Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Joseph Kasheku Musukuma (76 total)

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa matatizo yaliyoulizwa na Mheshimiwa Mgeni kwenye swali namba 106 yanafanana kabisa na matatizo yaliyoko Jimbo la Geita Vijijini. Takribani wanawake wazee wanne kwa mwezi wanauwawa kwa kukatwa mapanga kwa imani ya kishirikina na Jeshi la Polisi halijawahi kufanikiwa kuwakamata wakataji mapanga hao kwa kuwa jiografia ya kutoka Geita kwenda eneo husika ni mbali.
Je, Serikali inajipangaje kupeleka gari maalum na kuunda Kanda Maalum kwa ajili ya kuokoa akina mama wanaokatwa mapanga kwenye Jimbo hilo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Polisi linajitahidi sana kuweza kukabiliana na mauaji haya, lakini kama ambavyo nimezungumza wakati nikijibu maswali wiki iliyopita kuhusiana na changamoto ambazo zinakabili Jeshi la Polisi. Naomba nichukue fursa hii kuweka sawa kidogo takwimu wakati nilikuwa najibu swali la Mheshimiwa Selasini juzi, nilieleza kwamba moja katika changamoto inakabili Jeshi letu la Polisi ni kwamba idadi ya polisi tulionao ni kidogo na kiukweli kihalisia takwimu zinaonyesha kwamba ukiangalia takwimu za kidunia polisi mmoja anatakiwa ahudumie kati ya watu 400 mpaka 450 takriban na siyo 300 mpaka 350. Sisi hapa nchi yetu polisi mmoja kwa upande wa Tanzania Bara anahudumia watu kwenye 1000 mpaka 1200. Kwa hiyo utaona ni tofauti kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa changamoto hizi na changamoto nyingine ambazo tumekuwa tukikabiliana nazo hatua kwa hatua kama hii ya usafiri, nataka nimhakikishie tu Mheshimiwa Musukuma kwamba tumekuwa na changamoto ya usafiri kwa muda mrefu lakini tumepata magari takribani magari 387 ambayo yameweza kugawiwa katika maeneo mbalimbali. Tutaangalia eneo hilo kama halijafika gari tuone ni jinsi gani na uzito wa hali yenyewe ilivyo tushauriane tuone ni nini tutakachofanya ili tuweze kukabiliana na tatizo hilo. Lakini mengine ni changamoto ambazo tunaenda nazo kadri ya uwezo wa bajeti unavyoruhusu.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kuwa Mkoa wa Geita ni mkubwa uliopo pembezoni mwa mikoa inayopokea wakimbizi na kuishi kwa wasiwasi kwa sababu ya nchi za jirani zenye machafuko. Ni lini Serikali inafikiria kuleta Kambi Rasmi ya Jeshi? (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Vikosi vya Jeshi vinapangwa kwa mujibu wa mahitaji ya kiulinzi. Kwa hiyo, zile sehemu ambazo zina mipaka au zile sehemu ambazo zina mahitaji maalum ya kiulinzi ndipo vikosi huwa vinapangwa. Hata hivyo, kwa sababu muda mrefu umepita toka waangalie utaratibu wa mpango wa vikosi katika nchi yetu, nakubaliana na Mheshimiwa Musukuma kwamba pengine wakati umefika wa kutuma timu za wataalam kwenda kuangalia endapo kutakuwa kuna ulazima wa kuweka vikosi sehemu hiyo. Ikithibitika kama hivyo ndivyo, basi tutashauriana ili waweze kuanzisha vikosi huko. (Makofi)
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa swali la msingi limeeleza jinsi watumishi wa migodini wanavyofukuzwa kazi kiholela, pengine wakifanya kazi kwa miaka minane, saba wanafukuzwa kutokana na magonjwa mbalimbali, na Serikali imeondoa fao la kujitoa kwenye Mifuko ya Jamii ikiweka masharti kwamba mpaka miaka 55.
Je, hawa waliofukuzwa kazi wakiwa na miaka tisa na umri wa miaka 40 wanapataje fao lao kwa kusuburi miaka 50 Maana watakuwa na miaka 100?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, Sera ya Hifadhi ya Jamii ambayo inaongoza masuala mazima ya Hifadhi ya Jamii katika nchi yetu ya Tanzania inaendana na Katiba ya nchi kifungu cha 11(1) ambacho Katiba ya nchi yetu inataka jamii kuangalia utaratibu mzima wa kuweka hifadhi ya wananchi na hasa pale wanapofikia umri wa uzeeni ama wanapopata matatizo mengine yoyote. Kwa hiyo, sera hiyo imekuwa ikituongoza kuunda mifuko hii ya Hifadhi ya Jamii kwa ajili ya kutoa kinga wakati wa uzeeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tumepata matatizo ya namna moja ama nyingine. Kadiri uchumi wa Tanzania ulivyoendelea kukua kumeongezeka sekta za kiuchumi ambazo unapata picha kabisa kwamba wafanyakazi ambao wamekuwa wakiajiriwa katika sekta hizo ni lazima watafanya kazi kwa muda mfupi sana, kama katika sekta za migodi, sekta za mashamba na sekta nyinginezo na hivyo basi kumekuwa na namna moja ama nyingine ya kuonekana kabisa kunahitajika kupitia tena sera ya Hifadhi ya Jamii, na kupitia sheria zetu ambazo zinaongoza Mifuko ya Hifadhi ya Jamiii ili kuyapitia mafao yanayotolewa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Kusudi la kufanya hivyo ndani ya Serikali ni kutazama kama sera na sheria tulizonazo zitakwenda kujibu matatizo ya wafanyakazi kama wa migodini kutokupata ama kupata fao la kujitoa kwa kuzingatia nature ya kazi zao. Haya yote yataongozwa na mikataba ya Kimataifa na sheria tulizonazo nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ninaomba nitoe wito kwa Watanzania na wafanyakazi wote watupe subira, na sisi Serikali tuko tunalifanyia kazi suala hili kwa nguvu. Nitoe onyo kwa waajiri wote wanaokiuka matakwa ya kisheria katika kuchangia mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa faida ya wafanyakazi. Na ninaomba niliarifu Bunge lako tukufu, tumeshaunda kikosi kazi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu na tunakaribia kuanza kufanya ukaguzi wa nguvu kwa kuzingatia pia Sheria ya Tanzania Extractive Industries Transparency and Accountability na tutapambana na wale wote wanaofanya udanganyifu katika kuchangia mafao ya wafanyakazi na hasa migodini.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona.
Kwa kuwa tatizo lililopo Kagera ni sawasawa na tatizo lililopo kwenye Jimbo la Geita Vijijini katika Msitu wa Lwande. Sisi kama Halmashauri tulipendekeza hekta 7,000 zirudishwe kwa wananchi kutoka kwenye hekta 15,000; na tukapeleka maombi yetu Wizarani. Je, ni lini Serikali itajibu maombi ya Wilaya yetu kuhusiana na hizo hekta 7000?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, nimetoa maelezo ya awali ambayo napenda niyasisitize tena; hakuna jambo zuri katika kushughulikia changamoto yoyote ile kama kufanya utafiti, kama kwenda kutafuta kiini cha tatizo, usipofanya hivyo ukatafuta suluhisho utafuta suluhisho pengine ukapata suluhisho la muda tu. Lakini ukitaka suluhisho la kudumu lazima ufanye utafiti, kama vile ambavyo ukiwa na maradhi unataka kutibiwa unakwenda kwanza maabara unafanya vipimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tumesema tunataka kwenda kwenye maeneo haya yote kwa ujumla wake ikiwemo kwenye eneo ambalo Mheshimiwa Joseph Musukuma analizungumzia. Napenda nimuombe Mheshimiwa Musukuma avute subira kidogo; maombi aliyopeleka Wizara ya Maliasili na Utalii hayatashugulikiwa na Maliasili tu peke yake. Tumesema tunakwenda kushirikisha Wizara zote ambazo ni wasimamizi au ni watumiaji wa ardhi ikiwemo TAMISEMI ambayo wamesema kwamba wamepitisha maombi kule, tunakwenda kushirikiana nao kwenda kutafuta ufumbuzi ambao utauwa ufumbuzi wa kudumu.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru; kwa kuwa Kanda ya Ziwa tunategemea kilimo na zao la pamba limekufa, tukahamasisha wakulima wetu walime zao la mpunga kama zao la biashara na bahati nzuri Mwenyezi Mungu akatujalia mpunga ukaiva wa kutosha na Rais wa Jamhuri ya Muungano alizunguka kwenye kampeni akisema wakulima hawatafungiwa masoko kwa kuwa wanalima kwa pesa zao na nguvu zao wenyewe.
Kwa kuwa Serikali imezuia wananchi na wafanyabiashara wa mpunga kupeleka nje, wakulima wetu kule wameivisha mpunga hawana sehemu ya kuweka huko nje na tunaenda kwenye msimu wa mvua. Je, Serikali ina mpango gani kama haijataka kufungua soko wa dharura wa kuweza ku-protect kile chakula kilichopo nje? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kurekebisha, Mheshimiwa Mbunge amesema Serikali imekataza wafanyabiashara kupeleka mazao nje, kauli sahihi ni kwamba Serikali imesitisha huku tukiweka utaratibu sawa kwa sababu tunajaribu kuangalia tuwe na utaratibu mzuri zaidi wa kuruhusu chakula kiende nje kwa sababu kuna hatari kubwa kwamba tukiendelea kufanya holela kama ilivyo sasa nchi yetu inaweza ikaingia katika janga la njaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka huu Ukanda mzima wa Kusini mwa Afrika unakabiliwa na njaa, nchi 13 kati ya nchi 15 za Jumuiya ya Kiuchumi ya Kusini mwa Afrika (SADC) zinakabiliwa na njaa ikiwemo Afrika ya Kusini. Utaratibu ambao tumekuwa tukiutumia kupeleka chakula nje ulikuwa unatoa fursa chakula chote kiishe bila kufuata utaratibu. Kwa hiyo tulichofanya ni kwamba tumefanya tathmini ya taratibu ambazo tunatumia ili kuja na utaratibu ambao utaturuhusu na kuwaruhusu wafanyabiashara wetu waweze kupeleka nje lakini katika hali ambayo haitatuacha katika hali ya njaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba utaratibu huo karibia unakamilika na muda si mrefu, namhakikishia kupitia Bunge lako tukufu kwamba utaratibu wa kawaida wa kupeleka chakula nje kwa wafanyabiashara utaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba wavute subira, Serikali ya Awamu ya Tano haina nia ya kukwamisha wafanyabiashara na Watanzania kutumia mazao yao kibiashara, sisi wenyewe tunatafuta masoko, lakini lazima tufanye kwa njia ambayo sio holela kwa sababu tuna majukumu vilevile ya kuhakikisha kwamba nchi yetu haiingii katika baa la njaa.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nilitaka kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Wananchi kwenye vijiji vya Majimbo yetu wanapojichukulia sheria mkononi, kunavyopigwa mwano, pengine kumetokea kibaka, polisi wanakuja kukamata viongozi wa vijiji na kuwa-suspect na ile kesi, lakini kwenye mgodi ni tofauti, zinapookotwa maiti zenye risasi za moto na matukio mengine mabaya, hakuna suspect yeyote anayekamatwa kutoka kwenye Mgodi wa GGM na zinachukuliwa maiti zinakwenda kutelekezwa hospitali ndugu wanakwenda kutambua na kuchukua bila kuchukuliwa hatua yoyote.
Je, Waziri yuko tayari kufuatana na mimi baada ya Bunge hili kwenda katika Kijiji cha Nyakabale ambacho kina wahanga zaidi ya 100 waliopigwa risasi za moto na kuumishwa mbwa wa mgodi, kwenda kuwaona na kuja kutoa majibu sahihi kwenye Bunge lijalo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama tatizo ndiyo hilo, kwa nini Mgodi wa GGM usiweke uzio kama ilivyo migodi mingine hapa nchini kama Acacia, Nyamongo na Kahama Mine?
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimejibu swali langu la msingi ambapo nilitolea mfano wa hatua ambayo Serikali ilichukua kwa askari ambaye aliwapiga risasi wananchi, kwa hiyo nadhani siyo kweli kwamba hakuna hatua hazijachukuliwa, hatua zinachukuliwa na huo ni mfano mmoja tu. Inawezekana pengine kuna baadhi ya matukio hayajachukuliwa hatua labda kwa kukosekana kupatikana taarifa kwa mamlaka husika. Sasa wazo lake hili alilolitoa la kuambatana mimi na yeye nadhani ni wazo la msingi ili aweze kunionesha maeneo ambayo yalipaswa kuchukuliwa hatua lakini hatua hazikuchukuliwa tuweze kuchukua hatua. Kwa hiyo ombi lake hilo tumelipokea kwa mikono miwili ni wajibu wetu kuweza kushirikiana na Waheshimiwa Wabunge kuwatumikia wananachi, hasa wanyonge, ambao wamekuwa wakionewa, kwa hiyo kwa kuwa yeye ana ushahidi basi tutafuatana pamoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kwamba Mgodi ya GGM haujawekwa uzio, hili siwezi nikalijibu sasa hivi kwa sababu sijafika kwenye mgodi huu. Lakini kwa kuwa tuna ziara hiyo mimi na yeye nadhani wakati huo utakuwa ni muafaka wakuweza kutembelea kuangalia mazingira pale tukashauriana kwa pamoja sasa na vyombo vinavyohusika na usalama kuimarisha usalama katika mgodi huo ili wananchi wasiweze kupata athari zaidi.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa swali la msingi lililoulizwa linafanana kabisa na matatizo yaliyopo kwenye Jimbo la Geita Vijijini ambapo mwaka 2013 Mheshimiwa Rais Mstaafu alipokuja kule tulimweleza kuhusiana na barabara mbadala ya kilometa 75 kuanzia Bugulula, Senga, Sungusila mpaka kwenda kuungana na Sengerema Mwamitiro kwamba ipande kutoka kwenye hadhi ya Halmshauri kwenda kwenye hadhi ya TANROADS na Mheshimiwa Rais Mstaafu alimwomba Mheshimiwa Rais wa sasa ambaye alikuwa Waziri kwamba atusaidie na akatuambia tufuate taratibu za Serikali na akatupa kuanzia shilingi milioni 400 tukaanza kukarabati ile barabara; na taratibu zote zimeshakamilika tumepeleka kuomba....

