Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Mohamed Omary Mchengerwa (17 total)

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA aliuliza:-
(a) Je, ni utaratibu upi uliotumika na Serikali kuzuia malipo ya 80% kwa mwezi kwa Majaji Wastaafu ambayo ni haki yao ya msingi na malipo ya mafao yao yanayotambulika kwa mujibu wa Sheria ya Majaji?
(b) Je, ni utaratibu upi unaotumika sasa kuzuia malipo hayo kwa baadhi ya Majaji?
WAZIRI WA SHERIA NA KATIBA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa, Mbunge wa Rufiji, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Katiba ya Jamhuri ya Muungano 1977, Ibara 142(1) na (5) imeelezea kuwa malipo ya mishahara na mafao ya Jaji wa Mahakama ya Rufani na Jaji wa Mahakama Kuu yanalipwa kupitia Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali. Aidha, Sheria ya Mafao na Maslahi ya Majaji ya mwaka 2007 na Sheria ya Mafao na Hitimisho la Kazi kwa Watumishi wa Umma Na.2 ya mwaka 1999 nazo zimefafanua kuwa malipo ya mishahara na mafao ya Jaji wa Mahakama ya Rufani na wa Mahakama Kuu yatalipwa na Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Fedha na Mipango hutekeleza wajibu wa kulipa 80% ya pensheni kwa Jaji aliyestaafu baada ya kupata na kuzifanyia uhakiki nyaraka zote muhimu kutoka Mahakama na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii ambayo Jaji husika alichangia. Kwa Jaji Mstaafu ambaye ana stahili ya kulipwa pensheni ya kila mwezi na PSPF au Mfuko wowote aliouchangia, stahili yake ya 80% hulipwa kwa kuongeza kiwango cha fedha inayopaswa kufikia 80% ya mshahara wa Jaji aliyeko madarakani.
Mheshimiwa Naibu Spika, endapo Jaji Mstaafu hastahili kulipwa pensheni ya kila mwezi kutokana na kutotimiza sharti la kuchangia muda wa chini katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii ambao ni kipindi cha miaka 15, asilimia 80 ya pensheni yake ya kila mwezi hulipwa na Hazina kwa asilimia 100. Malipo haya ya asilimia 80 huhuishwa kila wakati na Hazina kulingana na viwango vya mishahara ya Majaji waliopo madarakani.
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA Aliuliza:-
Jimbo la Rufiji ni miongoni mwa majimbo yasiyo na barabara hata nusu kilometa.
Je, ni lini Serikali itafikiria kujenga barabara kuelekea Makao Makuu ya Wilaya yaani kutoka Nyamwage – Utete yenye urefu
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa Mbunge wa Rufiji kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, jumla ya kilometa 717.5 za barabara kuu ya Dar es Salaam Kibiti hadi Lindi kutoka Jaribu Mpakani hadi Malendego zimejengwa kwa lami na ziko katika Wilaya ya Rufiji na Wilaya mpya ya Kibiti; hivyo Wilaya ya Rufiji inayo barabara ya lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Nyamwage – Utete yenye urefu wa kilometa 33.8 ni barabara Mkoa na inahudumiwa na Wakala wa Barabara kupitia ofisi ya meneja wa TANROADS wa Mkoa wa Pwani. Barabara hii imekuwa ikitengewa fedha na kufanyiwa matengenezo ya aina mbalimbali kila mwaka na inapitika vizuri katika majira yote ya mwaka. Katika mwaka wa fedha 2015/2016 barabara hii imetengewa shilingi milioni 100 kwa ajili ya ukarabati.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika mwaka 2016/2017 barabara hii imetengewa shilingi milioni 579.147 kwa ajili ya matengenezo mbalimbali na shilingi milioni 85 kwa ajili ya ukarabati. Aidha, Wizara kupitia Wakala wa Barabara itafanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hii ili iweze kujengwa kwa kiwango cha lami kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA aliuliza:-
Wakulima wa zao la korosho Jimbo la Rufiji wameibiwa zaidi ya shilingi 900,000,000 kwa mwaka 2011 kutoka kwa Vyama vya Msingi vya Kimani, Mwasani, Kibiti na Ikwiriri.
Je, ni lini Serikali itachukua hatua kali dhidi ya vyama hivyo?
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mchengerwa kuna Wandengereko tunakaa maeneo mengine.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa, Mbunge wa Rufiji, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2012 Mrajisi wa Vyama vya Ushirika nchini alifanya ukaguzi katika Vyama vya Ushirika wa Korosho katika Mkoa wa Pwani na kubaini upotevu wa fedha wa shilingi 2,655,182,760.46 uliosababishwa na viongozi na watendaji wa Vyama vya Ushirika. Aidha, uhakiki uliofanywa na Ofisi ya Mrajisi huyo unaonesha kuwa wakulima wa korosho wa Mkoa wa Pwani wanavidai vyama vya msingi jumla ya shilingi 3,195,135,103, deni ambalo linatokana na sababu mbalimbali za kibiashara kama vile anguko la bei ya korosho katika soko la dunia. Mchanganuo wa deni hilo kwa kila Wilaya ni kama ifuatavyo; Mkuranga ni shilingi 1,931,224,587, Rufiji shilingi 1,215,018,100, Kibaha Mjini shilingi 758,880, Bagamoyo ni shilingi 10,275,960 na Mafia shilingi 7,857,576.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na ukaguzi huo ilibainika kwamba Mkoa wa Pwani ulikuwa na viongozi 822 wa Vyama vya Ushirika waliodaiwa kuhusika na upotevu wa fedha za wakulima wa korosho. Kwa Wilaya ya Rufuji viongozi 41 wa vyama walibainika kufanya ubadhirifu huo na hivyo kwa kutumia kifungu cha 95 cha Sheria ya Ushirika Na.6 ya mwaka 2013, Mrajisi aliwaandikia hati ya madai na kuwataka kulipa fedha zilizopotea.
