Answers to Primary Questions by Hon. Mohamed Omary Mchengerwa (10 total)
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE Aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha inaendelea kuhuisha miundo ya utumishi kwa kada mbalimbali kwa kuwa utaratibu wa kuajiri na kupandisha vyeo ndani ya Utumishi umekuwa ukibadilika kulingana na majukumu ya kiutendaji na maendeleo ya kiuchumi?
WAZIRI WA NCHI OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa hii ni mara yangu ya kwanza kusimama hapa kama Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, nimesimama hapa mara nyingi kama Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria kwa kipindi cha tatu sasa cha uenyekiti wangu. Nanze kuchukua fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa imani kubwa aliyonayo kwangu. Nimuahidi tu kwamba nitakwenda kuchapa kazi kwelikweli, kwenda kupunguza au kumaliza kabisa kero za watumishi wa umma wanyonge ambao ndio msingi wa Taifa letu hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pili baada ya kumshukuru Mheshimiwa Rais, niwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Rufiji, kwa namna moja au nyingine wamekuwa wakiniamini wakati wote waliponichagua mwaka 2015, lakini pia mwaka 2020 nilishinda kwa kishindo kwa kura ambazo hazipata kutokea.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda sasa kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Alice Karungi Kaijage Mbunge wa Viti Maalum wa Mkoa wa Pwani kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Mujibu wa Kanuni D. 6(2) ya Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma za Mwaka 2009, Watumishi wa Umma huajiriwa na kupandishwa vyeo kwa kuzingatia sifa zilizoainishwa katika Miundo ya Maendeleo ya Utumishi ya Kada husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua mabadiliko ya kiutendaji pamoja na maendeleo ya kiteknolojia na kiuchumi Wizara mbalimbali zimekuwa zikihuisha miundo ya maendeleo ya kiutumishi ya kada mbalimbali zilizo chini yake kwa kuongeza sifa za kielimu, vigezo vya kuajiri na kupandisha vyeo watumishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa, kwa kutambua mabadiliko ya kiutendaji na maendeleo ya kiteknolojia na kiuchumi, kuanzia mwaka 2014 Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imekuwa ikiziwezesha Wizara Taasisi na Wakala za Serikali kuhuisha miundo yake ya maendeleo ya kiutumishi kadri ya mahitaji mapya yanavyojitokeza. Kwa mfano katika kipindi hicho miundo iliyohuishwa ni pamoja na ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Fedha na Mipango, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni, pamoja na Taasisi za Umma na Wakala wa Serikali.
MHE. SYLVIA F. SIGULA aliuliza: -
Je, nini mpango wa Serikali wa kutoa ajira rasmi na zisizo rasmi kupitia tasnia ya Sanaa?
WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa hii ni mara yangu ya kwanza kusimama kwenye Bunge lako hili Tukufu katika Wizara hii mpya ya Utamaduni Sanaa na Michezo, nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema na mjawa wa kadiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, namshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniamini kwa mara nyingine na kuniteua katika Wizara hii. Naomba nimthibitishie Mheshimiwa Rais kwamba Wizara yetu hii pamoja na watendaji wa Wizara tutajipanga kweli kweli ili matamanio yake aliyokusudia katika Wizara hii yaweze kutimia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nijibu swali la Mheshimiwa Sylvia Francis Sigula, kwanza kwa kutambua mchango wake kwa vijana. Amekuwa na mchango mzuri kwa vijana, nasi kama Wizara tunampongeza sana kwa kuwasemea vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kwa kutambua kwamba swali lake ni la msingi na la muhimu sana, ili kuwavutia wadau hasa vijana kujiajiri katika Sekta ya Sanaa, mpango wa Serikali ni kuendelea kuboresha mazingira ya kazi za sanaa kwa kufanya mambo kadhaa. Moja ya mambo makubwa ambayo tunakwenda kuyafanya ni: -
Kwanza, ni kuhakikisha vifaa na vitendea kazi vya sanaa vinapatikana kwa bei nafuu kwa kufanya mapitio kwenye kodi za vifaa husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, tutakwend kupitia upya tozo kwenye Kanuni za BASATA, COSOTA na Bodi ya Filamu Tanzania ili ziwe rafiki kwa walipaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, tutakwenda kuanzisha mifumo mbalimbali ya kieleketroniki ya usajili, ambayo mingine tunayo lakini tutakwenda kubuni na kuendeleza mingine ya maombi ya vibali na leseni pamoja na mfumo rasmi wa ukusanyaji mirabaha kutoka kwa watumiaji wa kazi za sanaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, tutakwenda kujenga miundombinu ya sanaa kama vile Arts Arena, National Art Gallery na One Stop Center, ambayo tayari tunayo inaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, tunakwenda kuanzisha Mfuko ambao utakaokuwa ni suluhisho la kimitaji na mafunzo kwa wadau wa Sekta ya Sanaa.