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Swali langu la msingi, Waziri wa Ujenzi anatoa kauli gani kuhusu kuipandisha barabara hii kuwa ya TANROAD angalau kwa kiasi cha changarawe?
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyosema ahadi ilitolewa na viongozi wetu na kwa maana hiyo, viongozi wetu walionesha dhamira ya kuitengeza hii barabara. Na mimi namhakikishia, sisi ambao tumekabidhiwa dhamana ya kutekeleza dhamira za viongozi wetu, tutalishughulikia hili. Kuhusu matengenezo Regional Manager wa Geita afanyie tathmini, apeleke taarifa makao makuu ili maamuzi sahihi yaweze kufanyika kwa haraka.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuwa wananchi wa Kilwa Kaskazini walichagua Mbunge anayekimbia kamera na anayeogopa Kanuni za Bunge. Sasa swali hili naomba nilielekeze kwenye matatizo yalioko kwenye Jimbo la Geita Vijijini walikochagua Mbunge makini na asiyeogopa Kanuni na kamera.
Naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri kwamba kwa kuwa wananchi wa Jimbo la Geita wana matatizo kama ya Kilwa. Swali, tumekuwa na mradi wa umwagiliaji wa Nzela Nyamboge ambao umedumu sasa kwa miaka 19 haujakamilika, ni lini mradi huu wa scheme ya umwagiliaji ya Nzela Nyamboge itatekelezwa?
Lakini naomba niulize swali la pili, wananchi wa Jimbo la Ilemela Maduka Tisa ambayo ndio center inayokuwa kwa kasi; wana malalamiko ya maji, na wameisha fuatilia hawajapata muafaka wa kupatiwa maji katika kitongoji cha Maduka Tisa, ni nini kauli ya Waziri kuhusiana na matatizo haya ya wananchi wa Ilemela na Jimbo la Geita Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza amesema mradi wa umwagiliaji wa Nzela, nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba mradi huu nitaufuatilia. Lakini nitoe taarifa kwamba Serikali imekamilisha kuunda Tume ya Umwagiliaji ambayo taratibu zake zimekamilika katika mwaka huu wa fedha 2015/2016. Kwa hiyo, sasa hivi Serikali inaanza kutenga fedha sasa, kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji ambao sasa una tume maalum ambayo ndio itashughulikia miradi ya umwagiliaji. Kwa hiyo, miradi yote ambayo ilikuwa imeanza tutahakikisha imekamilika, miradi mipya itaanza na kama mlivyoona kwenye kitabu cha Wizara ya Maji cha bajeti, tunaanza kufanya utafiti mkubwa kwa ajili ya kuweka miradi ya umwagiliaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Maduka Tisa, Kijiji cha Ilemela, Mheshimiwa Mbunge kama unavyofahamu katika Awamu ya Kwamza ya Programu ya Maendeleo ya Maji iliyoanza mwaka 2006/2007 tulikuwa tumepanga kutekeleza miradi 1,810. Tumekamilisha miradi 1,210 sasa hivi kuna miradi 374 ambayo utekelezaji wake unaendelea na kuna miradi 226 ambayo miradi hiyo haikuanza.
Katika bajeti ambayo mmeipitisha Waheshimiwa Wabunge juzi, tunalenga kwanza kukamilisha miradi ambayo utekelezaji unaendelea na kuanza ile ambayo ilikuwa haijaanza, baadae tunaendelea sasa kuweka miradi mipya. kwa hiyo, katika hii Programu ya Pili, nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, hawa wananchi wa Maduka Tisa, tutahakikisha kwamba tumewapatia maji.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekti, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wa Mkoa wa Geita, hususan Jimbo la Bukombe mwaka wa jana walivyogawiwa mbegu na pembejeo mbegu zile hazikuota, na waliahidiwa kupewa fidia, hawakupewa na sasa wanaogawa mbegu ni wale wale waliowatia hasara mwaka jana. Je, Serikali inawahakikishiaje wale wananchi, kama zile mbegu hazitaota ni nani ataingia gharama ya kuwafidia?
Swali la pili, asilimia kubwa ya Jimbo la Geita vijijini linategemea sana uvuvi. Kumekuwa na operation nyingi sana za kukamata wavuvi na mitego midogo midogo, na kuchoma mitego yao kwa Wakuu wa Wilaya.
Je, Serikali inafanya operation lini kwenye viwanda vinavyotengeneza, vinafahamika na makontena yanayoingia, badala ya kwenda kuwasumbua wale wavuvi maskini?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli katika misimu miwili ya nyuma mfulilizo kuna baadhi ya mbegu ambazo ziligawanywa na Mfuko wa Kuendeleza Zao la Pamba kupitia ginneries mbalimbali ambazo hazikuota na hasa mbegu ambazo hazikuota ni zile ambazo zilikuwa zimenyonyolewa nyuzi. Utaratibu ulifanyika wa kujua ni nani aliyekuwa amefanya kosa kwa sababu batch hizo hizo kuna maeneo ziliota vizuri na kuna maeneo mengine hazikuota vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo wataalam waliingia katika kutafiti ni kutu gani kimesababisha mbegu ambazo zimezalishwa sehemu moja, maeneo mengine siziote na maeneo mengine ziote. Ziko sababu mbalimbali, zingine zikiwemo za upandaji usiokuwa sahihi wa mbegu hizo, lakini ziko pia mbegu ambazo zilibainika kwamba wakati zinanyonyolewa wauzaji wa hiyo pamba walikuwa wamezimwagia maji ili kuongeza uzito wa pamba yao, kudanganya katika ununuzi na hivyo kuzifanya zipoteze ubora hata wakati zinanyonyolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili ni complex ili kujua ukweli kwamba kosa ni la msambazaji au ni la aliyezinyonyoa au ni la mkulima aliyeuza mbegu ambayo ilikuwa imemwagiwa maji. Tutakapokuwa tumejiridhisha exactly nani aliyefanya jambo hilo ni nani, huyo ndiye tutakaye mchukulia hatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu operations zinazoendelea nchi nzima kwenye uvuvi, kwanza hili swali siyo mahali pake, lakini nitalijibu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, uvuvi haramu tutaushambulia na kupigana nao vita popote utakapojitokeza na kwa namna zote. Kwa hiyo, hatukomei katika kukamata wavuvi wenye nyavu, isipokuwa tunakwenda kwa wazalishaji, wasambazaji na waingizaji wa hizo zana haramu nchini. Ndiyo maana umeona tumekamata viwanda wanazalisha nyavu haramu, malori ya wanaosafirisha, tumeingia kwenye maduka mahali zinakouzwa na tunawakamata wavuvi wenyewe wanaotumia hizo zana haramu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka kwenda hatua zaidi, kwamba sasa tunaanzisha utaratibu wa kwenda na mashua huko huko ziwani, tutawahukumu huko huko, wale tutakaowakuta wanatumia zana haramu. Na humu barabarani kama agizo lilivyo la Mkuu wa nchi, tukikukamta hata wewe una malori tunakushitaki na ku-confiscate kila kitu ulichonacho.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa Majimbo yote ya Kanda ya Ziwa tunategemea uvuvi na tumekuwa tukiona kweli jitihada za Serikali katika kupambana na wavuvi haramu kuchoma nyavu na vitu vingine; lakini zile samaki zinazovuliwa na wavuvi haramu zinauzwa viwandani. Hatujawahi kuona hata siku moja operation inapelekwa kwenye viwanda na kwenye maduka. Je, Mheshimiwa Waziri anatuhakikishiaje Wabunge wa Kanda ya Ziwa atafanya lini ziara na kulifanya zoezi hili kuwa endelevu kwenye maduka na viwanda vinavyonunua samaki zinazovuliwa na wavuvi haramu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, vita dhidi ya uvuvi haramu kama tulivyosema ni vita kwa mtu yeyote ambaye anajihusisha na uvuvi haramu kuanzia uagizwaji wa zana ambazo zinatumika kwenye uvuvi haramu wenyewe, lakini vile vile hata kwenye samaki na biashara ambayo inatokana na uvuvi haramu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, hii vita haimbagui mtu yeyote, haitamwacha mtu yeyote na tayari Mheshimiwa Waziri alishatoa tamko kwamba watu wote wanaojihusisha na uvuvi haramu wamepewa fursa ya ku-surrender vifaa vile kwa sababu kuna operation kubwa. Nimwahidi tu kwamba, hiyo operation itakapokuja itaenda vile vile kwenye viwanda na mtu yeyote ambaye anajihusisha na biashara ya uvuvi haramu.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri aliahidi kuja kufanya ziara katika Mkoa wa Mara na hususan Wilaya ya Rorya, lakini kwa sababu zisizoweza kuzuilika alikomea Musoma.
Je, yuko tayari sasa baada ya Bunge hili kuambana na Mbunge wa Rorya ili kwenda kuona usumbufu wa wale wananchi wa Rorya?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, sijawahi kwa kweli kuahidi kwenda Wilaya ya Rorya, lakini ahadi yangu ipo palepale ya kuzuru Mkoa wa Mara mzima. Kutokana na tatizo hili kwamba Rorya kweli ina special conditions za kutembelea, naomba tu Mheshimiwa Mbunge ajenge hoja mimi nina muda wa kutosha wa kuweza kufika huko na tukakagua maeneo mbalimbali. Lakini ziara ya Mkoa wa Mara ipo palepale tutafuatana na Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, kwa sababu lengo letu kubwa ni kukagua vilevile Magereza Mkoani Mara.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa wananchi wa Geita walipewa magwangala fake, na kwa kuwa Sheria ya Leseni ya Uchimbaji Mkubwa inawataka wachimbaji wakubwa kila baada ya miaka mitano wamege baadhi ya eneo wawarudishie wachimbaji wadogo. Je, Wizara iko tayari sasa kulimega eneo la Nyamatagata na Samina kuwarudishia wananchi kuwafuta machozi kwa magwangala fake waliyopewa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa namshukuru Mheshimiwa Musukuma, katika jitihada ambazo ziliwasababisha wananchi wapewe magwangala ni pamoja na Mheshimiwa Mbunge. Kwa hiyo, tunakupongeza Mheshimiwa Musukuma. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitambue kwamba shughuli za utafiti na uchimbaji wa madini kwa kawaida kabisa, ni za kupata na kupotea. Sasa ni jambo la kawaida, mwekezaji anaweza akawekeza kwenye kuchimba na akakosa. Kama ambavyo ilikuwa kwenye magwangala, wananchi walitarajia pangekuwa na thamani, lakini bahati mbaya hapakuwa na thamani. Kwa hiyo, nilitaka tu kumwelewesha Mheshimiwa Musukuma na ninampongeza sana. Pia kwa wachimbaji wote, ni jambo la kawaida mchimbaji kuanza kuchimba na asipate madini ya thamani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba tu kusema, suala la Nyamatagata na Samina, ni kweli kabisa Serikali inazungumza na Mgodi wa GGM pamoja na wawekezaji wengine, hivi sasa tuko katika hatua nzuri. Mwaka 2016 Kampuni ya GGM ilirusha ndege kuangalia maeneo ambayo hayahitaji.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Musukuma nikuhakikishie kwamba mara baada ya taratibu hizi kukamilika, wananchi wa Nyamatagata na Samina, maeneo ambayo yataachiwa na mgodi, basi yatatengwa rasmi kwa ajili ya wananchi, lakini baada ya kukamilisha mazungumzo na mgodi.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kwa kuwa matatizo yaliyopo Simiyu yanafanana sana na matatizo yaliyopo Mkoa wa Geita na Kagera, Serikali imetangaza wafugaji watoke kwenye Pori la
Kimisi na Burigi na wakatii sheria. Sasa wale askari wanaoendesha ile operesheni wanazifuata ng’ombe vijijini kilometa saba mpaka kumi na kuzirudisha porini na baadaye kuwafilisi wananchi hawa. Je, ni nini kauli ya Waziri kuhusiana
na uonevu unaoendelea kule Burigi na Kimisi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Spika, ni kweli kama alivyoeleza kwamba tayari katika zoezi linaloendelea la kuondoa mifugo katika misitu na hifadhi kuna changamoto ambazo zimeripotiwa. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara imepokea changamoto hizo na inaendelea kujadiliana ndani ya Serikali kuangalia namna ya kuzitatua kwa muda mfupi.
MHE. MUSUKUMA J. KASHEKU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nilitaka tu kumwambia kwamba, yale aliyoyajibu hapa si sawa na uhalisia ulioko kule Jimboni.
Wananchi wangu wa vijiji vya Bugurula, Kasota, Nyawirimila, Sungusila na Kakubiro, wamewekewa matangazo mwezi mmoja uliopita na wakapelekewa barua za kuondoka kwenye vijiji ambavyo tayari vina shule na sasa Waziri anasema wao hawakuwa na huo mpango na hawajafanya wanaendelea na utaratibu na wameweka vigingi. Nilikuwa nataka kujua Waziri kama hizi taarifa alizozitoa ni sahihi ili niwaambie wale wananchi wangu kule wayang’oe yale matangazo yaliyowekwa kule? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kutokana na mkanganyiko wa mipaka ya vijiji na mapori ya hifadhi kumesababisha mpaka tunavyozungumza sasa kuna operesheni zinafanyika kwenye Mkoa wa Geita na Mkoa wa Biharamulo, Serikali ilitoa tangazo la siku tatu wananchi waondoe mifugo iliyopo kwenye hifadhi; siku tatu ng’ombe zitoke kwenye eneo la hifadhi kana kwamba hizi ng’ombe sijui zina mota miguuni, lakini wananchi wa Kisukuma hawakuwa na tatizo walitii amri bila shuruti.
Na kwa kuwa waliopo kule wahifadhi wameidanganya Serikali kwa kuwaambia kuna mifugo milioni 60 na kule hakuna mifugo milioni 60; wamezikosa baada ya kupewa hiyo bajeti ya operesheni wakaikosa mifugo wananza kukamata sasa kilometa saba kwenye vijiji na wakati kuna beacon zinazoonesha mipaka ya kijiji. Je, Waziri
husika anatoa kauli gani kwa wananchi ambao
wamekamatiwa ng’ombe zao Ngara, Katente na Chato walioko mahakamani na wameshapewa hukumu ya ng’ombe zao?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Mheshimiwa Mbunge ni Mjumbe wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii na kwa hiyo kwa kiasi kikubwa anafahamu uzito, upana na ukubwa wa changamoto inayohusiana na suala la uhifadhi na
muingiliano wa shughuli za kibinadamu katika maeneo mbalimbali nchi nzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto hii ni kubwa na haifanani kutoka mahali pamoja hata mahali pengine. Yapo matatizo yanayohusiana na wakulima na yapo matatizo yanayohusiana na wafugaji. Katika swali lake la msingi Mheshimiwa Mbunge alizungumzia juu ya suala la maeneo ya vijiji ambayo yamo ndani ya hifadhi ya Geita na kweli lilikuwa ni suala la mipaka baina ya vijiji na maeneo hayo husika. Na kama nilivyojibu kwenye jibu la msingi ni kwamba Wizara yangu kwa niaba
ya Serikali haijafanya operesheni yoyote ya kuondoa wanavijiji katika maeneo hayo. Lakini nimesikia alivyosema kwamba kuna matangazo yamebandikwa huko ambayo sisi kama Wizara hata ninaposimama wakati huu mahali hapa
bado hatuwezi kuthibitisha uwepo wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya hapa kwa kuwa Serikali ni pana iko mamlaka ya Wilaya, Mkoa na ipo Serikali Kuu kupitia Wizara, sote sisi ni Serikali. Baada ya hapa nikutane naye ili tuweze kufuatilia matangazo hayo juu ya uwepo wake na
uhalali wake ili tuweze kujua namna ya kuweza kushughulikia tatizo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusu swali lake la wale wafugaji na mifugo katika maeneo ya Geita, Biharamulo na maeneo mengine ambapo zipo operesheni zinaendelea sasa hivi zikiendeshwa na mamlaka za Mikoa na Wilaya huko zilipo, kama nilivyotoa maelezo katika jibu langu la msingi, migogoro ipo katika maeneo mengi, lakini kila mahali, kila mgogoro ni wa aina yake; chanzo tofauti, ukubwa tofauti na kwa hiyo tarajia kwamba utatuzi wake pia utakuwa upo
tofauti. Katika maeneo aliyoyataja uingiaji wa mifugo katika maeneo yaliyohifadhiwa ni mkubwa sana tena uliopelekea hata kuingia kwa mifugo kutoka nchi jirani na yeye amesema.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Serikali kupitia
Mamlaka ya Mkoa imeendelea kufanya operesheni hizo kwa sababu kimsingi hatua za Serikali tulizotangaza kwamba zinaendelea kuchukuliwa haziwezi kukamilika leo au kesho
kwa sababu zinafuata taratibu za kushughulikia changamoto za Kiserikali ambazo aghalabu huchukua muda mrefu. Katika kipindi hicho tukiacha ng’ombe waendelee kubaki katika
maeneo hayo ya hifadhi, wakati utakapofika
tumekwishapata ufumbuzi wa nini kifanyike hifadhi hizo hazitakuwepo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimuombe
Mheshimiwa Mbunge utaratibu ambao unaendelea hivi sasa wa Serikali wa kushughulikia changamoto hizo kwa uzito wake na katika maeneo ambayo athari ni kubwa huo utakuwa ni
utaratibu wa Serikali na aendelee kuunga mkono jitihada za Serikali za kuamua kusimamia uhifadhi kwa maslahi ya nchi yetu hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama kutakuwa na jambo lingine ambalo ni mahususi kuhusiana na hatua hizo ambazo Serikali inachukua katika ngazi hizo za Mikoa na Wilaya basi anaweza kulileta, nimesema yeye ni Mjumbe wa Kamati
inayosimamia maliasili kwahiyo tunaweza kupokea maoni yake juu ya namna bora zaidi ya kuweza kushughulikia tatizo hili lakini kwa mujibu wa sheria. Katika hili sheria, kanuni na taratibu zitazingatiwa katika kushughulikia changamoto hizi.

