MHE. DKT. MEDARD M. KALEMANI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali. Pia ninatoa shukurani nyingi sana kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia shilingi milioni 226 kwa ukarabati na kujenga madarasa manne kwenye Shule Kongwe ya Rudeba, Kata ya Iparamasa. Namshukuru Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Waziri pia, kwa kututengea shilingi milioni 890, kwa ajili ya ukarabati wa madarasa mengine yaliyobaki. Kuna shule kongwe 169, nyingi zina uchakavu na kwa kweli fedha iliyotengwa nakubaliana nayo, lakini ni ndogo.
Mheshimiwa Naibu Spuka, swali langu la kwanza; ninamwomba Mheshimiwa Waziri atembelee shule zote kongwe na ninamwomba atembelee ndani ya miezi hii miwili kabla Bunge halijakwisha akatoe tamko ili ukarabati uanze.
Mhshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; fedha hizi shilingi milioni 890 zitatoka lini ili ujenzi na ukarabati wa madarasa ya shule zote kongwe ikiwemo Ilyamchele, Nyambogo, Ichwankima, Kasenga, Nyamirembe, Buzirayombo nao ufanyike kwa haraka? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Medard Kalemani kwa kutaka kuhakikisha kwamba, katika jimbo lake Sekta ya Elimu inawekewa kipaumbele na hasa katika shule hizi chakavu, shule kongwe za msingi. Kuhusu swali lake la kwanza, ninaomba mimi na Mheshimiwa Mbunge tukae, tujadili na tupange ratiba inayotekelezeka, ili tuweze kuona tunafanyaje kuhusiana na kuzitembelea shule hizi kongwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la pili, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, katika Serikali hii ya Awamu ya Sita, uwekezaji wa zaidi ya shilingi trilioni 5.1 umefanyika katika Sekta ya Elimu katika shule kongwe. Shule kongwe 832 zimeweza kufanyiwa ukarabati katika kipindi cha miaka minne na katika Jimbo lake la Chato jumla ya shilingi bilioni 1.53 zimeletwa, kwa ajili ya kuhakikisha zinakarabati shule kongwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, hata fedha hizi milioni 890 ambazo zimetengwa kwa mwaka huu wa fedha zimetengwa kwa ajili ya kuhakikisha zinakarabati shule hizo kongwe, lakini nitumie nafasi hii kuendelea kutoa msisitizo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha kwamba anaendelea kuzifanyia tathmini shule hizi Kongwe 169 katika Jimbo la Mheshimiwa Mbunge na kuziweka katika mpango na bajeti kwa ajili ya kuendelea kuzikarabati ili shule hizi ziweze kuwa katika hali nzuri na kuwanufaisha wanafunzi wetu.