Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Dr. Medard Matogolo Kalemani (8 total)

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, niungane na wenzangu waliotangulia, kwanza kabisa kumshukuru Mwenyezi Mungu, kwa mara ya kwanza kabisa kuonekana kwenye Bunge lako Tukufu na mimi nikichangia Mpango wa Maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kumshukuru sana Mheshimiwa Rais pamoja na azma ya Serikali ya hapa kazi tu, haijaishia kwenye maneno. Mwanzoni mwa mwezi huu Mheshimiwa Rais alizindua mradi wa kuzalisha umeme wa Kinyerezi Namba II megawatt 240, lakini mwishoni mwa wiki hii pia amezindua pia ujenzi wa flyover katika barabara ya kuelekea uwanja wa ndege na kama haitoshi juzi amezindua pia ukamilishaji wa Daraja la Kigamboni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe Watanzania wote, Waheshimiwa Wabunge na sisi wananchi, tufanye kazi moja ya kutwanga maendeleo, hakuna kazi nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze sasa kumshukuru Mheshimiwa Waziri wa Fedha katika mchango huu wa Mpango wa Maendeleo wa Pili. Katika Mpango huu nijielekeze moja kwa moja katika ukurasa wa 10, kadhalika ukurasa wa 28. Ukurasa wa 10 Waheshimiwa Wabunge, suala la nishati limezungumzwa kwa kirefu sana japo kwa maneno machache, nami niongezee sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama mnavyotambua Waheshimiwa Wabunge, Serikali ya Awamu ya Tano, kwa wananchi na Waheshimiwa Wabunge tunasema suala la nishati sasa ni la kufa na kupona. Tutake tusitake tutazalisha umeme wa kutosha kujenga viwanda vyetu. Ninawashukuru Waheshimiwa Wabunge, kwa ridhaa yako Naibu Spika kwa jinsi ambavyo wanaunga mkono kuelekeza nguvu za wananchi kwenye kuzalisha umeme wa kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukurasa wa 10 wa Mpango huu umezungumza kwamba mwaka 2016 tungefikisha megawatt 2,780, bado tunatembea 2016 inaendelea, lakini hata hivyo nguvu kubwa sasa inayoonekana niwatoe wasiwasi Waheshimiwa Wabunge na wananchi, sasa hivi megawatt tunazozipata kwenye nishati asilimia kubwa ni kutokana na gesi asilia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaeleze Waheshimiwa Wabunge, kwa sasa hivi Kinyerezi peke yake tuna uwezo wa kupata zaidi ya megawatt 700. Hapo nyuma tulikuwa tunapata megawatt chini ya 300. Lakini kwa sababu tunataka gharama za umeme zishuke na haziwezi kushuka kama hatuzalishi umeme wa gesi na umeme wa maji, niseme tu kwenye upande wa umeme wa maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo kina cha maji cha Mtera kinatosha, kinaongezeka, leo tuna milimita 697 kati ya 698 ambalo ni ongezeko kubwa linatupatia uhakika kwamba tutakuwa na umeme wa kutosha tunakoelekea. Kihansi kati milimita 1,190 tuna milimita 1,782, tunapungukiwa kidogo. Kidatu tuna milimita 471 kati ya milimita 478, kwa hiyo tunakwenda vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi kubwa ambayo nataka niwaeleze wananchi ni kupungua kwa gharama za umeme. Mwezi huu gharama za umeme zilizokuwa zinakwaza wananchi tumeondoa gharama za maombi ambayo ilikuwa ni shilingi 6,000.00. tumeziondoa, kadhalika tumeondoa gharama za kufanyiwa service (service charge) ambazo pia zilikuwa zinakwaza sana wawekezaji. Lakini wananchi wa vijijini sasa hivi gharama ambayo wanaweza kuwa nayo kimsingi kwa umeme wetu wa REA ni bure isipokuwa VAT ya shilingi 27,000/=.
Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo ni juhudi kubwa sana ya Serikali. Na niwahakikishie wananchi kwamba kwa sasa, niongezee japo kidogo jambo ambalo liliulizwa jana kwa Wizara ya Mambo ya Ndani, kwamba wazee wetu sasa hivi inaonekana kuwa wana macho mekundu kwa sababu ya kupuliza kwenye moto. Sasa hivi moto unaokuja sasa siyo wa kupuliza, ni wa umeme wa kukandamiza. (Makofi)
Kwa hiyo, niwahakikishie wananchi kwamba kutakuwa na umeme vijijini, wataweza kujenga viwanda vidogovidogo kama ambavyo wanafanya nchi nyingine za Thailand na China. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba juhudi za maksudi zinaelekezwa kwenye umeme, pia juhudi za maksudi kuendeleza viwanda vidogo vidogo kwa kutumia umeme itaongezeka kwa kiwango kikubwa. Kama mnavyofahamu sasa hivi tunatarajia, kwenye bajeti yetu tutaeleza kwa upana zaidi, tunatarajia kwenye Awamu hii ya Tatu inayokuja tuunganishe umeme zaidi ya vijiji 6,000, ukiunganisha nguvu hiyo kwa wananchi wa vijijini kwa namna yoyote ile mwenye kuweza kusuka nywele kwa kutumia umeme atatumia umeme.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kalemani naomba umalize, muda wako umekwisha.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara, mmi pia nitajielekeza kwenye sayansi na teknolojia, na maelezo yangu ni dakika tano hadi kumi tu kwa sababu ni sayansi na takwimu peke yake. Nimesoma kwa kina sana taarifa ya Mheshimiwa Waziri na nimesikiliza kwa makini sana michango ya Waheshimiwa Wabunge, niwapongeze sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao, ninakiri na kuamini kwamba wasiwasi walionao Waheshimiwa Wabunge kuhusiana na ushamilifu wa tasnia ya nishati ya miundombinu mingine pamoja na viwanda, inatakiwa iangaliwe kwa umakini mkubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijasahau niunge mkono hoja hii ya Mheshimiwa Waziri kwa asilimia mia moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na takwimu za kisayansi. Tunapozungumza viwanda na biashara, tunapozungumza karne ya viwanda vya kati na ikiwezekana vya juu tunamaanisha miundombinu mingi sana na lazima nikubali kuna changamoto, siyo suala la siku moja wala mwaka mmoja. Lakini nishati kwenye viwanda ndiyo uchumi wenyewe, huwezi ukazungumza viwanda, huwezi ukazungumza chochote kama hujazungumza nishati ya umeme, kwa hiyo nakubaliana na Waheshimiwa Wabunge na wananchi wengine wanaochangia kwa hoja hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nianze kutaja takwimu, Serikali namna ambavyo imejipanga na nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wa Bunge lililopita kwa sababu mlipitisha mipango hii na sasa ni utekelezaji wake. Leo Tanzania tumegundua kiasi kikubwa kweli cha gesi ambacho mnajua sasa ni trilioni cubic feet 57 wote tunajua, ni gesi nyingi kwa Afrika sisi ni wa kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyeki, leo tunapozungumza uwezo wa kuzalisha umeme, Tanzania kwa leo anayetuongoza kwa Afrika Mashariki ni Kenya peke yake mwenye megawatts 2,357, Tanzania ni ya pili. Tanzania tuna megawatts jumla wake 1554.12; Wanyarwanda wana megawatts 49, Waburundi