Mheshimiwa Naibu Spika, viongozi wa Vyama vya Mwaseni 11, Kilima Ngorongo tisa, Ikwiriri 11 na Kibiti 10 walihusika. Kiasi wanachodaiwa viongozi hao ni shilingi 68,878,188 katika mchanganuo ufuatao:- Mwaseni shilingi 5,152,906, Kilima Ngorongo shilingi 22,104,384, Ikwiriri shilingi 20,549,494 na Kibiti shilingi 21,071,398. Viongozi wa vyama hivi vyote kutoka Wilaya ya Rufiji bado hawajalipa fedha wanazodaiwa na taratibu zinakamilishwa za kuwapeleka mahakamani.
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi tarehe 5 Novemba, 2015 ni viongozi 79 tu kati ya 822 wa Mkoa wote wa Pwani waliokuwa wamerejesha jumla ya shilingi 24,260,163.19. Kwa viongozi ambao hawajarejesha, taratibu zimeandaliwa za kuwafikisha katika vyombo vya sheria ili hatua ziweze kuchukuliwa ambapo hadi tarehe 8/06/2016 tayari majalada 11 yalikuwa yamefunguliwa polisi na kufikishwa katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mkoa wa Pwani.
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA aliuliza:-
Mradi wa REA umekuwa ukisuasua katika maeneo ya vijiji vya Rufiji hususan Tarafa ya Mkongo, Kata za Mkongo, Ngorongo, Kipungila na Kata ya Mwaseni na Ngarambe.
Je, ni lini mradi huo utakamilika katika hatua inayofuata?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa, Mbunge wa Rufiji, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa REA Awamu ya III ambao utafuata sasa na ambao unatekelezwa baada ya Mradi wa REA Awamu ya II katika Wilaya ya Rufiji unatekelezwa na Mkandarasi MBH Power Ltd. Wigo wa kazi katika Wilaya hii unahusisha ujenzi wa njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 217.34; ujenzi wa njia ya umeme msongo wa kilovoti 04 yenye urefu wa kilometa 64.18; ufungaji wa transfoma 40 na kuwaunganishia umeme wateja wapatao 2,059.
Mradi umekamilika kwa asilimia 76 zikijumuisha ujenzi wa kilometa 201 za msongo wa kilovoti 33; ujenzi wa kilometa 23 za msongo wa kilovoti 0.4; kufunga transfoma 17 pamoja na kuwaunganishia umeme wateja 256. Mradi huu hadi kukamilika utagharimu shilingi bilioni 7.74.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kata za Mkongo, Ngorongo, Kipungila, Mwaseni na Ngarambe ujenzi wa njia ya umeme msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilomita 94 kutoka Ikwiriri hadi Mloka umekamilika kwa asilimia 90. Ujenzi wa njia ya usambazaji umeme wa msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu kilomita 24.64 imekamilika kwa asilimia 45 na ufungaji wa transfoma 14 unatarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi Septemba 2016. Kazi hizi zinatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Oktoba, 2016. Kazi hii hadi kukamilika itagharimu shilingi bilioni 3.15.
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA aliuliza:-
Sheria zinatoa ridhaa kwa watu kuwinda ndani ya hifadhi:-
Je, Serikali inachukua hatua gani kutoa ridhaa kwa wananchi waishio maeneo ya hifadhi kupata ruhusa kisheria ili kuweza kuvua samaki ndani ya mabwawa kama ilivyokuwa miaka ya nyuma kwa wanakijiji waishio maeneo ya hifadhi hususan Kata za Mwaseni, Mloka na nyingine?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa, Mbunge wa Rufiji, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1994 wananchi wa Kata za Mwaseni, Mloka, Ngoroko na Kipungila Wilayani Rufiji waliruhusiwa kuingia ndani ya Pori la Akiba Selous na kuvua samaki. Hata hivyo, baadhi ya wanavijiji walikiuka taratibu zilizokuwa zimewekwa kwa kuingia ndani ya hifadhi bila kujiandikisha na kuvua samaki kinyume cha sheria. Aidha, baadhi yao walibainika kujihusisha na vitendo vya ujangili wa wanyamapori kama vile utoaji wa taarifa za mwenendo wa doria na uwindaji wa wanyamapori, uvuvi haramu wa kutumia sumu, ukataji miti ovyo kwa ajili ya kukaushia samaki na kutengeneza mitumbwi na uharibifu wa mazingira kutokana na uchomaji wa moto ovyo kinyume cha sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia hali ya usalama katika maeneo ya uhifadhi ya wanyamapori, kwa sasa Wizara yangu itaendelea kutoruhusu uvuvi kufanyika ndani ya Pori la Akiba Selous. Hata hivyo, Wizara yangu inawashauri wananchi wa Kata za Mwaseni, Mloka na nyinginezo zilizo jirani kutumia mabwawa mengineyo yaliyopo nje ya pori yenye fursa kubwa ya kufanya shughuli za uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya mabwawa hayo ni Zumbi katika Vijiji vya Nyaminywili, Kipugira na Kipo, Bwawa la Ruwe karibu na Mkongo, Bwawa la Lugongo katika Kijiji cha Mtanza na Bwawa la Zimbwini katika Mji wa Kibiti.
Mabwawa hayo na Mto Rufiji vinatoa fursa ya shughuli za uvuvi, hivyo kusaidia kuinua kipato cha wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua mahitaji ya wananchi katika maeneo haya, ya kufanya kazi na kujiletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii, Wizara yangu inaendelea kushauriana na Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji kuhusu namna ya kutekeleza mpango wa kuwajengea mabwawa ya samaki ili pamoja na mabwawa ya asili yaliyopo yawawezeshe kufanya shughuli za uvuvi endelevu.
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA Aliuliza:-
Matatizo ya mipaka kati ya wanakijiji na maeneo ya hifadhi husababisha migogoro kati ya wanakijiji na watumishi wa hifadhi.