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa nitoe majibu ya ziada pamoja na majibu mazuri ambayo yametolewa na Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la msitu katika Wilaya na eneo lilozunguka Mji wa Geita limefikishwa pia kwenye Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Geita na maazimio yaliyofikishwa yameletwa kwetu kwa ajili ya kufikiria ni namna
gani katika maeneo ambayo watu wanaishi tunaweza kupunguza eneo la msitu kwa ajili ya matumizi mengine ili kukidhi hali halisi ya Mji Mkuu wa Mkoa ambao sasa uko pale Geita.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, jambo hili
tunaendelea kulizungumza na Mheshimiwa Mbunge awe na subira wakati Serikali ya Mkoa na Wilaya inapoongea na Wizara kuhusu msitu huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo la pili; wapo ng’ombe ambao ni wengi sana katika maeneo ya misitu ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyataja. Mifugo hii ipo kwenye maeneo ya hifadhi kinyume cha sheria zetu; kinyume cha Sheria ya Uhifadhi wa Misitu Na. 5 ya mwaka 2009 kifungu cha 21(1). Na wananchi hawa wanajua kwamba wapo kwenye Hifadhi za Taifa kinyume cha sheria; walipewa muda wa kuondoka na tangazo la Mkoa na muda ule ukamalizika. Huwezi kusema mtu ambaye anafanya makosa ya kisheria kwamba hakupewa muda wa kutosha wa kufanya makosa yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nitumie nafasi hii kuwashauri wafugaji wote ambao wana mifugo yao ndani ya maeneo ya Hifadhi za Taifa kinyume cha sheria zetu kwamba watoe mifugo hiyo mapema iwezekanavyo kabla Serikali haijachukua hatua ya kisheria kudhibiti mifugo hiyo.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Wananchi wa Jimbo la Geita Vijijini miaka 56 ya uhuru hawajawahi kuona lami. Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni aliwaahidi lami kwenye barabara ya kutoka Geita – Bugurula – Nzela mpaka Nkome. Sasa namuuliza Mheshimiwa Waziri, je, ni lini Serikali imejipanga kuanza kufanya upembuzi yakinifu na kuanza kutengeneza kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA
MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo kawaida ya kutaja terehe kamili ya lini barabara itaanza kujengwa katika Wizara yetu kwa sababu taratibu zake za kufikia hadi ujenzi ni nyingi na zinahusisha taasisi mbalimbali ambazo huwezi ukazipangia muda wa kukamilisha hatua yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, ni ahadi ya Serikali ya Awamu ya Tano kwamba suala hili tutalitekeleza kama ambavyo Mheshimiwa Rais aliahidi wakati wa kampeni katika kipindi hiki cha miaka mitano.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Wananchi wa Jimbo la Geita Vijijini hususan Jimbo la Geita Vijijini ndilo Jimbo pekee linaloongoza kwa kupata chakula kingi kila mwaka kwenye Kanda ya Ziwa; wamekuwa na kilio cha barabara yao kutoka Senga - Sungusila - Lubanga mpaka Iseni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge watatu walionitangulia wote wamekuwa wakiomba Serikali barabara hii ichukuliwe angalau tu kwa kiwango changalawe sio lami na Serikali imekuwa ikitoa ahadi kila siku tunafanya tunafanya, na mipango yote sisi kwenye RCC tumeshabariki. Sasa nataka kujua Waziri ni lini barabara hii unaichukua na kuiweka kwenye angalau kiwango cha molami tu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Musukuma kwanza kwa kutukumbusha kuhusu barabara hii. Aliiongelea muda mrefu, kuanzia miaka ya nyuma na sasa tunamuhakikishi kwamba hii barabara itachukuliwa na TANROADS, kwa maana ya kukasimiwa. Barabara hii haijakidhi vigezo vya kupandishwa hadhi, lakini Waziri ameshakubali na ameshaikasimu barabara hii ili iweze kutekelezwa na TANROADS Mkoa wa Geita.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Ziwa Victoria kumekuwa na meli nyingi ambazo zimekuwa zikisaidia wananchi kubeba mizigo na abiria kwenda Ukerewe na nchi za jirani. Hivi sasa ni meli moja tu inayotembea MV Umoja imepaki, MV Serengeti imepaki, inayotembea ni MV Clarias peke yake. Wananchi wanaoenda visiwani hasa Ukerewe wanatumia feri za mizigo, sasa za kwetu zimeharibika, sina hakika kama Wizara imeshindwa kukarabati zile feri ama watumishi walioko kule wanafanya mipango na wale watu wenye maferi. Nataka kujua kwa Waziri ni lini feri hizi zitaanza ku-operate kwa muda muafaka?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba tunazo meli ambazo zimesimama kwa sababu ya kuharibika ikiwa ni pamoja na MV Umoja na MV Serengeti na hata hii MV Clarias siyo muda mrefu sana imekarabatiwa ni karibuni tu imeanza kutoa hiyo huduma, nayo ilikuwa imeharibika.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti iliyopita ya 2016/2017, tulitenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa meli za Ziwa Victoria, nimhakikishie pamoja na kwamba taratibu za kumpata mtu wa kuweza kufanya hiyo kazi zimeshakamilika, muda siyo mrefu kazi hiyo itaanza na kazi hiyo itakapokamilika meli hizo zitarudi majini. Aidha, tuna mpango wa muda mrefu wa kujenga meli mpya itakayohudumia Ziwa Victoria na maziwa mengine Tanganyika na Nyasa, kwa Nyasa tumeshakamilisha ili kuhakikisha kwamba meli hizo ambazo zimefanya kazi muda mrefu sana katika maziwa hayo zinapunguziwa uzito na meli mpya zitakazokuwa zimejengwa. Utaratibu wa kujenga meli hiyo bado tunaendelea nao na muda si mrefu tunatarajia kupata mkandarasi wa kujenga meli hiyo.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kwa kuwa Halmashauri ya Geita DC haina Engineer wa maji na Mheshimiwa Naibu Waziri alishuhudia hilo kwamba Engineer tuliyekuwa naye hakuwa na cheti cha kuwa Engineer wa maji kwenye Halmshauri yetu, na tulimsimamisha mpaka sasa hatuna Engineer, je, Serikali ina mpango gani wa kuleta Engineer wa maji kwenye Halmashauri ya Geita DC?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWAlA ZA MKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kutokana na matatizo yaliyojitokeza pale Geita ilionekana kwamba Injinia yule kipindi kile ilikuwa hatoshi kusimamia miradi ya maji katika Halmashauri ya Geita.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo naomba nimhakikishie kwamba tunafanya harakati. Tumekuwa na changamoto ya mainjinia katika maeneo mbalimbali lakini eneo la Geita tumelipa kipaumbele kwa sababu kuna miradi hii mikubwa ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa Serikali katika eneo lile na ukanda ule ni kutumia Ziwa Victoria, kwa hiyo eneo lake tutalipa kipaumbele. Kwa hiyo Mheshimiwa Musukuma naomba avute subira tu kidogo hili jambo tuliweke vizuri, tutapata injinia mzuri ambaye atatusaidia katika miradi ya maji katika eneo lake.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kutambua uwakilishi wangu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa muda mrefu nimekuwa nikisikia Wabunge wanalalamika na kuwatetea sana wasanii pindi wanapopata matatizo kwamba tunawatumia kwenye chaguzi lakini baada ya chaguzi hatuwasaidii. Hata hivyo, waganga wa kienyeji kwa karama niliyonayo nikiangalia humu ndani wakati wa uchaguzi wawili, watatu hamkupita kwao labda Mzee Selasini...
Na siyo Wabunge peke yake ni jamii nzima na waganga hawa baada ya chaguzi…
Sawa Mheshimiwa Spika. Waganga hawa baada ya chaguzi tunawatelekeza na kuwatumia Polisi.
e, Serikali haioni umuhimu wa kujenga chuo cha kuwasaidia waganga hata kama ni kwa elimu ndogo? (Makofi)
WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Musukuma kwa swali lake la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba nchi yetu inathamini na kuheshimu kazi za waganga wa asili na ndiyo maana tumepitisha Sera ya Waganga wa Asili na Tiba Mbadala ya 2002 lakini pia kanuni. Lengo la sera hii ni kuendeleza tiba asili na tiba mbadala kwa sababu ni kweli asilimia 60 ya Watanzania wanatumia huduma za waganga wa tiba asili na tiba mbadala.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, siyo tu kujenga chuo lakini tunalo pia Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala ambalo linafanya mafunzo ya mara kwa mara kwa waganga wetu especial katika kuhifadhi dawa zao na kufanya ufumbuzi. Sasa hivi tumeweka mfumo mzuri wa kuwasajili waganga wetu, tumewateua ma-DMO wote kuwa ni wasajili wasaidizi kwa ajili waganga wetu wa asili na tunaendelea kuwaenzi kwa sababu wana mchango mkubwa sana katika kutatua huduma za afya kwa wananchi. (Makofi)
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matatizo yaliyoko Songwe yanafanana kabiasa na matatizo yaliyoko kwenye Jimbo la Geita Vijijini. Jimbo la Geita Vijijini lina wakazi kama 650,000, na tuna vituo viwili vikubwa ambavyo wasimamizi wao ni askari wenye nyota mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumelalamika muda mrefu sana kwa ngazi ya Mkoa wetu naona sasa tutafute msada huku kwa Waziri. Jimbo zima na vituo hivi vikubwa havina askari wa kike, kwa hiyo askari wa kiume wanawapekua wanawake.
Sasa pengine kwa kuwa sisi ni vijijini hakuna haki za binadamu, nilikuwa namuomba Mheshimiwa Waziri, ni lini utatuletea askari wa kike kwenye vituo vile vikubwa ili wake zetu wakapekuliwe na askari wa kike na si askari wa kiume? (Makofi).
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yake ni ya msingi tutaifanyia kazi.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuwa matatizo yaliyopo kwenye mwambao wa Pwani hayana tofauti sana na matatizo yaliyoko kule Geita. Mkoa wa Geita unayo bandari bubu inaitwa Nungwe ambayo inatumiwa na Mgodi wa GGM kushusha shehena kubwa.
Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari baada ya kumaliza shughuli za Bunge afuatane na Wabunge wa Geita akalione lile eneo ili Serikali iweze kuipitisha kuwa bandari halali na watumiaji wengine waweze kupita pale? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru kwa hiyo taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Musukuma kuhusu hiyo bandari bubu ya Nungwe na niko tayari kufuatana nae pamoja na Wabunge wengine wa Geita ili tukaiangalie hiyo kwa undani na tuone kama ipo katika orodha ambayo inashughulikiwa na viongozi wa Mikoa wa Ziwa Victoria katika kushughulikia suala la kudhibiti bandari bubu. (Makofi)
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mawasiliano mbali na simu, mawasiliano ni pamoja na barabara, wananchi wa Jimbo la Geita Vijijini Sengerema na Buchosa kumekuwa na kero kubwa sana ya TANROAD Mkoa wa Mwanza kuweka mzani kwenye barabara ya vumbi, kitendo ambacho hatukioni kwenye mikoa mingine yoyote Tanzania. Je, Waziri yuko tayari kutoa kauli ili mizani inayowekwa kwenye barabara ya vumbi ambayo ni mbaya iondolewe mara moja?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemsikia Mheshimiwa Mbunge na ninachoweza kumwahidi ni kwamba nitalifanyia kazi suala hilo, nikalione hilo eneo, nijue kwa nini wameweka mizani katika barabara ya aina hiyo, baada ya hapo tutachukua hatua. (Makofi)
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kwa kuwa matatizo yaliyoko kule Manyamanyama hayana tofauti sana na matatizo yaliyoko kwenye Jimbo la Geita. Mwaka jana mwezi Machi, Waziri wa Afya alikipandisha Kituo cha Afya Nzela na kuwa hospitali ya wilaya kwa kuwa Wilaya ya Geita haina hospitali ya wilaya lakini kumekuwa na mkanganyiko kati ya TAMISEMI na Wizara ya Afya na Waziri hajawahi kutembelea eneo lile akaliona pengine akawa na huruma kama alivyopata huruma ya Waziri wa Afya. Je, ni lini Waziri wa TAMISEMI ataambatana na mimi kwenda kuona kituo kile kilichopandishwa hadhi na majengo na ubora ulioko pale ili aweze kuridhia na mambo yaende mbele? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nipongeze majibu mazuri ya Naibu wangu, Mheshimiwa Kandege aliyoyatoa katika maswali ya awali yaliyojitokeza, hata hivyo, naomba kujibu swali la mtani wangu Mheshimiwa Musukuma, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kuambatana, namwomba Mheshimiwa Mbunge kwanza aondoe hofu, kama tulivyokwenda katika Jimbo lake na katika Mkoa wa Geita mara nyingi na kufanya kazi kubwa sana, nimwambie mara baada ya Bunge hili la bajeti nitaomba twende kwa ziara maalum kwa sababu Mkoa wa Geita miongoni mwa mambo tunayokwenda kuyafanya ni ujenzi wa hospitali zingine za wilaya katika mkoa huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina kila sababu kufika Geita kuangalia maeneo muafaka wapi tutajenga hospitali hizo kwa manufaa mapana ya watani zangu Wasukuma wa Mkoa wa Geita ili waweze kupata huduma nzuri ya afya. Kwa hiyo, Mheshimiwa Musukuma asihofu tutaondoka pamoja. (Makofi)
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kuwa Halmashauri ya Geita inaudai mgodi wa GGM zaidi ya dola milioni 12; tumekaa tukakubaliana watulipe kwa awamu. Awamu ya kwanza ilikuwa itekelezwe mwezi wa pili, lakini utekelezaji huo haujafanyika na Halmashauri haina nguvu tena ya kuudai Mgodi wa GGM. Je, Wizara inaisaidiaje Halmashauri ya Geita ili tuweze kulipwa pesa hizo?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Halmashauri ya Geita inaudai GGM service levy. Tulitoa ushauri kama Wizara kwamba wakae kwa pamoja na waangalie ni namna gani Kampuni ya GGM inaweza ikawalipa wale Halmashauri ya Geita, yaani wakae kwa pamoja waelewane ili wangalie namna bora ya kuweza kulipa kidogo kidogo deni hilo na wameshakaa na nilipokwenda mara ya mwisho mwezi wa pili walisema kwamba wanakwenda kukaa na Halmashauri, ili waweze kusaini memorandum of understanding, namna ya kuweza kulipa deni hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama hawajalipwa mpaka sasahivi, naomba nishirikiane na Mbunge kwamba nifuatilie. Sisi kama Wizara tuko pamoja tutahakikisha kwamba haki ya Halmashauri ya Geita italipwa kama inavyostahili. Ahsante sana.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Ni hivi juzi tu siku mbili, tatu zilizopita Wabunge wa Geita tumeletewa barua inayoonesha CSR iliyotolewa na GGM 2017/2018 dola 9,600,000 lakini katika majibu ya Waziri amesema ni dola milioni 6.5 na hizi barua ambazo tumeletewa tayari ziko kwa Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya na baadhi ya wananchi wameshazipata, lakini kwa majibu ya Wizara ina maana tunachanganyikiwa tujue ipi ni sahihi na ipi siyo sahihi.
Mheshimiwa Spika, sasa ni nini kauli ya Wizara kuweza kuisaidia Halmashauri angalau kufanya auditing kujua uongo uko Wizarani au uongo uko mgodini. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Spika, ni kwamba GGM tuliwaeleza tarehe 27 Februari, 2018 watuandikie breakdown ya kuonesha ni jinsi gani wametumia fedha za CSR na majibu waliyonipa ni kwamba kwa mwaka 2017 wametumia kama nilivyosema katika jibu la msingi dola 6,358,000. Mheshimiwa Musukuma anachosema dola milioni 9.7 ni jumla ya miaka miwili yaani mwaka 2016 na 2017 kajumlisha kapata 9.7 lakini swali la msingi limeuliza mwaka 2017 jibu ni milioni 6.358. Mheshimiwa Spika, ahsante.
Waheshimiwa Wabunge, tunaendelea na Wizara ya Maliasili na Utalii. Swali linaulizwa na Mheshimiwa Hawa Mchafu.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwa kuwa, Halmashauri ya Geita iligawanywa mara mbili, Geita Mjini na Geita Vijijini; na kwamba mpaka sasa Ofisi za Mkurugenzi wa Geita Vijijini ziko mjini; je, TAMISEMI inafikiriaje kumhamisha Mkurugenzi wa Geita Vijijini kurudi vijijini ambako ni Nzela ili aweze kuwa karibu na wananchi wake?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, swali hili la Mheshimiwa Musukuma ni swali la kiutendaji zaidi, naomba nilifanyie kazi baada ya kurudi ofisini.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Niipongeze sana Wizara ya Madini kwa kipindi cha mpito toka Mheshimiwa Rais aliposema leseni ambazo hazifanyiwi kazi na watu wanaomiliki leseni nyingi na zinazoisha waruhusiwe wachimbaji wadogo waweze kuchimba. Mkoa wa Geita una raha kwa kuachiwa maeneo ya Rwamgasa, Nyakafulu, Stamico, Tembo-Mine na Bingwa. Je, Wizara ni lini mtawamilikisha wachimbaji wadogo ambao tayari wako kwenye maeneo ambayo yalikuwa leseni zake zimeisha na nyingine hazitumiki? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Musukuma, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli anawapenda wachimbaji wadogo. Kwa kweli ametuelekeza tuwalee wachimbaji wadogo, tuwasimamie na tuwasaidie waweze kuchimba kwa tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu maeneo ambayo wameweza kupatiwa kwa ajili ya uchimbaji, ili tuweze kuwahalalisha ni lazima tuwapatie leseni. Naomba kutoa taarifa kwenye Bunge lako Tukufu kwamba ndani ya wiki hii tunayo maombi zaidi ya 8,000 ya uchimbaji mdogo tunaanza kutoa leseni. Ahsante.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Dhana ya uvuvi haramu imeenea sana kwenye kauli za Mawaziri, lakini kule ziwani kuna aina za samaki kama 30 na samaki pia wana makuzi tofauti, ni kama binadamu. Ukichukua umri wa Musukuma ukachukua na umri wa Mwalongo, tuko sawa, lakini ukituangalia kwa maumbile tulivyo tuko tofauti na unapotupa nyavu ziwani inakuja na samaki za aina tofauti wakiwepo wenye tabia kama yangu na Mwalongo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ukiwapima kwenye rula hawalingani lakini umri ni mmoja. Kwa kuwa sheria yenyewe ndiyo inajichanganya, ni lini Wizara itakuja na sheria ambayo itam-favour pia mvuvi anapokumbana na matatizo kama ya maumbile ya binadamu? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; Mheshimiwa Waziri wakati operesheni hii inapoendelea, kumekuwa na tabia ya kukamata nyavu saa nne na zinachomwa saa sita. Mfano mzuri ni kwenye Kisiwa cha Izumacheri kilichopo Jimbo la Geita Vijijini ambapo Maafisa Uvuvi walikamata nyavu ambazo siyo haramu lakini wakanyimwa rushwa, wakachoma nyavu dakika 15 zilizofuata na nyavu hizi ni halali. Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kufuatana na mimi kwenda kusikiliza SACCOS hiyo na kutoa adhabu kwa wale waliohusika na suala hili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la lini Serikali itakuja na sheria mpya itakayowasaidia wavuvi waweze kufanya shughuli zao kwa uzuri zaidi, hasa ikizingatiwa hili analolisema la kwamba samaki wako wa aina tofauti na ile nyavu inapoingia inakwenda kuzoa hata wengine wasiohusika.
Mheshimiwa Spika, Serikali tupo katika hatua ya mwisho ya maboresho ya Sheria yetu ya Uvuvi na itakapokuwa tayari itaingia humu Bungeni ambapo Waheshimiwa Wabunge watashiriki kikamilifu katika kuhakikisha kwamba sheria ile tunaiboresha kwa pamoja kwa maslahi mapana ya Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ameeleza juu ya suala linalohusu nyavu, ya kwamba nyavu hizi zinapokamatwa ghafla tu zinachomwa moto na akanitaka kama niko tayari niweze kufuatana naye kwa ajili ya kuweza kwenda kuwachukulia hatua wale watumishi wa Serikali ambao wanatenda kinyume.
Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Musukuma na Waheshimiwa Wabunge wote na hata wananchi wote wanaoshughulika katika shughuli hizi za uvuvi, Wizara yangu tuko tayari kabisa sisi kama viongozi kwa specific cases kama hii anayoizungumzia Mheshimiwa Musukuma, tutakwenda popote pale na endapo tutabaini watumishi wetu wametenda kinyume sisi kama Mawaziri tuko tayari kuwachukulia hatua kwa ajili ya mustakabali mpana zaidi wa wananchi na wavuvi wetu. (Makofi)
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Kisiwa cha Izumacheri hawana usafiri tofauti na usafiri wa Meli ya MV Chato, leo ni mwaka wa tatu toka tumeingia Bungeni Mheshimiwa Rais aliahidi, meli hiyo inapaki juu ya jiwe, na ni mwaka wa pili tunaahidiwa kuletewa pesa kwa ajili ya ujenzi wa gati.
Je, Mheshimiwa Waziri uko tayari kuambatana nami baada ya Bunge kwenda kuona adha ya meli inayo-park juu ya jiwe ili uweze kuachia pesa kwa ajili ya ujenzi wa gati hilo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Rais aliahidi ujenzi wa gati kwa eneo hilo na bado Serikali inatambua na inaendelea kufuatilia namna ya utekelezaji wa ahadi hiyo ya Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumewaagiza TPA toka mwaka jana mwanzoni, wanaendelea na utaratibu wa kutuletea gharama halisi za kutengeneza gati eneo hilo ili wananchi waweze kupata huduma kwa usahihi. Nieleze tu kwamba niko tayari kuongozana na Mheshimiwa Musukuma kwenda kuangalia eneo hilo kwa ajili ya kuweka gati. Ahsante. (Makofi)
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa matatizo yaliyoelezwa na Waheshimiwa Wabunge wenzangu ni sawa kabisa na matatizo yaliyoko Jimboni kwangu. Jimbo la Geita Vijijini lenye population ya watu kama 1,000,000 halina kabisa Kituo cha Afya hata kimoja, baada ya Kituo cha Afya Nzela kupanda hadhi na kuwa Hospitali ya Wilaya. Je, Wizara haioni umuhimu wa kutusaidia pesa ili tuweze kujenga kituo kwa wananchi walioko Ibisabageni na Rubanga kuliko na umbali wa kilometa 80 mpaka kukipata Kituo cha Afya kilichopandishwa hadhi ya kuwa Hospitali ya Wilaya? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kweli tunafahamu changamoto kubwa ya afya kule Geita Vijijini na hata hivyo namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa sababu kwa pamoja tumeshirikiana kuhakikisha Kituo cha Afya cha Nzela kile cha kwanza kimekuwa ni cha kisasa zaidi. Hata hivyo, kwa vile tunajua changamoto ni kubwa, ndiyo maana Geita DC sasa hivi tunaenda kuipa Hospitali ya Wilaya rasmi sasa katika bajeti yetu ya mwaka 2018/2019.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, katika Mpango wa Serikali wa sasa, nia yetu ni kwamba kabla ya mwezi wa Tisa mwishoni kuelekea mwezi wa Kumi tutakuwa tumeweka miundombinu ya kisasa katika Kituo cha Afya cha Nyarugusu, nadhani ni Zahanati lakini tutai-upgrade. Lengo kubwa ni kwamba wachimbaji ambao ni population kubwa ya eneo lile waweze kupata huduma nzuri sana ya afya na kuwahudumia wananchi wa Geita kwa ujumla wake. (Makofi) Mheshimiwa Spika, nashukuru.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, nimpongeze Waziri kwa majibu mazuri, lakini naona majibu yake hayajitoshelezi.
Mheshimiwa Spika, kwa kifungu cha 105(3) kama alivyoainisha Mheshimiwa Naibu Waziri, ni kwamba mgodi utapokea maelekezo kutoka kwenye mabaraza mawili maana yake Geita Mjini na Vijijini, na mgodi utatulipa kama shilingi bilioni 9.1. Lakini kwa mchanganuo wa Halmashauri zetu, Halmashauri ya Geita Vijijini inapata asilimia 46, asilimia 54 zinabaki Geita Mjini. Sasa kwa maelezo na mchanganuo aliyoutoa Waziri CSR ya Halmashauri ya Geita inaingiaje kwenye Chato, Bukombe na Mbogwe? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; Geita Vijijini na Mjini tuna mgogoro na Mgodi wa GGM, tunawadai dola bilioni 12 wewe mwenyewe unafahamu na mlishauri watulipe kwanza dola laki nane mwezi wa kwanza, leo ni mwezi wa tano hatuoni majibu na hawatusikilizi, tumeshapeleka demand, sasa tunataka kupelekana mahakamani na Mgodi wa Geita unazidi kusafirisha dhahabu Jumanne na Ijumaa, na ili kibali cha kusafirisha dhahabu kitoke lazima walipe kodi za Serikali ninyi Wizara ndio mtoe kibali cha kusafirisha.
Mheshimiwa Spika, kwa nini Wizara isichukue action ya kutusaidia kuwanyima kibali ili waweze kutulipa hata kesho hizo dola laki nane? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Spika, katika swali la kwanza, ni kwamba mgawanyo wa fedha katika Halmashauri ya Mji na Halmashauri ya Geita Vijijini, haya ni makubaliano ambayo wao wenyewe walifikia na Baraza la Madiwani na Mheshimiwa Mbunge naye ni Mjumbe, kwa hiyo, walifikia maamuzi haya na huu ndiyo msimamo wa Halmashauri na hivyo ndivyo mgawanyo utakavyokuwa.
Mheshimiwa Spika, kuhusu shilingi hizo bilioni alizozitaja ambazo ni sawasawa na dola laki nane ambazo walisema kwamba wanatakiwa wapewe na Mgodi wa GGM, ni kwamba mpaka sasa hivi GGM wako tayari kutoa hizo fedha. Mgogoro uliokuwepo ilikuwa ni Halmashauri ipi au akaunti ya Halmashauri ipi ipewe fedha hizo, na mpaka hapa ninapozungumza ni kwamba tayari Mkuu wa Mkoa kesho kutwa, siku ya tarehe 10 Mei, anakaa na hizi Halmashauri mbili, anakaa na hiyo GGM waelewane kwa pamoja ni Halmashauri ipi akaunti yake iweze kupewa fedha hizo na wao waweze kutafuta utaratibu wa kuweza kugawana fedha hizo.
Mheshimiwa Spika, la mwisho kwa kuongezea, suala la Halmashauri ya Mbogwe na halmashauri nyingine, Chato na maeneo mengine, napenda kumwambia Mheshimiwa Mbunge kwamba waendelee kushiriki vile vikao vya Halmashauri ili waweze kuelewana vizuri kupitia Sekretarieti ya Mkoa waangalie ni namna gani ya kugawanya hizo fedha, sisi kama Wizara tutasimamia tu kuhakikisha GGM wameweza kutoa fedha za CSR. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwana naomba niweke kumbukumbu sawa. Mimi ni Mbunge wa Geita, siyo Geita Vijijini. Hakuna Jimbo la Geita Vijijini.

