Answers to supplementary Questions by Hon. Mohamed Omary Mchengerwa (4 total)
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri ninayo maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa ili muundo fulani wa utumishi wa kada fulani uhuishwe lazima kwanza kada husika maombi yapelekwe Serikalini ndipo ifanyiwe kazi, kwa hiyo kama ikikwama kwenye meza fulani ya kamishna ina maana huo uhuishwaji unakwama. Kwa kuzingatia hivyo, je, Serikali haioni vema sasa kuwa na utaratibu wa kuwa na kipindi maalum cha kufanya uhakiki wa kada zote za Utumishi wa Umma na pia kufanya uhakiki wa Utumishi wa Umma pamoja na takwimu za Utumishi, hii yote kuleta usawa katika Utumishi wa Umma na pia kuboresha na kupandisha morale ya kazi ya watumishi? Mfano mzuri ni kada ya uhuishaji wa muundo wa kada ya maafisa kazi hawa Labour Officers.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa stahiki, stahili kwa watumishi pamoja na mafao yao hukokotolewa kuzingatia kiwango cha mshahara anacholipwa mtumishi. Kwa kuona umuhimu huu, je, Serikali sasa italipa kipaumbele suala zima la kuhakiki kada za kiutumishi kwa wakati? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu kweye swali la msingi kwamba Serikali itaendelea kuhuisha miundo ya maendeleo ya utumishi kwa kadri ambavyo inaletwa kwenye Wizara yetu. Nitoe kumbukumbu tu kwa Mheshimiwa Mbunge aweze kufahamu kwamba kuanzia mwaka 2011 Serikali imekuwa ikihuisha miundo ya maendeleo ya utumishi hasa kwa kada hii ya ualimu, ambapo ilifanya nyongeza ya madaraja kutokana na nafasi zao za walimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia mwaka 2014 Wizara iliendelea kufanya namna hiyo na mwaka 2015 Wizara ya Fedha pia Wizara yetu iliendelea kuhuisha miundo hasa kwenye kada mbalimbali ikizingatiwa baadhi ya watendaji kwenye kada hizo maafisa mipango, manunuzi, maaafisa ugavi, wahasibu na wakaguzi. Nitoe rai tu kwa Mheshimiwa Mbunge afahamu kwamba Wizara yetu itaendelea kuhuisha miundo mbalimbali ya maendeleo ya utumishi kwa kadri itakavyoona inafaa. Kwa hiyo nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba asiwe na hofu.
Mheshimiwa Naibu Spika, na kwa swali la pili, kuhusu stahiki za mafao za watumishi kama ambavyo nimeulizwa. Katika utumishi wa umma stahiki na stahili za utumishi zimeanisha katika miongozo na nyaraka mbalimbali zinazotolewa kuhuishwa mara kwa mara na Serikali. Nyaraka hizo huainisha makundi mbalimbali ya utumishi na stahiki wanazotakiwa kupata.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu kwenye swali langu la msingi, kwa mujibu wa kanuni ile ile Kanuni D. 6(2) za Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma, Kanuni hii iliwahi kutolewa mwaka 2009; watumishi wa Umma kuajiriwa na kupandishwa vyeo na kubadilishwa kada (Recategorization) kwa kuzingatia sifa walizonazo na zinazooneshwa katika Miundo ya Maendeleo ya Utumishi katika kada mbalimbali zilizoainishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Miundo ya Maendeleo ya Utumishi wa kada mbalimbali katika Utumishi wa Umma imeainisha ngazi za mishahara, kuanzia cheo cha kuingilia katika Utumishi wa Umma (entry point) hadi cheo cha mwisho kwa kila kada kulingana na kiwango cha elimu na kwa kuzingatia uzito wa majukumu ya kada husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kuliarifu Bunge lako hili Tukufu kuwa Serikali itaendelea kuhuisha stahiki na stahili mbalimbali za watumishi wa umma pamoja na viwango vya mishahara ya kada mbalimbali kwa kuzingatia sera za kibajeti na uzito wa majukumu ya kada husika ili viweze kutumika kukokotoa mafao mbalimbali ya umma. (Makofi)
MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri wa Utumishi, lakini kumekuwa na nyaraka zitolewazo na miongozo na Menejimenti ya Utumishi wa Umma zinazokinzana kabisa na Sheria mama ya Utumishi wa Umma. Je, lini hizi nyaraka na miongozo vitafutwa ili sheria mama za kiutumishi zitumike?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, lazima nikiri kwamba tunapokuwa na nyaraka basi sheria ndiyo hufuata mkondo wake. Tunapokuwa na sheria ambayo inayokinzana na Katiba ni dhahiri Katiba inakuwa juu ya ile sheria, lakini tunapokuwa na nyaraka inakinzana na sheria basi sheria ndiyo inafuata mkondo wake.