Je, Serikali inachukua hatua gani kurejesha mahusiano kati ya watumishi wa hifadhi na wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa, Mbunge wa Rufiji, kama kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba matatizo ya mipaka kati ya vijiji na maeneo ya hifadhi mara kadhaa imesababisha migogoro kati ya wananchi na wahifadhi na wakati mwingine hata kusababisha maafa katika baadhi ya maeneo.
Wizara yangu imeendelea kuchukua hatua mballimbali katika kudumisha na kuboresha mahusiono baina ya wananchi na wahifadhi zikiwemo:-
(a) Kuendelea kutoa elimu ya uhifadhi na faida zake na kuwakumbusha wahifadhi juu ya umuhimu wa kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na utaratibu.
(b) Kusaidia kuimarisha uwezo wa usimamizi wa maliasili katika ngazi za vijiji na Wilaya ikiwemo kuhamasisha uanzishwaji wa Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori (Wildlife Management Areas – WMAs) na kuimarisha zilizopo.
(c) Kuhakikisha wananchi wanaoishi katika maeneo yanayopatikana na hifadhi wanafaidika na faida zitokanazo na uhifadhi katika maeneo yao kwa mujibu wa kanuni na taratibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu itaendelea kushikiana na wadau mbalimbali katika kutekeleza sera taratibu za uhifadhi shirikishi ili kuboresha uhifadhi na kudumisha mahusiano na mashirikiano kati ya wahifadhi na wananchi.
MHE. ABDALLAH H. ULEGA (K.n.y. MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA) aliuliza:-
Mheshimiwa Spika, maeneo mengi ya Pwani huwa na madini mbalimbali.
Je, eneo la Rufiji lina madini gani ili wananchi hawa washauriwe ipasavyo kutouza maeneo yao?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa Mbunge wa Rufiji lililo ulizwa kwa niaba yake na Mheshimiwa Abdallah Hamis Ulega, Mbunge wa Mkuranga kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika ni kweli kwamba katika ukanda wa Pwani ya Tanzania kunapatikana madini ya aina mbalimbali ambayo ni pamoja na Barite, Chokaa, Chumvi, Clay, Dhahabu, Flourite, Jasi, Kaolin, Mchanga, Mercury, Niobium, Ruby, Rutile, Titanium, Zircon pamoja na Gesi Asilia.
Mheshimiwa Spika, Wakala wa Jiolojia Tanzania GST kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Kampuni ya Beak Consultants GmbH ya nchini Ujerumani ilifanya utafiti wa awali wa mwaka 2013 na 2014. Kutokana na utafiti huo madini yaliyobainika katika eneo la Rufiji ni pamoja na madini ya Chokaa na Niobium ambayo hupatikana katika eneo la Milima Luhombero, vilevile kuna viashiria vya uwepo wa madini ya dhahabu, mchanga pamoja na maeneo mengine ambapo kuna madini ya ujenzi pamoja na madini ya gesi asilia. Utafiti wa kina unahitajika ili kubaini kiasi halisi cha mashapo ya madini hayo kabla ya kuanza uchimbaji wake, ingawa machimbo ya mchanga pamoja na madini ya kokoto yanaendelea kuchimbwa.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO (K.n.y. MHE. MOHAMED MCHENGERWA) aliuliza:-
Ni takribani miaka miwli sasa Serikali imeshindwa kuwahakikishia wananchi wa Jimbo la Rufiji kuwa na umeme wa uhakika kufuatia hitilafu ya mara kwa mara kwenye mitambo ya umeme unaozalishwa na gesi kutoka Kilwa.
Je, ni lini Serikali itawaunganisha wananchi wa Rufiji, Kibiti na Kilwa kwenye Gridi ya Taifa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Omary Mohamed Mchengerwa, Mbunge wa Rufiji, lililoulizwa kwa niaba yake na Mheshimiwa Mbunge maarufu sana wa Kihesa Mgagao, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Kilwa, Rifiji pamoja na Kibiti zimeunganishwa katika Gridi ya Taifa kupitia utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Somangafungu, Lindi hadi Kinyerezi, Dar es Salaam. Ujenzi wa mradi huu utaanza mwezi Julai, 2018 na utakamilika mwaka 2019/2020.
Mheshimiwa Spika, kazi za ujenzi wa mradi huu zinahusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 400 yenye urefu wa kilometa 198 kutoka Somangafungu, Lindi hadi Kinyerezi, Dar es Salaam. Lakini pia, kujenga Kituo cha Kupoza Umeme, lakini pamoja na mambo mengine mradi huu utaunganisha wateja mbalimbali na kusafirisha umeme utakaozalishwa kutoka Kituo cha Somangafungu chenye uwezo wa kuzalisha megawati 240. Mradi utafadhiliwa na Kampuni ya Sumitomo ya Japan kwa gharama ya dola za Marekani milioni 340.
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA aliuliza:-
(a) Je, Serikali ina hisa kiasi gani katika Kiwanda cha Sukari cha Kagera?
(b) Je, kiasi cha fedha kilichokopwa na mwekezaji kwa guarantee ya Serikali kimeshalipwa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa, Mbunge wa Rufiji, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
• Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali haimiliki hisa katika Kiwanda cha Sukari cha Kagera na Serikali kupitia PSRC ilibinafsisha kiwanda hicho kwa Kampuni ya Kagera Saw Mills Limited kwa kuuza hiza zake zote mnamo mwaka 2001.
• Mheshimiwa Spika, mwekezaji alikopa kiasi cha dola za Kimarekani milioni 65 kwa kutumia guarantee ya Serikali mwaka 2004 ikiwa ni guarantee ya miaka 12. Hadi sasa zaidi ya dola za Kimarekani milioni 56.88 zimesharejeshwa sawa na asilimia 87.5 ya mkopo wote. Aidha, marejesho ya sehemu ya mkopo uliobaki wa dola za Kimarekani milioni yatafikia ukomo wake mwezi Julai, 2019.
MHE. ALLY S. UGANDO (K.n.y. MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA) aliuliza:-