wana megawatt 185; Waganda wana megawatts 185.6; kwa hiyo sisi ni wa pili na tunatembea. Tunakwenda mbali na hapa tunazungumzia umeme utakaozalisha viwanda vidogo vidogo na vya kati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunazungumza tuna uhakika wa umeme nimezungumza kwa ujumla wa megawatts nilizotaja, lakini bado tunaendelea na kugundua umeme wa maji, wenzangu wa Kigoma wamezungumza, Kigoma wanatumia umeme wa mafuta ni kweli na wanatumia zaidi ya shilingi milioni sitakwa siku, sasa umeme wa Malagarasi unakuja, tunaanza kujenga Malagarasi kuanzia mwezi wa tisa mwakani na ni ujenzi wa miaka mitatu, 2019/2020 umeme wa maji Kigoma unatembea na tunawatundikia umeme huo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kusema umeme wa viwanda ndiyo huo tunaosema umeme unaotabirika. Sasa hivi wananchi wa Kigoma wanatumia takribani megawatts 15, sasa megawatts 44.8 za Malagarasi zinawatosha na maeneo ya jirani watautumia. Kwa hiyo, viwanda vya tumbaku vya Kigoma, viwanda vya samaki vya Kigoma, viwanda vyote vya nguo na kadhalika vitatembea sasa kwa umeme wa maji. Kwa hiyo, nataka kuwaondoa wasiwasi wanachi wa Kigoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili niunge hoja mkono vizuri kwenye hoja ya viwanda nilikuwa nazungumza ugunduzi wa umeme, tunatoka sasa kwenye umeme wa mafuta tunaelekea kwenye umeme wa gesi na maji. Mwaka huu tarehe 1 Aprili, tumeachana na umeme wa mafuta megawatts 70 wa Aggreko, kwa sababu tunataka kutumia umeme wa gesi tunaanza sasa kusafirisha umeme naomba wananchi na Waheshimiwa Wabunge ninapokuwa nataja zile megawatts muwe mnashangilia basi kwa sababu ni juhudi zenu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa na hizi ni juhudi zenu Waheshimiwa Wabunge leo Kinyerezi I tunazalisha megawatts 150 na tunaongeza megawatts 185 extention yake. Kinyerezi II Mheshimiwa Rais amezindua tena megawatts 240, Kinyerezi III megawatts 300, Kinyerezi IV itakuja baada ya miezi miwili megawatts 320, huo ni umeme wa gesi peke yake na bado tunaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mtwara kuelekea Songea, Symbion na TANESCO wataanza tena megawatts 600. Waheshimiwa Wabunge, suala la umeme, suala la viwanda ni la kufa na kupona, Waheshimiwa Wabunge nizungumzie usafirishaji wa umeme. Tunaanzia Zambia, tunachota umeme Zambia unaoitwa ZTK tunasafirisha kwa kilovolt 400, tunautoa Zambia kuuleta Iringa – Mbeya kilometa 292, tunasafirisha kilowatts 400. Lakini tunautoa huo huo wa megawatts tunaupeleka mpaka Arusha mpaka Namanga, kilometa 412; sasa huu umeme unapita wapi siyo kwa watu na viwanda? Lakini bado tunapeleka umeme North West Grid wenzangu wanajua, umeme huo unatoka Mbeya unapita Sumbawanga, unapita Mpanda, unapita Kigoma mpaka Nyakanazi kilometa 1,284. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizo ni kilovolt 400 za umeme na hapa tunataka tuwaeleze wananchi kwamba sasa umeme utakuwa ni uhakika, lakini bado tuna umeme unaotoka North East Grid kutoka Dar es Salaam Kinyerezi unapita kwa mwenzangu Chalinze Mheshimiwa Kikwete unakwenda mpaka Tanga, una kwenda mpaka Arusha kilometa 664 za umeme, zote ni kilovolt 400 lakini bado tunatembeza umeme huo kutoka Makambako kwenda Songea kilovolt 220 na ni kilometa 100 zote hizo tunatembeza umeme, tunatoa umeme kutoka Geita kwenda Nyakanazi kilovolt 220 kilometa 133, huo ni umeme na yote haya yanajenga viwanda vyetu. Waheshimiwa Wabunge naomba tukumbuke sasa tumedhamiria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu bei ya umeme, bei ya kuunganisha umeme sasa hivi ukijaza fomu ni bure, ukishaunganishiwa service charges sasa hivi ni bure, sasa tunataka umeme gani wananchi, Waheshimiwa Wabunge tutajenga viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kutaja ndugu zangu juhudi ambazo tumezifanya, sasa hivi tunapozungumza kuhusu ugunduzi pale Madimba - Mtwara leo tunazalisha trilioni themanini cubic feet za gesi na tunaweza tukafikisha 130 tunachohitaji watu wajitokeze kuusomba umeme wa gesi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunazalisha umeme mwingi wa gesi kuliko mahitaji pale Mtwara, lakini bado pale Songosongo tuna uwezo wa kuzalisha sasa hivi trilioni cubic feet 130 hadi 200 na hakuna wanaousomba, tunasubiri viwanda. (Makofi)
Waheshimiwa Wabunge, takwimu tunazosema ni za kisayansi na tunataka tujenge viwanda vya kisayansi na siyo maneno. Nilisema nitatumia dakika tano tu kwa sababu nikibaki humu nitawa-bore, lengo langu ni kuwaletea takwimu za kisayansi zilizokusudia kujenga umeme, viwanda pamoja na miundombinu yote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungemze jambo la mwisho ambalo tulieleza kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, kwamba leo Watanzania wanaopata umeme kweli ni wachache asilimia 40 lakini tunakusudia ifikapo mwaka 2025 Watanzania zaidi ya asilimia 75 watakuwa wanatumia umeme wa uhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, natamani niendelee lakini nataka wananchi na Wabunge wabaki na kumbukumbu hizi, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na wananchi kwamba sasa Awamu ya Tano inakuja na umeme unaotabirika wenye gharama nafuu na ambao pia sasa hautakuwa unakatika, tukishaunganisha hizi kilovolt 400 leo ni kweli umeme unakatika kwa sababu tunatumia msongo mdogo zaidi 132 na 220, ifikapo mwaka 2019, tutakuwa tumeshaunganisha miundombinu yote ya kilovolt 400 na umeme sasa utakuwa ni wa uhakika ambao utakuwa haukatikikatiki. Tunajipanga kwa hilo ili kusudi viwanda vya sasa viweze kujengwa kwa uhakika na wananchi wafanye biashara zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache maneno mengi sipendi, nataka mtakapokuja hapa kupitisha bajeti yetu tutaendelea kutundika umeme katika viwanda ili vianzwe kujengwa na maendeleo yaje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nami naomba pia leo kwa mara ya kwanza kabisa nihutubie Bunge lako Tukufu kwa niaba ya Watanzania wote, nikiwakilisha Jimbo la Chato. Nianze sasa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uhai mkubwa na kupata fursa ya kuongea na kuunga mkono hoja hii ya Wizara ya Nishati na Madini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa nguvu kubwa kabisa nimshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuchaguliwa na kuaminika kwa Watanzania wote kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Makamu wa Rais, mama yetu Mheshimiwa Suluhu Hassan, kwa mara ya kwanza kupata Makamu wa Rais kwa akinamama hapa Tanzania. Ni