Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Muhammed Amour Muhammed (9 total)

MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED aliuliza:-
Kumekuwa na unyanyasaji mkubwa unaofanywa na JWTZ wa kuwanyang‟anya wavuvi samaki wao licha ya kwamba watu hao wanajitafutia kipato kupitia bahari kama Watanzania.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuondoa unyanyasaji huo unaofanywa na Jeshi la Wananchi kwa wananchi wake?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Muhammed Amour Muhammed, Mbunge wa Bumbwini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa haijawahi kupokea tuhuma yoyote inayohusu unyanyasaji unaofanywa na askari wa JWTZ kwa wavuvi nchini. Aidha, kama tuhuma hizi zina ushahidi ni bora zikafikishwa sehemu husika ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua zinazostahili.
Mheshimiwa Spika, nataka nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu kwamba, wanajeshi kama walivyo raia wote wanapaswa kuheshimu sheria za nchi na pale wanapokwenda kinyume huchukuliwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa sheria na kanuni za jeshi.
MHE. RICHARD P. MBOGO (K.n.y. MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED) aliuliza:-
Kwa muda mrefu kumekuwepo na tatizo la wanafunzi wanaoingia vyuo vikuu kukosa mikopo na elimu ya juu ni suala la Muungano:-
Je, Serikali ya Muungano inaipatia SMZ kiasi gani cha fedha kwa mwaka kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi hao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (K.n.y. WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Muhammed Amour Muhammed, Mbunge wa Bumbwini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu hutoa mikopo kwa kuzingatia kwamba muombaji ni raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, awe muhitaji aliyedahiliwa katika chuo cha elimu ya juu. Mikopo inayotolewa inatoa umuhimu wa kipekee kwa vipaumbele vya Taifa ambavyo ni Uhandisi wa Gesi na Mafuta, Sayansi za Afya, Ualimu, Ualimu wa Sayansi na Hisabati na Uhandisi wa Kilimo na Maji. Aidha, wanafunzi yatima na wale wenye ulemavu hupewa kipaumbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kuwepo kwa vyuo vya elimu ya juu Tanzania Bara na Visiwani. Aidha, Serikali inatambua kuwa fursa za kusoma elimu ya juu zinapatikana vyuo vyote vya elimu ya juu hapa nchini ambapo kumekuwepo na wanafunzi wa elimu ya juu wanaotoka Zanzibar na kusomea Tanzania Bara na wengine hutoka Tanzania Bara na kusomea vyuo vikuu vilivyoko Zanzibar. Hivyo basi, kupitia Bodi ya Mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu Serikali inawatangazia wale wanaotarajia kujiunga na vyuo vikuu vyote nchini wanaohitaji mikopo kuomba mikopo bila kujali kama anatoka Tanzania Bara au Zanzibar.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kwamba hakuna tengeo maalum la fedha kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa ajili ya kugharamia mikopo ya elimu ya juu. Mikopo inatolewa kwa muombaji aliyekidhi vigezo na sifa za kitaaluma bila kujali anakotoka sehemu gani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, katika fomu ya kuwasilisha maombi ya mikopo hii hakuna mahali panapomtaka muombaji kutaja anakotoka sehemu gani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hivyo Bodi inawatambua waombaji wote kuwa ni Watanzania.
MHE. ALLY SALEH ALLY (K.n.y. MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED) Aliuliza:-
Suala la usalama wa raia na mali zao ni moja ya dhamana ya Jeshi la Polisi nchini; ni muda sasa Zanzibar wananchi wamekuwa wakipigwa, kunyanyaswa na kunyang‟anywa mali zao kunakofanywa na vikosi vya SMZ.
Je, nini kauli ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano kuhusiana na matukio hayo huko Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Muhammed Amour Muhammed, Mbunge wa Bumbwini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kuwa usalama wa raia na mali zao ndiyo dhamana kuu au kazi ya msingi ya Jeshi la Polisi nchini. Taarifa hizo hadi sasa hazijapata uthibitisho sahihi kutoka kwa wale ambao wanadai kutendewa vitendo hivyo, kwani hakuna taarifa yoyote iliyoripotiwa kwenye vituo vya polisi Visiwani Zanzibar kuhusiana na uhalifu huo. Kwa mujibu wa taratibu zilizopo ni kwamba mtu yeyote ambaye anafanyiwa kitendo chochote cha uhalifu anapaswa kutoa taarifa kwenye kituo cha polisi, ili hatua za kiuchunguzi na kiupelelezi zifanyike ili kubaini wahalifu ambao wamehusika na hatua stahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi bado inasisitiza kuwa haitambui uwepo wa vitendo hivyo na inatoa wito kwa wananchi wote ambao watafanyiwa au wamefanyiwa vitendo kama hivyo, watoe taarifa kwenye vituo vya polisi au kwa viongozi wa polisi waliopo Makao Makuu Zanzibar na Dar es Salaam ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa dhidi ya vitendo hivyo kwa watuhumiwa.