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Geita DC ina population ya takribani watu 1,200,000 kwa sensa ya mwaka 2012/2013. Sasa kwa majibu ya Serikali, inavyoonekana, bado tutakwenda hata uchaguzi ujao tukiwa bado tunakaa Halmashauri moja. Je, Serikali inatoa kauli gani ya uharaka kwa ajili ya kuharakisha hizo taasisi zilizobaki ili tuweze kupata mgawanyo wa Halmashauri mbili?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, naomba Mheshimiwa Waziri atamke kitu kwamba kulingana na ukubwa na wingi wa watu wa Halmashauri ya Geita DC, Serikali inaona umuhimu gani wa kutuongezea ceiling ya bajeti kwa wingi wa watu tulionao?

Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kama nilivyojibu kwenye jibu langu la msingi ni kwamba suala la kugawa Mamlaka za Serikali za Mitaa linatakiwa lianzishwe na mamlaka yenyewe kwenye eneo hilo. Nimesema tayari jambo hili limejadiliwa kwenye Halmashauri yao ya Wilaya ya Geita. Sasa ni wajibu wao kupeleka mjadala huo kwenye ngazi ya Wilaya na ngazi ya Mkoa, nasi tupo tayari kupokea mapendekezo yao na tuangalie uharaka na ulazima wa kufanya maamuzi ya kugawa Halmashauri hiyo.

Mheshimiwa Spika, jibu la swali la pili ni kwamba bajeti ya Serikali inategemea na uwezo uliopo. Nia ya Serikali ni njema kabisa kwamba bajeti iongezeke na kila mtu angeweza kupata mgao ambao angehitaji. Hili nalo linategemea pia uwezo wa Serikali, kadri itakavyoruhusu basi bajeti itaongezeka ili huduma iweze kupelekwa kwa wananchi wa Geita na maeneo mengine ya nchi. Ahsante.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru matatizo yaliyoko Singida ni sawa kabisa na matatizo yaliyoko Geita DC, Hospitali ya Wilaya ya Geita imepandishwa hadhi takriban miezi sita na tunaishukuru sana Serikali kwa sababu imetuletea vifaa vingi x-ray machine, Ultra sound, machine za meno, vitu vya theatre, lakini vitu hivi vyote viko store kwa sababu hatuna wataalam na hospitali ile inaendeshwa na AMO na Madaktari wetu wengi bado wako Geita Mjini wamekaa tu ofisini. Je, ni nini kauli ya Serikali kumwelekeza Mganga Mkuu wa Mkoa apeleke watu wenye hadhi ya kuendesha Hospitali ya Wilaya?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Joseph Musukuma kwa kazi kubwa ambayo ameendelea kuifanya kufuatilia Hospitali hii ya Nzela katika Wilaya ya Geita na nilipata fursa ya kutembelea hospitali hii na ni hospitali kubwa na iliyojengwa kisasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe maelekezo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhambi kubwa sana kama hospitali imekamilika na vifaa vipo na haitoi huduma zile zilizokusudiwa wakati sisi kama Serikali tulishapeleka wataalam. Nitumie fursa hii kumkumbusha Mganga Mkuu na kumwelekeza Mganga Mkuu wa Mkoa kuhakikisha kwamba wale wataalam wote ambao Serikali imewapatia na wapo mjini hawako katika kituo cha kazi kuhakikisha kwamba mara moja wanafika kule na wanatoa huduma kwa wananchi.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, Kata ya Izumacheli inaundwa na Vijiji vitatu, Kijiji cha Izumacheli, Kijiji cha Butwa na Kijiji cha Runazi na ina takriban wakazi kama elfu 40 wako katikati ya ziwa. Tunaishukuru pia Serikali ilituletea meli ya MV Chato ambayo inapita pale mara mbili kwa wiki. Swali langu, meli hii haina sehemu ya kupaki, inapaki juu ya jiwe, kitendo ambacho ni hatari sana kwa maisha ya Wananchi wa Izumacheli.

Je, Mheshimiwa Naibu Waziri ni nini kauli ya Serikali kulichukulia hili suala serious, ili kuwaepusha wananchi wale wasipate matatizo katika maisha yao?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa, wananchi hawa tumewaahidi sana zaidi ya mara tatu sasa kwamba, daraja litatengenezwa, gati itatengenezwa na Mheshimiwa Naibu Waziri na Serikali imeonesha nia ya kuweza kuwasaidia wananchi hawa. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari sasa baada ya Bunge hili kwenda kujionea sehemu ambayo meli inaendelea kupaki kupakia abiria mpaka sasa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHATA J. NDITIYE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Joseph Musukuma, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Musukuma kwa jitihada kubwa mbalimbali anazozifanya katika kuwatetea na kuwapigania wananchi wa Jimbo la Geita Vijijini ambako yeye ni Mbunge mahiri. Sasa naomba nijibu maswali yake kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa ni kweli kwamba, tumekwishaanza mchakato karibu miaka miwili iliyopita ambapo upembuzi yakinifu umefanyika na usanifu wa kina umeshafanyika kwa ajili ya kujenga gati eneo la Izumacheli, lakini pia tumeshatoa shilingi milioni 200 kwa ajili ya hatua za mwanzo za kuanza ujenzi wa gati hiyo. Kwenye bajeti ya mwaka huu kama Mheshimiwa atapigana ipitishwe tunategemea kutenga pesa nyingine zaidi kwa ajili sasa ya kuendelea kwa kasi kubwa sana ili wananchi wa Izumacheli na maeneo ya Butwa, Ilasi na vijiji vinavyozunguka waweze kupata huduma ya kivuko.