historia kubwa, Watanzania wote tunajivunia na hasa akinamama wenzetu. Tunawapongeza sana akinamama kwa kuwakilishwa na Makamu wa Rais wa akinamama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee pia kumpongeza Waziri Mkuu. Nampongeza Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa kwa kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kadhalika kwa aina ya pekee kabisa nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Ally Mohamed Shein kuchaguliwa kuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa aina ya pekee nimpongeze sana Profesa Sospeter Muhongo, Waziri wangu anavyonisimamia na kuniongoza katika kusimamia majukumu makubwa ya Wizara ya nishati na madini. Nawashukuru sasa kwa nafasi ya pekee wananchi wangu wapendwa, wananchi wa Chato walivyonichagua kwa kura nyingi na wananchi wote kuwawakilisha kama Mbunge wao, naamini wataendelea kunirejesha mpaka uzee wangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa aina ya pekee sasa, niishukuru sana familia yangu, wazazi wangu walivyovumilia kwa kipindi chote katika kutekeleza majukumu yangu ya Wizara ya Nishati na Madini, nawapongeza sana Mwenyezi Mungu awajaalie uhai na uzima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, sasa nijielekeze kwenye kuunga mkono hoja. Kabla sijasahau, niseme naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, waliochangia ni wengi, zaidi ya Wabunge 109, lakini naweza nisijibu hoja zao zote, nitakachofanya, tuombe sana Bunge lako Tukufu kwa ridhaa ya Kanuni za Bunge, itambue ushiriki wa Waheshimiwa Wabunge hawa 109 kwa sababu sitaweza kuwataja, lakini waingie kwenye Hansard. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nianze sasa na kujielekeza kwenye hoja za msingi. Kambi ya Upinzani Bungeni imetoa hoja za msingi sana katika kuonesha kuwa na wasiwasi kana kwamba tutaweza kupata kweli nishati ya umeme ya kuweza kutufikisha kwenye uchumi wa viwanda? Wamekuwa na wasiwasi kwamba, sasa hivi tuna takriban megawatts wanasema 2,780 ndiyo ilikuwa maximum.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mnyika kwamba hizo megawatts 2,780 ambazo tulikusudia kuzifikisha, sasa nimhakikishie miaka mitano ijayo tutakuwa na zaidi ya megawatts 3,000; lakini kuja kufikia mwaka 2025 tutakuwa na zaidi ya megawatts 10,000. Ili kumthibithishia sasa, nimweleze tu kwa upande wa nishati ya gesi, sasa hivi tuna installed capacity nyingi za kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama unavyofahamu, pale Kinyerezi tuna megawatts 150 ambazo tayari tunazo. Tunaendelea kupanua megawatts 185, tutakuwa nazo; Kinyerezi II pia tutakuwa na megawatts 240, unatambua Mheshimiwa Rais alizindua hivi karibuni. Tunaendelea na kuwekeza kwenye nishati hiyo hiyo; tutaendelea kuwa na Kinyerezi III ambayo itakuwa na megawatts 300; lakini bado upo uwezekano mkubwa kuwa na Kinyerezi IV megawatts 320. Bado tuna Somanga Fungu, tuna megawatts 350; bado tuna Kilwa Energy, megawatts 320 na kadhalika. Huo ni umeme wa gesi na tuna uhakika kwamba umeme utakuwa mwingi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee tu kusema, tutakuwa na umeme mwingi wa uhakika sana hasa kwenye nishati ya maporomoko ya maji. Tunatarajia kuwa na megawatts 80 za kutoka Rusumo ambazo tutazigawanya megawatts 26.7 kila nchi. Hizo ni nguvu kubwa, itasaidia sana kwa wananchi wa Ngara na maeneo ya jirani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bado tuna umeme wa Kakono wa maji, sasa hivi tunatumia umeme wa kutoka Uganda kwa wenzetu wa Kagera. Sasa tutaachana na umeme wa Kagera kwa kutoa Uganda, tutaanza kutengeneza umeme wetu. Pale Kakono tutakuwa na megawatts 87 na tutausafirisha kwa kilomita 38.8 kutoka Kakono mpaka kwenda Kyaka. Huo ni umeme wa uhakika, nataka niwahakikishie wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunazo nguvu nyingi za umeme, tunapozungumza tutaachana na matatizo ya umeme, tuna uhakika na hizo ni takwimu za kisayansi. Niendelee sasa kusema tu, kuwa na nguvu ya umeme na bila kusafirisha bado haisaidii, niwahakikishie sana Watanzania kwamba sasa nguvu kubwa ya umeme tutakayokuwa nayo kama tulivyoeleza kwenye taarifa yetu ya bajeti, tunaanza sasa kuusafirisha umeme huo ambao utatatua tatizo kubwa la kukatika kwa umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi tatizo la kukatika kwa umeme wananchi naomba niwaeleze, ni kwa sababu ya mambo yafuatayo: kwanza, umeme tulionao ni kweli una low voltage. Ili kuondokana na low voltage, sasa tunakuja na umeme mkubwa wa Kilovoti 400 na huu umeme utatapakaa nchi nzima. Nianze kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, tutakuwa na umeme wa kilovoti 400 tunaosafirisha kutoka Mbeya unapita Sumbawanga, unaenda Kigoma, unaenda Mpanda mpaka Nyakanazi. Huo urefu mkubwa sana, ni kilomita 1,148. Umeme huo huo tutausafirisha kutoka Nyakanazi mpaka Geita, kilomita 133; umeme huo huo tunautoa Nyakanazi na tutautoa Geita mpaka Bulyankhulu, kilomita 50. Ukanda huo utakuwa na umeme wa uhakika.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati huo huo tutaanza kuzalisha umeme wa Malagarasi. Umeme wa Malagarasi ndiyo utakuwa mkombozi wa umeme mkubwa kwa wananchi wa Kigoma na maeneo ya jirani kama Ngara. Huo umeme tunaanza kuutekeleza kuanzia mwakani na utakamilika 2019. Kwa hiyo, niwahikikishie wananchi wa Kigoma na eneo la jirani kwamba tunapozungumza eneo la umeme, kwa sasa hivi tumejifunga mkanda, ni suala la kufa na kupona, Watanzania wote watapata umeme wa uhakika ifikapo 2025. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuzungumzia suala hilo hilo la umeme. Tutausafirisha umeme mwingine; nataka niwaeleze mwone jinsi Tanzania nzima itapata umeme wa kutosha. Tutakuwa na umeme wa kutoka North East Grid na huo umeme tutaanza sasa kuutoa Kinyerezi kwa upande wa mashariki. Utatoka Kinyerezi utaenda Chalinze, utaenda Tanga mpaka Arusha mpaka Namanga kilomita 664. Kwa hiyo, Watanzania wa maeneo yale watakuwa wana uhakika wa umeme ambao haukatikikatiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la kusafirisha umeme mkubwa ni kuhakikisha kwamba umeme uliopo sasa ni mkubwa, unatosha kwa matumizi ya viwandani, matumizi ya nyumbani na biashara ndogo ndogo pamoja na biashara kubwa. (Makofi)