MHE. SALEH ALLY SALEH (K.n.y. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED) Aliuliza:- Kwa kipindi kirefu sasa kumekuwa na matendo ya dhahiri yanayoonesha kuvunjwa kwa haki za binadamu hapa nchini bila ya Serikali kuchukua hatua yoyote.
Je, Serikali haioni kwamba wananchi watakosa imani na Serikali yao?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA Alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Muhammed Amour Muhammed, Mbunge wa Bumbwini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya jukumu la msingi kwa Serikali ni kukuza, kulinda na kuhifadhi haki za binadamu na wajibu wao hapa nchini. Jukumu hilo ni la kikatiba ambapo Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kama ilivyorekebishwa mara kwa mara na Katiba ya Zanzibar ya 1984 kama ilivyorekebishwa mara kwa mara pamoja na kuainisha haki za binadamu, imeipa Serikali wajibu wa kukuza, kulinda na kuhifadhi haki hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kupitia Bunge lako Tukufu, nchi yetu imeridhia mikataba mbalimbali ya Kimataifa na kikanda ambayo inaweka misingi ya haki hizo na wajibu wa Serikali katika kuhakikisha nchi inaendeshwa kwa kufuata misingi ya haki za binadamu. Aidha, Bunge lako Tukufu kwa nyakati tofauti limetunga sheria mbalimbali zinazolinda na kukuza haki za binadamu pamoja na kutoa nafuu (remedy) kwa raia pale haki za binadamu zinapovunjwaaidha na Serikali au mtu binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha haki za binadamu zinalindwa, zinadumishwa na zinastawishwa hapa nchini, Katiba imeipa Mahakama mamlaka ya kusikiliza na kuamua mashauri yanayohusu haki za binadamu na wajibu wao kama ulivyoainishwa katika Katiba. Aidha, Serikali imeunda taasisi mbalimbali zinazoshughulikia hifadhi ya haki za binadamu. Taasisi hizo ni pamoja na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Mabaraza mbalimbali kama yale ya Ardhi na Kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mahakama pamoja na taasisi hizi zimekuwa zikichukua hatua pindi vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu vinapotokea na kuripotiwa au kufikishwa kwa maamuzi. Serikali kupitia vyombo vyake, imejidhatiti kuhakikisha kuwa kitendo chochote kinachovunja haki za binadamu kinachukulia hatua stahiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwasihi Waheshimiwa Wabunge tushirikiane na vyombo vyetu vilivyopewa mamlaka na dhamana ya kulinda haki pale tunapopata taarifa za vitendo vya uvunjwaji wa haki za binadamu vimefanyika au vinaweza kufanyika ili hatua stahikina za haraka za kisheria zichukuliwe.
MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED aliuliza:-
Kwa kipindi kirefu sasa Bandari za Tanga na Mkokotoni zimekuwa zikitumika na kusababisha maafa makubwa kwa watumiaji.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha usalama wa wasafiri hao?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Muhammed Amour Muhammed, Mbunge wa Bumbwini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kuhakikisha kuwa wakazi wa maeneo ya Tanga, Visiwa vya Unguja na Pemba wanapata huduma bora na salama na hivyo kuwaepusha na usafiri wa vyombo vya majini visivyokidhi matakwa katika kubeba abiria na mizigo. Baadhi ya hatua hizo ni pamoja na:-
(a) Kuhakikisha kuwa vyombo hivyo ni salama kabla havijaanza kutoa huduma. Kwa sababu hiyo SUMATRA hufanya ukaguzi wa lazima (Statutory Inspection) wa vyombo kila baada ya mwaka ili kubaini kwamba vyombo hivyo vinaendelea kukidhi ubora na usalama wa kuelea majini. Aidha, SUMATRA hufanya kaguzi za kushtukiza ili kuhakikisha kuwa vyombo vya majini vinaendelea kuwa salama wakati wote.