Mheshimia Naibu Spika, swali la pili, mimi niko tayari baada ya kipindi hiki cha Bunge kwenda na Mheshimiwa Musukuma kutembelea maeneo ambayo yana changamoto ya usafiri.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Sina sababu ya kumjibu rafiki yangu Mheshimiwa Bashe kwa sababu alikuwa mwenzetu huku alikuwa anazijua vizuri takwimu.

Mheshimiwa Spika, nilichokisema ni sahihi. Swali langu la kwanza hivi viuadudu tunapokuwa tumelima pamba vinakuja wakati ambapo siyo sahihi na vinapokuja vingine vime- expire. Hizi takwimu anazozisoma Mheshimiwa Bashe ni takwimu za makaratasi. Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari tutakapomaliza Bunge hili twende kwa wananchi wangu wa Kijiji cha Rubanga, Isirwabutondwe, ukajionee madhara waliyoyapata kipindi kilichopita?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, katika msimu wa pamba 2018/2019 kumeingia mdudu anaitwa ushirika na Waziri anaufahamu kabisa. Tumekuwa na matatizo makubwa sana kati ya mkulima na wanunuzi wa pamba uliosababishwa na ushirika. Yote haya yamesababishwa na Serikali kutokutusikiliza sisi wakulima. Ushirika ni chombo ambacho kimetuvuruga sana wakulima wa pamba pamoja na kwake Mheshimiwa Bashe miaka ya nyuma lakini Serikali ilichukua uamuzi wa kusema sasa ushirika lazima ununue pamba kwa bei inayotaka ushirika. Sasa Mheshimiwa Waziri nilikuwa nauliza kwa sababu Serikali inautambua ushirika na una asset zake ambazo zinaweza kukopeshwa benki, mko tayari sasa kutoa kauli kwamba wakope hela bank ili waingie kwenye ushindani na makampuni mengine ili msimu ujao kusitokee vurugu iliyotokea mwaka huu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, kwanza nikiri kwamba ni ukweli usiofichika kwamba wakulima wa pamba kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya kupewa baadhi ya viuadudu vikiwa chini ya kiwango. Sisi kama Wizara ya Kilimo tumeamua kwamba katika msimu wa mwaka huu ambao sasa hivi wakulima wamelima viuadudu vyote vitakavyosambazwa msambazaji atasaini mkataba wa quality assurance ili pale ambapo atapeleka kiuadudu ama dawa itakuwa na tatizo la ubora atakuwa heard responsible na kushtakiwa kwa uhujumu uchumi kwa sababu kile ni kitendo cha kuhujumu uchumi wa mkulima na taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, lakini mbali na hapo, tumewataka wasambazaji wote ambao wataingia makubaliano ya kusambaza dawa hizi wahakikishe wana-provide extension services. Kwa sababu si sahihi kwenda ku-damp dawa katika go-down bila kushiriki katika zoezi la kutoa elimu ya usambazaji na upulizaji wa dawa. Kwa hiyo, usambazaji katika msimu huu utaendana pamoja na makubaliano juu ya suala la ubora na yeyote atakayesambaza dawa ambayo itakuwa chini ya ubora atachukuliwa hatua za kisheria na business as usual katika suala la dawa halitakuwepo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la ushirika, kwanza kuhakikisha ushirika unajengwa ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi na Serikali iliyoko madarakani inasimamia utekelezaji wa ilani wa chama kilichopo madarakani. Ni sahihi kwamba kumekuwepo na viongozi wa ushirika ambao siyo waaminifu. Tatizo hili si tu linasababishwa na ushirika lakini vilevile wako baadhi ya wanunuzi wa pamba na Mheshimiwa Musukuma anawajua na sisi wote tunajua kwamba wanafanya mchakato wa kuvuruga mfumo ili waweze ku-benefit.

Mheshimiwa Spika, sisi kama Serikali tumeamua safari hii kwanza ushirika haununui pamba anayenunua pamba ni mfanyabiashara binafsi. Tunachokifanya ni kwamba tunatumia Ushirika na Vyama vya Msingi ili wakulima waweze kukusanya pamba yao sehemu moja na kupitia ushirika kudhibiti suala la ubora ambalo linaathiri zao la pamba katika soko la dunia. Msimu huu haujasababishiwa matatizo yake na ushirika msimu huu bei ya pamba imekumbwa na tatizo katika soko la dunia.

Mheshimiwa Spika, msimu ujao kutakuwa hakuna malipo ya cash, wakulima wote watatakiwa wawe bank account, Vyama vyote vya Msingi vitakuwa na bank account na wafanyabiashara wote watalipa fedha za wakulima kupitia bank account. Hivi tunavyoongea bank ya CRDB na NMB wanazunguka vijijini kuwafungulia wakulima wa pamba akaunti bila gharama. Akaunti zao zitakuwa bure ili msimu ujao tusikumbane na matatizo yaliyotokea katika msimu huu.

Mheshimiwa Spika, lakini niwaombe Waheshimiwa Wabunge na ninyi mshiriki katika suala la kuhakikisha katika ngazi za AMCOS viongozi wanaopatikana ni waaminifu ili waweze kusimamia vyama vya ushirika na kuweza kufikia lengo la Serikali kujenga ushirika uliokuwa imara.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuskhuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuulizwa swali la nyongeza.

Jimbo la geita Vijijini lina population ya watu takribani 450,000 mpaka 500,000 na halina Kituo cha afya hata kimoja. Je, Serikali haioni umhimu wa kutupatia kituo chaafya katika Kijiji cha Ibisabageni, Tarafa ya Isuramtundwe kwa ajili ya kuokoa wale akina mama wanaosafiri kwa umbali wa Kilometa 80 kuipata hospitali ya Wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Musukuma kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba uniruhusu kwa dhati kabisa nimpongeze Mheshimiwa Musukuma jinsi ambavyo amekuwa akipigania suala zima lafya na yeye amekuwa akijinasibu kwamba katika maeneo ambayo yamefanikiwa kujengwa hospitali nzuri ya Wilaya ni pamoja na kwenye Jimbo lake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, adhma ya Serikali ni kuhakikisha kwamba inasogeza huduma za afya kwa wananchi. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kama ambavyo amekuwa akitoa imani kwa Serikali azidi kuiamini kwamba pale ambapo wananchi na hasa sehemu ambayo population ni kubwa kama ambavyo ametaja katika eneo lake hakika kwa kadri bajeti itakavyokuwa inaruhusu kwa siku za usoni na wao tutawajengea kituo cha afya.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Halmashauri ya Geita DC ina population zaidi ya watu 1,300,000 na tunaye OCD mmoja peke yake ambaye anafanya kazi kwenye Halmashauri hiyo ya watu 1,300,000 plus Geita Mjini yenye watu zaidi ya 600,000.

Je, Waziri ananiambiaje kuhusiana na kutafuta Kanda Maalum Nzela ili kumsaidia OCD wa Geita, kumpunguzia ukubwa wa eneo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, maamuzi ya kutengeneza kanda maalum yanategemea sababu mbalimbali au vigezo mbalimbali ikiwemo ukubwa wa kijiografia, hali ya uhalifu katika eneo husika na kadhalika. Kwa hiyo, sitaki nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunaweza kufanya hilo jambo kama ambavyo amependekeza kwa sasa hivi, kwa sababu sina hakika kwamba eneo hilo imekidhi vigezo ambavyo vinahitajika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, tunalipokea na tuone, kama imekidhi vigezo na kama hali itaruhusu, basi tutalitafakari na kulitolea maamuzi sahihi kwa wakati muafaka.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba kuuliza swali langu la nyongeza:-

Barabara ya kutoka Senga Ibisabageni mpaka Sima ni barabara inayotuunganisha Mkoa wa Geita na Mkoa wa Mwanza na Serikali ilitupa fedha upande wa Geita na upande wa Mwanza. Upande wa Geita tulishalima eneo letu tukamaliza lakini upande wa Mwanza umebakiza kama kilomita tatu na leo ni mara ya tatu namuuliza Mheshimiwa Waziri.

Je, Mheshimiwa Waziri uko tayari kufuatana na mimi kwenda kuona zile kilomita tatu tu ambazo upande wa Mwanza wameshindwa kumaliza ili watu waanze kupitisha magari yao pale? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, niko tayari kufuatana naye. (Makofi)
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nashukuru pia majibu ya Serikali lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri anafahamu kwamba Halmashauri ya Wilaya ya Geita Mji na Geita Vijijini, tulikuwa tunaudai Mgodi wa Geita kiasi cha dola 12,830,000 na anafahamu vizuri kwamba ilifikia mahali mpaka tukaandamana tukawekwa ndani mimi nikiwa mmoja wao. Baada ya kutolewa pale tulikaa kwenye kikao cha pamoja pamoja na Wizara ya Madini na TAMISEMI, Waziri akaamua kwamba wakatulipe kwanza dola 800,000 halafu tufanye mazungumzo ya haraka ili waweze kulipa dola milioni 12,830,000.

Mheshimiwa Mwenyekit, lakini baada ya kutoka hapa documents zote tulizokuwa tunafuatilia sisi kama Halmashauri mbili, ziliporwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa. Toka walipochukua nyaraka zile Ofisi ya Mkuu wa Mkoa mpaka leo miaka mitatu hakuna kinachoendelea. Swali la kwanza, ni nini kauli yako kwa Mkuu wa Mkoa kurudisha nyaraka kwenye Halmashauri zetu kwa kuwa tuna wanasheria wazuri ili tuendelee na mchakato wa kudai fedha zetu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, toka tumezaliwa tunaijua Bacliff haifanyi kazi ni utafiti usiokamilika. Miaka karibia hamsini na kitu ni utafiti usiokamilika; na kwa sasa leseni ile imeisha na kauli ya Rais ni kuzifuta leseni ambazo hazifanyi kazi ili wapewe wachimbaji wadogo na wewe mwenyewe Waziri unajisifu hapa na unaona tunavyofanya vizuri wachimbaji wadogo, tunafukuzana sasa na migodi mikubwa katika kukusanya dhahabu. Ni lini leseni hii itafutwa ili eneo lile warudishiwe wachimbaji wadogo?
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Joseph Kasheku Msukuma, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kulikuwa na mgogoro wa ulipaji wa service levy kwa Mgodi wa GGM pamoja na Halmashauri hizo mbili nilizozitaja za Geita Mji pamoja na Halmashauri ya Geita Vijijini. Ukweli pia ni kwamba kulikuwa na tofauti ya namna ya kukokotoa hiyo service levy, maana wao GGM mwanzo walikuwa wanalipa kwa mujibu wa MDA yao, kwa maana ya kulipa dola 200,000 kwa mwaka lakini baadaye marekebisho yalivyofanywa ya kuweka addendum kwenye MDA mwaka 2004, ikaonekana sasa malipo yaanze kulipwa kwa mujibu wa sheria yaani 0.3% ya mapato yote ya mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tofauti hiyo imechukua muda mrefu na Serikali imekuwa ikishirikiana na Halmashauri ya Geita pamoja na Mheshimiwa Mbunge anafahamu sisi Wizara tumesukuma sana jambo hili. Hata hivyo, hapo katikati Waheshimiwa Madiwani wa Geita waliamua kupeleka jambo hili mahakamani na Mheshimiwa Mbunge anafahamu jambo hili lilishapelekwa mahakamani. Kuhusu nyaraka zile kupotezwa na nini, nadhani tuwaachie mahakama nao wao kama wanazo nadhani watazipeleka mahakamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ni lile linalohusiana na Mgodi wa Bacliff. Ni kweli kwamba Mgodi wa Bacliff umechukua muda mrefu sana na kumekuwa na matatizo mengi sana, kwanza ya kileseni lakini pili ya kiubia. Yote hayo tunayafanyia kazi na hivi navyozungumza hapa nawasiliana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuangalia namna gani ule ubia utaweza kusimamiwa, ama pengine kama kuna haja ya kuuvunja uweze kuvunjwa. Ile leseni anayoizungumzia, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini hatujatoa leseni hiyo ambayo inahitaji kuhuishwa kwa sasa, kwa sababu bado kuna mambo ambayo tunahitaji kuyakamilisha kabla ya kufanya hivyo. Ahsante.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kunipa nafasi niulize swali langu. Nilikuwa napenda kuiuliza Serikali kwamba sisi tusiokuwa na vitambi tunakula vyakula vyote hivyo ambavyo Mheshimiwa Dkt. Ulega amevizungumza na hatujawahi kuona mabadiliko yoyote katika maumbile yetu. Je, Serikali inatushauri tule nini zaidi kwa sababu vya wanga, vinywaji vyote tumetumia bado tuko kwenye maumbile haya haya.

Je, Serikali inatushauri tule nini ili na sisi tubadilike tufanane na wao? (Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, nataka kujua watu wa aina yake ambao miili yao haina shukurani kama ulivyoiita wafanyeje? Na yeye anataka kupata kitambi, namshauri Mheshimiwa Musukuma na yeye ikiwezekana apate kuwaona watalaam wa lishe nina hakika watampangia diet ambayo itampelekea na yeye kupata mwili anaouhitaji.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kwanza nisikitike sana kwa majibu yaliyotolewa na Mheshimiwa Naibu Waziri hayaendani kabisa na maeneo ya Jimbo langu la Geita.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bahati nzuri Waziri mhusika Mheshimiwa Kangi Lugola familia yake maana yake Mama yake na Dada zake wanaishi kwenye Jimbo langu, na Mheshimiwa Kangi Lugola mwenyewe ameishi kwenye Jimbo langu anayajua mazingira na majibu yaliyotolewa siyo sahihi. Kwa mfano, ukichukulia kituo cha Nyarugusu, Nyakagwe, Buziku, Bwanga na Chato Vijijini haya yote ni mazingira ambayo karibia tunafanana lakini wenzetu tayari wana Askari wa Kike. Sasa ninataka kujua ni lini Serikali itanipatia Askari wa Kike kwa kuwa majibu waliyotoa ni ya uwongo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Centre ya Nkome ni centre ya tatu kwenye Mkoa wetu wa Geita kwa ukubwa. Kituo kilichopo pale kinaongozwa na Inspekta na nimekijenga mimi kama Mbunge. Tatizo linaloonekana hapa kwamba hakuna makazi ya kuweza kumuweka Askari wa Kike, wajibu wa kujenga makazi bora ya askari ni ya Wizara.

Je, ni lini Serikali itachukua dharura ya kwenda kujenga hiyo nyumba anayotakiwa kukaa Askari wa Kike? (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba taratibu hasa zinazohusu upekuzi ni lazima Askari wa Kike ampekue mtuhumiwa wa kike. Majibu mazuri kwenye swali la msingi ameyasema Naibu Waziri wangu, kwamba hata pale ambapo kunakuwa na changamoto ya kutokuwepo Askari wa Kike upo utaratibu ama wa kumtumia mgambo wa kike ama kumtumia Mke wa Askari ambaye yuko jirani na mahali ambapo kuna mtuhumiwa. Najua suala la Mheshimiwa Musukuma nimeshamwagiza tayari Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Geita kupeleka Askari wa Kike kwenye Kituo cha Polisi cha Nkome. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wapo Waheshimiwa Wabunge wengi ambao wamekuwa wakiomba tuwapelekee Askari wa Kike kwenye vituo vya Polisi. Ninajua Waheshimiwa Wabunge Askari wa Kike wanapokuwa katika maeneo mbalimbali ni faraja kwa wananchi kwa sababu Askari wa Kike wao wanaruhusiwa hata kuwapekua watuhumiwa wa kiume. Kwa hiyo ninajua kwamba Mheshimiwa Musukuma anatarajia kuona Askari wa Kike katika maeneo mbalimbali ya vituo vya Polisi. Kwa hiyo nimpe faraja kwamba pale ambapo kuna changamoto kama hiyo na juzi tumepata Askari kutoka Chuo chetu cha Polisi Moshi, tutawapelekea Askari wa Kike.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi/ Kicheko)
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Matatizo yalioko katika Daraja la Rorya ni sawa kabisa na matatizo yaliyoko kwenye Jimbo la Geita Vijijini kwenye Daraja la Blengete, Kata ya Isilobutundwe na tumeshaandika maandiko mengi lakini hatujawahi kupata majibu. Je, Wizara au Waziri yuko tayari sasa baada ya Bunge hili kuongozana nami kwenda kuona ili aone umuhimu wa kutupatia pesa hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kasheku Musukuma, Mbunge wa Geita Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameelezea daraja katika eneo hilo ni muhimu sana katika shughuli za kiuchumi za wananchi, lakini pia kwa shughuli za kijamii. Niwapongeze sana akiwemo mwenyewe Mheshimiwa Musukuma kwa jitihada za kufuatilia daraja hilo liweze kujengwa ili wananchi waweze kupata huduma. Naomba nimhakikishie kwamba, kadri ya upatikanaji wa fedha Serikali itaendelea kulipa kipaumbele eneo hilo la daraja na litaanza ujenzi pale bajeti itakapotengwa na fedha itakapopatikana.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa sheria inawaruhusu wachezesha bonanza kulipa asilimia 0.03 ya mapato yao, nataka kumuuliza Waziri, je, ni nani anayejumlisha mapato yao kwa mwaka?