Waheshimiwa Wananchi na Waheshimiwa Wabunge, nataka tena niwahakikishie, tunao mradi ninaousema wa backbone. Huu mradi ni wa umeme mkubwa. Ni umeme ambao unatoka Iringa unapita Dodoma unakwenda Singida mpaka Shinyanga na unatumika kwa maeneo yote ya Kanda ya Ziwa na ndiyo umeme wa uhakika mkubwa tunaouzungumzia, siyo umeme wa kutakatikakatika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, suala la kukatika kwa umeme, baada ya miradi hii kukamilika mwaka 2018/2019 yatapungua kwa kiasi kikubwa sana. Sasa hivi niseme tu, siyo kwamba sasa hivi tuna mgao wa umeme. Hatuna mgawo, isipokuwa kuna kukatikakatika kwa umeme kutokana na sababu nilizozitaja hapo awali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka niwahakikishie hilo kwamba tunaposema kutakuwa na nguvu kubwa ya umeme, ni umeme wa nguvu kubwa utakaofaa viwandani. Naelewa Mheshimiwa Matiko anajua kwamba, kuna mgao wa umeme na dada yangu naomba uridhike kuwa tatizo hilo litapungua sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie REA na ninapokuwa najibu haya, najibu kwa ujumla wake kwa sababu maswali ni mengi sana. Nizungumzie REA. Ni kweli kabisa REA, awamu ya pili imekwenda maeneo yote tuliyopeleka awamu hiyo, lakini umeme unaishia kwenye vituo tu vya vijiji na siyo kwa wananchi. Lengo kubwa la mradi wa REA, awamu ya pili lilikuwa ni kusafirisha miundombinu ya umeme ili kufikisha vituo vikubwa na baadaye usambazaji kwenda kwa wananchi katika vitongoji uendelee.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa awamu inayokuja, wananchi wengi wameuliza, Waheshimiwa Wabunge mmeuliza kwamba umeme unapita kwenye nyuso za watu. Sasa unakuja mradi unaoitwa underground distribution transformer. Mradi huu unaanza kutekelezwa kuanzia Januari mwakani na utakamilika miezi 18 tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la mradi wa distribution hiyo ninayosema ni ya underground, siyo chini ya ardhi Mheshimiwa Matiko kama unavyosema. Lengo lake, ni kupita kila mahali ambapo transformer na miradi mikubwa ya umeme ambapo Kilovoti 33 imepita, itakuwa sasa inatandaza umeme kutoka kwenye vituo hivyo kwenda kwenye miji ya wananchi. Kwa hiyo, umeme huo utafika kwenye kaya za wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka niwahakikishie suala kwamba kuna maeneo yameachwa, yatazibwa pengo pamoja na mradi tunaosema wa underground distribution transformer. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mradi mwingine huo huo ambao sasa utapita kwenye njia zilizopitisha umeme wa kilovoti 33, kutandaza umeme kutoka kwenye vituo hivyo umbali wa kilomita 10. Huo unaitwa European Union Distribution Grid na utasaidia sana kueneza umeme kwenye maeneo yote.
Mheshimiwa Naibu Spika, huo mradi pia unagharamiwa takriban shilingi bilioni 58.4 na mradi ule utakapokuwa unapita, maeneo yote ambayo hayakufikiwa na umeme kwa umbali wa kilomita 10 kutoka kwenye nguzo kubwa, sasa utapatiwa umeme wa uhakika na baadaye utapitisha umeme huo huo wa kilovoti 400.
Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, nilikuwa nataka tu kueleza maelezo ya kina kabisa kabisa kuhakikisha kwamba umeme unaokuja ni mkubwa na utaingia kwenye Vijiji vyetu na wananchi wote watapata umeme wa uhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie sasa kuzungumzia kwenye suala la umeme kuhusiana na kuunganisha Vijiji kwa Vijiji. REA awamu ya tatu ni kweli kabisa, kama tunavyosema REA ya awamu ya pili inakamilika mwezi Juni mwaka huu. Tunachofanya sasa hivi ni kukamilisha uhakiki kutambua vijiji ambavyo havijapata umeme hadi leo, lakini vilikuwa kwenye scope ya REA II, lakini kadhalika ni kuainisha vijiji vyote ambavyo havijapata umeme ama vilikuwa kwenye scope ama havikuwepo kwa sababu lengo kubwa ni kupelekea umeme katika vijiji vyote vilivyosalia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Waheshimiwa Wabunge wala wasiwe na wasiwasi kwamba wanahitaji kuona orodha ama kijiji chako kitasahaulika REA ya awamu ya tatu itapeleka umeme kwenye vijiji vyenu vyote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba hili tatizo la akinamama kujifungua kwa kutumia tochi, hili tatizo la akinamama kuonekana na macho mekundu na wakadhaniwa ni wachawi, kwenye hii awamu ya tano miaka mitano hadi kumi ijayo litatokomea kabisa. Tunataka akinamama badala ya kupuliza moto wa mkaa waanze sasa kukandamiza na kuona mwanga mweupe wakati wa usiku. Nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwa sababu Serikali imejipanga, ina uhakika wa kuwapatia umeme wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie bei ya umeme. Umeme unapokuwa mwingi na umeme unapokuwa wa uhakika, kwa kawaida gharama za umeme zinashuka bei. Kwa sasa kwa sababu tunatumia kwa kiwango kikubwa umeme wa gesi na kiwango kikubwa sana pia umeme wa maji, tunataka sasa kuachana na umeme wa mafuta.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua tulizochukua kuachana na umeme wa mafuta ni kama ifuatavyo:-
Kwanza, mikataba yote iliyokuwa inatumia umeme wa mafuta inapokwisha sasa hatuiendelezi. Huo ni uamuzi wa Serikali. Kwa hiyo, tumeachana na umeme wa Aggreko, tumeachana na umeme wa Symbion kwenye mikataba ya dharura. Sasa hiyo ni kuonesha kwamba Serikali imejipanga kuhakikisha kwamba umeme tunaoutumia ni wa gharama nafuu na unaondoa gharama kubwa kwa Serikali na wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, gharama za umeme kwa sasa kama mnavyojua, sasa hivi ili uunganishe umeme kwa wananchi wa Vijijini, ni sh. 27,000/=.
Mheshimiwa Naibu Spika, mbali na hapo, Mheshimiwa Waziri wangu wakati anawasilisha bajeti yake alieleza kwa kina sana, kwanza tumepunguza gharama zote za kuunganisha na kuomba umeme, lakini kadhalika tunatarajia wananchi watakapoanza kutumia umeme mwingi wa gesi, gharama huenda zikapungua zaidi. Kwa sasa tumeanzia kuondoa gharama za umeme wanapoomba leseni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa tumeanzia na kuondoa gharama za umeme wananchi wanapoomba leseni. Kwa hiyo, wananchi wetu sasa hivi, twende tuwaeleze huko kijijini hawatakiwi kuwasilisha ombi kwa kulilipia, anakwenda anajaza fomu, anaipeleka, anapata umeme, kimsingi ni bure, ukiondoa ile gharama ya kodi ya VAT 28,000. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini akiunganishiwa umeme pia, ataendelea kuutumia umeme huo, TANESCO akija kufanya service halipii kitu chochote na penyewe ni bure. Kwa hiyo, tuwatangazie wananchi wajue sera za Serikali, lakini ili kusema kwamba tuna bei ya chini, tunajilinganisha na nani? Sisi tunaeleza mambo ya kisayansi. Kwa sasa hivi sisi tunazalisha Megawatts kwa ujumla wake 1,554.12 kwa sasa kwa ujumla wake. Kwenye taarifa yetu tumesema 1,461 zipo kwenye grid lakini ukijumlisha na ule ambao haupo kwenye grid ni 1,554.12.