Wananchi wa Kata za Mwaseni, Mloka, Ngoroko na Kipungila Wilayani Rufiji waliruhusiwa kuingia ndani ya Hifadhi ya Selous na kuvua samaki na hivyo kuinuka kiuchumi. Baada ya marekebisho ya mipaka ya hifadhi wamezuiwa kuingia kwenye hifadhi na wakati mwingine wanatendewa vitendo kinyume na sheria.
(a) Je, Serikali inachukua hatua gani kusaidia wananchi wa maeneo hayo ili waweze kupata kipato?
(b) Je, Serikali inachukua hatua gani kurejesha amani kati ya vijiji vinavyozunguka maeneo ya mipaka ya hifadhi na watumishi wa hifadhi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa, Mbunge wa Rufiji, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuanzia mwaka 1990 Pori la Akiba la Selous lilianzisha Mpango wa Ushirikishwaji Jamii zinazozunguka pori hilo katika uhifadhi chini ya mradi ulioitwa Selous Conservation Programme (SCP). Katika kutekeleza mpango huo, wananchi wa jirani waliruhusiwa kuvua samaki ndani ya Pori la Akiba la Selous kwa ajili ya kitoweo baada ya kuombwa na wananchi wa Vijiji vya Kata za Mwaseni na Ngorongo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kibali hicho kilisitishwa baada ya kuwepo ukiukwaji wa masharti yaliyotolewa ambapo baadhi ya wanavijiji waliingia ndani ya hifadhi bila kujisajili au kujiandikisha na kuvua samaki kwa ajili ya kufanya biashara kinyume na kusudio la kibali hicho. Aidha, baadhi ya wanavijiji walitumia fursa hiyo kufanya ujangili ndani ya pori kwa kuingia na silaha walizoficha ndani ya mitumbwi yao na kuua tembo, faru na wanyamapori wengine. Kutokana na sababu hizi, Serikali haina mpango wa kuruhusu uvuvi katika Pori la Akiba Selous. Nashauri Mheshimiwa Mbunge kushirikiana na Serikali kuelimisha wananchi kuvua katika mabwawa yaliyo nje ya hifadhi pamoja na kuhamasisha ufugaji wa samaki kibiashara ili kujipatia kitoweo na kipato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali katika kuimarisha mahusiano mema kati ya wahifadhi na jamii inayozunguka maeneo yanayohifadhiwa itaendelea kuhakikisha inatoa elimu kwa jamii na kushirikiana nayo kwenye shughuli mbalimbali za kimaendeleo.
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA aliuliza:-
Mradi wa Kilimo wa RUBADA - Rufiji, umekuwa mradi wa kitapeli ambao watu wachache wanajinufaisha na rasilimali za Rufiji bila ya Wana-Rufiji kupata maendeleo yoyote.
Je, ni lini Serikali itafikiria kuleta mradi wa kilimo katika Bonde la Mto Rufiji ambalo kwa miaka mingi liko tupu bila shughuli yoyote ya kilimo hasa ikizingatiwa kuwa bonde hilo lina kila kitu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, kabla ya kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa, Mbunge wa Rufiji, lenye sehemu mbili, naomba nianze kutoa maelezo ya utangulizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Rubada siyo mradi, bali ilikuwa ni Mamlaka ya Uendelezaji wa Bonde la Rufiji kwa maana ya Rufiji Basin Development Authority.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo haya, sasa naomba nianze kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni vema nikiri tu kwamba kulikuwepo upungufu wa kiutendaji ndani ya RUBADA. Kutokana na hali hiyo, Wizara ilifanya uchunguzi mwezi ule wa Oktoba, 2014 na tarehe 8 Aprili, 2015 Wakurugenzi watatu wa RUBADA walisimamishwa kazi na hatimaye tarehe 21 Januari, 2016 Bodi ya RUBADA iliwafukuza kazi rasmi Wakurugenzi wawili.
Aidha, kutokana na mabadiliko ya kisera, kisheria na kimfumo, imeonekana kuwa RUBADA imekosa uhalali wa kuendelea kuwepo. Hivyo Serikali mnamo mwezi Septemba, 2017 ilileta Muswada wa Sheria Bungeni ukipendekeza kuifuta RUBADA. Bunge liliridhia kuifuta RUBADA na shughuli zake kuhamishiwa taasisi nyingine za kiserikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaelewa fursa zilizopo katika Bonde la Rufiji. Hatua kadhaa zimechukuliwa kutumia vizuri fursa hizi. Mathalani, Serikali inatekeleza mradi mkubwa wa Bwawa Stiegler’s Gorge kwa ajili ya umeme wa megawati 2,100. Bwawa hili pia litawezesha kuhifadhi maji kwa ajili ya umwagiliaji, mifugo na uvuvi. Pia upo mradi wa Bwawa la Maji la Kidunda ambalo pamoja na kutoa uhakika wa maji ya kunywa kwa Jiji la Dar es Salaam litatumika pia kwa umwagiliaji, mifugo na uvuvi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya kilimo kwa kushirikiana na Wizara ya sekta ya kilimo imeandaa programu ya kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili kwa maana ya (ASDP II) ambapo ina maeneo ya kipaumbele 23 na jumla ya miradi ya uwekezaji kwa maana ya Investment Projects 56 ya kipaumbele ambayo inajumuisha miradi iliyopo katika Bonde la Mto Rufiji ambayo ilikuwa ikiratibiwa na RUBADA chini ya uliokuwa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN). Miradi hiyo ni kama vile iliyopo maeneo ya Muhoro, Tawi, Bumba na Msoro. ASDP II inalenga kuendeleza miradi hiyo iliyopo Bonde la Mto Rufiji kama kuweka miundombinu ya umwagiliaji ambapo wananchi wengi watanufaika kupitia programu hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kaka yangu kuwa miradi hii ikikamilika italifanya Bonde la Mto Rufiji kuwa lulu ya maendeleo. Kwa maana hiyo, namwomba kaka yangu Mheshimiwa Mchengerwa avute subira kidogo kuona mabadiliko haya tarajiwa na yenye matokeo chanya.
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA aliuliza:-

Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na. 2 ya Mwaka 2018 yamemwondoa Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kushitaki kesi zote za jinai nchini, lakini Katiba ya Jamhuri ya Muungano inamtambua Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika mambo ya Muungano:-

Je, kumwondoa moja kwa moja Mwanasheria Mkuu wa Serikali hakuwezi kuathiri makosa ya jinai ya uhaini yanayoweza kutokea Zanzibar kukwama kwa kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka hana mamlaka kwa mujibu wa Katiba na mambo ya Muungano kushitaki Zanzibar?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa, Mbunge wa Rufiji, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Ibara ya 59(b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Sheria ya Ofisi ya Mashitaka, Sura ya 430, masuala ya ufunguaji, uendeshaji na usimamizi wa mashitaka ya jinai nchini yako chini ya Mkurugenzi wa Mashitaka na siyo Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Kwa upande wa Zanzibar, masuala hayo yanaongozwa na Ibara ya 56(a) ya Katiba ya Zanzibar na Sheria ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka Na. 2 ya Mwaka 2010. Katika Katiba zote mbili na sheria zake, mamlaka ya mwisho ya kufungua, kuendesha na kusimamia mashitaka ya jinai ni ya Mkurugenzi wa Mashitaka. Hivyo, masuala ya jinai siyo suala la Muungano.

Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kuwa tarehe 13 Februari, 2018 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alifanya mabadiliko ya muundo wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ambapo pamoja na mambo mengine alianzisha Ofisi Huru ya Taifa ya Mashitaka. Ili kuendana na mabadiliko hayo ya muundo, yalifanyika kurekebisha kwenye Sheria ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (Utekelezaji wa Majukumu) Sura ya 268 kwa kukifuta Kifungu cha 8 na kukibadilisha kupitia Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na. 2 ya Mwaka 2018.

Mheshimiwa Spika, marekebisho hayo yamemwondoa Mkurugenzi wa Mashitaka na iliyokuwa Division ya Mashitaka kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Hivyo, mabadiliko hayo hayajaathiri kwa namna yoyote ufunguaji, uendeshaji na usimamizi wa mashauri ya jinai nchini. Bado kwa mujibu wa Ibara ya 59(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 Mkurugenzi wa Mashitaka anaendelea kuwa na mamlaka ya juu ya mashauri yote ya jinai nchini.

Mheshimiwa Spika, makosa yote ya jinai yanayotokea katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yanaendelea kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria zilizopo na hayawezi kukwama kwa kuwa kuna mifumo mizuri ya kikatiba, kisheria na kitaasisi ya kuyashughulikia.
MHE. MOSHI S. KAKOSO (K.n.y. MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA) aliuliza:-

Bonde la Mto Rufiji lina eneo kubwa lenye rutuba ambalo lingetumika vizuri lingeweza kulisha Mji wa Dar es Salam na viwanda vyote nchini, RUBADA imechukua maeneo hayo ambayo inakadiriwa kuwa na ukubwa wa hekta 500,000 na kuwapa baadhi ya wawekezaji ambao wengi wao ni matapeli na madalali wa viwanja/mashamba:-

Je, lini Serikali itamua kunyang’anya maeneo yote ambayo wawekezaji wameshindwa kuwekeza kwa kadri walivyoomba ili Sera ya Serikali ya Viwanda iweze kutimia?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa, Mbunge wa Jimbo la Rufiji, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Uendeshaji wa Bonde la Mto Rufiji (RUBADA) ilianzishwa na Sheria ya Bunge Namba 5 ya mwaka 1975 na kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali Namba.146 tarehe 1 Julai 1976. Mojawapo ya majukumu ya RUBADA ilikuwa kusimamia matumizi ya ardhi ya kilimo kwenye Bonde la Mto Rufiji ikiwemo kuratibu upatikanaji wa ardhi kwa wawekezaji kwa ajili ya shughuli za kilimo.

Mheshimiwa Spika, kwa kumbukumbu zilizopo, RUBADA haikuwahi kuchukua eneo la ardhi lenye ukubwa wa hekta 500,000 na kuwapa wawekezaji. RUBADA ilikuwa inamiliki hekta 21 katika Kituo cha Ikwiriri, hekta 12.675 katika Kambi ya Vijana Mkongo, hekta 1.15 katika Kambi ya Utete, hekta 5,128 katika Shamba la Ngalimila Kilombero, Mkoani Morogoro, hekta 5,800 katika Shamba la Mngeta, Kilombero, Mkoani Morogoro na eneo la kilometa za mraba 13,907 kwa ajili ya majengo na viwanja Jijini Dar es Salaam. Aidha, ardhi yote nyingine kwenye eneo la Bonde la Mto Rufiji lilikuwa linamilikiwa na Halmashauri 29 za Wilaya, Vijiji na wananchi mbalimbali.