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, Wachina hawa wanaochezesha mabonanza wanarundika pesa zao nyumbani wala hawapeleki benki. Mfano mzuri ilitokea Morogoro, ulipofanyika msako Morogoro walikutwa na bilioni 2.5, ukafanyika msako Arusha wakakutwa na bilioni 5.0 ndani. Sasa sisi kama Halmashauri kupata ile asilimia tunayoitaka kwenye levy tunaipataje? Je, Serikali wako tayari kuruhusu kwamba, kule Halmashauri tuweke makufuli pamoja pale kwenye zile slot machine, ili wanapoenda kufungua watendaji wetu tujumuike nao ili tuweze kupata hesabu vizuri kwa ajili ya kukusanya hiyo service levy? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Musukuma, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza katika jibu langu la msingi wanaohusika na ukusanyaji wa mapato ya service levy ni Mamlaka ya Serikali za Mitaa wenyewe kwa mujibu wa sheria iliyowekwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, naomba kumshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Musukuma kwamba, anajali na anaijali Serikali kwa kuangalia uchumi wa nchi unavyokwenda. Hata hivyo, Mheshimiwa Musukuma ushauri wake tumeuchukua na tutaufanyia kazi kwa mujibu wa sheria kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali za Mitaa kama ilivyo sheria. (Makofi)
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza, na nimpongeze pia Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kutupandisha daraja kutuita kidato cha saba.

Mheshimiwa Spika, watumishi wa darasa la saba ambao waliondolewa kazini walifanya kazi zao kwa uaminifu, wengine walikuwa watendaji na watu wengine; lakini tamko hili lilitoka na waraka ukatoka mpaka leo asilimia 95 hawajawahi kulipwa wala kuitwa wala kupokelewa tu na waajiri. Sasa ningemwomba Mheshimiwa Waziri kama anaweza kutoa commitment angalau akatupa kopi ya zile nyaraka sisi Waheshimiwa Wabunge ili tuweze kwenda kutetea wale waliondolewa na hawajapata stahiki zao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Musukuma kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, watumishi ambao hawakujiendeleza mpaka kufika Desemba, 2020 walikuwa kama 1,491, ambao hawakujiendeleza, na hivyo walikosa sifa ya kurejeshwa katika utumishi wa Umma.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema awali wakati najibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Londo, kwamba Mheshimiwa Rais wetu, mama yetu Samia Suluhu Hassan alitoa agizo lake siku ya Mei Mosi pale Mwanza. Kwamba hawa 1491 stahiki zao zilipwe; na tayari ofisi yetu ya Utumishi ilishatoa waraka tarehe 21 Mei, 2021 kwa waajiri wote kuanza kuhakiki madeni haya na kuangalia stahiki walizotakiwa kulipwa hawa wa darasa la saba. Naamini baada ya muda mfupi hawa 1491 wataanza kulipwa, kwa sababu ilikuwa ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais na hivyo tutalitekeleza kama aliyoelekeza yeye Mheshiwa Rais. Ahsante sana.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa swali niulize swali dogo la nyongeza. Natambua Wizara imetupa mradi mkubwa wa maji kutoka Nkome kwenda Nzela Rwezela lakini nilitaka kuuliza swali dogo. Tunayo Kata ya Rubanga haina kabisa mfumo wa maji na kina mama wanatembea umbali wa kilometa 10 kupata maji katika Kijiji cha Mwamitilwa, Mtakuja, Ludenge, Je. Serikali haioni umuhimu wa kunipatia angalau visima viwili viwili katika vijiji hivyo vitano? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Kata ya Rubanda, Serikali inafahamu umuhimu wa kuleta visima na kama nilivyoongea na wewe Mheshimiwa Musukuma, wewe ni Mbunge ambaye umefatilia suala hili kwa karibu, tayari tumekutengea visima viwili vya kuanzia katika mwaka wetu wa fedha ujao. (Makofi)
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa zao la parachichi ni zao ambalo linasifika na linaingiza kipato kikubwa kwenye Taifa letu, ni sawa sawa kabisa na zao la nanasi lililoko jimboni kwangu. Zao hili linaonekana kama tunda tu la kuliwa holela holela, lakini ukienda kwenye masoko kama Dubai linauzwa mpaka dola 30 wakati kwetu Usukumani linauzwa shilingi 200/= mpaka shilingi 500/=.

Je, Wizara mmejipangaje kutusaidia wakulima wa mananasi, hasa kwenye Jimbo la Geita Vijijini ili nalo liwe na soko kama soko la parachichi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba, Mkoa wa Geita ni mmoja kati ya mikoa inayozalisha nanasi na vilevile katika mikoa mingine kama ya Pwani, Wilaya ya Chalinze na Wilaya ya Bagamoyo ni miongoni mwa wilaya zinazozalisha nanasi kwa kiwango kikubwa. Hatua tunayochukua sasa hivi kama Wizara, cha kwanza, ili kuweza ku-meet international standards na mazao yetu ya matunda yaweze kuuzwa katika masoko ya Kimataifa na vilevile yaweze kukidhi mahitaji ya viwanda vyetu vya ndani vya juice; hatua tunayochukua sasa hivi kama Wizara, tumewaagiza TARI ili kuweza kuzalisha mbegu ambazo zitakidhi viwango vya viwanda na kukidhi ubora unaostahili kuweza kumsaidia mkulima.

Mheshimiwa Spika, changamoto tuliyonayo katika subsector ya matunda ya nanasi na machungwa, kwa muda mrefu kumekuwa hakuna uwekezaji wa kutosha tuliofanya kama nchi katika eneo hili kwa sababu lilikuwa halionekani kama ni eneo la kimkakati. Kama Wizara, sasa hivi sekta ya matunda na mbogamboga imepewa kipaumbele kikubwa na tumeagiza TARI Selian kuwa ndiyo kituo halisi kwa ajili ya kufanya research and development.

Mheshimiwa Spika, katika bajeti yetu Mungu akijalia mwezi ujao mtaona kwamba, uwekezaji tunauweka katika research and development ili mazao ya mananasi na matunda yaweze kukidhi mahitaji ya soko la ndani na soko la Kimataifa na viwanda vyetu viweze kupata matunda wanayostahili.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi tuna soko la Shinyanga, Jambo amefungua kiwanda cha ku-process nanasi. Tunamhakikishia Mheshimiwa Musukuma, mimi mwenyewe nitachukua hatua ya kuwaunganisha wakulima wake moja kwa moja waweze kuuza kwa Jambo pale Shinyanga. (Makofi)
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, wananchi wa Isulwabutundwe, Dubanga, Isamilo, Mkolani, Busekeseke ni wananchi wavumilivu sana. Barabara hizi hazijalimwa kwa miaka 10 sasa; na tunaishukuru Serikali tumepata kiasi cha shilingi milioni 580 kwa ajili ya kulima kama alivyoeleza Mheshimiwa Naibu Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika barabara hizi, barabara ya Isamilo - Mkolani – Busekeseke ina urefu wa kilometa 18, tumepata morum kilometa 7; hii nyingine ya Mkoba Bridge – Isulwabutundwe – Mkolani – Dubanga tumepata kilometa tano. Sasa Mheshimiwa Waziri nilikuwa naomba kuuliza: Serikali haioni umuhimu wa kuweza kuongeza fedha kwa dharura ili kipande kilichobaki kuwekewa moorum kilimwe kwa pamoja, maana kukilima nusu kitaondoka, halafu tena mwakani tutaanza upya.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Wananchi wa Nyamikoma kupitia daraja la Kimilawinga, daraja hili inaponyesha mvua halipitiki kabisa na wananchi hawa ni lazima wapite Kimilawinga waende Lwenge, waende Kamwanga kwa ajili ya kupata mahitaji na mpaka Nzela:

Je, Serikali haioni umuhimu wa kutenga pesa sasa kwa ajili ya kwenda kujenga daraja hili kwa dharura? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Swali la kwanza dogo ambalo aliuliza Mheshimiwa Kasheku Musukuma ni kutaka Serikali iongeze fedha katika zile barabara tulizozitoa ili kuhakikisha yale maeneo ambayo Moorum haijawekwa, basi yawekwe na yalimwe kwa pamoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimjibu tu Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mwaka wa fedha huu unaokuja, kuna fedha vile vile imetengwa kwa maana ya mwaka 2021/ 2022 kwa ajili ya barabara hizo. Kwa hiyo, ninaamini kabisa kwamba zimepelekewa fedha na itafanya kazi kwa mwaka wa fedha unaokuja kwa sababu huu mwaka sasa tunaumalizia na ndiyo kazi ambazo zinazoendelea kwa wakati uliopo.

Mheshimwa Naibu Spika, jambo la pili, amezungumzia daraja linalopita Kinilawinga na amehitaji kwamba Serikali ilijenge kwa dharura. Nafikiri suala la madaraja siku zote, ninyi wote hapa mnatambua kabisa kwamba daraja linahitaji tathmini kwanza, baada ya tathmini ndiyo ujue gharama yake ni kiasi gani? Kwa hiyo, niagize tu TARURA wakafanye tathmini katika eneo hilo halafu walete Ofisi ya Rais, TAMISEMI. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza, Halmashauri ya Geita Vijijini yenye makao makuu yake Nzela tumepima viwanja vikakamilika mwezi wa 12 mwaka jana na mwezi wa kwanza tulileta barua ya maombi kwa ajili ya kupitisha ile kamati ya ugawaji wa viwanja toka mwezi wa kwanza mpaka leo hatujawahi kupata majibu kutoka Ofisi ya Katibu Mkuu ambaye ndio mwenye idhini ya kuidhinisha hiyo kamati.

Je nini kauli ya Serikali kuhusiana na barua hiyo ya kuidhinisha hiyo kamati ilituendelee kuuza viwanja ambavyo viko tayari?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba nilichukuwe swali la Mheshimiwa Musukuma kama alivyosema kama kweli wameshaleta ofisini nikitoka hapa mchana nakwenda kuangalia kama yapo na tuweze kujua kwa nini mpaka leo haijaidhinishwa. Kwa sababu taratibu tunasema kamati zile zikishaletwa kazi ya waziri ni kuweza kuridhia ili zikaanze kufanya kazi. Sasa haiwezekana iwe imekuja kwa muda wote huo halafu majibu hajapa naomba nilichukuwe ili mchana niweze kuangalia nitampa majibu yake.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Namshukuru pia Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali na wananchi wa Jimbo la Geita Vijijini wamekusikia. Hata hivyo, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa majibu haya sasa ni mara ya pili napewa katika katika Bunge lako Tukufu, namuomba Mheshimiwa Waziri yupo tayari sasa baada tu ya Bunge hili kuambatana nami kwenda kuona mazingira halisi ya wananchi wangu wanavyokaa ili aweze kutekeleza mradi huu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, mradi huu unaishia katika Kijiji cha Idoselo, Vijiji vya Mkorani, Ibisabageni, Dubanga, Isulobutundwe vijiji ambavyo wananchi wake wanachota maji umbali wa kilometa tisa, 10 mpaka 20. Je, Wizara haioni umuhimu wa kunipatia angalau visima wakati wao wakisubiri mradi huu wa maji uende mpaka kwao?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunilinda suala la kuambatana na Mheshimiwa Musukuma lakini mara baada ya kutoa kibali hicho nitakuwa mtiifu kwako nitakwenda kutimiza majukumu yangu.

Mheshimiwa Spika, swali la pili kuhusiana na visima, nimtoe hofu Mheshimiwa Musukumu tutakuja kuangalia hali halisi, wataalam wetu tutawaagiza wafike pale. Tumetenga visima vingi sana ili maeneo yote ambayo ulazaji wa mabomba unakuwa ni mgumu basi huduma ya visima vya maji iweze kupatikana. (Makofi)
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kwanza, niishukuru sana Serikali kwa kutusaidia pesa na kuweza kumalizia ujenzi wa madarasa ya Form Five na Six pale Nzela.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la kwanza, majibu ya Serikali kuhusiana na Shule ya Sekondari Lubanga hayajajitosheleza vizuri kwa kuwa tumekuwa tukisuasua, hata hayo madarasa mawili yamejengwa na Mbunge pamoja na nguvu za wananchi. Kwa sababu maombi nimeshaleta zaidi ya mara tano, ni lini Serikali mtatupatia pesa kwa ajili ya kujenga madarasa na mabweni kwa ajili ya Form Five na Six pale Lubanga? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ili Mheshimiwa Naibu Waziri aone nachokiomba kina umuhimu, naomba commitment yake baada ya Bunge twende wote akaone ule umbali wa kutoka Lubanga kwenda kwenye hiyo shule ya Form Five na Six ambayo itafunguliwa mwezi waliopanga, ni kilometa 105, ni lini Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Joseph Kasheku Musukuma, Mbunge wa Jimbo la Geita, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza ametaka tu commitment ya Serikali kwamba ni lini sasa Shule ya Lubanga itapelekewa fedha ili yale madarasa mengine yakamilike na shule hii tuweze kuifungua kwa wakati. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge tumelipokea suala hili, tutatafuta fedha na tutaziweka katika miradi ambayo inafuatia ili kuhakikisha katika mwaka wa fedha unaokuja shule hii iwe imekamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili alikuwa ananiomba tuweze kuongozana mara baada ya Bunge, nimpe taarifa kwamba nitakuwa na ziara katika Mkoa mzima wa Geita. Kwa hiyo, niseme tu kabisa kwamba nitakwenda pamoja naye mpaka katika eneo hili analolisema kujionea kwa pamoja. Ahsante sana.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali la mwisho.

Mheshimiwa Spika, miaka mitatu iliyopita ni kweli iliundwa timu ya mawaziri wanane na walizunguka kwenye wilaya baadhi ya wilaya na wilaya nyingi. Lakini, ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri ziara ile ya mawaziri imekuwa kama ni ya kificho ficho, yaani tunawasikia tu, walipita, walipita, yaani sehemu hata ambazo hazina umuhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa na sisi ndiyo tunaolalamikiwa kila siku tunakuja kuuliza haya maswali. Kwa nini Serikali au Waziri asiweke mpango mzuri, timu inapoenda kwa mfano Wilaya ya Geita tujulishwe Wabunge na sisi tushiriki kwenye kuonyesha ile mipaka ili kuondoa ile sintofahamu. Ni hayo tu. (Makofi)
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Musukuma kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, timu yetu ilikuwa na hadidu za rejea, haikuwa kutembea tu, na kuchunguza kila kitu, tulikuwa tumepewa hadidu za rejea na mambo fulani za kushughulikia, ilikuwa ni migogoro maalumu yenye mwiingiliano kati ya hifadhi na wananchi na vijiji, kulikuwa na migogoro hiyo maalumu.

Mheshimiwa Spika, lakini katika kufanya kazi hii nimesema hatukupita kila mahali kwa sababu tulikuwa tayari tuna taarifa, moja ya taarifa kubwa tuliyokuwa nayo ilikuwa migogoro ya wafugaji na wakulima ambayo ilikuwa ni Tume ya Bunge iliundwa hapa na Bunge lako Tukufu nayo tulitumia na tume nyingi nyingi na taarifa mbalimbali. Lakini tukawa tunataka kujiridhisha juu ya yale yaliyoandikwa kwa hiyo tulienda sehemu chache sana.