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzetu wa Kenya, kwa Afrika Mashariki ndiyo wanaoongoza peke yao wao wana megawatts 2,357, lakini nchi nyingine zote ziko chini yetu. Waganda kwa sasa wana megawatts 849, sasa hivi watu wa Burundi wenyewe wana megawatts 49 na wenzetu wa Rwanda wana megawatts 185.9, kwa hiyo, sisi ukiji-rank bado tupo juu kwa maana ya kuzalisha umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwaeleze, maana yake Waheshimiwa Wabunge tunapozungumza masuala ya umeme kwa sababu tunazungumza uchumi lazima tuzungumze kwa takwimu. Sasa tunajilinganisha vipi kwa bei…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri naomba umalizie. Naomba uwe unamalizia, kengele ya pili tayari.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, sijazungumzia madini, nataka nizungumzie kwenye madini, nikimbie basi niende kwenye madini nizungumze kidogo. Pamoja na kwamba nimejieleza sana kwenye masuala ya umeme, lakini pia nizungumze kidogo kwenye tasnia ya madini.
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe tu kusema, kwa sasa Wizara yetu inatenga maeneo mengi kwa ajili ya kuwagawia wananchi. Tumesema ni kilometa 12,000 tunatenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo. Maeneo yatakayotengewa sasa leseni na utafiti unaoendelea yako ya Kasubuya hekta 498, Malengwa hekta 682, yako pia ya Geita takribani hekta 2001 na mpaka kule Chato-Msasa hekta 12,28 na kadhalika na kadhalika. Nyamongo tunaendelea kufanya utafiti kugundua maeneo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba muda umekwisha, napenda sana nipatiwe muda niendelee kusema zaidi kwa sababu ni nafasi ya pekee lakini kwa sababu muda umekwenda sana...
NAIBU SPIKA: Wakati mwingine Mheshimiwa.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu niunge mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kuchangia bajeti ya Wizara hii muhimu. Pamoja na raha sana zilizotolewa na Mheshimiwa aliyemaliza kuzungumza na mimi basi nizungumze machache.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kuchangia kidogo tu kuhusiana na mikakati ya Serikali kuhusiana na masuala ambayo yamezungumzwa na wenzetu wa Kambi ya Upinzani. Nikubaliane na taarifa ya Kambi ya Upinzani ukurasa wa nane na tisa kwamba yapo mambo ya msingi katika mgodi wetu wa Nyamongo kwamba wananchi hawahitaji kunyanyaswa, kudhulumiwa na Serikali kufumbia macho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kufafanua kidogo, nikubaliane na Waheshimiwa Wabunge kwamba zipo sababu za makusudi za Serikali yetu kuchukua hatua dhidi ya unyonyaji unaoweza kujitokeza kwa wananchi wetu. Nikubaliane kwa kusema tu kwamba, Serikali imechukua hatua madhubuti na niwapongeze sana Waheshimiwa Wabunge wa Tarime, Mheshimiwa Heche pamoja na Mheshimiwa Matiko wameshirikiana sana na Serikali hii kuhakikisha kwamba migogoro ya North Mara inamalizika mara moja. Hivi karibuni Serikali yetu imechukua hatua ambazo pia ni shirikishi kwa kuwashirikisha viongozi wa vitongoji wa North Mara kadhalika kuwashirikisha Waheshimiwa Wabunge wanaotoka karibu na mgodi huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme tu inawezekana taarifa ya Kambi ya Upinzani ingekuwa nzuri sana kama ingeweza kutambua juhudi zinazochukuliwa na Serikali katika kuondoa matatizo ya Nyamongo kuliko kuacha kama ilivyo. Nitambue tu kwamba Mheshimiwa Heche pamoja na Waheshimiwa Wabunge wameshirikishwa sana kwenye utatuzi wa migogoro hiyo. Wananchi wa Mara wana masuala ya msingi sana, ni kweli kuna masuala ya mazingira, kuna masuala ya mashimo, kuna masuala ya ajira na kadhalika lakini Serikali haijayafumbia macho. Nataka Waheshimiwa Wabunge pamoja na wananchi wajue kwamba Serikali inachukua hatua madhubuti za kuondokana na migogoro ya North Mara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama hiyo haitoshi niseme tu kwamba ile timu iliyoundwa na Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini ambayo kwa sasa bado inakamilisha taarifa zake hatua zitakazochukuliwa pia zitakuwa ni shirikishi. Zitashirikisha Waheshimiwa Wabunge, Madiwani pamoja na Wenyeviti wa Vitongoji husika wa North Mara. Kwa hiyo, nilitaka kuliweka vizuri hilo siyo kweli kwamba Serikali imeyafumbia macho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mgogoro wa Bismarck na mgodi wa Acacia. Ni vizuri tukatambua Sera ya Uwekezaji pamoja na Sera zote za Nishati, Madini na za Mazingira zinahamasisha sana uwekezaji wa ndani na nje. Kwa kutambua hilo, nikubaliane kwamba kampuni ya Bismarck ni ya wazalendo na miaka ya 96 ilipewa leseni ya kutafuta madini kule Mgusu, lakini mwaka 2012 yenyewe ikaamua kuachia leseni zile. Hii ni kwa sababu za kiteknolojia za uchimbaji na mambo mengine. Baadaye sasa maeneo yale yakaombwa kumilikishwa na kampuni ya Pangea Minerals ambayo ni subsidiary company ya Barrick ambapo sasa wanaita Acacia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niseme sasa na ni jambo la msingi sana Waheshimiwa Wabunge tukitambua kuwa Bismarck ambayo pia ni kampuni ya Watanzania waliamua tu kufanya makubaliano ya kwao kabisa kimkataba na kampuni ya Acacia. Baada ya kutofautiana wakaamua kupelekana kwenye mahakama za usuluhishi za nje. Nitake tu kukubaliana na Waheshimiwa na niwaombe kwamba inapotokea mazingira ya namna hiyo watuletee taarifa Serikalini ili Serikali iyafanyie kazi kwa ufasaha. Sasa hivi suala linalozungumzwa la Bismarck na kampuni ya Acacia wala halipo hapa, wamepelekana wao kwenye usuluhishi wa kimataifa nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tungependa sana Waheshimiwa Wabunge tuleteeni taarifa lakini kwa sasa hivi kulizungumza suala hilo lipo kwenye mahakama ya usuluhishi tutakuwa tunaingilia mhimili mwingine. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge niwaombe sana tuvute subira kwenye masuala haya mawili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nichangie kidogo kuhusu ajira. Mheshimiwa aliyemaliza kuzungumza wa upande wa pili amesema kwamba wananchi wanaachiwa mashimo, hakuna ajira na wanaajiriwa kwenye kazi ndogo ndogo. Nitoe mfano kwa kampuni ya North Mara, ajira kwa Watanzania ni 968 ambapo wageni ni 57. Kwenye mgodi wa Bulyanhulu Watanzania walioajiriwa ni 1,755 na wageni wapo 71. Mgodi wa GGM Watanzania walioajiriwa ni 1,568 na wageni 68.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia uwiano ule bado Watanzania tunapata ajira lakini nikubaliane tuna haja ya kuongeza zaidi. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge niseme tu kwamba michango ya wawekezaji wa nje nayo ni mikubwa na inachangia kwenye pato la Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja hii. Ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote niunge
mkono hoja, pia niungane na waliotoa pole kwa wenzetu wana-CCM ambao walipata
majeruhi huko Moshi, tuwaombee ndugu, jamaa na wengine wapate kupumzika salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nitajielekeza kwenye mambo ya msingi na niwapongeze
sana Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia, kwenye hoja za maandishi pamoja na zile za
maneno. Kwa ujumla tuna hoja 30 za maneno na za maandishi nane, kwa hiyo, zilikuwa ni hoja
nyingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge nianze tu na
kuzungumza kidogo, kuhusiana na masuala ya kazi ya kusambaza umeme, hasa kwa Shirika letu
la TANESCO. Nikubaliane na Waheshimiwa Wabunge speed kulingana na uharaka wa
utandazaji umeme kwa kweli haulingani na uwezo wa TANESCO kwa sasa, lakini tunachofanya
ili kuendana na changamoto hizo sasa Serikali imeweka mikakati ya kufuata ili kuhakikisha
kwamba wananchi wanapata umeme kwa haraka kutoka katika shirika letu la TANESCO.