Katika kipindi chote ilipokuwepo RUBADA imewezesha upatikanaji wa Hati Miliki usio wa moja kwa moja yaani (Derivative Right of Occupancy) wa eneo la hekta 2,000 katika eneo la Nyumbunda, Nyambili na Bungu, Wilaya ya Kibiti kwa mwekezaji FJS African Starch Development kwa ajili ya kilimo na ujenzi wa kiwanda cha kuchakata mihogo. Aidha, Serikali haitasita kuchukua ardhi hiyo ya kilimo iwapo itathibitika kuwa mwekezaji ameshindwa kuendeleza kwa shughuli za kilimo na uzalishaji wa mazao ya kilimo.
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA aliuliza:-

Wilaya ya Rufiji ni moja ya Wilaya kongwe nchini na inakadiriwa kuwa na watu takribani 350,000; eneo la Wilaya ni kubwa na huwalazimu wananchi kusafiri umbali wa kilometa 100 kufuata huduma za kibenki.

Je, ni lini Serikali itapeleka huduma za kibenki katika Wilaya ya Rufiji?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa, Mbunge wa Rufiji, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa upatikanaji wa huduma za kifedha na hasa karibu na maeneo ya wananchi ili kuwawezesha kuendesha shughuli zao za kiuchumi. Aidha, kufuatia mabadiliko ya sekta ya fedha nchini ya mwaka 1991 Serikali ilitoa uhuru kwa mabenki kufanya tathimini na utafiti ili kuamua kuhusu maeneo ya kupeleka huduma za kibenki kulingana na taarifa za utafiti uliofanywa pamoja na vigezo vya benki husika. Kwa kuwa benki zinajiendesha kibiashara maamuzi ya kufungua tawi sehemu yoyote hapa nchini huzingatia vigezo hivyo.

Mheshimiwa Spika, wananchi wa Wilaya ya Rufiji wanapata huduma za kifedha kupitia kituo cha makusanyo ya fedha cha NMB yaani cash collection point kilichopo Kata ya Utete pamoja na mawakala wa benki hususan Benki ya NMB na CRDB waliopo katika Wilaya ya Rufiji.

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kumwomba Mheshimiwa Mbunge wa Rufiji aendelee kuwahimiza wananchi wake kutumia fursa zilizopo za kupata huduma za kifedha kupitia kituo hicho cha makusanyo ya fedha cha NMB, mawakala wa benki na simu za mkononi wakati Serikali ikiendelea kufanya jitihada za kuboresha miundombinu muhimu pamoja na kufanya majadiliano na kuyashawishi baadhi ya mabenki ili kuona jinsi ya kupunguza baadhi ya vikwazo vinavyoweza kusababisha gharama za uendeshaji wa shughuli za kibenki katika Wilaya ya Rufiji kuwa juu.
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA aliuliza:-

Katika bajeti ya Mwaka wa Fedha 2016/2017 Serikali iliahidi kujenga kiwanda cha sukari katika Jimbo la Rufiji, hata hivyo ardhi iliyokusudiwa kujengwa kiwanda hicho kwa sasa amepewa mwekezaji ambaye hana nia ya kujenga kiwanda hicho:-

Je, ni lini Serikali itaamua kutumia Sheria ya Ardhi Na. 113 na 114 kuichukua ardhi hiyo kutoka kwa mwekezaji na kuyapa Mashirika ya Umma ili kujenga Kiwanda cha Sukari Rufiji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Omar Mchengerwa, Mbunge wa Rufiji, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa Serikali iliahidi kujenga kiwanda cha sukari Wilayani Rufiji baada ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kukamilisha kazi ya kuainisha maeneo yanayofaa kwa kilimo cha miwa Wilayani Rufiji na maeneo mengine nchini. Serikali kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania, kwa maana ya TIC, ilipata mwekezaji kutoka nchi ya Mauritius, Kampuni ya Rufiji Sugar Plant na Kampuni ya Agro Forest Plantations.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kampuni ya Rufiji Sugar Plant inategemea kuwekeza katika Vijiji vya Tawi hekta 6,600, Nyamwange hekta 1,728 ambapo Kampuni ya Agro Forest Plantation inatarajia kuwekeza katika Vijiji vya Muhoro Magharibi hekta 5,710 Muhoro Mashariki hekta 1,529 na Vijiji vya Chumbi A, B na C hekta 1,926.77. Taratibu za kupata ardhi kwenye Serikali zote za vijiji ngazi ya wilaya ilianza mwaka 1912 na kukamilika mwaka 1916. Nyaraka zote zimewasilishwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambayo inaendelea na taratibu zake za kujiridhisha ili itoe hati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi iliyofanywa na mwekezaji hadi sasa ni kupima mipaka ya maeneo husika, kuchukua sampuli za udongo katika vijiji vyote na kupima kiasi cha kemikali zilizopo ardhini kwa kuzingatia masharti ya kanuni za kilimo. Aidha, taratibu za uwekezaji zitaendelea baada ya kampuni hizi kupewa hatimiliki za ardhi kwenye maeneo husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Mbunge awe na subira wakati Serikali inaendelea kukamilisha taratibu hizi.
MHE. MARIAM N. KISANGI (K.n.y. MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA) aliuliza:-