MHE. AMEIR ABDALLAH AMEIR aliuliza: -
Je, kuna mkakati gani wa kuhakikisha utalii wa ndani unaimarika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA K.n.y. WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -
Mheshimiwa Spika, Kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utaii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ameir Abdallah Ameir, Mbunge kutoka Baraza la Wawakilishi kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika; katika kuhakikisha utalii wa ndani unaendelea kuimarika nchini, Wizara inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kukuza utalii wa ndani ikiwemo: -
i. Kuwa na huduma bora zenye gharama nafuu kwenye vivutio zikiwemo malazi, chakula, usafiri na viingilio;
ii. Kuendelea kuhamasisha makundi mbalimbali ya kijamii ikiwa ni pamoja na wanafunzi, wajasiriamali, wafanyakazi na makundi maalum kutembelea maeneo ya vivutio vya utalii na pia kufanya mikutano; na
iii. Kuendelea kutoa elimu kwa umma na kutumia chaneli maalum (Tanzania Safari Channel) ya kutangaza utalii kwa lengo la kutangaza vivutio vya utalii pamoja na kuhamasisha wananchi kutembelea vivutio hivyo.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuongeza maeneo ya utalii, kuibua vivutio na mazao mapya ya utalii na kuendeleza miundombinu ya utalii katika kanda zote za utalii nchini.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua kero ya nyani, kima, tumbili na ngedere kwa Wananchi wanaopakana na Mlima Kilimanjaro?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA K.n.y. WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu suali la Mheshimiwa Profesa Patrick Alois Ndakidemi, Mbunge wa Moshi Vijijini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro ina vituo vya askari wanyamapori kwenye Wilaya zote zinazopakana na Hifadhi, ambapo Moshi kuna vituo vinne, Rombo kuna vituo vitatu, Hai kuna kituo kimoja, Siha kuna kituo kimoja na Longido kuna vituo viwili. Vituo hivyo vina askari wa Jeshi la Uhifadhi ambao kwa kushirikiana na maafisa wa wanyamapori kutoka wilaya husika wamekuwa wakifanya kazi ya kuwafukuza wanyamapori wakali na waharibifu pindi wanapovamia makazi ya wananchi au mashamba yao.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa wito kwa wananchi wa Jimbo la Moshi Vijijini wanaopatwa na madhara ya wanyamapori, wakiwemo nyani, kima, tumbili na ngedere na kadhalika kutoa taarifa kwa askari wa uhifadhi wa vituo hivyo pale wanyamapori hao wanapoingia kwenye maeneo yao ili waweze kudhibiti wanyamapori hao.
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza:-
Je, kuna mpango gani kuvuna/kuwahamisha Tembo kutoka katika Pori la Rungwa, Muhesi na Kizigo ambao wanaingia katika Vijiji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA K.n.y. WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inakiri kuwepo kwa changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu wakiwemo tembo. Kwa sasa Serikali inaendelea kutekeleza Mkakati wa Udhibiti Wanyamapori Wakali na Waharibifu wa Mwaka 2020/2024. Wizara inaendelea kufanya yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, ni kutoa elimu juu ya kujikinga na wanyamapori wakali na waharibifu; pili, kujenga vituo vya askari wanyamapori ili kusogeza huduma karibu na wananchi; na zaidi ya hapo ni kufunga mikanda (GPS collars) tembo kwa kuanzisha timu maalum.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuwashirikisha wananchi kwa kutoa mafunzo kwa askari wa vijiji ili kuongeza nguvu ya kudhibiti tembo katika maeneo ya wananchi, nakushukuru.
