Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Saada Salum Mkuya (2 total)

MHE. SAADA SALUM MKUYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa maelezo yake, lakini Mheshimiwa Waziri najua kwamba karafuu ya Zanzibar ndiyo Karafuu ambayo ni quality duniani kote. Je, Wizara ya Biashara na Viwanda ya Tanzania ina mkakati gani kushirikiana na Wizara ya Biashara na Viwanda ya Zanzibar kuhakikisha kwamba tunajenga kiwanda ambacho kita-absolve karafuu ya Zanzibar kwa ajili ya kutengeneza products, kusafirisha nje lakini vile vile kupatia vijana ajira kama ambavyo tunaelezwa na ndiyo mategemeo yetu?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, maelekezo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu Zanzibar ilikuwa ni kwamba Makatibu Wakuu wa Wizara ya Viwanda Zanzibar na wale wa Tanzania kwa upande wa Bara wakutane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa napenda nitoe maelekezo kwamba wanapokutana sasa, kwa sababu najua wananisikiliza; na suala la Karafuu na Kiwanda na lenyewe waliunganishe walete majibu hapa tuweze kupata suluhu ya kutengeneza Kiwanda Zanzibar. (Makofi)
MHE. SAADA MKUYA SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; katika mikakati ambayo imeorodheshwa ni kazi gani hasa zimefanyika katika kituo cha Afya cha Jeshi kilichopo Welezo ambacho kinahudumia wananchi wengi na hali yake ni mbaya sana. Kwa hiyo, hii mikakati imeorodheshwa lakini katika mwaka 2016/2017 ni kazi gani hasa zimefanyika katika kituo kile.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; namwomba Mheshimiwa Waziri tukiondoka Dodoma tufuatane, mguu kwa mguu twende katika Jimbo la Welezo tukatembelee kituo hiki cha afya, kipo katika hali mbaya na kinahudumia wananchi wengi na wengi wanakitegemea. Kwa hivyo, akienda akiona utajua sasa ni jinsi gani anaweza kukisaidia. (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika mikakati niliyoielezea kuna baadhi ambayo imeshaanza na kuna baadhi ambayo bado tunategemea itaanza siku za usoni. Lile la Bima ya Afya ambayo kwa kweli tunadhani ndio itakuwa mkombozi wa kuboresha huduma za afya, hilo bado halijaanza, tupo katika mchakato na ni matumaini yetu kwamba likianza fedha nyingi zitapatikana ili kuweza kuboresha vituo hivi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa yale yaliyoanza ni msaada uliotolewa na Serikali ya Marekani na Ujerumani. Tumeshafanya ukarabati na tumenunua vifaa, lakini tumeanza na ngazi za Hospitali za Rufaa za Jeshi. Kwa sababu hata kwenye Jeshi kuna vituo vya afya, hospitali na hospitali kuu. Kwa hivyo, kazi iliyofanyika kwa mfano katika Hospitali Kuu ya Lugalo, kazi zilizofanyika katika Ali Khamis Camp Pemba, kazi zilizofanyika Mwanza na kadhalika ni kubwa na tunajua kwamba kazi hii haijakamilika kwa sababu bado kuna vituo hatujavifikia ikiwemo hicho cha Welezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachoweza kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge ni kwamba tutafika, tunakwenda kwa awamu ili na chenyewe tukiboreshe wananchi pamoja na Wanajeshi waweze kupata huduma nzuri zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la kutembelea katika kituo hicho, nataka kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba nipo tayari, nitakapofanya ziara ya eneo la Unguja, basi moja ya kazi zangu itakuwa ni kufuatana naye kwenda kuangalia kituo hicho.