La kwanza kabisa, tunawashukuru Bunge lililopita lilitupitishia bajeti ya kuanzisha ofisi 47
kwa ngazi za Wilaya, sasa tunaanza utaratibu wa kuimarisha ofisi na kujenga ofisi nyingine mpya
katika maeneo ambako hakuna ofisi. Hii ni hatua madhubuti sana kuharakisha upatikanaji wa
umeme katika maeneo yale.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sambamba na hilo kwa sababu wakati mwingine ni
ufinyu wa bajeti, ili kupambana na hatua hiyo, TANESCO sasa imeanza utaratibu ufuatao:-
Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, kwanza kabisa tulishaagiza
transfoma zote pamoja na nguzo yataanza sasa kununuliwa hapa nchini. Hii itarahisisha sana
usambaziji wa umeme kwa kasi kubwa. Kwa hiyo, tuna imani kwamba kwa hatua hii
itaharakisha sana usambazaji wa umeme mijini na vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua ya pili, wakati tunajipanga kujenga ofisi, tumeanza sasa
kuanzisha madawati ya huduma kwa wateja mahala ambako kuna wateja wengi, badala ya
kusubiri kujenga ofisi mpya. Hii ni hatua madhubuti itaturahisishia sana kusambaza umeme kwa
wananchi wengi na kwa muda mfupi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua nyingine tumeagiza shirika letu, kuanzia Januari mwaka
huu, litaanza sasa kufata wateje walipo badala ya lenyewe kufuatwa na wateja. Hii itasidia
sana, kwa sababu maeneo mengine kwa wananchi hawawezi kufikia ofisi zetu na hata wakifika
inakuwa kwa gharama kubwa na wakati mwingine wanakata tamaa. Kwa hiyo, sasa
wataalamu wa TANESCO wa shirika letu wataanza kufuata wateja walipo ili kuharakisha
huduma hizi mahsusi. Kwa hiyo, tunaamini kwamba utaratibu huu utachangia sana kuharakisha
uzambazaji wa umeme ili kulingana na kasi ya ukuaji wa umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika sambamba na hilo nizungumzie kidogo kukatikakatika kwa
umeme. Ni kweli, hasa maeneo ya Lindi na Mtwara hata kule Geita kwa Mheshimiwa Kanyasu
na maeneo ya Dar es Salaam. Kazi inayofanyika sasa hivi ni pamoja na ukarabati wa
miundombinu ambayo kwa kiasi kikubwa mingi imekuwa ya muda mrefu. Sasa katika kipindi hiki
kifupi, maeneo mengi yataendelea kupata shida kidogo, lakini ni tatizo la muda mfupi, jitihada
madhubuti zinafanyika ili kurekebisha hali hii. Ni matarajio yetu ndani ya miezi hii miwilii ukarabati
wa maeneo mengi utakuwa umekamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa suala la Lindi na Mtwara nielezee kidogo. Lindi na Mtwara
wananchi wa Lindi wanatumia megawati 18. Kwa sasa mashine moja imeharibika, inafanyiwa
ukarabati hasa kuhakikisha kwamba ile mashine iliyoharibika inafanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sambamba na hilo ujenzi wa kusafirisha umeme sasa
kutoka Mtwara kwenda Lindi ambako kituo cha kupoza umeme pale Mnazi Mmoja kinajengwa
na kinatarajiwa kukamilika ndani ya miezi miwili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kwa wananchi wa Mtwara baada ya kituo kile
kukamilika, hasa kile kituo cha substation kutoka kilovolti 33 kwenda kilovolti 130 zitakapokamilika
matatizo ya kukatika umeme kwa wananchi wa Lindi na Mtwara yatatatulika kwa mara moja.
Kwa hiyo ni vizuri tuwaeleze wananchi wa Mtwara, ni kero hata kwetu sisi tunaliona lakini ni
jambo ambalo linafanyiwa kazi kwa kina sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo lilizungumzwa, ni suala la sera ya mafuta
kutafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili. Ni kweli kabisa suala la kutafsiri lugha za kigeni sasa ni muhimu
sana kwa sababu watumiaji wengi ni Watanzania ambao ndio kwa kiasi kikubwa wanatumia
lugha ya Kiswahili. Mkatati umeshaanza, timu ya wataalam imeshaundwa inayojumuisha wizara
yetu pamoja na taasisi zinazojumuisha Wizara yetu; lakini kazi hii itafanyika kwa kushirikiana na
TUKI ambao ni wataalam wa kutafsiri.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ili kuepika kufanya kazi na TUKI peke yake, na kuna
masuala mengine ya kiteknolojia na ya kitaalam zaidi, lazima timu mbili zifanye kazi kwa
pamoja. Kwa hiyo, utaratibu unaofuata sasa ni kukaa pamoja ili kuanza kazi hiyo mara moja. Ni
matarajio yetu ndani ya miezi miwili/mitatu timu hiyo itakuwa imeshaanza kazi, pamoja na TUKI.