MHE. PRISCUS J. TARIMO aliuliza: -
Je, kuna mpango gani kusaidia Halmashauri zinazozunguka Mbuga/Hifadhi za Taifa kupitia CSR kutoka kwenye mapato ya utalii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA K.n.y. WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Priscus Jacob Tarimo, Mbunge wa Moshi Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia utekelezaji wa Sera ya Uwajibikaji Kijamii (Community Social Responsibility - CSR) Serikali inatekeleza miradi ya ujirani mwema kwa jamii zinazozunguka maeneo yaliyohifadhiwa ikiwemo Hifadhi za Taifa, Mapori ya Akiba, Mapori Tengefu na Hifadhi za Wanyamapori za Jamii. Katika kutekeleza Sera hiyo, Halmashauri za Wilaya pamoja na jamii zinazozunguka maeneo yaliyohifadhiwa, zinanufaika na mapato yanayotokana na utalii ikiwemo kupatiwa miradi mbalimbali ya kijamii inayoibuliwa na wananchi kwenye sekta mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuhakikisha Halmashauri za Wilaya pamoja na wananchi wanaopakana na maeneo yaliyohifadhiwa wananufaika kutokana na mapato ya utalii kupitia utekelezaji wa Sera ya Uwajibikaji Kijamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI aliuliza:-
Je, lini Serikali itamaliza mgogoro wa mpaka wa Pori la Usumbwa Forest Reserve na Hifadhi ya Pori la Kigosi Moyowosi – Ushetu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA K.n.y. WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Peter Cherehani, Mbunge wa Ushetu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Pori la Usumbwa Forest Reserve ambalo kwa sasa ni Hifadhi ya Taifa Kigosi, haina mgogoro wowote wa mpaka na wananchi wa Ushetu. Kwa sasa kilichopo, wananchi wa Ushetu waliwasilisha maombi ya kumegewa eneo ambapo Serikali inaendelea na tathmini na pindi itakapokamilika, wananchi watajulishwa, nakushukuru.
MHE. BENARDETA K. MUSHASHU aliuliza: -
Je, lini Serikali itapeleka Walimu wa kutosha katika Shule za Msingi na Sekondari Mkoani Kagera?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Benardeta Kasabago Mushashu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2022 Serikali iliajiri Walimu 9,800 na Mkoa wa Kagera ulipangiwa walimu ajira mpya 640. Kati ya hao, walimu 351 wa shule za msingi na 289 kwa shule za Sekondari. Kwa mwaka 2023 Serikali iliajiri Walimu 13,130 na Mkoa wa Kagera ulipangiwa walimu 590, kati yao, walimu 312 ni kwa shule za msingi na 278 ni kwa shule za Sekondari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua mahitaji ya Walimu katika Mkoa wa Kagera na maeneo mengine nchini. Hata hivyo serikali kila mwaka inaendelea kupunguza mahitaji ya walimu katika sekta ya elimu; na hivi karibuni Serikali itatangaza ajira za walimu baada ya taratibu za kibali kutoka Ofisi ya Rais – Utumishi kukamilika na kadiri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. RASHID A. SHANGAZI K.n.y. MHE. ELIBARIKI I. KINGU aliuliza: -
Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa madarasa katika Shule ya Msingi Mahaya – Singida?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Immanuel Elibariki Kingu, Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka 2023/2024 Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi ambayo Jimbo la Singida Magharibi lipo imetengewa shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya shule za msingi. Aidha, Shilingi milioni 595.6 zimetumika kujenga shule mpya moja na vyumba vya madarasa vinne katika shule mbili za msingi katika Jimbo la Singida Magharibi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Shule ya Msingi Mayaha imetengewa bajeti kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mawili kwa mwaka wa fedha 2024/2025. Serikali itaendelea kuongeza madarasa katika shule hii kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza: -
Je, Serikali ina mkakati gani wa kutoa ajira za kutosha kwa Walimu ili kuondoa upungufu uliopo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Ramadhani Sima, Mbunge wa Jimbo la Singida Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka 2022 Serikali iliajiri walimu 9,800 wa shule za msingi na sekondari na kwa mwaka 2023 Serikali iliajiri walimu 13,130 wa shule za msingi na sekondari. Serikali inatambua mahitaji ya Walimu kote nchini. Hata hivyo Serikali kila mwaka inaendelea kupunguza mahitaji ya walimu katika sekta ya elimu na hivi karibuni Serikali itatangaza ajira za walimu baada ya taratibu za kibali kutoka Ofisi ya Rais – Utumishi kukamilika na kadiri ya upatikanaji wa fedha.