taifa hili, tuna maingiliano ya muda mrefu; tuna maingiliano toka karne ya 16 na nyuma huko, tumeishi kwa udugu sana, tumeishi kwa mapenzi, tumeishi kwa furaha wala hakuna tatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na matatizo mengi yanayojitokeza madogo madogo, lakini yamekuwa yanapatiwa ufumbuzi na mambo yanakwenda. Leo isifike wakati Mpango huu ukawa hautekelezeki kwa sababu ya mtu mmoja tu peke yake. Nikimtaja mtu anayeitwa Jecha Salum Jecha, mseme laanatullah, kwa Kiswahili “laana za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake.” (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, viongozi mbalimbali ambao wanaitakia mema nchi hii, naomba nimtaje kwa heshima kubwa Komredi Salim Ahmed Salim, alisema kwamba lazima tatizo la Zanzibar lipatiwe ufumbuzi, lakini pia Mheshimiwa Bernard Membe aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje katika Serikali ya Awamu ya Nne, kwa ufasaha kabisa alisema tatizo hili lazima tulipatie ufumbuzi. Vilevile Jaji Warioba, watu hawa ni watu wenye heshima kubwa katika nchi hii, ni watu ambao tunawaheshimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili tatizo lisichukuliwe kama ni tatizo dogo tu. Niwaambie kitu kimoja; tunapanga mipango hapa, hata Kenya na Burundi wana mipango wanapanga, inakuwa sasa? Mara Garissa limelipuka! Mara hapa, mara pale, kwasababu mnaonea watu waliokuwa hawana silaha. Watu waliokuwa hawana silaha, wanatafuta namna.
Kwa mfano, Waziri Mkuu aliyepita alikaa pale wakati Mheshimiwa Mama Asha Bakari, Marehemu, Mungu amrehemu, alipokuwa akisema nchi hii haipatikani kwa vikaratasi. Sasa ukisema nchi hii haipatikani kwa vikaratasi, maana yake ni kwamba, huo ni ugaidi, tutafute utaratibu mwingine. Hata Mheshimiwa Lukuvi naye aligusagusa sana kwenye swali hili, mtu mbaya sana yule! Tuendelee lakini. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niseme kwa busara kabisa, viongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakae pamoja tuone namna gani wanalishughulikia tatizo la Zanzibar na uchaguzi usifanyike. Uchaguzi kwanza ukae pembeni, usifanyike tuone ni namna gani Serikali hii inatatua tatizo letu hili, kwa sababu mkiacha uchaguzi ule ukifanyika, na sisi tumetangaza rasmi kuwa hatushiriki kwenye uchaguzi ule; ninyi mnaona ni busara hiyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mnaona ni busara, endeleeni na uchaguzi, lakini niwaonye kitu kimoja, Serikali mnanisikia vizuri sana, mpo hapo. Haya makundi yote yaliyojitokeza kama Islamic State, Al-shabab, Boko Haram yalitokana na kudhulumiwa haki zao. Haya hayakuwa bure! Hayakujitengeneza tu, yalijitengeneza baada ya kudhulumiwa. Sasa msije mkatuharibia nchi yetu kwa kumlinda mtu mmoja tu. Serikali ya Muungano mmewabeba sana Serikali ya Zanzibar! Mmewabeba mwaka 2000… (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Ngwali!
MHE. AHMED JUMA NGWALI: Naam!
MWENYEKITI: Huo mfano ulioutumia, chimbuko la hayo makundi uliyoyataja wewe, una ushahidi kwamba misingi yake ndiyo hiyo?
MWENYEKITI: Unaweza ukatuthibitishia hapa?
MWENYEKITI: Mimi nakusihi sana, ufute tu hiyo kauli yako, tusifike mbali.
MHE. AHMED JUMA NGWALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nafuta kauli yangu, haina shida. (Kicheko/Makofi)
MBUNGE FULANI: Taarifa, Mheshimiwa Mwenyekiti.
MWENYEKITI: Taarifa! Keti tu Mheshimiwa Ngwali, muda wako umekwisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. AHMED JUMA NGWALI: Mheshimiwa Spika, mimi jina langu naitwa Ahmed Juma Ngwali, siitwi Ahmed Ali Ngwali.