Kwa kupitia swali lako kama ulivyoliuza nitapata fursa ya kukaa na watendaji na kuangalia zile nyaraka zote ambazo zinakinzana na sheria iliyopo na tutafanya maamuzi kutokana na namna. Lakini pia ikikupendeza nitaomba nipate nyaraka hizo ili niweze kuzipitia na kushaurina na watendaji katika Wizara yangu. (Makofi)
MHE. SYLVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa ni jukumu la Serikali kukuza, kuibua na kuendeleza sanaa nchini, tunatambua kuna vijana wengi sana nchini wana vipaji, lakini wanashindwa kuvitumia vipaji vyao kulingana na mazingira magumu yaliyopo ya kufanya vipaji hivyo na huenda vipaji hivyo vingeweza kuwapatia ajira.
Je, ni nini mpango wa Serikali wa kuibua, kuendeleza na kusimamia vipaji hivi vya vijana walioko katika nchi yetu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, tunatambua kwamba kuna taasisi na watu binafsi wanaofanya matamasha ya kuibua vipaji: -
Je, ni nini kauli ya Serikali katika kuwaidia hizi taasisi au watu binafsi wanaofanya matamasha na jitihada za kusaidia kuinua vipaji Tanzania?
WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Sylvia kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpe taarifa tu Mheshimiwa Mbunge kwamba pamoja na maswali ya msingi ambayo yalijieleka moja kwa moja kwenye swali la kwanza ambalo limeulizwa kama swali la nyongeza, Wizara yetu inajipanga vyema kutafuta vijana wenye vipaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwataarifu Waheshimiwa Wabunge kwamba mimi na wasaidizi wangu tumejipanga kupita katika kila mtaa ili kuweza kutafuta vijana wenye vipaji mbalimbali. Pia, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, Serikali imejipanga vizuri; na Mheshimiwa Rais tayari ameshaanzisha mfuko maalum ambao utawasaidia vijana wenye vipaji.
Kwa hiyo, tutapita kila mtaa, kila kijiji, kila wilaya, kila halmashauri katika kila mkoa kuhakikisha kwamba tunawasaka vijana wenye vipaji na kuweza kuwasaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili linalozungumzia matamasha yanayofanywa na baadhi ya watu na taasisi, sisi kama Wizara hatutakuwa na jambo dogo. Nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge, kwamba Wizara haitakuwa na jambo dogo, kila jambo litakuwa na uzito wake. Kwa hiyo tutashiriki katika kila kitu kinachofanyika kinachohusu utamaduni, sanaa na michezo ambacho wenzetu katika taasisi mbalimbali wamekuwa wakitusaidia Serikali.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa sanaa imekuwa chanzo kikuu cha ajira kwa vijana wetu, je, Serikali haioni kuwa umefika wakati sasa wa kutumia vyuo vyetu vya VETA kama vituo vya kuibua na kuendeleza vipaji vya sanaa kwa vijana wetu?
WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa majibu ya swali la nyongeza kwa Mheshimiwa Mbunge wa Mikumi, mchapa kazi kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na ushauri mzuri aioutoa kuhusu matumizi ya vyuo vya VETA, lakini sisi kama Serikali tunakwenda mbele zaidi. Tunategemea kutumia baadhi ya shule tulizonazo kutengeneza academy mbalimbali. Tutatumia shule aidi ya 56 ambazo Serikali imejipanga kuzitumia kwa ajili ya kuendeleza na kukuza vipaji katika maeneo hayo.