Serikali imerejesha vyuo vilivyokuwa vya maendeleo kuwa chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Je, Serikali haioni umuhimu wa kukibadili Chuo cha Maendeleo Ikwiriri FDC kuwa VETA ili kubadili fikra za wananchi wa Rufiji, Kibiti na Ikwiriri na hatimaye kuleta mwamko wa elimu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa, Mbunge wa Rufiji kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, elimu ya ufundi na mafunzo ufundi stadi hutolewa katika shule na vyuo katika viwango na madaraja mbalimbali kulingana na malengo yake. Katika ngazi ya shule za sekondari, elimu ya ufundi hutolewa ili kumuandaa mwanafunzi kujiunga na vyuo vya ufundi stadi na ufundi wa kati. Vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi huandaa mafundi mchundo na vyuo vya ufundi wa kati huandaa mafundi sanifu. Aidha, vyuo vikuu hundaa wahandisi katika fani mbalimbali zinzohusiana na ufundi.

Mheshimiwa Spika, Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi vilianzishwa kwa lengo la kumsaidia wananchi kubaliana na changamoto za kimaendeleo katika mazingira yake kwa kumapatia maarifa na stadi anuwai. Vyuo hivi hutoa elimu ya ufundi stadi katika hatua ya kwanza hadi ta tatu. Pia mafunzo ya ujasiliamali, kilimo, uvuvi, mifugo n.k hutolewa kulingana na mahitaji ya eneo husika.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali haina mapango wa kuvibadili Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi kuwa VETA. Badala yake, Serikali imejikitia katika viboresha vyuo hivyo kwa kuvikarabati na kuviongezea vifaa vya kuviongezea vifaa vya kujifunzia na kufundishia ili viweze kutoa mafunzo bora zaidi. Awamu ya kwanza ukarabati wa Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi 20 ipo katika hutua za mwisho za ukamishaji awamu ya pili inataraji kuanza mapema mwezi Juni, 2019. Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Ikwiriri kilikuwa katika awamu ya kwanza na ukarabati umekamilika. Aidha, katika mwaka wa fedha 2019/2020 Rufiji n miongoni mwa Wilaya zilizotengewa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha Ufundi stadi cha Wilaya cha VETA.
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA aliuliza:-

Matatizo ya maji katika Jimbo la Rufiji ni ya muda mrefu kwenye maeneo kadhaa hususan Kata ya Ngarambe maji hupatikana kwa umbali zaidi ya kilometa 7 - 10 na kwa kuwa Serikali sasa inaleta sera ya Maji ndani ya mita 400:-

Je, ni lini Serikali itatua kero ya maji katika Kata ya Ngarambe, Mbwala, Chumbi, Muholo, Kipugila na maeneo mbalimbali ya Tarafa ya Ikwiriri hata kwa kuchimba visima?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa, Mbunge wa Rufiji, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua changamoto ya huduma ya maji katika Halmashauri ya Rufiji na kwa sasa tayari baadhi ya kata hizo zimeanza kupewa kipaumbele kwa kujengewa miradi ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kata ya Mbwala kuna mradi wa kisima kirefu ambao unatumia teknolojia ya dizeli. Mradi huo kwa sasa una changamoto ya uendeshaji kwani wananchi wanatumia gharama kubwa kwa kununua mafuta ya uendeshaji wa mitambo ya mradi huo. Halmashauri inaendelea na taratibu za kutumia teknolojia ya umeme wa REA ambao tayari umeshafika katika kata hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kata ya Chumbi vimechimbwa visima viwili ambapo kwa sasa vipo katika hatua ya usanifu wa miradi. Kata ya Muholo imewekwa katika utekelezaji wa miradi ya awamu ya pili ambapo kwa sasa usanifu katika visima viwili umekamilika. Wizara imeshatoa kibali kwa ujenzi wa miundombinu kwani miundombinu ya awali ilichakaa na haifai tena kwa mradi. Katika mwaka wa fedha 2019/2020 Halmashauri ya Rufiji imetengewa jumla ya shilingi milioni 871.98 kwa ajili ya kuendelea kukamilisha miradi ya zamani ya kujenga miradi mipya.