Kwa hiyo, suala la kutafsiri linafanyika na utaratibu tumeshauanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulinda Tanzanite. Kwanza niseme kwamba ni kweli kabisa
madini ya Tanzanite hapa ulimwenguni yanapatikana Tanzania peke yake, hakuna sehemu
nyingine, kwa maana ya yanakochimbwa. Lakini nikiri kwamba, yako matatizo na changamoto
ambazo zimesababisha pia control yake kuwa kidogo. Hata hivyo hatua za Kiserikali ambazo
zimefanyika, ni vizuri kuwaambia Waheshimiwa Wabunge kwamba hili neneo kuanzia mwaka
2001 lilianza kutengwa kama eneo tengefu ili kuhakikisha kwamba rasilimali ya Tanzanite
haitoroshwi nje bila kuzingatia utaratibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni changamoto kidogo, ilikuwa ngumu na ujenzi wa fence
ulifanyika mwaka 2005, lakini kwa bahati mbaya sana wananchi wanaozunguka maeneo yale
waling‟oa fence pamoja na vyuma. Kwa hiyo, mkakati unaofanyika sasa ni kujenga fence ya
mawe pamoja na tofali, tunatafuta fedha kwa ajili ya kujenga fence hiyo. Kwa hiyo, nikushukuru
Mheshimiwa Ndassa yeye alikuwa Mwenyekiti wa Nishati na Madini huko nyuma huko nyuma
kwa kuliona hili, lakini jitihada zinafanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, mikakati mingi sana imefanyika katika eneo hili. Pamoja na
kuanzisha Police Post, kimejengwa Kituo mahususi cha polisi pale Mererani ili kuhakikisha
kwamba udhibiti unakuwa imara na ambao kwa kweli ni shirikishi. Tunaamini kwamba hatua hizi
zimechangia kwa kiasi kikubwa kusaidia madini yetu yasiende nje sana. Lakini pia, kuna joint
committee iliyoundwa ikishirikisha taasisi mbalimbali ikiwemo Uhamiaji, TRA na nyingine ili
kudhibiti utoroshaji huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sambamba na hayo ili kupunguza utoroshaji wa madini
ya Tanzanite, mwaka 2010 Sheria ya Madini Mpya ilivyotungwa ilipunguza kiasi cha mrabaha
kutoka asilimia tano kwa madini yaliyokatwa kurudi asilimia moja ili kuvutia Watanzania wengi
kukata madini ya Tanzanite hapa nchini. Kwa hiyo, hizo ni hatua ambazo Serikali imechukua,
ambazo ni vizuri sana kuwaeleza wananchi, lakini pia, changamoto tunazichukua bado
tutaendelea kuimarisha ulinzi zaidi katika eneo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu REA III nikubaliane na Waheshimiwa Wabunge wengi,
REA II iliyokamilika hivi sasa kwanza niseme imekamilika kwa asilimia 95.8 na asilimia 4.2 iliyobaki
ni kwa ajili ya kuwaunganishia umeme wateja. Sasa kazi ya kuunganisha umeme inategemea
mambo mawili, la kwanza utayari wa mwenye nyumba, mtaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, basi nijielekeze la
mwisho, nizungumzie kuhusiana na mikakati ya REA III. REA III imeshaanza maeneo ya mikoa sita
kama nilivyotaja juzi, Mkoa wa Pwani, Mara, Arusha, Iringa, Njombe, Mbeya pamoja na
Songwe, kwa hiyo, tumeshaanza na utaratibu utakwenda hivyo kwa nchi nzima, na mpaka
kufikia tarehe 31 Machi nchi nzima sasa wakandarasi watakuwa wameingia kwenye mikoa yote
kwa ajili ya kutekeleza Mradi wa REA III.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi zitakazofanyika, nisaidie kunipa dakika moja kwenye hili, ni
pamoja na kufikisha umeme kwenye vijiji vyote vilivyosalia ambavyo ni 7,873 pamoja na
vitongoji vyake. Lakini kazi ya pili ni kupeleka umeme kwenye taasisi zote za umma, hapa nina
maana ya hospitali, zahanati, magereza, polisi, shule, masoko pamoja na pampu za maji. Kwa
hiyo, huu ni mradi mkubwa, tunatarajia wananchi wote watapata umeme kwa kupitia mradi
huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia utapeleka umeme kwenye maeneo ambayo yako nje na
gridi, hasa visiwani pamoja na yale ambayo yanapitiwa na Hifadhi za Taifa. Ni mradi wa miaka
minne hadi mitano, kwa hiyo, mwaka wa 2020/2021 tuna matarajio kwamba vijiji vingi vitakuwa
vimepata umeme kupitia mradi huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie tu kusema jambo hili ambalo nadhani ni tamu sana
kwa Waheshimiwa Wabunge. Hatua tunayofanya kwa sasa ni utandazaji wa umeme shirikishi.
Kabla mkandarasi hajaingia kwenye site yoyote ile ataanza kwanza kupiga hodi kwa Mbunge husika. Hii itasaidia sana kupeleka umeme maeneo ambako wananchi mnajua vipaumbele,
lakini pia ataenda hata kwa Mheshimiwa DC na Mkuu wa Mkoa ili kusaidia katika usimamizi
wake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo kwa sababu muda ni mfupi,
ningependa niseme mengi sana kuhusu hili, nashukuru sana. Naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
NAIBU WAZIRI WA NIASHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa fursa hii. Nianze na mimi kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kazi kubwa waliyofanya, pamoja na Katibu Mkuu. Hata hivyo, awali ya yote nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa namna anavyosimamia rasilimali za nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yako mambo ambayo yamezungumzwa kwa wingi sana katika bajeti hii na yanahusu sana kwa kiasi kikubwa Wizara ya Nishati na Madini. Hata hivyo nitajielekeza sana kwenye hoja za nishati kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Spika, suala la LNG, suala la kiwanda cha kusindika gesi; Waheshimiwa Wabunge wameuliza kama mradi upo ama haupo.

Mheshimiwa Spika, nataka nilieleze Bunge lako Tukufu kwamba mradi wa LNG wa Lindi bado upo na wala hautahamishwa, hauendi Msumbiji wala sehemu yoyote. Na hapo tulipofika sasa tuko katika utekelezaji na tarehe 24 mwezi huu watalaam wanaondoka kwenda Trinidad & Tobago kwa ajili ya kukamilisha mazungumzo na wajenzi; na wajenzi watakaojenga ni makampuni makubwa ya ExxonMobil, BG Shell, pamoja na TPDC. Kwa hiyo, mradi huo upo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lipo suala la ujnzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Uganda hadi Tanga.

Mheshimiwa Spika, nilitaka tu kutoa taarifa kwa sababu ni suala la maendeleo, tunajenga viwanda. Utaratibu wa ujenzi wa bomba hili umeshaanza na sasa nitoe taarifa sahihi kwamba bomba hili litafika katika mikoa minane ya nchi yetu na wilaya 24 na urefu wa kilometa 1,445 kwa kiasi kikubwa katika Tanzania. Hatua inayofuata katikati ya mwezi unaokuja tutasaini, lakini pia tutafanya uzinduzi na ujenzi wa jiwe la msingi huko Tanga katika eneo linaloitwa Chongoleani, Mjini Tanga. Kwa hiyo, ujenzi unaanza na utekelezaji utakamilika mwaka 2025. Kwa hiyo, Ujenzi wa Mradi wa Bomba la Mafuta unaendelea vizuri.

Mheshimiwa Spika, mradi wa Makambako Songea; huu ni mradi muhimu sana. Wananchi walio wengi wa maeneo ya Mikoa ya Njombe, Songea na Wilaya zake wanautarajia sana mradi huu, uko katika hatua nzuri. Hata hivyo niseme tu commitment ya Serikali, kwa mwaka huu wa fedha tumetenga bilioni kumi na moja kwa ajili ya kwenye mradi huu, na ujenzi umeshaanza kufika katika hatua nzuri na mwezi Oktoba mwakani utakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini niwaambie tu shughuli kubwa zinazofanyika katika mradi huu, ya kwanza kabisa ni ujenzi wa vituo vya kupoza umeme vilivyoko Madaba, Njombe pamoja na Songea Mjini na utakamilika hivi karibuni. Mradi mzima utagharimu Swedish Krona milioni 620, Dola za Marekani milioni 20 na shilingi bilioni 17 za Tanzania. Kwa hiyo, utekelezaji ukwenda vizuri mwezi Agosti mwakani utakamilika.