Mheshimiwa Spika, tunajua nchi hii kuna migogoro ya mipaka kati ya vijiji na vijiji ambayo si ngumu sana kusuluhisha. Tumeagiza sana viongozi wa mikoa na wilaya kwa sababu mwenye mamlaka ya kuunda maeneo ya utawala ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hakuna kijiji kilichoanzishwa wala wilaya wala mkoa ambayo mipaka yake haikuandikwa kwenye GN ni suala la kwenda kusoma GN kwenye uwanda na kuamua mpaka upo wapi kwa sababu hawatakiwi kuunda mipaka ya utawala, mipaka ya utawala imeshaandikwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ipo migogoro mingi inayoendelea vijiji na vijiji kata kwa kata, sijui tarafa kwa tarafa ni uzembe tu. Tukishirikiana migogoro hii itaisha kwa sababu ina maandishi yake. Kwa hiyo, Mheshimiwa Musukuma nataka kukuomba kama kuna mgogoro wa mpaka wa wilaya usisubiri ile tume, tuambie hizo ndiyo kazi zetu za kila siku.

Mheshimiwa Spika. kwa hiyo, tutenganishe kati ya ile kazi ya Tume na shughuli zetu za migogoro kila siku, shughuli kama kuna migogoro mingine mliyonayo Waheshimiwa Wabunge tupeni hizo ndiyo kazi zetu, wizara yangu inatatua migogoro kila siku, kama kuna mtu unamgogoro usisubiri Kamati ya Mawaziri msife na hiyo migogoro tupeni tuifanyie kazi hata sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tutatuma wataalamu, tunavyo vifaa vya kutosha na wizara yangu hivi sasa imeanzisha Ofisi za Ardhi kila mkoa, kuna ma-surveyor kuna kila mtu, tutakuja kuainisha mipaka. Na katika kuahinisha mipaka Mheshimiwa Musukuma ndiyo tunavyofanya tunachukua viongozi wa pande mbili zote wanaobishania mipaka tunaamua kwa pamoja hatuendi sisi peke yetu, na ndiyo maana hata hii ya uhakiki wa Maliasili ipo mipaka iliyowekwa kwenye Hifadhi na Maliasili.

Mheshimiwa Spika, lakini tunataka tuunde timu maalumu ambayo wananchi na majirani pale na viongozi watahusika katika kuhakiki mipaka ya hifadhi ili waridhike kwamba mipaka hiyo inafanana kabisa na ile mipaka iliyoandikwa kwenye GN za Serikali.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kazi hiyo tupeni tuifanye msisubiri kamati ya watu wa nane ni kazi yetu ya kila siku.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Napenda kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Barabara inayotoka Geita kwenda Nkome ina kilometa 57 na ilishafanyiwa upembuzi yakinifu muda mrefu na ikawekwa mpaka beacon na alama za kuanza mkandarasi. Leo tunazungumza ni karibia mwaka wa pili, tunaahidiwa kila siku: Ni lini Mheshimiwa Waziri atakuja kuuona Mji wa Nzera ambao ndiyo Makao Makuu ya Halmashauri ya Mji wa Geita; haijawahi kuona lami; kila mwaka tunaahidiwa na leo ni mwaka wa nne?

Mheshimiwa Spika, swali la pili: Barabara ya Kamanga – Sengerema – Buchosa – Nkome ni barabara ambayo imeng’oa Wabunge zaidi ya sita, upande wa Sengerema na upande wa Buchosa; lakini tumekuwa tukipata ahadi zilezile za Serikali kwamba mwakani tunajenga, mwakani tunajenga; sasa nataka kumwuliza Mheshimiwa Waziri, tufundishe njia ambayo unaona ni nzuri na sisi tupite kama ni dirishani angalu tupate hiyo lami. Bado tunapenda kuendelea kuwa Wabunge.

Naomba commitment ya Serikali, ni lini mtaanza kutengeneza Barabara ya Kamanga – Sengerema – Buchosa – Nkome?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG.
GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Musukuma Joseph Kasheku, Mbunge wa Geita Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, beacon zilizowekwa haikuwa usanifu wa kina; na fedha iliyotengwa kwenye bajeti ya mwaka huu tunaoutekeleza inakwenda kufanya kazi. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, yako maandalizi ambayo yanaendelea kwa ajili ya kuanza huo mchakato wa kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina yakiwa ni maandalizi ya kuijenga hiyo barabara kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, barabara hii ya pili aliyoisema ya Kamanga – Sengerema – Buchosa hadi Nkome, naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba itatekelezwa kama ilivyoahidiwa kwenye Mpango wetu na kama ilivyoelezwa kwenye Ilani yetu ya Uchaguzi ya mwaka 2020 - 2025. Pia nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunaendelea kutafuta fedha na ikipatikana hizi barabara zote zitajengwa kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, matatizo yaliyopo katika Jimbo la Manonga ni sawa kabisa na matatizo yaliyopo kwenye Jimbo la Geita. Kata ya Nkome ina zahanati ambayo kwa mwezi inazalisha watoto wasiopungua 400 na Mheshimiwa Naibu Waziri amefika pale Silinde. Mheshimiwa Waziri juzi tu tumefika ukajionea hali halisi chumba kidogo ukakuta kinamama zaidi ya wanne wanajifungua pale. Sasa nimeshauliza humu mara mbili mara tatu ninapata tu ahadi ambazo hazijatekelezeka?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba kupata majibu ya uhakika kwamba ni lini sasa kwa kuwa Mawaziri wote wamefika pale mtanipa fedha ya dharula ili niweze kuwaokoa wale wananchi wa Kata ya Nkome? Ahsante sana.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijajibu swali la Mheshimiwa Musukuma, kwanza naomba unipe nafasi nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa imani yake kwangu, kwa kunipa majukumu ya kumsaidia katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Rais wetu kwamba, kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu nitatumia maarifa na jitihada zote na kwa ushirikiano wa Waheshimiwa Wabunge naamini mtanipa ushirikiano ili nisiweze kumwangusha Mheshimiwa Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nijibu swali la Mheshimiwa Musukuma kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli siku si nyingi niliambatana na Mheshimiwa Musukuma kwenda kwenye Jimbo lake la Geita Vijijini. Kwanza nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Musukuma kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuwatetea wananchi wake wa Geita Vijijini. Kama nilivyomuahidi Mheshimiwa Musukuma tukiwa Geita Vijijini, muda wowote Serikali tukipata fedha tutaangalia namna ya kuboresha Zahanati ya Nkome ili iweze kuwa Kituo cha Afya ili wananchi wa Kata Nkome pamoja na maeneo ya jirani waweze kupata huduma nzuri kwa mujibu wa Sera ya Kituo cha Afya. Nashukuru.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Matatizo yaliyoko kwenye Pori la Mbogwe ni sawa kabisa na matatizo yaliyoko kwenye Jimbo la Geita Vijijini, Hifadhi ya Rwande, ambayo kimsingi ilishapoteza sifa ya hifadhi.

Sasa ombi langu Mheshimiwa Waziri, atakuwa tayari baada ya vikao hivi kutembelea Jimbo la Geita Vijijini ili aweze kuja kuona lile pori badaye tuwe na utaratibu wa kuwarudishia wananchi waweze kuendelea kulima?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Joseph Kasheku Musukuma, Mbunge wa Geita Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, niko tayari kuambatana na Mheshimiwa Musukuma kwenda jimboni kwake na kutembelea pori hilo ili pamoja na Wizara ya Ardhi na wadau wengine tukubaliane namna ya kuli-manage ili wananchi waweze kupata fursa nzuri. Nashukuru sana.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kuna halmashauri ambazo zina hospitali mbili za wilaya ikiwemo na halmashauri ninayotoka mimi ya Geita. Sasa Serikali itapeleka magari mawili kwa sababu ukipeleka gari moja linakuwa na mgongano wa hoja kwa sababu kuna hospitali mbili na Wabunge wawili tofauti.

Je, Serikali ipo tayari kupeleka magari mawili katika Halmashauri ya Geita?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Joseph Kasheku Musukuma Mbunge wa Jimbo la Geita Vijijini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, magari yanapelekwa kwenye halmashauri na halmashauri ziko 184 magari yako 195. Kwa hiyo, kila halmashauri ikiwepo halmashauri ya Mji wa Geita lakini pia Halmashauri ya Wilaya ya Geita watapata gari moja moja, ahsante.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Natambua kwamba kila hospitali ya Wilaya inayo shida ya kupata Madaktari Bingwa na upatikanaji wake kidogo unakuwa ni mgumu. Pia kuna Halmashauri zinakuwa na uwezo wa kusomesha Madaktari Bingwa, mojawapo ikiwa ni hospitali yangu. Sheria ya Utumishi inasema tukimsomesha at least afanye Miezi 36 ndiyo aweze kuhama. Sasa kwa sisi ambao tumepeleka Madaktari wakapata huo Ubingwa, halafu wakarudi ndani ya wiki moja wakahamishwa.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri anasemaje kuhusu hilo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kwenye hili suala la Madaktari Bingwa siyo tu kwa hospitali za Wilaya hata za Mikoa kuna baadhi ya Mikoa ukimpeleka Daktari Bingwa ana-resign anakwenda sehemu nyingine. Tulichokubaliana ni kwamba kama ni Wilaya au Mkoa ametokea pale Daktari kwenda kusomea Ubingwa, anapewa mkataba maalum wa kufanya kazi na Halmashauri au Mkoa huo kwa muda wa Miaka mitano bila kuhama. Kwa hiyo, hilo likianza kutekelezwa na tumeanza kutekeleza huo mkakati ili kuzuia wasihame tena, hivyo, nafikiri hiyo itasaidia sana. Mheshimiwa Musukuma hebu uje kwangu tuone kilichotokea kwenye eneo lako ili tuone kwa yule mliyemsomesha kama tunaweza kufanya lolote. (Makofi)
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, wananchi wa Jimbo la Geita Vijijini wanalazima kufuata huduma za Mahakama ya Wilaya kilometa 60. Je, ni lini Wizara itakuwa tayari sasa kwenda kujenga Mahakama ya Wilaya kwenye Jimbo hilo?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Musukuma, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, sasa hivi tuko kwenye mkakati wa kuendelea na utekelezaji wa ujenzi wa Mahakama za Wilaya katika Wilaya 18. Ninapenda tu kumwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba ujezi wa jengo ambalo linahitajika katika Wilaya yake linaenda kuanza katika kipindi cha fedha kijacho kwa ajili ya kutekeleza mpango huu wa maboresho ya Mahakama nchini. Ahsante.
MHE. DKT. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, umenipandisha cheo nafaa kuwa profesa, nakushukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa Miji 28 ni mradi ambao ulikuwa unaifaidisha sana Geita Mjini na Geita Vijijini, lakini kila tukiuliza hapa tunaambiwa tunakamilisha makaratasi.

Je, Mheshimiwa Waziri, ni lini mradi wa Miji 28 ambao unalifaidisha Jimbo la Geita kwa Kata utaanza? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Daktari Musukuma kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi ya Miji 28 tayari tumefikia hatua nzuri sasa ya manunuzi na mradi huu unaelekea kwenye utekelezaji kabla ya mwezi Juni, 2022.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Ningependa kumuuliza swali la nyongeza Mheshimiwa Naibu Waziri. Naipongeza Serikali kwa kumaliza Mgogoro wa Ngorongoro vizuri kabisa kwa kuwahamisha wale wananchi waliokuwa Kata ya Ngorongoro kwenda Kilindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Nyatwali iliyopo Bunda ni sawa sawa na kata iliyoko Ngorongoro. Ile kata ina hamishwa yote ikiwa na miundombinu ya shule, hospitali na vitu vyote, na ni kata ya enzi na enzi. Hata hivyo, kuna double standard ya Serikali. Inaonekana kule watalipwa milioni mbili ilhali kule watu walihamishwa kistaarabu mpaka na ng’ombe wakabebwa kwenye gari.

Je, Serikali ina mpango gani wa kumaliza Mgogoro wa Nyatwali?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Musukuma, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Nyatwali na vijiji jirani vinavyozunguka kata hiyo, Serikali ilitoa mapendekezo ya kulichukua eneo hilo kutokana na changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikijitokeza katika eneo hilo. Wananchi hawa wako kihalali na hii sentensi Serikali kila siku tumekua tukiiongelea; wako kihalali sio wavamizi na vijiji vilivyoko pale vimesajiliwa kihalali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu uliopo, Serikali inapoona kuna umuhimu wa eneo lile kulichukua kwa maslahi ya Taifa, hapa nikisema maslahi ya Taifa, tuna resources nyingi ambazo tunazitumia kwa maslahi ya Taifa. Kwa hiyo, hata hili eneo tunaliangalia kwa upana zaidi na si kwa wananchi wachache.
Kwa hiyo, tunachofanya, tumefanya uthamini na wananchi waliomba mapendekezo kwamba badala ya heka kulipwa milioni mbili basi wanaomba milioni tatu. Ahadi tuliyoitoa ni kwamba tathmini ifanyike watathmini waingie uwandani waone halafu Serikali itaona nini kifanyike na tutarejesha kwa wananchi mrejesho ambao utakuwa ni muafaka kati ya wananchi na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa tahadhari tu, hawa wanaohamishwa ni kwa mujibu wa sheria za nchi. Ngorongoro imekuwa treated tofauti na maeneo mengine. Mara nyingi Waheshimiwa Wabunge wanadai pale ambapo wananchi wanahamishwa wanataka walinganishe na Ngorongoro. Suala la Ngorongoro lipo tofauti kabisa na maeneo mengine, ahsante.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Geita ina majimbo mawili na hospitali mbili za wilaya. Sasa kwa maelezo ya Waziri, ina maana likija gari moja itakuwa ni ugomvi ikakae hospitali gani; aidha, likae Jimbo la Geita Vijijini au Busanda, ambapo kila jimbo lina hospitali: Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari sasa special kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Geita kuleta magari mawili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Joseph Kasheku Musukuma, Mbunge wa Jimbo la Geita Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, magari ya wagonjwa yatakayonunuliwa ni magari 195, nasi tuna Halmashauri 184. Kwa hiyo, utaona tuna magari 11 ya ziada na tutaangalia mazingira ambayo tuna ulazima wa kuongeza gari kwenye Halmashauri, tutaongeza. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutafanya tathmini kuona magari yaliyopo Geita Vijijini na Mjini na uhitaji na hivyo tunaweza kufanya maamuzi. Kwa hiyo, tutafanya hivyo kwa kadri ya mazingira. Ahsante.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, ningependa kumuuliza Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa miji 28 ulikuwa ni mradi mkombozi sana kwenye majimbo ambayo hatujawahi kuona maji ya bomba, kila nikiuliza mnaahidi mwezi mmoja unaniambia nini ili wananchi wangu wapate faraja ya maji ya miji 28?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge, lakini nataka nimtie moyo ukiona giza linatanda ujue kumekucha. Taratibu zote zinazohusiana na manunuzi ya mradi wa miji 28 zimekwishakamilika na kabla ya Bunge la Bajeti ya Wizara yetu ya Maji tutakaa na Waheshimiwa Wabunge tukubaliane lini tunakwenda kusaini mradi ule taratibu zote tumeshakamilisha tunaenda kwenye signing ya mradi, ahsante sana.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Jimbo la Geita Vijijini wananchi wake hawajawahi kuona lami na tulipata lami kilometa 20 kutoka Nkome mpaka Kijiji cha Igate na upembuzi yakinifu tayari Mkandarasi tayari.

Je, ni lini mkandarasi huyo anaingia site kuanza kazi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Musukuma, Mbunge wa Geita kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, tupo kwenye hatua za mwisho kabisa ili mkandarasi aweze kukabidhiwa hiyo site na nadhani Mheshimiwa Musukuma pia anajua kwamba taratibu zote karibu zimeshakamilika kwa hiyo kilichobaki tu ni hatua za mwisho ili mkandarasi aweze kukabidhiwa hiyo site.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Swali hili nimeliuliza mwaka 2020, 2021 na nikajibiwa majibu haya haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ametaja kwamba halmashauri ya Geita ina shule za sekondari tatu sisi halmashuri ya Geita tuna majimbo mawili, jimbo la Busanda na Jimbo la Geita. Shule mbili ziko jimbo la Busanda. Jimbo la Geita lina population ya zaidi ya watu laki saba na nusu, kwangu, tuna shule moja. Watoto wanalazimika kutembea kilometa 80. Sasa, bado nahitaji majibu sahihi ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Kata ya Nkome ina wanafunzi 9500 ina shule nne; na miundo mbinu yote ya madarasa tumejitosheleza, tunapungukiwa tu ujenzi wa bweni kwa ajili ya kufungua kidato cha tano na cha sita.