Mheshimiwa Spika, sihitaji makofi wala sihitaji vijembe. Nimekuja hapa na nimesimama hapa nina jambo langu ambalo naiomba Serikali inisikilize kwa umakini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna Sheria ya Wakfu, (Commission Ordinance) ya mwaka 1953, Sheria hiyo ikafanyiwa marekebisho mwaka 1956. Ilikuwa Sheria namba 7 na ikafanyiwa marekebisho ikawa Sheria Namba 9. Jambo la kushangaza, sheria hiyo mpaka leo ipo, Sheria hiyo inahusu Wakfu ya Waislamu. Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Kwanza Mwalimu Nyerere akaiacha hiyo commission hakuwahi kuiunda pia Mheshimiwa Rais Mwinyi akapita hiyo commission haikuundwa, akapita Rais wa Tatu Mheshimiwa Benjamin Mkapa pia hiyo commission haikuundwa na Rais wa Awamu ya Nne Mheshimiwa Jakaya Kikwete commission haijawahi kuundwa.
Mheshimiwa Spika, kwa hivyo mali za waislamu zimekuwa zikiibiwa. Hiyo commission ni muhimu sana kwa ajili ya maslahi ya waislamu na mali zao.
Kuna Sheria ya Mirathi ambayo ndani ya Sheria ya Mirathi sasa imeingizwa sehemu ya Sheria ya Wakfu ambayo imeeleza mambo mengi. Inashangaza sana! Sheria ya Wakfu ipo halafu ikatiwa ndani ya Sheria ya Mirathi.
Mheshimiwa Spika, mirathi na wakfu ni mambo mawili tofauti, hayafanani!
SPIKA: Mheshimiwa Ngwali, neno moja dogo tu….
MHE. AHMED JUMA NGWALI: Naam.
SPIKA: Umesema mali za waislam zinaibiwa tukashtuka, ni kitu gani? Unaweza ukafafanua kidogo?
MHE. AHMED JUMA NGWALI: Tunakwenda, tulia…
SPIKA: Ni jambo kubwa hilo!
MHE. AHMED JUMA NGWALI: Mheshimiwa Spika, tulia!
Mheshimiwa Spika, nirudi hapo ambapo unapotaka sasa, kwasababu tu hii commission ya kusimamia mali za waislamu….
MHE. DKT. SULEIMAN ALLY YUSSUF: Mheshimiwa Spika, Taarifa!
SPIKA: Mheshimwa Ngwali pokea Taarifa.
TAARIFA....
MHE. AHMED JUMA NGWALI: Mheshimiwa Spika nimepokea vizuri na muda wangu nilindie.
Mheshimiwa Spika, tunachosema sasa ni kuiomba Serikali, hii commission ya Wakfu ianze kufanya kazi, kwa sababu sheria tayari ipo na kila kitu kipo, waislamu wengi wanapata shida na kuchelewa kwa Serikali kuanzisha wakfu hii kumesababisha mali za wakfu zilizowekwa waislamu hawajui ni kiasi gani zilikuwepo, kiasi gani zilizopo sasa, zilizouzwa na zilizofanyiwa mambo mengine. Kuna waislamu wengi wanataka kuweka mali lakini kwa sababu commission bado haijaundwa ni shida sana wanaogopa mali zao kupotea, hata mimi nataka kuweka wakfu.
Mheshimiwa Spika, katika hili tunaiomba Serikali kwa nia njema kwa sababu Serikali ina nia njema, hii sheria ipo, hawajaifuta, siyo tu kwamba hawajaifuta, wameitengenezea utaratibu mwingine mzuri ili kupitia katika Sheria ya Mirathi waislamu waweze kufaidika na hiyo Sheria ya Mirathi.
Mheshimiwa Spika, ikiwa Wakoloni mwaka 1953 walikuwa na sheria hii, wala jambo hili siyo la dini, jambo hili ni la kisheria. Wakoloni ndiyo waliokuja na dini, wao ndiyo waliokuwa na dini, kwa nini waliweka utaratibu kwamba watu hawa waisalmu waishi hivi na watu hawa wa dini nyingine waishi hivi, hivyo tunaiomba Serikali kwamba kama Rais hajateua au kama kateua atuambie hao watu aliowateua katika hiyo commission ni akina nani na kwa mujibu wa ile sheria Rais anayo mamlaka ya kuchagua siyo chini ya watu nane na katika hao watu watano watakuwa waislamu, pia Rais atachagua Mwenyekiti atateua na Katibu. Vilevile Rais atachagua kwa mapenzi yake anayoyaona na Tume ile inaweza kukaa kwa muda ambao Rais atapenda. Katika hali hiyo tunaiomba Serikali hii Tume ianzishwe.
Mheshimiwa Spika, suala la pili, nataka kuzungumzia Sheria ya Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo. Sheria hii inafanya kazi vizuri sana kwa upande wa Tanzania Bara lakini kwa upande wa Zanzibar hii sheria ni tatizo.