(b) Kuweka na kutekeleza mikakati ya namna ya kudhibiti uibukaji na matumizi ya bandari bubu katika mwambao wa Pwani kwa kuwa vyombo vingi vinavyoanza safari zake katika bandari zisizo rasmi siyo rahisi kufuata masharti ya ubora na usalama wa kuelea majini. SUMATRA inashirikisha uongozi wa Serikali za Vijiji na Kata, vikundi vya kudhibiti uvuvi haramu na usimamizi wa mazingira ya mialo ambao husaidia kusimamia utaratibu wa uondokaji wa vyombo katika mialo ili kuhakikisha vyombo vinavyotumika vinatambulika na kuacha taarifa ya orodha ya abiria na mizigo.
(c) Kuhimiza sekta binafsi kuwekeza katika utoaji wa huduma za usafiri kwa kutumia meli za kisasa kati ya Tanga, Unguja na Pemba ili wananchi wapate huduma bora na za kutosha kupitia bandari rasmi hivyo kuondoa mazingira yanayolazimisha kutumia bandari bubu.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA (K.n.y MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED) aliuliza:-
Kumekuwa na tatizo la kuvuja kwa mitihani ya Taifa hapa nchini hususani ile ya kidato cha nne (CSEE) hali inayoondoa ufanisi hasa ikizingatiwa matokeo yanayotoka yamejaa udanganyifu. Je, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti tatizo hili?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Muhammed Amour Muhammed, Mbunge wa Bumbwini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imeweza kudhibiti na kuondoa tatizo la kuvuja kwa mitihani ya kidato cha nne, ambapo kwa mara ya mwisho ilikuwa ni mwaka 2008 katika somo la hisabati pekee. Changamoto inayoendelea kujitokeza ni kwa baadhi ya watahiniwa kujihusisha na udanganyifu wakati mitihani inapofanyika kwa kuingia katika chumba cha mtihani na vitu visivyoruhusiwa kama vile notes na simu ya mkononi kwa ajili ya kufanya mawasiliano ndani ya chumba cha mtihani.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeendelea kujidhatiti na kuikabili changamoto ya udanganyifu katika mitihani kwa kuimarisha usimamizi na kutoa elimu kwa watahiniwa kuhusu madhara ya kufanya udanganyifu. Wizara imekuwa ikitoa adhabu ikiwa ni pamoja na kufutiwa matokeo ya mitihani pale inapothibitika kuwepo kwa udanganyifu huo. Mfano, watahiniwa waliofutiwa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2011 ni 3,303, mwaka 2012 ni 789,
mwaka 2013 ni 272, mwaka 2014 ni 184, mwaka 2015 ni 87 na
mwaka 2016 ni 126.
MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED aliuliza:-
(a) Je, Serikali imejipangaje kuhakikisha inashirikisha sekta binafsi ili kufikia dhamira ya kuwa nchi ya viwanda na yenye uchumi wa kati?
(b) Je, Serikali haioni kwamba dhamira hiyo ya kuelekea nchi ya viwanda na uchumi wa kati ni ndoto tu na haiwezi kufikiwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTONY P. MAVUNDE K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Muhammed Amour Muhammed, Mbunge wa Bumbwini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
• Mheshimiwa Mwenyekiti, dhima ya mpango wa pili wa miaka mitano ni kujenga uchumi wa viwanda ili kuchochea mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu. Katika mpango huo, imebainishwa wazi kuwa ni jukumu la sekta binafsi kujenga viwanda. Serikali inabaki na jukumu la kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na ufanyaji biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili Serikali iweze kutekeleza majukumu ya ujenzi wa viwanda kwa ufanisi, Serikali imetekeleza yafuatayo; kwanza, kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara kuhakikisha vikwazo vyote vinaondolewa.
Pili, kupitia Wizara na mamlaka husika kutenga maeneo ya kujenga viwanda kuanzia ngazi ya vijiji mpaka ngazi ya Taifa; tatu, kuweka miundombinu ya umeme, barabara, maji, mawasiliano na usafiri wa anga; nne, kupitia taasisi kama SIDO, TIRDO, TANTRADE na kutoa elimu na mwongozo wa kujenga viwanda na tano, kuhamasisha wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza katika maeneo ya kipaumbele.
• Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la Dira ya Taifa 2025 ni kuona nchi yetu inakuwa Taifa lenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Ili kutimiza dhamira hiyo, tunatekeleza Mipango ya Maendeleo mitatu ya miaka mitano mitano. Pia upo mkakati wa fungamanisho la maendeleo ya viwanda ukiongoza utekelezaji wa mipangi tajwa hapo juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tathmini ya utekelezaji wa mipango mitatu ya maendeleo ambapo sasa tumefikia nusu, inaonesha dhahiri kuwa Taifa letu litafikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 likiongozwa na Sekta ya Viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati kuna hitaji kubwa la uwekezaji katika viwanda vinavyotegemea malighafi kutoka kwa wananchi, mpaka sasa maendeleo ni mazuri kwa viwanda vinavyozalisha biashara zinazotumika kwa wingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa uchumi wa viwanda ni jambo ambalo limeshaanza na kufikia uchumi wa kati mwaka 2025 ni jambo linalowezekana.
MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED aliuliza:-
Kwa kipindi cha kirefu sasa nchi yetu imekuwa ikipeleka Askari wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) nje ya nchi ambako kuna vita vya wenyewe kwa wenyewe na kusababisha misiba mikubwa sana kwa Askari wetu:- Je, Serikali inasema nini kuhusiana na kadhia hiyo?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Muhammed Amour Muhammed, Mbunge wa Bumbwini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania kama Mwanachama wa Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, Jumuiya za Kikanda kama East Africa Community na SADC na Jumuiya ya Nchi za Maziwa Makuu inao wajibu wa kushiriki katika Ulinzi wa Amani katika nchi mbalimbali. Madhumuni ya kupeleka askari wetu huko ni kwenda kulinda amani na sio kushiriki kwenye mapigano. Kwa bahati mbaya sana, yapo matukio ya kushambuliwa kwa askari wetu yaliyofanywa na vikundi vya waasi yaliyopelekea kupoteza maisha ya baadhi ya askari wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Wananchi wa Tanzania limechukua hatua ya kutoa mafunzo ya kutosha kwa vikosi vyetu vinavyopewa jukumu hili, pamoja na kuwaongezea vifaa vya kisasa ili waweze kujilinda dhidi ya mashambulio ya vikundi vya waasi. Hivyo, mtazamo wa Serikali ni kuendelea kushiriki katika shughuli za Ulinzi wa Amani katika nchi mbalimbali ili kutimiza wajibu wetu Kimataifa na huku tukichukua kila tahadhari kuepusha maafa yaliyowahi kutokea.
MHE. HAMAD SALIM MAALIM - (K.n.y. MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED) aliuliza:-
Kwa kuwa huu ni wakati wa Sayansi na Teknolojia na vijana wetu wamekuwa wakizitafuta syllabus za Masomo mbalimbali madukani bila mafanikio:-
Je, Serikali haioni kuwa huu ni wakati muafaka wa kuziweka syllabus hizo mtandaoni?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Muhamed Amour Muhamed, Mbunge wa Bumbwini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inafanya kila jitihada kuhakikisha kuwa wadau wa elimu wanapata mahitaji yao ya Mitaala na Mihtasari kwa lengo la kufanikisha utoaji wa elimu nchini. Katika kuhakikisha hili, Wizara kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania, husambaza Mihtasari nchi nzima. Aidha, ili kukidhi mahitaji kwa wadau mbalimbali, Mihtasari imekuwa ikipatikana duka la TET na maduka ya vitabu nchini ambayo, wenye maduka ya vitabu huenda kununua kwenye duka la TET.
Mheshimiwa Spika, kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia nchini, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kupita TET, imeshaanza kuweka mihtasari kwenye mtandao wa Taasisi ya Elimu Tanzania ili kuongeza wigo wa upatikanaji wa mihtasari hiyo. Baadhi ya mitaala na mihtasari ambayo tayari imewekwa kwenye mtandao wa Taasisi ya Elimu Tanzania ni Mitaala na Mihtasari ya Elimu ya awali, Msingi na Sekondari.
Mheshimiwa Spika, aidha, lengo la Wizara kwa sasa ni kuweka Mitaala na Mihtasari ya Masomo yote kwenye mtandao ili iwafikie walengwa kwa urahisi na kwa wakati. Wadau wote wa elimu wanashauriwa kutembelea Mtandao wa Taasisi ya Elimu Tanzania (http://www.tie.go.tz) ili waweze kuona na kupakua Mtaala na Mihtasari husika.