Je Serikali iko tayari kupeleka pesa kwenye kata ya Nkome ili tuweze kufungua pia kidato cha tano na sita?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Joseph Kasheku Musukuma kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba majibu tuliyotoa kwa sasa ni sahihi kwa kuwa ni kweli Halmashauri ya Geita ina majimbo mawili, kwa maana ya Geita na Busanda ambao wana hizi shule za kidato cha tano na sita tatu. Ninajua mahitaji makubwa ambayo yako pale, ndiyo maana kwa sasa tumesema tunaendelea kuziimarisha ili kuongeza idadi ya wanafunzi wakati tunatafuta fedha kuhakikisha tunaongeza shule nyingine. Kwa hiyo nimwondoe shaka Mheshimiwa Mbunge, kwamba Serikali inapopata fedha itafanya hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusu hii Shule ya Sekondari Nkome ambayo ina idadi kubwa ya wanafunzi na wanahitaji Bweni tu. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI niseme ombi hili tumelipokea na litafanyiwa kazi. Ahsante.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, barabara ya Sengerema - Buchosa inaunganisha na Mkoa wa Geita kipande kidogo tu cha kilometa 14 kutoka Nyehunge kwenda Nzela, Serikali imeishia Nyehunge.

Je, Serikali ina mapango gani kuunganisha kutoka Nyehunge kwenda Nzela ambako Mheshimiwa Waziri unapita?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tunatambua kwamba tuna kila sababu ya kuunganisha Mkoa na Mkoa. Bahati nzuri hiyo barabara mimi nimeipita, kama nilivyosema kwamba mpango wa Serikali ni kuziunganisha Mkoa na Mkoa kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, kadri fedha itakavyopatikana barabara hii ya kutoka Nyehunge hadi Nzela kipande kilichobaki pia kitajengwa kwa kiwango cha lami ikiwa ni pamoja na Nzela hadi Kome ambayo iko kwenye hatua za manunuzi. Ahsante. (Makofi)
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, ningependa kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri mradi wa miji 24 ni mradi ambao ulikuwa ni mkombozi sana kwenye Mji wa Geita ambapo Jimbo la Geita Vijijini kata tano zilikuwa zinafaidika Senga, Kagu, Nyawilimilwa, Bugurura na Kakubiro. Lakini tumekuwa tukiahidiwa kila siku hatuoni mwelekeo; je, ni lini Serikali itaanza sasa kutekeleza mradi huo wa miji 24?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Musukuma kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa NaibU Spika, kwanza niseme siyo vijiji mini 24 bali ni miji 28, lakini vile vile Geita Mjini kata hizo tatu zinakwenda kunufaika hivi punde subira yavuta heri. Maandalizi yote yamekamilika tunasubiri tu kusaini, tunasubiri na muda na nafasi ya Mheshimiwa Rais.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, namshukuru Waziri kwa majibu mazuri, lakini mwaka 2020 wakati wa kampeni Mheshimiwa Rais aliposimama pale katika Makao Makuu ya Halmashauri ya Geita aliahidi kilometa tatu na mwaka 2021/2022 TAMISEMI, ilitenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kilometa moja, lakini mpaka leo tunaenda mwaka wa Serikali kumalizika hatujawahi kuiona hiyo kilomita moja.

Je, kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri ni kwamba sasa mtatekeleza kilomita mbili na sio kilometa moja?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKAO NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Joseph Kasheku Musukuma, kama ifuatavyo;

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kama fedha hizi zipo katika bajeti ambazo zimetengwa, nitalifuatilia na nimelipokea ili kuhakikisha kwamba linatekelezeka kama ambavyo limeainishwa katika bajeti, ahsante.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa kituo cha afya Nkome?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ni kweli Zahanati ya Nkome inazalisha wakina mama wengi sana kwa mwezi na inahudumia wananchi wengi kwa ujumla wake. Pia, nimhakikishie kwamba tayari imekwishaingizwa kwenye orodha ya vituo vya afya ambavyo vinatafutiwa fedha kwa ajili ya kujengwa ili iweze kutoa huduma kwa ngazi ya kituo cha afya. Ahsante.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Ningependa kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri; barabara ya Nkome – Nzela – Geita yenye urefu wa kilometa 20 mwaka wa tatu Mkandarasi amepatikana tunasubiri kusaini.

Je, huna mafuta nikuwekee ili tuende tukasaini kesho? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali ya Mama Samia Suluhu Hassan haiwezi kukosa mafuta ya kwenda kusaini, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tunatambua umuhimu wa hiyo barabara ni suala la muda tu na ipo kwenye mipango, muda ukifika nina hakika barabara hii tutaisaini kwa sababu tayari imeishatengewa fedha na kila kitu kimekamilika. Kwa hiyo, tunachosubiri tu ni suala la taratibu zikamilike ili Mkandarasi aweze kuanza kazi hiyo ya kujenga kwa kiwango cha lami. Ahsante. (Makofi)
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, namuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri, Zahanati ya Kijiji cha Nkome nimekizungumza humu mara tatu; inazalisha shule kila mwezi, maana yake watoto zaidi ya 550; na kwa sasa tumeenda zaidi tunafika karibia 600 kwa mwezi; mliniahidi kuongeza uwezo wa ile zahanati ili iwe Kituo cha Afya, tathmini zote zimefanyika na mwezi huu wametoka kukagua tena, na fedha ipo shilingi milioni 500; lini hiyo fedha itakuja? Lini Mheshimiwa Naibu Waziri atakuja ili akaangalie huo uzalishaji wa hiyo zahanati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Musukuma, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kwamba Zahanati hii ya Nkome aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge, kwa kweli imezidiwa kwa idadi kubwa ya wananchi katika eneo lile na Serikali ishaweka mpango wa kupandisha hadhi kuwa Kituo cha Afya. Mwenyewe amesema wiki moja, mbili zilizopita wataalamu kutoka Ofisi ya Rais, TAMISEMI, walifika kufanya tathmini kwa ajili ya kutumia fedha za Benki ya Dunia kujenga Kituo cha Afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo hili liko on track na tutahakikisha tunajenga Kituo cha Afya hiki mapema iwezekanavyo. Ahsante. (Makofi)
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, namuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri, Zahanati ya Kijiji cha Nkome nimekizungumza humu mara tatu; inazalisha shule kila mwezi, maana yake watoto zaidi ya 550; na kwa sasa tumeenda zaidi tunafika karibia 600 kwa mwezi; mliniahidi kuongeza uwezo wa ile zahanati ili iwe Kituo cha Afya, tathmini zote zimefanyika na mwezi huu wametoka kukagua tena, na fedha ipo shilingi milioni 500; lini hiyo fedha itakuja? Lini Mheshimiwa Naibu Waziri atakuja ili akaangalie huo uzalishaji wa hiyo zahanati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Musukuma, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kwamba Zahanati hii ya Nkome aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge, kwa kweli imezidiwa kwa idadi kubwa ya wananchi katika eneo lile na Serikali ishaweka mpango wa kupandisha hadhi kuwa Kituo cha Afya. Mwenyewe amesema wiki moja, mbili zilizopita wataalamu kutoka Ofisi ya Rais, TAMISEMI, walifika kufanya tathmini kwa ajili ya kutumia fedha za Benki ya Dunia kujenga Kituo cha Afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo hili liko on track na tutahakikisha tunajenga Kituo cha Afya hiki mapema iwezekanavyo. Ahsante. (Makofi)
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, ninataka kumwambia Mheshimiwa Naibu Waziri, kwanza Halmashauri ya Wilaya ya Geita, hatuna tatizo na barabara yoyote kusema kwamba kuna sehemu ambako hakupitiki katika kutekeleza miradi iliyopagwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka kuuliza maswali yangu mawili ya nyongeza. Halmashauri ya Geita inapokea bilioni 4.3 kila mwaka. Mwaka 2022/2023 tulitenga hizo pesa na hazikutumika. Tunavyozungumza bajeti yetu imeisha mwezi wa Disemba 2023, hatujatumia hata asilimia moja. Miradi hii inasimamiwa na Wizara tatu; Wizara ya Fedha, Wizara ya Madini na Wizara ya TAMISEMI. Hakuna hata Waziri mmoja aliyewahi kuja kuikagua miradi hii; je, Mheshimiwa Waziri upo tayari kufuata na mimi kwenda kunithibitishia hiyo miradi uliyotajiwa imekamilika? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, miradi ya Serikali inatekelezwa, kwa mfano, kwa milioni 500 shule inakamilika au kituo cha afya kinakamilika na majengo saba. Miradi inayotekelezwa na CSR ni jengo moja ambalo halikamiliki kwa miaka mitatu hadi leo. Mheshimiwa Waziri upo tayari kufuatana na mimi kwenda kuthibitisha hayo majibu uliyoyatoa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, nimekubali kwamba tutakwenda na Mheshimiwa Musukuma. Tukafanye ziara na ninamhakikishia Serikali inaendelea kupitia kanuni ili kuhakikisha miradi hii inakamilika kwa wakati na kwa thamani ya fedha.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nimeuliza zaidi ya mara tano, je, ni lini Mheshimiwa Waziri atatoa pesa kiasi cha shilingi milioni 500 ili kuweza kukamilisha Zahanati ya Nkome, ambayo Waziri anaifahamu, zahanati ambayo kwa mwezi inazalisha wastani wa watoto 420? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Musukuma na pia nawapongeza wananchi wa kata hiyo kwa kweli, kasi ya kuleta watoto ni kubwa sana, watoto 400 kwa mwezi ni kasi kubwa sana. Sisi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa tumefika pale, mimi mwenyewe nilifanya ziara na tumeweka mpango wa kutafuta fedha ili vituo kama vile vipandishwe hadhi kuwa vituo vya afya. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali ipo kazini inatafuta fedha, mara ikipatikana tutakwenda kujenga kituo cha afya katika eneo lile. Ahsante sana.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu. Mimi sikuuliza swali la kisera, nimeuliza swali la jimbo langu. Ukitaja shilingi bilioni 44, kwanza unanichongea kwa wapiga kura wangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni kwamba, kweli tumepokea fedha, shilingi milioni 150 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya Mkurugenzi, lakini baadhi ya halmashauri tulizohamanazo, zile halmashauri 31 tulipewa shilingi milioni 150, wengine wameshaongeza shilingi milioni 300 mpaka shilingi milioni 350, unakuta nyumba za Wakurugenzi zina mpaka swimming pool, zina mageti, zina fence na kila kitu; lakini halmashauri yangu ina shilingi milioni 150. Ni lini utaongeza pesa ili tuwe na uwiano na wale uliowapelekea shilingi milioni 330? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kama kwa miaka mitano tutajenga nyumba tatu kwa hizi halmashauri ambazo tulizirudisha vijijini, Wakuu wa Idara wapo 18, it means kuna miaka 30 huko mbele ili watu wetu wawe ndani. Ni lini Serikali itakubaliana na mawazo tunayoyatoa humu Bungeni kwamba yapo mashirika ya Serikali kama National House, Watumishi House ziingie mkataba na hizi halmashauri, kwani tuna uwezo wa kulipa hata kidogo kidogo ili waweze kujenga kwa mara moja tuepukane na hili suala la kupewa nyumba tatu kwa miaka mitano? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze tu kwa kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tumetoa taarifa kwa upana kwa maana ya sura ya kitaifa ili wananchi wajue kazi kubwa inayofanywa na Serikali yao katika ujenzi wa miundombinu ya nyumba za watumishi, lakini pia katika majengo ya utawala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunatambua kuna baadhi ya halmashauri waliongezewa fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za Wakurugenzi au Wakuu wa Idara pale ambapo fedha haikutosha. Moja ya jukumu la Mkurugenzi ni kuwasilisha taarifa rasmi Ofisi ya Rais, TAMISEMI akielezea hatua iliyofikiwa baada ya kuanza utekelezaji na fedha kumalizika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nitumie nafasi hii kumwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Geita awasilishe andiko linaloelezea hatua waliyofikia kwenye ujenzi na kiasi gani cha fedha kinahitajika ili Serikali iweze kuchukua hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Serikali ilishatoa maelekezo kwa Wakurugenzi wote wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kutumia fursa za Watumishi Housing na National Housing kuingia mikataba na kukubaliana kujenga nyumba za Wakuu wa Idara na watumishi wengine ili waanze kulipa kwa awamu. Kwa hiyo, ni suala tu la wao kutekeleza, lakini Serikali ilishatoa maelekezo na kuna baadhi ya halmashauri ambazo tayari zilianza kutekeleza utaratibu huu, ahsante
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Ningependa kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri, Zahanati ya Kijiji cha Nkome ni zahanati inayohudumia akinamama wanaojifungua 420 kwa mwezi; Naibu Waziri Mheshimiwa Silinde alifika akajionea zahanati hiyo yenye kachumba kadogo ambako alikuta akinamama zaidi ya 15 wanajifungua na yeye mwenyewe akaahidi kuleta fedha kwa ajili ya kuipanua ile zahanati kuwa kituo cha afya. Je, leo ni mwaka umekwisha ni lini sasa Serikali inaleta fedha kwa ajili ya kwenda kujenga Kituo cha Afya Nkome?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Joseph Kasheku Musukuma, Mbunge wa Jimbo la Geita Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Zahanati ya Nkome ni moja ya zahanati ambayo inahudumia wananchi wengi sana, lakini ina ufinyu wa majengo na likiwemo jengo la kujifungulia. Tulitoa maelekezo kwa Halmashauri kutuletea Andiko tujue kwanza ukubwa wa eneo lile la Zahanati ya Nkome, lakini pili tuweke mpango wa kuhakikisha tunapanua ile zahanati kuwa kituo cha afya. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mpango wa Serikali uko vilevile na sasa tutapokea maandiko kutoka halmashauri na baada ya hapo tutatafuta fedha kwa ajili kupanua Zahanati ya Nkome kuwa Kituo cha Afya. Ahsante.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Geita lina vituo vya afya vinne vilivyokamilika kikiwemo Kituo cha Ibisabageni, Bugarama, Kasota, Kakubiro na vituo vyote hivi havijapata vifaatiba. Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kulitembelea jimbo langu ili aweze kujionea baadaye atuletee fedha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge, hakika anafanya kazi kubwa sana ya uwakilishi katika jimbo lake. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa siyo tu kwamba niko tayari kuambatana naye kwenda kuangalia mazingira katika vituo vya afya alivyovitaja, lakini naomba nimhakikishie kwamba katika mwaka huu wa fedha zimetengwa fedha mahususi kabisa kwa ajili ya kuhakikisha vituo vya afya na zahanati zote zinaweza kupatiwa fedha kwa ajili ya kununua vifaa na vifaatiba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba fedha zitakuja kwa ajili ya kuhakikisha huduma za afya msingi zinaboreshwa katika jimbo lake, kwa kuhakikisha vifaa na vifaatiba vinapatikana katika vituo vya afya alivyovitaja.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Wananchi wa Mkoa wa Geita wanategemea Bandari ya Mwanza na Bukoba. Sasa Mkoa wa Geita unakua na unajitegemea; tunalo eneo zuri kabisa la bandari ambayo haijaboreshwa ya Nkome ambayo ingetumika kushusha mizigo kutoka Kenya na Uganda. Je, Serikali ina mpango gani wa kuiboresha Bandari ya Nkome ili wananchi wa Mkoa wa Geita tuweze kuitumia kushusha mizigo yetu kutoka nje? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, tayari Serikali inafanya maboresho makubwa kwenye Ziwa Victoria kwa namna mbili; moja, tunajenga Bandari ya North Mwanza, Bandari ya Kemondo na Bandari ya Bukoba pamoja na kununua meli mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, baada ya kukamilisha hatua hiyo, tutakwenda kwenye hatua ya pili ya kutazama maeneo mengine kulingana na uhitaji wake ambayo ni pamoja na eneo la Nkome ambalo Mheshimiwa Mbunge ameulizia.