Kwa mfano, fedha zikitoka Hazina ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinakwenda katika Ofisi ya Makamu wa Rais, zikitoka Ofisi ya Makamu wa Rais zinakwenda Hazina Zanzibar, zikitoka Hazina Zanzibar zinakwenda kwa Makamu wa Pili wa Rais, zikitoka kwa Makamu wa Pili wa Rais zinakwenda kwenye ofisi ya Haji Omar Kheir, Tawala za Mikoa na Vikosi vya SMZ, zikitoka hapo ndiyo ziingie katika Halmashauri za Majimbo. Sasa hii inashangaza sana, huo mlolongo hata hizo fedha zikifika inakuwa ni muda mrefu sana.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine baya zaidi ni kwamba pesa zile hazikaguliwi kwa sababu Mdhibiti na Mkaguzi wa Mahesabu ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano hawezi ku-cross over akaenda kukagua Hazina ya Zanzibar. Kwa hiyo, kwa miaka mitano fedha zile au kama ushahidi kuna mtu alete ushahidi kama upo, miaka mitano fedha zile hazijakaguliwa! Mwisho wa siku wanakuja watu kutoka katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais na karatasi zao eti wanakagua fedha ambazo zinatoka katika Hazina ya Jamhuri ya Mungano na ni fedha za Muungano. Wala sheria haijasema mahali popote kwamba mwenye mamlaka ya kwenda kukagua zile fedha ni mtu fulani kwa hivyo zile fedha za Serikali zinapotea, Serikali yenyewe ipo na haina habari! Naomba Serikali kwenye jambo hilo walitazame vizuri na sisi tutaweka input zetu katika kuleta maerekebisho ya sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine nataka kuuliza ambalo ni dogo tu, ile Mahakama ya Kadhi imefikia wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Serikali tunataka mtuambie tu kwamba ile Mahakama ya Kadhi imeshindikana, haipo ama vipi kwa sababu ile mimi naithamini sana kwa sababu iliahidiwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2010-2015 ikasema kwamba ile ni moja katika mkakati wa Chama cha Mapinduzi kuhakikisha kwamba Mahakama ya Kadhi inasimama.
Mheshimiwa Spika, nashukuru.
Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. AHMED JUMA NGWALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, sitaki nijihuzishe sana na mazungumzo yaliyopita, naomba nijielekeze kwenye hoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijachangia hoja hii niliamua kwanza nipitie Sheria ya Baraza la Michezo, Sheria Namba 12 ya mwaka 1967 ikafanyiwa marekebisho na Sheria Namba 6 ya mwaka 1971 pamoja na Kanuni za Michezo na Kanuni za Usajili Namba 442 ya mwaka 1999.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipitia hii sheria, ukistajabu ya Musa utayakuta ya Firauni, bahati nzuri sana Mwanasheria Mkuu yupo, lakini Waziri wa Sheria Mheshimiwa Mwakyembe pia yupo. Naomba ninukuu Kifungu cha12 cha Sheria ya Baraza la Michezo, Kifungu hicho kinachohusu usajili wa vilabu kinasema;
“Msajili atakataa kusajili au kutoa msamaha wa usajili kwa chama cha michezo, ikiwa (a) Ikiwa ameridhika kwamba chama hicho ni tawi la au; kimeshirikishwa au; kina uhusiano na shirika au kikundi chochote chenye mwelekeo wa kisiasa isipokuwa chama au chombo chochote cha Chama cha Afro-Shiraz cha Zanzibar au chombo chochote cha chama hicho.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, Afro-Shiraz ipo kwenye Sheria ya Baraza la Michezo, Chama cha Afro-Shiraz hakipo tena hata katika Katiba ya Zanzibar, hata katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini sheria hiyo tayari imeshafanyiwa marekebisho na bado Chama cha Afro-Shiraz kinaonekana baada ya miaka sijui mingapi kwa sababu ilikufa mwaka 1977.