Mheshimiwa Spika, katika mradi huu kazi zitakazofanyika ni pamoja na kujenga transmission line ya urefu wa kilometa 250 kutoka Njombe hadi Songea, transmission ya kusambaza umeme katika vijiji 120 katika Wilaya nilizozitaja na kuwaunganishia umeme wateja 22,700. Kwa hiyo ni mradi mkubwa na unakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mradi wa Kusambaza Umeme Mijini, maana wako Wabunge wamehoji kwamba tunapeleka umeme vijijini tu lakini mjini hatuendi. Niseme tu kwamba tumepata Dola za Kimarekani milioni 424 kwa ajili ya ujenzi na miundombinu ya mijini ili kuhakikisha kwamba
mijini tunakuwa na umeme wa kutosha ili viwanda vinavyojengwa mijini sasa viwe endelevu na kazi hii inafanyika vizuri. Kazi zitakazofanyika, ili nitumie nafasi hii vizuri, sana sana ni ufungaji wa transfoma kubwa na ndogo zinazoanzia KVA 50, KVA 100, KVA 200 hadi KVA 315. Hii ni katika kuhakikisha kwamba umeme mijini pia unaimarika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, REA Awamu ya Tatu; ninatambua kwamba muda ni mfupi sana, lakini niwape taarifa Waheshimiwa Wabunge kwamba tarehe 24 Juni (kesho kutwa tu) tunaanza sasa uzinduzi rasmi wa mradi mkubwa wa REA Awamu ya Tatu katika mikoa yote Tanzania Bara. Tunaanza na Mkoa wa Manyara tarehe 24, tarehe 4 hadi 5 tunakwenda Katavi na Rukwa, tukitoka Katavi na Rukwa tunaenda Mtwara na Lindi halafu tunaenda Kigoma. Kwa hiyo, wananchi wa Kagera Nkanda, Kazumulo pamoja na kule Kagera tutaendelea kuzindua hadi mikoa yote ikamilike kwa muda mfupi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, muda ni mfupi, lakini niendelee kuzungumza kidogo suala la usambazaji wa gesi majumbani.

Mheshimiwa Spika,…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzunguzaji)

NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana kwa kunisikiliza.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. DKT. MEDARD M. KALEMANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika miradi ya barabara za Mikoa inayotengenezwa kwa kutumia fedha za Mfuko wa Barabara kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018, barabara kwa ajili ya upgrading to DSD Mkuyuni kutoka Chato Mjini, eneo la Mkuyuni imewekwa kilometa nne tu. Ukweli ni kwamba barabara hii ina urefu wa kilometa 18 kutoka Chato Mjini kupitia Mkuyuni, Rubambangwe JCT, Kanyama, Ilemela hadi Busarara. Barabara hii inaunganisha barabara inayotoka Nyamilembe hadi Katoke inayoungana na barabara ya Biharamulo kuelekea Bukoba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa barabara hii ni muhimu katika kuunganisha barabara kuu ya kwenda Biharamulo na Bukoba na kwa kuwa, ilikuwa katika sehemu ya ahadi za Serikali tangu Bunge la Kumi katika miaka ya 2013/2014, naomba sasa ijengwe kama ilivyotarajiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ukurasa 285 katika jedwali la barabara zilizotengewa fedha kwa kiwango cha lami barabara hii inaonekana kuwa kilometa nne tu ndizo zitakazojengwa kwa gharama ya millioni 300 pamoja na kwamba barabara hii haiishii hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa barabara hii ni mwendelezo wa kilometa nne zilizotajwa katika bajeti ya Wizara zinaishia njiani katika JCT ya Rubambungwe na kuiacha sehemu kubwa bila kujengwa kwa kiwango cha lami. Naiomba sasa Wizara ya Uchukuzi, Ujenzi na Mawasiliano waingize sehemu nzima ya barabara hii yenye jumla ya kilometa 18 ili ijengwe kwa kiwango cha lami katika mwaka huu wa bajeti 2017/2018, badala ya kujenga kilometa nne tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia wakati Mheshimiwa Waziri anahitimisha hoja asisitize kuwa barabara hii itatekelezwa ili wananchi wa maeneo haya na maeneo jirani wapate unafuu wa kufanya shughuli zao za kiuchumi kwa kuwa na usafiri rafiki na rahisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nichukue nafasi fupi sana kuchangia katika Wizara hii, lakini awali ya yote niwapongeze sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri na timu yake ya wataalam. Nawapongeza kwa kazi kubwa waliyofanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala ambalo nitachangia kwa kiasi kikubwa sana ni matumizi mbadala ya mkaa pamoja na kuni. Kama ambavyo wameeleza wenzetu katika taarifa hii, mkakati waliouweka ni pamoja na kuonyesha kwamba matumizi ya mkaa pamoja na kuni yanapungua kwa kiwango kikubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo mkakati mkubwa na wenye dhamana kubwa ya kuhakikisha kwamba mkakati wa kuni na mkaa unaisha na kwamba sasa tunatumia nishati mbadala ni Wizara yetu ya Nishati na Madini, kwa hiyo nitajielekeza kwenye hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni tuna mpango wa kimataifa wa matumizi endelevu unaotaka kuhakikisha kuwa matumizi ya mkaa pamoja na kuni yatakomea ifikapo mwaka 2030.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na hayo, kwanza kabisa nitumie nafasi hii kuwaeleza Waheshimiwa Wabunge na wananchi kwa ujumla kwamba matumizi ya mkaa katika nchi zinazoendelea hadi sasa yanafikia asilimia 90 ya nishati ya umeme duniani. Hiyo ni takwimu ya Benki ya Dunia. Lakini pamoja na hayo bado kwa nchi zetu zinazoendelea hasa zilizoko chini ya Kusini mwa Afrika, pamoja na maendeleo ya nchi za Afrika tani milioni 2.3 kwa nishati tunayotumia inatokana na kuni pamoja na mkaa. Kwa hiyo, ni changamoto kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama Serikali, mpango madhubuti uliopo ni kwamba, moja, sisi ni wanachama wa kimataifa wa matumizi mbadala ya nishati ya kuni pamoja na mkaa. Mkakati madhubuti ambao Serikali tumechukua, napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge, ni kwamba sasa Shirika letu la TPDC kuanzia mwaka 2013/2014 lilianza rasmi kujenga miundombinu ya matumizi ya gesi kuanzia mijini mpaka vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa hatua ya kwanza, tumeanza na Dar es Salaam. Mwaka 2014/2015 tumeshaunganisha wateja 70 ambao tumewaunganishia miundombinu ya gesi katika maeneo ya Mikocheni. Kwa hiyo, ni hatua kubwa, lakini hatua ya pili tumepeleka matumizi hayo hayo ya gesi kwenye magari yetu. Hadi sasa tunapozungumza magari takriban 60 yanatumia gesi, hiyo ni hatua ya kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hatua ya pili ni kupeleka miundombinu ya matumizi ya gesi, na hii gesi ninayoizungumzia ni ya aina hii ya mathane, si ile gesi ambayo tumeizoea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua kuna taarifa yetu itakuja hapo baadaye tutaeleza kwa upana zaidi; lakini kwa ufupi tu niseme kwamba kuanzia mwaka 2017/2018 tutaunganisha matumizi ya gesi katika Mikoa ya Mtwara na Lindi pamoja maeneo yote ya Dar es Salaam yakiwemo maeneo ya Mbagala, Kurasini, Buguruni na maeneo mengine ya jiji ya Dar es Salaam. Tunatarajia wananchi 30,000 tunawaunganishia gesi ili matumizi makubwa ya mkaa na kuni yapungue. Asilimia 70 ya mkaa unaotumika hapa nchini unaingia Dar es Salaam, kwa hiyo tukishaunganisha gesi kwa wananchi wa Dar es Salaam tutapunguza kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira, hiyo ni hatua ya kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua ya pili, kwa sababu muda ni mfupi sana, inahusu usambazaji wa umeme mijini na vijijini. Kama ambavyo mnajua tunapeleka umeme katika mikoa yote katika miji yote na vitongoji vyetu. Tuna mpango wa kendeleza umeme mijini, na mpango huu unaanza mwaka 2017/2018 kwa maeneo ya mjini…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.