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepata maswali mengi ya kujiuliza kwanza, kwa nini iwe Afro-Shiraz isiwe TANU. Kwa hiyo, inaonekana kwamba Waziri hata alipochaguliwa kuwa Waziri hata hii sheria hakuipitia. Inaonekana Serikali haipitii sheria na kuangalia sheria ambazo zinatakiwa kufanyiwa marekebisho. Jambo la msingi Serikali pitieni sheria ni aibu. Leo tunakuta Afro-Shiraz katika Sheria ya Michezo, ASP. Baada ya kuweka sawa hilo, tuendelee sasa na soka, mimi ni mdau mkubwa wa soka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha sana, Tanzania leo unasimama hapa unazungumza, ni ya mwisho katika viwango vya FIFA katika mpira wa miguu katika East Africa ni ya mwisho. Ya kwanza ni Uganda, ambayo inashika nafasi ya 72, ya pili ni Rwanda ambayo inashika nafasi ya 87, ya tatu ni Kenya inayoshika nafasi ya 116, ya nne ni Burundi inayoshika nafasi ya 122, lakini Tanzania inashika nafasi ya 129. Tumewazidi kila kitu hizo nchi nyingine. Hizo ni takwimu ambazo ukitaka kuzidadavua nenda kwenye website ya FIFA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha sana kwa sisi watu wa michezo kuona leo Taifa kama Tanzania ndiyo Taifa la mwisho kabisa katika soka kwa East Africa. Ukubwa wa nchi, uchumi wetu, tunapitwa na Kenya tu kwenye uchumi, kwenye population, kwenye eneo tuko juu. Maana yake ni kwamba hakuna mkazo katika michezo hasa soka mchezo ambao unapendwa na watu wengi Tanzania hasa ukifanya tafiti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine Wazungu wanasema one swallow does not make a summer. Inashangaza sana leo Mheshimiwa Nape, alikuja kwa mbwembwe sana na kumtangaza kama Mbwana Samatta ndiyo shujaa wa Tanzania katika mpira wa Kimataifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ni ya mwisho katika nchi zenye wachezaji wa wanaocheza Kimataifa. Tanzania ni ya mwisho, nataka nikupe takwimu. Tanzania ina wachezaji kumi tu nje ya nchi, Mheshimiwa Nape huwajui, nina hakika huwajui. Lakini Rwanda ina wachezaji 17 wanaocheza nje soka la kulipwa, Burundi wana wachezaji 25, Kenya wana wachezaji 32 wanaocheza nje na Uganda wana wachezaji 41. Watu wanajitahidi kadri siku zinavyokwenda kuwekeza katika mpira wa miguu, ndiko wanakotakiwa wawekeze kwa sababu mpira wa miguu, mfano chukua mchezaji mmoja tu, Victor Wanyama mchezaji wa Kenya anayecheza Southampton ya Uingereza analipwa kwa wiki pound 30,000 ni sawa na shilingi karibu milioni 300 kwa wiki moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnakwenda kuwekeza kwenye boda boda, hii ni Serikali gani isiyokuwa na mipango mizuri bwana eeh? Mnakwenda kuwekeza kwenye boda boda Rais anasema mshahara mwisho shilingi milioni 15, kwa mwezi Yaya Touré wa hapo Ghana anapata zaidi ya bilioni tatu kwa mwezi.
Jambo lingine ambalo ni muhimu sana ni suala la mapato ya michezo. FIFA wanakuwa na Financial Assistance Program (FAP) wanatoa dola 250,000 lakini wana Goal Project ambazo wanatoa dola 400,000. Tanzania Football Federation inapotoka nje kuwakilisha nchi inawakilisha kama Tanzania ambapo Zanzibar nao wanahitaji kupata hizo fedha. Hakuna takwimu zozote zinazoonesha kwamba Zanzibar wanapata hizo fedha, lakini kuna vyama tofauti vya michezo kama International Basket Ball Federation (FIBA) wanaleta fedha ndani, Zanzibar hatupati, tuna International Boxing Association wanaleta fedha hazipatikani, kuna Internationa Golf Federation zinakuja fedha kutoka nje hatupati, kuna Internationa Handball Federation hatupati fedha, kuna sports association chungu nzima za nje, Zanzibar hatujui mambo haya yanakwenda vipi, wala mambo yanakuwa vipi yaani tupo tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukichukuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ukiisoma hii iko katika mambo ya Muungano, mambo ya nje ni mambo ya Muungano, kwa hivyo mnavyotoka International Zanzibar tupo. Zanzibar tukizungumza tayari unatoka nje tu ya nchi, tukiwa ndani fanyeni shughuli zenu za ndani lakini kwa nini mnapokwenda nje misaada ile ya kimichezo Zanzibar hatuioni au mnaipeleka wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Nape namalizia kwa kusema tunakwenda katika Olympic ya Rio de Janeiro 2016. Tanzania toka mwaka 1964 ina medali mbili tu za shaba, Kenya wana medali 86, wana medali 25 za dhahabu, kama haujaja na medali lazima ujiuzulu kwa sababu hatuwezi tena kuvumilia kuona kwamba Tanzania ndiyo imekuwa shamba la bibi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, siungi mkono hoja.